Back to Languages
Swahili - Chapter 69
Translation by Ali Muhsin Al Barwani
Verse 1
Tukio la haki
Verse 2
Nini hilo Tukio la haki
Verse 3
Na nini kitakujuulisha nini hilo Tukio la haki
Verse 4
Thamudi na A'di waliukadhibisha Msiba unao situsha
Verse 5
Basi Thamudi waliangamizwa kwa balaa kubwa mno
Verse 6
Na ama A'di waliangamizwa kwa upepo mkali usio zuilika
Verse 7
Alio wapelekea masiku saba, na siku nane, mfululizo bila ya kusita. Utaona watu wamepinduka kama kwamba ni magongo ya mitende yalio wazi ndani
Verse 8
Basi je! Unamwona mmoja wao aliye baki
Verse 9
Na Firauni na walio mtangulia, na miji iliyo pinduliwa chini juu, walileta khatia
Verse 10
Wakamuasi Mtume wa Mola wao Mlezi, ndipo Yeye Mola akawakamata kwa mkamato ulio zidi nguvu
Verse 11
Maji yalipo furika Sisi tulikupandisheni katika safina
Verse 12
Ili tuyafanye hayo kuwa ni waadhi kwenu na kila sikio linalo sikia liyahifadhi
Verse 13
Na litapo pulizwa barugumu mpulizo mmoja tu
Verse 14
Na ardhi na milima ikaondolewa, na ikavunjwa kwa mvunjo mmoja
Verse 15
Siku hiyo ndio Tukio litatukia
Verse 16
Na mbingu zitapasuka, kwani siku hiyo zitakuwa dhaifu kabisa
Verse 17
Na Malaika watakuwa pembezoni mwa mbingu; na wanane juu ya hawa watakuwa wamebeba Kiti cha Enzi cha Mola wako Mlezi
Verse 18
Siku hiyo mtahudhurishwa - haitafichika siri yoyote yenu
Verse 19
Basi ama atakaye pewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, atasema: Haya someni kitabu changu
Verse 20
Hakika nalijua ya kuwa nitapokea hisabu yangu
Verse 21
Basi yeye atakuwa katika maisha ya kupendeza
Verse 22
Katika Bustani ya juu
Verse 23
Matunda yake yakaribu
Verse 24
Waambiwe: Kuleni na mnywe kwa furaha kwa sababu ya mlivyo tanguliza katika siku zilizo pita
Verse 25
Na ama atakaye pewa kitabu chake katika mkono wake wa kushoto, basi yeye atasema: Laiti nisingeli pewa kitabu changu
Verse 26
Wala nisingeli jua nini hisabu yangu
Verse 27
Laiti mauti ndiyo yangeli kuwa ya kunimaliza kabisa
Verse 28
Mali yangu hayakunifaa kitu
Verse 29
Madaraka yangu yamenipotea
Verse 30
(Pasemwe): Mshikeni! Mtieni pingu
Verse 31
Kisha mtupeni Motoni
Verse 32
Tena mtatizeni katika mnyororo wenye urefu wa dhiraa sabiini
Verse 33
Kwani huyo hakika alikuwa hamuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu
Verse 34
Wala hahimizi kulisha masikini
Verse 35
Basi leo hapa hana jamaa wa kumwonea uchungu
Verse 36
Wala hana chakula ila usaha wa watu wa Motoni
Verse 37
Chakula hicho hawakili ila wakosefu
Verse 38
Basi naapa kwa mnavyo viona
Verse 39
Na msivyo viona
Verse 40
Kwa hakika hii ni kauli iliyo letwa na Mjumbe mwenye hishima
Verse 41
Wala si kauli ya mtunga mashairi. Ni machache sana mnayo yaamini
Verse 42
Wala si kauli ya kuhani. Ni machache mnayo yakumbuka
Verse 43
Ni uteremsho utokao kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote
Verse 44
Na lau kama angeli tuzulia baadhi ya maneno tu
Verse 45
Bila ya shaka tungeli mshika kwa mkono wa kulia
Verse 46
Kisha kwa hakika tungeli mkata mshipa mkubwa wa moyo
Verse 47
Na hapana yeyote katika nyinyi ambaye angeli weza kutuzuia
Verse 48
Kwa hakika hii ni mawaidha kwa wachamngu
Verse 49
Na hakika Sisi bila ya shaka tunajua kwamba miongoni mwenu wapo wanao kadhibisha
Verse 50
Na hakika bila ya shaka itakuwa ni majuto kwa wanao kataa
Verse 51
Na hakika hii bila ya shaka ni haki ya yakini
Verse 52
Basi litakase jina la Mola wako Mlezi Mtukufu