Back to LanguagesPrevious ChapterNext Chapter EnglishArabicUrduHindiTamilBengali
Swahili - Chapter 67 - Al-Mulk
Translation by Ali Muhsin Al Barwani — Permalink
Verse 1 — Surah Al-Mulk 67:1
AMETUKUKA ambaye mkononi mwake umo Ufalme wote; na Yeye ni Mwenye uweza juu ya kila kitu
Verse 2 — Surah Al-Mulk 67:2
Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Na Yeye ni Mwenye nguvu na Mwenye msamaha
Verse 3 — Surah Al-Mulk 67:3
Aliye umba mbingu saba kwa matabaka. Huoni tafauti yoyote katika uumbaji wa Mwingi wa Rehema. Hebu rudisha nadhari! Unaona kosa lolote
Verse 4 — Surah Al-Mulk 67:4
Tena rudisha nadhari mara mbili, nadhari yako itakurejea mwenyewe hali ya kuwa imehizika nayo imechoka
Verse 5 — Surah Al-Mulk 67:5
Na kwa hakika tumeipamba mbingu ya karibu kwa mataa, na tumeyafanya ili kuwapigia mashetani, na tumewaandalia adhabu ya Moto uwakao kwa nguvu
Verse 6 — Surah Al-Mulk 67:6
Na kwa walio mkufuru Mola wao Mlezi ipo adhabu ya Jahannamu. Na ni marejeo maovu yalioje hayo
Verse 7 — Surah Al-Mulk 67:7
Watakapo tupwa humo watausikia mngurumo wake na huku inafoka
Verse 8 — Surah Al-Mulk 67:8
Inakaribia kupasuka kwa hasira. Kila mara likitupwa kundi humo walinzi wake huwauliza: Kwani hakukujieni mwonyaji
Verse 9 — Surah Al-Mulk 67:9
Watasema: Kwani! Ametujia mwonyaji, lakini tulimkadhibisha, na tukasema: Mwenyezi Mungu hakuteremsha chochote. Nyinyi hamumo ila katika upotovu mkubwa
Verse 10 — Surah Al-Mulk 67:10
Na watasema: Lau kuwa tungeli sikia, au tungeli kuwa na akili, tusingeli kuwa katika watu wa Motoni
Verse 11 — Surah Al-Mulk 67:11
Wakakiri dhambi zao. Basi kuangamia ni kwa watu wa Motoni
Verse 12 — Surah Al-Mulk 67:12
Hakika wanao mwogopa Mola wao Mlezi kwa ghaibu, watapata maghfira na ujira mkubwa
Verse 13 — Surah Al-Mulk 67:13
Na ficheni kauli zenu, au zitangazeni; hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani
Verse 14 — Surah Al-Mulk 67:14
Asijue aliye umba, naye ndiye Mjua siri, Mwenye khabari
Verse 15 — Surah Al-Mulk 67:15
Yeye ndiye aliye idhalilisha ardhi kwa faida yenu, basi tembeeni katika pande zake, na kuleni katika riziki zake. Na kwake Yeye ndio kufufuliwa
Verse 16 — Surah Al-Mulk 67:16
Mnadhani mko salama kwa alioko juu kuwa hatakudidimizeni kwenye ardhi, na tahamaki hiyo inatikisika
Verse 17 — Surah Al-Mulk 67:17
Au mnadhani mko salama kwa alioko juu ya kuwa Yeye hakupelekeeni kimbunga chenye changarawe? Mtajua vipi maonyo yangu
Verse 18 — Surah Al-Mulk 67:18
Na bila ya shaka walikwisha kanusha walio kuwa kabla yao; basi kulikuwaje kukasirika kwangu
Verse 19 — Surah Al-Mulk 67:19
Kwani hawawaoni ndege walioko juu yao namna wanavyo zikunjua mbawa zao, na kuzikunja? Hawawashikilii ila Mwingi wa rehema. Hakika Yeye ni Mwenye kuona kila kitu
Verse 20 — Surah Al-Mulk 67:20
Au ni lipi hilo jeshi lenu la kukunusuruni badala ya Mwingi wa Rehema? Hakika makafiri hawamo ila katika udanganyifu
Verse 21 — Surah Al-Mulk 67:21
Au ni nani huyo ambaye atakupeni riziki kama Yeye akizuia riziki yake? Bali wao wanakakamia tu katika jeuri na chuki
Verse 22 — Surah Al-Mulk 67:22
Je! Anaye kwenda akisinukia juu ya uso wake ni mwongofu zaidi, au yule anaye kwenda sawasawa katika Njia Iliyo Nyooka
Verse 23 — Surah Al-Mulk 67:23
Sema: Yeye ndiye aliye kuumbeni tangu mwanzo, na akakupeni masikio na macho, na nyoyo. Ni kidogo kabisa shukrani zenu
Verse 24 — Surah Al-Mulk 67:24
Sema: Yeye ndiye aliye kutawanyeni katika ardhi, na kwake mtakusanywa
Verse 25 — Surah Al-Mulk 67:25
Na wanasema: Lini ahadi hii, ikiwa mnasema kweli
Verse 26 — Surah Al-Mulk 67:26
Sema: Hakika ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu; na hakika mimi ni mwonyaji tu mwenye kubainisha
Verse 27 — Surah Al-Mulk 67:27
Lakini watakapo iona karibu, nyuso za walio kufuru zitahuzunishwa, na itasemwa: Hayo ndiyo mliyo kuwa mkiyaomba
Verse 28 — Surah Al-Mulk 67:28
Sema: Mwaonaje, ikiwa Mwenyezi Mungu atanihiliki mimi na walio pamoja nami, au akiturehemu, ni nani atakaye walinda makafiri na adhabu chungu
Verse 29 — Surah Al-Mulk 67:29
Sema: Yeye ndiye Mwingi wa Rehema; tunamuamini Yeye, na juu yake tunategemea. Mtakuja jua ni nani aliye katika upotovu ulio dhaahiri
Verse 30 — Surah Al-Mulk 67:30
Sema: Mwaonaje, yakiwa maji yenu yamedidimia chini, nani atakueleteeni maji yanayo miminika