Back to Languages

Swahili - Chapter 11 - Hud

Translation by Ali Muhsin Al Barwani — Permalink

Verse 1 — Surah Hud 11:1

Alif Lam Ra. Hiki ni Kitabu ambacho Aya zake zimewekwa wazi, kisha zikapambanuliwa, kilicho toka kwa Mwenye Hikima na Mwenye Khabari

Verse 2 — Surah Hud 11:2

Ili msimuabudu isipo kuwa Allah, Mwenyezi Mungu. Hakika mimi kwenu ni mwonyaji na mbashiri nitokae kwake

Verse 3 — Surah Hud 11:3

Na ili mumwombe msamaha Mola wenu Mlezi, kisha mtubie kwake. Atakustarehesheni starehe nzuri mpaka muda maalumu. Na atampa kila mwenye fadhila, fadhila yake. Na ikiwa mtakengeuka basi mimi nakukhofieni adhabu ya hiyo Siku Kubwa

Verse 4 — Surah Hud 11:4

Marejeo yenu ni kwa Mwenyezi Mungu tu. Naye ni Muweza wa kila kitu

Verse 5 — Surah Hud 11:5

Hebu angalia! Ati wanafunika vilivyomo vifuani mwao ili wamfiche Mwenyezi Mungu! Jueni kuwa wanapo jigubika nguo zao Yeye anajua wanayo yaficha na wanayo yatangaza. Hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani

Verse 6 — Surah Hud 11:6

NA HAKUNA mnyama yoyote katika ardhi ila riziki yake iko kwa Mwenyezi Mungu. Naye anajua makao yake na mapitio yake. Yote yamo katika Kitabu chenye kubainisha

Verse 7 — Surah Hud 11:7

Na Yeye ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Na Kiti chake cha Enzi kilikuwa juu ya maji, ili akufanyieni mtihani ajuulikane ni nani miongoni mwenu mzuri zaidi wa vitendo. Na wewe ukisema: Nyinyi hakika mtafufuliwa baada ya kufa; wale walio kufuru husema: Hayakuwa haya ila ni uchawi uliyo wazi

Verse 8 — Surah Hud 11:8

Na tukiwacheleweshea adhabu mpaka muda ulio kwisha hisabiwa wao husema: Nini kinacho izuia hiyo adhabu? Jueni! Siku itakapo wajia basi haitoondolewa hiyo kwao. Na yatawazunguka yale waliyo kuwa wakiyafanyia mzaha

Verse 9 — Surah Hud 11:9

Na tukimwonjesha mtu rehema inayo toka kwetu, kisha tukamwondolea, hukata tamaa akakufuru

Verse 10 — Surah Hud 11:10

Na tukimwonjesha neema baada ya madhara yaliyo mpata husema: Taabu zimekwisha niondokea. Hakika yeye hujitapa na kutafakhari

Verse 11 — Surah Hud 11:11

Ila wale walio subiri wakatenda mema. Hao watapata msamaha na ujira mkubwa

Verse 12 — Surah Hud 11:12

Basi labda utaacha baadhi ya yale yaliyo funuliwa kwako, na kifua kitaona dhiki kwa hayo, kwa sababu wanasema: Mbona hakuteremshiwa khazina, au wakaja naye Malaika? Wewe ni mwonyaji tu, na Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wa kila kitu

Verse 13 — Surah Hud 11:13

Au wanasema: Ameizua? Sema: Basi leteni Sura kumi zilizo zuliwa mfano wa hii, na waiteni muwawezao badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema kweli

Verse 14 — Surah Hud 11:14

Na wasipo kuitikieni, basi jueni ya kwamba (hii Qur'ani) imeteremshwa kwa ujuzi wa Mwenyezi Mungu, na kwamba hapana mungu ila Yeye. Basi je! Nyinyi ni Waislamu

Verse 15 — Surah Hud 11:15

Wanao taka maisha ya dunia na pumbao lake tutawalipa humo vitendo vyao kaamili. Na wao humo hawatopunjwa

Verse 16 — Surah Hud 11:16

Hao ndio ambao hawatakuwa na kitu Akhera ila Moto, na yataharibika waliyo yafanya, na yatapotea bure waliyo kuwa wakiyatenda

Verse 17 — Surah Hud 11:17

Basi je, mtu aliye na dalili wazi itokayo kwa Mola wake Mlezi, inayo fuatwa na shahidi anaye toka kwake, na kabla yake kilikuwa Kitabu cha Musa kilicho kuwa mwongozi na rehema - hao wanamuamini, na anaye mkataa katika makundi, basi Moto ndio pahala pa miadi yao. Basi usiwe na shaka juu ya hayo. Hii ni Haki itokayo kwa Mola wako Mlezi; lakini watu wengi hawaamini

Verse 18 — Surah Hud 11:18

Na nani aliye dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo? Hao watahudhurishwa mbele ya Mola wao Mlezi, na mashahidi watasema: Hawa ndio walio mtungia uwongo Mola wao Mlezi. Laana ya Mwenyezi Mungu iwapate walio dhulumu

Verse 19 — Surah Hud 11:19

Ambao wanazuilia Njia ya Mwenyezi Mungu, na wanaitakia ipotoke, na wanaikataa Akhera

Verse 20 — Surah Hud 11:20

Hao hawawezi kushinda katika ardhi, wala hawana walinzi isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Watazidishiwa adhabu. Hawakuwa wakiweza kusikia wala hawakuwa wakiona

Verse 21 — Surah Hud 11:21

Hao ndio walio zikhasiri nafsi zao, na yakawapotea waliyo kuwa wakiyazua

Verse 22 — Surah Hud 11:22

Bila ya shaka hakika wao ndio wenye kukhasiri huko Akhera

Verse 23 — Surah Hud 11:23

Hakika wale walio amini, na wakatenda mema, na wakanyenyekea kwa Mola wao Mlezi, hao ndio watu wa Peponi, na humo watadumu

Verse 24 — Surah Hud 11:24

Mfano wa makundi mawili ni kama kipofu kiziwi, na mwenye kuona na anasikia. Je, wawili hawa wanakuwa sawa kwa kufananishwa? Basi, je, hamfikiri

Verse 25 — Surah Hud 11:25

Na Sisi tulimtuma Nuhu kwa watu wake, akawaambia: Hakika mimi ni mwonyaji kwenu ninaye bainisha

Verse 26 — Surah Hud 11:26

Ya kwamba msimuabudu isipo kuwa Mwenyezi Mungu tu. Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya Siku Chungu

Verse 27 — Surah Hud 11:27

Na wakasema wakuu walio kufuru katika kaumu yake: Hatukuoni wewe ila ni mtu tu kama sisi, wala hatukuoni wamekufuata ila wale walio kuwa kwetu watu duni, wasio kuwa na akili. Wala hatukuoneni kuwa mna ubora wowote kutushinda sisi. Bali tuna hakika nyinyi ni waongo

Verse 28 — Surah Hud 11:28

Akasema: Enyi watu wangu! Hebu fikirini! Ikiwa mimi ninayo hoja wazi iliyo toka kwa Mola wangu Mlezi, na amenipa rehema kutoka kwake, nayo ikakufichikieni; je, tukulazimisheni kuikubali hali nyinyi mnaichukia

Verse 29 — Surah Hud 11:29

Na enyi watu wangu! Mimi sikuombeni mali kwa ajili ya haya. Mimi sina ujira ila kwa Mwenyezi Mungu; na mimi sitawafukuza walio amini. Hakika wao watakutana na Mola wao Mlezi, lakini mimi nakuoneni mnafanya ujinga

Verse 30 — Surah Hud 11:30

Na enyi watu wangu! Ni nani atakaye nisaidia kwa Mwenyezi Mungu nikiwafukuza hawa? Basi je, hamfikiri

Verse 31 — Surah Hud 11:31

Wala sikwambiini kuwa nina khazina za Mwenyezi Mungu; wala kuwa mimi najua mambo ya ghaibu; wala sisemi: Mimi ni Malaika. Wala siwasemi wale ambao yanawadharau macho yenu kuwa Mwenyezi Mungu hatawapa kheri - Mwenyezi Mungu anajua yaliomo katika nafsi zao - hapo bila ya shaka ninge kuwa miongoni mwa wenye kudhulumu

Verse 32 — Surah Hud 11:32

Wakasema: Ewe Nuhu! Umejadiliana, na umekithirisha kutujadili. Basi tuletee hayo unayo tuahidi, ukiwa miongoni mwa wasemao kweli

Verse 33 — Surah Hud 11:33

Akasema: Mwenyezi Mungu atakuleteeni akipenda. Wala nyinyi si wenye kumshinda

Verse 34 — Surah Hud 11:34

Wala nasaha yangu haikufaini kitu nikitaka kukunasihini, ikiwa Mwenyezi Mungu anataka kukuachieni mpotee. Yeye ndiye Mola wenu Mlezi; na kwake mtarejeshwa

Verse 35 — Surah Hud 11:35

Au ndio wanasema: Ameizua? Sema: Ikiwa nimeizua, basi kosa hilo ni juu yangu, na mimi sikhusiki na makosa myatendayo

Verse 36 — Surah Hud 11:36

Na akafunuliwa Nuhu akaambiwa: Hataamini yeyote katika watu wako ila wale walio kwisha amini. Basi usisikitike kwa waliyo kuwa wakiyatenda

Verse 37 — Surah Hud 11:37

Na unda jahazi mbele ya macho yetu na kwa mujibu wa ufunuo wetu. Wala usinisemeze kuwatetea walio dhulumu. Kwani hao bila ya shaka watazamishwa

Verse 38 — Surah Hud 11:38

Na akawa anaunda jahazi, na kila wakipita wakuu wa kaumu yake wakimkejeli. Yeye akasema: Ikiwa nyinyi mnatukejeli na sisi tunakukejelini kama mnavyo tukejeli

Verse 39 — Surah Hud 11:39

Nanyi mtakuja jua ni nani itakaye mfikia adhabu ya kumhizi, na itakaye mteremkia adhabu ya kudumu

Verse 40 — Surah Hud 11:40

Hata ilipo kuja amri yetu, na tanuri ikafoka maji, tulisema: Pakia humo wawili wawili, dume na jike, kutoka kila aina, na ahali zako, isipo kuwa wale ambao imekwisha wapitia hukumu; na watu walio amini. Na hawakuamini pamoja naye ila wachache tu

Verse 41 — Surah Hud 11:41

Na akasema: Pandeni humo kwa Bismillahi, Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, kwenda kwake na kusimama kwake. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu

Verse 42 — Surah Hud 11:42

Ikawa inakwenda nao katika mawimbi kama milima. Na Nuhu akamwita mwanawe naye alikuwa mbali: Ewe mwanangu! Panda pamoja nasi, wala usiwe pamoja na makafiri

Verse 43 — Surah Hud 11:43

Akasema: Nitakimbilia mlimani unilinde na maji. (Nuhu) akasema: Leo hapana wa kulindwa na amri ya Mwenyezi Mungu ila aliye mrehemu mwenyewe. Na wimbi likawatenganisha, akawa katika walio zama

Verse 44 — Surah Hud 11:44

Na ikasemwa: Ewe ardhi! Meza maji yako. Na Ewe mbingu! Jizuie. Basi maji yakadidimia chini, na amri ikapitishwa, na (jahazi) likasimama juu ya (mlima) wa Al Juudiy. Na ikasemwa: Wapotelee mbali watu walio dhulumu

Verse 45 — Surah Hud 11:45

Na Nuhu alimwomba Mola wake Mlezi: Ee Mola Mlezi wangu! Hakika mwanangu ni katika ahali zangu, na hakika ahadi yako ni haki. Na Wewe ni Mwenye haki kuliko mahakimu wote

Verse 46 — Surah Hud 11:46

Akasema: Ewe Nuhu! Huyu si katika ahali zako. Mwendo wake si mwema. Basi usiniombe jambo usio na ujuzi nalo. Mimi nakuwaidhi usije ukawa miongoni mwa wajinga

Verse 47 — Surah Hud 11:47

Nuhu akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Mimi najikinga kwako nisikuombe nisio na ujuzi nalo. Na kama hunisamehe na ukanirehemu, nitakuwa katika walio khasiri

Verse 48 — Surah Hud 11:48

Ikasemwa: Ewe Nuhu! Shuka kwa salama itokayo kwetu, na baraka nyingi juu yako na juu ya watu walio pamoja nawe. Na zitakuwapo kaumu tutakazo zistarehesha, na kisha zitashikwa na adhabu chungu itokayo kwetu

Verse 49 — Surah Hud 11:49

Hizi ni katika khabari za ghaibu tunazo kufunulia. Hukuwa ukizijua wewe, wala watu wako, kabla ya hii. Basi subiri! Hakika Mwisho ni wa wachamngu

Verse 50 — Surah Hud 11:50

Na kwa kina A'adi tulimtuma ndugu yao Hud. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu! Nyinyi hamna mungu isipo kuwa Yeye. Nyinyi si chochote ila ni wazushi tu

Verse 51 — Surah Hud 11:51

Enyi watu wangu! Sikuombeni ujira kwa ajili ya haya. Haukuwa ujira wangu ila kwa Yule aliye niumba. Basi hamtumii akili

Verse 52 — Surah Hud 11:52

Na enyi watu wangu! Muombeni msamaha Mola wenu Mlezi, kisha mtubie kwake. Atakuleteeni mbingu zenye kunyesha mvua ya kumiminika, na atakuzidishieni nguvu juu ya nguvu zenu. Wala msigeuke mkawa wakosefu

Verse 53 — Surah Hud 11:53

Wakasema: Ewe Hud! Hujatuletea dalili wazi. Wala sisi hatuiachi miungu yetu kwa kufuata kauli yako. Na wala sisi hatukuamini wewe

Verse 54 — Surah Hud 11:54

Sisi tunasema: Baadhi katika miungu yetu imekusibu kwa baa. Akasema: Hakika mimi namshuhudisha Mwenyezi Mungu, na nyinyi shuhudieni, ya kwamba mimi najitenga mbali na hao mnao wafanya washirika

Verse 55 — Surah Hud 11:55

Mkamwacha Yeye. Basi nyote nyinyi nipangieni vitimbi, na kisha msinipe muhula

Verse 56 — Surah Hud 11:56

Hakika mimi nimemtegemea Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wangu na Mola Mlezi wenu. Hapana kiumbe yeyote ila Yeye anamwendesha atakavyo. Hakika Mola wangu Mlezi yuko juu ya Njia Iliyo Nyooka

Verse 57 — Surah Hud 11:57

Na ikiwa watarudi nyuma, basi mimi nimekwisha kufikishieni niliyo tumwa kwenu. Na Mola wangu Mlezi atawaleta watu wengine badala yenu, wala nyinyi hamumdhuru kitu Yeye. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kuhifadhi kila kitu

Verse 58 — Surah Hud 11:58

Ilipo fika amri yetu, tulimwokoa Hud na walio amini pamoja naye, kwa rehema itokayo kwetu. Na tukawaokoa na adhabu ngumu

Verse 59 — Surah Hud 11:59

Na hao ndio kina A'adi. Walizikanusha Ishara za Mola wao Mlezi, na wakawaasi Mitume wake, na wakafuata amri ya kila jabari mwenye inda

Verse 60 — Surah Hud 11:60

Na wakafuatishiwa laana katika dunia hii na Siku ya Kiyama. Basi tambueni mtanabahi! Hakika kina A'adi walimkufuru Mola wao Mlezi. Na tambueni mtanabahi kuwa hakika waliangamizwa kina A'adi, kaumu ya Hud

Verse 61 — Surah Hud 11:61

Na kina Thamud tuliwapelekea ndugu yao Saleh. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Yeye ndiye aliye kuumbeni katika ardhi, na akakuwekeni humo. Basi mwombeni msamaha, kisha mtubu kwake. Hakika Mola wangu Mlezi yupo karibu, anaitikia maombi

Verse 62 — Surah Hud 11:62

Wakasema: Ewe Saleh! Hakika kabla ya haya ulikuwa unatarajiwa kheri kwetu. Je, unatukataza tusiwaabudu waliyo kuwa wakiwaabudu baba zetu? Na hakika sisi tuna shaka na wasiwasi kwa hayo unayo tuitia

Verse 63 — Surah Hud 11:63

Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa ninazo dalili zilizo wazi kutokana na Mola wangu Mlezi, naye akawa kanipa rehema kutoka kwake - je, ni nani atakaye ninusuru kwa Mwenyezi Mungu nikimuasi? Basi nyinyi hamtanizidishia ila khasara tu

Verse 64 — Surah Hud 11:64

Enyi watu wangu! Huyu ngamia wa Mwenyezi Mungu ni Ishara kwenu. Basi mwacheni ale katika ardhi ya Mwenyezi Mungu; wala msimguse kwa ubaya, isije ikakuangamizeni adhabu iliyo karibu

Verse 65 — Surah Hud 11:65

Wakamchinja. Basi (Saleh) akasema: Stareheni katika mji wenu muda wa siku tatu. Hiyo ni ahadi isiyo kuwa ya uwongo

Verse 66 — Surah Hud 11:66

Basi ilipo kuja amri yetu tulimwokoa Saleh na wale walio amini pamoja naye kwa rehema yetu kutokana na hizaya ya siku ile. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kushinda

Verse 67 — Surah Hud 11:67

Na ukelele uliwaangamiza wale walio dhulumu, wakapambazukiwa nao ni maiti majumbani mwao

Verse 68 — Surah Hud 11:68

Kama kwamba hawakuwako huko. Hebu zingatieni! Hakika kina Thamud walimkufuru Mola wao Mlezi. Hebu zingatieni! Thamud wamepotelea mbali

Verse 69 — Surah Hud 11:69

Na wajumbe wetu walimjia Ibrahim kwa bishara njema, wakasema: Salama! Naye akasema: Salama! Hakukaa ila mara akaleta ndama wa kuchoma

Verse 70 — Surah Hud 11:70

Basi alipoona mikono yao haimfikilii aliwatilia shaka, na akawaogopa. Wakasema: Usiogope! Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya Lut

Verse 71 — Surah Hud 11:71

Na mkewe alikuwa kasimama wima, akacheka. Basi tukambashiria (kuzaliwa) Is-haq, na baada ya Is-haq Yaaqub

Verse 72 — Surah Hud 11:72

Akasema: Je, hivyo mimi nizae, na hali yangu ni kikongwe na huyu mume wangu ni kizee? Hakika haya ni mambo ya ajabu

Verse 73 — Surah Hud 11:73

Wakasema: Je, unastaajabia amri ya Mwenyezi Mungu? Rehema ya Mwenyezi Mungu na baraka zake ziko juu yenu, enyi watu wa nyumba hii! Hakika Yeye ndiye Msifiwa wa kutukuzwa

Verse 74 — Surah Hud 11:74

Basi khofu ilipo mwondoka Ibrahim, na ikawa ile bishara imemfikia, alianza kujadiliana nasi juu ya kaumu ya Lut

Verse 75 — Surah Hud 11:75

Hakika Ibrahim alikuwa mpole, ana huruma, na mwepesi wa kurejea kwa Mwenyezi Mungu

Verse 76 — Surah Hud 11:76

(Akaambiwa): Ewe Ibrahim! Wachilia mbali haya! Kwa hakika amri ya Mola wako Mlezi imekwisha kuja, na hakika hao itawafikia adhabu isiyo rudi nyuma

Verse 77 — Surah Hud 11:77

Na wajumbe wetu walipo kuja kwa Lut' aliwahuzunukia na akawaonea dhiki. Akasema: Hii leo ni siku ngumu

Verse 78 — Surah Hud 11:78

Wakamjia kaumu yake mbio mbio. Na kabla ya haya walikuwa wakitenda maovu. Yeye akasema: Enyi watu wangu! Hawa binti zangu, ndio wametakasika zaidi kwenu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, wala msinihizi mbele ya wageni wangu. Hivyo, hamna hata mtu mmoja miongoni mwenu aliye ongoka

Verse 79 — Surah Hud 11:79

Wakasema: Bila shaka umekwisha jua hatuna haki juu ya binti zako, na unayajua tunayo yataka

Verse 80 — Surah Hud 11:80

Akasema: Laiti ningeli kuwa na nguvu kwenu, au nategemea kwenye nguzo yenye nguvu

Verse 81 — Surah Hud 11:81

(Wajumbe) wakasema: Ewe Lut'! Sisi ni wajumbe wa Mola wako Mlezi. Hawa hawatakufikia. Na wewe ondoka pamoja na ahali zako usiku ungalipo. Wala yeyote miongoni mwenu asitazame nyuma, isipo kuwa mkeo, kwani yeye utamfika msiba utakao wafika hao. Hakika miadi yao ni asubuhi. Je, asubuhi si karibu

Verse 82 — Surah Hud 11:82

Basi ilipo fika amri yetu tuliigeuza nchi juu chini, na tukawateremshia mvua ya changarawe za udongo mgumu ulio kamatana wa Motoni

Verse 83 — Surah Hud 11:83

Zilizo tiwa alama kwa Mola wako Mlezi. Na haya hayako mbali na wenye kudhulumu wengineo

Verse 84 — Surah Hud 11:84

Na kwa watu wa Madyana tuliwatumia ndugu yao Shua'ib. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye, wala msipunguze vipimo na mizani. Mimi nakuoneni mmo katika hali njema, nami nakukhofieni adhabu ya Siku kubwa hiyo itakayo kuzungukeni

Verse 85 — Surah Hud 11:85

Na enyi watu wangu! Timizeni vipimo na mizani kwa uadilifu wala msiwakhini watu vitu vyao; wala msieneze uovu katika nchi mkafanya uharibifu

Verse 86 — Surah Hud 11:86

Alivyo kubakishieni Mwenyezi Mungu ndiyo bora kwa ajili yenu, ikiwa nyinyi ni Waumini. Wala mimi siye mlinzi wenu

Verse 87 — Surah Hud 11:87

Wakasema: Ewe Shua'ibu! Ni sala zako ndizo zinazo kuamrisha tuyaache waliyo kuwa wakiyaabudu baba zetu, au tuache kufanya tupendavyo katika mali zetu? Ama hakika wewe ni mstahamilivu kweli na mwongofu

Verse 88 — Surah Hud 11:88

Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa ninayo dalili wazi inayo tokana na Mola wangu Mlezi, na ikawa Yeye ameniruzuku riziki njema kutoka kwake? Wala mimi sipendi kukukhalifuni nikafanya yale ninayo kukatazeni. Sitaki ila kutengeneza kiasi ninavyo weza. Na sipati kuwezeshwa haya ila na Mwenyezi Mungu. Kwake Yeye ninategemea, na kwake Yeye naelekea

Verse 89 — Surah Hud 11:89

Na enyi watu wangu! Kukhalifiana nami kusikupelekeeni hata mkasibiwa kama walivyo sibiwa watu wa Nuhu, au watu wa Hud, au watu wa Saleh. Na watu wa Lut' si mbali nanyi

Verse 90 — Surah Hud 11:90

Na ombeni msamaha kwa Mola wenu Mlezi, tena tubuni kwake. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kurehemu na Mwenye upendo

Verse 91 — Surah Hud 11:91

Wakasema: Ewe Shua'ibu! Mengi katika hayo unayo yasema hatuyafahamu. Na sisi tunakuona huna nguvu kwetu. Lau kuwa si jamaa zako tunge kupiga mawe, wala wewe si mtukufu kwetu

Verse 92 — Surah Hud 11:92

Akasema: Enyi watu wangu! Kwani jamaa zangu ni watukufu zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu? Na Yeye mmemueka nyuma ya migongo yenu! Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kuyazunguka yote mnayo yatenda

Verse 93 — Surah Hud 11:93

Na enyi watu wangu! Fanyeni mwezayo, na mimi pia ninafanya. Karibuni mtajua ni nani itakaye mfikia adhabu ya kumhizi, na nani aliye mwongo. Na ngojeni, mimi pia ninangoja pamoja nanyi

Verse 94 — Surah Hud 11:94

Na ilipo fika amri yetu, tulimwokoa Shua'ibu na wale walio amini pamoja naye kwa rehema yetu. Na ukelele uliwanyakua walio dhulumu, na wakapambaukiwa majumbani mwao wamekufa kifudifudi

Verse 95 — Surah Hud 11:95

Kama kwamba hawakuwamo humo. Zingatia walivyo angamia watu wa Madyana, kama walivyo angamia watu wa Thamud

Verse 96 — Surah Hud 11:96

Na hakika tulimtuma Musa pamoja na Ishara zetu na uthibitisho ulio wazi

Verse 97 — Surah Hud 11:97

Kwa Firauni na waheshimiwa wake. Lakini wao walifuata amri ya Firauni, na amri ya Firauni haikuwa yenye uwongofu

Verse 98 — Surah Hud 11:98

Siku ya Kiyama atawatangulia watu wake na atawaingiza Motoni. Na muingio muovu ulioje huo

Verse 99 — Surah Hud 11:99

Nao wamefuatishiwa laana hapa duniani na Siku ya Kiyama. Ni mabaya yalioje watakayo pewa

Verse 100 — Surah Hud 11:100

Hizi ni katika khabari za miji, tunakusimulia. Mingine ipo bado na mingine imefyekwa

Verse 101 — Surah Hud 11:101

Na Sisi hatukuwadhulumu, lakini wao wenyewe wamejidhulumu. Na miungu yao waliyo kuwa wakiiomba badala ya Mwenyezi Mungu haikuwafaa kitu ilipo kuja amri ya Mola wako Mlezi. Na hiyo miungu haikuwazidishia ila maangamizo tu

Verse 102 — Surah Hud 11:102

Na ndio kama hivyo ndivyo inavyo kuwa Mola wako Mlezi anapo ikamata miji inapo kuwa imedhulumu. Hakika mkamato wake ni mchungu na mkali

Verse 103 — Surah Hud 11:103

Hakika katika haya ipo ishara kwa yule anaye ogopa adhabu ya Akhera. Hiyo ndiyo Siku itakayo kusanyiwa watu, na hiyo ndiyo Siku itakayo shuhudiwa

Verse 104 — Surah Hud 11:104

Na Sisi hatuiakhirishi ila kwa muda unao hisabiwa

Verse 105 — Surah Hud 11:105

Siku hiyo itakapo fika, hatosema hata mtu mmoja ila kwa idhini yake Mwenyezi Mungu. Kati yao watakuwamo waliomo mashakani na wenye furaha

Verse 106 — Surah Hud 11:106

Ama wale wa mashakani hao watakuwamo Motoni wakiyayayatika na kukoroma

Verse 107 — Surah Hud 11:107

Watadumu humo muda wa kudumu mbingu na ardhi, isipo kuwa apendavyo Mola wako Mlezi. Hakika Mola wako Mlezi hutenda apendavyo

Verse 108 — Surah Hud 11:108

Na ama wale walio bahatika, wao watakuwamo Peponi wakidumu humo muda wa kudumu mbingu na ardhi, isipo kuwa apendavyo Mola wako Mlezi. Hicho ni kipawa kisio na ukomo

Verse 109 — Surah Hud 11:109

Basi usiwe na shaka juu ya wanayo yaabudu hao. Hawaabudu ila kama walivyo abudu baba zao zamani. Na hakika Sisi tutawatimilizia fungu lao bila ya kupunguzwa

Verse 110 — Surah Hud 11:110

Na kwa yakini tulimpa Musa Kitabu; zikazuka khitilafu ndani yake. Na lau kuwa si neno lilio kwisha tangulia kutoka kwa Mola wako Mlezi, bila ya shaka ingeli hukumiwa baina yao. Na hakika wao wamo katika shaka juu yake inayo wahangaisha

Verse 111 — Surah Hud 11:111

Na hakika Mola wako Mlezi atawatimilizia malipo ya vitendo vyao. Hakika Yeye anayo khabari ya wayatendayo

Verse 112 — Surah Hud 11:112

Basi, simama sawa sawa kama ulivyo amrishwa, wewe na wale wanao elekea kwa Mwenyezi Mungu pamoja nawe; wala msikiuke mipaka. Hakika Yeye anayaona yote myatendayo

Verse 113 — Surah Hud 11:113

Wala msiwategemee wanao dhulumu, usije ukakuguseni Moto. Wala nyinyi hamna walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, wala tena hamtasaidiwa

Verse 114 — Surah Hud 11:114

Na shika Sala katika ncha mbili za mchana na nyakati za usiku zilizo karibu na mchana. Hakika mema huondoa maovu. Huu ni ukumbusho kwa wanao kumbuka

Verse 115 — Surah Hud 11:115

Na subiri, kwani Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa wanao fanya wema

Verse 116 — Surah Hud 11:116

Basi mbona hawakuwamo katika watu wa kabla yenu wenye vyeo na wasaa wanao kataza uharibifu katika nchi, isipo kuwa wachache tu, ambao ndio tulio waokoa? Na walio dhulumu walifuata starehe zao, na wakawa ni wakosefu

Verse 117 — Surah Hud 11:117

Wala hakuwa Mola wako Mlezi wa kuihiliki miji kwa dhulma tu na hali watu wake ni watenda mema

Verse 118 — Surah Hud 11:118

Na Mola wako Mlezi angeli penda ange wafanya watu wote wakawa umma mmoja. Lakini hawaachi kukhitalifiana

Verse 119 — Surah Hud 11:119

Isipo kuwa wale ambao Mola wako Mlezi amewarehemu; na kwa hiyo ndio Mwenyezi Mungu amewaumba. Na litatimia neno la Mola wako Mlezi: Kweli kweli nitaijaza Jahannam kwa majini na watu pamoja

Verse 120 — Surah Hud 11:120

Na yote tunayo kusimulia katika khabari za Mitume ni ya kukupa nguvu moyo wako. Na katika haya imekujia haki na mawaidha na ukumbusho kwa Waumini

Verse 121 — Surah Hud 11:121

Na waambie wale wasio amini: Fanyeni muwezavyo, nasi pia tunafanya

Verse 122 — Surah Hud 11:122

Na ngojeni, na sisi tunangoja

Verse 123 — Surah Hud 11:123

Na ni vya Mwenyezi Mungu tu vyote vilivyo fichikana katika ardhi na mbingu, na mambo yote yatarejezwa kwake. Basi muabudu Yeye na umtegemee Yeye. Na Mola wako Mlezi haghafiliki na yale mnayo yatenda