Na kadhaalika Mola wako Mlezi atakuteuwa na atakufundisha tafsiri ya mambo. Na atatimiza neema zake juu yako na juu ya ukoo wa Yaa'qub, kama alivyo watimizia hapo zamani baba zako Ibrahim na Is-haq. Hakika Mola wako Mlezi ni Mjuzi Mwenye hikima
Pale walipo sema: Hakika Yusuf na nduguye wanapendwa zaidi na baba yetu kuliko sisi, hali sisi ni kikundi chenye nguvu. Hakika baba yetu yumo katika upotofu wa dhaahiri
Basi walipo mchukua na wakakubaliana wamtumbukize ndani ya kisima, tulimfunulia Yusuf: Hapana shaka yoyote utakuja waambia kwa jambo lao hili, na wala wao hawatambui
Wakasema: Ewe baba yetu! Hakika tulikwenda kushindana na tukamwacha Yusuf penye vitu vyetu. Basi mbwa mwitu akamla. Lakini wewe hutuamini ijapo kuwa tunasema kweli
Wakaja na kanzu yake ina damu ya uwongo. Akasema: Bali nafsi zenu zimekushawishini kutenda kitendo. Lakini subira ni njema; na Mwenyezi Mungu ndiye wa kuombwa msaada kwa haya mnayo yaeleza
Ukafika msafara, wakamtuma mchota maji wao, naye akatumbukiza ndoo yake. Alisema: Kheri Inshallah! Huyu hapa mvulana! Wakamficha ili kumfanya ni bidhaa. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa wanayo yatenda
Na yule aliye mnunua huko Misri alimwambia mkewe: Mtengenezee makaazi ya hishima huyu; huenda akatufaa au tukamfanya mwenetu. Na kama hivyo tulimweka Yusuf katika nchi ili tumfundishe kufasiri mambo. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kushinda katika jambo lake, lakini watu wengi hawajui
Na yule bibi wa nyumba aliyo kuwamo Yusuf alimtamani kinyume cha nafsi yake, na akafunga milango. Akamwambia: Njoo! Yusuf akasema: Audhubillahi! Najikinga na Mwenyezi Mungu. Huyu bwana wangu kaniweka maskani nzuri, na hakika wenye kudhulumu hawatengenekewi
Na hakika yule mwanamke alimtamani, na Yusuf angeli mtamani lau kuwa hakuona ishara ya Mola wake Mlezi. Hayo hivyo ni kwa ajili tumuepushe na uovu na uchafu. Hakika yeye alikuwa katika waja wetu walio safishwa
Na wote wawili wakakimbilia mlangoni, na mwanamke akairarua kanzu yake Yusuf kwa nyuma. Na wakamkuta bwana wake mlangoni. Mwanamke akasema: Hapana malipo ya mwenye kutaka kumfanyia maovu mkeo isipo kuwa kufungwa au kupewa adhabu chungu
Yusuf akasema: Yeye ndiye aliye nitaka bila ya mimi kumtaka. Na shahidi aliye kuwa katika jamaa za mwanamke alisema: Ikiwa kanzu yake imechanwa mbele basi mwanamke amesema kweli, naye Yusuf ni katika waongo
Na wanawake wa mjini wakawa wanasema: Mke wa Mheshimiwa anamtamani mtumishi wake! Hakika amesalitika kwa mapenzi. Sisi hakika tunamwona yumo katika upotovu ulio dhaahiri
Alipo sikia yule bibi masengenyo yao aliwaita, na akawawekea matakia ya kuegemea, na akampa kila mmoja wao kisu. Akamwambia Yusuf: Tokeza mbele yao. Basi walipo mwona waliona ni kitu kikubwa kabisa, na wakajikata mikono yao. Wakasema: Hasha Lillahi! Huyu si mwanaadamu. Hakuwa huyu ila ni Malaika mtukufu
Yule bibi aksema: Huyu basi ndiye huyo mliye nilaumia! Na kweli mimi nilimtaka naye akakataa. Na akitofanya ninayo muamrisha basi hapana shaka atafungwa gerezani, na atakuwa miongoni mwa walio chini kabisa
Yusuf akasema: Ee Mola Mlezi wangu! Nastahabu kifungo kuliko haya anayo niitia. Na usipo niondoshea vitimbi vya wanawake mimi nitamili kwao, na nitakuwa katika wajinga
Wakaingia gerezani pamoja naye vijana wawili. Mmoja wao akasema: Hakika mimi nimeota nakamua mvinyo. Na mwingine akasema: Mimi nimeota nimebeba mikate juu ya kichwa changu, na ndege wanaila. Hebu tuambie tafsiri yake, kwani sisi tunakuona wewe ni katika watu wema
Akasema: Hakitakufikilieni chakula mtakacho pewa ila nitakwambieni hakika yake kabla hakijakufikieni. Haya ni katika yale aliyo nifundisha Mola wangu Mlezi. Hakika mimi nimeacha mila ya watu wasio muamini Mwenyezi Mungu, na wakawa hawaiamini Akhera
Na nimefuata mila ya baba zangu, Ibrahim, na Is-haq, na Yaa'qub. Hatuna haki ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote. Hiyo ni katika fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yetu na juu ya watu; lakini watu wengi hawashukuru
Hamuabudu badala yake ila majina tu mliyo yapanga nyinyi na baba zenu. Mwenyezi Mungu hakuyateremshia hayo uthibitisho wowote. Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu tu. Yeye ameamrisha msimuabudu yeyote isipo kuwa Yeye tu. Hiyo ndiyo Dini Iliyo Nyooka. Lakini watu wengi hawajui
Enyi wafungwa wenzangu wawili! Ama mmoja wenu atamnywesha bwana wake mvinyo. Na ama mwengine atasulubiwa, na ndege watamla kichwa chake. Imekwisha katwa hukumu ya hilo jambo mlilo kuwa mkiuliza
Na akamwambia yule aliye jua kuwa atavuka katika wale wawili: Nikumbuke kwa bwana wako. Lakini Shet'ani alimsahaulisha kumtaja kwa bwana wake. Basi Yusuf akakaa gerezani miaka kadhaa
Na siku moja mfalme alisema: Hakika mimi nimeota ng'ombe saba wanene wanaliwa na ng'ombe saba walio konda. Na mashuke saba mabichi na mengine makavu. Enyi waheshimiwa! Nambieni maana ya ndoto zangu, ikiwa nyinyi mnaweza kuagua ndoto
Yusuf! Ewe mkweli! Tueleze nini maana ya ng'ombe saba wanene kuliwa na ng'ombe saba walio konda. Na mashuke saba mabichi na mengine makavu, ili nirejee kwa watu wapate kujua
Na mfalme akasema: Mleteni kwangu! Basi mjumbe alipo mjia Yusuf alisema: Rejea kwa bwana wako ukamuulize khabari ya wale wanawake walio jikata mikono yao. Hakika Mola wangu Mlezi anazijua vyema hila zao
Mfalme alisema: Mlikuwa mna nini mlipo mtaka Yusuf kinyume na nafsi yake? Wakasema: Hasha Lillahi! Sisi hatukujua ubaya wowote kwake. Mke wa Mheshimiwa akasema: Sasa haki imedhihiri. Mimi ndiye niliye mtaka kinyume na nafsi yake, na hakika yeye ni katika wakweli
NAMI sijitoi lawamani. Kwa hakika nafsi ni mno kuamrisha maovu, isipo kuwa ile ambayo Mola wangu Mlezi aliyo irehemu. Hakika Mola wangu Mlezi ni Msamehevu na Mwenye kurehemu
Basi namna hivi tukampa Yusuf cheo katika nchi; anakaa humo popote anapo penda. Tunamfikishia rehema zetu tumtakaye, wala hatupuuzi malipo ya wafanyao mema
Basi walipo rejea kwa baba yao, walisema: Ewe baba yetu! Tumenyimwa chakula zaidi, basi mpeleke nasi ndugu yetu ili tupate kupimiwa; na yakini sisi tutamlinda
Je, nikuaminini kwa huyu ila kama nilivyo kuaminini kwa nduguye zamani? Lakini Mwenyezi Mungu ndiye Mbora wa kulinda, naye ndiye Mbora wa kurehemu kuliko wenye kurehemu wote
Na walipo fungua mizigo yao wakakuta bidhaa zao wamerudishiwa. Wakasema: Ewe baba yetu! Tutake nini zaidi? Hizi bidhaa zetu tumerudishiwa. Wacha tuwaletee watu wetu chakula, na tutamlinda ndugu yetu, na tutaongeza shehena ya ngamia. Na hicho ni kipimo kidogo
Akasema: Sitampeleka nanyi mpaka mnipe ahadi kwa Mwenyezi Mungu kwamba lazima mtamrejeza kwangu, ila ikiwa mmezungukwa. Basi walipo mpa ahadi yao alisema: Mwenyezi Mungu ndiye Mtegemewa kwa tuyasemayo
Na akasema: Enyi wanangu! Msiingie mlango mmoja, bali ingieni kwa milango mbali mbali. Wala mimi sikufaeni kitu mbele ya Mwenyezi Mungu. Hukumu haiko ila kwa Mwenyezi Mungu tu. Juu yake Yeye mimi nimetegemea, na juu yake Yeye wategemee wanao tegemea
Na walipo ingia kama alivyo waamrisha baba yao, haikuwafaa kitu kwa Mwenyezi Mungu, isipo kuwa ni haja tu iliyo kuwa katika nafsi ya Yaa'qub aliitimiza. Na hakika yeye alikuwa na ilimu kwa sababu tulimfundisha; lakini watu wengi hawajui
Na alipo kwisha watengenezea mahitaji yao akakitia kikopo cha kunywea maji katika mzigo wa nduguye huyo, kisha mnadi akanadi: Enyi wasafiri! Hapana shaka nyinyi ni wezi
Basi akaanza kwenye mizigo yao kabla ya mzigo wa nduguye. Kisha akakitoa katika mzigo wa nduguye. Hivi ndivyo tulivyo mpangia Yusuf. Hakuweza kumzuia nduguye kwa sharia ya mfalme isipo kuwa alivyo taka Mwenyezi Mungu. Tunawatukuza kwenye vyeo tuwatakao; na juu ya kila ajuaye yupo ajuaye zaidi
Wakasema: Ikiwa huyu ameiba, basi nduguye vile vile aliiba zamani. Lakini Yusuf aliyaweka siri moyoni mwake wala hakuwaonyesha. Akawaambia: Nyinyi mko katika hali mbaya zaidi, na Mwenyezi Mungu anajua zaidi hayo mnayo singizia
Walipo kata tamaa naye wakenda kando kunong'ona. Mkubwa wao akasema: Je! Hamjui ya kwamba baba yenu amechukua ahadi kwenu kutokana na Mwenyezi Mungu, na kabla ya hapo mlimkosa katika agano lenu juu ya Yusuf? Basi mimi sitotoka nchi hii mpaka baba yangu anipe ruhusa au Mwenyezi Mungu anihukumie. Na Yeye ndiye Mbora wa mahakimu
Rudini kwa baba yenu, na mwambieni: Ee baba yetu! Mwanao ameiba. Na sisi hatutoi ushahidi ila kwa tunayo yajua. Wala sisi hatukuwa wenye kuhifadhi mambo ya ghaibu
Akasema: Bali nafsi zenu zimekushawishini kwenye jambo fulani. Subira ni njema! Asaa Mwenyezi Mungu akaniletea wote pamoja. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye hikima
Enyi wanangu! Nendeni mkamtafute Yusuf na nduguye, wala msikate tamaa na faraji ya Mwenyezi Mungu. Hakika hawakati tamaa na faraji ya Mwenyezi Mungu isipo kuwa watu makafiri
Basi walipo ingia kwa Yusuf walisema: Ewe Mheshimiwa! Imetupata shida, sisi na watu wetu. Na tumeleta mali kidogo. Basi tupimie kipimo na fanya kama unatupa sadaka. Hakika Mwenyezi Mungu huwalipa watoao sadaka
Wakasema: Kumbe wewe ndiye Yusuf? Akasema: Mimi ndiye Yusuf, na huyu ni ndugu yangu. Mwenyezi Mungu ametufanyia hisani. Hakika anaye mcha Mungu na akasubiri, basi Mwenyezi Mungu haachi ukapotea ujira wa wafanyao mema
Na akawapandisha wazazi wake kwenye kiti cha enzi. Na wote wakaporomoka kumsujudia. Na akasema: Ewe baba yangu! Hii ndiyo tafsiri ya ile ndoto yangu ya zamani. Na Mwenyezi Mungu ameijaalia iwe kweli. Na Mwenyezi Mungu amenifanyia wema kunitoa gerezani, na kukuleteni kutoka jangwani baada ya Shet'ani kuchochea baina yangu na ndugu zangu. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mpole kwa alitakalo. Bila ya shaka Yeye ni Mjuzi Mwenye hikima
Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika umenipa utawala, na umenifunza tafsiri ya mambo. Ewe Muumba wa mbingu na ardhi! Wewe ndiye Mlinzi wangu katika dunia na Akhera. Nifishe hali ya kuwa ni Muislamu na nichanganyishe na watendao mema
Sema: Hii ndiyo Njia yangu - ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa kujua - mimi na wanao nifuata. Na ametakasika Mwenyezi Mungu! Wala mimi si katika washirikina
Na hatukuwatuma Mitume kabla yako isipo kuwa wanaume tulio wafunulia wahyi miongoni mwa watu wa mijini. Je! Hawatembei katika ardhi wakaona jinsi ulivyo kuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao? Na hakika nyumba ya Akhera ni bora kwa wamchao Mungu. Basi hamfahamu
Hata Mitume walipo kata tamaa na wakaona kuwa wamekadhibishwa, hapo ikawajia nusura yetu, wakaokolewa tuwatakao. Na adhabu yetu haitowawacha kaumu ya wakosefu
Kwa hakika katika hadithi zao limo zingatio kwa wenye akili. Si maneno yaliyo zuliwa, bali ni ya kusadikisha yaliyo kabla yake, na ufafanuzi wa kila kitu, na ni uwongofu na rehema kwa kaumu yenye kuamini