Mwenyezi Mungu aliye ziinua mbingu bila ya nguzo mnazo ziona, ametawala kwenye Ufalme wake, na amefanya jua na mwezi yamt'ii, kila kimoja kinakwenda kwa kiwango maalumu. Anayapanga mambo, na anazipambanua Ishara ili mpate kuwa na yakini kukutana na Mola wenu Mlezi
Na ndiye aliye itandaza ardhi na akaweka humo milima na mito. Na katika kila matunda akafanya dume na jike. Huufunika usiku juu ya mchana. Hakika katika haya zimo Ishara kwa watu wanao fikiri
Na katika ardhi vimo vipande vilivyo karibiana, na zipo bustani za mizabibu, na mimea mingine, na mitende yenye kuchipua kwenye shina moja na isio chipua kwenye shina moja, nayo inatiliwa maji yale yale. Na tunaifanya baadhi yao bora kuliko mengine katika kula. Hakika katika hayo zimo ishara kwa watu wanao tia mambo akilini
Na kama ukistaajabu, basi cha ajabu zaidi ni huo usemi wao: Ati tukisha kuwa mchanga kweli tutakuwa katika umbo jipya? Hao ndio walio mkufuru Mola wao Mlezi. Na hao ndio watao kuwa na makongwa shingoni mwao, na hao ndio watu wa Motoni. Humo watadumu
Na wanakuhimiza ulete maovu kabla ya mema, hali ya kuwa zimekwisha pita kabla yao adhabu za kupigiwa mfano. Na hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye msamaha kwa watu juu ya udhalimu wao. Na hakika Mola wako Mlezi ni Mkali wa kuadhibu
Kila mtu analo kundi la malaika mbele yake na nyuma yake linamlinda kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo naf- sini mwao. Na Mwenyezi Mungu anapo watakia watu adhabu hakuna cha kuzuia wala hawana mlinzi yeyote badala yake
Na radi inamtakasa Mwenyezi Mungu kwa kumhimidi, na Malaika pia, kwa kumkhofu. Naye hupeleka mapigo ya radi yakampata amtakaye. Nao wanabishana juu ya Mwenyezi Mungu. Na Yeye ni Mwenye adhabu kali
Wa kuombwa kweli ni Yeye tu. Na hao wanao waomba badala yake hawawajibu chochote; bali ni kama mwenye kunyoosha viganja vyake kwenye maji ili yafike kinywani mwake, lakini hayafiki. Na maombi ya makafiri hayako ila katika upotovu
Sema: Ni nani Mola Mlezi wa mbingu na ardhi? Sema: Mwenyezi Mungu. Sema: Basi je, mnawafanya wenginewe badala yake kuwa ni walinzi, nao hawajifai wenyewe kwa jema wala baya? Sema: Hebu kipofu na mwenye kuona huwa sawa? Au hebu huwa sawa giza na mwangaza? Au wamemfanyia Mwenyezi Mungu washirika walio umba kama alivyo umba Yeye, na viumbe hivyo vikawadanganyikia? Sema: Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu. Na Yeye ni Mmoja Mwenye kushinda
Ameteremsha maji kutoka mbinguni. Na mabonde yakamiminika maji kwa kadiri yake. Na mafuriko yakachukua mapovu yaliyo kusanyika juu yake. Na kutokana na wanavyo yayusha katika moto kwa kutaka mapambo au vyombo hutokea povu vile vile. Namna hivyo Mwenyezi Mungu ndivyo anavyo piga mifano ya Haki na baat'ili. Basi lile povu linapita kama takataka tu basi. Ama kinacho wafaa watu hubakia kwenye ardhi. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo piga mifano
Walio muitikia Mola wao Mlezi watapata wema. Na wasio muitikia, hata wangeli kuwa navyo vyote viliomo katika ardhi na mfano wa hivyo, bila ya shaka wangeli vitoa kujikombolea! Hao watapata hisabu mbaya kabisa, na makao yao ni Jahannamu. Na hapo ni pahala pabaya mno
Na ambao husubiri kwa kutaka radhi ya Mola wao Mlezi, na wakashika Sala, na wakatoa, kwa siri na kwa uwazi, katika tulivyo wapa; na wakayaondoa maovu kwa wema. Hao ndio watakao pata malipo ya Nyumba ya Akhera
Nayo ni Bustani za milele, wataziingia wao na walio wema miongoni mwa baba zao, na wake zao, na vizazi vyao. Na Malaika wanawaingilia katika kila mlango
Na wale wanao vunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya kuzifunga, na wanakata aliyo amrisha Mwenyezi Mungu yaungwe, na wanafanya fisadi katika nchi: hao ndio watakao pata laana, na watapata Nyumba mbaya
Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye, na humkunjia kwa kipimo. Na wamefurahia maisha ya dunia. Na uhai wa dunia kwa kulingana na Akhera si kitu ila ni starehe ndogo
Na wanasema walio kufuru: Kwa nini hakuteremshiwa muujiza kutoka kwa Mola wake Mlezi. Sema: Hakika Mwenyezi Mungu humwacha kupotea amtakaye, na humwongoa anaye elekea kwake
Ndio kama hivi tumekutuma kwa umma ambao wamekwsiha pita kabla yao umati nyengine, ili uwasomee tunayo kufunulia, na wao wanamkufuru Rahmani, Mwingi wa Rehema! Sema: Yeye ndiye Mola wangu Mlezi. Hapana mungu isipo kuwa Yeye. Juu yake nimetegemea, na kwake ndio marejeo yangu
Na kama ingeli kuwako Qur'ani ndiyo inayo endeshewa milima, na kupasuliwa ardhi, na kusemeshewa wafu, (basi ingeli kuwa Qur'ani hii). Bali mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu. Je, hawajajua walio amini kwamba lau kuwa Mwenyezi Mungu ange penda bila ya shaka angeli waongoa watu wote? Wala walio kufuru hawaachi kusibiwa na balaa kwa waliyo yatenda, au ikawateremkia karibu na nyumbani kwao, mpaka ifike ahadi ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu havunji miadi yake
Je! Anaye isimamia kila nafsi kwa yale iliyo yachuma...? Na wamemfanyia Mwenyezi Mungu kuwa na washirika! Sema watajeni. Au ndio mnampa khabari ya yale asiyo yajua katika ardhi; au ni maneno matupu? Bali walio kufuru wamepambiwa vitimbi vyao na wamezuiliwa njia. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha apotee basi hana wa kumwongoa
Mfano wa Bustani waliyo ahidiwa wachamngu, kati yake inapita mito, matunda yake ni ya daima, na pia kivuli chake. Huu ndio mwisho wa wale walio walio jilinda. Na mwisho wa makafiri ni Moto
Na tulio wapa Kitabu wanafurahia uliyo teremshiwa. Na katika makundi mengine wapo wanao yakataa baadhi ya haya. Sema: Nimeamrishwa nimuabudu Mwenyezi Mungu, na wala nisimshirikishe. Kuendea kwake Yeye ndiyo ninaita, na kwake Yeye ndio marejeo yangu
Na ndio kama hivi tumeiteremsha Qur'ani kuwa ni hukumu kwa lugha ya Kiarabu. Na ukifuata matamanio yao baada ya kukujia ilimu hii, hutakuwa na rafiki wala mlinzi mbele ya Mwenyezi Mungu
Na hakika Sisi tulikwisha watuma Mitume kabla yako, na tukajaalia wawe na wake na dhuriya. Na haiwi kwa Mtume kuleta miujiza isipo kuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Kila kipindi kina hukumu yake
Je! Hawakuona kwamba tunaifikia ardhi tukiipunguza nchani mwake? Na Mwenyezi Mungu huhukumu, na hapana wa kupinga hukumu yake, naye ni Mwepesi wa kuhisabu
Na walipanga walio kuwa kabla yao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye mipango yote. Yeye anajua inayo chuma kila nafsi. Na makafiri watajua ni ya nani nyumba ya mwisho Akhera