Back to LanguagesPrevious ChapterNext Chapter
Swahili - Chapter 21 - Al-Anbiya
Translation by Ali Muhsin Al Barwani — Permalink
Verse 1 — Surah Al-Anbiya 21:1
IMEWAKARIBIA watu hisabu yao, nao wamo katika mghafala wanapuuza
Verse 2 — Surah Al-Anbiya 21:2
Hayawafikilii mawaidha mapya kutoka kwa Mola wao Mlezi ila huyasikiliza na huku wanafanya mchezo
Verse 3 — Surah Al-Anbiya 21:3
Zimeghafilika nyoyo zao. Na wale walio dhulumu hunong'onezana kwa siri: Ni nani ati huyu isipo kuwa ni binaadamu tu kama nyinyi! Mnauwendea uchawi hali nanyi mnaona
Verse 4 — Surah Al-Anbiya 21:4
Alisema: Mola wangu Mlezi anayajua yasemwayo mbinguni na katika ardhi. Na Yeye ni Mwenye kusikia Mwenye kujua
Verse 5 — Surah Al-Anbiya 21:5
Lakini wao walisema: Hizo ni ndoto za ovyo ovyo, bali amezizua tu, bali huyo ni mtunga mashairi. Basi atuletee miujiza kama walivyo tumwa wale wa mwanzo
Verse 6 — Surah Al-Anbiya 21:6
Hawakuamini kabla yao watu wa mji tulio uangamiza. Basi, je, wataamini hawa
Verse 7 — Surah Al-Anbiya 21:7
Na kabla yako hatukuwatuma ila watu wanaume tulio wapa wahyi (ufunuo). Basi waulizeni wenye ilimu ikiwa nyinyi hamjui
Verse 8 — Surah Al-Anbiya 21:8
Wala hatukuwafanya miili isiyo kula chakula, wala hawakuwa wenye kuishi milele
Verse 9 — Surah Al-Anbiya 21:9
Kisha tukawatimizia miadi, na tukawaokoa wao na tulio wataka, na tukawateketeza walio pita mipaka
Verse 10 — Surah Al-Anbiya 21:10
Na hakika tumekuteremshieni Kitabu ambacho ndani yake yamo makumbusho yenu. Je! Hamzingatii
Verse 11 — Surah Al-Anbiya 21:11
Na mingapi katika miji iliyo kuwa ikidhulumu tumeiteketeza, na tukawasimamisha baada yao watu wengine
Verse 12 — Surah Al-Anbiya 21:12
Basi walipo ihisi adhabu yetu, mara wakaanza kukimbia
Verse 13 — Surah Al-Anbiya 21:13
Msikimbie! Na rejeeni kwenye zile zile starehe zenu, na maskani zenu, mpate kusailiwa
Verse 14 — Surah Al-Anbiya 21:14
Wakasema: Ole wetu! Hakika sisi tulikuwa madhaalimu
Verse 15 — Surah Al-Anbiya 21:15
Hakikuacha hicho kuwa kilio chao mpaka tukawafanya kama walio fyekwa, wamezimika
Verse 16 — Surah Al-Anbiya 21:16
Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yao kwa mchezo
Verse 17 — Surah Al-Anbiya 21:17
Kama tungeli taka kufanya mchezo tunge jifanyia Sisi wenyewe, lau kwamba tungeli kuwa ni wafanyao mchezo
Verse 18 — Surah Al-Anbiya 21:18
Bali tunaitupa kweli juu ya uwongo ikauvunja na mara ukatoweka. Na ole wenu kwa mnayo yazua
Verse 19 — Surah Al-Anbiya 21:19
Na ni vyake Yeye tu Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na katika ardhi. Na walioko kwake hawafanyi kiburi wakaacha kumuabudu, wala hawachoki
Verse 20 — Surah Al-Anbiya 21:20
Wanamtakasa usiku na mchana, wala hawanyong'onyei
Verse 21 — Surah Al-Anbiya 21:21
Au wamepata miungu katika ardhi inayo fufua
Verse 22 — Surah Al-Anbiya 21:22
Lau wangeli kuwamo humo miungu wengine isipo kuwa Mwenyezi Mungu basi bila ya shaka hizo mbingu na ardhi zingeli fisidika. Subahana 'Llah Ametakasika Mwenyezi Mungu, Bwana wa A'rshi (Kiti cha Enzi), na hayo wanayo yazua
Verse 23 — Surah Al-Anbiya 21:23
Yeye hahojiwi kwa ayatendayo, na wao ndio wanao hojiwa kwa wayatendayo
Verse 24 — Surah Al-Anbiya 21:24
Au wanawaabudu miungu mingine badala yake? Sema: Leteni ushahidi wenu! Haya ni ukumbusho wa hawa walio nami, na ukumbusho wa walio kabla yangu. Lakini wengi wao hawaijui kweli, na kwa hivyo wanapuuza
Verse 25 — Surah Al-Anbiya 21:25
Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimfunulia ya kwamba hapana mungu isipo kuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu
Verse 26 — Surah Al-Anbiya 21:26
Na wanasema: Arrahman, Mwingi wa Rehema, ana mwana! Subhanahu, Ametakasika na hayo! Bali hao (wanao waita wana) ni watumwa walio tukuzwa
Verse 27 — Surah Al-Anbiya 21:27
Hawamtangulii kwa neno, nao wanafanya amri zake
Verse 28 — Surah Al-Anbiya 21:28
Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Wala hawamwombei yeyote ila yule anaye mridhia Yeye, nao kwa ajili ya kumwogopa wananyenyekea
Verse 29 — Surah Al-Anbiya 21:29
Na yeyote kati yao atakaye sema: Mimi ni mungu, badala yake, basi huyo tutamlipa malipo yake Jahannamu. Hivyo ndivyo tuwalipavyo wenye kudhulumu
Verse 30 — Surah Al-Anbiya 21:30
Je! Hao walio kufuru hawakuona kwamba mbingu na ardhi zilikuwa zimeambatana, kisha Sisi tukazibabandua? Na tukajaalia kwa maji kila kilicho hai? Basi je, hawaamini
Verse 31 — Surah Al-Anbiya 21:31
Na tukaweka katika ardhi milima iliyo thibiti ili isiwayumbishe, na tukaweka humo njia pana ili wapate kuongoka
Verse 32 — Surah Al-Anbiya 21:32
Na tukaifanya mbingu kuwa dari iliyo hifadhiwa, lakini wanazipuuza Ishara zake
Verse 33 — Surah Al-Anbiya 21:33
Na Yeye ndiye aliye umba usiku na mchana na jua na mwezi, vyote katika anga vinaogelea
Verse 34 — Surah Al-Anbiya 21:34
Nasi hatukumjaalia mwanaadamu yeyote kabla yako kuwa na maisha ya milele. Basi je! Ukifa wewe, wao wataishi milele
Verse 35 — Surah Al-Anbiya 21:35
Kila nafsi itaonja mauti; na tunakujaribuni kwa mtihani wa shari na kheri. Na kwetu Sisi mtarejeshwa
Verse 36 — Surah Al-Anbiya 21:36
Na wakikuona walio kufuru hawakufanyi wewe ila ni kitu cha maskhara tu, (wakisema): Je! Ndiye huyu anaye itaja miungu yenu? Na hali wao wanakataa kumkumbuka Arrahman, Mwingi wa Rehema
Verse 37 — Surah Al-Anbiya 21:37
Mwanaadamu ameumbwa na haraka. Nitakuonyesheni Ishara zangu. Basi msinihimize
Verse 38 — Surah Al-Anbiya 21:38
Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi mnasema kweli
Verse 39 — Surah Al-Anbiya 21:39
Lau wangeli jua wale walio kufuru wakati ambao hawatauzuia Moto kwenye nyuso zao wala migongo yao, na wala hawatanusuriwa
Verse 40 — Surah Al-Anbiya 21:40
Bali utawafikia kwa ghafla, na utawashitua na wala hawataweza kuurudisha, wala hawatapewa muhula
Verse 41 — Surah Al-Anbiya 21:41
Na Mitume walio kabla yako walikwisha dhihakiwa. Kwa hivyo wale walio wafanyia maskhara yaliwafika yale waliyo kuwa wakiyafanyia dhihaka
Verse 42 — Surah Al-Anbiya 21:42
Sema: Nani anaye kulindeni usiku na mchana na Arrahmani Mwingi wa Rehema? Bali wao wanapuuza kumkumbuka Mola wao Mlezi
Verse 43 — Surah Al-Anbiya 21:43
Au wao wanao miungu watao weza kuwakinga nasi? Hao hawawezi kujinusuru nafsi zao, wala hawatalindwa nasi
Verse 44 — Surah Al-Anbiya 21:44
Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka umri ukawa mrefu kwao. Je, hawaoni ya kwamba Sisi tunaifikia ardhi tukiipunguza ncha zake? Basi je! Hao ni wenye kushinda
Verse 45 — Surah Al-Anbiya 21:45
Sema: Mimi nakuonyeni kwa Wahyi. Na viziwi hawasikii wito wanapo onywa
Verse 46 — Surah Al-Anbiya 21:46
Na wanapo guswa na mpulizo mmoja tu wa adhabu itokayo kwa Mola wako Mlezi, bila ya shaka wao husema: Ole wetu! Hakika tulikuwa wenye kudhulumu
Verse 47 — Surah Al-Anbiya 21:47
Nasi tutaweka mizani za uadilifu kwa Siku ya Kiyama. Basi nafsi haitadhulumiwa kitu chochote. Hata ikiwa ni uzito wa chembe ya khardali tutaileta. Nasi tunatosha kuwa washika hisabu
Verse 48 — Surah Al-Anbiya 21:48
Na kwa yakini tuliwapa Musa na Haaruni kipambanuzi, na mwangaza, na makumbusho kwa wachamngu
Verse 49 — Surah Al-Anbiya 21:49
Ambao wanamkhofu Mola wao Mlezi faraghani, na wanaiogopa Saa ya Kiyama
Verse 50 — Surah Al-Anbiya 21:50
Na haya ni makumbusho yaliyo barikiwa, tuliyo yateremsha. Basi je! Mnayakataa
Verse 51 — Surah Al-Anbiya 21:51
Na hakika tulikwisha mpa Ibrahim uwongofu wake zamani, na tulikuwa tunamjua
Verse 52 — Surah Al-Anbiya 21:52
Alipo mwambia baba yake na watu wake: Ni nini haya masanamu mnayo yashughulikia kuyaabudu
Verse 53 — Surah Al-Anbiya 21:53
Wakasema: Tumewakuta baba zetu wakiyaabudu
Verse 54 — Surah Al-Anbiya 21:54
Akasema: Bila ya shaka nyinyi na baba zenu mmekuwa katika upotofu ulio dhaahiri
Verse 55 — Surah Al-Anbiya 21:55
Wakasema: Je! Umetujia kwa maneno ya kweli au wewe ni katika wachezao tu
Verse 56 — Surah Al-Anbiya 21:56
Akasema: Bali Mola wenu Mlezi ni Mola Mlezi wa mbingu na ardhi ambaye ndiye aliye ziumba. Na mimi ni katika wenye kuyashuhudia hayo
Verse 57 — Surah Al-Anbiya 21:57
Na Wallahi! Nitayafanyia vitimbi masanamu yenu haya baada ya mkisha geuka kwenda zenu
Verse 58 — Surah Al-Anbiya 21:58
Basi akayavunja vipande vipande, ila kubwa lao, ili wao walirudie
Verse 59 — Surah Al-Anbiya 21:59
Wakasema: Nani aliye ifanyia haya miungu yetu? Hakika huyu ni katika walio dhulumu
Verse 60 — Surah Al-Anbiya 21:60
Wakasema: Tumemsikia kijana mmoja akiwataja. Anaitwa Ibrahim
Verse 61 — Surah Al-Anbiya 21:61
Wakasema: Mleteni mbele ya macho ya watu, wapate kumshuhudia
Verse 62 — Surah Al-Anbiya 21:62
Wakasema: Je! Wewe umeifanyia haya miungu yetu, ewe Ibrahim
Verse 63 — Surah Al-Anbiya 21:63
Akasema: Bali amefanya hayo huyu mkubwa wao. Basi waulizeni ikiwa wanaweza kutamka
Verse 64 — Surah Al-Anbiya 21:64
Basi wakajirudi nafsi zao, wakasema: Hakika nyinyi mlikuwa madhaalimu
Verse 65 — Surah Al-Anbiya 21:65
Kisha wakarejea kwenye ule ule upotovu wao wakasema: Wewe unajua kwamba hawa hawesemi
Verse 66 — Surah Al-Anbiya 21:66
Akasema: Basi nyinyi mnawaabudu asiye kuwa Mwenyezi Mungu wasio kufaini kitu wala kukudhuruni
Verse 67 — Surah Al-Anbiya 21:67
Aibu yenu nyinyi na hivyo mnavyo viabudu badala ya Mwenyezi Mungu! Basi nyinyi hamtii akilini
Verse 68 — Surah Al-Anbiya 21:68
Wakasema: Mchomeni moto, na muinusuru miungu yenu, ikiwa nyinyi ni watendao jambo
Verse 69 — Surah Al-Anbiya 21:69
Sisi tukasema: Ewe moto! Kuwa baridi na salama kwa Ibrahim
Verse 70 — Surah Al-Anbiya 21:70
Wao walimkusudia maovu, lakini Sisi tukawafanya wao ndio walio khasiri
Verse 71 — Surah Al-Anbiya 21:71
Na tukamwokoa yeye na Luut'i tukawapeleka kwenye nchi tulio ibariki kwa ajili ya walimwengu wote
Verse 72 — Surah Al-Anbiya 21:72
Naye tukampa Is-haq, na Yaaqub kuwa ni ziada. Na wote tukawajaalia wawe watu wema
Verse 73 — Surah Al-Anbiya 21:73
Na tukawafanya maimamu wakiongoa watu kwa amri yetu. Na tukawafunulia watende kheri, na washike Sala, na watoe Zaka; na walikuwa wanatuabudu Sisi tu
Verse 74 — Surah Al-Anbiya 21:74
Na Luut'i tukampa hukumu na ilimu na tukamwokoa na ule mji ulio kuwa ukifanya maovu. Hakika hao walikuwa watu wabaya, wachafu
Verse 75 — Surah Al-Anbiya 21:75
Na tukamuingiza katika rehema yetu. Hakika yeye ni miongoni mwa watenda mema
Verse 76 — Surah Al-Anbiya 21:76
Na Nuhu alipo ita zamani, nasi tukamuitikia, na tukamwokoa yeye na watu wake kutokana na shida kubwa
Verse 77 — Surah Al-Anbiya 21:77
Na tukamnusuru na watu walio zikanusha Ishara zetu. Hakika hao walikuwa watu wabaya. Basi tukawazamisha wote
Verse 78 — Surah Al-Anbiya 21:78
Na Daud na Suleiman walipo kata hukumu katika kadhiya ya konde walipo lisha humo mbuzi wa watu usiku. Na Sisi tulikuwa wenye kushuhudia hukumu yao hiyo
Verse 79 — Surah Al-Anbiya 21:79
Tukamfahamisha Suleiman. Na kila mmoja wao tulimpa hukumu na ilimu. Na tuliifanya milima na ndege kuwa pamoja na Daud imnyenyekee na imtakase Mwenyezi Mungu. Na Sisi ndio tulio fanya hayo
Verse 80 — Surah Al-Anbiya 21:80
Na tukamfundisha kuunda mavazi ya vita kwa ajili yenu ili yakuhifadhini katika kupigana kwenu. Je! Mtakuwa wenye kushukuru
Verse 81 — Surah Al-Anbiya 21:81
Na tukamsahilishia Suleiman upepo wa kimbunga wendao kwa amri yake kwenye ardhi tuliyo ibarikia. Na Sisi ndio tunao jua kila kitu
Verse 82 — Surah Al-Anbiya 21:82
Na pia mashet'ani wanao mpigia mbizi na kufanya kazi nyenginezo. Na Sisi tulikuwa walinzi wao
Verse 83 — Surah Al-Anbiya 21:83
Na Ayyubu, alipo mwita Mola wake Mlezi, akasema: Mimi yamenipata madhara. Na Wewe ndiye unaye rehemu kuliko wote wanao rehemu
Verse 84 — Surah Al-Anbiya 21:84
Basi tukamwitikia, na tukamwondolea madhara aliyo kuwa nayo, na tukampa watu wake na mfano wao pamoja nao kuwa ni rehema inayo toka kwetu, na ukumbusho kwa wafanyao ibada
Verse 85 — Surah Al-Anbiya 21:85
Na Ismail, na Idris, na Dhulkifli - wote walikuwa miongoni mwa wanao subiri
Verse 86 — Surah Al-Anbiya 21:86
Na tukawaingiza katika rehema yetu. Hakika wao walikuwa katika watu wema
Verse 87 — Surah Al-Anbiya 21:87
Na Dhun-Nun alipoondoka hali ameghadhibika, na akadhani ya kwamba hatutakuwa na uwezo juu yake. Basi aliita katika giza: Hapana mungu isipo kuwa Wewe Subhanaka Uliye takasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa wenye kudhulumu
Verse 88 — Surah Al-Anbiya 21:88
Basi tukamwitikia na tukamwokoa kutokana na dhiki. Na hivyo ndivyo tunavyo waokoa Waumini
Verse 89 — Surah Al-Anbiya 21:89
Na Zakariya alipo mwita Mola wake Mlezi: Mola wangu Mlezi! Usiniache peke yangu, na Wewe ndiye Mbora wa wanao rithi
Verse 90 — Surah Al-Anbiya 21:90
Basi tukamwitikia, na tukampa Yahya na tukamponyeshea mkewe. Hakika wao walikuwa wepesi wa kutenda mema, na wakituomba kwa shauku na khofu. Nao walikuwa wakitunyenyekea
Verse 91 — Surah Al-Anbiya 21:91
Na mwanamke aliye linda uke wake, na tukampulizia katika roho yetu, na tukamfanya yeye na mwanawe kuwa ni Ishara kwa walimwengu
Verse 92 — Surah Al-Anbiya 21:92
Kwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi. Kwa hivyo niabuduni Mimi
Verse 93 — Surah Al-Anbiya 21:93
Nao wakalikata jambo lao hili mapande mapande baina yao. Wote watarudi kwetu
Verse 94 — Surah Al-Anbiya 21:94
Na atendaye mema naye ni Muumini basi haitakataliwa juhudi yake. Na hakika Sisi tunamwandikia
Verse 95 — Surah Al-Anbiya 21:95
Na haiwi kwa wana-mji tulio uangamiza, ya kwamba hawatarejea
Verse 96 — Surah Al-Anbiya 21:96
Mpaka watapo funguliwa Juju na Maajuju wakawa wanateremka kutoka kila mlima
Verse 97 — Surah Al-Anbiya 21:97
Na miadi ya haki ikakaribia. Hapo ndipo yatapo kodoka macho ya walio kufuru (na watasema:) Ole wetu! Bila ya shaka tulikuwa tumeghafilika na haya, bali tulikuwa wenye kudhulumu
Verse 98 — Surah Al-Anbiya 21:98
Hakika nyinyi na hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Jahannamu; huko mtaingia tu
Verse 99 — Surah Al-Anbiya 21:99
Lau kuwa hawa ni miungu, wasingeli ingia. Na wote watadumu humo
Verse 100 — Surah Al-Anbiya 21:100
Lao wao humo ni kupiga mayowe, na wala hawatasikia (jenginelo)
Verse 101 — Surah Al-Anbiya 21:101
Ama wale ambao wema wetu umewatangulia, hao watatenganishwa na hayo
Verse 102 — Surah Al-Anbiya 21:102
Hawatausikia mvumo wake, na wao watadumu katika yale zinayo yatamani nafsi zao
Verse 103 — Surah Al-Anbiya 21:103
Hicho Kitisho Kikubwa hakito wahuzunisha. Na Malaika watawapokea (kwa kuwaambia): Hii ndiyo Siku yenu mliyo kuwa mkiahidiwa
Verse 104 — Surah Al-Anbiya 21:104
Siku tutakapo zikunja mbingu kama mkunjo wa karatasi za vitabu. Kama tulivyo anza umbo la mwanzo tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu yetu. Hakika Sisi ni watendao
Verse 105 — Surah Al-Anbiya 21:105
Na hakika tulikwisha andika katika Zaburi baada ya Kumbukumbu, ya kwamba nchi watairithi waja wangu walio wema
Verse 106 — Surah Al-Anbiya 21:106
Hakika katika haya yapo mawaidha kwa watu wafanyao ibada
Verse 107 — Surah Al-Anbiya 21:107
Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote
Verse 108 — Surah Al-Anbiya 21:108
Sema: Hakika imefunuliwa kwangu ya kwamba hakika Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Je! Mmesilimu
Verse 109 — Surah Al-Anbiya 21:109
Na kama wakigeuka, basi sema: Nimekutangazieni sawa sawa, wala sijui yako karibu au mbali hayo mliyo ahidiwa
Verse 110 — Surah Al-Anbiya 21:110
Hakika Yeye anajua kauli ya dhaahiri na anajua myafichayo
Verse 111 — Surah Al-Anbiya 21:111
Wala sijui pengine huu ni mtihani tu kwenu na starehe mpaka muda kidogo
Verse 112 — Surah Al-Anbiya 21:112
Sema: Mola wangu Mlezi! Hukumu kwa haki. Na Mola wetu Mlezi ni Mwingi wa Rehema, aombwaye msaada juu ya mnayo yazua