(Alif, Lām, Rā) Yametangulia maelezo kuhusu herufi zilizokatwa na kutengwa. Hizo ni aya tukufu miongoni mwa aya za Kitabu kitukufu kilichoteremshwa kwa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye. Nazo ni aya za Qur’ani zenye kufafanua kweli kwa matamko mazuri zaidi na yaliyo wazi zaidi na yenye kuonyesha zaidi makusudio. Kitabu na Qur’ani ni kitu kimoja ; na hapa Mwenyezi Mungu Ameyakusanya pamoja majina mawili
Makafiri watatamani, watakapowaona Waumini walioasi wakitoka Motoni, lau wao walikuwa ni wenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu wakawa ni wenye kutoka kama wao
Waache, ewe Mtume, hao makafiri wapate kula na wastarehe na ulimwengu wao na iwashughulishe tamaa ya huo ulimwengu wasimtii Mwenyezi Mungu, watakuja kujua mwisho wa mambo yao ambayo ni hasara ya duniani na Akhera
Na wakiomba kuteremshiwa adhabu, kwa kukukanusha, ewe Mtume, basi sisi hatuuangamizi mji, isipokuwa uwapo wakati wa kuangamizwa umeshapangwa; hatutawaangamiza mpaka waufikie mfano wa wale waliowatangulia
Na Mwenyezi Mungu Akawajibu: Sisi hatuwateremshi Malaika isipokuwa kwa adhabu ambayo haina kucheleweshwa kwa asiyeamini na hawakuwa ni wenye kuachwa wakati Malaika watakapoteremka
Hakika sisi tumeiteremsha Qur’ani kwa Nabii Muhammad, rehema na amani zimshukiye, na hakika sisi tunachukua ahadi kuitunza isiongezwe, isipunguzwe wala sehemu yoyote katika hiyo isipotee
Hakuna Mjumbe yoyote aliwajia wao isipokuwa walikuwa wakimfanyia shere.Katika haya pana kumliwaza Mtume, rehema na amani zimshukie. Na kama walivyokufanyia hawa, hivyo ndivyo walivyofanyiwa Mitume kabla yako
Kama tulivyoutia ukafiri kwenye nyoyo za ummah waliotangulia kwa sababu ya kuwafanyia shere Mitume na kuwakanusha, hivyo ndivyo tunavyofanya kwenye nyoyo za washirikina miongoni mwa watu wako waliofanya uhalifu wa kumkanusha Mwenyezi Mungu na kuwakanusha Mitume Wake
hawauamini Ukumbusho ulioteremshwa kwako. Na umeshapita mwendo wa wamwanzo wa kuwaangamiza wakanushaji. Na hawa ni kama wao, wataangamizwa wenye kuendelea na ukafiri na ukanushaji miongoni mwao
Na lau tuliwafungulia makafiri wa Makkah mlango wa mbingu, wakaendelea kupanda kuingia ndani wapate kuyashuhudia yaliyomo mbinguni ya ajabau za ufalme wa Mwenyezi Mungu, hawangaliamini
Na miongoni mwa dalili za uweza wetu ni kwamba sisi tumeweka kwenye uwingu wa karibu vituo ya sayari kushukia, ambayo kwayo zinajulikana njia, nyakati, urutuba na ukavu, na tumeupamba uwingu huu kwa nyota ili wenye kuziangalia wataamali na wazingatie
Isipokuwa aliyetega sikio kusikiliza maneno ya watu wa juu baadhi ya nyakati, akafikiwa na sayari inayotoa mwangaza na kumchoma.Na huenda Shetani akamddokeza rafiki yake baadhi ya habari alizozisikia kwa kutegea kabla hajateketezwa na kimondo
Na ardhi tumeinyosha ikawa kunjufu, tukaweka juu yake majabali yenye kuiimarisha , tuakaotesha kila aina ya mimea ambayo waja wanaihitajia kwa kipimo kinachojulikana
Na tukawawekea nyinyi humo vitu mnavyovihitajia katika maisha yenu miongoni mwa makulima, wanyama, aina mbalimbali ya shughuli za kujipatia maisha na vinginevyo. Na tukawaumbia nyinyi watoto, watumishi na wanyama manaonufaika nao. Na riziki zao haziko juu yenu, bali ziko juu ya Mwenyezi Mungu Bwana wa viumbe vyote kwa wema utokao Kwake na ukarimu
Na hakuna chochote cha manufaa ya waja isipokuwa ziko kwetu hazina zake za kila aina, na hatukiteremshi isipokuwa kwa kadiri iliyowekewa mpaka, kama vile tutakavyo. Hazina zote ziko mkononi mwa Mwenyezi Mungu, Anampa Anayemtaka na Anamzuilia Anayemtaka, kulingana na rehema Yake kunjufu na hekima Yake kubwa
Na tunatuma upepo na tunaufanya uwe mtiifu kwetu uyajaze mawingu yabubujishe maji na yanyeshe na yanywesheze miti, hapo majani yake yafunguke na mafumba yake yajitokeze. Na mvua inabeba heri na nafuu na tunayateremsha maji yake tuliyowatayarishia nyinyi kwa ajili ya kunywa kwenu, ardhi yenu na wanayama wenu. Na nyinyi si waweza wa kuyahifadhi na kuyaweka akiba, lakini sisi tunawahifadhia kwa kuwahurumia na kuwafanyia hisani
Ndio sisi tunaompa uhai aliyekufa kwa kumpatisha kutoka kwenye hali ya kutokuwako, na tunamfisha aliyekuwa hai baada ya ajali yake kukoma. Na sisi ndio wenye kuirithi ardhi na walioko juu yake
Na hakika Mola wako Ndiye Atakayewakusanya wao wahesabiwe na walipwe. Hakika Yeye ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji Wake mambo, ni Mwingi wa ujuzi, hakuna kinachofichika Kwake
Kwa hakika tulimuumba Ādam kwa udongo mkavu, ukigongwa unasikiwa sauti. Na udongo huu mkavu ni miongoni mwa udongo mweusi uliogeuka rangi yake na harufu yake kwa kipindi kirefu cha kukaa kwake
Kumbuka, ewe Mtume, pindi Mola wako Aliposema kuwaambia Malaika, «Mimi nitamuumba mtu kutokana na udongo mkavu. Na udongo huu mkavu unatokana na udongo mweusi uliogeuka rangi
«Basi nitakapomtengeneza na kulikamilisha umbo lake na nikapuliza roho ndani yake, mwangukieni hali ya kusujudu,» sijida ya maamkizi na heshima na si sijida ya ibada
Iblisi akasema akionyesha kiburi chake na uhasidi wake, «Hainasibiani na mimi nimsujudie mtu uliyempatisha kutokana na udongo mkavu, uliokuwa mweusi na uliogeuka.»
Mwenyezi Mungu Akamwambia, «Wewe ni miongoni mwa wale niliowapa muda na kuchelewesha kuwaangamiza mpaka siku ambayo viumbe wote watakufa baada ya Mpulizo wa kwanza
Akasema Iblisi, «Mola wangu, kwa sababu ya vile ulivyonipoteza na kunipotosha nitawapambia vizazi vya Ādam kukuasi katika ardhi na nitawapoteza wote wasiione njia ya uongofu
Kwa kweli, wale waja wangu ambao wamenitakasia mimi sitakupatia uwezo juu ya nyoyo zao ili uwapoteze kwa uwezo huo na njia iliyonyoka. Lakini uwezo wako utakuwa ni juu ya yule aliyekuandama miongoni mwa wapotofu washirikina ambao wameukubali usimamizi wako na kukutii badala ya kunitii mimi.»
Na tutawaondolea yaliyomo ndani ya nyoyo zao ya chuki na uadui, wataishi Peponi wakiwa ndugu wapendanao, watakaa kwenye vitanda vikubwa na nyuso zao zitaelekeana katika hali ya kuungana na kupendana
Na wapashe habari, ewe Mtume, kuhusu wageni wa Ibrāhīm miongoni mwa Malaika ambao walimpa habari njema za kupata mwana na za kuangamia kwa jamaa za Lūṭ
Pindi walipoingia kwake na wakamwamkia kwa kusema, «Amani.» Hapo naye akawarudishia maamkizi ya amani. Kisha akwaletea chakula na wao wasikile, na hapo akasema, «Sisi ni wenye kicho na nyinyi.»
Ibrāhīm akasema, huku yuwaona ajabu, «Mnanipa habari njema za kupata mwana na mimi nishakuwa mtu mzima, na mke wangu pia, ni kwa njia gani mnanipa habari njema hizo za kushangaza?»
Kwa hivyo, toka miongoni mwao , wakiwa pamoja na wewe watu wako waumini, baada ya kupita sehemu ya usiku. Na wewe nenda nyuma yao isije mmoja wao akasalia nyuma ikampata adhabu. Na jichungeni asije mmoja wenu akageuka na akatazama nyuma yake asije akaona adhabu na pia naye ikampata. Na kimbilieni kule ambako Amewaamrisha Mwenyezi Mungu, ili mpate kuwa mahali salama penye amani
Na wakaja wakazi wa mji wa Lūṭ mpaka kwa Lūṭ pindi walipojua kwamba kwake kuna wageni, huku wana furaha na nderemo kwa wageni wake, ili wawachukue wafanye nao machafu
Watu wake wakasema, «Kwani sisi si tulikukataza kumkaribisha mgeni yoyote miongoni mwa walimwengu - na walikuwa wakiwakatia njia wasafiri - kwa kuwa sisi tunataka kufanya machafu na wao?»
Lūṭ akasema kuwaambia, «Hawa wanawake wenu ni mabinti zangu, waoeni iwapo mnataka kumaliza hamu zenu, wala msiyafanye mliyokatazwa na Mwenyezi Mungu ya kuwajia wanaume.» Amewaita hao wanawake kuwa ni mabinti zake, kwa kuwa Nabii wa ummah ana cheo cha baba kwao
Muumba Anaapa kwa Anayemtaka na kwa Anachokitaka. Ama muumbwa haifai kwake kuapa isipokuwa kwa jina la Mwenyezi mungu. Na Ameapa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kwa uhai wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, kwa kumtukuza kwa watu, kwamba watu wa Lūṭ wako kwenye sahau kali, wana shaka na wako kwenye ushindani
Kwa hakika, katika kule kuwaangamiza kwetu pana ushahidi waziwazi kwa wenye kuamini na wenye kutenda matendo yanayoambatana na sheria za Mwenyezi Mungu
Na kwa hakika, wakazi wa mji uliozingirwa na miti, nao ni watu wa Shu'ayb, walikuwa ni wenye kuzidhulumu nafsi zao kwa kumkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume wao mtukufu
Hivyo basi tuliwaadhibu kwa mtetemeko na adhabu ya siku ya uvuli. Na kwa hakika, makazi ya watu wa Lūṭ na watu wa Shu'ayb yako katika njia iliyo wazi, watu wanayapitia katika safari zao na wanapata mazingatio
Na kwa hakika, walimkanusha Mtume Ṣāliḥ, amani imshukiye, watu wa bonde la Hijr, nao ni kina Thamūd, wakawa kwahilo ni wenye kuwakanusha Mitume wote. Kwani mwenye kumkanusha Mtume mmoja huwa amewakanusha Mitume wote, kwani wao wako kwenye Dini moja
Na tuliwapa watu wa Ṣāliḥ aya zetu zinazojulisha usahihi wa mambo ya haki ambayo amekuja nayo kwao Mtume Ṣāliḥ, na miongoni mwayo ni ngamia, waszingatie kwa aya hizo na wakawa ni wenye kujiweka mbali nazo na kuzipa mgongo
Na hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyoko baina yake isipokuwa kwa haki, zikiwa ni zenye kujulisha ukamilifu wa muumba wake na uweza Wake, na kwamba Yeye Ndiye Ambaye ibada yoyote haifai kufanyiwa isipokuwa Yeye, Peke Yake, Asiyekuwa na mshirika. Na ule wakati ambao Kiyama kitasimama hauna budi ni wenye kuja, ili kila mtu apate kulipwa kwa yale aliyoyatenda. Basi wasamehe, ewe Mtume, hao washirikina, usiwachukulie na uyaachilie mbali wanayoyatenda
Hakika Mola wako Ndiye Muumba wa kila kitu, Ndiye Anayekijua, kwa hivyo hakuna kitu chochote kinachomshinda wala kufichika Kwake katika ardhi wala mbinguni
Na kwa kweli tumekupa, ewe Mtume, ufunguo wa Qur,ani, nao ni hizo aya saba (za sura ya Fatiha) zinazokaririwa katika kila Swala, na tumekupa Qur,ani tukufu
Usiziangalie kwa macho yako mawili zile starehe za duniani ambazo tuliwastarehesha nazo makafiri aina mbalimbali, na usisikitike juu ya ukafiri wao, na uwanyenyekee wenye kumuamini MwenyeziMungu na Mtume wake
Na ni mwenye kuwaonya nyinyi isije ikawapata adhabu kama ile Aliyoiteremsha Mwenyezi Mungu kwa wale walioigawanya Qur,ani, wakaiamini baadhi yake na wakaikanusha baadhi nyingine miongoni mwa Mayahudi, Wanaswara na makafiri wa Kikureshi
«Na wao ni wale walioifanya Qur’ani kuwa ni vigawannyo na mafungu.» Kati yao kuna wanaosema, ‘ni uchawi’ na kati yao kuna wanaosema, ‘ni ukuhani’ na kati yao kuna wanaosema yasiyokuwa hayo ili wawazuie watu kufuata uongofu
Naapa kwa Mola wako, tutawahesabu tena tutawahesabu Siku ya Kiyama, na tutawalipa tena tutawalipa wote kwa kuigawanya kwao Qur’ani, kwa kuzua kwao urongo, kuibadilisha, kuipotoa na yasiyokuwa hayo
Na utangaze waziwazi ulinganizi wa haki ambao Amekuamrisha nao Mwenyezi Mungu, wala usiwajali washirikina, kwani kwa kweli Amekutakasa Mwenyezi Mungu kutokana na hayo wanayoyasema
Kimbilia kwa Mola wako pindi unaponyongeka moyo wako, na uitakase dhati Yake kwa kumshukuru na kumsifu. Na uwe ni miongoni mwa wenye kuswali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na wenye kumuabudu, kwani kwa kweli hilo litakutosheleza na lile lenye kukutia kero
Na uendelee kumuabudu Mola wako muda wa uhai wako mpaka ikujie yakini isiyokuwa na shaka nayo ni kifu. Na Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, alitekeleza amri ya Mola Wake, kwani hakuacha kuendelea kumuabudu Mwenyezi Mungu mpaka ikamjia yakini ya kifo kutoka kwa Mola Wake