Back to Languages

Swahili - Chapter 26 - Ash-Shuara

Translation by Abdullah Muhammad Abu Bakr — Permalink

Verse 1 — Surah Ash-Shuara 26:1

«Ṭā, Sīn, Mīm.» Yametangulia maelezo kuhusu herufi za mkato mwanzo wa sura ya Al-Baqarah

Verse 2 — Surah Ash-Shuara 26:2

Hizi ni aya za Qur’ani yenye kufafanua kila kitu, yenye kupambanua baina ya uongofu na upotevu

Verse 3 — Surah Ash-Shuara 26:3

Huenda wewe, ewe Mtume, kwa kuwa una hamu sana ya kutaka wao waongoke, ukajiangamiza mwenyewe kwa kuwa wao hawakukuamini na hawakufuata kimatendo uongofu wako. Basi usifanye hivyo

Verse 4 — Surah Ash-Shuara 26:4

Tukitaka tutawateremshia wakanushaji, miongoni mwa watu wako, miujiza itokayo mbinguni yenye kuwaogopesha itakayowalazimisha wao kuamini, na hapo shingo zao ziwe zimenyongeka na kudhalilika. Lakini hatukutaka hilo, kwani Imani yenye kunufaisha ni kuyaamini yaliyoghibu kwa hiyari

Verse 5 — Surah Ash-Shuara 26:5

Na hauwajii washirikina hawa ukumbusho, kutoka kwa Mwingi wa rehema unaoanzwa kuteremshwa, kitu baada ya kitu, wenye kuwaamrisha na kuwakataza na kuwakumbusha Dini ya kweli, isipokuwa wanaupa mgongo na hawaukubali

Verse 6 — Surah Ash-Shuara 26:6

Kwa hakika washaikanusha Qur’ani na washaifanyia shere, basi zitawajia wao habari za jambo ambalo walikuwa wakilifanyia shere na dharau, na itawashukia wao adhabu ikiwa ni malipo ya kumuasi Mola wao

Verse 7 — Surah Ash-Shuara 26:7

Je, wanakanusha na hali wao hawakuiangalia ardhi ambayo ndani yake tumeotesha kila aina nzuri ya mimea ambayo hakuna awezae kuiyotesha isipokuwa Mola wa viumbe vyote

Verse 8 — Surah Ash-Shuara 26:8

Kwa hakika, katika kuitoa mimea kwenye ardhi ni dalili wazi ya ukamilifu wa uweza wa Mwenyezi Mungu, na wengi wa watu hawakuwa ni wenye kuamini

Verse 9 — Surah Ash-Shuara 26:9

Na kwa hakika Mola wako Ndiye Mshindi wa kila kiumbe, ni Mwenye kurehemu Ambaye rehema Yake imeenea kila kitu

Verse 10 — Surah Ash-Shuara 26:10

Na wakumbushe watu wako, ewe Mtume, pindi Mola wako Alipomuita Mūsā kuwa awaendee watu madhalimu

Verse 11 — Surah Ash-Shuara 26:11

nao ni watu wa Fir’awn na uwaambie wayaogope mateso ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na waache ukafiri na upotevu walionao

Verse 12 — Surah Ash-Shuara 26:12

Mūsā akasema, «Mola wangu! Mimi ninaogopa wasije wakanikanusha juu ya utume

Verse 13 — Surah Ash-Shuara 26:13

na moyo wangu ukaingia kero kwa kunikanusha, na ulimi wangu usiwe na ufasaha wa kulingania. Basi mtume Jibrili aende na wahyi kwa ndugu yangu Hārūn, ili anisaidie na aniamini kwa ninayoyasema, na awafafanulie kile ninachowaambia, kwani yeye ana ufasaha zaidi wa matamshi kuliko mimi

Verse 14 — Surah Ash-Shuara 26:14

Na watanishika na kosa la kumuua mwanamume wa jamii ya Qibṭī miongoni mwao, na kwa hivyo ninaogopa wasiniue kwa ajili yake.»

Verse 15 — Surah Ash-Shuara 26:15

Mwenyezi Mungu Akamwambia Mūsā, «Sivyo hivyo! Hawatakuua. Na nimekubali matakwa yako juu ya Hārūn. Basi endeni mkiwa na miujiza yenye kuonyesha ukweli wenu. Sisi tuko pamoja na nyinyi kwa ujuzi, utunzi na usaidizi tunasikiliza

Verse 16 — Surah Ash-Shuara 26:16

Mjieni Fir’awn na mumwambie, «Sisi tumetumwa kwako na kwa watu wako kutoka kwa Mola wa viumbe wote

Verse 17 — Surah Ash-Shuara 26:17

kwamba uwaache Wana wa Isrāīl waende na sisi.»

Verse 18 — Surah Ash-Shuara 26:18

Fir’awn akasema kumwambia Mūsā kwa kumsimanga, «Je, hatukukulea kwenye majumba yetu ukiwa mchanga, ukakaa kwenye utunzi wetu miaka (mingi) katika umri wako

Verse 19 — Surah Ash-Shuara 26:19

ukafanya tendo la jinai kwa kumuua mwanamume miongoni mwa watu wangu, ulipompiga na ukamsukuma, na wewe ni miongoni mwa wakanushaji neema zangu na kukataa uola wangu

Verse 20 — Surah Ash-Shuara 26:20

Mūsā akasema kumjibu Fir’awn, «Nilifanya uliyoyataja kabla Mwenyezi Mungu Hajaniletea wahyi na kunitumiliza kama Mtume

Verse 21 — Surah Ash-Shuara 26:21

ndipo nilitoka kwenu kwa kukimbia kuelekea Madyan nilipoogopa usije ukaniua kwa nililolifanya bila kukusudia, Na Mola wangu Akanitunuku unabii na elimu na Akanifanya ni miongoni mwa Mitume

Verse 22 — Surah Ash-Shuara 26:22

Na kwani huko kulelewa nyumbani kwako unakuona ni neema kutoka kwako juu yangu, na hali wewe umewafanya Wana wa Isrāīl ni watumwa , unawachinja wana wao wa kiume na unawaachilia wanawake wao ili watumwe na wadharauliwe?»

Verse 23 — Surah Ash-Shuara 26:23

Fir’awn akamwambia Mūsā, «Na huyo Mola wa viumbe wote Ambaye unadai kwamba wewe ni mjumbe Wake, ni kitu gani?»

Verse 24 — Surah Ash-Shuara 26:24

Mūsā akasema, «Yeye ni Mmiliki na Mwenye kuipelekesha mbingu na ardhi na vilivyoko baina ya viwili hivyo. Iwapo nyinyi mna yakini na hilo, basi aminini.»

Verse 25 — Surah Ash-Shuara 26:25

Fir’awn akasema kuwaambia walioko pambizoni mwake miongoni mwa watukufu wa watu wake, «Je, hamusikii maneno ya Mūsā ya ajabu kwamba kuna mola asiyekuwa mimi?»

Verse 26 — Surah Ash-Shuara 26:26

Mūsā akasema, «Mola Ambaye mimi nawalingania nyinyi Kwake ni Yule Aliyewaumba nyinyi na Aliyewaumba wa mwanzo. Basi vipi nyinyi mnamuabudu ambaye ni kiumbe kama nyinyi na yeye ana mababa waliotoeka kama mababa zenu?»

Verse 27 — Surah Ash-Shuara 26:27

Fir’awn akasema kuwaambia wale watu wake makhsusi akiwapandisha ghadhabu zao, kwa kuwa Mūsā amemkanusha yeye, «Kwa kweli, huyu mjumbe wenu aliyeletwa kwenu ni mwendawazimu , asema maneno yasiyofahamika.»

Verse 28 — Surah Ash-Shuara 26:28

Mūsā akasema, «Mola wa Mashariki na Magharibi na vilivyoko baina ya viwili hivyo, na vilivyomo ndani yake vya mwangaza na giza. Hili linapelekea kuwa ni lazima kumuamini Yeye Peke Yake, iwapo nyinyi ni miongoni mwa watu wa akili na kuzingatia.»

Verse 29 — Surah Ash-Shuara 26:29

Fir’awn akamwambia Mūsā kwa kumtisha, «Ukichukua mwingine aseyekuwa mimi ukamfanya ni mola nitakufunga jela pamoja na wale niliowafunga.»

Verse 30 — Surah Ash-Shuara 26:30

Mūsā akasema, «Je, utanifanya mimi ni miongoni mwa wafungwa jela, hata nikikuletea hoja ya kukata ambayo kwa hiyo utabainika ukweli wangu?»

Verse 31 — Surah Ash-Shuara 26:31

Fir’awn akasema, «Basi ilete ikiwa wewe ni miongoni mwa wakweli katika madai yako.»

Verse 32 — Surah Ash-Shuara 26:32

Hapo Mūsā akaitupa fimbo yake na ikageuka kuwa nyoka wa kikweli, si kiinimacho kama wanavyofanya wachawi

Verse 33 — Surah Ash-Shuara 26:33

Na akautoa mkono wake kwenye uwazi wa kanzu yake uliofunguliwa kifuani au chini ya kwapa lake, na papo hapo ukawa mweupe kama barafu, na sio weupe wa mbalanga, ukawashangaza waangaliaji

Verse 34 — Surah Ash-Shuara 26:34

Fir’awn akasema kuwaambia watukufu wa watu wake, kwa kuogopa wasije wakaamini, «Kwa kweli Mūsā ni mchawi hodari

Verse 35 — Surah Ash-Shuara 26:35

Anataka kuwatoa nyinyi, kwa uchawi wake, kwenye ardhi yenu. Basi mnatoa shauri gani kuhusu yeye nipate kuyafuata maoni yenu?»

Verse 36 — Surah Ash-Shuara 26:36

Watu wake wakamwambia, «Msubirishe Mūsā na Hārūn, na utume askari mijini wawakusanye wachawi

Verse 37 — Surah Ash-Shuara 26:37

Watakujia na kila anayejua uchawi na akawa hodari kuufahamu.»

Verse 38 — Surah Ash-Shuara 26:38

Wakakusanywa wachawi, na wakapangiwa wakati maalumu, nao ni wakati wa mchana wa siku ya Pambo ambayo wanajitenga na shughuli zao, na wanajikusanya na kujipamba, ili wakutane na Mūsā

Verse 39 — Surah Ash-Shuara 26:39

na wawahimize watu kujumuika kwa matarajio kwamba ushindi uwe ni wa wachawi

Verse 40 — Surah Ash-Shuara 26:40

Sisi tunatarajia ushindi uwe ni wa wachawi ili tujikite kwenye dini yetu

Verse 41 — Surah Ash-Shuara 26:41

Na wachawi walipomjia Fir’awn walimwambia, ‘Je, sisi tutakuwa na malipo ya mali au heshima ikiwa tutakuwa ni wenye kumshinda Mūsā?»

Verse 42 — Surah Ash-Shuara 26:42

Fir’awn akasema, «Ndio, nyinyi mtapata kwangu malipo mnayoyataka, na nyinyi hapo mtakuwa ni miongoni mwa wenye kusogezwa karibu na mimi.»

Verse 43 — Surah Ash-Shuara 26:43

Mūsā akasema kuwaambia wachawi, akitaka kuutangua uchawi wao na kuonyesha kuwa kile alichokileta si uchawi, «Tupeni mtakavyovitupa vya uchawi.»

Verse 44 — Surah Ash-Shuara 26:44

Basi wakatupa kamba zao na fimbo zao, na zikawadhihirikia watu kwenye akili zao kuwa ni nyoka wanaotembea, na wakaapa kwa enzi ya Fir’awn kwa kusema, «Sisi ni wenye kushinda.»

Verse 45 — Surah Ash-Shuara 26:45

Hapo akaitupa Mūsā fimbo yake, na papo hapo ikawa ni nyoka mkubwa, akawa anavimeza vile vilivyotokana na wao, hao wachawi, vya uzushi na bandia

Verse 46 — Surah Ash-Shuara 26:46

Waliposhuhudia hilo na wakajua kuwa halitokani na udanganyifu wa wachawi, walimuamini Mwenyezi Mungu na wakamsujudia

Verse 47 — Surah Ash-Shuara 26:47

na wakasema, «Tumemuamini Mola wa viumbe vyote

Verse 48 — Surah Ash-Shuara 26:48

Mola wa Mūsā na Hārūn.»

Verse 49 — Surah Ash-Shuara 26:49

Fir’awn akasema kuwaambia wachawi kwa kukataa, «Mumemkubali Mūsā bila ya idhini yangu!» Na akasema akiashiria kuwa kitendo cha Mūsā ni uchawi, «Yeye ni mkubwa wenu aliyewafundisha nyinyi uchawi, basi mtayajua mateso yatakayowafikia. Nitaikata mikono yenu na miguu yenu kitafauti: kwa kuukata mkono wa kulia na mguu wa kushoto au kinyume chake, na nitawasulubu nyote.»

Verse 50 — Surah Ash-Shuara 26:50

Wachawi walisema kumwambia Fir’awn, «Hakuna madhara ya duniani yatakayotupata, kwa kweli sisi ni wenye kurudi kwa Mola wetu, Atupe neema ya kuendelea

Verse 51 — Surah Ash-Shuara 26:51

Sisi tunataraji Mola wetu Atusamehe makosa yetu ya ushirikina na mengineyo kwa kuwa sisi ndio Waumini wa mwanzo katika watu wako.»

Verse 52 — Surah Ash-Shuara 26:52

Na Mwenyezi Mungu Akampelekea wahyi Mūsā, amani imshukie, kwamba, «Enda usiku pamoja na walioamini miongoni mwa Wana wa Isrāīl, ili Fir’awn na askari wake, ambao watawafuata nyinyi, wasije wakawafikia kabla ya kufika kwenu baharini.»

Verse 53 — Surah Ash-Shuara 26:53

Fir’awn akawatuma askari wake, alipopata habari kwamba Wana wa Isrāīl wameenda usiku, wakusanye jeshi lake kutoka miji ya utawala wake

Verse 54 — Surah Ash-Shuara 26:54

Fir’awn akasema, «Kwa kweli, Wana wa Isrāīl waliokimbia pamoja na Mūsā ni pote twevu lenye idadi ndogo

Verse 55 — Surah Ash-Shuara 26:55

Na wao wamevijaza hasira vifua vyetu kwa kuwa wameenda kinyume na dini yetu na wametoka bila ya idhini yetu

Verse 56 — Surah Ash-Shuara 26:56

na sisi sote tuko macho, tuko tayari nao.»

Verse 57 — Surah Ash-Shuara 26:57

Mwenyezi Mungu Akamtoa Fir’awn na watu wake kwenye ardhi ya Misri yenye mabustani, mabubujiko ya maji

Verse 58 — Surah Ash-Shuara 26:58

hazina za mali na majumba mazuri

Verse 59 — Surah Ash-Shuara 26:59

Na kama tulivyowatoa, tuliwapatia nyumba hizo Wana wa Isrāīl baada yao wao

Verse 60 — Surah Ash-Shuara 26:60

Hivyo basi Fir’awn na askari wake walimkuta Mūsā na waliokuwa pamoja na yeye wakati wa kuchomoza jua

Verse 61 — Surah Ash-Shuara 26:61

Yalipoonana makundi mawili, watu wa Mūsā walisema, «Kwa hakika jumuiko la Fir’awn ni lenye kutufikia na kutuangamiza.»

Verse 62 — Surah Ash-Shuara 26:62

Mūsā alisema kuwaambia, «Sivyo! Mambo si kama mlivyotaja. Hamtafikiwa. Kwa hakika Mwenyezi Mungu Yupo na mimi kwa msaada, Ataniongoza njia ya kuokoka mimi na kuokoka nyinyi.»

Verse 63 — Surah Ash-Shuara 26:63

Hapo tukampelekea wahyi Mūsā kwamba, «Piga bahari kwa fimbo yako!» Akapiga. Na bahari ikapasuka njia kumi na mbili kwa idadi ya kabila za Wana wa Isrāīl. Na kila kipande kilichojitenga na bahari ni kama jabali kubwa

Verse 64 — Surah Ash-Shuara 26:64

Na tulimsogeza karibu Fir’awn na watu wake mpaka wakaingia baharini

Verse 65 — Surah Ash-Shuara 26:65

Na tukamuokoa Mūsā na waliokuwa pamoja na yeye wote. Bahari ikaendelea kuachana kwake (kwa ule mpasuko) mpaka wakavuka kwenye nchi kavu

Verse 66 — Surah Ash-Shuara 26:66

Kisha tukamzamisha Fir’awn na waliokuwa pamoja na yeye kwa kuifanya bahari iwafinike baada ya wao kuingia ndani wakimfuata Mūsā na watu wake

Verse 67 — Surah Ash-Shuara 26:67

Kwa hakika, katika hilo lililotukia pana mazingatio ya ajabu yenye kuonyesha dalili ya uweza wa Mwenyezi Mungu. Na wengi wa wafuasi wa Fir’awn hawakuwa ni wenye kuamini, pamoja na alama hii yenye kushinda

Verse 68 — Surah Ash-Shuara 26:68

Na hakika ya Mola wako Ndiye Mshindi, Ndiye Mwenye kurehemu. Kwa nguvu Zake na ushindi Amewaangamiza makafiri wakanushaji, na kwa rehema Yake Amemuokoa Mūsā na waliokuwa pamoja na yeye wote

Verse 69 — Surah Ash-Shuara 26:69

Na wasimulie makafiri, ewe Mtume, habari ya Ibrāhīm

Verse 70 — Surah Ash-Shuara 26:70

alipomwambia babake na watu wake, «Mnaabudu kitu gani?»

Verse 71 — Surah Ash-Shuara 26:71

Wakasema, «Tunaabudu masanamu, tunaketi na kuendelea kuwaabudu.»

Verse 72 — Surah Ash-Shuara 26:72

Akasema Ibrāhīm akiwatanabahisha uharibifu wa njia yao, «Kwani wanasikia maombi yenu mnapowaomba

Verse 73 — Surah Ash-Shuara 26:73

Au wanawapatia manufaa mkiwaabudu? Au wanawafanya mupate madhara mkiacha kuwaabudu?»

Verse 74 — Surah Ash-Shuara 26:74

Wakasema, «Haliwi lolote katika hayo, lakini tuliwakuta mababa zetu wakiwaabudu, na sisi tukawaiga katika yale ambayo walikuwa wakiyafanya.»

Verse 75 — Surah Ash-Shuara 26:75

Ibrāhīm akasema, «Je, mumefikiria kuvitia akilini hivyo mnavyoviabudu, miongoni mwa masanamu yasiyosikia wala kunufaisha wala kudhuru

Verse 76 — Surah Ash-Shuara 26:76

nyinyi na mababa zenu waliowatangulia

Verse 77 — Surah Ash-Shuara 26:77

Kwani hao mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni maadui zangu. Lakini Mola wa viumbe wote na Mmiliki wa mambo yao, Yeye Peke Yake Ndiye ninayemuabudu

Verse 78 — Surah Ash-Shuara 26:78

Yeye Ndiye Aliyeniumba kwa sura nzuri zaidi. Yeye ananiongoza kwenye maslahi ya dunia na Akhera

Verse 79 — Surah Ash-Shuara 26:79

Na Yeye Ndiye Anayenineemesha kwa chakula na kinywaji

Verse 80 — Surah Ash-Shuara 26:80

Na nikipatikana na ugonjwa, Yeye Ndiye Anayeniponyesha na kuniondolea

Verse 81 — Surah Ash-Shuara 26:81

Na Yeye Ndiye Atakayenifisha duniani kwa kuichukua roho yangu, kisha Atanihuisha Siku ya Kiyama, hakuna awezaye hilo isipokuwa Yeye

Verse 82 — Surah Ash-Shuara 26:82

Na Ambaye ninatarajia Atanisamehe dhambi zangu Siku ya Malipo.»

Verse 83 — Surah Ash-Shuara 26:83

Ibrāhīm akasema akimuomba Mola wake, «Mola wangu! Nitunukie elimu na fahamu, na unikutanishe na watu wema, na unikusanye mimi na wao Peponi

Verse 84 — Surah Ash-Shuara 26:84

«Na unifanye niwe na sifa nzuri na utajo mwema kwa wale watakaokuja baada yangu mpaka Siku ya Kiyama

Verse 85 — Surah Ash-Shuara 26:85

«Na unifanye mimi niwe miongoni mwa waja wako utakaowarithisha starehe za Peponi.»

Verse 86 — Surah Ash-Shuara 26:86

Hii ni dua ya Ibrāhīm, amani imshukiye, ya kumuomba Mwenyezi Mungu Amuokoe babake na upotevu na Ampe uongofu, ili Amghufirie na Amsamehe, kama Ibrāhīm alivyomuahidi babake kumuombea Mungu, na ilipomfunukia kuwa yeye ni mwenye kuendelea kwenye ukafiri na ushirikina mpaka afe alijiepusha naye

Verse 87 — Surah Ash-Shuara 26:87

«Na usinipe unyonge Siku hiyo, ambayo watu watatoka makaburini ili wahesabiwe na walipwe

Verse 88 — Surah Ash-Shuara 26:88

Siku ambayo mali na watoto havitamfaa yoyote miongoni mwa waja

Verse 89 — Surah Ash-Shuara 26:89

isipokuwa yule aliyemjia Mwenyezi Mungu kwa moyo uliyosalimika na ukafiri, unafiki na uovu.»

Verse 90 — Surah Ash-Shuara 26:90

Na Pepo itasogezwa karibu kwa wale waliojiepusha na ukafiri na matendo ya uasi na wakamuelekea Mwenyezi Mungu kwa kumtii

Verse 91 — Surah Ash-Shuara 26:91

Na Moto utaonyeshwa waziwazi kwa makafiri ambao walipotea njia ya uongofu na wakayafanyia ujasiri yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu na wakawakanusha Mitume Wake

Verse 92 — Surah Ash-Shuara 26:92

Na wataambiwa kwa kulaumiwa, «Wako wapi waungu wenu ambao mlikuwa mkiwaabudu

Verse 93 — Surah Ash-Shuara 26:93

badala ya Mwenyezi Mungu na mkidai kwamba wao watawaombea leo? Je, watawanusuru na wawazuilie adhabu isiwafikie au watajinusuru kwa kuikinga adhabu isiwafikie?» Hakuna chochote katika hayo

Verse 94 — Surah Ash-Shuara 26:94

Hapo watakusanywa na watupwe kwenye Jahanamu kwa vichwa vyao, mara baada ya nyingine mpaka watakapotulia humo: wao, wale waliowapoteza

Verse 95 — Surah Ash-Shuara 26:95

na wasaidizi wa Iblisi waliowapambia shari; hakuna yoyote kati yao atakayeponyoka

Verse 96 — Surah Ash-Shuara 26:96

Watasema wakikiri makosa yao, na huku wanagombana, ndani ya Jahanamu, na wale waliowapoteza wao

Verse 97 — Surah Ash-Shuara 26:97

«Tunaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba sisi, duniani, tulikuwa kwenye upotevu ulio waziwazi, haukuwa umefichika

Verse 98 — Surah Ash-Shuara 26:98

tulipowafanya nyinyi kuwa ni sawa na Mola wa viumbe wote, Anayestahiki kuabudiwa, Peke Yake

Verse 99 — Surah Ash-Shuara 26:99

Na hakuna kilichotutia kwenye mwisho huu mbaya isipokuwa ni wahalifu ambao walitulingania tumuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu

Verse 100 — Surah Ash-Shuara 26:100

«Hapana yoyote wa kutuombea na kututoa kwenye adhabu

Verse 101 — Surah Ash-Shuara 26:101

wala mwenye kutupenda kikweli na kutuhurumia

Verse 102 — Surah Ash-Shuara 26:102

«Tunatamani tupatiwe fursa ya kurudi ulimwenguni tupate kuwa miongoni mwa wenye kuamini na kuokolewa.»

Verse 103 — Surah Ash-Shuara 26:103

Hakika katika habari ya Ibrāhīm iliyotangulia kuna mazingatio kwa mwenye kuzingatia. Na wengi wenye kuisikia habari hii hawakuwa ni wenye kuamini

Verse 104 — Surah Ash-Shuara 26:104

Na kwa hakika, Mola wako Ndiye Mshindi Aliye Muweza wa kuwalipiza wakanushaji, Ndiye Mwenye kuwarehemu waja Wake Waumini

Verse 105 — Surah Ash-Shuara 26:105

Waliukanusha watu wa Nūḥ ujumbe wa Nabii wao. Wakawa, kwa kufanya hivyo, ni wakanushaji wa Mitume wote, kwa kuwa kila Mtume anaamrisha kuwaamini Mitume wote

Verse 106 — Surah Ash-Shuara 26:106

Kumbuka pindi aliposema kuwaambia wao ndugu yao Nūḥ, «Je, hamumuogopi Mwenyezi Mungu kwa kuacha kumuabudu asiyekuwa Yeye

Verse 107 — Surah Ash-Shuara 26:107

Mimi kwenu nyinyi ni Mtume muaminifu katika yale ninayowafikishia

Verse 108 — Surah Ash-Shuara 26:108

Basi ifanyeni Imani kuwa ndio kinga yenu na adhabu ya Mwenyezi Mungu, na nitiini mimi katika yale ninayowaamrisha ya kumuabudu Yeye Peke Yake

Verse 109 — Surah Ash-Shuara 26:109

na sitaki kutoka kwenu malipo yoyote ya kuufikisha ujumbe, malipo yangu hayako juu ya yoyote isipokuwa Mola wa viumbe wote, Mwenye kuendesha mambo ya viumbe Vyake

Verse 110 — Surah Ash-Shuara 26:110

Basi jihadharini na mateso Yake na mnitii mimi kwa kufuata amri Zake na kujiepusha na makatazo Yake.»

Verse 111 — Surah Ash-Shuara 26:111

Watu wake wakamwambia, «Vipi tutakuamini na tutakufuata na hali hao waliokufuata ni watu wanyonge na wale wa hali ya chini miongoni mwao?»

Verse 112 — Surah Ash-Shuara 26:112

Nūḥ, amani imshukie, aliwajibu kwa kusema, «Sikupewa jukumu la kujua matendo yao. Jukumu nililopewa ni kuwalingania wao kwenye Imani. Na linalozingatiwa ni Imani, na sio cheo, ukoo, kazi na ujuzi wa sanaa

Verse 113 — Surah Ash-Shuara 26:113

«Hesabu yao, ili walipwe kwa matendo yao na yaliyomo ndani ya nafsi zao, ni juu ya Mola wangu Anayeona na kujua siri zote. Lau mnatambua hilo hamngalisema maneno haya

Verse 114 — Surah Ash-Shuara 26:114

«Na mimi si mwenye kuwafukuza wale wanaouamini ulinganizi wangu, namna itakavyokuwa hali yao, kwa kufuata matakwa yenu, ili mniamini

Verse 115 — Surah Ash-Shuara 26:115

Mimi sikuwa isipokuwa ni mwonyaji ambaye onyo lake liko wazi.»

Verse 116 — Surah Ash-Shuara 26:116

Hapo watu wa Nūḥ waliacha kubishana na wakaamua kutoa vitisho, hivyo basi wakamuambia, «Usiporudi nyuma, ewe Nūḥ, ukaacha huo ulinganizi wako, utakuwa ni miongoni mwa wenye kuuawa kwa kupigwa mawe.»

Verse 117 — Surah Ash-Shuara 26:117

Nūḥ aliposikia neno lao hili, alimuomba Mola wake kwa kusema, «Mola wangu! Kwa hakika watu wangu wameamua kuendelea kunikanusha

Verse 118 — Surah Ash-Shuara 26:118

basi amua baina yangu na wao uamuzi wa kumwangamiza mwenye kukataa kukupwekesha na akamkanusha Mtume wako. Na uniokoe mimi, na Waumini walio pamoja na mimi, na adhabu utakayowaadhibu makafiri.»

Verse 119 — Surah Ash-Shuara 26:119

Basi tukamuokoa na wale walio pamoja na yeye katika jahazi iliyojazwa aina mbalimabali za viumbe alivyovibeba pamoja na yeye

Verse 120 — Surah Ash-Shuara 26:120

Kisha tukawazamisha, baada ya kumuokoa Nūḥ na wale waliokuwa pamoja na yeye, wale waliosalia kati ya wale ambao hawakuamini na wakaukataa ushauri aliyowapa

Verse 121 — Surah Ash-Shuara 26:121

Hakika katika maelezo ya Nūḥ na yale yaliyokuwa ya kuokolewa Waumini na kuangamizwa wakanushaji ni alama na ni zingatio kubwa kwa waliokuja baada yao. Na wengi wa wale waliokisikia kisa hiki hawakuwa ni wenye kumuamini Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na sheria Zake

Verse 122 — Surah Ash-Shuara 26:122

Na kwa kweli Mola wako Ndiye Mshindi katika kuwatesa waliomkanusha na wakaenda kinyume na amri Yake, Mwenye rehema kwa waja Wake walioamini

Verse 123 — Surah Ash-Shuara 26:123

Walimkanusha watu wa kabila la ‘Ād Mtume wao Hūd, amani imshukiye, na kwa hivyo wakawa ni wakanushaji wa Mitume wote, kwa kuwa ulinganizi wao ni mmoja katika misingi yake na malengo yake

Verse 124 — Surah Ash-Shuara 26:124

Alipowaambia ndugu yao Hūd, «Je, hamumchi MwenyeziMungu mukamtakasia ibada

Verse 125 — Surah Ash-Shuara 26:125

Mimi nimetumwa kwenu niwaongoze na niwaonyeshe njia, ni mtunzi wa ujumbe wa Mwenyezi Mungu, ninaufikisha kwenu kama Alivyoniamrisha Mola wangu

Verse 126 — Surah Ash-Shuara 26:126

Basi iogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu na mnitii mimi katika kile ninachowaitia nyinyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu

Verse 127 — Surah Ash-Shuara 26:127

na sitaki kutoka kwenu, kwa kuwaongoza nyinyi kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu, aina yoyote ya malipo. Malipo yangu hayako juu ya yoyote isipokuwa Mola wa viumbe wote

Verse 128 — Surah Ash-Shuara 26:128

«Je mnajenga kila mahali palipoinuka jengo refu mkawa mnatazama kutoka hapo na mnawacheza shere wapita njia? Huo ni upuuzi na upitaji kiasi, na hauwaletei nyinyi faida yoyote katika dini au katika dunia

Verse 129 — Surah Ash-Shuara 26:129

Na mnafanya majumba imara na ngome zilizojengwa madhubuti, kama kwamba nyinyi mtakaa milele duniani na hamtakufa

Verse 130 — Surah Ash-Shuara 26:130

Na mnapomshika mtu kwa nguvu na mkamakinika kumuua au kumpiga, basi mnalifanya hilo kwa kutendesha nguvu hali ya kufanya maonevu

Verse 131 — Surah Ash-Shuara 26:131

«Basi muogopeni Mwenyezi Mungu na mkifuate kile ninachowalingania, kwani hilo lina nafuu zaidi kwenu

Verse 132 — Surah Ash-Shuara 26:132

na mcheni Mwenyezi Mungu Aliyewapa aina mbalimbali za neema zisizofichika kwenu

Verse 133 — Surah Ash-Shuara 26:133

Amewapa wanyama hawa: ngamia ng’ombe, mbuzi na kondoo, na Amewapa watoto

Verse 134 — Surah Ash-Shuara 26:134

na Amewapa mabustani yenye matunda, na Amewatolea maji kwenye chemchemi zinazopita

Verse 135 — Surah Ash-Shuara 26:135

Hūd, amani imshukiye, akasema akiwatahadharisha wao, «Mimi ninaogopa , mkiendelea na yale mliyo nayo ya ukanushaji, uonevu na kuzikufuru neema, asije Mwenyezi Mungu Akawateremshia nyinyi adhabu katika Siku ambayo shida yake ni kubwa kwa kitisho cha adhabu yake

Verse 136 — Surah Ash-Shuara 26:136

Wakamwambia, «Ni sawa kwetu kutukumbusha, kututisha na kuacha kufanya hivyo, hatutakuamini

Verse 137 — Surah Ash-Shuara 26:137

Na wakasema, «Haikuwa dini hii tuliyonayo isipokuwa ni dini ya watu wa mwanzo na desturi zao

Verse 138 — Surah Ash-Shuara 26:138

na sisi si wenye kuadhibiwa kwa tunalolifanya katika yale ambayo unatuonya nayo ya adhabu.»

Verse 139 — Surah Ash-Shuara 26:139

Wakaendelea kumkanusha, na Mwenyezi Mungu Akawaangamiza kwa upepo wa baridi ulio mkali. Kwa hakika, katika kuangamiza huko kuna mazingatio kwa wanaokuja baada yao, na hawakuwa wengi wao, wale waliokisikia kisa chao, ni wenye kukuamini wewe

Verse 140 — Surah Ash-Shuara 26:140

Hakika Mola wako Ndiye Mwenye nguvu, Mshindi kwa anayoyataka ya kuwaangamiza wakanushaji, Mwenye huruma kwa Waumini

Verse 141 — Surah Ash-Shuara 26:141

Watu wa kabila la Thamūd waliukanusha ujumbe wa Mtume wao Ṣāliḥ na wakaukanusha mwito wake wa kumpwekesha Mwenyezi Mungu, na kwa hivyo wakawa wamewakanusha Mitume wote, kwa kuwa wao wote wanalingania kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu

Verse 142 — Surah Ash-Shuara 26:142

Pindi alipowaambia wao ndugu yao Ṣāliḥ»Je, hamuogopi mateso ya Mwenyezi Mungu, mkampwekesha kwa ibada

Verse 143 — Surah Ash-Shuara 26:143

Mimi nimetumilizwa kwenu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ni mwenye kuutunza ujumbe huu kama nilivyoupokea kutoka kwa Mwenyezi Mungu

Verse 144 — Surah Ash-Shuara 26:144

Basi jihadharini na mateso Yake, Aliyetukuka, na fuateni kile nilichowalingania mkifuate

Verse 145 — Surah Ash-Shuara 26:145

Na mimi sitaki malipo kwa kuwashauri na kuwaongoza, malipo yangu hayako isipokuwa kwa Mola wa viumbe wote

Verse 146 — Surah Ash-Shuara 26:146

«Je, Awaache Mola wenu katika starehe mlizonazo, hali ya kuwa mumetulia katika dunia hii mkiwa mumesalimika na adhabu na kuondoka na kufa

Verse 147 — Surah Ash-Shuara 26:147

Mkiwa kwenye mabustani yenye matunda, chemchemi zinazopita

Verse 148 — Surah Ash-Shuara 26:148

nafaka nyingi na mitende ambayo matunda yake yamestawi, yamelainika na yameiva

Verse 149 — Surah Ash-Shuara 26:149

na mnachonga kutoka kwa majabali majumba hali ya kuwa ni wamahiri wa kuyachonga, mkiwa na kiburi na majivuno.»

Verse 150 — Surah Ash-Shuara 26:150

Basi ogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu na mkubali ushauri wangu

Verse 151 — Surah Ash-Shuara 26:151

na msiandame amri ya wenye kuzidhulumu nafsi zao, waliokolea katika kumuasi Mwenyezi Mungu

Verse 152 — Surah Ash-Shuara 26:152

waliozoea kufanya uharibifu kwenye ardhi, uharibifu usiotengenezeka

Verse 153 — Surah Ash-Shuara 26:153

Watu wa Thamūd walimwambia Nabii wao Ṣāliḥ, «Wewe hukuwa isipokuwa ni miongoni mwa wale waliofanyiwa uganga wa uchawi mwingi, mpaka uchawi ukaathiri akili yako

Verse 154 — Surah Ash-Shuara 26:154

Hukuwa wewe isipokuwa ni mmoja wa wanadamu unaofanana na sisi katika ubinadamu, basi vipi utakuwa tafauti na sisi kwa utume? Basi leta hoja wazi inayoonyesha kuwa utume wako umethibiti, iwapo wewe ni mkweli katika madai yako kwamba Mwenyezi Mungu Amekutumiliza kwetu.»

Verse 155 — Surah Ash-Shuara 26:155

Ṣāliḥ akasema kuwaambia- na hapo alikuwa amewaletea ngamia ambaye Mwenyezi Mungu alimtolea kwenye jiwe-, «Huyu ni ngamia wa Mwenyezi Mungu. Yeye ana hisa ya maji siku maalumu, na nyinyi mna hisa ya maji kwa siku nyingine. Haifai kwenu nyinyi kunywa siku ile ambayo ni hisa yake, na yeye hatakunywa siku ambayo ni hisa yenu

Verse 156 — Surah Ash-Shuara 26:156

Na msimguse kwa kitu chochote cha kumdhuru, kama kipigo au mauaji au mfano wake, kwani mkifanya hivyo, Mwenyezi Mungu Atawaangamiza nyinyi kwa adhabu ya Siku ambayo shida yake ni kubwa kwa sababu ya papatiko litakalotukia Siku hiyo na shida

Verse 157 — Surah Ash-Shuara 26:157

Basi wakamchinja ngamia, wakawa ni wenye kujuta kwa walilolifanya walipokuwa na uhakika kuwa watashukiwa na adhabu, na majuto yao yasiwafae kitu

Verse 158 — Surah Ash-Shuara 26:158

Basi adhabu ya Mwenyezi Mungu ikawashukia, ile ambayo Ṣāliḥ, amani imshukiye, aliwaahidi nayo, na ikawaangamiza. Kwa hakika, katika kuwaangamiza watu wa Thamūd pana mazingatio kwa mwenye kuuzingatia mwisho huu; na wengi wao hawakuwa ni wenye kuamini

Verse 159 — Surah Ash-Shuara 26:159

Na kwa hakika Mola wako Ndiye Mshindi, Mwenye kutendesha nguvu, Mwenye kuwatesa maadui Wake, Mwenye huruma kwa walioamini miongoni mwa viumbe Wake

Verse 160 — Surah Ash-Shuara 26:160

watu wa Lūṭ waliukanusha utume wake, wakawa kwa hilo ni wakanushaji wa Mitume waliosalia, kwa kuwa lile walilolileta la kumpwekesha Mwenyezi Mungu na misingi ya Sheria ni moja

Verse 161 — Surah Ash-Shuara 26:161

Pindi ndugu yao Lūṭ alipowaambia, «Je, hamuogopi adhabu ya Mwenyezi Mungu

Verse 162 — Surah Ash-Shuara 26:162

Mimi ni mjumbe kutoka kwa Mola wenu aliye muaminifu juu ya utekelezaji wa ujumbe Wake kwenu

Verse 163 — Surah Ash-Shuara 26:163

Basi jihadharini na mateso ya Mwenyezi Mungu kwa kumkanusha kwenu mjumbe Wake, na nifuateni mimi katika yale ninayowalingania

Verse 164 — Surah Ash-Shuara 26:164

Na siwaombi malipo yoyote juu ya ulinganizi wangu wa kuwaongoza, malipo yangu hayako isipokuwa kwa Mola wa viumbe wote

Verse 165 — Surah Ash-Shuara 26:165

«Mnawaingilia binadamu wanaume

Verse 166 — Surah Ash-Shuara 26:166

na mnawaacha wake zenu ambao Mwenyezi Mungu Amewaumbia nyinyi ili mstarehe na mzaane? Lakini nyinyi ni watu, kwa uasi huu, wenye kuyakiuka yale ambayo Mwenyezi Mungu Amewaruhusu ya halali na kuyaendea ya haramu.»

Verse 167 — Surah Ash-Shuara 26:167

Watu wa Lūṭ wakasema, «Usipoacha, ewe Lūṭ, kutukataza kuwajia wanaume na kukichafua kitendo hicho (cha kuwajia wanaume), utakuwa ni miongoni mwa wenye kufukuzwa kutoka miji yetu.»

Verse 168 — Surah Ash-Shuara 26:168

Lūṭ akasema kuwaambia wao, «Mimi ni miongoni mwa wale wanaokichukia sana kitendo chenu mnachokifanya cha kuwajia wanaume.»

Verse 169 — Surah Ash-Shuara 26:169

Kisha Lūṭ akamuomba Mola wake, alipokata tamaa kuwa watamsikiliza, alisema, «Mola wangu! Niokoe mimi na uwaokoe jamaa zangu na kile wanachokifanya watu wangu cha uasi huu mchafu na (utuokoe na) adhabu yako itakayowapata.»

Verse 170 — Surah Ash-Shuara 26:170

Basi tukamuokoa yeye na watu wa nyumbani kwake na wale wote walioukubali ulinganizi wake

Verse 171 — Surah Ash-Shuara 26:171

isipokuwa mkongwe miongoni mwa watu wa nyumbani kwake, naye ni mke wake ambaye hakushirikiana na wao katika kuamini, hivyo basi akawa ni mwenye kusalia kwenye adhabu na maangamivu

Verse 172 — Surah Ash-Shuara 26:172

Kisha tukawaangamiza wasiokuwa wao, miongoni mwa makafiri, kuwaangamiza kukubwa

Verse 173 — Surah Ash-Shuara 26:173

na tukawateremshia wao mawe kutoka juu kama mvua yakawaangamiza. Ilikuwa mvua mbaya sana ya wale walioonywa na Mitume wao na wasiwakubalie. Kwa hakika, wao wameteremshiwa aina mabaya zaidi za maangamivu na uvunjaji

Verse 174 — Surah Ash-Shuara 26:174

Kwa hakika, katika mateso hayo yaliyowateremkia watu wa Lūṭ pana mazingatio na mawaidha ya kuwafanya wenye kukanusha wawaidhike. Na wengi wao hawakuwa ni wenye kuamini

Verse 175 — Surah Ash-Shuara 26:175

Na kwa kweli Mola wako Ndiye Mshindi Mwenye nguvu ya kuweza kuwashurutisha wakanushaji, Mwenye huruma kwa waja Wake wema

Verse 176 — Surah Ash-Shuara 26:176

Walimkanusha watu wa nchi yenye miti iliyoshikana Mtume wao Shu’ayb kuhusu utume wake, na kwa hivyo waliukua wamekanusha jumbe zote za Mitume

Verse 177 — Surah Ash-Shuara 26:177

Alipowaambia wao Shu’ayb, «Je, hamuogopi kuwa Mwenyezi Mungu Atawatesa kwa ushirikina wenu na kufanya kwenu matendo ya uasi

Verse 178 — Surah Ash-Shuara 26:178

Mimi nimetumilizwa kwenu kutoka kwa Mwenyezi Mungu niwaongoe, ni mtunzi wa kile alichoniletea mimi Mwenyezi Mungu cha wahyi wa utume

Verse 179 — Surah Ash-Shuara 26:179

Basi yaogopeni mateso ya Mwenyezi Mungu na mkifuate kile ninachowaitia cha uongofu wa Mwenyezi Mungu mupate kuongoka

Verse 180 — Surah Ash-Shuara 26:180

Na sitaki kwenu, kwa kule kuwalingania kwangu kwenye kumuamini Mwenyezi Mungu, malipo yoyote. Malipo yangu hayako isipokuwa kwa Mola wa viumbe wote.”

Verse 181 — Surah Ash-Shuara 26:181

Shu’ayb akaendelea kuwaambia- na walikuwa wakipunguza vipimo na mizani-, «Watimizieni watu vipimo kwa kuwakamilishia, na msiwe ni kati ya wale wanaowapunja watu haki zao

Verse 182 — Surah Ash-Shuara 26:182

na mpime kwa mizani ya uadilifu iliyolingana sawa

Verse 183 — Surah Ash-Shuara 26:183

na msiwapunje watu chochote katika haki zao kwenye vipimo au mizani au vinginevyo, na msizidishe uharibifu katika ardhi kwa kufanya ushirikina, kuua, kunyang’anya, kuwatisha watu na kutekeleza vitendo vya uasi

Verse 184 — Surah Ash-Shuara 26:184

«Na jihadharini na mateso ya Mwenyezi Mungu Aliyewaumba na Akawaumba watu wa mataifa yaliyowatangulia.»

Verse 185 — Surah Ash-Shuara 26:185

Wakasema, «Ukweli ni kwamba wewe, ewe Shu’ayb, ni miongoni mwa wale waliopatwa na uchawi ukawashika sana ukawaondoa akili zao

Verse 186 — Surah Ash-Shuara 26:186

Na wewe hukuwa isipokuwa ni mfano wetu sisi katika ubinadamu, basi vipi utahusika peke yako kwa utume bila ya sisi? Na kwa kweli, dhana yetu kubwa kuhusu wewe ni kuwa wewe ni miongoni mwa warongo katika kile unachokidai cha utume

Verse 187 — Surah Ash-Shuara 26:187

Iwapo wewe ni mkweli katika madai yako ya utume, basi muombe Mwenyezi Mungu Atuangushie vipande vya adhabu kutoka mbinguni vitumalize.»

Verse 188 — Surah Ash-Shuara 26:188

Shu’ayb akawaambia wao, «Mola wangu Anayajua zaidi yale mnayoyafanya ya ushirikina na uasi na mateso mnayostahili.»

Verse 189 — Surah Ash-Shuara 26:189

Wakaendelea kumkanusha, likawapata wao joto kali, wakawa wanatafuta mahali pa hifadhi ili wajifinike. Kikawafinika kiwingu, kikawapatia ubaridi na upepo laini, na walipokusanyika chini yake, moto uliwawakia na ukawachoma, basi hapo yakawa maangamivu yao wote katika siku yenye kitisho kikali

Verse 190 — Surah Ash-Shuara 26:190

Hakika katika mateso hayo yaliyowashukia kuna ushahidi wazi juu ya uweza wa Mwenyezi Mungu katika kuwapatiliza wakanushaji kwa adhabu na kuna mazingatio kwa mwenye kuzingatia. Na hawakuwa wengi wao ni wenye kuamini na kuwaidhika kwa hayo

Verse 191 — Surah Ash-Shuara 26:191

Na kwa hakika, Mola wako, ewe Mtume, Ndiye Yeye Aliye Mshindi katika kuwatesa Kwake wale Anaowatesa miongoni mwa maadui Wake, Ndiye Anayewarehemu waja Wake wanaompwekesha

Verse 192 — Surah Ash-Shuara 26:192

Na kwa hakika, hii Qur’ani ambayo ndani yake zimetajwa habari hizi za kweli imeteremshwa na Muumba viumbe na Mmiliki wa mambo yote

Verse 193 — Surah Ash-Shuara 26:193

Jibrili muaminifu ameshuka nayo

Verse 194 — Surah Ash-Shuara 26:194

akakusomea mpaka ukaikusanya moyoni mwako, kwa kuihifadhi na kuielewa, upate kuwa ni mmoja wa wajumbe wa Mwenyezi Mungu wenye kuwafanya watu wao waogope mateso ya Mwenyezi Mungu, upate kuwaonya, kwa Teremsho hili, binadamu na majini wote

Verse 195 — Surah Ash-Shuara 26:195

Ameshuka nayo Jibrili kwako kwa lugha ya Kiarabu yenye maana yaliyo wazi, yenye ushahidi unaoonekena, ikikusanya kile wanachokihitajia cha kutengeneza mambo ya Dini yao na dunia yao

Verse 196 — Surah Ash-Shuara 26:196

Na kwa hakika, utajo wa hii Qur’ani umethibitishwa katika Vitabu vya Manabii waliotangulia, vimeibashiri na kukubali kuwa ni ya kweli

Verse 197 — Surah Ash-Shuara 26:197

Je, haiwatoshi hawa kuwa ni ushahidi kwamba wewe ni mtume wa Mwenyezi Mungu na kwamba Qur’ani ni kweli kuwa wasomi wa Wana wa Isrāīl wana ujuzi wa usahihi wa hilo na wale walioamini miongoni mwao kama ‘Abdullāh bin Sallām

Verse 198 — Surah Ash-Shuara 26:198

Na lau tungaliiteremsha Qur’ani kwa baadhi ya wale wasiozungumza lugha ya Kiarabu

Verse 199 — Surah Ash-Shuara 26:199

wakawasomea makafiri wa Kikureshi kisomo cha Kiarabu kilicho sawa, wangaliikanusha pia na wangalizua sababu ya ukanushaji wao

Verse 200 — Surah Ash-Shuara 26:200

Hivyo ndivyo tulivyotia ndani ya nyoyo za wahalifu kuikanusha Qur’ani na hilo likawa limejikita ndani ya hizo nyoyo

Verse 201 — Surah Ash-Shuara 26:201

na hii ikawa ni sababu ya udhalimu wao na uhalifu wao. Basi hapana njia ya wao kubadilika kwa kuyaacha waliyonayo ya kuikanusha Qur’ani mpaka waishuhudie adhabu kali walioahidiwa

Verse 202 — Surah Ash-Shuara 26:202

Hapo adhabu iwashukie ghafla na hali wao hawajui kuja kwake kabla ya hapo

Verse 203 — Surah Ash-Shuara 26:203

na hapo waseme, watakaposhtushwa nayo, kwa majuto ya Imani iliyotupita tukaikosa, «Je, sisi ni wenye kupatiwa nafasi na kucheleweshwa tupate kutubia kwa Mwenyezi Mungu ushirikina wetu na tuyapatilize yaliyotupita?»

Verse 204 — Surah Ash-Shuara 26:204

Je, hawa wamedanganyika na kule kuwapa muhula kwangu ndipo wakawa wanataka kuteremka adhabu kwa haraka juu yao kutoka mbinguni

Verse 205 — Surah Ash-Shuara 26:205

Je, umejua, ewe Mtume, lau tungaliwastarehesha kwa uhai wa miaka mingi kwa kuwacheleweshea muda wao wa kuishi

Verse 206 — Surah Ash-Shuara 26:206

kisha iwashukie adhabu ilioahidiwa

Verse 207 — Surah Ash-Shuara 26:207

Hakutawafaa kitu kule kustarehe kwao kwa umri mrefu na maisha mazuri wasipotubia kutokana na ushirikina wao. Basi adhabu ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuwashukia hivi karibuni (ulimwenguni) au baadaye (huko Akhera)

Verse 208 — Surah Ash-Shuara 26:208

Na hatukuuangamiza mji wowote, miongoni mwa miji katika mataifa yote, isipokuwa baada ya kuwatumiliza Mitume kwao wawaonye

Verse 209 — Surah Ash-Shuara 26:209

ili wawe ni makumbusho kwao na uzindushi wa yale yenye uokofu kwao. Na hatukuwa ni wenye kudhulumu kwa kuwaadhibu watu kabla ya kuwapelekea Mtume

Verse 210 — Surah Ash-Shuara 26:210

Na Qur’ani hawakuiteremsha mashetani kwa Muhammad, kama wanavyodai makafiri

Verse 211 — Surah Ash-Shuara 26:211

na hilo halifai kutoka kwao na wala hawaliwezi

Verse 212 — Surah Ash-Shuara 26:212

kwa kuwa wao ni wenye kuzuiliwa kuisikiliza Qur’ani kutoka mbinguni, ni wenye kupigwa na vimondo

Verse 213 — Surah Ash-Shuara 26:213

Hivyo basi usiabudu, pamoja na Mwenyezi Mungu, muabudiwa yoyote asiyekuwa Yeye, ufanyapo hivyo utateremkiwa na adhabu ile iliyowashukia hawa walioabudu, pamoja na Mwenyezi Mungu, asiyekuwa Yeye

Verse 214 — Surah Ash-Shuara 26:214

Na watahadharishe, ewe Muhammad, watu wako wa karibu, ukianzia na wale walio karibu na wewe zaidi, isije adhabu yetu ikawashukia

Verse 215 — Surah Ash-Shuara 26:215

Na uwe laini wa mwenendo na maneno, kwa unyenyekevu na huruma, kwa yule ambaye imekufunukia kutoka kwake kuitika mwito wako

Verse 216 — Surah Ash-Shuara 26:216

Basi wakienda kinyume na amri yako na wasikufuate, jiepushe na vitendo vyao na yale waliyonayo ya ushirikina na upotevu

Verse 217 — Surah Ash-Shuara 26:217

Na Umuachie jambo lako Mwenyezi Mungu, Aliye Mshindi Ambaye hakuna wa kushindana na Yeye wala wa kumlazimisha, Mwenye kurehemu Ambaye Hawaachi wenye kumtegemea

Verse 218 — Surah Ash-Shuara 26:218

Na Ambaye Anakuona unaposimama kuswali ukiwa peke yako ndani ya usiku

Verse 219 — Surah Ash-Shuara 26:219

Na Anaona vile unavyogeuka, pamoja na wenye kumsujudia katika Swala zao wakiwa na wewe, ukiwa katika hali ya kusimama, kurukuu na kusujudu na kuketi

Verse 220 — Surah Ash-Shuara 26:220

Hakika Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Anayesikia kusoma kwako na kumtaja kwako, Ndiye Anayejua nia yako na matendo yako

Verse 221 — Surah Ash-Shuara 26:221

Je, niwapashe habari, enyi watu, ni nani ambaye mashetani wanamshukia

Verse 222 — Surah Ash-Shuara 26:222

Wanamshukia kila mwingi wa urongo, mwingi wa madhambi miongoni mwa makuhani

Verse 223 — Surah Ash-Shuara 26:223

Mashetani wanasikiliza kwa kuiba, wanayanyakuwa maneno kutoka sehemu za juu wakawatupia makuhani na wale wanaokuwa na mwenendo wao miongoni mwa watu wenye matendo mabaya. Na wengi wa hawa ni warongo, kwani mmoja wao husema kweli katika neno moja na akaongeza juu yake maneno mia moja ya urongo

Verse 224 — Surah Ash-Shuara 26:224

Na washairi, mashairi yao yanasimama juu ya ubatilifu na urongo, na wanafuatana na wao wapotevu waliopotoka kama wao

Verse 225 — Surah Ash-Shuara 26:225

Kwani huoni, ewe Nabii, kwamba wao wanaenda kama mtu aliyekosa mwelekeo, wanavama ndani ya kila aina ya fani za urongo, uzushi, uvunjaji heshima, kutukana nasaba na kuwataja vibaya wanawake waliojihifadhi

Verse 226 — Surah Ash-Shuara 26:226

na kwamba wao wanayasema wasiyoyatenda, wanapita mipaka katika kuwasifu watu wa ubatilifu na wanawatia kasoro watu wa haki

Verse 227 — Surah Ash-Shuara 26:227

Mwenyezi Mungu amewavua, kati ya hao washairi, wale washairi walioongoka kwa kuamini na kufanya matendo mema, na wakamtaja Mwenyezi Mungu kwa wingi, wakatunga mashairi juu ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, na kumsifu Yeye, Mwenye utajo mtukufu, na kumtetea Mtume Wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wakasema maneno ya busara yenye mawaidha na adabu nzuri, na wakaunusuru Uislamu wakawa wanamtukana anayeutukana au anayemtukana Mtume wake kwa kuwarudi washairi makafiri. Na watajua wale waliozidhulumu nafsi zao kwa ushirikina na matendo ya uasi, wakawadhulumu wasiokuwa wao kwa kuwanyima haki zao au kuwafanyia uadui au tuhuma za urongo, ni marejeo gani ya shari na maangamivu watakayorejea. Kwa kweli, hayo ni mageuko mabaya. Tunamuomba Mwenyezi Mungu salama na afya