Back to LanguagesPrevious ChapterNext Chapter EnglishArabicUrduHindiTamilBengali
Swahili - Chapter 20 - Ta-Ha
Translation by Ali Muhsin Al Barwani — Permalink
Verse 1 — Surah Ta-Ha 20:1
Verse 2 — Surah Ta-Ha 20:2
Hatukukuteremshia Qur'ani ili upate mashaka
Verse 3 — Surah Ta-Ha 20:3
Bali ni mawaidha kwa wenye kunyenyekea
Verse 4 — Surah Ta-Ha 20:4
Materemsho yatokayo kwa aliye umba ardhi na mbingu zilizo juu
Verse 5 — Surah Ta-Ha 20:5
Arrahmani, Mwingi wa Rehema, aliye tawala juu ya Kiti cha Enzi
Verse 6 — Surah Ta-Ha 20:6
Ni vyake vyote viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi, na viliomo baina yao, na viliomo chini ya ardhi
Verse 7 — Surah Ta-Ha 20:7
Na ukinyanyua sauti kwa kusema... basi hakika Yeye anajua siri na duni kuliko siri
Verse 8 — Surah Ta-Ha 20:8
Mwenyezi Mungu! Hapana mungu isipo kuwa Yeye. Yeye ana majina mazuri kabisa
Verse 9 — Surah Ta-Ha 20:9
Na je! Imekufikia hadithi ya Musa
Verse 10 — Surah Ta-Ha 20:10
Alipo uona moto, akawaambia watu wake: Ngojeni! Mimi nimeuona moto, huenda nikakuleteeni kijinga kutoka huo moto, au nikapata uongofu kwenye moto
Verse 11 — Surah Ta-Ha 20:11
Basi alipo ufikia akaitwa: Ewe Musa
Verse 12 — Surah Ta-Ha 20:12
Hakika Mimi ndiye Mola wako Mlezi! Basi vua viatu vyako. Kwani upo katika bonde takatifu la T'uwa
Verse 13 — Surah Ta-Ha 20:13
Nami nimekuteua wewe; basi sikiliza unayo funuliwa
Verse 14 — Surah Ta-Ha 20:14
Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu. Hapana mungu ila Mimi tu. Basi niabudu Mimi, na ushike Sala kwa ajili ya kunikumbuka Mimi
Verse 15 — Surah Ta-Ha 20:15
Hakika Saa itakuja bila ya shaka. Nimekaribia kuificha, ili kila nafsi ilipwe kwa iliyo yafanya
Verse 16 — Surah Ta-Ha 20:16
Kwa hivyo asikukengeushe nayo yule ambaye haiamini na akafuata pumbao lake ukaja kuhiliki
Verse 17 — Surah Ta-Ha 20:17
Na nini hicho kilichomo mkononi mwako wa kulia, ewe Musa
Verse 18 — Surah Ta-Ha 20:18
Akasema: Hii ni fimbo yangu; naiegemea na ninawaangushia majani kondoo na mbuzi wangu. Tena inanifaa kwa matumizi mengine
Verse 19 — Surah Ta-Ha 20:19
Akasema: Itupe, ewe Musa
Verse 20 — Surah Ta-Ha 20:20
Akaitupa. Mara ikawa nyoka anaye kwenda mbio
Verse 21 — Surah Ta-Ha 20:21
Akasema: Ikamate, wala usiogope! Tutairudisha hali yake ya kwanza
Verse 22 — Surah Ta-Ha 20:22
Na uambatishe mkono wako kwenye ubavu. Utatoka mweupe pasipo kuwa na madhara yoyote. Hiyo ni ishara nyengine
Verse 23 — Surah Ta-Ha 20:23
Ili tukuonyeshe baadhi ya ishara zetu kubwa
Verse 24 — Surah Ta-Ha 20:24
Nenda kwa Firauni; kwani hakika yeye amepindukia mipaka
Verse 25 — Surah Ta-Ha 20:25
(Musa) akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Nikunjulie kifua changu
Verse 26 — Surah Ta-Ha 20:26
Na unifanyie nyepesi kazi yangu
Verse 27 — Surah Ta-Ha 20:27
Na ulifungue fundo lililo katika ulimi wangu
Verse 28 — Surah Ta-Ha 20:28
Wapate kufahamu maneno yangu
Verse 29 — Surah Ta-Ha 20:29
Na nipe waziri katika watu wangu
Verse 30 — Surah Ta-Ha 20:30
Harun, ndugu yangu
Verse 31 — Surah Ta-Ha 20:31
Kwake yeye niongeze nguvu zangu
Verse 32 — Surah Ta-Ha 20:32
Na umshirikishe katika kazi yangu
Verse 33 — Surah Ta-Ha 20:33
Ili tukutakase sana
Verse 34 — Surah Ta-Ha 20:34
Na tukukumbuke sana
Verse 35 — Surah Ta-Ha 20:35
Hakika Wewe unatuona
Verse 36 — Surah Ta-Ha 20:36
Akasema: Hakika Umepewa maombi yako, ewe Musa
Verse 37 — Surah Ta-Ha 20:37
Na hakika tulikwisha kufanyia hisani mara nyengine
Verse 38 — Surah Ta-Ha 20:38
Pale tulipo mfunulia mama yako yaliyo funuliwa
Verse 39 — Surah Ta-Ha 20:39
Ya kuwa mtie katika kisanduku, na kisha kitie mtoni, na mto utamfikisha ufukweni. Atamchukua adui yangu naye ni adui yake. Na nimekutilia mapenzi yanayo tokana kwangu, na ili ulelewe machoni mwangu
Verse 40 — Surah Ta-Ha 20:40
Dada yako alipo kwenda na akasema: Je! Nikujuulisheni mtu wa kuweza kumlea? Basi tukakurejesha kwa mama yako ili macho yake yaburudike, wala asihuzunike. Na ulimuuwa mtu, nasi tukakuokoa katika dhiki, na tukakujaribu kwa majaribio mengi. Ukakaa miaka kwa watu wa Madyana. Kisha ukaja kama ilivyo kadiriwa, ewe Musa
Verse 41 — Surah Ta-Ha 20:41
Na nimekuteuwa kwa ajili ya nafsi yangu
Verse 42 — Surah Ta-Ha 20:42
Nenda, wewe na ndugu yako, pamoja na ishara zangu, wala msichoke kunikumbuka
Verse 43 — Surah Ta-Ha 20:43
Nendeni kwa Firauni. Hakika yeye amepindukia mipaka
Verse 44 — Surah Ta-Ha 20:44
Mwambieni maneno laini, huenda akazingatia au akaogopa
Verse 45 — Surah Ta-Ha 20:45
Wakasema: Ewe Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tunaogopa asije akapindukia mipaka juu yetu au kufanya jeuri
Verse 46 — Surah Ta-Ha 20:46
Akasema: Msiogope! Hakika Mimi ni pamoja nanyi. Nasikia na ninaona
Verse 47 — Surah Ta-Ha 20:47
Basi mwendeeni, na mwambieni: Hakika sisi ni Mitume wa Mola wako Mlezi! Basi waache Wana wa Israili watoke nasi, wala usiwaadhibu. Sisi tumekuletea ishara itokayo kwa Mola wako Mlezi. Na amani itakuwa juu ya aliye fuata uwongofu
Verse 48 — Surah Ta-Ha 20:48
Hakika tumefunuliwa sisi kwamba hapana shaka adhabu itamsibu anaye kadhibisha na akapuuza
Verse 49 — Surah Ta-Ha 20:49
(Firauni) akasema: Basi Mola wenu Mlezi ni nani, ewe Musa
Verse 50 — Surah Ta-Ha 20:50
Akasema: Mola wetu Mlezi ni yule aliye kipa kila kitu umbo lake, kisha akakiongoa
Verse 51 — Surah Ta-Ha 20:51
Akasema: Nini hali ya karne za kwanza
Verse 52 — Surah Ta-Ha 20:52
Akasema: Ilimu yake iko kwa Mola wangu Mlezi katika Kitabu. Mola wangu Mlezi hapotei wala hasahau
Verse 53 — Surah Ta-Ha 20:53
Ambaye amekufanyieni ardhi kuwa tandiko, na akakupitishieni humo njia, na akakuteremshieni kutoka mbinguni maji. Na kwa hayo tukatoa namna mbali mbali za mimema
Verse 54 — Surah Ta-Ha 20:54
Kuleni, na mchunge wanyama wenu. Hakika katika hayo zipo ishara kwa wenye akili
Verse 55 — Surah Ta-Ha 20:55
Kutokana nayo (ardhi) tumekuumbeni, na humo tunakurudisheni, na kutoka humo tutakutoeni mara nyengine
Verse 56 — Surah Ta-Ha 20:56
Na hakika tulimwonyesha ishara zetu zote. Lakini alikadhibisha na akakataa
Verse 57 — Surah Ta-Ha 20:57
Akasema: Ewe Musa! Hivyo umetujia kututoa katika nchi yetu kwa uchawi wako
Verse 58 — Surah Ta-Ha 20:58
Basi sisi hakika tutakueletea uchawi kama huo. Basi weka miadi baina yetu na wewe, ambayo tusiivunje sisi wala wewe, mahali patapo kuwa sawa
Verse 59 — Surah Ta-Ha 20:59
Akasema: Miadi yenu ni siku ya Sikukuu; na watu wakusanywe kabla ya adhuhuri
Verse 60 — Surah Ta-Ha 20:60
Basi Firauni akarudi na akatengeneza hila yake, kisha akaja
Verse 61 — Surah Ta-Ha 20:61
Musa akamwambia: Ole wenu! Msimzulie Mwenyezi Mungu uwongo, asije akakufutilieni mbali kwa adhabu. Na mwenye kuzua lazima ashindwe
Verse 62 — Surah Ta-Ha 20:62
Basi wakazozana kwa shauri yao wenyewe kwa wenyewe, na wakanong'ona kwa siri
Verse 63 — Surah Ta-Ha 20:63
Wakasema: Hakika hawa wawili ni wachawi, wanataka kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wao, na waondoe mila zenu zilizo bora kabisa
Verse 64 — Surah Ta-Ha 20:64
Kwa hivyo kusanyeni hila zenu zote, kisha mfike kwa kujipanga safu, na kwa yakini atafuzu kweli kweli leo atakaye shinda
Verse 65 — Surah Ta-Ha 20:65
Wakasema: Ewe Musa! Je! Utatupa wewe, au tutakuwa sisi wa kwanza kutupa
Verse 66 — Surah Ta-Ha 20:66
Akasema: Bali tupeni nyinyi! Tahamaki kamba zao na fimbo zao zikaonekana mbele yake, kwa uchawi wao, kuwa zinapiga mbio
Verse 67 — Surah Ta-Ha 20:67
Basi Musa akaingia khofu nafsi yake
Verse 68 — Surah Ta-Ha 20:68
Tukasema: Usikhofu! Hakika wewe ndiye utakaye shinda
Verse 69 — Surah Ta-Ha 20:69
Na kitupe kilicho katika mkono wako wa kulia; kitavimeza walivyo viunda. Hakika walivyo unda ni hila za mchawi tu, na mchawi hafanikiwi popote afikapo
Verse 70 — Surah Ta-Ha 20:70
Basi wachawi wakaangushwa wanasujudu. Wakasema: Tumemuamini Mola Mlezi wa Harun na Musa
Verse 71 — Surah Ta-Ha 20:71
(Firauni) akasema: Oh! Mnamuamini kabla sijakupeni ruhusa? Hakika yeye ndiye mkubwa wenu aliye kufundisheni uchawi. Basi kwa yakini nitakukateni mikono yenu na miguu yenu kwa kutafautisha. Na nitakutundikeni misalabani katika vigogo vya mitende, na hapo kwa yakini mtajua ni nani katika sisi aliye mkali wa kuadhibu na kuiendeleza adhabu yake
Verse 72 — Surah Ta-Ha 20:72
Wakasema: Hatutokukhiari wewe kuliko ishara waziwazi zilizo tujia, na kuliko yule aliye tuumba. Basi hukumu utavyo hukumu; kwani wewe unahukumu haya ya maisha ya duniani tu
Verse 73 — Surah Ta-Ha 20:73
Hakika sisi tumemuamini Mola wetu Mlezi ili atusamehe makosa yetu na uchawi ulio tulazimisha kuufanya. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mbora na Mwenye kudumu zaidi
Verse 74 — Surah Ta-Ha 20:74
Hakika ataye mjia Mola wake Mlezi naye ni mkhalifu, basi kwa yakini, yake huyo ni Jahannamu. Hafi humo wala haishi
Verse 75 — Surah Ta-Ha 20:75
Na atakaye mjia naye ni Muumini aliye tenda mema, basi hao ndio wenye vyeo vya juu
Verse 76 — Surah Ta-Ha 20:76
Bustani za milele zipitazo mito kati yake, wadumu humo. Na hayo ni malipo ya mwenye kujitakasa
Verse 77 — Surah Ta-Ha 20:77
Na tulimfunulia Musa: Toka usiku na waja wangu, na uwapigie njia kavu baharini. Usikhofu kukamatwa, wala usiogope
Verse 78 — Surah Ta-Ha 20:78
Firauni akawafuata pamoja na majeshi yake. Basi kiliwafudikiza humo baharini kilicho wafudikiza
Verse 79 — Surah Ta-Ha 20:79
Na Firauni aliwapoteza watu wake wala hakuwaongoa
Verse 80 — Surah Ta-Ha 20:80
Enyi Wana wa Israili! Hakika tulikuokoeni na adui yenu, na tukakuahidini upande wa kulia wa mlima. Na tulikuteremshieni Manna na Salwa
Verse 81 — Surah Ta-Ha 20:81
Kuleni katika vitu vizuri hivyo tulivyo kuruzukuni, wala msiruke mipaka katika hayo, isije ikakushukieni ghadhabu yangu. Na inaye mshukia ghadhabu yangu basi huyo ameangamia
Verse 82 — Surah Ta-Ha 20:82
Na hakika Mimi ni Mwingi wa Kusamehe kwa anaye tubia, na akaamini, na akatenda mema, tena akaongoka
Verse 83 — Surah Ta-Ha 20:83
Na nini kilicho kutia haraka ukawaacha watu wako, ewe Musa
Verse 84 — Surah Ta-Ha 20:84
Akasema: Hao wapo nyuma yangu wananifuatia. Na nimefanya haraka kukujia, Mola wangu Mlezi, ili uridhike
Verse 85 — Surah Ta-Ha 20:85
(Mwenyezi Mungu) akasema: Sisi tumewatia mtihani watu wako baada yako, na Msamaria amewapoteza
Verse 86 — Surah Ta-Ha 20:86
Musa akarudi kwa watu wake kwa ghadhabu na kusikitika. Akasema: Enyi watu wangu! Kwani Mola wenu Mlezi hakukuahidini ahadi nzuri? Je, umekuwa muda mrefu kwenu au mmetaka ikushukieni ghadhabu ya Mola wenu Mlezi, ndio maana mkavunja miadi yangu
Verse 87 — Surah Ta-Ha 20:87
Wakasema: Sisi hatukuvunja miadi yako kwa khiari yetu, lakini tulibebeshwa mizigo ya mapambo ya watu, basi tukaitupa. Na hivyo ndivyo alivyo toa shauri Msamaria
Verse 88 — Surah Ta-Ha 20:88
Na akawaundia ndama, kiwiliwili chenye sauti. Na wakasema: Huyu ndiye mungu wenu, na mungu wa Musa, lakini alisahau
Verse 89 — Surah Ta-Ha 20:89
Je! Hawakuona kuwa hakuwarudishia neno, wala hakuweza kuwadhuru wala kuwafaa
Verse 90 — Surah Ta-Ha 20:90
Na hakika Harun alikwisha waambia kabla yake: Enyi watu wangu! Hakika nyinyi mmetiwa mtihanini tu kwa kitu hiki. Na kwa yakini Mola wenu Mlezi ni Arrahmani, Mwingi wa Rehema. Basi nifuateni mimi, na t'iini amri yangu
Verse 91 — Surah Ta-Ha 20:91
Wakasema: Hatutaacha kumuabudu mpaka Musa atapo rejea kwetu
Verse 92 — Surah Ta-Ha 20:92
(Musa) akasema: Ewe Harun! Ni nini kilicho kuzuia, ulipo waona wamepotea
Verse 93 — Surah Ta-Ha 20:93
Hata usinifuate? Je, umeasi amri yangu
Verse 94 — Surah Ta-Ha 20:94
Akasema: Ewe mwana wa mama yangu! Usinishike ndevu zangu, wala kichwa changu. Kwa hakika naliogopa usije sema: Umewafarikisha Wana wa Israil, na hukungojea kauli yangu
Verse 95 — Surah Ta-Ha 20:95
(Musa) akasema: Ewe Msamaria! Unataka nini
Verse 96 — Surah Ta-Ha 20:96
Akasema: Niliona wasiyo yaona wao, nikashika gao katika unyao wa Mtume. Kisha nikalitupa. Na hivi ndivyo ilivyo nielekeza nafsi yangu
Verse 97 — Surah Ta-Ha 20:97
(Musa) akasema: Basi ondoka! Na kwa yakini utakuwa katika maisha ukisema: Usiniguse. Na hakika una ahadi kwako isiyo vunjwa. Na mtazame huyo mungu wako uliye endelea kumuabudu - Sisi kwa hakika tutamchoma moto, kisha tutamtawanya baharini atawanyike
Verse 98 — Surah Ta-Ha 20:98
Hakika Mungu wenu ni Allah, Mwenyezi Mungu, tu. Hapana Mungu isipo kuwa Yeye. Ujuzi wake umeenea kila kitu
Verse 99 — Surah Ta-Ha 20:99
Namna hivi tunakuhadithia katika khabari za yaliyo tangulia. Na hakika tumekuletea kutoka kwetu mawaidha ya kukumbukwa
Verse 100 — Surah Ta-Ha 20:100
Atakaye jitenga nayo, basi kwa yakini Siku ya Kiyama atabeba mzigo
Verse 101 — Surah Ta-Ha 20:101
Wadumu humo. Na ni mzigo muovu kwao kuubeba Siku ya Kiyama
Verse 102 — Surah Ta-Ha 20:102
Siku litakapo pulizwa barugumu, na tukawakusanya wakhalifu Siku hiyo, hali macho yao ya kibuluu
Verse 103 — Surah Ta-Ha 20:103
Watanong'onezana wao kwa wao: Hamkukaa ila siku kumi tu
Verse 104 — Surah Ta-Ha 20:104
Sisi tunajua zaidi watakayo yasema, atakapo sema mbora wao katika mwendo: Nyinyi hamkukaa ila siku moja tu
Verse 105 — Surah Ta-Ha 20:105
Na wanakuuliza khabari za milima. Waambie: Mola wangu Mlezi ataivuruga vuruga
Verse 106 — Surah Ta-Ha 20:106
Na ataiacha tambarare, uwanda
Verse 107 — Surah Ta-Ha 20:107
Hutaona humo mdidimio wala muinuko
Verse 108 — Surah Ta-Ha 20:108
Siku hiyo watamfuata muitaji asiye na upotofu. Na sauti zote zitamnyenyekea Arrahmani Mwingi wa Rahema. Basi husikii ila mchakato na mnong'ono
Verse 109 — Surah Ta-Ha 20:109
Siku hiyo uombezi haufai kitu, ila wa aliye mruhusu Arrahmani Mwingi wa Rehema na akamridhia kusema
Verse 110 — Surah Ta-Ha 20:110
Yeye anajua yaliyo mbele yao, na yaliyo nyuma yao. Wala wao hawawezi kumjua Yeye vilivyo
Verse 111 — Surah Ta-Ha 20:111
Na zitadhalilika nyuso mbele ya Aliye Hai Milele, Mwangalizi Mkuu. Na atakuwa ameharibikiwa mwenye kubeba dhulma
Verse 112 — Surah Ta-Ha 20:112
Na anaye tenda mema, naye ni Muumini, basi hatakhofu kudhulumiwa wala kupunjwa
Verse 113 — Surah Ta-Ha 20:113
Na namna hivi tumeiteremsha Qur'ani kwa Kiarabu, na tumekariri humo maonyo ili wapate kuogopa na kujilinda na iwaletee makumbusho
Verse 114 — Surah Ta-Ha 20:114
Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa Haki. Wala usiifanyie haraka hii Qur'ani, kabla haujamalizika ufunuo wake. Na sema: Mola wangu Mlezi! Nizidishie ilimu
Verse 115 — Surah Ta-Ha 20:115
Na hapo zamani tuliagana na Adam, lakini alisahau, wala hatukuona kwake azma kubwa
Verse 116 — Surah Ta-Ha 20:116
Na tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam! Wakasujudu, isipo kuwa Iblisi, alikataa
Verse 117 — Surah Ta-Ha 20:117
Tukasema: Ewe Adam! Hakika huyu ni adui yako na wa mkeo. Basi asikutoeni katika Bustani hii, mkaingia mashakani
Verse 118 — Surah Ta-Ha 20:118
Hakika humo hutakuwa na njaa wala hutakuwa uchi
Verse 119 — Surah Ta-Ha 20:119
Na hakika hutapata kiu humo wala hutapata joto
Verse 120 — Surah Ta-Ha 20:120
Lakini Shet'ani alimtia wasiwasi, akamwambia: Ewe Adam! Nikujuulishe mti wa kuishi milele na ufalme usio koma
Verse 121 — Surah Ta-Ha 20:121
Basi wakaula wote wawili, na uchi wao ukawadhihirikia na wakaanza kujibandika majani ya Bustani. Na Adam akamuasi Mola wake Mlezi, na akapotea njia
Verse 122 — Surah Ta-Ha 20:122
Kisha Mola wake Mlezi akamteuwa, naye akamkubalia toba yake, naye akamwongoa
Verse 123 — Surah Ta-Ha 20:123
Akasema: Ondokeni humu nyote, hali ya kuwa ni maadui nyinyi kwa nyinyi. Na ukikufikieni uwongofu kutoka kwangu basi atakaye ufuata uwongofu wangu, hatapotea wala hatataabika
Verse 124 — Surah Ta-Ha 20:124
Na atakaye jiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa kipofu
Verse 125 — Surah Ta-Ha 20:125
Aseme: Ewe Mola wangu Mlezi! Mbona umenifufua kipofu, nami nilikuwa nikiona
Verse 126 — Surah Ta-Ha 20:126
(Mwenyezi Mungu) atasema: Ndivyo vivyo hivyo. Zilikufikia ishara zetu, nawe ukazisahau; na kadhaalika leo unasahauliwa
Verse 127 — Surah Ta-Ha 20:127
Na hivi ndivyo tutakavyo mlipa kila apitaye kiasi, na asiye amini ishara za Mola wake Mlezi. Na hakika adhabu ya Akhera ni kali zaidi, na inadumu zaidi
Verse 128 — Surah Ta-Ha 20:128
Je! Haikuwabainikia tu; vizazi vingapi tuliviangamiza kabla yao, nao wanatembea katika maskani zao? Hakika katika hayo zimo ishara kwa wenye akili
Verse 129 — Surah Ta-Ha 20:129
Na lau kuwa si neno lililo kwisha tangulia kutoka kwa Mola wako Mlezi na muda ulio wekwa, bila ya shaka inge fika adhabu (hapa hapa)
Verse 130 — Surah Ta-Ha 20:130
Yavumilie haya wayasemayo. Na umtakase Mola wako Mlezi kwa kumsifu kabla ya kuchomoza jua, na kabla halijachwa, na nyakati za usiku pia umtakase, na ncha za mchana ili upate ya kukuridhisha
Verse 131 — Surah Ta-Ha 20:131
Wala usivikodolee macho tulivyo wastareheshea baadhi ya watu miongoni mwao, kwa ajili ya mapambo ya duniani, ili tuwajaribu. Na riziki ya Mola wako Mlezi ni bora na inadumu zaidi
Verse 132 — Surah Ta-Ha 20:132
Na waamrishe watu wako kusali, na uendelee mwenyewe kwa hayo. Sisi hatukuombi wewe riziki, bali Sisi ndio tunakuruzuku. Na mwisho mwema ni kwa mchamngu
Verse 133 — Surah Ta-Ha 20:133
Na walisema: Kwa nini hakutuletea muujiza kutoka kwa Mola wake Mlezi? Je! Haikuwafikilia dalili wazi ya yaliyomo katika Vitabu vya kale
Verse 134 — Surah Ta-Ha 20:134
Na lau kuwa tuliwaangamiza kwa adhabu kabla yake, wangeli sema: Ewe Mola wetu Mlezi! Kwa nini usituletee Mtume tukazifuata ishara zako kabla hatujadhilika na kuhizika
Verse 135 — Surah Ta-Ha 20:135
Sema: Kila mmoja anangoja. Basi ngojeni! Hivi karibuni mtajua nani mwenye njia sawa na nani aliye ongoka