Basi itakuwaje hali ya yule anayeiba na kupunja katika vipimo vyote hivyo, au yule anayeiba katika vipimo hivyo na huku awapunja watu vitu vyao? Hakika huyo yuwastahiki mateso zaidi kuliko wapunguzaji wa vipimo vya vibaba na mizani. Kwani hawaamini wale wapunjaji ya kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mwenye kuwafufua na kuwahesabu juu ya vitendo vyao
Siku watakaposimama watu mbele ya Mweyezi Mungu ili Awahesabu kwa machache na mengi walioyatenda, hali ya kuwa wao Siku Hiyo ni wenye kumnyenyekea Mwenyezi Mungu, Mlezi wa viumbe vyote
Hakika hiyo itakuwa ni jela ya kudumu na adhabu iliyo na uchungu. Penye jela hiyo ni pale walipoandikiwa kuwa watakwenda. Wameandikiwa na imepitishwa. Hapana kitakachozidishwa wala kupunguzwa
Na hakika zimezibwa nyoyo zao zikawa hazimkubali Mwenyezi Mungu. Na kile kilichoziziba nyoyo hizo ni kufinikwa na wingi wa madhambi wanayoyafanya. Mambo hayako kama vile wanavyodai makafiri! Bali hakika wao, Siku ya Kiyama watazibwa wasimuone Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kushinda. Aya hii ni ushahidi kwamba Waumini watamuona Mola Wao Peponi
Na hawa makafiri wanapowaona Maswahaba wa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wamefuata uongofu, huwa wakisema, «Hakika hawa wamepotea kwa kumfuata Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie
Basi Siku ya Kiyama wale waliomkubali Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakafanya vitendo vinavyolingana na sheria Zake, watawafanyia maskhara makafiri kama makafiri walivyokuwa wakiwafanyia mashara duniani
Juu ya viti vya fahari, watakuwa Waumini wanaangalia yale Aliyowapa Mwenyezi Mungu miongoni mwa mambo matukufu na neema, wakiwa Peponi. Na neema kubwa ya zote ni kuangalia Uso wa Mwenyezi Mungu Mtukufu