Back to Languages

Swahili - Chapter 18 - Al-Kahf

Translation by Ali Muhsin Al Barwani — Permalink

Verse 1 — Surah Al-Kahf 18:1

Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu, ambaye amemteremshia mja wake Kitabu, wala hakukifanya kina upogo

Verse 2 — Surah Al-Kahf 18:2

Kimenyooka sawa, ili kitoe onyo kali kutoka kwake, na kiwabashirie Waumini watendao mema kwamba watapata ujira mzuri

Verse 3 — Surah Al-Kahf 18:3

Verse 4 — Surah Al-Kahf 18:4

Na kiwaonye wanao nena: Mwenyezi Mungu ana mwana

Verse 5 — Surah Al-Kahf 18:5

Wao hawana ujuzi wa jambo hili, wala baba zao. Ni neno kuu hilo litokalo vinywani mwao. Hawasemi ila uwongo tu

Verse 6 — Surah Al-Kahf 18:6

Huenda ukajihiliki nafsi yako kwa ajili yao, kuwasikitikia kwa kuwa hawayaamini mazungumzo haya

Verse 7 — Surah Al-Kahf 18:7

Kwa hakika tumevifanya vilioko juu ya ardhi kuwa ni pambo lake ili tuwafanyie mtihani, ni nani kati yao wenye vitendo vizuri zaidi

Verse 8 — Surah Al-Kahf 18:8

Na hakika Sisi tutavifanya vyote vilio juu ya ardhi kuwa kama nchi ilio pigwa na ukame

Verse 9 — Surah Al-Kahf 18:9

Bali unadhani ya kwamba wale Watu wa Pangoni na Maandishi walikuwa ni ajabu miongoni mwa ishara zetu

Verse 10 — Surah Al-Kahf 18:10

Vijana hao walipo kimbilia kwenye pango walisema: Mola wetu Mlezi! Tupe rehema itokayo kwako, na tutengezee uwongofu katika jambo letu

Verse 11 — Surah Al-Kahf 18:11

Tukayaziba masikio yao kuwalaza humo pangoni kwa muda wa miaka kadhaa wa kadhaa

Verse 12 — Surah Al-Kahf 18:12

Kisha tukawazindua ili tujue ni lipi katika makundi mawili lilio hisabu sawa muda walio kaa

Verse 13 — Surah Al-Kahf 18:13

Sisi tunakusimulia khabari zao kwa kweli. Hakika wao walikuwa ni vijana walio muamini Mola wao Mlezi. Na Sisi tukawazidisha uwongofu

Verse 14 — Surah Al-Kahf 18:14

Na tukazitia nguvu nyoyo zao walipo simama na wakasema: Mola wetu Mlezi ni Mola Mlezi wa mbingu na ardhi. Hatutamwita mwenginewe kabisa badala yake kuwa ni Mungu. Hivyo itakuwa tumesema jambo la kuvuka mpaka

Verse 15 — Surah Al-Kahf 18:15

Hawa watu wetu wameshika miungu mingine badala yake Yeye. Kwa nini basi hawawatolei uthibitisho ulio dhaahiri? Na nani aliye dhaalimu zaidi kuliko anaye mzulia uwongo Mwenyezi Mungu

Verse 16 — Surah Al-Kahf 18:16

Na mkijitenga nao na vile wanavyo viabudu badala ya Mwenyezi Mungu, basi kimbilieni pangoni, akufungulieni Mola wenu Mlezi rehema yake, na akutengenezeeni ya kukufaeni katika mambo yenu

Verse 17 — Surah Al-Kahf 18:17

Na unaliona jua linapo chomoza linainamia kuliani mwao kutoka hapo pangoni; na linapo kuchwa linawakwepa kushotoni, na wao wamo katika uwazi wa pango. Hizo ni katika ishara za Mwenyezi Mungu. Ambaye Mwenyezi Mungu anamwongoa basi huyo ni mwenye kuongoka. Na anaye muacha kupotea basi hutampatia mlinzi wala mwongozi

Verse 18 — Surah Al-Kahf 18:18

Nawe utawadhania wamacho, na hali wamelala. Nasi tunawageuza kulia na kushoto. Na mbwa wao amenyoosha miguu yake ya mbele kizingitini. Kama ungeli watokea hapana shaka ungeli geuka kuwakimbia, nawe umejaa khofu

Verse 19 — Surah Al-Kahf 18:19

Na kwa namna hii tuliwainua usingizini wapate kuulizana wao kwa wao. Alisema msemaji katika wao: Mmekaa muda gani? Wakasema: Tumekaa siku moja au sehemu ya siku. Wakasema: Mola wenu Mlezi anajua zaidi muda mlio kaa. Hebu mtumeni mmoja wenu na hizi fedha zenu ende mjini, akatazame chakula chake kipi kilicho bora kabisa akuleteeni cha kukila. Naye afanye mambo hayo kwa busara, wala asikutajeni kabisa kwa yeyote

Verse 20 — Surah Al-Kahf 18:20

Kwani wao wakikutambueni watakupigeni mawe, au watakurudisheni katika dini yao; na hapo hamtafanikiwa kabisa

Verse 21 — Surah Al-Kahf 18:21

Na namna hivi tuliwa juulisha kwa watu wapate kujua ya kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli, na kwamba Saa haina shaka. Walipo kuwa wakigombania jambo lao wao kwa wao walisema: Jengeni jengo juu yao. Mola wao Mlezi anawajua vyema. Wakasema walio shinda katika shauri yao: Bila ya shaka tutawajengea msikiti juu yao

Verse 22 — Surah Al-Kahf 18:22

Watasema: Walikuwa watatu, wa nne wao ni mbwa wao. Na wanasema: Walikuwa watano, wa sita wao ni mbwa wao. Wanavurumisha ovyo. Na wanasema: Walikuwa saba, na wa nane wao ni mbwa wao. Sema: Mola wangu Mlezi ndiye anaye jua sawa sawa hisabu yao. Hawawajui ila wachache tu. Basi usibishane juu yao ila kwa mabishano ya juu juu tu hivi. Wala usiulize khabari zao kwa yeyote yule

Verse 23 — Surah Al-Kahf 18:23

Wala usisema kamwe kwa jambo lolote lile: Hakika nitalifanya hilo kesho

Verse 24 — Surah Al-Kahf 18:24

Isipo kuwa Mwenyezi Mungu akipenda. Na mkumbuke Mola wako Mlezi pale unapo sahau, na sema: Asaa Mola wangu Mlezi ataniongoa kwenye uwongozi ulio karibu zaidi kuliko huu

Verse 25 — Surah Al-Kahf 18:25

Na walikaa katika pango lao miaka mia tatu, na wakazidisha tisa

Verse 26 — Surah Al-Kahf 18:26

Sema: Mwenyezi Mungu anajua zaidi muda walio kaa. Ni zake tu siri za mbingu na ardhi. Kuona kulioje na kusikia kwake! Hawana mlinzi isipo kuwa Yeye, wala hamshirikishi yeyote katika hukumu yake

Verse 27 — Surah Al-Kahf 18:27

Na soma uliyo funuliwa katika Kitabu cha Mola wako Mlezi. Hapana wa kubadilisha maneno yake. Wala nawe hutapata makimbilio isipo kuwa kwake

Verse 28 — Surah Al-Kahf 18:28

Na isubirishe nafsi yako pamoja na wanao muomba Mola wao Mlezi asubuhi na jioni, hali ya kuwa wanataka radhi yake. Wala macho yako yasiwaruke kwa kutaka pambo la maisha ya dunia. Wala usimt'ii tuliye mghafilisha moyo wake asitukumbuke, na akafuata matamanio yake yakawa yamepita mpaka

Verse 29 — Surah Al-Kahf 18:29

Na sema: Hii ni kweli itokayo kwa Mola wako Mlezi. Basi atakaye, aamini. Na atakaye, akatae. Hakika Sisi tumewaandalia wenye kudhulumu Moto ambao utawazunguka kama khema. Na wakiomba msaada watasaidiwa kwa kupewa maji kama mafuta yaliyo tibuka. Yatayo wababua nyuso zao. Kinywaji hicho ni kiovu mno! Na matandiko hayo ya kupumzikia ni maovu mno

Verse 30 — Surah Al-Kahf 18:30

Hakika wale walio amini na wakatenda mema - hakika Sisi hatupotezi ujira wa anaye tenda mema

Verse 31 — Surah Al-Kahf 18:31

Hao watapata Bustani za milele, zinazo pita mito kati yake. Humo watapambwa kwa mavazi ya mikononi ya dhahabu, na watavaa nguo za kijani za hariri na at'ilasi, huku wakiegemea humo juu ya makochi. Ni malipo bora hayo! Na matandiko mazuri mno ya kupumzikia

Verse 32 — Surah Al-Kahf 18:32

Na wapigie mfano wa watu wawili: mmoja wao tulimpa vitalu viwili vya mizabibu, na tukavizungushia mitende, na kati yake tukatia mimea ya nafaka

Verse 33 — Surah Al-Kahf 18:33

Na hivyo vitalu viwili vikitoa mazao yake, wala hapana kitu katika hayo kilicho tindikia. Na ndani yake tukapasua mito

Verse 34 — Surah Al-Kahf 18:34

Naye alikuwa na mazao mengi. Basi akamwambia mwenzake naye akibishana naye: Mimi nimekushinda wewe kwa mali na nguvu za watu

Verse 35 — Surah Al-Kahf 18:35

Na akaingia kitaluni kwake, naye hali anajidhulumu nafsi yake. Akasema: Sidhani kabisa kuwa haya yataharibika

Verse 36 — Surah Al-Kahf 18:36

Wala sidhani kuwa hiyo Saa (ya Kyama) itatokea. Na ikiwa nitarudishwa kwa Mola wangu Mlezi, bila ya shaka nitapata marejeo bora zaidi kuliko haya

Verse 37 — Surah Al-Kahf 18:37

Mwenzake akamwambia kwa kubishana naye: Je! Unamkufuru aliye kuumba kutokana na udongo, tena kutokana na tone la manii, kisha akakufanya mtu kaamili

Verse 38 — Surah Al-Kahf 18:38

Lakini Yeye Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu Mlezi. Wala simshirikishi na yeyote

Verse 39 — Surah Al-Kahf 18:39

Na lau kuwa ulipo ingia kitaluni kwako ungeli sema: Mashaallah! Alitakalo Mwenyezi Mungu huwa! Hapana nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu. Ikiwa unaniona mimi nina mali kidogo na watoto kuliko wewe

Verse 40 — Surah Al-Kahf 18:40

Basi huenda Mola wangu Mlezi akanipa kilicho bora kuliko kitalu chako, naye akapitisha kudra yake kutoka mbinguni kukilitea hicho chako, na kikageuka ardhi tupu inayo teleza

Verse 41 — Surah Al-Kahf 18:41

Au maji yake yakadidimia wala usiweze kuyagundua

Verse 42 — Surah Al-Kahf 18:42

Yakateketezwa matunda yake, akabaki akipindua pindua viganja vyake, kwa vile alivyo yagharimia, na miti imebwagika juu ya chanja zake. Akawa anasema: Laiti nisingeli mshiriki Mola wangu Mlezi na yeyote

Verse 43 — Surah Al-Kahf 18:43

Wala hakuwa nacho kikundi cha kumsaidia badala ya Mwenyezi Mungu, wala mwenyewe hakuweza kujisaidia

Verse 44 — Surah Al-Kahf 18:44

Huko ulinzi ni wa Mwenyezi Mungu wa Haki tu. Yeye ndiye mbora wa malipo, na mbora wa matokeo

Verse 45 — Surah Al-Kahf 18:45

Na wapigie mfano wa maisha ya dunia. Hayo ni kama maji tunayo yateremsha kutoka mbinguni, yakachanganyika na mimea ya ardhi, kisha hiyo mimea ikawa vibuwa vinavyo peperushwa na upepo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu

Verse 46 — Surah Al-Kahf 18:46

Mali na wana ni pambo la maisha ya dunia. Na mema yanayo bakia ni bora mbele ya Mola wako Mlezi kwa malipo, na bora kwa matumaini

Verse 47 — Surah Al-Kahf 18:47

Na siku tutapo iondoa milima na ukaiona ardhi iwazi, na tukawafufua - wala hatutamwacha hata mmoja kati yao

Verse 48 — Surah Al-Kahf 18:48

Na wakahudhurishwa mbele ya Mola wako Mlezi kwa safu (wakaambiwa): Mmetujia kama tulivyo kuumbeni mara ya kwanza! Bali mlidai kwamba hatutakuwekeeni miadi

Verse 49 — Surah Al-Kahf 18:49

Na kitawekwa kitabu. Basi utawaona wakosefu wanavyo ogopa kwa yale yaliomo humo. Na watasema: Ole wetu! Kitabu hichi kina nini! Hakiachi dogo wala kubwa ila huliandika? Na watayakuta yote waliyo yatenda yamehudhuria hapo. Na Mola wako Mlezi hamdhulumu yeyote

Verse 50 — Surah Al-Kahf 18:50

Na tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam! Walimsjudia isipo kuwa Iblisi. Yeye alikuwa miongoni mwa majini, na akavunja amri ya Mola wake Mlezi. Je! Mnamshika yeye na dhuriya zake kuwa marafiki badala yangu, hali wao ni adui zenu? Ni ovu mno badala hii kwa wenye kudhulumu

Verse 51 — Surah Al-Kahf 18:51

Sikuwashuhudisha kuumbwa kwa mbingu na ardhi, wala kuumbwa kwa nafsi zao. Wala sikuwafanya wapotezao kuwa ni wasaidizi

Verse 52 — Surah Al-Kahf 18:52

Na siku atakapo sema (Mwenyezi Mungu): Waiteni hao mlio dai kuwa ni washirika wangu. Basi watawaita, na wao hawato waitikia. Nasi tutaweka baina yao maangamio

Verse 53 — Surah Al-Kahf 18:53

Na wakhalifu watauona Moto na watajua ya kwamba wao lazima wataingia humo; wala hawatapata pa kuuepuka

Verse 54 — Surah Al-Kahf 18:54

Na bila ya shaka tumewaelezea watu katika hii Qur'ani kila namna ya mfano. Lakini mwanaadamu amezidi kuliko kila kitu kwa ubishi

Verse 55 — Surah Al-Kahf 18:55

Na hapana kilicho wazuia watu kuamini ulipo wajia uwongofu na wakaomba maghfira kwa Mola wao Mlezi, isipo kuwa yawafikie ya wale wa zamani, au iwafikie adhabu jahara

Verse 56 — Surah Al-Kahf 18:56

Na hatuwatumi Mitume ila wawe wabashiri na waonyaji. Na walio kufuru wanabishana kwa uwongo, ili kwa uwongo huo waivunje kweli. Na wanazifanya Ishara zangu na yale waliyo onywa kuwa ni mzaha

Verse 57 — Surah Al-Kahf 18:57

Na ni nani dhaalimu mkubwa zaidi kuliko yule anaye kumbushwa Ishara za Mola wake Mlezi, naye akazipuuza na akasahau yaliyo tangulizwa na mikono yake? Hakika Sisi tumeweka vifuniko juu ya nyoyo zao ili wasifahamu, na uziwi kwenye masikio yao. Na ukiwaita kwenye uwongofu hawakubali kabisa kuongoka

Verse 58 — Surah Al-Kahf 18:58

Na Mola wako Mlezi ni Msamehevu Mwenye rehema. Lau angeli wachukulia kwa mujibu waliyo yachuma, bila ya shaka angeli wafanyia haraka kuwaadhibu. Lakini wanayo miadi ambayo hawatapata makimbilio yoyote ya kuepukana nayo

Verse 59 — Surah Al-Kahf 18:59

Na miji hiyo tuliwaangamiza watu wake walipo dhulumu. Na tukawawekea miadi ya maangamizo yao

Verse 60 — Surah Al-Kahf 18:60

Na pale Musa alipo mwambia kijana wake: Sitoacha kuendelea mpaka nifike zinapo kutana bahari mbili, au nitaendelea kwa muda mrefu

Verse 61 — Surah Al-Kahf 18:61

Basi wawili hao walipo fika zinapo kutana hizo bahari mbili walimsahau samaki wao, naye akashika njia yake kaporonyokea baharini

Verse 62 — Surah Al-Kahf 18:62

Walipo kwisha pita alimwambia kijana wake: Tupe chakula chetu cha mchana. Kwa hakika tumepata machofu kweli kwa hii safari yetu

Verse 63 — Surah Al-Kahf 18:63

Akasema (kijana): Waona! Pale tulipo pumzika penye jabali basi mimi nilimsahau yule samaki. Na hapana aliye nisahaulisha nisimkumbuke ila Shet'ani tu. Naye akashika njia yake baharini kwa ajabu

Verse 64 — Surah Al-Kahf 18:64

(Musa) akasema: Hayo ndiyo tuliyo kuwa tunayataka. Basi wakarudi nyuma kwa kufuata njia waliyo jia

Verse 65 — Surah Al-Kahf 18:65

Basi wakamkuta mja katika waja wangu tuliye mpa rehema kutoka kwetu, na tukamfunza mafunzo yaliyo toka kwetu

Verse 66 — Surah Al-Kahf 18:66

Musa akamwambia: Nikufuate ili unifunze katika ule uwongofu ulio funzwa wewe

Verse 67 — Surah Al-Kahf 18:67

Akasema: Hakika wewe hutaweza kuvumilia kuwa pamoja nami

Verse 68 — Surah Al-Kahf 18:68

Na utawezaje kuvumilia yale usiyo yajua vilivyo undani wake

Verse 69 — Surah Al-Kahf 18:69

Akasema: Inshaallah, Mwenyezi Mungu akipenda, utaniona mvumilivu, wala sitoasi amri yako

Verse 70 — Surah Al-Kahf 18:70

Akasema: Basi ukinifuata usiniulize kitu mpaka mimi nianze kukutajia

Verse 71 — Surah Al-Kahf 18:71

Basi wawili hao wakatoka, hata walipo panda jahazi (yule mtu) akaitoboa. (Musa) akasema: Unaitoboa uwazamishe watu wake? Hakika umefanya jambo baya

Verse 72 — Surah Al-Kahf 18:72

Akasema: Sikukwambia hutaweza kuvumilia kuwa pamoja nami

Verse 73 — Surah Al-Kahf 18:73

(Musa) akasema: Usinichukulie kwa niliyo sahau, wala usinipe uzito kwa jambo langu

Verse 74 — Surah Al-Kahf 18:74

Basi wakatoka wawili hao mpaka wakamkuta kijana, akamuuwa. (Musa) akasema: Ala! Umemuuwa mtu asiye na kosa, na wala hakuuwa! Ama hakika umefanya jambo baya kabisa

Verse 75 — Surah Al-Kahf 18:75

AKASEMA: Je! Sikukwambia kwamba hakika wewe huwezi kuvumilia kuwa pamoja nami

Verse 76 — Surah Al-Kahf 18:76

Akasema: Nikikuuliza kitu chochote baada ya haya usifuatane nami, kwani umekwisha pata udhuru kwangu

Verse 77 — Surah Al-Kahf 18:77

Basi wakatoka mpaka wakawafikia watu wa mji mmoja. Wakawaomba watu wake wawape chakula, nao wakakataa kuwakaribisha. Hapo wakakuta ukuta unataka kuanguka, (yule mja mwema) akausimamisha. (Musa) akasema: Ungeli taka ungeli chukua ujira kwa haya

Verse 78 — Surah Al-Kahf 18:78

(Yule mtu) akasema: Huku ndio kufarikiana baina yangu na wewe. Sasa nitakueleza maana ya yale uliyo kuwa huwezi kuyastahamilia

Verse 79 — Surah Al-Kahf 18:79

Ama ile jahazi ilikuwa ya masikini za Mungu wafanyao kazi baharini. Nilitaka kuiharibu, kwani nyuma yao alikuwako mfalme anaghusubu majahazi yote

Verse 80 — Surah Al-Kahf 18:80

Na ama yule kijana, wazazi wake walikuwa ni Waumini. Tukakhofu asije watia mashakani kwa uasi na ukafiri

Verse 81 — Surah Al-Kahf 18:81

Basi tulitaka Mola wao Mlezi awabadilishie aliye bora zaidi kuliko huyo kwa kutakasika, na aliye karibu zaidi kwa huruma

Verse 82 — Surah Al-Kahf 18:82

Na ama ukuta, huo ulikuwa ni wa vijana wawili mayatima kule mjini. Na chini yake ilikuwako khazina yao; na baba yao alikuwa ni mtu mwema. Basi Mola wako Mlezi alitaka wafikie utu uzima na wajitolee khazina yao wenyewe, kuwa ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Wala mimi sikutenda hayo kwa amri yangu. Hiyo ndiyo tafsiri ya hayo ambayo wewe hukuweza kuyasubiria

Verse 83 — Surah Al-Kahf 18:83

Na wanakuuliza khabari za Dhul- Qarnaini. Waambie: Nitakusimulieni baadhi ya hadithi yake

Verse 84 — Surah Al-Kahf 18:84

Sisi tulimtilia nguvu katika ardhi na tukampa njia za kila kitu

Verse 85 — Surah Al-Kahf 18:85

Verse 86 — Surah Al-Kahf 18:86

Hata alipo fika machwea-jua aliliona linatua katika checmchem yenye matope meusi. Na hapo akawakuta watu. Tukasema: Ewe Dhul-Qarnaini! Ama uwaadhibu au watwae kwa wema

Verse 87 — Surah Al-Kahf 18:87

Akasema: Ama aliye dhulumu basi tutamuadhibu, na kisha atarudishwa kwa Mola wake Mlezi amuadhibu adhabu isiyo juulikana

Verse 88 — Surah Al-Kahf 18:88

Na ama aliye amini na akatenda mema basi atapata malipo mazuri. Nasi tutamwambia lilio jepesi katika amri yetu

Verse 89 — Surah Al-Kahf 18:89

Kisha akaifuata njia

Verse 90 — Surah Al-Kahf 18:90

Hata alipo fika matokeo ya jua aliliona linawachomozea watu tusio wawekea pazia la kuwakinga nalo

Verse 91 — Surah Al-Kahf 18:91

Ndio hivyo hivyo. Na Sisi tulizijua vilivyo khabari zake zote

Verse 92 — Surah Al-Kahf 18:92

Kisha akaifuata njia

Verse 93 — Surah Al-Kahf 18:93

Hata alipo fika baina ya milima miwili, alikuta nyuma yake watu ambao takriban hawakuwa wanafahamu lolote

Verse 94 — Surah Al-Kahf 18:94

Wakasema: Ewe Dhul-Qarnaini! Hakika Juju-wa-maajuju wanafanya uharibifu katika nchi. Basi je, tukulipe ujira ili utujengee baina yetu na wao ngome

Verse 95 — Surah Al-Kahf 18:95

Akasema: Yale Mola wangu aliyo niwezesha ni bora zaidi. Lakini nyinyi nisaidieni kwa nguvu zenu. Nitakujengeeni kizuizi baina yenu na wao

Verse 96 — Surah Al-Kahf 18:96

Nileteeni vipande vya chuma. Hata alipo ijaza nafasi iliyo kati ya milima miwili, akasema: Vukuteni. Hata alipo kifanya (chuma) kama moto akasema: Nileteeni shaba iliyo yayuka niimwagie

Verse 97 — Surah Al-Kahf 18:97

Basi hawakuweza kuukwea, wala hawakuweza kuutoboa

Verse 98 — Surah Al-Kahf 18:98

Akasema: Hii ni rehema itokayo kwa Mola wangu Mlezi. Na itapo fika ahadi ya Mola wangu Mlezi atauvunja vunja. Na ahadi ya Mola wangu Mlezi ni kweli tu

Verse 99 — Surah Al-Kahf 18:99

Na siku hiyo tutawaacha wakisongana wao kwa wao. Na baragumu litapulizwa, na wote watakusanywa pamoja

Verse 100 — Surah Al-Kahf 18:100

Na siku hiyo tutawadhihirishia wazi Jahannamu makafiri waione

Verse 101 — Surah Al-Kahf 18:101

Wale ambao kwamba macho yao yalikuwa paziani hayanikumbuki, na wakawa hawawezi kusikia

Verse 102 — Surah Al-Kahf 18:102

Je, wanadhani walio kufuru ndio wawafanye waja wangu ndio walinzi wao badala yangu Mimi? Hakika Sisi tumeiandaa Jahannamu iwe ndipo mahala pa kuteremkia makafiri

Verse 103 — Surah Al-Kahf 18:103

Sema: Je, tukutajieni wenye khasara mno katika vitendo vyao

Verse 104 — Surah Al-Kahf 18:104

Ni wale ambao juhudi yao katika maisha ya dunia imepotea bure, nao wanadhani kwamba wanafanya kazi nzuri

Verse 105 — Surah Al-Kahf 18:105

Hao ni wale walio zikanusha Ishara za Mola wao Mlezi na kukutana naye. Kwa hivyo vitendo vyao vimepotea bure, na wala Siku ya Kiyama hatutawathamini kitu

Verse 106 — Surah Al-Kahf 18:106

Hiyo Jahannamu ni malipo yao kwa walivyo kufuru na wakafanyia kejeli Ishara zangu na Mitume wangu

Verse 107 — Surah Al-Kahf 18:107

Hakika wale walio amini na wakatenda mema mashukio yao yatakuwa kwenye Pepo za Firdausi

Verse 108 — Surah Al-Kahf 18:108

Watadumu humo; hawatataka kuondoka

Verse 109 — Surah Al-Kahf 18:109

Sema: Lau kuwa bahari ndio wino kwa maneno ya Mola wangu Mlezi, basi bahari ingeli malizika kabla ya kumalizika maneno ya Mola wangu Mlezi, hata tungeli ileta mfano wa hiyo kuongezea

Verse 110 — Surah Al-Kahf 18:110

Sema: Mimi ni mwanaadamu kama nyinyi. Ninaletewa Wahyi kwamba Mungu wenu ni Mungu Mmoja. Mwenye kutaraji kukutana na Mola wake Mlezi basi naatende vitendo vyema, wala asimshirikishe yeyote katika ibada ya Mola wake Mlezi