Na nyota iliyo mbinguni na miti ya ardhini, vinamjua Mola wao, vinamsujudia na vinanyosha shingo zao kufuata vile ambavyo vimepangiwa vifuate vya maslahi ya waja Wake na manufaa yao
Bas ni neema gani za Mola wenu, za kidini na za kidunia, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha? Na ni jawabu nzuri ilioje ya majini alipowasomea wao Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, sura hii, kila akipita kwenye aya hii walikuwa wakisema, «Hakuna chochote miongoni mwa neema zako, ewe Mola wetu, tunachokanusha. Sifa njema zote ni zako.» Na hivi ndivyo inavyotakiwa kwa mja anapoelezewa neema za Mwenyezi Mungu na mema Yake akubali na amshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema hizo
Mola wa pande mbili za Mashariki ya jua, katika kusi na kaskazi, na Mola wa pande mbili za Magharibi ya jua, katika kusi na kaskazi, kwani vyote viko chini ya uendeshaji Wake na ulezi Wake
Ni Yake Yeye, Aliyetakasika na kutukuka, mamlaka ya kuyaendesha majahazi makubwa yanayotembea baharini kwa manufaa ya watu, yenye kusimamisha juu milongoti yake na matanga yake kama vile majabali
na utasalia uso wa Mola wako Mwenye utukufu, ubora, kheri nyingi na upaji. Katika aya hii pana kuthibitisha sifa ya uso kwa Mwenyezi Mungu kwa namna inavyonasibiana na Yeye, kutakasika ni Kwake, bila kufananisha wala kueleza namna ulivyo
Wanamuomba Yeye walioko mbinguni na ardhini haja zao. Hakuna yoyote anayejitosheleza kutomhitajia Yeye, kutakasika ni Kwake. Kila siku Yeye Yuko kwenye jambo: Anatukuza na Anatweza, Anatoa na Anazuia
Nitawatengea kipindi cha kuwahesabu na kuwalipa kwa matendo yenu mliyoyafanya, enyi vizito viwili:-majini na binadamu-, tuwatese watu wa maasia na tuwape malipo mema watu wa utiifu
Enyi mkusanyiko wa majini na binadamu! Mkiweza kuihepa amri ya Mwenyezi Mungu na uamuzi Wake kwa kukimbia kwenye pambe za mbingu na ardhi basi fanyeni, na hamuwezi kufanya hivyo isipokuwa kwa nguvu na hoja na amri inayotoka kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. (Na vipi mtaweza kufanya hivyo na hali nyinyi hamzimilikii nafsi zenu manufaa yoyote wala madhara)
Na pindi mbingu itakapopasuka na kuachana Siku ya Kiyama, ikawa nyekundu kama rangi ya waridi na kama mafuta yaliyochemshwa na risasi iliyoyayushwa, kutokana na mambo magumu na vituko vya Siku ya Kiyama
mara wanaadhibiwa kwenye Jaḥīm, na mara nyingine wananyweshwa Hāmīm, nacho ni kinywaji kilichofikia upeo wa ukali wa moto, kinakata tumbo na sehemu za ndani ya mbavu
Na anayemcha Mwenyezi Mungu, miongoni mwa waja Wake binadamu na majini, akaogopa kusimama kwake mbele Yake, akamtii na akaacha kumuasi atakuwa na mabustani mawili ya Pepo
Na wale wanaoogopa kusimama mbele ya Mola Wao watakuwa na mabustani mawili ya Pepo, ambayo ndani yake watastarehe, hali ya kutegemea juu ya matandiko yaliyojazwa dibaji nzito. Na matunda ya mabustani mawili hayo ya pepo yako karibu nao
Katika matandiko hayo wapo wake macho yao yanawatazama waume zao tu, hawawatazami wengineo, wamefungamana na wao. Hakuna aliyewaingilia, kabla ya hao waume zao, binadamu yoyote wala jini
Zimekithiri mno baraka za Jina la Mola wako, na kheri Zake zimekuwa nyingi, Mwenye haiba kubwa, utukufu wenye kukamilika na takrima kwa wenye kumtegemea Yeye