Onjeni ukali wa Moto huu. Vumilieni uchungu wake na ukali wake au msiyavumilie hayo, hamtahafifishiwa adhabu na hamtatoka humo. Ni sawasawa kwenu nyinyi mkivumilia au mkitovumilia. Hakika nyinyi mnalipwa tu yale mliokuwa mkiyafanya duniani
Watajistarehesha kwa vile Alivyowapa Mwenyezi Mungu vya neema miongoni mwa aina mbalimbali za ladha na starehe, na Atawaokoa mwenyezi Mungu kutokana na adhabu ya Moto
Na wale walioamini na wakafuatwa na watoto wao katika hiyo Imani, Tutawakutanisha watoto wao nao katika daraja yao Peponi, hata kama hawakufikia matendo ya wazazi wao, ili wazazi wafurahike na watoto wao pamoja na wao katika daraja zao. Watakusanywa baina yao kwenye hali nzuri zaidi, na hatutawapunguzia chochote katika matendo yao mema. Kila mtu anafungwa na matendo yake aliyoyachuma, hatobeba dhambi za watu wengine
Na miongoni mwa starehe hizo ni kuwa wao watapeana gilasi ya pombe, mmoja wao atampa mwenzake, ili furaha yao ikamilike. Kinywaji hiki kinatafautiana na pombe ya duniani, hakimleweshi akili mwenye kukinywa, wala hakisababishi kubobokwa, wala maneno ya makosa na maasia
Na watawazunguka watumishi waliotayarishwa kuwatumikia kama kwamba wao katika usafi na weupe na utungaji nidhamu ni lulu iliyohifadhiwa kwenye mashaza yake
Watasema, «Sisi tulikuwa kabla, huko duniani, na sisi tuko baina ya watu wetu, tunamuogopa Mola wetu, tuna hadhari na adhabu Yake na mateso yake Siku ya Kiyama
Mwenyezi Mungu Akatuneemesha kwa uongofu na taufiki na Akatuokoa na adhabu ya vuke la Jahanamu, nalo ni moto wake na joto lake. Sisi tulikuwa, hapo kabla, tukimnyenyekea Yeye Peke Yake, hatumshirikishi na Yeye yoyote asiyekuwa Yeye, Atulinde na adhabu ya vuke la Motoni na Atupeleke kwenye starehe ya Peponi
Mwenyezi Mungu Akatukubalia maombi yetu, na Akatupa tulichokiomba. Hakika Yeye Ndiye Mwingi wa kheri, Mwenye kurehemu. Na miongoni mwa wingi wa kheri Zake na rehema Zake kwetu ni kule kutupa radhi zake na Pepo, na kutuepusha na hasira Zake na Moto.»
Basi wawaidhie, ewe Mtume, wale uliotumilizwa kwao kwa Qur’ani, kwani hukuwa wewe, kwa neema ya Mwenyezi Mungu Aliokuneemesha kwayo ya unabii na busara ya akili, ni kuhani anayetoa habari za ghaibu bila ujuzi wala mwendawazimu asiyejua analolisema, kama wanavyodai
Au zinawaamuru akili zao, hao wakanushaji, ziseme neno hili linalogongana (kuwa sifa ya ukuhani, utungaji mashairi, na wendawazimu haiwezekani kukutana wakati mmoja)? Bali wao ni watu waliruka mipaka katika uasi
Je, wameumbwa hawa washirikina bila kuwako mwenye kuwaumba na kuwapatisha au wao wamejiumba wenyewe? Na yote mambo mawili haya yametanguka na hayawezekani. Na kwa hivyo, inalazimika kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyewaumba, na Yeye Peke Yake Ndiye Ambaye hakuna anayepasa kuabudiwa, wala kufaa kuabudiwa, isispokuwa Yeye
Au wanazo wao hazina za Mola wako wanazitumia? Au wao ni majebari wanaowagandamiza viumbe vya Mwenyezi Mungu kwa kuwatendesha nguvu na kuwanyanyasa? Mambo si hivyo, bali wao ndio walemevu walio madhaifu
Au wao wana ngazi ya kupandia mbinguni wanasikiliza huko wahyi kwamba yale waliyonayo ndio haki? Basi na aje, yule anayedai kuwa amesikia hilo, na hoja ya waziwazi yenye kusadikisha madai yake
Au je unawataka, ewe Mtume, hawa washirikina wakupatie malipo ya kuwafikishia Ujumbe, wakawa wao wana tabu na dhiki ya kujilazimisha malipo unayoyataka kutoka kwao
Au je wao wana ujuzi wa ghaibu wakawa wanawaandikia watu na kuwapa habari yake? Mambo si hivyo, kwani hakika ya mambo ni kwamba hakuna anayejua ghaibu iliyo mbinguni na ardhini isipokuwa Mwenyezi Mungu
Au wao wana muabudiwa anayestahiki kuabudiwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu? Ametakasika Mwenyezi Mungu na kutukuka na yale wanayoshirikisha. Kwani Yeye Hana mshirika katika mamlaka, na Hana mshirika katika Upweke na ustahiki wa kuabudiwa
Na wakikiona hawa washirikina kipande cha mbingu kinawaangukia, kikiwa ni adhabu kwao, hawataacha yale waliyo nayo ya ukanushaji, na watasema, «Haya ni mawingu yamekusanyika na kupandana.»
Katika Siku hiyo havitawazuilia wao vitimbi vyao kotokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu kitu chochote, na hatawanusuru yoyote kuwaokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu
Hakika madhalimu hawa watakuta adhabu duniani, kabla ya adhabu ya Siku ya Kiyama, ya kuuawa, kukamatwa mateka, adhabu ya kaburini na nyinginezo. Lakini wengi wa watu hawajui hilo
Na uivumilie, ewe Mtume, hukumu ya Mola wako na amri Yake juu ujumbe Aliyokubebesha na juu ya makero yanayokupata kutoka kwa watu wako, hakika wewe uko kwenye maangalizi yetu, hifadhi na utunzi. Na umtakase Mola Wako kwa kumsifu unaposimama kuswali na unapoinuka kutoka usingizini
Na kwenye kipindi cha usiku mtakase Mola wako kwa kumsifu, umtukuze na umswalie. Na ufanye hayo kwenye kipindi cha Swala ya Asubuhi wakati wa nyota kuondoka. Katika aya hizi pana kuthibitisha sifa ya macho mawili kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa inavyonasibiana na Yeye, bila kufananisha na viumbe Vyake au kuieleza dhati Yake vile ilivyo, kutakasika na kila sifa ya upungufu ni Kwake na sifa njema zote ni Zake, kama lilivyothibiti hilo katika Sunnah na kukubaliana juu yake wanavyuoni waliopita wa Ummah huu