Sisi tumemuumba binadamu kutokana na tone la manii la mchanganyiko wa maji ya mwanamume na maji ya mwanamke, ili tumtahini kwa lazima za kisheria baadaye, hivyo basi tumfanya ni mwenye masikio ya kusikia na macho ya kuonea, apate kuzisikia aya na kuziona dalili
Sisi tumembainishia na kumfahamisha njia ya uongofu na upotevu na wema na ubaya ili awe ima ni mwenye kuamini na kushukuru. Au awe ni mwenye kukanusha na kukataa
Hakika watu wa utiifu na ukweli wa Imani wanaotekeleza haki za Mwenyezi Mungu, watakunywa, Siku ya Kiyama, kutoka kwenye kikombe ambacho ndani yake mna Pombe lililochanganywa na aina bora kabisa ya harufu nzuri, nayo ni maji ya kafuri
Hao walikuwa huko duniani wanatekeleza kile walichojilazimisha nafsi zao cha utiifu kwa Mwenyezi Mungu, na wakiogopa mateso ya Mwenyezi Mungu, Siku ya Kiyama, ambayo madhara yake ni hatari na ubaya ni wenye kusambaa na kuenea kwa watu isipokuwa wale ambao Mwenyezi Mungu Amewarehemu
Na wanalisha chakula, pamoja na kuwa wanakipenda na kukihitajia, kumpa fukara asiyeweza kuchuma, asiyemiliki chochote katika vitu vya kilimwengu, na kumpa mtoto aliyefiliwa na babake kabla ya kubaleghe na asiye na mali, na kumpa mtu aliyetekwa vitani miongoni mwa washirikina na wengineo
na huku wanasema katika nafsi zao, «Hakika sisi tunawafanyia wema kwa kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu na kutaka malipo yake. Hatutaki badala wala hatukusudii kushukuriwa wala kusifiwa na nyinyi
Kwa kweli, sisi tunaiogopa, kutoka kwa Mola wetu, Siku ngumu ambayo ndani yake nyuso zitakunjana na mapaji yatasinyaa kutokana na mambo yake mazito na vituko vyake vikubwa
Na watawazunguka wema hawa wakiwatumikia wavulana wenye hali moja ya kudumu, ukiwaona utawadhania, kwa uzuri wao na usafi wa rangi zao na mng’aro wa nyuso zao, kuwa ni lulu iliyotenganishwa inayong’ara
Juu ya miili yao pana nguo zilizoipamba, ambazo sehemu zake za ndani kuna hariri nyembamba ya rangi ya kijani, na nje yake kuna hariri nene. Na miongoni mwa mapambo watakayovishwa ni makuku ya fedha. Na Mola wao Atawanywesha, juu ya sterehe hizo, kinywaji kisicho na uchafu wala rojo
Na wataambiwa, «Hakika nyinyi mmetayarishiwa haya yakiwa ni badala ya matendo yenu mema, na matendo yenu duniani yalikuwa ni yenye kukubaliwa na kuridhiwa na Mwenyezi Mungu.»
Hakika sisi tumekuteremshia Qur’ani, ewe Mtume, materemsho yanayotoka kwetu, ili uwakumbushe watu yale yaliyomo ndani ya maagizo mema, matahadharisho ya ubaya, malipo mazuri na mateso
Basi yavumilie maamuzi ya Mola Wako Aliyokupangia na uyakubali, na usonge mbele kufuata maamrisho yake ya Kidini, na usiwatii washirikina waliovama kwenye matamanio au waliokolea kwenye ukafiri na upotevu
Kwa hakika hawa washirikina wanaupenda ulimwengu na wanaushughulikia, na wanakuacha nyuma ya migongo yao kule kufanya matendo ya kuwafaa Akhera na kuwaokoa katika Siku yenye shida kubwa
Hakika ndani ya sura hii, kwa yaliyomo ya kuvutia na kuogopesha, ya kuahidi mema na kuonya mabaya, kuna mawaidha kwa viumbe wote. Basi mwenye kujitakia wema nafsi yake ya duniani na Akhera, na ashike njia ya Imani na uchamungu itakayomfikisha kwenye msamaha wa Mwenyezi Mungu na radhi Zake
Na hamtataka jambo lolote miongoni mwa mambo isipokuwa kwa makadirio ya Mwenyezi Mungu na matakwa Yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa hali za viumbe Vyake, ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji na utengezaji Wake
Anamuingiza Anayemtaka miongoni mwa waja Wake katika rehema Yake na radhi Yake, na wao ni wale walioamini. Na Amewaandalia madhalimu waliokiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu adhabu yenye kuumiza