Back to Languages

Swahili - Chapter 71 - Nuh

Translation by Abdullah Muhammad Abu Bakr — Permalink

Verse 1 — Surah Nuh 71:1

Kwa hakika sisi tulimpeleka Nūḥ kwa watu wake na tukamwambia, «Waonye watu wako kabla ya kufikiwa na adhabu yenye kuumiza.»

Verse 2 — Surah Nuh 71:2

Nūḥ akasema, «Enyi watu wangu! Mimi kwenu nyinyi ni mwonyaji waziwazi, anayewaonya nyinyi adhabu ya Mwenyezi Mungu iwapo mtamuasi

Verse 3 — Surah Nuh 71:3

Na mimi ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu kwenu. Muabuduni Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Peke Yake na muogopeni Yeye na nitiini mimi katika kile ninachowaamrisha nyinyi na kuwakataza. Basi mkinitii mimi na mkanikubalia

Verse 4 — Surah Nuh 71:4

Mwenyezi Mungu Atawasamehe dhambi zenu na kuwafinikia, atawarefushia umri wenu mpaka kipindi kilichokadiriwa katika ujuzi wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka. Kwani kifo kikija hakicheleweshwi kabisa. Lau mngalijua hilo mngalifanya haraka kuamini na kutii.»

Verse 5 — Surah Nuh 71:5

Nūḥ akasema, «Mola wangu! Kwa hakika mimi nimewalingania watu wangu usiku na mchana ili wakuamini wewe na wakutii

Verse 6 — Surah Nuh 71:6

Ulinganizi wangu kwao ili waamini, haukuwaongezea kitu isipokuwa ni kukimbia na kuipa mgongo haki

Verse 7 — Surah Nuh 71:7

Na mimi kila nikiwalingania wao ili wakuamini wewe, ipate kuwa hiyo ni njia ya wewe kuwasamehe dhambi zao, hutia vidole vyao masikioni mwao, ili wasisikie ulinganizi wa haki, na hujifinika nguo zao wasipate kuniona, na hujikita kwenye ukafiri wao na hufanya kiburi sana cha kutoikubali haki

Verse 8 — Surah Nuh 71:8

Kisha mimi ni kawalingania wao kwenye Imani waziwazi na sio kwa kujificha

Verse 9 — Surah Nuh 71:9

Kisha nikawatangazia wao ulinganizi kwa sauti kubwa wakati mwingine, na nikausirisha huo ulinganizi kwa sauti ya chini wakati mwingine

Verse 10 — Surah Nuh 71:10

Ni kawaambia watu wangu, ‘Muombeni Mola wenu msamaha wa dhambi zenu na tubieni Kwake kutokana na ukafiri wenu, hakika Yeye ni Mwingi wa kusamehe kwa anayetubia miongoni mwa waja Wake na akurudia Kwake.’»

Verse 11 — Surah Nuh 71:11

Mtakapotubia na mkaomba msamaha, Mwenyezi Mungu Atawateremshia mvua nyingi ya mfululizo

Verse 12 — Surah Nuh 71:12

Atayaongeza mali yenu na pia watototo wenu, Atawafanya muwe na mabustani ya nyinyi kuneemeka kwa matunda yake na uzuri wake, na Atawajaalia nyinyi muwe na mito ambayo mtaitumia kwa kuipatia maji mimea yenu na pia wanyama wenu

Verse 13 — Surah Nuh 71:13

Mnani nyinyi, enyi watu, hamuogopi ukuu wa Mwenyezi Mungu na uweza Wake

Verse 14 — Surah Nuh 71:14

na hali yeye Amewaumba nyinyi katika miongo yenye kufuatana : tone la manii, kisha pande la damu, kisha nofu la nyama, kisha mifupa na nyama

Verse 15 — Surah Nuh 71:15

Kwani hamtazami namna alivyoumba Mwenyezi Mungu mbingu saba zilizopandana, kila uwingu juu ya mwingine

Verse 16 — Surah Nuh 71:16

Akajaalia mwezi, katika mbigu hizi, ni wenye mwangaza,, na Akajaalia jua ni taa yenye kung’ara ili kuwapatia mwangaza watu walioko ardhini

Verse 17 — Surah Nuh 71:17

Mwenyezi Mungu aliumba asili yenu kutokana na ardhi

Verse 18 — Surah Nuh 71:18

kisha Atawarudisha humo ardhini baada ya kufa, na Awatoe Siku ya kufufuliwa kuwatoa kihakika

Verse 19 — Surah Nuh 71:19

Na Mwenyezi Mungu Amewafanyia hii ardhi ni tandiko kama mkeka

Verse 20 — Surah Nuh 71:20

Ili mfuate humo njia zilizo kunjufu

Verse 21 — Surah Nuh 71:21

Nūḥ alisema, «Mola wangu! Kwa hakika watu wangu wameendelea sana kuniasi na kunikanusha, na wanyonge miongoni mwao wakawafuata viongozi wapotevu ambao mali yao na watoto wao havikuwaongezea isipokuwa upotevu wa duniani na mateso ya Akhera

Verse 22 — Surah Nuh 71:22

Na hao viongozi wa upotevu wakawafanyia wafuasi wao wanyonge vitimbi vikubwa

Verse 23 — Surah Nuh 71:23

na wakawaambia, ‘Msiache kuwaabudu waungu wenu mkaelekea kwenye kumubadu Mwenyezi Mungu Peke Yake, ambaye Nūḥ anawalingania nyinyi mumuabudu, na msimuache Wadd, Suwā‘, Yghūth, Ya’ūq wala Nasr.» Na haya ni majina ya masanamu wao ambao walikuwa wakiyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, na yalikuwa ni majina ya watu wema. Walipokufa, Shetani alitia kwenye mawazo ya watu wao wawasimamishie masanamu na picha ili wapate moyo, kama wanavyodai, wa kuwa watiifu wanapoyaona. Walipoondoka hao waliosimamisha masanamu na muda mrefu ukapita, wakaja watu wasiokuwa wao, Shetani aliwatia tashwishi kwamba wakale wao waliopita walikuwa wakiyaabudu haya masanamu na picha na kutawasali nayo. Hii ndio hekima ya kuharamishwa masanamu na kuharamishwa ujengaji wa makuba juu ya makaburi. Kwa kuwa hayo kwa kupitiwa na muda yanakuwa ni yenye kuabudiwa na wajinga

Verse 24 — Surah Nuh 71:24

Na hawa wafuatwa wamewapoteza watu wengi kwa vile walivyowapambia njia za upotofu upotevu. Kisha Nūḥ akaendelea kusema, «Na usiwaongezee, ewe Mola wetu, hawa waliozidhulumu nafsi zao kwa ukanushaji na ushindani isipokuwa kuwaepusha na haki.»

Verse 25 — Surah Nuh 71:25

Kwa sababu ya dhambi zao na ukakamavu wao juu ya ukafiri na uasi, walizamishwa kwa mafuriko na wakaingizwa baada ya kuzamishwa kwenye Moto unaowakia sana na kuchoma, na wasimpate, badala ya Mwenyezi Mungu, mwenye kuwaokoa au kuwaepushia adhabu ya Mwenyezi Mungu

Verse 26 — Surah Nuh 71:26

Na akasema Nūḥ, amani imshukie, baada ya kukata tama na watu wake, «Mola wangu! Usimuache yoyote miongoni mwa wale wanaokukanusha kuwa ni mwenye kuishi juu ardhi akizunguka na kutembea

Verse 27 — Surah Nuh 71:27

Hao ukiwaacha, bila kuwaangamiza, watawapoteza waja wako waliokuamini na kuwapotosha njia ya haki, na haji yoyote kutokana na migongo yao na vizazi vyao isipokuwa yule aliyepotoka na njia ya haki na kukukanusha wewe sana na kukuasi

Verse 28 — Surah Nuh 71:28

Mola wangu! Nisamehe mimi, wazazi wangu wawili, mwenye kuingia nyumbani kwangu na hali yeye ameamini, wanaume na wanawake waliokuamini wewe, na usiwaongezee makafiri isipokuwa maangamivu na hasara, duniani na Akhera.»