Swahili

    Translation: swa-abdullahmuhamma

    Author: Abdullah Muhammad Abu Bakr

    Ufunguzi

    Surah 1

    [1] Naanza kusoma Qur’an kwa jina la Mwenyezi Mungu nikiomba msaada Wake. «Allah» ni jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa baraka Mwenye kutukuka, Anayestahiki kuabudiwa na sio mwingine. Nalo ni jina mahsusi zaidi miongoni mwa majina ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, na haitwi kwa jina hili yoyote isipokuwa Yeye Aliyetakasika na sifa za upungufu. «Al-Raḥmān» Mwenye rehema nyingi Ambaye rehema Zake zimewanea viumbe vyote. «Al-Raḥīm» mwenye kuwarehemu Waumini. Na majina mawili haya, kati ya majina ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, yanakusanya uthibitishaji wa sifa ya urehemefu kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kama inavyonasibiana na haiba Yake

    [2] Kila jinsi ya sifa njema ni ya Mwenyezi Mungu, Mwenye sifa ambazo zote ni za ukamilifu, Mwenye neema za nje na za ndani, za kidini na za kidunia. Na ndani yake kuna amri ya Mwenyezi Mungu kwa waja Wake wamsifu Yeye kwa kuwa Yeye Ndiye Mstahiki wa kusifiwa Peke Yake

    [3] Mwingi wa rehema Ambaye rehema Zake zimewaenea viumbe vyote, Mwenye kuwarehemu Waumini. Na majina mawili haya ni miongoni mwa majina ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka

    [4] Na Yeye, kutakasika ni Kwake, Peke Yake Ndiye Mwenye mamlaka ya Siku ya Kiyama, nayo ni Siku ya Malipo kwa matendo yaliyofanywa na waja. Muislamu anapoisoma aya hii katika kila rakaa, inamkumbusha siku ya Akhera na inamhimiza ajitayarishe kufanya matendo mema na kujiepusha na maasia na mabaya

    [5] Sisi tunakuabudu wewe peke yako, na tunataka msaada kwako peke yako katika mambo yetu yote. Mambo yote yako mkononi mwako, hakuna asiyekuwa wewe anayemiliki chochote katika hayo hata kadiri ya uzito wa chungu mdogo. Katika aya hii kuna dalili ya kuwa mja haifai aelekeze kitu chochote miongoni mwa aina za ibada, kama kuomba, kutaka kunusuriwa, kuchinja na kutufu, isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake. Pia ndani yake kuna ponya ya nyoyo kutokana na ugonjwa wa kufungamana na asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na kutokana na ugonjwa wa ria, kujiona na kiburi

    [6] Tuonyeshe, tuongoze na tupe taufiki ya kuelekea njia iliyonyoka na ututhibitishe juu yake mpaka tukutane na wewe, nayo ni Uislamu ambao ndio njia iliyo wazi yenye kufikisha kwenye radhi za Mwenyezi Mungu na kwenye Pepo yake, njia tuliyoonyeshwa na aliye mwisho wa Mitume wa Mwenyezi Mungu na Manabii Wake, Muhammad, reheme ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwani hakuna kufaulu kwa mja isipokuwa kwa kusimama imara juu yake

    [7] Njia ya wale uliowaneemesha miongoni mwa Manabii, wakweli wa imani, mashahidi na wema. Wao ndio watu wa uongofu na kusimama imara. Na usitufanye kuwa miongoni mwa wale waliofuata njia ya waliokasirikiwa, wale walioijua haki na wasiifuate kivitendo, nao ni Mayahudi na wale waliofanana na wao; wala usitufanye ni miongoni mwa wapotevu, nao ni wale ambao hawakuongoka kwa ujinga waliokuwa nao, wakapotea njia, nao ni Wanaswara na waliofuata mwenendo wao. Katika dua hii kuna ponya ya moyo wa Muislamu ya ugonjwa wa ukanushaji, ujinga na upotevu, na ni dalili kwamba neema kubwa zaidi kuliko zote ni neema ya Uislamu. Basi mwenye kuwa mjuzi zaidi wa haki na akawa mfuataji zaidi wa hiyo haki, basi huwa ni aula zaidi wa njia iliyonyoka. Na hapana shaka kwamba Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ndio watu aula zaidi wa hilo baada ya Manabii, amani iwashukie. Basi aya hii yaonyesha utukufu wao na ukubwa wa daraja yao, Mwenyezi Mungu Awe radhi nao. Ni sunna kwa msomaji aseme katika Swala baada ya kusoma Fatiha «Āmīn», na maana yake ni: Ewe Mola! Takabali. Nayo si aya katika sura ya Fatiha kwa maafikiano ya wanavyuoni. Na kwa hivyo wamekubaliana kwa umoja wao kutoiandika kwenye Misahafu

    Ng'ombe

    Surah 2

    [1] “Alif Lām Mīm” Herufi hizi na nyinginezo, miongoni mwa herufi zilizotajwa mwanzo wa sura, zinaashiria kuwa Qur’ani haigiziki. Washirikina waliwekewa biri walete kitu kama Qur’ani, wakashindwa kushindana nayo, paomoja na kuwa imebuniwa na herufi hizi hizi ambazo Waarabu wanazitumia. Kulemewa kwa Waarabu kuja na Qur’ani kama hii, ingawa walikuwa ni mafasaha wa watu, ni dalili ya kuwa Qur’ani ni wahyi (wahy) utokao kwa Mwenyezi Mungu

    [2] Qurani hii ni kitabu kisicho na shaka kuwa kinatoka kwa Mwenyezi Mungu. Haifai kwa mtu yoyote kufanya shaka juu yake kwa uwazi wake. Wananufaika kwayo wenye uchajimungu (taqwā), wenye kujikinga kwa elimu yenye manufaa na amali njema, na wao ndio wanaomuogopa Mwenyezi Mungu na kufuata hukumu Zake

    [3] Nao ndio wanao amini ghaibu (ghayb), ambayo haifikiliwi na hisia zao na akili zao pekee, kwa kuwa haijulikani isipokuwa kupitia wahyi wa Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani imshukie, kama kuamini Malaika, pepo, moto, na mengineyo katika yale yaliyoelezwa na Mtume Wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie yeye. Imani (Īmān) ni neno lililokusanya kumkubali Mwenyezi Mungu, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Siku ya Mwisho na Kadari (Qadar), kheri yake na shari yake. Na kutilia nguvu kukubali huko kwa maneno na vitendo, kwa moyo, ulimi na viungo. Na wao, pamoja na kuamini kwao mambo ya ghaibu yasiyoonekana, wanasimamisha Swala kwa kuchunga nyakati zake na kuzitekeleza ipasavyo kulingana na sheria ya Mwenyezi Mungu kwa Nabii wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye yeye. Kadhalika, katika kile tulichowapa wao, miongoni mwa mali, wanatoa sadaka ya mali zao ya wajibu na ya suna

    [4] Na wao ndio ambao wanayaamini yaliyoteremshwa kwako, ewe Mtume, ya Qurani, na yalioteremshwa kwako ya hekima, ambayo ni Sunnah, na Vitabu vyote vilivyoteremshwa kwa Mitume kabla yako, kama Taurati, Injil na vinginevyo, na wanaiamini Nyumba ya Maisha baada ya kufa na yaliyomo ndani ya Nyumba hiyo ya kuhesabiwa na kulipwa. Wanaamini hayo kwa nyoyo zao, imani ya kidhati inayodhihiri kwenye ndimi zao na viungo vyao. Kutajwa Siku ya Mwisho mahususi ni kwa sababu kuiamini ni mojawapo ya vitu vikubwa zaidi vyenye kusukuma na kuhimiza kufanya vitendo vya kumtii Mwenyezi Mungu, kujiepusha na vitendo vya haramu na kuifanyia hesabu nafsi

    [5] Wenye sifa hizi wako kwenye nuru inayotoka kwa Mola wao na taufiki inayotoka kwa Muumba Wao na Mwongozi Wao. Wao ndio wenye kufuzu, waliopata matakwa yao na kuokoka na shari ya vitu walivyovikimbia

    [6] Hakika wale walioyakanusha yalioteremshwa kwako kutoka kwa Mola Wako, kwa njia ya kiburi na ujeuri, hakutapatikana kuamini kutoka kwao; ni sawa kwao ukiwa utawatisha na kuwaonya adhabu ya Mwenyezi Mungu au utaacha kufanya hivyo, kwa sababu wao wameamua kukakamia kwenye njia yao ya batili

    [7] Mwenyezi Mungu amewapiga muhuri nyoyo zao, masikizi yao na ameweka finiko juu ya macho yao ya kuonea kwa sababu ya ukafiri na ujeuri walionao, baada ya haki kuwabainikia. Mwenyezi Mungu hakuwaafikia kwenye uongofu. Wao watapata adhabu kali katika Moto wa Jahanamu

    [8] Miongoni mwa watu kuna kundi linalokuwa katika hali ya kutokuwa na uamuzi, linasimama baina ya Waumini na makafiri, nao ni wanafiki wanaosema kwa ndimi zao, “Tumemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho,’ na hali wao, katika undani yao, ni warongo, hawakuamini

    [9] Wanaitakidi, kwa ujinga wao, kuwa wao wanamdanganya Mwenyezi Mungu na Waumini, kwa kudhihirisha kwao Imani na kuficha kwao ukafiri, na wao hawamdanganyi yoyote isipokuwa nafsi zao wenyewe, kwa kuwa madhara ya kudanganya kwao yanawarudia wao. Na kwa kuwa ujinga wao umekolea na nyoyo zao zimeharibika, huwa hawana hisia ya hilo

    [10] Ndani ya nyoyo zao kuna shaka na uharibifu, ndipo wakaomjwa kwa kufanya maasia yenye kuwafanya wastahiki kuadhibiwa, na Mwenyezi Mungu akawazidishia shaka. Watakuwa na adhabu yenye uchungu kwa sababu ya urongo na unafiki wao

    [11] Wanapopewa nasaha wakome kufanya uharibifu katika ardhi kwa kukanusha na kuasi kutoa siri za Waumini na kuwategemea makafiri, huwa wakisema kwa urongo na kubisha, “Sisi ndio watu wakutengeneza.”

    [12] Hili wanalolifanya na kudai kuwa ni utengefu ndio uharibifu wenyewe, lakini wao, kwa ujinga wao na ujeuri wao, hawana hisia ya hilo

    [13] Na waambiwapo wanafiki, “Aminini kama walivyoamini masahaba, nako ni kuamini kwa moyo, ulimi na viungo,” huwa wakibisha na kusema, “Basi, tuamini kama vile madhaifu wa akili na maoni walivyoamini, tuwe kama wao katika upumbavu?” Mwenyezi Mungu aliwajibu kwamba udhaifu wa akili na maoni ni wao peke yao. Na wao hawajui kuwa msimamo walionao ndio upotevu na hasara

    [14] Hawa wanafiki wakikutana na waumini huwa wakisema, “Tumeiamini Dini ya Uislamu kama nyinyi,” na wakiondoka kwenda kwa viongozi wao makafiri wasiomjalli Mwenyezi Mungu, huwa wakiwahakikishia kuwa wao wako kwenye mila ya ukafiri, hawajaiacha, na kuwa wao walikuwa wakiwacheza shere waumini

    [15] Mwenyezi Mungu anawacheza shere wao na kuwapa muhula, ili wazidi kupotea, kuwa na shaka na kutokuwa na uamuzi, na Atawalipa kwa kuwacheza shere kwao Waislamu

    [16] Hao ndio wanafiki. Wamejiuza wenyewe katika mapatano ya hasara. Walichukuwa ukafiri na kuacha Imani. Hawakupata faida yoyote, bali walipata hasara ya kukosa uongofu. Huko ndiko kupata hasara kukubwa

    [17] Hali ya wanafiki ambao wameuamini, kidhahiri sio kindani, utume wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie yeye, kisha wakakanusha, wakawa wanaenda huku na kule kwenye giza la upotevu wao bila kujua wanapoenda wala kuwa na matarajio ya kutoka kwenye giza hilo, inafanana na hali ya kikundi cha watu, kwenye usiku wa giza, ambapo mmoja wao aliwasha moto mkubwa ili wapate joto na mwangaza. Moto ulipowaka na kung’arisha pambizo zake, ulizimika na giza likaenea. Wakawa watu hao wako kwenye giza, hawaoni chochote wala hawaongoki kupajua penye njia ya kujua matoko

    [18] Wao ni viziwi, hawaisikii haki kwa kuizingatia, ni mabubu, hawaitamki haki, ni vipofu, hawauoni mwangaza wa uongofu. Kwa hivyo, hawawezi kurudi kwenye Imani ambayo waliiacha na kuchukuwa upotevu badali yake

    [19] Au hali yao inafanana na hali ya kikundi kingine cha wanafiki ambao haki inawadhihirikia wakati mwengine, na huwa na shaka nayo wakati mwengine. Hali yao ni ile ya watu wanaotembea jangwani, wakanyeshewa na mvua nyingi, iliyofuatana na giza lingi lililopandana, mpigo wa radi pamoja na mng’aro wa pepe na vimondo vyenye kuchoma. Hivyo vinawafanya wao, kwa vituko vyake, kuweka vidole vyao kwenye masikio yao, kwa kuogopa kufa. Na Mwenyezi Mungu Amewazunguka makafiri, hawamponyoki wala hawamshindi

    [20] Hizo pepe, kwa mng’aro wake, zinakaribia kuwatoa macho yao. Pamoja na hivyo, kila pepe ikiwang’arishia njia, wanatembea kwenye mwangaza wake, na ikiondoka, njia huwa na giza ikawabidi wasimame pale waliopo. Lau si Mwenyezi Mungu kuwapa muda, Angewaondolea masikizi yao ya kusikia na macho yao ya kuonea. Na Yeye ni mwenye uweza wa kufanya hilo wakati wowote. Yeye ni Muweza wa kila kitu

    [21] Mwito utokao kwa Mwenyezi Mungu kwa binadamu wote: Muabuduni Mwenyezi Mungu Ambaye Amewalea kwa neema zake, na mumuogope wala msiende kinyume na dini Yake. Kwani yeye ndiye Aliyewaumba kutoka kwenye hali ya kutokuwako, na Akawaumba waliokuwa kabla yenu, ili muwe ni miongoni mwa wenye kumcha Mwenyezi Mungu ambao Yeye Ameridhika nao na wao wameridhika na Yeye

    [22] Mola wenu ni Yule Aliyewafanyia ardhi iwe ni tandiko, ili maisha yenu yawe mepesi juu yake, na mbingu ziwe zimejengeka madhubuti, na Akateremsha mvua kutoka kwenye mawingu, Akatoa kwa mvua hiyo matunda na mimea aina mbalimbali ili iwe ni riziki kwenu. Basi, msimuwekee Mwenyezi Mungu washirika katika ibada, hali nyinyi mnajua kuwa Mwenyezi Mungu Amepwekeka katika kuumba, kuruzuku na kustahiki kuabudiwa

    [23] Na mkiwa, enyi makafiri, muna shaka juu ya Qurani tuliyomteremshia mja wetu Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani imshukie, na mkadai kuwa haitoki kwa Mwenyezi Mungu, basi leteni sura moja inayofanana na sura ya Qurani, na takeni msaada kutoka kwa yoyote mnayemuweza ili awasaidie, iwapo nyinyi ni wakweli katika madai yenu

    [24] Mkiwa hamuwezi sasa, na hamtaweza wakati unaokuja kabisa, basi uogopeni Moto, kwa kumuamini Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kumtii Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. Moto ambao kuni zake ni watu na mawe, umeandaliwa wenye kumkanusha Mwenyezi Mungu na Mitume Wake

    [25] Waambie, ewe Mtume, watu wa Imani na amali nzuri, habari yenye kuwajaza furaha, kuwa wao huko Akhera watakuwa na Mabustani ya ajabu, ambayo inapita mito chini ya majumba yake makubwa na miti yake yenye vivuli. Kila Anapowaruzuku Mwenyezi Mungu humo aina yoyote ya matunda yenye ladha, watasema, “Mwenyezi Mungu Alituruzuku aina hii ya matunda kipindi cha nyuma.” Watakapoionja wataikuta ni tafauti tamu yake na ladha yake, ingawa inafanana na aina iliyopita kwa rangi, sura na jina. Na katika hayo Mabustani ya Peponi watakuwa na wake waliosafishika na kila aina ya uchafu, wa nje, kama mkojo na damu ya hedhi, na wandani, kama kusema urongo na kuwa na tabia mbaya. Na wao, katika Pepo na starehe zake, watakaa milele, hawafi humo wala hawatoki

    [26] Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Halionei haya jambo la haki lolote kulitaja, liwe ni kubwa au dogo, hata kama ni kukipigia mfano kitu kidogo sana, kama mbu na nzi na mfano wake, katika vitu Alivyovipigia mfano Mwenyezi Mungu kuonyesha kushindwa kwa kila kitu kinachoabudiwa kisichokuwa Mwenyezi Mungu. Ama waumini, wao wanajua hekima ya Mwenyezi Mungu katika kupigia mfano kitu kikubwa au kidogo miongoni mwa viumbe Vyake. Ama makafiri, wanafanya maskhara na kusema, “Ni nini lengo la Mwenyezi Mungu kupigia mfano vidudu hivi vitwevu?” Mwenyezi Mungu anawajibu kwamba makusudio ni kuwafanyia mtihani na kupambanua Mwenye Imani na kafiri. Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu, kwa mifano hii, anawaepusha na haki watu wengi, kwa kuifanyia kwao maskhara, na Anawapa taufiki kwayo wengineo kupata nyongeza ya Imani na uongofu. Na Mwenyezi Mungu Hamdhulumu yeyote, kwani Hawaepushi na haki isipokuwa wenye kutoka nje ya utiifu Kwake

    [27] Wale ambao wanavunja ahadi ya Mwenyezi Mungu Aliyoichukuwa kwao kuwa wampwekeshe Yeye na wamtii, hali ya kuwa Ameiitilia mkazo ahadi hiyo kwa kuleta Mitume na kuteremsha vitabu, na wanaenda kinyume na dini ya Mwenyzi Mungu, kama kukata zao na kueneza uharibifu katika ardhi. Basi wao ndio wenye hasara duniani na Akhera

    [28] Vipi mtaukanusha, enyi washirikina, umoja wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kumshirikisha mwengine katika Ibada, pamoja na kuwa kuna dalili zisizopingika kuhusu hilo katika nafsi zenu? Mlikuwa hamko, hamjaumbwa, Akawafanya muweko kwa kuwaumba, Akapuliza kwenu uhai, kisha Atawafisha baada ya kumalizika muda wenu wa kuishi Aliowaekea, kisha Atawarudisha mkiwa na uhai Siku ya Kufufuliwa, kisha mtarejeshwa Kwake mhesabiwe na mlipwe

    [29] Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Ndiye Aliyeumba kwa ajili yenu kila kilichoko kwenye ardhi miongoni mwa neema ambazo mnanufaika nazo, kisha Akaelekea na kukusudia kuumba mbingu, Akazifanya mbingu saba. Na Yeye ni Mjuzi wa kila kitu, na elimu Yake, Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu, imevizunguka vitu vyote Alivyoviumba

    [30] Kumbuka, ewe Mtume, Aliposema Mola wako kuwaambia Malaika, “Mimi nitawaweka watu kwenye ardhi, ili waiimarishe kwa kupishana: wakiondoka watu watakuja wengine baada yao.” Wakasema, “Ewe Mola wetu! Tufundishe na utuongoze, ni kwa hekima gani kuwaumba hawa, pamoja na kuwa mambo yao yatakuwa ni kuleta uharibifu katika ardhi na kumwaga damu kwa dhulma na uonevu, na hali sisi tuko chini ya amri yako: tunakuepusha na mabaya maepusho yanayonasibiana na Sifa zako njema na utukufu Wako, na tunakusifu kwa kila sifa za ukamilifu na utukufu?” Mwenyezi Mungu Akasema kuwaambia, “Mimi najua msiyoyajua kuhusu uzito wa maslahi katika kuwaumba wao.”

    [31] Na ili kubainisha utukufu wa Ādam, Amani imshukiye, Mwenyezi Mungu Alimfundisha majina ya vitu vyote, kisha Akaviorodhesha hivyo vitu kwa Malaika na kuwaambia, “Niambieni majina ya vitu hivi vilivyoko, ikiwa nyinyi ni wakweli kwamba nyinyi mnastahiki zaidi uimarishaji wa ardhi kuliko wao.”

    [32] Malaika walisema, “Tunakuepusha na kila sifa pungufu, ewe Mola wetu! Sisi hatuna ujuzi isipokuwa ule uliyotufundisha. Wewe, Peke Yako, Ndiye Mjuzi wa mambo ya viumbe vyako, Ndiye Mwenye Hekima katika uendeshaji Wako.”

    [33] Mwenyezi Mungu Alisema, “Ewe Ādam! Waambie majina ya vitu hivi ambayo walishindwa kuyajua.” Ādam alipowaambia hayo majina, Mwenyezi Mungu Alisema kuwaambia Malaika, “Niliwaambia kuwa Mimi ninayajua yaliyofichika kwenu, ya mbinguni na ardhini, na ninayajua mnayoyafanya kwa dhahiri na mnayoyafanya kwa siri.”

    [34] Na taja kwa watu, ewe Mtume, takrima ya Mwenyezi Mungu kwa Ādam Aliposema Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kuwaambia Malaika, “Msujudieni Ādam kwa njia ya kumheshimu na kuonyesha fadhila zake.” Wote walitii amri, isipokuwa Iblisi alikataa kusujudu kwa sababu ya kiburi na uhasidi, akawa ni miongoni mwa wenye kumkanusha Mwenyezi Mungu, wenye kuasi amri Yake

    [35] Mwenyezi Mungu Akasema, “Ewe Ādam! Kaa wewe na mkeo Ḥawwā’ kwenye pepo na stareheni kwa matunda yake kwa furaha na ukunjufu popote pale mnapotaka humo, na tahadharini na mti huu, msije mkaingia katika maasia mkawa ni wenye kukiuka amri ya Mwenyezi Mungu.”

    [36] Shetani akawaingiza makosani, kwa kuwashawishi mpaka wakala katika ule mti, ikasababisha kutolewa kwao kwenye Pepo na starehe zake. Na Mwenyezi Mungu Aliwaambia, “Shukeni ardhini, mkiteta nyinyi kwa nyinyi- yaani: Ādam, Ḥawwā’ na Shetani-, na nyinyi katika hiyo ardhi muna utulivu na makao na kunufaika kwa vilivyomo mpaka muda wa maisha yenu ukome.”

    [37] Ādam alipokea matamko ya kuomba ili akubaliwe, aliyoletewa na Mwenyezi Mungu, kwa njia ya ilham (ilham), yaliyokusanya toba na kutaka msamaha, nayo ni neno Lake Aliyetukuka, “Ewe Mola wetu! Tumejidhulumu nafsi zetu. Na Usipotusamehe na Kuturehemu, hakika tutakuwa ni miongoni mwa waliyopata hasara.” (:23). Mwenyezi Mungu Alikubali toba yake na Akamsamehe. Kwani Yeye, Aliyetukuka, ni Mwingi wa kukubali toba ya Mwenye kutubia miongoni mwa waja Wake na ni Mwenye Kuwarehemu

    [38] Tulisema, “Shukeni kutoka Peponi nyote! Na utawajia, nyinyi na vizazi vyenu vinavyofuatia, ujumbe wenye mambo ya kuwaongoza kwenye haki. Wenye kuufuata huo kwa vitendo, hawatakuwa na hofu kuhusu mustakbala wao wa Akhera, wala hawatakuwa na huzuni juu ya vitu walivyovikosa vya ulimwenguni

    [39] Na wenye kukataa na kukanusha aya zetu zinazosomwa na dalili za Umoja Wetu, basi hao ndio ambao watasalia Motoni, wakiwa humo milele: hawatatoka humo.”

    [40] Enyi kizazi cha Ya’qūb, tajeni neema za Mwenyezi Mungu zilizo nyingi kwenu, nishukuruni na timizeni wasia Wangu kwenu kuwa muviamini Vitabu Vyangu na Mitume Wangu Wote, mfuate Sheria Zangu kivitendo. Mkifanya hivyo, nitawatimizia niliyowaahidi ya kuwarehemu katika ulimwengu na kuwaokoa kesho Akhera. Na Mimi, Peke Yangu, niogopeni na muwe na hadhari na mateso Yangu ikiwa mtavunja ahadi na kunikanusha

    [41] Na iaminini Qur,ani, enyi wana wa Isrāīl, ambayo niliiteremsha kwa Muhammad, aliye Nabii na Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukie yeye, ambayo inalingana na yale mnayoyajua yaliyo sahihi katika Taurati. Na msiwe ni kundi la mwanzo la Watu wa Kitabu (ahl al-kitāb) kuikanusha. Na wala msizibadilishe aya zangu kwa thamani chache ya taka za dunia zenye kuondoka. Na Kwangu Mimi, Peke Yangu, fanyeni vitendo vya kunitii na acheni kuniasi

    [42] Wala msichanganye haki niliyowafafanulia, na batili mliyoizusha. Na jihadharini kuificha haki iliyo wazi ya sifa za Nabii na Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ambazo zimo ndani ya vitabu vyenu. Na nyinyi mnazipata hizo zimeandikwa kwenu, katika vitabu mnavyovijua vilivyoko mikononi mwenu

    [43] Na ingieni kwenye dini ya Uislamu: Msimamishe Swala kwa njia sahihi kama alivyokuja nayo Nabii wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, mtekeleze Zaka za lazima kwa namna iliyowekwa na Sheria, na mue pamoja na wanaorukuu katika ummah wake, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [44] Ni ubaya ulioje wa hali yenu na hali ya wasomi wenu, mnapoamrisha watu kufanya mambo ya kheri na kuziacha nafsi zenu, hamziamrishi ziingie kwenye hiyo kheri kubwa, nayo ni Uislamu, na hali nyinyi mnaisoma Taurati ambayo ndani yake muna sifa za Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na ulazima wa kumfuata! Kwani hamzitumii akili zenu kisawa

    [45] Jisaidieni, katika mambo yenu, kwa subira za kila aina, na pia kwa Swala ambayo ni ngumu isipokuwa kwa wanyenyekevu

    [46] Wenye kumcha Mwenyezi Mungu na kutaraji Malipo yaliyoko Kwake, wenye kuamini kwa yakini kuwa wao ni wenye kukutana na Mola wao, Aliyetukuka na kushinda, baada ya kufa, na kuwa wao ni wenye kurejea Kwake Siku ya Kiama kwa kuhesabiwa na kulipwa

    [47] Enyi kizazi cha Ya’qūb! Kumbukeni neema zangu nyingi juu yenu, mnishukuru kwa neema hizo na mkumbuke kuwa Mimi nimewatukuza nyinyi juu ya watu wa zama zenu, kwa wingi wa Mitume na Vitabu vilivyoteremshwa kama Taurati na Injili

    [48] Iogopeni Siku ya Kiama, Siku ambayo hakuna mtu wa kumfaa mwengine kitu chochote, wala Mwenyezi Mungu hatakubali maombezi kwa Makafiri na wala hatakubali kutoka kwao kitu chochote cha kuwakomboa, hata kama kilikuwa ni mali yote yaliyoko ardhini, na hakuna yoyote atakayeweza kujitokeza kuwanusuru wao na kuwaokoa na adhabu

    [49] Kumbukeni neema Yetu juu yenu, tulipowaokoa nyinyi na mateso ya Fir'awn na wafuasi wake, waliokuwa wakiwaonjesha nyinyi adhabu kali sana, wakiwaua watoto wenu wa kiume kwa wingi na kuwaacha wanawake wenu kwa kutumika na kudhalilishwa. Katika hilo, ni mtihani kwenu kutoka kwa Mola wenu. Na katika kuokolewa kwenu na yeye, ni neema kubwa ambayo inapasa kwenu mumshukuru Mwenyezi Mungu Aliyetukuka katika kila zama zenu na vizazi vyenu

    [50] Kumbukeni neema Yetu juu yenu, tulipoipambanua bahari kwa ajili yenu na tukafanya ndani yake njia kavu, mkavuka na tukawaokoa na Fir'awn na askari wake na msizame majini. Fir'awn na askari wake walipoingia kwenye njia mlizopitia, tuliwazamisha majini mbele ya macho yenu

    [51] Kumbukeni neema Yetu juu yenu, tulipompa Musa agizo la masiku arubaini la kuiteremshiwa Taurati, iwe ni uongofu na nuru kwenu, na punde tu alipoondoka mlichukua fursa ya kuwa yeye hayupo kwa muda mchache, mkamfanya ndama, mliyomtengeneza kwa mikono yenu, kuwa ni mungu wenu wa kuabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu. Huu ni ukanushaji Mwenyezi Mungu mbaya kabisa. Na nyinyi mlikuwa madhalimu kwa kumfanya ndama ni Mungu

    [52] Kisha tukawasamehe kitendo hiki kibaya, tukakubali toba yenu baada ya kurudi Musa kwa kutarajia kuwa mtamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema Zake na fadhila Zake juu yenu, na hamtaendelea kwenye ukafiri na uasi

    [53] Na Kumbukeni neema Yetu juu yenu, tulipompa Mūsā Kitabu chenye kupambanua baina ya haki na batili- nacho ni Taurati- ili muongoke na mtoke kwenye upotevu

    [54] Na Kumbukeni neema Zetu kwenu, aliposema Mūsā kuwaambia watu wake, “Hakika nyinyi mlijidhulumu nafsi zenu kwa kumfanya ndama ni mungu, basi tubieni kwa Muumba wenu kwa kuuana nyinyi kwa nyinyi. Kufanya hivyo ni bora kwenu mbele ya Muumba wenu kuliko kukaa milele Motoni.” Na nyinyi mlifuata amri hiyo, ndipo Mwenyezi Mungu Akawafanyia wema kwa kuikubali toba yenu. Hakika Yeye, Aliyetukuka, ni Ndiye Mwingi wa kukubali toba za wenye kutubia miongoni mwa waja wake na ni Ndiye Mwenye kuwarehemu

    [55] Na Kumbukeni pindi mliposema, “Ewe Mūsā! Hatutakuamini kuwa maneno tunayoyasikia kutoka kwako ni maneno ya Mwenyezi Mungu mpaka tumuone Mwenyezi Mungu waziwazi,” ukashuka moto kutoka mbinguni, na nyinyi mnauona kwa macho yenu, ukawaua kwa sababu ya madhambi yenu na ujasiri wenu kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka

    [56] Kisha tukawahuisha baada ya kufa kwenu kwa kimondo cha moto, ili muishukuru neema ya Mwenyezi Mungu kwenu. Kifo hiki kilikuwa ni adhabu kwao, kisha aliwafufua wakaendelea kuishi mpaka muda wao kumalizika

    [57] Na Kumbukeni neema Zetu mlipokuwa mnahangaika kwenye ardhi, tukawaletea kiwingu cha kuwafinika ili kiwakinge na joto la jua, tukawateremshia mann, nacho ni ktu kifananacho na gundi chenye ladha ya asali; na tukawateremshia salwa, nayo ni aina ya ndege wafananao na tomboro; na tukawaambia, “Kuleni vitu vizuri tulivyowaruzuku na msiende kinyume na dini ya Mwenyezi Mungu,” lakini hamkufuata amri. Na wao hawakutudhulumu sisi kwa kuzikanusha neema hizi, lakini walikuwa wakijidhulumu nafsi zao, Kwani mwisho mbaya wa dhuluma utawarudia wao

    [58] Na Kumbukeni neema yetu kwenu, tuliposema, “Ingieni mji wa Baitul Maqdis na kuleni vizuri vyake, mahali popote pa mji huo, kwa starehe. Na muwe, katika kuingia kwenu, wanyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu, wadhalilifu Kwake na mseme, ‘Ewe Mola wetu, tuondolee madhambi yetu,’ tutawaitikia, tutawasamehe na kuyafanya yasitirike.” Na wenye Kufanya wema katika amali zao tutawazidishia kheri na thawabu

    [59] Wale wajeuri waliyo wapotevu, katika wana wa Isrāīl, walibadilisha neno la Mwenyezi Mungu na wakaipotoa kauli pamoja na kitendo. Kwani waliingia, na huku wakijikokota kwa matako na wakisema, “habbah fī sha’rah’ (mbegu unyweleni.)”, wakiifanyia maskhara dini ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu Aliwateremshia adhabu kutoka mbinguni kwa sababu ya kuasi kwao na kutoka kwao kwenye utiifu kwa Mwenyezi Mungu

    [60] Na Kumbukeni neema Yetu kwenu, mlipokuwa na kiu katika kuzunguka kwenu, alipotuomba Musa, kwa unyenyekevu, tuwaletee maji watu wake. Tukasema, “Lipige hilo jiwe kwa fimbo yako.” Akalipiga, na chemchemi zikabubujika hapo jiweni sehemu kumi na mbili, ikilingana na idadi ya makabila yao, pamoja na kulijulisha kila kabila chemchemi yake ya kutumia, ili wasigombane. Na tukawaambia, “Kuleni na kunyweni riziki ya Mwenyezi Mungu wala msitembee katika ardhi kuleta uharibifu.”

    [61] Na Kumbukeni, tulipowateremshia chakula tamu na ndege wa kuvutia, mkawa hamjali, kama ilivyo desturi yenu, ikawapata dhiki na machovu na mkasema, “Ewe Mūsā! Sisi hatutavumilia chakula hicho kwa hicho kisichobadilika siku zote. Basi tuombee Mola wako Atutolee chakula katika mimea ya ardhini kama mboga, matango, mbegu zinazoliwa, adasi na vitunguu.” Musa akawaambia, kwa kuwapinga vikali, “Vipi mnataka hivyi ambavyo ni duni zaidi na mnaacha riziki yenye manufaa ambayo Mwenyezi Mungu amewachagulia? Ondokeni jangwani na mshuke mjini. Huko mtavipata mnavyovitamani sana kwenye mashamba na masoko.” Waliposhuka, iliwabainikia kuwa wao wanatanguliza chaguo lao,kila mahali, juu ya chaguo la Mwenyezi Mungu na wanayafadhilisha matamanio yao juu ya vitu ambavyo Mwenyezi Mungu Alilowachagulia. Kwa hivyo, sifa ya unyonge na umasikini wa moyo iliwaambata, na wakaondoka na kurudi wakiwa wamo kwenye ghadhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuipa mgongo dini ya Mwenyezi Mungu, na kwa kuwa wao walikuwa wakikanusha aya za Mwenyezi Mungu na kuua Manabii kwa udhalimu na uadui. Yote hayo ni kwa sababu ya kuasi kwao na kuivuka mipaka ya Mola wao

    [62] Hakika Waumini wa ummah huu waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake na wakatekeleza Sheria Yake, na wale waliokuwa kabla ya kutumilizwa Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, miongoni mwa ummah waliopita katika Mayahudi, Wanaswara na Wasabai (Sābiūn), nao ni watu walioko kwenye tabia za maumbile na hawana dini maalumu wanayoifuata, wote hawa wakimuamini Mwenyezi Mungu, imani ya sawa iliyotakasika, wakaiamini Siku ya kufufuliwa na Malipo na wakafanya amali zenye kumridhi Mwenyezi Mungu, basi thawabu zao zimethibiti kwa Mola wao. Wao hawatakuwa na khofu juu ya mambo yao ya Akhera ambayo wao watayakabili. Na wala wao hawatahuzunika juu ya mambo ya dunia waliyoyakosa. Ama baada ya kutumilizwa Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukie yeye, kuwa ni mwisho wa Manabii na Mitume, kwa watu wote, Mwenyezi Mungu Hatakubali dini, kwa yoyote, isipokuwa ile aliyokuja nayo ambayo ni Uislamu

    [63] Na kumbukeni, enyi Wana wa Isrāīl, tulipochukua kutoka kwenu ahadi ya mkazo ya kumuamini Mwenyezi Mungu na kumpwekesha kwa ibada, na tukaliinua jabali la Tūr juu yenu na tukawaambia, “Chukueni, kwa bidii na jitihadi, Kitabu tulichowapa na mkitunze. Na mkitofanya hivyo, tutaliangusha hili jabali juu yenu liwafinike, na msiisahau Taurati kwa maneno na vitendo, mpate kunicha na kuiogopa adhabu Yangu.”

    [64] Kisha mlienda kinyume na mkaasi mara nyingine, baada ya kuchukuwa ahadi ya mkazo na kunyanyuliwa jabali, kama desturi yenu daima. Na lau si wema wa Mwenyezi Mungu na rehema Yake kuikubali toba yenu na kuyasamehe makosa yenu, mungalikuwa ni wenye hasara ya duniani na ya Akhera

    [65] Hakika mlijua, enyi kongamano la Mayahudi na Wanaswara, adhabu iliyowapata mababu zenu waliopita, watu wa kijiji kilichoasi amri ya Mwenyezi Mungu katika yale aliyowachukulia ahadi ya kuitukuza Siku ya Jumamosi. Wakafanya hila ya kuvua samaki siku ya Jumamosi kwa kuweka mitego na kufukua mashimo. Walipofanya hivyo, Mwenyezi Mungu aliwageuza kuwa manyani wenye kudharauliwa

    [66] Tukakifanya kijiji hicho ni mazingatio kwa watu wa vijiji vya karibu ambao itawafikia habari yake na vituko vilivyotokea huko, na ni mazingatio kwa mwenye kufanya madhambi kama hayo baada yake. Na pia tulikifanya ni mawaidha kwa watu wema, wapate kujua kuwa wao wako kwenye haki, ili wasimame imara juu yake

    [67] Na Kumbukeni, enyi wana wa Isrāīl, makosa ya mababu zenu, ushindani wao mwingi na kujadiliana kwao na Mūsā, rehema na amani zimshukie, pindi alipowaambia, “Hakika Mwenyezi Mungu Anawaamuru mchinje ng’ombe.” Wakasema, wakiwa na kiburi, “Unatufanyia mzaha na kutuchezea?” Mūsā akawajibu, “Ninajilinda kwa Mwenyezi Mungu nisiwe ni miongoni mwa wanaofanya stihizai.”

    [68] Walisema, “Tuombee Mola wako atufafanulie sifa ya ng’ombe huyu.” Akawajibu, “Mwenyezi Mungu Anawaambia kwamba sifa yake ni asiwe mkubwa wa miaka wala mdogo. Yeye ni wa katikati baina ya uzee na ujana, basi fanyeni haraka kutii amri ya Mola wenu.”

    [69] Wakarudi kwenye kujadili kwao wakisema, “Mwambie Mola wako Atufafanulie rangi yake.” Akasema kuwaambia, “Yeye anasema kwamba huyo ni rangi ya manjano iliyoiva sana, anayemtia furaha mwenye kumwangalia.”

    [70] Wana wa Isrāīl walimwambia Mūsā, “Tuombee Mola wako Atufafanulie sifa zake nyingine zisizokuwa zilizotangulia. Sababu ng’ombe wenye sifa hizi ni wengi. Kwa hivyo, tumechanganyikiwa hatujui tuchague yupi. Na sisi, Mwenyezi Mungu Anapotaka, tutaongokea kumjua ng’ombe ambaye ilitolewa amri achinjwe.”

    [71] Mūsā aliwaambia, “Mwenyezi Mungu Anasema kwamba huyo ni ng’ombe asiyetumiwa kwa kazi ya kulima ardhi ya kilimo, hakutayarishwa kutia maji, hana kasoro yoyote na hana alama yoyote ya rangi isiyokuwa rangi ya ngozi yake.” Wakasema, “Sasa umekuja na ukweli wa sifa ya ng’ombe.” Wakalazimika kumchinja baada ya muda mrefu wa mbinu za kuchelewesha. Na walikuwa karibu kutofanya hilo kwa ushindani wao. Hivi ndivyo walivyojitilia mkazo, ndipo Mwenyezi Mungu Akawafanyia mkazo

    [72] Na Kumbukeni, mlipomuua mtu, mkabishana kuhusu yeye, akawa kila mmoja ajiepushia nafsi yake tuhuma ya kuua na hali Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyafichua yale ambayo mlikuwa mkiyaficha kuhusu kifo cha yule aliyeuawa

    [73] Tukasema, “Mpigeni aliyeuliwa kwa sehemu ya yule ng’ombe aliyechinjwa, Mwenyezi Mungu atamfufua akiwa hai na atawaambia muuaji wake ni nani.” Basi wakampiga kwa ile sehemu ya ng’ombe, Mwenyezi Mungu Akamhuisha na akamtaja muuaji wake. Hivyo ndivyo Anavyohuisha Mwenyezi Mungu wafu Siku ya Kiyama na kuwaonyesha nyinyi, Wana wa Isrāīl, miujiza Yake yenye dalili ya ukamilifu wa uweza wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, ili mfikiri kwa akili zenu mpate kujiepusha na vitendo vya kumuasi

    [74] Lakini nyinyi hamkufaidika na hilo. Kwani baada ya miujiza yote hii yenye kupita mipaka ya uwezo wa kiumbe, nyoyo zenu zilikuwa ngumu na shupavu kwa namna ambayo hakuna kheri iliopenyeza ndani, na hazikulainika mbele ya miujiza yenye kushinda niliyowaonesha, mpaka nyoyo zenu zikafikia hadi ya kuwa ni kama jiwe gumu, bali zililishinda jiwe kwa ugumu wake. Kwani miongoni mwa mawe kuna yanayopanuka na kutoboka na maji yakabubujika kwa wingi kutoka humo mpaka yakawa ni mito yenye kupata. Na miongoni mwayo kuna yanayofanya nyufa, yakapasuka na kuchimbuka maji ya chemchemi na mikondo. Na miongoni mwayo kuna yanayoanguka kutoka juu ya milima kwa kumwogopa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kumuadhimisha. Na Mwenyezi Mungu Hakuwa ni Mwenye kughafilika kwa mnayoyafanya

    [75] Enyi waislamu! Kwani mumesahau vitendo vya Wana wa Isrāīl, ndipo nafsi zenu zikawa na tamaa kuwa Mayahudi wataiamini dini yenu? Wanavyuoni wao walikuwa wakisikia maneno ya Mwenyezi Mungu ya Taurati, kisha wakiyapotoa kwa kuyageuza na kuyapa maana yasiyo sahihi baada ya kuyafahamu maana yake ya kweli, au kwa kuyageuza matamshi yake, hali wanajua kuwa wao wanayapotoa maneno ya Mwenyezi Mungu kwa kusudi na urongo

    [76] Hawa Mayahudi, wakikutana na Waumina, wanasema kwa ndimi zao, “Tumeamini dini yenu na Mtume wenu aliyebashiriwa katika Taurati.” Na wakiwa faragha, wao kwa wao, hawa wanafiki wa kiyahudi, huwa wakiambiana kwa njia ya kukemeana, “Vipi nyinyi mnawahadithia Waumini yale ambayo Mwenyezi Mungu Amewabainishia katika Taurati kuhusu Muhammad, mkawapa hoja juu yenu mbele ya Mola wenu Siku ya Kiyama? Kwani hamfahamu mkajihadhari?”

    [77] Je, kwani wanafanya uhalifu wote huu na hali wao hawajui kuwa Mwenyezi Mungu Anayajua yote wanayoyaficha na kuyadhihirisha

    [78] Na kati yao kuna watu wasiojua kusoma na kuandika, na wasioijua Taurati na yaliyomo ndani yake ya sifa za Nabii na Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na hawana chochote kuhusu hayo isipokuwa ni maneno ya urongo na dhana mbovu

    [79] Maangamivu na onyo kali kwa wanavyuoni wa shari wa Kiyahudi ambao wanaandika kitabu kwa mikono yao kisha wanaosema, “Hiki kinatoka kwa Mwenyezi Mungu.” Nacho kinaenda kinyume na yale ambayo Mwenyezi Mungu Amemteremshia Nabii wake Mūsā rehema na amani zimshukie, ili wapokee, kwa kitendo hicho, manufaa ya ulimwenguni. Basi wao watapata mateso yenye kuangamiza kwa sababu ya kuuandika kwao ubatilifu huu kwa mikono yao, na watapata mateso yenye kuangamiza kwa sababu ya mali ya haramu wanayoyachukua kwa shughuli yao hiyo, kama hongo na mfano wake

    [80] Walisema Wana wa Israili, “Moto hautupati huko Akhera isipokuwa kwa siku chache zinazohesabika.” Waambie, ewe Mtume, kwa kuyavunja madai yao, “Kwani nyinyi muna ahadi, kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ya jambo hilo? Mwenyezi Mungu Haendi kinyume ahadi yake. Lakini nyinyi munasema kuhusu Mwenyezi Mungu msiyoyajua kwa kuzua kwenu urongo.”

    [81] Hukumu ya Mwenyezi Mungu imethibiti kwamba mwenye kutenda makosa mpaka yakamtia ukafirini na madhambi yake yakamtawala yeye sehemu zake zote, na hali hii haiwi isipokuwa kwa mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, wote hao, washirikina na makafiri, ndio wenye kukaa Motoni makao ya milele yasiyokatika

    [82] Na hukumu ya Mwenyezi Mungu iliyothibiti, kwa upande mwengine, ni kwamba wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake imani ya kikweli iliyosafika na Wakafanya vitendo vinavyoambatana na Sheria ya Mwenyezi Mungu Aliyowapelekea Mitume Wake kwa njia ya Wahyi, hao watakaa Peponi makao ya milele yasiyokatika huko Akhera

    [83] Na Kumbukeni, enyi Wana wa Isrāīl, tulipochukua ahadi ya mkazo kwenu kwamba mtamuabudu Mwenyezi Mungu peke Yake Asiye na mshirika, muwafanyie wema wazazi wawili na watoto waliofiliwa na baba zao nao wako chini ya umri wa kubaleghe na masikini na kwamba muwaambie watu maneno mazuri, pamoja na kusimamisha Swala na kutoa Zaka. Kisha mkageuka na mkavunja ahadi, isipokuwa wachache katika nyinyi waliosimama imara juu yake. Na nyinyi bado mnaendelea kugeuka kwenu

    [84] Na Kumbukeni, enyi Wana wa Isrāīl, tulipochukua kwenu ahadi ya mkazo katika Taurati ya kuharamisha umwagaji damu baina yenu, nyinyi kwa nyinyi, na kutoana majumbani nyinyi kwa nyinyi. Kisha mkakubali hilo na hali nyinyi mnashuhudia kuwa ni kweli

    [85] Kisha nyinyi kwa nyinyi mnauana, baadhi yenu wanawaua wengine, na baadhi yenu wanawatoa wengine majumbani mwao; na kila kundi kati yenu linajitafutia nguvu kwa maadui dhidi ya ndugu zake kwa njia ya udhalimu na uonevu. Na mkijiwa nao, hao ndugu zenu, ni mateka kwenye mikono ya maadui, mnafanya haraka kuwakomboa kwa kulipa fidia, pamoja na kuwa imeharamishwa kwenu kuwatoa majumbani mwao. Ni ubaya ulioje mnaoufanya wa kuziamini baadhi ya hukumu za Taurati na kuzikanusha nyingine! Basi Malipo ya wanaoyafanaya hayo si mengine ila ni unyonge na fedheha ulimwenguni, na Siku ya Kiyama watapelekwa kwenye adhabu kali sana ndani ya Moto. Na Mwenyezi Mungu si Mwenye kughafilika kwa mnayoyafanya

    [86] Hao ndio waliofadhilisha uhai wa ulimwenguni juu ya Akhera, basi hawatapunguziwa adhabu wala wao hawatakuwa na msaidizi wa kuwanusuru na adhabu ya Mwenyezi Mungu

    [87] Hakika tulimpa Mūsā Taurati, na kuwaleta baada yake Mitume wengine miongoni mwa Wana wa Isrāīl. Na tulimpa ' Īsā mwana wa Maryam miujiza iliyo wazi na kumtilia nguvu kwa Jibrili, amani imshukie. Kwani nyinyi mumekuwa kila Mtume anapowajia na Wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, usiolingana na matamanio yenu, mnamfanyia kiburi, wengine mkiwakanusha na wengine mkiwaua

    [88] Wana wa Isrāīl walisema kumwambia Nabii na Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, “Nyoyo zetu zimezibwa kwa namna ambayo maneno yako hayapenyezi ndani yake.” Mambo si kama walivyodai. Bali nyonyo zao zimelaaniwa, zimepigwa muhuri juu ya hiyo laana. Na wao wamefukuzwa kutoka kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu kwa sababu ya kukanusha kwao. Wao hawaamini isipokuwa imani chache isiyowafaa

    [89] Na ilipowajia Qur’ani inayotoka kwa Mwenyezi Mungu, ikisadikisha yale ambayo waliokuwa nayo kwenye Taurati, waliikanusha na kuukataa utume wa Muhammad, rehema na mani zimshukie. Na walikuwa, kabla ya kutumilizwa kwake, wakitumai kusaidiwa na yeye dhidhi ya washirikina wa Kiarabu, na walikuwa wakisema, “Umekaribia wakati wa kutumilizwa Mtume wa zama za mwisho ambaye sisi tutamfuata na tutapigana na nyinyi tukiwa pamoja na yeye.” Alipowajia huyo Mtume, ambaye walizijua sifa zake na ukweli wake, walimkataa na walimkanusha. Basi laana ya Mwenyezi Mungu imshukie kila aliyemkanusha Nabii na Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad, rehema na amani zimshukie, na kukanusha Kitabu chake ambacho Mwenyezi Mungu alimletea kwa njia ya Wahyi

    [90] Ni baya chaguo la Wana wa Isrāīl walilojichagulia. Kwani walibadilisha imani kwa ukafiri, (kwa kuacha imani na kuchukua ukafiri) kwa dhulma na uhasidi kwa kuwa Mwenyezi Mungu, kwa fadhila ZAke, Alimteremshia Nabii Wake na Mtume Wake Muhammad, rehema na amani zimshukie. Basi wakarudi na hali ya kuwa Mwenyezi Mungu Ana ghadhabu juu yao kwa kumkanusha kwao Nabii Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, baada ya kuwa na ghadhabu juu yao kwa kuipotoa Taurati. Na wenye kukanusha unabii wa Muhammad, rehema na amani zimshukie, wana adhabu yenye kuwabadilisha na kuwafanya wanyonge

    [91] Na baadhi ya Waislamu wanaposema kuwaambia Mayahudi, “Aminini Qur’ani,” wanasema, “Sisi tunaviamini vilivyoteremshwa kwa Mitume wetu.” Na wao wanakanusha vilivyoteremshwa na Mwenyezi Mungu baada yake, pamoja na kuwa ndio haki inayosadikisha vile walivyonavyo. Lau wao walikuwa wanaviamini vitabu vyao kikweli, wangaliiamini Qur’ani iliyozisadikisha. Waambie, ewe Mtume, “Iwapo nyinyi mnayamini yale mliyoteremshiwa na Mwenyezi Mungu kwenu, kwa nini mliwaua Manabii wa Mwenyezi Mungu wakati wa nyuma?”

    [92] Hakika Nabii wa Mwenyezi Mungu, Mūsā, aliwajia nyinyi na miujiza iliyo wazi yenye dalili ya ukweli wake, kama mafuriko, nzige, chawa, vyura na mengineyo katika yale aliyoyataja Mwenyezi Mungu katika Qur’ani tukufu. Pamoja na hivyo, mumemchukuwa ndama mkamfanya ni muabudiwa, baada ya Mūsā kuondoka kuenda kukutana na Mola wake. Na nyinyi kwa kufanya hivyo mnavuka mipaka ya Mwenyezi Mungu

    [93] Na Kumbukeni, wakati tulipochukua kwenu ahadi yenye mkazo ya kuikubali Taurati aliyokuja nayo Mūsā, mkavunja ahadi, tukaliinua jabali la Tūr juu ya vichwa vyenu na tukasema, “Tuchukueni tulichowapa kwa bidii, na msikie na mtii, au tutaliangusha jabali juu yenu.” Mkasema, “Tumesikia kauli yako na tumeasi amri yako,” kwa kuwa ibada ya ndama imetangamana na nyoyo zenu kwa sababu ya kuendelea kwenu sana kwenye ukafiri. Waambie, ewe Mtume, Ni mbaya iliyoje hiyo njia ya ukafiri na upotevu ambayo imani yenu imewapeleka, iwapo nyinyi mnayasadiki yale yaliyoteremshwa kwenu

    [94] Sema, ewe Mtume, kuwaambia Mayahudi ambao wanadai kuwa Pepo ni yao peke yao, kwa kudai kuwa wao tu, bila watu wengine, ndio mawalii wa Mwenyezi Mungu na kuwa wao ni watoto Wake na vipenzi Vyake, “Mambo yakiwa ni hivyo, waapizeni kufa waliyo warongo katika nyinyi au wasiokuwa katika nyinyi, iwapo nyinyi ni wakweli katika madai yenu haya.”

    [95] Na hawatalifanya hilo kabisa, kwa wanayoyajua ya ukweli wa Nabii Muhammad, rehema na amani zimshukie, na ya urongo na uzushi wao, na kwa ukafiri na uasi walioufanya unaopelekea kukoseshwa Pepo na kuingia Motoni. Na Mwenyezi Mungu Anawajua madhalimu miongoni mwa waja wake na Atawalipa kwa dhulma zao

    [96] Na utajua tena utajua, ewe Mtume, kuwa Mayahudi ni wenye kupenda mno, miongoni mwa watu, maisha marefu, hata yawe ni maisha ya unyonge na udhalilifu namna gani. Kupenda kwao maisha marefu kunazidi vile washirikina wanavyoyapenda. Myahudi anatamani lau ataishi miaka elfu moja. Na umri huo, lau aufikia, hautamwepusha na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, hakuna kitu chochote chenye kufichika Kwake katika matendo yao, na Atawalipa, kwa hiyo matendo yao, adhabu wanayostahiki

    [97] Sema, ewe Mtume, kuwaambia Mayahudi waliposema, “Jibrili ni adui yetu miongoni mwa Malaika.”: “Mwenye kuwa ni adui wa Jibrili, basi ajue kuwa yeye ameiteremsha Qur’ani na kuitia ndani ya moyo wako kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, ikiwa ni yenye kuvisadikisha vitabu vya Mwenyezi Mungu vilivyoitangulia, yenye kuongoza kwenye njia ya haki na yenye kuwapa wenye kuamini bishara ya kila wema wa dunia na Akhera.”

    [98] Mwenye kumfanyia uadui Mwenyezi Mungu, Malaika Wake, Wajumbe Wake ambao ni Malaika au binadamu, hasahasa Malaika wawili: Jibrili na Mikaili, huwa amemfanyia uadui Mwenyezi Mungu. Sababu Mayahudi walidai kwamba Jibrili ni adui wao na Mikaili ni rafiki yao. Mwenyezi Mungu Akawajulisha kwamba mwenye kuwa adui wa mmoja katika wao huwa ni adui wa Mwengine na pia ni adui wa Mwenyezi Mungu. Kwani Mwenyezi Mungu ni adui wa wenye kuyakanusha yale aliyoyateremsha kwa Mtume wake Muhammad, rehema na amani zimshukie

    [99] Hakika tulikuteremshia aya zilizo wazi, zinazoonyesha kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kikweli; na hawazikanushi aya hizo isipokuwa wenye kutoka nje ya Dini ya Mwenyezi Mungu

    [100] Ni ubaya ulioje wa hali ya Wana wa Isrāīl katika kuvunja kwao ahadi! Kila wanapotoa ahadi, kinatoka kikundi cha watu katika wao wakaitupa na wakaivunja. Utawaona wanaifunga ahadi leo na kuitangua kesho. Bali wengi wao hawayaamini aliyokuja nayo Nabii wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake Muhammad, rehema na amani zimshukiye yeye

    [101] Na alipowajia Muhammad, rehema na amani zimshukie, na Qur’ani inayoafikiana na Taurati waliyonayo, kilitoka kikundi cha watu katika wao wakakitupa kitabu cha Mwenyezi Mungu, na kukiweka nyuma ya migongo yao. Hali yao ni hali ya wajinga wasiojua uhakika wake

    [102] Na Mayahudi walifuata yale ambayo mashetani walikuwa wanawasimulia wachawi katika kipindi cha ufalme wa Sulaimān mwana wa Dāwūd. Na Sulaymān hakukufuru na wala hakujifundisha uchawi. Lakini mashetani ndio walimkanusha Mwenyezi Mungu kwa kuwafundisha watu uchawi, kwa kuwaharibia dini yao. Mayahudi pia waliufuata uchawi ulioshushwa kwa malaika wawili: Hārūt na Mārūt, katika ardhi ya Babil ilyoko Iraq, ukiwa ni mtihani na majaribio kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa waja Wake. Na hao Malaika wawili hawakuwa wakimfunza yoyote mpaka wamnasihi na kumuonya asijifunze uchawi na kumwambia, “Usikufuru kwa kujifunza uchawi na kuwatii mashetani.” Basi watu walikuwa wakijifunza kutoka kwa Malaika wawili vitu vinavyozusha chuki baina ya mume na mke mpaka wakafarikana. Na wachawi hawana uwezo wa kumdhuru, kwa uchawi wao, yoyote isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na hukumu Yake. Na wachawi hawajifunzi ila shari yenye kuwadhuru na kutowapa nafuu. Mashetani waliupeleka uchawi kwa Mayahudi, ukaenea kwao mpaka wakaufadhilisha juu ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Na Mayahudi walijua kwamba mwenye kuchagua uchawi na kuacha haki, hatakuwa na fungu lolote la kheri huko Akhera. Ni ubaya ulioje uchawi na ukafiri waliojichagulia nafsi zao kuwa ni badala ya Imani na kumfuata Mtume, lau walikuwa na elimu yenye kuzalisha vitendo vya kufuata mawaidha wapewayo

    [103] Na lau Mayahudi waliamini na kumuogopa Mwenyezi Mungu, wangalikuwa na yakini kuwa thawabu za Mwenyezi Mungu ni bora kwao kuliko uchawi na kuliko yale waliyoyapata kupitia huo uchawi. Lau walikuwa wanajua thawabu na malipo yanayopatikana kwa kuamini na kumcha Mwenyezi Mungu, ujuzi wa kihakika, wangaliamini

    [104] Enyi ambao mliamini, msiseme kumwambia Mtume Muhammad, rehema na amani zimshukie, “Rā’nā.” Yaani: tupatie masikizi yako, utufahamu na utufahamishe. Sababu Mayahudi walikuwa wakisema maneno haya kumwambia Nabii, rehema na amani zimshukie, wakipotoa ndimi zao kwa neno hilo, wakikusudia kumtukana na kumnasibisha na kutoelewa. Na semeni badala yake, enyi Waumini, “Undhurnā.” Yaani: tuangalie na utuchunge. Lina maana yale-yale yanayokusudiwa. «Na msikie Kitabu cha Mola wenu mnachosomewa na mkifahamu.» Na wenye kukanusha wana adhabu yenye kuumiza

    [105] Makafiri, miongoni mwa Watu wa Kitabu na washirikina, hawapendi mteremshiwe kheri, hata kama ni ndogo kabisa, itokao kwa Mola wenu, iwe ni Qur’ani au elimu au ushindi au bishara njema. Mwenyezi Mungu Anamhusisha Amtakaye kwa rehema Zake za unabii na utume. Mwenyezi Mungu ni Mwenye vipaji vingi venye kuenea

    [106] Tunaipoibadilisha aya au kuiondoa kutoka nyoyoni na akilini, tunaileta yenye manufaa zaidi kwenu kuliko hiyo au tunaileta iliyo mfano wake katika utekelelezaji na thawabu. Na kila mojawapo ya aya hizo ina hekima yake. Kwani hujui, ewe Nabii, kwamba Mwenyezi Mungu ni Muweza, hakuna kitu kinachomshinda

    [107] Kwani hukujua, ewe Nabii, wewe na ummah wako, kwamba Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Ndiye Mwenye kumiliki, Ndiye Mwenye kuendesha mambo ya mbinguni na ardhini? Anafanya Analolitaka na Anatoa uamuzi Anaotaka. Anawaamrisha waja Wake na kuwakataza Anavyotaka, na ni juu yao kutii na kukubali. Na wajue wenye kumuasi Yeye kuwa hakuna rafiki mwenye kuwasaidia wala muokozi mwenye kuzuia adhabu ya Mwenyezi Mungu isiwapate

    [108] Bali nyinyi mnataka, enyi watu, kumuuliza Mtume wenu Muhammad, rehema na amani zimshukie, awapatie mambo, kwa njia ya ukaidi na ujeuri, kama yalivyotakwa, mfano wa hayo, kutoka kwa Mua. Na jueni kwamba mwenye kuchagua ukafiri na kuacha Imani, ashatoka nje ya njia ya Mwenyezi Mungu iliyolingana sawa na ameingia kwenye ujinga na upotevu

    [109] Wengi wa Watu wa Kitabu watamani kuwarudisha nyinyi, baada ya kuamini kwenu, muwe makafiri kama mlivyokuwa kabla mkiabudu masanamu. Haya ni kwa sababu ya chuki zilizojaa kwenye nafsi zao, baada ya kuwabainikia ukweli wa Nabii na Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad, rehema na amani zimshukiye, katika yale aliyokuja nayo. Basi lipuzeni lolote la ubaya au makosa lililotoka kwao. Na sameheni ujahili wao mpaka Mwenyezi Mungu Alete hukumu Yake ya kupigana na wao (na hili lilikuwa), na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu; hakuna kitu chochote kimshindacho

    [110] Jishughulisheni, enyi Waumini, kutekeleza Swala kwa namna sahihi ipasavyo na kutoa Zaka zilizofaradhiwa. Na mjue kwamaba kila kheri mnayoitangulizia nafsi zenu, mtapata thawabu zake Akhera mbele ya Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye Aliyetukuka ni Mwenye kuyaona matendo yenu na Atawalipa kwayo

    [111] Mayahudi na Wanaswara, kila mmoja katika wao anadai kuwa Pepo itaingiwa na pote lake peke yake, hataingia asiyekuwa katika pote hilo. Hayo ni mawazo yao maovu. Waambie, ewe Mtume, “Leteni dalili yenu juu ya ushahidi wa hilo mnalolidai iwapo nyinyi ni wakweli katika madai yenu.”

    [112] Mambo si kama walivyodhania kuwa Pepo ni ya pote fulani tu, si ya pote lingine. Hakika ataingia Peponi mwenye kumtakasa Mwenyezi Mungu Peke Yake Asiye na mshirika na akawa ni mwenye kumfuata Mtume Muhammad, rehema na amani zimshukie, katika maneno yake yote na vitendo vyake vyote. Basi mwenye kufanya hayo atakuwa na thawabu ya matendo yake mbele ya Mola wake huko Akhera, nayo ni kuingia Peponi, hali ya kuwa wao, hao wenye kuingia Peponi, hawaogopi mambo ya Akhera yanayowakabili mbele yao, wala hawahuzuniki juu ya hadhi za ulimwengu zilizowapita

    [113] Na walisema Mayahudi, “Wanaswara hawako kwenye dini sahihi. Ndivyo hivyo kama walivyosema Wanaswara kuhusu Mayahudi, na hali wote wanasoma Taurati na Injili, ambapo ndani yake kuna ulazima wa kuwaamini Mitume wote. Hivyo ndivyo pia walivyosema wasiojua miongoni mwa washirikina: Waarabu na wengineo. Yaani, walisema kumwambia kila mwenye dini, “Wewe huko kwenye kitu chochote cha maana.” Basi Mwenyezi Mungu Ataamua baina yao Siku ya Kiyama katika yale mambo ya kidini waliotafautiana juu yake, na kumlipa kila mtu kwa matendo yake aliyoyafanya

    [114] Hakuna dhalimu zaidi kuliko wale waliozuia kutajwa Mwenyezi Mungu katika msikiti, kama kusimamisha Swala na kusoma Qur’ani na mengine mfano wa hayo, na wakafanya bidii kuifanya magofu kwa kuivunja au kuifunga au kwa kuwazuia Waumini kuijia. Madhalimu hao haikuwa yapasa kwao kuingia hiyo msikiti isipokuwa wakiwa katika hali ya kuogopa na kutishika wasipate adhabu. Kwa matendo yao hayo, watakuwa na unyonge na fedheha ulimwenguni, na watakuwa na adhabu kali kesho Akhera

    [115] Zote pande mbili, upande wa kuchomoza jua na wa kutwa kwake na vilivyo baina yake, ni vya Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye Mmiliki wa ardhi yote. Basi pande wowote mnaouelekea kwenye Swala zenu kwa kuwa mmeamrishwa na Mwenyezi Mungu, Hakika nyinyi huwa mnaukusudia Uso Wake, hamkutoka kwenye ufalme Wake na utiifu wenu Kwake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye rehema za kuenea kwa waja Wake, ni Mjuzi wa vitendo vyao, hakuna chochote chenye kufichika Kwake Asikijue

    [116] Na walisema Mayahudi na Wanaswara, “Mwenyezi Mungu Amejifanyia mtoto.” Ameepukana Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa pungufu ni Kwake, na neno hilo la batili! Kwani wote walioko mbinguni na ardhini ni milki Yake na ni watumwa Wake. Wote wanamnyenyekea Yeye na wanapelekewa wakiwa chini ya uendeshaji Wake

    [117] Na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Ndiye Muumba mbingu na ardhi, bila ya kuwa na mfano uliotangulia. Na Anapolikadiri jambo na Akataka liwe, huliambia, “Kuwa,” likawa

    [118] Walisema wajinga miongoni mwa Watu wa Kitabu na wengineo kumwambia Nabii na Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad, rehema na amani zimshukie, kwa njia ya inadi, “Si aseme na sisi Mwenyezi Mungu moja kwa moja Atuambie kwamba wewe ni Mtume Wake au itujie miujiza itokayo kwa Mwenyezi Mungu yenye kuonyesha ukweli wako.” Neno kama hili walilisema ummah waliopata kuwaambia Mitume wao, kwa njia ya ukaidi na ujeuri, kwa sababu ya kufanana nyoyo za waliotangulia na waliofuata katika ukafiri na upotevu. Hakika Tumezifafanua aya kwa wale wanaoamini Imani ya kikweli, kwa kumuamini kwao Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kuzifuata kwao Sheria Alizowawekea

    [119] Sisi tumekutumiliza, ewe Mtume, kwa Dini ya haki iliyotiliwa nguvu kwa hoja na miujiza. Basi ifikishe kwa watu, pamoja na kuwapa Waumini bishara ya kheri ya dunia na ya Akhera, na kuwatisha wakaidi na adhabu ya Mwenyezi Mungu inayowangojea. Na baada ya kufikisha ujumbe, hutaulizwa juu ya ukafiri wa wenye kukukanusha. Wao wataingia Motoni, Siku ya Kiyama, wala hawatatoka humo

    [120] Na hawataridhika nawe, ewe Mtume, Mayahudi wala Wanaswara isipokuwa ikiwa utaacha Dini yako na ukafuata Dini yao. Waambie, “Dini ya Uislamu ndiyo Dinii sahihi” Na ukifuata matamanio ya hao, baada ya wahyi uliokujia, hutakuwa na rafiki wa kukunufaisha kwa Mwenyezi Mungu wala msaidizi wa kukunusuru. Maneno haya ingawa anaambiwa Mtume, yanalekezwa kwa ummah wote

    [121] Wale Mayahudi na Wanaswara tuliowapa Kitabu, wanakisoma kisomo cha sawasawa, wanakifiuata kipasavyo kufuatwa na wanayaamini yaliyomo ndani yake ya kuwaamini Mitume wa Mwenyezi Mungu, ambao miongoni mwao ni wa mwisho wao, Nabii wetu na Mtume wetu Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie,. Na hawayapotoi wala hawayabadilishi yaliyokuja ndani yake. Hawa ndio waliomuamini Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na aliyoteremshiwa. Ama wale waliogeuza sehemu ya Kitabu na wakaficha baadhi yake, hao ndio waliomkanusha Nabii wa Mwenyezi Mungu Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na yale aliyoteremshiwa. Na wenye kumkanusha, hao watakuwa ni wetu wenye hasara kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu

    [122] Enyi kizazi cha Ya’qūb, tajeni neema zangu kubwa kwenu na mkumbuke kuwa niliwatukuza juu ya watu wa zama zenu kwa wingi wa Manabii wenu na kwa Vitabu walivyoteremshiwa

    [123] Na ogopeni vitisho vya Siku ya Hesabu. Kwani hapo, hakuna nafsi itakayoifaa kitu chochote nafsi nyingine, wala Mwenyezi Mungu Hatakubali fidia, kutoka kwa hiyo nafsi, ya kuiyokoa na adhabu, wala hainufaiki kwa kuombewa na hakuna yoyote wa kuinusuru

    [124] Na Kumbuka, ewe Nabii, wakati Mwenyezi Mungu Alipomfanyia mtihani Ibrāhīm kwa amri Alizomkalifisha nazo, akazitekeleza na kusimama nazo kwa njia nzuri. Mwenyezi Mungu Akamwambia, “Mimi nimekufanya wewe ni kiigizo kwa watu.” Ibrāhīm akasema, “Ewe Mola wajaalie baadhi ya watu wa kizazi chake ni viongozi kwa ukarimu Zako.” Mwenyezi Mungu Akamjibu kwamba madhalimu hawatapata uongozi wa kidini

    [125] Na Kumbuka, ewe Nabii, wakati tulipoifanya Alkaba ni marejeo ya watu; wanakuja kuikusudia, kisha wanarudi makwao kwa watu wao, kisha wanairudia tena, ni makusanyiko yao katika Hija, Umra, kutufu na kuswali, na pia ni amani kwao: hakuna adui anayewashambulia wakiwa hapo na tukasema, “Pafanyeni hapo Maqām Ibrāhīm ni mahali pa kuswali. Maqām Ibrāhīn ni jiwe ambalo Ibrāhīm alisimama juu yake alipokuwa akijenga Alkaba. Na tulimletea Wahyi Ibrahīm na mtoto wake Ismāīl kwa kuwaambia, «Isafisheni Nyumba Yangu na kila najisi na uchafu kwa ajili ya wenye kuabudu kwa kutufu pambizoni mwa Alkaba au kuketi Itikafu (I’tikāf) Msikitini na kuswali hapo.”

    [126] Na Kumbuka, ewe Nabii, wakati Aliposema Ibrāhīm akiwa katika maombi, “Ewe Mola wangu! ijaalie Makkah ni mji wenye amani usiokuwa na kitisho, uwaruzuku watu wake aina ya matunda na uwahusu kwa riziki hii wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho.” Mwenyezi Mungu Alisema, “Na mwenye kukufuru katika wao nitamruzuku ulimwenguni na kumstarehesha starehe chache, kasha nitamlazimisha kwa nguvu kwenda Motoni. Ubaya wa marejeo na makao ni mwisho huu.”

    [127] Na Kumbuka, ewe Nabii, wakati Ibrāhīm na Ismāīl walipoinua misingi ya Alkaba, huku wakimuomba Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu, “Ewe Mola wetu! Tutakabalie amali zetu njema na dua zetu! Kwani wewe Ndiye mwenye kusikia maneno ya waja wako, Ndiye mwenye kujua hali zao

    [128] “Ewe Mola wetu, na utujaalie, sisi wawili, ni wenye kusimama imara juu ya Uislamu, ni wenye kukufuata kwa Imani. Utuonyeshe njia za kukuabudu. Utusamehe madhambi yetu. Hakika Wewe Ndiye Mwingi wa kukubali toba za waja wako, Ndiye mkunjufu wa rehema kwao

    [129] “Ewe Mola wetu, mtumilize katika ummah huu mjumbe miongoni mwa watu wa kizazi cha Ismāīl, awasomee aya Zako na awafundishe Kitabu na Sunnah, awasafishe na ushirikina na tabia mbaya. Hakika Wewe Ndiye Mshindi asiyeshindwa na kitu, Ndiye Mwenye hekima Anayeviweka vitu vyote mahali pake.”

    [130] Hakuna yoyote anayeipa mgongo Dini ya Ibrahim, nayo ni Uislamu, isipokuwa safihi aliye mjinga. Na hakika tulimchagua Ibrahim duniani kuwa Nabii na Mtume, na kesho Akhera kuwa ni miongoni mwa watu wema ambao wana daraja za juu kabisa

    [131] Na sababu ya kuchaguliwa kwake huku ni kukimbilia kwake kwenye Uislamu bila kusita. Alipoambiwa na Mola wake, “Itakase nafsi yako kwa Mwenyezi Mungu kwa kujisalimisha Kwake.» alikubali Ibrāhīm na kusema, “Nimejisalimisha kwa Mola wa viumbe vyote, kwa kumtakasa, kumpwekesha, kumpenda na kurudi Kwake kwa kutubia.”

    [132] Na Ibrāhīm na Ya’qūb waliwahimiza watoto wao kusimama imara juu ya Uislamu wakiwaambia, “Enyi watoto wetu! Mwenyezi Mungu Amewachagulia Dini hii, nayo ni Uislamu, Msiiache muda wa uhai wenu, na msifikiwe na mauti isipokuwa na nyinyi muko kwenye Dini hii.”

    [133] Je mlikuwa muko, enyi Mayahudi, pindi kifo kilipomjia Ya’qūb, alipowakusanya watoto wake na kuwauliza, “Mtaabudu nini baada ya kufa kwangu?” Wakasema, “Tutamuabudu Mola wako na Mola wa baba zako: Ibrāhīm, Ismā'īl na Is’ḥāq Ambaye ni Mola Mmoja; na sisi ni wenye kufuata amri Yake na kumdhalilikia.”

    [134] Hao ni Ummah waliopita miongoni mwa wale waliowatangulia nyinyi. Wao wana amali zao, na nyinyi muna amali zenu. Wala hamtaulizwa kuhusu amali zao. Na wao hawataulizwa kuhusu amali zenu. Na kila mmoja atalipwa kulingana na aliyoyatenda. Mtu hateswi kwa kosa la yoyote mwengine. Na haimnufaishi mtu ila Imani yake na uchaji Mungu wake

    [135] Na Mayahudi walisema kuwaambia ummah wa Mtume Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukie yeye, “Ingieni kwenye dini ya Kiyahudi mtapata uongofu. Na Wanaswara waliwaambia kama hayo. Waambie, ewe Mtume, “Uongofu ni kuwa sote tufuate Mila ya Ibrāhīm ambaye alijiepusha na kila dini ya ubatilifu na kufuata Dini ya haki, na hakuwa ni miongoni mwa waliomshirikisha Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.”

    [136] Semeni, enyi Waumini, kuwaambia Mayahudi na Wanaswara, “Tumemuamini Mwenyezi Mungu, Aliye Mmoja, Anayeabudiwa kwa haki; na tumeiamini Qur’ani tuliyoteremshiwa ambayo Mwenyezi Mungu alimletea Wahyi Nabii wake na Mtume Wake Muhammad, rehema na amani zimshukie; na tumeziamini Kurasa alizoteremshiwa Ibrāhīm na watoto wake wawili: Ismāīl na Is’ḥāq, na alizoteremshiwa Ya’qūb na Asbāṭ - Manabii wanaotokana na watoto wa Ya’qūb waliokuwa katika makabila kumi na mbili ya Wana wa Isrāīl-; na tumeiamini Taurati aliyopewa Mūsā na Injil aliyopewa Īsā na Wahyi ulioteremshwa kwa Mitume wote. Hatumbagui yoyote miongoni mwao katika kuamini. Na sisi ni wenye kumdhalilikia Mwenyezi Mungu kwa kumtii na kumuabudu.”

    [137] Wakiyaamini Makafiri, miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara na wengineo, kama yale milyoyaamini nyinyi katika yale aliyokuja nayo Mtume, basi wameongoka kwenye haki; na wakikataa, basi wao wako kwenye upinzani mkubwa. Mwenyezi Mungu Atakutosheleza, ewe Mtume, shari lao na Atakupa ushindi juu yao. Yeye Ndiye Msikizi wa maneno yenu, Ndiye Mjuzi wa hali zenu

    [138] Jilazimisheni na Dini ya Mwenyezi Mungu ambayo Ameifanya inasibiane na maumbile yenu. Kwani hakuna maumbile mazuri kuliko yale ambayo Mwenyezi Mungu Amewaumbia watu. Jilazimisheni nayo na mseme, “Sisi ni wenye kuiandama, ni watiifu kwa Mola wetu katika kufuata kwetu mila ya Ibrāhīm.”

    [139] Sema, ewe Mtume, kuwaambia Watu wa Kitabu, “Je mnajadiliana na sisi juu ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtakasa, hali ya kuwa Yeye ni Mola wa viumbe wote, hahusiki na watu fulani tu bila ya wengine? Sisi tuna amali zetu, na nyinyi muna zenu. Na sisi tunamtakasia Mwenyezi Mungu ibada na utiifu; hatumshirikishi kitu chochote na hatumuabudu yoyote isipokuwa Yeye.”

    [140] Au je, Mnasema, kwa njia ya kujadili kuhusu Mwenyezi Mungu kwamba Ibrāhīm na Ismā'īl na Is’ḥāq na Ya’qūb na Asbāṭ - Manabii waliokuwa katika makabila kumi na mbili ya Wana wa Isrāīl wanaotokana na wana wa Ya’qūb - walikuwa katika dini ya Kiyahudi au ya Kinaswara? Huu ni urongo. Kwani hao walitumilizwa na kufa kabla ya Taurati na Injili. Waambie, ewe Mtume, “Kwani ni nyinyi mnaoijua zaidi dini yao au ni Mwenyezi Mungu Aliyetukuka?” Na Mwenyezi Mungu Ameshaeleza katika Qur’ani kwamba wao walikuwa Waislamu wenye msimamo uliolingana sawa. Na hakuna yoyote dhalimu zaidi kuliko nyinyi mnapouficha ushahidi uliothibiti kwenu kutoka kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kudai kinyume chake kwa kumzulia Mwenyezi Mungu urongo. Na Mwenyezi Mungu si Mwenye kughafilika na chochote katika vitendo vyenu. Yeye ni Mwenye kuvidhibiti na ni Mwenye kuwalipa kwavyo

    [141] Hao ni ummah waliopita miongoni mwa wale waliowatangulia nyinyi. Wao wana amali zao, na nyinyi muna amali zenu. Wala nyinyi hamtaulizwa kuhusu amali zao. Na wao hawataulizwa kuhusu amali zenu. Katika aya hii pana kukata njia ya kujifungamanisha na viumbe kwa kujiamabatisha nao, kutoghurika kwa kunasibiana na wao, kwa kuwa linalozingatiwa ni kumuamini Mwenyezi Mungu na kumuabudu Peke Yake na kuwafuata Mitume Wake, na kwamba mwenye kumkanusha Mtume yoyote katika wao, huwa amewakanusha Mitume wote

    [142] Watasema wajinga na madhaifu wa akili, miongoni mwa Mayahudi na mfano wao, wakiwa katika hali ya kufanya maskhara na kupinga, «Ni kitu gani kilichowageuza hawa Waislamu kuacha kibla chao ambacho walikuwa wakisali kukielekea mwanzo wa Uislamu?»(Nacho ni Baitul Maqdis). Waambie, ewe Mtume, «Upande wa Mashariki na wa Magharibi na katikati yake ni milki ya Mwenyezi Mungu. Hapana upande wowote, miongoni mwa pande zote, ulioko nje ya milki Yake. Yeye Anamuongoza Amtakaye, miongoni mwa waja Wake, kumuelekeza njia ya uongofu iliyo sawa.» Katika hayo, pana ujulishaji kwamba mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu, katika kufuata amri Zake, na kwa hivyo, popote tuelekezwapo tutaelekea

    [143] Na kama tulivyowaongoza, enyi Waislamu, kwenye njia sahihi katika Dini, tumewafanya kuwa ni ummah bora ulio muadilifu, ili mue mashahidi juu ya ummah waliopita, kesho Akhera, kwamba Mitume wao waliwafikishia jumbe za Mola wao, na ili Mtume, kesho Akhera, awe vilevile ni shahidi juu yenu, kwamba yeye aliwafikishia ujumbe wa Mola wake. Wala hatukukifanya, ewe Mtume, kile kibla cha Baitul Maqdis ulichokuwa ukikielekea, kisha tukakugeuza tukakuelekeza Alkaba (iliyopo Makkah) isipokuwa ni yapate kuonekana yale tuliyoyajua hapo kale, ujuzi unaofungamana na thawabu na adhabu, ili tumtenganishe yule ambaye atakufuata na kukutii na kuelekea pamoja nawe pale utakapoelekea na yule aliye dhaifu wa imani, awe ni mwenye kubadilika na kuritadi kwa kuacha Dini yake kwa shaka yake na unafiki wake. Hali hii ya kugeuka Muislamu katika Swala yake, kuacha kuelekea Baitul Maqdis na kuelekea Alkaba ni ngumu na nzito, isipokuwa kwa wale walioongozwa na Mwenyezi Mungu na kupewa neema ya Imani na uchajimungu. Na wala hakuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupoteza imani yenu Kwake na kumfuata kwenu Mtume Wake kwa kuzibatilisha Swala zenu mlipokuwa mnaelekea kibla cha zamani. Hakika Yeye Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na upungufu wowote na Aliyetukuka, kwa watu ni Mpole na Mwenye huruma

    [144] Hakika Tunauona mzunguko wa uso wako upande wa mbinguni mara baada ya mara, huku ukingojea kuteremka Wahyi juu yako kuhusiana na Kibla. Basi hakika Tutakuepusha na Baitul Maqdis Tukuelekeze kwenye kibla unachokipenda na unachokiridhia, nacho ni upande wa Msikiti wa Ḥarām ulioko Makkah. Basi, elekeza uso wako huko. Na popote mtakapokuwa, enyi Waislamu, na mkataka kuswali, elekeeni upande wa Msikiti wa Haram. Na hakika wale ambao Mwenyezi Mungu amewapa elimu ya Kitabu miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara wanajua kwamba kugeuzwa kwako kuelekezwa Alkaba ndio haki iliyothibiti katika vitabu vyao. Na wala Mwenyezi Mungu hakuwa ni Mwenye kughafilika juu ya yale wayafanyayo hawa wapinzani wenye shaka, na Atawalipa kwayo

    [145] Na lau utawaletea wale waliopewa Taurati na Injili aina yoyote ya hoja na dalili kwamba kuelekea kwako Alkaba katika swala ndio haki kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hawangalikifuata kibla chako, kwa inadi na kiburi. Na wala wewe si mwenye kukifuata kibla chao mara nyingine. Wala baadhi yao si wenye kufuata kibla cha baadhi yao. Na lau utafuata matamanio ya nafsi zao kuhusu kibla na mengineyo, baada ya ujuzi uliyoupata kuwa wewe uko kwenye haki na wao wako kwenye batili, wewe wakati huo utakuwa ni miongoni mwa waliozidhulumu nafsi zao. Haya ni maelezo kuambiwa ummah wote, na ni kitisho na kemeo kwa kila afuataye matamanio ya wanaoenda kinyume na Sheria ya Kiislamu

    [146] Wale Tuliowapa Taurati na Injili miongoni mwa wanavyuoni wa Kiyahudi na wajuzi wa Kinaswara wanajua ya kwamba Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu, kwa sifa zake zilizotajwa katika vitabu vyao, kama vile wanavyowajuwa wana wao. Na hakika kuna kundi kati yao wanaificha haki na wao wanaujuwa ukweli wake na kuwa sifa zake zimethibiti

    [147] Yale yaliyoteremshwa kwako, ewe Nabii, ndiyo haki kutoka kwa Mola wako. Kwa hivyo, usiwe ni kati ya wale wanaoyatilia shaka. Maneno haya, ingawa anambiwa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, yanaelekezwa kwa ummah wote

    [148] Kila ummah, miongoni mwa ummah wa kila aina, una kibla chake anachokielekea kila mmoja katika wao kwenye swala yake. Basi kimbilieni, enyi Waumini, hali ya kushindana katika kutenda vitendo vyema ambavyo Ameviwajibisha kwenu Mwenyezi Mungu katika Dini ya Kiislamu. Mwenyezi Mungu Atawakusanya nyote Siku ya Kiyama kutoka popote mtakapokuwa. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu

    [149] Na mahali popote ulipotoka, ewe Nabii, ukiwa msafiri au ukitaka kuswali, elekeza uso wako upande wa Msikiti wa Haram. Kuelekea kwako huko ndio haki iliyothibiti kutoka kwa Mola wako. Na Mwenyezi Mungu hakuwa ni Mwenye kughafilika juu ya yale mnayoyatenda na Atawalipa kwa hayo

    [150] Na mahali popote utokapo, ewe Nabii, elekea Msikiti wa Haram. Na popote mnapokuwa, enyi Waislamu, katika nchi yoyote miongoni mwa nchi za ardhi, elekezeni nyuso zenu upande wa Msikiti wa Haram, ili watu wapinzani wasiwe na hoja yoyote kwenu kwa njia ya ugomvi na mjadala, baada ya kuelekea huko, isipokuwa wale madhalimu na wenye ukaidi kati yao. Hao watabakia kwenye mjadala wao. Basi, msiwaogope wao, niogopeni Mimi kwa kufuata amri Yangu na kujiepusha na katazo Langu na ili nikamilishe neema Zangu kwenu kuwachagulia sheria zilizokamilika zaidi, na ili mpate kuongoka kufuata haki na usawa

    [151] Kama Tulivyowaneemesha kwa kuelekea Alkaba, Tumewaletea mjumbe anayetokana na nyinyi, anawasomea aya zibainishazo haki kuitenga na batili, kuwasafisha na uchafu wa ushirikina na tabia mbaya, kuwafundisha Kitabu, Sunna na hukumu za Sheria na kuwafundisha habari za Mitume na visa vya ummah waliopita, mambo ambayo mlikuwa hamyajui

    [152] Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Amewaamrisha Waumini wamtaje Yeye na Akatoa ahadi kwa hilo malipo bora zaidi, nayo ni kumsifu yule anayemtaja Yeye mbele ya viumbe walioko juu. Pia Amewaamrisha Waumini wamshukuru Yeye Peke Yake kwa maneno na vitendo na wasizikanushe neema Zake juu yao

    [153] Enyi Waumini, takeni msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika mambo yenu yote, kwa kusubiri juu ya mikasa na misiba, na kuacha maasia na madhambi na kusubiri juu ya kufanya mambo ya utiifu na yale yanayomkurubisha mtu kwa Mola wake, na kwa Swala ambayo kwayo nafsi inapata utulivu na ambayo inakataza machafu na maovu. Hakika Mwenyezi Mungu Yuko pamoja na wenye kusubiri kwa msaada Wake, taufiki Yake na muelekezo Wake. Katika hii Aya kuna kuthibitisha kuwa Mwenyezi Mungu Yuko pamoja na Waumini kimahsusi, upamoja unaolazimiana na yaliyotangulia kutajwa. Ama kuwa Mwenyezi Mungu yuko pamoja na viumbe kijumla kunakolazimiana na elimu Yake na kuwa ujuzi Wake umezunguka kila kitu, basi upamoja huo ni wa viumbe vyote

    [154] Na wala msiseme, enyi Waumini, kuhusu wale wanaouawa hali ya kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, kuwa wao wamekufa. Bali wao wako hai, uhai maalumu unaowahusu wao, ndani ya Makaburi yao. Wala hakuna anayejua yako vipi maisha hayo isipokuwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, lakini nyinyi hamuyahisi maisha hayo. Katika haya, pana ushahidi kwamba kuna neema za kaburini

    [155] Tutawapa, tena tutawapa, mtihani wa kitu hafifu cha hali ya kuogopa, njaa, upungufu wa mali, iwe ni uzito kuyapata au yaondoke, upungufu wa watu: kwa kufa au kufa-shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu, na kwa upungufu wa matunda ya mitende na mizabibu na nafaka: kwa kupungua mazao yake au kuharibika kwake.Wape, ewe Nabii, habari njema, wale wenye subira juu ya haya na mfano wake, kwa yale yatakayowafurahisha na kuwapendeza ya mwisho mwema duniani na Akhera

    [156] Miongoni mwa sifa za hawa wenye kusubiri ni kwamba wao wanapofikwa na kitu wanachokichukia husema, «Sisi ni waja waliomilikiwa na Mwenyezi Mungu, tunaoendeshwa kwa amri Yake na mapitisho Yake. Anafanya kwetu Alitakalo. Na sisi Kwake, Peke Yake, ni wenye kurudi kwa kufa, kisha kwa kufufuliwa ili kuhesabiwa na kulipwa

    [157] Hao wenye kusubiri wana utajo mwema kutoka kwa Mola wao na rehema kubwa kutoka Kwake, Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu, na hao ndio walioongoka njia ya uongofu

    [158] Hakika Swafa na Marwa, nayo ni majabali mawili madogo karibu ya Alkaba upande wa Mashariki, ni miongoni mwa alama za dini ya Mwenyezi Mungu zilizo wazi ambazo Mwenyezi Mungu Amezifanya ni sehemu za ibada kwa waja Wake kusai baina yake. Hivyo basi, yoyote mwenye kuikusudia Alkaba kwa kuhiji au kufanya Umra, si dhambi kwake kusai baina ya hayo majabali mawili, bali ni wajibu kwake kufanya hivyo. Na yule mwenye kufanya mambo ya kutii amri, kwa hiyari yake, hali ya kumtakasia Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushukuru, Analipa juu ya kichache kwa kingi, ni Mwenye kuzijua amali za waja Wake: Hazipotezi wala Hampunji yoyote chochote hata kama ni uzito wa chungu mdogo

    [159] Hakika wale ambao wanazificha aya zilizo waziwazi, zijulishazo utume wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na yale aliyokuja nayo, nao ni wanavyuoni wa Kiyahudi na wajuzi wa Kinaswara na wengineo, miongoni mwa wafichao yalyoteremshwa na Mwenyezi Mungu, baada ya sisi kuyadhihirisha kwa watu katika Taurati na Injili, hao Mwenyezi Mungu Atawafukuza kutoka kwenye rehema Yake, na viumbe wote watawaapiza laana

    [160] Isipokuwa wale waliorudi hali ya kutubia makosa yao, wakarekebisha waliyoyaharibu na wakayabainisha waliyoyaficha. Hao nitazikubali toba zao na nitawalipa kwa kuwasamehe. Na mimi ni Mwenye kukubali mno toba ya mwenye kutubia kati ya waja Wangu na ni Mwenye huruma kwao kwa kuwapa taufiki ya kutubia na kukubali toba kutoka kwao

    [161] Hakika wale waliokanusha imani na wakaficha haki na wakaendelea hivyo mpaka kufa kwao, juu yao kuna laana ya Mwenyezi Mungu na Malaika na watu wote kwa kuwatoa kwenye rehema Yake

    [162] Watadumu kwenye laana na Moto. Hawatapunguziwa adhabu, wala hawatapumzishwa na kungojewa kwa udhuru wowote watakaoutoa

    [163] Na Mola wenu, enyi watu, ni Mola Mmoja Aliyepwekeka katika dhati Yake, majina Yake, sifa Zake na vitendo Vyake na uja wa viumbe Vyake Kwake. Hapana apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye, Mwingi wa rehema, Mwenye kusifika kwa sifa ya rehema katika dhati Yake, vitendo Vyake kwa waja Wake wote, na Mwenye kuwarehemu waumini

    [164] Hakika, katika kuumba mbingu kwa kuzifanya ziinuke juu na ziwe kunjufu, na ardhi kwa majabali yake, mabonde yake na bahari zake, na katika kutafautiana usiku na mchana kwa urefu na ufupi, giza na muangaza, na kuandamana kwao kwa kila mmoja kukaa pahali pa mwingine, na katika majahazi yanayopita baharini, yanayobeba vitu vinavyowanufaisha watu, na katika maji ya mvua Aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, Akaipa uhai ardhi kwa maji hayo ikawa rangi ya kijani yenye kupendeza baada ya kuwa kavu isiyokuwa na mimea, na vile Alivyoeneza Mwenyezi Mungu humo kila kitambaacho juu ya ardhi hiyo, na katika yale Aliyowaneemesha kwayo ya kuugeuza upepo na kuuelekeza, na katika mawingu yanayopelekwa baina ya mbingu na ardhi, hakika, katika dalili zote hizo zilizopita, pana alama za upweke wa Mwenyezi Mungu na ukubwa wa neema Zake kwa watu wanaoelewa sehemu za hoja na wanaozifahamu dalili za Mwenyezi Mungu Aliyetukuka juu ya upweke Wake na kustahiki Kwake Peke Yake kuabudiwa

    [165] Pamoja na hizi hoja za kukata, kinatoka kikundi cha watu wakichukua, badala ya Mwenyezi Mungu, masanamu na wategemewa wakiwafanya ni kama Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kuwapa mapenzi, heshima na twaa, Mambo yasiyostahiki kufanyiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu Peke Yake. Na Waumini, mapenzi yao kwa Mwenyezi Mungu ni makubwa zaidi kuliko mapenzi ya hawa makafiri kwa Mwenyezi Mungu na kwa waungu wao. Sababu Waumini wamemtakasia Mwenyezi Mungu mapenzi yao yote. Na hao makafiri wamemshirikisha Mwenyezi Mungu katika mapenzi. Na lau wangalijua wale waliojidhulumu nafsi zao kwa kumshirikisha Mwenyezi Mungu katika maisha ya kidunia, pindi watakapoiona adhabu ya Akhera, kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye Peke Yake Mwenye nguvu zote na kwamba Mwenyezi Mungu ni mkali wa adhabu, hawangaliwafanya wasiokuwa Mwenyezi Mungu kuwa ni waungu wakawa wanawaabudu, badala ya Mwenyezi Mungu, na kujikurubisha nao Kwake

    [166] Watakapoiyona adhabu ya Akhera, watajitenga wale viongozi waliofuatwa kujiepusha na wale waliowafuata katika ushirikina na zitawakatikia wao aina zote za mawasiliano waliyojifungamanisha nayo duniani: ya ujamaa, ufuasi, dini na mengineyo yasiyokuwa hayo

    [167] Na wale wafuasi watasema, «Twatamani tuwe na marejeo ya duniani, ili tutangaze kujitenga kwetu na hawa viongozi kama walivyotangaza kujitenga kwao na sisi.» Na kama Alivyowaonesha Mwenyezi Mungu ukali wa adhabu Yake, Siku ya Kiyama, Atawaonesha vitendo vyao viovu kuwa ni majuto kwao. Na hawatakuwa ni wenye kutoka Motoni kabisa

    [168] Enyi watu, kuleni katika riziki ya Mwenyezi Mungu, iliyoko kwenye ardhi, ile ambayo Amewahalalishia nyinyi, nayo ni iliyo tohara isiyokuwa najisi, inayonufaisha isiyodhuru wala msifuate njia za Shetani katika kuhalalisha, kuharamisha, uzushi na maasia. Hakika Yeye ni adui yenu mwenye uadui uliyo wazi

    [169] Hakika Shetani anawaamuru mfanye kila sampuli ya dhambi baya linalowatia uovuni, na kila maasia yenye upeo wa uchafu, na mumzulie Mwenyezi Mungu urongo, kama kuharamisha halali na mangineyo, pasi na ujuzi wowote

    [170] Na pindi Waumini wasemapo, wakiwanasihi viongozi wa upotofu, «Fuateni Aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu miongoni mwa Qur’ani na uongofu,» wao huendelea kuwa wakakamavu katika kuwaigiza wakale wao washirikina, huku wakisema, «Hatufuati dini yenu, bali tunayafuata yale tuliyowakuta wazazi wetu wakiyafanya.» Wanawafuata baba zao hata kama walikuwa hawaelewi chochote kutoka kwa Mwenyezi Mungu wala hawana muelekeo wowote

    [171] Na sifa za waliokufuru na wale walinganizi wao katika uongofu na imani ni kama sifa ya mchunga anayewapigia kelele wanyama na kuwakaripia, hali wao hawaelewi maana ya maneno yake isipokuwa wanasikia mwito na mlio wa sauti tu. Makafiri hao ni viziwi wameziba masikizi yao wasisikie haki, ni mabubu wamezifunga ndimi zao wasiitamke haki, ni vipofu macho yao hayazioni hoja za haki zilizo wazi. Kwa hivyo, wao hawatumii akili zao kwa mambo yenye kuwafaa

    [172] Enyi Waumini, kuleni katika vyakula mnavyovipenda vilivyo halali ambavyo tumewaruzuku, wala msiwe kama makafiri ambao wanaviharamisha vizuri na kuvihalalisha viovu na mumshukurie Mwenyezi Mungu neema Zake kubwa kwenu kwa nyoyo zenu, ndimi zenu na viungo vyenu, iwapo kwa kweli nyinyi mnafuata amri Yake, ni wenye kusikia na kumtii Yeye, mnamuabudu Yeye Peke Yake Asiyekuwa na mshirika

    [173] Hakika Mwenyezi Mungu Amewaharamishia nyinyi kinachowadhuru, kama mfu ambaye hakuchinjwa kwa njia ya kisheria, na damu inayotiririka, na nyama ya nguruwe, na vichinjwa ambavyo vilikusudiwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Na katika wema wa Mwenyezi Mungu na usahilishaji Wake kwenu ni kwamba Amewahalalishia nyinyi kuvila vitu hivi vilivyoharamishwa wakati wa dharura. Hivyo basi, yoyote ambaye dharura ilimpelekea kula kitu katika hivyo, pasi na kuwa ni mwenye kudhulumu katika kula kwake kwa kupitisha kipimo cha haja yake, wala kuikiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu katika yale aliyohalalishiwa, basi huyo hana dhambi kwa hilo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe waja Wake, ni Mwenye huruma kwao

    [174] Hakika wale wafichao yale Aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu katika vitabu vyake miongoni mwa sifa za Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na mengineyo ya haki na wakawa na pupa la kuchukua badali ndogo ya pambo la maisha ya duniani kama malipo ya kuficha hayo. Hawa hawakili kile wakilacho kwa kuficha haki isipokuwa moto wa Jahanamu utakaokuwa ukiwaka kwa ukali katika matumbo yao. Wala Mwenyezi Mungu Hatasema nao Siku ya Kiyama kwa hasira Zake na machukivu Yake juu yao, wala Hatawatakasa na uchafu wa madhambi yao na ukafiri wao, na itawapata adhabu iumizayo

    [175] Hao wanaosifika na sifa hizi wamechagua upotevu wakaacha uongofu, na wakachagua adhabu ya Mwenyezi Mungu wakaacha msamaha wake. Ni ujasiri ulioje wao wa kuchagua Moto kwa kufanya vitendo vya watu wa Motoni! Anastaajabu Mwenyezi Mungu kwa kujitokeza kwao kulifanya hilo. Basi oneni ajabu, enyi watu, juu ya ujasiri wao na uvumilivu wao kwenye Moto na kukaa kwao humo. Maneno haya yametumika kwa njia ya kuwatweza na kuwachezea

    [176] Adhabu hiyo ambayo wamestahili iwapate, ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu Ameteremsha Vitabu Vyake, kwa Mitume Wake, vikiwa ni vyenye kukusanya haki iliyo wazi, wakaikanusha haki hiyo. Na kwa hakika, wale waliohitalifiana katika Kitabu, wakaamini baadhi yake na kukanusha baadhi yake, wako katika ugonvi na mfarakano ulio mbali na uongofu na usawa

    [177] Hapana kheri, mbele ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, kuelekea kwenye Swala upande wa mashariki na magharibi, iwapo hilo halitokamani na amri ya Mwenyezi Mungu na sheria Yake. Hakika kheri yote iko katika imani ya aliyemuamini Mwenyezi Mungu na akamkubali kuwa Ndiye muabudiwa, Peke Yake, Hana mshirika Wake, na akaiamini Siku ya kufufuliwa na Malipo, na akawaamini Malaika wote na vitabu vyote vilivyoteremshwa, na Mitume wote bila kubagua, na akatoa mali yake kwa hiyari yake, pamoja na kuwa anayapenda sana, kuwapa jamaa zake na mayatima wenye uhitaji waliofiliwa na wazazi wao hali wao wako chini ya umri wa kubaleghe, na akawapa masikini ambao ufukara umewaelemea, na wasafiri wanaohitaji walio mbali na watu wao na mali yao, na waombaji ambao imekuwa ni dharura kwao kuomba kwa uhitaji wao mkubwa, na akatoa mali yake katika kuwakomboa watumwa na mateka, na akasimamisha Swala na akatoa zaka za faradhi, na wale wenye kutekeleza ahadi, na mwenye kusubiri katika hali ya ufukara wake na ugonjwa wake na katika vita vikali. Hao wenye kusifika kwa sifa hizo, ndio waliokuwa wakweli katika imani zao, na wao ndio waliojikinga mateso ya Mwenyezi Mungu wakajiepusha na vitendo vya kumuasi

    [178] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafanya vitendo vinavyoambatana na Sheria ya Mwenyezi Mungu Alioifanya faradhi kwenu kwamba mlipize kisasi kwa muuaji aliyeua kwa kukusudia, kwa sharti ya kufanya usawa na kufananisha malipo: auawe muungwana kwa kumuua mfano wake, na mtumwa kwa mfano wake, na mwanamke kwa mfano wake. Na yule atakayesamehewa na msimamizi wa aliyeuawa kwa kumuondolea kisasi na kutosheka kwa kuchukua dia, nayo ni kiwango cha mali maalumu akitoacho mhalifu kikiwa ni badali ya kusamehewa, ni juu ya pande mbili zijilazimishe tabia njema: yule msimamizi adai diya yake bila kutumia nguvu, na yule muuaji ampatiye haki yake kwa wema bila kuchelewesha wala kupunguza. Msamaha huo, pamoja na kupokea hiyo dia, ni masahilisho ya Mola wenu na ni huruma kwenu kwa ule usahali na kujinufaisha. Hivyo basi,mwenye kumuua muuaji baada ya msamaha na kupokea dia, atapata adhabu kali ya kuuawa kwa njia ya kisasi duniani au kutiwa Motoni Akhera

    [179] Na hakika katika kuwekwa sheria ya kisasi na utekelezaji wake kwa kutarajia kufikia uchaji Mwenyezi Mungu na kumuogopa kwa kumtii daima, kuna maisha ya amani kwenu, enyi wenye akili timamu

    [180] Mwenyezi Mungu Amewafaradhia nyinyi, iwapo mmoja wenu zimedhihiri kwake alama za mauti na vitangulizi vyake, akiwa ameacha mali, atoe wasia wa sehemu ya mali yake iyende kwa wazazi wake wawili na jamaa zake alio karibu naye, pamoja na kuchunga uadilifu, asimuache masikini na akatoa wasia wake kwa tajiri, wala wasia wake usizidi thuluthi ya mali. Hiyo ni haki thabiti ambayo wenye kumcha Mwenyezi Mungu waitenda. Hii ilikuwa kabla ya kuteremka zile aya ambazo Mwenyezi Mungu aliweka fungu la kila mrith

    [181] Yule atakaye kuubadilisha wasia wa maiti baada ya kuusikia kutoka kwake kabla hajafariki, dhambi litakuwa ni la yule aliyebadilisha na kugeuza. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuusikia wasia wenu na maneno yenu, ni Mjuzi zaidi wa yale yanayofichwa na nyoyo zenu kuhusu kuelekea upande wa haki na uadilifu au ujeuri na udhalimu, na Atawalipa kwa hilo

    [182] Basi yoyote atakayejua kuwa mwenye kuusia amepinduka, kwa kuiacha haki katika wasia wake kwa njia ya kukosea au kukusudia, akamnasihi mtoaji wasia, wakati wa kutoa wasia, afanye uadilifu, na iwapo hilo halikuwa akaleta upatanishi kati ya pande zinazohusika kwa kugeuza wasia ili ulingane na Sheria, basi atakuwa hana dhambi katika kupatanisha huku. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kuwasamehe waja wake, ni Mwenye huruma kwao

    [183] Enyi ambao mumemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mukaifuata Sheria Yake kivitendo, Mwenyezi Mungu Amewafaradhia kufunga, kama Alivyowafaradhia uma waliokuweko kabla yenu, ili mupate kumcha Mola wenu na kuweka kinga kati yenu na maasia, kwa kumtii na kumuabudu Peke Yake

    [184] Amewafaradhia Mwenyezi Mungu kufunga siku zinazojulikana idadi yake, nazo ni siku za mwezi wa Ramadhani. Basi yule kati yenu atakuwa mgonjwa, ikawa ni uzito kwake kufunga, au akawa ni msafiri, basi aweza kufungua. Na itamlazimu kufunga idadi ya siku nyengine zinazolingana na idadi ya siku alizokula. Na ni juu ya wale ambao kwao ni vigumu kufunga na ikawa inawaelemea maelemeo yasiyochukulika, kama mzee mkongwe na mngonjwa asiyetarajiwa kupoa, watoe fidiya ya kila siku ambayo watafungua, nayo ni kulisha masikini. Na yule atakayezidisha katika kiwango cha fidiya, kwa hiyari yake, basi hilo ni bora kwake. Na kufunga kwenu ni bora kwenu, pamoja na kuhimili shida, kuliko kutoa fidiya, iwapo mnazijua fadhila kubwa zipatikanazo kwenye kufunga mbele ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka

    [185] Mwezi wa Ramadhani ambao Ameanza Mwenyezi Mungu kuteremsha Qur’ani katika usiku wa cheo na utukufu, laylatul qadr, ilii kuwaongoza watu kwenye haki. Ndani yake Amezifungua wazi dalili za uongofu wa Mwenyezi Mungu na upambanuzi baina ya haki na batili. Kwa hivyo, mtu atakayeufikia mwezi huo, akawa ni mzima na mkazi wa mjini, basi na aufunge mchana wake. Mgojwa na msafiri wanaruhusiwa kufungua, kisha walipe idadi ya siku walizofungua. Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Anawatakia usahali na wepesi katika Sheria Zake, wala Hawatakii uzito na mashaka, na ili mupate kukamilisha idadi ya kufunga mwezi mzima na mumalize kufunga kwa kwa kumtukuza Mwenyezi Mungu katika Idi ya Mfungo na mpate kumshukuru juu ya zile neema Alizowaneemesha nazo za uongofu, taufiki na usahali

    [186] Na watakapo kukuuliza, ewe Nabii, waja Wangu kuhusu Mimi, waambie, «Mimi Niko karibu na wao, Nasikia maombi ya muombaji yoyote anaponiomba.Basi, ni wanitii Mimi katika Niliowaamrisha nayo na Niliowakaza nayo na waniamini Mimi, wapate kuongokewa kwenye maslahi yao ya dini yao na dunia yao. Katika ayah ii pana utoaji habari kutoka Kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu, kuhusu ukaribu Wake kwa waja Wake, ukaribu unaolingana na utukufu Wake

    [187] Amewahalalishia Mwenyezi Mungu masiku ya mwezi wa Ramadhani kuwaingilia wake zenu. Wao ni sitara na hifadhi kwenu, na nyinyi ni sitara na hifadhi kwao. Anajua Mwenyezi Mungu kwamba nyinyi mulikuwa mkizidhiki nafsi zenu kwa kuenda kinyume na yale ambayo Mwenyezi Mungu Aliyaharimisha kwenu ya kuwaingilia wanawake baada ya Isha katika masiku ya kufunga- hilo lilikuwa mwanzo wa Uislamu-, Mwenyezi Mungu Alikubali toba yenu na Akawatolea nafasi kwa hili jambo. Basi sasa waingilieni na mtafute kile Alichowakadiria Mwenyezi Mungu, miongoni mwa watoto, na kuleni na kunyweni mpaka ujitokeze kwenu mwangaza wa asubuhi utengane na weusi wa usiku kwa kujitokeza alfajiri ya kweli. Kisha kamilisheni kufunga kwa kujizuia na venye kutangua mpaka kuingia usiku kwa kutwa jua. Wala musiwaingilie wake zenu, au kufanya kitu cha kusababisha kuwaingilia, iwapo muko kwenye itikafu misikitini, sababu hilo laharibu itikafu- nako ni kukaa msikitini kwa muda maalumu kwa nia ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka-. Hukumu hizo, ambazo mwenyezi Mungu Amezifanya ni Sheria kwenu, ndiyo mipaka Yake itenganishayo kati ya halali na haramu. Basi msiikaribie, ili msije mkaingia katika haramu. Kwa mfano wa ubainifu huu ulio wazi, Mwenyezi Mungu Anazifafanua aya Zake na hukumu Zake kwa watu, ili wamche na kumuogopa

    [188] Na wasile baadhi yenu mali ya wengine kwa njia ya batili, kama kuapa yamini la urongo, kunyang’anya, kuiba, kuhonga, kula riba na mfano wa hayo.Wala msipeleke kwa mahakimu hoja potofu ili mpate kula kwa njia ya utesi mali ya kikundi cha watu wengine kwa njia ya batili, hali ya kuwa nyinyi mnajua uharamu wa hilo juu yenu

    [189] Wanakuuliza watu wako, ewe Nabii, kuhusu miezi michanga na kubadilika hali zake. Waambie, Mwenyezi Mungu Ameifanya miezi kuwa ni alama za watu kujua nyakati za ibada zao zilizowekewa wakati, mfano wa Saumu na Hija, na nyakati za kuamiliana kwao. Kheri haiko katika mambo mliyoyazowea wakati wa ujahilia na mwanzo wa Uislamu ya kuingia majumbani kupitia kwa nyuma, wakati mnapotia nia ya Hija au ya Umra, mkidhani kwamba huko ndiko kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Lakini kheri ni kile kitendo cha mwenye kumcha Mwenyezi Mungu na akajiepusha na maasia. Na ingieni majumbani kupitia kwenye milango yake wakati mnapohirimia Hija au Umra. Na muogopeni Mwenyezi Mungu katika mambo yenu yote ili mupate kufaulu kuyapata yote mnayoyapenda ya kheri ya dunia na ya Akhera

    [190] Na piganeni, enyi Waumini, ili kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu, na wale wanaopigana na nyinyi, wala msifanye yaliyokatazwa ya kukatakata viungo, kufanya hiyana (ya kuchukua kitu katika ngawira kabla ya kugawanywa), kumuua asiyefaa kuuawa miongoni mwa wanawake, watoto, wazee na wanaoingia kwenye hukumu yao. Hakika Mwenyezi Mungu Hawapendi wale wanaokiuka mipaka Yake na kuyahalalisha yalioharamishwa na Mewnyezi Mungu na Mtume Wake

    [191] Na waueni wale wanaopigana na nyinyi miongoni mwa Washirikina popote mtakapowakuta, na muwtoe kutoka pahali walipowatoa, napo ni Maka. Na fitina, ambayo ni ukafiri na ushirikina na kuwazuia watu na Uislamu, ni mbaya zaidi kuliko nyinyi kuwaua wao. Wala msiwaanzie vita katika Msikiti wa Haramu, kwa kuheshimu sehemu zake tukufu, mpaka wao wawaanzie vita humo. Na iwapo watawapiga vita katika Msikiti wa Haramu, basi waueni hapo. Mfano wa malipo hayo ya kutisha yatakuwa ndiyo malipo ya Makafiri

    [192] Na iwapo watayaacha yale walionayo ya ukafiri na ya kuwapigeni vita kwenye Msikiti wa Haramu na wakaingia katika Imani, kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwasamehe waja Wake, ni Mwenye huruma na wao

    [193] Na endeleeni, enyi Waumini, kuwapiga vita washirikina wafanyao uadui mpaka kusiweko tena kuwafitini Waislamu na dini yao wala kumshirikisha Mwenyezi Mungu, na ibakie dini kuwa ni ya Mwenyezi Mungu Peke Yake, hali ya kuwa safi, haabudiwi yoyote pamoja na Yeye. Na iwapo watakomeka na ukafiri na vita, basi komekeni nao.Kwani mateso hayawi ela kwa wale wanaoendelea na ukafiri wao na uadui wao

    [194] Kuwapiga kwenu vita, enyi Waumini, hao washirikina, katika mwezi ambao Mwenyezi Mungu Ameharamisha vita, ni malipo ya wao kuwapiga nyinyi vita mwezi mtukufu.Na yule anayekeuka yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu ya pahali na zama, atapewa mateso yanayofanana na kitendo chake na yanayotokana na jinsi ya kosa alilolifanya. Basi atakayewafanyia uadui kwa vita au chinginecho, wapeni adhabu ifananayo na uovu wao, wala pasiwe na dhiki kwenu kuhusu hilo. kwa sababu wao ndio wenye kuanza uadui. Na muogopeni Mwenyezi Mungu na msipitishe kipimo cha kufanana kuadhibu. Na juenu kuwa Mwenyezi Mungu Yuko pamoja na wale wamchao na wanaomtii kwa kutekeleza Aliyoyafanya faradhi na kuyaepuka Aliyoyafanya haramu

    [195] Na endeleeni, enyi Waumini, kutoa mali kwa kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kupigana jihadi katika njia yake. Wala msiziingize nafsi zenu kwenye maangamivu kwa kuacha jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na kuacha kutoa katika njia Yake. Na fanyeni wema katika kutoa na kutii, na mzifanye amali zenu zote ni zenye kutakasika kwa kukusudiwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. Kwa hakika Mwenyezi Mungu Anawapenda watu wenye kutakasa nia na kufanya wema

    [196] Na tekelezeni Hija na Umra ziwe zimekamilika, zimetakasika na kukusudiwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.Na iwapo kitwazuia, kwenda kuzikamilisha baada ya kuzihirimia, kizuizi chochote, kama adui na ugonjwa, lililo wajibu kwenu ni kuchinja kitakacho kuwa chepesi kwenu miongoni mwa ngamia, ng’ombe, mbuzi au kondoo, hali ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, ili mpate kutoka katika ihramu zenu kwa kunyoa nywele za kichwa au kuzipunguza.Wala msinyoe vichwa vyenu, mkiwa mumezuiwa, mpaka mwenye kuzuiwa amchinje mnyama wake pale pahali alipozuiwa kisha ajitoe kwenye ihramu yake kama alivyochinja Mtume(S.A.W) hapo Hudaibiya kisha akanyoa kichwa chake. Na asiyekuw yule aliyezuiwa, hatachinja mnyama wake mpaka afike ndani ya eneo la tukufu la Maka, ambapo ndipo pahali pake, sku ya idi ambayo ni siku ya kumi na siku zifuatazo za Tashrīq. Na ambaye kati yenu atakuwa mngonjwa au ana udhia katika kichwa chake akawa anahitajia kunyoa, naye yuko kwenye ihramu, basi atanyoa na ni juu yake atoe fidya: afunge siku tatu au awape sadaka masikini sita, kila mmoja nusu pishi ya chakula, au achinje mbudi au kondoo awape mafukara wa eneo tukufu la Maka. Na pindi mtakapo kuwa kwenye hali ya amani na afya, basi atakaye kujistarehesha kwa kufanya Umra ndani ya Hija, nako ni kuihalalishia mambo alioharamhshiwa kwa sababu ya ihramu baada ya kumaliza Umra yake, inampasa kuchinja kiwezekanacho katika wanyama. Na yule aliyekosa mnyama wa kuchinja, itamlazimu afunge siku tatu ndani ya miezi ya Hija na siku saba mtakapo kumaliza amali za Hija na mkarudi kwenu; hizo ni siku kumi kamili, hapana budi kuzifunga.Mnyama huyo wa kuchinjwa, na yale yaliyopasa juu yake ya kufunga, ni kwa yule ambaye watu wake si wakazi wa ardhi tukufu ya Haram. Na muogopeni Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na mujilazimishe kuzitekeleza amri Zake na kujiepusha na Makatazo Yake, na mjue kwamba Mwenyezi Mungu ni mkali wa mateso kwa yule aendaye kinyume na amri Zake na na kufanya Aliyoyakemea

    [197] Wakati wa Hija ni miezi ijulikanayo, nayo ni Mfungomosi, Mfungopili na siku kumi za Mfungotatu.Basi mwenye kujilazimisha nafsi yake kuhiji ndani ya miezi hiyo, kwa kutia nia ya kuhirimia Hija, ni haramu kwake kuundama na vitangulizi vyake vya kimaneno na kivitendo. Pia ni haramu kwake kutoka kwenye twaa ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kwa kutenda maasia, kubishana, katika Hija, kuletako hasira na chuki. Na wema wowote mnaoufanya, Mwenyezi Mungu Anaujua, na Atamlipa kila mtu kwa amali yake. Na jichukulieni akiba ya chakula na kinwaji kwa safari ya Hija, na akiba ya amali njema kwa nyumba ya Akhera. Hakika akiba iliyo bora zaidi ni kumuogopa Mwenyezi Mungu. Basi niogopeni, enyi wenye akili timamu

    [198] Hapana ubaya wowote kwenu kutafuta riziki itokayo kwa Mola wenu, kwa kupata faida ya biashara, ndani ya siku za Hija.Basi mtakapo kuondoka, baada ya kutwa jua, mkirejea kutoka Arafa- napo ni pahali ambapo Mahujaji husimama siku ya tisa ya Mfungotatu-, mtajeni Mwenyezi Mungu kwa kuleta Tasbihi, Talbiyah(Labbaika Allahumma labbaika..) na dua katika sehemu tukufu ya Al- Mashcar al-Harām: Muzdalifa. Na mumtaje Mwenyezi Mungu kwa njia ya kisawa Aliyowaongoza nayo. Na mlikuwa kabla yauongofu huo mko katika upotevu, hamuijui haki

    [199] Na iwe kuondoka kwenu kutoka kisimamo cha Arafa, ambapo ndipo alipoondoka Ibrahim, amani imshukie, ni katika hali ya kumkhalifu, kwa hilo, yule asiyesimama hapo miongoni mwa watu wa zama za ujinga. Na muombeni Mwenyezi Mungu Awasamehe madhambi yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaghufiria waja wake waombao maghufira, wanaotubia, ni mwenye huruma kwao

    [200] Basi mtakapokamilisha ibada yenu na mkamaliza amali zenu za Hija, mtajeni Mwenyezi Mungu na mumsifu kwa wingi kama vile mnavyotaja fahari za wazee wenu na zaidi ya hivyo. Kwani wamo miongoni mwa watu kikundi ambacho hima yao yote ni dunia. Hapo, wao huomba wakisema, «Ewe Mola wetu, tupe duniani afya, mali na wana.» Hao hawana Akhera hisa wala fungu lolote, kwa kuipuza Akhera na kujishughulisha na dunia tu

    [201] Na miongoni mwa watu kuna kikundi chenye Imani kinachosema katika dua yake, «Mola wetu, tupe duniani afya, mali, elimu inufaishayo, vitendo vyema na mengineyo katika mambo ya dini na dunia. Na katika Akhera, tupe Pepo na utuepushie adhabu ya Moto.» Dua hii ni miongoni mwa dua zilizokusanya. Kwa hivyo, ilikuwa ni dua ambayo Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, alikuwa akiiyomba mara nyingi zaidi, kama ilivyothibiti kwenye Sahihi Mbili: ya Bukhari na ya Muslim

    [202] Wale wenye kuomba dua hii wana thawabu kubwa kwa sababu ya amali njema walizozichuma. Mwenyezi Mungu ni mwepesi wa kuvihesabu vitendo vya waja wake na Mwenye kuwalipa navyo

    [203] Na mtajeni Mwenyezi Mungu kwa kuleta Tasbihi na Takbiri, katika siku chache, nazo ni siku za tshrīq: siku ya kumi na moja, kumi na mbili na kumi na tatu za mwezi wa Mfungotatu.Atakaye kufanya haraka kuondoka Mina kabla ya kutwa jua la siku ya kumi na mbili, baada ya kurusha vjiwe, hana makosa. Na yule atakaye kuchelewa kwa kulala Mina kungojea mpaka arushe vijiwe siku ya kumi na tatu, pia hana makosa, kwa aliyemcha Mwenyezi Mungu katika Hija yake. Na kuchelewa ni bora zaidi, maana huko ni kujiongezea mapato katika ibada na kufuata kitendo cha Nabii Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie. Na muogopeni Mwenyezi Mungu, enyi Waislamu, na mumweke mbele katika amali zenu zote; na mjue kwamba nyinyi kwake Yeye Peke Yake mtakusanywa baada ya kufa kwa ajili ya kuhesabiwa na kulipwa

    [204] Na baadhi ya watu miongoni mwa wanafiki yanakuvutia, ewe Mtume, maneno yake yaliyo fasaha ambayo kwayo anataka fungu la hadhi za duniani, si za Akhera, na anaapa huku akimshuhudisha Mwenyezi Mungu yaliyo moyoni mwake ya kuupenda Uislamu, hali ya kuwa yeye ana uadui na utesi mkubwa juu ya Uislamu na Waislamu. Huo ni upeo wa ujasiri juu ya Mwenyezi Mungu

    [205] Na anapoondoka kutoka kwako, ewe Mtume, hufanya bidii na akachangamka katika ardhi ili alete uharibifu humo na kutilifisha mazao ya watu na kuua wanyama wao. Na Mwenyezi Mungu Hapendi uharibifu

    [206] Na anaponasihiwa mnafiki huyo mharibifu na akaambiwa, «Mche Mwenyezi Mungu,ujihadhari na adhabu Yake na ukomeke na kuleta uharibifu katika ardhi,» huwa hakubali nasaha. Bali kile kiburi chake na mori wa kijinga humfanya kutenda maovu zaidi. Basi adhabu yenye kumtosheleza yeye na kumkifu ni Jahanamu. Na hakika uovu wa tandiko ndilo hilo

    [207] Na baadhi ya watu huziuza nafsi zao kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu, kwa kupigana jihadi katika njia Yake na kujilazimisha kumtii. Na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja, Anawarehemu waja wake Waumini rehema kunjufu, katika ulimwengu wao na Akhera yao, na kuwalipa malipo mazuri zaidi

    [208] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu kuwa ndiye Mola na Muhammad kuwa ndiye Mtume na Uislamu kuwa ndiyo Dini, ingieni katika sheria zote za Uislamu, hali ya kutekeleza hukumu zake zote, wala msiache chochote kati yazo, wala msiandame njia za Shetani katika yale anayowaitia ya maasia.Hakika Shetani kwenu ni adui mwenye uadui uliyo wazi. Basi jihadharini naye

    [209] Na iwapo mtapondoka kwenye njia ya haki, baada ya kujiliwa na hoja wazi-wazi za Qur’ani na Suna, basi jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mshindi katika ufalme Wake, hakuna chochote kilicho nje ya mamlaka Yake, ni Mwingi wa hekima kwenye amri Zake na Makatazo yake, Anaweka kila kitu pahali pake palinganapo nacho

    [210] Hawangojei hawa wakaidi wenye kukanusha, baada ya kusimama dalili wazi, isipokuwa Awajie Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kushinda, kwa namna inayolingana na Yeye, Aliyetakasika na kila sifa mbaya, katika vivuli vya Mawingu Siku ya Kiyama ili Aamue baina yao kwa hukumu adilifu, na waje Malaika. Wakati huo, Atahukumu Mwenyezi Mungu, kati yao, hukumu Yake. Na kwake Yeye Peke Yake hurudishwa mambo yote ya viumbe

    [211] Waulize, ewe Mtume, Wana wa Isrāīl wanaokufanyia ukaidi, «Ni aya ngapi zilizo wazi tulizowapa katika vitabu vyao zinazowaongoza wao njia ya haki, wakazikanusha,wakazipa nyongo na wakazipotosha kwa kuzitoa kwenye malengo yake.» Na atakayebadisha neema ya Mwenyezi Mungu, nayo ni dini Yake, na akaikanusha baada ya kuijua na hoja yake kumsimamia, basi Mwenyezi Mungu ni Mkali wa mateso kwake

    [212] Wale walioukanusha upweke wa Mwenyezi Mungu wamepambiwa maisha ya dunia na vilivyomo humo vya matamanio na vilivyo tamu, na huku wao wanawafanyia shere Waumini. Na hawa wanaomcha Mola wao watakuwa juu ya Makafiri wote Siku ya Kiyama, ambapo Mwenyezi Mungu Atawatia katika Pepo ya daraja za juu na Atawateramsha Makafiri ndani ya mashimo ya Moto ya chini. Mwenyezi Mungu Anamruzuku Amtakaye, katika viumbe vyake, bila ya hesabu

    [213] Watu walikuwa ni kundi moja, wameafikiana katika kumuamini Mwenyezi Mungu, kisha walitafautiana katika dini yao.Hapo ndipo Mwenyezi Mungu Aliwatuma Manabii, wakiwa ni walinganizi wa dini ya Mwenyezi Mungu, ni wabashiri wa Pepo kwa anayemtii Mwenyezi Mungu na ni waonyi wa Moto kwa anayemkanusha na kumuasi. Na Akateremsha, pamoja nao, vitabu vya mbinguni vilivyokusanya haki, ili wahukumu baina ya watu kwa yaliyomo ndani, katika yale waliyotafautiana juu yake. Na hawakutafautiana juu ya jambo la Mtume na Kitbu alichokuja nacho, kwa uhasidi na udhalimu, isipokuwa ni wale ambao Mwenyezi Mungu Amewapa Taurati na wakayajua yaliyomo ndani miongoni mwa hoja na hukumu. Hapo Mwenyezi Mungu, kwa fadhila zake, aliwaafikia Waumini kuipambanua haki na batili na kuyajua yale waliotafautiana juu yake. Mwenyezi Mungu Anampa taufiki amtakaye, miongoni mwa waja wake, kufuata njia iliyonyooka

    [214] Kwani mlidhani, enyi Waumini, kwamba mtaingia Peponi, na bado haijawapata mitihani kama ile iliyowapata Waumini waliopita kabla yenu: ya ufukara, maradhi, kitisho na babaiko, na wakatikiswa kwa aina nyingi za misukosuko ya kutisha, mpaka akasema Mtume wao na Waumini pamoja naye, kwa njia ya kuharakisha nusura ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, «Ni lini hiyo nusura ya Mwenyezi Mungu?» Jueni kwamba nusura ya Mwenyezi Mungu iko karibu na Waumini

    [215] Wanakuuliza watu wako, ewe Nabii, «Ni kitu gani wakitoe, katika aina za mali zao, kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka? Na watoe kumpa nani?» Waambie, «Toeni kheri yoyote iliyo tahfifu kwenu katika aina za mali mazuri ya halali, na utoaji wenu uwe ni kwa wazazi wawili, walio karibu katika watu wenu na kizazi chenu, mayatima, mafukara na msafiri mwenye uhitaji aliye mbali na watu wake na mali yake. Na kheri yoyote mtakayoifanya, basi Mwenyezi Mungu Aliyetukuka ni mwenye kuijua.»

    [216] Mwenyezi Mungu Amewafaradhia, enyi Waumini, kupigana na Makafiri, hali ya kuwa ni jambo lenye kuchukiwa na nyinyi kimaumbile, kwa uzito wake na hatari zake nyingi. Na huenda mkakichukia kitu nacho, kwa uhakika wake, ni kheri kwenu. Na huenda mkakipenda kitu kwa ajili ya raha na ladha za karibu zilizomo, nacho, kwa uhakika wake, ni shari kwenu. Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Analijua lenye kheri kwenu, na nyinyi hamlijui hilo. Kwa hivyo harakisheni kupigana jihadi katika njia Yake

    [217] Wanakuuliza washirikina, ewe Mtume, kuhusu mwezi mtukufu wa Haram, «Inafaa kupigana ndani yake?» Waambie, «Kupigana katika mwezi mtukufu wa Ḥarām ni jambo kubwa kwa Mwenyezi Mungu kuuhalalisha na kumwaga damu ndani yake. Na kuwazuia kwenu watu kuingia katika Uislamu, kwa kuwaadhibu na kuwatisha na kumkanusha kwenu Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na dini Yake, na kuwzuia Waislamu wasiingie kwenye Msikiti wa Haram, na kumtoa Nabii na waliogura naye kutoka huko, ambao wao ndiwo wakazi na wasimamizi wake, hilo ni dhambi kubwa mno na nikosa kubwa mno kwa Mwenyezi Mungu kuliko kupigana katika mwezi mtukufu wa Haram. Na ushirikina mlionao ni jambo kubwa zaidi na baya zaidi kuliko kuua katika mwezi mtukufu wa Haram. Na Makafiri hawa hawatatishika na kukomeka na makosa yao, bali wao ni wenye kuendelea nayo. Wala hawataacha kuwapiga vita mpaka wawatoe kwenye Uislamu kuwatia kwenye ukafiri, iwapo wataweza kulihakikisha hilo. Na mwenye kuwatii wao, kati yenu, enyi Waislamu, akaacha dini yake na akafa katika ukafiri, basi amali zake zitapotea duniani na Akhera na atakuwa ni miongoni mwa watakaodumu kwenye moto wa Jahanamu, hatatoka humo milele

    [218] Hakika wale ambao walimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakazitumia Sheria zake, wale waioyaacha Makaazi yao na wakapigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, hao ni wenye kutaraji kupata fadhila za Mwenyezi Mungu na thawabu Zake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasamehe madhambi ya waja Wake Waumini, ni Mwenye kuwarehemu rehema kunjufu

    [219] Wanakuuliza Waislamu, ewe Nabii, hukumu ya kutumia khamr kwa kunywa, kuuza na kununua. Khamr ni kila chenye kulewesha kinachofinika akili na kuziba, kiwe ni chenye kunywewa au kuliwa. Na wanakuuliza kuhusu hukumu ya kamari. Kamari ni kupokea au kutoa mali kwa bahati nasibu, nayo ni mashindano ambayo yana kupeana badali kutoka pande mbili za ushindani. Waambie, «Katika hayo pana madhara mengi na uharibifu mwingi katika dini na dunia, na akili na mali. Na yamo, katika mambo mawili hayo, manufaa kwa watu, kwa upande wa kuchuma mali na mengineyo. Na madhambi yake ni makubwa zaidi kuliko manufaa yake, kwani huzuia kumtaja Mwenyezi Mungu na kusali, na yote mawili yanaleta uadui na kuchukiana kati ya watu na yanaharibu mali. Huu ulikuwa ni utayarishaji wa kuyaharamisha mambo mawili hayo. Na wanakuuliza kuhusu kiwango ambacho wao wakitoe katika mali yao kwa njia ya sadaka na kujitolea.Waambie, «Toeni kiwango kinachozidi baada ya mahitaji yenu.» Mfano wa haya maelezo yaliyo wazi, Mwenyezi Mungu Anawabainishia aya na hukumu za Sheria, ili mpate kuyafikiria yenye manufaa kwenu

    [220] duniani na Akhera. Na wanakuuliza, ewe Mtume, kuhusu mayatima, waingiliane nao vipi katika maisha yao na mali yao. Waambie, «Kuwatengezea kwenu mambo yao ni bora. Basi, wafanyieni daima yanayowafaa wao zaidi.Na iwapo mtatangamana nao katika mambo ya maisha, basi wao ni ndugu zenu katika Dini. Na ni juu ya ndugu kuyalinda maslahi ya ndugu yake.Mwenyezi Mungu Anamjua mpotezaji wa mali ya mayatima na yule mwenye pupa la kuyahifadhi. Na lau Mwenyezi Mungu Angetaka, angewatia dhiki na mashaka kwa kuwaharamishia mtangamano. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mshindi katika ufalme Wake, ni Mwingi wa hekima katika uumbaji Wake, uendeshaji mambo Wake na upitishaji sheria Wake

    [221] Wala msiwaoe, enyi Waislamu, wanawake washirikina wanaoabudu masanamu mpaka waingie katika Uislamu. Na mjue kwamba mwanamke kijakazi, asiyekuwa na mali wala utukufu wa nasaba, anayemuamini Mwenyezi Mungu, ni bora kuliko mwanamke mshirikina, hata kama huyo mshirikina muungwana atawavutia. Wala msiwaoze wanawake wenu waumini, wakiwa ni vijakazi au waungwana, wanaume washirikina mpaka wamuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Na mjue kwamba mtumwa mwenye Imani, pamoja na ufukara wake, ni bora kuliko mshirikina, hata kama huyo mshirikina atawavutia. Hao wasifikao na ushirikina, wanaume na wanawake, wanamwita kila atangamanaye nao kwenye mambo yapelekayo Motoni. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu, Anawaita waja Wake kwenye dini Yake ya haki inayowapeleka Peponi na kusamehawa madhambi yao kwa idhini Yake. Na Yeye Anabainisha aya Zake na hukumu Zake kwa watu, ili wapate kukumbuka na wazingatie

    [222] Na wanakuuliza kuhusu hedhi, nayo ni damu inayotiririka kimaumbile kutoka kwenye uzao wa wanawake katika nyakati maalumu.Waambie, ewe Mtume, «Hiyo hedhi ni udhia wenye manyezi unaomdhuru mwenye kuusongelea. Hivyo basi, jiepusheni kuwaingilia wanawake kwenye kipindi cha hedhi mpaka damu ikome. Damu ikomapo, na wakaoga, waingilieni kupitia pale pahali Alipowahalalishia Mwenyezi Mungu, napo ni tupu ya mbele siyo ya nyuma. Hakika Mwenyezi Mungu Anawapenda waja Wake wenye kutubia na kuomba msamaha kwa wingi na Anawapenda waja Wake wenye kujisafisha ambao hujitenga na maovu na uchafu

    [223] Wake zenu ni pahali pa makulima yenu, mnaweka tone la manii ndani ya uzao wao, wakatoka humo watoto kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo, waingilieni pale pahali pake pa kuingiliwa tu, napo ni tupu ya mbele, kwa namna yoyote mtakayo. Na zitangulizieni nafsi zenu amali njema kwa kuzitunga amri za Mwenyezi Mungu. Na muogopeni Mwenyezi Mungu na mjue kwamba mtakutana na Yeye kwa kuhesabiwe Siku ya Kiyama. Na wape bishara njema Waumini, ewe Nabii, kwa yale ambayo yatawafurahisha na kuwapendeza ya malipo mema huko Akhera

    [224] Wala msikifanye, enyi Waislamu, kiapo chenu kwa Mwenyezi Mungu kuwa ni chenye kuwazuia nyinyi kufanya wema, kuunga kizazi, kumcha Mwenyezi Mungu na kusuluhisha kati ya watu. Nako ni iwapo mtaitwa kufanya lolote katika hayo, mkakataa na kutoa hoja kwamba mliapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa hamtalifanya. Bali ni juu ya Mwenye kuapa ageuze kiapo chake, afanye vitendo vya kheri na atoe kafara ya kiapo chake wala asizowee jambo hilo. Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasikia maneno yenu, ni Mwenye kuzijua hali zenu zote

    [225] Mwenyezi Mungu Hatawaadhibu nyinyi kwa sababu ya viyapo vyenu mnavyoviapa bila kukusudia, lakini Atawaadhibu kwa viapo vilivyokusudiwa na nyoyo zenu. Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe kwa yule anayetubia Kwake, ni Mpole kwa mwenye kumuasi kwa kuwa hamharakishii mateso

    [226] Wale wanaoapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba hawatawaingilia wake zao, wana muda wa kusubiriwa wa miezi minne. Iwapo watarudi kabla kumalizika hiyo miezi mine, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasamehe makosa yaliyofanywa na wao ya kiapo kwa sababu ya kurudi kwao, ni Mwenye huruma nao

    [227] Na iwapo wameamua kutaliki, kwa kuendelea kwao na kiapo chao na kuacha kuundama, Basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasikia maneno yao, ni Mjuzi wa Malengo yao, na Atawalipa kwayo

    [228] Na wanawake waliotalikiwa, waingiao hedhini, itawalazimu kungojea bila kuolewa muda wa twahara tatu au hedhi tatu baada ya kutalikiwa. Kukaa kwao kipindi hicho cha eda ni ili wahakikishe kuwa uzao ni safi, hawana mamba. Wala haifai kuolewa na mume mwengine katika kipindi hicho mpaka kiishe. Wala si halali kwao kukificha kile Alichokiumba Mwenyezi Mungu katika zao zao miongoni mwa mimba au hedhi, iwapo hao wanawake walioachwa ni wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho kikweli. Na waume wa wale waliotalikiwa wana haki ya kuwarejea wake zao hao iwapo bado wamo kwenye maeda yao. Na hilo la kuwarejea inapasa liwe ni kwa lengo la kheri na kutengeneza, wala lisiwe ni kwa lengo la kuwadhuru na kuwatesa kwa kulirefusha eda. Na wanawake wana haki kwa waume zao kama waume walivyo na haki kwa wake zao, kwa njia ya wema. Na wanaume kwa wake zao wana cheo cha zaidi kwa kukaa nao kwa uzuri, kutangamana nao kwa wema, kusimamia nyumba na kwamba talaka iko mikononi mwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mshindi, Ana enzi na uwezo wa kutendesha nguvu, ni Mwingi wa hekima, Huweka kila kitu mahali pake panapalingana

    [229] Talaka ambayo mtu anaweza kumrejea mke wake ni mara mbili, moja baada ya nyegine. Basi hukumu ya Mwenyezi Mungu, baada ya kila talaka, ni kumshikilia mwanamke kwa wema na tangamano zuri baada ya kumrejea au kumpa nafasi ya kwenda kwao pamoja na maelewano mema kwa kumtekelezea haki zake, na asimtaje mtalaka wake kwa uovu. Wala si halali kwenu, enyi Waumini, kuwapokonya chochote miongoni mwa vile mlivyowapa, kama mahari na vinginevyo. Isipokuwa wakiogopa waliooana kuwa hawataweza kutekeleza haki za unyumba, hapo mambo yao yatawekwa mbele ya mawalii. Na watakapochelea hao mawalii kuwa wanyumba wao hawataweza kutekeleza haki na mipaka ya Mwenyezi Mungu, hakuna kosa kwa waliooana katika kile atakacho kukitoa mwanamke kumpa mume kama ridhaa ya kupata talaka. Hukumu hizo ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu, inayopambanua kati ya halali na haramu, basi msiikeuke. Na wenye kusubutu kuikeuka mipaka ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, hao ndio madhalimi wa nafsi zao kwa kuzihatarisha adhabu ya Mwenyezi Mungu

    [230] Na iwapo mume atamtaliki mkewe talaka ya tatu, basi mke huyo atakuwa si halali tena kwa mume huyo, isipokuwa atakapoolewa na mwanamume mwengine ndoa sahihi na akaingiliwa katika ndoa hiyo, iwapo ndoa hiyo ni ya kutakana, na si kwa nia ya kumhalalisha yule mwanamke kwa mume wake wa kwanza. Na iwapo yule mume mwengine atamuacha mke yule, au akafa na eda lake likaisha, basi hapana dhambi kwa yule mwanamke na mume wake wa kwanza kuoana kwa kifungo cha ndoa kipya na mahari mapya, ikiwa wawili hao waonelea kwamba watazitekeleza hukumu za Mwenyezi Mungu Alizoziweka kwa waliooana. Hizo ni sheria za Mwenyezi Mungu zilizowekewa mipaka, Anazifunua wazi kwa watu wanaozijua hukumu Zake na mipaka Yake, kwani ni wao wanaonufaika nazo

    [231] Pindi mtakapowataliki wanawake wakakaribia siku za kumaliza eda lao, basi warejeeni hali ya kuwa nia zenu ni kuwatekelezea haki zao kwa njia nzuri, kisheria na kidesturi, au waacheni mpaka eda lao limalizike. Na kueni na hadhari, isije ikawa kuwarejea ni kwa lengo la kuwadhuru kwa kuwafanyia uadui katika haki zao. Na yoyote atakayelifanya hilo, ameshaidhulumu nafsi yake kwa kustahiki mateso. Na wala msizifanye aya za Mwenyezi Mungu na hukumu Zake kuwa ni mchezo na upuzi. Nakumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu kwenu, kwa kuwafanya Waislamu na kuwafafanulia hukumu Zake. Na yakumbukeni yale Aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, ya Qur’ani na mafundisho ya Mtume Wake. Na mshukuruni Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kwa neema hizi zilzo kubwa. Mwenyezi Mungu Anawakumbusha hayo na Anawatisha msende kinyume nayo. Basi, mcheni Mwenyezi Mungu na mumlindize. Na mjue kwamba Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu, hapana kitu chenye kufichika Kwake, na Atamlipa kila mmoja kwa anayostahiki alipwe

    [232] Na mtakapowaacha wake zenu chini ya talaka tatu na eda lao likaisha bila nyinyi kuwarejea, basi msiwadhiki, enyi mawalii, hao walioachwa kwa kuwazuia kurudi kwa waume zao, kwa kufunga ndoa upya, wakiwa wenyewe wametaka hilo na yakapatikana maridhiano kisheria na kidesturi. Hilo aidhiwa kwalo aiyekuwa, miongoni mwenu, ni mkweli kwenye imani yake kwa Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hakika kuacha kuwazuia na kuwawezesha waume kuwaoa waliokuwa wake zao, ni jambo lenye kukuza zaidi na kutakasa zaidi heshima zenu, na ni lenye nafuu kubwa zaidi na thawabu nyingi zaidi kwenu. Na Mwenyezi Mungu Anayajua yenye maslahi kwenu; na nyinyi hamjui hilo

    [233] Na ni juu ya wanawake waliozaa kuwanyonyesha watoto wao muda wa miaka miwili kamili, kwa yule atakaye kukamilisha unyonyeshaji. Na ni wajibu kwa mababa kuwadhamini wanyonyeshaji, waliopewa talaka, kwa chakula chao na mavazi yao kwa njia ipendekezayo kisheria na kimila. Kwani Mwenyezi Mungu hamkalifishi mtu ela kiasi cha uwezo wake. Na haifai kwa wazazi wawili kumfanya mototo aliyezaliwa kuwa ni njia ya kudhuriana kati yao. Na inamlazimu mrithi, mzazi anapokufa, kile kinachomlazimu mzazi, kabla hajafa, cha matumizi na mavazi. Na wazazi wanapotaka kumuachisha mtoto kunyonya, kabla kukamilisha miaka miwili, basi si makosa kwao iwapo wameridhiana na kushawiriana kwa hilo na kufikia kwenye uamuzi wenye maslahi ya mtoto. Na iwapo wazazi wawili wamekubaliana kumpa mtoto mnyonyeshaji mwengine asiyekuwa mamake ili amnyonyeshe, pia si makosa kwao., iwapo baba atampa mama haki yake, na pia atampa mwenye kunyonyesha haki kwa mujibu wa desturi zinazoeleweka kwa watu. Na muogopeni Mwenyezi Mungu katika hali zenu zote. Na mjue kwamba Mwenyezi Mungu kwa mnayoyafanya ni muoni na Atawalipa kwayo

    [234] Na wale wanaofariki kati yenu wakawaacha wake zao baada ya kufa kwao, italazimu wakae eda muda wa miezi minne na siku kumi, wasitoke majumbani mwao, wasijipambe wala wasiolewe. Na pindi muda huo uliotajwa uishapo, si dhambi kwenu, enyi mawalii wa wanawake, kwa yale watakayo kujifanyia nafsi zao, ya kutoka, kujipamba na kuolewa kwa njia iliyowekwa na Sheria. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kutakasika na kila sifa mbaya, ni Mtambuzi wa vitendo vyenu vya wazi na viliyofichika, na Atawalipa kwavyo

    [235] Na wala nyinyi hamna dhambi, enyi wanaume, katika ishara mnazozitoa za kutaka kuwaoa wanawake waliofiliwa na waume zao au wale waliopewa talaka ya mwisho, wakiwa wako katika eda lao. Pia hamna dhambi katika mawazo yanayowapitia ndani ya nafsi zenu ya kutaka kuwaoa wamalizapo eda lao. Mwenyezi Mungu Anajua kwamba nyinyi mtawataja wanawake walio kwenye eda na hamtasubiri kuweza kunyamaza kutowataja, kwa udhaifu wenu. Kwa ajili hiyo, Mwenyezi Mungu amewahalalishia kuwataja kwa ishara au kwa kudhamiria ndani ya nafsi zenu. Na jihadharini kuagana nao kisiri, kwa kuzini, au kukubaliana kuoana wakiwa bado wako kwenye eda, isipokuwa mtakaposema neno lenye maana kwamba mfano wake, mwanamke huyo, waume huwa wanampendelea. Wala msikusudie kufunga ndoa katika kipindi cha eda mpaka muda wake umalizike. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu Anayajua yaliyomo katika nafsi zenu, kwa hivyo muogopeni Yeye. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe kwa mwenye kutubia dhambi zake, ni Mpole kwa waja Wake, Hana haraka ya kuwatesa

    [236] Hakuna dhambi juu yenu, enyi wanaume, iwapo mtawataliki wanawake baada ya kufunga ndoa nao na kabla ya kuwaingilia au kuwatajia mahari. Hivyo basi, waliwazenikwa kuwapa kitu chenye kuwanufaisha kwa kuwaliwaza na kuwaondolea maudhi ya talaka na kumaliza chuki. Kiliwazo hiki kinalazimu kulingana na hali ya mwanamume aliyetoa talaka: tajiri kulingana na ukunjufu wa hali yake na maskini kulingana na kile alichonacho. Kiliwazo hiko kiwe ni chenye kuambatana na Sheria. Nacho ni haki iliyothibiti juu ya wale wanaowafanyia wema watalaka wao na kujifanyia wema wao wenyewe kwa kumtii Mwenyezi Mungu

    [237] Na iwapo mtawataliki wanawake, baada ya kufunga ndoa nao na kabla hamjawaingilia, na mkawa mumejilazimisha kuwapa kiasi maalumu cha mahari, basi inawapasa muwape nusu ya mahari mliyokubaliana, isipokuwa iwapo watalaka hao watasamehe na kuiacha ile nusu ya mahari iliyopasa wapewe, au iwapo mume atasamehe kwa kumuachia mtalaka mahari yote. Na kusamehe kwenu, enyi wanaume na wanawake, ni jambo lililo karibu zaidi na kumcha Mwenyezi Mungu na kumtii. Wala msisahau, enyi watu, fadhila na wema kati yenu ambao ni kutoa ambacho si wajibu kwenu kukitoa na kusameheana haki. Hakika Mwenyezi Mungu, kwa mnayoyafanya, ni mwenye ni mwenye kuona. Anawahimiza kufanya kheri na kuwasongeza kufanya wema

    [238] Zihifadhini, enyi Waislamu, Swala tano zilizofaradhiwa kwa kudumu nazo katika kuzitekeleza kwa nyakati zake, masharuti yake, nguzo zake yanayopasa yake. Na muhufadhi swala iliyo katikati ya swala hizo, nayo ni Swala ya Alasir Na simameni katika Swala zenu hali ya kumtii Mwenyezi Mungu, kumnyenyekea na kumdhalilikia

    [239] Na iwapo mtawaogopa maadui maadui wenu, swalini swala ya khofu, mkiwa mwatembea au mumepanda, kwa namna yoyote ile mnayoiweza, hata kama ishara, au hata kama hamkulekea kibla. Na pindi khofu yenu itakapokwisha, swalini swala ya amani na mumtaje Mwenyezi Mungu humo. Wala msiipunguze kwakuitoa kwenye namna yake ya asili. Na mshukuruni Mwenyezi Mungu kwa kuwafundisha mambo ya ibada na hukumu ambayo hamkuwa na ujuzi nayo

    [240] Na waume wanaofariki na wakaacha wake baada yao, inawalazimu waume hao wawekee wasia hao wake zao kwamba waliwazwe mwaka mzima kuanzia siku ya kufariki, kwa kupewa Makao katika nyumba ya mume, bila ya kutolewa na mawarithi kwa muda wa mwaka. Hilo likiwa ni maliwazo kwa yule mke na ni wema kwa aliyefariki. Na iwapo wanawake hao waliofiliwa watatoka, kwa hiyari yao kabla mwaka kumalizika, basi hamna makosa, nyinyi warithi, katika hilo. Pia, hakuna makosa kwa hao wanawake kwa kitendo chao cha halali walichojifanyia nafsi zao. Mwenyezi Mungu ni Mshindi katika ufalme Wake, ni Mwingi wa hekima katika amri Zake na Makatazo Yake. Aya hii, hukumu zake zimeondolewa kwa neno Lake Mwenyezi Mungu Aliyetukaka, «Na wale wanaofariki kati yenu na wakaacha wake zao, (Basi wake hao) wajizuie nafsi zao miezi mine na siku kumi»

    [241] Na wanawake waliotalikiwa wanastahiki wapewe kiliwazo cha mavazi na matumizi kwa mujibu wa mpango unaojulikana na kupendekezwa na kisheria. Hiyo ikiwa ni haki juu ya wale wanaomuogopa Mwenyezi Mungu katika amri Zake na Makatazo Yake

    [242] Mfano wa maelezo hayo yaliyo wazi, katika hukumu za watoto na wanawake, Anawabainishia Mwenyezi Mungu mafunzo aya Zake na hukumu Zake kuhusu kila mnachokihitajia katika maisha yenu ya ulimwengu na marejeo yenu ya Akhera, ili mzitie akilini nz mzitumie

    [243] Kwani hujui, ewe Mtume, kisa cha waliokimbia kutoka ardhi yao na nyumba zao, wakiwa ni maelfu mengi, wakiogopa kufa kwa sabababu ya janga la ugonjwa hatari au vita, Mwenyezi Mungu Akawaambia, «Kufeni», wakafa, papo hapo, kwa mara moja, ikiwa ni adhabu kwao kwa kukimbia kadara ya Mwenyezi Mungu, kisha Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Akawahuisha baada ya muda kupita, ili waukamilishe muda wa uhai wao, na ili wapate kuwaidhika na kutubia? Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kubwa kwa watu, kwa neema zake nyingi, lakini watu wengi hawazishukuru fadhila za Mwenyezi Mungu zilio kwao

    [244] Na piganeni nao, enyi Waislamu, hao makafiri ili kuinusuru Dini ya Mwenyezi Mungu, na mjue kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasikia maneno yenu na ni Mwenye kuzijua nia zenu na vitendo vyenu

    [245] Ni yupi ambaye atatoa katika njia ya Mwenyezi Mungu, kutoa kuliko kuzuri kwa kutarajia malipo, Mwenyezi Mungu Apate kumuongezea nyongeza nyingi zisizohesabika za thawabu na malipo mema? Hakika Mwenyezi Mungu Anazuia na Anatoa. Kwa hivyo, toeni wala msijali, kwani Yeye Ndiye Mruzuku, Anambana Anayemtaka, miongoni mwa waja Wake, katika riziki na Anaikunjua, hiyo riziki, kwa wengine. Ana hekima kubwa katika hayo. Na Kwake Yeye Peke Yake mtarudi baada ya kufa, na hapo Atawalipa kwa vitendo vyenu

    [246] Kwani hukukijua, ewe Mtume, kisa cha watukufu na mabwana, miongoni mwa Wana wa Isrāīl, baada ya zama za Musa kupita? Walipomtaka Mtume wao amtawalishe kwao mfalme, wapate kukusanyika chini ya uongozi wake na wapate kupigana na maadui zao katika njia ya Mwenyezi Mungu. Nabii wao akawaambia, «Je, mambo ni kama vile ninavyoyatarajia kwamba lau mtafaradhiwa kupigana katika njia ya Mwenyezi Mungu kuwa hamtapigana? Kwani mimi nachelea mtaogopa na mtakimbia vitani.» Wakasema wakikanusha matarajio ya Nabii wao, «Ni kizuizi kipi kitakacho kutuzuia tusipigane katika njia ya Mwenyezi Mungu, ambapo adui yetu ametutoa kwenye Makao yetu na akatutenganisha na na watoto wetu kwa kutuua na kututeka?» Basi Mwenyezi Mungu Alipowafaradhia kupigana wakiwa na mfalme Aliyewachagulia walikuwa waoga na wakakimbia vitani, isipokuwa wachache kati yao waliojikita imara kwa fadhila za Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu Anawajua mno madhalimu, wenye kuzivunja ahadi zao

    [247] Na Mtume wao aliwaambia, «Hakika Mwenyezi Mungu Amewaltea Tālūt kuwa ni mfalme, ikiwa ni kuyaitikia maombi yenu, ili awaongoze katika kupigana na adui yenu kama mlivyoomba.» Wakasema wakuu wa Wana wa Isrāīl, «Vipi Tālūt atakuwa mfalme kwetu, hali yeye hastahiki hilo? Yeye si katika wajukuu wa wafalme, wala hatoki kwenye nyumba ya utume na wala hakupewa ukunjufu wa mali ya kujisaidia nayo katika ufalme wake. Sisi tuna haki zaidi ya huu ufalme kuliko yeye. Kwani sisi ni wajukuu wa wafalme na tunatoka kwenye nyumba ya utume.» Mtume wao akawaambia, «Hakika Mwenyezi Mungu Amewachagulia, na Yeye, Aliyetakasika na kila sifa mbaya, Anayajua zaidi mambo ya waja Wake, na Amemuengezea ukunjufu wa elimu na nguvu ya mwili ya kupigana na adui. Na Mwenyezi Mungu ni Mmiliki wa ufalme. Anampa ufalme wake Anayemtaka katika waja wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa fadhila na utoaji, ni Mjuzi kabisa wa ukweli wa mambo, hapana chenye kufichika Kwake.»

    [248] Mtume wao aliwaambia, «Hakika alama ya ufalme wake ni kuwajilieni sanduku ambalo ndani yake muna Taurati,- Sanduku ambalo maadui wao walikuwa wamewanyang’anya-. Ndani yake muna utulivu kutoka kwa Mola wenu unaozithibitisha nyoyo za wenye ikhlasi. Na muna ndani yake mabaki ya vitu vilivyoachwa na jamaa za Musa na jamaa za Hārūn, kama fimbo na vipande vya mbao, yanabebwa na Malaika. Hakika muna katika hayo hoja kubwa kuwa Tālūt amechaguliwa kuwa mfalme wenu kwa amri ya Mwenyezi Mungu, iwapo mnamuamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake.»

    [249] Alipotoka Twalut na askari wake kwenda kupigana na watu majabari, aliwaambia, «Mwenyezi Mungu Atawapa mtihani wa subira kwa mto uliyo mbele yenu mtakaouvuka, ili abainike mwenye Imani na aliye mnafiki. Yoyote kati yenu atakaye kunywa maji ya mto huo, si katika mimi, wala hafai kuwa na mimi kwenye jihadi. Na yule ambaye hatayaonja maji hayo, yeye ni katika mimi, kwa kutii amri yangu, na anafaa kwa jihadi. Isipokuwa aliyeruhusiwa na akateka mteko mmoja kwa mkono wake, huyo hana lawama. Basi walipofika mtoni, waliyaangukia maji na waliyanywa sana isipokuwa idadi ya watu wachache kati yao, walisubiri juu ya kiu na joto na wakatosheka na mteko wa mkono. Wakati huo wale walioasi amri, walirudi nyuma. Tālūt pamoja na wale Waumini wachache walipouvuka mto - walikuwa watu zaidi ya mia tatu na kumi- kwa ajili ya kupambana na maadui zao na wakaona wingi wa maadui zao na wingi wa silaha walionazo, walisema, «Hatuna uwezo leo wa kupigana na Jālūt na askari wake wenye nguvu. Hapo, wale wliokuwa na yakini ya kukutana na Mola Wao walijibu wakiwakumbusha ndugu zao juu ya Mwenyezi Mungu na uwezo Wake, «Nivikundi vingapi vichache, venye imani na subira, viliyashinda, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, makundi yaliyokuwa na watu wengi makafiri wenye kuasi, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu Yupo pamoja na wenye subira kwa taufiki Yake na nusra Yake na malipo Yake mema

    [250] Na walipojitokeza kwa Jālūt na askari wake na wakaiona hatari kwa macho yao, walifazaika na kumuelekea kwa Mwenyezi Mungu kwa maombi na kunyenyekea huku wakisema, «EweMola wetu! Tumiminie subira nyingi kwenye nyoyo zetu, Uzithibitishe nyayo zetu ziwe thabiti muda wa kupigana na adui, zisiwe na uoga wa kukimbia vita, na Utunusuru kwa msaada wako juu ya watu makafiri

    [251] Hapo waliwashinda kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na Dāwūd, Amani imshukiye, alimuua Jālūt, kiongozi wa majabari. Na Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, baada ya hapo, Akampa Dāwūd ufalme na utume katika Wana wa Isrāīl, na Alimfundisha Aliyoyataka miongoni mwa elimu. Na lau kama si himaya ya Mwenyezi Mungu, kwa kuwatumia baadhi ya watu- nao ni wale watiifu Kwake na wanaomuamini- kuwazuia wengine- nao ni wanaomuasi Mwenyezi Mungu na kumshirikisha-, basi ardhi ingaliharibika kwa ushindi wa ukafiri na kupata nguvu uharibifu na wenye kufanya maasia. Lakini Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kwa viumbe wote

    [252] Hizo ni hoja za Mwenyezi Mungu na dalili Zake tunakusimulia wewe, ewe Nabii, kwa kweli, na hakika wewe ni miongoni mwa Mitume walio wakweli

    [253] Mitume hawa watukufu, Mwenyezi Mungu Amewatukuza baadhi yao juu ya wengine, kulingana na neema za Mwenyezi Mungu juu yao. Miongoni mwao kuna ambao Mwenyezi Mungu Amesema nao, kama Mūsā na Muhammad, rehema na amani ziwashukie. Katika hili pana kuthibitisha sifa ya kusema kwa Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, kwa namna inayonasibiana na utukufu Wake. Na miongoni mwao kuna ambao Mwenyezi Mungu Aliwainua daraja nyingi za juu, kama Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa kuenea ujumbe wake, kutia kikomo cha unabii kwake, kwa kuwatukuza ummah wake juu ya ummah wengine na yasiyokuwa hayo. Na Mwenyezi Mungu Alimpa 'Īsā mwana wa Maryam, amani imshukie, hoja zilizo wazi, ambazo ni miujiza yenye kushinda, kama kumponya aliyezaliwa kipofu, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, na kumponya mwenye barasi, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na kama kuhuisha kwake waliokufa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu Alimpa nguvu kwa Jibrili, amani imshukie. Na lau Mwenyezi Mungu Alitaka wasipigane hao waliokuja baada ya hawa Mitume, baada ya kuwafunukia wao hoja zilizo wazi, hawangalipigana. Lakini ilitokea tafauti baina yao: katika wao kuna aliyejikita kwenye Imani yake, na katika wao kuna aliyeshikilia kukanusha. Na lau Mwenyezi Mungu Alitaka, baada ya hizo tafauti zilizotokea zilizopelekea kupigana, hawangalipigana, lakini Mwenyezi Mungu Anampa taufik ya kumtii Yeye na kumuamini Anayemtaka, na Anamuondolea taufiki Yake Anayemtaka akamuasi na kumkanusha, Kwani Yeye Anafanya na kuchagua Analolitaka

    [254] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na kumsadiki Mtume Wake na kufanya amali zinazoambatana na uongofu Wake! Toeni Zaka zilizofaradhiwa na mtoe sadaka ya vitu mlivyopewa na Mwenyezi Mungu kabla haijaja Siku ya Kiyama, wakati ambapo hakuna kuuziana ikapatikana faida, wala mali ambayo nyinyi mtajikomboa nayo nafsi zenu kutokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu, wala urafiki wa rafiki wenye kuwaokoa, wala muombezi anayemiliki kuwafanya mpunguziwe adhabu. Na makafiri ndio madhalimu na wakeukaji mipaka ya Mwenyezi Mungu

    [255] Mwenyezi Mungu Ndiye Ambaye hakuna yoyote anayestahiki uungu na kuabudiwa isipokua Yeye. Ndiye Aliye hai Ambaye Amekusanya maana yote ya uhai mkamilifu unaolingana na utukufu Wake. Ndiye Msimamizi wa kila kitu. Kusinzia hakumshiki wala kulala. Kila kilichoko kwenye mbingu na kilichoko kwenye ardhi ni milki Yake. Na hatajasiri mtu yoyote kuombea mbele Yake isipokuwa kwa ruhusa Yake. Ujuzi Wake umevizunguka vitu vyote vilivyopita, vilivyoko na vitakavyo kuja. Anajua yaliyo mbele ya viumbe katika mambo ambayo yatakuja na yaliyo nyuma yao katika mambo yaliyopita. Na hakuna yoyote, katika viumbe, mwenye kuchungulia chochote katika elimu Yake isipokuwa kadiri ile ambayo Menyezi Mungu Amemjulisha na kumuonesha. Kursiy Yake imeenea kwenye mbingu na ardhi. Kursiy ni mahali pa nyayo za Mola, uliyo mkubwa utukufu Wake, na hakuna ajuwae namna ilivyo isipokuwa ni Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. Wala hakumlemei Mwenyezi Mungu Aliyetakata kuzitunza. (hizo mbingu na ardhi).Yeye Ndiye Aliye juu ya viumbe Vyake vyote, kwa dhati Yake na sifa Zake, Aliyekusanya sifa za utukufu na kiburi. Aya hii ni aya tukufu zaidi katika Qur’ani, na inaitwa Āyah al- Kursīy

    [256] Kwa kuwa Dini hii imekamilika na hoja zake ziko wazi, haihitajii ilazimishwe kwa watu ambao jizya (jizyah) inapokewa kutoka kwao. Kwani dalili ziko wazi ambazo kwa dalili hizo inabainika haki, ikawa kando na batili, na uongofu, ukawa kando na upotevu. Basi mwenye kukanusha vyote vinavyoabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu na akamuamini Mwenyezi Mungu, huwa amethibiti na kulingana kwenye njia bora na ameshikamana na kamba imara ya Dini isiyokatika. Na Mwenyezi Mungu ni Msikizi wa maneno ya waja Wake, ni Mjuzi wa nia zao na vitendo vyao na Atawalipa kwa hayo

    [257] Mwenyezi Mungu Anawasimamia Waumini kwa kuwanusuru, kuwaafikia na kuwahifadhi, Anawatoa kutoka kwenye magiza ya ukafiri kuwapeleka kwenye nuru ya Imani. Na wale waliokufuru, wanusuru wao na wasaidizi wao ni wale wafananishwao na Mwenyezi Mungu na masanamu wanaowaabudu wasiokuwa Mwenyezi Mungu. Hao wanawatoa wao kutoka kwenye nuru ya Imani kuwapeleka kwenye magiza ya ukafiri. Wao ndio watu wa Motoni wenye kutindikia humo, wenye kusalia humo milele na si wenye kutoka humo

    [258] Je umewahi kuona, ewe Mtume, hali ya kustaajabisha zaidi kuliko ile ya yule aliyemjadili Ibrāhīm, amani imshukie, juu ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na juu ya uola Wake, kwa kuwa Mwenyezi Mungu Alimpa ufalme, alipofanya ujeuri na kumuuliza Ibrāhīm, «Ni nani Mola wako?» Alisema, amani imshukie, «Mola wangu ni Ambaye Anavipa viumbe uhai vikahuika na Anaviondolea uhai vikafa. Yeye Ndiye Aliyepwekeka kwa kuhuisha na kufisha.» Akasema, «Mimi nahuisha na kufisha.» Yaani: namuua nimtakaye kumuua, na namuachilia nimtakaye kumuachilia. Ibrāhīm akasema kumwambia, «Mwenyezi Mungu ninayemuabudu Analitoa jua upande wa mashariki. Je unaweza wewe kugeuza mwenendo huu wa kimungu, ulifanye litokeze upande wa magharibi?» Akapigwa na mshangao huyu kafiri na ikakatika hoja yake. Hali yake ni ile ya madhalimu, Mwenyezi Mungu Hawaongozi kwenye haki na usawa

    [259] Au je uliona, ewe Mtume, mfano wa yule aliyepita kwenye kijiji ambacho nyumba zake zilikuwa zimevunjika na kuangukia misingi yake na akasema, «Vipi Mwenyezi Mungu Atakihuisha kijiji hiki baada ya kuwa kimekufa?» Mwenyezi Mungu Akamfisha miaka mia moja kisha Akamrudishia roho yake na Akamwambia, «Ni kwa muda gani ulikuwa umekufa?» Akasema, «Nilikuwa nimekufa kwa muda wa siku moja au sehemu ya siku.» Akampa habari kuwa alikuwa amekufa kwa muda wa miaka mia. Na Akamuamrisha akiangalie chakula chake na kinywaji chake vipi Mwenyezi Mungu Amevihifadhi visiharibike muda huu mrefu. Na Akamuamrisha amtazame punda wake aone vipi Mwenyezi Mungu Alimuhuisha baada ya kuwa mifupa iliyotapakaa. Na Akamwambia, «Na ili tukufanye wewe ni dalili kwa watu.» Yaani: dalili iliyo wazi ya uweza wa Mwenyezi Mungu kufufua baada ya kufa. Na akamuamrisha aitazame mifupa aone vipi Mwenyezi Mungu Anavyoiinua baadhi yake juu ya mingine na kuiunganisha baadhi yake na mingine na kuivisha nyama baada ya kushikana na kisha kuirudishia uhai.Yalipomfunukia hayo waziwazi alikubali ukubwa wa Mwenyezi Mungu na kuwa Yeye ni Muweza wa kila kitu. Na akawa ni dalili kwa watu

    [260] Na Kumbuka, ewe Mtume, maombi ya Ibrahim kwa Mola wake Amuoneshe namna ya Ufufuzi. Mwenyezi Mungu Alimwambia, «Kwani huamini?» Akasema, «La! Nakuamini. Lakini nataka hilo ili nipate yakini zaidi juu ya yakini niliyonayo.» Akasema, «Chukua ndege wanne, uwe nao, uwachinje na uwakatekate kisha weka sehemu ya hao ndege juu ya kila jabali. Kisha waite, watakujia kwa haraka.» Ibrahim, amani imshukie, akawita. Papo hapo kila sehemu ikarudi mahali pake, na papo hapo wakamjia kwa haraka. Na ujue kuwa Mwenyezi Mungu ni Mshindi, hakuna kimshindacho, ni Mwenye hekima katika maneno Yake, vitendo Vyake, sheria Yake na makadirio Yake

    [261] Na miongoni mwa vitu bora zaidi vinavyowanufaisha Waumini ni kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu. Na mfano wa Waumini wenye kutoa mali yao katika njia ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa mbegu iliyopandwa kwenye ardhi nzuri, muda si muda ikatoa mte wenye sehemu saba. Kila sehemu ikatoa suke moja na kila suke likawa na mbegu mia. Na Mwenyezi Mungu Anamuongezea thawabu anayemtaka, kulingana na kadiri ya Imani aliyonayo yule mtoaji na ikhlasi yake iliyo timamu.Na fadhila za Mwenyezi Mungu zimeenea, na Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, ni Mjuzi wa yule anayestahiki kuzipata, ni Mwenye kuchungulia nia za waja Wake

    [262] Wale ambao wanatoa mali yao katika jihadi na aina mbali-mbali za kheri, kisha wasifuatishe, yale waliyoyatoa ya kheri, kwa kumsumbulia waliyempa wala kumkera, kwa neno au kitendo, kwa kumhisisha kuwa wamemfadhili, watapata thawabu kubwa mbele ya Mola wao na hawatakuwa na kicho kuhusu mustakbala wao wa Akhera wala hawatahuzunika juu ya kitu chochote kilichowapita wasikipate katika ulimwengu

    [263] Maneno mazuri kujibiwa muombaji na kusamehe utiriri wake katika kuomba, ni bora kuliko sadaka inayofuatiwa na kero na ubaya kutoka kwa mtoaji sadaka. Na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Hana haja ya sadaka za waja, ni Mpole Hana haraka nao ya kuwatesa

    [264] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, msiziondoe thawabu za vitu vile mlivyovitoa sadaka kwa usumbulizi na kero. Kwani huyu, mwenye kufanya haya, anafanana na mtu atowaye mali yake ili watu wamuone na wamsifu ilhali yeye hamuamini Mwenyezi Mungu wala hana yakini na Siku ya Akhera. Mfano wa huyo ni mfano wa jiwe laini lenye mchanga juu yake, lililonyeshewa na mvua nyingi, ikaondoa ule mchanga, ikaliacha tupu halina kitu juu yake. Basi hawa wenye kufanya ria ndivo walivyo, amali zao zinapotea mbele ya Mwenyezi Mungu na hawapati chochote cha thawabu kwa utoaji wao. Na Mwenyezi Mungu hawaafikii makafiri kuifikia haki katika vitu wanvyovitoa na mengineyo

    [265] Na mfano wa wale ambao wanatoa mali yao kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu na kwa kuwa na itikadi iliyojikita ya kuwa ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli, ni kama mfano wa bustani kubwa iliyoko kwenye ardhi ya juu iliyo nzuri iliyonyeshewa na mvua nyingi, yakaongezeka kwa wingi matunda yake. Na hata kama haingalinyeshewa na mvua nyingi, rasharasha la mvua lingalitosha kuifanya itoe ongezeko lingi la matunda. Basi hivyo ndivyo ulivyo utoaji wa watu wenye ikhlasi; amali zao zinakubaliwa mbele ya Mwenyezi Mungu na kuongezwa, ziwe ni chache au ni nyingi. Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye kuchungulia siri, Ndiye Mwenye kuyaona ya nje na ya ndani, Anampa thawabu kila mtu kulingana na ikhlasi yake

    [266] Je anapendelea mmoja wenu awe na bustani yenye mitende na mizabibu, ambayo inapita chini ya miti yake maji tamu, na ndani yake ana kila aina ya matunda, na amefikia hali ya ukongwe ya kutoweza kupanda mimea kama hii, na ana watoto wadogo wanaohitaji bustani hii, na katika hali hii ukavuma upepo mkali uchomao, ukaja ukaiteketeza? Hivi ndivyo hali ya wasio na ikhlasi kataka utoaji wao; watakuja Siku ya Kiyama na hawana jema lolote lao. Kwa ufafanuzi huu, Mwenyezi Mungu Anawabainishia mambo yanayowafaa nyinyi, ili mtaamali na kumtakasia Mwenyezi Mungu utoaji wenu

    [267] Enyi mlioniamini na mkawafuata Mitume wangu, toeni miongoni mwa halali mliyoichuma na ile tuliyowatolea kutoka kwenye ardhi. Na wala msikusudie kutoa kibaya, katika hiyo halali, kuwapa mafukara, ambacho lau nyinyi mngalipewa, hamngalikipokea isipokuwa mkiwa mtapuuza ubaya na upungufu ulionacho. Ni vipi nyinyi mnaridhika kumpa Mwenyezi Mungu kitu ambacho hamridhiki nacho mkipewa? Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu Aliyewaruzuku Anajitosha kutohitajia sadaka zenu, ni Mstahiki wa kusifiwa na Mhimidiwa kwa kila hali

    [268] Uchoyo huu na kuchagua kibaya kukitoa sadaka yatokana na Shetani ambaye anawaogopesha nyinyi ufukara na kuwahimiza uchoyo, na anawaamrisha nyiyi maasia na kumfanyia kinyume Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetakata na kutukuka, Anawaahidi nyinyi, kwa kutoa kwenu, msamaha wa madhambi yenu na riziki kundufu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nyongeza zenye kuenea, ni Mjuzi wa nia na vitendo

    [269] Mwenyezi Mungu Anampa taufiki ya usawa katika kunena na kutenda Anayemtaka miongoni mwa waja Wake. Na yoyote ambaye Mwenyezi Mungu Amemneemesha kwa hilo, Hua Amempa kheri nyingi. Na hatakumbuka hilo na kunufaika nalo isipokuwa wenye akili zenye kung’ara kwa nuru ya Mwenyezi Mungu na uongofu Wake

    [270] Mali yoyote mnayoyatoa na mengineyo, machache au mengi, au sadaka mnayoitoa kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, au mkajilazimisha nafsi zenu chochote, cha mali au kinginecho, basi Mwenyezi Mungu Anayajua hayo; na Yeye Ndiye Mwenye kuchungulia nia zenu, na Atawalipa kwa hayo. Na yoyote mwenye kuzuia haki ya Mwenyezi Mungu ni dhalimu. Na madhalimu hawana wenye kuwanusuru ambao watawazuia wasipate adhabu ya Mwenyezi Mungu

    [271] Mkizidhihirisha zile mnazozitoa sadaka kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, ni sadaka nzuri mliyoitoa. Na mkizitoa kwa siri mkawapa mafukara, ni bora zaidi kwenu kwa kuwa hivyo ni mbali na ria. Na katika utoaji sadaka pamoja na ikhlasi kuna kusamehewa madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu Anayajua mambo ya ndani; hakuna kinachofichika Kwake katika mambo yenu na Atamlipa kila mtu kwa amali yake

    [272] Si jukumu lako, ewe Mtume, kuwapa makafiri taufiki ya uongofu, lakini Mwenyezi Mungu Anavifungua vifua vya Anaowataka kwa Dini Yake na kuwaafikia kuifuata. Na mali yoyote mnayoyatoa, nafuu yake itawarudia nyinyi wenyewe kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na Waumini hawatoi isipokuwa kwa kutafuta radhi ya Mwenyezi Mungu. Na mali yoyote mnayoyatoa, kwa kumtakasia Mwenyezi Mungu, mtapewa kikamilifu thawabu zake na hamtapunguziwa chochote katika hizo. Katika hii aya pana kuthibitisha sifa ya Uso kwa Mwenyezi Mungu Aliyetakata na kila sifa pungufu (wajh Allah) kwa namna inayonasibiana na Yeye

    [273] Wapeni sadaka zenu mafukara Waislamu ambao hawawezi kusafiri kutafuta riziki, kwa kuwa wameshughulika na jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, ambao huwadhania wao wasiowajua kuwa hawahitaji sadaka kwa kuwa wamejizuia na kuomba.Utawajua kwa alama zao na athari ya uhitaji walionao. Hawaombi kabisa. Na wakiomba, kwa kukosa budi, hawaombi kwa utiriri. Na mali yoyote mnayoyatoa katika njia ya Mwenyezi Mungu, hakuna chochote, katika hayo, chenye kufichika kwa Mwenyezi Mungu.Na Mwenyezi Mungu Atalipa kwayo malipo mengi zaidi na makamilifu zaidi Siku ya Kiyama

    [274] Wale ambao wanatoa mali zao kwa kumridhisha Mwenyezi Mungu, mchana na usiku, kwa siri na kwa dhahiri, watapata malipo yao mbele ya Mola wao, na wala hapana khofu juu yao kuhusu mambo watakayoyakabili Akhera wala hawatakuwa na huzuni juu ya vitu vya kidunia vilivyowapita wasivipate. Sheria hiyo ya Ki- Mungu yenye hekima, ndiyo njia ya Uislamu katika utoaji, yenye kuondoa mahitaji ya mafukara kwa heshima na utu, kusafisha mali ya matajiri na kuhakikisha kusaidiana juu ya wema na ucha-Mungu ili kutaka radhi za Mwenyezi Mungu bila maonevu au kulazimisha

    [275] Wale wenye kuamiliana kwa riba- nayo ni nyongeza juu ya rasilmali-, hawainuki kutoka kwenye makaburi yao Siku ya Mwisho isipokuwa ni kama anavyoinuka yule anayepigwa na Shetani akapatwa na wazimu. Hivo ni kwa kuwa wao walisema kwamba biashara ni kama riba, kwa kuwa yote mawili ni halali na yanapelekea mali kuongezeka. Mwenyezi Mungu Akawakanusha na Akabainisha kwamba Yeye Amehalalisha biashara na Ameharamisha riba. Kwa kuwa katika kuuza na kununua kuna nafuu kwa watu binafsi na kwa jamii na katika riba kuna unyonyaji, hasara na maangamivu. Basi mwenye kumfikia yeye makatazo ya Mwenyezi Mungu ya riba akakomeka, achukue iliyopita kabla ya kumfikia yeye uharamu wake, na hana makosa kwa hilo. Na mambo yake ya siku zake za baadae yako kwa Mwenyezi Mungu. Akiwa ataendelea na toba yake, basi Mwenyezi Mungu Hapotezi malipo ya wenye kufanya wema; na akiwa atarudia kwenye riba, basi kitendo chake hiko baada ya kufikiwa na makatazo ya Mwenyezi Mungu, kitamfanya astahili mateso, kwa kuwa hoja imesimama juu yake. Kwa ajili ya hii Alisema Mwenyezi Mungu, «Basi hao ni watu wa Motoni; Wao ndani yake watakaa milele»

    [276] Mwenyezi Mungu Anaiyondoa riba yote au Anamnyima mlaji riba baraka ya mali yake asinufaike nayo. Na Anazikuza sadaka na kuzifanya ziwe nyingi na Anawaongezea malipo wenye kutoa sadaka maradufu na Anawabarikia katika mali yao. Na Mwenyezi Mungu Hampendi kila mwenye kushikilia kwenye ukafiri wake, mwenye kujihalalishia ulaji riba, mwenye kukolea nadani ya dhambi na haramu na kumuasi Mwenyezi Mungu

    [277] Hakika wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakatenda matendo mema, wakatekeleza Swala kama Alivyoamrisha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakatoa Zaka za mali yao, wana thawabu kubwa zinazowahusu wao mbele ya Mola wao na Mruzuku wao. Na hawatapatwa na woga katika Akhera yao, wala masikitiko juu ya mambo mazuri ya kilimwengu waliyoyakosa

    [278] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na mkamfuata Mtume Wake, muogopeni Mwenyezi Mungu na muache kutaka ziada iliyosalia juu ya rasilmali zenu, ambayo mlistahiki kupata kabla riba haijaharamishwa, iwapo imani yenu ni ya kidhati kimaneno na kivitendo

    [279] Msipokomeka na hilo mlilokatazwa na Mwenyezi Mungu, basi kuweni na yakini ya vita kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na mkirudi kwa Mola wenu na mkaacha kula riba, ni haki yenu mchukue madeni yenu bila ya nyongeza, hamumdhulumu yoyote kwa kuchukua zaidi ya rasilmali zenu wala hamudhulumiwi na yoyote kwa kupunguza kiwango cha pesa mlichokopesha

    [280] Na iwapo mdaiwa hawezi kulipa, mpeni muhula mpaka Mwenyezi Mungu Atakapomfanyia sahali riziki na kuwarudishia mali yenu. Na mkiacha rasilmali yote au baadhi yake mkamuondolea mdaiwa, hilo ni bora zaidi kwenu, mkiwa mnajua fadhila yake ya kuwa hilo ni bora kwenu katika ulimwengu na Akhea

    [281] Na itahadharini, enyi watu, Siku matakaporejeshwa kwa Mwenyezi Mungu, nayo ni Siku ya Kiyama, mtakapo kuorodheshwa kwa Mwenyezi Mungu ili Awahesabu na Amlipe kila mmoja miongoni mwenu kwa alilolitenda la kheri au la shari bila ya kufikiwa na maonevu. Katika aya hii pana ishara kwamba kujiepusha na mapato ya riba yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu, ni kukamilisha Imani na haki za Imani za kutekeleza Swala, kutoa Zaka na kufanya amali njema

    [282] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na mkamfuata Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, mkiamiliana kwa mkopo mpaka muda maalumu, usajilini kwa maandishi ili kuhifadhi mali na kuondoa ugomvi. Na asimame kuandika mtu muaminifu mwenye kudhibiti. Na asilikatae hilo yule mtu aliyetunukiwa na Mwenyezi Mungu ujuzi wa uandishi. Na asimame mdaiwa kufanya imla ya deni iliyo juu yake. Na amchunge Mola wake na asipunguze chochote katika deni iliyo juu yake. Iwapo mdaiwa amezuiwa matumizi kwa ubadhirifu wake na utumiaji wake unaopita kiasi, au akawa ni mdogo au ni mwendawazimu, au hawezi kusema kwa ububu au kwa ulemavu wa kutoweza kusema kabisa, basi na asimamie shughuli ya kufanya imla msimamizi wa mdaiwa kwa niaba yake. Na takeni ushahidi wa Waislamu wawili wanaume, waliobaleghe, wenye akili na waadilifu. Iwapo hawatopatikana wanaume wawili, takeni ushahidi wa mwanamume mmoja na wanawake wawili mnaoridhika na ushahidi wao, ili akisahau mmoja wao (hao wanawake wawili) yule mwengine amkumbushe. Na ni juu ya mashahidi kukubali mwito wa mwenye kuwaita kutoa ushahidi. Na ni juu yao kutoa ushahidi wao wakitakiwa kufanya hivyo. Na msichoke kuisajili deni, iwe ni kubwa au ni ndogo, mpaka wakati wake maalumu wa kulipa. Kwani hilo ni la usawa zaidi katika Sheria ya Mwenyezi Mungu na uongofu Wake, na linasaidia sana kabisa katika kusimamisha ushahidi na kuutekeleza, na liko karibu zaidi na kuondoa shaka kuhusu deni yenyewe, kiasi chake na muda wake. Lakini, iwapo ni jambo la kuuza na kununua, kwa kuchukua bidhaa na kutoa thamani yake papo hapo, basi hakuna haja ya kusajili, na inapendekezwa kushuhudisha hilo ili kuepusha ugomvi na utesi. Na katika mambo ya lazima kwa shahidi na mwandishi ni kutekeleza ushahidi kwa njia zake na usajili kama Alvyoamrisha Mwenyezi Mungu. Na hafai kwa mwenye haki na kwa yule ambaye haki iko juu ya shingo yake kuwadhuru waandishi na mashahidi. Pia, haifai kwa waandishi na mashahidi kuwadhuru wanaohitajia uandishi wao na ushahidi wao. Na mkifanya mliyokatazwa, huko ni kutoka nje ya twaa ya Mwenyezi Mungu; na mwisho mbaya wa kitendo hiko utawafikia. Na muogopeni Mwenyezi Mungu katika maamrisho Yake yote aliyowaamrisha nayo na akawakataza nayo. Na Mwenyezi Mungu Anawajulisha yote yanayotengeneza ulimwengu wenu na Akhera yenu. Na Mwenyezi Mungu kwa kila jambo ni Mjuzi. Hakuna kitu chochote kinachofichika Kwake kuhusu mambo yenu, na Atawalipa kwa hayo

    [283] Na mkiwa muko safarini, na msipate mwenye kuwaandikia, mpatieni yule mwenye haki kitu kiwe ni dhamana ya haki yake hadi mdaiwa atakapolipa deni yake. Na iwapo nyinyi kwa nyinyi mumeaminiana, hapana makosa kuacha kuandika, kushuhudisha na kuweka rahani, na deni itabaki ni amana kwenye shingo ya mdaiwa, ni juu yake kuilipa. Na ni juu yake amchunge Mwenyezi Mungu asimfanyiye hiana mwenzake. Na akikataa mdaiwa deni iliyo juu yake, na ikawa pana mtu aliyekuweko na kushuhudia, huyo itamlazimu kuutoa wazi ushahidi wake. Na mwenye kuuficha ushahudi huu, ni mtu mwenye moyo wa hiana na urongo. Na Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye kuchungulia siri zote, Ndiye Ambaye ujuzi Wake umezunguka mambo yenu yote, na Atawahesabu kwa hayo

    [284] Ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyo baina yake, kwa kuvimiliki, kuvipekesha na kuvijua. Hakuna chochote kinachofichika Kwake. Na chochote mnachokidhihirisha, kati ya viliomo ndani ya nafsi zenu au mnachokificha, Mwenyezi Mungu Anakijua, na Atawahesabu nacho. Atamsamehe Anayemtaka na Atampatiliza Anayemtaka. Na Mwenyezi Mungu ni muweza wa kila kitu. Baadaye Mwenyezi Mungu aliwakirimu Waislamu Akasamehe maneno ya mtu kuiyambia nafsi yake na mawazo ya moyo, yakiwa hayatafuatiwa na maneno au vitendo, kama ilivyothibiti kutoka kwa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [285] Ameamini na kuyakinisha Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, yale aliyoletewa kwa njia ya wahyi kutoka kwa Mola wake. Na ni haki kwake aiyakinishe. Na Waumini pia wameamini na kufanya amali zinazoambatana na Qur’ani Tukufu. Kila mmoja katika wao amemuamini Mwenyezi Mungu kuwa ni Mola na Muabudiwa, Aliyesifika kwa sifa za utukufu na ukamilifu, na kuwa Mwenyezi Mungu Anao Malaika watukufu, na kuwa Yeye Ameteremsha Vitabu na Ametuma Mitume kwa waja Wake. Hatuwaamini, sisi Waumini, baadhi yao na kuwakanusha baadhi yao. Bali tunawaamini wao wote. Na wanasema, Mtume na Waumini, «Tumeusikia, ewe Mola wetu, wahyi uliouleta na tumetii katika yote hayo. Tunatarajia uyasamehe, kwa wema Wako, madhambi yetu. Wewe Ndiye Ambaye Uliyetulea kwa neema Zako Ulizotuneemesha nazo. Kwako, Peke Yako, ndio marejeo yetu na mwisho wetu.»

    [286] Dini ya Mwenyezi Mungu ni sahali, haina uzito ndani yake. Mwenyezi Mungu hawatakii waja Wake wasiyoyaweza. Mwenye kufanya uzuri atapata uzuri, na mwenye kufanya ubaya atapata ubaya. Ewe Mola wetu! Usitutese tukisahau chochote miongoni mwa vitu ulivyotufaradhia au tukikosea kwa kufanya kitu chochote ulichotukataza kukifanya. Ewe Mola wetu! Na usitukalifishe kufanya matendo magumu uliyowakalifisha waliokuwa kabla yetu, miongoni mwa waasi, yakiwa ni mateso kwao. Ewe Mola wetu! Na usitubebeshe tusiyoyaweza ya amri ngumu na mikasa. Na uyafute madhambi yetu, uzisitiri aibu zetu na utufanyiwe wema. Wewe Ndiye Mwenye kuyamiliki mambo yetu na kuyaendesha. Tunusuru juu ya wale waliokataa Dini yako na kuukataa umoja wako na wakamkanusha Nabii wako Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, Na ujaalie mwisho mwema uwe ni wetu juu yao, ulimenguni na Akhera

    Aali Imran

    Surah 3

    [1] «Alif, Lām, Mīm» Yametangulia maelezo kuhusu matamko haya katika mwanzo wa sura ya Al-Baqarah

    [2] Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu. Hapana muabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye, Anayesifika kwa uhai mkamilifu unaonasibiana na utukufu Wake.Anayesimamia kila kitu

    [3] Amekuteremshia wewe, ewe Mtume, Qur’ani kwa haki ambayo haina shaka, inayoshuhudia ukweli wa Vitabu na Mitume kabla yake. Na Aliiteremsha Taurati kwa Musa, amani imshukie, na Injili kwa Īsā, amani imshukie

    [4] kabla ya kuteremka Qur’ani, ili kuwaongoza Wacha-Mungu kwenye Imani na kutengeneza dini yao na dunia yao. Na Aliteremsha yenye kupambanua baina ya haki na batili. Na wale ambao wamekanusha aya za Mwenyezi Mungu zilizoteremshwa, wana adhabu kubwa. Na Mwenyezi Mungu ni Mshindi Asiyeshindwa, ni Mwenye kumtesa anayezikanusha hoja na dalili Zake na kupwekeka Kwake kwa uungu

    [5] Hakika Mwenyezi Mungu, ujuzi Wake umewazunguka viumbe wote. Hakuna kitu chenye kufichika Kwake katika ardhi wala katika mbingu, kiwe kichache au kingi

    [6] Yeye Peke Yake Ndiye Ambaye Anawaumba nyiyi katika zao za mamama zenu kama Atakavyo: wanaume, wanawake, wazuri, wabaya, waovu na wema. Hapana mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye, Mshindi Asiyeshindwa, Mwenye hekima katika amri Zake na uendeshaji mambo Wake

    [7] Yeye Peke Yake Ndiye Ambaye Aliyekuteremshia Qur’ani ambayo katika hiyo kuna aya zenye maana yaliyo wazi; hizo ndizo msingi wa Kitabu ambao unategemewa ikitokea tashwishi, na ambao chochote kinachohalifiana nao kinarudishwa na kuoanishwa nao. Na katika hiyo kuna aya zingine mutashabihat: zinazoleta tashwishi kwa kuwa zinabeba zaidi ya maana mamoja, kwa namna ambayo haiwezekani kujuwa maana iliyokusudiwa isipokuwa kwa kuziambatanisha na muhkam: aya zenye maana yaliyo wazi. Basi wenye nyoyo zenye ugonjwa zilizopotoka, kwa ubaya wa nia zao, huzifuata hizi aya zenye tashwishi peke yake, ili kutia tashwishi kwa watu kwa lengo la kuwapoteza kwa kuzifasiri kuambatana na madhehebu yao yaliyo batili. Ilihali hakuna ajuwaye uhakika wa maana ya aya hizi isipokuwa Mwenyezi Mungu. Na wale waliovama kwenye elimu wanasema, «Tumeiamini hii Qur’ani, kwani yote imetujia kutoka kwa Mola wetu kwa ulimi wa Mtume Wake Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie,.» na wanairudisha yenye tashwishi katika Qur’ani na kuiyoanisha na iliyo wazi yake. Hakika ni kwamba wanaoyafahamu na kuyazingatia maana kama ilivyo sahihi ipasavyo ni wale wenye akili timamu

    [8] Na wanasema, «Ewe Mola wetu, usizipotoe nyoyo zetu na kukuamini Wewe, baada ya kutuneemesha kwa uongofu wa kufuata Dini Yako; na utupe miongoni mwa fadhila zako, rehema yenye kuenea. Kwani Wewe Ndiye Mpaji: Mwingi wa fadhila na vipaji vipaji., unampa unayemtaka bila ya hesabu

    [9] Ewe Mola Wetu, sisi tunakubali na kushuhudia kwamba Wewe utawakusanya watu Siku isiyo na shaka , nayo ni Siku ya Kiyama. Hakika Wewe huendi kinyume na ahadi uliyowapa waja Wako.»

    [10] Hakika wale waliokanusha Dini ya haki na wakaikataa, hayatawafaa wao mali yao wala watoto wao kuwaepushia chochote katika adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwashukia ulimwenguni, wala hayatawakinga wao na adhabu Yake Akhera. Na hawa ndio kuni za Moto Siku ya Kiyama

    [11] Hali ya makafiri katika kukanusha kwao na adhabu itakayowashukia ni kama hali ya jamaa za Fir’aun na wale makafiri waliokuwa kabla yao. Wao walizikanusha aya za Mwenyezi Mungu zilizo wazi, Mwenyezi Mungu akawapatiliza kwa kuwatesa kwa sababu ya kukanusha kwao na kushindana. Na Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kutesa kwa aliyemkufuru Yeye na kuwakanusha Mitume Wake

    [12] Sema, ewe Mtume, kuwaambia makafiri miongoni mwa Mayhudi na wengineo na wale ambao waliudharau ushindi wako katika Badr, «Nyinyi mtashindwa duniani na mtakufa ukafirini, na mtakusanywa mpelekwe kwenye Moto wa Jahanamu, ambao utakuwa ni tandiko la milele kwenu; tandiko baya sana ni hilo.»

    [13] Hakika yalikiwa kwenu, enyi Mayahudi wakaidi, ni ushuhuda mkubwa yale mapambano ya Badr yaliyotukia baina ya makundi mawili: kundi moja linapigana kwa ajili ya Dini ya Mwenyezi Mungu, nalo ni kundi la Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na Masahaba wake, na kundi lingine lenye kumkanusha Mwenyezi Mungu, linapigana kwa ajili ya batili. Ukiwatazama Waumini kwa macho utawaona kuwa ni mara mbili ya ile idadi yao. Na Mwenyezi Mungu Alilifanya hilo kuwa ni sababu ya ushindi wa Waislamu juu yao. Na Mwenyezi Mungu Anawasaidia kwa nusura Yake anaowataka katika waja Wake. Hakika katika tukio hili pana mazingatio makubwa kwa wenye busara ambao wanaongokea kujua hukumu zake na matendo Yake

    [14] Wamepambiwa watu kupenda matamanio ya wanawake na watoto wa kiume na mali mengi ya dhahabu , fedha, farasi wazuri, wanyama wa mifugo miongoni mwa ngamia, ng’ombe na mbuzi na kondoo na ardhi inayotayarishwa kwa kupandwa miti na makulima. Hayo ni mazuri ya uhai wa kilimwengu na pambo lake lenye kutoweka. Na kwa Mwenyezi Mungu kuna marejeo mazuri na thawabu, nayo ni Pepo

    [15] Sema ,ewe Mtume, «Je, ni wape habari ya yaliyo bora kuliko yale waliyopambiwa watu katika maisha haya ya kilimwengu? Wale waliomchunga Mwenyezi Mungu na wakaogopa mateso Yake, watakuwa na Pepo ambazo inapita mito chini ya majumba yake ya fahari na miti yake. Watakaa milele humo. Na watakuwa nao humo wake waliotakasika na hedhi na nifasi na tabia mbaya. Na watakuwa na malipo makubwa zaidi kuliko hayo, nayo ni radhi za Mwenyezi Mungu.» Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuchungulia siri za viumbe wake, ni Mjuzi wa hali zao na atawalipa kwa hayo

    [16] Waja hawa wacha-Mungu huwa wakisema, «Mola wetu, sisi tumekuamini Wewe na tumemfuata Mtume Wako Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, tusamehe madhambi tuliyoyatenda na utuepushe na adhabu ya Moto.»

    [17] Hawa ndio waliosifika kwa subira juu ya kumtii Mwenyezi Mungu, kuepuka maasia na juu ya shida zinazowafikia zilizokadiriwa na Mwenyezi Mungu. Na ndio waliosifika kwa ukweli wa maneno na vitendo na kutii kikamilifu. Na ndio waliosifika kwa utoaji, wa siri na wadhahiri, na kwa kuleta istighfar: kuomba msamaha, katika mwisho wa usiku, kwa kuwa wakati huo unatarajiwa zaidi kukubaliwa amali na kujibiwa dua

    [18] Mwenyezi Mungu Ameshuhudia kuwa Yeye Ndiye Aliyepwekeka kwa uungu. Na Ameambatanisha ushahidi wake na ule wa Malaika na watu wa elimu juu ya kitu kitukufu zaidi chenye kushuhudiwa, nacho ni Tawhīd umoja Wake Aliyetukuka na kusimamia Kwake haki na uadilifu. Hapana Mola isipokuwa Yeye, Aliye Mshindi Ambaye hakuna kitu Atakacho kiwe kikakataa kuwa, Mwenye hekima katikia maneno Yake na vitendo Vyake

    [19] Hakika dini ambayo Mwenyezi Mungu Aliwachagulia waja Wake na Akawatumiliza kwayo Mitume Wake na ambayo Hakubali isipokuwa hiyo ni Uislamu. Nao ni kumnyenyekea Mwenyezi Mungu, Peke Yake, kwa kumtii na kujisalimisha Kwake kwa udhalilifu na kuwafuata Mitume katika yale waliotumilizwa kwayo katika kila kipindi mpaka wakahitimishwa kwa kuja Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ambaye, Hakubali Mwenyezi Mungu dini kutoka kwa yoyote, baada ya kutumilizwa kwake, isipokuwa Uislamu ambao alitumilizwa nao. Na tafauti baina ya Watu wa Kitabu, miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara, iliyowafanya watengane wawe mapote na makundi, haikutokea ela baada ya kuthibiti hoja juu yao kwa kupelekwa Mitume na kuteremshwa Vitabu; hiyo ilitokana na uadui na uhasidi kwa kutafuta ulimwengu.Na yoyote mwenye kuzikanusha aya za Mwenyezi Mungu zilizoteremshwa na alama Zake zenye kujulisha uola Wake na uungu Wake, basi Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa hesabu, na Atawalipa kwa yale waliokuwa wakiyafanya

    [20] Wakijadiliana na wewe, ewe Mtume, Watu wa Kitabu juu ya Tawhīd: kumuwahidisha na kumpwekesha Mwenyezi Mungu, baada ya kuwasimamishia hoja, waambie, «Mimi nimemtakasia Mwenyezi Mungu Peke Yake, si mshirikishi Yeye na yoyote; na pia wale Waumini walionifuata wamemtakasia Mwenyezi Mungu na kumtii.» Na waambie wao na wale washirikina, Waarabu na wengineo, «Mkiingia kwenye Uislamu, basi nyinyi muko kwenye njia ya sawa, uongofu na haki. Na mkirudi nyuma, hesabu yenu iko kwa Mwenyezi Mungu. Mimi sina langu isipokuwa ni kufikisha ujumbe. Na mimi nimewafikishia na nimesimamisha hoja juu yenu.» Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona waja, hakuna chochote chenye kufichika kwake katika mambo yao

    [21] Hakika wale wanaozikanusha dalili zilizo wazi na yale waliokuja nayo Mitume, wakawaua Manabii kwa udhalimu bila haki yoyote, na wakawaua wale ambao wanaamrisha uadilifu na kufuata njia ya Mitume, wape bishara ya adhabu yenye uchungu

    [22] Hao ndio ambao amali zao zilitanguka ulimwenguni na Akhera. Hakuna amali yao yoyote itakubaliwa, na hawatakuwa na yoyote mwenye kuwanusuru kutokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu

    [23] Je, umeona, ewe Mtume, hali ya kustaajabisha zaidi kuliko hali ya hawa Mayahudi, ambao Mwenyezi Mungu Amewapa fungu katika Kitabu wakajua kuwa yale uliyoyaleta ni haki, wanaitwa wafuate yaliyokuja katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu, nacho ni Qur’ani, ili kitoe uamuzi katika mambo waliotafautiana juu yake, kisha wengi wao wanakataa uamuzi huo iwapo haulingani na matamanio yao, kwa kuwa desturi yao ni ni kuipa mgongo haki

    [24] kujiepusha huko na haki, sababu yake ni itikadi mbaya walionayo Watu wa Kitabu kwamba wao hawataadhibiwa isipokuwa siku chache. Itikadi hii iliwapelekea wao wamfanyiye ujasiri Mwenyezi Mungu na waidharau Dini Yake na waendelee na dini yao ya batili ambayo walijidanganya nayo nafsi zao

    [25] Vipi hali zao zitakuwa, Atakapowakusanya Mwenyezi Mungu ili wahesabiwe katika Siku isiyo na shaka kuja kwake, nayo ni Siku ya Kiyama, na kila mmoja apate malipo ya aliyoyatenda, na wao bila kudhulumiwa kitu chochote

    [26] Sema ,ewe Nabii, ukielekea kwa Mola wako kwa dua, «Ewe Ambaye Una ufalme wote, Wewe Ndiye Ambaye Unamtunuku ufalme, mali na umakinifu katika ardhi Umtakaye miongoni mwa waja Wako, na Unauondoa ufalme kutoka kwa Umtakaye. Na Unampa enzi ya ulimwengu na ya Akhera Unayemtaka, na Unamfanya awe na unyonge Unayemtaka. Kheri ipo mikononi mwako. Wewe, Peke Yako, juu ya kila kitu , ni Muweza.» Katika ayah hii pana kuthibitisha sifa ya Mkono kwa Mwenyezi Mungu kwa namna inayonasibiana na Yeye, utakatifu ni Wake

    [27] «Na miongoni mwa dalili za uwezo Wako, ni kuwa Wewe Unautia usiku ndani ya mchana, na Unautia mchana ndani ya uslku, huu ukarefuka na ule ukafupika. Na Unatoa chenye uhai kutoka kwa kilichokufa kisichokuwa na uhai, kama kutoa mazao kutokana na mbegu na kama kumtoa Muumini kutoka kwa kafiri. Na Unatoa kilichokufa kutoka kwa chenye uhai, kama kutoa yai kwenye kuku. Na Unamruzuku Unayemtaka katika waja Wako bila hesabu.»

    [28] Mwenyezi Mungu Anawakataza Waumini kuwafanya makafiri kuwa ni wategemewa, kwa mapenzi na kwa kutaka himaya, badala ya Waumini. Na yoyote mwenye kuwafanya wao ni wategemewa, huyo ameshakuwa mbali na Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu Yuko mbali na yeye. Isipokuwa mkiwa ni madhaifu wenye kuogopa, hapo Mwenyezi Mungu Amewapa ruhusa muwasairi ili kujiepusha na shari lao, mpaka mtakapopata nguvu. Na Mwenyezi Mungu Anawatahadharisha nyinyi na Yeye. basi mcheni na muogopeni. Na Kwake Peke Yake ndio marejeo ya viumbe kwa kuhesabiwa na kulipwa

    [29] Sema, ewe Nabii, Kuwaambia Waumini, «Mkiyaficha yaliyomo ndani ya nyoyo zenu ya kuwafanya makafiri ni wategemewa na wasaidizi au mkiyadhihirisha hayo, hakitafichika chochote katika hayo kwa Mwenyezi Mungu. Kwani ujuzi Wake umezunguka kila kilichoko mbinguni na kilichoko ardhini, na Ana uwezo kamili juu ya kila kitu

    [30] Na katika Siku ya Kiyama, Siku ya Malipo, kila nafsi italikuta jema lolote ililolifanya linaingojea likiwa limeongezwa ili ilipwe nalo. Na pia baya iliolifanya italikuta linaingojea vilevile, hapo itatamani lau ilikuwa baina yake na hilo tendo baya zama zirefu. Basi jitayarisheni kwa Siku hii, na muogope mateso ya Mola Aliye Jabari. Na pamoja na ukali wa mateso Yake, Yeye, Aliyetakata na sifa za upungufu, ni Msifika kwa ukamilifu wa huruma kwa waja

    [31] Sema, ewe Mtume, «Ikiwa nyinyi munampenda Mwenyezi Mungu kikweli, nifuateni mimi na kuniaminini, ndani na nje, ndipo Mwenyezi Mungu Atawapenda na Atawasamehe madhambi yenu.Kwani Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe madhambi ya waja Wake Waumini, ni Mwingi wa rehema kwao.» Aya hii tukufu yamhukumu kila anayedai kumpenda Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na akawa hamfuati Nabii Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kama ipasavyo kufuatwa, na wala hamtii katika maamrisho yake na makatazo yake, kuwa yeye ni mrongo katika madai yake mpaka amfuate Mtume , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kama ipasavyo kufuatwa

    [32] Sema, ewe Mtume, «Mtiini Mwenyezi Mungu kwa kufuata Kitabu Chake, na mtiini Mtume kwa kufuata mwenendo wake wakati wa uhai wake na baada ya kufa kwake.Wakiwa watakupa mgongo na kukamaa kwenye ukafiri na upotevu walionao, wao hawatakuwa wanastahili mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Kwani Mwenyezi Mungu Hawapendi makafiri

    [33] Hakika Mwenyezi Mungu Amemchagua Ādam, Nūḥ, jamii ya Ibrāhīm na jamii ya 'Imrān Akawafanya kuwa ni bora wa watu wa zama zao

    [34] Manabii hawa na Mitume ni mlolongo wa usafi wenye kuungana katika kumtakasa Mwenyezi Munguna, kumpwekesha na kutenda vitendo vinavyoambatana na wahyi Wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasikia maneno ya waja Wake, ni Mjuzi wa vitendo vyao na Atawalipa kwavyo

    [35] kumbuka, ewe Mtume, ilivyokuwa kuhusu mambo ya Maryam na mama yake na mtoto wake 'Īsā, amani imshukie, ili kuwarudi, kwa hayo, wale wanoadai uungu wa 'Īsā au kuwa yeye ni Mwana wa Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, aliposema mke wa 'Imran wakati aliposhika mimba, «Ewe Mola wangu, mimi nimekutakasia kilioko ndani ya tumbo langu kiwe ni chako Peke Yako kwa kutumikia Baitulmaqdis. Basi takabali kutoka kwangu. Hakika Wewe Peke Yako Ndiye Msikizi wa dua yangu, Ndiye Mjuzi wa nia yangu.»

    [36] Mimba yake ilipotimia na akamzaa mtoto wake alisema, «Mola wangu, mimi nimemzaa mwanamke ambaye hafai kwa kutumikia Baitulmaqdis,» Na Mwenyezi Mungu Anajua zaidi kwa alichokizaa na atamjaalia kuwa na jambo kubwa. Mke wa 'Imran aliendelea kusema, «Na Mwanamume niliyemtaka kwa kutumika si kama Mwanamke kwa hilo. Kwa kuwa mwanamume ni mwenye nguvu zaidi wa kutumika na kusimamia utumishi. Na mimi nimempa jina la Maryam. Na mimi nimemlinda kwako, yeye na watoto wake , kutokana na Shetani aliyefukuzwa kwenye rehema Yako.»

    [37] Mwenyezi Mungu Akamjibu maombi yake na Akaikubali nadhiri yake na kuipokea vizuri na Akamsimamia binti yake, Maryam, kwa kumtunza na Akamkuza makuzi mazuri. Mwenyezi Mungu Akamsahilishia kwa kumjaalia Zakaria, amani imshukie, kuwa ni mlezi wake; naye akamuweka mahali pake pa kuabudu. Na alikuwa kila akimjia mahali hapo, anakuta ana chakula kizuri kilichotayarishwa. Akasema, «Ewe Maryam, umepata kutoka wapi chakula hiki kizuri?» Akasema, «Hiyo ni riziki itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu Anamruzuku Anayemtaka miongoni mwa waja Wake bila ya hesabu.»

    [38] Alipoona Zakariyyā vile Mwenyezi Mungu Alivyomkirimu Maryam kwa riziki Yake na fadhila Zake, alielekea kwa Mola wake akisema, «Ewe Mola wangu, nipe kutoka Kwako mtoto mwema mwenye kubarikiwa. Wewe ni Msikizi wa maombi ya anayekuomba.»

    [39] Hapo Malaika walimuita, naye yuko katika hali ya kusimama mbele ya Mwenyezi Mungu katika mahali pake pa Swala, huku anamuomba Yeye, wakamuambia. «Mwenyezi Mungu Anakupa habari yenye kukufurahisha, nayo ni kwamba utaruzukiwa mtoto ambaye jina lake ni Yaḥyā, ambaye atalisadikisha neno la Mwenyezi Mungu, naye ni 'Īsā mwana wa Maryam, amani imshukie. Huyo Yaḥyā atakuwa ni bwana wa kaumu yake, atakuwa na cheo na daraja kubwa, atakuwa ni mwenye kujihifadhi: hatendi madhambi wala hafuati matamanio ya kudhuru na atakuwa ni Nabii miongoni mwa watu wema ambao walifikia kilele cha wema.»

    [40] Zakariyyā akasema akiwa na furaha na kwa kustaajabu, «Mola wangu! Vipi nitakuwa na mtoto hali ya kuwa uzee umenifikia hadi ya kunifikia na mke wangu ni tasa, hazai.? Akasema, «Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu Anavyofanya Anayoyataka katika mambo ya ajabu yanayokwenda kinyume na mambo ya kawaida.»

    [41] Zakariyyā akasema, «Mola wangu, nijaalia alama ambayo itakuwa ni dalili kwangu ya kupata matoto ili nipate kuingiwa na furaha na bashasha.» Akasema, «Alama yako uliyoitaka ni kutoweza kusema na watu kwa siku tatu isipokuwa kwa kuwashiria, pamoja na kuwa wewe uko sawa na mzima. Na katika kipindi hiki, kithirisha kumataja Mola wako na umswaliye katika nyakati za mwisho wa mchana na mwanzo wake

    [42] Na kumbuka, ewe Mtume, pindi Malaika waliposema, «Ewe Maryam, hakika Mola wako Amekuchagua kwa kumtii na Amekusafisha na tabia duni na Amekuchagua kati ya wanawake wa ulimwengu wote katika zama zako

    [43] «Ewe Maryam, Endelea daima kumtii Mola wako, simama kwa utulivu na unyenyekevu na usujudu na urukuu pamoja na wenye kurukuu kwa kumshukuru Mola wako juu ya neema Alizokutunukia.»

    [44] Hizo tulizokusimulia, ewe Mtume, ni miongoni mwa habari za ghaibu alizokujulisha Mwenyezi Mungu kwa njia ya wahyi. Kwani wewe hukuwa pamoja na wao walipotafautiana juu ya nani mwenye haki zaidi na anayefaa kumlea Maryam, ukatokea utesi baina yao, wakapiga kura kwa kuzitupa kalamu zao, ikamwangukia Zakariyyā akapata ushindi wa kumlea

    [45] Kadhalika hukuwako huko, ewe Nabii wa Mwenyezi Mungu, pindi Malaika waliposema, «Ewe Maryam, Mwenyezi Mungu Anakubashiria mtoto ambaye kupatikana kwake kutatokana na neno la Mwenyezi Mungu, yaani Atamwambia, ‘Kuwa,’ na atakuwa, jina lake ni Al-Masīḥ ‘Īsā mwana wa Maryam. Yeye atakuwa na jaha katika ulimwengu na Akhera na atakuwa ni miongoni mwa wenye kukurubishwa kwa Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama

    [46] Na atasema na watu na hali yeye ni mtoto mchanga wa kunyonya kabla hajafikia wakati wa kusema. Na atawaita wao kwa Mwenyezi Mungu, akiwa mkubwa wakati ambapo nguvu zake zitakuwa zimeshikana na ubarobaro wake umekamilika, kwa yale aliyoletewa wahyi na Mwenyezi Mungu. Kusema huku ni kuhusu utume, ulinganizi na uongozi. Na yeye anahesabiwa kuwa ni mmoja wa watu wema na wenye utukufu wa maneno na vitendo

    [47] Maryam alisema kwa kustaajabu, «Vipi mimi nitakuwa na mtoto na sina mume wala si malaya?» Malaika akamuambia, «Tukio hili kwako si jambo lililo mbali kwa Mwenyezi Mungu Muweza Ambaye Anakipatisha chochote anachokitaka kutokana na kisichokuweko. Akitaka kitu chochote kipatikane Anakiambia, «Kuwa,» nacho kikawa

    [48] Na Atamfundisha kuandika, njia ya kuufikia usawa katika kusema na kutenda, Taurati ambayo Mwenyezi Mungu Alimletea Musa, amani imshukie, kwa njia ya wahyi, na Injili ambayo Mwenyezi Mungu Alimteremshia yeye

    [49] Na Atamjaalia awe Mtume kwa Wana wa Isrāīl na atawaambia wao, «Mimi nimewajia na alama kutoka kwa Mola wenu inayoonesha kuwa mimi nimetumilizwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Nayo ni kuwa nitawafanyia kwa udongo kitu chenye mfano wa ndege, nitapuliza ndani yake na kitakuwa ndege wa kikweli kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na nitamponya aliyezaliwa kipofu na mwenye barasi na nitamhuisha aliyekufa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na nitawaambia chakula mnachokula na mnachoweka akiba majumbani mwenu. Hakika katika mambo makubwa haya, ambayo hayako kwenye uwezo wa wanaadamu, pana dalili kwamba mimi ni Nabii wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, iwapo nyinyi ni wenye kuamini hoja za Mwenyezi Mungu na alama Zake, ni wenye kukiri kumpwekesha

    [50] «Na nimewajia nyinyi kuyasadikisha yaliyomo ndani ya Taurati, na ili niawahalalishie, kwa wahyi unaotoka kwa Mwenyezi Mungu, baadhi ya yale ambayo Mwenyezi Mungu Aliwaharamishia, yakiwa ni usahilishaji na huruma kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na nimewajia na hoja kutoka kwa Mola wenu ya ukweli wa ninayowaambia. Basi Mcheni Mwenyezi Mungu na msiende kinyume na amri Yake na mnitii mimi katika yale ninayowafikishia kutoka kwa Mwenyezi Mungu

    [51] «Hakika Mwenyezi Mungu Ambaye ninawalingania nyinyi Kwake Ndiye Peke Yake Mola wangu na Mola wenu, basi muabuduni Yeye. Mimi na nyinyi tuko sawa katika uja wetu na unyenyekevu wetu Kwake. Na hii ndio njia ambayo haina mpeteko.»

    [52] Alipohisi 'Īsā kutoka kwao ukakamavu juu ya ukafuri, aliita kwa watu wake halisi kwa kusema, «Ni nani atakayekuwa na mimi katika kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu.» Wale wasafiwa wa 'Īsā walisema, «Sisi ni wenye kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu na wenye kuilingania, tumemuamini Mwenyezi Mungu na tumekufuata; na ushuhudie, ewe 'Īsā, kuwa sisi tumejisalimisha kwa Mwenyezi Mungu kwa kumpwekesha na kumtii

    [53] «Ewe Mola wetu! Tumeiamini Injili uliyoiteremsha na tumemfuata Mtume Wako 'Īsā, amani imshukie, basi tujaalie ni miongoni mwa waliokutolea ushahidi juu ya umoja Wako na kuwatolea ushahidi Manabii juu ya utume wao.» Nao ni ummah wa Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ambao wanawatolea ushahidi mitume kuwa wao wamewafikishia ummah wao

    [54] Wale waliomkanusha 'Īsā, miongoni mwa Wana wa Isrāīl, walifanya vitimbi kwa kumpangia wenye kumuua. Mwenyezi Mungu akamtoa anayefanana na 'Īsā kwa mtu ambaye aliwaashiria wauaji kwake, wakamshika wakamuua na wakamsulubu wakidhani kuwa ni 'Īsā, amani imshukie. Na Mwenyezi Mungu ni bora wa wenye kufanya vitimbi. Katika haya pana kuthibitisha sifa ya makr (vitimbi) kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa namna inayonasibiana na utukufu Wake na ukamilifu Wake, kwa kuwa ni vitimbi vya haki na ni katika kukabiliana na vitimbi vya wenye vitimbi

    [55] Na vitimbi vya Mwenyezi Mungu kwao ni pale Aliposema Mwenyezi Mungu kumaambia 'Īsā, «Mimi nitakutwaa kutoka kwenye ardhi bila ya kupatikana na baya lolote, nitakuinua mpaka kwangu kwa mwili wako na roho yako, nitakuokoa na watu waliokukanusha na nitawafanya wale waliokufuata wewe, yaani,waliyo kwenye dini yako, na kufuata yale uliyokuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu ya dini na bishara ya Mtume Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wakamuamini Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, baada ya kutumilizwa kwake, wakashikamana na Sheria aliyokuja nayo, wawe na ushindi juu ya wale walioukanusha utume wako hadi Siku ya Kiyama; kisha mwisho wenu nyote mtarudi kwangu Siku ya Hesabu, ili nitoe uamuzi juu ya tafauti mliokuwa nazo kuhusu 'Īsā, amani imshukie

    [56] «Ama wale waliomkanusha al- Masīḥ miongoni mwa Mayahudi, au wakamzidishia sifa miongoni mwa Wanaswara, nitawaadhibu adhabu kali katika ulimwengu: kwa kuuawa, kunyang’anywa mali na kuondolewa ufalme, na katika Akhera kwa Moto; na hawatakuwa na msaidizi mwenye kuwanusuru na kuwaepushia adhabu ya Mwenyezi Mungu.»

    [57] Na ama wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake na wakafanya matendo mema, Mwenyezi Mungu Atawapa thawabu za matendo yao zikiwa kamili zisizopunguzwa. Na Mwenyezi Mungu Hawapendi wenye kujidhulumu kwa ushirikina na ukafiri

    [58] Hayo tuliyokusimulia kuhusu habari ya 'Īsā ni miongoni mwa dalili zilizo wazi za usahihi wa utume wako na usahihi wa Qur’ani yenye hekima inayopambanua baina ya haki na batili; haina shaka wala ubishi

    [59] Hakika mfano wa Mwenyezi Mungu kumuumba 'Īlsa, bila ya baba, ni kama mfano wa Mwenyezi Mungu kumuumba Adam, bila ya baba wala mama. Mwenyezi Mungu Alimuumba kutokana na mchanga wa ardhi kisha Akamwabia, «kuwa kiumbe», akawa. Basi madai ya uungu wa 'Īsā kwa kuwa aliumbwa bila ya baba, ni madai ya urongo. Ādam, amani imshukie, aliumbwa bila ya baba wala mama, na wote wamekubaliana kwamba yeye ni mja miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu

    [60] Haki isiyo na shaka kuhusu mambo ya 'Īsā ni ile iliyokujia, ewe Mtume, kutoka kwa Mola wako. Endelea kwenye yakini yako na juu ya msimamo ulionao wa kuacha uzushi. Na usiwe ni miongoni mwa wenye shaka. Katika haya pana kumtia moyo Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kumtuliza

    [61] Basi yoyote mwenye kujadiliana nawe , ewe Mtume, kuhusu Al-Masīḥ ‘Īsā mwana wa Maryam, baada ya ujuzi uliokufikia juu ya ‘Īsā, amani imshukie, waambie, «Njooni tuwahudhurishe watoto wetu wa kiume na watoto wenu wa kiume, wanawake wetu na wanawake wenu na sisi wenyewe na nyinyi wenyewe, kisha tuelekee kwa Mwenyezi Mungu kwa kumuomba Ayashukishe mateso Yake na laana Yake juu ya warongo katika maneno yao, wenye kukamaa katika upotofu wao.»

    [62] Hakika hili nililokuhadithia, ewe Mtume, kuhusu mambo ya ‘Īsā ndio habari ya kweli isiyo na shaka. Na hakuna muabudiwa anayestahiki ibada isipokuwa ni Mwenyezi Mungu Peke Yake. Na hakika Mwenyezi Mungu Ndiye Mshindi katika ufalme Wake, Ndiye Mwenye hekima katika upelekaji mambo Wake na vitendo Vyake

    [63] Na wakikataa kukuamini na kukufuata, basi wao ndio waharibifu. Na Mwenyezi Mungu Anawajua na Atawalipa kwa hilo

    [64] Sema, ewe Mtume, kuwaambia Watu wa Kitabu miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara, «Njooni kwenye neno la uadilifu na haki tushikamane nalo sote. Nalo ni sisi kuielekeza ibada yetu kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake. Na tusimfanye yoyote kuwa ni mshirika pamoja na Yeye, awe ni sanamu au msalaba au Shetani au kinginecho. Na wala wasiwadhalilikie baadhi yetu watu wengine kwa kuwatii badala ya Mwenyezi Mungu.» Basi wakiukataa mwito huu mzuri, waambieni wao, enyi Waumini, «Kuweni ni mashahidi kwetu kuwa sisi tumejisalimisha kwa Mola wetu na tumenyosha shingo zetu Kwake kwa kukubali kuwa ni waja Wake na kwa kumtakasa.» Na mwito huu kwenye neno la sawa, kama unavyoelekezwa kwa Mayahudi na Wanaswara, unaelekezwa pia kwa wenye mwenendo kama wao

    [65] Enyi watu wa vitabu vilivyoteremshwa, miongoni Mwa Mayahudi na Wanaswara, vipi kila mmoja kati yenu anabisha kwamba Ibrāhīm, amani imshukie, alikuwa kwenye mila yake. Ilhali Taurati na Injili hazikuteremshwa ela baada yake? Kwani hamufahamu upotofu wa maneno yenu kwamba Ibrāhīm alikuwa Myahudi au Mnaswara, na hali mnajua kuwa Uyahudi na Unaswara ulizuka baada ya kufa kwake kwa muda

    [66] Ndio nyinyi enyi hawa, mliomjadili Mtume wa Mwenyezi Mungu , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, juu ya mambo ya dini yenu ambayo muna ujuzi nayo, katika yale yaliyomo ndani ya vitabu vyenu mnayoitakidi usahihi wake. Lakini ni kwa nini nyinyi mnayajadili mambo ya Ibrāhīm ambayo hamuna ujuzi nayo? Na Mwenyezi Mungu Anayajua mambo pamoja na kuwa yamefichika, na nyinyi hamjui

    [67] Ibrāhīm hakuwa ni Myahudi wala Mnaswara, kwa kuwa Uyahudi haukuwa, wala Unaswara, isipokuwa baada yake. Lakini alikuwa mfuasi na mtiifu wa amri ya Mwenyezi Mungu, aliyejisalimisha Kwake, na hakuwa ni miongoni mwa washirikina

    [68] Hakika wenye haki zaidi na Ibrāhīm na wanaohusika naye zaidi ni wale waliomuamini, wakausadiki utume wake na wakaifuata dini yake na huyu Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na waliomuamini yeye.Na Mwenyezi Mungu ni Msaidizi wa wenye kumuamini yeye na kufuata Sheria Yake

    [69] Lilitamani kundi la Mayahudi na Manaswara lau wangaliwapoteza nyinyi, enyi Waislamu, wakawatoa kwenye Uislamu. Wao hawampotezi yoyote isipokuwa nafsi zao na wafuasi wao; na wao hawalielewi hilo wala hawalijui

    [70] Enyi watu wa Taurati na Injili! Vipi nyinyi mnakanusha aya za Mwenyezi Mungu ambazo aliziteremsha kwa Mitume wake katika Vitabu vyenu, na ndani yake muna kuwa Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ndiye Mtume anayengojewa na kuwa aliyowajia nayo ndio haki. Na nyinyi mnashuhudia hilo, lakini mnalikanusha

    [71] Enyi watu wa Taurati na Injili! Kwa nini nyinyi mnachanganya haki iliyo ndani ya vitabu vyenu, kwa yale ya ubatilifu mliyoyapotosha na kuya kwa mikono yenu, na kuzificha kwenu sifa za Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ziliomo ndani ya vitabu hivyo viwili na (kuficha kwenu) kwamba Dini yake ndiyo ya haki, na hali nyinyi mnajua hilo

    [72] Na pote la watu wa Kitabu miongoni mwa Mayahudi lilisema, «Sadikini kilichoteremshwa kwa walioamini mwanzo wa mchana na mkanushe mwisho wake. Huenda wao wakafanya shaka juu ya dini yao na wakaiacha

    [73] «Na msimsadiki kikweli isipokuwa yule aliyefuata dini yenu akawa Myahudi.» Waambie, ewe Mtume, «Uongofu na taufiki ni uongofu wa Mwenyezi- Mungu na taufiki Yake ya kuongoza kwenye Imani sahihi.» Na walisema, «Msiidhihirishe kwa Waislamu elimu mlionayo, wasije wakajifunza kutoka kwenu wakawa sawa na nyinyi katika kuijua na wakawa na ubora juu yenu au wakaichukua kuwa ni hoja kutoka kwa Mola wenu wakawashinda kwayo.» Waambie, ewe Mtume, «Fadhila na vipawa na mambo yote yako mkononi mwa Mwenyezi Mungu na yako chini ya uendeshaji Wake, Anampa Amtakaye miongoni mwa waliomuamini Yeye na Mtume Wake. Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu na ni Mjuzi: Anawaenea, kwa elimu Yake na upaji Wake, viumbe Vyake vyote vinavyostahiki fadhila Zake na neema Zake.»

    [74] Mwenyezi Mungu Anawahusisha Anaowataka katika viumbe Wake kwa kuwapa utume na kuwaongoa kwenye Sheria kamilifu kabisa. Na Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye ihsani na upaji mwingi wenye kuenea

    [75] Na miongoni mwa Watu wa Kitabu, katika Mayahudi, kuna ambaye lau utamuamini kwa mali mengi atakutekelezea bila hiana. Na miongoni mwao kuna ambaye lau utamuamini kwa dinari moja hatakutekelezea, mpaka ufanye juhudi kubwa ya kumfuata. Sababu ya hilo, ni itikadi mbovu inayowafanya wajihalalishie mali ya Waarabu kwa njia ya batili. Na wanasema, «Hatuna dhambi wala kosa kwa kula mali yao, kwa kuwa Mwenyezi Mungu ameyahalalisha kwetu.» Huu ni urongo wa kumzulia Mwenyezi Mungu; wanausema kwa ndimi zao na hali wanajua kuwa wao ni warongo

    [76] Mambo si kama vile walivyodai hawa warongo. Mchaji-Mungu kikweli ni yule aliyetekeleza ahadi aliyomuahidi Mwenyezi Mungu ya kutekeleza amana na kumuamini Yeye na Mitume Wake na akajilazimisha kufuata uongofu Wake na Sharia Yake na akamuogopa Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, kwa kufuata Aliyoamrisha na kujiepusha na Aliyokataza. Na Mwenyezi Mungu Anawapenda wachamungu wenye kujikinga na ushirikina na maasia

    [77] Hakika wale ambao wanabadilisha ahadi ya Mwenyezi Mungu na wasia Wake Aliowausia katika Vitabu Alivowateremshia Mitume wao, kwa kupokea kitu kitwevu miongoni mwa vyombo vya ulimwengu na taka zake, wao hawana fungu la thawabu katika Akhera. Na Mwenyezi Mungu Hatasema na wao maneno ya kuwafurahisha; wala hatawaangalia kwa jicho la huruma Siku ya Kiyama na wala Hatawasafisha kutokana na uchafu wa madhambi na ukafiri. Na watakuwa na adhabu yenye kuumiza

    [78] Miongoni mwa Mayahudi kuna watu wanaoyapotoa maneno na kuyaondoa mahali pake. Na wanayabadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu, ili kuwafanya wasiokuwa wao wadhanie kuwa hayo ni miongoni mwa maneno yaliyoteremshwa katika Taurati, nayo si katika maneno yaliyomo kwenye Taurati kabisa, na wanasema, «Haya yanatoka kwa Mwenyezi Mungu, yameletwa kwa Nabii Wake Mūsā kwa njia ya wahyi.» Nayo hayatoki kwa Mwenyezi Mungu. Na wao, kwa ajili ya ulimwengu wao, wanasema urongo kumzulia Mwenyezi Mungu, na hali wanajua kuwa wao ni warongo

    [79] Haitakiwi kwa binadamu yoyote ateremshiwe kitabu na Mwenyezi Mungu chenye kutoa uamuzi kwa viumbe Wake na achaguliwe kuwa ni Nabii, kisha awaambie watu, «Niabuduni mimi badala ya Mwenyezi Mungu.» Lakini atasema, «Kuweni ni watu wa busara, wenye kuelewa na wajuzi wa wahyi wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, mliokuwa mkiwafundisha wengine na mnaousoma kwa kuuhifadhi, kuujua na kuuelewa..»

    [80] Na haikuwa kwa yoyote katika wao awaamrishe nyinyi kuwafanya Malaika na Mitume ni wola wasiokuwa Mwenyezi Mungu ambao nyinyi mnawaabudu. Je, inaingia akilini, enyi watu, yeye awaamrishe kumkanusha Mwenyezi Mungu baada ya kufuata kwenu amri yake

    [81] kumbuka, ewe Mtume, pindi Alipochukua Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, ahadi ya mkazo kwa Manabii wote kwamba, «Nikiwaletea Kitabu na hekima kisha akaja kwenu mjumbe kutoka kwangu, mwenye kusadikisha vitabu mlivyonavyo, mtamuamini na kumnusuru? Je, mumekiri na kukubali hilo na mumechukua juu yake ahadi yangu ya mkazo?» Wakasema, «Tumekubali hilo.» Akasema, «Kueni mashahidi, baadhi yenu juu ya wengine, na kueni mashahidi kwa hilo juu ya ummah wenu, na mimi ni Mwenye kushuhudia pamoja na nyinyi juu yenu na juu yao. Katika haya pana ahadi nzito Aliyoichukua Mwenyezi Mungu kutoka kwa kila Nabii amuamini Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kuchukua ahadi nzito kutoka kwa ummah wa Manabii wote juu ya hilo

    [82] Basi mwenye kuupa mgongo ulinganizi wa Uislamu baada ya maelezo haya na ahadi hii Aliyoichukuwa Mwenyezi Mungu kutoka kwa Manabii Wake, hao ndio wenye kutoka nje ya dini ya Mwenyezi Mungu na twaa ya Mola wao

    [83] Je, wanataka hawa wenye kutoka nje ya twaa ya Mwenyezi Mungu, miongoni mwa Watu wa Kitabu, dini isiyokuwa dini ya Mwenyezi Mungu nayo ni Uislamu ambao Mwenyezi Mungu Alimtumiliza nao Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, hali ya kuwa wote walioko mbinguni na ardhini wamejisalimisha na kufuata na kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu kwa hiyari, kama walivyo Waumini, na kwa kulazimika wakati wa shida ambapo hilo haliwanufaishi, nao ni makafiri, kama vilivyonyenyekea Kwake viumbe vyote. Na Kwake watarejeshwa Siku ya Marejeo, na alipwe kila mmoja kwa amali yake? Hili ni onyo kutoka kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kwa yoyote, katika viumbe Vyake, atakayerudi Kwake juu ya mila isiyokuwa ya Kiislamu

    [84] Waambie, ewe Mtume, «Tumemuamini Mwenyezi mungu na tumetii. Hatuna Mola isipokuwa Yeye, na hatuna muabudiwa isipokuwa Yeye. Tumeuamini wahyi Aliouteremsha kwetu na ule Aliouteremsha kwa Ibrāhīm aliye rafiki halisi wa Mwenyezi Mungu, na wanawe wawili, Ismā'il na Is’ḥāq, na mwana wa mwanawe,Ya'qūb mwana wa Is’ḥāq, na Asbāṭ: nao ni Manabii waliokuwa katika makabila kumi na mbili wanaotokana na watoto wa Ya'qūb, na wahyi uliopewa Mūsā na ‘Īsā wa Taurati na Injili, na wahyi Aliouteremsha Mwenyezi Mungu kwa Manabii Wake. Tunayaamini hayo yote. Wala hatumbagui yoyote katika wao. Na sisi tunamfuata Mwenyezi Mungu Peke Yake kwa kumtii na kumuabudu, tunakiri Kwake kuwa Yeye Ndiye Mola, Ndiye Mungu na Ndiye wa kuabudiwa

    [85] Na Mwenye kutafuta dini isiyokuwa dini ya Kiislamu, ambayo ni kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu kwa kumpwekesha na kumfuata kwa kumtii na kumdhalilikia, na kwa Mtume wake aliye Nabii wa mwisho Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa kumuamini na kumfuata na kumpenda kwa dhahiri na kwa siri, basi hiyo haitakubaliwa kwake, na yeye Akhera atakuwa ni miongoni mwa wenye kupata hasara ambao walizifanyia ubahili nafsi zao kwa kuzinyima mambo yenye kuzinufaisha

    [86] Vipi Mwenyezi Mungu Atawaafikia, wamuamini Yeye na wamfuate, watu walioukanusha unabii wa Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, baada ya kuuamini na kushuhudia kuwa Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ni mkweli na yale aliyokuja nayo ni ya kweli na zikawajia wao hoja zinazotoka kwa Mwenyezi Mungu na dalili za usahihi wake? Na Mwenyezi Mungu Hawaafikii kwenye haki na usawa watu madhalimu, nao ni wale waliopotoka kwenye haki wakafuata batili, wakachagua ukafiri badala ya Imani

    [87] Madhalimu hao, malipo yao ni kuwa wao watashukiwa na laana ya Mwenyezi Mungu na Malaika na watu wote. Wao wamefukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu

    [88] Ni wenye kukaa milele Motoni; hawataondolewa adhabu kidogo ili wapumzike wala hawatacheleweshewa kwa udhuru wowote watakaoutoa

    [89] Isipokuwa waliorudi kwa Mola wao kwa kutubia kidhati baada ya ukafiri wao na udhalimu wao na wakayatengeneza, kwa toba yao, waliyoyaharibu. Mwenyezi Mungu Ataikubali hiyo toba, kwani Yeye ni Mwingi wa kusamehe madhambi ya waja wake, ni Mwenye huruma kwao

    [90] Hakika wale waliokufuru baada ya kuwa wao wameamini na wakaendelea kwenye ukafiri mpaka kufa, haitakubaliwa toba kutoka kwao mauti yakiwasimamia. Na wao ndio waliopotea njia wakakosa kuifikia

    [91] Hakika wale waliokanusha unabii wa Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na wakafa juu ya kumkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, haitakubaliwa kutoka kwa mmoja wao, Siku ya Kiyama, dhahabu iliyojaa ardhi iwe ni fidia ya nafsi yake kutokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu, lau atajikomboa nayo kikweli. Wao wana adhabu yenye kuumiza; na hawana yoyote wa kuwaokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu

    [92] Hamuwezi kupata Pepo ng’o! mpaka mtoe sadaka katika vile vitu mnavyovipenda. Na chochote mnachokitoa sadaka, kiwe ni kichache au ni kingi, basi Mwenyezi Mungu Anakijua mno na Atamlipa kila mtoaji malipo yanayolingana na kitendo chake

    [93] Vyakula vyote vizuri vilikuwa ni halali kwa wana wa Ya'qūb, amani imshukiye, isipokuwa vile ambavyo Ya’qūb alijiharamishia yeye mwenyewe kwa sababu ya ugonjwa uliompata. Na hayo yalikuwa kabla ya Taurati haijateremshwa. Taurati ilipoteremshwa, Mwenyezi Mungu Aliwaharamishia Wana wa Isrāīl baadhi ya vyakula vilivyokuwa halali kwao. Na hilo ni kwa sababu ya dhuluma zao na uovu wao. Waambie, ewe Mtume, «Ileteni Taurati na muyasome yaliyomo ndani yake iwapo muna hakika ya madai yenu kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha humo uharamu wa aliojiharamishia Ya'qūb nafsi yake, ili mpate kuujua ukweli wa yale yaliyokuja katika Qur’ani ya kwamba Mwenyezi Mungu Hakuwaharamishia Wana wa Isrāīl chochote kabla ya kuteremka Taurati, isipokuwa yale ambayo Ya'qūb alijiharamishia nafsi yake

    [94] Basi yule atakayemzulia Mwenyezi Mungu urongo baada ya kuisoma Taurati na ukweli kuwa wazi, basi hao ndio madhalimu wanaomzulia Mwenyezi Mungu ya batili

    [95] Waambie, ewe Mtume, Mwenyezi Mungu Amesema kweli katika Aliyoyatolea habari na yale ya Sheria Aliyoipitisha. Basi iwapo nyinyi ni wakweli katika mahaba yenu na kujinasibisha kwenu na rafiki halisi wa Mwenyezi Mungu, Ibrāhīm, amani imshukiye, fuateni mila yake Aliyoipitisha Mwenyezi Mungu kupitia kwa ulimi wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie. Kwani hiyo ndiyo haki isiyokuwa na shaka. Na wala hakuwa Ibrāhīm, amani imshukie, ni kati ya wale wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu, katika kumpwekesha na kumuabudu, na yoyote

    [96] Hakika nyumba ya mwanzo iliyojengwa kwa ajili ya kumuabudu Mwenyezi Mungu ni hiyo nyumba ya Mwenyezi Mungu takatifu iliyoko Maka. Na nyumba hiyo imebarikiwa, mema huko huongezwa na rehema huko hushuka. Na katika kuielekea nyumba hiyo kwenye Swala na kuiendea kipindi cha kutekeleza Hija na Umra, pana wema na uongofu kwa watu wote

    [97] Katika Nyumba hii kuna alama waziwazi ya kwamba hiyo ni katika ujenzi wa Ibrāhīm na kwamba Mwenyezi Mungu ameitukuza na kuipa heshima. Kati ya alama hizo ni Maqām ya Ibrāhīm, amani imshukie, nayo ni lile jiwe ambalo alikuwa akisimama juu yake wakati alipokuwa akiziinua nguzo za Alkaba, yeye na mwanawe Ismā'īl. Na yoyote mwenye kuingia Nyumba hii atapata amani ya nafsi yake, hapana yoyote atakayemkusudia kwa uovu. Na Mwenyezi Mungu Amewajibisha kwa mwenye uwezo katika watu, popote atakapokuwa kuiendea nyumba hii ili kutekeleza matendo ya Hija. Na yoyote mwenye kuikanusha faradhi ya Hija, basi huyo amekufuru. Na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi naye, Hana haja ya hija yake wala amali yake na wala Hana haja na viumbe vyake vyote

    [98] Sema, ewe Mtume, kuwaambia waliepewa vitabu kati ya Mayahudi na Wanaswara, «Kwa nini mnazikanusha hoja za Mwenyezi Mungu zinazojulisha kwamba dini ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu na mnayakanusha yaliyomo kwenye vitabu vyenu miongoni mwa dalili na hoja juu ya hilo hali ya kuwa nyinyi mnajua? Na Mwenyezi Mungu ni shahidi juu ya kitendo chenu mnachokifanya.» Katika haya, pana makemeo na ahadi ya adhabu kwao

    [99] Sema, ewe Mtume, kuwaambia Mayahudi na Wanaswara, «Mbona mnamzuia kuingia katika Uislamu yule mtu atakaye hivyo na mnamtakia upotofu na kupinduka kwenye lengo na muelekeo wa kisawa, na nyinyi mnajua kwamba niliyokuja nayo ndiyo haki?» Basi, Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika kwa mnayoyatenda, na Atawalipa kwa hayo

    [100] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazitumia Sheria Zake kwa kuzifuata, iwapo mtalitii kundi la Mayahudi na Wanaswara, miongoni mwa wale ambao Mwenyezi Mungu Amewapa Taurati na Injili, watawapoteza na watawatia shaka katika dini yenu, ili mupate kurudi nyuma na kuikanusha haki baada ya kuwa mlikuwa waumini wa haki hiyo, basi msiwaamini juu ya dini yenu wala msiwakubalie rai yoyote au shauri

    [101] Na vipi mtamkufuru Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, ilhali mnasomewa aya za Qur’ani, na Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, anazifikisha aya hizo kwenu? Na yoyote atakayetegemea kwa Mwenyezi Mungu, akashikamana na Qur’ani na mafundisho ya Mtume (Sunnah), basi huyo ameafikiwa kufuata njia iliyo wazi na mpango uliolingana sawa

    [102] Enyi ambao mumemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata Sheria Zake, muogopeni Mwenyezi Mungu kwa namna inavyopasa mumuogope. Nako ni Atiiwe wala Asiasiwe, Ashukuriwe wala asikufuriwe na Akumbukwe wala Asisahauliwe. Na dumuni katika kushikamana na Uislamu wenu mpaka mwisho wa uhai wenu, ili mkutane na Mwenyezi Mungu na nyinyi muko katika hali hiyo

    [103] Shikamaneni nyote na Kitabu cha Mola wenu na uongofu wa Mtume wenu, wala msitende ambayo yatapelekea kutengana kwenu. Na ikumbukeni neema kubwa ambayo Mwenyezi Mungu Amewaneemesha nayo, pindi mlipokuwa, enyi Waumini, kabla ya Uislamu ni maadui, Mwenyezi Mungu Akazikusanya nyoyo zenu juu ya kumpenda Yeye na kumpenda Mtume Wake, na akatia ndani ya nyoyo zenu mahaba ya kupendana wenyewe kwa wenyewe, hapo mkawa, kwa fadhila Zake, ni ndugu mpedanao. Na mlikuwa kwenye ukingo wa moto wa Jahanamu, Mwenyezi Mungu Akawaongoza kwa Uislamu na Akawaokoa na Moto. Na kama Mwenyezi Mungu Alivyowafunulia wazi alama za imani iliyo sahihi, hivyo hivyo Anawabainishia yote yale ambayo ndani yake muna kutengenea kwenu, mpate kuongoka kweye njia ya uongofu na mpate kuiandama ili msipotee mkaiepuka

    [104] Na kiweko miongoni mwenu, enyi Waumini, kikundi kitakacholingania katika kheri, kiamrishe mema, nayo ni yale yanayojulikana uzuri wake kisheria na kiakili, na kikataze maovu, nayo ni yale yanayojulikana uovu wake kisheria na kiakili. Na hao ndio watakaofaulu kupata Pepo zenye neema

    [105] Na wala msiwe, enyi Waumini, kama waliopewa vitabu, ambao ulizuka uadui kati yao na kuchukiana, wakatengana makundi na vyama mbalimbali na wakatafautiana kwenye misingi ya dini yao baada ya haki kuwa wazi kwao. Na hao wanastahili adhabu kubwa iumizayo

    [106] Siku ya Kiyama zitakuwa nyeupe nyuso za watu wema ambao wamemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafuata amri Yake; na zitakuwa nyeusi nyuso za watu waovu kati ya wale waliomkanusha Mtume Wake na wakaasi amri Yake. Basi wale ambao nyuso zao zitakuwa nyeusi wataambiwa kwa kulaumiwa, «Je, mumekufuru baada ya kuamini kwenu, mkachagua ukafiri mkaacha Imani? Basi ionjeni adhabu kwa sababu ya ukafiri wenu.»

    [107] Ama wale ambao nyuso zao zitakuwa nyeupe kwa mn’garo wa neema na kwa yale mema ambayo walipewa bishara nayo, wao watakuwa katika Pepo ya Mwenyezi Mungu na starehe zake. Wao watasalia humo, hawatatoka humo milele

    [108] Hizi ni aya za Mwenyezi Mungu na hoja Zake zenye kung’ara, tunakusomea na kukusimulia, ewe Mtume, kwa ukweli na yakini. Na Mwenyezi Mungu Hakuwa ni mweye kumdhulumu yoyote katika viumbe Wake wala si mwenye kupunguza chochote katika vitendo vyao, kwani Yeye ni Hakimu Mwenye uadilifu Asiyedhulumu

    [109] Na ni Vyake, Yeye Mwenyezi Mungu Peke Yake, vyote vilivyo mbinguni na vilivyo ardhini, ni milki Yake Pekee kwa kuviumba na kuvisimamia. Na marejeo ya viumbe wote ni Kwake Yeye Peke Yake, na Atamlipa kila mmoja kwa kadiri anayostahiki

    [110] Nyinyi, enyi uma wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ni bora wa ummah na ni watu wenye manufaa zaidi kwa watu, mnaamrisha mema, nayo ni yale yanayofahamika uzuri wake kisheria na kiakili, na mnakataza maovu , nayo ni yale yanayoeleweka ubaya wake kisheria na kiakili, na mnamuamini Mwenyezi Mungu kikweli-kweli imani inayotiliwa nguvu na vitendo. Na lau kama Mayahudi na Wanaswara waliopewa Vitabu wangalimuamini Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na yale aliyowajia nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu kama mlivyoamini nyinyi, lingekuwa hilo ni bora kwao dunianina Akhera. Katiika hao wako Waumini waukubalio ujumbe wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wanaoufuata kivitendo ujumbe huo, nao ni wachache. Na wengi wao ni watokaji nje ya dini ya Mwenyezi Mungu na twaa Yake

    [111] Hawatawadhuru nyinyi hawa watu waovu, miongoni mwa watu waliopewa Vitabu, isipokuwa kile kitakachoyaudhi masikizi yenu cha matamshi ya ushirikina na ukafiri na mengineyo. Na wakiwapiga vita, watashindwa na watakimbia hali ya kuwapa mgongo, kisha hawatapata ushindi juu yenu kwa hali yoyote

    [112] Amejaalia Mwenyezi Mungu utwevu na unyonge kuwa ni jambo lenye kuambatana nao Mayahudi na wala haliwaepuki. Kwa hivyo, wao daima ni madhalili wenye kudharauliwa popote waliopo, isipokuwa watakapokuwa na mafungamano na Mwenyezi Mungu na makubaliano na watu ambayo kwayo watajiwekea usalama wa nafsi zao na mali zao. Hayo ndiyo mapatano ya kujidhamini kwao na kujilazimisha kwao kufuata hukumu za Uislamu. Na wamerudi nyuma wakiwa wamepata hasira za Mwenyezi Mungu zilizowastahili. Na wamepigwa na unyonge na umasikini. Kwa hivyo, humuoni Myahudi isipokuwa utamkuta ameshukiwa na hofu na babaiko kwa kuwaogopa Waumini. Hilo ndilo Alilowajaalia Mwenyezi Mungu kwa sababu ya kumkufuru kwao Mwenyezi Mungu, kukeuka kwao mipaka Yake na kuwaua kwao Manabii, kwa udhalimu na uonevu. Na hakuna lolote lililowafanya wao wawe majasiri wa kuyatenda haya isipokuwa ni kule kufanya kwao maasia na kukiuka kwao mipaka ya Mwenyezi Mungu

    [113] Waliopewa Vitabu hawako sawa: kati yao liko kundi lifuatalo njia iliyolingana sawa juu ya amri ya Mwenyezi Mungu, lenye kumuamini Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na ambalo watu wake wanasimama usiku wakizisoma aya za Qur’ani tukufu na wakielekea kwa Mwenyezi Mungu kwa kumuomba katika Swala zao

    [114] Wanamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, wanaamrisha mambo ya kheri yote na wanakataza aina zote za shari na wanakimbilia kufanya mema. Hao ni miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu wema

    [115] Na kitendo chochote, kichache au kingi, kati ya vitendo vyema yatakayofanywa na kikundi hiki kilichoamini, hakitapotea mbele ya Mwenyezi Mungu. Bali watashukuriwa na watapewa malipo yake. Mwenyezi Mungu Anawajua zaidi wacha-Mungu ambao wametenda mema na wakajitenga na yaliyoharamishwa kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu na kutaka thawabu Zake

    [116] Hakikia wale waliozikufuru aya za Mwenyezi Mungu na wakawakanusha Mitume Wake, mali yao wala watoto wao havitawatetea wao kivyovyote wasipatwe na adhabu ya Mwenyezi Mungu, duniani wala Akhera. Hao ni watu wa Motoni watakaodumu humo pasi na kutoka

    [117] Mfano wa wanachokitoa makafiri, katika mambo ya kheri, katiika maisha haya ya ulimenguni na thawabu wanazozitumaini, ni mfano wa upepo ulio na baridi kali uliovuma juu ya mashamba ya watu waliokuwa wanangojea kwa hamu matokeo mema ya upepo huo. Na kwa sababu ya madhambi yao, upepo huo haukubakisha chochote. Na makafiri hawa, hawatapata thawabu huko Akhera. Na Mwenyezi Mungu hatakuwa Amewadhulumu kwa hilo, lakini ni wao walijidhulumu nafsi zao kwa ukafiri wao na kuasi kwao

    [118] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata Sheria Zake kivitendo, msiwafanye makafiri kuwa ni wategemewa, kinyume cha Waumini, mkawa mnawapa siri zenu. Kwani wao hawakomi kuziharibu hali zenu, na wanayafurahia madhara na maovu yanayowafika. Zimedhihiri chuki nyingi katika maneno yao. Na yanayofichwa na nyoyo zao ya uadui kwenu ni makubwa zaidi na ni mazito. Kwa hakika, tushawaelezea nyinyi alama na hoja za uovu wao ili mpate kuwaidhika na muwe na tahadhari, iwapo mnayatia akilini mawaidha ya Mwenyezi Mungu, amri Zake na makatazo Yake

    [119] Huu ndio ushahidi wa makosa yenu kwa kuwapenda wao. Nyinyi mnawapenda na mnawafanyia wema, na wao hawawapendi. Na wanawabebea nyinyi uadui na chuki, ilhali nyinyi mnaviamini vitabu vyote vlivyoteremshwa, kikiwemo kitabu chao, na wao hawakiamini kitabu chenu. Basi vipi mtawapenda? Na wanapokutana na nyinyi wanasema kinafiki, «Tumeamini na tumesadiki.» Na wanapokuwa faragha, wenyewe kwa wenyewe, yaonekena wana kero na masikitiko. Hapo huwa wakiziuma ncha za vidole vyao, kutokana na hasira kali walionayo juu ya mshikamano wa Waislamu, kuwa neno lao ni moja, kuwa Uislamu umepata nguvu na kuwa wao wamekuwa wanyonge kwa sababu ya kupata nguvu Uislamu. Waambie, ewe Mtume, «Kufeni kwa hasira zenu kali mlizonazo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona yanayofichwa ndani ya vifua na Atamlipa kila mmoja kwa aliyoyatanguliza ya kheri au ya shari.»

    [120] Na miongoni mwa uadui wa watu hawa ni kwamba nyinyi, enyi Waumini, mpatwapo na jambo jema la ushindi au ngawira, wao hupatwa na butwaa na huzuni; iwapo mtapatwa na maudhi ya kushindwa au upungufu wa mali, watu na matunda, wao hulifurahia hilo. Na mkiwa na subira juu ya yaliyowafika na mkamuogopa Mwenyezi Mungu katika yale Aliyowaamrisha na Akawakataza nayo, hautawadhuru udhia wa vitimbi vyao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyazunguka yote wanayoyafanya hao makafiri ya uharibifu na Atawalipa kwayo

    [121] Na kumbuka,ewe Mtume, pindi ulipotoka nyumbani kwako, ukiwa umevaa mavazi ya vita, huku wazipanga safu za Masahaba wako, na unamuweka kila mmoja mahali pake ili kukutana na washirikina katika vita vya Uhud. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuzisikia kauli zenu, ni Mwenye kuvijua vitendo vyenu

    [122] Kumbuka, ewe Mtume, yale mambo yaliyowahusu kina Banū Salimah na Banū Ḥārithah wakati walipowaza kurudi nyuma, wao na kiongozi wao, mnafiki Abdullāh bin Ubayy bin Salūl, kwa kuogopa kukutana na adui. Lakini Mwenyezi Mungu Aliwalinda na Akawahifadhi wakaenda pamoja na wewe wakimtegemea Mwenyezi Mungu. Na kwa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, na wajitegemeze Waumini

    [123] Hakika Mwenyezi Mungu Aliwanusuru nyinyi, enyi Waumini, katika Badr juu ya maadui zenu washirikina pamoja na uchache wa idadi yenu na vifaa vyenu. Kwa hivyo, muogopeni Mwenyezi Mungu kwa kutekeleza amri Zake na kujiepusha na makatazo Yake, ili mpate kumshukuria neema Zake

    [124] Kumbuka, ewe Nabii, yale yaliyowahusu Masahaba wako kwenye vita vya Badr pindi walipoona uzito katika nafsi zao kwa kuwa Makureshi wamepata msaada wa kivita, na Sisi tukakuletea Wahyi uwaambie, «Kwani hauwatoshi msaada wa Mola wenu wa kuwaletea Malaika elfu tatu walioteremshwa kutoka mbinguni mpaka kwenye sehemu ya vita wakawa wanawapa moyo na wanapigana pamoja na nyinyi?»

    [125] Ndio, unawatosha nyinyi msaada huu. Na kuna bishara nyingine kwenu, iwapo mtakuwa na subira ya kupambana na maadui zenu na mkamuogopa Mwenyezi Mungu kwa kuyatenda Aliyowamrisha na kuyaepuka Aliyowakataza. Na watakuja makafiri wa Maka kwa haraka kupigana na nyinyi, wakidhani kwamba wao watawamaliza. Mwenyezi Mungu Atawapa nyinyi msaada wa Malaika elfu tano wakiwa wamejitia alama zilizo wazi, wao na farasi wao

    [126] Na Mwenyezi Mungu Hakuuleta msaada huu wa Malaika isipokuwa ni kwa ajili ya kuwapa bishara kwa msaada huo na ili nyoyo zenu zitulie na ziwe nzuri kwa ahadi ya Mwenyezi Mungu kwenu. Na msaada wa hakika unatoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye kushinda Ambaye Hashindwi, Mwenye hekima katika uendeshaji mambo Wake na matendo Yake

    [127] Na ilikuwa nusura ya Mwenyezi Mungu katika vita vya Badr ni kwa ajili Apate kukiangamiza kikundi cha makafiri kwa kuuawa na yule atakayeokoka na kifo kati yao, basi atarudi akiwa na huzuni, upetwe na dhiki za nafsi yake na unaonekana kwake utwevu na aibu

    [128] Huna, ewe Mtume, katika mambo ya waja chochote kile. Bali mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Peke Yake, Asiyekuwa na mshirika. Na huenda, baadhi ya hawa waliokupiga vita, vifua vyao vikaufungukia Uislamu, wakasilimu na Mwenyezi Mungu Akazikubali toba zao. Na yule atakayesalia katika ukafiri wake, Mwenyezi Mungu Atamuadhibu duniani na Akhera kwa sababu ya udhalimu wake na uadui wake

    [129] Ni vya Mwenyezi Mungu Pekee vilioko mbinguni na vilioko ardhini; Anamsamehe Amtakaye kati ya waja Wake kwa rehema Zake na Anamuadhibu Amtakaye kwa uadilifu Wake. Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasamehe madhambi ya waja Wake na ni Mwenye huruma kwao

    [130] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata Sheria Zake kivitendo, tahadharini na aina zote za riba na msichukue katika mkopo zaidi ya rasilmali zenu, hata kama ni kidogo. Basi itakuwaje iwapo ziada hiyo itaongezeka kila ufikapo muda wa kulipa deni? Na muogopeni Mwenyezi Mungu kwa kujilazimisha kufuata Sheria Zake ili mpate kufaulu duniani na Akhera

    [131] Na jiwekeeni kizuizi baina yenu na moto ambao umeandaliwa makafiri

    [132] Na mtiini Mwenyezi Mungu, enyi waumini, katika yale Aliyowaamrisha kwayo ya twaa nay ale Aliyowakataza nayo ya kula riba na mengineyo. Na mtiini Mtume ili mpate kurehemewa na msiiadhibiwe

    [133] Na kimbilieni, kwa kumtii kwenu Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ili kupata msamaha mkubwa utokao kwa Mola wenu na mpate Pepo kunjufu, upana wake ni sawa na mbingu na ardhi, Ameiandaa Mweyezi Mungu kwa wachamungu

    [134] Wale ambao wanatoa mali yao katika hali ya wepesi na uzito, na wanaozuia hasira zilizo ndani ya nafsi zao kwa kusubiri, na wanaowasamehe waliowadhulumu wanapokuwa na uwezo. Huu ndio wema ambao Mwenyezi Mungu Anawapenda wenye kuwa nao

    [135] Na wale ambao wakitenda dhambi kubwa au wakizidhulumu nafsi zao kwa kutenda dhambi chini ya hizo, wanaikumbuka ahadi ya Mwenyezi Mungu ya malipo mema kwa wanaomtii na malipo mabaya kwa wanaomuasi na wanaelekea kwa Mola wao hali ya kutubia wakawa wanamuomba Awasamehe madhambi yao na wakawa wana yakini kwamba hapana anayasamehe madhambi isipokuwa Mwenyezi Mungu. Na wao kwa sababu hiyo hawaendelei kwenye maasia, na wao wanajua kwamba wakitubia Mwenyezi Mungu Atawakubalia toba yao

    [136] Hao waliosifiwa kwa sifa hizo, malipo yao ni kwamba Mwenyezi Mungu Atayasitiri madhambi yao na watapata mabustani ya Peponi ambayo maji tamu yatakuwa yanapita chini ya miti yake na majumba yake ya fahari, ilhali ya kukaa humo milele; hawatotoka humo kamwe. Na malipo bora ya wenye kutenda mema ni msamaha na Pepo

    [137] Mwenyezi Mungu Anawazungumzia Waumini walipopatwa na mikasa siku ya vita vya Uhud kwa kuwaliwaza kwamba wamepita kabla yao ummah wengi ambao waumini kati yao walitahiniwa kwa kupigana na makafiri na ukawa ushindi ni wao. Basi, tembeeni katika ardhi mkizingatia yale yaliyowafika wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu na na Mtume Wake

    [138] Hii Qur’ani ni ufafanuzi uliyo wazi na ni uongozi kwenye njia ya haki na ni ukumbusho ambao nyoyo za wachamungu zainyenyekea. Nao (hao wachamungu) ni wale wanaomuogopa Mwenyezi Mungu. Wamehusishwa nayo (hiyo Qur’ani kuwa nyoyo zao zinainyenyekea na kuikubali) kwa kuwa wao ndio wanaofaidika nayo, si wengine

    [139] Wala msidhoofike, enyi Waumini, kupigana na maadui wenu, wala msihuzunike kwa yaliyowapata huko Uhud. Na nyinyi ndio washindi na mwisho mwema ni wenu iwapo mtamuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mtafuata Sheria Zake

    [140] Iwapo yatawapata, enyi Waumini, majaraha au mauaji kwenye vita vya Uḥud, na mkahuzunika kwa hilo, washirikina pia walipatwa na majaraha na mauaji kama hayo katika vita vya Badr. Hizo ni siku Mwenyezi Mungu huzigeuza kati ya watu: wakati mwengine kushinda na wakati mwengine kushindwa. Kwani katika hayo kuna hekima, mpaka yadhihiri yale Aliyoyajua Mwenyezi Mungu hapo azal (kale isiyokuwa na mwanzo), ili Mwenyezi Mungu Ampambanue aliyekuwa mkweli wa Imani na asiyekuwa mkweli, na ili Awakirimu watu miongoni mwenu kwa kuwafanya wafe mashahidi. Na Mwenyezi Mungu Hawapendi waliozidhulumu nafsi zao na wakakaa kwa kuacha kupigana katika njia Yake

    [141] Na kushindwa huku kuliotokea katika vita vya Uhud kulikuwa ni kuwafanyia mtihani, kuwasafisha Waumini, kuwatakasa na wanafiki na ni maangamivu kwa makafiri

    [142] Enyi Maswahaba wa Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie! Kwani mnadhani kwamba mtaingia Peponi na bado hamjapewa mitihani ya vita na mambo mazito? Haitapatikana kwenu kuingia Peponi tu, hivi hivi, mpaka mjaribiwe na Awajuwe Mwenyezi Mungu, ujuzi ulio wazi kwa viumbe, wale wapiganao jihadi kati yenu katika njia Yake na wenye subira ya kupambana na maadui

    [143] Na kwa hakika mlikuwa, enyi Waumini, kabla ya vita vya Uhud mnatamani kukutana na maadui zenu, ili mpate utukufu wa jihadi na kufa mashahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu ambao walibahatika nao ndugu zenu kwenye vita vya Badr. Basi hilo ndilo, Iimeshapatikana kwenu, mlilolitamani na mkaliomba. Basi jitokezeni mpigane na msubirishane

    [144] Hakuwa Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ni kiumbe aina nyingine, isipokuwa yeye ni Mtume wa jinsi ya Mitume wengine waliokuweko kabla yake, afikisha ujumbe wa Mola wake. Basi iwapo atakufa, kwa kumalizika muda wake, au atauawa, kama walivyoeneza uvumi maadui, kwani mtarudi nyuma na kuacha dini yenu na kuyaacha aliyowaletea Mtume wenu? Basi yoyote miongoni mwenu atakayerudi nyuma akaiacha dini yake, yeye hatamdhuru Mwenyezi Mungu chochote, bali ataidhuru nafsi yake madhara makubwa. Ama atakayekuwa na msimamo imara juu ya Imani yake na akamshukuru Mola wake juu ya neema ya Uislamu, hakika Mwenyezi Mungu Atamlipa malipo mazuri kabisa

    [145] Hakuna yoyote atakayekufa isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na makadirio Yake na mpaka aufikishe muda ambao Mwenyezi Mungu Amempangia. Hayo ni maandishi yaliyopangiwa wakati. Na yoyote ambaye kwa vitendo vyake anataka manufaa ya duniani, tutampa tulichomgawia cha riziki, na hatakuwa na fungu lolote kesho Akhera. Na yoyote ambaye anataka kwa vitendo vyake malipo ya Mwenyezi Mungu huko Akhera , tutampa kile alichokitaka na tutampa malipo yake kamili pamoja na fungu lake duniani la riziki alilogawiwa. Kwani huyu kwa utiifu wake na jihadi yake ametushukuru; na wenye kushukuru tutawalipa mema

    [146] Wengi kati ya Mitume waliotangulia, walipigana pamoja nao makundi mengi ya watu waliowafuata. Hawakudhoofika kwa yale yaliyowapata ya majaraha au mauaji, kwani hayo yalikuwa katika njia ya Mola wao. Wala hawakulemewa wala hawakumnyenyekea adui yao, bali walisubiri kwa yaliyowapata. Na Mwenyezi Mungu Anawapenda wenye kusubiri

    [147] Na halikuwa neno la hawa wenye kusubiri isipokuwa ni kusema, «Ewe Mola wetu! Tusamehe madhambi yetu na yaliyotokea kwetu ya kuruka mipaka katika mambo ya dini yetu na uzithibitishe nyayo zetu, tusipate kukimbia tunapopigana na adui yetu na utunusuru na yule anayepinga umoja wako na unabii wa Manabii wako

    [148] Basi Aliwapa Mwenyezi Mungu, wale wenye kusubiri, malipo yao duniani kwa kuwanusuru na maadui zao, kwa kuwafanya wakae kwa utulivu katika ardhi na kwa malipo mema yaliyo makubwa Akhera, nayo ni mabustani ya Peponi yaliyojaa neema. Na Mwenyezi Mungu Anampenda kila mtenda wema katika kumuabudu Mola wake na kuamiliana kwake na viumbe Wake

    [149] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata sheria Zake kivitendo! Iwapo mtawatii walioukanusha uungu wangu na wasiwaamini Mitume wangu, miongoni mwa Mayahudi, Wanaswara, wanafiki na washirikina, katika yale wanayowaamrisha nyinyi nayo na wanayowakataza nyinyi nayo, watawapoteza njia ya haki na mtaritadi muache dini yenu na mrudi na hasara iliyo wazi na maangamivu ya kikweli

    [150] Hakika wao hawatawanusuru nyinyi; bali Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye kuwanusuru na Ndiye Mnusuru bora Asiyehitajia nusura ya mtu Mwengine

    [151] Tutatia fazaa na hofu kubwa katika nyoyo za waliokufuru, kwa sababu ya kumshirikisha kwao Mwenyezi Mungu na wale wanaodaiwa kuwa ni waungu. Wao hawana dalili au hoja kuwa waungu hao wana haki ya kuabudiwa pamoja na Mwenyezi Mungu. Basi hali yao hapa duniani ni papatiko na babaiko kwa kuwaogopa Waumini. Ama mahali pao watakaposhukia Akhera ni Moto. Na hili ni kwa sababu ya udhalimu wao na uadui wao. Na makao maovu kwao ni makao haya

    [152] Na kwa hakika Aliwahakikishia nyinyi Mwenyezi Mungu yale Aliyowaahidi ya kuwanusuru pindi mlipokuwa mnawaua makafiri katika vita vya uhud kwa idhini Yake Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. Mpaka mlipokuwa waoga, mkawa madhaifu wa kupigana na mkatafautiana: je, mtasalia kwenye sehemu zenu za kivita au mtaziacha, ili mkusanye ngawira pamoja na wanaokusanya? Na mkaiasi amri ya Mtume wenu alipowaamrisha msiondoke kwenye sehemu zenu kwa vyovyote vile. Hapo ndipo pigo la kushindwa likawapata baada ya kuwaonesha mnayoyapenda ya ushindi, na ikadhihirika kuwa kati yenu kuna wanaotaka ngawira na kati yenu kuna wanaotaka Akhera na malipo yake. Kisha Mwenyezi Mungu Aliziepusha nyuso zenu na maadui wenu ili awape mtihani. Kwa hakika Aliyajua Mwenyezi Mungu majuto yenu na toba yenu, ndipo Akawasamehe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kubwa kwa Waumini

    [153] Kumbukeni, enyi maswahaba wa Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, hali zenu zilivyokuwa, mlipokuwa mnalipanda jabali mkiwakimbia maadui zenu, wala hamgeuki kumwangalia yoyote kwa sababu ya yale yaliyowafikia ya babaiko, kuogopa na fazaa. Na huku Mtume wa Mwenyezi Mungu , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, amekita kwenye uwanja wa vita, anawaita nyuma yenu kwa kuwaambia, «Njooni kwangu, enyi waja wa Mwenyezi Mungu,» hali ya kuwa nyinyi hamsikii wala hamuangalii. Hapo yakawa malipo yenu ni kupatwa na machungu, dhiki na kero. Aliyafanya hayo Mwenyezi Mungu ili msihuzunike kwa mliyoyakosa ya ushindi na ngawira wala yaliyowafikia ya kuingiwa na kicho na kushindwa. Mwenyezi Mungu ni Mtambuzi wa matendo yenu yote; hakuna chochote katika hayo kinachofichika Kwake

    [154] Kisha ikawa ni katika rehema ya Mwenyezi Mungu kwa waumini waliomtakasia nia kwamba Aliingiza kwenye nyoyo zao , baada ya kero na usumbufu uliowafika, utulivu na Imani thabiti kuhusu ahadi ya Mwenyezi Mungu kwao. Miongoni mwa alama za utulivu huo ni usingizi uliolifinika kundi katika wao, nalo ni lile la wale waliokuwa na ikhlasi na yakini kwa Mola wao. Na kundi lingine ilikuwa hamu ya watu wake ni kuziokoa nafsi zao; azma yao ilikuwa dhaifu, wakashughulishwa na nafsi zao na wakawa na dhana mbaya kwa Mola wao, kwa Dini Yake na kwa Mtume Wake.Wakadhani kwamba Mwenyezi Mungu Hatalitimiza jambo la Mtume Wake na kwamba Uislamu hautasimama ukaimarika. Kwa hivyo, utawaona ni wenye majuto juu ya kutoka kwao. Na huwa wakiambiana wao kwa wao, «Je tulikuwa na chaguo lolote katika kutoka kwetu kwenda kupigana?» Waambie, ewe Mtume, «Mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu. Yeye Ndiye Aliyepanga kutoka kwenu na (Ndiye Aliyepanga yale) yaliyowafikia.» Nao wanayaficha katika nafsi zao wasiyoyadhihirisha kwako ya majuto juu ya kutoka kwao kwenda mapiganoni. Huwa wakisema, «Lau kama tungalikuwa na hiyari japo ndogo, hatungeuawa hapa.» Waambie, «Ajali ziko mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Hata kama mlikuwa majumbani mwenu, na Mwenyezi Mungu Akakadiria mufe, wangalitoka wale ambao Mwenyezi Mungu Amewakadiria mauti, kwenda pale watakapouawa.» Na Hakuyafanya hayo Mwenyezi Mungu isipokuwa ni kuwapa nyinyi mtihani juu ya yaliyomo ndani ya vifua vyenu ya shaka na unafiki na ili Ampambanue mwema na maovu na lipate kudhihirika kwa watu jambo la Muumini na lile la mnafiki, la maneno na vitendo. Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi wa yaliyomo kwenye nyoyo za viumbe Wake. Hakuna chochote, katika mambo yao, kinachofichika Kwake

    [155] Hakika wale waliokimbia kati yenu, enyi Maswahaba wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwenye vita siku waliokutana Waumimini na washirikina katika vita vya Uhud, ni Shetani ndiye aliyewatosa kwenye dhambi hili kutokana na baadhi ya madhambi waliyoyafanya. Kwa kweli Mwenyezi Mungu Amewasamehe na hakuwaadhibu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa Msamaha kwa wenye madhambi wanaotubia, ni Mpole Asiyekuwa na haraka ya kuwatesa wenye kumuasi

    [156] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata Sheria Zake kivitendo, msijifananishe na makafiri ambao hawamuamini Mola wao. Kwani wao huwaambia ndugu zao, miongoni mwa makafiri, wanapotoka kwenda kutafuta maisha yao katika ardhi au wanapokuwa pamoja na wapiganaji, wakafa au wakauawa, «Lau kama hawa hawangetoka wala hawangepigana na wakabakia pamoja na sisi, hawangekufa wala hawangeuawa.» Neno hili linawaongezea machungu, maudhiko na majuto yanayobakia katika nyoyo zao. Ama Waumini, wao wanajua kwamba hili limetokana na kadara ya Mwenyezi Mungu, ndipo Mwenyezi Mungu Huziongoza nyoyo zao na Huwasahilishia misiba. Na Mwenyezi Mungu Anambakisha hai yule Aliyemkadiria kuishi, hata kama ni msafiri au ni mpiganaji. Na Anamfisha yule ambaye muda wake wa kuishi umekoma, hata kama ni mkazi wa mji. Na Mwenyezi Mungu kwa kila mlifanyalo ni Mwenye kuliona, na Atawalipa kwalo

    [157] Na iwapo mtauawa, enyi Waumini, katika hali ya kupigana katika njia ya Mwenyezi Mungu au mkafa vitani, Mwenyezi Mungu Atawasamehe madhmbi yenu na Atawarehemu rehema itokayo Kwake. Hapo mtafaulu kwa kuyapata mabustani ya Peponi yenye starehe nyingi. Hayo ni bora kuliko dunia na wanavyovikusanya wapenda dunia

    [158] Na iwapo ajali zenu zitakoma katika haya maisha ya dunia na mkafa juu ya matandiko yenu au mkauawa katika uwanja wa mapigano, ni kwa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Mtakusanywa; na huko Atawalipa kwa matendo yenu mliyoyatenda

    [159] Na kwa ajili ya rehema za Mwenyezi Mungu kwako na maswhaba wako, ewe Nabii, Mwenyezi Mungu Alikuneemesha ukawa laini kwao. Na lau ungalikuwa na tabia mbaya, mwenye moyo mgumu, maswahaba wako wangalijitenga na kuwa mbali na wewe. Kwa hivyo, usiwe na hasira nao kwa yaliyotokea kwao katika vita vya Uhud. Basi muombe Mwenyezi Mungu, ewe Nabii, Awasamehe na uwashauri katika mambo yanayohitajia ushauri. Na utakapoazimia kufanya jambo kati ya mambo yoyote, baada ya kushauri, litekeleze hali ya kumtegemea Mwenyezi Mungu, Peke Yake. Hakika Mwenyezi Mungu Anawapenda wenye kujitegemeza Kwake

    [160] Iwapo Mwenyezi Mungu Atawapa msaada na nusura Yake, hapana yoyota awezaye kuwashinda. Na iwapo Atawaacha kuwasaidia na kuwanusuru, basi ni nani awezaye kuwanusuru nyinyi baada ya Yeye kuacha kuwanusuru? Na kwa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, nawajitegemeze Waumini

    [161] Haiwi kwa Mtume kuwafanyia hiana maswahaba wake kwa kutwaa kitu katika ngawira ambayo Mwenyezi Mungu Hakumtengea. Na yoyote mwenye kulifanya hilo, miongoni mwenu, atakuja Siku ya Kiyama akiwa amekibeba kile alichokitwaa, ili afedheheshwe nacho mbele ya kila mtu katika kisimamo kinachojumuisha watu wote. Kisha itapewa kila nafsi malipo kamili ya ilichokichuma pasi na kupunguzwa wala kufanyiwa dhuluma

    [162] Yule ambaye lengo lake ni radhi za Mwenyezi Mungu, halingani na yule ambaye ametopea kwenye maasia na kumkasirisha Mola wake na akastahiki kwa hilo makazi ya Jahanamu ambayo mwisho mbaya wa mtu kuishilia ni hapo

    [163] Watu wa Peponi wenye kufuata yenye kumridhisha Mwenyezi Mungu wanatafautiana daraja. Na watu wa Motoni wanaofuata yenye kumkasirisha Mwenyezi Mungu wanatafautiana katika matobwe. Wao hawalingani. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuziona amali zao, hakifichiki chochote Kwake katika matendo yao

    [164] Hakika Mwenyezi Mungu Amewapa neema Waumini, miongoni mwa Waarabu, Alipomtumiliza Mtume atokaye katika jinsi yao, akawa anawasomea wao aya za Qur’ani, anawatakasa na ushirikina na tabia mbaya na anawafundisha Qur’ani na Suna, pamoja na kwamba kabla ya Mtume huyu walikuwa kwenye upotevu na ujinga ulio wazi

    [165] Kwa nini mlipopatwa na msiba uliowakumba siku ya Uhud, ingawa mumewapata washirikina mara mbili yake siku ya Badr, mlisema kwa kustaajabu, «Mambo haya yatakuwa vipi, na sisi ni Waislamu, Mtume wa Mwenyezi Mungu yuko na sisi, na hawa ni washirikina?» Sema uwaambie, ewe Nabii, «Haya yaliyowapata yamesababishwa na nyinyi wenyewe kwa kuenda kinyume kwenu na amri ya Mtume wenu na kuelekea kwenu kukusanya ngawira.» Kwa hakika, Mwenyezi Mungu Anafanya Atakalo na Anahukumu Atakavyo. Hakuna mwenye kuitangua hukumu Yake

    [166] Na yale yaliyotokea kwenu ya majaraha au ya mauaji katika vita vya Uhud, siku ulipokutana mkusanyiko wa Waumini na mkusanyiko wa washirikina, na ukawa ushindi, mwanzo wa vita, ni wa Waumini kisha, mara ya pili, ukwa ni wa washirikina, yote hayo yalikuwa kwa uamuzi wa Mwenyezi Mungu na mpango Wake, ili yajitokeze yale Aliyoyajua Mwenyezi Mungu tangu kale, ili Awapambanue Waumini wa kweli miongoni mwenu

    [167] Na ili Awapambanue wanafiki ambao Mwenyezi Mungu Ameyafungua wazi yaliyomo ndani ya nyoyo zao, walipokuwa Waumini wawaambia, «Njooni mpigane pamoja na sisi katika njia ya Mwenyezi Mungu au kuweni ni msaada kwetu kwa kutufanya tuwe wengi.» Wakasema, «Lau kama tunajua kuwa nyinyi mtapigana na yoyote tungalikuwa na nyinyi dhidi yao.» Wao katika ukafiri, siku hii ya leo, wako karibu zaidi kuliko kuwa wao wako karibu na Imani.Kwani wao wanayasema kwa midomo yao yasiokuwa kwenye nyoyo zao. Na Mwenyezi Mungu Anayajua zaidi wanayoyaficha vifuani mwao

    [168] Wanafiki hawa ndio wale walioketi wakawaambia ndugu zao waliopata msiba pamoja na Waislamu kwenye vita vyao na washirikina siku ya Uhud, «Lau kama watu hawa wangalitutii hawangaliuawa.» Sema, ewe Mtume, uwaambie «Zizuieni nafsi zenu na kifo, ikiwa nyinyi ni wa kweli katika madai yenu kwamba wao kama wangaliwatii hawangaliuawa na kwamba mumeokoka na mauti kwa kukaa kwenu kutokwenda vitani.»

    [169] Wala usidhani, ewe Mtume, kwamba wale waliouawa katika njia ya Mwenyezi Mungu ni wafu hawahisi chochote. Bali wao wako hai uhai wa barzakh kwenye ujirani wa Mola wao Ambaye walipigana jihadi kwa ajili Yake na wakafa katika njia Yake, inawapitia riziki yao huko Peponi na wananeemeshwa

    [170] Furaha iliwaenea, wakati Mola wao Alipowaneemesha na kuwapa neema na radhi zenye kuwaliwaza macho yao, zikiwa ni miongoni mwa ukarimu Wake na takrima Yake. Watakuwa wakiwafurahia ndugu zao wenye kupigana jihadi waliowaacha duniani wakiwa hai, wakiwatarajia wafaulu kama walivyofaulu wao. Kwa kuwa wao waelewa kwamba hao ndugu zao, waliowaacha duniani wakiwa hai, watapata heri waliyoipata wao, iwapo watakufa mashahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu hali ya kumtakasia Yeye, na kwamba hawatakuwa na chochote cha kuogopa kuhusu mambo ya mustakbali wao huku Akhera wanayoyakabili wala hawatakuwa na huzuni juu ya yale yaliyowapita wakayakosa ya hadhi za kilimwengu

    [171] Hakika wao watakuwa wamejawa na furaha kwa neema za Mwenyezi Mungu na vipawa Vyake vingi na hakika Mwenyezi Mungu Hayapotezi malipo ya ya wenye kumuamini, bali Anayakuza na kuyaongeza kwa fadhila Zake

    [172] Wale waliouitikia mwito wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakatoka kuwafuata washirikina mpaka kijiji cha Ḥamrā’ al-Asad baada ya kushindwa katika vita vya Uḥud, pamoja na maumivu na majaraha waliyokuwa nayo, wakafanya upeo wa juhudi zao na wakashikamana na mwongozo wa Mtume wao, basi watenda wema hao na wacha-Mungu hao watapata thawabu kubwa

    [173] Wao ni wale walioambiwa na baadhi ya washirikina , «Abu Sufyani na wenzake wameamua kuwarudia nyinyi ili kuwamaliza, basi jihadharini nao na mjikinge na kukutana nao, kwani hamna nguvu za kupambana nao.» Tahadhari hiyo iliwazidishia yakini na kuikubali kikweli ahadi ya Mwenyezi Mungu kwao na haikuwazuia na uamuzi wao. Hapo walikwenda wakielekea pale Mwenyezi Mungu Alipotaka na wakasema, «Ḥasbunā Allāh wa Ni’ma al Wakīl» Yaani, Mtosheleza wetu ni Mwenyezi Mungu na Yeye Ndiye Wakili mwema Mwenye kutegemezewa mipango ya waja Wake

    [174] Basi wakarudi kutoka Ḥamrā’ al Asad kuja Madina wakiwa wana neema za Mwenyezi Mungu kwa kupata thawabu nyingi na nyongeza za daraja ya juu zitokazo Kwake, huku Imani na yakini zimeongezeka kwao, maadui wa Mwenyezi Mungu wamewadhalilisha, wamefaulu kwa kusalimika na kuuawa na kupigana, na wamefuata mambo ya kumridhisha Mwenyezi Mungu kwa kumtii Yeye na Mtume Wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye ihsani na vipawa vingi vyenye kuwaenea wao na wengineo

    [175] Hakika anyewazorotesha nyinyi katika hilo ni Shetani. Amewajia kuwafanya nyinyi muwaogope wasaidizi wake. Basi msiwaogope washirikina, kwani wao ni wanyonge, hakuna mwenye kuwanusuru. Niogopeni mimi kwa kuelekea kwangu kwa utiifu, iwapo nyinyi kweli mnaniamini na mnamfuata Mtume wangu

    [176] Wasikutie huzuni moyoni mwako hawa makafiri, ewe Mtume, kwa kukimbilia kwao kukanusha na kuingia kwenye upotevu. Hakika wao, kwa hilo, hawatamdhuru Mwenyezi Mungu chochote. Hakika ni kwamba wao wazidhuru nafsi zao kwa kuzinyima utamu wa Imani na thawabu kubwa. Mwenyezi Mungu Anataka Asiwape malipo mema yoyote huko Akhera, kwa kuwa wao wamejiepusha na ulinganizi wa haki. Na wao watapata adhabu kali

    [177] Hakika wale walioibadili Imani kwa kuandama ukafiri, hawatamdhuru Mwenyezi Mungu chochote. Bali madhara ya kitendo chao yatawarudia wenyewe. Na huko Akhera watapata adhabu iumizayo

    [178] Wala wasidhani wakanushaji kwamba sisi tukiwarefushia umri wao, tukawastarehesha kwa starehe za duniani na tusiwaadhibu kwa ukafiri wao na madhambi yao kwamba watakuwa wamepata heri ya nafsi zao. Hakika tunawacheleweshea adhabu na ajali zao ili wazidishe dhuluma na ukeukaji mipaka. Na watapata adhabu yenye kuwadhalilisha na kuwatweza

    [179] Hakuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaacha , enyi wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wenye kuzifuata Sheria Yake kivitendo, juu ya hivyo mlivyo ya kuchanganyikana mwenye Imani na mnafiki, mpaka Ampambanue muovu na mwema, ili ajulikune mnafiki na Muumini mkweli. Na haikuwa ni katika hekima ya Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, kwamba Atawafunulia ghaibu Anayoijua kuhusu waja Wake, mkamjua Muumini kati yao na mnafiki. Lakini Yeye Anawapambanua kwa misukosuko na mitihani. Isipokuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anamteua Amtakaye katika wajumbe Wake ili kumuonesha ujuzi wa ghaibu kwa wahyi utokao Kwake. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Na iwapo mtaamini, imani ya kweli, na mkamuogopa Mola wenu kwa kumtii, mtapata malipo makubwa mbele ya Mwenyezi Mungu

    [180] Wala wasidhani wale wanaozifanyia ubakhili neema za Mwenyezi Mungu Alizowaneemesha kwa kuwafadhili kwamba ubakhili huo ni bora kwao. Bali hiyo ni shari kwao. Kwani mali hayo waliyoyakusanya yatakuwa ni kitanzi cha moto kitakachowekwa shingoni mwao Siku ya Kiyama. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Ndiye Mwenye kumiliki ufalme ; na Yeye Ndiye Atakayesalia baada ya kutoweka viumbe Wake wote. Yeye Ndiye Mtambuzi wa matendo yenu yote, na Atamlipa kila mtu kwa kadiri anayostahiki

    [181] Hakika Amelisikia Mwenyezi Mungu neno la Mayahudi ambao walisema, «Mwenyezi Mungu ni muhitji kwetu, Anatutaka tumkopeshe mali, na sisi ni matajiri.» Tutaliandika neno hili walilolisema na tutaandika kwamba wao wako radhi na yale yaliyofanyika ya kwamba mababa zao waliwaua Manabii wa Mwenyezi Mungu kwa dhuluma na uadui. Tutawaadhibu kwa hilo huko Akhera na tutawaambia, nao wamo Motoni waadhibiwa, «Ionjeni adhabu ya Moto unaounguza.»

    [182] Adhabu hiyo kali ni kwa sababu ya yale mliyoyatanguliza katika maisha yenu ya duniani kati ya maasia ya kimaneno, ya kivitendo na ya kiitikadi, na kwamba Mwenyezi Mungu si Mwenye kuwadhulumu waja Wake

    [183] Mayahudi hawa walipoitwa kuufuata Uislamu, walisema, «Mwenyezi Mungu Ametuusia katika Taurati kwamba tusimsadiki yoyote atakayetujia na neno la kwamba yeye ni mjumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu mpaka atuletee sadaka, ambayo kwayo atajisogeza karibu na Mwenyezi Mungu, hapo ushuke moto kutoka mbinguni uiteketeze.» Sema uwaambie,ewe Mtume, «Nyinyi ni warongo kwa hayo mnayoyasema. Kwani mababa zenu kabla yangu walijiliwa na Mitume, wakiwa na hoja na dalili za ukweli wao na pia hayo mliyoyasema ya kuleta sadaka ambayo itateketezwa na moto. Basi mbona mababa zenu waliwaua Mitume hao, iwapo nyinyi ni wakweli katika madai yenu?»

    [184] Basi ikiwa Mayahudi hawa na makafiri wengineo watakukanusha, ewe Mtume, hakika wabatilifu wamewakanusha Mitume wengi kabla yako waliowajia kaumu zao kwa miujiza mingi yenye kushinda, hoja zilizo wazi, vitabu vya mbinguni ambavyo ni nuru inayoondosha giza na Kitabu chenye ufafanuzi, kilicho wazi

    [185] Nafsi yoyote, hapana budi, itayaonja mauti. Na kwa hivyo, viumbe wote watarudi kwa Mola wao ili Awahesabu. Na kwa hakika mtalipwa malipo yenu kikamilifu Siku ya Kiyama juu ya vitendo vyenu bila kupunguziwa. Basi yule ambaye Mola wake Atamkirimu, Akamuokoa na Moto na Akamtia Peponi, huyo atakuwa amepata upeo wa ayatakayo. Na hayakuwa maisha ya duniani isipokuwa ni kiliwazo cha kuondoka. Basi msighurike nayo

    [186] Mtapewa mtihani, tena mtapewa mtihani, enyi Waumini, katika mali yenu kwa kutakiwa mtoe matumizi ya wajibu na yanayopendekezwa na kwa mikasa inayoyakumba. Pia mtapewa mtihani katika nafsi zenu kwa kutakiwa mtekeleze ya wajibu ya kumtii Mwenyezi Mungu na kwa misiba inayowafikia ya majaraha au mauaji na kuwakosa vipenzi vyenu. Hilo litaendelea mpaka apambanuke mwenye imani ya kweli na mwenginewe. Na mtasikia, tena mtasikia, kutoka kwa Mayahudi, Wanaswara na washirikina maneno yatakayoudhi masikizi yenu katika matamshi ya ushirikina na kuitukana dini yenu. Na iwapo mtasubiri, enyi Waumini, juu ya hayo yote na mkamcha Mwenyezi Mungu kwa kujilazimisha kumtii Yeye na kujiepusha na kumuasi, hakika hilo ni miongoni mwa mambo ambayo yanakusudiwa kidhati na kushindaniwa

    [187] Na kumbuka, ewe Mtume, pindi Mwenyezi Mungu Alipochukua ahadi ya mkazo juu ya wale ambao Mwenyezi Mungu Amewapa Kitabu, miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara, Mayahudi walipewa Taurati na Wanaswara walipewa Injili, ili wavitumie na wawafahamishe watu yaliyomo ndani yake wala wasiyafiche. Lakini wao waliiacha ahadi hiyo na hawakujilazimisha nayo. Na wakachukua thamni duni ikiwa ni badali ya wao kuificha haki na kukipotoa Kitabu. Ni mabaya yalioje manunuzi waliyonunua ya kuipoteza kwao ahadi na kubadilisha kwao Kitabu

    [188] Wala msiwadhanie wale wanaofurahia matendo maovu waliyoyafanya, kama Mayahudi, wanafiki na wengineo, na wakawa wanapenda kuwa watu wawataje vizuri kwa mambo ambayo hawakuyafanya, basi msiwadhanie wao kuwa ni wenye kuokoka na adhabu ya Mwenyezi Mungu duniani. Na watakuwa na adhabu iumizayo kesho Akhera. Katika haya kuna onyo kali kwa kila mwenye kutenda kitendo kiovu na kukifurahia na kwa kila mwenye kujigamba kwa ambacho hakukifanya ili watu wamsifu na kumshukuru

    [189] Ni wa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, ufalme wa mbinguni na ardhini na vilivyomo humo. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu

    [190] Hakika, katika kuziumba mbingu na ardhi, pasi na kuwa na mfano uliotangulia, na katika kufuatana usiku na mchana na kutafautiana kwao, urefu na ufupi, pana dalili na hoja kubwa zinazobainisha upweke wa Mwenyezi Mungu kwa walio na akili timamu

    [191] Ambao wanamtaja Mwenyezi Mungu katika hali zao zote, wakiwa wamesimama, wakiwa wameketi na wakiwa wamelala kwa mbavu zao, huku wana mazingatio juu ya uumbaji wa mbingu na ardhi hali ya kusema, «Ewe Mola wetu, Hukuuleta uumbaji huu kwa upuzi; Wewe Umetakasika na hilo! Basi tuepushie adhabu ya Moto

    [192] «Ewe Mola wetu! Tuokue na Moto, kwani hakika Wewe, ewe Mwenyezi Mungu, yoyote Utakayemuingiza Motoni kwa madhambi yake, ushamfedhehesha na kumtweza. Na watenda madhambi, wanaozidhulumu nafsi zao, hawatakuwa na yoyote wa kuwatetea wasipate adhabu ya Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama

    [193] «Ewe Mola wetu! Sisi Tumemsikia mlinganizi, naye ni Mtume wako Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, anawaita watu wakuamini Wewe na kukubali Umoja wako na kuzifuata kivitendo Sheria zako, tukauitikia ulinganizi wake na tukauamini utume wake. Basi tusamehe madhambi yetu, uzisitiri aibu zetu na utukutanishe na watu wema

    [194] «Ewe Mola wetu! Tupe yale uliyotuahidi kwenye ndimi za Mitume wako, ya kupata ushindi, umakinifu, taufiki na uongofu. Wala usitufedheheshe, kwa madhambi yetu, Siku ya Kiyama. Hakika wewe ni Mkarimu, Huendi kinyume na ahadi ulizowaahidi waja wako.»

    [195] Na Mwenyezi Mungu Akaitikia maombi yao kwamba Yeye Hazipotezi juhudi za yoyote aliyetenda amali njema, awe ni mwanamume au ni mwanamke. Kwani wao, katika undugu wa kidini, kukubaliwa amali zao na kulipwa kwazo, ni sawa. Kwa hivyo, wale waliohama kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, wakatolewa kwenye majumba yao, wakaudhiwa katika kumtii Mola wao na kumuabudu kwao Yeye Peke Yake, wakapigana na wakauawa katikia njia ya Mwenyezi Mungu kwa kulikuza neno Lake, hao Mwenyezi Mungu Atawapa sitara kwa maasia waliyoyafanya kama Alivyowasitiri nayo duniani na Hatawahesabu kwayo. Na atawaingiza, tena Atawaingiza, kwenye mabustani ya Peponi ambayo inapita mito chini ya majumba yake ya fahari na miti yake. Hayo yakiwa ni malipo kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na kwa Mwenyezi Mungu kuna malipo mazuri

    [196] Usihadaike, ewe Mtume, kwa yale waliyonayo wenye kumkufuru Mwenyezi Mungu, ya ukunjufu wa riziki, hali nzuri ya maisha na kuhama kwao kutoka mahali kwenda pengine kwa ajili ya biashara na kutaka faida na mali. Kwa muda mchache, yote hayo yatawaondokea na watakuwa ni wenye kufungika na kuwekwa dhamana kwa vitendo vyao viovu

    [197] Hiyo ni starahe ndogo yenye kuondoka.Kisha marejeo yao Siku ya Kiyama ni Motoni. Na huo Moto ni tandiko ovu mno

    [198] Lakini wale waliomuogopa Mola wao , wakazifuata amri Zake na wakajiepusha na makatazo Yake, Mwenyezi Mungu Amewaandalia mabustani ya Pepo ambayo mito inapita chini ya majumba yake ya fahari na miti yake. Mabustani hayo yatakuwa ni makazi yao ya kudumu; hawatatoka humo. Na yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ni makubwa zaidi na bora zaidi kwa watiifu kuliko yale ya starehe za ulimwengu ambazo hao waliokufuru wanatanga huku na kule kwa kuzitafuta

    [199] Baadhi ya waliopewa vitabu wanamuamini Mwenyezi Mungu kuwa ni Mola Mmoja na Mungu Mwenye kuabudiwa, wanaiamini Qur’ani mliyoteremshiwa nyinyi na Taurati na Injili walizoteremshiwa wao, hali ya kumdhalilikia Mwenyezi Mungu na kumnyenyekea. Hawazibadilishi aya za Mwenyezi Mungu kwa thamani ndogo ya takataka za duniani wala hawayafichi Aliyoyataremsha Mwenyezi Mungu na wala hawayapotoshi kama wanavyofanya wengineo miongoni mwa waliopewa Vitabu. Hao watapata thawabu kubwa mbele ya Mola wao Siku ya kukutana Naye, na watapewa malipo yao kamili, bila ya kupunguzwa. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhesabu. Hakumshindi Yeye kuyadhibiti matendo yao na kuwahesabu wao kwayo

    [200] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo, kuweni na subira juu ya kumtii Mola wenu na juu yaliyowashukia ya madhara na shida, na washindeni maadui zenu katika kusubiri wasipate kuwa wasubirifu zaidi kuliko nyinyi, na simameni wima katika kumpiga vita adui yangu na adui yenu. Na muogopeni Mwenyezi Mungu, katika hali zenu zote, ili mfaulu kupata radhi Zake ulimwenguni na Akhera

    Wanawake

    Surah 4

    [1] Enyi watu, muogopeni Mwenyezi Mungu, mjilazimishe na amri Zake na mjiepushe na makatazo Yake. Kwani Yeye Ndiye Aliyewaumba nyinyi kutokana na nafsi moja, nayo ni Ādam, amani imshukiye, na Akaiuumba, kutokana na nafsi hiyo, ya pili yake, nayo ni Ḥawwā. Na Akaeneza, kutokana na nafsi mbili hizo, wanaume wengi na wanawake wengi katika sehemu za ardhi hii. Na mchungeni Mwenyezi mungu Ambaye kupitia Kwake mnaombana nyinyi kwa nyinyi. Na jihadharini msije mkakata vizazi vyenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuzichunguza hali zenu zote

    [2] Na wale waliofiliwa na baba zao wakiwa bado hawajabaleghe, na mkawa nyinyi ndio wasimamizi wao, wapeni mali zao wafikapo umri wa kubaleghe, muonapo kutoka kwao kuwa wana uwezo wa kuhifadhi mali zao. Na wala msichukuwe kizuri katika mali zao na mkaweka mahali pake kibaya katika mali zenu. Wala msichanganye mali zao na mali zenu ili mpate kula mali zao kwa hila. Na mwenye kujasiri kulitenda hilo, hakika huyo amefanya dhambi kubwa

    [3] Na iwapo mtachelea kwamba hamtafanya usawa kwa mayatima wa kike ambao wako chini ya usimamizi wenu, kwa kutowapa mahari yao kama wanawake wengine, basi waacheni na oeni waliowapendeza kati ya wanawake wengine, wawili au watatu au wanne. Na iwapo mtaogopa kutofanya uadilifu kati yao, basi toshekeni na mke mmoja, au toshekeni kwa mliowamiliki. Hilo, nililolifanya ni Sheria kwenu kuhusu mayatima wa kike na kuhusu kuoa mke mmoja hadi wane au kuwa na mke mmoja tu au mjakazi aliyemlilikiwa na kutiwa usuriani, liko karibu zaidi na kutofanya ujeuri na kuvuka mipaka

    [4] Na wapeni wanawake, enyi waume, mahari yao, kipewa kinacholazimu na faradhi iliyopasa, kwa roho yenu safi. Na iwapo zitakuwa safi nafsi zao kwenu na kuwatunuku chochote katika mahari, basi kichukueni na mkitumie mnavyotaka, kwani hicho ni halali iliyo nzuri

    [5] Wala msiwape, enyi wasimamizi, wale wafujaji, kati ya wanaume, wanawake na watoto, mali zao ambazo ziko chini ya mikono yenu, kwani wataziweka sehemu isiyokuwa yake. Mali hizi ndizo ambazo juu yake yanasimama maisha ya watu. Wapeni matumizi na mavazi, kwenye mali hizo, na muwaambie maneno mazuri yanayopendeza na muamiliane nao kwa tabia njema

    [6] Wajaribuni mayatima walio chini ya mikono yenu mpate kuujua uwezo wao wa kutumia vizuri mali zao. Mpaka watakapofika miaka ya kubaleghe, mkawajua kuwa ni wema katika dini yao na wana uwezo wa kuhifadhi mali zao, basi wapeni mali zao. Wala msizifuje kwa kuzitumia mahali ambapo si pake kwa kupita mpaka wa matumizi na kukimbilia kuzila kabla hawajazichukua kutoka kwenu. Na mwenye mali katika nyinyi, ajizuie na atosheke na utajiri alionao, na asichukue chochote katika mali ya yatima. Na ambaye ni fukara, basi achukue kadiri ya haja yake wakati wa dharura. Na mtakapojua kuwa wao wana uwezo wa kuzihifadhi mali zao baada ya kubaleghe kwao na mkawapa mali zao, wawekeni mashahidi wakiwa ni dhamana kuwa mali yao yamewafikia kikamilifu, ili wasipate kulikanusha hilo. Na yawatosha nyinyi kwamba Mwenyezi Mungu ni shahidi juu yenu na Atawahesabu kwa mliyoyafanya

    [7] Wanaume, wadogo na wakubwa, wana fungu lililopasishwa na Mwenyezi Mungu katika mali yalioachwa na wazazi wawili au jamaa wa karibu, yawe ni kidogo mali hayo au ni mengi, katika mafungu maalumu yaliyo wazi yaliyofaradhiwa na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kushinda, kwa hawa wanaume na pia wanawake

    [8] Watakapohudhuria, kikao chakugawanywa urithi, jamaa wa maiti wa karibu wasiokuwa na haki ya kurithi au waliofiwa na baba zao nao ni wadogo au wasiokuwa na mali, basi wapeni chochote katika mali hayo, kwa njia ya kuwapumbaza, kabla mali hayajagawanywa kwa wenyewe. Na waambieni neno zuri lisilokuwa chafu wala baya

    [9] Na waogope wale ambao lau watakufa na wataacha nyuma yao watoto wadogo madhaifu, wakawachelea dhuluma na kupotea, basi na wamchunge Mwenyezi Mungu juu ya wale mayatima na wengineo walio chini ya mikono yao. Nako ni kuwahifadhia mali yao, kuwalea vizuri na kuwaondolea ya kuwaudhi. Na wawaambie maneno yanayolingana na usawa na wema

    [10] Wale wanaozifuja mali za mayatima wakawa wazichukua pasi na haki, hakika wanakula Moto utakaowaka matumboni mwao Siku ya Kiyama; wataungia Moto ambao watalisikia joto lake

    [11] Mwenyezi Mungu Anawausia na kuwaamrisha, kuhusu wana wenu atakapokufa mmoja wenu na akaacha watoto wa kiume na wa kike, kwamba urithi wote ni wao: mtoto wa kiume atapata mfano wa fungu la watoto wawili wa kike, iwapo itakuwa hakuna mawarithi wengine isipokuwa ni wao tu. Iwapo atawaacha watoto wa kike peke yao, basi watoto wa kike wawili au zaidi watapata theluthi mbili ya alichokiacha.. Na iwapo mrithi ni binti mmoja, basi atapata nusu ya mali, na wazazi wawili wa maiti, kila mmoja atapata sudusi. Hii ni iwapo maiti ana mtoto wa kiume au wa kike, mmoja au zaidi. Iwapo maiti hana mwana, na wakawa mawarithi wake ni wazazi wake wawili, basi mamake atapata theluthi na babake atapata kilichosalia. Na iwapo maiti ana ndugu, wawili au zaidi, wawe ni wanawake au ni wanaume, basi mamake atapata sudusi, baba atapata kilichosalia na ndugu hawatapata kitu. Mgawanyo huu wa mali yalioachwa hufanyika baada ya kutoa wasia aliousia maiti katika kiwango cha theluthi, au baada ya kutoa deni adaiwalo. Baba zenu na watoto wenu ambao wamepangiwa kurithi, hamjui ni yupi katika wao mwenye manufaaa ya ukaribu zaidi na nyinyi katika dunia yenu na Akhera yenu. Kwa hivyo, msimfanye mmoja kati yao ni bora kuliko mwengine. Hili mliousiwa nalo limefaradhiwa kwenu na Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa viumbe Wake, ni Mwenye hekima katika Sheria Alizowaekea

    [12] Na nyinyi, enyi wanaume, muna nusu ya kilioachwa na wake zenu baada ya kufa kwao, iwapo hawana watoto wa kiume au wa kike, na ikiwa wana watoto, basi mtapata robo ya walichokiacha ambacho mtakirithi baada ya kutekeleza wasia wao unaofaa au baada ya kulipa deni lao kwa wastahiki. Na wake zenu, enyi waume, watapata robo ya mlichokiacha iwapo hamuna mwana wa kiume au wa kike kutoka kwao, hao wake zenu, au wengineo mliokuwa mumewaoa. Na iwapo mtakuwa na mwana wa kiume au wa kike, basi hao wake zenu watapata thumni ya mlichokiacha. Hiyo robo au thumni itagawanywa kati yao; na iwapo ni mke mmoja, basi hiyo robo au thumni itakuwa ndio fungu lake. Hii ni baada ya kutekeleza kile mlichousia kitekelezwe katika nyasia zifaazo, au kulipa deni lenu. Na iwapo mwanamume au mwanamke atakufa, na akawa hana mwana wala mzazi, na akawa na ndugu mmoja wa kwa mama, wa kiume au wa kike, basi kila mmoja kati yao wawili atapata sudusi; wakiwa ni zaidi ya mmoja watashirikiana katika theluthi itakayogawanywa baina yao kwa usawa bila kutafautisha baina ya mwanamume na mwanamke. Hili ndilo fungu Alilowaekea Mwenyezi Mungu ndugu wa kwa mama, wa kiume na wa kike, likiwa ni urithi wao, baada ya kutekeleza wasia wa aliyekufa iwapo aliusia chochote ambacho hakina madhara kwa mawarithi au baada ya kulipa madeni yake. Kwa hili Amewausia Mola wenu, wasia wenye manufaa kwenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi mno kwa yanayowafaa viumbe Wake, ni Mpole, Hana haraka ya kuwaadhibu

    [13] Hukumu hizo za Kimungu zilizowekwa na Mwenyezi Mungu, kuhusu mayatima, wanawake na mirathi, ni Sheria Zake zioneshazo kuwa zinatoka kwa Mwenyezi Mungu Aliye Mjuzi, Aliye Mwingi wa hekima. Na yoyote mwenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake katika hukumu hizi na nyenginezo zilizowekwa na Mwenyezi Mungu kwa waja Wake, Atamuingiza kwenye mabustani ya Peponi, yenye miti mingi na majumba ya fahari mengi, inayopita chini yake mito yenye maji tamu. Watasalia kwenye neema hii, hawatoki humo. Malipo hayo ndio kufuzu kukubwa

    [14] Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake , kwa kuzikanusha hukumu za Mwenyezi Mungu na kuzikiuka Sheria Zake kwa waja Wake, kwa kuzibadilisha au kuacha kuzitumia, huyo Atamuingiza Motoni, adumu humo; na atapata adhabu ya kumtweza na kumfanya mnyonge

    [15] Na wale wanaozini katika wanawake wenu, washuhudisheni kwao, enyi viongozi na makadhi, wanaume wanne waadilifu miongoni mwa Waislamu, Na iwapo watatoa ushahidi juu yao kwa hilo, wazuieni, wanawake hao, majumbani mpaka yamalizike maisha yao kwa kufa au Mwenyezi Mungu awape njia ya kuwaokoa na hilo

    [16] Na wawili wenye kujiingiza kwenye kitendo cha uzinifu basi waudhini kwa kuwapiga, kuwahama na kuwaaibisha. Wakitubia na kitendo walichokifanya na wakajirekebisha kwa kufanya mambo mema, wasameheni na kuacha kuwaudhi. Faida inayotokana na aya hii na ile kabla yake ni kwamba wanaume wakifanya kitendo cha uzinifu wataudhiwa., ama wanawake watafungwa na kuudhiwa. Kifungo, kikomo chake ni kifo. Na udhia, kikomo chake ni toba na kutengea. Hii ilikuwako mwanzo wa Uislamu, kisha ikaondolewa kwa Sheria iliowekwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, nayo ni kupigwa mawe mpaka kufa, kwa yule ambaye ashaoa au ashaolewa, wakiwa wote wawili ni watu huru, waliobaleghe, wenye akili na ambao wameingilia au kuingiliwa katika ndoa sahihi. Ama wasiokuwa hao, adhabu yao ni kupigwa mbati mia na kuhamishwa mwaka mzima. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuzikubali toba za waja Wake wanaotubia, ni Mwenye huruma kwao

    [17] Kwa kweli, Mwenyezi Mungu Anaikubali toba itokayo kwa wale wanaofanya maasia na madhambi kwa ujinga wao wa kutojua ubaya wake na kwamba yanasababisha hasira za Mwenyezi Mungu.- Kwa hivyo, kila anayemuasi Mwenyezi Mungu, kwa kukosea au kwa kusudi, yeye ni mjinga kwa kuzingatia maana haya, hata kama anajua kuwa ni haramu.- kisha, hao wanaokubaliwa toba zao, wakarudi kwa Mola wao kwa majuto na kutii kabla ya kukabiliwa na mauti. Basi hao ndio wale ambao Mwenyezi Mungu Anaikubali toba yao. Na Mwenyezi Mungu daima ni Mjuzi kwa viumbe Wake, ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji Wake mambo na makadirio Yake

    [18] Kukubaliwa toba si kwa wale wanaoendelea kufanya maasia bila ya kurudi kwa Mola wao mpaka wakafikiwa na shida ya mauti, hapo mmoja wao aseme, «Mimi sasa nimetubia.» Kama ambavyo haikubaliwi toba ya wale wanaokufa na hali wao ni wenye kukanusha, ni wenye kupinga upweke wa Mwenyezi Mungu na ujumbe wa Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie. Hao wenye kuendeleza maasia hadi kufa kwao, na wakanushaji ambao wanakufa na huku ni makafiri, tumewatayarishia adhabu iumizayo

    [19] Enyi mlioamini, haifai kwenu kuwafanya wake wa baba zenu ni miongoni mwa mali yalioachwa kurithiwa, mkawa mnafanya mtakavyo kwao: kwa kuwaoa, kuwakataza wasiolewe au kuwaoza waume wengine, hali ya kuwa wao hawayataki hayo yote. Na pia haifai kwenu kuwadhuru wake zenu kwa kuwa mnawachukia, ili wapate kusamehe baadhi ya mlivyowapa, mahari au vinginevyo. Isipokuwa wakiwa wamefanya jambo ovu, kama uzinifu, hapo mnayo nafasi ya kuwazuia mpaka mkitwae mlichowapa. Na kule kukaa kwenu na wake zenu yatakikana kuwe ni juu ya misingi ya heshima na mapenzi na kuwatekelezea haki zao. Na iwapo mtawachukia kwa sababu yoyote katika sababu za kidunia, basi kuweni na subira. Kwani huenda mkachukia jambo, miongoni mwa mambo, na ikawa ndani yake muna kheri nyingi

    [20] Na mnapotaka kubadilisha mke mahali pa mke mwengine, na mkawa mumempa yule mnayetaka kumtaliki mali mengi yakiwa ni mahari yake. Si halali kwenu kuchukua chochote katika mali hayo. Je mnayachukua kwa njia ya urongo na uzushi ulio wazi

    [21] Na vipi itakuwa ni halali kwenu kukichukua mlichowapa cha mahari, na kila mmoja kati yenu amejiliwaza na mwenzake kwa kuingiliana na walichukua kutoka kwenu ahadi iliyo nzito ya kuwa mtashikamana nao kwa wema au mtaepukana nao kwa ihsani

    [22] Wala msiwaoe wanawake walioolewa na baba zenu, isipokuwa yaliyopita mliyoyafanya katika zama za jahiliyyah (kabla ya Uislamu). Hayo hamtalipwa kwayo. Hakika ndoa ya watoto kuwaoa waliokuwa wake wa baba zao ni jambo baya lenye upeo wa ubaya, na ni jambo lenye kuchukiza ambalo Mwenyezi Mungu Anamchukia mwenye kulifanya. Na ubaya wa njia na mwenendo ni huo mliokuwa mkiufanya zama za ujinga wenu( kabla ya Uislamu)

    [23] Mwenyezi Mungu Amewaharamishia kuwaoa mama zenu, wanaingia kwenye uharamu huu manyanya wa upande wa baba na upande wa mama, na mabinti zenu, wanaingia kwenye uharamu huu mabinti wa watoto wa kiume au wa kike na kwenda chini, na dada zenu kwa baba na mama au kwa baba au kwa mama, na mashangazi zenu, nao ni ndugu wa kike wa baba zenu na babu zenu, na makhalati zenu, nao ni dada za mama zenu na nyanya zenu, na mabinti wa ndugu wa kiume na mabinti wa ndugu wa kike; na waingia humo watoto wao, na mama zenu waliowanyonyesha, na dada zenu mlionyonya nao; na Mtume , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ameharamisha kwa ajili ya kunyonya kila aliyeharamishwa kwa ajili ya ukaribu wa nasaba. Pia ni haramu kuwaoa mama za wake zenu, muwe mumewaingilia hao wake zenu au hamukuwaingilia, na mabinti wa wake zenu wa mababa wengine ambao kawaida wanalelewa majumbani mwenu na chini ya uangalizi wenu, wao ni haramu kuwaoa hata kama hawamo majumbani mwenu, lakini kwa sharti ya kuwaingilia mama zao. Na iwapo hamkuwaingilia mama zao , na mkawataliki au wakafa kabla ya kuwaingilia, hapo hapana makosa kuwaoa mabinti wao. Pia amewaharamishia Mwenyezi Mungu kuwaoa waliokuwa wake wa watoto wenu watokao migongoni mwenu, na wale walioshikanishwa na wao ambao ni watoto wenu wa kiume kwa kunyonya. Kuharamishwa huku kunakuwa kwa kufunga ndoa, awe yule mtoto wa kiume amemuingilia mkewe au hakumuingilia. Pia Amewaharamishia kuwakusanya pamoja, kwenye ndoa, dada wawili wa nasaba au wa kunyonya, isipokuwa yale yaliopita mlioyafanya katika zama za kabla ya Uislamu. Kadhalika, haifai kuwakusanya, kindoa, mwanamke na shangazi yake au khalati yake, kama ilvyokuja katika Sunnah. Mwenyezi Mungu daima ni Mwenye kuwasamehe watenda madhambi pindi wanapotubia. Ni Mwenye huruma nao, Hawakalifishi wasiloliweza

    [24] Na ni haramu kwenu kuwaoa wanawake walioolewa, isipokuwa wale mliowateka katika jihadi. Hao ni halali kwenu kuwaoa baada ya kutakasika vizazi vyao kwa kipindi kimoja cha hedhi. Mwenyezi Mungu Amewaandikia uharamu wa kuwaoa hao, na Amewaruhusu kuwaoa wangineo, miongoni mwa wale Aliowahalalishia kuwataka kwa ndoa mkitumia pesa zenu kujihifadhi msitende haramu. Basi wale mliostarehe nao, miongoni mwao, kwa ndoa sahihi, wapeni mahari yao ambayo ni haki yao iliyolazimishwa na Mwenyezi Mungu juu yenu. Na si makosa kwenu, kwa makubaliano yaliyofikiwa baina yenu kwa kuridhiana, kupunguza au kuongeza kiwango cha mahari baada ya kuamuliwa kiwango chake. Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mambo ya waja Wake, ni Mwenye hekima katika hukumu zake na uendeshaji Wake

    [25] Na asiyeweza kujimudu mahari ya Waumini waungwana, basi ni hiyari yake aoe wengineo miongoni mwa wanawake wenu waumini waliomilikiwa. Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ndiye Mjuzi wa ukweli wa Imani yenu. Baadhi yenu mnatokana na wengine katika nyinyi. Basi waoeni kwa ruhusa ya watu wao, na wapeni mahari yao mliokubaliana nayo kwa moyo wenu safi, na wawe ni wenye kujiepusha na haramu, si wenye kudhihirisha zina, wala si wenye kuzini kwa siri kwa kufanya urafiki na wanaume. Wakiolewa na wakafanya kitendo kichafu cha kuzini, adhabu yao ni kadiri ya nusu ya adhabu ya walio huru. Huyo aliyeruhusiwa kuoa wajakazi wenye sifa zilizotajwa, ameruhusiwa iwapo anachelea kuingia kwenye uzinifu na ikawa ni uzito kwake kuvumilia kutoundama. Na kuvumilia kutooa wajakazi pamoja na kujihifadhi ni aula na bora zaidi. Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ni Mwingi wa msamaha kwenu, ni Mwenye kuwahurumia sana kwa kuwaruhusu muwaoe wao(hao wajakazi) mkishindwa kuwaoa waungwana

    [26] Katika kuwaekea Sheria hizi, Mwenyezi Mungu Anataka kuwafunulia wazi alama za dini Yake iliyolingana na hukumu Zake zenye hekima, kuwaonesha njia za Mitume na watu wema waliokuwa kabla yenu katika halali na haramu na kuwakubalia toba zenu kwa kuwarudisha kwenye kumtii Mwenyezi Mungu. Na Yeye, Aliyetakasika na sifa pungufu, ni Mjuzi wa yale yenye kutengeneza mambo ya waja Wake, ni Mwenye hekima katika sheria Zake Alizowaekea

    [27] Na Mwenyezi Mungu Anataka kuwakubalia toba zenu na kuyasamehe makosa yenu; na wale wanaofuata matamanio yao na starehe zao, wanataka mupotoke muwe kando na Dini kabisa

    [28] Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa sheria Zake Alizowaekea, Anataka kuwafanyia sahali na kutowafanyia mkazo, kwa kuwa nyinyi mumeumbwa mkiwa madhaifu

    [29] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Yake kivitendo! Si halali kwa baadhi yenu kula mali ya wengine kati yenu pasi na haki, isipokuwa ikiwa itaambatana na Sheria na chumo la halali litokanalo na kuridhiana baina yenu. Na wala msiuane nyinyi kwa nyinyi mkaziangamiza nafsi zenu kwa kufanya maasia yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma sana katika kila Alilowaamrisha kwalo na kuwakataza nalo

    [30] Na Mwenye kutenda Aliyoyakataza Mwenyezi Mungu ya kuchukua mali ya haramu, kama kuiba, kunyang’anya na kudanganya, kwa dhuluma na kukiuka mipaka ya Sheria, Mwenyezi Mungu Atamuingiza kwenye Moto alionje joto lake. Na hilo kwa Mwenyezi Mungu ni jepesi

    [31] Mkijiepusha, enyi Waumini, na madhambi makubwa, kama kumshrikisha Mwenyezi Mungu, kuwaasi wazazi wawili, kumuua mtu bila ya haki na mengineyo, tutawasamehe madhambi yenu madogo yaliyo chini ya hayo na tutawaingiza mahali pema pa kuingia, napo ni Pepo

    [32] Wala msiyatamani mambo ambayo Mwenyezi Mungu Amewafadhilisha kwayo, baadhi yenu juu ya wengine, ya vipewa na riziki na mengineyo. Kwani Mwenyezi Mungu Amewapa wanaume malipo kulingana na matendo yao na Amewapa wanawake malipo kulingana na matendo yao. Na muombeni Mwenyezi Mungu Aliye Mkarimu na Mpaji Awape nyongeza za ukarimu Wake, badala ya kutamani tu. Hakika Mwenyezi Mungu kwa kila kitu ni Mjuzi, na Yeye Anayajua zaidi yanayowafaa waja Wake miongoni mwa kheri Aliyowagawia

    [33] Kila mmoja katika nyinyi tumemwekea warithi wenye kukirithi kilichoachwa na wazazi wawili na jamaa wa karibu. Na wale mliofungamana nao kwa mayamini yaliyotiliwa mkazo kuwa mtanusuriana na mtawapa kitu katika urithi, basi wapeni walichokadiriwa. Kurithiana kwa mikataba ya kunusuriana kulikuwako mwanzo wa Uislamu , kisha hukumu yake ikaondolewa kwa kuteremka aya za mirathi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuona kila kitu katika vitendo vyenu na Atawalipa kulingana navyo

    [34] Wanaume ni wasimamizi wa kuwaelekeza wanawake na kuwatunza, kwa kile ambacho Mwenyezi Mungu Amewatunuku nacho cha sifa za usimamizi na kutukuzwa, na mahari na matumizi waliyowapa hao wanawake. Basi wale walio wema katika wao, hao wanawake, kwa kuhifadhiwa na Mwenyezi Mungu na kuafikiwa, wanasimama imara kufuata sheria ya Mwenyezi Mungu, wanamtii Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na wanatunza kila lisilojulikana na waume zao katika mambo waliyoaminiwa nayo. Na wale katika wao mnaochelea kuwafanyia nyinyi ujeuri kwa kuacha kuwatii, wapeni nasaha kwa maneno mazuri; iwapo maneno mazuri hayakuzaa matunda kwao, wahameni vitandani wala msiwakaribie. Iwapo kuwahama hakukuwafanya waathirike na kubadili mwenendo wao, basi wapigeni kipigo kisicho na madhara. Na wakiwa watawatii, jihadharini kuwafanyia maonevu. Kwani Mwenye zi Mungu Aliye juu, Aliye Mkubwa Ndiye Msaidizi wao, na Yeye ni Mwenye kuwalipiza wale waliowadhulumu na kuwaonea

    [35] Na mkijua, enyi wasimamizi wa mume na mke, kuwa kuna ugomvi baina yao unaopelekea kutengana, wapelekeeni mwamuzi muadilifu wa upande wa mume na mwamuzi muadilifu wa upande wa mke, ili watazame na kutoa uamuzi wenye maslahi ya wao wawili. Na kwa kuwa wale waamuzi wawili wana hamu ya kupatanisha na wanatumia njia nzuri, Mwenyezi Mungu Atawatilia taufiki baina ya mume na mke. Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, hakuna chochote kinachofichamana Kwake kuhusu mambo ya waja Wake, ni Mtambuzi wa yaliyomo ndani ya nafsi zao

    [36] Na muabuduni Mwenyezi Mungu na mtiini Yeye Peke Yake, wala msimfanyie mshirika katika ustahiki wa kuwa Ndiye Mola na Ndiye Mwenye kuabudiwa, na wafanyieni wema wazazi wawili na mtekeleze haki zao na haki za jamaa wa karibu, na mayatima na wahitaji, na jirani wa karibu na wa mbali, na rafiki wa safari na wa mjini, na msafiri mwenye uhitaji, na waliomilikiwa na nyinyi, wanaume na wanawake. Hakika Mwenyezi Mungu Hawapendi, katika waja Wake, wenye kiburi na kujigamba kwa watu

    [37] Nao ni wale wanaojizuia kutumia na kutoa kile Alichowaruzuku Mwenyezi Mungu, wakawaamuru wengineo kufanya ubahili, wakazikanusha neema za Mwenyezi Mungu juu yao na wakazificha fadhila Zake na vipewa Vyake. Na tumewaandalia wenye kukanusha adhabu yenye kudhalilisha

    [38] Na pia tumewaandalia adhabu hii wale ambao wanatoa mali yao kwa njia ya ria na kujitangaza na hawamuamini Mwenyezi Mungu, kiitikadi na kivitendo, wala Siku ya Kiyama. Matendo haya mabaya ni miongoni mwa yale yanayolinganiwa na Shetani. Na yoyote yule ambaye Shetani atakuwa ni mwenye kushikamana na yeye, basi mtu mbaya wa kushikamana naye na kufanya naye urafiki ni yeye

    [39] Kwani kuna madhara gani yatakayowafika wao lau walimuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, kiitikadi na kivitendo, na wakayatoa yale Aliyowapa Mwenyezi Mungu kwa kutaka thawabu na kuwa na ikhlasi. Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kuwajua wao na kuyajua wayafanyayo na Atawahesabu kwayo

    [40] Mwenyezi Mungu Hampunguzii yoyote malipo ya matendo yake hata kama ni kadiri ya chungu. Na uwapo huo uzito wa chungu ni jambo jema, basi Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na sifa pungufu, Atamuongezea na kumkuzia mwenye kulifanya, na Atamkirimu kwa nyongeza, kwa kumpa kutoka Kwake thawabu kubwa ambazo ni Pepo

    [41] Vipi itakuwa hali ya watu, Siku ya Kiyama, pindi Mwenyezi Mungu Atakapomleta Mtume wa kila uma, ili atoe ushahidi juu yake kwa yale uliyoyafanya, na atakapo kukuleta wewe, ewe Mtume, utoe ushahidi juu ya uma wako kwamba wewe uliwafikishia ujumbe wa Mola wako

    [42] Siku litakapokuwa hilo, watatamani, wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na wakampinga Mtume wasimtii, lau Mwenyezi Mungu Angaliwafanya sawasawa, wao na ardhi, wakawa mchanga ili wasifufuliwe. Na wao hawawezi kumficha Mwenyezi Mungu chochote kilichoko ndani ya nafsi zao, kwa kuwa Mwenyezi Mungu Atakuwa Amefunga midomo yao na kutolewa ushahidi juu yao na viungo vyao wenyewe kwa yale waliokuwa wakiyafanya

    [43] Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Yake kivitendo, msiikaribie Swala wala msisimame kwenda kusali mkiwa katika hali ya ulevi mpaka muyaelewe na muyajue mnayoyasema. -Hii ilikuwa kabla ya kuthibitishwa uharamu wa pombe katika hali zote-.Na wala msikaribie Swala mkiwa na hadathi kubwa, nayo ni janaba. Na pia, mkiwa na janaba, msizikaribe sehemu za Swala, nazo ni misikiti, isipokuwa kwa mpita njia, katika nyinyi, kutoka kwenye mlango hadi mlango mwingine, mpaka mjitwahirishe kwa kuoga. Na mkiwa katika hali ya ugonjwa, mkawa hamuwezi kutumia maji, au hali ya safari, au mmoja wenu akaja kutoka kwenye haja kubwa au ndogo au mkawaingilia wanawake na msipate maji ya kujisafisha, ujieni mchanga uliyo tohara mjipanguse nao nyuso zenu na mikono yenu. Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha, Anayasamehe makosa yenu na Anawasitiria

    [44] Kwani hukujua, ewe Mtume, mambo ya Mayahudi waliopewa fungu la elimu kwa Taurati iliyowajia, wanatoa uongofu na kuchukua upotevu badala yake, wanaacha hoja na dalili walizonazo zenye kuonesha ukweli wa ujumbe wa Mtume Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, na wanawatakia nyinyi, enyi Waumini, muende kombo na njia iliyolingana ili muwe wapotevu kama wao

    [45] Na Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na sifa pungufu na kutukuka, Anaujua zaidi kuliko nyinyi, enyi Waumini, uadui wa hawa Mayahudi juu yenu. Na inatosha kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Msimamizi wa kuwasimamia, na inatosha kuwa Yeye Ndiye Mnusuru wa kuwanusuru juu ya maadui zenu

    [46] Miongoni mwa Mayahudi kuna kundi lililozoea kuyabadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu na kuyageuza kinyume cha vile yalivyo kwa kumzulia Mwenyezi Mungu urongo na kusema kumwambia Mtume , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, «Tumesikia neno lako na tumeasi amri yako, na sikia kutoka kwetu mwana kutosikia,» na wanasema, «tupe masikizi yako,» yaani, tuelewe na utufahamishe, huku wakizipotoa ndimi zao kwa hilo wakikusudia kumnasibisha na upumbavu, kulingana na lugha yao, na kuitukana dini ya Uislamu. Na lau wao walisema, «Sami'nā wa ata'nā (tumesikia na tumetii),» badala ya kusema «'Aṣaynā» (tumeasi), na walisema «Isma'» (sikia) bila kuongeza «Ghayra musma'» (mwana kutosikia) na walisema, «Unzumā» (tuangalie na utuchunge) badala ya kusema,»Rā'inā», ingalikuwa ni bora kwao mbele ya Mwenyezi Mungu na lingalikuwa ni neno la uadilifu zaidi. Lakini Mwenyezi Mungu Aliwatoa kwenye rehema Yake kwa sababu ya ukafiri wao na kukanusha kwao unabii wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, kwa kuwa hawaamini isipokuwa Imani chache isiyowanufaisha

    [47] Enyi watu wa Kitabu , Aminini na mufuate kivitendo yale tuliyoyateremsha kwenye Qur’ani, yenye kusadikisha Vitabu vilivyoko kwenu, kabla hatujawaadhibu kwa matendo yenu mabaya tukazifuta nyuso na kuzigeuza upande wa migongo au tukawapa laana waharibifu hawa kwa kuwageuza kuwa manyani na nguruwe, kama tulivyowapa laana watu wa Jumamosi ambao walikatazwa kuvua siku hii wasikatazike, Mwenyezi Mungu Akawakasirikia na Akawafukuza kutoka kwenye rehema Yake. Na amri ya Mwenyezi Mungu ni yenye kupita kwa hali yoyote

    [48] Hakika Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Hamghofirii wala Hamsamehe aliyemshirikisha Yeye na yoyote miongoni mwa viumbe Wake au akamkufuru kwa aina yoyote ya ukafiri mkubwa. Lakini Anayasamehe na kuyafuta madhambi yaliyo chini ya ushirikina kwa Anayemtaka miongoni mwa waja Wake. Na yoyote anayemshirikisha Mwenyezi Mungu na mwingine, hakika amefanya dhambi kubwa

    [49] Kwani hukujua, ewe Mtume, hali ya wale wanaojisifu wenyewe na kuyasifu matendo yao kuwa yametakasika na kuwa yako mbali na uovu? Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Peke Yake Ndiye Ambaye Anamsifu Amtakaye miongoni mwa waja Wake, kwa kuwa Yeye Ndiye Ajuwaye ukweli wa matendo yao. Na wala hawatapunguziwa chochote katika matendo yao, hata kama ni kadiri ya uzi ulio kwenye mwanya wa koko ya tende

    [50] Watazame, ewe Mtume, kwa kuyaonea ajabu mambo yao, vipi wanamzulia Mwenyezi Mungu urongo, na hali Yeye Ndiye Anayetakaswa na kila lisilokuwa laiki na Yeye? Uzushi huu unatosha kuwa ni dhambi kubwa lenye kuonyesha wazi itikadi yao mbovu

    [51] Kwani hukujua, ewe Mtume, mambo ya wale Mayahudi waliopewa sehemu ya elimu, wanakiamini kila kiabudiwacho badala ya Mwenyezi Mungu, miongoni mwa masanamu na mashetani wa kibinadamu na wa kijini, imani inayowapelekea wao kuhukumiana kwa sheria isiyokuwa ya Mwenyezi Mungu, na wanasema kuwaambia wale waliomkufuru Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, «Hawa makafiri wako kwenye njia iliyo sawa zaidi na yenye uadilifu zaidi kuliko wale walioamini»

    [52] Hao ndio ambao umezidi uharibifu wao na umeenea upotevu wao. Mwenyezi Mungu,Aliyetukuka, Amewatoa kwenye rehema Yake. Na yoyote ambaye Mwenyezi Mungu Anamfukuza kwenye rehema Yake, hutampatia wa kumnusuru na kumuepushia adhabu mbaya

    [53] Je, kwani wao wana fungu la utawala? Na lau walipewa, hawangalimpa yoyote kitu chochote katika hilo, hata kama ni kadiri ya kitone kilichoko kwenye koko ya tende

    [54] Au je, kwani wao wanamhusudu Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye kwa neema za unabii na utume alizopewa na Mwenyezi Mungu na kuwahusudu Masahaba wake kwa neema ya kuongozwa kwenye Imani, kuukubali utume, kumfuata Mtume na kupewa uwezo katika ardhi, wakawa wanatamani neema hizi ziwaondokee? Hakika sisi tuliwapa watu wa kizazi cha Ibrāhīm, amani imshukiye, Vitabu Alivyoviteremsha Mwenyezi Mungu kwao, wahyi mwingine usiokuwa kitabu chenye kusomwa na tukawapa , pamoja na hayo, utawala wenye kuenea

    [55] Miongoni mwa hawa ambao walipewa fungu la elimu, kuna aliyeamini ujumbe wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye na akafuata Sheria aliyokuja nayo kivitendo. Na miongoni mwao kuna aliyekengeuka na asiitike mwito wake na akawakataza watu kumfuata. Wenye kuwatosha nyinyi, enyi wenye kukanusha, ni moto wa Jahanamu ambao utawashwa kwenu

    [56] Hakika wale waliokanusha aya za Mwenyezi Mungu alizoziteremsha, wahyi wa kitabu Chake, dalili na hoja Zake, tutawaingiza kwenye Moto ambao watalionja joto lake; kila zikiungua ngozi zao tunawageuzia ngozi nyengine, ili adhabu yao na uchungu vipate kuendelea. Mwenyezi Mungu Aliyetukuka ni Mshindi, hakuna chochote chenye kumlemea, ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji mambo Wake na uamuzi Wake

    [57] Na wale ambao nyoyo zao zilitulia kwa kumuamini Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, kuukubali ujumbe wa Mtume Wake, Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, na wakasimama imara juu ya utiifu, tutawaingiza kwenye mabustani ya Pepo ambayo, chini ya majumba yake ya fahari na miti yake, inapita mito. Watastarehe humo milele na hawatatoka humo. Watakuwa na wake humo waliotakaswa na Mwenyezi Mungu na kila maudhi. Na tutawatia kwenye vivuli vilivyoshikana vilivyorefuka Peponi

    [58] Mwenyezi Mungu Anawaamrisha nyinyi kutekeleza aina zote za amana mlizoaminiwa nazo kwa wenyewe, msizifanyie dharau. Na Anawaamrisha muhukumu baina ya watu kwa uadilifu na uhaki, mtakapohukumu baina yao.Hilo ni jambo bora zaidi Analowaidhia Mwenyezi Mungu na kuwaongoza mlifanye. Hakika Mweyezi Mungu Aliyetukuka ni Msikizi wa maneno yenu, Anayajua matendo yenu na Anayaona

    [59] Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Yake kivitendo, zikubalini amri za Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na wala msimuasi, mkubalini Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, kwa yale Aliyokuja nayo ya haki na watiini watawala wa mambo yenu isipokuwa katika kumuasi Mwenyezu Mungu. Na mnapotafautiana baina yenu katika kitu chochote, basi irudisheni hukumu yake kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na Sunnah ya Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, iwapo nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na Siku ya Mwisho Imani ipasavyo. Kurudisha huko kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunnah ni bora kwenu kuliko kubishana na kusema kwa maoni, na ni mazuri kabisa marejeo yake na mwisho wake

    [60] Kwani hukujua, ewe Mtume, mambo ya wale wanafiki wenye kudai kuwa wameyaamini yale uliyoteremshiwa, nayo ni Qur’ani, na yale waliyoteremshiwa Mitume kabla yako, ilhali wao wanataka kuhukumiwa, katika ugomvi unaotokea baina yao, kwa sheria ya batili, isiyowekwa na Mwenyezi Mungu, na wao waliamrishwa kuikataa batili? Shetani anataka kuwaepusha na njia ya haki na kuwaweka mbali nayo kabisa. Katika aya hii kuna dalili kwamba Imani ya kweli inalazimu kufuata sheria ya Mwenyezi Mungu na kuitumia katika kutoa uamuzi juu ya kila jambo. Kwa hivyo, mwenye kudai kuwa ni Muumini na akachagua uamuzi wa Shetani juu ya uamuzi wa Mwenyezi Mungu, huwa ni Mrongo katika madai yake

    [61] Na hawa wanaponasihiwa na kuambiwa, «Njooni kwenye yale yaliyoateremshwa na Mwenyezi Mungu na kwa Mtume na uongofu wake», utawaona wale wenye kudhihirisha Imani na kuficha ukafiri, wanakugeuka na kukupa mgongo

    [62] Hali ya wanafiki hawa itakuwa namna gani, watakapofikiwa na misiba kwa sababu ya makosa yaliyotendwa na mikono yao kisha wakakujia, ewe Mtume, wakitoa udhuru na kukuhakikishia kwamba wao hawakuwa na malengo yoyote, kwa matendo yao hayo, isipokuwa ni kutenda wema na kuleta upatanishi baina ya wagomvi

    [63] Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu Anaujua uhakika unafiki ulio ndani ya nyoyo zao. Basi jiepushe nao, uwaonye ubaya wa mambo waliyonayo na uwaambie maneno yenye kuwaathiri kwa njia ya kuwakemea

    [64] Hatukumtumiliza Mtume yoyote, miongoni mwa Mitume wetu, isipokuwa ni afuatwe kwa amri ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na uamuzi Wake. Na lau kwamba hawa waliojidhulumu nafsi zao kwa kutenda mabaya, walikujia, ewe Mtume, katika uhai wako, hali ya kutubia na kumuomba Mwenyezi Mungu Awasamehe madhambi yao, nawe ukawaombea msamaha, wangalimkuta Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kukubali toba, ni Mwingi wa kurehemu

    [65] Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Anaapa kwa nafsi Yake tukufu, kwamba hawa hawataamini kikweli mpaka wakufanye wewe ni hakimu kwenye ugomvi unaotokea baina yao katika uhai wako na watake uamuzi wa Sunnah yako baada ya kufa kwako, kisha wasiingiwe na dhiki katika nafsi zao kwa matokeo ya hukumu yako, na wakwandame, pamoja na hivyo, kwa kukufuata kikamilifu. Kutoa uamuzi kulingana na aliyokuja nayo Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, kutoka kwenye Qur’ani na Sunnah katika kila jambo katika mambo ya kimaisha, pamoja na kuridhika na kusalimu amri, ni miongoni mwa uthabiti Imani

    [66] Na lau tuliwalazimisha wanafiki hawa, wenye kuhukumiana kwa taghut (sheria zisizokuwa za Mwenyezi Mungu), wauane wao kwa wao au watoke kwenye majumba yao, hawangalifuata amri hiyo isipokuwa wachache katika wao. Na lau kwamba wao walikubali nasaha walizonasihiwa, hilo lingalikuwa ni lenye kuwanufaisha na ni lenye kutia nguvu zaidi Imani yao

    [67] na tungaliwapa thawabu kubwa kutoka kwetu, duniani na Akhera

    [68] na tungaliwaongoza wao na kuwalekeza njia ya Mwenyezi Mungu iliyo ya sawa

    [69] Na mwenye kukubali amri za Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na uongofu wa Mtume Wake Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, basi hao ni wale ambao wana utukufu wa mambo na vyeo. Wao watakuwa pamoja na wale waliopewa neema na Mwenyezi Mungu miongoni mwa Mitume na wakweli wa Imani, ambao kuamini kwao yaliyoletwa na Mitume kulikamilika kiitikadi, kimaneno na kivitendo na mashahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu na Waumini wema. Na wazuri wa marafiki wa mtu kuwa nao Peponi ni hao

    [70] Vipewa vingi hivyo vinatoka kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake. Na inatosha kuwa Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Anazijua hali za waja Wake na Anawajua wenye kustahiki thawabu nyingi kati yao kwa matendo mema waliyoyafanya

    [71] Enyi mlioamini, kuweni na hadhari kwa kujiandaa na adui yenu, tokeni kupambana naye kundi baada ya kundi au mkiwa pamoja

    [72] Hakika miongoni mwenu kuna watu wenye kujichelewesha kutoka kuenda kupambana na maadui kwa kuona uzito kufanya hivyo, na kufanya bidii kuwavunja moyo wengine kwa kusudi. Itokeapo mkapatikana kuuawa na kushindwa, huwa wakisema kwa furaha, «Mwenyezi Mungu Ametulinda kwa kutokuwako na wale waliopatikana na mambo ambayo nafsi zetu zinayachukia.» Na hilo la kutokuwa na nyinyi huwa likiwafurahisha

    [73] Na itokeapo mkapata fadhila za Mola wenu na ngawira, wao wanasema, kwa uhasidi na majuto, kama kwamba hakukuwa na mapenzi ya waziwazi baina yenu, «Laiti mimi nilikuwa pamoja na wao nikafaulu kupata yale waliyoyapata: ya kuokoka, ushindi na ngawira.»

    [74] Basi na wapigane jihadi, katika njia ya kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu na kulitukuza neno Lake, wale wanaouza uhai wa dunia kwa Akhera na thawabu zake. Na yoyote mwenye kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kidhati, akauawa au akashinda, basi tutampa malipo makubwa

    [75] Na ni lipi linalowazuia, enyi Waumini, kupigana jihadi katika njia ya kuitetea dini ya Mwenyezi Mungu na kuwatetea waja Wake wanaodhalilishwa, miongoni mwa wanaume na wanawake na watoto waliodhulumiwa, na ambao hawana ujanja wala njia ya kufanya isipokuwa ni kumtaka Mola wao Awnusuru wakimuomba kwa kusema, «Mola wetu, tutoe kwenye mji huu (Makkah) ambao watu wake wamejidhulumu nafsi zao kwa kukufuru na wamewadhulumu Waumini kwa kuwakera, na utuletee kutoka Kwako msimamizi wa kusimamia mambo yetu na mtetezi wa kututetea dhidi ya madhalimu»

    [76] Wale walio wakweli katika Imani zao, kiitikadi na kivitendo, wanapigana jihadi katika njia ya kuitetea haki na watu wake, na wale waliokufuru wanapigana katika njia ya uonevu na uharibifu katika ardhi. Basi wapigeni vita watu wa ukafiri na ushirikina wanaomfuata Shetani na kutii amri yake. Hakika mipango ya Shetani anayowapangia wafuasi wake ni dhaifu

    [77] Kwani hukujua, ewe Mtume, mambo ya wale walioambiwa, kabla ya kuruhusiwa kupigana jihadi, «Izuieni mikono yenu kupigana na maadui wenu washirikina. Na jilazimisheni kutekeleza yale mliyofaradhiwa ya Swala na Zaka»? Na Mwenyezi Mungu Alipowafaradhia kupigana, kulitokea kundi la watu katika wao iliobadilika hali yao wakawa wana kicho cha kuwaogopa watu kama vile wanavyomuogopa Mwenyezi Mungu au zaidi na wakawa wanaidhihirisha hofu kubwa iliyowaingia na kusema, «Ewe Mola wetu, kwa nini ulitufaradhia kupigana? Lau wewe ulitupa muhula mpaka muda mchache.» Wakitumai kupata starehe ya maisha ya ulimwengu. Waambie, ewe Mtume, Starehe ya ulimwengu ni chache, na Akhera na yaliyomo ndani ni makubwa zaidi na ni yenye kusalia zaidi kwa mwenye kuwa na uchamungu, akafanya aliyoamrishwa na akajiepusha na aliyokatazwa. Na Mola wako Hatamdhulumu yoyote, hata kama ni kadiri ya uzi unoakuwako kwenye mwanya wa koko ya tende

    [78] Popote mliopo mtafikiwa na kifo, pawe ni mahali popote pale mnapokuwa, muda wenu ukikoma, hata kama mupo ndani ya ngome zilizoimarishwa zilizoko mbali na kiwanja cha mapambano na mapigano. Na wakipatikana na mambo ya kuwafurahisha ya starehe ya maisha haya (ya ulimwenguni), wanayanasibisha kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kuwa Ndiye Aliyewapatia, na watokewapo na matukio wanayoyachukia, wanayanasibisha kwa Mtume Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kuwa yamesababishwa na yeye kwa ujinga wao na kwa fikira zao kuwa yeye amewaletea nuhusi. Na hawakujua kwamba yote yanatokana na Mwenyezi Mungu Peke Yake, kwa uamuzi Wake na makadirio Yake. Basi kwa nini wao hawakaribii kuelewa maneno yoyote unayowaelezea

    [79] Chochote kinachokupata, ewe binadamu, cha wema na neema, kinatoka kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Peke Yake, kwa ukarimu na hisani. Na chochote kinachokufika cha tabu na mashaka ni kwa sababu ya vitendo vyako vibaya na makosa na madhambi yaliyotendwa na mikono yako miwili. Na tumekutumiliza, ewe Mtume, kuwa ni Mtume kwa watu wote uwafikishie ujumbe wa Mola wako. Na inatosha kuwa Mwenyezi Mungu ni shahidi juu ya ukweli wa utume Wako

    [80] Yoyote mwenye kumkubali Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, na akafuata uongofu wake kivitendo, basi amemkubali Mwenyezi mungu Aliyetukuka na amefuata amri Yake. Na yoyote aliyekataa kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, basi hatukukutumiliza, ewe Mtume, kwa hawa wenye kukataa uwe ni mtunzi wa kuyadhibiti matendo yao na kuwahesabu kwa hayo. Hesabu yao ni juu yetu

    [81] Na hawa wenye kukataa, wakiwa kwenye baraza ya Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, wanajidhihirisha kuwa wanamtii Mtume na kuyafuata yale aliyokuja nayo, na wakiwa mbali na yeye na wakaondoka kwenye baraza yake, linatoka kundi katika wao likapanga njama kinyume cha yale waliyoyadhihirisha ya kumtii. Na wao hawakujua kwamba Mwenyezi Mungu Anadhibiti hesabu ya yale wanayoyapanga na kwamba Yeye Atawalipa kwa hayo malipo kamili. Basi wape mgongo na usiwajali, kwani wao hawatakudhuru. Na tegemea kwa Mwenyezi Mungu, kwani yeye Peke Yake Ndiye Mwenye kukutosha kwa usimamizi na utetezi

    [82] Kwani hawa hawaiangalii Qur’ani na haki iliyokuja nayo, kwa kuitaamali na kuizingatia, namna ilivyokuja kwa utaratibu uliopangika unaomfanya mtu awe na yakini kuwa inatoka kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake? Na lau yalikuwa yatoka kwa asiyekuwa Yeye, wangalipata ndani yake tafauti kubwa

    [83] Na likiwajia, hawa ambao Imani haijakita ndani ya nyoyo zao, jambo ambalo inapasa lifichwe linalofungamana na usalama, ambao heri yake itarudi kwa Uislamu na Waislamu, au hofu, ambayo inatia babaiko ndani ya nyoyo zao, wanalitoa nje na kulitangaza kwa watu. Na lau wao walilipeleka, lile liliowajia, kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye na kwa wenye ujuzi na ufahamu, wangaliujua uhakika wake wale wachambuzi kati yao. Na lau si Mwenyezi Mungu kuwafanyia wema na kuwaonea huruma, Mungalimfuata Shetani na mawazo mnayotiwa naye, isipokuwa wachache katika nyinyi

    [84] Basi pigana jihadi, ewe Nabii, katika njia ya Mwenyezi Mungu na kulitukuza neno Lake. Hulazimishwi kitendo cha asiyekuwa wewe wala hutaadhibiwa kwacho. Na wahimize Waumini kupigana jihadi na uwavutie wafanye hivyo, kwani huenda Mwenyezi Mungu Akazuia, kwa ajili yako na wao, mashambulizi ya makafiri na nguvu zao. Na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Ana nguvu nyingi zaidi na Ana adhabu kubwa zaidi kwa makafiri

    [85] Mwenye kumshughulikia mwingine apate mema, atapata fungu la thawabu kwa huko kuingilila kwake kati. Na mwenye kujishughulisha juu ya kumdhuru mwingine, Atapata fungu la mzigo wa dhambi. Na Mwenyezi Mungu ni Shahidi na ni Mtunzi wa kila jambo

    [86] Na Muislamu akiwatolea salamu, muitikieni kwa maneno mazuri zaidi na kwa furaha zaidi, au muitikieni salamu kama vile alivyowatolea. Na kila mmoja ana thawabu zake na malipo yake. Hakika Mwenyezi Mungu Aliyetukuka ni Mwneye kulipa kwa kila kitu (mnachokifanya)

    [87] Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Aliyepwekeka kwa uungu wa viumbe wote, Ndiye Atakayewakusanya nyinyi Siku ya Kiyama isiyokuwa na shaka, kwa kuhesabiwa na kulipwa. Na hakuna yoyote mkweli zaidi wa maneno anayoyatolea habari kuliko Mwenyezi Mungu

    [88] Muna nini nyinyi, enyi Waumini, mumetafautiana makundi mawili kuhusu wanafiki: kundi linasema kwamba wapigwe vita na lingine halisemi hivyo? Na hali Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Amewatia kwenye ukafiri na upotevu kwa sababu ya vitendo vyao. Kwani mnataka kumpa uongofu yule ambaye Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Ameuepusha moyo wake na dini Yake? Na yoyote ambaye Mwenyezi Mungu Ameacha kumuafikia kufuata dini Yake na yale Aliyoyaamrisha, basi hana njia ya kufikia kwenye uongofu

    [89] Hawa wanafiki waliwatamania nyinyi Waumini lau mlikanusha uhakika wa lile ambalo nyoyo zenu zimeliamini kama vile wao walivyolikanusha kwa nyoyo zao, ili muwe sawa na wao katika kukanusha. Basi msiwafanye ni wasafiwa wenu mpaka wagure katika njia ya Mwenyezi Mungu kama ushahidi wa ukweli wa Imani yao. Basi wakiyakataa yale waliyolinganiwa kwayo, washikeni popote waliopo na muwaue, wala msimfanye yoyote katika wao kuwa ni msimamizi badala ya Mwenyezi Mungu wala ni mwokozi ambaye mnataka awaokoe

    [90] Lakini wale wanaofungamana na watu ambao baina yenu na wao pana ahadi na mapatano, msipigane nao. Pia msipigane na wale waliowajia na nyonyo zao zina dhiki, hawataki kupigana na nyinyi na pia hawataki kupigana na watu wao, wakawa hawako na nyinyi wala hawako na watu wao, basi msipigane nao. Na lau Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Alitaka, Angaliwapa nguvu juu yenu wakashirikiana na maadui zenu washirikina katika kupigana na nyinyi. Lakini Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Aliwaepusha nanyi kwa fadhila Zake na uwezo Wake. Basi wakiwaacha wasipigane na nyinyi na wakawafuata na kujisalimisha kwenu, hamna njia yoyote ya kupigana na wao

    [91] Mtawapata watu wengine miongoni mwa wanafiki wanapenda kuzituliza nafsi zao upande wenu kwa kuwaonyesha kuwa wana Imani na pia wanapenda kujituliza upande wa watu wao walio makafiri kwa kuwaonyesha kuwa wao wako kwenye ukafiri. Kila wakirudishwa kwenye mahali pa ukafiri na makafiri, huingia kwenye hali mbaya zaidi. Basi hawa wasipojiepusha na nyinyi, wakajisalimisha kwenu kikamilifu na wakajizuia wasipigane na nyinyi, washikeni kwa nguvu na muwaue popote waliopo. Wale ndio ambao waliofikia, katika njia hii mbaya sana, kiasi cha kuwapambanua wao na wasiokuwa wao; wao ndio ambao tumewapa nyinyi hoja iliyo wazi ya kuwaua na kuwateka

    [92] Si haki kwa yoyote aliyeamini kumfanyia uadui ndugu yake aliyeamini kwa kumuua bila haki isipokuwa afanye hilo kimakosa kwa kutokusudia. Na yoyote ambaye kosa hilo lilitokea kwake, basi ni juu yake aache huru shingo iliyoamini na atoe dia iliyokadiriwa kiwango chake kuwapa mawalii wa aliyeuawa, isipokuwa iwapo watamuachia kwa njia ya sadaka na watamsamehe. Iwapo muuliwa anamuamini Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na anaiamini haki aliyoteremshiwa Mtume Wake Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na akawa ni katika ukoo wa watu makafiri ambao ni maadui wa Waislamu, basi ni juu ya muuaji aache huru shingo iliyoamini. Na iwapo muuliwa ni miongoni mwa watu ambao baina yenu na wao kuna ahadi na mapatano, basi ni juu ya yule aliyemuua, ili Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Amkubalie toba yake, aache huru shingo iliyoamini; asipopata uwezo wa kuacha huru shingo iliyoamini, ni juu yake afunge miezi miwili yenye kufuatana. Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, ni Mjuzi wa hakika ya mambo ya waja Wake, ni Mwenye hekima katika sheria Zake Alizowawekea

    [93] Na mwenye kumfanyia uadui Muumini akamuua kwa kusudi pasi na haki, mwisho wake atakaoishia ni Jahanamu, hali ya kukaa milele humo, pamoja na kukasirikiwa na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kufukuzwa kwenye rehema Yake, iwapo Mwenyezi Mungu Atamlipa kwa kosa lake. Na Mwenyezi Mungu Amemuandalia adhabu kali zaidi kwa uhalifu huu mkubwa aliyoufanya. Lakini Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu, Atawasamehe na kuwafadhili wenye Imani kwa kutowapa malipo ya kukaa milele ndani ya Jahanamu

    [94] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo, mnapotoka kwenye ardhi hali ya kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, kuweni na uangalifu wa mnayoyafanya na mnayoyaacha. Na msimkanushie Imani yoyote ambaye imedhihiri kwake chochote katika alama za Uislamu na akawa hakuwapiga vita nyinyi, sababu pana uwezekano ya kuwa yeye ni Muumini anayeificha Imani yake. Msifanye hivyo kwa kutaka starehe za uhai wa kilimwengu kwani kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka pana nyongeza na vipewa vinavyowatosha. Na nyinyi mlikuwa hivyo mwanzo wa Uislamu, mkiificha Imani yenu kwa jamaa zenu washirikina, kisha Mwenyezi Mungu Akawaneemesha na Akawatukuza kwa Imani na kwa nguvu Alizowapa. Basi kuweni kwenye ubainifu na ujuzi katika mambo yenu. Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa matendo yenu yote, ni Mwenye kuyaona mambo yenu ya ndani, na Atawalipa kwayo

    [95] Wenye kusalia nyuma wakaacha kuhudhuria jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, isipokuwa wenye nyudhuru kati yao, hawalingani na wenye kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao. Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Amewafadhilisha wenye kupigana jihadi juu ya wenye kukaa na Ameitukuza daraja yao Peponi kwa kiwango cha juu. Na Mwenyezi Mungu Amewaahidi wote: wenye kupigana jihadi kwa mali yao na kwa nafsi zao na wenye kukaa, miongoni mwa watu wenye nyudhuru, kwa kutoa kwao na kujitolea katika njia ya haki. Na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Amewafadhilisha wale wenye kupigana jihadi juu ya wenye kukaa kwa kuwapa thawabu nyingi

    [96] Thawabu nyingi hizi ni daraja za juu, katika mabustani ya Pepo, zitokazo kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, walizopewa waja Wake maalumu wenye kupigana katika njia Yake, na msamaha wa madhambi yao na rehema kunjufu ambayo ndani yake wananeemeshwa. Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa anayetubia Kwake na kurejea, ni Mwingi wa rehema kwa wenye kumtii, wenye kupigana jihadi katika njia Yake

    [97] Hakika wale ambao Malaika waliwafisha na wao wako katika hali ya kujidhulumu wenyewe kwa kukaa katika nchi ya ukafiri na kuacha kuhama, Malaika watawaambia kwa njia ya kuwalaumu, «Mlikuwa katika nini kuhusu mambo ya Dini yenu?’ watasema, «Tulikuwa wanyonge nchini kwetu, tumelemewa kuweza kujiepushia dhuluma na maonevu.» Malaika watawaambia kwa njia ya kuwalaumu, «Kwani ardhi ya Mwenyezi Mungu haikuwa kunjufu mkatoka kwenye ardhi yenu mkaenda ardhi nyingine ambapo mtaaminika na Dini yenu?» Basi hao makao yao ni Moto. Na haya ni makao mabaya ya mtu kuishilia

    [98] Wataepushwa na mwisho huo wakongwe wanaume na wanawake na watoto ambao hawawezi kujiondolea udhalimu na uonevu na hawajui njia yoyote ya kuwaokoa wao na mateso

    [99] Wanyonge hawa ndio wanaotarajiwa kupata msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, kwa kuwa Yeye Anaujua uhakika wa mambo yao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha, Anawasamehe makosa yao na Anawafinikia na kuwasitiria

    [100] Na yoyote mwenye kutoka kwenye ardhi ya ushirikina kwenda kwenye ardhi ya Uislamu kwa ajili ya kukimbia na dini Yake, akitaraji fadhila za Mola wake na akikusudia kuinusuru dini Yake, atapata katika ardhi mahali pa kuelekea ambapo ataneemeka, pawe ni sababu ya yeye kupata nguvu na maadui zake kuwa wanyonge, pamoja na kupata ukunjufu wa riziki na maisha. Na yoyote mwenye kutoka nyumbani kwake kwa lengo la kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye na kulitukuza neno la Mwenyezi Mungu kisha akapatikana na kifo kabla ya kufikia lengo lake, basi malipo ya kitendo chake yameshathibiti kwa Mwenyezi Mungu, kwa fadhila Zake na wema Wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha, ni Mwingi wa huruma kwa waja Wake

    [101] Na mnaposafiri, enyi Waumini, kwenye ardhi ya Mwenyezi Mungu, hamuna makosa wala dhambi kukupunguza Swala, mkiogopa kufanyiwa uadui na makafiri mkiwa kwenye Swala. Safari nyinygi za Waislamu, katika mwanzo wa Uislamu, zilikuwa za kutisha. Na kupunguza Swala ni ruhusa iliyotolewa kwenye safari, katika hali ya amani au vitisho. Hakika makafiri ni wenye kudhihirisha uadui wao kwenu, basi jihadharini nao

    [102] Na ukiwa, ewe Nabii, kwenye kiwanja cha vita na ukataka kuswalisha, basi kundi moja lisimame nawe ili kuswali, huku wakiwa wameshika silaha zao. Watu wa kundi hili wakiwa kwenye sijda, basi lije kundi lingine liwe nyuma yenu likiwa limeelekea upande wa adui wenu. Watu wa kundi la kwanza watimize rakaa ya pili na kutoa salamu. Kisha watu wa kundi lingine, ambalo bado halijaanza kuswali, waje kukufuata katika rakaa yao ya kwanza, kisha wamalize wenyewe rakaa yao ya pili. Na wajihadhari na adui wao na washike silaha zao. Kwani wenye kukanusha dini ya Mwenyezi Mungu wanatamani mughafilike na silaha zenu na vyombo vyenu wapate kuwashambulia kwa mara moja na kuwaua. Na hamuna makosa, kukiwa na mvua yenye kuwasumbua au mkawa wagonjwa, kuaacha silaha zenu pamoja na kuwa na hadhari. Hakika Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Amewaandalia wenye kuikanusha dini Yake adhabu ya kuwatweza na kuwadhalilisha

    [103] Mtakapomaliza Swala, endeleeni kumtaja Mwenyezi Mungu katika hali zenu zote. Na hali ya kicho iondokapo, itekelezeni Swala kikamilifu, wala msiifanyie dharau, kwani Swala ni faradhi katika nyakati zijulikanazo katika Sheria

    [104] Wala msiwe walegevu katika kuwatafuta maadui wenu na kupigana nao. Mkiwa mnahisi uchungu wa vita na matokeo yake, basi maadui wenu pia wanahisi uchungu wake zaidi, na pamoja na hivyo, hawakomi kupigana nanyi. Basi nyinyi ni aula kwa hilo kuliko wao, kwa kuwa nyinyi mnatarajia thawabu, nusura na kupewa nguvu, na wao hawatarajii hayo. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa hali zenu zote, ni Mwenye hekima katika maamrisho Yake na uendeshaji mambo Wake

    [105] Sisi tumekuteremshia Qur’ani, ewe Muhammad, iliyokusanya haki, ili utoe uamuzi baina ya watu wote kwa wahyi ambao Mwenyezi Mungu Amekuletea na Akakufahamisha. Basi usiwe ni mwenye kuwatetea wale wanaozifanyia hiana nafsi zao, kwa kuificha haki, kwa kuwa wamekudhihirishia maneno yaliyo kinyume na ukweli

    [106] Na utake msamaha kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka katika hali zako zote. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe kwa wanaotarajia nyongeza za mema Yake na vipewa vya msamaha Wake, ni Mwingi wa huruma kwao

    [107] Na usiwatetee wanaozifanyia hiana nafsi zao kwa kumuasi Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na sifa za upungufu, Hampendi yule ambaye hiana yake imekuwa kubwa na dhambi zake zimekuwa nyingi

    [108] Wao wanajificha na watu ili wasipate kuyaona matendo yao mabaya, wala hawajifichi na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka wala hawamuonei haya, ilhali Yeye, Mtukufu wa mambo, Yupo na wao kwa ujuzi Wake, Anawaona wanapopanga, kipindi cha usiku, maneno Asiyoridhika nayo. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ameyazunguka(kwa ujuzi Kwake) maneno yao yote na vitendo vyao vyote, hakuna kitu chochote chenye kufichika Kwake

    [109] Haya nyinyi, enyi Waumini, mnatoa hoja za kuwatetea hawa mahaini wa nafsi zao katika huu uhai wa kilimwengu. Basi, ni nani mwenyemuhoji Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa kuwatetea wao Siku ya kufufuliwa na kuhesabiwa? Au ni nani atakayekuwa wakili wao Siku ya Kiyama

    [110] Na mwenye kufanya tendo baya au akajidhulumu nafsi yake kwa kufanya mambo yaliyo kinyume na hukumu ya Mwenyezi Mungu na sheria Yake, kisha akarudi kwa Mwenyezi Mungu kwa kujuta kwa aliyoyafanya akitaraji Amsamehe na dhambi zake Amsitirie, basi atamkuta Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha na ni mwingi wa huruma kwake

    [111] Na Mwenye kufanya dhambi kwa kusudi, hakika huwa akijidhuru nafsi yake peke yake. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ni Mjuzi wa uhakika wa mambo ya waja Wake, ni Mwingi wa hekima katika hukumu Zake Azitowazo kwa waja Wake

    [112] Na mwenye kufanya kosa bila kukusudia au akatenda dhambi kwa kusudia kisha akamsingizia, yale aliyoyafanya, mtu asiye na hatia, atakuwa amebeba urongo na dhambi zilizo wazi

    [113] Na lau si Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kukuneemesha, ewe Mtume, kukurehemu kwa neema ya unabii na kukuhifadhi, kwa taufiki Yake, kwa wahyi Aliokuletea, wangaliazimia watu, miongoni mwa wale wanaozifanyia hiana nafsi zao, kukupotosha na njia ya haki. Na wao kwa kufanya hivyo, huwa hawampotoshi yoyote isipokuwa nafsi zao. Na hawawezi kukudhuru kwa kuwa Mwenyezi Mungu Amekuhifadhi, Amekuteremshia Qur’ani na Sunnah yenye kuifafanua, na Amekuongoza ukajua elimu ambayo hukuwa ukiijua hapo nyuma. Na fadhila za Mwenyezi Mungu Alizokuhusisha nazo ni jambo kubwa

    [114] Hakuna manufaa katika mengi ya maneno ya watu ya siri baina yao, isipokuwa yawapo ni mazungumzo yenye kuita kwenye kufanya mema ya utoaji sadaka au maneno mazuri au kuleta upatanishi baina ya watu. Na mwenye kuyafanya mambo hayo, kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, akitarajia thawabu Zake, tutampa thawabu nyingi zilizo kunjufu

    [115] Na mwenye kuenda kinyume na Mtume , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye baada ya kubainikiwa na haki na akafuata njia isiyokuwa njia ya Waumini na haki ambayo wako nayo, basi tutamuacha na muelekeo wake, hatutamuongoza kwenye heri na tutamtia ndani ya Moto wa Jahanamu, akiteseka kwa joto lake. Ni mabaya yaliyoje marejeo haya kuwa ndio mwisho wa mtu

    [116] Hakika Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Hasamehe Akishirikishwa na Anasamehe madhambi yaliyo chini ya ushirikina kwa Anayemtaka miongoni mwa waja Wake. Na mwenye kumfanyia Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Aliye Mmoja, Aliye Pekee, mshirika yoyote, miongoni mwa waja Wake, atakuwa yuko mbali sana na haki

    [117] Vile wanavyoviabudu washirikina badala ya Mwenyezi Mungu si chochote isipokuwa ni masanamu yasiyonufaisha wala kudhuru, na hawaabudu isipokuwa Shetani aliyemuasi Mwenyezi Mungu aliyefikia kiasi kikubwa cha kuharibika na kuharibu

    [118] Mwenyezi Mungu Alimfukuza kwenye rehema Yake. Na Shetani Akasema, «Nitalichukua fungu maalumu la waja wako niwapoteze kimaneno na kivitendo

    [119] «Na nitawaepusha na haki wenye kunifuata, nitawaahidi kwa urongo mambo wanayoyatamani, nitawaita wayakate na kuyapasua masikio ya wanyama-hoa kwa kuwapambia walifanye jambo hili la ubatili na nitawalingania wageuze umbo la Mwenyezi Mungu Alilowaumbia nalo katika tabia za kimaumbile na hali ya viumbe vile walivyo.» Na mwenye kukubali mwito wa Shetani na kumfanya yeye ndiye muokozi wake badala ya Mwenyezi Mungu, ameangamia maangamivu yaliyo wazi

    [120] Shetani anawaahidi wafuasi wake ahadi za urongo na anawavutia kwa matamanio ya urongo yenye udanganyifu; ahadi zake kwao hazikuwa isipokuwa ni udanganyifu usio na ukweli wala dalili

    [121] Hao marejeo yao ni Jahanamu; na hawatapata mapenyo wala mahali pa kukimbilia ili kuepukana nayo

    [122] Na wale waliokuwa wakweli katika kumuamini kwao Mwenyezi Mungu, Aliyetukua, na wakafuatanisha Imani yao na matendo mema, basi Mwenyezi Mungu Atawaingiza, kwa ukarimu Wake, ndani ya mabustani ya Pepo ambayo chini ya majumba yake ya fahari na miti yake inapita mito, hali ya kukaa milele humo. Hiyo ni ahadi inayotoka kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ambaye Haendi kinyume na ahadi Yake. Na hapana yoyote aliye mkweli zaidi, katika neno lake na ahadi yake, kuliko Mwenyezi Mungu Aliyetukuka

    [123] Fadhila hizi kubwa hazipatikani kwa matamanio mnayoyatamani, enyi Waislamu, wala kwa matamanio ya Mayahudi na Wanaswara waliopewa Kitabu. Hakika zinapatikana kwa kumuamini Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kikweli na kuyafanya vizuri matendo ya kumridhisha. Na yoyote mwenye kufanya tendo baya, atalipwa kwalo, na hatompata, asiyekuwa Mwenyezi Mungu, mtegemewa mwenye kusimamia mambo yake wala msaidizi mwenye kumnusuru na kumuepushia adhabu mbaya

    [124] Na mwenye kufanya matendo mema, awe ni mwanamume au mwanamke, hali ya kuwa anamuamini Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na haki Aliyoiteremsha, basi hao Mwenyezi Mungu Atawaingiza Peponi, nyumba ya starahe ya daima, na hawatopunguziwa chochote katika thawabu za matendo yao, hata kama ni kadiri ya kitone kilichoko kwenye koko ya tende

    [125] Hakuna yoyote aliye mwema wa dini kuliko yule aliyejisalimisha kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Peke Yake, kwa moyo wake na viungo vyake vyote, hali ya kuwa ni mwema wa maneno na vitendo, mwenye kufuata amri ya Mola wake, akawa amefuata mila ya Ibrāhīm na Sheria aliyoileta na amejiepusha na itikadi mbaya na sheria zilizo batili. Na Mwenyezi Mungu Alimteua Ibrāhīm, rehema na amani zimshukiye, na Akamfanya ni msafiwa Wake miongoni mwa viumbe Wake. Katika aya hii pana kuthibitisha sifa ya al-khullah (ubui) kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, nao ni daraja ya juu kabisa ya mapenzi na uteuzi

    [126] Ni vya Mwenyezi Mungu viumbe vyote vilivyoko ulimwenguni. Hivyo ni milki Yake, Aliyetukuka, Peke Yake. Na Mwenyezi Mungu Amekizunguka kila kitu, hakuna kitu chochote, katika mambo ya waja Wake, chenye kufichika Kwake

    [127] Watu wanakutaka, ewe Nabii, uwaelezee mambo yaliyowatatiza kuyafahamu yanayowahusu wanawake na hukumu zao. Sema, «Mwenyezi Mungu Anawafafanulia kuhusu mambo yao na yale mnayosomewa ndani ya Qur’ani kuhusu mayatima wa kike ambao hamuwapi mafungu yao waliyoandikiwa na Mwenyezi Mungu ya mahari, mirathi na haki nyiginezo, na mkawa mnapenda kuwaoa au hamuna hamu ya kuwaoa. Na pia Mwenyezi Mungu Anawafafanulia kuhusu mambo ya madhaifu miongoni mwa watoto na ulazima wa kuwasimamia mayatima kwa uadilifu na kuacha kuwafanyia maonevu kwa kuwanyima haki zao. Na wema wowote mnaoufanya, Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anaujua, hakuna kinachofichika Kwake kuhuso huo na mwengineo

    [128] Na mwanamke akijua kuwa mumewe ana majivuno na madharau na hashughuliki naye, si makosa kwa wao wawili kusikilizana kwa namana ya kuwaridhisha wao wawili kuhusu kugawa siku na matumizi. Kwani masikilizano ni bora zaidi na ni afadhali zaidi. Na nafsi zimeumbwa zikiwa na tabia ya pupa na ubahili, kama kwamba ubahili upo mbele ya hizo nafsi, hauepukani nazo. Na mkiamiliana na wake wenu vizuri na mkamcha Mwenyezi Mungu juu yao, basi Mwenyezi Mungu ni Mjuzi sana wa mnayoyafanya, katika hayo na mengineyo, hakuna kinachofichika Kwake, na Atawalipa kwa hayo

    [129] Na hamtaweza, enyi wanaume, kuhakikisha uadilifu kamili wa mapenzi na muelekeo wa moyo kati ya wanawake, namna mtakavyofanya bidii juu ya hilo. Basi msimpe mgongo, yule msiokuwa na haja naye, kabisa-kabisa mkamuacha akawa ni kama mwanamke ambaye hana mume wala hakutalikiwa, mkaja mkapata madhambi. Na mkizitengeneza amali zenu mkafanya uadilifu katika ugawaji wenu baina ya wake zenu na mkamchunga Mwenyezi Mungu mkamuogopa juu yao, basi Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa waja Wake, ni Mwingi wa huruma kwao

    [130] Na ukitokea utengano baina ya mwanamume na mkewe, Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika, atamtosheleza kila mmoja kati yao kwa fadhila Zake na ukunjufu wa neema Zake. Kwani Yeye, Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu na Aliyetukuka, ni Mkunjufu wa fadhila na neema, ni Mwingi wa hekima katika hukumu Zake Anazozipitisha kwa waja Wake

    [131] Ni milki ya Mwenyezi Mungu vilivyoko kwenye mbingu na vilivyoko kwenye ardhi na vilivyoko baina ya hivyo viwili. Na tuliwausia wale waliopewa Vitabu kabla yenu, miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara, na tukawausia nyinyi pia, enyi ummah wa Muhammad, mumche Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na msimame kutekeleza amri Zake na kuepuka makatazo Yake, na tukawaelezea kwamba nyinyi mkiukanusha upweke wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na sheria Zake, basi Mwenyezi Mungu Hawahitajii nyinyi, kwa kuwa vyote vilivyoko kwenye mbingu na vilivyoko kwenye ardhi ni Vyake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha kutowahitjia viumbe Wake, ni Mwingi wa kuhimidiwa katika sifa Zake na vitendo Vyake

    [132] Ni milki ya Mwenyezi Mungu viumbe vilivyoko katika ulimwengu huu. Na inatosha kuwa Yeye, Aliyetakasika na kila sifa pungufu, ni Msimamizi na Mtunzi wa mambo ya viumbe Vyake

    [133] Akitaka Mwenyezi Mungu Atawaangamiza, enyi watu, na awalete watu wengine wasiokuwa nyinyi. Na Mwenyezi Mungu kwa hili ni Muweza

    [134] Mwenye kuwa na hamu miongoni mwenu, enyi watu, ya kupata malipo ya duniani na akaipa mgongo Akhera, basi mbele ya Mwenyezi Mungu kuna malipo ya dunia na Akhera. Basi na atake kutoka kwa Mwenyezi Mungu , Peke Yake, wema wa dunia na Akhera, kwani Yeye Ndiye Anayevimiliki hivyo viwili. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasikia maneno ya waja Wake, ni Mwenye kuziona nia zao na vitendo vyao, na Atawalipa kwa hayo

    [135] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo, kuweni ni wasimamizi wa uadilifu, wenye kutekeleza ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, hata kama ni kinyume na maslahi ya nafsi zenu au baba zenu au mama zenu au jamaa zenu, namna atakavyokuwa yule mwenye kutolewa ushahidi awe ni tajiri au masikini, kwani Mwenyezi Mungu ni bora kwa wao wawili kuliko nyinyi, na ni Mjuzi zaidi wa mambo ambayo yana maslahi kwao. matamanio na mapendeleo yasiwapelekee nyinyi kuacha uadilifu. Na mkiupotoa ushahidi, kwa ndimi zenu, mkautoa kwa namna isiyokuwa ya kweli, au mkaupuuza kwa kuacha kuutekeleza au kwa kuuficha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa matendo yenu ya ndani na Atawalipa kwayo

    [136] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo, endeleeni kwenye msimamo mlionao wa kumuamini Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Imani thabiti, kumuamini Mtume Wake Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, na kuwatii wao wawili, kuiamini Qur’ani Aliyoiteremsha kwake na kuviamini vitabu vyote Alivyoviteremsha Mwenyezi Mungu kwa Mitume. Na mwenye kumkanusha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Malaika Wake waliotukuzwa, vitabu Vyake Alivyoviteremsha ili kuwaongoza viumbe Wake, Mitume Wake Aliowachagua kufikisha ujumbe Wake na Siku ya Mwisho ambayo watu katika siku hiyo watafufuka baada ya kufa ili waorodheshwe na wahesabiwe, atakuwa ametoka kwenye Dini na atakuwa yuko mbali sana na njia ya haki

    [137] Hakika wale walioingia kwenye Imani, kisha wakarudi kwenye ukafiri, kisha wakarejea kwenye Imani, kisha wakarudi tena kwenye ukafiri, kisha wakavama na kuendelea kwenye ukafiri, Mwenyezi Mungu Hatakuwa ni Mwenye kuwasamehe wala kuwaonesha njia ya uongofu ambayo kwayo wataokoka na mwisho mbaya

    [138] Wape bishara, ewe Mtume, wanafiki - nao ni wale wanaodhihirisha Imani na kuficha ukafiri- kuwa wao watakuwa na adhabu yenye kuumiza

    [139] Ambao wanawategemea makafiri na kuwafanya ni wasaidizi wao, na wanaacha kuwapenda Waumini na kuwategemea, wala hawana haja ya mapenzi yao. Kwani wanatafuta, kwa hilo kuokolewa na kupata hifadhi kwa makafiri? Hili wao hawalimiliki. Kwani uokozi, enzi na nguvu, vyote ni vya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Peke Yake

    [140] Mola wenu Amewateremshia, enyi Waumini, katika Kitabu Chake kwamba mkisikia aya za Mwenyezi Mungu zinakanushwa na zinafanyiwa shere, basi msikae pamoja na wakanushaji hao wanaofanya shere, isipokuwa wakiingia kwenye mazungumzo yasiokuwa mazungumzo ya kukanusha na kuzifanyia shere aya za Mwenyezi Mungu. Nyinyi mkikaa nao, na wao wako katika hali hiyo, mtakuwa ni kama wao, kwa kuwa nyinyi mmeridhika na ukafiri wao na uchezaji shere wao. Na mwenye kuridhika na maasia ni kama mwenye kuyafanya. Hakika Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ni Mwenye Atawakusanya wanafiki na makafiri wote ndani ya Moto wa Jahanamu ambapo humo watakumbana na ukali wa adhabu

    [141] Wanafiki ndio wale wanaongojea yatakayowashukia nyinyi, enyi Waumini, ya misukosuko na vita. Iwapo Mwenyezi Mungu Amewaneemesha kwa fadhila Zake, Akawanusuru juu ya adui yenu na mkapata ngawira, wao wanasema, «Kwani hatukuwa na nyinyi tukiwasaidia?» Na iwapo wakanushaji wa Dini hii wamepata sehemu ya ushindi na ngawira, wao wanasema kuwaambia, «Kwani hatukuwasaidia nyinyi kwa kile tulichowapatia na kuwahami na Waumini?» Basi Mwenyezi Mungu Ataamua baina yao na nyinyi Siku ya Kiyama. Na Mwenyezi Mungu Hatawapa makafiri njia ya kuwashinda waja Wake wema. Basi mwisho mwema ni wa wacha- Mungu, duniani na Akhera

    [142] Hakika mbinu ya wanafiki hawa ni kumhadaa Mwenyezi Mungu kwa Imani wanaojionyesha nayo na ukafiri wanaouficha, kwa kudhani kuwa mbinu yao itafichamana kwa Mwenyezi Mungu, na hali ni kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye Anayewahadaa na ni Mwenye kuwalipa malipo yanayofanana na vitendo vyao. Wanafiki hawa wanaposimama kutekeleza Swala, wanasimama kufanya hivyo kwa uvivu, wanakusudia, kwa kuswali kwao, kuonekena na kusikika. Na wao hawamtaji Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, isipokuwa kumtaja kwa uchache

    [143] Hali ya hawa wanafiki ni kutokuwa na msimamo, kuchangayikiwa na kubabaika, hawathibiti kwenye hali moja, hawako pamoja na Waumini wala hawako pamoja na makafiri. Na yoyote ambaye Mwenyezi Mungu Ameupotoa moyo wake usimuamini na usishikamane na uongofu Wake, huyo hutampatia njia ya kufikia uongofu na yakini

    [144] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na mkafuata sheria Yake! Msiwapende na kuwategemea wenye kukanusha Dini ya Mwenyezi Mungu na mkaacha kuwapenda kuwategemea Waumini na kuwapenda. Je, mnataka kwa kuwapenda maadui wenu kumpa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, hoja iliyo wazi kuwa nyinyi si wakweli katika Imani yenu

    [145] Hakika wanafiki watakuwa kwenye mahandaki ya chini kwa chini ya Moto Siku ya Kiyama. Na hutawapatia wao, ewe Mtume, yoyote wa kuwaokoa atakayewakinga wao wasifikie mwisho huu mbaya

    [146] Isipokuwa wale ambao walirejea kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, wakatubia Kwake, wakazirekebisha hali zao zilizoharibika za ndani na za nje, wakawategemea waja Wake Waumini, wakashikamana na dini ya Mwenyezi Mungu na wakamtakasia Yeye, Aliyetakasika kutokana na kila sifa ya upungufu. Hao ni pamoja na Waumini duniani na Akhera; na Mwenyezi Mungu Atawapa Waumini malipo kubwa

    [147] Mwenyezi Mungu hatawapa adhabu iwapo nyinyi mumefanya amali njema na mumemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Kwani Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu, Hana haja na yoyote asiyekuwa Yeye. Yeye Atawaadhibu waja kwa makosa yao. Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwarudishia shukrani waja Wake kwa utiifu wao Kwake, ni Mjuzi wa kila kitu

    [148] Hapendi Mwenyezi Mungu kwa yoyote adhihirishe neno ovu. Lakini yaruhusiwa kwa aliyedhulumiwa amtaje aliyemdhulumu kwa uovu alionao, ili akibainishe alichodhulumiwa nacho. Na daima Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasikia mnayoyadhihirisha na ni Mwenye kuyajua mnayoyaficha kati ya hayo

    [149] Amehimiza Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwamba watu wasamehe, na Akaweka msingi wa jambo hilo kwa kuwa Muumini, ima aidhihirishe kheri au aifiche. Na vilevile katika kukosewa, ima adhihirishe kuwa amekosewa katika hali ya kutafuta haki yake kwa aliyemkosea au asamehe na apuuze. Na kusamehe ni bora. Kwani miongoni mwa sifa za Mwenyezi Mungu ni kuwasamehe waja Wake pamoja na uwezo Wake juu yao

    [150] Hakika wanaomkanusha Mwenyezi Mungu na Mitume Wake, kati ya Mayahudi na Wanaswara, na kutaka kutenganisha baina ya Mwenyezi Mungu na Mitume Wake, kwa kumuamini kwao Mwenyezi Mungu na kuwakanusha Mitume Wake Aliowatuma kwa viumbe Wake, au wautambue ukweli wa baadhi ya Mitume na kuacha kuwatambua wengine na wadai kwamba baadhi yao wamemzulia Mola wao urongo na wanataka kujifanyia njia ya kuelekea kwenye upotofu waliouanzisha na uzushi waliouzua

    [151] Hao ndio wenye ukafiri wa hakika usiokuwa na shaka. Na tumewaandalia makafiri adhabu itakayowadhili na kuwatweza

    [152] Na wale walioukubali upweke wa Mwenyezi Mungu na wakautambua unabii wa wajumbe Wake wote na wasimbague yoyote kati yao na wakaifuata kivitendo sheria ya Mwenyezi Mungu, hao Atawapa malipo yao na thawabu zao kwa kumuamini kwao Yeye na Mitume Wake. Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa waja Wake, ni Mwenye huruma kwao

    [153] Wanakutaka Mayahudi, ewe Mtume, uwaonyeshe miujiza mfano wa miujiza ya Mūsā iwe ni ushahidi kwako kuwa ni mkweli, nao ni uwateremshie kurasa zitokazo kwa Mwenyezi Mungu hali ya kuwa zimeandikwa, kama vile Mūsā alivyoleta mbao kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Usione ajabu, ewe Mtume, kwani wakale wao walimtaka Mūsā, amani imshukie, awaletee makubwa zaidi. Walimtaka Awaonyeshe Mwenyezi Mungu waziwazi, hapo wakateremshiwa moto uliowaua kwa sababu ya kuzidhulumu nafsi zao walipolitaka jambo ambalo si haki yao. Na baada ya Mwenyezi Mungu kuwahuisha, baada ya kufa kwao, na wakaishuhudia miujiza iliyo waziwazi, kutoka kwa Mtume Mūsā, inayopinga katakata ushirikina, waliabuduu kigombe badala ya Mwenyezi Mungu. Kisha tuliwasamehe kosa lao la kuabudu ndama kwa sababu ya kutubia kwao na tukampa Mūsā hoja kubwa zilizotilia nguvu ukweli wa utume wake

    [154] Na tukaliinua juu ya vichwa vyao jabali la Tūr walipokataa kujilazimisha na ahadi iliyotiliwa mkazo waliyoitoa ya kuwa watazitumia hukumu za Taurati. Na tukawaamrisha waingie lango la Bait al-Maqdis hali ya kusujudu , nao wakaingia wakijikokota kwa matako yao. Na tukawaamrisha wasifanye uadui kwa kuvua siku ya Jumamosi, wakafanya uadui hivyo hivyo na wakavua. Na tukachukua kutoka kwao ahadi ya mkazo, pia waliivunja hivyo hivyo

    [155] Tukawalaani kwa sababu ya kuvunja kwao ahadi, kukanusha kwao aya za Mwenyezi Mungu zinazojulisha ukweli wa Mitume Wake, kuua kwao Manabii wa Mwenyezi Mungu kwa maonevu na uadui na kwa kusema kwao, «Nyoyo zetu zimezibwa kwa vifiniko, hatuyafahamu uyasemayo.» Bali Mwenyezi Mungu ameziziba kwa sababu ya ukafiri wao. Kwa hivyo, hawataamini isipokuwa Imani isiyowafaa

    [156] Na vile vile tuliwalaani kwa sababu ya ukafiri wao na kumzulia kwao Maryam urongo kwa yale waliyomsingizia nayo ya uzinifu na hali yeye yupo mabali na hilo

    [157] Na- pia tuliwalaani- kwa sababu ya neno lao, kwa njia ya kukejeli na shere, «Sisi tumemuua Al- Masīh,, ‘Īsā mwana wa Maryam, mjumbe wa Mwenyezi Mungu.» Na wala wao hawakumuua ‘Īsā wala hawakumsulubu, bali walimsulubu mwanamume aliyefanana naye kwa kudhani kwao kuwa yeye ndiye ‘Īsā. Na yoyote aliyedai kwamba walimuua, miongoni mwa Mayahudi na pia wale waliomsalimisha kwao, miongoni mwaWanaswara, wote hao wako kwenye shaka na kuchanganyikiwa; hawana ujuzi wowote isipokua ni kufuata dhana tu, na wala hawana yakini ya kuwa walimuua, bali wana shaka nalo hilo na wanalidhania tu

    [158] Bali Mwenyezi Mungu Alimpaisha ‘Īsā kwa mwili wake na roho yake akiwa hai na Alimuokoa na wale waliokufuru. Na Mwenyezi Mungu ni Mshindi katika ufalme Wake, ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji mambo Wake na mapitisho Yake

    [159] Na kwa hakika hatasalia yoyote, kati ya wale waliopewa Kitabu, baada ya kuteremka ‘Īsā zama za mwisho, isipokuwa atamuamini Nabii ‘Īsā kabla ya kufa kwake, amani imshukie, na siku ya Kiyama Nabii ‘Īsā atakuwa ni shahidi kwamba waliomkanusha walikuwa warongo na waliomuamini walikuwa wakweli

    [160] Na kwa sababu ya dhuluma ya Mayahudi kwa madhambi makubwa waliyoyafanya, Mwenyezi Mungu Aliwaharamishia vyakula vizuri vilivyokuwa halali kwao, na pia kwa sababu ya kuzizuia nafsi zao na kuwazuia wengine wao wasiifuate dini ya Mwenyezi Mungu iliyo ya sawa

    [161] Na kwa sababu ya kutumia kwao riba ambayo walikatazwa wasitumie na kujihalalishia kwao mali za watu pasi na haki. Na tumewatayarishia waliomkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake adhabu iumizayo huko Akhera

    [162] Lakini wale waliojikita katika elimu katika hukumu za Mwenyezi Mungu kati ya Mayahudi na wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, wanayaamini yale Aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu kwako, ewe Mtume, nayo ni Qur’ani, na yale Aliyoyateremsha kwa Mitume kabla yako, kama Taurati na Injili, wanatekeleza Swala kwa nyakati zake, wanatoa Zaka za mali zao na wanamuamini Mwenyezi Mungu, kufufuliwa na malipo. Hao Mwenyezi Mungu Atawapa thawabu kubwa, nayo ni Pepo

    [163] Hakika sisi tumekuletea wahyi, ewe Mtume, ili ufikishe ujumbe kama tulivyomletea wahyi Nūḥ na Manabii wengine baada yake. Na tumewapelekea wahyi Ibrāhīm, Ismā’īl, Isḥāq, Ya‘qūb na Asbāṭ, nao ni Manabii waliokuwa katika makabila kumi na mbili ya wana wa Isrāīl wanaotokana na kizazi cha Ya’qūb, na pia ‘Īsā, Ayyūb, Yūnus, Hārūn na Sulaimān na tukampa Dāwūd Zaburi, nacho ni kitabu na kurasa zilizoandikwa

    [164] Na tumewatumiliza Mitume ambao tumekuelezea habari zao katika Qur’ani, kabla ya aya hii, na Mitume wengine ambao hatukukuelezea hahabari zao kwa hekima tuliyoikusudia.Na Mwenyezi Mungu Alisema na Mūsā waziwazi ili kumtukuza kwa sifa hii. Katika aya hii tukufu kuna uthibitisho wa sifa ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ya kusema kama inavyolingana na utukufu Wake, na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu Alisema na Nabii Wake Mūsā, amani imshukie, kikweli bila ya mtu wa kati (baina yao)

    [165] Nimweatuma wajumbe kwa viumbe wangu wakatoe habari njema ya malipo yangu mema na waonye juu ya adhabu yangu, ili wanadamu wasiwe na hoja watakayoifanya ni kisingizio cha udhuru baada ya kutumiliza Mitume. Na daima Mwenyezi Mungu ni Mshindi katika mamlaka Yake, ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji mambo Wake

    [166] Iwapo Mayahudi na wengineo watakukanusha, ewe Mtume, hakika Mwenyezi Mungu Anashuhudia kuwa wewe ni Mtume Wake Aliyemteremshia Qur’ani tukufu; Ameiteremsha kwa ujuzi Wake. Na vilevile Malaika wanashuhudia ukweli wa wahyi uliyoletewa. Na ushahidi wa Mwenyezi Mungu Peke Yake unatosha

    [167] Hakika wale walioupinga unabii wako na wakawazuia watu kuufuata Uislamu, wamekuwa mbali kabisa na njia ya haki

    [168] Hakika wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakadhulumu kwa kuendelea kwao na ukafiri, Mwenyezi Mungu Hatakuwa ni Mwenye kuwasamehe madhambi yao wala kuwaongoza njia ya kuwaokoa

    [169] Isipokuwa njia ya moto wa Jahanamu, hali ya kuwa wao ni wenye kukaa humo milele. Na hilo kwa Mwenyezi Mungu ni jepesi; hivyo basi, hakuna chenye kumshinda

    [170] Enyi watu, amewajia nyinyi Mjumbe wetu,Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na Uislamu, Dini ya haki, kutoka kwa Mola wenu, basi ikubalini na muifuate, kwani kuiyamini ni bora kwenu. Na iwapo mtaendelea na ukafiri wenu, basi Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Hana haja nanyi, na pia Hana haja ya kuamini kwenu, kwa kuwa Yeye ni Mmiliki wa vilivyo mbinguni na ardhini. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi mno wa maneno yenu na vitendo vyenu, ni Mwingi wa hekima katika uwekaji Sheria Wake na amri Zake. Na iwapo mbingu na ardhi zimemnenyekea Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, katika kuwa na kukadiriwa, kama viumbe vyingine vyote vilivyomnyenyekea, basi ni bora kwenu mumwamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, muiamini Qur’ani Aliyomteramshia na muifuate Dini hiyo kisheria hadi ulimwengu wote uwe ni wenye kumnyenyekea Mwenyezi Mungu kimpango uliokadiriwa na kisheria. Katika aya hii kuna dalili ya kuwa ujumbe wa Nabii wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, unakusanya ulimwengu wote

    [171] Enyi watu wa Injili! Msiikiuke itikadi ya haki katika dini yenu, na msiseme kuhusu Mwenyezi Mungu isipokuwa haki. Hivyo basi, msimfanye kuwa Ana mke wala msimfanye kuwa ana mwana; hakika Al-Masīḥ ‘Īsā, mwana wa Maryam, ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu Amemtummliza kwa haki na Amemuumba kwa neno ambalo Amemtuma nalo Jibrili alipeleke kwa Maryam, nalo ni neno Lake, «Kuwa!» na ikawa. Nalo ni mvivio kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, aliouvivia Jibrili kwa amri ya Mola Wake. Kwa hivyo , aminini kwamba Mwenyezi Mungu ni Mmoja na mjisalimishe Kwake na muwaamini Mitume Wake katika yale waliowaletea kutoka kwa Mwenyezi Mungu na myafuate kivitendo. Wala msimfanye ‘Īsā na mamake kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu. Komeni na matamshi hayo! Itakuwa bora kwenu kuliko hayo mliyonayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mola Mmoja, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake. Vilivyoko mbinguni na ardhini ni milki Yake. Basi vipi Atakuwa na mke au mtoto kati ya hivyo? Inatosha kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Msimamizi wa kupanga mambo ya viumbe Wake na kuendesha maisha yao. Hivyo basi, mtegemeeni, Yeye Peke Yake, kwani Yeye Ndiye Mwenye kuwatosha

    [172] Kabisa hatadinda wala hatakataa Al- Masīḥ kuwa ni mja wa Mwenyezi Mungu. Vilevile hawatadinda Malaika waliokaribishwa kukubali kuwa wao ni waja wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka. Na yoyote mwenye kudinda kufuata kikamilifu na kunyenyekea na akafanya kiburi, Basi hao Mwenyezi Mungu Atawafufua Awakusanye Kwake Siku ya Kiyama, Atoe uamuzi baina yao kwa hukumu Yake ya uadilifu na Amlipe kila mmoja kwa kile anachostahili

    [173] Ama wale ambao wamemuamini Mwenyezi Mungu, kiitikadi, kimaneno na kivitendo, wakasimama imara kufuata sheria Zake, basi Yeye Atawalipa thawabu za vitendo vyao na Atawaongeza kutokana na fadhila Zake. Na ama waliokataa kumtii Mwenyezi Mungu na wakafanya kiburi kwa kutojidhalilisha Kwake, Atawaadhibu adhabu iumizayo. Hawatampata wa kuwasimamia atakayewaokoa na adhabu Yake, wala wa kuwanusuru ambaye atawanusuru badala ya Mwenyezi Mungu

    [174] Enyi watu, kwa hakika imekuja kwenu ushahidi kutoka kwa Mola wenu, nao ni Mtume wetu Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na yale aliyokuja nayo miongoni mwa maelezo yaliyo waziwazi na hoja za yakini, kubwa ya hizo ni Qur’ani tukufu, zenye kutolea ushahidi ukweli wa unabii wake na utume wake wa mwisho; na tumewateremshia Qur’ani ikiwa ni uongofu na ni nuru yenye kufafanua mambo waziwazi

    [175] Ama wale waliomuamini Mwenyezi Mungu kiitikadi, kimaneno na kivitendo, na wakashikamana na Nuru ambayo waliteremshiwa, Atawaingiza Peponi ikiwa ni rehema na fadhila kutoka Kwake na Atawaafikia kufuata njia iliolingana sawa, itakayopelekea kwenye mabustani ya Peponi

    [176] Wanakuuliza, ewe Nabii, kuhusu hukumu ya urithi wa kalalah, naye ni aliyekufa akiwa hana mwana wala mzazi. Sema, «Mwenyezi Mungu Anawafafanulia hukumu yake, kwamba yoyote atakayefariki na akawa hana mwana wala mzazi, na akawa ana dada yake wa kwa baba na mama au wa kwa baba tu. Basi dada huyo atapata nusu ya mali yaliyoachwa na aliyefariki. Na iwapo aliyefariki ni huyo dada, na akawa hana mwana wala mzazi, basi kaka yake, wa kwa baba na mama au wa kwa baba, atarithi mali yote. Na iwapo yule aliyefariki, bila ya kuacha mwana wala mzazi, ana dada zake wawili, basi wao watapata theluthi mbili ya mali aliyoyaacha. Na watakapokusanyika pamoja kwenye urithi ndugu wa kiume na wa kike wasiokuwa wa kwa mama basi kila mmoja, katika ndugu wa kiume, atapata mfano wa mafungu mawili ya mwanamke. Mwenyezi Mungu Anawafafanulia namna ya kugawanya urithi na hukumu ya aliyefariki bila ya kuacha mwana wala mzazi, ili msije mkapotea kwenye njia ya haki kuhusu hukumu ya mambo ya uraihi. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzu wa mwisho wa mambo na yaliyo na heri kwa waja Wake

    Meza Iliyoandaliwa

    Surah 5

    [1] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata sheria Zake kivitendo, timizeni ahadi za Mwenyezi Mungu zilizotiliwa mkazo za kuamini Sheria za Dini na kuzifuata, na tekelezeni ahadi mlizopeana nyinyi kwa nyinyi miongoni mwa amana mlizowekeana, biashara na mengineyo kati ya yale yasiyoenda kinyume na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na mafundisho ya Mtume Wake Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie. Na hakika Mwenyezi Mungu Amewahalalishia wanyama wa mifugo, nao ni ngamia, ng’ombe na mbuzi na kondoo, isipokuwa yale ambayo Mwenyezi Mungu amewaelezea ya kuwaharamishia mfu, damu na mengineyo; na ya kuwaharamishia kuwinda mkiwa kwenye hali ya ihramu (kwa ibada ya Hija au Umra). Kwa hakika Mwenyezi Mungu Anahukumu Anachokitaka kulingana na hekima Yake na uadilifu Wake

    [2] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuta sheria Zake kivitendo, msivuke mipaka ya Mwenyezi Mungu na alama Alizoziwekea hiyo mipaka yake. Na msihalalishe vita katika miezi mitukufu, nayo ni Mfungopili, Mfungotatu, Mfungone na Rajabu- na hilo lilikuwa katika mwanzo wa Uislamu-. Na msivunje heshima ya wanyama waliokusudiwa kuchinjwa katika ibada ya Hija, wala msivunje heshima ya vitu walivyovishwa navyo. Kwani walikuwa wakiwavalisha kwenye shingo zao miseja ya sufi au ya nyoya, ikiwa ni kitambulisho kwamba mnyama huyo ni wa kuchinjwa katika ibada ya Hija na kwamba mwenye mnyama anaenda Hija. Wala msihalalishe kuwapiga vita wenye kuikusudia Nyumba tukufu, ambao wanazitafuta fadhila za Mwenyezi Mungu zinazowatengezea maisha yao na kumridhisha Mola wao. Na pindi mnapomaliza ibada yenu ya Hija, mnahalalishiwa kuwinda. Na isiwapelekee nyinyi kuwachukia baadhi ya watu kwa kuwa waliwazuia nyinyi kufika Msikiti mtukufu, kama ilivyotokea katika mwaka wa Hudaibiyah, kuacha kuwafanyia uadilifu. Na saidianeni kati yenu, enyi Waumini, kufanya wema na kumcha Mwenyezi Mungu wala msisaidiane kwenye mambo ya madhambi, maasia na kuivuka mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na jihadharini kuenda kinyume na amri ya Mwenyezi Mungu, kwani Yeye ni Mkali wa kutesa

    [3] Mwenyezi Mungu Amewaharamishia mfu, naye ni mnyama aliyekufa mwenyewe bila ya kuchinjwa. Na pia Amewaharamishia nyinyi damu inayotiririka inayomwagwa, nyama ya nguruwe, mnyama ambaye wakati wa kuchinjwa ametajiwa jina lisilokuwa la Mwenyezi Mungu, mnyama aliyenyongwa kwa kuzibwa pumzi zake mpaka akafa, mnyama aliyekufa kwa kupigwa gongo au jiwe, mnyama aliyeanguka kutoka mahali pa juu au aliyeanguka kisimani akafa na mnyama aliyekufa kwa kupigwa pembe na mwenzake. Na pia Amewaharamishia mnyama aliyeliwa na mnyama mwingine kama simba, chuimarara, mbwamwitu na mfano wake. Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na sifa za upungufu, Amewatoa, miongoni mwa wale Aliowaharamisha, kuanzia wale walionyongeka na waliofuatia, wale mliowahi kuwachinja kabla hawajafa, hao ni halali kwenu. Na Amewaharamishia nyinyi wanyama waliochinjiwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu miongoni mwa vitu vilivyosimamishwa viabudiwe, viwe ni mawe au vinginevyo. Na Amewaharamishia kutaka kujua mambo, mliyoandikiwa na msiyoandikiwa, kwa viapo; navyo ni vipande ambavyo walikuwa wakitaka uamuzi kwavyo wakitaka kufanya jambo kabla hawajalifanya. Hayo mliyotajiwa katika aya hii kati ya yaliyoharamishwa, yakifanywa, huwa ni kutoka kwenye amri ya Mwenyezi Mungu na twaa Yake na kwenda kwenye maasia. Sasa imekatika tamaa ya makafiri kwamba nyinyi mtaiacha Dini yenu muende kwenye ushirikina baada ya mimi kuwapa ushindi juu yao. Basi msiwaogope wao na mniogope mimi. Leo nimeshawakamilishia dini yenu, Dini ya Uislamu, kwa kuuhakikisha ushindi na kuikamilisha Sheria, nimewatimizia neema zangu kwenu kwa kuwatoa kwenye giza la ujinga na kuwapeleka kwenye mwangaza wa Imani na nimewaridhia kwamba Uislamu ndio Dini, basi shikamaneni nayo wala msiiache. Na yule aliyepatikana na dharura ya njaa ikambidi ale mfu, na akawa hakukusudia kutenda kosa, basi inafaa kwake kumla. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kumsamehe na ni Mwenye huruma naye

    [4] Wanakuuliza Maswahaba wako, ewe Nabii, «Ni kipi walichohalalishiwa kukila?» Waambie, «Mumehalalishiwa kula vilivyo vizuri na viwindwa vya wanyama mliowafundisha kati ya wanyama wanaowinda kwa kutumia makucha na meno yao, miongoni mwa mbwa, chui na kozi na kama hao kati ya wale wanaofundishwa. Mnawafundisha kuwatafutia viwindwa kwa yale Mwenyezi Mungu Aliyowafundisha. Basi kuleni wanyama waliowashikia na mlitaje jina la Mwenyezi Mungu wakati mnapowatuma kuwawindia. Na muogopeni Mwenyezi Mungu katika yale Aliyowaamrisha na yale Aliyowakataza.» Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhesabu

    [5] Na miongoni mwa ukamilifu wa neema ya Mwenyezi Mungu kwenu leo hii, enyi Waumini, ni kwamba Amewahalalishia vilivyo halali vizuri. Na vichinjwa vya Mayahudi na Wanaswara, iwapo watawachinja wanyama wao kuambatana na sheria yao, ni halali kwenu ; na vichinjwa vyenu ni halali kwao. Na Amewahalalishia nyinyi, enyi Waumini, kuwaoa wanawake wanaojihifadhi, nao ni wale walio huru kati ya wanawake Waumini wanaojizuia na uzinifu. Vilevile ni halali kuwaoa wanawake walio huru wanaojiepusha na uzinifu, miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara, iwapo mtawapa mahari yao na mkawa mumejihifadhi kwa kutofanya uzinifu na kuweka mahawara na mkawa mumejiaminisha kuwa hamutaathirika na dini yao. Na mwenye kuzikataa sheria za fmani, basi vitendo vyake vimishaharibika, na yeye, Siku ya Kiyama, atakuwa ni miongoni mwa wenye kupata hasara

    [6] Enyi mlioamini! Mkitaka kuinuka ili kuswali, hali ya kuwa hamuna udhu, basi osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka kwenye visukusuku (Kisukusuku ni kiungo kilichoko kati ya mkono na nyoka-mkono). Na pakeni maji kwenye vichwa vyenu na muoshe miguu yenu pamoja na macho mawili ya miguu ( nayo ni mifupa miwili iliyojitokeza katika makutano ya muundi na nyayo). Na mtakapopatikana na tukiyo la hadathi kubwa ya kuondoa utohara, basi jitahirisheni kwa kuoga kabla ya kuswali. Na mkiwa ni wagonjwa au muko safarini katika hali ya afya, au iwapo mmoja wenu amemaliza haja yake, au amemuingilia mke wake, na mkawa hamkupata maji, basi ipigeni ardhi kwa mikono yenu na mupukuse nyuso zenu na mikono yenu kwayo. Mwenyezi Mungu Hataki kuwadhiki katika jambo la kujitoharisha, ndipo Akawatolea nafasi na kuwahurumia kwa kuwaruhusu kutayamamu (kutumia mchanga) badala ya kutumia maji katika kujitoharisha. Ruhusa ya kutayamamu ilikuwa ni katika kuzikamilisha neema ambazo zinapelekea kumshukuru Mneemeshaji kwa kumtii katika yale Aliyoyamrisha na kuyakataza

    [7] Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu kwenu katika sheria Yake Aliyowaekea na kumbukeni ahadi Yake Yeye Aliyetukuka, Aliyoichukua kwenu ya kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kuwasikiliza na kuwatii. Na mcheni Mwenyezi Mungu katika Aliyowaamrisha na Aliyowakataza. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mnayoyaficha katika nafsi zenu

    [8] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie,, kuweni wasimamizi wa haki kwa ajili ya kuzitafuta radhi za Mwenyezi Mungu, muwe mashahidi kwa uadilifu. Wala kusiwapelekee nyinyi kuwachukia watu kuacha kufanya uadilifu. Fanyeni uadilifu baina ya maadui na vipenzi kwa daraja moja sawasawa. Kufanya uadilifu huko kuko karibu zaidi na kumuogopa Mwenyezi Mungu. Na jihadharini na kufanya udhalimu, hakika Mwenyezi Mungu ni Mtambuzi wa mnayoyafanya na Atawalipa kwa hayo

    [9] Mwenyezi Mungu Amewapa ahadi, wale ambao wamemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakatenda mema, kwamba Atawasamehe madhambi yao na Atawalipa Pepo kwa hilo. Na Mwenyezi Mungu Haendi kinyume na ahadi Yake

    [10] Na wale waliokanusha upweke wa Mwenyezi Mungu unaoijulisha haki iliyo waziwazi na wakazikanusha dalili zake walizokuja nazo Mitume, hao ndio watu wa Motoni watakaosalia humo

    [11] Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na mkazifuata sheria Zake kivitendo, yakumbukeni yale Aliyowaneemesha Mwenyezi Mungu, miongoni mwa neema ya usalama, kutia uoga kwenye nyoyo za maadui zenu waliotaka kuwavamia, Mwenyezi Mungu Akawaepusha na nyinyi na Akaweka kizuizi kati yao na yale waliyoyataka kwenu. Na mcheni Mwenyezi Mungu, muwe na hadhari naye. Na mtegemeeni Mwenyezi Mungu, Peke Yake, katika mambo yenu ya kidini na ya kidunia na muwe na hakika ya kupata msaada Wake na uokozi Wake

    [12] Na kwa hakika Mwenyezi Mungu Alichukua kwa Wana wa Isrāīl ahadi ya mkazo kwamba wamtakasiye ibada Yeye Peke Yeke. Na Mwenyezi Mungu Alimuamrisha Mūsā awawekee wao viongozi kumi na mbili kulingana na idadi ya koo zao, wachukue kwao ahadi ya mkazo ya kumsikiliza na kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na kukifuata Kitabu Chake. Na Mwenyezi Mungu Aliwaambia Wana wa Isrāīl, «Mimi niko pamoja nanyi kwa hifadhi yangu na nusura yangu. Iwapo mtasimamisha Swala na mtawapa Zaka za faradhi wanaostahiki kupewa na mtawaamini Mitume wangu katika yale wanayoyatolea habari, mtawanusuru na mtatoa katika njia yangu, hakika nitawafutia makosa yenu na nitawaingiza ndani ya mabustani ya Peponi ambayo mito inapita chini ya majumba yake ya fahari.Basi mwenye kuikana ahadi hii, kati yenu, hakika amejiepusha na njia ya haki na kuifuata njia ya upotevu.»

    [13] Kwa sababu ya hawa Mayahudi kuvunja ahadi zao zilizotiliwa mkazo, tuliwafukuza kutoka kwenye rehama yetu na tukazijaalia nyoyo zao kuwa ngumu, hazilainiki kwa Imani, wanayageuza maneno ya Mwenyezi Mungu ambayo Alimteremshia Mūsā, nayo ni Taurati, na wakaacha kuitumia sehemu ya yale waliyokumbushwa nayo. Na utaendelea , ewe Mtume, kupata kutoka kwa Mayahudi uhaini na uvunjaji ahadi, kwani wao wako kwenye njia ya mababu zao, isipokuwa wachache miongoni mwao. Basi samehe kwa mabaya wanayokutendea na usiwe na chuki juu yao. Hakika Mwenyezi Mungu Anampenda anayefanya uzuri wa kusamehe na kutokuwa na chuki kwa aliyemfanyia ubaya. (Hivi ndivyo vile watu wapotovu wanapata njia ya kufikia malengo yao mabaya kwa kuyapotoa maneno ya Mwenyezi Mungu na kuyapa maana ambayo siyo yake. Wakishindwa kupotoa na kugeuza maana, wanayaacha yale yasioafikiana na matamanio yao katika sheria ya Mwenyezi Mungu ambayo hawatathibiti juu yake isipokuwa wachache waliyohifadhiwa na Mwenyezi Mungu kati yao)

    [14] Na tulichukua ahadi ya mkazo kwa wale waliodai kuwa wao ni wafuasi wa Al-Masīḥ ‘Īsā mwana wa Maryam, na hali wao sio hivyo, kama ile tulioichukua kwa Wana wa Isrāīl, kwamba watamfuata Mtume wao, watamnusuru na watamsaidia, lakini walibadilisha Dini yao na wakaacha kutumia sehemu ya yale waliyokumbushwa nayo, kama walivyofanya Mayahudi. Kwa hivyo tulitia uadui na chuki kati yao mpaka Siku ya Kiyama. Na Mwenyezi Mungu Atawapa habari, Siku ya Hesabu, ya yale ambayo wao walikuwa wakiyafanya, na Atawatesa kwa matendo yao

    [15] Enyi watu mliopewa Kitabu , miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara! Amewajia nyinyi mjumbe wetu Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kuwafafanulia mengi ambayo mlikuwa mkiyaficha kwa watu katika yale yaliyomo ndani ya Taurati na Injili, na kuacha kuyafafanua yale ambayo busara haitaki yafafanuliwe. Hakika umewajia kutoka kwa Mwenyezi Mungu mwngaza na Kitabu chenye ufafanuzi, nacho ni Qur’ani tukufu

    [16] Kwa kitabu hiki chenye ufafanuzi, Mwenyezi Mungu Anawaongoza wenye kufuata yenye kumridhi Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, njia za amani na usalama, Anawatoa kutoka kwenye giza la ukafiri kuwapeleka kwenye mwangaza wa Imani na Anawaafikia wao kufuata dini Yake iliyolingana sawa

    [17] Kwa hakika wamekufuru Wanaswara wanaosema kwamba Mwenyezi Mungu ni Al-Masīh mwana wa Maryam. Sema, ewe Mtume, kuwaambia Wanaswara hawa wajinga, «Lau Al-Masīh angalikuwa Mungu, kama wanavyodai, angaliweza kuuzuia uamuzi wa Mwenyezi Mungu ukimjia wa kumwangamiza yeye na mama yake na watu wote wa ardhini. Na mama yake ‘Īsā alikufa, hakuweza kumkinga na kifo. Vilevile hawezi kujitetea nafsi yake. Kwani wote wawili ni waja miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu, hawawezi kujiepusha na maangamivu. Hii ni dalili kuwa yeye ni mwanadamu kama wanadamu wengine. Na vitu vyote vilivyoko mbinguni na ardhini ni milki ya Mwenyezi Mungu, Anaumba na kupatisha anachotaka na yeye ni muweza wa kila kitu. Hakika ya tawhīd (kumpwekesha Mwenyezi Mungu) inawajibisha kupwekeka Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa sifa za uola na uungu; hakuna yoyote anayeshirikiana naye, katika viumbe Wake, kwa hilo. Na mara nyingi sana watu huingia kwenye ushirikina na upotevu kwa kuwatukuza Mitume na watu wema kupita kiasi, kama walivyopita kiasi Wanaswara katika kumtukuza Al-Masīh. Ulimwengu wote ni wa Mwenyezi Mungu, na viumbe viko kwenye mkono Wake Peke Yake. Na miujiza na alama kubwa zinazodhihiri, marejeo yake ni Mwenyezi Mungu.Anaumba, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, na Anafanya Anachotaka

    [18] Mayahudi na Wanaswara walidai kuwa wao ni wana wa Mwenyezi Mungu na vipenzi vyake. Sema kuwaambia, ewe Mtume, «Basi ni kwa nini Atawaadhibu kwa madhambi yenu.» Lau mlikuwa ni vipenzi Vyake hangaliwaadhibu. Kwani Mwenyezi Mungu Hampendi isipokuwa Anayemtii. Na waambie wao, «Bali nyinyi ni viumbe kama walivyo binadamu wengine, mkifanya wema mtalipwa mema kwa wema wenu, na mkifanya ubaya mtalipwa shari kwa ubaya wenu.» Mwenyezi Mungu Atamsamehe Anayemtaka, na Atamuadhibu Anayemtaka. Yeye Ndiye Anayeumiliki ufalme, Anaupeleka Anavyotaka na Kwake ndio marudio. Na hapo Atatoa uamuzi kwa waja Wake na Atamlipa kila mmoja anachostahiki

    [19] Enyi Mayahudi na Wanaswara, amewajia mjumbe wetu Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie,, ili kuwafunulia haki na uongofu baada ya kipindi kirefu cha wakati baina ya kumtuma yeye na kumtuma ‘Īsā mwana wa Maryam, ili msije mkasema, «Hakutujia mjumbe, mwenye kutoa bishara wala mwenye kuonya.» Hakika ashawajia kutoka kwa Mwenyezi Mungu mjumbe anayempa bishara njema mwenye kumuamini na anayemuonya mwenye kumuasi. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu, wa kumtesa mwenye kuasi na kumpa thawabu mwenye kutii

    [20] Na kumbuka, ewe Mtume, pindi aliposema Mūsā, amani imshukie, kuwaambia watu wake, «Enyi Wana wa Isrāīl, Kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu kwenu, pindi Alipochagua Manabii kati yenu, Akawafanya wafalme, mnayatawala mambo yenu baada ya kuwa mumetawaliwa na Fir‘aun na watu wake. Na hakika Aliwatunuku nyinyi aina mbalimbali za neema ambazo Hakumtunuku nazo yoyote miongoni mwa walimwengu wa zama zenu

    [21] «Enyi watu wangu, Ingieni kwenye ardhi takatifu, yaani iliyotakaswa, nayo ni Bait al-Maqdis na sehemu zilizo kando-kando yake, ambayo Mwenyezi Mungu Ametoa ahadi muingie na mkapigane na makafiri waliyo humo wala msirudi nyuma mkaacha kupigana na hao majabari, kwani mkifanya hivyo mtaikosa heri ya duniani na heri ya Akhera.»

    [22] Walisema, «Ewe Mūsā, hakika huko kuna watu wakali wenye nguvu ambao hatuna uwezo wa kupigana nao. Na sisi hatutaweza kuingia huko na wao wako. Watakapotoka huko, sisi tutaingia.»

    [23] Walisema watu wawili kati ya wale wanaomuogopa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ambao Mwenyezi Mungu Aliwapa neema kwa kumtii kwao Yeye na kumtii Mtume Wake, kuwaambia Wana wa Isrāīl, «Ingieni kwa majabari hao kupitia lango la mji wao, ikiwa ni mojawapo ya njia za kutafuta sababu za ushindi. Mtakapoingia langoni, mtawashinda. Na kwa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, jitegemezeni, iwapo nyinyi mnamuamini Mtume Wake katika yale Aliyowaletea, mnaiandama sheria Yake kivitendo.»

    [24] Watu wa Mūsā walisema kumwambia, «Hatutaungia mji huo kabisa, iwapo hao majabari wamo humo. Hivyo basi, nenda wewe na Mola wako mkapigane. Ama sisi, tunakaa hapa- hapa na hatutapigana na wao.» Hii inaonesha kushikilia kwao kuenda kinyume na Mūsā, amani imshukie

    [25] Mūsā alielekea kwa Mola wake akiomba, «Mimi sina uwezo isipokuwa wa nafsi yangu na ndugu yangu, basi hukumu kati yetu na watu wenye kuasi.»

    [26] Mwenyezi Mungu Alisema kumwambia Nabii Wake Mūsā, amani imshukie, «Hakika hiyo ardhi takatifu ni haramu kwa hawa Mayahudi kuiingia kwa muda wa miaka arubaini, watakuwa wakitanga katika ardhi wakiwa kwenye hali ya mshangao. Basi usiwasikitikie, ewe Mūsā, watu waliotoka kwenye utiifu wangu.»

    [27] Wasimulie, ewe Mtume, Wana wa Isrāīl habari ya wana wawili wa Ādam, Qābīl na Hābīl, nayo ni habari ya kweli, alipotoa kila mmoja wao sadaka, nayo ni ile inayotolewa ili kujisogeza karibu kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka. Hapo Mwenyezi Mungu Aliikubali sadaka ya Hābīl kwa kuwa alikuwa mcha-Mungu, na Hakuikubali sadaka ya Qābīl, kwa kuwa hakuwa mcha-Mungu. Qābīl alimhusudu ndugu yake na akasema, «Nitakuua.» Hābīl akajibu, «Kwa hakika Mwenyezi Mungu Huikubali sadaka itokayo kwa wale wenye kumuogopa.»

    [28] Hābīl akasema, akimpa mawaidha ndugu yake, «Iwapo utaunyosha mkono wako kwangu ili uniue, hutapata kutoka kwangu mfano wa kitendo chako. Mimi namuogopa Mwenyezi Mungu mola wa viumbe wote

    [29] «Mimi nataka urudi ukiwa umebeba dhambi la kuniua mimi na dhambi lililokuwa juu yako kabala ya hilo, upate kuwa ni miongoni mwa watu wa Motoni na watakaosalia humo. Na hayo ndiyo malipo ya wanaofanya uadui.»

    [30] Basi ilimpambia Qābīl nafsi yake amuue ndugu yake, akamuua na akawa ni kati ya waliopata hasara, ambao waliuza Akhera yao kwa dunia yao

    [31] Qābīl alipomuua ndugu yake, hakujua aufanye nini mwili wake. Hapo Mwenyezi Mungu Alimtuma kunguru, akawa anafukuwa shimo katika ardhi ili amzike humo kunguru aliyekufa, ili amjulishe Qābīl namna ya kuuzika mwili wa ndugu yake. Qābīl alistaajabu na akasema, «Kwani nimeshindwa kufanya vile kunguru huyu alivyofanya nikapata kuificha aibu ya ndugu yangu?» Hapo Qābīl alimzika ndugu yake. Na baada ya hasara aliyorudi nayo, Mwenyezi Mungu alimpa mateso ya majuto

    [32] Kwa sababu ya uhalifu huu wa mauaji, tuliwaekea sheria Wana wa Isrāīl kwamba yoyote mwenye kumuua mtu pasi na sababu ya kulipiza kisasi au ya uharibifu katika ardhi, kwa aina yoyote kati ya aina za uharibifu zinazopelekea mauaji, kama ushirikina na uharamia, atakuwa ni kama kwamba amewaua watu wote kwa jinsi atakavyostahili mateso makubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na kwamba yule atakayejizuia asiue mtu ambaye Mwenyezi Mungu Ameharamisha kuuawa, ni kama kwamba amewahuisha watu wote. Hivyo basi, kulinda heshima ya binadamu mmoja ni kulinda heshima ya binadamu wote. Hakika Mitume wetu waliwajia Wana wa Isrāīl kwa hoja na dalili juu ya usawa wa yale waliyowalingania kwayo ya kumuamini Mola wao na kuyatekeleza yale yaliyofanywa wajibu kwao na Mola wao. Kisha, wengi kati yao, baada ya kujiwa na Mitume ni wenye kupita mipaka ya Mwenyezi Mungu kwa kuyafanya yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu na kuyaacha maamrisho yake

    [33] Hakika malipo ya wale wanaompiga vita Mwenyezi Mungu na wanaojitokeza wazi kumfanyia uadui na kuzifanyia uadui hukumu zake na hukumu za Mtume Wake na kufanya uharibifu katika ardhi kwa kuwaua watu na kupora mali, ni wauawe au wasulubiwe pamoja na kuuawa (Kusululubiwa ni kufungwa mhalifu juu ya bao) au ukatwe mkono wa kulia wa mpiga vita na mguu wake wa kushoto. Iwapo hatatubu {kwa kuendelea na uharamia wake}, ukatwe mkono wake wa kushoto na mguu wa kulia, au wahamishwe wapelekwe mji usiokuwa wao, wafungwe kwenye jela ya mji huo mpaka iyonekane toba yao. Na haya ndiyo malipo Aliyoyaandika Mwenyezi Mungu kwa wenye kupiga vita; nayo ni unyonge wa duniani. Na huko Akhera itawapata adhabu kali iwapo hawatatubia

    [34] Lakini atakayekuja kati ya wale wanaopiga vita kabla hamjawatia mkononi na akaja akiwa mtiifu mwenye majuto, atafutiwa yale yaliyokuwa ni haki ya Mwenyezi Mungu. Na jueni, enyi Waumini, kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa waja Wake, ni Mwenye kuwarehemu

    [35] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Yake kivitendo, muogopeni Mwenyezi Mungu na mjisogeze karibu Kwake kwa kumtii na kufanya yanayomridhisha, na mpigane jihadi katika njia Yake ili mpate kufaulu kwa kuingia mabustani ya Pepo Yake

    [36] Hakika wale walioukanusha upweke wa Mwenyezi Mungu na sheria Yake, lau walikuwa wao wamemiliki vyote vilivyoko ardhini na wakavimiliki vyingine mfano wake, na wakataka kuzikomboa nafsi zao, Siku ya Kiyama, na adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa hivyo walivyovimiliki, Mwenyezi Mungu Hangalikubali hilo. Na itawapata wao adhabu yenye kuumiza

    [37] Makafiri hawa watataka watoke Motoni kwa ajili ya visanga vyake wanavyovipata, lakini hawatakuwa na njia yoyote ya kufanya hivyo. Na watakuwa na adhabu ya kudumu

    [38] Na mwizi wa kiume na mwizi wa kike, wakateni, enyi watawala, mikono yao kuambatana na Sheria. Hayo yakiwa ni malipo yao kwa kuchukua kwao mali ya watu pasi na haki, na ni mateso ambayo kwayo Mwenyezi Mungu Anawazuia wengineo kufanya mfano wa kitendo chao. Na Mwenyezi Mungu ni Mshindi katika mamlaka Yake, ni Mwenye hekima katika amri Zake na makatazo Yake

    [39] Basi yule atakayetubia baada ya wizi wake na akawa mwema katika vitendo vyake vyote, kwa hakika Mwenyezi Mungu Ataikubali toba yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwasamehe waja Wake, ni Mwenye huruma kwao

    [40] Kwani hujui, ewe Mtume, kwamba Mwenyezi Mungu ni Muumba wa ulimwengu, ni Mwenye kuuendesha na Mwenye kuumiliki na kwamba Yeye, Aliyetukuka, Ndiye Mfanya wa Alitakalo, Anamuadhibu Amtakaye na Anamsamehe Amtakaye; na Yeye juu ya kila kitu ni Muweza

    [41] Ewe Mtume! Wasikuhuzunishe wale ambao wanakimbilia kuukanusha unabii wako miongoni mwa wanafiki ambao wameonyesha Uislamu na huku nyoyo zao ni tupu, kwani mimi ni Mwenye kukuokoa na wao. Na lisikuhuzunishe lile la kukimbilia kwa Mayahudi kuukanusha unabii wako, kwani wao ni watu wanaosikiliza urongo, wanayakubali yanayozuliwa na wanavyuoni wao na wanawasikiliza watu wengine wasiohudhuria kwenye baraza yako; na wengine hawa wanayageuza maneno ya Mwenyezi Mungu baada ya kuyaelewa na wanasema, «Yakiwajia kutoka kwa Muhammad yanayolingana na yale tuliyoyageuza na tukayapotosha katika hukumu za Taurati, basi yatumieni. Na yakiwajia kutoka kwake yanayokwenda kinyume na hayo, basi jihadharini kuyakubali na kuyatumia.» Na ambaye Mwenyezi Mungu Ataka apotee, basi hutaweza, ewe Mtume, kulizuia hilo lisiwe kwake na wala huwezi kumuongoza.. Na hakika hawa wanafiki na Mayahudi, Mwenyezi Mungu Hakutaka kuzitakasa nyoyo zao na uchafu wa ukafiri, wana udhalilifu na fedheha hapa duniani, na watapata, huko Akhera, adhabu kubwa

    [42] Mayahudi hawa wanakusanya kati ya usikilizaji urongo na ulaji haramu. Basi watakapokujia wakishtakiana kwako, basi hukumu kati yao au waache. Na usipohukumu kati yao, hawataweza kukudhuru kwa chochote. Na iwapo utahukumu, basi hukumu kati yao kwa uadilifu. Hakika Mwenyezi Mungu Anawapenda waadilifu

    [43] Kitendo cha Mayahudi hawa ni cha kushangaza. Wao wanashitakiana kwako, ewe Mtume, na wao hawakuamini wewe wala Kitabu chako, pamoja na kuwa ile Taurati wanayoiamini wanayo, na humo muna hukumu ya Mwenyezi Mungu; kisha wanaondoka baada ya kutoa hukumu yako, iwapo haikuwaridhisha, wakakusanya kati ya kuzikataa sheria zao na kuipa mgongo hukumu yako. Na hawakuwa hao, wanaosifika na sifa hizo, ni wenye kumuamini Mwenyezi Mungu, kukuamini wewe na kuikubali hukumu uliyoitoa

    [44] Hakika tumeiteremsha Taurati. Ndani yake muna uongozi wa kumuepusha mtu na upotevu na ufafanuzi wa hukumu ambazo Mitume wamezitumia katika kuhukumu. Mitume ambao waliiandama na kuikubali hukumu ya Mwenyezi Mungu kati ya Mayahudi na wasitoke nje ya hukumu Yake wala wasiipotoshe. Pia walihukumu, kutumia sheria hiyo, wafanyi ibada wa Kiyahudi na wasomi wao ambao wanawalea watu kwa sheria za Mwenyezi Mungu. Hilo ni kwamba Manabii wao waliwaamini kwa kuwapa majukumu ya kuifikisha Taurati, kukielewa Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kukitumia. Na wacha-Mungu na wanavyuoni walikuwa ni mashahidi ya kwamba Manabii wao walihukumu kati ya Mayahudi kwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anasema kuwaambia wasomi wa Kiyahudi na wanavyuoni wao, «Msiwaogope watu katika kupitisha hukumu yangu, kwani wao hawawezi kuwanufaisha nyinyi wala kuwadhuru. Lakini niogopeni, kwani mimi Ndiye Mwenye kunufaisha, Mwenye kudhuru. Wala msichukue, kwa kuacha kuhukumu kwa sheria nilizoziteremsha, badali twevu.» Kwani kuhukumu kwa ambayo hayakuteremshwa na Mwenyezi Mungu ni katika vitendo vya makafiri. Na wenye kubadilisha hukumu ya Mwenyezi Mungu Aliyoiteremsha kwenye Kitabu Chake, wakaificha, wakaikana na wakahukumu kwa isiyokuwa hiyo wakiitakidi uhalali wake na kufaa kwake, basi hao ndio makafiri

    [45] Na tulilifanya ni lazima kwao katika Taurati kwamba mtu huuawa akiua mtu, hutolewa jicho akitoa jicho la mtu, hukatwa pua akikata pua ya mtu, hukatwa sikio akikata sikio la mtu, na hung’olewa jino aking’oa jino la mtu na kwamba hulipizwa kisasi kwa kutia mtu majaraha. Mwenye kusamehe haki yake ya kulipiza kisasi kwa aliyemfanyia uadui, basi huko ni kujifutia na kujiondolea sehemu ya madhambi ya yule aliyefanyiwa uadui. Na yule asiyehukumu kwa yaliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu, katika kisasi na megineyo, basi hao ni wakiukaji wa mipaka ya Mwenyezi Mungu

    [46] Na tukawafuatishia, Manabii wa Wana wa Isrāīl, ‘Īsā mwana wa Maryam akiwa ni mwenye kuyaamini yaliyomo ndani ya Taurati na kuzitumia hukumu zilizomo kati ya zile ambazo hazikufutwa na Kitabu chake na tukamteremshia Injili ikiwa ni yenye kuongoza kwenye haki na yenye kuyaeleza yale ambayo watu hawakuyajua katika hukumu za Mwenyezi Mungu na ni yenye kutoa ushahidi juu ya ukweli wa Taurati kwa hukumu zake ilizokusanya Na tumeifanya ni bainifu kwa wale wanaomuogopa Mola wao, ni yenye kuwakemea wasiyafanye yaliyoharamishwa

    [47] Basi na wahukumu watu wa Injili, ambao alitumwa kwao Īsā, kwa yaliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu ndani yake. Na wale ambao hawakuhukumu kwa yaliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu, Basi hao ndio wenye kutoka kwenye amri Yake, wenye kumuasi

    [48] Na tumekuteremshia wewe, ewe Mtume, Qur’ani. Na yote yaliyomo ndani yake ni haki, yanatoa ushahidi juu ya ukweli wa Vitabu kabla yake na kwamba -vitabu hivyo- vinatoka kwa Mwenyezi Mungu, hali ya kuuthibitisha usahihi uliomo, kuufafanua upotovu uliomo na kuzifuta baadhi ya sheria zake. Kwa hivyo, wahukumu kati ya wale Mayahudi wanaoshitakiana kwako kwa sheria zile ulizoteremshiwa katika hii Qur’ani, wala usiiepuke haki, ambayo Mweyezi Mungu Amekuamrisha uitumie, ukafuata matakwa yao na yale waliyoyazoea. Kwani kila kundi la watu tumewawekea sheria na njia iliyo wazi ya wao kuifuata. N a lau Mwenyezi Mungu Angalitaka, Angalizifanya sheria zenu kuwa ni moja, lakini Yeye, Aliyetukuka, Alizifanya zitafautiane ili awape mtihani, ili mtiifu na mwenye kuasi wajulikane waziwazi. Basi yakimbilieni yale yaliyo bora kwenu katika Makao Mawili yenu(duniani na Akhera), kwa kuyafuata yaliyomo kwenye Qur’ani kivitendo. Kwani mwisho wenu ni kurudi kwa Mwenyezi Mungu; huko Atawapa habari ya yale mliyokuwa mkitafautiana juu yake, na hapo Atamlipa kila mmoja kwa amali yake

    [49] Hukumu, ewe Mtume , kati ya Mayahudi kwa Aliyokuteremshia Mwenyezi Mungu katika Qur’ani, wala usiyafuate matakwa ya wale wanaoshitakiana kwako. Na jihadhari nao wasikuzuie na baadhi ya Aliyokuteremshia Mwenyezi Mungu ukaacha kuyatumia. Na iwapo wataikataa hukumu unayoitoa, basi jua kwamba Mwenyezi Mungu Anataka kuwaepusha na njia ya uongofu kwa sababu ya madhambi waliyotangulia kuyafanya. Na kwa hakika, wengi wa watu wako nje ya utiifu wa Mola wao

    [50] Je, wanataka Mayahudi hawa uhukumu kati yao kwa yale ya upotevu na ujinga waliyoyazoea washirikina wanaoabudu masanamu? Hayo hayawi wala hayafai kabisa. Na ni nani aliye muadilifu zaidi kuliko Mwenyezi Mungu katika hukumu Yake kwa aliyeziifahamu sheria za Mwenyezi Mungu, akamuamini na akawa na yakini kwamba hukumu ya Mwenyezi Mungu ndiyo ya haki

    [51] Enyi mlioamini, msiwafanye Mayahudi na Wanaswara ni washirika na wasaidizi wenu juu ya watu wa Imani. Hii ni kwa kuwa wao hawawapendi Waumini. Mayahudi wanasaidiana wao kwa wao, na hivyo hivyo ndivyo walivyo Wanaswara. Na makundi yote mawili yanakutana kwenye kuwafanyia nyinyi uadui. Na nyinyi, enyi Waumini, mnafaa zaidi kusaidiana nyinyi kwa nyinyi. Na yoyote mwenye kuwategemea wao katika nyinyi, basi yeye atakuwa ni miongoni mwao, na hukumu yake ni yao. Mwenyezi Mungu Hatawaafikia madhalimu wanaowategemea makafiri

    [52] Mwenyezi Mungu Anasimulia habari ya kikundi cha wanafiki kwamba wao walikuwa wakikimbilia kupendana na Mayahudi kwa kuwa ndani ya nyoyo zao mulikuwa na shaka na unafiki, na walikuwa wakisema, «Sisi tunapendana nao kwa kuogopa wasije wakawashinda Waislamu wakatudhuru sisi pamoja na wao.» Mwenyezi Mungu, uliotukuka utajo Wake, Anasema: Huenda Mwenyezi Mungu Akauleta ushindi- yaani ushindi wa kuukomboa mji wa Makkah-, Akamnusuru Nabii Wake na Akaupa nguvu Uislamu na Waislamu juu ya makafiri au Akatayarisha mambo ambayo yataifanya iyondoke nguvu ya Mayahudi na Wanaswara, na hapo waje wawanyenyekee Waislamu. Wakati huo watajuta wanafiki kwa yale waliyoyaficha kwenye nafsi zao ya kuwategemea Mayahudi na Wanaswara

    [53] Wakati huo watasema baadhi ya Waumini kuwaambia wengine, wakionea ajabu hali ya wanafiki, pindi mambo yao yatakapofichuka, «Je, hawa ndio wale ambao waliapa viapo vizito kwamba wao wako nasi?» Zimebatilika amali za wanafiki walizozifanya ulimwenguni, hawana malipo mema ya amali hizo, kwa kuwa wao walizifanya bila ya Imani. Hapo basi, wamepata hasara ya ulimwenguni na Akhera

    [54] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata sheria zake kivitendo, Yoyote kati yenu atakayerudi nyuma akaiacha Dini yake, na akachukua badala yake dini ya Kiyahudi au ya Kinaswara au dini nyengineyo, basi hao hawatamdhuru Mwenyezi Mungu chochote; na Atawaleta watu bora kuliko wao: Anaowapenda na wanaompenda, wenye huruma kwa Waumini, wakali kwa makafiri, wanapigana jihadi na maadui wa Mwenyezi Mungu na hawamuogopi, kwa kumridhisha Mwenyezi Mungu, yoyote. Kuneemeshwa huko ni miongoni mwa nyongeza za Mwenyezi Mungu anazompa Amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa fadhila, ni Mjuzi wa anayestahiki fadhila Zake katika waja Wake

    [55] Hakika msaidizi wenu , enyi Waumini, ni Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na Waumini wanaojilazimisha na Swala za faradhi na wanatekeleza Zaka kwa hiari yao na hali wao ni wanyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu

    [56] Na mwenye kushikamana na Mwenyezi Mungu na akafuata muongozo wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na akawa na muelekeo wa Waumini, basi yeye ni katika kundi la Mwenyezi Mungu, na kundi la Mwenyezi Mungu ndilo la washindi wenye kunusurika

    [57] Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Yake kivitendo, msiwafanye wale wanaoifanyia shere na kuichezea Dini yenu, miongoni mwa waliopewa Vitabu na makafiri, kuwa ni wasimamizi wa mambo yenu. Na muogopeni Mwenyezi Mungu mkiwa nyinyi mnamuamini Yeye na mnaziamini sheria Zake

    [58] Na anapoadhini mwadhini wenu, enyi Waumini, kuita watu kwenye Swala, Mayahudi, Wanaswara na washirikina wanafanya shere na kuukejeli mwito wenu wa hiyo Swala. Hii ni kwa sababu ya ujinga wao wa kutomjua Mola wao na kwa kuwa wao hawajui uhakika wa ibada

    [59] Sema, ewe Mtume, kuwaambia hao wanaofanya shere kati ya hao waliiopewa Kitabu, «Mnalolikuta kuwa ni jambo la kutukanika au ni la aibu, hilo kwetu ni zuri kusifika nalo. Na hilo ni lile la kumuamini kwetu Mwenyezi Mungu na vitabu Vyake vilivyoteremshwa kwetu na waliokuwa kabla yetu na kuamini kwetu kwamba wengi wenu muko nje ya njia ilyo nyofu.»

    [60] Sema, ewe Nabii, kuwaambia Waumini, «Je, niwajulishe yule ambaye atalipwa, Siku ya Kiyama, malipo makali zaidi kuliko hawa wenye kutoka nje ya utiifu?» Hao ni waliowatangulia wao ambao Mwenyezi Mungu Aliwafukuza kwenye rehema Yake, Aliwakasirikia na akawageuza maumbile yao Akawafanya manyani na ngurue kwa kuasi kwao, kuzua kwao urongo na kuwa na kiburi, kama ambavyo walikuwa kati yao wenye kuabudu Tāghūt (kila kinachoabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu nacho kimeridhika). Hao, ni pabaya mno mahali pao huko Akhera; na harakati zao ulimwenguni zilikosa mwelekeo wa njia ya sawa

    [61] Na wakiwajia nyinyi, enyi Waumini, wanafiki wa Kiyahudi husema, «Tumeamini,» na hali wao wako ukafirini na wanaendelea nao : hakika wameingia kwenu wakiwa na ukafiri wanaouitakidi ndani ya nyoyo zao, kisha wametoka wakiwa bado wanaushikilia ukafiri huo. Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi wa siri zao hata wakionyesha kinyume cha hivyo

    [62] Na utawaona, ewe Mtume, wengi miongoni mwa Mayahudi wanayakimbilia maasia ya kusema urongo, uzushi, kuzifanyia uadui hukumu za Mwenyezi Mungu na kula mali ya watu kinyume na haki. Ni maovu mno matendo yao na uadui wao

    [63] Mbona viongozi wao na wasomi wao hawawakatazi hawa ambao wanayakimbilia madhambi na kufanya uadui, kusema urongo, uzushi na kula mali za watu kinyume na haki? Ni kiovu mno walichokifanya, walipoacha kukataza munkar (mabaya)

    [64] Mwenyezi Mungu Anamjulisha Mtume Wake sehemu ya makosa ya Mayahudi, kitu walichokuwa wakikizungumza kwa siri baina yao, kuwa wao walisema, «Mkono wa Mwenyezi Mungu umefungwa kutotenda mema, Ametufanyia ubahili riziki kwa kutubania na kutotupanulia.» Walisema hilo wakati walipopatwa na ukame na ukosefu wa mvua. Mikono yao ndiyo iliyofungwa, kwa maana: mikono yao imezuiliwa kutenda mema, na Mwenyezi Mungu Amewafukuza kutoka kwenye rehema Yake kwa sababu ya neno lao. Mambo sivyo kama wanavyomzulia Mola wao, bali mikono Yake miwili imekunjuliwa, haikuzuiliwa wala hakuna pingamizi ya kumzuia kutoa. Kwani Yeye ni Mpaji, ni Karimu, Anatoa kulingana na hekima na yale yenye maslahi kwa waja. Kwenye aya hii kuna thibitisho la sifa ya Mikono miwili kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetakasita na kila sifa ya upungufu na kutukuka, kama inavyolingana na Yeye, pasi na kufananisha wala kueleza namna ilivyo. Lakini wao watazidi ukiukaji mipaka na ukafiri kwa sababu ya chuki yao na uhasidi wao kwa kuwa Mwenyezi Mungu Amekuchagua wewe kwa utume. Mwenyezi Mungu Anayatolea habari makundi ya Mayahudi kwamba wao wataendelea, mpaka Siku ya Kiyama, kufanyiana uadui wao kwa wao na kuchukiana wao kwa wao. Kila wanapopanga njama ya kuwafanyia vitimbi Waislamu, kwa kuzusha fitina na kuuwasha moto wa vita, Mwenyezi Mungu Anavikomesha vitimbi vyao na kuutenganisha mkusanyiko wao. Na Mayahudi hawataacha kuendelea kumuasi Mwenyezi Mungu kwa kufanya yanayoleta uharibifu na misukosuko katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Hawapendi waharibifu

    [65] Lau kama Mayahudi na Wanaswara wangalimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, wakazifuata amri Zake na kuyaepuka makatazo Yake, tungaliwafutia madhambi yao na tungaliwatia kwenye mabustani ya Pepo ya starehe katika Nyumba ya Akhera

    [66] Na lau kama wao wangaliyatekeleza yaliyomo ndani ya Taurati na Injili na yale uliyoteremshiwa wewe, ewe Mtume, nayo ni Qur’ani, wangalipata riziki kutoka kila njia: tukawateremshia mvua na kuwaoteshea matunda. Na haya ni malipo ya duniani. Na kwa hakika, miongoni mwa watu waliepewa Kitabu, lipo kundi la wastani lililojikita kwenye haki. Na wengi kati yao , vitendo vyao ni viovu na wamepotea njia ya sawa

    [67] Ewe Mtume, fikisha wahyi wa Mwenyezi Mungu uliyoteremshwa kwako kutoka kwa Mola wako. Na iwapo utapunguza bidii katika kuufikisha, ukaficha chochote katika wahyi huo, basi utakuwa hukuufikisha ujumbe wa Mola wako. Na kwa hakika, Mtume , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, alifikisha ujumbe wa Mola wake kikamilifu. Basi yoyote atakayedai kuwa yeye alificha chochote, katika yale aliyoteremshiwa, atakuwa amemzulia Mwenyezi Mungu na Mtume Wake urongo mkubwa. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ni Mwenye kukulinda na kukuokoa na maadui zako. Si juu yako lolote isipokuwa ni kufikisha. Kwa hakika Mwenyezi Mungu hamuelekezi kwenye uongofu aliyepotea njia ya haki na akayapinga uliyokuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu

    [68] Sema, ewe Mtume, kuwaambia Mayahudi na Wanaswara, «Nyinyi hamuna fungu lolote la dini, madhali hamkuyafuata kivitendo yaliyomo ndani ya Taurati na Injili na Qur’ani aliyokuja nayo Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie,.» Na hakika wengi wa wale waliopewa Kitabu, haiwaongezei kuteremshiwa wewe Qur’ani isipokuwa ni ujabari na kukanusha. Kwa hivyo, wao wanakuhusudu kwa kuwa Mwenyezi Mungu Amekutuma kwa ujumbe huu wa mwisho, ambao Ameeleza humo aibu zao. Basi usiwe na huzuni, ewe Mtume, juu ya kule kukukanusha kwao

    [69] Hakika wale walioamini (nao ni Waislamu), Mayahudi na al- Ṣābiūn (Masabai, nao ni watu waliosalia kwenye umbile lao na hawana dini fulani waifuatayo), Wanaswara (nao ni wafuasi wa al-Masīḥ), waliomuamini Mwenyezi Mungu miongono mwao Imani kamilifu, nayo ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu, kumuamini Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na yale aliyokuja nayo, wakaiyamini Siku ya Mwisho na wakatenda matendo mema, basi hao hawatakuwa na hofu yoyote juu ya janga la Siku ya Kiyama wala wao hawatakuwa na huzuni juu ya yale waliyoyaacha nyuma yao duniani

    [70] Kwa hakika tulichukuwa ahadi ya mkazo kwa Wana wa Isrāīl katika Taurati kuwa watasikia na watatii na tukawapelekea kwa ahadi hiyo Mitume wetu. Lakini walivunja ile ahadi iliyochukuliwa kwao, wakafuata matamanio yao na wakawa kila akiwajia Mtume, miongoni mwa hao Mitume, kwa yale ambayo nafsi zao haziyataki, wanamfanyia uadui: wakawakanusha baadhi yao na wakawaua wengine

    [71] Na walidhania waasi hawa kwamba Mwenyezi Mungu Hatawatia mkononi kwa kuwaadhibu kwa sababu ya kuasi kwao na kutakabari kwao, ndipo wakaendelea katika matamanio yao na wakawa vipofu wa kutouona uongofu na wakawa viziwi wa kutoisikia na kutonufaika na haki. Hapo Mwenyezi Mungu Aliwateremshia adhabu Yake, wakatubia na Mwenyezi Mungu Akawakubalia toba zao. Kisha wengi wao walikuwa vipofu na viziwi baada ya kubainikiwa na haki. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona matendo yao, mazuri na mabaya, na Atawalipa kwa matendo yao hayo

    [72] Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anaapa kwamba wale ambao walisema, «Mwenyezi Mungu Ndiye al-Masīh, mwana wa Maryam,» wameshakufuru kwa maneno yao haya. Na Alitoa habari Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwamba al- Masīh, alisema kuwaambia Wana wa Isrāīl, «Muabuduni Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Asiye na mshirika, kwani mimi na nyinyi katika uja tuko sawa.» Kwa hakika, yoyote atakayemuabudu mwengine, pamoja na Mwenyezi Mungu, Aliye Pweke, basi Mwenyezi Mungu Ataifanya Pepo kuwa ni haramu kwake na Ataufanya Moto kuwa ndio makao yake na hatakuwa na msaidizi wa kumuokoa nao Moto huo

    [73] Hakika wamekufuru Wanaswara waliosema, «Mwenyezi Mungu ni mkusanyiko wa vitu vitatu: Baba, Mwana na Roho mtakatifu.» Kwani Wanaswara hawa hawakujua kwamba watu hawana isipokuwa muabudiwa Mmoja, Hakuzaa wala Hakuzaliwa? Na iwapo wenye kusema maneno haya hawatakoma na uzushi wao na urongo wao, hakika itawapata wao adhabu iliyo kali iumizayo kwa sababu ya kumkufuru kwao Mwenyezi Mungu

    [74] Mbona Wanaswara hawa hawarudi kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na wakatubia kwa waliyoyasema na wakamuomba msamaha Mwenyezi Mungu Aliyetukuka? Kwani Mwenyezi Mungu , Aliyetukuka, ni Mwenye kuyasamehe madhambi ya wenye kutubia, ni Mwenye huruma kwao

    [75] Hakuwa al-Masih, mwana Maryam isipokuwa ni Mtume kama wale Mitume waliomtangulia; na mamake aliamini Imani ya dhati, kiilimu na kivitendo. Na wote wawili wanahitajia chakula kama walivyo binadamu wengineo. Na anayehitaji chakula ili aishi, hawi ni mungu. Basi izingatie, ewe Mtume, hali ya hawa makafiri.Tumekufafanulia alama zinazoonyesha upweke wetu na ubatilifu wa yale wanayoyadai kuhusu Mitume wa Mwenyezi Mungu. Kisha wao, pamoja na hilo, wanapotea njia ya haki ambayo sisi tunawaongoza waifuate. Kisha hebu angalia, vipi wanaepushwa na haki baada ya ufafanuzi huu

    [76] Sema, ewe Mtume, kuwaambia makafiri hawa, «Vipi mtamshirikisha Mwenyezi Mungu na asiyeweza kuwadhuru chochote wala kuwaletea manufaa yoyote?» Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye kuyasikia maneno ya waja Wake, Ndiye Mwenye kuzijua hali zao

    [77] Sema, ewe Mtume, kuwaambia Wanaswara, «Msiikiuke haki katika yale mnayoyaamini kuhusu mambo ya al-Masih. Wala msifuate matamanio yenu kama Mayahudi walivyofuata matamanio yao katika mambo ya dini, wakaingia kwenye upotevu, wakawafanya watu wengi wamkanushe Mwenyezi Mungu na wakatoka kwenye njia nyofu, wakaifuata njia ya upotovu na upotevu

    [78] Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anatoa habari kwamba Amewafukuza kutoka kwenye rehema Yake makafiri miongoni mwa Wana wa Isrāīl, kama ilivyoandikwa kwenye kitabu ambacho Mwenyezi Mungu Alikiteremsha kwa Dāwūd, amani imshukie, nacho ni Zaburi, na kwenye kitabu Alichokiteremsha kwa Īsā, amani imshukie, nacho ni Injili, kwa sababu ya kuasi kwao na kuyafanyia uadui kwao mambo Aliyoyatukuza Mwenyezi Mungu Aliyetukuka

    [79] Walikuwa, Mayahudi hawa, wakiyafanya maasia waziwazi, wakiridhika nayo na hawakuwa wakikatazana wao kwa wao maovu yoyote waliyoyafanya. Na hili ni katika vitendo vyao viovu. Na kwa hilo walistahiki kufukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka

    [80] Utawaona, ewe Mtume, wengi wa hawa Mayahudi wanawafanya washirikina kuwa ni wategemewa wao. Ni baya mno hilo walilolifanya la mshikamano huo uliokuwa ni sababu ya kukasirikiwa kwao na Mwenyezi Mungu na kukaa kwao milele kwenye adhabu ya Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama

    [81] Na lau hawa Mayahudi ambao wanasaidiana na washirikina walikuwa wamemuamini Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na Mtume Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na wakayakubali yale yaliyoteremshwa kwake, nayo ni Qur’ani tukufu, hawangaliwafanya makafiri kuwa ni marafiki na waokozi. Lakini wengi katika wao wako nje ya twaa ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake

    [82] Utakuta tena utakuta, ewe Mtume, kwamba watu wenye uadui mno kwa wale waliokukubali wakakuamini na wakakufuata ni Mayahudi, kwa sababu ya ukaidi wao, ukanushaji wao na kuichukia kwao haki, na wale wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu kingine, kama wanaoabudu masanamu na wengineo. Na utakuta tena utakuta kwamba walio karibu mno kimapenzi na Waislamu ni wale waliosema, «Sisi ni Wanaswara.» Hilo ni kwamba miongoni mwao kuna wasomi wanaoijua dini yao, wacha-Mungu, wanaofanya jitihadi ya ibada kwenye mindule, na kwamba wao ni wanyenyekevu, hawafanyi kiburi cha kutiubali haki. Hao ndio wale walioukubali ujumbe wa Mtume Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na wakauamini

    [83] Na miongoni mwa yale yanayoonyesha mapenzi yao kwa Waislamu ni kuwa kundi katika wao (nao ni tume ya watu wa Habashah walipoisikia Qur’ani) yalibubujika machozi macho yao wakawa na yakini kuwa hiyo ni haki iliyoteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, wakamuamini Mwenyezi Mungu, wakamfuata Mtume Wake na wakanyenyekea kwa Mwenyezi Mungu wakimuomba awatukuze kwa heshima ya kushirikiana na umati wa Muhammad, amani imshukie, katika kuwatolea ushahidi umma wengine Siku ya Kiyama

    [84] Na walisema, «Kwani tuna lawama gani sisi kwa kumuamini kwetu Mwenyezi Mungu, kuikubali haki ambayo alikuja nayo kwetu Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kumfuata kwetu yeye, na hali tunatumai kuwa Mola wetu Atatutia kwenye Pepo Yake, Siku ya Kiyama, pamoja na walio watiifu Kwake?»

    [85] Mwenyezi Mungu Akawalipa, kwa waliyoyasema ya kujienzi kwa kuuamini kwao Uislamu na kutaka kwao kuwa pamoja na watu wema, mabustani ya Pepo ambayo, chini ya miti yake inapita mito, hali ya kukaa humo, hawatatolewa humo wala hawatahamishwa. Hayo ndiyo malipo ya wema wao wa maneno na vitendo

    [86] Na wale ambao waliukanusha upweke wa Mwenyezi Mungu, wakaukataa unabii wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na wakazikanusha aya Zake zilizoteremshwa kwa Mitume Wake, hao ndio watu wa Motoni wenye kukaa daima humo

    [87] Enyi ambao mliamini, msiharamishe vizuri alivyowahalalishia Mwenyezi Mungu, miongoni mwa vyakula na vinywaji na kuoa wanawake, mkayatia mkazo mambo ambayo Mwenyezi Mungu Ameyatolea nafasi kwenu, na msipite mipaka ya vitu alivyoviharamisha Mwenyezi Mungu. Kwani Mwenyezi Mungu Hawapendi wenye kupita mipaka

    [88] Na mstarehe, enyi Waumini, kwa halali nzuri Aliyowapa Mwenyezi Mungu na kuwatunukia. Na mcheni Mwenyezi Mungu kwa kufuata amri Zake na kujiepusha na makatazo Yake. Kwani kumuamini kwenu Mwenyezi Mungu kunawalazimisha nyinyi kumcha Yeye na kumtunza

    [89] Mwenyezi Mungu Hatawapa mateso, enyi Waislamu, kwa mayamini mliyoapa bila ya kukusudia, mfano wa vile baadhi yenu wanavyosema, «Sivyo, naapa kwa Mwenyezi Mungu», «Kwa Nini? Naapa kwa Mwenyezi Mungu.» Lakini Yeye Atawapa mateso, kwa sababu ya mayamini mliyoyakusudia ndani ya nyonyo zenu. Basi mkiwa hamtekelezi yamini, dhambi lake litafutwa na Mwenyezi Mungu, kwa kafara mtakayotoa mliyowekewa na Mwenyezi Mungu ya kuwalisha masikini kumi, kila masikini mmoja apewe nusu ya pishi [kadiri ya kilo mbili na nusu] ya chakula cha kati na kati kinachotumiwa na watu wa mji aliyoko, au kuwavisha kwa kumpa kila maskini mavazi yanayomtosha kulingana na desturi, au kuacha huru mmilikiwa kumtoa kwenye utumwa. Basi mwenye kuapa ambaye hakutekeleza yamini lake ana hiari afanye mojawapo ya mambo matatu. Asipopata chochote kati ya hayo, ni juu yake afunge siku tatu. Kufanya hayo ndio kafara ya kutoyatekeleza mayamini yenu. Na yachungeni mayamini yenu, enyi Waumini, kwa kujiepusha na kuapa au kutekeleza kiapo mnapoapa au kutoa kafara msipotekeleza kiapo. Na kama alivyowaelezea Mwenyezi Mungu hukumu ya mayamini na namna ya kujivua nayo, ndivyo Anavyowaelezea hukumu za dini Yake, ili mumshukuru Yeye kwa kuwaongoza nyinyi kwenye njia iliyolingana sawa

    [90] Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo! Hakika pombe: nayo ni kila kinacholewesha kinachofinika akili, al-maysir, nayo ni kamari ambayo inakusanya aina za kuwekeana dau na mfano wake, kama zile za kuekeana badali kutoka pande mbili za wacheza kamari na kuzuia kumtaja Mwenyezi Mungu, al-ansab: mawe ambayo washirikina walikuwa wakichinja mbele yake kwa njia ya kuyatukuza na yale yanayosimamishwa ili kujisongeza karibu yake kwa ibada na al-azlam: vipande vinavyotumiwa na makafiri kutafuta uamuzi kabla ya kufanya au kuacha kufanya jambo. Hayo yote ni dhambi inayopambiwa na Shetani. Basi jiepusheni na madhambi haya, huenda nyinyi mkafuzu kwa kupata Pepo

    [91] Hakika Shetani anataka, kwa kuwapambia madhambi, kuweka baina yenu chenye kuleta uadui na chuki, kwa sababu ya kunywa pombe na kucheza kamari, na kuwaepusha na kumtaja Mwenyezi Mungu na kuswali, kwa kutokuwa na akilil katika unywaji pombe na kujishughulisha na pumbao la uchezaji kamari. Basi komekeni na hayo

    [92] Na Fuateni amri, enyi Waislamu, ya kumtii Mwenyezi Mungu na kumtii Mtume Wake Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, katika kila mnalolifanya na mnaloliacha. Na mcheni Mwenyezi Mungu na mumtunze katika hayo. Na mkikataa kufuata amri na mkayafanya mliyokatazwa, basi jueni kuwa jukumu la mjumbe wetu Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ni ufikishaji ulio wazi

    [93] Waumini waliokunywa pombe kabla haijaharamishwa hawana dhambi kwa kufanya hilo, iwapo wataiacha, wakajikinga na mambo yanayomkasirisha Mwenyezi Mungu na wakatanguliza matendo mema yanayoonyesha kuwa wao wanamuamini Yeye na wana hamu Mwenyezi Mungu, aliyetukuka, Awe radhi nao, kisha wakazidi kumtunza Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, na kumuamini mpaka wakawa, kwa ile yakini yao, wanamuabudu kama kwamba wao wanamuona. Hakika Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anawapenda wale ambao wamefikia kiwango cha ihsani (iḥsān) mpaka wakawa kuiamini kwao ghaibu (al-ghayb) ni kama vile wanavyoyaamini wanayoyaona

    [94] Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo, Mwenyezi Mungu Atawapa mtihani wa baadhi ya viwindwa vya barani, watakaokuja karibu na nyinyi kwa namna isiyo ya kawaida muweze kuwashika wadogo wao bila kutumia silaha na kuwashika wakubwa wao kwa kutumia silaha, ili Mwenyezi Mungu Awajue, ujuzi uliyofunuka wazi kwa viumbe, wale wanaomuogopa Mola wao kwa ghaibu kwa kuwa wana yakini kuwa ujuzi wa Mwenyezi Mungu kuhusu wao umekamilika, na kwa hivyo waache kuwinda wakiwa katika hali ya ihram (ihramu: kuingia kwenye ibada ya Hija au Umra). Basi yoyote mwenye kuvuka mpaka wake, baada ya maelezo haya, akafanya ujasiri wa kuwinda, na hali yeye yuko kwenye ihramu, anastahili adhabu kali

    [95] Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo, msiue viwindwa wa barani na nyinyi muko kwenye ihramu ya Hija au Umra au mkawa muko ndani ya Haram. Na yoyote mwenye kuua kiwindwa yoyote kati ya viwindwa wa barani kwa kusudi, basi malipo yake ni achinje, miongoni mwa wanyama- howa: ngamia au ng’ombe au mbuzi na kondoo, anayefanana na kiwindwa huyo, baada ya waadilifu wawili kumfanyia makadirio, na amgawe kwa masikini wa eneo la Ḥarām au anunue chakula kwa thamani ya mfano wake na awagawie masikini wa eneo la Haram, kila masikini nusu pishi au afunge, badala yake, siku moja kwa kila nusu pishi ya chakula hicho. Mwenyezi Mungu Ameyapasisha malipo haya , ili mkosa apate matokeo ya kitendo chake. Na wale ambao ilitukia kwao kufanya lolote kama hilo kabla ya kuharamishwa, basi Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ashawasamehe. Na yoyote mwenye kurudia uhalifu huo kwa kusudi, baada ya kuharamishwa, huyo amejihatarisha kupata mateso ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu katika mamlaka Yake, na miongoni mwa enzi Yake ni kuwa Yeye atamtesa anayemuasi Akitaka, hakuna chenye kumzuia kufanya hivyo

    [96] Mwenyezi Mungu Amewahalalishia, enyi Waislamu, mtapokuwa kwenye hali ya ihramu, viwindwa wa baharini, nao niwale wavuliwao baharini wakiwa hai, na chakula chake, nacho ni kiumbe kilichokufa kitokacho humo, kwa ajili mnufaike mkiwa ni wakazi au ni wasafiri. Na Ameharamishia viwindwa wa barani muko kwenye ihramu ya Hija au ya Umra. Na muogopeni Mwenyezi Mungu na mtekeleze amri Zake zote na mjiepushe na makatazo Yake yote, mpaka mfuzu kwa thawabu Zake kubwa na msalimike na ukali wa mateso Yake mnapofufuliwa ili mhesabiwe na mlipwe

    [97] Mwenyezi Mungu Amewafadhili waja Wake kwa kuijaalia Alkaba, Nyumba takatifu, ni utengenefu wa Dini yao na amani ya uhai wao. Hivyo ni kwa kuwa wamemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakasimamisha faradhi Zake. Na Ameharamisha uadui na kupigana katika miezi mitakatifu (nayo ni Mfungopili, Mfungotatu, Mfungone na Rajabu) ili mtu yoyote asimfanyie mwingine uadui katika miezi hiyo. Na Ameharamisha, Aliyetukuka, kuwavamia wanyama- howa wanaotolewa kuwa ni tunu kwa Haram. Kadhalika, Ameharamisha kuvivunjia heshima qalaid, navyo ni vitu vilivyovishwa shingoni mwa hao wanyama kuonyesha kuwa wanakusudiwa kuchinjwa kwa ibada. Hivyo basi, ni mupate kujua kuwa Mwenyezi Mungu Anayajua yote yaliyo mbinguni na ardhini, miongoni mwayo ni sheria Alizoziweka kuwahami viumbe Wake wasidhuriane wao kwa wao. Na pia mupate kujua kwamba Mwenyezi Mungu kwa kila kitu ni Mjuzi, hakuna chochote chenye kufichika Kwake

    [98] Jueni, enyi watu, kwamba Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, ni Mkali wa mateso kwa anyemuasi na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa Kusamehe, ni Mwingi wa rehema kwa anayetubia na kurejea

    [99] Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anawaelezea kwamba shughuli ya Mtume Wake , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ni kuongoza kwa kuelekeza na kufikisha na kwamba uongofu wa taufiki uko mkononi mwa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, na kwamba mambo yaliyomo ndani ya nafsi za watu, katika yale wanayoyafanya kwa siri na wanayoyatangaza, ya uongofu na upotevu, Mwenyezi Mungu Anayajua

    [100] Sema, ewe Mtume, «Hakilingani kiovu na chema cha kila kitu»: Kafiri halingani na Muumini, mwenye kuasi halingani na mtiifu, mjinga halingani na mjuzi, na mwenye kufanya uzushi halingani na mwenye kufuata njia, na mali ya haramu hayalingani na ya halali, ingawa unakuvutia wewe, ewe binadamu, wingi wa viovu na idadi kubwa ya watu wake. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, enyi wenye akili bora, kwa kujiepusha na machafu na kufanya mazuri, mpate kufuzu kwa kulifikia lengo kubwa, nalo ni radhi ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na kufaulu kupata Pepo

    [101] Enye ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu, Mtume wake na mkafuata sheria Yake kivitendo, msiulize mambo ya Dini ambayo hamkuamrishwa chochote kuhusu hayo, kama kuuliza kuhusu mambo ambayo hayajatukia au yale ambayo yatapelekea mikazo ya Sheria ambayo lau mlikalifishwa nayo yangalikuwa ni magumu kwenu, na lau mliyauliza wakati wa uhai wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie,, wakati Qur’ani inateremka, mungalielezewa, na pengine mkakalifishwa nayo na mkalemewa nayo. Hayo Mwenyezi Mungu Ameyaacha ili kuwapumzisha waja Wake nayo. Na Mwenyezi Mungu ni Msamehefu sana kwa waja wake wanapotubia, ni Mpole sana kwao, Hawaadhibu wakirudi Kwake

    [102] Mfano wa maswali hayo, waliwahi waliokuwa kabla yenu kuwauliza Mitume wao. Walipoamrishwa yale waliokuwa wakiyauliza waliyakanusha na wasiyatekeleze. Basi, tahadharini msiwe kama wao

    [103] Mwenyezi Mungu Hakuwawekea washirikina yale waliyoyazua ya kuacha kunufaika na baadhi ya wanyama wa mifugo na kuwafanya ni wa masanamu. Nao ni baḥīrah: anayekatwa sikio lake akiwa amezaa idadi fulani ya watoto, sāibah: anayeachiwa masanamu, waṣīlah: ambaye amezaa watoto wa kike mfululizo na hāmī: ngamia dume iwapo, kutokana na yeye, wamazaliwa idadi fulani ya ngamia. Lakini makafiri waliyanasibisha hayo kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa kumzulia urongo. Na wengi wa makafiri hawapambanui baina ya haki na batili

    [104] Na hawa makafiri, wanaoharamisha yaliyohalalishwa na Mwenyezi Mungu, wanapoambiwa, «Njooni kwenye hukumu zilizoteremshwa na Mwenyezi Mungu na uwamuzi wa Mtume Wake, ili halali na haramu ziwafunukie, wao huwa wakisema, «Yanatutosha yale tuliyoyarithi kwa baba zetu ya maneno na vitendo.» Je wanayasema hayo ingawa baba zao walikuwa hawajui chochote: yaani, hawaielewi haki, hawaitambui wala hawaongoki kuifikia? Basi vipi watawafuata na hali ni hii? Kwa kweli, hakuna mwenye kuwafuata isipokua mjinga zaidi kuliko wao na mpotevu zaidi wa njia

    [105] Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na mkafuata sheria Yake kivitendo, jilazimisheni nafsi zenu kujishughulisha kumtii Mwenyezi Mungu na kujiepusha na kumuasi na endeleeni daima kufanya hivyo, hata kama watu hawatakubaliana na nyinyi. Mkifanya hivyo, hautawadhuru nyinyi upotevu wa mwenye kupotea madhali nyinyi mnajilazimisha na njia ya usawa, mnaamrisha mema na mnakataza maovu. Kwa Mwenyezi Mungu ndiko marejeo yenu nyote kesho Akhera, huko atawapa habari ya matendo yenu na atawapa malipo yake

    [106] Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na mkafuata sheria Yake kivitendo, mmoja wenu akiwa karibu na kufa, basi ni juu yake awashuhudishe wasia wake waaminifu wawili miongoni mwa Waislamu, au wawili wengine miongoni mwa wasiokuwa Waislamu ikibidi hivyo, na kusiwe na Waislamu. Hao mtawashuhudisha iwapo muko safarini kwenye ardhi na mkafikiwa na kifo. Na iwapo mtautilia shaka ushahidi wao, wasimamisheni baada ya Swala, yaani, swala ya Waislamu, hasa Swala ya Alasiri, waape kwa Mwenyezi Mungu kiapo cha dhati kwamba wao hawachukui kwa ushahidi wao thamani ya kilimwengu kama badala, wala hawamfanyii mapendeleo jamaa yao na wala hawafichi kwa kiapo chao ushahidi wa Mwenyezi Mungu uliyoko kwao na kwamba wao wakilifanya hilo, basi wao watakuwa ni miongoni mwa waliofanya hatia

    [107] Wakigundua wanaohusika na maiti kuwa wale mashahidi wawili wamefanya makosa ya hiana katika ushahidi au wasia, basi na wasimame mahali pao pa ushahidi watu wawili wenye ujamaa na aliyekufa waape kwa Mwenyezi Mungu: Ushahidi wetu wa kweli unastahiki zaidi kukubaliwa kuliko ushahidi wao wa urongo. Na sisi hatukukiuka haki katika kutoa ushahidi wetu. Na tukifanya dhuluma na kutoa ushahidi usio wa haki, basi sisi tutakuwa ni miongoni mwa madhalimu wenye kukiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu

    [108] Hukumu hiyo ya kuapa baada ya Swala na kutokubali ushahidi wa hao wawili, baada ya kuutilia shaka, ndiyo inayouleta karibu zaidi uwezekano wa wao kutoa ushahidi kama ulivyo kwa kuogopa adhabu ya Akhera au kwa kuchelea yamini lao la urongo lisikataliwe na wale wenye haki baada ya kuapa kwao na asije akafedheheka yule mrongo ambaye yamini lake lilikakataliwa hapa ulimwenguni baada ya kufunuka uhaini wake. Na muogopeni Mwenyezi Mungu, enyi watu, na mumtunze msije mukaapa kiapo cha urongo na msije mkanyakuwa kwa mayamini yenu mali ya haramu. Na msikie mnayowaidhiwa nayo. Na Mwenyezi Mungu Hawaongozi watu wenye nyendo mbaya waliotoka nje ya utiifu Wake

    [109] Na ikumbukeni, enyi watu, Siku ya Kiyama, siku Mwenyezi Mungu atakapo kuwakusanya Mitume, amani iwashukie, na awaulize kuhusu majibu ya watu wao waliyoyapata, pindi walipowalingania kwenye tawhīd (kumpwekesha Mwenyezi Mungu). Na wao watajibu, «Hatuna ujuzi, sababu hatuyajui yaliyomo ndani ya nyoyo za watu wala yale waliyoyazua baada yetu. Hakika yako wewe ni Mjuzi wa kila kitu kilichofichika na kilicho wazi

    [110] Atakaposema Mwenyezi Mungu, Siku ya Kiyama, «Ewe ‘Īsā mwana wa Maryam! Kumbuka neema yangu kwako, nilipokuumba bila ya baba, na kwa mamako, nilipomteua juu ya wanawake wa ulimwengu na nikamuepusha na hatia aliyobandikwa nayo.» Miongoni mwa neema hizi kwa ‘Īsā ni kwamba Mwenyezi Mungu Alimpa nguvu na Akamsaidia kwa Jibrili, amani imshukie, akasema na watu na yeye ni mchanga wa kunyonya kabla ya wakati wa kusema na akawaita wao kuja kwa Mwenyezi Mungu na yeye ni mkubwa, nguvu zake zimeshikana, na ubarobaro wake umekamilika, kwa wahyi wa tawhīd ambao Mwenyezi Mungu Alimletea. Na miongoni mwa hizo ni kwamba Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Alimfundisha kuandika na (kusoma) maandishi bila ya mwalimu, Alimpa nguvu ya kufahamu na kuelewa, Alimfundisha Taurati Aliyomteremshia Mūsā, amani imshukie, Injili Aliyomteremshia yeye ili kuwaongoza watu. Na miongoni mwa neema hizi ni kwamba yeye anasinyanga kwa udongo kama umbo la ndege na kisha anapuliza kwenye umbo hilo na likawa ni ndege kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na miongoni mwazo ni kwamba yeye anamponyesha aliyezaliwa kipofu akawa anaona na anamponyesha mwenye mbalanga ikarudi ngozi yake kuwa na uzima kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na miongoni mwazo ni kwamba yeye anamuomba Mwenyezi Mungu Awahui wafu, na wakainuka kutoka kwenye makaburi yao wakiwa hai. Yote hayo ni kwa matakwa Mwenyezi Mungu , Aliyetukuka, na idhini Yake. Nayo ni miujiza yenye kushinda, inautilia nguvu unabii wa ‘Īsā, amani imshukie. Kisha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, Anamkumbusha neema Yake kwake alipowazuia Wana wa Isrāīl walipotaka kumuua na akawajia wao na miujiza iliyo wazi yenye kuonyesha dalili za unabii wake. Hapo walisema waliokufuru kati yao, «Hakika haya aliyokuja nayo ‘Īsā, miongoni mwa dalili zilizo wazi, ni uchawi uliofichuka

    [111] Na ukumbuke, ewe ‘Īsā, nilipotia ilhamu na msukumo katika nyoyo za watu, miongoni mwa wale waliosafiwa nawe, kuwafanya wauamini upweke wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na unabii wako, wakasema, «Tumeamini, ewe Mola wetu. Na ushuhudie kuwa sisi ni wenye kukunyenyekea na ni wenye kufuata kwa utiifu amri Yako

    [112] Na ukumbuke waliposema Ḥawāriyyūn (wasafiwa wa Nabii ‘Īsā kati ya wafuasi wake), «Ewe ‘Īsā mwana wa Maryam! Je, Anaweza Mola wako, ukimuomba, kututeremshia meza ya chakula kutoka mbinguni?» Jawabu yake ilikuwa ni kuwataka wao wajikinge na adhabu ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, wakiwa ni wenye kuamini Imani ya kikweli

    [113] Ḥawāriyyūn wakasema, «Tunataka kula kutoka kwenye meza hiyo, nyoyo zetu zipate kutulia kwa kuishuhudia, tupate kujua kwa yakini ukweli wako kuhusu unabii wako na tupate kuwa ni wenye kuishuhudia miujiza hii kwamba Mwenyezi Mungu Ameiteremsha iwe ni hoja kwetu juu ya upweke Wake na uwezo Wake kufanya Alitakalo na pia iwe ni hoja kwako juu ya ukweli kuhusu unabii wako.»

    [114] ‘Īsā mwana wa Maryam Aliyakubali matakwa ya Ḥawāriyyūn akamuomba Mola wake , Aliyetukuka na kuwa juu, kwa kusema, «Mola wetu! Tuteremshie meza ya chakula kutoka mbinguni, tupate kuifanya siku hiyo ya kuteremka kwake ni sikukuu kwetu, sisi tutaitukuza na pia watakaokuja baada yetu, na hiyo meza itakuwa ni alama na ni hoja kutoka kwako , ewe Mwenyezi Mungu, juu ya upweke wako na juu ya ukweli wa unabii wangu, na ututunuku miongoni mwa vipewa vyako vyingi, na wewe ndiye bora wa wenye kuruzuku.»

    [115] Mwenyezi Mungu, aliyetukuka, Akasema, «Mimi ni Mwenye kuwateremshia Meza ya chakula. Basi yoyote mwenye kuukanusha upweke wangu, miongoni mwenu, na unabii wa ‘Īsā, amani imshukie, baada ya kuteremka meza, nitamuadhibu adhabu kali ambayo sitamuadhibu nayo yoyote miongoni mwa viumbe.» Meza iliteremka kama alivyoahidi Mwenyezi Mungu

    [116] Na kumbuka pindi atakaposema Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Siku ya Kiyama, «Ewe ‘Īsā mwana wa Maryam! Kwani wewe uliwaambia watu, ‘nifanyeni mimi na mamangu kuwa ni waabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu’?» ‘Īsā akajibu, kwa kumtakasa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na kumuepusha na sifa za upungufu, «Haipasii kwangu kuwaambia watu yasiyokuwa haki. Nikiwa nimesema hili, basi ushalijua. Kwani hakuna chochote kinachofichika kwako. Wewe unayajua yaliyomo ndani ya nafsi yangu, na mimi siyajui yaliyomo ndani ya nafsi yako. Hakika yako wewe Ndiye Mjuzi wa kila kitu, kilichofichamana au kuwa wazi.»

    [117] ‘Īsā, amani imshukie, atasema, «Ewe Mola wangu! Sikuwaambia wao isipokuwa yale uliyonitumia wahyi nayo na ukaniamrisha kuyafikisha, ya kukupwekesha wewe tu na kukuabudu. Na mimi nilikuwa nikishuhudia vitendo vyao na maneno yao nilipokuwa nikiishi na wao. Na uliponikamilishia muda wangu wa kuishi kwenye ardhi, ukanipaza mbinguni nikiwa hai, ulikuwa wewe ndiye Mwenye kuzichungulia siri zao, na wewe ni Mwenye kushuhudia kila kitu, hakifichiki kwako chochote cheneye kufichika ardhini au mbinguni

    [118] Hakika yako wewe , ewe Mwenyezi Mungu, ukiwa utawaadhibu, basi wao ni waja wako, na wewe ndiye Mjuzi wa hali zao, unawafanya unavyotaka kwa uadilifu wako. Na ukiwa utawasamehe, kwa rehema yako, wale waliofuata njia za kuwafanya wasamehewe, basi wewe ndiye Mshindi Asiyeshindwa, Mwenye hekima katika uendeshaji mambo Wake na amri Zake. Aya hii inamsifu Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa hekima Yake, uadilifu Wake na ukaimilifu wa ujuzi Wake

    [119] Mwenyezi Mungu Atamwambia ‘Īsā Siku ya Kiyama, «Hii ndiyo Siku ya Malipo ambayo kutawafaa wale waliompwekesha Mwenyezi Mungu kule kumpwekesha kwao Mola wao na kufuata kwao sheria Yake, ukweli wao wa nia zao, maneno yao na matendo yao. Watakuwa na mabustani ya Pepo, inayopita mito chini ya majumba yake ya fahari, hali ya kukaa humo milele. Mwenyzi Mungu Ameridhika nao ndipo Akayakubali mema yao, na wao wameridhika na Yeye kwa malipo mazuri mengi aliyowapa. Malipo hayo na kuwa Yeye Ameridhika na wao ndiko kufuzu kukubwa

    [120] Ni wa Mwenyezi Mungu Peke Yake ufalme wa mbinguni na ardhini na vilivyomo ndani yake, na Yeye, Aliyetakata na kila sifa mbaya, kwa kila kitu ni muweza; hakuna kitu kinachomshinda

    Wanyama

    Surah 6

    [1] Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mwenye sifa ambazo zote ni sifa za ukamilifu, Mwenye neema za nje na za ndani, za kidini na za kidunia, Ambaye Aliumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake, Aliumba giza na mwangaza kwa kupishana usiku na mchana. Katika hili pana ishara ya utukufu wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na kuwa Yeye Peke Yake Anastahiki kuabudiwa. Haifai kwa yoyote kumshirikisha mwengine na Yeye. Na pamoja na uwazi huu, makafiri wanamsawazisha mwingine na Mwenyezi Mungu na wanamshirikisha na Yeye

    [2] Yeye Ndiye Ambaye Alimuumba baba yenu Ādam kutokana na udongo na nyinyi mnatokana na kizazi chake, kisha Akaandika muda wa kusalia kwenu katika uhai huu wa kilimwengu, na Akaandika muda mwingine maalumu hakuna aujuwao isipokuwa Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu, nayo ni Siku ya Kiyama. Kisha nyinyi baada ya haya mnashuku juu ya uwezo wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, wa kufufua baada ya kufa

    [3] Na Mwenyezi Mungu, Aliyetakata na kila sifa ya upungufu, Ndiye Mola Mwenye kuabudiwa kwa haki mbinguni na ardhini. Na miongoni mwa dalili za uungu wake ni kwamba Yeye Anayajua yote mnayoyaficha, enyi watu, na mnayoyadhihirisha na Anayajua matendo yenu yote, mazuri na mabaya. Na kwa ajili hii, Yeye Peke Yake, Aliyetukuka na kuwa juu, Ndiye Mola Anayestahiki kuabudiwa

    [4] Makafiri hawa Ambao wanamshirikisha mwingine na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, wamejiwa na hoja zilizo wazi na dalili dhahiri juu upweke wa Mwenyezi Mungu, Aiyetukuka na kuwa juu, na ukweli wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, juu ya utume wake na yale aliyokuja nayo. Lakini punde tu yalipowajia waliyaepuka na kukataa kuyakubali na wasiyaamini

    [5] Makafiri hawa waliikataa haki ambayo alikuja nayo Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na wakawafanyia shere walinganizi wake kwa sababu ya ujinga walionao kuhusu Mwenyezi Mungu na kughurika kwao na muhula Aliowapa. Basi watakuja kuyaona yale waliyoyafanyia shere kuwa ni haki na ni kweli. Na Mwenyezi Mungu Atawabainishia wakanushaji urongo wao na uzushi wao na awalipe kwa hayo

    [6] Kwani hawayajui, hawa wanaoukanusha upweke wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na kustahiki Kwake, Peke Yake, kuabudiwa na wanaomkanusha Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie,, yale yaliyowashukia watu waliokanusha kabla yao ya maangamivu na uharibifu? Hao tuliwapa utulivu kwenye ardhi kwa namna ambayo hatukuwapa nyinyi, enyi makafiri, utulivu kama huo na tuliwaneemesha kwa kuwateremshia mivua na kupita mito chini ya makao yao kwa njia ya kuwanyoshea na kuwapa muhula, wakazikanusha neema za Mwenyezi Mungu na wakawakanusha Mitume. Hapo tuliwaangamiza kwa sababu ya madhambi yao na tukawaumba baada yao watu wengine walioshika nafasi zao katika kuiamirisha ardhi

    [7] Na lau tulikuteremshia kitabu kutoka mbinguni, katika kurasa, wakazigusa washirikina hawa kwa mikono yao, wanagalisema, «Uliokuja nao ni uchawi ulio wazi uliobainika»

    [8] Na walisema washirikina hawa, «Si Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Amteremshie Muhammad Malaika kutoka mbinguni ili amsadiki kwa yale aliyokuja nayo Ya utume.» Na lau tulimteremsha Malaika kutoka mbinguni kwa kujibu ombi lao, uamuzi wa kuwaangamiza ungalipitishwa, na wasingepewa muhula wa kutubia, kwani imetangulia kwenye ujuzi wa Mwenyezi Mungu kuwa wao hawataamini

    [9] Na lau kama tulimfanya mtume aliyeteremshwa kwao ni Malaika, kwani hawakukinai na Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, tungalimfanya Malaika huyo kwenye sura za mwanadamu, ili waweze kumsikia na kusema naye. Kwani haimkiniki kwao kumuona Malaika katika sura zake za kimalaika. Na lau Malaika aliwajia kwa sura za mtu, jambo hilo lingaliwafanya wachanganyikiwe kama lilivyowafanya wachanganyikiwe jambo la Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [10] Na kwa kuwa kutaka kwao kuteremshwa Malaika kulikuwa ni kwa njia ya kumfanyia shere Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, Mwenyeyezi Mungu, Aliyetukuka, Aliwaelezea kwamba kuwafanyia shere Mitume, amani iwashukie, si jambo jipya; kwani jambo hilo lilitukia kwa makafiri waliopita kuwafanyia Mitume wao, wakazungukwa na adhabu ambayo walikuwa wakiifanyia shere na wakipinga kuja kwake

    [11] Sema kuwaambia, ewe Mtume, «Endeni katika ardhi kisha muangalie: namna gani Mwenyezi Mungu aliwaletea maangamivu na hizaya mwishoni? Basi tahadharini yasiwafikie mfano wa maanguko yao, na ogopeni yasije yakawashukia nyinyi kama yale yaliyowashukia wao.»

    [12] Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Ni ya nani mamlaka ya mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake?» Sema, «Ni ya Mwenyezi Mungu. Na kama mnavyolikubali hilo na kulijua, basi muabuduni Yeye Peke Yake. Mwenyezi Mungu Amechukua ahadi juu ya nafsi Yake kurehemu, Hatawaangusiliza waja Wake kwa kuwatesa. Kwa hakika Atawakusanya nyinyi kwenye Siku ya Kiyama ambayo haina shaka ili mhesabiwe na mlipwe. Wale waliomshirikisha Mwenyezi Mungu wamejiangamiza nafsi zao; wao hawampwekeshi Mwenyezi Mungu wala hawaiamini ahadi Yake ya Pepo na Moto na hawaukubali unabii wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [13] Ni wa Mwenyezi Mungu umiliki wa kila kitu, kilicho mbinguni na ardhini, kilichotulia na kinachotembea, kilichofichika na kilicho wazi. Vyote ni watumwa Wake na viumbe Vyake na viko chini ya utendeshaji nguvu Wake, uendeshaji Wake na upangaji Wake. Yeye Ndiye Msikizi wa maneno ya waja Wake, Ndiye Mjuzi wa siri zao na matendo yao

    [14] Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na asiyekuwa Yeye, «Je, nimchukue asiyekuwa Mwenyezi Mungu kuwa ni msaidizi na ni mwokozi, na hali Yeye ni Muumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake, na Yeye Ndiye Mwenye kuwaruzuku viumbe Wake na hakuna mwenye kumruzuku Yeye?» Sema,ewe Mtume, «Mimi nimeamrishwa niwe ni wa mwanzo aliyemnyenyekea Yeye na kumwandama katiika umma huu. Na nimekatazwa kuwa ni miongoni mwa wanaomshirikisha Yeye na asiyekuwa Yeye

    [15] Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu na asiyekuwa Yeye, «Mimi naogopa nikimuasi Mola wangu, nikaenda kinyume na maamrisho Yake, na nikamshirikisha Yeye na asiyekuwa Yeye, kuteremkiwa na adhabu kubwa Siku ya Kiyama

    [16] Yule ambaye Mwenyezi Mungu Amemuepushia adhabu kali hiyo, basi Amemrehemu. Kuepushwa huko ndiko kufaulu kuliko wazi kwa kuokolewa na adhabu kubwa

    [17] Na Akikupatia Mwenyezi Mungu jambo la kukudhuru, kama ufukara na ugonjwa, hakuna mwenye kuliondoa hilo isipokuwa Yeye; na Akikupatia zuri, kama utajiri na afya, hakuna mwenye kuondoa wema wake na hakuna mwenye kuzuia mapitisho Yake, kwani Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu, ni muweza wa kila kitu

    [18] Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu, Ndiye Mwenye kutendesha nguvu, Aliye juu ya waja Wake. Shingo zimemdhalilikia na majabari wamenyongeka Kwake. Yeye Ndiye Mwenye hekima Anayeweka vitu mahali pake kulingana na hekima Yake. Ndiye Mtambuzi Ambaye hakuna kitu chenye kufichika Kwake. Na mwenye kusifika na sifa hizi inapasa asishirikishwe. Katika aya hii pana kuthibitisha sifa ya ujuu kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kuwa Yuko juu ya ya viumbe vyake vyote; ujuu wa aina zote unaonasibiana na utukufu Wake, kutakasika na kila sifa ya upungufu ni Kwake

    [19] Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Ni kitu gani chenye ushahidi zaidi katika kuthibitisha ukweli wangu katika haya ninayowaambia kwamba mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu?» Sema, «Mwenyezi Mungu ni shahidi baina yangu mimi na nyinyi.» Yaani: yeye Ndiye Mjuzi wa niliyokuja nayo kwenu na yale mtakayonambia. «Na Mwenyezi Mungu Ameniletea mimi Qur’ani hii kwa njia ya wahyi ili ni waonye nayo adhabu ya Mwenyezi Mungu isiwashukie, na niwaonye nayo ummah wengine ambao itawafikia.» Nyinyi mnakubali kwamba, pamoja na Mwenyezi Mungu, pana waabudiwa wengine mnaowashirikisha Naye. Waambie, ewe Mtume, «Mimi sitoi ushahidi juu ya lile mlilolikubali. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mola mmoja Asiye na mshirika. Na mimi nimejiepusha na kila mshirika mnayemuabudu pamoja na Yeye

    [20] Wale tuliowapa Taurati na Injili wanamjua Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa sifa Zake zilizoandikwa kwao kama wanavyowajua watoto wao. Na kama ilivyo wao hawachanganyikiwi kuwajua watoto wao walio mbele yao kuwapambanua na wengine, vilevile Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, hachanganyiki na mwingine, kwa sababu ya uwazi wa sifa zake zilizo ndani ya vitabu vyao. Lakini wao walifuata matamanio yao, walipomkanusha Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na yale aliyokuja nayo, ndipo wakapata hasara nafsi zao

    [21] Hakuna yoyote mwenye udhalimu mbaya zaidi kuliko yule aliyemzulia Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, urongo na akadai kwamba Yeye Ana washirika katika ibada, au akadai kwamba Yeye Ana mtoto au mke, au akazikanusha hoja Zake na dalili ambazo kwazo Aliwapa nguvu Mitume Wake, amani iwashukie. Hakika ya mambo ni kwamba madhalimu waliomzulia Mwenyezi Mungu urongo hawafaulu na hawapati matakwa yao ulimwenguni wala Akhera

    [22] Na wajihadhari washirikina hawa wenye kuzikanusha aya za Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na Siku ambayo tutawafufua kisha tutasema kuwaambia, «Wako wapi waungu wenu ambao mlikuwa mkidai kuwa wao ni washirika na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ili wawaombee nyinyi?»

    [23] Kisha hayakuwa majibu yao, walipojaribiwa na kupewa mtihani kwa kuulizwa kuhusu washirika wao, isipokuwa walijitoa na wao na wakaapa kwamba wao hawakuwa ni wenye kumshirikisha yoyote na Mwenyezi Mungu

    [24] Fikiri, ewe Mtume, vipi washirikina hawa wanasema urongo juu ya nafsi zao, na wao kesho Akhera watajiepusha na ushirikina! Yatawaondokea wao na kuwapotea yale waliokuwa wakiyadhania ya kuwa waungu wao watawaombea

    [25] Kati ya washirikina hawa kuna wanaokusikiliza usomapo Qur’ani, ewe Mtume, na isifike kwenye nyoyo zao. Kwa kuwa wao, kwa sababu ya kufuata matamanio yao, tumeweka vifuniko juu ya nyoyo zao wasipate kuifahamu Qur’ani. Na tumejaalia kwenye masikio yao uzito na uziwi, hayasikii wala hayafahamu chochote. Na wanapoziona dalili nyingi zenye kuonyesha ukweli wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, hawaziamini. Na hata wakikujia , ewe Mtume, baada ya kuzishuhudia dalili zenye kuonesha ukweli wako, huwa wakisema wenye kuzikanusha aya za Mwenyezi Mungu, «Haya tunayoyasikia si chochote isipokuwa ni ngano zinazohadithiwa na watu wa kale zisizo na ukweli.»

    [26] Na washirikina hawa wanawakataza watu kumfuata Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kumsikiliza, na wao wenyewe wanajiepusha naye. Na wao hawamuangamizi yoyote, kwa kuzuia kwao njia ya Mwenyezi Mungu isifuatwe, isipokuwa nafsi zao wenyewe, na wao hawatambui kuwa wajishughulisha na mambo ya kuzitia kwenye maangamivu

    [27] Na lau utawaona, ewe Mtume, washirikina hawa Siku ya Kiyama, utaona jambo kubwa, nalo ni wakati wao watakapofungwa juu ya Moto, na watakaposhuhudia yaliyomo humo miongoni mwa minyororo na pingu, na kujionea kwa macho yao mambo makubwa hayo na vituko hivyo. Hapo watasema, «Twatamani turudishwe kwenye maisha ya kilimwengu, tupate kuziamini aya za Mwenyezi Mungu na tuzitumie na tuwe ni miongoni mwa Waumini.»

    [28] Mambo si kama hivyo! Bali Siku ya Kiyama yatawadhihirikia wao yale waliokuwa wakiyafanya kwa nafsi zao, ya kuamini ukweli wa yale ambayo Mitume walikuja nayo ulimwenguni, ingawa walikuwa wakiwadhihirishia wafuasi wao kinyume chake. Na lau ilikadiriwa warudishwe ulimwenguni na waongezewe muda, wangalirudi kwenye upinzani kwa kukufuru na kukanusha. Na kwa kweli wao ni warongo katika neno lao, «Lau tutarudishwa ulimwenguni hatungalizikanusha aya za Mola wetu na tungalikuwa Waumini.»

    [29] Na hawa washirikina wanaokanusha kufufuliwa wanasema, «Hakuna maisha isipokuwa maisha haya tuliyonayo, na sisi si wenye kufufuliwa baada yakufa kwetu.»

    [30] Na lau utawaona, ewe Mtume, wenye kukanusha kufufuliwa watakapofungwa mbele ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ili uamuzi wa Mwenyezi Mungu upite kuhusu wao Siku ya Kiyama, ungaliona hali mbaya sana, pindi Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, Atakaposema, «Je, ufufuzi huu, mliokuwa mkiukanusha ulimwenguni, si kweli?» Watasema, «Kwani? Tunaapa kwa Mola wetu kuwa huu ni kweli.» Hapo Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Atasema, «Basi onjeni adhabu kwa mlivyokuwa mkikufuru,» yaani, adhabu ambayo mlikuwa mkiikanusha ulimwenguni kwa sababu ya kumkataa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na Mtume Wake Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [31] Hakika wamepata hasara wale waliokanusha kufufuliwa baada ya kufa. Mpaka Kiyama kitakaposimama na wakashutushwa kwa mwisho mbaya, watazipigia nafsi zao kelele za majuto juu ya kile walichokipoteza katika maisha yao ya ulimwenguni, hali ya kwamba wanabeba madhambi yao juu ya migongo yao. Ni mibaya iliyoje mizigo hiyo mizito iliyo miovu ambayo wataibeba

    [32] Maisha ya kilimwengu hayakuwa, katika wingi wa hali zake, isipokuwa ni udanganyifu na ubatilifu. Na matendo mema, kwa kutengeneza nyumba ya Akhera, ndiyo bora kwa wenye kumcha Mwenyezi Mungu, wakajikinga na adhabu Yake kwa kumtii na kujiepusha na mambo ya kumuasi. Kwani hamuelewi, enyi washirikina mlioghurika na pambo la uhai wa kilimwengu, mukayatanguliza yanayosalia mbele ya yanayomalizika

    [33] Hakika sisi tunajua kwamba msimamo wa kaumu zako wa kukukanusha waziwazi unakutia huzuni moyoni mwako. Basi subiri na ujitulize. Kwani wao hawakukanushi wewe kutoka ndani ya roho zao; wao waamini ukweli wako, lakini wao kwa udhalimu na uadui walionao, wanazikataa hoja zilizo wazi zinazoonyesha ukweli wako, ndipo wakakufanya mrongo kwa yale uliyokuja nayo

    [34] Hakika makafiri waliwakanusha Mitume kabla yako Aliyowatuma Mwenyezi Mungu, Aliyotukuka, kwa umma wao. Wao waliudhiwa katika kufuata njia Yake na wakasubiri juu ya hilo na wakaendelea katika ulinganizi wao na bidii yao mpaka ikawajia nusura ya Mwenyezi Mungu. Na hakuna mwenye kuyageuza maneno ya Mwenyezi Mungu, nayo ni yale Aliyoyateremsha kwa Nabii Wake Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, yenye ahadi Yake kwamba Atampa ushindi juu ya wanaomfanyia uadui. Na hakika imekujia wewe, ewe Mtume, habari ya Mitume waliokuwa kabla yako na nusura ya Mwenyezi Mungu iliyohakikishika kwao na mateso ya Mwenyezi Mungu na ghadhabu Zake zilizowafikia wenye kuwakanausha. Basi wewe una kiolezo chema na mfano wa kuiga kutoka kwa Mitume waliotangulia. Katika hili pana kumliwaza Mtume , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [35] Na iwapo umekuwa ni mzito kwako, ewe Muhammad, upinzani wa hawa washirikina na kujiepusha kwao kukubali ulinganizi wako, basi ukiweza kujifanyia mapito ndani ya ardhi, au ngazi ya kupandia mbinguni ili uwaletee alama na dalili ya usahihi wa maneno yako, zisizokuwa hizi tulizokuletea, fanya hivyo. Na lau Mwenyezi Mungu Alitaka kuwakusanya kwenye uongofu ambao nyinyi munao na kuwaongoza kwenye Imani, Angalifanya hivyo. Lakini Hakulitaka hilo, kwa hekima Anayoijua Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake. Basi, usiwe kabisa ni miongoni mwa wale wajinga ambao huzuni zao zilizidi na wakawa na majonzi mpaka hayo yakawapelekea kwenye babaiko kubwa

    [36] Hakika wale wanaokukubali wewe, ewe Mtume, kwa yale unayoyalingania ya uongofu ni wale ambao wanayasikia maneno kwa kuyakubali. Ama makafiri, wao wamo kwenye hesabu ya wafu. Kwani uhai wa kikweli unakuwa kwa Uislamu. Na wafu, Mwenyezi Mungu Atawatoa kutoka kwenye makaburi yao wakiwa hai. Kisha watarudi Kwake Siku ya Kiyama ili watimiziwe hesabu yao na malipo yao

    [37] Na washirikina walisema, kwa ujeuri na kiburi, «Kwa nini Mwenyezi Mungu Hateremshi alama iyoneshayo ukweli wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, miongoni mwa alama za kimiujiza.» Waambie, ewe Mtume, «Mwenyezi Mungu ni muweza wa kuwateremshia miujiza, lakini wengi wao hawajui kwamba kuteremsha miujiza kunakuwa kulingana na hekima Yake, Aliyetukuka.»

    [38] Hakuna katika ardhi mnyama yoyote anayetembea chini au ndege anayepaa juu kwa mbawa zake isipokuwa ni aina ya makundi yaliyoumbwa kama nyinyi. Hatukuacha katika Allawh, Almaḥfūd (Ubao Uliohifadhiwa) chochote isiopokuwa tumekithibitisha. Kisha wao, Siku ya Kiyama, watafufuliwa wapelekwe kwa Mola wao, na hapo Mwenyezi Mungu Atamhesabu kila mtu kwa alilolitenda

    [39] Na wale waliozikanusha hoja za Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ni viziwi hawasikii yanayowafaa, ni mabubu hawaitamki haki. Wao wametunduwaa kwenye giza, hawakufuata njia iliyolingana sawa. Yule ambaye Mwenyezi Mungu Anataka kumpoteza Anampoteza na yule Anayetaka kumuongoza Anamfanya awe kwenye njia iliyolingana sawa

    [40] Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina, «Nipeni habari, ikiwajia adhabu ya Mwenyezi Mungu ulimwenguni, au ikawajia saa ya nyinyi kufufuliwa, je, mutamuomba hapo asiyekuwa Mwenyezi Mungu awaondolee shida iliyowakumba, iwapo nyinyi ni wakweli kwamba waungu wenu mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu wanawanufaisha au kuwadhuru?»

    [41] Bali hapo mtamuomba Mola wenu Aliyewaumba, si mwingine, na mtamtaka Awaokoe na Awaondolee shida kubwa zilizowashukia Akitaka, kwani Yeye Ndiye Muweza wa kila kitu; na wakati huo mtaacha masanamu wenu na wategemewa wenu

    [42] Hakika tuliwatuma, ewe Mtume, Wajumbe kuwaendea makundi ya watu kabla yako kuwalingania kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, wakawakanusha na tukawapa mtihani katika mali yao, kwa ufukara mwingi na dhiki za maisha, na tukawapa mitihani katika miili yao, kwa magonjwa na kuumwa, ili wajidhalilishe kwa Mola wao na wanyenyekee Kwake Peke Yake kwa ibada

    [43] Basi si ilipowajia, umma hawa wenye kukanusha, mitihani yetu wajidhalilishe kwetu. Lakini wao nyoyo zao zilisusuwaa na Shetani aliwapambia yale ambayo waliokuwa wakiyafanya ya maasia na wakiyaleta ya ushirikina

    [44] Basi walipoacha kufuata amri za Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa kuzipa mgongo, tuliwafungulia milango ya kila kitu miongoni mwa riziki, ndipo tukawabadilishia shida kwa kuwapa raha ya maisha, na tukawabadilishia magonjwa kwa kuwapa uzima wa miili, kwa kuwavuta kidogo kidogo. Hata watakapofanya kiburi na wakajiona kwa mema na neema tulizowapa, tutawashushia adhabu ya ghafla, wakitahamaki watajikuta wamekata tamaa wamekatika na kila zuri

    [45] Watu hawa walimalizwa na kuangamizwa walipomkanusha Mwenyezi Mungu na kumkanusha Mtume Wake; hakuna yoyote aliyesalia kati yao. Shukrani na sifa njema ni za Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Muumba na Mwenye kumiliki kila kitu, kwa kuwapa ushindi mawalii Wake na kuwaangamiza maadui Zake

    [46] Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina hawa, «Nambieni ikiwa Mwenyezi Mungu Ameyaondoa masikizi yenu Akawafanya viziwi, Akayaondoa macho yenu Akawafanya vipofu na Akapiga mhuri juu ya nyoyo zenu mkawa hamufahamu neno, basi ni mola gani asiyekuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, awezaye kuwarudishia nyinyi vitu hivyo?» Angalia, ewe Mtume, ni namna gani sisi tunawatolea hoja aina mbalimbali, kisha wao baada yake wanakataa kukumbuka na kuzingatia

    [47] Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina hawa, «Nambieni iwapo mateso ya Mwenyezi Mungu yamewashukia ghafla na hali kwamba nyinyi hamuna hisia nayo, au yakawa waziwazi yanaonekana na nyinyi mnayaangalia: Je, kwani kuna wanaoteswa isipokuwa wale watu madhalimu ambao wamekiuka mpaka kwa kuipeleka ibada kwa asiyekuwa Mwenyezi mungu, Aliyetukuka, na kwa kukanusha kwao Mitume Yake?»

    [48] Na hatuwatumi wajumbe wetu isipokuwa wenye kuwapa bishara njema wenye kututii kuwa watakuwa na starehe ya daima, na kuwapa onyo wenye kuasi kuwa watakuwa na adhabu kali. Basi mwenye kuamini, akawasadiki mitume na akafanya mema, hao hawataogopa wakati wa kukutana na Mola wao wala hawatakuwa na masikitiko juu ya chochote walichokikosa miongoni mwa hadhi za kilimwengu

    [49] Na wale waliozikanusha aya zetu za Qur’ani na miujiza, hao itawapata adhabu Siku ya Kiyama kwa sababu ya ukafiri wao na kutoka kwao kwenye twaa ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka

    [50] Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina hawa, «Mimi sidai kuwa ninamiliki hazina za mbingu na ardhi nikawa ninazitumia nitakavyo; na sidai kuwa mimi najua al-ghayb (yasiyoonekana); na sidai kuwa mimi ni Malaika. Mimi ni Mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu, nafuata yale nliyoteremshiwa kwa njia ya wahyi na nawafikishia watu wahyi Wake.» Waambie, ewe Mtume, washirikina hawa. «Je, kafiri aliye kipofu wa kutoziona aya za Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, asiziamini yuko sawa na Muumini anayeziona aya za Mwenyezi Mungu na akaziamini? Kwani nyinyi hamuzifikirii aya za Mwanye ili muione haki na muiamini?»

    [51] Na watishe, ewe Mtume, kwa hii Qur’ani wale ambao wanajua kuwa wao watafufuliwa wapelekwe kwa Mola wao. Wao wanaiyamini ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kuwalipa mema wenye kufanya wema na kuwalipa maovu wenye kufanya uovu. Wao hawana, isipokuwa Mwenyezi Mungu, mtegemewa mwenye kuwanusuru wala muombezi mwenye kuwaombea mbele Yake Aliyetukuka Akawaokoa na adhabu Yake. Kwani huenda wao wakamcha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa kuyafanya maamrisho na kuyaepuka makatazo

    [52] Na usiwatenge, ewe Nabii, kukaa na wewe Waislamu wanyonge wanaomuabudu Mola wao mwanzo wa mchana na mwisho wake, hali wakitaka, kwa matendo yao mema, radhi za Mwenyezi Mungu. Kitu chochote kuhusu hesabu ya maskini hawa hakiko juu yako; hesabu yao iko juu ya Mwenyezi Mungu. Na si juu yao chochote kuhusu hesabu yako. Basi ukiwatenga , utakuwa ni miongoni mwa wenye kuivuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, wenye kuweka vitu mahali pasipokuwa pake

    [53] Na hivyo basi Mwenyezi Mungu Amewapa mtihani waja Wake kwa kutafautiana mafungu yao ya riziki na umbo, Akawafanya baadhi yao matajiri na wengine maskini, baadhi yao wenye nguvu na wengine madhaifu Na Akawafanya baadhi yao ni wahitaji wa wengine ili kuwajaribu kwa hilo, wapate makafiri matajiri kusema, «Ni madhaifu hawa, miongoni mwetu, Mwenyezi Mungu Amewapa neema ya Uislamu?» Kwani Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, si Mjuzi zaidi wa wanaoshukuru neema Yake Akawaafikia kwenye uongofu wa dini Yake

    [54] Na wakikujia, ewe Nabii, wale wanaoamini aya za Mwenyezi Mungu zenye kushuhudia ukweli wako juu ya Qur’ani na mengineyo, kutaka fatuwa kuhusu toba ya madhambi yao yaliyotangulia, basi wakirimu kwa kuwarudishia salamu na uwape bishara ya rehema ya Mwenyezi Mungu iliyo kunjufu. Kwani Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu, Ametoa ahadi Yake Mwenyewe kuwarehemu waja Wake kwa kuwafanyia wema kwamba mwenye kufanya dhambi kwa kutojua mwisho wake mbaya na kuwa linapelekea kukasirikiwa na Mwenyezi Mungu-Basi kila mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu kwa kukosea au kwa kusudi huwa ni mjinga kwa mtizamo huu, ingawa ajua kuwa ni haramu- kisha baada yake akatubia na akaendelea kufanya matendo mema, basi Mwenyezi Mungu Atamsamehe dhambi lake, kwani Yeye ni Mwingi wa kusamehe kwa waja Wake wenye kutubia, ni Mwingi wa rehema kwao

    [55] Na mfano wa ufafanuzi huu tuliokufafanulia, tunakufafanulia, ewe Mtume, hoja zilizo wazi kwa kila mtu, ili ifunuke njia ya watu wa haki wanayoikanusha watu wa batili, na ifunuke njia ya watu wa batili wenye kuwaendea kinyume Mitume

    [56] Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Hakika Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, Amenikataza niabudu masanamu ambao mnaowaabudu badala Yake.» Na uwaambie, «Sitafuata matamanio yenu. Nitakuwa nimepotea njia ya sawa nikifuata matamanio yenu na sitakuwa ni miongoni mwa walioongoka.»

    [57] Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Mimi niko kwenye hoja iliyo wazi ya sheria ya Mwenyezi Mungu Aliyoniletea kwa njia ya wahyi. Nayo ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu Peke Yake kwa ibada. Na hili mlilikanusha. Na haliko kwenye uwezo wangu jambo la kuwateremshia adhabu mnayoitaka kwa haraka. Na uamuzi wa kuchelewesha hilo uko tu kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka. Yeye Anahadithia ukweli na Yeye Ndiye bora wa kupambanua baina ya haki na batili kwa uamuzi Wake na hukumu Yake.»

    [58] Sema, ewe Mtume, «Lau mimi nina mamlaka ya kuwateremshia adhabu ambayo mnaitaka kwa haraka, ningaliiteremsha kwenu, na uamuzi, baina yangu mimi na nyinyi, ungalitoka. Lakini hilo liko kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka. Na Yeye Anawajua zaidi madhalimu ambao wamepita mipaka yao wakawashirikisha wengine pamoja na Yeye

    [59] Na kwa Mwenyezi Mungu , Aliyetukuka na kuwa juu, kuna mafātih( al-ghayb, yaani: hazina za mambo ya ghaibu yaliyofichika, hakuna azijuwazo ila Yeye. Miongoni mwazo ni ujuzi wa Kiyama, kuteremka mvua, viliyomo ndani ya zao, matendo ya siku zinazokuja na mahala mtu atakapokufa. Na Anajua kila kilichoko barani na baharini. Na hakuna jani, linaloanguka kutoka kwenye mmea wowote, isipokuwa Yuwalijua. Na kila chembe iliyofichika ardhini na kila kibichi na kikavu, kimethibitishwa kwenye kitabu kilicho wazi kisicho na utatizi nacho ni Al-Lawh(Al-Maḥfūẓ ( Ubao Uliohifadhiwa)

    [60] Na Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Anayezichukua roho zenu usiku kwa namna inayofanana na vile roho hizo zinachukuliwa kipindi cha kifo, na Anayajua matendo mnayoyafanya mchana, kisha Anazirudisha roho zenu kwenye miili yenu kwa kuamka kutoka usingizini kipindi cha mchana kwa namna inayofanana na kuhuisha baada kufa, ili umalizike muda maalumu uliowekwa wa maisha yenu ulimwenguni. Kisha marejeo yenu ni kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, baada ya kufufuliwa kwenu kutoka kwenye makaburi yenu mkiwa hai. Kisha Atawaelezea yale mliokuwa mkiyafanya kipindi cha maisha yenu ya ulimengu. Kisha Atawalipa kwa hayo

    [61] Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ndiye Al-Qāhir (Mtendesha nguvu), Aliye juu ya waja Wake, ujuu wa kila namana usio na mipaka unaonasibiana na utkufu Wake, kutakata na kila sifa mbaya ni Kwake na kutukuka ni Kwake. Kila kitu kinaunyenyekea utukufu Wake na ukubwa Wake. Yeye Anawatuma kwa waja Wake Malaika kuyadhibiti matendo yao na kuyahesabu. Mpaka kifo kinapomshukia mmoja wao, Malaika wa mauti na wasaidizi wake wanaichukua roho yake, na wao hawaachi kutekeleza walichoamrishwa kukifanya

    [62] Kisha hawa waliokufa watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Mola wao wa kweli. Jua utanabahi kwamba hukumu na uamuzi baina ya waja Wake, Siku ya Kiyama, ni Vyake Yeye tu. Na Yeye Ndiye Mwpesi wa wenye kuhesabu

    [63] Waambie, ewe Mtume, hawa washirikina, «Ni nani mwenye kuwaokoa na vitisho vya magiza ya bara na bahari? Kwani si Mwenyezi Mungu mnayemuomba kwenye matatizo mkionesha unyonge wenu kwa dhahiri na kwa siri? Huwa mkisema, ‘Hakika Mola wetu Akituokoa na vitisho hivi, tutakuwa ni wenye kushukuru kwa kumuabudu, Aliyeshinda na kutukuka, Peke Yake, Asiye na mshirika.»

    [64] Waambie, ewe Mtume, «Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Ndiye Mwenye kuwaokoa na vitisho hivyi na kila tatizo, kisha nyinyi baada ya hapo mnawashirikisha wengine pamoja Naye katika ibada.»

    [65] Sema, ewe Mtume, «Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, Ndiye Muweza, Peke Yake, kuwatumia adhabu kutoka juu yenu, kama kupigwa majiwe au mvua ya mafuriko na mfano wake, au kutoka chini ya miguu yenu, kama mitetemeko ya ardhi na kuzama ndani ardhi, au Awavurugie mambo yenu muwe makundi yanayozozana, mnauana nyinyi kwa nyinyi,» Angalia, ewe Mtume, vipi tunazifanya aina mbalimbali hoja zetu zilizo wazi kwa hawa washirikina ili waelewe na wazingatie

    [66] Na waliikanusha hii Qur’ani makafiri kati ya watu wako, ewe Mtume; nayo ni kitabu chenye ukweli katika kila kilichokuja nacho, Waambie, «Mimi si mlinzi wala mtunzi juuu yenu. Mimi ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu, nawafikishia nyinyi yale niliotumwa nayo kwenu

    [67] Kila habari ina kituo cha kutulia na kikomo cha kukomea, hapo haki na batili zitafunuka. Na mtajua, enyi makafiri, mwisho wa jambo lenu, itakaposhuka adhabu ya Mwenyezi Mungu kwenu

    [68] Na uwaonapo, ewe Mtume, washirikina wanaoleta maneno juu ya aya za Qur’ani, kwa urongo na kwa kufanya shere, jiepushe na wao mpaka waingie kwenye maneno mengine. Na iwapo Shetani amekusahaulisha jambo hili, basi baada ya kukumbuka usikae pamoja na watu wenye uadui walioleta maneno ya urongo juu ya aya za Mwenyezi Mungu

    [69] Na wale Waumini wanaomuogopa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, wakatii amri Zake na wakaepuka makatazo Yake, hawana jaukumu lolote juu ya hesabu ya Mwenyezi Mungu kwa wale wenye kuvama kwenye maneno yasiyofaa, wenye kuzifanyia shere aya za Mwenyezi Mungu. Lakini ni juu yao wawaidhie waache kulete maneno hayo ya batili, kwani huenda wao wakamcha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka

    [70] Na waache, ewe Mtume, hawa washirikina ambao wameifanya dini ya Uislamu ni mchezo na pumbao, wazifanyia shere aya za Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na yamewaghuri wao maisha ya kilimwengu pamoja na pambo lake. Na wakumbushe, kwa Qur’ani, hawa washirikina na wengineo, ili nafsi isifungike kwa madhambi yake na kumkanusha kwake Mola wake. Haina, isipokuwa Mwenyezi Mungu, mlinzi mwenye kuinusuru akaiokoa na adhabu Yake, wala muombezi mwenye kuiyombea mbele Yake. Na ikitoa ili kujikomboa kiwango kiwacho cha fidia haitakubaliwa kwake. Hao ndio ambao wamefungika na dhambi zao. Watakuwa na kinywaji moto sana na adhabu yenye kuumiza Motoni, kwa sababu ya kumkanusha kwao Mwnyezi Mungu, Aliyetukuka, Mtume Wake, Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na dini ya Uislamu

    [71] Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Je, tuabudu, asiyekuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, masanamu yasionufaisha wala kudhuru? Je, turudi ukafirini baada ya Mwenyezi Mungu kutuongoza kwenye Uislamu, tukafanana, katika kurudi kwetu ukafirini, na aliyeharibika akili yake kwa kusawazwa na mashetani akapotea njia ardhini na hali yeye ana marafiki wenye akili, wenye Imani, wamwita kwenye njia ya sawa ambayo wao wako akawa anakataa?» Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Uongofu wa Mwenyezi Mungu Aliyenituma mimi ndio uongofu wa haki. Na sote tumeamrishwa tujisalimishe kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Bwana wa vuimbe vyote, kwa kumuabudu, Peke Yake, Asiye na mshirika, kwani Yeye Ndiye Mola na Mmiliki wa kila kitu.»

    [72] Na hivyohivyo tumeamrishwa tusimamishe Swala kikamilifu, tumuogope Yeye kwa kufanya maamrisho Yake na kuepuka makatazo Yake. Na Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu, Ndiye Ambaye Kwake Yeye watakusanywa viumbe wote Siku ya Kiyama

    [73] Na Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa pungufu ni Kwake, Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi kwa haki. Na taja,ewe Mtume, Atakaposema Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama, «Kuwa» na ikawa kulingana na amri Yake, kama kupepesa macho au muda mfupi zaidi. Neno lake Ndio haki iliokamilika. Na ni Wake ufalme, Peke Yake, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Siku Malaika atakapovuvia Parapanda, mvuvio wa pili ambao, kwa huo, roho zitarudi kwenye miili. Na Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni kwake, Ndiye Anayeyajua yaliyofichika na hisi zenu, enyi watu, mnayoyaona kwa macho yenu. Yeye Ndiye Mwenye hekima, Anayeweka mambo mahali pake, Mtambuzi wa mambo ya viumbe Vyake. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ndiye Anayehusika na mambo haya na mengineyo, mwanzo na mwisho, kuanzisha kuumba na ukomo wake. Na Yeye, Peke Yake, Ndiye Ambaye inapasa kwa waja kufuata sheria Yake, kujisalimisha kwa hukumu Yake na kuwa nahamu ya kupata radhi Zake na msamaha Wake

    [74] Na kumbuka, ewe Mtume, mahujiano ya Ibrāhīm, amani imshukiye, na baba yake Āzar. Ibrāhīm alipomwambia, «Je, unawafanya masanamu ni waungu, unawaabudu badala ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka? Mimi nakuona wewe na watu wako muko kwenye upotevu uliyo wazi, muko kando na njia ya haki

    [75] Na kama tulivyomuongoza Ibrāhīm, amani imshukiye, kwenye haki katika jambo la ibada, tunamuonesha ufalme mkubwa unaokusanya mbingu na ardhi na uwezo wenye kushinda, ili awe miongoni mwa wenye kuvama katika Imani

    [76] Giza la usiku lilipomuingilia Ibrāhīm, amani imshukiye, na kumfinika, alijadiliana na watu wake ili kuwathibitishia kuwa dini yao ni ya urongo. Na wao walikuwa wakiabudu nyota. Ibrāhīm, amani imshukiye, aliona nyota, akasema, akiwavuta watu wake, ili awathibitishie tawhīd (upweke wa Mwenyezi Mungu) kihoja, «Hii ni mola wangu.» Nyota ilipozama alisema, «Mimi siwapendi waungu wanaozama.»

    [77] Ibrāhīm alipouona mwezi umechomoza alisema kuwaambia watu wake kwa njia ya kumvuta mtesi, «Huu ni mola wangu.» Ulipozama, alisema, akiwa ahitajia uongofu wa Mola wake, «Asiponiongoza Mola wangu kwenye usawa juu ya kumpwekesha Yeye nitakuwa ni miongoni mwa watu waliopotea njia ya sawa kwa kumuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka

    [78] Alipoliona jua limechomoza, alisema kuwaambia watu wake, «Hili ni mola wangu, hili ni kubwa kuliko nyota na mwezi.» Lilipozama, alisema kuwaambia watu wake, «Mimi nimejiepusha na ushirikina mulionao wa kuabudu mizimu, nyota na masanamu mnayoabudu badala ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka

    [79] «Mimi nimeelekea kwa uso wangu, katika ibada, kwa Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, Peke Yake, kwani Yeye Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi, nikiwa kando na ushirikina na nikielekea kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Na mimi sikuwa ni miongoni mwa wenye kuwashirikisha wengine pamoja na Mwenyezi Mungu.»

    [80] Watu wake walimjadili kuhusu kumpwekesha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, akasema «Mwanijadili juu ya kumpwekesha kwangu Mwenyezi Mungu kwa ibada, na hali Yeye Ameniongoza nikaujua upweke Wake? Na iwapo nyinyi mnanitisha na waungu wenu wasije wakanidhuru, basi mimi siwaogopi na hawatanidhuru isipokuwa Mola wangu Atake jambo. Mola wangu Ameenea kila kitu kwa ujuzi. Basi hamkumbuki mkajua kuwa Yeye, Peke Yake, Ndiye Mstahiki wa kuabudiwa

    [81] «Na ni vipi nitaogopa masanamu yenu na hali nyinyi hamumuogopi Mola wangu Aliyewaumba na Akayaumba masanamu yenu ambayo mnamshirikisha nayo Mwenyezi Mungu katika ibada, bila ya kuwa na hoja yoyote juu ya hilo? Basi ni lipi kati ya makundi mawili, kundi la washirikina na kundi la wenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu, lenye haki zaidi ya utulivu na usalama na kuaminika na adhabu ya Mwenyezi Mungu? Iwapo mnajua ukweli wa ninayoyasema, niambieni.»

    [82] Wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafuata sheria Yake kivitendo, na wasichanganye imani yao na ushirikina, wao ndio wenye utulivu na usalama na wao ndio walioongozwa kwenye njia ya haki

    [83] Hoja hiyo ambayo Ibrāhīm, amani imshukiye, aliwahoji nayo watu wake ndiyo hoja yetu tuliyomuongoza nayo mpaka hoja yao ikakatika. Tunamtukuza daraja tunayemtaka, miongoni mwa waja wetu, ulimwenguni na Akhera, Hakika Mola wako ni Mwenye hekima katika kuendesha mambo ya waja Wake, ni Mjuzi kuhusu wao

    [84] Na tulimneemesha Ibrāhīm, amani imshukiye, kwa kumruzuku Is’ḥāq kuwa mtoto wake na Ya‘qūb kuwa mjukuu. Na wote wawili tuliwaongoza kwenye njia ya uongofu. Pia tulimuongoza Nūḥ kwenye haki, kabla ya Ibrāhīm na Isḥāq na Ya’qūb. Na pia tuliwaongoza kwenye haki, kati ya kizazi cha Nūḥ, Dāwūd, Sulaimān, Ayyūb, Yūsuf, Mūsā na Hārūn, amani iwashukie. Na kama tulivyowajazi Manabii hawa kwa wema wao, ndivyo tunavyomjazi kila mwema

    [85] Na vilivile tulimuongoza Zakariyyā, Yaḥyā, ‘Īsā na Ilyās. Na Manabii wote hawa, amani iwashukie, ni miongoni mwa watu wema

    [86] Na tulimuongoza, vilevile, Ismā‘īl, Ilyasa‘ na Lūṭ,. Na Mitume wote hawa tuliwatukuza juu ya watu wa zama zao

    [87] Na pia tuliwaongoza kwenye haki tuliowataka kuwaongoza kati ya wazazi wa hawa, watoto wao na ndugu zao. Na tuliwateua wao wafuate Dini yetu na wafikishe ujumbe wetu kwa wale tuliowatuma kwao. Na tuliwaonesha njia sahihi, isiyopotoka, nayo ni ile ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na kumwepusha na mambo ya kumshirkisha

    [88] Uongofu huo ni taufiki ya Mwenyezi Mungu ambayo kwayo Anamuongoza Anayemtaka miongoni mwa waja Wake. Na lau hawa Manabii walimshirikisha Mwenyezi Mungu, kwa kuchukulia na kukadiria, amali zao zingalipomoka. Kwani Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Hakubali amali yoyote pamoja na ushirikina

    [89] Manabii hao tuliowaneemesha kwa uongofu na unabii, ndio wale tuliowapa Kitabu, kama vile kurasa za Ibrāhīm, Taurati ya Muūsā, Zaburi ya Dāwūd na Injili ya Īsā. Na tuliwapa ufahamu wa Vitabu hivi na tukawateua kufikisha wahyi wetu. Na iwapo makafiri wa watu wako, ewe Mtume, watazikanusha aya za hii Qur’ani, basi tumewategemezea watu wengine jambo hilo, - yaani: Muhājirūn (masahaba waliohamia Madina pamoja na Mtume) na Ans,ār (masahaba wenyeji wa Madina) na wafuasi wao mpaka Siku ya Kiyama- ambao hawatakuwa ni wenye kuzikanusha. Bali watakuwa ni wenye kuziamini, ni wenye kuzitumia

    [90] Manabii hao waliotajwa ndio ambao Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Amewaongoza kwenye dini Yake ya haki. Basi fuata uongofu wao, ewe Muhammad, na andama njia yao. Waambie washirikina, «Mimi sitaki kutoka kwenu, kwa kufikisha Uislamu, badala ya ulimwengu. Malipo yangu yako kwa Mwenyezi Mungu. Na Uislamu ni kuita watu wote kwenye njia iliyolingana sawa na ni ukumbusho kwenu na kwa kila aliyekuwa kama nyinyi, kati ya wale wanaoendelea kwenye batili; huenda nyinyi mkawaidhika nao mkanufaika

    [91] Na hawa washirikina hawakumtukuza Mwenyezi Mungu ipasavyo kumtukuza, kwani walikanusha kwamba Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Amemteremshia yoyote miongoni mwa binadamu, chochote katika wahyi wake. Waambie, ewe Mtume, «Iwapo mambo ni kama mnavyodai, ni nani aliyeteremsha kitabu alichokuja nacho Mūsā kwa watu wake, kikiwa ni mwangaza kwa watu na mwongozo kwao?» Kisha maneno yakaelekea kwa Mayahudi kwa kuwakemea kwa kusema «Mnakigawanya kitabu hiki kwenye kurasa mbalimbali, nyingine mnazionesha na nyingi katika hizo mnazificha.- Kati ya hizo walizozificha ni maelezo ya sifa za Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na unabii wake.- Pia Mwenyezi Mungu Aliwafundisha, nyinyi Waarabu, Qur’ani ambayo Aliiteremsha kwenu, ndani yake mna habari ya walio kabla yenu na walio baada yenu na yatakayokuwa baada ya kufa kwenu, habari ambazo hamkuwa mkizijuwa, nyinyi wala wazazi wenu.» Sema, «Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyeiteremsha.» Kisha waache hawa wavame na kucheza katika mazungumzo yao ya ubatili

    [92] Na hii Qur’ani ni Kitabu tulichokuteremshia, chenye manufaa makubwa, kinatoa ushahidi juu ya ukweli wa vitabu vilivyoteremshwa vilivyokuja kabla yake na juu ya kwamba vinatoka kwa Mwenyezi Mungu. Tumekiteremsha ili uwatishie nayo, watu wa Makkah na walioko pambizoni mwake kwenye majimbo yote ya ardhi, adhabu ya Mwenyezi Mungu na mateso Yake. Na wenye kuamini uhai wa Akhera, wanaamini kwamba Qur’ani ni maneno ya Mwenyezi Mungu na wanajilazimisha kusimamisha Swala kwa nyakati zake

    [93] Ni nani mbaya zaidi wa udhalimu kuliko yule aliyemzulia Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, neno la urongo, akadai kwamba Yeye Hakumtuma mjumbe yoyote miongoni mwa wanadamu, au akafanya madai ya urongo kwamba Mwenyezi Mungu Amemletea wahyi na hali hakumletea wahyi wowote, au akadai kwamba yeye ni muweza wa kuteremsha mfano wa Qur’ani Aliyoiteremsha Mwenyezi Mungu? Na lau wawaona hawa wenye kupita mpaka, nao wako kwenye vitisho vya kufa, ungaliona jambo la kufazaisha, huku Malaika wakizitwaa roho zao, wameikunjua mikono yao kwa adhabu, wanawaambia, «Zitoeni nafsi zenu. Leo mtadhalilishwa upeo wa kudhalilishwa, kama mlivyokuwa mkisema urongo juu ya Mwenyezi Mungu na mkiona kiburi kufuata aya Zake na kuandama Mitume Wake.»

    [94] Hakika mumetujia ili muhesabiwe na mulipwe mkiwa peke yenu, kama tulivyowafanya mpatikane ulimwenguni mara ya kwanza mkiwa miguu mitupu, hamuna nguo, mumeviacha nyuma yenu vitu ambavyo tuliwamakinisha navyo miongoni mwa mali ya ulimwenguni mliokuwa mkijigamba nayo. Na hatuwaoni masanamu wako na nyinyi Akhera ambao mlikuwa mkiitakidi kuwa watawaombea na mkidai kuwa ni washirika pamoja na Mwenyezi Mungu katika ibada. Mashikamano yaliyokuwa kati yenu ulimenguni yameondoka, na yamewaondokea yale mliokuwa mkiyadai kwamba waungu wenu ni washirika wa Mwenyezi Mungu katika ibada, na imefunuka wazi kwamba nyinyi ndio mliopata hasara ya nafsi zenu, watu wenu na mali yenu

    [95] Hakika Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anapasua mbegu ukatoka mmea, na Anapasua koko ukatoka mti. Anatoa chenye uhai kutokana na kilichokufa, kama vile binadamu na mnyama kutokana na tone la manii ya binadamu na mnyama. Na Anatoa kilichokufa kutokana na chenye uhai, kama tone la manii linalotokana na binadamu na mnyama. Huyo Ndiye Mwenyezi Mungu. Yaani Mwenye kufanya hili ni Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Asiye na mshirika, Anayestahiki kuabudiwa. Basi vipi nyinyi mtaepushwa na haki mpelekwe kwenye batili mkamuabudu pamoja na Yeye mwingine asiyekuwa Yeye

    [96] Na Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Ndiye Ambaye Alipasua mwangaza wa asubuhi kutoka kwenye giza la usiku, na Akaufanya usiku ni wakati wa utulivu, anatulia humo anayechoka mchana na kupata fungu lake la mapumziko, na Akalifanya jua na mwezi zinatembea katika njia zake kwa hesabu ya sawsawa iliyokadiriwa, haibadiliki wala haigongani. Hayo ndiyo makadirio ya Al- ’Azīz, Mwenye kushinda, ambaye ufalme Wake umeshinda, Al- ’Alīm, Aliye Mjuzi wa maslahi ya viumbe Wake na kuendesha mambo yao. Al- ’Azīz na Al- ’Alīm ni miongoni mwa majina ya Mwenyezi Mungu mazuri yanayoonesha ukamilifu wa ushindi na ujuzi

    [97] Na Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Aliyewawekea, enyi watu, nyota ni alama ya nyinyi kujua njia kipindi cha usiku mnapopotea kwa sababu ya giza lingi, barani na baharini. Tumezifafanua hoja zilizo wazi, ili wazizingatie miongoni mwenu wenye elimu ya kumjua Mwenyezi Mungu na sheria Yake

    [98] Na Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Aliyeanza kuwaumba, enyi watu, kutokana na Ādam, amani imshukiye, Alipomuumba kwa udongo, kisha mkawa nyinyi ni kizazi chenye kuendelea kutokana na yeye, Akawafanyia kituo cha nyinyi kutulia, nacho ni zao za wanawake; na Akawafanyia hazina ya nyinyi kuhifadhiwa , nayo ni migongo ya wanaume. Tumeshawabainishia hoja na kuwapambanulia dalili na kuzithibitisha kwa watu wenye kufahamu vituo vya hoja na sehemu za mazingatio

    [99] Na Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za pungufu ni Kwake, Nadiye Aliyetaramsha mvua kutoka kwenye mawingu, Akatoa kwayo mimea ya kila kitu, Akatoa, kutokana na mimea, nafaka na miti mibichi, kisha akatoa kwenye mimea ya nafaka mbegu zilizoshikana, kama masuke ya mahindi, ngano na mpunga. Na Akatoa kutoka kwenye kizao cha mtende, nacho ni kile ambacho karara la tende linachomoza hapo, mitungo ambayo kuitunda ni karibu. Na Akatoa, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, mashamba ya mizabibu. Na Akatoa mizaituni na mikomamanga ambayo majani yake yanafanana na matunda yake yanatafautiana kimaumbile, uatamu na kitabia. Angalieni, enyi watu, matunda ya mimea hii inapotoa mazao na kuiva kwake na kustawi kwake yanapostawi. Hakika katika hayo, enyi watu, kuna dalili ya ukamilifu wa uwezo wa muumba vitu hivi, hekima Yake na rehema Yake kwa watu wenye kumuamini Yeye, Aliyetukuka, na kuzifuata sheria Yake kivitendo

    [100] Na hawa washirikina wamefanya majini ni washirika wa Mwenyezi Mungu katika ibada, kwa kuitakidi kwao kuwa wao wanalete manufaa au madhara, na hali Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Amewaumba wao na wanavyoviabudu kutoka kwenye ‘adam ( hali ya kutokuwako). Basi ni Yeye Aliyepwkeka kwa kuumba, Peke Yake, na inapasa Apwekeke kwa kuabudiwa Peke Yake, Asiye na mshirika. Na, kwa kweli, hawa washirikina walisema urongo kumzulia Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, walipomnasibishia Yeye watoto wa kiume na wakike, kwa kutojua kwao sifa Zake za ukamilifu zinazompasa. Ameepuka na kuwa juu ya yale, ambayo walimnasibisha nayo washirikina, ya urongo na uzushi

    [101] Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ndiye Aliyezipatisha mbingu na ardhi na vilivyomo humo, kwa namna isiyokuwa na mfano uliotangulia. Vipi Awe na mtoto, na hakuwa na mke? Ametukuka Mwenyezi Mungu kutukuka kukubwa na yale wanayoyasema washirikina, Na Yeye Ndiye Aliyeumba kila kitu kutokana na hali ya kutokuwako na hakuna chochote chenye kufichika Kwake katika mambo ya viumbe

    [102] Huyo, enyi washirikina, Ndiye Mola wenu, Aliyeshinda na kutukuka; hapana Mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye; Mwenye kuumba kila kitu. Basi mwandameni na mumnyenyekee kwa kumtii na kumuabudu. Na Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, ni Mtegemewa na ni Mtunzi, Anayaendesha mambo ya viumbe vyake

    [103] Macho hayamuoni Mwenyezi Mungu ulimwenguni. Ama kwenye nyumba ya Akhera, Waumini watamuona Mola wao bila kumuenea. Na Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, anayafikia macho na kuyazunguka, na kuyajua vile yalivyo. Na Yeye ni Al-Latīf (Mpole) kwa mawalii Wake, Anayejua mambo yenye upeo wa udogo, Al-Khabīr (Mtambuzi) Anayejua mambo ya ndani

    [104] Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Mumejiwa na hoja zilizo wazi kutoka kwa Mola wenu, mnaonea nazo uongofu na upotevu, miongoni mwa zile zilizokusanywa na Qur’ani na akaja nazo Mtume, rehema na amani zimshukiye. Basi mwenye kufunukiwa na hoja hizi na akayaamini yale yanayolekezwa nazo, faida yake itamfikia mwenyewe. Na yule ambaye hakuuona uongofu baada ya hoja kumfunukia , basi amejikosea mwenyewe. Na mimi si mtunzi wa kudhibiti matendo yenu. Mimi ni mfikishaji tu. Na Mwenyezi Mungu Anamuongoza Anayemtaka na Anampoteza Anayemtaka kulingana na ujuzi Wake na hekima Yake.»

    [105] Na kama tulivyowafafanulia washirikina, katika hii Qur’ani, hoja zilizo wazi juu ya jambo la kumpwekesha Mwenyezi Mungu, utume na marejeo ya Kiyama, tunawafafanulia hoja katika kila wasichokijua. Na hapo wanasema urongo, «Umejifunza kutoka kwa watu wa Kitabu!» Na ili tufafanue haki, kwa kuzileta aya, kwa watu wanaoijua na kuikubali na kuifuata, nao ni waliomuamini Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kile alichoteremshiwa

    [106] Fuata, ewe Mtume, wahyi tuliokuteremshia, wenye maamrisho na makatazo ambayo, kubwa lake ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, na kuita watu huko. Na usijali ushindani wa washirikina na madai yao ya urongo

    [107] Na lau Mwenyezi Mungu Alitaka wasishirikishe hawa washirikina hawangalishirikisha, lakini Yeye, Aliyetukuka, ni Mjuzi wa yatakayokuwa ya ubaya wa uchaguzi wao na kufuata kwao matamanio yaliyopotoka. Na hatukukufanya wewe ni mchunguzi wa kuwatunzia matendo yao wala hukuwa ni msimamizi wao wa kuwapangia maslahi yao

    [108] Na msiyatukane, enyi Waislamu, masanamu ambyo washirikina wanayaabudu, kwa ajili ya kuziba kipengele, ili hilo lisije likawafanya wao wamtukane Mwenyezi Mungu kwa ujinga na kwa uadui, bila ya kuwa na ujuzi. Na kama tulivyowapambia hawa matendo yao mabaya, yakiwa ni mateso kwao kwa uchaguzi wao mbaya, ndivyo tulivyowapambia kila umma matendo yao. Kisha marejeo yao wote ni kwa Mola wao; hapo Mwenyezi Mungu Awaambie matendo yao waliokuwa wakiyatenda ulimwenguni kisha Awalipe kwayo

    [109] Na waliapa washirikina hawa viyapo vya mkazo, «Lau Atatujia Muhammad kwa alama yenye miujiza, tutayaamini yale aliyoyaleta.» Sema, ewe Mtume, «Kuja kwa miujiza yenye kushinda kunatokana na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka. Yeye Ndiye Mwenye uwezo wa kuileta Akitaka.» Na nilipi liwajulishalo nyinyi, enyi Waumini: huenda miujiza hii ikija hawataiamini hawa washirikina?.»

    [110] Na tutazigeuza nyoyo zao na macho yao, tuweke kizuizi baina yake na kunufaika na alama za Mwenyezi mungu, wasiziamini kama walivyokuwa hawakuziamini aya za Qur’ani zilipoteremka kwa mara ya kwanza, na tutawaacha wao wameduwaa katika kumuasi kwao Mwenyezi Mungu, hawaongoki kwenye haki na usawa

    [111] Na lau kama sisi tungaliyaitikia maombi ya washirikina hawa na kuwateremshia Malaika kutoka mbinguni na tukawafufulia wafu wakazungumza nao na tukawakusanyia kila kitu walichokitaka wakakiona ana kwa ana, hawangaliyakubali yale uliyowaitia, ewe Mtume, na hawangaliyatumia, isipokuwa yule ambaye Mwenyezi Mungu Alimtakia uongofu. Lakini wengi wa hawa makafiri hawaijui haki ambayo umekuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu

    [112] Na kama tulivyokujaribu wewe, ewe Mtume, kwa maadui zako miongoni mwa washirikina, tuliwajaribu Manabii wote, amani iwashukie, kwa maadui miongoni mwa waasi wa watu wao na maadui miongoni mwa waasi wa majini, wanapelekeana wenyewe kwa wenyewe maneno waliyoyapamba kwa uharibifu, ili adanganyike mwenye kuyasikia na apate kupotea njia ya Mwenyezi Mungu. Na lau Mola wako, Aliyetukuka na kuwa juu, Alitaka, angaliweka kizuizi kati yao na ule uadui, lakini huo ni mtihani kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Basi waache na kile wanachokibuni cha urongo na uzushi

    [113] Na ili zielekee huko nyoyo za makafiri ambao hawaamini maisha ya Akhera wala hawayafanyii matendo ya kuwafaa, na ili nafsi zao zipate kuyapenda, na ili wapate kuyafanya maovu ambayo wao ni wenye kuyafanya. Katika haya, pana onyo kubwa kwao

    [114] Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Kwani kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, Aliye Mola wangu na Mola wenu, natafuta uamuzi kati yangu na nyinyi, na hali Yeye, kutakasika na sifa pungufu ni Kwake, Amewateremshia Qur’ani ambayo ndani yake pana ufafanuzi wa uamuzi wa yale ambayo mlikuwa mkiteta juu yake kuhusu mambo yangu na mambo yenu?» Na Wana wa Isrāīl waliopewa na Mwenyezi Mungu Taurati na Injili wana ujuzi wa yakini kwamba hii Qur’ani imeteremshwa kwako, ewe Mtume, kutoka kwa Mola wako kwa haki. Basi usiwe, tena usiwe, ni miongoni mwa wenye shaka juu ya chochote ambacho tumekuletea wahyi

    [115] Na limekamilika neno la Mola wako, nalo ni Qur’ani, likiwa lina ukweli wa habari na maneno, lenye uadilifu wa hukumu. Hakuna anayeweza kuyabadilisha maneno yake yaliyokamilika. Na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Ndiye Mwenye kuyasikia wanayoyasema waja Wake, Ndiye mwenye kuyajua mambo yao yaliyo waziwazi na yaliyojificha

    [116] Na lau itakadiriwa, ewe Mtume, kwamba wewe uliwasikiliza wengi kati ya watu wanaokaa ardhini, kwa kweli wanagalikupoteza ukawa kando na dini ya Mwenyezi Mungu. Kwani wao hawaendi isipokuwa kwenye yale wanayoyaona kuwa ni haki kwa kuwaiga wakale wao. Na hawakuwa wao isipokuwa tu wanadhania na wanasema urongo

    [117] Na kwa hakika, Mola wako Ndiye Anayewajua zaidi wenye kupotea njia ya uongofu; na Yeye Anawajuwa zaidi, kuliko nyinyi, wale walio kwenye njia ya uongofu na usawa; hafichiki Kwake yoyote katika wao

    [118] Basi kuleni, kati ya wanyama waliochinjwa, wale ambao jina la Mwenyezi Mungu lilitajwa wakati wa kuchinjwa, iwapo nyinyi mnaziamini hoja za Mwenyezi Mungu, aliyetukuka, zilizo wazi

    [119] Na kitu gani kinachowazuia, enyi Waislamu, kumla mnyama ambaye jina la Mwenyezi Mungu lilitajwa wakati wa kuchinjwa, ambapo Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Amewaelezea nyinyi yote aliyoyaharamisha kwenu? Lakini yale ya haramu ambayo dharura imepelekea yatumiwe, kwa sababu ya njaa, kama mfu, basi mumehalalishiwa. Na wengi, kati ya wapotofu, wanawapoteza wafuasi wao na kuwaepusha na njia ya Mwenyezi Mungu katika kuhalalisha haramu na kuharamisha halali kwa matakwa yao kwa ujinga walionao. Kwa hakika, Mola wako, ewe Mtume, Ndiye Amjuwaye zaidi yule aliyekiuka mipaka Yake katika hayo; na Yeye Ndiye Atakayesimamia hesabu yake na malipo yake

    [120] Na acheni, enyi watu, maasia yote, yaliyo waziwazi na yaliyo ya siri. Hakika wale wanaofanya maasia, Mola wao Atawatesa kwa sababu ya yale maovu ambyo walikuwa wakiyafanya

    [121] Na wala msile, enyi Waislamu, katika vichinjwa, yule ambaye halikutajwa jina la Mwenyezi Mungu wakati wa kuchinjwa, kama mfu na aliochinjiwa masanamu na majini na wasiokuwa hao. Na kwa hakika kuwala wanyama hao ni kutoka kwenye twaa ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka. Na majini waasi wanawatia marafiki zao, miongoni mwa mashetani wa kibinadamu, ushawiwishi wa kuwatatiza kuhusu uharamu wa kula mfu; wanawaamrisha wawaambie Waislamu wanapobishana nao, «Hakika nyinyi, kwa kutokula kwenu mfu, huwa hamli anachokiua Mwenyezi Mungu, ambapo mnakula mnachokichinja.» Na iwapo mtawasikiliza, enyi Waislamu, katika kuhalalisha mfu, basi nyinyi mtakuwa sawa na wao katika ushirikina

    [122] Je, yule ambaye amekufa katika upotofu, ameangamia na ameshangaa, tukaufufua moyo wake kwa Imani, tukamuongoza kwenye Imani na tukamuafikia kuwafuata Mitume Wake, akawa anaishi kwenye miangaza ya uongofu, atakuwa ni kama mfano wa yule aliye ndani ya ujinga, matamanio ya moyo na namna mbalimbali za upotevu, asiyeongokewa kwenye sehemu yoyote ya kupenya na hana wa kumuokoa na yale ambayo yumo ndani yake? Hao wawili hawalingani. Na kama nilivyomuachilia kafiri huyu anayebishana na nyinyi, enyi Waumini, nikampambia vitendo vyake viovu akaviona ni vyema, vilevile nimewapambia wenye kukanusha vitendo vyao viovu ili wapaswe, kwa hilo, kupata adhabu

    [123] Na mfano huu uliopatikana kwa viongozi wa makafiri huko Maka wa kuzuia dini ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, tumeweka katika kila mji watu waovu wanaongozwa na wakubwa wao, ili wapate kufanya vitimbi humo kwa kuzuia dini ya Mwenyezi Mungu; na wao hawazifanyii vitimbi isipokuwa nafsi zao, na wala hawalihisi hilo

    [124] Na pindi inapowajia washirikina hawa, miongoni mwa watu wa Maka, hoja iliyo waziwazi juu ya unabii wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wanasema baadhi ya wakubwa wao, «Kamwe hatutaukubali unabii wake mpaka Mwenyezi Mungu Atupe unabii na miujiza mfano wa Aliyowapa wajumbe wake waliotangulia» Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Aliwajibu kwa neno lake,: “Mwenyezi Mungu Anajua zaidi wapi Auweke ujumbe Wake.» Kwa maana kuwa Anawajua wale wanaofaa kubeba ujumbe Wake na kuufikisha kwa Watu. Utawapata unyonge wakiukaji mipaka hawa, na watakuwa na adhabu iumizayo ndani ya Moto wa Jahanamu kwa sababu ya vitimbi vyao kwa Uislamu na watu wake

    [125] Basi yule ambaye Mwenyezi Mungu Anataka kumuafukia aikubali haki, Anakikunjua kifua chake kukubali Imani na upweke wa Mwenyezi Mungu; na yule ambaye Anataka kumpoteza , Anakifanya kifua chake kiwe katika hali ya dhiki kubwa na kukunjika katika kuukubali uongofu, kama hali ya anayepaa kwenye tabaka za anga za juu, hapo akapatwa na uzito mkubwa wa kuvuta pumzi. Na kama anavyovifanya Mwenyezi Mungu vifua vya makafiri vibanike sana na kukunjika, hivyo basi ndivyo Atakavyowapatia adhabu wale wasiomuamini

    [126] Na haya tuliliyokubainishia, ewe Mtume, ndio njia inayofikisha kwenye radhi za Mola Wako na Pepo Yake. Tumezifunua wazi hoja kwa yule anayekumbuka miongoni mwa wenye akili zilizokomaa

    [127] Wale wanaokumbuka watapata mbele ya Mola wao, Aliyetukuka na kuwa juu, Siku ya Kiyama Nyumba ya Salama na Amani, isiyo na makero, nayo ni Pepo. Na yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, ni Mwenye kuwanusuru na kuwalinda; hayo yakiwa ni malipo kwao kwa matendo yao mema

    [128] Na kumbuka, ewe Mtume, ile Siku Atakayowakusanya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, makafiri na wategemewa wao, miongoni mwa mashetani wa kijini, na kuwaambia, «Enyi mkusanyiko wa majini, hakika mumewapoteza binadamu wengi.» Na watasema wategemewa wao miongoni mwa makafiri wa kibinadamu, «EweMola wetu, kila mmoja katika sisi amenufaika na mwengine, na tumefikia kikomo ambacho umekiweka kwetu kwa kumalizika uhai wetu wa duniani.» Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Atasema Awaambie, «Moto ndio mashukio yenu, mtakaa milele, isipokuwa yule ambaye Mwenyezi Mungu Ametaka asikaye milele,» miongoni mwa walioasi wenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Hakika Mola wako ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji Wake na utengenezaji Wake, ni Mjuzi mno wa mambo yote ya waja Wake

    [129] Na kama tulivyowapa uwezo mashetani wa kijini juu ya makafiri wa kibinadamu wakawa ni wategemewa wao, hivyohivyo tunawapa uwezo madhalimu wa kibinadamu juu ya wenyewe kwa wenyewe duniani kwa sababu ya maasia wayafanyayo

    [130] Enyi majini na binadamu mlio washirikina, kwani hawakuwajia Mitume miongoni mwenu- Maandiko yanaonesha kuwa Mitume wanatoka kwa wanadamu tu.- wanaowapa habari za alama zangu zilizo wazi, zinazokusanya maamrisho na makatazo, zinazofafanua kheri na shari na wanaowaonya kukumbana na adhabu yangu Siku ya Kiyama? Watasema washirikina hawa, maijini na binadamu, «Tumeshuhudia juu ya nafsi zetu kwamba Mitume wako wametufikishia aya zako na wametuonya makutano ya Siku yetu hii, na sisi tukawakanusha.» Na hawa washirikina, liliwadanganya wao pambo la maisha ya dunia. Na walizishuhudilia nafsi zao kwamba wao walikuwa wakiukataa upweke wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na wakiwafanya warongo Mitume Wake, amani iwashukie

    [131] Ili asiadhibiwe yoyote kwa kujidhulumu nafsi yake kwa kufanya maovu na hali ulinganizi wa Uislamu haujamfikia, sisi tulituma Mitume na tukateremsha Vitabu kwa kuwaondolea majini na binadamu hoja watakayoichukua kama kisingizio. Hivyo ndivyo tulivyowaondolea hoja umma waliyopita, hatukumuadhibu yoyote isipokuwa baada ya kuwapelekea Mitume

    [132] Na kila mwenye kufanya vitendo vya kumtii Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, vya kumuasi ana daraja kutokana na vitendo vyake, Mwenyezi Mungu Atamfikishia viwango hivyo na Atamlipa kwavyo. Na Mola wako, ewe Mtume, Hakuwa ni Mwenye kughafilika na wanayoyafanya waja Wake

    [133] Na Mola wako, ewe Mtume, Aliyewaamrisha watu kumuabudu, Ndiye Mkwasi Peke Yake, na viumbe wote wanamhitajia Yeye. Na Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Mwenye rehema kunjufu. Na lau Alitaka Angaliwaangamiza na Akawaleta watu wengine wasiokuwa nyinyi watakaokuwa badala yenu baada ya kumalizika kwenu na watende matendo ya kumtii Yeye, Aliyetukuka, kama Alivyowaleta nyinyi kutokamana na kizazi cha watu wengine waliokuwako kabla yenu

    [134] Hakika yale mateso ambayo Anawaahidi nayo Mola wenu, enyi washirikina, kwa ukafiri wenu, ni yenye kuwapata. Na hamutamlemea Mola wenu kwa kumkimbia. Kwani Yeye ana uwezo wa kuwarudisha, hata kama mtakuwa mumegeuka mumekuwa mchanga na mifupa

    [135] Sema, ewe Mtume, «Enyi watu wangu, fanyeni kwa njia yenu, na mimi nitafanya kwa njia yangu ambayo Mola wangu, Aliyetukuka na kuwa juu, Aliniwekea. Mtakuja kujua, pindi mateso yatakapowashukia, ni nani atakayekuwa na mwisho mwema?» Hakika hatafaulu kupata radhi za Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na Pepo yule aliyekiuka mpaka Wake na akadhulumu, na akamshirikisha pamoja na Mwenyezi Mungu asiyekuwa Yeye

    [136] Na wale wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, waliziweka kando sehemu ya vitu Alivyoviumba miongoni mwa mazao, matunda na wanyama howa wakawapatia wageni na maskini; na wakaziweka kando sehemu nyingine za vitu hivi kwa washirika wao, miongoni mwa masanamu na mizimu. Basi zile zilizotengewa washirika wao zafikishwa kwao peke yao, na hazifiki kwa Mwenyezi Mungu; na zile zilizotengewa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, zinafika kwa washirika wao. Ni mbaya ulioje uaumuzi wa hao watu na kigawanyo chao

    [137] Na kama ambavyo mashetani waliwapambia washirikina wamtengee Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, katika mazao na wanyama howa, fungu maalumu na fungu kwa washirika wao, vilevile mashetani wamewapambia wengi kati ya washirikina kuwaua watoto wao kwa kuchelea ufukara, ili wawaingize wazazi hawa kwenye maangamivu kwa kuziua nafsi ambazo Mwenyezi Mungu Ameharamisha kuuliwa isipokuwa kwa haki, na ili wawavurugie dini yao iwachanganyikie wapate kupotea na waangamie. Na lau Angalitaka Mwenyezi Mungu wasiifanye hilo hawangalilifanya, lakini Yeye Amelikadiria liwe kwa kujua Kwake uovu wa hali yao na marejeo yao. Basi waache, ewe Mtume, na mambo yao, katika yale ya urongo wanayoyazua , na Mwenyezi Mungu Atahukumu baina yako na wao

    [138] Na walisema washirikina kwamba ngamia hawa na makulima haya ni vitu haramu; haifai kuvila kwa mtu yoyote isipokuwa yule wanayemruhusu, kulingana na madai yao, miongoni mwa wasimamizi wa mizimu na wengineo. Na hawa ni ngamia ambao ilipewa heshima migongo yao, haifai kupandwa wala kubebeshwa vitu juu yake kwa namana yoyote. Na hawa ni ngamia ambao hawawatajii jina la Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, katika jambo lolote linalowahusu wao.Waliyafanya hayo kwa urongo utokao kwao, kumzulia Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu Atawalipa kwa urongo waliokuwa wakimzulia Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake

    [139] Na walisema washirikina, «Watoto waliyomo ndani ya wanyama howa, wakizaliwa wakiwa hai, ni halali tu kwa wanaume kati yetu na ni haramu kwa wanawake miongoni mwetu.» Na wakizaliwa nao wamekufa wanashirikiana katika kuwatumia. Mwenyezi Mungu Atawatesa kwa kujiwekea sheria za kuhalalisha na kuharamisha ambazo Mwenyezi Mungu hakuziruhusu. Hakika Yeye Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji Wake mambo ya viumbe Wake, Mjuzi sana kuhusu wao

    [140] Hakika wamepata hasara na wameangamia wale ambao, kwa udhaifu wa akili zao na kwa ujinga wao, waliwaua watoto wao na wakaziharamisha, kwa kumzulia Mwenyezi Mungu urongo, zile Alizowaruzuku. Wako mabali na haki na hawakuwa ni miongoni mwa watu wa uongofu na muelekeo wa sawa. Kuhalalisha na kuharamisha ni miongoni mwa mambo mahususi ya uungu katika uwekaji sheria. Halali ni Aliyoihalalisha Mwenyezi Mungu, na haramu ni Aliyoiharamisha Mwenyezi Mungu. Na haipasii kwa yoyote kati ya viumbe wake, awe mmoja au kundi, kuwaekea sheria waja Wake ambayo Mwenyezi Mungu Hakuidhinisha

    [141] Na Mwenyezi Mungu, kutkata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Ndiye Aliyewaanzishia mashamba: miongoni mwa mimea yake kuna ile iliyoinuliwa juu ya ardhi na kuegemezewa vitu vyingine, kama mizabibu, na miongoni mwayo kuna isiyoinuliwa, bali inasimama yenyewe kwenye vigogo vyake, kama mitende na miti mingine ya mazao. Mimea yote hiyo ikiwa ina tamu tafauti. Mizabibu na mikomamanga, maumbile yake yanafanana na matunda yake yanatafautiana tamu yake. Kuleni, enyi watu, matunda yake na mtoe Zaka zake zilizolazimishwa kwenu siku mnapoyavuna na kuyatungua, na msiikiuke mipaka ya usawa katika kutoa mali na kula chakula na mengineyo. Hakika Yeye, Mwenyezi Mungu, Hawapendi wenye kukiuka mipaka Yake kwa kutumia mali katika njia zisokuwa zake

    [142] Na Ameleta katika wanyama wale ambao wametayarishwa kwa kubebeshwa kwa kuwa ni wakubwa na ni warefu, kama ngamia. Na miongoni mwao kuna waliotayarishwa si kwa kubebeshwa kwa kuwa ni wadogo na wafupi, kama ng’ombe, mbuzi na kondoo. Kuleni wale Aliyowahalalishia nyinyi Mwenyezi Mungu miongoni mwa hawa wanyama, wala msiwaharamishe wale Aliyowahalalisha miongoni mwao kwa kufuata njia za Shetani kama walivyofanya washirikina. Hakika Shetani, kwenu nyinyi, ni adui mwenye uadui wa wazi

    [143] Wanyama hawa ambao Mwenyezi Mungu Amewaruzuku waja Wake, miongoni mwa ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo, ni aina nane: nne kati ya hizo ni mbuzi na kondoo, nao ni kondoo: waume na wake, na mbuzi: wume na wake. Sema, ewe Mtume, uwaambie hao washirikina, «Kwani Mwenyezi Mungu Amewaharamisha madume wawili wa mbuzi na kondoo?» Wakisema, «Ndio», watakuwa wamesema urongo kuhusu hilo. Sababu wao hawalifanyi kila dume la kondoo na mbuzi kuwa ni haramu. Na waambie, «Kwani Mwenyezi Mungu Amewaharamisha majike wawili wa mbuzi na kondoo?» wakisema, «Ndio», watakuwa pia wamesema urongo. Sababu wao hawamuharamishi kila mwanambuzi na mwanakondoo mke. Na sema uwaambie, «Kwani Mwenyezi Mungu Amewaharamisha watoto walio matumboni mwa majike wawili wa mbuzi na kondoo walio na mimba?» Wakisema, «Ndio.» Watakuwa wamesema urongo pia. Kwani hawaiharamishi kila mimba ya namna hiyo. Nambieni kwa misingi ya elimu inayoonesha usahihi wa msimamo wenu, mkiwa ni wakweli katika hayo mnayoyanasibisha kwa Mola wenu

    [144] Na aina nne nyingine ni aina mbili za ngamia, waume na wake, na aina mbili za ng’ombe, waume na wake. Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina hao, «Kwani Mwenyezi Mungu Amewaharamisha madume wawili au majike wawili? Au Ameharamisha vilivyomo ndani ya matumbo ya majike wawili, wawe madume au majike? Au mlikuwa, enyi washirikina, mupo pindi Mwanyezi Mungu Alipowapa wasia wa uharamu huu wa wanyama howa? Hakuna dhalimu mbaya zaidi kuliko yule aliyemzulia Mwenyezi Mungu urongo, ili awapotoshe watu, kwa ujinga wake, na njia ya uongofu. Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Hamuelekezi kwenye muelekeo wa sawa yule aliyekiuka mpaka wake, akamzulia urongo Mola wake na akawapoteza watu

    [145] Sema, ewe Mtume, mimi sipati, kati ya yale aliyoniletea wahyi Mwenyezi Mungu, kitu kilicho haramu kwa mwenye kukila, kati ya vile mnavyovitaja kwamba vimeharamishwa miongoni mwa wanyama howa, isipokuwa awe amekufa bila kuchinjwa, au ni damu itiririkayo, au iwe ni nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni najisi, au akawa ni mnyama ambaye kuchinjwa kwake kumetoka nje ya utiifu wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kama akiwa mnyama aliyechinjwa ametajiwa jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu, wakati wa kuchinjwa. Basi mwenye kulazimika kula chochote kati ya hizo zilizoharamishwa kwa dharura ya njaa kali, pasi na kutaka kujifurahisha wala kukiuka mpaka wa dharura, hakika Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ni mwenye kumsamehe, ni mwenye huruma naye. Na hakika imethibiti, baadaye, kwa mafundisho ya Mtume kuwa ni haramu kula kila mnyama mwitu anayewinda kwa kutumia meno, kila ndege anayewinda kwa kutumia kucha, punda na mbwa

    [146] Na watajie washirikina hawa, ewe Mtume, wanyama na ndege tuliowaharamishia Mayahudi: nao ni kila ambaye hana pasuko vidoleni mwake, kama ngamia na mbuni, na mafuta ya ng’ombe, mbuzi na kondoo isipokuwa yale mafuta yaliyoshikana na migongo ya wanyama hao na tumbo zao, au yaliyoshikana na mfupa wa mkia na mbavu na mfano wake. Uharamishaji huu uliotajwa juu ya Mayahudi ni adhabu kutoka kwetu kwa sababu ya matendo yao maovu. Na sisi ni wakweli kwa yale tuliyoyaeleza kuhusu wao

    [147] Na wakikufanya mrongo, ewe Mtume, wanaokwenda kinyume na wewe miongoni mwa washirikina, Mayahudi na wengineo, waambie, «Mola wenu, Aliyetukuka na kuwa juu, ni Mwenye rehema kunjufu. Na wala haiyepushwi adhabu Yake kwa watu walitenda maovu wakapata madhambi na wakajitokeza wazi na ubaya. Katika haya pana onyo kwao, kwa kwenda kwao kinyume na Mtume , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [148] Watasema wale walioshirikisha, «Lau Mwenyezi Mungu Alitaka tusishirikishe, sisi na baba zetu, na tusihararamishe kitu chochote kinyume na matakwa Yake, hatungalifanya hilo.» Hapo Mwenyezi Mungu Aliwarudi kwa kuwaeleza kwamba utata huu ulivumishwa na makafiri kabla yao, wakautumia kuukanusha ulinganizi wa Mitume wao na wakaendelea kufanya hivyo mpaka ikawateremkia adhabu ya Mwenyezi Mungu. Waambie, ewe Mtume, «Je, mnayo elimu sahihi mtuoneshe, juu ya wanyama howa na makulima mliyoharamisha na juu ya madai yenu kwamba Mwenyezi Mungu Aliwatakia ukafiri, Akauridhia kwenu na Akaupendelea kwenu? Hamuna mnachofuata, katika mambo ya dini, isipokuwa dhana tu; na hamukuwa nyinyi isipokuwa mnasema urongo.»

    [149] Sema, ewe Mtume, kuwaambia wao, «Mwenyezi Mungu, Alietukuka na kuwa juu, Ndiye Mwenye hoja ya mkato, yenye kuzikata dhana zenu. Na lau Alitaka Angaliwaongoza nyote kwenye muelekeo wa sawa.»

    [150] Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Waleteni mashahidi wenu ambao watatoa ushahidi kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyeharamisha vile mlivyoviharamisha vya makulima na wanyama howa.» Wakitoa ushahidi huo, kwa urongo na uzushi, usiwaamini wala usikubaliane na wale waliojitolea uamuzi wenyewe kulingana na mapendeleo ya nafsi zao, wakazikanusha aya za Mwenyezi Mungu katika yale waliyoyashikilia ya kukiharamisha Alichokihalalisha Mwenyezi Mungu na kukihalalisha Alichokiharamisha Mwenyezi Mungu. Wala usiwafuate wale ambao hawayaamini maisha ya Akhera wala wasiotenda vitendo vya kuwafaa huko na wale ambao Mola wao wanamshirikisha wakawa wanamuabudu mwingine pamoja na Yeye

    [151] Waambie, ewe Mtume, «Njooni niwasomee Yale Aliyoyaharamishia Mwenyezi Mungu: Msishirikishe pamoja na Mwenyezi Mungu kitu chochote, miongoni mwa viumbe Vyake katika kumuabudu Yeye; bali zielekezeni aina zote za ibada Kwake Yeye Peke Yake, kama kucha, kutaraji, kuomba na megineyo. Muwafanyie wema wazazi wawili kwa kuwasaidia, kuwaombea Mungu na mengineyo ya wema kama hayo Msiwaue watoto wenu kwa sababu ya ufukara uliowshukia, kwani Mwenyezi Mungu Anawaruzuku nyinyi na wao. Wala msiyasongelee madhambi makubwa yaliyo wazi na yaliyofichika. Na msiiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu Ameharamisha kuuawa, isipokuwa kwa njia ya haki, nayo ni kuchukuliwa kisasi kwa aliyeua, au kwa uzinifu baada ya kuoa au kuolewa, au kuacha Uislamu. Hayo yaliyotajwa ni miongoni mwa yale ambayo Mwenyezi Mungu Amewkataza nayo na Akawapa maagizo muyaepuke na ni miongoni mwa yale Aliyowaamrisha nyinyi kwayo. Amweausia nayo Mola wenu ili mupate kuyaitia akilini maamrisho Yake na Makatazo Yake

    [152] «Wala msiyasogelee, enyi wasimamizi, mali ya yatima isipokuwa kwa namana ya kuyatengeneza na kuyafanya yenye faida, mpaka atakapofikia myaka ya kubaleghe na awe mwangalifu. Na pindi afikiapo umri huo, mpeni mali yake. Na tekelezeni vipimo na mizani kwa usawa kwa namna ambayo utekelezaji utakuwa umefanyika kwa ukamilifu. Na mtakapojibidiisha uwezo wenu, hapana ubaya kwenu katika yale ambayo huenda yakawa na upungufu upande wenu. Kwani hatumlazimishi mtu isipokuwa uwezo wake. Na msemapo, basi jitahidini katika maneno yenu kuchunga usawa pasi na kupotoka kwenye haki kwenye utoaji habari au ushahidi au hukumu au kwenye uombezi, hata kama yule ambaye neno hilo linamuhusu yeye ana ujamaa na nyinyi, msilemee upande wake bila ya haki. Na tekelezeni yale aliyowaagiza mufanye ya kujilazimisha na sheria Yake. Hukumu hizo mlizosomewa, Mola wenu Amewausia mzifuate kwa matarajio kwmba mkumbuke mwisho wa mambo yenu

    [153] «Na miongoni mwa mambo aliyowausia Mwenyezi Mungu ni kwamba huu Uislamu ndio njia ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, iliyolingana sawa. Basi ifuateni wala msifuate njia za upotevu zikawatawanya na kuwaepusha na njia ya Mwenyezi Mungu iliyolingana sawa. Muelekeo huo upande wa njia nyofu, ndio Aliowausia nao Mwenyzi Mungu ili mjikinge na adhabu Yake kwa kuyatekeleza maamrisho Yake na kijitenga na makatazo Yake.»

    [154] Kisha sema, ewe Mtume, uwaambie hawa washirikina, «Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ndiye Aliyempa Mūsā Taurati, kwa kuzitimiza neema Zake kwa watu wa mila yake wanaofanya wema, na kwa kufafanua kila kitu katika mambo ya dini yao, na kuwapa uongofu na muelekeo wa njia iliyolingana sawa, na kuwarehemu, kwa matumaini kuwa watakubali kwamba kuna kufufuliwa baada ya kufa na kuna hesabu na malipo, na hilo liwafanya watende mema

    [155] Na hii Qur’ani ni kitabu tulichokiteremsha kwa Nabii wetu Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie. Kheri yeke ni nyingi. Basi kifuateni kwa yale anayowaamrisha na kuwakataza. Na muogopeni Mwenyezi Mungu msije mkaenda kinyume na amri Yake yoyote, kwa matumaini kuwa mtarehemewa na mtaokolewa na adhabu Yake na mpate malipo Yake mema

    [156] Na tumeiteremsha hii Qur’ani, ili msije mkasema, enyi makafiri wa Kiaarabu, «Hakika Kitabu kutoka mbinguni waliteremshiwa Mayahudi na Wanaswara; na sisi tuna mambo ya kutushughulisha kutowahi kuvisoma vitabu vyao; na sisi hatuna ujuzi navyo wala maarifa.»

    [157] Na ili msije mkasema, enyi washirikina, «Lau kama sisi tuliteremshiwa kitabu kutoka mbinguni, kama walivyoteremshiwa Mayahudi na Wanaswara, tungalikuwa na muelekeo madhubuti sana kwenye njia ya haki kuliko wao.» Hakika kimewajia Kitabu kwa lugha ya Kiarabu chenye ufafanuzi. Na hiyo ni hoja iliyo wazi kutoka kwa Mola wenu, ni muongozo wa njia ya haki na ni rehema kwa umma huu. Na hapana yoyote mbaya wa dhuluma na uadui kuliko yule aliyezikanusha hoja za Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na akazipa mgongo. Basi hawa wenye kupa mgongo tutawatesa mateso makubwa kwenye Moto wa Jahanamu, kwa sababu ya kuzipa mgongo kwao aya zetu na kuzuia kwao njia zetu

    [158] Kwani wanangojea, hawa wenye kukataa na wakazuia watu wasiifuate njia ya Mwenyezi Mungu, isipokuwa awajie wao Malaika wa mauti na wasaidizi wake kuzichukua roho zao au aje Mola wako, ewe Mtume, kutoa uamuzi kati ya waja wake Siku ya Kiyama, au zije baadhi ya alama za Kiyama na vitambulisho vyake vinavyoashiria kuja kwake, navyo ni kuchomoza jua kutoka upande wake wa Magharibi? Basi litakapokuwa hilo hakuna nafsi yoyote itakayofaidika na Imani yake, iwapo haikuwa imeamini kabla ya hapo, wala hayatakubaliwa matendo mema mapya ya hiyo nafsi, ikiwa ilikuwa imeamini, iwapo haikuwa imeyatenda kabla ya hapo. Waambie, ewe Mtume, «Ngojeeni kuja kwake, ili mpate kumjua aliye kwenye usawa na aliye kwenye makosa, na mtenda maovu na mtenda mema. Sisi tunalingojea hilo.»

    [159] Hakika wale walioigawanya dini yao, baada ya kuwa mkusanyiko mmoja juu ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kufuata sheria Yake kivitendo, wakawa ni makundi na mapote, wewe, ewe Mtume, uko mbali na wao. Hukumu yao iko kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kisha Yeye Atawapa habari za matendo yao, Amlipe aliyetubia miongoni mwao na akafanya wema, kwa wema wake na Amtese mtenda maovu kwa uovu wake

    [160] Mwenye kukutana na Mola wake, Siku ya Kiyama, akiwa na jema moja miongoni mwa matendo mazuri, atapata mema mfano wake mara kumi. Na mwenye kukutana na Mola wake akiwa ana ovu moja, hatateswa isipokuwa kadiri ya mfano wa ovu hilo, na wao hawatadhulumiwa hata kiasi cha uzito wa chungu mdogo

    [161] Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Mimi Ameniongoza Mola wangu kwenye njia iliyolingana sawa yenye kufikisha kwenye Pepo Yake, nayo ni Dini ya Uislamu yenye kusimamia mambo ya dunia na ya Akhera; nayo ni Dini ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu, Dini ya Ibrāhīm, amani imshukiye. Na Ibrāhīm, amani imshukiye, hakuwa ni miongoni mwa wenye kumshirikisha pamoja na Mwenyezi Mungu asiyekuwa Yeye.»

    [162] Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Hakika Swala yangu na nusuk yangu, yaani kuchinja kwangu ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Peke Yake; si kwa ajili ya masanamu wala wafu wala majini wala wasiokuwa hao kati ya wale, wasiokuwa Mwenyezi Mungu, mnaowachinja na kutaja majina yasiyokua jina Lake, kama mnavyofanya.. Pia uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe wote

    [163] «Asiye na mshirika katika uungu Wake wala katika uola Wake wala katika majina Yake na sifa Zake. Kumpwekesha huko Mwenyezi Mungu kulikosafishika ndiko Alikoniamrisha mimi Mola wangu, Aliyetukuka na kuwa juu. Na mimi ni wa kwanza kumfuata Mwenyezi Mungu kikamilifu katika umma huu.»

    [164] Sema, ewe Mtume, «Kwani natafuta mola mwingine asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na hali Yeye ni Muumba wa kila kitu, ni Mwenye kukimiliki na kukiendesha?» Na hafanyi Mwanadamu yoyote tendo baya isipokuwa dhambi zake zitamshukia mwenyewe, wala haitabeba, nafsi yenye dhambi, dhambi za nafsi nynigine. Kisha marejeo yenu ni kwa Mola wenu Siku ya Kiyama, awape habari ya yale mliokuwa mkitafautiana juu yake katika mambo ya dini.»

    [165] Na Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Aliyewafanya nyinyi mushike nafasi za waliowatangulia katika ardhi baada ya Mwenyezi Mungu kuwaondoa na kuwaweka nyinyi badala yao, mupate kuiamirisha baada yao kwa kumtii Mola wenu. Na amewainua daraja baadhi yenu, katika mapato na nguvu, juu ya wengine ili kuwapa mtihani katika alichowapa miongoni mwa neema Zake, apate kuwa wazi kwa watu mwenye kushukuru na asiyeshukuru. Hakika Mola wako ni Mwepesi wa adhabu kwa aliyemkanusha na kumuasi. Na Yeye ni Mwingi wa msamaha kwa aliyemuamini na akafaya matendo mema na akatubia na dhambi yenye kuangamiza, ni Mwenye huruma Kwake. Al-Ghafūr (Mwingi wa kusamehe)na Al-Raḥīm (Mwenye kurehemu) ni majina mawili matukufu katika majina ya Mwenyezi Mungu

    Miinuko

    Surah 7

    [1] «Alif, Lām, Mīm, Ṣād.» Yametangulia maneno kuhusu herufi zilizokatwa na kutengwa mwanzo wa sura ya Al-Baqarah

    [2] Hii Qur’ani ni Kitabu kitukufu, Mwenyezi Mungu Amekiteremsha kwako, ewe Mtume. Basi pasiwe na shaka katika kifua chako kwamaba imeteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na usiwe na wasiwasi katika kuifikisha kwa watu na kuwaonya nayo. Tumeiteremsha kwako ili uwatishe nayo makafiri na uwakumbushe Waumini

    [3] Yafuateni, enyi watu, hayo yaliyoteremshwa kutoka kwa Mola wenu miongoni mwa Qur’ani na Sunnah(mafundisho ya Mtume) kwa kufuata maamrisho na kuepuka makatazo Na wala msiwafuate wategemewa badala ya Mwenyezi Mungu, kama mashetani na wasomi wa Kiyahudi na watawa wa Kinaswara. Hakika nyinyi ni mara chache mnapowaidhika na kuzingatia na mkarudi kwenye haki

    [4] Na miji mingi tuliwaangamiza watu wake kwa sababu ya kwenda kinyume kwao na Mitume wetu na kuwakanusha. Hilo likawaletea utwevu wa duniani uliounganishwa na unyonge wa Akhera. Basi adhabu yetu iliwajia, wakati mwingine wakiwa wamelala usiku, na wakati mwingine wakiwa wamelala mchana. Mwenyezi Mungu Amezihusu nyakati mbili hizi kwa kuwa ni nyakati za utulivu na mapumziko. Hivyo basi, kuja kwa adhabu kwenye nyakati mbili hizi kunababaisha zaidi na adhabu yenyewe huwa ni kali zaidi

    [5] Basi hawakuwa na neno la kunena ilipoteremka adhabu isipokuwa ni kukubali kwao kwamba walifanya madhambi na walikosea na kwamaba wao wanastahili kupata adhabu iliyowashukia

    [6] Basi tutawauliza, tena tutawauliza, wale watu waliopelekewa Mitume, «Mliwajibu vipi Mitume wetu?» Na tutawauliza, tene tutawauliza, wale Mitume kuhusu kuufikisha kwao ujumbe wa Mola wao na namna walivyojibiwa na wale watu waliotumwa kwao

    [7] Tutawaelezea, tena tutawaelezea, viumbe wote yale waliyoyatenda, kutokana na ujuzi wetu wa vitendo vyao ulimwenguni katika yale tuliyowaamrisha na tuliyowakataza. Na wala hatukwa mbali na wao katika hali yoyote ile

    [8] Na kuvipima vitendo vya watu Siku ya Kiyama kutakuwa ni kwa mizani ya kikweli, kwa usawa na uhaki ambao hauna maonevu. Basi yoyote yule ambaye mizani za vitendo vyake zitakuwa nzito, kwa wingi wa mema yake, hao ndio watakaofaulu

    [9] Na yoyote yule ambaye mizani za vitendo vyake zitakuwa nyepesi, kwa wingi wa maovu yake, hao ndio waliopoteza bahati yao ya kupata radhi ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa sababu ya kukiuka kwao mipaka kwa kuzikanusha aya za Mwenyezi Mungu , Aliyetukuka, na kukosa kuzifuata

    [10] Kwa hakika tumewapa utulivu, enyi watu, katika ardhi, na tumewaekea humo vitu mtakavyovitumia katika maisha yenu miongoni mwa vyakula na vinywaji; na pamoja na hayo, shukrani zenu juu ya neema za Mola wenu ni chache

    [11] Na kwa hakika, tumwaneemesha nyinyi kwa kumuumba chanzo chenu - naye ni baba yenu Ādam- kutokana na kutokuwako kamwe, kisha tukamtia sura ya umbo lake lililo bora kuliko lile la viumbe wengi. Kisha tuliwaamuru Malaika wetu, amani iwashukie, wamsujudie kwa ajili ya kumtukuza na kumuheshimu na kuonyesha ubora wa Ādam. Nao wakamsujudia wote, isipokuwa Iblisi, ambaye alikuwa pamoja na wao, hakuwa ni miongoni mwa wenye kumsujudia Ādam kwa kumuhusudu kwa heshima hii kubwa aliyopewa

    [12] Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Akasema hali ya kumkemea Iblisi kwa kuacha kwake kumsujudia Ādam, «Ni lipi lililokuzuia usisujudu nilipokuamuru?» Iblisi akasema, «Mimi ni bora kuliko yeye, kwa kuwa mimi nimeumbwa kwa moto na yeye ameumbwa kwa udongo.» Akaona kuwa moto ni bora kuliko udongo

    [13] Mwenyezi Mungu Akasema kumwambia Iblisi, «Shuka kutoka Peponi, kwani haifai kwako kufanya ujeuri humo; toka Peponi, kwani wewe ni miongoni mwa wanyonge waliyo watwevu

    [14] Iblisi akasema kumwambia Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, alipokata tamaa na rehema Yake, «Nipe muda mpaka Siku ya watu kufufuliwa, ili nipate kumpoteza ninayeweza kumpoteza kati ya wanadamu.»

    [15] Akasema Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, «Wewe ni miongoni mwa wale niliowaandikia kucheleweshwa kipindi chao cha kufa mpaka Mvivio wa Kwanza katika Parapanda pindi viumbe wote watakapokufa.»

    [16] Iblisi akasema, Mwenyezi Mungu Amlaani, «Kwa sababu ya kuwa wewe umenipoteza, nitafanya bidii katika kuwapoteza binadamu wawe kando ya njia yako iliyolingana sawa na nitawazuia wao wasiuuandame Uislamu ambao wanasibiana na umbile lao ulilowaumbia

    [17] «Kisha nitawajia kutoka pande zote na pambizo niwazuie wasiifuate haki, niwapambie batili, niwafanye wavutike na dunia na niwatie shaka kuhusu Akhera. Na hutawapata wengi wa wanadamu ni wenye kukushukuru wewe kwa neema zako.»

    [18] Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Akasema, kumwambia Iblisi, «Toka Peponi ukiwa umechukiwa na umefukuzwa. Nitaujaza Moto wa Jahanamu kwa kukuingiza wewe humo na binadamu wote watakaokufuata

    [19] «Na ewe Ādam, keti wewe pamoja na mke wako Ḥawwā’ Peponi na kuleni matunda yaliyo humo popote mnapotaka na wala msile matunda ya mti huu (Aliwatajia mti huo), mkifanya hilo mtakuwa ni madhalumu wenye kukiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu.»

    [20] Hapo Shetani aliwashawishi Ādam na Ḥawwā’ ili awatokomeze kwenye kumuasi Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa kula matunda ya mti ule ambao Mwenyezi Mungu Aliwakataza kuula, ili mwisho wao uwe ni kufunukwa na tupu zao zilizokuwa zimesitiriwa. Na akawaambia, katika kujaribu kwake kuwafanyia vitimbi, «Hakika Mola wenu Amewakataza kula matunda ya mti huu ili msipate kuwa Malaika na ili msipate kuwa ni miongoni mwa wenye kuishi milele.»

    [21] Na Shetani Aliwaapia Ādam na Ḥawwā’ kwa Mwenyezi Mungu kwamba yeye ni miongoni mwa wale wanaowapa nasaha kwa kuwashauri kula kutoka mti ule, huku yeye ni mrongo katika hilo

    [22] Hapo yeye aliwatia wao ujasiri na akawadanganya wakala kutoka mti huo ambao Mwenyezi Mungu Aliwakataza wasiukaribie. Walipokula kutoka mti huo, ziliwafunuka tupu zao na kikaondoka kile ambacho Mwenyezi Mungu Aliwasitiri nacho kabla ya wao kufanya uhalifu huo, wakawa wanayaambatisha majani ya miti ya Peponi kwenye tupu zao. Hapo Mola wao, Aliyetukuka na kuwa juu, Aliwaita, «Kwani sikuwakataza kula kutoka mti ule na nikawaambia kwamba Shetani, kwenu nyinyi, ni adui ambaye uadui wake uko waziwazi?» Katika aya hii kuna ushahidi kwamba kukaa uchi ni kati ya mambo makubwa na kwamba hilo ni jambo lililokowa lachukiza na linaloendelea kuchukiza katika tabia, na ni ovu kwenye akili za watu

    [23] Ādam na Ḥawwā’ walisema, «Ewe Mola wetu, tumejidhulumu nafsi zetu kwa kula kutoka kwenye mti ule. Na iwapo hutatusamehe na kuturehemu, tutakuwa ni miongoni mwa waliopoteza bahati zao katiku ulimengu wao na Akhera yao.» Maneno haya ndiyo yale aliyoyapokea Ādam kutoka kwa Mola wake akayatumia katika kumuomba, ndipo Mola wake Akaikubali toba yake

    [24] Akasema, Aliyetukuka, kumwambia Ādam, Ḥawwā’ na Iblisi, «Shukeni kutoka mbinguni muende ardhini, baadhi yenu mkiwa ni maadui ya wengine. Huko mtakuwa na mahala pa nyinyi kutulia na pa kujiliwaza mpaka muda wenu ukome.»

    [25] Mwenyezi Mngu, Aliyetukuka, Akasema kumwambia Ādam, Ḥawwā’ na kizazi chao, «Huko ardhini mtaishi, yaani mtapitisha siku za uhai wenu duniani, na huko kitakuwa kifo chenu, na kutoka huko Mola wenu atawatoa na awakusanye mkiwa hai Siku ya Ufufuzi.»

    [26] Enyi wanadamu, tumewaekea vazi lenyi kusitiri tupu zenu, nalo ni vazi la lazima, na vazi la pambo na kujirembesha, nalo ni vazi la kujikamilisha na kujifurahisha. Na vazi la uchaji Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa kutekeleza maamrisho na kujiepusha na makatazo, ndilo vazi bora kwa aliyeamini. Hayo Ndiyo ambayo Mwenyezi Mungu Amewaneemesha nayo miongoni mwa alama za uola wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, upweke Wake, wema Wake na rehema Zake kwa waja Wake, ili mpate kuzikumbuka neema hizi na mumshukuru Mwenyezi Mungu juu yake

    [27] Enyi wanadamu! Asiwadanganye Shetani akawapambia maasia, kama alivyowapambia wazazi wenu, Ādam na Ḥawwā’, akawatoa Peponi kwa sababu hiyo, akawavua vazi lao ambalo Mwenyezi Mungu Aliwasitiri nalo ili tupu zao zifunuke. Shetani na kizazi chake na viumbe wa jinsi yake wanawaona nyinyi, na nyinyi hamuwaoni, basi jichungeni nao. Hakika sisi tumewafanya Mashetani ni wategemewa wa makafiri ambao hawampwekeshi Mwenyezi Mungu wala hawawaamini Mitume Wake wala hawautumii muongozo Wake

    [28] Na makafiri wanapofanya tendo ovu, wanajitetea kwa kusema kwamba hilo ni miongoni mwa yale waliyoyapokea kutoka kwa baba zao na kwamba hilo ni katika yale Aliyoyaamrisha Mwenyzi Mungu. Waambie, ewe Mtume, «Mwenyezi Mungu Hawaamrishi waja Wake vitendo vichafu na viovu. Je, mnasema, kumsingizia Mwenyezi Mungu msiyoyajua, urongo na uzushi?»

    [29] Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina hawa, «Mola wangu Ameniamrisha usawa, na Amewaamrisha nyinyi mumtakasie ibada katika kila sehemu za ibada, hasa katika misikiti, na mumuombe Yeye hali ya kumtakasia utiifu na ibada, na muamini kufufuliwa baada ya kufa. Na kama Alivyowaleta kutoka kuwa hamkuwako,Yeye ni Muweza kuwarudishia uhai mara nyingine.»

    [30] Mwenyezi Mungu Amewafanya waja wake makundi mawili: kundi moja Amelielekeza kwenye uongofu, kwenye njia iliyolingana; na kundi lingine limelazimika kupotea njia iliyolingana, kwani wao wamewafanya Mashetani ni wategemewa wao badala ya Mwenyezi Mungu, waliwasikiliza Mashetani kwa ujinga wao na kudhania kwao kuwa wao wamefuata njia ya uongofu

    [31] Enyi wanadamu! Kuweni, kila mnapotekeleza Swala, katika hali ya pambo linalokubalika kisheria la nguo zinazofinika tupu zenu na muwe katika hali ya usafi, utohara na mfano wake. Na kuleni na kunyweni katika vizuri Alivyowapa Mwenyezi Mungu, wala msikiuke mipaka ya wastani, kwani Mwenyezi Mungu Hawapendi wakiukaji wenye kupitsha kiasi katika vyakula na vinywaji na mengineyo

    [32] Sema, ewe Mtume, uwaambie hao wajinga miongoni mwa washirikina, «Ni nani aliyewaharamishia vazi zuri ambalo Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Amelifanya kuwa ni pambo kwenu? Na ni nani Aiyewaharamishia kujistarehesha kwa chakula kizuri cha halali kilichoruzukiwa na Mwenyezi Mungu?» Sema, ewe Mtume, uwaambie hawa washirikina, «Kwa hakika vile alivyoviruhusu Mwenyezi mungu, miongoni mwa mavazi na vitu vizuri miongoni mwa vyakula na vinywaji, ni haki kwa walioamini pamoja na wengineo katika maisha ya ulimwenguni, na ni haki kwa walioamini peke yao Siku ya Kiyama. Maelezo kama hayo ni mafundisho ambayo Mwenyezi Mungu Anayaelezea kwa watu wenye kuyajua mambo wanayoelezwa na kuyaelewa wanayofafanuliwa

    [33] Sema,ewe Mtume, kuwaambia washirikina hawa, «Hakika Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyeyafanya matendo maovu kuwa ni haramu, yale yaliyo waziwazi na yale yaliyofichika, na Ameyakataza maasia yote, na miongoni mwa makubwa zaidi ya maasia ni kuwafanyia watu uadui, kwani hilo liko kando na haki. Na Amewaharamishia kuabudu, pamoja na Mwenyezi Mungu, Aliyetuka, vitu vyingine kati ya vile ambavyo Hakuviteremshia ushahidi wala hoja, kwani afanyaye hayo hana kithibitisho chochote. Na Amewaharamishia kumnasibishia Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, sheria ambayo Hakuipasisha kwa kumzulia urongo,» kama madai ya kwamba Mwenyezi Mungu Ana mwana na kuharamisha baadhi ya vilivyo halali katika mavazi na chakula

    [34] Kila kikundi kilichojikusanya kumkanusha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na kuwakanusha Mitume Wake, amani iwashukie, kina wakati wa kushukiwa na mateso. Huo wakati, Aliouweka Mwenyezi Mungu wa kuwaangamiza, hawatakawia nao, japokuwa kwa muda mfupi, wala hawataungulia

    [35] Enyi wanadamu! Pindi watakapokuja kwenu Mitume wangu, miongoni mwa watu wenu, wakiwasomea aya za Kitabu changu na kuwafahamisha hoja juu ya ukweli wa yale waliyokuja nayo, basi watiini, kwani mwenye kujikinga na hasira zangu na akayatengeneza matendo yake, hao hawatakuwa na hofu na mateso ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Siku ya Kiyama wala hawatahuzunika juu yale yaliyowapita miongoni mwa hadhi za duniani

    [36] Na makafiri ambao wamezikanusha hoja za kumpwekesha Mwenyezi Mungu na wakaacha kuzifuata kwa kujiona bora, hao ni watu wa Motoni wenye kukaa milele humo, hawatatoka humo kabisa

    [37] Hakuna yoyote aliye na udhalimu zaidi kuliko yule anayemzulia Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, urongo au akazikanusha aya Zake zilizoteremshwa, hao itawafikia sehemu yao ya adhabu waliyoandikiwa katika Al-Lawh( Al-Mhfūd) (Ubao uliohifadhiwa) mpaka atakapowajia Malaika wa mauti pamoja na wasaidizi wake kuzichukua roho zao, watawaambia, «Wako wapi wale mliokuwa mnawaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, kati ya washirika, wategemewa na masanamu, waje wawaokoe na janga lililowafika?» Watasema, «Wametutoroka.» Wakati huo watakiri makosa kwamba wao duniani walikuwa ni wenye kuupinga na kuukanusha upweke wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka

    [38] Hapo Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Atasema kuwaambia washirikina hawa wazushi, «Ingieni Motoni mkiwa pamoja na makundi ya walio mfano wenu katika ukafiri, waliotangulia kabla yenu, kati ya majini na wanadamu. Kila kundi la mila mimoja likiingia Motoni litalaani watu wa kundi lingine linalofanana nalo, waliokuwa ni sababu ya kupotea kwake kwa kuwafuata. Mpaka watakapokutana ndani ya Moto wote pamoja: wa mwanzo, miongoni mwa wafuasi wa mila za kikafiri, na wa mwisho miongoni mwao; hapo watasema wa mwisho, waliokuwa ni watu wa kuandama ulimwenguni, kuwaambia viongozi wao, «Mola wetu, hawa ndio waliotupoteza wakatupotosha na haki, basi wape adhabu nyongeza ya Moto.» Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Atasema, «Kila mmoja atapata nyongeza.» Yaani, kila mmoja kati yenu na wao atapata adhabu nyongeza ya Moto, «lakini nyinyi wafuasi hamuijui ile sehemu ya adhabu na machungu ambayo kila kundi miongoni mwenu ataipata.»

    [39] Hapo watasema wale waliofuatwa miongoni mwa viongozi na wengineo kuwaambia wafuasi wao, «Sisi na nyinyi tuko sawa katika uharibifu na upotevu na katika kufanya vitendo ambavyo ndio sababu ya kupata adhabu, kwa hivyo, nyinyi hamuna ubora juu yetu.» Mwenyezi Mungu Atawaambia wao wote, «Basi ionjeni adhabu,» yaani adhabu ya Jahanamu «kwa makosa mliyoyatenda.»

    [40] Hakika wale makafiri ambao hawakuzikubali hoja zetu na aya zetu zinazojulisha upweke wetu na ambao hawakuzitumia sheria zetu kwa kiburi na majivuno, vitendo vyao maishani, na pia roho zao wakati wa kufa, havitafunguliwa milango ya mbingu. Na haiwezekani kwa makafiri hawa kuingia Peponi isipokuwa iwapo ngamia ataingia kwenye tundu ya sindano; na hilo ni muhali. Na mfano wa malipo haya tutawalipa wale ambao uovu wao umezidi na kukiuka kwao mipaka kumepindukia

    [41] Makafiri hawa ni wenye kukalishwa milele Motoni. Watapata humo kwenye Moto wa Jahanamu tandiko chini yao, na juu yao kutakuwa na mifiniko inayowafinika. Na mfano wa mateso haya mabaya Atawatesa nayo Mwenyezi Mungu wale madhalimu ambao wamekiuka mipaka Yake, wakamkanusha na wakamuasi

    [42] Na wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na wakafanya vitendo vyema kwa kiasi cha uwezo wao, kwani Mwenyezi Mungu Hamlazimishi mtu matendo isipokuwa yale ayawezayo, hao ni watu wa Peponi, wao humo ni wenye kukaa milele, hawatoki humo kabisa

    [43] Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ataziondoa chuki na mafundo ndani ya vifua vya watu wa Peponi. Na miongoni mwa kukamilika neema zao ni kwamba mito ya maji itakuwa ikipita chini yao. Na watasema watu wa Peponi pindi watakapoingia humo, «Shukrani ni za Mwenyezi Mungu Aliyetuafikia kufanya vitendo vyema ambavyo vimetupatia starehe hizi ambazo tuko nazo. Na hatukuwa tuna uwezo wa kuifuata njia iliyolingana sawa kama si Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kutuongoza kufuata njia hii na kutuwezesha kukita juu yake. Mitume wa Mola wetu wametuletea habari za ukweli za ahadi njema kwa wenye kumtii na za kuwaonya wenye kumuasi. Na wataitwa kwa kupongezwa na kukirimiwa waambiwe, «Hiyo ndiyo pepo Mwenyezi Mungu Aliyowapa ni urathi kwa rehema Zake na kwa mliyoyatanguliza ya Imani na matendo mema.»

    [44] Watu wa Peponi, baada ya kuingia humo, watawaita watu wa Motoni wawaambie, «Sisi tumeshapata kuwa ni kweli tuliyoahidiwa na Mola wetu, kupitia ndimi za Mitume Wake, kuhusu kuwalipa wanaomtii. Je, nyinyi mumeyapata mliyoahidiwa na Mola wenu, kupitia ndimi za Mitume Wake, kuwa ni kweli kuhusu kuwaadhibu wanaomuasi?» Hapo watu wa Motoni watawajibu watu wa Peponi wakiwaambia, «Ndio, kwa kweli tumeyapata yale Aliyotuahidi Mola wetu kuwa ni kweli.» Hapo Atatangaza mwenye kutangaza, akiwa kati baina ya watu wa Peponi na watu wa Motoni akisema, «Laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie watu madhalimu» ambao walikiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu na wakamkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake

    [45] Makifiri hawa ndio wale waliokuwa wakiipuuza njia ya Mwenyezi Mungu iliyolingana sawa, na wakiwazuia watu wasiifuate, na wakitaka kwamba njia ya kuifuata iwe kombo ili kusiwe na yoyote wa kuielewa; na wao, kuhusu Akhera na mambo yake, ni wenye kukanusha

    [46] Na baina ya watu wa Peponi na watu Motoni patakuwa na kizuizi kikubwa kinaitwa Al-A’rāf. Na juu ya kizuizi hiki kutakuwa na wanaume wanaowajuwa watu wa Peponi na watu wa Motoni kwa alama zao kama weupe wa nyuso za watu wa Peponi na weusi wa nyuso za watu wa Motoni. Wanaume hawa ni watu ambao vitendo vyao vizuri na viovu viko sawasawa, na wao wana matumaini ya kupata rehema ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka. Wanaume hao wa hapo Al-A’rāf watawaita watu wa Peponi kwa maamkuzi wakiwaambia, «Salamun 'alaykum»(Amani iwe juu yenu.) Watu hawa wa Al-A’rāf bado hawajaingia Peponi, na wao wana matumaini ya kuingia

    [47] Na yatakapogeuzwa macho ya watu wa Al-A’rāf upande wa watu wa Motoni watasema, «Ewe Mola wetu, usitufanye kuwa pamoja na watu madhalimu» kwa ya ushirikina wao na ukafiri wao

    [48] Na watu walioko Al-A’rāf watawaita wanaume, miongoni mwa viongozi wa makafiri waliomo motoni, wanaowajua kwa alama zao fulani zinazowatenganisha wawaambie, «Hayakuwafaa chochote mali mliokuwa mkiyakusanya ulimwenguni wala watu; pia hakikuwafaa kiburi chenu kilichowafanya nyinyi msimuamini Mwenyezi Mungu na msiikubali haki.»

    [49] Je madhaifu na mafukara hawa, kati ya watu wa Peponi, ndio wale mlioapa huko duniani kwamba Mwenyezi Mungu Hatawakusanya Siku ya Kiyama Awatie kwenye rehema na Hatawaingiza Peponi? Ingieni Peponi, enyi watu wa Al- A'rāf, hakika mumesamehewa; hamna tene kicho cha kupata adhabu ya Mwenyezi Mungu, wala hamtahuzunika juu ya hadhi za duniani zilizowapita

    [50] Watu wa Motoni wataomba msaada kwa watu wa Peponi wawamiminie maji au chakula Mwenyezi Mungu Alichowaruzuku. Na wao watawajibu kwamba Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ameviharamisha vinywaji na vyakula kwa walioukanusha upweke Wake na wakawafanya Mitume Wake kuwa ni warongo

    [51] Wale ambao Mwenyezi mungu, Aliyetukuka, Atawanyima starehe za Akhera ni wale ambao waliifanya Dini, ambayo Mwenyezi Mungu Amewaamuru kuifuata, kuwa ni pumbao, na yakawadanganya wao maisha ya ulimwenguni, wakashughulishwa na mapambo yake wasifanye matendo ya kuwafaa Akhera, hao Atawasahau Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Siku ya Kiyama, na Atawaacha ndani ya adhabu iumizayo, kama walivyoyaacha matendo ya kuwafaa kwa kukutana na Siku yao hii, na kwa kuwa wao walikuwa wakizikanusha dalili za Mwenyezi Mungu na hoja Zake pamoja na kujua kwao kuwa ni za ukweli

    [52] Hakika tumewaletea makafiri Qur’ani tuliyokuteremshia wewe, ewe Mtume, tuliyoibainisha, inayokusanya elimu kubwa, yenye kuongoza, kutoa kwenye upotevu, kupeleka kwenye njia ya usawa, hali ya kuwa ni rehema kwa watu wanaomuamini Mwenyezi Mungu na kuzitumia sheria Zake. Amewahusu wenye kuamini kwa kuwataja, bila ya wengine, ni kwamba wao ndio wenye kunufaika nayo

    [53] Kwani kuna wanachokingojea makafiri isipokuwa mateso, ambayo ndiyo kikomo cha mambo yao, waliyoahidiwa katika Qur’ani? Siku kitakapokuja kikomo cha mambo yao, cha kuhesabiwa, kulipwa na mateso Siku ya Kiyama, watasema makafiri walioiacha Qur’ani na wakaikanusha duniani, «Sasa imetubainikia kwamba Mitume wa Mola wetu wamekuja na haki na wametupa ushauri mzuri. Je, tunaweza kupata marafiki na waombezi wapate kutuombea kwa Mola wetu? Au tunaweza kupewa nafasi ya kurudi duniani mara nyingine tupate kufanya matendo ya kumfanya Mwenyezi Mungu Awe radhi na sisi? Hakika wamepata hasara nafsi zao kwa kuingia Motoni na kukaa milele humo, na vimewaondokea vile ambavyo walikuwa wakiviabudu badala ya Mwenyezi Mungu na yale ambayo walikuwa wakiyazua miongoni mwa yale ambayo Shetani alikuwa akiwaadi nayo

    [54] Hakika Mola wenu, enyi watu, ni Yule Aliyeanzisha mbingu na ardhi kutoka kwenye 'adam (hali ya kutokuwako) kwa Siku Sita, kisha Akalingana, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, juu ya 'Arsh, -yaani : Alikuwa juu- mlingano unaonasibiana na utukufu na ukubwa Wake. Yeye , kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Anauingiza usiku kwenye mchana ukaufinika mpaka mwangaza wake ukaondoka, na Anauingiza usiku kwenye mchana mpaka giza lake likaondoka. Na daima kila mojawapo, kati ya viwili hivyi, kinafuata kingine kwa kasi. Na Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Aliyeumba jua, mwezi na nyota zikiwa zinamtii Yeye, Anazipelekesha, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, vile Anavyotaka, nazo ni miongoni mwa alama kubwa za Mwenyezi Mungu. Jua utanabahi kwamba ni wake Yeye, kutakasika na sifa za upungufu na kutukuka ni Kwake, uumbaji wote, na ni Yake Yeye amri yote. Ametukuka Mwenyezi Mungu, umeendelea ukuu Wake na Ameepukana na kila upungufu, Bwana wa viumbe wote

    [55] Muombeni, enyi Waumini, Mola wenu, kwa kujidhalilisha Kwake, kwa siri na kwa dhahiri.Na maombi yawe kwa unyenyekevu na yawe mbali na kujionyesha.Hakika Mwenyezi Mungu Hawapendi wanaokiuka mipaka ya sheria Zake. Na ukiukaji mkubwa ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu, kama vile kuwaomba wafu, masanamu na wengineo mfano wao wasiokuwa Mwenyezi Mungu

    [56] Wala msilete katika ardhi aina yoyote ya uharibifu, baada ya Mwenyezi Mungu kuitengeneza kwa kutuma Mitume, amani iwashukie, na kuimarika kwa utiifu wa Mwenyezi Mungu. Na muombeni Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, mkimtakasia maombi yenu, kwa kuogopa mateso Yake na kuwa na matumaini kupata malipo Yake mazuri. Hakika rehema ya Mwenyezi Mungu iko karibu na wenye kufanya wema

    [57] Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ndiye Anayetuma upepo mzuri mororo wenye kubashiria mvua ambayo upepo huo unaisukuma kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na hapo viumbe vikangiwa na furaha kwa hiyo rehema ya Mwenyezi Mungu. Na pindi ifikapo wakati ambapo upepo umebeba mawingu yaliyobebeshwa mvua, Mwenyezi Mungu Huyapeleka kwa upepo huo ili kuihuisha nchi iliyopigwa na ukame ardhi yake na kukauka miti yake na mimea yake ya nafaka, Mwenyezi Mungu hapo Akaiteremsha, kwa mawingu hayo, mvua, Akaitoa kwayo nyasi, miti na mimea ya nafaka, na miti ikarudi kujaa sampuli ya matunda. Kama tunavyoihuisha ardhi hii kwa mvua, vilevile tutawatoa wafu kutoka makabarini mwao baada ya kutoweka kwao, ili muwaidhike na mchukulie dalili juu ya upweke wa Mwenyezi Mungu na uwezo Wake wa kufufua

    [58] Na ardhi nzuri, ikiteremkiwa na mvua, inatoa mimea kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na matakwa Yake, ikiwa mizuri na kwa njia ya wepesi. Hivyo ndivyo alivyo Muumini, zikiteremka aya za Mwenyezi Mungu kwake, hunufaika nazo na huzalisha kwake maisha mema. Ama ardhi ya chumvi iliyo mbovu; hiyo haitoi mimea isipokuwa mibovu isiyokuwa na faida, tena kwa shida, na haitoi mimea mizuri. Hivyo ndivyo alivyo kafiri, hanufaiki kwa aya za Mwenyezi Mungu. Mfano wa sampuli hiyo nzuri katika kueleza, ndiyo namna tunavyoleta hoja na dalili mbalimbali kuthibitisha haki kwa watu wanaozishukuru neema za Mwenyezi Mungu na wanaomtii

    [59] Hakika tulimtuma Nūḥ kwa watu wake, ili awalinganie kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa pungufu ni Kwake, na kumtakasia ibada, akasema, «Enyi watu wangu, muabuduni Mwenyezi Mungu, Peke Yake, na mumnyenyekee kwa kumtii, nyinyi hamna Mola anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu, mtakasieni ibada. Msipofanya na mkasalia kwenye kuabudu masanamu yenu, hakika mimi nawaogopea msishukiwe na adhabu ya Siku ambayo shida yenu itakuwa kubwa, nayo ni Siku ya Kiyama.»

    [60] Mabwana wao na wakubwa wao walisema, «Sisi tunaitakidi, ewe Nūḥ, wewe uko kwenye upotevu waziwazi uko kando ya njia sawa.»

    [61] Nūḥ Akasema, «Enyi watu wangu, mimi si mpotevu katika jambo lolote kwa njia yoyote, lakini mimi ni mjumbe kutoka Mola wa viumbe wote; Mola wangu na Mola wenu na Mola wa viumbe wote

    [62] «Nawafikishia nyinyi lile niliotumwa nalo kutoka kwa Mola wangu, na wapa ushauri kwa kuwaonya na adhabu ya Mwenyezi Mungu na kuwapa bishara njema ya malipo yake mema, na mimi nayajua, kuhusu sheria Yake, msiyoyajua

    [63] «Je imewafanya nyinyi muone ajabu kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ameteremsha kwenu yale ambayo yatawakumbusha mambo yenye kheri kwenu, kwa ulimi wa mtu miongoni mwenu, mnaoujua ukoo wake na ukweli wake, ili awaogopeshe adhabu ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na mateso Yake, na ili mujikinge na hasira Zake kwa kumuamini na kwa kutarajia kufaulu kupata rehema Zake na malipo Yake mema mengi

    [64] Basi walimkanusha Nūḥ, tukamuokoa na wale walioamini pamoja na yeye katika jahazi, na tukawazamisha makafiri waliokanusha hoja zetu zilizowazi. Wao walikuwa vipofu wa nyoyo kwa kutoiona haki

    [65] Hakika tulimtuma, kwenda kwa watu wa kabila la 'Ād, ndugu yao Hūd, walipoabudu masanamu badala ya Mwenyezi Mungu, akawaambia, «Muabuduni Mwenyezi Mungu, Peke Yake, hamna mola anayestahiki kuabudiwa isipokuwaYeye, Aliyetukuka na kuwa juu, mtakasieni ibada. Je, hamuiogopi adhabu ya Mwenyezi Mungu na hasira Zake kwenu?»

    [66] Wakasema wale viongozi waliokufuru katika watu wa Hūd, «Sisi tunajua kwamba wewe, kwa kutuita sisi kuacha kuabudu waungu wetu na kumuabudu Mwenyezi Mungu, Peke Yake, ni mpungufu wa akili, na sisi tunaamini kwamba wewe, kwa hayo usemayo, ni katika wale wanaomzuluia Mwenyezi Mungu warongo.»

    [67] Hūd akasema, «Enyi watu wangu, sina upungufu katika akili yangu, isipokuwa mimi ni mjumbe kutoka kwa Mola wa viumbe wote

    [68] «Ninawafikishia nyinyi yale ambayo Amenituma nayo Mola wangu kwenu. Na mimi kwenu, katika yale niliyowaita kwayo ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kuitumia sheria Yake, ni mshauri mwenye imani, ni muaminifu juu ya wahyi wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka

    [69] Je, imewafanya nyinyi muone ajabu kwamba Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ameteremsha kwenu yale ambayo yanawakumbusha mambo yaliyo na kheri kwenu, kwa ulimi wa mtu katika nyinyi, mnaoujua ukoo wake na ukweli wake, ili awaogopeshe adhabu ya Mwenyezi mungu? Na kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu juu yenu, Alipowafanya nyinyi mshike nafasi ya waliokuwa kabla yenu katika ardhi baada ya kuwaangamiza kaumu ya Nūḥ, na akawazidishia miili yenu nguvu na ukubwa. Basi kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu nyingi juu yenu kwa kutarajia kufanikiwa mafanikio makubwa duniani na Akhera.»

    [70] ’Ād walisema kumwambia Hūd, amani imshukie, «Je, umetuita tumuabudu Mwenyezi Mungu, Peke Yake, na tuihame ibada ya masanamu ambayo tumeirithi kutoka kwa mababa zetu? Basi tuletee adhabu ambayo unatutusha nayo iwapo wewe ni miongoni mwa wakweli katika hayo usemayo.»

    [71] Hūd alisema kuwaambia watu wake, «Mshashukiwa na adhabu na ghadhabu kutoka kwa Mola wenu, Aliyetukuka na kuwa juu, «Mwajadiliana na mimi juu ya masanamu hawa mliowaita waungu, nyinyi na mababa zenu? Mwenyezi Mungu Hakuteremsha hoja yoyote wala dalili ya kuwa waabudiwe, kwani wao wameumbwa, Hawadhuru wala hawanufaishi; mwenye kuabudiwa peke yake si mwengine ni Muumba, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake. Basi ngojeni kuteremkiwa na adhabu, kwani mimi, pamoja na nyinyi, nangojea kuteremka kwake. Huu ni upeo wa kuonya na kutisha.»

    [72] Basi adhabu ya Mwenyezi Mungu ikatukia kwa kutumwa upepo mkali juu yao. Mwenyezi Mungu akamuokoa Hūd na walioamini pamoja na yeye kwa rehema kubwa kutoka kwake, Aliyetukuka. Na Akawaangamiza makafiri wote miongoni mwa watu wake, Akawavunjavunja mpaka wa mwisho wao. Na wao hawakuwa ni Waumini kwa kuwa walikusanya baina ya kukanusha aya za Mwenyezi Mungu na kuacha kufanya vitendo vyema

    [73] Na tulimtuma, kwenda kwa watu wa kabila la Thamūd, ndugu yao Ṣāliḥ, walipoabudu masanamu badala ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka. Ṣāliḥ aliwaambia, «Enyi watu wangu, muabuduni Mwenyezi Mungu, Peke Yake, hamna mola anyestahiki kuabudiwa isipokuwa Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu, mtakasieni ibada, nimewajia na hoja juu ya ukweli wa yale ninayowaitia kwayo. Nayo ni kuwa nilimuomba Mwenyezi Mungu mbele yenu, Akawatolea kutoka kwenye jiwe hili ngamia mkubwa kama mlivyoomba, basi muacheni ale kwenye malisho yaliyoko kwenye ardhi ya Mwenyezi Mungu, na msimfanyie lolote la kumdhuru, mkifanya hivyo, mtapatwa na adhabu iumizayo

    [74] Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu, Alipowafanya nyinyi mnashika nafasi za waliokuwa kabla yenu katika ardhi, baada ya kabila la ‘Ād, Akawamakinisha nyinyi katika ardhi nzuri, mkaifanya makao, mkajenga kwenye mabonde yake majumba makubwa na mkayachonga majabali yake ili mfanye majumba mengine. Basi kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu juu yenu na msizunguke katika ardhi kwa uharibifu

    [75] Wakasema mabwana na wakubwa wa wale waliokuwa wakijiona kuwa ni wakubwa, miongoni mwa watu wa Ṣāliḥ, kuwaambia wale waliokuwa wakiwafanya wanyonge na kuwadharau, «Kwani mnajua kwamba Ṣāliḥ ametumwa kwetu na Mwenyezi Mungu?» Wale walioamini walisema, «Sisi tunayaamini yale ambayo Mwenyezi Mungu Amemtuma nayo na tunaifuata sheria aliyokuja nayo

    [76] Wakasema wale waliojiona, «Sisi ni wenye kuyakanusha hayo mliyoyaamini nyinyi na kuyafuata kuhusu unabii wa Ṣāliḥ.”

    [77] Wakamchinja ngamia kwa kutojali onyo la Ṣāliḥ, na wakaingiwa na kiburi kilichowafanya wasifuate amri ya Mola wao na wakasema, kwa njia ya shere na kwa kuona kuwa adhabu iko mbali na wao, «Ewe Ṣāliḥ, tuletee hiyo adhabu ambayo unatuonya nayo, iwapo wewe ni miongoni mwa Mitume wa Mwenyezi Mungu!»

    [78] Basi wale waliokufuru walishikwa na tetemeko kali ambalo lilizitoa nyoyo zao, wakawa wameangamia katika mji wao, wamegandama na ardhi kwa magoti yao na nyuso zao, hakuna yoyote kati yao aliyeponyoka

    [79] Ṣāliḥ, amani imshukie, alijiepusha na watu wake, walipomchinja ngamia, na maangamivu yakawa ni yenye kuwashukia, na akasema kuwaambia, «Enyi watu wangu! Nimewafikishia yale Mola wangu Aliyoniamuru niwafikishie, kuhusu maamrisho Yake na makatazo Yake, na nimewafanyia bidii kiasi nilichoweza katika kuwavutia kwenye kheri na kuwakemea shari na kuwa muaminifu, lakini nyinyi hamuwapendi waaminifu kwenu, ndipo mkayakataa maneno yao na mkamtii kila shetani aliyelaaniwa.»

    [80] Na mkumbuke, ewe Mtume, Lūṭ, amani imshukie, pindi aliposema kuwaambia watu wake, «Je, mnafanya kitendo kibaya kilichofikia upeo wa ubaya? Hakuna yoyote, miongoni mwa viumbe, aliyefanya kitendo hiko kabla yenu

    [81] Nyinyi mnawaendea wanaume kwenye sehemu zao za nyuma, hali ya kuingiwa na matamanio ya kufanya hivyo, bila kujali uovu wake, huku mkiacha kile alichowahalalishia Mwenyezi Mungu kwa wake zenu. Bali nyinyi ni watu mliopita kiasi katika kukiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu. Hakika kuwaendea wanaume badala ya wanawake ni miongoni mwa machafu ambayo yalianzishwa na kaumu ya Lūṭ, na hawakutanguliwa na yoyote katika viumbe

    [82] Hayakuwa majibu ya watu wa Lūṭ, alipowapinga kwa kitendo chao kilichofikia upeo wa ubaya, isipokuwa ni kuambiana wao kwa wao, «Mtoeni Lūṭ na wafuasi wake nchini mwenu, kwa kuwa yeye na wanaomfuata ni watu wanaojiepusha na kuwajia wanaume kwenye sehemu zao za nyuma.»

    [83] Basi Mwenyezi Mungu Akamuokoa Lūṭ, na wafuasi wake na adhabu, Alimuamuru auhame mji ule, isipokuwa mke wake, kwani yeye alikuwa ni miongoni mwa walioangamia, waliosalia ndani ya adhabu ya Mwenyezi Mungu

    [84] Na Mwenyezi Mungu Akawaadhibu makafiri wa kaumu ya Lūṭ, kwa kuwateremshia wao mvua ya mawe, Akaigeuza nchi yao Akaifanya juu ni chini na chini ni juu. Tazama ulivyokuwa mwisho wa wale waliojasiri kufanya matendo ya kumuasi Mwenyezi Mungu na wakawakanusha Mitume Wake

    [85] Hakika tulimtuma, kwa watu wa kabila linalokaa Madyan, ndugu yao Shu'ayb, amani imshukie, akasema kuwaambia, «Enyi wtu wangu, muabuduni Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Asiye na mshirika. Hamna mola anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu. Mtakasieni ibada.Hakika imewajia nyinyi hoja, kutoka kwa Mola wenu, juu ya ukweli wa yale ninayowaitia. Watekelezeeni watu haki zao kwa kutimiza vipimo na mizani. Na msiwapunguzie haki zao mkawadhulumu. Wala msifanye uharibifu katika ardhi, kwa ukafiri na kudhulumu, baada ya kuwa imetengenezwa kwa sheria za Mitume waliopita, amani iwashukie. Hayo niliyowaitia nyinyi ni bora kwenu katika ulimwengu wenu na Akhera yenu, iwapo nyinyi ni wenye kuniamini katika yale ninayowaitia, ni wenye kuzifuata sheria za Mwenyezi Mungu kivitendo

    [86] «Na wala msikae katika kila njia mkiwatisha watu kwa kuwaua wakitowapa mali yao, mkimzuia aliyemuamini Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, na akatenda mema asifuate njia iliyonyoka, na mkataka njia ya Mwenyezi Mungu iwe kombo, na mnaipotoa mkifuata matamanio yenu, na mnawafukuza watu wasiifuate. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, juu yenu ilipokuwa idadi yenu ni chache Mwenyezi Mungu akawafanya muwe wengi mkawa mna nguvu, wenye enzi. Na angalieni, ulikuwa vipi mwisho wa wale waharibifu katika ardhi na ni yapi yaliyowashukia ya maangamivu na kuvunjikiwa

    [87] Na iwapo kundi miongoni mwenu waliyakubali yale Aliyonituma nayo Mwenyezi Mungu na kundi la watu wengine wasiyakubali hayo, basi ngojeni, enyi wakanushaji wa hukumu ya Mwenyezi Mungu inayotoa uamuzi baina yetu na nyinyi, itakapowashukia adhabu Yake ambayo aliwaonya nayo. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, ni bora wa wenye kuhukumu baina ya waja Wake

    [88] Walisema watukufu na wakubwa wa watu wa Shu'ayb waliokataa, kwa kiburi, kumuamini Mwenyezi Mungu na kumfuata Mtume Wake Shu'ayb, amani imshukiye, «Tutakutoa, ewe Shu'ayb, wewe na walio pamoja na wewe kutoka kwenye miji yetu, isipokuwa ukiwa utarudi kwenye dini yetu.» Shu'ayb akasema akilipinga na kulionea ajabu neno lao, «Je, tuwafuate nyinyi kwenye dini yenu na mila yenu ya batili hata kama sisi tunaichukia kwa kujua kwetu ubatili wake?»

    [89] Akasema Shu'ayb kuwaambia watu wake, kwa kuongezea, «Tutakuwa tumemzulia Mwenyezi Mungu urongo tukirudi kwenye dini yenu baada ya Mwenyezi Mungu kutuokoa nayo. Haiwezekani kwetu kugeuka kuifuata dini isiyokuwa ya Mola wetu, isipokuwa iwapo Mwenyezi Mungu, Mola wetu, Ametaka. Hakika Mola wetu Amekienea kila kitu kwa ujuzi, kwa hivyo Anakijua kinachowafaa waja. Ni kwa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, mategemeo yetu ya kupata uongofu na ushindi. Ewe Mola wetu, toa uamuzi wa haki kati yetu na watu wetu, na wewe ndiye bora wa wenye kutoa uamuzi

    [90] Wakasema watukufu na wakubwa wenye kukanusha, wenye kupinga ulinganizi wa Tawhīd (kumpwekesha Mwenyezi Mungu) waliofikia kiwango cha juu katika ujeuri na uasi, wakitahadharisha kwamba Shu'ayb asifuatwe, «Kwa hakika, lau mnamfuata Shu'ayb, nyinyi kwa hivyo ni wenye kuangamia.»

    [91] Hapo watu wa Shu'ayb wakashikwa na mtetemeko mkali, wakawa wameangushwa kwenye mji wao hali ya kuwa wamekufa

    [92] Wale ambao walimkanusha Shu'ayb walikuwa kama kwamba hawakukaa kwenye nyumba zao wala hawakustarehe humo. Kwani walimalizwa, isibaki alama yoyote yao, wakapatikana na hasara na maangamivu duniani na Akhera

    [93] Shu'ayb alijiepusha na wao, alipokuwa na yakini kwamba adhabu ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuwashukia, na akasema, «Enyi watu wangu, ‘Nimewafikishia ujumbe wa Mola wangu na nimewashauri muingie kwenye Dini ya Mwenyezi Mungu na muache hayo mliyonayo; hamkusikia wala hamkutii. Vipi mimi niwasikitikie watu walioukataa upweke wa Mwenyezi Mungu na wakawakanusha Mitume Wake?’»

    [94] Na hatukumtuma Nabii kwenye kijiji chochote kuwalingania watu wake kumuabudu Mwenyezi Mungu na kuwakataza ushirikina ambao wanao, kisha wakamkanusha, isipokuwa tuliwapa mtihani wa shida na mikasa, tukawatia kwenye miili yao magonjwa na ndwele, na katika mali yao ufukara na uhitaji, kwa matumaini kwamba wanyenyekee, waelekee kwa Mwenyezi mungu na warudi kwenye haki

    [95] Kisha tukaigeuza hali nzuri ya mwanzo mahali pa hali mbaya, wakawa wana afya katika miili yao, na ukunjufu na neema katika mali zao, ili kuwapa muhula, kwani wakashukuru. Hayo yote hayakuwa na faida kwao, na hawakuzingatia wala hawakukomeka na ushirikina waliokuwa nao na wakasema, «Hii ndiyo hali ya ulimwengu kwa watu wake, kuna siku njema na siku mbaya; na hayo ndiyo yaliyowapitia baba zetu hapo nyuma.» Basi, punde si punde, tuliwashika kwa adhabu wakiwa wametulia, hawakuwa wakifikiria kuwa wataangamizwa

    [96] Na lau watu wa miji waliwaamini Mitume wao wakawafuata na kujiepusha na aliyoyakataza Mwenyezi Mungu, Angaliwafungulia Mwenyezi Mungu milango ya heri kwa kila njia. Lakini wao walikanusha, Mwenyezi Mungu Akawatesa kwa adhabu yenye kuangamiza kwa sababu ya ukafiri wao na maasia yao

    [97] Kwani wanadhani hawa watu wa mijini kuwa wao wameokoka na wamesalimika na adhabu ya Mwenyezi Mungu kuwa haitawafika kipindi cha usiku wakiwa wamelala

    [98] Au kwani wanajiaminisha watu wa mijini kuwa wamesalimika na adhabu ya Mwenyezi Mungu kuwa haitawafika kipindi cha mchana wakiwa wameghafilika, wameshughulika na mambo ya dunia yao? Mwenyezi Mungu Amezihusu nyakati mbili hizi kwa kuzitaja, kwa kuwa mwanadamu nyakati hizi huwa wameghafilika zaidi, kwa hivyo kuja adhabu katika nyakati hizi huwa na kitisho zaidi na ni kali zaidi

    [99] Je, wamejiaminisha, watu wa miji iliyokanusha, na vitimbi vya Mwenyezi Mungu kwao na kuwapa Kwake wao muhula, kwa kuwaachilia na yale Aliyowaneemesha nayo katika dunia yao, kwa njia ya kuwatesa sababu ya vitimbi vyao? Basi hawajiaminishi na vitimbi vya Mwenyezi Mungu isipokuwa watu wenye kuangamia

    [100] Kwani haikuwafunukia wale waliokaa kwenye nchi baada ya watu wake waliopita kuangamizwa kwa maasia yao, na wakafuata miendo yao, kwamba lau tunataka tungaliwaadhibu kwa makosa yao, kama tulivyowafanyia waliopita kabla yao, na kwamba tutazipiga chapa nyoyo zao, haki isiingie na wasisikie mawaidha wala makumbusho

    [101] Miji hiyo iliyotangulia kutajwa, nayo ni miji ya watu wa Nūḥ„ Hūd, Ṣāliḥ, Lūṭ, na Shu'ayb, tunakupatia, ewe Mtume, habari zake na zile zinazohusu mambo ya Mitume wa Mwenyezi Mungu waliotumwa kwa watu wa miji hiyo, zinazofanya mazingatio yapatikane kwa wenye kuzingatia na pia makemeo kwa madhalimu. Hakika watu wa miji hiyo walijiwa na Mitume wetu na hoja zilizo wazi juu ya ukweli wao, lakini hawakuwa ni wenye kuyaamini yale waliyokuja nayo hao Mitume kwao kwa sababu ya kupita mipaka kwao na kuikanusha haki. Na mfano Alivyopiga chapa Mwenyezi Mungu kwenye nyoyo za makafiri hawa waliotajwa, Atapiga mhuri kwenye nyoyo za wenye kumkanusha Muhammad (S.A.W)

    [102] Na hatukuwapata wengi wa watu waliopita kuwa wana uaminifu wala utekelezaji ahadi, na hatukuwapata wengi wao isipokuwa ni watokaji nje ya utiifu wa Mwenyezi Mungu na ufuataji amri Yake

    [103] Kisha tulimtuma, baada ya Mitume waliotangulia kutajwa, Mūsā mwana wa 'Imrān kwa miujiza yetu iliyo wazi aende kwa Fir'awn na watu wake, wakaikataa na kuikanusha kwa udhalimu na upinzani. Tazama kwa mazingatio, namna gani tuliwafanya na tuliwazamisha hadi wa mwisho wao, huku Mūsā na watu wake wakiona? Na huo ndio mwisho wa waharibifu

    [104] Na Mūsā alisema kumwambia Fir'awn akimzungumzia na akimfikishia ujumbe, «Mimi ni mjumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Muumba viumbe wote na Mwenye kupanga hali zao na marejeo yao

    [105] «Nastahili nisiseme kuhusu Mwenyezi Mungu isipokuwa ukweli na inapasa kwangu nijilazimishe nayo. Nimewajia na dalili na hoja zenye ushindi kutoka kwa Mola wenu juu ya ukweli wa yale ninayowatajia. Basi waachilie, ewe Fir'awn, Wana wa Isrāīl pamoja na mimi kutoka kwenye kifungo chako na ukandamizaji wako, na wape uhuru wa kumuabudu Mwenyezi Mungu.»

    [106] Fir'awn alisema kumwambia Mūsā, «Ukiwa umekuja na alama, kama unavyodai, basi niletee na uihudhurishe mbele yangu, ili madai yako yawe ya sawa na ukweli wako uthibiti, iwapo wewe ni mkweli katika madai yako kuwa wewe ni mjumbe wa Mola wa viumbe.»

    [107] Hapo Mūsā aliitupa fimbo yake na ikageuka nyoka mkubwa anayeonekana waziwazi

    [108] Na akauvuta mkono wake kutoka kwenye uwazi wa kanzu iliyofunguliwa kifuani au chini ya kapwa lake, na papo hapo ukawa mweupe kama maziwa usio na mbalanga, ukiwa ni alama kwa Fir'awn; akiurejesha unarudi rangi yake ya mwanzo, kama ulivyo mwili wake

    [109] Watukufu wa watu wa Fir'awn walisema, «Hakika Mūsā ni mchawi, anayatawala macho ya watu kwa kuwadanganya mpaka ikawaingia kwenye fikira zao kuwa fimbo ni nyoka, na kukiona kitu kinyume na vile kilivyo, na yeye ana ujuzi mwingi wa uchawi na ana uhodari nao

    [110] «Yuwataka kuwatoa nyinyi nyote kwenye nchi yenu.» Fir'awn akasema, «Mnanipa shauri gani, enyi watu watukufu, juu ya mambo ya Mūsā?»

    [111] Wakasema waliohudhuria mjadala wa Mūsā miongoni mwa mabwana wa watu wa Fir’awn na wakubwa wao, «Mfanye Mūsā na Hārūn wangojee, na upeleke askari kwenye miji ya Misri na majimbo yake

    [112] «Ili wakukusanyie kila mchawi mwenye ujuzi mwingi wa uchawi

    [113] Wachawi wakamjia Fir'awn wakasema, «Je, tutakuwa na zawadi na mali tukimshinda Mūsā?»

    [114] Fir'awn akasema, «Ndio, mtakuwa na malipo na ukaribu na mimi mkimshinda.»

    [115] Wakasema wachawi wa Fir'awn kumwambia Mūsā, kwa njia ya kujiona na kutojali. «Ewe Mūsā, chaguwa uwe ni wa mwanzo kutupa fimbo yako au tuwe sisi ni wa mwanzo kutupa.»

    [116] Akasema Mūsā kuwaambia wachawi, «Tupeni nyinyi.» Walipotupa kamba na fimbo, waliyaroga macho ya watu yakaona kwamba yale waliyoyafanya ni ya kweli, na hali yalikuwa ni kiinimacho na vitu vya kudhania, na waliwatisha watu vitisho vikali na walikuja na uchawi wa nguvu ulio mwingi

    [117] Hapo Mwenyezi Mungu Alimletea wahyi mja Wake na Mtume Wake Mūsā, amani imshukiye, katika kisimamo hicho kikubwa ambacho hapo Mwenyezi Mungu Alipambanua baina ya ukweli na urongo, akimuamuru akitupe kilichoko kwenye mkono wake wa kulia, nacho ni fimbo yake. Akaitupa na papo hapo ikawa inavimeza vile wanavyovitupa na kuwafanya watu wadhanie kuwa ni vya kweli na ilhali ni vya urongo

    [118] Hapo haki ikajitokeza na ikafunuka kwa aliyehudhuria na kuiona kuhusu mambo ya Mūsā, amani imshukie, na kuwa yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, analingania haki, na ukabatilika urongo waliokuwa wakiufanya

    [119] Wakashindwa wachawi wote katika mahala walipokusanyika, na akaondoka Fir'awn na watu wake wakiwa wanyonge, waliozidiwa nguvu na kushindwa

    [120] Wakapomoka wachawi kwa nyuso zao kwa kumsujudia Mola wa viumbe wote, kwa uwezo mkubwa wa Mwenyezi Mungu waliouona

    [121] Wakasema, «Tumemamini Mola wa viumbe wote

    [122] «Naye ni Mola wa Mūsā na Hārūn.» Naye ni Ambaye ni lazima ibada ielekezwe Kwake, Peke Yake, si kwa mwingine

    [123] Fir'awn akasema kuwaambia wachawi, «Mumemuamini Mwenyezi Mungu kabla sijawapa idhini mumuamini? Hakika kumuamini kwenu Mwenyezi Mungu, kumsadiki kwenu Mūsā na kuukubali kwenu unabii wake ni hila mlizozipanga nyinyi na Mūsā ili muwatoe watu wa mji wenu kutoka humo, na ili muzivamie heri zake na mufaidike nazo peke yenu.Basi mtajua, enyi wachawi, adhabu na mateso yatakayowashukia nyinyi

    [124] «Nitaikatakata mikono yenu na miguu yenu, enyi wachawi, kwa kupishana: kwa kuukata mkono wa kulia na mguu wa kushoto au mkono wa kushoto na mguu wa kulia, kisha nitawatungika nyinyi nyote juu ya vigogo vya mitende kwa njia ya kuwatesa na ili kuwafanya watu watishike.»

    [125] Walisema wachawi kumwambia Fir'awn, «Tuna uhakika kwamba sisi ni wenye kurejea kwa Mwenyezi mungu na kwamba adhabu Yake ni kali zaidi kushinda adhabu yako. Tutasuburi kikwelikweli leo kwa adhabu yako, tupate kuokoka na adhabu ya Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama

    [126] «Na wewe hukutupata na jambo lolote la kutuaibisha na kutupinga kwalo, ewe Fir'awn, isipokuwa ni kule kuamini kwetu na kukubali kwetu hoja za Mola wetu na dalili Zake alizokuja nazo Mūsā ambazo wewe huwezi kuleta mfano wake wala yoyote mwingine asiyekuwa Mwenyezi Mungu Ambaye ni Yake mamlaka ya mbingu na ardhi. Mola wetu! Tumiminie subira kubwa na uthabiti juu yake, na utufishe tukiwa ni wenye kwndama amri yako, wenye kumfuata Mtume wako.»

    [127] Watukufu na wakubwa miongoni mwa watu wa Fir'awn walisema kumwambia Fir'awn, «Unamuacha Mūsā na watu wake, Wana wa Isrāīl, wawaharibu watu katika nchi ya Misri kwa kuwageuzia dini yao na kuwaletea ibada ya Mwenyezi Mungu Peke Yake, Asiye na mshirika, na kuacha kukuabudu wewe na kuwaabudu waungu wako?» Fir'awn akasema,»Tutawaua watoto wa kiume wa Wana wa Isrāīl, na tutawaacha watoto wao wa kike waishi ili watumike; na sisi tuko juu yao kwa nguvu za ufalme na mamlaka.»

    [128] Akasema Mūsā kuwaambia watu wake, miongoni mwa Wana wa Isrāīl, «Takeni msaada kwa Mwenyezi Mungu Awaokoe na Fir'awn na watu wake, na subirini juu ya shida zinazowapata nyinyi na watoto wenu kutoka kwa Fir 'awn. Kwani ardhi yote ni ya Mwenyezi Mungu Anamrithisha Anayemtaka miongoni mwa waja Wake. Na mwisho mwema ni wa anyemcha Mwenyezi Mungu akafanya maamrisho Yake na akajiepusha na makatazo Yake

    [129] Walisema watu wa Mūsā, miongoni mwa Wana wa Isrāīl, kumwambia Nabii wao Mūsā, «Tulisumbuliwa na tukaudhiwa na nguvu za Fir'awn na watu wake, kwa kuuawa watoto wetu wa kiume na kuachiliwa wanawake wetu, kabla hujatujia na baada ya kutujia.» Mūsā akawaambia, «Huenda Mola wenu Akamuangamiza adui yenu, Fir'awn na watu wake, na Awaweke nyinyi katika ardhi yao badala yao, baada ya kuangamia kwao, Aangalie namna mtakavyofanya: mtashukuru au mtakufuru?»

    [130] Hakika tulimpa Fir'awn na watu wake mtihani wa chaka na ukame na upungufu wa matunda yao na nafaka zao ili wakumbuke na wakome, waache upotevu wao na wakimbilie kwa Mola wao kwa kutubia

    [131] Ukiwajia Fir'awn na watu wake urutuba na chakula huwa wakisema, «Hii ni yetu tunayoistahiki.» Na ukiwapata wao ukame na chaka huwa wakiona wameingiliwa na ukorofi na huwa wakisema, «Haya ni kwa sababu ya Mūsā na walio pamoja na yeye.»Jua utanabahi kwamba yanayowapata ya ukame na chaka ni kwa uamuzi wa Mwenyezi Mungu na makadirio Yake, na ni kwa sababu ya madhambi yao na ukafiri wao. Lakini wengi wa watu wa Fir'awn hawalijui hilo, kwa kuvama kwao kwenye ujinga na upotevu.»

    [132] Watu wa Fir'awn wakasema kumwambia Mūsā, «Alama yoyote utakayotuletea, na dalili na hoja zozote utakazotusimamishia ili utuepushe na dini ya Fir'awn tuliyonayo, sisi si wenye kukuamini,»

    [133] Tukawapelekea wao mafuriko yenye kumaliza yaliyozamisha makulima na matunda; tukapeleka nzige wakazila nafaka zao, matunda yao, milango yao, sakafu zao na nguo zao; na tukapeleka chawa wanaoharibu matunda na kumaliza wanyama na mimea; tukapeleka vyura wakajaa kwenye vyombo vyao na vyakula vyao na malazi yao; na pia tukapeleka damu, ikawa mito yao na visima vyao vimegeuka damu, wasipate maji safi ya kunywa. Hii ni miujiza kati ya miujiza ya Mwenyezi Mungu, hakuna aiwezae isipokuwa Yeye, baadhi yake imetengwa na mingine. Pamoja na haya yote, watu wa Fir'awn walijiona watukufu, wakafanya kiburi kwa kukataa kumuamini Mwenyezi Mungu, wakawa ni watu wanatenda mambo Anayoyakataza Mwenyezi Mungu ya maasia na uhalifu kwa, ujeuri na uasi

    [134] Na adhabu ilipomteremkia Fir'awn na watu wake, walimkimbilia Mūsā na wakasema, «Ewe Mūsā, tuombee Mola wako, kwa wahyi aliokuletea Mwenyezi Mungu kwamba adhabu huondolewa kwa kutubia. Na ukituondolea adhabu tuliyonayo, tutayaamini uliyokuja nayo, na tutayafuata uliyotuitia kwayo, na tutawaachilia, pamoja na wewe, Wana wa Isrāīl, hatutawazuia waende na wewe pale wanapotaka

    [135] Mwenyezi Mungu Alipowaondolea adhabu Aliyoiteremsha kwao, mpaka muda ambao hapana budi wataufikia na waadhibiwe, ambapo hapo hakutawanufaisha kule kupewa muhula kuliotangulia na kuondolewa kwao adhabu mpaka wakati wa kufika kwake, punde si punde wanarudi kuvunja ahadi waliyomuahidi Mola wao na Mūsā na wanaendelea na kudumu na ukafiri wao na upotevu wao

    [136] Basi tukawalipiza ulipokuja muda uliowekwa kwa wao kuangamizwa, kwa kuwashushia mateso yetu, nayo ni kuwazamisha baharini, kwa sababu ya kuikanusha kwao miujiza iliyodhihiri kwa Mūsā na wakawa wanaipuuza; na kupuuza huko ndio sababu ya kukanusha

    [137] Tukawarithisha Wana wa Isrāīl, waliokuwa wakifanywa wanyonge, pande za mashariki na magharibi ya ardhi, nazo ni sehemu za miji ya Sham, tulizozitia baraka kwa kutoa mazao na matunda na mito. Na limetimia neno jema la Mola wako, ewe Muhammad, kwa Wana wa Isrāīl kwa kuwapa utulivu katika ardhi kwa sababu ya kuvumilia kwao makero ya Fir'awn na watu wake. Na tukayavunjavunja yale maamirisho na mashamba ambayo Fir'awn na watu wake walikuwa wakiyatengeneza, na majengo na majumba na mengineyo waliokuwa wakiyajenga

    [138] Na tuliwakatia Wana wa Isrāīl bahari, wakapita kwa watu waliokuwa wamekaa na kuendelea kuabudu masanamu wao. Wana wa Isrāīl wakasema, «Tufanyie, ewe Mūsā, sanamu tupate kumuabudu na kumfanya mungu kama hawa watu walivyo na masanamu wanaowaabudu.» Mūsā akawaambia, «Hakika yenu nyinyi,enyi watu, ni wajinga wa kujua utukufu wa Mwenyezi Mungu, na hamjui kwamba ibada haifai kufanyiwa yoyote isipokuwa Mwenyezi Mungu, Aliye Mmoja, Mwenye kutendesha nguvu

    [139] Hakika hawa wanaowakalia hawa masanamu, ushirikina waliomo ndani yake umeangamizwa, na ni yenye kuangamiza na ni ya urongo yale waliokuwa wakiyafanya ya kuwaabudu masanamu hao ambao hawawazuilii adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwashukia

    [140] Mūsā akasema kuwaambia watu wake, «Je, niwatafutie muabudiwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyewaumba na Akawatukuza juu ya walimwengu wa zama zenu kwa wingi wa Mitume watokanao na nyinyi, kumuangamiza adui yenu na kwa miujiza Aiyowahusu nayo.»

    [141] Na kumbukeni, enyi Wana wa Isrāīl, neema zetu kwenu tulipowaokoa na kifungo cha Fir'awn na jamaa zake na unyonge na utwevu mliokuwa nao, wa kuchinjwa watoto wenu wa kiume na kuwaacha wanawake wenu ili watumike na wadharauliwe. Na katika kupitia kwenu mateso mabaya zaidi na maovu zaidi kisha kuwaokoa ni mtihani utokao kwa Mwenyezi Mungu kwenu na neema kubwa

    [142] Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Alimpa ahadi Mūsā ya kuzungumza na Mola wake masiku thelathini, kisha Akamuengezea muda wa masiku kumi baada yake, ukakamilika wakati ambao Mwenyezi Mungu Alimuwekea Mūsā wa kusema na Yeye kuwa masiku arubaini. Na Mūsā alisema kumwambia ndugu yake Hārūn, alipotaka kwenda kuzungumza na Mola wake, «Kuwa ni badala yangu kwa watu wangu mpaka nitakaporudi, na uwahimize wamtii Mwenyezi Mungu na wamuabudu, na usifuate njia ya wale ambao wanaleta uharibifu katika ardhi.»

    [143] Na alipokuja Mūsā kwa wakati uliowekwa nao ni muda wa masiku arubaini na Akasema na yeye Mola wake kwa kumpa wahyi wake, maamrisho Yake na makatazo Yake, alifanya hamu ya kumuona Mwenyezi Mungu akataka amtazame. Mwenyezi Mungu Akamwambia, «Hutoniona!»Yaani hutaweza kuniona ulimwenguni. «Lakini liangalie jabali, likitulia mahali lilipo nitakapolitokezea, basi utaniona.» Alipojitokeza Mola wake kwa lile jabali alilifanya lipondeke liwe sawa na ardhi. Hapo Mūsā alianguka akiwa amezimia. Alipopata fahamu kutoka kwenye hali ya kuzimia alisema, «Kwa kukutakasisha, ewe Mola wangu, na kila sifa isiyolingana na utukufu wako, mimi natubia kwako kutokana na kuomba kwangu kukuona katika uhai huu wa kilimwengu, na mimi ni wa mwanzo wa wenye kukuamini miongoni mwa watu wangu.»

    [144] Mwenyezi Mungu Akasema, «Ewe Mūsā, Mimi nimekuchagua kati ya watu kwa ujumbe wangu kwa viumbe wangu niliokutuma kwao na kwa kusema kwangu na wewe pasi na mtu wa kati. Basi chukua niliyokupa kati ya maamrisho yangu na makatazo yangu, ushikamane nayo na uyatumie na uwe ni miongoni mwa wenye kumshukuru Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa utume aliokupa na Akakuhusu kwa maneno Yake

    [145] Na tulimuandikia Mūsā katika Taurati mawaidha ya kila anachokihitajia katika hukumu za Dini yake, ili yapatikane makemeo na mazingatio, na maelezo yanayofafanua mambo ambayo walikalifishwa nayo ya halali na ya haramu, maamrisho na makatazo, visa, mambo ya itikadi, habari na mambo yasiyoonekana. Mwenyezi Mungu Alimwambia, «Basi yashike kwa nguvu.» Yaani, ishike Taurati kwa kwa bidii na hima. «Na uwaamrishe watu wako wazitumie sheria za Mwenyezi Mungu zilizomo humo. Hakika mwenye kushirikisha miongoni mwao na wengineo, mimi nitamuonesha huko Akhera nyumba ya waasi, nayo ni Moto wa Mwenyezi Mungu ambao Ameutayarisha kwa maadui Wake waliyotoka nje ya utiifu Wake.»

    [146] Nitazipotoa nyoyo za wenye kufanya kiburi wakaacha kunitii na wenye kuwafanyia watu kiburi pasi na haki zisizielewe hoja na dalili zinazoonesha ukubwa wangu, sheria yangu na hukumu zangu, wawe hawamsikilizi Mtume yoyote kwa kiburi chao. Na wakiona, hawa wenye kuifanyia Imani kiburi, kila alama hawaiyamini, kwa sababu ya kupa mgongo kwao na kupingana kwao na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Wakiiyona njia ya uongofu hawaifanyi ni njia, na wakiiyona njia ya upotevu wanaifanya kuwa ni njia na ni dini. Hayo ni kwa sababu ya kukanusha kwao aya za Mwenyezi Mungu na kughafilika kwao kuziangalia na kuyatia akilini maana yake

    [147] Na wale ambao walizikanusha aya za Mwenyezi Mungu, hoja Zake na kukutana na Mwenyezi Mungu huko Akhera, matendo yao mema yatapomoka kwa sababu ya kukosekana sharti yake, nayo ni kumuamini Mwenyezi Mungu na kukubali kwamba malipo Yake ni kweli. Hawatalipwa huko Akhera isipokuwa malipo ya yale ambayo walikuwa wakiyafanya ulimwenguni ya ukafiri na maasia, nayo ni kukaa milele Motoni

    [148] Na walitengeneza watu wa Mūsā, baada ya yeye kuwaacha kwenda kuzungumza na Mola Wake, sanamu wa kigombe asiye na roho anayetoa sauti, kutokana na dhahabu yao, wakamfanya ni muabudiwa. Kwani hawajui kwamba yeye hasemi na wao na hawaongozi wao kwenye kheri yoyote? Walijasiri kufanya jambo hili ovu, wakawa ni wenye kujidhulumu nafsi zao, ni wenye kuweka kitu mahala pasipokuwa pake

    [149] Na walipojuta wale walioabudu kigombe badala ya Mwenyezi Mungu pale aliporudi Mūsā kwao, na wakaona kwamba walipotea njia ya sawa, na waliondoka kwenye dini ya Mwenyezi Mungu, walianza kuukubali uja na kuomba kufutiwa makosa yao wakasema, «Mola wetu Asipoturehemu kwa kukubali toba yetu, na kufinika kwayo madhambi yetu, tutakuwa ni wenye kuangamia ambao matendo yao mema yamepita bure.»

    [150] Aliporejea Mūsā kwa watu wake akiwa na hasira na huzuni, kwa kuwa Mwenyezi Mungu Alimpa habari kwamba watu wake wamepatikana na mtihani na kwamba Sāmirīy amewapoteza. Mūsā alisema, «Ni ubaya ulioje mlioufanya nyuma yangu baada ya mimi kuondoka! Je mumeitangulia amri ya Mola wenu?» Yaani, mulikufanyia haraka kuja kwangu kwenu, na hali ni jambo lililopangwa na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka?. Mūsā alizitupa mbao za Taurati kwa kuwakasirikia watu wake walioabudu kigombe na kwa kumkasirikia ndugu yake Hārūn. Akakishika kichwa cha Hārūn na akakivuta upande wake. Hārūn alisema kwa kubembeleza, «Ewe mwana wa mamangu, ‘Hakika hawa watu walinidharau, waliniona ni mnyonge na walikaribia kuniua, kwa hivyo usiwafurahishe maadui kwa unayonifanya na usiniingize katika hasira zako ukanifanya ni pamoja na wale walioenda kinyume na amri yako na wakaabudu kigombe.’»

    [151] Mūsā Alisema, ulipomfunukia udhuru wa ndugu yake na kujua kuwa yeye hakufanya uzembe katika kusimama imara juu ya amri ya Mwenyezi Mungu, «Mola wangu nisamehe ghadhabu zangu na umsamehe ndugu yangu yaliyopita kati yake na Wana wa Isrāīl, na ututie ndani ya rehema yako kunjufu, kwani wewe una huruma na sisi zaidi kuliko kila mwenye huruma.»

    [152] Hakika wale waliomfanya kigombe ni mungu itawapata wao ghadhabu kali kutoka kwa mola wao na unyonge katika uhai wa kilimwengu, kwa sababu ya kumkanusha kwao Mola wao. Na kama tulivyofanyia hawa, tutawafanyia wazushi wenye kuleta uzushi katika Dini ya Mwenyezi Mungu; na kila mwenye uzushi katika Dini ni mnyonge

    [153] Na wale waliofanya maovu ya ukafiri na maasia kisha wakarejea, baada ya kuyafanya, kwenye Imani na matendo mema, hakika Mola wako baada ya toba ya kidhati ni Msamehefu mno wa vitendo vyao viovu si Mwenye kuwafedhehi kwavyo, ni Mwenye kuwarehemu wao na kila aliye mfano wao miongoni mwa wenye kutubia

    [154] Zilipotulia hasira za Mūsā alizichukua mbao baada ya kuwa alizitupa chini, na ndani yake mlikuwa na maelezo ya haki na rehema kwa wanaomcha Mwenyezi Mungu na kuogopa mateso Yake

    [155] Na Mūsā alichagua miongoni mwa watu wake wanaume sabiini walio bora kati yao, akatoka na wao akaenda hadi Tū,r Sīnā’ kwa wakati na muda ambao Mwenyezi Mungu Alimuagizia akutane na Yeye pamoja nao ili watubie kwa yale yaliyokuwa kwa wahuni wa Wana wa Isrāīl ya kuabudu kigombe. Walipokuja mahala hapo walisema, «Hatutakuamini, ewe Mūsā mpaka tumuone Mwenyezi Mungu waziwazi, basi utakaposema na Yeye tuoneshe.» Papo hapo walishikwa na mtetemeko mkali wakafa. Akasimama Mūsā akimnyenyekea Mwenyezi Mungu na akasema, «Ewe Mola wangu, niwaambie nini Wana wa Isrāīl nikiwajia na hali wewe umewaangamiza wabora wao? Lau unataka ungaliwaangamiza wote kabla ya hali hii ya kuwa mimi niko na wao. Hilo lingalikuwa sahali zaidi kwangu. Unatuangamiza kwa yale waliyoyafanya wachache wa akili miongoni mwetu? Kitendo hiki ambacho watu wangu wamekifanya cha kuabudu kigombe, hakikuwa isipokuwa ni majaribu na mtihani, unampoteza kwayo unayemtaka miongoni mwa viumbe wako na unamuongoza kwayo unayemtaka kumuongoza. Ni wewe mtegemewa wetu na mwenye kutunusuru, tughufirie dhambi zetu na uturehemu kwa rehema zako; na wewe ndiye bora wa wenye kusamehe makosa na kusitiri dhambi

    [156] «Na utujaalie ni miongoni mwa wale uliowaandikia matendo mema ulimwenguni na Akhera. Sisi tumerejea kwako hali ya kutubia.» Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Akasema kumwambia Mūsā, «Adhabu yangu nitampatiliza kwayo ninayemtaka miongoni mwa viumbe wangu, kama nilivyowapatiliza hawa niliowapatia katika watu wako, na rehema yangu imewaenea viumbe wangu wote, nitawaandikia wale wanaomcha Mwenyezi Mungu na kuogopa mateso Yake, wakazitekeleza faradhi Zake na wakayaepuka mambo ya kumuasi, na wale ambao wao wanaziamini dalili za tawhīd (kumpwekesha Mwenyezi Mungu) na hoja zake

    [157] Rehema hii nitawaandikia wale wanaomuogopa Mwenyezi Mungu na kujiepusha na mambo ya kumuasi, na wanaomfuata Mtume aliye Nabii, ambaye hasomi wala haandiki, naye ni Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani imshukiye, ambaye wanazipata sifa zake na mambo yake yaandikwa huko kwao katika Taurati na Injili; anawaamrisha kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtii na kila lijulikanalo kuwa ni lema, na anawakataza ushirikina na maasia na kila lijulikanalo kuwa ni baya, na anawahalalishia vizuri vya vyakula na vinywaji na kuoana, na anawaharamishla vichafu vya hivyo kama nyama ya nguruwe na vile ambavyo walikuwa wakijihalalishia miongoni mwa vyakula na vinywaji ambavyo aliviharamisha Mwenyezi Mungu, na anawaondolea wao mambo magumu waliokalifishwa nayo kama kukata mahali pa najisi nguoni, kuzichoma moto ngawira, ulazimu wa kisasi juu ya aliyeua kwa kukusudia au kwa kukosea. Basi wale ambao walimuamini Nabii asiyejua kuandika wala kusoma kilichoandikwa, Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani imshukiye, na wakaukubali unabii wake, wakamheshimu, wakamtukuza na wakamuhami na wakaifuata Qur’ani aliyoteremshiwa, wakaufuata mwendo wake kivitendo, hao ni wenye kufaulu kwa kupata yale ambayo Mwenyezi Mungu Aliwaahidi waja wake Waumini

    [158] Waambie, ewe Mtume, watu wote, «Mimi ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu kwenu nyote, si kwa baadhi yenu bila ya wengine, Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake. Haifai kuelekezwa uungu na ibada isipokuwa Kwake, zilizotukuka sifa Zake, Mwenye uwezo wa kupatisha viumbe, kuwaondosha na kuwafufua. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na kubalini upweke Wake, na muaminini Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani imshukiye, Nabii asiyesoma wala kwandika, anayemuamini Mwenyezi Mungu na yale aliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wake na yale waliyoteremshiwa manabii kabla yake; Mfuateni Mtume huyu na jilazimisheni kuyafanya anayowaamrisha kwayo ya kumtii Mwenyezi Mungu kwa kutaraji muafikiwe kufuata njia iliyolingana sawa.»

    [159] Na miongoni mwa Wana wa Isrāīl wanaotokana na jamaa za Mūsā kuna kundi la watu ambao wanasimama imara juu ya haki, wanawaongoza watu kwenye hiyo haki na wanafanya usawa katika kutoa uamuzi katika mambo yao

    [160] Na tuliwagawa watu wa Mūsā miongoni mwa Wana wa Isrāīl makabila kumi na mbili, kwa idadi ya Asbāṭ- wana wa Ya’qūb-, kila kabila ikajulikana kupitia kiongozi wake. Na tulimpelekea wahyi Mūsā, walipotaka watu wake kwake maji ya kunywa waliposhikwa na kiu katika kuzunguka kwao, tukamwambia, «Lipige hilo jiwe kwa fimbo yako.» Akalipiga na pakabubujika chemchemi za maji sehemu kumi na mbili, na watu wa kila kabila, miongoni mwa yale makabila kumi na mbili, walijua mahali pao pa kunywa, hakuna kabila litakaloingia sehemu ya kunywa ya kabila lingine. Na tukawafinika kiwingu juu yenu, na tukawateremshia mann- kitu kinachofanana na gundi chenye ladha kama ya asali- na salwā- ndege wanaofanana na wale wanaoitwa sumānā (tomboro), na tukawaambia, «Kuleni vitu vizuri tulivyowaruzuku.» Walivichukia na kuvichoka hivyo kwa muda mrefu wa kuvitumia na wakasema, «Hatutavumilia juu ya chakula kimoja.» Na wakataka kubadilishiwa kizuri walichonacho kwa ambacho ni kiovu. Na wao hawakutudhulumu sisi walipoacha kumshukuru Mwenyezi Mungu na kuacha kusimama na yale Aliyoyalazimisha Mwenyezi Mungu juu yao, lakini walikuwa wakizidhulumu nafsi zao, kwa kuwa walizikosesha kila jema na kuzipeleka kwenye shari na mateso

    [161] Na kumbuka, ewe Mtume, uasi kwa Wana wa Isrāīl Mola wao, kutakata na sifa pungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, na Nabii wao Mūsā, amani imshukiye, na kugeuza kwao maneno waliyoamrishwa wayaseme pindi Alipowaambia Mwenyezi Mungu, «kaeni mji wa Baitul Maqdis na kuleni matunda yake, nafaka zake na mimea yake popote mtakapo na wakati wowote mtakao na semeni, ‘tuondoshee dhambi zetu,’ na ingieni mlangoni mkimnyenyekea Mwenyezi Mungu, tutawasamehe makosa yenu na hatutawaadhibu kwayo, na tutawaongezea walio wema kheri mbili: za ulimwengu na Akhera

    [162] Waliomkanusha Mwenyezi Mungu kati yao waliligeuza neno ambalo Mwenyezi Mungu Aliwaamrisha waliseme, wakaingia mlangoni wakijikokota kwa matako yao na wakasema, «habbah fī sha'rah» (mbegu kwenye unywele), hapo tukawateremshia adhabu kutoka mbinguni, tukawaangamiza kwayo, kwa sababu ya udhalimu wao na uasi wao

    [163] Na waulize, ewe Mtume, hawa Mayahudi kuhusu habari ya watu wa kijiji kilichokuwa karibu ya bahari, ambacho watu wake walikuwa wakipita mipaka siku ya Jumamosi kwa kufanya mambo yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu, kwani Alikuwa Amewaamrisha waitukuze siku ya Jumamosi na wasivue samaki siku hiyo. Mwanyezi Mungu Akawajaribu na kuwapa mtihani, wakawa samaki wao wawajia siku ya Jumamosi kwa wingi wakiwa juu ya uso wa bahari, na Jumamosi ikipita wakawa samaki wanapotea na hawawaoni kabisa. Basi wakawa wafanya hila ya kuwatega siku ya Jumamosi kwenye mashimo na kuwavua baada yake. Na kama tulivyowaelezea vile Mwenyezi Mungu Alivyowajaribu na kuwapa mtihani kwa kuwatoa samake juu ya bahari katika siku ambayo waliharamishiwa kuwavua na kuwaficha wasiwaone katika siku ambazo ni halali kwao kuwavua, ndivyo tunavyowafanyia mtihani wao kwa sababu ya uasi wao na kutoka kwao kwenye utiifu wa Mwenyezi Mungu

    [164] Na kumbuka, ewe Mtume, pindi kundi kati yao waliposema kuwaambia kundi lingine lililokuwa likiwapa mawaidhia wale waliopita mipaka siku ya Jumamosi na likiwakataza wasimuasi Mwenyezi Mungu siku hiyo, «Kwa nini nyinyi mnawaidhia watu ambao Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaangamiza ulimwenguni kwa kumuasi au ni Mwenye kuwaadhibu adhabu kali kesho Akhera?» Wakanena wale waliokuwa wakiwakataza wasimuasi Mwenyezi Mungu, «Tunawaidhia na tunawakataza ili tuwe na udhuru kuhusu wao na kwa ajili ya kutekeleza wajibu wa Mwenyezi Mungu juu yetu ya kuamrisha mema na kukataza maovu na kwa matumaini kwamba watamcha Mwenyezi Mungu, watamuogopa na watatubia kutokana na kumuasi kwao Mola wao na kupita mipaka ya mambo yaliyoharamishiwa kwao.»

    [165] Basi lilipoacha lile pote ambalo lilikiuka mipaka siku ya Jumamosi yale waliyokumbushwa na likaendelea kwenye upotevu wake na kukiuka mipaka kwake katika siku hiyo na lisiyakubali mawaidha waliyopewa na pote lenye kuwaidhia, Mwenyezi Mungu Aliwaokoa wale waliokuwa wanakataza maasia Yake na akawapatia wale waliokiuka mipaka siku ya Jumamosi adhabu kali mno kwa sababu ya kuenda kinyume kwao na amri ya Mwenyezi Mungu na kutoka kwao kwenye utiifu Wake

    [166] Basi pote hilo lilipoasi na likayakiuka yale ambayo Mwenyezi Mungu Alioyakataza ya kutowinda siku ya siku ya Jumamosi, Mwenyezi Mungu Aliwaambia (watu wa pote hilo), «Kuweni manyani hali ni wanyoge ni wenye kuwekwa mbali na kila jema.» Na wakawa hivyo

    [167] Na kumbuka, ewe Mtume, pindi Alipotangaza Mola wako, tangazo wazi, kwamba Atawapelekea Mayahudi mwenye kuwaonjesha adhabu mbaya na kuwadhalilisha mpaka Siku ya Kiyama. Hakika Mola wako ni Mpesi wa kutesa kwa anayestahili kuteswa kwa sababu ya ukafiri wake na uasi wake. Na hakika Yeye ni Mwingi wa kusamehe dhambi za wenye kutubia, ni Mwnye huruma kwao

    [168] Na tuliwagawanya Wana wa Isrāīl makundi: kati yao kuna wanaosimama kutekeleza haki za Mwenyezi Mungu na haki za waja Wake, na kati yao kuna wenye kufanya kasoro wenye kuzidhulumu nafsi zao. Na hawa tuliwapa mtihani wa maisha ya neema na ukunjufu wa riziki; na pia tuliwapa mtihani wa maisha ya dhiki, misiba na matatizo kwa matarajio kuwa watarudi kumtii Mola wao na watatubia kutokana na vitendo vya kumuasi

    [169] Wakaja, baada ya hawa ambao tulieleza sifa zao, badala mbovu. Walichukua Kitabu kutoka kwa wakale wao, wakakisoma na wakakijua, na wakaenda kinyume na hukumu zake, wakawa wanachukua kile wanacholetewa cha starahe ya ulimwenguni kinachotokana na njia mbaya za mapato kama hongo na mfano wake. Hayo ni kwa sababu ya wingi wa pupa lao na uroho wao, na wanasema pamoja na hayo, «Mwenyezi Mungu Atatusamehe,» wakitamani kwa Mwenyezi Mungu mambo yasiyofaa, na ikiwajia Mayahudi hawa starahe yenye kuondoka, miongoni mwa vitu vya haramu, huichukua na kuihalalisha, huku wakiendelea kufanya madhambi yao na kutumia haramu. Kwani hazikuchukuliwa kwao ahadi juu ya kuisimamisha Taurati na kufuata kivitendo yaliyomo ndani yake na kwamba hawatasema juu ya Mwenyezi Mungu isipokuwa ukweli na kwamba hawatamzulia urongo, wakayajua yaliyomo Kitabuni, wakayapoteza na wakaenda kinyume na ahadi ya Mwenyezi Mungu kwao katika hilo? Na nyumba ya Akhera ni bora zaidi kwa wanaomcha Mwenyezi Mungu, wakafuata amri Zake na wakaepuka makatazo Yake. Kwani hawa wanaochukua mapato duni hawaelewi kwamba yaliyo mbele ya Mwenyezi Mungu ni bora zaidi na yenye kusalia zaidi kwa wachamungu

    [170] Na wanaoshikamana na Kitabu, wanaoyafuata kivitendo yaliyomo ndani yake miongoni mwa mambo ya itikadi na hukumu na wanaodumu na Swala kwa mipaka yake na wasiyozipoteza nyakati zake, Mwenyezi Mungu Atawalipa kwa matendo yao mema na hatayapoteza

    [171] Na kumbuka, ewe Mtume, pindi tulipoliinua jabali juu ya Wana wa Isrāīl likawa kama kwamba ni kiwingu kinachowafinika, wakawa na yakini kuwa kitawaangukia iwapo hawatazikubali hukumu zilizomo kwenye Taurati, na tukawaambia,»Chukueni tulichowapa kwa nguvu.» Yaani, fuateni kivitendo tulichowapa kwa bidii yenu, na yakumbukeni yaliyomo kwenye Kitabu chetu ya ahadi na masharti tuliyoyachukuwa kwenu kwamba mtayatekeleza yaliyomo ndani yake, ili mumche Mola wenu mpate kuokoka na mateso Yake

    [172] Na kumbuka, ewe Mtume, pindi Mola wako Alipowatoa wana wa Ādam kutoka kwenye migongo ya baba zao, Akawathibitishia upweke Wake kwa kuwatia tabia ya kimaumbile kwamba Yeye ni Mola wao, ni Muumba wao na ni Mmiliki wao; wakamkubalia hilo kwa kuchelea wasije kukanusha Siku ya Kiyama wasikubali chochote katika hilo na wasije wakadai kwamba hoja ya Mwenyezi Mungu haijasimama kwao na wala hawajui chochote juu yake, bali wao walikuwa wameghafilika na hilo

    [173] Na ili msiseme, «Hakika baba zetu walishirikisha kabla yetu na wakavunja ahadi, na sisi tukawafuata, basi je utatuadhibu kwa yale waliyoyafanya wale ambao waliyaharibu matendo yao kwa kumfanya Mwenyezi Mungu ana mshirika katika ibada?»

    [174] Na kama tulivyozipambanua hizo aya na tukaeleza ndani yake tulichowafanyia watu waliopita, ndivyo tunavyozipambanua aya na kuzieleza kwa watu wako, ewe Mtume, kwa kutazamia kwamba watarudi waache ushirikina wao na warajee kwa Mola wao

    [175] Na wasimulie,ewe Mtume, watu wako habari ya mwanamume mmoja miongoni mwa Wana wa Isrāīl, tuliyompa hoja zetu na dalili zetu, akajifunza hizo kisha akazikanusha na akazitupa nyuma ya mgongo wake, akashindwa na Shetani na akawa ni miongoni mwa wapotevu wenye kuangamia, kwa sababu ya kuenda kinyume kwake na amri ya Mola wake na kumtii kwake Shetani

    [176] Na lau tulitaka kukitukuza cheo chake kwa aya tulizompa tungalifanya, lakini yeye alitegemea ulimwengu na akafuata matamanio yake, na akafadhilisha ladha zake na hawaa zake juu ya Akhera, na akakataa kumtii Mwenyezi Mungu na akaenda kinyume na amri Yake. Mfano wa mwanamume huyu ni mfano wa mbwa: ukimfukuza au ukimuacha hutoa ulimi wake katika hali zote mbili. Basi hivyo ndivyo alivyo yule aliyejivua aya za Mwenyezi Mungu kwa kuziacha, huwa akiendelea katika ukafiri wake ikiwa utafanya bidii kumlingania au utampuuza. Sifa hii, ewe Mtume, ndiyo sifa ya watu hawa waliokuwa wapotevu kabla hujawajia kwa uongofu na utume. Basi simulia, ewe Mtume, habari za watu waliopita, kwani katika kutolea kwako habari zao ni miujiza mikubwa zaidi; na huenda watu wako wakazingatia juu ya yale uliyowajia nayo na wakakuamini

    [177] Ni mfano mbaya ulioje! Mfano wa watu waliokanusha hoja za Mwenyezi Mungu na dalili Zake wakazikataa na hali kwamba ni nafsi zao wenyewe walikuwa wakizidhulumu kwa sababu ya kukanusha kwao hoja hizi na dalili

    [178] Yule ambaye Mwenyezi Mungu Anamuafikia kumuamini Yeye na kumtii, huyo ndiye aliyeafikiwa; na yule ambaye Anamuachilia Asimuafikiye, huyo ndiye mwenye hasara, mwenye kuangamia. Kuongoza na kupoteza kunatokana na Mwenyezi Mungu Peke Yake

    [179] Na kwa hakika tuliuumbia Moto - ambao ndani yake Mwenyezi Mungu Atawaadhibu wanaostahili kuadhibiwa huko Akhera- majini na binadamu wengi, wana nyoyo lakini hawaelewi kwazo, hawatazamii malipo mazuri wala hawaogopi mateso; na wana macho hawaangalii kwayo aya za Mwenyezi Mungu na dalili Zake, na wana masikio hawasikii kwayo aya za Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kuzitia akilini. Hawa ni kama wanyama wasioelewa waambiwacho, wasiofahamu wakionacho na wasiotia akilini kwa nyoyo zao kizuri na kibaya wakaweza kuzitenganisha. Bali wao wamepotea zaidi kuliko hao wanyama, kwani wanyama wanaona yanayowafaa na yanayowadhuru na wanamfuata mchungaji wao. Ama wao ni kinyume cha hilo, wao ndio wenye kughafilika na jambo la kumuamini Mwenyezi Mungu na kumtii

    [180] Na Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Ana Majina Mazuri yanayoonyesha ukamilifu wa uwezo Wake, na majina Yake yote ni mazuri. Basi ombeni kutoka Kwake, kwa majina Yake, mnachotaka na muwaacheni wale wanaogeuza majina Yake kwa kuzidisha na kupunguza au kupotoa, kama kumuita kwa majina hayo asiyeyastahiki, kama vile washirikina wanavyowaita, kwa majina hayo, waungu wao, au ayape majina hayo maana ambayo Mwenyezi Mungu Hakuyataka wala Mtume Wake. Basi watapata malipo ya matendo yao mabaya waliokuwa wakiyafanya ulimwenguni ya kumkanusha Mwenyezi Mungu, kuyapotoa majina Yake na kuwafanya warongo Mitume Wake

    [181] Na miongoni mwa wale tuliowaumba kuna kundi la watu bora wanaoongoka kwenye haki na wanaita watu waifuate, na kwa hiyo wanahukumu na wanafanyia watu uadilifu; na wao ni viongozi wa uongofu, kati ya wale ambao Mwenyezi Mungu Amewaneemesha kwa Imani na kufanya amali njema

    [182] Na wale ambao walizikanusha aya zetu wakazikataa na wasiwaidhike nazo, tutawafungulia milango ya riziki na njia za maisha katika ulimwengu, kwa kuwavuta kidogo kidogo mpaka wahadaike kwa yale ambayo wako nayo na waitakidi kuwa wao wako kwenye kitu cha maana, kisha tutawatesa kwa ghafla kwa namna wasioijua. Haya ni mateso yatokao kwa Mwenyezi Mungu ya kukanusha hoja za Mwenyezi Mungu na aya Zake

    [183] Na nitawapa muhula hawa ambao walizikanusha aya zetu mpaka wadhanie kwamba wao hawatateswa, waongeze ukafiri na uasi. Na kwa hivyo, waongezewe adhabu. Kwani vitimbi vyangu ni vigumu, yaani: ni vya nguvu na vikali havizuiliwi kwa nguvu wala kwa hila

    [184] Kwani hawafikirii hawa ambao walizikanusha aya zetu wakazingatia kwa akili zao na wakajua kwamba Muhammad hana wazimu? Yeye hakuwa isipokuwa ni mwenye kuwaonya wao mateso ya Mwenyezi Mungu kwa kumkanusha kwao Yeye, iwapo hawataamini, na ni mshauri muaminifu

    [185] Au kwani hawaangalii, hawa wakanushaji aya za Mwenyezi Mungu, kwenye ufalme wa Mwenyezi Mungu uliyo mkubwa na mamlaka Yake yenye uwezo wa kushinda, mbinguni na ardhini na chochote kile Alichokiumba Mwenyezi Mungu, zimetukuka sifa Zake, kwenye vitu viwili hivyo, wakalitia akilini hilo na wakalizingatia kwa akili zao na wakaangalia muda wa kikomo cha maisha yao ambao huenda ukawa umesongea karibu wakawa watakufa kwenye ukafiri wao na watakuwa kwenye adhabu ya Mwenyezi Mungu na mateso yake makali? Basi ni kitisho gani na onyo gani baada ya onyo la Qur’ani wataliamini na watalifanyia kazi

    [186] Yoyote ambaye Mwenyezi Mungu Anampoteza njia ya sawa hakuna mwenye kumuongoza, na Atawaacha wao ndani ya ukafiri wao wakiwa wanaduwaa na wanapigwa na bumbuazi

    [187] Wanakuuliza, ewe Mtume, makafiri wa Makkah kuhusu Kiyama: kusimama kwake ni lini? Waambie, elimu ya kusimama kwake iko kwa Mwenyezi Mungu, haitoi nje isipokuwa Yeye, imekuwa nzito kuijua na imefichika kwa watu wa mbinguni na ardhini. Hakuna Malaika aliyekaribishwa wala Mtume aliyetumilizwa anayejua wakati wa kusimama kwake. Hakiji isipokuwa kwa ghafla. Hawa watu wanakuuliza kuhusu hiko Kiyama kama kwamba wewe una pupa la kukijua, una bidii sana ya kukiuliza. Waambie, «Ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu Ambaye Anayajua yaliyofichika kwenye mbingu na ardhi. Lakini wengi wa watu hawajui kwamba hilo hakuna anayelijua isipokuwa Mwenyezi Mungu.»

    [188] Sema, ewe Mtume, «Siwezi kuiletea mema nafsi yangu wala kuiepushia shari yenye kuifikia, isipokuwa iwapo Mwenyezi Mungu Alitaka. Na lau mimi ningalikuwa najua yaliyofichika ningalifanya njia ambazo najua kwamba zitaniongezea maslahi na manufaa na ningalijikinga na shari yenye kuwa kabla haijatukia. Mimi si yoyote isipokuwa ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu, Amenituma kwenu, naogopesha mateso Yake na natoa bishara njema ya thawabu Zake kuwalipa watu wanaoamini kuwa mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na wakafuata sheria Yake kivitendo

    [189] Yeye Ndiye ambaye Aliyewaumba nyinyi, enyi watu, kutokana na nafsi moja, nayo ni Ādam, amani imshukiye. Na akaumba kutokana na nafsi hiyo ya pili yake, nayo ni Ḥawwā’, ili aliwazike naye na ajitulize. Alipomuundama - makusudio ni jinsi ya mke na mume miongoni mwa kizazi cha Ādam - alibeba maji mapesi, akainuka nayo na akakaa nayo mpaka mimba ikatimia. Kilipokaribia kipindi cha kuzaa kwake na akawa mzito, walimuomba, mume na mke, Mola wao, «Tunaapa lau utatupatia mwanadamu aliye sawa, aliye mwema, hakika tutakuwa ni wenye kukushukuru kwa kutupa mtoto mwema.»

    [190] Mwenyezi Mungu Alipowaruzuku, yule mume na mke, mtoto mwema walimfanyia Mwenyezi Mungu washirika katika mtoto yule ambaye Mwenyezi Mungu Alipwekeka katika kumuumba wakamfanya ni mja wa asiyekuwa Mwenyezi Mungu; Ametukukuka Mwenyezi Mungu na Ameepukana na kila mshirika

    [191] Je, washirikina hawa wawashirikisha viumbe vya Mwenyezi Mungu katika ibada ya Mwenyezi Mungu, hali washirikishwa hao hawawezi kuumba chochote, bali wao wameumbwa

    [192] Wala hawawezi kuwanusuru wenye kuwaabudu au kuzilinda nafsi zao na ubaya. Iwapo wao hawaumbi kitu, bali wao wameumbwa na hawawezi kuwalinda wanaowaabudu, wasipatikane na mambo wanayoyachukia, wala kuzilinda nafsi zao. Basi vipi wanafanywa ni waungu? Huu haukuwa isipokuwa ni upeo wa udhalimu na upeo wa uchache wa akili

    [193] Na mnapowalingania, enyi washirikina, masanamu hawa ambao mliwaabudu badala ya Mwenyezi Mungu kwenye uongofu, hawasikii ulinganizi wenu wala hawawafuati nyinyi; inalingana sawa kuwalingania au kuwanyamazia. Kwani wao hawasikii wala hawaoni wala hawaongozi wala hawaongozwi

    [194] Kwa hakika wale ambao mnawaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, enyi washirikina, wamemilikiwa na Mola wao, kama mlivyomilikiwa nyinyi na Mola wenu. Basi iwapo nyinyi, kama mnavyodai, ni wakweli kwamba wao wanastahiki wafayiwe chochote kile cha ibada, waiteni wawaitikie. Iwapo watawaitikia na watawapatia matakwa yenu, mtakuwa ni wakweli, na isipokuwa hivyo, itakuwa wazi kwamba nyinyi ni warongo mnamzulia Mwenyezi Mungu uzushi mkubwa kabisa

    [195] Je, waungu hawa na masanamu wana miguu ya kutembelea na nyinyi katika haja zenu? Au wao wana mikono ya kuwatetea na kuwanusuru juu ya anayewatakia shari na maovu? Au wao wana macho ya kutazamia, wakapata kuwajulisha yale waliyoyashuhudia na wakayaona miongoni mwa yale yaliyofichika kwenu mkawa hamuyaoni? Au wao wana masikio ya kusikia kwayo, wapate kuwapa habari ya yale msiyoyasikia? Iwapo waungu wenu ambao mnawaabudu hawana vyombo hivi, kuna maana gani kuwaabudu, ilhali wao hawana vitu hivi ambavyo kwavyo kunapelekea kujipatia manufaa au kujiepushia madhara? Waambie, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina wenye kuwaabudu masanamu, «Waiteni waungu wenu ambao mliwafanya ni washirika wa Mwenyezi Mungu katika ibada, kisha kusanyikeni kunifanyia ubaya na maudhi, msinipe muhula na lifanyieni haraka hilo, kwani mimi siwajali waungu wenu kwa kuwa nategemea hifadhi ya Mwenyezi Mungu Peke Yake

    [196] «Hakika mtegemewa wangu ni Mwenyezi Mungu Ambaye Anasimamia kunihifadhi na kunipa ushindi. Yeye Ndiye Ambaye Aliniteremshia Qur’ani kwa haki na Yeye Anawasimamia walio wema miongoni mwa waja wake na anawapa ushindi juu ya maadui zao na Haachi kuwasaidia.»

    [197] Na wale waungu ambao nyinyi mnawaomba, enyi washirikina, badala ya Mwenyezi Mungu, hawawezi kuwanusuru nyinyi wala kuzinusuru nafsi zao

    [198] Na iwapo mtawaita, enyi washirikina, hao waungu wenu kwenye kulingana sawa na haki hawatasikia mwito wenu. Na utawaona, ewe Mtume, waungu wa hawa washirikina miongoni mwa wenye kuabudu mizimu, wanakuelekea kama wanaokutazama na hali wao hawaoni kwa kuwa wao hawana macho wala busara

    [199] Kubali, ewe Nabii, wewe na wafuasi wako kiwango cha kati cha tabia za watu na vitendo vyao, wala usitake kutoka kwao mambo magumu ili wasije wakachukia; na amrisha kwa kila neno jema na kitendo kizuri; na jiepushe na kushindana na mafidhuli na usijisawazishe na wajinga wenye uchache wa akili

    [200] Na iwapo utashikwa na hasira, ewe Nabii, zitokazo kwa Shetani au ukahisi, kutoka kwake, wasiwasi au ulegevu wa kufanya mema au himizo la kufanya ovu, basi tafuta himaya kwa Mola wako kwa kujilinda Kwake. Kwani Yeye ni Msikizi wa kila neno ni Mjuzi wa kila kitendo

    [201] Hakika wale wanaomcha Mwenyezi Mungu miongoni mwa viumbe wake, kwa kuogopa mateso Yake kwa kuzitekeleza faradhi Zake na kuyaepuka makatazo Yake, likiwapata tukio lolote la wasiwasi wa Shetani, wanayakumbuka yale Aliyowalazimisha Mwenyezi Mungu juu yao ya kumtii na kutubia Kwake, na punde si punde wanakomeka na kumuasi Mwenyezi Mungu wakiwa kwenye hoja ya wazi, wenye kufuata amri ya Mwenyezi Mungu na wenye kumuasi Shetani

    [202] Na ndugu wa mashetani, nao ni wapotofu miongoni mwa wapotevu wa wanadamu ambao mashetani wanawasukuma kwenye upotevu na upotofu. Na mashetani wa kijini hawaachi nafasi iwapite katika kuwasukuma kwao mashetani wa kibinadamu kwenye upotofu. Na mashetani wa kibinadamu hawaachi nafasi iwapite katika kuyafanya yale ambayo mashetani wa kijini wanayafanyia ushawishi

    [203] Na usipowajia, ewe Mtume, washirikina hawa na aya wanasema, «Si uitunge na uizue wewe mwenyewe.» Waambie, ewe Mtume, «Hili si langu, na haifai kwangu mimi nilifanye. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu Ameniamuru kufuata wahyi nilioletewa kutoka Kwake. Nao ni hii Qur’ani ninayowasomea, inayokusanya hoja na dalili zinazotoka kwa Mola wenu na yenye ufafanuzi, inayoongoza Waumini kwenye njia iliyolingana sawa, na ni rehema ambayo kwayo Mwenyezi Mungu Anawarehemu waja Wake Waumini

    [204] Na isomwapo Qur’ani isikilizeni, enyi watu, na mnyamaze ili muielewe kwa matarajio kwamba Mwenyezi Mungu Awarehamu kwayo

    [205] Na mtaje Mola wako, ewe Mtume, ndani ya nafsi yako kwa kumnyenyekea Mwenyezi Mungu na kumdhalilikia, hali ya kumcha Yeye moyoni, na umuombe kwa namna ya kati na kati baina ya kutoa sauti na kuifanya chini, katika mwanzo wa mchana na mwisho wake, na usiwe ni miongoni mwa wenye kughafilika kumtaja Mwenyezi Mungu na kupumbaa katika nyakati zao zinginezo

    [206] Hakika wale waliyoko mbele ya Mola Wako miongoni mwa Malaika hawafanyi kiburi kwa kuacha kumuabudu Mwenyezi Mungu, bali wao wanaandama amri Zake, wanamtakasa mchana na usiku na wanamwepusha na mambo yasiyonasibiana na Yeye, na Yeye Peke Yake wanamsujudia

    Nyara

    Surah 8

    [1] Masahaba Zako wanakuuliza, ewe Nabii, kuhusu ngawira siku ya Badr: utawagawia vipi? Waambie, «Jambo lake limeachiwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake» Mtume ndiye mwenye kusimamia ugawaji wake kwa amri ya Mola wake. Basi jikingeni na mateso ya Mwenyezi Mungu wala msithubutu kumuasi, na muache kubishana na kuteta kwa sababu ya mali, na mzitengeneze hali zenu, na mjilazimishe utiifu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake iwapo nyinyi ni Waumini, kwani Imani inapelekea kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake

    [2] Hakika wenye kumuamini Mwenyezi Mungu kikweli ni wale ambao akitajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao zinaingiwa na kicho, wasomewapo aya za Mwenyezi Mungu zinawazidishia Imani pamoja na Imani waliyo nayo kwa kuyazingatia maana yake na kwa Mola wao wanategemea: hawamtaraji isipokuwa Yeye na hawamuogopi isipokuwa Yeye

    [3] Wale ambao wanaendelea kutekeleza Swala zilizofaradhiwa kwa nyakati zake, na katika kile tulichowaruzuku wanatoa kwenye yale tuliyowaamrisha

    [4] Hawa wanaofanya matendo haya ndio wenye kuyaamini kikweli, nje na dani, yale Aliyowateremshia Mwenyezi Mungu, watakuwa na daraja za juu mbele ya Mwenyezi Mungu, msamaha wa dhambi zao na riziki nzuri ambayo ni Pepo

    [5] Na kama mlivyotafautiana juu ya ugawaji wa ngawira, na Mwenyezi Mungu Akauondoa kwenu na Akauweka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, rehema na amani zimshukiye, hivyo ndivyo Mola wako Alivyokuamrisha utoke Madina uende kupambana na msafara wa Makureshi kwa wahyi aliyokujia nao Jibrili, pamoja na kuwa kundi miongoni mwa Waumini walichukia kutoka

    [6] Likawa linabishana na wewe, ewe Nabii, kundi hilo la Waumini kuhusu kupigana baada ya kuonekana wazi kwamba hilo ni lenye kutukia, wakawa kama kwamba wao wanaongozwa kupelekwa kwenye kifo na hali wakikitazama waziwazi

    [7] Na kumbukeni, enyi wabishi, ahadi ya Mwenyezi Mungu kwenu kuwa mtapata ushindi juu ya moja ya mapote mawili: msafara na bidhaa unazozibeba au jeshi la maadui, mpigane nalo na mlishinde. Na nyinyi mnapenda kupata ushindi juu ya msafara badala ya kupigana. Na Mwenyezi Mungu Anataka kuuthibitisha Uislamu na kuukuza kwa kuwaamuru nyinyi kupigana na makafiri na kuwamaliza makafiri kwa kuwaangamiza

    [8] Ili Mwenyezi Mungu Aupe nguvu Uislamu na watu wake na auondoe ushirikina na watu wake ingawa washirikina watalichukia hilo

    [9] Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu kwenu siku ya Badr mlipoomba mpate ushindi juu ya adui yenu, Mwenyezi Mungu Akakubali maombi yenu kwa kusema, «Mimi nitawasaidia kwa Malaika elfu moja kutoka mbinguni wakifuatana hawa baada ya wengine

    [10] Mwenyezi Mungu Hakuufanya msaada huo usipokuwa ni bishara kwenu ya ushindi na ili nyoyo zenu zitulie na muwe na yakini ya kupata ushindi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwani ushindi watoka kwa Mwenyezi Mungu tu, si kwa ukali wa zana zenu na nguvu zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mshindi katika ufalme Wake ni Mwenye hekima katika upelekeshaji Wake na uwekaji sheria Wake

    [11] Kumbukeni pindi Mwenyezi Mungu Alipowatia usingizi, ili kuwapa hisia ya amani ya kutoogopa kwamba adui yenu atawashinda, na kuwateremshia kutoka mawinguni maji safi, ili mjisafishe kwayo na uchafu wa nje na Awaondolee, ndani, wasiwasi na mawazo yanayoletwa na Shetani, na ili Aziimarishe nyoyo zenu kwa kuvumilia kwenye vita, na ili nyayo za Waumini ziwe thabiti zisiteleze kwa kuifanya ngumu ardhi ya mchanga kwa mvua hiyo

    [12] Pindi Mola wako, ewe Nabii, Alipowapelekea wahyi Malaika ambao Mwenyezi Mungu Aliwasaidia nao Waislamu katika vita vya Badr, «Mimi nipo na nyinyi, nawasaidia na kuwahami, watieni hima wale walioamini, nitaweka kwenye nyoyo za waliokanusha kicho kingi, unyonge na utwevu.» Vipigeni, enyi Waumini, vichwa vya makafiri na wapigeni wao kila ncha na kila kiungo

    [13] Hayo yaliyojiri ya kuwapiga makafiri vichwa vyao, shingo zao na ncha zao ni kwa kuwa wao walienda kinyume na amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Na yoyote mwenye kwenda kinyume cha amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, basi Mwenyezi Mungu ni Mkali wa mateso kwake ulimwenguni na Akhera

    [14] Adhabu hiyo niliyoiharakisha kwenu, enyi makafiri mnaoenda kinyume na amri za Mwenyezi Mungu ulimwenguni, ionjeni katika maisha ya kilimwengu, na huko Akhera mtakuwa na adhabu ya Moto

    [15] Enyi wale ambao walimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafuata sheria Yake kivitendo, mpambanapo na waliokanusha katika vita wakawa wanasongea karibu yenu msiwape migongo yenu na mkakubali kushindwa na wao, lakini kuweni imara na wao, kwani Mwenyezi Mungu yuko pamoja na nyinyi na ni Mwenye kuwapa ushindi juu yao

    [16] Na yoyote katika nyinyi atawapa mgongo wake kwenye vita, isipokuwa kwa kupenya kama mbinu ya vita ya kuwachimba makafiri au kujiunga na mjumuiko wa Waislamu waliyo vitani popote waliopo, basi huyo amestahili kukasirikiwa na Mwenyezi Mungu, na makao yake ni Moto wa Jahanamu ambao ni mahali pabaya sana pa kuishia na kukomea

    [17] Nyinyi, enyi Waumini, hamukuwaua washirikina siku ya Badr, lakini Mwenyezi Mungu ndiye Aliwaua, kwa kuwa Aliwasaidia nyinyi kufanya hilo. Na hukurusha uliporusha, ewe Nabii, lakini ni Mwenyezi Mungu Aliyerusha, kwa kuwa Alikifikisha kile ulichokirusha kwenye nyuso za washirikina; na ili Mwenyezi Mungu Awafanyie mtihani wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na Awafikishe kwa sababu ya jihadi kwenye daraja za juu, na Awajulisha wao neema Zake kwao wapate kumshukuru, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, kwa hilo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msikizi wa dua zenu na maneno yenu mliyoyaficha na mliyoyafanya waziwazi, ni Mjuzi wa yenye nafuu kwa waja Wake

    [18] Kitendo hiki cha kuwaua washirikina na kuwarushia waliposhindwa na mtihani mzuri wa kuwapa ushindi Waumini juu ya maadui zao, huo unatoka kwa Mwenyezi Mungu kuja kwa Waumini, na kwamba Mwenyezi Mungu, mbeleni, ni mwenye kuvikosesha nguvu na kuvimaliza vitimbi vya makafiri mpaka wawe wanyonge na wafuate haki au waangamie

    [19] Muombapo, enyi makafiri, kwa Mwenyezi Mungu Ayalete mateso na adhabu Yake kwa wale wenye kupita mipaka na kudhulumu, basi Mwenyezi Mungu Ameshaitikia maombi yenu Alipowaletea mateso Yake yaliyokuwa ni adhabu kwenu na ni mazingatio kwa wacha-Mungu. Na iwapo mtakomeka, enyi makafiri, kumkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na kumpiga vita Nabii Wake, rehema na amani zimshukiye, hilo ni bora kwenu katika ulimwengu wenu na Akhera yenu. Na mkirudi vitani na kumpiga vita Muhammad, rehema na amani zimshukiye, na kuwapiga vita wafuasi wake Waumini, basi tutarudia kuwashinda kama mlivyoshindwa Siku ya Badr. Na hautawafaa mkusanyiko wenu kitu chochote kama ambavyo haukuwafaa siku ya Badr, pamoja na wingi wa idadi yenu na zana zenu na uchache wa idadi ya waumini na zana zao. Na Mwenyezi Mungu yuko pamoja na Waumini kwa kuwasaidia na kuwapa ushindi

    [20] Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, kuweni na utiifu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake katika yale Aliyowaamrisha kwayo na Akawakataza nayo, na msiache kumtii Mwenyezi Mungu na kumtii Mtume Wake na hali nyinyi mnazisikia hoja na dalili zinazosomwa kwenu kwenye Qur’ani

    [21] Wala msiwe, enyi Waumini, katika kwenda kinyume kwenu na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, rehema na amani zimshukiye, ni kama washirikina na wanafiki ambao wakisikia Kitabu cha Mwenyezi Mungu kinasomwa kwao huwa wakisema, «Tumesikia kwa masikio yetu,» na hali wao kwa hakika hawayazingatii wanayoyasikia wala hawayatii akilini

    [22] Hakika waovu zaidi wa wanaotembea kwenye ardhi, miongoni mwa viumbe vya Mwenyezi Mungu, mbele ya Mwenyezi Mungu ni viziwi ambao masikio yao yamezibana kutoisikia haki wakawa hawasikii, mabubu ambao ndimi zao zimeshikwa kutoitamka haki wakawa hawatamki. Hawa ndio wale wasioelewa maamrisho na makatazo yanayotoka kwa Mwenyezi Mungu

    [23] Na lau Mwenyezi Mungu Alijua kwamba ndani ya hawa kuna kheri yoyote Angaliwafanya wasikie mawaidha ya Qur’ani na mazingatio yake mpaka wazifahamu hoja na dalili za Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka. Lakini Yeye Alijua kwamba hamna kheri kwao na kwamba wao hawataamini. Na lau Aliwasikilizisha, kwa kukadiria na kukisia, wangaliipa mgongo Imani kwa kusudi na ujeuri, baada kuielewa. Na wao ni wenye kuipa mgongo, hawazunguki kuitazama haki kwa njia yoyote

    [24] Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu kuwa ni Mola na Muhammad kuwa ni Nabii na ni Mtume, Itikieni mwito wa Mwenyezi Mungu na wa Mtume kwa kumtii awaitapo kwenye haki yenye kuwapa uhai. Kwani katika kuitikia mwito huo kunatengeneza maisha yenu katika ulimwengu na Akhera. Na mjue, enyi Waumini, kwamba Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ndiye Mwenye kuendesha kila kitu na Ndiye Muweza, Anaingilia kati baina ya mtu na kile ambacho moyo wake unakitamani. Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Anayestahiki kuitikiwa Akiwaita, kwani mamlaka ya kila kitu yako mkononi Mwake. Na jueni kwamba nyinyi mtakusanywa kwa Siku isiyo na shaka, ambapo kila mmoja atalipwa kwa analostahili kulipwa

    [25] Na jihadharini, enyi Waumini, na mtihani na mkasa yenye kuwaenea waliofanya makosa na wasiofanya, hawahusishwi nayo wenye maasia wala aliyefanya dhambi; bali yanawapata watu wema pamoja nao iwapo wanaweza kukataza udhalimu wasiukataze. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mkali wa mateso kwa mwenye kwenda kinyume na maamrisho Yake na makatazo Yake

    [26] Na kumbukeni, enyi Waumini, neema za Mwenyezi Mungu juu yenu mlipokuwa ndani ya Maka ni wachache wa idadi mnanyanyaswa, mnaogopa msije mkanyakuliwa na makafiri kwa haraka, Akawapatia makao ya nyinyi kuhamia nayo ni Madina na akawapa nguvu kwa kuwapa ushindi juu yao siku ya Badr na Akawapa vyakula kati ya vitu vizuri ambavyo ngawira ni miongoni mwavyo, ili mumshukuru Yeye kwa alichowaruzuku nacho na kuwaneemesha

    [27] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na makazifuata sheria Zake kivitendo, msimhini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake kwa kuyaacha Aliyowalazimisha nayo na kuyafanya Aliyowakataza nayo, na wala msifanye kasoro katika yale ambayo Mwenyezi Mungu Aliwaamini nayo, na hali nyinyi mnajua kwamba ni amana inayopasa kutekelezwa

    [28] Na mjue, enyi Waumini, kwamba mali yenu ambayo Mwenyezi Mungu Amewapa jukumu la kuyasimamia, na watoto wenu ambao Mwenyezi Mungu Amewapa, ni mtihani kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ni majaribio kwa waja Wake, ili Ajue: watamshukuru kwa neema hizo na kumtii au watashughulika nazo wamsahau Yeye? Na jueni kwamba mbele ya Mwenyezi Mungu kuna heri na thawabu kubwa kwa anayemcha na kumtii

    [29] Enyi wale ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakazifuata sheria Zake kivitendo, mkimuogopa Mwenyezi Mungu, kwa kufanya maamrisho Yake na kuepuka makatazo Yake, Atawafanya muwe na upambanuzi baina ya ukweli na urongo, Atawafutia madhambi yenu yaliyopita na Atawafinikia, Hatawaadhibu kwayo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye hisani na vipewa vyingi vyenye kuenea

    [30] Na kumbuka, ewe Mtume, wanapofanya njama washirikina wa Maka wakufunge au wakuue au wakuhamishe kutoka mjini kwako. Wanakufanyia njama, na Mwenyezi Mungu Aliwarudushia njama zao, ikiwa ni malipo yao, na Mwenyezi Mungu Anafanya njama; na Mwenyezi Mungu ni bora wa wenye kufanya njama

    [31] Na pindi wanaposomewa, hawa ambao walimkanusha Mwenyezi Mungu, aya za Qur’ani tukufu, wao husema kwa ujinga wao na kuikejeli kwao haki, «Tumeshalisikia hili hapo nyuma, na lau tunataka tungalisema maneno yafananayo na hii Qur’ani. Haikuwa Qur’ani hii unayotusomea, ewe Muhammad, isipokuwa ni maneno ya urongo ya watu wa kale

    [32] Na kumbuka, ewe Mtume, neno la washirikina miongoni mwa watu wako wakimuomba Mwenyezi Mungu, «Iwapo hili alilokuja nalo Muhammad ndio haki itokayo kwako, basi tuteremshie mawe kutoka mbinguni au tuletee adhabu inayoumiza.»

    [33] Na hakuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetakata na sifa za upungufu na kutukuka, ni Mwenye kuwaadhibu washirikina hawa na hali wewe, ewe Mtume, uko pamoja nao, na hakuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaadhibu wao na hali wao wanaomba msamaha wa madhambi yao

    [34] Na vipi wao wasistahili adhabu ya Mwenyezi Mungu na hali wao wanawazuia mawalii wake Waumini kutufu Alkaba na kuswali ndani ya msikiti wa H(arām. Na wao hawakuwa ni mawalii wa Mwenyezi Mungu. Mawalii Wake si wengine isipokuwa wale wanaomuogopa Yeye kwa kutekeleza faradhi Alizoziweka na kujiepusha na mambo ya kumuasi. Lakini wengi zaidi wa makafiri hawajui, na kwa hivyo walidai kwamba wana jambo ambalo wasiokuwa wao wana haki nalo zaidi)

    [35] Hakukuwa kuswali kwao kwenye Msikiti wa H(arām isipokuwa ni kupiga mbinja na kupiga makofi, basi onjeni adhabu ya kuuawa na kutekwa siku ya Badr kwa sababu ya kukanusha kwenu na vitendo vyenu ambavyo hakuna mwenye kujitokeza kuvitenda isipokuwa makafiri wenye kukataa upweke wa Mola wao na utume wa Nabii wao)

    [36] Hakika ya wale wenye kukanusha upweke wa Mwenyezi Mungu na wakamuasi Mtume Wake wanatoa mali yao kuwapa washirikina na watu wa upotevu wanaofanana na wao ili kuzuia njia ya Mwenyezi Mungu isifuatwe na kuwazuia Waumini wasimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Basi watatoa mali yao kwa lengo hilo, kisha mwisho wa utoaji wao utakuwa ni majuto na hasara juu yao, kwani mali yao yatamalizika na hawatapata wanaoyatarajia ya kuzima nuru ya Mwenyezi Mungu na kuzuia njia Yake isifuatwe, kisha mwishowe Waumini watawashinda. Na wale waliokufuru watakusanywa wapelekwe kwenye Jahanamu waadhibiwe humo

    [37] Mwenyezi Mungu Atawakusanya na Atawatweza hawa ambao walimkanusha Mola wao na wakatoa mali yao kuwazuia watu kumuamini Mwenyezi Mungu na kuzuia njia Yake isifuatwe, ili Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Apate kukipambanua kichafu na kizuri, na ili Ayakusanye Mwenyezi Mungu mali ya haramu, yaliyotumiwa kuwazuia watu na dini ya Mwenyezi Mungu, Ayaweke baadhi yake juu ya mengine yawe yamekusanyikana na kupandana kisha Ayatie kwenye Moto wa Jahanamu. Makafiri hawa ndio wenye kupata hasara duniani na Akhera

    [38] Sema, ewe Mtume, kuwaambia wale waliokanusha upweke wa Mwenyezi Mungu miongoni mwa Washirikina wa watu wako kwamba watakomeka na ukafiri na kumfanyia uadui Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, na wakarudi kumuamini Mwenyezi Mungu Peke Yake na kutompiga vita Mtume na Waumini, Mwenyezi Mungu Atawasamehe madhambi yaliyopita, kwani Uislamu unafuta yaliyopita. Na watakaporudia washirikina hawa kukupiga vita baada ya tukio ambalo ulipata ushindi juu yao siku ya Badr, basi mwendo wa watu wa mwanzo umetangulia, nao ni kwamba wao wakikanusha na wakaendelea kwenye ukaidi wao, tutawaletea adhabu na mateso kwa haraka

    [39] Na piganeni na washirikina, enyi waumini, mpaka usiweko ushirikina na uzuiliaji wa njia ya Mwenyezi Mungu na kusiabudiwe isipokuwa Mwenyezi Mungu Peke Yake Asiye na mshirika, ili chuki ziwaondokee waja wa Mwenyezi Mungu katika ardhi na mpaka dini, utiifu na ibada vitakasiwe Mwenyezi Mungu tu bila mwingine. Wakiwa watakomeka na kuwafitini Waumini na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na wakawa kwenye dini ya haki pamoja na nyinyi, basi Mwenyezi Mungu hakifichiki Kwake wanachokifanya cha kuacha ukafiri na kuingia kwenye Uislamu

    [40] Na wakiyapa mgongo hawa washirikina yale mliyowaitia, enyi Waumini, ya kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na kuacha kuwapiga vita nyinyi, na wakakataa isipokuwa kuendelea kwenye ukafiri na kuwapiga vita nyinyi, basi kuweni na yakini kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwasaidia na kuwapa ushindi juu yao. Yeye Ndiye bora wa kuwasaidia na kuwapa nyinyi ushindi na wale wenye kujitegemeza Kwake juu ya maadui zenu

    [41] Na jueni, enyi Waumini, kwamba kile mlichokipata kutoka kwa adui yenu kupitia jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, basi mafungu manne kati ya mafungu yake matano yapewe wapiganaji ambao walishiriki vitani, na fungu moja lililosalia kati ya yale mafungu matano litagawanywa sehemu tano: ya kwanza ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume, iwekwe kwenye manufaa ya Waislamu wote; ya pili ni ya jamaa wa karibu na Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, nao ni waliozalikana na Hashim na waliozalikana na Muttalib. Wamwekewa sehemu hiyo ya tano mahali pa sadaka, kwani sadaka si halali kwao. Ya tatu ni ya mayatima; ya nne ni ya masikini, na ya tano ni ya msafiri aliyemalizikiwa na matumizi, iwapo nyinyi mnaukubali upweke wa Mwenyezi Mungu, mnamtii Yeye, ni wenye kuyaamini yale Aliyomteremshia mja Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, miongoni mwa aya, usaidizi na ushindi katika siku Aliyopambanua baina ya haki na upotofu hapo Badr, siku lilipokutana kundi la Waumini na kundi la washirikina. Na Mwenyezi Mungu juu ya kila kitu ni Mwenye uwezo, Hashindwi na chochote

    [42] Na kumbukeni pindi mlipokuwa kwenye upande wa bonde lililokuwa karibu sana na mji wa Madina na maadui zenu wameshukia kwenye upande wa bonde la mbali, na msafara wa biashara upande wenu wa chini unaelekea kwenye ufuo wa Bahari Nyekundu. Na lau kama mungalijaribu kuweka maelewano ya makutano hayo mungalitafautiana, lakini Mwenyezi Mungu Aliwakusanya bila kuagana ili Alipitishe jambo ambalo ililazimu lifanyike kwa kuwaokoa vipenzi Vyake na kuwadhalilisha maadui Wake kwa kuuawa na kushikwa mateka. Na hili lilifanyika ili apate kuangamia mwenye kuangamia kati yao kutokamana na hoja ya Mwenyezi Mungu iliyomthibitikia akaiyona na ikaondoa udhuru wake, na apate kuishi mwenye kuishi kutokamana na hoja ya Mwenyezi Mungu iliyomthibitikia na kujitokeza wazi kwake. Na kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasikia maneno ya makundi mawili hayo, hakifichiki Kwake chochote, ni Menye kuzijua nia zao

    [43] Na kumbuka, ewe Nabii, pindi Mwenyezi Mungu Alipokuonyesha uchache wa maadui zako ukiwa usingizini na ukawajulisha Waumini kuhusu hilo, ndipo nyoyo zao zikapata nguvu na wakawa na ujasiri wa kupigana nao. Na kama Anagalikuonyesha Mola wako wingi wa maadui zako, basi wangalisita Maswahaba wako kupambana nao, na mungalipatwa na uoga na mkatafautiana kuhusu kupigana, lakini Mwenyezi Mungu Aliepusha jambo la nyinyi kushindwa na Akaokoa na mwisho mbaya wa hilo. Hakika Yeye ni Mjuzi mno wa yaliyofichika nyoyoni na maumbile ya nafsi

    [44] Na kumbuka pia pindi walipojitokeza maadui kwenye ardhi ya mapigano mkawaona kuwa ni wachache mkawa na ujasiri juu yao, na Akawafanya nyinyi ni wachache kwenye macho yao, ili waache kujiandaa kupigana na nyinyi, ili Mwenyezi Mungu Alipitishe jambo ambalo hapana budi lifanyike, ili itimie ahadi ya Mwenyezi Mungu kwenu ya himaya na ushindi. Hapo likawa neno la Mwenyezi Mungu ndilo la juu, na neno la wale waliokanusha ndilo la chini, Na kwa Mwenyezi Mungu ndiko marudio ya mambo yote, Apate kumlipa kila mmoja kwa anachostahili kulipwa

    [45] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata sheria Zake kivitendo, mkutanapo na kundi la watu wa ukafiri wakawa wamejitayarisha kupigana na nyinyi, basi thibitini na msishindwe na wao na mumtaje Mwenyezi Mungu kwa wingi, hali ya kuomba na kunyenyekea, Awateremshie ushindi na uwezo wa kumshinda adui yenu, ili mufaulu

    [46] Na mjilazimishe kumtii Mwenyezi Mungu na kumtii Mtume Wake katika hali zenu zote. Wala msitafautiane ikawa ni chanzo cha neno lenu kuwa mbalimabali na nyoyo zenu kutengana, mkaja kuwa madhaifu na nguvu zenu kuondoka na ushindi wenu; na subirini mnapokutana na adui. Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wenye kusubiri, kwa kuwasaidia, kuwapa ushindi na kuwapa nguvu, na Hatawaacha

    [47] Na Msiwe kama mfano wa washirikina ambao walitoka nchini mwao kwa majivuno na kujionyesha ili wawazuie watu wasiingie kwenye dini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu kwa wanayoyafanya ni Mwenye kuyazunguka. Hakifichiki Kwake chochote

    [48] Na kumbukeni pindi Shetani Alipowapambia washirikina yale waliyoyajia na waliyoyakusudia na akawaambia, «Hamuna yoyote Atakayewashinda leo, na mimi ni msaidizi wenu.» Basi yalipopambana makundi mawili: washirikina wakiwa pamoja na Shetani, na Waislamu wakiwa pamoja na Malaika, alirudi nyuma Shetani akaienda zake na akasema kuwaambia washirikina, «Mimi ni mwenye kujitenga na nyinyi; mimi nawaona Malaika msiowaona waliokuja kuwasaidia Waislamu. Hakika mimi namuogopa Mwenyezi Mungu.» Basi akawaacha na akajitenga nao. Na Mwenyezi Mungu ni Mkali wa mateso kwa aliomuasi na asitubiye toba ya kidhati

    [49] Na kumbukeni waliposema watu wenye shaka na unafiki na wagonjwa wa nyoyo, huku wauona uchache wa Waislamu na wingi wa maadui wao, «Imewadanganya hawa Waislamu dini yao, ndipo ikawaingiza kwenye matatizo haya.» Na hawa wanafiki hawakuelewa kwamba mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu na akawa na uhakika wa ahadi Yake, basi Mwenyezi Mungu Hatamuacha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye ushindi, hakuna chochote kinachomshinda, ni Mwenye hekima katika uendeshaji Wake mambo na utengezaji Wake

    [50] Na lau ingalionekana, ewe Mtume, hali ya Malaika ya kuzichukua roho za Makafiri na kuzitoa, na huku wao wanawapiga nyuso zao wakiwaelekea, na wanawapiga migongo yao wakiwakimbia na wanawaambia, «Onjeni adhabu inayounguza», ungaliona jambo kubwa. Na msururu huu wa maneno ingawa sababu yake ni vita vya Badr, lakini unakusanya hali ya kila kafiri

    [51] Malipo hayo ambayo yamewapata nyinyi, enyi washirikina, ni kwa sababu ya matendo yenu maovu katika maisha yenu ya duniani. Na Mwenyezi Mungu hamdhulumu yoyote, kati ya viumbe Wake, kitu chochote hata kadiri ya uzito wa chungu mdogo. Bali Yeye Ndiye Mwamuzi Muadilifu Asiyedhulumu

    [52] Hakika yale yaliyowapata washirikina siku hiyo ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu katika kuwatia adabu wakiukaji mipaka miongoni mwa umma waliotangulia, mfano wa Fir'awn na waliomtangulia, walipowakanusha Mitume wa Mwenyezi Mungu na wakazipinga aya Zake. Kwa hakika Mwenyezi Mungu Aliwateremshia mateso Yake kwa sababu ya madhambi yao. Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Asiyeshindwa, ni Mkali wa mateso kwa aliyemuasi na asitubie kutokana na dhambi zake

    [53] Malipo hayo maovu ni kwamba Mwenyezi Mungu pindi Anapowaneemesha watu neema yoyote, hawaondolei mpaka wabadilishe hali yao njema iwe mbovu, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuzijua hali zao, kwa hivyo huwapitishia yale yaliyolingana na ujuzi Wake na matakwa Yake

    [54] Hali ya Makafiri hawa ni kama hali ya Makafiri wa jamaa za Fir'awn ambao walimkanusha Mūsā, na ni kama hali ya wale waliowakanusha Mitume wao miongoni mwa watu waliopita. Mwenyezi Mungu Aliwaangamiza kwa sababu ya madhambi yao na Akawazamisha jamaa za Fir'awn baharini. Na kila umma kati yao walikuwa wanatenda mambo ambayo haikufaa wao kuyatenda, ya kukanusha kwao Mitume wa Mwenyezi Mungu na kupinga kwao aya za Mwenyezi Mungu na kushirikisha kwao, katika ibada, asiyekuwa Yeye

    [55] Hakika wabaya mno wa wale wanaotembea juu ya ardhi mbele ya Mwenyezi Mungu ni Makafiri wanaoendeleza ukafiri; wao hawawaamini Mitume wa Mwenyezi Mungu, hawaukubali upweke Wake wala hawazifuati sheria Zake

    [56] Miongoni mwa wabaya hao ni Mayahudi ambao waliingia pamoja na wewe katika mapatano kwamba hawatakupiga vita wala hawatamsaidia yoyote dhidi yako, kisha wanazivunja ahadi zao mara kwa mara hali ya kuwa wao hawamuogopi Mwenyezi Mungu

    [57] Pindi utakapopambana na hawa, wanaovunja ahadi na mapatano, katika vita, wape adhabu ambayo itatia kicho kwenye nyoyo za wegine na itaitawanya mikusanyiko yao, huenda wao wakazingatia wasiwe na ujasiri wa kufanya kama yale waliyoyafanya waliotangulia

    [58] Na ukiogopa, ewe Mtume, hiana ambayo ishara zake zimejitokeza, kutoka kwa kundi lolote, basi watupilie mbali ahadi yao, ili zote pande mbili ziwe zimelingana kwa kujua kwamba hapana tena mapatano baada ya leo. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kuenda kinyume na ahadi zao, wavunjaji ahadi na mapatano

    [59] Na wasidhanie wale ambao walizikanusha aya za Mwenyezi Mungu kwamba wao washapita na washaokoka na kwamba Mwenyezi Mungu Hawawezi; hakika wao hawatakwepa adhabu ya Mwenyezi Mungu

    [60] Na Tayarisheni, enyi makundi ya Waislamu,ili kukabiliana na maadui wenu, chochote mkiwezacho cha wingi wa watu na zana, ili muingize, kwa hio, kicho katika nyoyo za maadui wa Mwenyezi mungu na maadui wenu wanaowavizia; na muwatishe wengine ambao uadui wao bado haujajitokeza kwenu hivi sasa, lakini Mwenyezi Mungu Anawajua na Anayajua yale ambayo wanayadhamiria. Na mali yoyote na vinginevyo mnavyovitoa katika njia ya Mwenyezi Mungu, vingi au vichache, Mwenyezi Mungu Atawapa badala yake duniani na Atawaekea thawabu zake mpaka Siku ya Kiyama; na nyinyi hamtapunguziwa malipo ya hayo chochote

    [61] Na wakielekea kuacha vita na wakapendelea kuishi kwa amani na nyinyi, basi nawe elekea huko, ewe Nabii, na uyategemeze mambo yako kwa Mwenyezi Mungu na uwe na imani na Yeye. Hakika Yeye Ndiye Mwenye kuyasikia maneno yao, Mwenye kuzijua nia zao

    [62] Na pindi wakitaka kukufanyia njama, Mwenyezi Mungu Atakukinga na udanganyifu wao. Yeye Ndiye Aliyekuteremshia ushindi na Akakutia nguvu kwa Waumini miongoni mwa Muhājirūn (waliohamia Madina kutoka Maka) na Anṣār (wenyeji wa Madina)

    [63] na Akaziweka pamoja nyoyo zao baada ya utengano, lau ungalitoa mali yaliyoko duniani kote hungaliweza kuziweka pamoja, lakini Mwenyezi Mungu Aliziweka pamoja juu ya Imani wakawa ni ndugu wanaopendana. Hakika Yeye ni Mshindi katika ufalme Wake, ni Mwenye hekima katika mambo Yake na uendeshaji Wake

    [64] Ewe Nabii, hakika Mwenyezi Mungu Atakukinga wewe na Atawakinga wale walio pamoja na wewe shari ya maadui wenu

    [65] Ewe Nabii, wahimize wanaokuamini kupigana vita. Iwapo watapatikana kati yenu watu ishirini wenye kusubiri kwenye kipindi cha kupambana na adui, watawashinda watu mia mbili kati yao. Na iwapo watapatikana kati yenu wapiganaji jihadi mia moja wenye subira, watawashinda Makahri elfu moja, kwa kuwa wao ni watu wasiokuwa na ujuzi na ufahamu wa yale ambayo Mwenyezi Mungu Amewaandalia wapiganaji jihadi katika njia Yake; kwani wao wapigania utukufu katika ardhi na kufanya uharibifu ndani yake

    [66] Sasa hivi Mwenyezi Mungu Amewapunguzia, enyi Waumini, kwa udhaifu mlio nao. Basi ikiwa watakuwako miongoni mwenu watu mia moja wenye subira, watawashinda Makafiri mia mbili. Na iwapo watakuwako kati yenu watu elfu moja, watawashinda watu elfu mbili kati yao kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. Na Mwenyezi Mungu Yuko pamoja na wenye subira kwa msaada Wake na nusura Yake

    [67] Haifai kwa Nabii awe na mateka miongoni mwa maadui wake mpaka aue kwa wingi, ili kutia kicho ndani ya nyoyo zao na aimarishe misingi ya Dini. Mnataka, enyi mkusanyiko wa Waislamu, kwa kuchukuwa kwenu fidia kutoka kwa mateka wa vita vya Badr, starehe ya ulimwenguni, na Mwenyezi Mungu Anataka kuikuza dini Yake ambayo kwayo hupatikana Akhera. Mwenyezi Mungu ni Mshindi Asiyeshindwa, ni Mwingi wa hekima katika sheria Zake

    [68] Lau si Kitabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu chenye mapitisho na Makadirio yaliyotangulia ya kuhalalisha ngawira na kukomboa mateka kwa umma huu, basi ingaliwapata adhabu kubwa kwa kuchukuwa kwenu ngawira na fidia kabla ya kuletwa sheria kuhusu mambo mawili hayo

    [69] Basi kuleni mlichokipata katika ngawira na fidia ya mateka, kwani hiyo ni halali nzuri. Na jilazimisheni na hukumu za Mwenyezi Mungu na sheria Zake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa waja Wake, ni Mwenye huruma nao

    [70] Ewe Nabii, waambie mliowateka siku ya vita vya Badr, «Msisikitike juu ya fidia iliyochukuliwa kutoka kwenu. Iwapo Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Atajua kwamba kwenye nyoyo zenu pana wema, basi Atawapa kilicho bora zaidi kuliko mali yaliyochukuliwa kutoka kwenu, kwa kuwarahisishia nyinyi, kwa hisani Yake, wema mwingi - Mwenyezi Mungu Alitekeleza ahadi Yake kwa 'Abbas, Mwenyezi Mungu Awe radhi naye, na wengineo- na Atawasamehe madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha wa madhambi ya waja Wake wanapotubia, ni Mwenye huruma kwao

    [71] Na wakitaka kukwendea kinyume mara nyingine, wale uliowaacha huru miongoni mwa mateka, basi usikate tamaa. Kwani wao tangu hapo walikuwa wamefanya uhaini kwa Mwenyezi Mungu na wakakupiga vita., na Mwenyezi Mungu Akakupa ushindi juu yao. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani, ni Mwenye hekima katika kuendesha mambo ya waja Wake

    [72] Hakika wale ambao wamemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakazifuata sheria Zake kivitendo, wakahama kwenda kwenye Nyumba ya Uislamu au nchi ambayo wataweza hapo kumuabudu Mola wao, wakapigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali na nafsi, na Wale ambao waliowaweka Wahamiaji katika nyumba zao, wakawaliwaza kwa mali yao nawakaitetea dini ya Mwenyezi Mungu, hao ni wenye kusaidiana wao kwa wao. Ama wale walioamini na wasigure kutoka kwenye Nyumba ya ukafiri, basi nyinyi hamlazimishwi kuwahami na kuwatetea mpaka watakapogura. Na wakifanyiwa maonevu na Makafiri na wakataka msaada wenu, basi wakubalieni, isipokuwa iwapo ni dhidi ya watu ambao kuna makubaliano ya mkazo baina yenu na wao na hawajayavunja. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona matendo yenu, Atamlipa kila mtu kwa kadiri ya nia yake na tendo lake

    [73] Na wale waliokanusha, ni wenye kusaidiana wao kwa wao. Na iwapo hamtakuwa, enyi Waumini, ni wenye kusaidiana nyinyi kwa nyinyi, basi kutapatikana katika ardhi kufitiniwa Waumini na dini ya Mwenyezi Mungu na uharibifu mkubwa wa kuzuiwa njia ya Mwenyezi Mungu na kutiwa nguvu misingi ya ukafiri

    [74] Na wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, wakaacha majumba yao wakaelekea Nyumba ya Uislamu au kwenye nchi ambayo ndani yake watapata utulivu wa kumuabudu Mola wao, wakapigana jihadi kwa kulikuza neno la Mwenyezi Mungu, na wale waliowahami ndugu zao Muhājirūn, wakawapa Makao na wakawaliwaza kwa mali na kwa kuwapa nguvu. Hao basi ndio Waumini wakweli kidhati. Watapata msamaha wa madhambi yao na riziki njema iliyo kunjufu katika mabustani ya Pepo ya starehe

    [75] Na wale walioamini, baada ya hawa Muhājirūn na Anṣār, wakagura na wakapigana jihadi pamoja na nyinyi katika njia ya Mwenyezi Mungu, basi hao ni katika nyinyi, enyi Waumini; wana haki mlizonazo nyinyi na wana majukumu mliyonayo. Na wenye ujamaa, kwenye hukumu ya Mwenyezi Mungu, baadhi yao wanapewa kipaumbele kwa wengine katika kurithiana kuliko Waislamu wa kawaida. Hakika Mwenyezi Mungu kwa kila kitu ni Mjuzi, Anayajua yanayowafaa waja Wake kuhusu kurithiana wao kwa wao kwa ujamaa na nasaba na kutorithiana kwa mapatano ya kujihami na yasiyokuwa hayo miongoni mwa yale yaliyokuwa mwanzo wa Uislamu

    Toba

    Surah 9

    [1] Hili ni elezo la kujiepusha litokalo kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na ni tangazo la kuachana kabisa na makubaliano yaliyokuwako kati ya Waislamu na Washirikina

    [2] Tembeeni, enyi washirikina, katika ardhi muda wa miezi minne, mutembee mnapotaka mkiwa kwenye amani bila kusumbuliwa na Waumini, na mjue kwamba nyinyi hamtayaponyoka mateso. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwatweza Makafiri na ni Mwenye kuwatia aibu hapa ulimwenguni na Moto kesho Akhera. Aya hii inawahusu wale waliokuwa na mapatano huru yasiyokuwa na muda au yule ambaye alikuwa kwenye makubaliano chini ya miezi mine, akamilishiwe miezi yake minne, au aliyekuwa na mapatano akayavunja

    [3] Na ni ujulisho kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ni onyo kwa watu siku ya kuchinja kwamba Mwenyezi Mungu Amejitenga na washirikina; na Mtume Wake pia Amejitenga na wao. Basi ikiwa mtarudi kwenye haki, enyi washirikina, na mkauacha ushirikina wenu, hilo ni bora kwenu. Na mkiipa mgongo haki kwa kutoukubali na mkakataa kuingia kwenye dini ya Mwenyezi Mungu, basi jueni kwamba nyinyi hamtaiponyoka adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na waonye, ewe Mtume, hawa wenye kuupa mgongo Uislamu, adhabu ya Mwenyezi Mungu iumizayo

    [4] Na wanavuliwa, kwenye hukumu iliyopita, washirikina walioingia pamoja na nyinyi kwenye makubaliano yenye muda ujulikanao, na wakawa hawakufanya hiana kwenye mapatano, wala hawakumsaidia yoyote katika maadui, basi watimizie ahadi yao mpaka mwisho wake uliowekwa Hakika Mwenyezi Mungu Anawapenda wachamungu ambao wanatekeleza waliyoamrishwa. Na ogopeni ushirikina na uhaini na maasia mengineyo

    [5] Basi pindi itakapomalizika miezi minne, ambayo ndani yake mliwapa amani washirikina, basi tangazeni vita juu ya maadui wa Mwenyezi Mungu popote walipo, na muwalenge kwa kuwazingira kwenye vituo vyao na muwavizie kwenye njia zao. Na iwapo watarudi nyuma kuacha ukafiri wao, wakaingia kwenye Uislamu na wakajilazimisha na sheria zake za kusimamisha Swala na kutoa Zaka, basi waacheni, kwani wameshakuwa ndugu zenu katika Uislamu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwasamehe waliotubia na wakarudi nyuma, ni Mwenye huruma kwao

    [6] Na pindi yoyote, miongoni mwa washirikina ambao damu zao na mali zao zimehalalishwa, akiomba kuingia kwenye himaya yako, ewe Mtume, na akataka amani, basi mkubalie maombi yake ili apate kuisikia Qur’ani tukufu na auone uongofu wake, kisha mrudishe alikotoka akiwa kwenye usalama. Hilo ni kwa sababu ya kumsimamishia hoja, kwa kuwa Makafiri hawaujui uhakika wa Uislamu, kwani huenda wakauchagua pindi ujinga wao ukiwaondokea

    [7] Haitakikani kwa washirikina wawe na makubaliano, mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, isipokuwa wale mliofanya makubaliano nao kwenye msikiti wa Ḥarām katika mapatano ya Hudaibiyah. Basi wakiendelea kutekeleza makubaliano yenu, na nyinyi endeleeni na wao kama hivyo. Hakika Mwenyezi Mungu Anawapenda wenye kumuogopa Mwenyezi Mungu, wenye kutekeleza ahadi zao

    [8] Tabia ya Makafiri ni kujilazimisha na makubaliano iwapo ushindi uko kwa wengine wasiokuwa wao. Lakini wakijihisi kuwa wana nguvu juu ya Waumini, basi wao hawachungi ujamaa wala makubaliano. Basi msidanganyike na vile wanavyowafanyia wawapo na kicho na nyinyi. Kwani wao wanawaambia maneno kwa ndimi zao ili mridhike na wao, lakini nyoyo zao zinakataa hilo. Na wengi wao ni wenye kuupiga vita Uislamu, ni wenye kuvunja ahadi

    [9] Wameziacha aya za Mwenyezi Mungu na wakachukua badala yake vitu vya kilimwengu vilivyo duni, wakaipa mgongo haki na wakawazuia wale wanaotaka kuingia kwenye Uislamu wasiingie. Ni jambo ovu walilolifanya na ni kitendo cha kuchukiza walichokitenda

    [10] Washirikina hawa wako kwenye vita dhidi ya Imani na watu wake, hawauekei uzito wowote ujamaa wa Muumini wala mapatano yake; walilonalo wao ni uadui na udhalimu

    [11] Na iwapo watakomeka na ibada ya asiyekuwa Mwenyezi mungu, wakalitamka neno la kumpwekesha, wakajilazimisha na sheria za Kiislamu za kusimamisha Swala na kutoa Zaka, basi hao ni ndugu zenu katika Uislamu. Na tunazieleza waziwazi aya na kuzifafanua kwa watu wenye kufaidika nazo

    [12] Na iwapo washirikina hawa watayavunja makubaliano ambayo mliyowekeana ahadi nao na wakaitukana dini ya Uislamu waziwazi, basi wapigeni vita, kwani wao ni viongozi wa upotevu, hawana ahadi wala dhamana, mpaka wakomeke na ukafiri wao na uadui wao juu ya Uislamu

    [13] Msiwe kwenye hali ya kutoamua kuhusu kupigana na hawa watu ambao walivunja ahadi zao na wakafanya hima kumtoa Mtume kutoka Maka, na wao ndio walioanza kuwaudhi hapo mwanzo. Je mnawaogopa? Au mnaogopa kupambana nao vitani? Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye haki zaidi ya nyinyi kumuogopa, iwapo kweli nyinyi ni Waumini

    [14] Enyi mkusanyiko wa Waumini,piganeni vita na maadui wa Mwenyezi Mungu, kwani Aliyetukuka na kushinda Atawaadhibu wao kwa mikono yenu na Atawafanya wanyonge kwa kushindwa na kutwezwa, Atawanusuru juu yao, Ataliinua neno Lake, Atavipoza, kwa kushindwa kwao, vifua vyenu ambavyo kwa muda mrefu viliingiwa na sikitiko na kero kutokana na vitimbi vya washirikina hawa

    [15] Na Ataziondoa hasira kwenye nyoyo za Waumini. Na yoyote mwenye kutubia, miongoni mwa wajeuri hawa, basi Mwenyezi mungu Humkubalia toba amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa ujuzi wa ukweli wa toba ya mwenye kutubia, ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji Wake mambo, utengenezaji Wake na sheria Zake Alizowaekea waja Wake

    [16] Ni katika mipango ya Mwenyezi Mungu kuwajaribu waja Wake. Basi msidhani, enyi mkusanyiko wa Waumini, kwamba MwenyeziMungu Atawaacha bila ya mtihani ili Apate kuwajua, ujuzi uliyofunuka wazi kwa viumbe, waja Wake ambao wamemtakasia Mola wao katika jihadi yao na hawakuwafanya wasiokuwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na Waumini kuwa ni washauri na marafiki. Na Mwenyezi Mungu ni Mtambuzi wa vitendo vyenu vyote na Atawalipa kwa vitendo hivyo

    [17] Si katika mambo ya washirikina kuziamirisha Nyumba za Mwenyezi Mungu huku wao wanautangaza ukafiri wao wa kumkanusha Mwenyezi Mungu na wanamfanya kuwa Ana washirika. Washirikina hawa, Siku ya Kiyama, vitendo vyao vyote vitaharibika na mwisho wao ni kukaa milele Motoni

    [18] Hawawi na hamu ya kujishughulisha na Nyumba za Mwenyezi Mungu na kuziamirisha. isipokuwa wale ambao wanamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, wanasimamisha Swala, wanatoa Zaka na hawaogopi, kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, lawama ya yoyote mwenye kulaumu. Hawa waamirishaji ndio waongofu wa njia ya haki

    [19] Mnayafanya, enyi watu, yale mnayoyasimamia ya kuwanwyesha mahujaji na kuuamirisha msikiti wa Ḥarām ni kama Imani ya aliyemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na akapigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu? Haziwi sawa hali za Waumini na hali za makafiri mbele ya Mwenyezi Mungu, kwani Mwenyezi Mungu halikubali tendo lolote bila ya Imani. Na Mwenyezi Mungu hawaelekezi watu wanaozidhulumu nafsi zao kwa ukafiri kwenye mambo mema

    [20] Wale waliomuamini Mwenyezi Mungu, wakaiacha Nyumba ya ukafiri wakielekea kwenye Nyumba ya Uislamu na wakatoa mali zao na nafsi zao katika jihadi ili kulikuza neno la Mwenyezi Mungu. Hawa wana daraja kubwa mno kwa Mwenyezi Mungu, na wao ndio wenye kufaulu kuzipata radhi Zake

    [21] Hakika Waumini hawa waliohama wana habari njema kutoka kwa Mola wao za rehema kunjufu na radhi ambayo hapatakuwa na hasira baada yake; na mwisho wao ni kwenda kwenye mabustani ya Pepo ya milele na neema zisizokoma

    [22] Hali ya kukaa kwenye mabustani hayo ya Pepo neema hizo kikao kisicho na kikomo. Na hayo ni malipo ya yale waliyoyatanguliza ya utiifu na vitendo vyema katika maisha yao ya ulimwenguni. Hakika Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ana malipo makubwa kwa aliyeamini na akafanya mema kwa kuzifuata amri Zake na kuyaepuka Makatazo Yake

    [23] Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Yake kivitendo, msiwafanye jamaa zenu, miongoni mwa kina baba, watoto na wengineo, kuwa ni marafiki (mnaowategemea) mkawa mnawasambazia siri za Waislamu na mnawataka ushauri katika mambo yenu, iwapo bado wako kwenye ukafiri na kuufanyia uadui Uislamu. Na yoyote atakayewafanya wao kuwa ni marafiki na akawapa mapenzi, atakuwa amemuasi Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na ameidhulumu nafasi yake dhuluma kubwa

    [24] Sema, ewe Mtume, kuwaambia Waumini, «Iwapo mtawafanya kina baba, watoto, ndugu , wake na jamaa wa karibu, mali mlizozikusanya, biashara ambazo mnaogopa zisikose soko na majumba yanayopendeza ambayo mumekaa ndani yake, (iwapo mtayafanya hayo) ni bora kuliko kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na jihadi katika njia Yake, basi yangojeni mateso ya Mwenyezi Mungu na adhabu Yake kwenu. Na Mwenyezi Mungu hawapi taufiki wenye kutoka nje ya utiifu Wake

    [25] Hakika Mwenyezi Mungu Amewasaidia kwa kuwapa ushindi katika matukio ya vita mengi mlipozishikilia sababu za ushindi na mkamtegemea Mwenyezi Mungu. Na siku ya vita vya Hunayn mlisema, «Hatutashindwa leo kwa uchache.» Hapo wingi wenu ukawadanganya usiwafae, na adui yenu akawalemea msipate pa kukimbilia kwenye ardhi iliyo pana, mkakimbia katika hali ya kushindwa

    [26] Kisha Mwenyezi Mungu Alimteremshia utulivu Mtume Wake na Waumini wakasimama imara, na Mwenyezi Mungu Akawaongezea askari wasiowaona miongoni mwa Malaika. Hapo Aliwapa ushindi juu ya adui yao na akawaadhibu wale waliokufuru. Hayo ni mateso ya Mwenyezi Mungu kwa wenye kuzuia dini ya Mwenyezi Mungu isifuatwe, wenye kuwakanusha Mitume Wake

    [27] Na atakayerudi nyuma akaacha ukafiri wake baada ya hilo, na akaingia kwenye Uislamu, basi Mwenyezi Mungu Anaikubali toba ya Anayemtaka katika wao na Anamsamehe dhambi zake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, ni mwingi wa kurehemu

    [28] Enyi mkusanyiko wa Waumini, hakika washirikina ni najisi na ni wachafu, hivyo basi msiwape nafasi kusongea kwenye eneo la Ḥarām baada ya mwaka huu wa tisa wa hijria (kalenda ya Kiislamu). Na iwapo mtachelea umasikini, kwa kukatikiwa na biashara zao, Mwenyezi Mungu Atawapa badala yake na Atawatosheleza kwa fadhila Zake Atakapo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi mno wa hali zenu, ni Mwingi wa hekima katika kuyapeleka mambo yenu

    [29] Enyi Waislamu, wapigeni vita Makafiri ambao hawamuamini Mwenyezi Mungu, wala hawaamini Kufufuliwa na Kulipwa, wala hawajiepushi na yale ambayo Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wameyakataza, wala hawajilazimishi na hukumu za sheria ya Uislamu, miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara, mpaka watoe jizia, ambayo nyinyi mnawalazimisha nayo, kwa mikono yao wakiwa wanyenyekevu na wanyonge

    [30] Hakika wamemshirikisha Mwenyezi Mungu Mayahudi walipodai kwamba 'Uzayr ni mwana wa Mwenyezi Mungu. Na wamemshirikisha Mwenyezi Mungu Wanaswara walipodai kwamba Al-Masīh( ni mwana wa Mwenyezi Mungu, Neno hili wamelizua wao wenyewe, na wao kwa hili wanafananisha na neno la washirikina kabla yao. Mwenyezi Mungu Awalaani washirikina wote. Vipi wao wajiepusha na ukweli na kuelekea kwenye urongo)

    [31] Mayahudi na Wanaswara wamewafanya wanavyuoni na watu wema kuwa ni waola wenye kuwaekea hukumu za sheria, wakawa wanajilazimisha kuzifuata na wanaacha sheria za Mwenyezi Mungu. Na pia walimfanya Al- Masīḥ, 'Īsā mwana wa Maryam, kuwa ni mungu, wakamuabudu. Na hakika Mwenyezi Mungu Amewaamrisha wao wamuabudu Yeye Peke Yake, bila ya mwingine. Yeye Ndiye Mungu wa haki. Hakuna mungu anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye. Amejiepusha na Ametakasika na kila kile wanachokizua watu wa ushirikina na upotevu

    [32] Makahfiri, kwa kukanusha kwao, wataka kuutangua Uislamu na kuzitangua hoja za Mwenyezi Mungu na dalili Zake, juu ya upweke Wake, Alizokuja nazo Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye. Na Mwenyezi Mungu Anakataa isipokuwa kuikamilisha dini Yake na kuipa nguvu, na kuliinua neno Lake, hata kama wenye kukanusha watalichukia hilo

    [33] Yeye Ndiye Aliyemtumiliza Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, kwa Qur’ani na dini ya Uislamu, ili Aifanye kuwa juu ya dini zote, ingawa washirikina wanaichukia dini ya haki-Uislamu- na kushinda kwake dini nyingine

    [34] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata sheria Zake kivitendo, hakika wengi wa wanavyuoni wa watu waliopewa Vitabu na watu wema wao wanakula mali za watu kwa njia isiyokuwa ya haki, kama hongo na vinginevyo, na wanakataza watu wasiingie kwenye Uislamu na wanazuia njia ya Mwenyezi Mungu isifuatwe. Na wale wanaozuia mali wakawa hawatekelezi Zaka zake wala hawatoi katika mali hizo haki za lazima, basi wape bishara ya adhabu iumizayo

    [35] Siku ya Kiyama yatawekwa mapande ya dhahabu na fedha kwenye Moto, na yataposhika moto sana, watachomwa nayo, hao wenyewe, nyuso zao, mbavu zao na migongo yao. Na wataambiwa kwa kuwaumbua, «Haya ndiyo mali yenu mliyoyakumbatia na mkazuia, katika mali hayo, haki za Mwenyezi Mungu. Basi onjeni adhabu iumizayo, kwa sababu ya kukusanya kwenu na kuzuia

    [36] Hakika idadi ya miezi, katika hukumu ya Mwenyezi Mungu na kulingana na ilivyoandikwa kwenye al-Lawḥ al-Maḥfūẓ (Ubao Uiohifadhiwa), ni miezi kumi na mbili, tangu siku Aliyoumba mbingu na ardhi. Kati ya hiyo, kuna minne mitakatifu ambayo Mwenyezi Mungu Ameharamisha ndani yake kupigana. Nayo ni Mfungopili, Mfungotatu, Mfungone na Rajabu. Hiyo ndyo Dini iliyolingana sawa. Basi ndani ya miezi hiyo msizidhulumu nafsi zenu, kwa kuwa uharamu wake umeongezwa. Na kwa kuwa kudhulumu katika miezi hiyo ni kubaya zaidi kuliko katika miezi mingineyo, haina maana kwamba kudhulumu katika miezi mingine kunaruhusiwa. Na wapigeni vita washirikina wote kama wanavyowapiga vita nyote. Na mjue kwamba Mwenyezi Mungu Yuko pamoja na wenye taqwā (uchajimungu) kwa msaada Wake na nusura Yake

    [37] Hakika yale Waarabu walikuwa wakiyafanya katika kipindi cha ujinga kwa kuiharamisha miezi minne kila mwaka, kwa idadi na sio kwa kuyataja majina ya miezi iliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu, wakawa waichelewesha baadhi yake au waitanguliza, na wakaiweka badala yake miezi ya uhalali kama wanavyotaka, kulingana na mahitaji yao ya kupigana. Hakika hayo ni katika kuzidisha ukafiri. Shetani anawapoteza kwa hayo wale waliokufuru : wanauhalalisha ule waliouchelewesha kuuharamisha kati ya miezi minne mwaka huu, na wanauhalalisha mwaka mwingine, ili walinganishe kiwango cha miezi minne, wapate kuihalalisha Aliyoiharamisha Mwenyezi Mungu kati ya hiyo. Shetani amewapambia vitendo viovu. Na Mwenyezi Mungu Hawaafikii watu Makafiri kufuata haki na usawa

    [38] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na Mkafuata sheria Zake kivitendo, mna nini nyinyi pindi mkiambiwa, «Tokeni mwnde jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu ili mkapigane na maadui wenu,» mnafanya uvivu na mnajikalia majumbani mwenu? Je mnapendelea mafungu yenu ya starehe za kilimwengu kuliko neema za kesho Akhera? Basi kile mnachostarehe nacho ulimwenguni ni kichache chenye kuondoka. Ama neema za Akhera ambazo Mwenyezi Mungu Ameziandalia Waumini ni nyingi zenye kudumu

    [39] Iwapo hamtatoka, enyi Waumini, kwenda kupigana na adui yenu , Mwenyezi Mungu Atawateremshia mateso Yake na atawaleta watu wengine ambao watatoka kwenda vitani waambiwapo watoke, watamtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Na nyinyi hamtamdhuru Mwenyezi Mungu chochote kwa kuikimbia kwenu jihadi, kwani Yeye ni mwenye kujitosheleza na nyinyi, na nyinyi ndio wahitaji Wake. Na Analolitaka Mwenyezi Mungu litakuwa hapana budi. Na Mwenyezi Mungu, juu ya kila kitu, ni Muweza, miongoni mwa kutetea dini Yake na Mtume Wake pasi na nyinyi

    [40] Enyi mkusanyiko wa Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, msipotoka pamoja na yeye anapowataka mtoke, na msipomtetea, basi Mwenyezi Mungu Alimsaidia na kumtetea siku ile Makafiri wa Kikureshi walipomtoa kwenye mji wake wa Maka, na yeye ni wapili kati ya wawili( yeye na Abu Bakr al-Siddiq, radhi ya Mwenyezi Mungu imshukiye) wakawafanya ibidi waingie pangoni katika jabali la Thawr, wakakaa humo siku tatu, pindi alipomwambia rafiki Yake Abu Bakr, alipomuona ameingiwa na kicho juu yake, «Usihuzunike, Mungu Yupo pamoja na sisi» kwa kutunusuru na kutupa nguvu. Hapo Mwenyezi Mungu Aliteremsha utulivu kwenye moyo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani imshukiye, na akamsaidia kwa askari ambao hakuna aliowaona kati ya wanadamu, nao ni Malaika. Hapo Mwenyezi Mungu Alimuokoa na adui yake, Akawafanya wanyonge maadui wake, Akalifanya neno la waliokanusha ndilo la chini na neno la Mwenyezi Mungu ndilo la juu. Na hilo ni kwa kuliinua juu jambo la Uislamu. Na Mwenyezi Mungu ni Mshindi katika ufalme Wake, ni Mwingi wa hekima katika kuyaendesha mambo ya waja Wake. Katika aya hii pana kitambulisho cha cheo cha Abu Bakr, radhi ya Mwenyezi Mungu zimshukie

    [41] Tokeni, enyi Waumini, kwenda kwenye jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, vijana kwa wazee, katika uzito na wepesi, vyovyote mtakavyokuwa, mtoe mali zenu katika njia ya Mwenyezi Mungu na mupigane kwa mikono yenu ili kulitangaza neno la Mwenyezi Mungu. Kutoka huko na kupigana huko ni bora kwenu katika hali zenu za sasa na za baadaye kuliko kuwa wazito, kuacha kutoa na kujikalisha nyuma. Basi iwpo nyinyi ni miongoni mwa walio na ujuzi wa ubora wa jihadi na thawabu zake mbele ya Mwenyezi Mungu, fanyeni mliyoamrishwa na muitikie mwito wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake

    [42] Mwenyezi Mungu, uliotukuka utukufu Wake, Ameliumbua kundi la wanafiki waliomtaka ruhusa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, ya kusalia nyuma na kutoenda kwenye vita vya Tabūk, kwa kueleza kwamba lau kutoka kwao kulikuwa ni kwa kuandama ngawira ya karibu iliyo nyepesi kuipata, wangalikuandama. Lakini walipoitwa kwenda kupigana na Warumi pambizoni mwa miji ya Shām katika kipindi cha joto, walitiana uvivu na wakajiweka nyuma. Na watatoa nyudhuru za kusalia kwao nyuma na kuacha kutotoka wakiapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba wao hawaliwezi hilo; wanaziangamiza nafsi zao kwa urongo na unafiki, na hali kwamba Mwenyezi Mungu yuwajua kuwa wao ni warongo katika zile nyudhuru zao wanazozitoa

    [43] Mwenyezi Mungu Amekusamehe, ewe Nabii, kwa yale yaliyotokea kwako, ya kuliacha lililo bora zaidi na la ukamilifu zaidi, nayo ni yale ya kuwaruhusu wanafiki kukaa wasiende kwenye jihadi. Ni kwa nini uwaruhusu hawa wakae wasiende vitani, usingojee mpaka wakufunukie waziwazi wale waliosema kweli katika kutaja nyudhuru zao na uwajue warongo miongoni mwao katika hilo

    [44] Si katika misimamo ya wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na Siku ya Mwisho kukutaka ruhusa, ewe Nubii, ya kusalia nyuma kwa kutoshiriki kwenye jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa nafsi na mali. Hiyo ni misimamo ya wanafiki tu. Na Mwenyezi Mungu Anamjua Anayemuogopa Yeye na kumcha kwa kuzitekeleza faradhi Zake na kujitenga na Makatazo Yake

    [45] Kwa hakika wanaoomba ruhusa ya kusalia nyuma kutoenda kwenye jihadi ni wale ambao hawamuamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho wala hawafanyi mema, na nyoyo zao zimekuwa na shaka kuhusu usahihi wa uliyokuja nayo, ewe Nabii, ya Uislamu na sheria zake. Wao wako kwenye shaka yao wanashangaa

    [46] Na lau wanafiki walitaka kutoka pamoja na wewe, ewe Nabii, kwenye jihadi, basi wangalijiandaa kwa matayarisho ya vyakula na vipando. Lakini Mwenyezi Mungu Amechukia kutoka kwao, ndipo ikawa ni uzito kwao kutoka, kwa mapitisho na Makadirio Yake, ingawa kisheria Amewaamrisha, na wakaambiwa, «Bakieni nyuma pamoja na waliokaa miongoni mwa wagonjwa, madhaifu, wanawake na watoto.»

    [47] Lau wanafiki wangalitoka pamoja na nyinyi, enyi Waumini, kwenye jihadi, wangalieneza mgongano katika safu zenu, ubaya na uharibifu, na wanagalikimbilia kueneza fitina na chuki baina yenu, kwa lengo la kutaka kuwafitini kwa kuwazorotesha msipigane jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Na katika nyinyi, enyi Waumini, kuna wapelelezi wa makafiri, wanazisikia habari zenu na wanazipeleka kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi mno wa wanafiki walio madhalimu na Atawalipa kwa hilo

    [48] Walipendelea wanafiki kuwafitini Waumini na Dini yao na kuwazuia wasiiifuate njia ya Mwenyezi Mungu kabla ya vita vya Tabūk, na mambo yao yakafunuka wakajulikana. Na walikuchafulia mambo, ewe Nabii, katika kuyavunja uliyokuja nayo, kama walivyofanya siku ya vita vya Uḥud na siku ya vita vya Khandaq. Na walikufanyia vitimbi mpaka usaidizi ukaja kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Akawatia nguvu askari Wake na Akaipa ushindi dini Yake, pamoja na kuwa wao wanaichukia

    [49] Miongoni mwa wanafiki hawa, kuna wale wanaoomba ruhusa ya kuketi wasiende kwenye jihadi na wanasema, «Usiniingize kwenye mtihani utakaonifikia, katika hali ya kutoka, wa fitina ya kuvutiwa na wanawake.» Hakika wanafiki hawa wameanguka kwenye fitina kubwa ya unafiki. Na kwa hakika, Moto wa jahanamu ni wenye kuwazunguka wanaomkanusha Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho; hakuna atakayeponyoka

    [50] Ewe Nbii! Unapofikiwa na furaha na ngawira, wanafiki wanasikitika, na unapopatwa na kero la kushindwa au matatizo, wanasema,»Sisi ni wenye busara na uhodari wa kupanga, tulijipangia kwa maslahi yetu kubakia nyuma na kutomfuata Muhammad.» Na hapo wanaondoka hali ya kuwa na furaha kwa waliyoyafanya na kwa mabaya yaliyokufika

    [51] Sema, ewe Nabii, uwaambie hao wanaovunja moyo kwa kujitoa, kwa kuwakemea na kuwaumbua, «Hakuna litakalotupata isipokuwa lile Alilolipitisha Mwenyezi Mungu juu yetu na Aliloliandika katika al-Lawḥ al-Maḥfūẓ (Ubao Uliohifadhiwa). Yeye Ndiye Mwenye kutupa ushindi juu ya maadui wetu.» Na kwa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, na wajitegemeze wale wanaoumuamini

    [52] Waambie, ewe Nabii, «Kwani kuna mnachokitazamia kwetu isipokuwa tufe mashahidi au tuwashinde? Na sisi tunatazamia kwenu kwamba Mwenyezi Mungu Atawapatia mateso ya haraka yanayotoka Kwake yawaangamize, au yanayotokana na mikono yetu tuwaue. Basi ngojeeni, na sisi tunalingojea, pamoja na nyinyi, lile ambalo Mwenyezi Mungu ni Mwenye kulifanya kwa kila kundi kati yetu na nyinyi.»

    [53] Sema, ewe Nabii, kuwaambia wanafiki, «Toeni mali zenu vile mtakavyo na namna mtakavyo, kwa hiari yenu au kwa kulazimishwa, Mwenyezi Mungu hatavikubali kutoka kwenu mnavyovitoa, kwa kuwa nyinyi ni watu mliotoka kwenye dini ya Mwenyezi Mungu na utiifu Kwake

    [54] Na sababu ya kutokubaliwa wanavyovitoa ni kwamba wao wameficha ukanushaji wao Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, na ukataaji wao ukweli wa Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kwamba wao hawaendi kuswali isipokuwa huku wanaona uzito, na kwamba hawatoi mali yao isipokuwa huku wao ni wenye kuchukia hilo. Wao hawana matarajio ya kupata malipo ya faradhi hizi wala hawaogopi mateso kwa kuziacha kwa ukafiri wao walionao

    [55] Zisikushangaze, ewe Nabii, mali za wanafiki hawa wala watoto wao. Hakika Mwenyezi Mungu Anataka kuwaadhibu kwa hizo hapa ulimwenguni, kwa tabu ya kuzipata na kwa mikasa inayozifikia kwa kuwa yatokeyapo hayo hawatarajii malipo mema kwa Mwenyezi Mungu, na zitoke nafsi zao wapate kufa juu ya kumkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake

    [56] Na wanawaapia wanafiki hawa, enyi Waumini, kwa urongo na ubatili, kwamba wao ni katika nyinyi, wala wao kamwe si katika nyinyi. Lakini wao ni watu waoga, wanaapa kwa kujikinga na nyinyi

    [57] Lau wanafiki hawa wapata mahala pa usalama na ngome ya kuwahifadhi, au pango kwenye jabali litakalowapa makao au handaki ndani ya ardhi itakaowaokoa na nyinyi, basi wangalikwenda huko mbiombio

    [58] Na miongoni mwa wanafiki, kuna wale wanaokutia kombo katika kugawanya sadaka: wapatapo fungu wanaridhika na wananyamaza, na wasipobahatika kupata fungu wanakukasirikia na kukuumbua

    [59] Na lau hawa wanaokutia kombo katika ugawaji wa sadaka waliridhika na kile ambacho Mwenyezi Mungu na Mtume Wake waliwagawia na wakasema, «Mwenyezi Mungu Ndiye Anayetutosha. Mwenyezi Mungu Atatupa kutokana na nyongeza Zake, na Mtume Wake atatupa kutokana na kile Mwenyezi Mungu Alichompa. Sisi tuna hamu Mwenyezi Mungu Atukunjulie na Atukwasishe tusihitajie sadaka wala tusichukue sadaka za watu.» Lau walifanya hivyo, ingalikuwa bora na yenye manufaa zaidi kwao

    [60] Zaka za lazima zinapewa wahitaji wasiomiliki kitu, masikini wasiomiliki kiwango kinachowatosha kwa mahitaji yao, wenye kuzishughulikia kwa kuzikusanya,wale ambao mwazizoeza nyoyo zao, miongoni mwa wale mnaotarajia wasilimu au ipate nguvu Imani yao au wawe na manufaa kwa Waislamu au mzuie kwazo madhara ya mtu yoyote yasiwafikie Waislamu. Pia zinatolewa katika kuacha huru watumwa na wale wenye mikataba ya uhuru. Na zinatolewa kupewa wenye kuingia kwenye madeni kwa sababu ya kuleta maelewano baina ya watu na wenye kulemewa na madeni waliyokopa kwa lengo lisiliokuwa la uharibifu au utumiaji wa kupita kiasi kisha wakashindwa kulipa. Na zinapewa wapiganaji katika njia ya Mwenyezi Mungu. Na zinapewa msafiri aliyeishiwa na matumizi. Ugawaji huu ni lazima Aliyoifaradhia Mwenyezi Mungu na Akaikadiria. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi mno wa mambo yanayowafaa waja Wake, ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji mambo Wake na sheria Zake

    [61] Miongoni mwa wanafiki kuna watu wanaomkera Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa maneno na wanasema, «Yeye anasikiliza kila aambiwalo na analiamini.» Waambie, «Muhammad ni sikio linalosikiliza kila jema. Anamuamini Mwenyezi Mungu na anawasadiki Waumini kwa yale wanayomwambia. Na yeye ni rehema kwa aliyemfuata na akaongoka kwa uongofu Wake. Na wenye kumkera Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, kwa namna yoyote ya kumkera, watakuwa na adhabu yenye kuumiza

    [62] Wanafiki wanaapa viapo vya urongo na wanatoa nyudhuru za kupanga ili kuwafanya Waumini waridhike na wao. Na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wanastahiki zaidi na inafaa zaidi wawaridhie kwa kuwaamini na kuwatii, iwapo kweli wao ni Waumini

    [63] Kwani hawakujua wanafiki hawa kwamba mwisho wa wale wanaompiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume Wake ni Moto wa Jahanamu, watakuwa na adhabu kali ndani yake? Mwisho huo ndio utwevu na unyonge mkubwa. Na miongoni mwa kupiga vita kwao huko ni kumkera Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, kwa kumtukana na kumtia kombo; Mwenyezi Mungu Atulinde na hilo

    [64] Wanafiki wanaogopa kuteremshwa sura kuhusu wao, yenye kuwapa habari ya ukafiri waliyouficha ndani ya nyoyo zao. Waambie, ewe Nabii, Endeleeni juu ya yale ambayo muko nayo ya kufanya shere na masihara. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuutoa nje ukweli wa yale mliokuwa na hadhari nayo

    [65] Na lau unawauliza, ewe Nabii, kuhusu yale matukano waliyokutukana wewe na Maswahaba zako watasema, «Sisi tulikuwa tukizungumza maneno bila kuyakusudia. Waambie, ewe Nabii, «Je ni Mwenyezi Mungu mlikuwa mkimcheza shere na aya Zake na Mtume Wake?»

    [66] Msitoe sababu, enyi mkusanyiko wa wanafiki! Kwani hakuna faida ya kutoa udhuru kwenu. Hakika mumekufuru kwa maneno haya mliyoyafanyia shere. Iwapo tutalisamehe kundi miongoni mwenu lililotaka msamaha na likatubia kidhati, tutaliadhibu kundi la watu wengine kwa sababu ya uhalifu wao wa kusema maneno haya maovu ya makosa

    [67] Wanafiki wa kiume na wanafiki wa kike ni aina moja katika kutangaza kwao Imani na kuficha kwao ukafiri. Wanaamrisha kukufuriwa Mwenyezi Mungu na kuasiwa Mtume Wake, na wanakataza Imani na utiifu, na wanaizuia mikono yao kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu. Wamemsahau Mwenyezi Mungu na kwa hivyo hawamtaji, na Yeye Amewasahau na rehema Yake hakuwaelekeza kwenye wema. Hakika wanafiki ndio waliotoka nje wakaacha kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake

    [68] Mwenyezi Mungu Amewaahidi wanafiki wa kiume na wanafiki wa kike na Makafiri kwamba mwisho wao ni kwenda kwenye Moto wa Jahanamu, wakae humo milele kabisa. Moto huo ni wenye kuwatosha, ukiwa ni mateso yao kwa kumkanusha kwao Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu Amewafukuza kwenye rehema Yake. Na watakua na adhabu ya daima

    [69] Hakika vitendo vyenu, enyi wanafiki, vya kucheza shere na ukafiri ni kama vitendo vya watu waliotangulia, waliokuwa na nguvu nyingi na mali na watoto zaidi kushinda nyinyi, wakajimakini na maisha ya kilimwengu, wakasterehe na vitu na ladha zilizomo. Basi na nyinyi, enyi wanafiki, mumestarehe kwa sehemu yenu ya matamanio yenye kumalizika kama starehe ya waliokuwa kabla yenu kwa mafungu yao ya vitu vya kilimwengu venye kumalizika. Na mumejiingiza katika kumzulia Mwenyezi Mungu urongo kama walivyojiingiza wale watu waliokuwa kabla yenu. Hao wenye kusifiwa kwa tabia hizi, ndio wale ambao mema yao yameondoka duniani na Akhera. Na wao ndio wenye kupata hasara kwa kuuza kwao sterehe za Akhera kwa vyeo na starehe za ulimwenguni

    [70] Kwani haikuwajia wanafiki hawa habari ya wale waliopita, miongoni mwa watu wa Nūḥ, kabila la 'Ād, kabila la Thamūd, watu wa Ibrāhīm, watu wa Madyan na watu wa Lūṭ, walipowajia Mitume na wahyi na aya za Mwenyezi Mungu wakawakanusha? Wote hawa Mwenyezi Mungu Aliwateremshia adhabu Yake, kuwalipiza wao kwa matendo yao mabaya. Mwenyezi Mungu Hakuwa ni mwenye kuwadhulumu, lakini ni wao wenyewe walijidhulumu nafsi zao kwa kukanusha na kupinga

    [71] Na wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, waume na wake, wanasaidiana wao kwa wao, wanaamrisha watu kuamini na kufanya vitendo vyema na wanawakataza kukanusha na kufanya maasia, wanatekeleza Swala, wanatoa Zaka, wanamtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wanakomeka kufanya yale waliyokatazwa. Hao Mwenyezi Mungu Atawarehemu, Atawaokoa na adhabu Yake na Atawatia Peponi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mshindi katika ufalme Wake, ni Mwingi wa hekima katika sheria Zake na hukumu Zake

    [72] Mwenyezi Mungu Amewaahidi wenye kumuaumini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, waume na wake, mabustani ya Pepo ambayo chini yake inapita mito, hali ya kukaa humo milele. Starehe zake haziwaondokei. yana majumba yaliojengwa vizuri yenye utulivu mzuri katika mabustani ya makao. Na radhi itokayo kwa Mwenyezi Mungu watakayoipata ni kubwa zaidi na ni bora zaidi kuliko starehe walizonazo. Ahadi hiyo ya malipo mema ya Akhera ndio kufaulu kukubwa

    [73] Ewe Nabii! Pigana vita na makafiri kwa upanga, na wanafiki kwa ulimi na kusimamisha hoja, na ukazane juu hayo mapote mawili. Na mahala pao pa kutulia ni Motoni; na ubaya wa mahala pa kuishia ni hapo watakapoishia wao

    [74] Wanafiki wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba wao hawakusema kitu cha kumkosea Mtume na Waislamu. Wao ni warongo. Hakika wamesema neno la ukafiri na wametoka kwa hilo kwenye Uislamu, na wamejaribu kumdhuru Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani imshukiye, Mwenyezi Mungu hakuwawezesha kulifanya hilo. Na wanafiki hawakupata kitu chochote cha kumtia kombo na kumkosoa, isipokuwa ni kwamba Mwenyezi Mungu Aliwaneemesha akawapa utajiri kwa milango ya heri na baraka Aliyomfungulia Nabii Wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye. Basi wakirudi makafiri hawa kwenye Imani na kutubia, hilo ni bora kwao, na wakigeuka nyuma au wakasalia hali ile walivyo, Mwenyezi Mungu Atawaadhibu adhabu iumizayo hapa duniani, kupitia mikono ya Waislamu, na kesho Akhera kwa Moto wa Jahanamu, na hapatakuwa na mwokoaji wa kuwaokoa wala msaidizi wa kuwakinga na janga la adhabu

    [75] Na miongoni mwa mafukara wa wanafiki, kuna wanaojipa ahadi ya mkazo wenyewe kwamba lau Mwenyezi Mungu Atampa mali, atayatolea sadaka, atafanya vile watu wema wanafanya katika mali yao na atafuata njia ya wema

    [76] Alipowapa Mwenyezi Mungu kutokana na hisani yake, walifanya ubakhili kutoa sadaka na kutumia mali katika wema, na waligeuka nyuma hali ya kuupa mgongo Uislamu

    [77] Ikawa malipo ya mambo waliyoyafanya na mwisho wao ni kwamba aliwaongezea unafiki juu ya unafiki wao, hawataweza kujisafisha nao mpaka Siku ya kuhesabiwa. Hayo ni kwa sababu ya kwenda kwao kinyume na ahadi walioitoa juu ya nafsi zao na kwa sababu ya unafiki wao na urongo wao

    [78] Kwani hawakujua wanafiki hawa kwamba Mwenyezi Mungu Anayajua wanayoyaficha ndani ya nafsi zao na yale wanayoyazungumza kwenye mabaraza yao ya vitimbi na njama na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mjuzi sana wa yaliyofichika yote? Basi Atawalipa kwa matendo yao ambayo Amewahifadhia na kuwadhibitia

    [79] Na pamoja na ubahili wawanafiki, wale wanaotoa sadaka hawavuki salama na kero lao. Pindi wale matajiri wakitoa sadaka ya mali mengi, wanawatia kombo na kuwatuhumu kuwa wanajionesha. Na pindi mafukara wakitoa sadaka kulingana na uwezo wao, wanawafanyia shere na kusema kwa njia ya kuwachezea, «Sadaka yao hii itafalia nini?» Basi Mwenyezi Mungu Anawafanyia shere wanafiki hawa. Na wao watakuwa na adhabu kali iumizayo

    [80] Waombee msamaha hao wanafiki, ewe Mtume, au usiwaombee msamaha, Mwenyezi Mungu Hatawasamehe, namna yatakayokuwa mengi na kukaririka maombi yako kutaka wasamehewe, kwa kuwa wao wamemkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Na Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Hawaafikii kwenye uongofu wale waliotoka nje ya utiifu Wake

    [81] Walifurahi wale waliojiweka nyuma wasimwandame Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani ziwashukiye, kwa kujikalia Madina wakienda kinyume na Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, na walichukia kupigana jihadi pamoja na Yeye kwa mali zao na nafsi Zao katika njia ya Mwenyezi Mungu na waliambiana wao kwa wao, «Msitoke katika kipindi cha joto.» Waambie, ewe Mtume, «Moto wa Jahanamu una joto zaidi,» lau wao wanalijua hilo

    [82] Basi na wacheke hao wanafiki waliojiweka nyuma wasimwandame Mtume wa Mwenyezi Mungu katika vita vya Tabūk, kidogo katika uhai wao wa kilimwengu wenye kumalizika, na walie sana katika Moto wa Jahanamu, ukiwa ni malipo ya yale ambayo walikuwa wakiyachuma duniani ya unafiki na ukafiri

    [83] Basi Akikurudisha Mwenyezi Mungu, ewe Mtume, kutoka kwenye vita ulivyopigana ukaja kwenye kundi la wanafiki waliothibiti juu ya unafiki, na wakakutaka ruhusa watoke na wewe kwenye vita vingine baada ya vita vya Tabūk, waambie, «Hamtatoka pamoja na mimi kabisa kwenye vita vyovyote, na hamtapigana pamoja na mimi na adui yoyote. Nyinyi mumeridhika kukaa mara ya kwanza, basi kaeni pamoja na wale waliojiweka nyuma wakaacha kupigana jihadi pamoja na Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie.»

    [84] Na usimswalie kabisa, ewe Mtume, yoyote aliyekufa miongoni mwa wanafiki na usisimame kwenye kaburi yake kumuombea, kwa kuwa wao wamemkanusha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na Mtume Wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, na wamekufa na wao wametoka kwenye utiifu. Hii ni hukumu yenye kuenea kwa kila mtu ambaye unafiki wake umejulikana

    [85] Na zisikushangaze mali za wanafiki hawa na watoto wao. Mwenyezi Mungu Anataka kuwaadhibu wao kwa hizo ulimwenguni, kwa kupambana kwao na shida katika kuzipata na kwa kufa kwao katika hali ya kumkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake

    [86] Na pindi sura yoyote ikiteremshwa kwa Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, inayoamrisha kumuamini Mwenyezi Mungu na kumtakasa na kupigana jihadi pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu, wale wenya uwezo wa kifedha miongoni mwa wanafiki wanakuomba ruhusa na wanasema, «Tuache pamoja na waliokaa wasioweza kutoka.»

    [87] Wanafiki hawa wameridhika na aibu, nayo ni kukaa majumbani pamoja na wanawake na watoto na wenye nyudhuru. Na Mwenyezi Mungu Amezipiga muhuri nyoyo zao kwa sababu ya unafiki wao na kujiweka kwao nyuma kuacha jihadi na kutoka pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, katika njia ya Mwenyezi Mungu. Wao hawayaelewi yale ambayo yana maslahi yao na uongofu wao

    [88] Iwapo wanafiki hawa watajikalisha nyuma waache kupigana, Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, amepigana jihadi, yeye na Waumini pamoja naye, kwa mali zao na nafsi zao. Wao wamepata ushindi na ngawira ulimwenguni, na watapata Pepo na mapokezi mema kesho Akhera. Na wao ndio wenye kufaulu

    [89] Amewatayarishia Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama, mabustani ya Pepo ambayo inapita mito chini ya miti yake, hali ya kukaa humo milele. Huko ndiko kufaulu kukubwa

    [90] Na kilikuja kikundi, miongoni mwa watu wa vitongoji vya Waarabu wa majangwani, kandokando ya mji wa Madina wakitoa nyudhuru kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, wakimuelezea udhaifu walionao na kutoweza kwao kutoka kwenda vitani. Na kuna watu waliojikalia bila kutoa udhuru wowote kwa kumfanyia ujasiri Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema wa Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye. Basi wale waliokufuru miongoni mwa hawa itawatapata adhabu kali, ya kuuawa na nyinginezo hapa duniani, na ya Moto kesho Akhera

    [91] Watu wenye nyudhuru, miongoni mwa madhaifu, wagonjwa na mafukara ambao hawamiliki mali ya kuwawezesha kufanya matayarisho ya kutoka, hawana makosa ya kujikalia, iwapo wamemtakasia Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wameifuata sheria Yake kivitendo. Hapana njia yoyote kwa wale waliozuiliwa na udhuru kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kupatiwa mateso na kutiwa makosani, iwapo wao ni waaminifu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa watenda wema (muhsinūn), ni Mwenye kuwarehemu

    [92] Pia hapana makosa kwa wale ambao wakikujia kutaka uwasaidie kuwachukua kwenda kwenye jihadi, unawaambia, «Sina wanyama wa mimi kuwapatia muwapande», hapo wakakuacha na kugeuka kwenda zao, na macho yao yanabubujika machozi kwa masikitiko ya kukosa utukufu wa jihadi na thawabu zake kwa kuwa hawakupata cha kutumia na cha kuwabeba lau walitoka kwenda kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu

    [93] Hakika makosa na lawama ni kwa wale matajiri waliokujia, ewe Mutme, kukutaka ruhusa ya kujikalia, nao ni wanafiki matajiri waliojichagulia kuketi pamoja na wanawake na wenye nyudhuru. Na Mwenyezi Mungu Amezipiga mhuri nyoyo zao kwa unafiki, haziingiwi na Imani. Wao hawajui mwisho wao mbaya kwa kubakia kwao nyuma na kuacha kwao kupigana jihadi pamoja na wewe

    [94] Watataka udhuru kwenu, enyi Wumini, hawa waliojikalisha nyuma na kuacha kupigana jihadi na washirikina, kwa kutumia maneno ya urongo, mtakaporudi kutoka kwenye jihadi ya vita vya Tabūk. Waambie, ewe Mtume, «Msitoe udhuru, hatutawaamini katika yale mnayoyasema. Mwenyezi Mungu Ashatupa habari, kuhusu mambo yenu, ambazo zimetupa uthibitisho wa urongo wenu. Mwenyezi Mungu Atayaona matendo yenu na Mtume Wake, iwapo mtatubia unafiki wenu au mtaendelea nao. Na Mwenyezi Mungu Atawaonesha watu matendo yenu waziwazi hapa duniani kisha mtarudishwa, baada ya kufa kwenu, kwa Yule Ambaye hayafichiki Kwake mambo yenu ya ndani na ya nje, ili Awape habari ya matendo yenu yote na Awape malipo yake

    [95] Mtakaporejea kwao kutoka vitani, wanafiki watawaapia nyinyi kwa Mwenyezi Mungu, wakitoa udhuru hali ya kuwa ni warongo, ili muwaache bila kuwauliza. Basi jiepusheni nao na muwape mgongo kwa kuwadharau, kwani wao ni wachafu wa ndani. Na mahali pao pa kushukia kesho Akhera ni Moto wa Jahanamu, ukiwa ni malipo ya yale waliokuwa wa kiyatenda ya madhambi na makosa

    [96] Wanawaapia nyinyi, enyi Waumini, wanafiki hawa kwa urongo ili mridhike nao. Basi mkiridhika nao, kwa kuwa hamjui urongo wao, hakika Mwenyezi Mungu Haridhiki na hawa wala wengineo kati ya wale walioendelea na uasi na kutoka nje ya utiifu wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake

    [97] Mabedui, wakazi wa jangwani, ni washupavu zaidi wa ukafiri na unafiki kuliko wakazi wa mjini. Hivyo ni kwa sababu ya ugumu wa tabia za, ususuavu wa nyoyo zao na kuwa mbali kwao na elimu, wanavyuoni, vikao vya mawaidha na dhikr (kumtaja Mwenyezi Mungu). Kwa hivyo wao wanastahilii zaidi wasijue mipaka ya Dini na zile sheria na hukumu ambazo Mwenyezi Mungu Ameziteremsha. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa hali za hawa wote, ni Mwenye hekima Katika uendeshaji Wake mambo ya waja Wake

    [98] Na miogoni mwa Mabedui kuna wanaohesabu wanachokitoa katika njia ya Mwenyezi Mungu kuwa ni kodi na ni hasara, hawatazamii, kwa kile wakitoacho, thawabu wala kujikinga na adhabu, na wana hamu mupatwe na misiba na maafa. Lakini mabaya yatawazunguka wao, sio Waislamu. Na Mwenyezi Mungu ni Msikizi wa wanayoyasema, ni Mjuzi wa nia zao mbaya

    [99] Na miongoni mwa Mabedui kuna wanaomuamini Mwenyezi Mungu na kukubali upweke Wake, kufufuliwa baada ya kufa na kuwa kuna thawabu na adhabu, na wanatarajia malipo mema kwa kile chochote wanachokitoa cha matumizi katika kupigana jihadi na washirikina, kwa kusudia radhi za Mwenyezi Mungu na mapenzi Yake, na kukifanya ni njia ya kumfanya apate maombi ya Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye. Jua utanabahi kwamba matendo haya yatawaweka wao karibu na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka. Mwenyezi Mungu Atawatia kwenye Pepo Yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha wa maovu waliyoyafanya, ni Mwenye kuwarehemu

    [100] Wale waliowatangulia watu mwanzo kwenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake miongoni mwa Muhājirūn waliowagura watu wao na jamaa zao wakaondoka kwenda kwenye Nyumba ya Uislamu, na Anṣār waliomhami Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, dhidi ya maadui wake makafiri, na wale waliowafuata wao kwa wema, katika usawa wa itikadi, maneno na vitendo, kwa kutafuta radhi ya Mwenyezi Mungu, Aliyetakata na sifa pungufu na kutukuka, Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu Ameridhika na wao kwa kumtii kwao Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na wao wameridhika na Yeye kwa malipo mazuri mengi Aliyowapatia kwa utiifu wao na Imani yao. Amewaandalia wao mabustani ya Pepo ambayo inapita mito chini yake, hali ya kukaa milele humo daima. Huko ndiko kufaulu kukubwa. Katika aya hii pana kuwasafisha Maswahaba, radhi za Mwenyezi Mungu ziwaendee, kuwafanya waadilifu na kuwasifu. Na kwa hivyo, kuwaheshimu wao ni katika misingi ya Imani

    [101] Miongoni mwa watu ambao wako pambizoni mwa Madina kuna Mabedui wanafiki, na miongoni mwa watu wa Madina pia kuna wanafiki waliojikita kwenye unafiki na kuzidi kuendelea nao kwa kupita mipaka katika uasi, kwa namna ambayo yanafichamana kwako, ewe Mtume, mambo yao. Sisi tunawajua. Tutawaadhibu mara mbili, kwa kuuawa na kutekwa na kukashifiwa duniani, na kwa adhabu ya kaburi baada ya kufa, kisha watapelekwa, Siku ya Kiyama, kwenye adhabu kubwa ndani ya Moto wa Jahanamu

    [102] Na wengine wa Madina na walio pambizoni mwake, walikubali makosa yao, wakajuta na wakatubia kwa hayo, walichanganya matendo mazuri, nayo ni kutubia, kujuta, kukubali makosa na mengineyo miongoni mwa matendo mema, kwa mengine mabaya, nayo ni kujikalia nyuma kumuacha Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na mengineyo miongoni mwa matendo mabaya. Basi hao yatarajiwa Mwenyezi Mungu Awaelekeze kutubia na aikubali toba yao kutoka kwao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa waja Wake, ni Mwenye kuwarehemu

    [103] Chukua, ewe Mtume, kwenye mali za hawa waliotubia, waliochanganya matendo mema na matendo mengine maovu, sadaka itakayowasafisha wao na uchafu wa madhambi yao na itakayowainua wao na kuwaondoa kwenye daraja za wanafiki kuwapeleka kwenye daraja za wenye ikhlasi; na watakie wao msamaha wa madhambi yao na uwaombee sitara ya hayo, kwani maombi yako na utakaji msamaha wako ni rehema na utulivu kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Msikizi wa kila maombi na kila neno, ni Mjuzi wa hali za waja Wake na nia zao, na Atamlipa kila mwenye kutenda kwa matendo aliyoyatenda

    [104] Kwani hawajui, hawa wenye kujikalisha nyuma na kuacha kwenda kwenye jihadi na wengineo, kwamba Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Ndiye Ambaye Anakubali toba ya waja Wake, Anachukua sadaka na Anatoa malipo yake, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kukubali toba ya waja Wake warejeapo Kwake, ni Mwenye kuwarehemu warudipo kutaka radhi Zake

    [105] Na sema, ewe Nabii, kuwaambia hawa wenye kujikalisha nyuma na kuacha kwenda kwenye jihadi, «Mfanyieni Mwenyezai Mungu yale ya kumridhisha ya kumtii na kutekeleza mambo ya lazima Aliyoyaweka na kuepuka maasia. Na Mwenyezi Mungu Atayaona matendo yenu na Mtume Wake na Waumini, na yatakuwa wazi mambo yenu, na mtarejeshwa Siku ya Kiyama kwa Anayejua yaliyofichika yenu na yaliyo wazi yenu, na hapo Atawapa habari ya yale ambayo mlikuwa mkiyafanya. Katika hii kuna tishio na onyo kwa anayeendelea kwenye ubatilifu wake na ukiukaji mipaka wake

    [106] Na miongoni mwa hawa waliojikalisha nyuma wakaacha kuwafuata, enyi Waumini, katika vita vya Tabūk kuna wengine walioahirishwa, ili Mwenyezi Mungu Aaamue juu yao uamuzi Atakaoutoa: ima Awaadhibu Mwenyezi Mungu au Awasamehe. Hawa ni wale waliojuta kwa yale ambayo walifanya. Nao ni Murarah mwana wa al-Rabī‘, Ka‘b mwana wa Mālik na Hilāl mwana wa Umayyaha. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa Anayestahili mateso au msamaha. Ni Mwingi wa hekima katika maneno Yake yote na vitendo Vyake

    [107] Na wanafiki waliojenga msikiti, kwa kuwadhuru Waumini, kumkanusha Mwenyezi Mungu na kuwagawanya Waumini, ili waswali humo baadhi yao na wauache msikiti wa Qubā’ ambao Waislamu wanaswali ndani yake, ili Waislamu watafautiane na wagawanyike kwa hilo, na kwa ajili ya kumngojea yule aliyempiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume Wake kabla ya hapo, naye ni Abū ‘Āmir al-Rāhib aliyeasi, ili pawe ni mahali pa kuwafanyia vitimbi Waislamu. Na wataapa tena wataapa, wanafiki hawa, kwamba wao hawakukusudia kwa kuujenga isipokuwa kuwafanyia wema na kuwahurumia Waislamu na kuwapa nafasi wanyonge wasioweza kwenda msikiti wa Qubā’ .Na Mwenyezi Mungu Anashuhudia kwamba wao ni warongo katika yale wanayoyaapia. Msikiti huo ulivunjwa na ukatiwa moto

    [108] Usisimame, ewe Nabii, kuswali katika msikiti huo kabisa. Kwani msikiti uliojengwa kwa misingi ya uchamungu kuanzia siku ya mwanzo, nao ni msikiti wa Qubā’, unafaa zaidi kwa wewe kusimama humo kwa kuswali. Kwani katika msikiti huu kuna watu wanapenda kujisafisha na najisi na uchafu kwa maji, kama wanavyojisafisha kwa kujiepusha na mambo yanayopelekea kufanya mambo yaliyoharamishwa na kuomba msamaha kutokana na madhambi na maasia. Na Mwenyezi Mungu Anawapenda wenye kujisafisha.Na iwapo msikiti wa Qubā’ ulijengwa juu ya misingi ya uchaji-Mungu, basi Msikiti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ni kama hivyo kwa njia ya ubora zaidi na ustahiki zaidi

    [109] Hawalingani: yule aliyeweka msingi wa jengo lake juu ya kumcha Mwenyezi Mungu na kumtii na kutaka radhi Zake na yule aliyeweka msingi wa jengo lake kandokando ya shimo linalokaribia kuanguka akajenga msikiti wa kudhuru, kukufuru na kuleta mgawanyiko baina ya Waislamu, ikampelekea yeye aanguke kwenye Moto wa Jahanamu. Na Mwenyezi Mungu Hawaongozi watu madhalimu waliokiuka mipaka Yake

    [110] Haliachi kuendelea, lile jengo wanafiki walilolijenga liwe ni madhara kwa msikiti wa Qubā’, kuwa ni ishara ya shaka unafiki uliojikita ndani ya nyoyo zao, mpaka nyoyo zao zikatike-katike kwa wao kuuawa au kufa au kwa kujuta kwao upeo wa kujuta nakurejea kwao kwa Mola wao na kumuogopa Yeye upeo wa kuogopa.Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa shaka waliyonayo hawa wanafiki na yale waliyoyakusudia kwa jengo lao, ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji mambo ya viumbe Vyake

    [111] Hakika Mwenyezi Mungu Amenunua kutoka kwa Waumini, nafsi zao na kuwapa wao , badala yake, Pepo na yale Aliyoyatayarisha ya starahe humo ndani, kwa kutoa kwao nafsi zao na mali zao katika kupigana jihadi na maadui wake kwa ajili ya kulitukuza neno Lake na kuidhihirisha dini Yake, wakaua na wakauawa. Hiyo ikiwa ni ahadi juu ya Mwenyezi Mungu iliyothibiti ndani ya Taurati iliyoteremshwa kwa Mūsā, amani imshukiye, na Injili iliyoteremshwa kwa ‘Īsā, amani imshukiye, na Qur’ani iliyoteremshwa kwa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani imshukiye. Na hakuna yoyote mwenye utekelezaji zaidi wa ahadi Yake kuliko Mwenyezi Mungu, kwa yule aliyetimiza ahadi yake kwa Mwenyezi Mungu. Basi onesheni furaha, enyi Waumini, kwa biashara yenu mliyoifanya na Mwenyezi Mungu na kwa ahadi Yake, ya Pepo na Radhi, kwenu. Na mapatano hayo ya biashara ndiyo kufaulu kukubwa

    [112] Na miongoni mwa sifa za Waumini hawa waliopewa bishara njema ya kuingia Peponi ni kwamba wao ndio wanaotubia, wenye kuondoka kwenye yale ambayo Mwenyezi Mungu Ameyakataza kwenda kwenye yale ambayo Mwenyezi Mungu Anayapenda na Anayaridhia, wale waliomtakasia ibada Mwenyezi Mungu Peke Yake na wakapindana katika kumtii, wale wenye kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa yote yale ambayo Aliwatahini nayo ya uzuri au ubaya, wenye kufunga, wenye kurukuu katika swala zao, wenye kusujudu katika hizo, wale ambao wanawaamrisha watu kila lile ambalo Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wameliamrisha na wanawakataza kila lile ambalo Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wamelikataza, wenye kutekeleza faradhi za Mwenyezi Mungu, wenye kumalizikia kwenye kufuata amri Yake na kuepuka katazo Lake, wenye kusimama imara katika kumtii na wenye kukomea pale penye mipaka Yake. Na wape bishara njema, ewe Nabii, waumini hawa waliosifika na sifa hizi ya radhi za Mwenyezi Mungu na Pepo Yake

    [113] Haifai kwa Nabii Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, na wale walioamini kuwaombea msamaha washirikina, hata kama ni jamaa zao wa karibu, baada ya kuwa imefunuka waziwazi kwamba wao ni watu wa Moto wa Jah(Im, kwa kufa kwao katika hali ya ushirikina. Na Mwenyezi Mungu Hawasamehe washirikina, kama alivyosema Aliyetukuka, «Hakika Mwenyezi Mungu Hasamehe Ashirikishwapo» na kama Alivyosema Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu, «Hakika yule anayemshirikisha Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu Ashamharimishia Pepo»)

    [114] Na hakukuwa kwa Ibrāhīm kule kumuombea msamaha babake mshirikina isipokuwa ni yatokana na ahadi aliyeitoa kwake, nayo ni neno lake, «Nitakuombea msamaha Mola wangu, kwani Yeye kwangu mimi Ana ukarimu mwingi.» Basi ilipomfunukia wazi Ibrāhīm kwamba babake ni adui wa Mwenyezi Mungu na kwamba kusihi na kukumbusha hakukufaa kitu kwake na kwamba yeye atakufa akiwa kafiri, alimuacha, akaacha kumuombea msamaha na akamwepuka. Kwa kweli, Ibrāhīm, amani imshukiye, ana unyenyekevu mkubwa kwa Mwenyezi Mungu, ni mwenye msamaha mwingi kwa kasoro zinazotoka kwa watu wake

    [115] Na Mwenyezi mungu Hakuwa ni Mwenye kuwapoteza watu baada ya kuwapa neema uongofu na taufiki, mpaka awaelezee waziwazi yale ambayo yatawapelekea kumcha Yeye na yale wanayoyahitajia ya misingi ya Dini na tagaa zake. Hakika Mwenyezi Mungu, kwa kila jambo, ni Mjuzi; Amewafundisha nyinyi yale ambayo hamkuwa mkiyajua, amewaelezea waziwazi yale ambayo mtanufaika nayo na Amewasimamishia hoja kwa kuwafikishia ujumbe Wake

    [116] Hakika Mwenyezi Mungu ni mmiliki wa mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake, Hana mshirika katika uumbaji, uendeshaji, ustahiki wa kuabudiwa na uwekaji sheria. Anampa uhai Anayemtaka na anamfisha Anayemtaka. Na hakuna yoyote, isipokuwa Mwenyezi Mungu, wa kuyasimamia mambo yenu wala wakuwapa ushindi juu ya adui wenu

    [117] Mwenyezi Mungu Alimuelekeza Nabii Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kurudi Kwake na kumtii, na Aliwakubalia toba Muhājirūn, waliogura nyumba zao na jamaa zao wakaenda kwenye Nyumba ya Uislamu, na pia Aliwakubalia toba waliomuhami Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, waliotoka pamoja na yeye kupambana na maadui katika vita vya Tabūk katika kipindi cha joto kali na shida ya chakula na vipando. Mwenyezi Mungu Aliwakubalia toba yao baada ya hali kufikia kiwango kwamba nyoyo za baadhi yao zilikaribia kuiyepuka haki na kupendelea ulegevu na utulivu. Lakini Mwenyezi Mungu Aliwathibitisha na Akawapa nguvu na Akawakubalia toba. Hakika Yeye kwao ni Mwingi wa upole ni mwenye huruma. Na miongoni mwa huruma Yake kwao ni kwamba Aliwapa neema ya kutubia, Akaikubali toba yao na Akawathibitisha juu yake

    [118] Na pia Alikubali toba ya wale watu watatu walioachwa nyuma - nao ni Ka‘b mwana wa Mālik, Hilāl mwana wa Umayyah na Murarah mwana wa a-Rabī'-. Wao walijikalisha nyuma wakaacha kumfuata Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wakasikitika masikitiko makubwa. Mpaka ilipofikia hadi ya ardhi kuwa dhiki na wao, pamoja na kuwa ni kunjufu, kwa majonzi na majuto kwa sababu ya kujikalisha nyuma kwao, na nafsi zao zikaingiwa na dhiki kwa hamu iliyowapata na wakahakikisha kwamba hakuna mahali pa kuhamia kumkimbia Mwenyezi Mungu isipokuwa ni Kwake, hapo Mwenyezi Mungu, Aliyetakata na sifa za upungufu na kutukuka, Aliwaafikia kwenye utiifu na kurejea kwenye yale yanayomridhisha Yeye. Hakika Yeye ni Ndiye Mwingi wa kukubali toba za waja Wake, Ndiye Mwenye kuwahurumia

    [119] Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkaitumia sheria Yake! Fuateni maamrisho ya Mwenyezi Mungu na epukeni makatazo Yake katika kila kitu mnachokitenda na mnachokiacha, na kuweni pamoja na wakweli katika Imani zao na ahadi zao na katika kila jambo miongoni mwa mambo yao

    [120] Haikuwa inafaa kwa watu wa mji wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na walio pambizoni mwao miongoni mwa wanaokaa jangwani, kujikalisha nyuma pamoja na watu wao majumbani mwao na kuacha kumfuata Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye. Na haikuwa inafaa kwao kuzipendelea nafsi zao mapumziko huku Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, yuko kwenye tabu na usumbufu. Hayo ni kwamba wao hawapatikani na kiu wala usumbufu wala njaa kwenye safari yao na jihadi yao katika njia ya Mwenyezi Mungu, na wala hawakanyagi ardhi yoyote ambayo kuikanyaga kwao inawatia hasira makafiri, na wala hawafaulu kumuua au kumshinda adui wa Mwenyezi Mungu na adui wao isipokuwa wataandikiwa, kwa hayo yote, thawabu ya tendo jema. Hakika Mwenyezi Mungu Hapotezi malipo ya muhsinūn: waliofanya wema kwa kukimbilia kwao kufuata amri ya Mwenyezi Mungu na kusimama kwao imara kutekeleza haki Yake inayowalazimu na haki ya viumbe Vyake

    [121] Na wala hawatoi matumizi, madogo au makubwa, katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawayapiti mabonde katika kutembea kwao pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, katika kupigana kwake jihadi, isipokuwa wataandikiwa thawabu ya tendo lao, ili Mwenyezi Mungu Awalipe mazuri zaidi ya wao kulipwa kwa matendo yao mema

    [122] Na haikuwa inafaa kwa Waumini watoke wote kupigana na adui yao, pia hailingani na wao wakae wote. Basi si watoke kupigana jihadi, katika kila kundi, watu ambao itapatikana kwao kutosheleza kufikia malengo. Hivyo ili wapate kujifunza, wale waliokaa wasiende vitani, na kujua hukumu mpya za dini ya Mwenyezi Mungu na zile zilizoteremshiwa Mtume Wake, na wapate kuwaonya jamaa zao kwa yale waliojifunza watakaporejea kwao, huenda wao wakajihadhari na adhabu ya Mwenyezi Mungu, kwa kutekeleza maamrisho Yake na kuepuka makatazo Yake

    [123] Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkaifuata sheria Yake kivitendo, anzeni kupigana na walio karibukaribu na Nyumba ya Uislamu , miongoni mwa makafiri, na wakute kutoka kwenu ushupavu na ukali. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wachamungu kwa msaada Wake na nusura Yake

    [124] Na pindi Mwenyezi Mungu Aiteremshapo sura, miongoni mwa sura za Qur’ani, kwa Mtume Wake, basi kati ya hawa wanafiki kuna wanaosema, kwa kukanusha na kufanya shere, «Ni nani wenu ambaye sura hii ilimfanya imani yake, kwa Mwenyezi Mungu na aya Zake, iongezeke? Basi wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake,, kule kuteremka sura, kuliwaongezea waolmani kwa kuijua na kuizingatia na kuiamini na kuitumia, na hali wao wanafurahia Imani na yakini Alizowapa Mwenyezi Mungu

    [125] Ama wale ambao wana unafiki na shaka ndani ya nyoyo zao katika dini ya Mwenyezi Mungu, basi kule kuteremka sura kunawaongezea unafiki na shaka juu ya unafiki na shaka walizokuwa nazo kabla ya hapo. Na hawa wataangamia wakiwa katika hali ya kumkanusha Mwenyezi Mungu na aya Zake

    [126] Kwani hawaoni wanafiki kwamba Mwenyezi Mungu Anawapa mitihani, kwa kuwaletea ukame na matatizo na kwa kuyatoa nje yale wanayoyaficha ya unafiki, mara moja au mara mbili kila mwaka? Kisha wao, pamoja na hayo, hawatubii kutokana na ukafiri wao na unafiki wao, wala hawazingatii wala hawakumbuki aya za Mwenyezi Mungu wazionazo

    [127] Na iteremshwapo sura, wanafiki huwa wakishiriana kwa macho, kwa kukataa kuteremka kwake, kucheza shere na kuwa na hasira, kwa yale yaliyoteremka humo ya kutaja aibu zao na matendo yao, kisha wanasema, «Je, kuna yoyote anayewaona mkiondoka kwa Mtume?» Iwapo hakuna yoyote aliyewaona huinuka na kuondoka kwa Mtume, rehema na amani zimshukiye, wakiogopa fedheha. Mwenyezi Mungu Amezipindua nyoyo zao Ameziepusha na Imani kwa sababu wao hawaelewi wala hawazingatii

    [128] Hakika amewajia nyinyi, enyi Waumini, mjumbe atokanao na watu wenu, Azionea uzito shida mlizonazo na masumbuko, ana pupa kwamba muamini na mambo yenu yafaulu na yeye kwa Waumini ni mwingi wa upole na huruma

    [129] Basi washirikina na wanafiki wakikupa mgongo kwa kuacha kukuamini, ewe Mtume, sema kuwaambia, «Mwenye kunitosha ni Mwenyezi Mungu; Ananitosheleza yote yanayonitia hamu, hapana muabudiwa yoyote wa haki isipokuwa Yeye, Kwake yeye nimetegemea na Kwake Yeye nimeyategemeza mambo yangu yote. Kwani Yeye Ndiye Mwenye kuninusuru na Mwenye kunisaidia. Na Yeye Ndiye Mola wa Arsh iliyo kubwa, ambayo ndiyo kiumbe kikubwa kabisa.»

    Yunus

    Surah 10

    [1] (Alif, Lām, Rā’.) Yametangulia maelezo juu ya herufi zilizotajwa kimkato mwanzo wa sura ya Al- Baqarah. Hizi ni aya za Kitabu kilichopangwa vizuri ambacho Mwenyezi Mungu Amekipanga na kukifafanua kwa waja Wake

    [2] Je, lilikuwa jambo la ajabu kwa watu lile la kuteremsha kwetu wahyi wa Qur’ani kwa mtu miongoni mwao anayewaonya mateso ya Mwenyezi Mungu na kuwapa habari njema wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake kwamba wao watapata malipo mazuri kwa matendo mema waliyoyatanguliza? Alipowajia Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa wahyi wa Mwenyezi Mungu na akawasomea, wakanushaji walisema, «Muhammad ni mchawi, na aliyokuja nayo ni uchawi wenye ubatilifu waziwazi.»

    [3] Hakika Mola wenu ni Mwenyezi Mungu Ambaye Alizipatisha mbingu na ardhi katika kipindi cha Siku Sita, kisha Akalingana, yaani Akawa juu ya 'Arsh, mlingano unaonasibiana na utisho Wake na utukufu Wake. Anaendesha mambo ya viumbe Vyake. Hakuna yoyote Anayempinga katika uamuzi Wake na hakuna muombezi yoyote anayeombea mbele Yake Siku ya Kiyama isipokuwa baada ya Yeye kumpa idhini kuombea. Basi muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wenu, Anayesifika kwa sifa hizi na mtakasiyeni ibada. Je, hamwaidhiki na mkazizingatia aya hizi na hoja

    [4] Kwa Mola wenu ndio marejeo yenu nyote Siku ya Kiyama. Na hili ndilo agizo la Mwenyezi Mungu lililo kweli. Yeye Ndiye Ambaye Anaanza kuumba viumbe kisha Atawarudisha baada ya kufa, Awafanye wawe hai kama walivyokuwa mwanzo, ili Awalipe waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na akafanya matendo mazuri malipo mazuri zaidi kwa uadilifu. Na wale waliokanusha upweke wa Mwenyezi Mungu na ujumbe wa Mtume Wake watakuwa na vinywaji vya maji moto sana yanayochoma nyuso na kukata tumbo; na watakuwa na adhabu inayoumiza kwa sababu ya ukafiri wao na upotevu wao

    [5] Mwenyezi Mungu Ndiye ambaye Alilifanya jua kuwa d,iyā’ (mwangaza), Akaufanya mwezi kuwa ni nūr (mng’aro) na Akaupangia mwezi njia zake za kupita. Ikawa kwa jua zinajulikana siku, na kwa mwezi inajulikana miezi na miaka. Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Hakuumba jua na mwezi isipokuwa ni hekima kubwa, na kuonesha ukamilifu wa uwezo wa Mwenyezi Mungu na ujuzi Wake; Anafafanua hoja na dalili kwa watu wanaojua hekima ya utengenezaji wa uumbaji

    [6] Hakika katika kupishana usiku na mchana na Alichokiumba Mwenyezi Mungu, katika mbingu na ardhi na zilizomo ndani yake zilizopangika na kutengenezeka miongoni mwa maajabu ya uumbaji, ni dalili na hoja zilizo wazi kwa watu wanaoogopa mateso ya Mwenyezi Mungu, ghadhabu Zake na adhabu Yake

    [7] Hakika ya wale ambao hawana matumaini ya kukutana na sisi Akhera kwa kuhesabiwa na yanayofuatia ya malipo juu ya matendo kwa kuwa wanakanusha kufufuliwa, wakaridhika na maisha ya ulimwenguni kuwa ni badala ya Akhera, wakajitegemeza nao huo ulimwengu, na wale ambao wao ni wenye kughafilika na alama zetu zilizoko ulimwenguni na zilizomo kwenye Sheria

    [8] Hao makao yao ni Moto wa Jahanamu huko Akhera, yakiwa ni malipo kwa yale ambayo wao walikuwa wakiyatenda katika ulimwengu wao ya madhambi na hatia

    [9] Hakika ya wale ambao walimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafanya mema, Mola wao Atawaonesha njia ya Pepo na Atawaafikia kufanya matendo yenye kuwafikisha kwake, kwa sababu ya Imani yao , kisha Atawapa malipo mema kwa kuingia Peponi na kuwashushia wao radhi Zake; chini ya sebule zao na majumba yao itakuwa ikipita mito, wakiwa ndani ya mabustani ya Pepo ya starehe

    [10] Maombi yao Peponi ni kuleta tasbihi (kusema Subhānaka Allāhumma), na maamkizi ya Mwenyezi Mungu na Malaika Wake kuwaamkia wao, na maamkizi yao, wao kwa wao, huko Peponi ni Salām. Na mwisho wa maombi yao ni kusema kwao, «Al-hamdu li Llāhi Rabbil- 'ālamīn» Yaani, shukrani na sifa njema ni za Mwenyezi Mungu, Muumba viumbe na Mwenye kuvilea kwa neema Zake

    [11] Na lau Mwenyezi Mungu Awaharakishia watu kuyakubali maombi yao ya kujitakia mabaya kama Anavyowaharakishia katika kuwakubalia maombi yao ya kujitakia mazuri wangaliangamia. Hivyo basi tunawaacha, wale ambao hawaogopi mateso yetu wala hawaamini kidhati kufufuliwa na kuhuishwa, ndani ya uasi wao na ujeuri wao hali ya kuwa wanashangaa na kuduwaa

    [12] Na impatapo binadamu shida, anatuomba tumsaidiye katika kumuondolea hiyo akiwa katika hali ya kuwa amelala kwa ubavu wake au ameketi au amesimama, kulingana na hali ile alivyo wakati mashaka yalipomshukia. Na tunapomuondolea ile shida iliyompata, huendelea kuifuata ile njia yake ya mwanzo kabla hajapatwa na mashaka na huyasahau yale aliokuwa nayo ya shida na matatizo na huacha kumshukuru Mola Wake aliyemuondolea yale aliyokuwa nayo ya matatizo. Na kama alivyopambiwa binadamu huyu kuendelea katika kukanusha kwake na kuwa na ujeuri baada ya Mwenyezi Mungu kukuondolea mashaka aliyokuwa nayo , vilevile walipambiwa wale waliopita kiasi katika kumzulia Mwenyezi Mungu urongo na Manabii Wake yale ambayo walikuwa wakiyafanya ya kumuasi Mwenyezi Mungu na kumshirikisha

    [13] Hakika tuliwaangamiza watu waliowakanusha Mitume wa Mwenyezi Mungu kabla yenu, enyi mliomshirikisha Mola wenu, waliposhirikisha na wakawajia Mitume wao kutoka kwa Mwenyezi Mungu wakiwa na miujiza iliyo wazi na hoja zenye kubainisha ukweli wa yale aliyekuja nayo. Basi watu hawa hawakuwa ni wenye kuwaamini Mitume wao na kuwafuata, kwa hivyo walistahili maangamivu. Na mfano wa maangamivu hayo ndivyo atakavyolipwa kila mhalifu mwenyekukiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu

    [14] Kisha tukawafanya nyinyi, enyi watu, ni badala yao katika ardhi baada ya makame ya wale walioangamizwa, ili tuangalie vipi mtafanya: mema au maovu, tupate kuwalipa kwa hayo, kulingana na matendo yenu

    [15] Na wasomewapo washirikina aya za Mwenyezi Mungu zilizo wazi tulizokuteremshia wewe, ewe Mtume, husema wale ambao hawaogopi Hesabu wala hawatarajii malipo wala hawaamini Siku ya kufufuliwa na kuhuishwa, «Lete qur’ani isiyokuwa hii, au tugeuze hii Qur’ani: uifanye halali kuwa haramu na haramu kuwa halali, ahadi kuwa onyo na onyo kuwa ahadi, na uondoe yaliyomo ndani yake ya kukashifu waungu wetu na kuzifanya za kipumbavu akili zetu.» Waambie, ewe Mtume,»Hilo haliko kwangu. Kwani mimi nafuata, katika kila ninalowaamrisha na ninalowakataza, yale ambayo Mola wangu Ameniteremshia na kuniamrisha kwayo. Mimi naogopa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, nikienda kinyume na amri Yake, adhabu ya siku iliyo kubwa , nayo ni Siku ya Kiyama

    [16] Waambie, ewe Mtume, «Lau Mwenyezi Mungu Alitaka, singaliwasomea hii Qur’ani, wala Mwenyezi Mungu Hangaliwajulisha nayo. Basi jueni kuwa hiyo ni haki itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Kwani nyinyi mnajua kwamba mimi nimekaa na nyinyi muda mrefu kabla Mola wangu Hajauleta wahyi wa hiyo (Qur’ani) kwangu, na kabla sijaisoma kwenu. Basi hamtumii akili zenu kwa kuzingatia na kufikiri?»

    [17] Hapana yoyote mwenye udhalimu mkubwa zaidi kuliko yule aliyemzulia Mwenyezi Mungu urongo au akazikanusha aya Zake. Hakika ni kwamba hawatafuzu waliowakanusha Manabii wa Mwenyezi Mungu na Mitume Wake wala hawatafaulu

    [18] Na hawa wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu na asiyekuwa Yeye wanaviabudu visivyowadhuru chochote wala kuwanufaisha ulimwenguni wala Akhera, na wanasema, «Sisi tunawaabudu wao ili watuombee mbele ya Mwenyezi Mungu.» Waambie, ewe Mtume, «Je, mnampa habari Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, jambo Asilolijua, katika mbingu au katika ardhi, kuhusu mambo ya waombezi hawa?» Kwa hakika lau kulikuwa na waombezi katika hizo wa kuwaombea nyinyi mbele Yake, Angalikuwa na ujuzi zaidi kuhusu wao kuliko nyinyi.» Kwani Mwenyenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ameepukana na wanachokifanya washirikina hawa cha kushirikisha kwao, katika ibada Yake, vitu visivyodhuru wala kunufaisha

    [19] Watu walikuwa kwenye dini moja, nayo ni Uislamu, kisha wakatafautiana baada ya hapo, wakakufuru baadhi yao na wengine wakasimama imara juu ya haki. Na lau kwamba si neno lilitangulia kutoka kwa Mwenyezi Mungu la kuwapa muhula wenye kuasi na kutowafanyia haraka kuwapatiliza kwa madhambi yao, basi wangaliamuliwa baina yao kwa kuwaangamiza watu wa ubatilifu miongoni mwao na kuwaokoa watu wa ukweli

    [20] Na makafiri hawa wakaidi wanasema «Basi si ateremshiwe Muhammad ujuzi, dalili na miujiza inayoonekana, kutoka kwa Mola wake, ambayo kwayo tutajua kuwa yeye yuko juu ya haki katika yale anayoyasema.» Waambie, ewe Mtume, «Hakuna ajuwaye ghayb (yasioonekena) isipokuwa ni Mwenyezi Mungu. Akitaka (kufanya wanayoyataka) Atafanya na akitaka (kutofanya) hatafanya. Basi ngojeni, enyi watu, uamuzi wa Mwenyezi Mungu baina yetu na nyinyi wa kuyaharakisha mateso Yake kwa wakosa kati yetu na kumnusuru mwenye haki; mimi nalingojea hilo

    [21] Na tunapowaonjesha washirikina usahali, faraja na neema baada ya uzito, shida na dhiki zilizowapata, punde si punde wanakanusha na kuzifanyia shere aya za Mwenyezi Mungu. Sema uwaambie, ewe Mtume, washirikina hawa wanaofanya shere, «Mwenyezi Mungu ni ni mpesi wa vitimbi, kuwavuta nyinyi kidogokidogo na kuwatesa.» Hakika watunzi wetu tunaowatuma kwenu, wanayasajili kwenu yale mnayoyafanyia vitimbi kuhusu aya zetu kisha tutawahesabu kwa hayo

    [22] Yeye Ndiye Anayewaendesha nyinyi, enyi watu, juu ya wanyama na vinginevyo barani, na ndani ya majahazi baharini, hata mnapokuwa humo na yakatembea kwa upepo mzuri na abiria wa hayo majahazi wakafurahi kwa huo upepo mzuri, ghafla majahazi hayo yanajiwa na upepo mkali, na mawimbi yakawajia abiria kutoka kila mahali, na wakawa na hakika kuwa maangamivu yamewazunguka, hapo wanamtakasia dua Mwenyezi Mungu Peke Yake, na wakaviacha vile ambavyo walikuwa wakiviabudu na wanasema, «Ukituokoa kutoka kwenye shida hii ambayo tuko nayo, kwa kweli tutakuwa ni miongoni mwa wale wenye kukushukuru kwa neema yako.»

    [23] Mwenyezi Mungu Alipowaondolea shida na mikasa, punde si punde wakawa wanafanya uharibifu na maasia katika ardhi. Enyi watu, hakika ukorofi wa udhalimu wenu unawarudia nyinyi wenyewe. Chukueni starehe katika uhai wa kilimwengu wenye kuondoka, kisha kwetu ndio mwisho wenu na marejeo yenu, hapo tutawapa habari ya matendo yenu yote na tutawahesabu juu ya hayo

    [24] Hakika mfano wa uhai wa kilimwengu na yale mnayojifahiri nayo baina yenu ya mapambo na mali ni kama mfano wa mvua tulioiteremsha kutoka juu kushuka ardhini, tukaotesha kwayo aina za mimea zilizochanganyika miongoni mwa zile zinazoliwa na watu katika matunda na zinazoliwa na wanyama katika nyasi, mpaka ulipoonekana wazi uzuri wa hii ardhi na mng’aro wake, na watu wa ardhi hii wakadhani kwamba wao ni waweza wa kuyavuna na kufaidika nayo, hapo amri yetu na hukumu yetu iliyajia kuwa ile mimea iliyoko juu yake iangamie na uzuri wake uondoke, kipindi cha usiku au mchana, tukaifanya mimea hii na miti imevunwa imekatwa, hakuna kitu katika ardhi hiyo, kama kwamba hapakuwa na mazao na mimea iliokuwa imesimama kabla ya hapo juu ya uso wa ardhi. Hivyo ndivyo kutoweka kunakomaliza yale mnayojigamba nayo baina yenu ya ulimwengu wenu na pambo lake, Mwenyezi Mungu Akayamaliza na kuyaangamiza. Na kama tulivyowafafanulia, enyi watu, mfano wa ulimwengu huu, na tukawajulisha uhakika wake, ndivyo tunavyofafanua hoja zetu na dalili zetu kwa watu wanaofikiri juu ya aya za Mwenyezi Mungu na wanaozingatia yanayowafaa duniani na Akhera

    [25] Na Mwenyezi Mungu Anawaita kwenye mabustani ya Pepo Yake Aliyowaandalia wanaojitegemeza Kwake, na Anawaongoza Anaowataka miongoni mwa viumbe vyake, Akawaafikia kuipata njia iliyolingana sawa, nayo ni Uislamu

    [26] Ni ya Waumini, waliofanya vizuri kumuabudu Mwenyezi Mungu,wakamtii katika yale Aliyowaamrisha na Akayakataza, Pepo na zaidi yake ambayo ni kuutazama Uso wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, huko Peponi, na kupata msamaha na radhi. Na wala nyuso zao hazitafinikwa na vumbi wala unyonge kama itakavyo kuwapata watu wa Moto. Hawa wanaosifika na sifa hizi ndio watu wa Peponi, ni wenye kukaa milele kabisa humo

    [27] Na wale waliofanya maovu ulimwenguni, wakakanusha na wakamuasi Mwenyezi Mungu, watapata mateso ya Mwenyezi Mungu huko Akhera ambayo ni malipo yanayofanana na matendo yao maovu waliyoyafanya, na watafinikwa na unyonge na utwevu. Na hawatapata yoyote mwenye kuzuia adhabu ya Mwenyezi Mungu isiwafikie Akitaka kuwatesa. Nyuso zao zitakuwa ni kama zilizovishwa sehemu za weusi wa usiku wenye giza. Hawa ndio watu wa Motoni wenye kukaa milele humo

    [28] Kumbuka, ewe Mtume, Siku ambayo tutawafufua viumbe wote ili wahesabiwe na walipwe, kisha tuseme kuwaambia waliomshirikisha Mwenyezi Mungu, «Jilazimisheni mahali mliopo, nyinyi na washirika wenu ambao mlikuwa mkiwaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, mpaka tuangalie mtafanya nini.» Hapo tutapambanua baina ya washirikina na wale wanaowaabudu, na watajitenga, wale walioabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu, na wale waliokuwa wanawaabudu, na watasema kuwaambia washirikina «Hamkuwa mkituabudu sisi ulimwenguni.»

    [29] Basi yatosha kuwa Mwenyezi Mungu ni Shahidi baina yetu na nyinyi. Hakika sisi hatukuwa tunayajua yale mliokuwa mkiyafanya. Na hakika sisi tulikuwa ni wenye kughafilika kuwa nyinyi mnatuabudu, hatukuwa tunalihisi hilo

    [30] Katika kisimamo hiko cha kuhesabiwa, kila nafsi itazipekua na kuziona hali zake na matendo yake, na italipwa kulingana na hayo : yakiwa ni mema atalipwa mema na yakiwa ni maovu atalipwa maovu. Na wote watarejeshwa kwa Mwenyezi Mungu Aliye Muamuzi Muadilifu. Hapo watu wa Peponi watatiwa Peponi, na watu wa Motoni watatiwa Motoni, na vitawaondokea washirikina vile ambavyo walikua wakiviabudu badala ya Mwenyezi Mungu kwa kumzulia Yeye urongo

    [31] Waambie, ewe Mtume, washirikina hawa, «Ni nani anayewaruzuku kutoka juu kwa mvua anayoiteremsha, na kutoka ardhini kwa mimea na miti aina mbalimabali anayoiotesha kutoka humo, ambayo miongoni mwayo mnakula nyinyi na wanyama wenu? Na ni nani anayemiliki hisia za kusikia na za kuona mnazostarehea, nyinyi na wengineo? Na ni nani anayemiliki uhai na kifo, katika ulimwengu wote, akawatoa wenye uhai na wafu, baadhi yao kutoka kwa wengine, katika viumbe mnavyovijua na msivyovijua? Na ni nani anayeyaendesha mambo ya mbinguni na ardhini na yaliyomo ndani yake, (anayeyaendesha) mambo yenu nyinyi na mambo ya viumbe vyote?» Watakujibu kwamba anayefanya yote hayo ni Mwenyezi Mungu. Waambie, «Basi si muogope mateso ya Mwenyezi Mungu mnapomuabudu mwingine pamoja na Yeye?»

    [32] Huyo Ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu! Yeye Ndiye kweli isiyo na shaka, Anayestahiki kuabudiwa Peke Yake, Asiye na Mshirika. Basi ni kitu gani kisichokuwa kweli isipokuwa ni upotevu? Basi vipi nyinyi mtaepushwa na kumuabudu Yeye muelekezwe kumuabudu asiyekuwa Yeye

    [33] Kama walivyokanusha washirikina hawa na walivyoendelea kwenye ushirikina wao, ndivyo lilivothibiti neno la Mola wako, hukumu Yake na uamuzi Wake juu ya wale waliotoka nje ya utiifu Wake wakaenda kumuasi na wakamkanusha, kwamba wao hawataamini upweke wa Mwenyezi Mungu wala unabii wa Nabii Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amawni zimshukiye, wala hawatafanya matendo yanayolingana na uongofu Wake

    [34] Sema, ewe Mtume, kuwaambia wao, «Je, kuna yoyote, miongoni mwa waungu wenu na waabudiwa wenu, mwenye kuanzisha kuumba chochote kisicho na asili (ya mfano uliotangulia) kisha akifanye kitoweke baada ya kukianzisha, kisha akirudishe kama namna kilivyokuwa kabla hajakifanya kitoweke?» Kwa hakika, wao hawawezi kufanya madai hayo. Sema, ewe Mtume, «Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Ndiye Anayeanzisha kuumba kisha Akakifanya kitoweke kile Alichokiumba, kisha Akakirudisha. Basi ni vipi nyinyi mnajiepusha na njia ya haki na kufuata ubatilifu, nao ni kumuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu?»

    [35] Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Je, kuna yoyote, miongoni mwa washirika wenu, mwenye kuongoza kwenye njia iliyolingana sawa?» Hakika wao hawawezi hilo. Waambie, «Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Anamuongoza aliyepotea njia ya uongofu na kumuelekeza kwenye haki. Basi ni yupi anayefaa zaidi kufuatwa: ni yule anayeongoza, peke yake, kwenye njia ya haki au ni yule ambaye haongoki, kwa kutojua kwake na kwa upotevu wake, nao ndio hao washirikina wenu ambao hawaongozi wala hawaongoki mpaka waongozwe? Basi muna nini nyinyi, vipi mnamsawazisha Mwenyezi Mungu na viumbe vyake?» Huu ni uamuzi uliotanguka

    [36] Na wengi wa washirikina hawa hawafuati, katika kuwafanya masanamu ni waungu na kuitakidi kwao kwamba hao masanamu wanawaleta karibu na Mwenyezi Mungu, isipokuwa urongo na dhana, nazo hazifai kitu mbele ya ukweli. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa wanayoyafanya washirikina hawa ya ukafiri na kukanusha

    [37] Haikuwa ni yenye kumkinika kwa yoyote kuja nayo Qur’ani hii kutoka kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, sababu ni kwamba hakuna yoyote awezae kufanya hilo miongoni mwa viumbe. Lakini Mwenyezi Mungu Aliiteremsha kusadikisha vitabu alivyowateremshia Manabii Wake, kwa kuwa dini ya Mwenyezi Mungu ni moja. Na katika hii Qur’ani kuna maelezo na ufafanuzi wa sheria ya Mwenyezi Mungu Aliyowaekea ummah wa Muhammad. Hapana shaka kwamba hii Qur’ani ni wahyi unaotoka kwa Mola wa viumbe wote

    [38] Au kwani wao wanasema kwamba Muhammad ameizua hii Qur’ani yeye mwenyewe? Wao wanajua kwamba yeye ni mwanadamu kama wao. Waambie, «Basi leteni sura moja inayofanana na hii Qur’ani katika mpango wake na uongozi wake, na takeni usaidizi wa kufanya hilo kwa mnayemuweza, badala ya Mwenyezi Mungu, miongoni mwa majini na binadamu, iwapo nyinyi ni wakweli katika madai yenu.»

    [39] Bali wao walifanya haraka kuikanusha Qur’ani mwanzo walipoisikia, kabla hawajazizingatia aya zake, na wakakikanusha kitu ambacho wao hawana ujuzi nacho, miongoni mwa habari ya Ufufuzi, Malipo, Pepo, Moto na vinginevyo, na bado haujawajia wao uhakika wa yale waliyoahidiwa katika Kitabu. Na kama walivyokanusha washirikina mambo Aliyowaonya nayo Mwenyezi Mungu, ndivyo walivyokanusha watu waliopita kabla yao. Basi tazama, ewe Mtume, ulikuwaje mwisho wa madhalimu? Baadhi yao Mwenyezi Mungu Aliwaangamiza kwa kuwadidimiza ardhini, wengine kwa kuwazamisha majini na wengine kwa kuwapa mateso mengineyo

    [40] Na miongoni mwa watu wako, ewe Mtume, kuna anayeiamini Qur’ani na miongoni mwao kuna asiyeiamini mpaka afe kwenye msimamo huo na afufuliwe juu yake. Na Mola wako ni Anawajua zaidi hao waharibifu ambao hawaiamini kwa njia ya udhalimu, ushindani na uharibifu, na Atawalipa juu ya uharibifu wao kwa adhabu iliyo kali zaidi

    [41] Na wakikukanusha, ewe Mtume, washirikina hawa waambie, «Mimi nina Dini yangu na matendo yangu, na nyinyi muna dini yenu na matendo yenu; nyinyi hamtaadhibiwa kwa matendo yangu, na mimi sitaadhibiwa kwa matendo yenu.»

    [42] Na miongoni mwa makafiri kuna wanaosikia maneno yako ya kweli na usomaji wako Qur’ani, lakini wao hawaongoki. Je, kwani wewe unaweza kuwasikizisha viziwi? Vilevile, huwezi kuwaongoa hawa isipokuwa Mwenyezi Mungu Atake kuwaongoa, kwa kuwa wao ni viziwi, hawaisikii haki na hawaielewi

    [43] Na miongoni mwao kuna wanaokutazama wewe na dalili za unabii wako wa kweli, lakini wao hawaioni nuru ya Imani Aliyokupa Mwenyezi Mungu. Je, unaweza , ewe Mtume, kuwaumbia vipofu macho ya kuwafanya wao waongoke. Vilevile huwezi kuwaongoa wao iwapo hawana busara. Hakika yote hayo yako kwa Mwenyezi Mungu

    [44] Mwenyezi Mungu Hawadhulumu watu kitu chochote, kwa kuwaongezea makosa yao na kuwapunguzia mema yao, lakini watu ndio wanaojidhulumu nafsi zao kwa kukufuru, kuasi na kwenda kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu na makatazo Yake

    [45] Na siku Mwenyezi Mungu Atawakusanya washirikina hawa, Siku ya kufufuliwa na kuhesabiwa, kama kwamba wao kabla ya hapo hawakukaa katika maisha ya duniani isipokuwa kadiri ya muda mchache wa kipindi cha mchana, watajuana wao kwa wao kama walivyokuwa duniani, kisha kujuana huko kutakatika na muda huo utapita. Hakika wamepata hasara wale waliokataa na kukanusha kuwa watakutana na Mwenyezi Mungu na kuwa Ana thwabu na Ana adhabu. Na hawakuwa ni wenye kuafikiwa kupata uongofu katika yale waliyoyafanya

    [46] Na iwapo tutakuonesha, ewe Mtume, katika uhai wako baadhi ya mateso tunayowaahidi duniani, au tukakufisha kabla hatujakuonesha hayo kwao, ni kwetu sisi peke yetu marejeo ya mambo yao katika hali zote mbili, kisha Mwenyezi Mungu ni Shahidi wa vitendo vyao waliokuwa wakivifanya duniani, hakuna chochote kati ya hivyo kinafichika Kwake, na Atawalipa malipo yao wanayostahiki kwa vitendo vyao hivyo

    [47] Na kila ummah uliopita kabla yenu, enyti watu, ulikuwa na mjumbe niliyemtuma kwao, kama nilivyomtuma Muhammad kwenu Alinganie kwenye Dini ya Mwenyezi Mungu na kuwa na utiifu Kwake. Basi huyo mjumbe wao atakapokuja Akhera, hapo kutaamuliwa baina yao kwa uadilifu, na wao hawatadhulumiwa katika malipo ya matendo yao chochote

    [48] Na washirikina katika watu wako, ewe Mtume, wanasema, «Ni lini kitasimama Kiyama iwapo wewe na waliokufuata ni miongoni mwa wakweli katika yale mnayotuahidi kwayo?»

    [49] Waambie, ewe Mtume, «Siwezi kuiepushia nafsi yangu madhara wala kuiletea manufaa isipokuwa Akiwa Mwenyezi Mungu Ametaka kuniepushia madhara au kuniletea manufaa. Kila watu wana wakati wa kumalizika muda wao na kipindi chao cha kuishi, basi ujapo wakati wa kumalizika kipindi chao cha kuishi na kukoma umri wao, hawatachelewa hata kwa muhula wa saa moja wala hautatangulia muda wa maisha yao mbele ya wakati maalumu

    [50] Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Nipeni habari ikiwajia adhabu ya Mwenyezi Mungu mchana au usiku, ni kitu gani mnachokifanyia haraka, enyi wahalifu, kuwa adhabu iteremke

    [51] Je, baada ya kushuka adhabu ya Mwenyezi Mungu kwenu, enyi washirikina, ndipo mtaamini, wakati ambapo Imani haitawafaa? Wakati huo mtaambiwa, ‘Je, sasa ndipo mnaamini na hapo nyuma mlikuwa mnaifanyia haraka?’»

    [52] Kisha wataambiwa waliozidhulumu nafsi zao kwa kumkanusha kwao Mwenyezi Mungu, «Onjeni adhabu ya Mwenyezi Mungu ya daima milele kwenu, kwani mnateswa isipokuwa ni kwa yale matendo ya kumuasi Mwenyezi Mungu mliokuwa mkiyafanya katika maisha yenu

    [53] Na hao washirikina miongoni mwa watu wako, ewe Mtume, wanataka uwape habari kuhusu adhabu Siku ya Kiyama, «Je, ni kweli hiyo? Waambie, ewe Mtume, «Ndio, naapa kwa Mola wangu, hiyo ni kweli isiokuwa na shaka.Na nyinyi si wenye kumlemea Mwenyezi Mungu Asiwafufue na kuwalipa, kwani nyinyi muko kwenye udhibiti wa Mwenyezi Mungu na mamlaka Yake

    [54] Na lau kwamba kila nafsi iliyomshirikisha na kumkanusha Mwenyezi Mungu itakuwa na vyote vilivyomo ardhini, na ikamkinika kuvifanya ni fidia yake ya kujikomboa na adhabu hiyo, ingalijikomboa kwavyo. Na wale ambao walidhulumu wataficha majuto yao watakapoiona adhabu ya Mwenyezi Mungu imewashukia wao wote. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, Atahukumu baina yao kwa uadilifu, na wao hawatadhulumiwa, kwa kuwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Hamuadhibu yoyote isipokuwa kwa dhambi zake

    [55] Jua utanabahi kwamba kila kilichoko mbinguni na ardhini ni milki ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, hakuna kitu chochote kati ya hivyo ni cha yoyote isipokuwa Yeye. Jua utanabahi kwamba kukutana na Mwenyezi Mungu kuko na adhabu Yake kwa washirikina ni yenye kuwa, lakini wengi wao hawaujui uhakika wa hilo

    [56] Hakika Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye kuhuisha na Mwenye kufisha, Hashindwi kuwahuisha watu baada ya kufa kwao, kama ambavyo hakumshindi Yeye kuwafisha Atakapo hilo. Na wao ni wenye kurejea Kwake baada ya kufa kwao

    [57] Enyi watu yamewajia nyinyi mawaidha kutoka kwa Mola wenu yanayowakumbusha mateso ya Mwenyezi Mungu na yanayowaonya makamio Yake, nayo ni Qur’ani na yale iliyoyakusanya ya miujiza na mawaidha ili kuzitengeneza tabia zenu na matendo yenu. Na ndani yake muna dawa ya yaliyomo nyoyoni ya ujinga na ushirikina na magonjwa mengineyo, na muna uongofu kwa viumbe wenye kuifuata iwaokoe na maangamivu. Mwanyezi mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, Ameijaalia ni neema na rehema kwa Waumini. Na Amewahusu Waumini kwa hilo, kwa kuwa wao ndio wenye kunufaika na Imani. Ama makafiri, hiyo Qur’ani kwao ni giza

    [58] Sema, ewe Mtume, kuwaambia watu wote, «Kwa wema wa Mwenyezi Mungu na rehema Yake, basi na wawe na furaha.» Wema wa Mwenyezi mungu na rehema Yake ni Uislamu ambao ni uongofu na ni Dini ya haki aliyokuja nayo Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwani Uislamu ambao Mwenyezi Mungu Amewaita wao waufuate, na Qur’ani ambayo Aliiteremsha kwa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye ni bora kuliko taka za ulimwengu wanazozikusanya na anasa zilizomo ndani yake zenye kutoeka kuondoka

    [59] Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa wanaokataa wahyi, «Nipeni habari juu ya hii riziki ya wanyama, mimea na vitu vizuri ambavyo Mwenyezi Mungu Amewaumbia nyinyi, mkajihalalishia baadhi ya hivyo na mkajiharamishia vinginevyo.» Waambie, «Je, Mwenyezi Mungu Amewaruhusu hilo au mnaongea maneno ya ubatilifu ya kumzulia Mwenyezi Mungu na mnasema urongo?» Hakika wao wanaongea maneno ya ubatilifu ya kumzulia Mwenyezi Mungu na wanasema urongo

    [60] Na hawa wanaomzulia Mwenyezi Mungu urongo, wakamnasibishia uharamishaji wa vitu ambavyo Yeye Hakuviharamisha kati ya riziki na vyakula, wanadhani kuwa Mwenyezi Mungu Atawafanya nini Siku ya Kiyama, siku ya wao kuhesabiwa, kwa urongo wao waliomzulia? Je,wanadhani kwamba Yeye Atawaacha na Atawasamehe? Mwenyezi Mungu Ana wema mwingi kwa viumbe Wake kwa kuacha Kwake kuyaharakisha mateso duniani kwa aliyemzulia urongo, na badala yake kumpa muhula. Lakini wengi zaidi wa watu hawamshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema wake juu yao kwa hilo

    [61] Na huwi, ewe Mtume, kwenye jambo lolote katika mambo yako, na husomi chochote kile katika aya za Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na hafanyi yoyote katika ummah huu tendo lolote lema au baya, isipokuwa sisi huwa ni mashahidi juu yenu ni wenye kuliona hilo, mnapolichukua na kulitenda, tukawahifadhia na tukawalipa kwalo. Na haufichamani na ujuzi wa Mwenyezi Mungu uzito wa chungu mdogo ardhini wala mbinguni, wala kitu kidogo kabisa wala kikubwa kabisa, isipokuwa kiko kwenye Kitabu kilichoko kwa Mwenyezi Mungu kilicho waziwazi chenye ufafanuzi, ujuzi Wake umekizunguka na Kalamu Yake imekiandika

    [62] Jueni mtanabahi kwamba mawalii wa Mwenyezi Mungu hawatakuwa na kicho cha mateso ya Mwenyezi Mungu Akhera, wala wao hawatasikitika juu ya hadhi za kilimwengu walizozikosa

    [63] Sifa za Mawalii hawa ni kwamba wao wamemuamini Mwenyezi Mungu na wamemfuata Mtume Wake na yale ambayo alikuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba wao wanamcha Mwenyezi Mungu kwa kuzifuata amri Zake na kuyaepuka matendo ya kumuasi

    [64] Mawalii hawa wana bishara njema kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuwa watapata ya kuwafurahisha katika maisha ya kilimwengu, na miongoni mwayo ni ndoto njema anayoiona mwenyewe au akaonewa na duguye, na watapata Pepo kesho Akhera. Mwenyezi Mungu Haendi kinyume na ahadi Yake wala Haigeuzi. Huko ndiko kufaulu kukubwa, kwa kuwa bishara hiyo imekusanya kuokoka na kila lifanyiwalo hadhari na kufaulu kupata kila litakwalo na kupendwa

    [65] Na yasikusikitishe, ewe Mtume, maneno ya washirikina juu ya Mola wao na kumzulia kwao Yeye urongo na kuishirikisha kwao mizimu ya masanamu pamoja na Yeye. Kwani Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyepwekeka kwa nguvu zilizokamilika na uwezo uliotimia, ulimwenguni na Akhera; na Yeye Ndiye Msikizi wa maneno yao Ndiye Mjuzi wa nia zao na matendo yao

    [66] Jueni mtanabahi kwamba ni wa Mwenyezi Mungu kila aliye mbinguni au ardhini miongoni mwa Malaika, binadamu, majini na wengineo. Na ni nini wanachofuata wale wanaowaomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu katika hao washirika? Hawana wanachokifuata isipokuwa shaka, na wao hawana lolote isipokuwa wanasema urongo katika yale ambayo wanamnasibisha nayo Mwenyezi Mungu

    [67] Yeye Ndiye Ambaye Amewaekea nyinyi, enyi wtu, usiku ili mtuliye ndani yake na mpumzike na usumbufu wa harakati za kutafuta maisha , na Amewaekea mchana ili muone ndani yake na muende mbio kutafuta riziki yenu. Hakika katika kupishana usiku na mchana na hali ya watu katiaka vipindi viwili hivyo pana dalili na hoja, kwa watu wanaozisikia hoja hizi na kuzitafakari, kwamba Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Ndiye Mstahiki wa kuabudiwa

    [68] Washirikina walisema, «Mwenyezi Mungu amejifanyia mwana» kama vile wanavyosema: ‘Malaika ni watoto wa kike wa Mwenyezi Mungu’, au ‘Al-Masīh( ni mwana wa Mwenyezi Mungu’. Mwenyezi Mungu Ametakasika na hayo yote na Ameepukana nayo! Yeye Ndiye Mkwasi Asiyemuhitajia kila asiyekuwa Yeye. Ni Vyake Yeye vyote vilivyoko kwenye mbingu na ardhi. Vipi basi Atakuwa na mwana miongoni mwa Aliyewaumba na hali ni kwamba kila kitu kinamilikiwa na Yeye? Na nyinyi hamuna dalili yoyote juu ya urongo mnaouzua. Je, mnasema kuhusu Mwenyezi Mungu maneno msiyoyajua ukweli wake na usawa wake)

    [69] Sema, «Hakika wale ambao wanamzulia Mwenyezi Mungu urongo, kuwa Amejifanyia mwana na kumuengezea mshirika, hawatapata matakwa yao ulimenguni wala Akhera.»

    [70] Hakika wao wanastarehe ulimwenguni, kwa ukafiri wao na urongo wao, starehe fupi. Kisha ukomapo muda wao wa kuishi, kuja kwetu ndio mwisho wao. Kisha tutawaonjesha adhabu ya Jahanamu kwa kumkufuru kwao Mwenyezi Mungu, kumkanusha kwao Mitume wa Mwenyezi Mungu na kupinga kwao aya Zake

    [71] Wasimulie, ewe Mtume, makafiri wa Maka habari ya Nūḥ, amani imshukiye, pamoja na watu wake alipowaambia, «Ikiwa imekuwa ni uzito kwenu kukaa kwangu na nyinyi kuwakumbusha hoja za Mwenyezi Mungu na dalili Zake, basi ni kwa Mwenyezi Mungu ndio mategemeo yangu, na matumaini yangu yako Kwake Yeye. Basi tayarisheni mambo yenu na waiteni washirika wenu, kisha msiyafanye mambo yenu yafichike bali yawe waziwazi yenye kuonekana, kisha amueni juu yangu mateso na mabaya mnayoyaweza wala msinipe muhula wa saa moja ya mchana

    [72] «Mkiupuuza mwito wangu, basi sikuwaomba malipo, kwa kuwa thawabu zangu ziko kwa Mwenyezi Mungu na malipo yangu yako juu Yake, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Peke Yake hakuna mwenye ushirika na Yeye, na nimeamrishwa niwe miongoni mwa wenye kufuata hukumu Yake.»

    [73] Basi wakamkanusha Nūḥ, watu wake katika yale Aliyowaitia kwayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo tulimuokoa Yeye na waliokuwa na Yeye kwenye jahazi, na tukawafanya wao washikilie nafasi ya waliokanusha katika ardhi, na tukawazamisha wale waliokataa hoja zetu. Hivyo basi, fikiria, ewe Mtume, namna ulivyokuwa mwisho wa watu wale ambao Mtume wao Aliwaonya adhabu ya Mwenyezi Mungu na mateso Yake

    [74] Kisha tukatuma, baada ya Nūḥ, Mitume kwenda kwa watu wao (Hūd, Ṣāliḥ„ Ibrāhīm, Lūṭ„ Shu'ayb na wengineo), kila Mtume Alikuja kwa watu wake kwa miujiza yenye kuonesha dalili ya utume Wake na ukweli wa yale aliyowaitia. Hawakuwa ni wenye kuyaamini wala kuyafanya yale ambayo watu wa Nūḥ na waliowatangulia miongoni mwa ummah waliopita. Na kama alivyopiga mhuri Mwenyezi Mungu juu ya nyoyo za hawa watu wasiamini, hivyo ndivyo anavyopiga mhuri juu ya nyoyo za wanaofanana na wao kati ya waliokuwa baada yao, miongoni mwa wale ambao walivuka mipaka ya Mwenyezi Mungu na wakaenda kinyume na yale, ambayo Mitume wao waliwaitia kwayo, ya kumtii Yeye, ikiwa ni mateso kwao kwa sababu ya matendo yao ya uasi

    [75] Kisha tukawatuma, baada Mitume hao, Mūsā na Hārūn, amani iwashukie, kwenda kwa Fir'awn na watukufu wa watu wake, wakiwa na miujiza yenye kuonesha dalili ya ukweli wao, wakafanya kiburi kwa kukataa kuikubali haki na wakawa ni watu washirikina, wahalifu na wakanushaji

    [76] Huo ukweli, ambao Alikuja nao Mūsā, ulipomfikia Fir'awn na watu wake, walisema, «Hakika miujiza aliyokuja nayo Mūsā ni uchawi mtupu ulio waziwazi.»

    [77] Mūsā aliwaambia akiona ajabu kwa maneno yao, «Mnaiyambia haki ilipowajia kuwa ni uchawi? Tazameni sifa za kitu kilichowajia na vilivyomo ndani yake, mtakikuta ni ukweli. Na wachawi hawafaulu wala hawafuzu ulimwenguni wala Akhera.»

    [78] Fir'awn na kundi lake wakasema kumwambia Mūsā, «Je, umetujia kutuepusha na yale ambayo tuliwakuta nayo wazazi wetu ya kuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu, mupate kuwa na utukufu na mamlaka, wewe na Hārūn, katika ardhi ya Misri? Basi sisi si wenye kukubali kwamba wawili nyinyi ni Mitume mliotumwa kwetu ili tumuabudu Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Asiye na mshirika.»

    [79] Na akasema Fir'awn, «Nileteeni kila mchawi mwenye uhodari wa uchawi.»

    [80] Wachawi walipomjia Fir'awn, Mūsā aliwaambia, «Tupeni chini kamba zenu na fimbo zenu mlizonazo.»

    [81] Walipozitupa kamba zao na fimbo zao, Mūsā aliwaambia, «Mlivyokuja navyo mkavitupa ni uchawi. Mwenyezi Mungu Ataviondoa mlivyokuja navyo na atavitangua. Hakika Mwenyezi Mungu Hakitengenezi kitendo cha anayetembea katika ardhi ya Mwenyezi Mungu kufanya mambo Anayoyachukia na kufanya uharibifu humo kwa kumuasi

    [82] Na Mwenyezi Mungu Atauimarisha ukweli niliokuja nao kutoka Kwake Ataufanya uwe juu ya ubatilifu wenu kwa maneno Yake na amri Yake, ingawa watu wahalifu wenye kufanya maasia, miongoni mwa jamaa za Fir'awn, wanachukia

    [83] Na hawakumuamini Mūsā, amani imshukiye, pamoja na hoja na dalili alizowaletea, isipokuwa kizazi cha watu wake, Wana wa Isrāīl, hali ya kuwa wao wana uoga na Fir'awn na kundi lake wasiwatese kwa kuwaadhibu na wasiwazuie na Dini yao. Na hakika Fir'awn ni mjeuri mwenye kiburi katika ardhi, na hakika Yeye ni miongoni mwa waliopita mpaka katika ukafiri na uharibifu

    [84] Na akasema Mūsā, «Enyi watu wangu, mkimuamini Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, na mkafuata sheria Yake, kuweni na imani na Yeye na jisalimisheni kwa amri Yake. Na kwa Mwenyezi Mungu jitegemezeni iwapo nyinyi ni wenye kumdhalilikia kwa utiifu

    [85] Watu wa Mūsā walisema kumwambia, «Tumemtegemea Mwenyezi Mungu Peke Yake Asiye na mshirika na tumemwachia Yeye mambo yetu. Ewe Mola wetu, usiwape ushindi juu yetu ikawa ni mtihani kwetu katika Dini yetu, au ikawa ni mtihani kwa makafiri kwa kupata ushindi wakasema: lau wao (wenye kumuamini Mūsā) wako kwenye haki hawangalishindwa

    [86] «Na utuokoe, kwa rehema yako, kutokana na watu makafiri, Fir'awn na kundi lake.» Kwani wao walikuwa wakiwalazimisha kufanya kazi ngumu

    [87] Na tuliwapelekea wahyi Mūsā na Hārūn kwamba watengezeeni watu wenu katika Misri majumba yenye kuwa ni makao na mahali pa hifadhi pa kukimbilia, na myafanye majumba yenu kuwa ni mahali pa kuswali ndani yake mkiwa na uoga, na tekelezeni Swala za faradhi kwa nyakati zake. Na wape Waumini wenye kumtii Mwenyezi Mungu bishara njema ya nguvu ya ushindi na thawabu nyingi kutoka Kwake, kutakata ni Kwake na kutukuka

    [88] Na Mūsā akasema, «Mola wetu, hakika wewe umempa Fir'awn na watukufu wa watu wake pambo la vitu vya duniani wasikushukuru, na wamejisaidia kwa vitu hivyo katika kupotoa watu na njia Yako. Mola wetu, yageuze Mali yao wasifaidike nayo, na uzipige mhuri nyoyo zao zisipate kuikunjukia Imani, wasiamini mpaka waione adhabu kali iumizayo.»

    [89] Akasema Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kuwambia wao wawili, «Yameshakubaliwa maombi yenu juu ya Fir'awn na kundi lake na mali zao,- Mūsā alikuwa akiomba, na Hārūn akiitika maombi yake, ndipo ikafaa kuyanasibisha maombi kwa wao wawili,- basi jikiteni kwenye Dini yenu na muendelee kumlingania Fir'awn na watu wake kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtii, na msifuate njia ya asiyejua ahadi yangu njema na onyo langu.»

    [90] Na tuliwakatia bahari Wana wa Isrāīl mpaka wakaivuka, wakafuatwa na Fir'awn na askari wake, kwa udhalimu na uadui, wakafuata njia ya bahari nyuma yao, mpaka Fir'awn alipozungukwa na hali ya kuzama alisema kwamba hapana Mola isipokuwa yule ambaye Wana wa Isrāī wamemuamini, na mimi ni miongoni mwa wenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu wenye kujisalimisha Kwake kwa kufuata na kutii

    [91] Je, sasa hivi, ewe Fir'awn, wakati kifo kimekushukia ndipo, unakubali kuwa wewe ni mja wa Mwenyezi Mungu na hali ulimuasi na ukawa ni miongoni mwa waharibifu wenye kuzuia njia Yake kabla ya adhabu Yake kukushukia! Basi toba haitokunufaisha wakati wa kukata roho na kushuhudia kifo na adhabu

    [92] Leo tutakujaalia uwe kwenye muinuko wa ardhi kwa mwili wako, akutazame mwenye kukanusha kuangamia kwako, ili uwe ni mazingatio kwa watu wenye kuja baada yako kuwaidhika na wewe. Na hakika wengi zaidi kati ya watu ni wenye kughafilika na hoja zetu na dalili zetu, hawazifikirii wala hawazizingatii

    [93] Hakika tuliwashukisha Wana wa Isrāīl mashukio mazuri yaliyoteuliwa katika miji ya Sham na Misri na tukawaruzuku riziki ya halali iliyo nzuri itokanayo na mazuri ya ardhi iliyobarikiwa. Na hawakutafautiana, katika mambo ya Dini yao isipokuwa baada ya kujiwa na ujuzi wa kuwafanya wao wawe pamoja na washikane, miongoni mwao ni yale yaliyomo ndani ya Taurati kuhusu habari ya unabii wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye. Kwa kweli, Mola wako, ewe Mtume, Atahukumu baina yao Siku ya Kiyama na Atatoa uamuzi katika yale waliokuwa wakitafautiana juu yake kuhusu mambo yako, wapate kuingia wakanushaji Motoni na Waumini Peponi

    [94] Basi uwapo na shaka,ewe Mtume, juu ya ukweli wa yale tuliyokupa habari yake, waulize wanaosoma Kitabu kabla yako miongoni mwa watu wa Taurati na Injili. Kwani hilo limethibiti kwenye vitabu vyao. Hakika umejiwa na ukweli wa yakini, kutoka kwa Mola wako, kwamba wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na kwamba hawa Mayahudi na Wanaswara wanajua ukweli wa hilo na wanapata sifa zako katika vitabu vyao, lakini wao wanalikataa hilo pamoja na kuwa walijua. Basi usiwe ni miongoni mwa wenye kufanya shaka juu ya usawa wa hilo na ukweli wake. Makusudio ya aya hii ni kusimamisha hoja kwa washirikina kwa ushahidi wa Watu wa Kitabu kati ya Wayahudi na Wanaswara ili kuukata udhuru wao

    [95] Na usiwe, wala usiwe, ewe Mtume, ni miongoni mwa waliokanusha hoja za Mwenyezi Mungu na dalili Zake, ukawa ni katika waliopata hasara ambao Mwenyezi Mungu Amewakasirikia na wamepata mateso Yake

    [96] Hakika ya wale ambao limethibiti kwao neno la Mola Wako la kuwafukuza kwenye rehema Yake na kuwaadhibu, hawaziamini hoja za Mwenyezi Mungu, hawaukubali upweke Wake wala hawazifuati sheria Zake kivitendo

    [97] Hata kama yatawajia wao kila mawaidha na mazingatio mpaka waishuhudie adhabu yenye kuumiza. Hapo wataamini, na haitawafaa Imani yao

    [98] Imani haikuwafaa watu wa mji wowote walioamini walipoishuhudia adhabu isipokuwa watu wa mji wa Yunus mwana wa Matta. Kwani wao walipohakikisha kwamba adhabu ni yenye kuwashukia, walirejea kwa Mwenyezi Mungu kwa kutubia kidhati; na ulipofunuka ukweli wa toba yao, Mwenyezi Mungu aliwaondolea adhabu ya hizaya baada ya kuwa karibu na wao, na Akawaacha ulimwenguni wakisterehe mpaka muda wao wa kuishi kukoma

    [99] Na lau Mola wako, ewe Mtume, Aliwatakia Imani watu wa duniani wote, wangaliyaamini, kwa umoja wao, yale uliyokuja nayo, lakini Yeye ana hekima katika hilo. Yeye Anamuongoza Anayemtaka na Anampoteza Anayemtaka, kulingana na hekima Yake, na haliko kwenye uwezo wako jambo la kuwatendesha nguvu watu juu ya kuamini

    [100] Haikuwa nafsi yoyote ni yenye kumuamini Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa idhini Yake na taufiki Yake. Basi usiisumbue nafsi yako katika hilo, kwani mambo yao yako kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu Ataajaalia adhabu na hizaya kwa wale ambao hawayatii akilini maamrisho Yake na makatazo Yake

    [101] Sema, ewe Mtume, kuwaambia watu wako, «Fikirini na mzingatie kwa yaliyomo mbinguni na ardhini miongoni mwa aya za Mwenyezi Mungu zilizo waziwazi.» Lakini aya, mazingatio na Mitume wenye kuwaonya waja wa Mwenyezi Mungu adhabu Yake, vyote hivyo havikuwa ni vyenye kuwanufaisha watu wasioamini chochote katika hivyo, kwa sababu ya kupa mgongo kwao na ujeuri wao

    [102] Je, hawa wanangojea isipokuwa hiyo siku watakapoishuhudia adhabu ya Mwenyezi Mungu mfano wa siku za wakale wao waliokanusha waliopita kabla yao? Sema, ewe Mtume, «Ingojeeni adhabu ya Mwenyezi Mungu; hakika mimi ni mwenye kuingojea pamoja na nyinyi kuteswa kwenu.»

    [103] Kisha tutawaokoa Mitume wetu na wale walioamini pamoja na wao. Na kama tulivyowaokoa hao tutakuokoa wewe, ewe Mtume, na waliokuamini wewe kwa wema utokao kwetu na rehema

    [104] Sema, ewe Mtume, kuwaambia watu hawa, «Iwapo muko kwenye shaka juu ya usawa wa Dini yangu ambayo nimewaitia kwayo, nayo ni Uislamu, na juu ya uthabiti wangu na kujikita kwangu juu yake, pamoja ya kuwa nyinyi muna matumaini ya kuniepusha nayo, basi mimi sitamuabudu katika hali yoyote ile, yoyote miongoni mwa wale mnaowaabudu mkajifanyia masanamu na mizimu, lakini namuabudu Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Mwenye kuwafisha na kuzitwaa roho zenu, na nimeamrishwa niwe ni miongoni mwa wenye kumuamini na wenye kufuata Sheria Zake kivitendo.»

    [105] Na ujisimamishe imara, ewe Mtume, juu ya dini ya Uislamu, hali ya kulingana sawa juu yake, usiwe ni mwenye kupotoka na kuwa kando nayo ukaelekea kwenye Uyahudi au Unaswara wala kumuabudu asiyekuwa Yeye. Wala usiwe ni miongoni mwa wale wanaoshirikisha, katika ibada ya Mola wao, waungu na wale wanaodai kuwa wanafanana na Yeye, kwani ufanyapo hilo utakuwa ni miongoni mwa watakaoangamia. Maneno haya ingawa anaambiwa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, pia wanaambiwa umma wote

    [106] Wala usiwaombe, ewe Mtume, wasiokuwa Mwenyezi Mungu miongoni mwa mizimu na masanamu, kwani wao hawanufaishi wala hawadhuru. Na ufanyapo hilo na ukawaomba wasiokuwa Mwenyezi Mungu, hapo wewe utakuwa ni miongoni mwa wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, wenye kujidhulumu nafsi zao kwa ushirikina na kufanya maasia. Maneno haya ingawa anaambiwa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, pia wanaambiwa umma wote

    [107] Na Mwenyezi Mungu Akikupatia, ewe Mtume, shida au mitihani, basi hakuna wa kuyaondoa hayo isipokuwa Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu, na Akikutakia furaha na neema, basi hakuna yoyote mwenye kuyazuia hayo. Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, Anampatia furaha na shida Anayemtaka kati ya waja Wake. Na Yeye ni Mwingi wa msamaha wa dhambi za wenye kutubia, ni Mwingi wa rehema kwa wanaomuamini na kumtii

    [108] Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa watu, «Amewajia nyinyi Mtume wa Mwenyezi Mungu na Qur’ani ambayo ndani yake muna maelezo ya kuwaongoa nyinyi. Basi mwenye kuongoka kwa uongofu wa Mwenyezi Mungu, hakika matunda ya kitendo chake yatamrudia yeye mwenyewe. Na mwenye kupotoka akawa kando na haki na akaendelea kwenye upotevu, hakika upotevu wake na madhara yake yatamshukia yeye mwenyewe. Na mimi si kuwakilishwa kwenu mpaka muwe Waumini. Mimi ni mjumbe mwenye kufikisha , nawafikishia yale niliyotumwa kwayo

    [109] Na uufuate, ewe Mtume, wahyi wa Mwenyezi Mungu Aliokutumia wewe na uutumie kivitendo. Na uwe na subira katika kumtii Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na katika kujiepusha na mambo ya kumuasi na kwa kuvumilia makero ya wenye kukukera katika kuufikisha ujumbe Wake, mpaka Mwenyezi Mungu Atoe uamuzi Wake kwao na kwako. Na Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu, Ndiye mbora wa kutoa uamuzi, kwa kuwa uamuzi Wake unakusanya uadilifu uliokamilika

    Hud

    Surah 11

    [1] Alif, Lām, Rā’. Maneno yashatangulia, kuhusu herufi zinazokatwa, katika mwanzo wa Sura ya Al-Baqarah. Hiki ni Kitabu ambacho Mwenyezi Mungu Amemteremshia Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, na ambacho aya zake zimepangwa vizuri zisizo na kasoro wala ubatilifu, kisha zimefafanuliwa kwa maamrisho na makatazo na maelezo ya halali na haramu yatokayo kwa Mwenyezi Mungu Aliye na hekima katika uendeshaji mambo Aliye Mtambuzi wa vile yanavyoishia

    [2] Na kuteremsha Qur’ani na kuzifafanua hukumu zake na kuzipambanua na kuipanga vizuri, ili mpate kumuabudu Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Asiye na mshirika. Mimi kwenu nyinyi, enyi watu, ni muonyaji kutoka kwa Mwenyezi Mungu mwenye kuwaonya mateso Yake na ni mwenye kuwabashiria habari njema ya malipo Yake mema

    [3] Na muombeni Awasamehe dhambi zenu kisha mrudi Kwake hali ya kujuta, Atawapumbaza katika ulimwengu wenu kwa kuwastarehesha vizuri kwa maisha mazuri humo mpaka ufikie kikomo muda wenu wa kuishi na Ampe kila mwenye wema wa elimu na matendo malipo makamilifu ya wema wake yasiyo na upungufu. Na mkiyapa mgongo yale ninayowaitia kwayo, basi nawachelea nyinyi kufikiwa na adhabu ya Siku ngumu, nayo ni Siku ya Kiyama. Hili ni onyo kali kwa aliyezipa mgongo amri za Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na akawakanusha Mitume Wake

    [4] Ni kwa Mwenyezi Mungu marejeo yenu baada ya kufa kwenu nyote, basi jitahadharini na mateso Yake. Na Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, ni Muweza wa kuwafufua nyinyi, kuwakusanya na kuwalipa

    [5] Hakika washirikina hawa wanaficha ukafiri katika nyoyo zao wakidhani kwamba yale ambayo nafsi zao zinayadhamiria yanafichika kwa Mwenyezi Mungu. Kwani hawajui wanapoifinika miili yao kwa nguo zao kwamba hayafichiki kwa Mwenyezi Mungu mambo yao ya siri na ya wazi? Hakika Yeye ni Mjuzi wa kila ambacho vifua vyao vinakifinika miongoni mwa nia, madhamirio na siri

    [6] Mwenyezi Mungu Amechukua dhamana kuviruzuku vyote vinavyotambaa kwenye uso wa ardhi, kwa hisani Yake, na Anajua mahala pa kutulia kwake katika uhai wake na baada ya kufa kwake, na Anajua mahala ambapo vitakufa. Yote hayo yameandikwa kwenye Kitabu kilichoko kwa Mwenyezi Mungu chenye kueleza yote hayo

    [7] Na Yeye Ndiye Ambaye Aliumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake kwa Siku Sita na Arshi Yake ilikuwa iko juu ya maji kabla ya hapo, Apate kuwajaribu nyinyi, ni nani kati yenu mzuri zaidi wa utiifu na utendaji. Utendaji wenye kumtakasia Mwenyezi Mungu, wenye kulingana na vile Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, alivyokuwa. Na lau unasema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina wa watu wako, «Nyinyi mtafufuliwa mkiwa hai baada ya kufa kwenu.» Watafanya haraka kukanusha na watasema, «Haikuwa hii Qur’ani unayotusomea isipokuwa ni uchawi ulio wazi.»

    [8] Na lau tutawacheleweshea adhabu, hawa washirikina, mpaka muda maalumu, wakaona imekawia, watasema kwa njia ya shere na kukanusha, «Ni kitu gani kinachozuia adhabu hii isitukie ikiwa ni kweli?» Jueni mtanabahi, siku itakapowajia adhabu hiyo hakuna atakayeweza kuwaondolea, wala yoyote mwenye kuizuia, na iatawazunguka wao, kutoka kila upande, adhabu waliokuwa wakiifanyia shere kabla haijawajia

    [9] Na lau tutampa mwanadamu neema ya afya na amani na zisokuwa hizo kisha tukamuondolea, hakika yeye atakuwa ni mwenye kukata tamaa sana na rehema ya Mwenyezi Mungu, ni mkanushaji sana wa neema ambazo Mwenyezi Mungu Amemneemesha nazo

    [10] Na lau tutamnyoshea mwanadamu dunia yake na tukamkunjulia riziki yake baada ya dhiki za maisha, atasema hapo, «Nimeondokewa na dhiki na shida.» Hakika yeye ni mwenye kujigamba kwa hizo neema, ni mwenye kuendelea sana katika kujifahiri na kujitukuza kwa watu

    [11] Lakini wale waliosubiri juu ya yaliyowapata ya shida kwa kumuamini Mwenyezi Mungu na kutaka malipo kutoka Kwake, wakafanya mema kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema Zake, wao watakuwa na msamaha wa dhambi zao na malipo makubwa Akhera

    [12] Huenda wewe, ewe Mtume, kwa ukafiri na ukanushaji mkubwa unaouona kwao, ukawa ni mwenye kuyaacha baaadhi ya yale unaoyoletewa wahyi kati ya yale ambayo Mwenyezi Mungu Alikuteremshia na Akakuamuru kuyafikisha, na kifua chako kikawa ni chenye kuhisi dhiki kwa hayo, kwa kuogopa wasije wakataka baadhi ya mambo kutoka kwako kwa njia ya kukusumbua, kama vile kusema, «Kwa nini asiteremshiwe mali mengi, au asijiwe na Malaika ambaye atamuamini katika ujumbe wake?» Basi wafikishie yale niliyokuletea wahyi kwayo, kwani lako wewe si lingine isipokuwa ni kuonya kwa yale uliyoletewa wahyi. Na Mwenyezi Mungu ni Mtunzi wa kila kitu, Anaendesha mambo yote ya viumbe vyake

    [13] Au je, washirikina hawa, miongoni mwa watu wa Makkah, wanasema kwamba Muhammad ameizua hii Qur’ani? Waambie basi, «Iwapo mambo ni kama mnavyodai, leteni sura kumi mfano wake za kuzuliwa, na muwaite mnaowaweza miongoni mwa viumbe wote wa Mwenyezi Mungu, ili wawasaidie kuzileta hizi sura kumi, iwapo nyinyi ni wa kweli katika madai yenu

    [14] Iwapo washirikina hawa hawatawaitikia nyinyi, ewe Mtume na walio pamoja na wewe, kwa yale mnayowaitia , kwa kulemewa kufanya hivyo, basi jueni kwamba hii Qur’ani, kwa hakika Mwenyezi Mungu Amemteremshia Mtume Wake kwa ujuzi Wake, na si maneno ya binadamu. Na jueni kwamba hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu. Je nyinyi, baada ya kusimama hoja hii kwenu, ni wenye kujisalimisha, ni wenye kunyosha shingo kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake

    [15] Yoyote atakaye, kwa matendo yake, maisha ya kilimwengu na starehe zake, tutawapa wao walichogawiwa cha malipo mazuri ya matendo yao katika uhai wa kilimwengu, yakiwa kamili yasiyopunguzwa

    [16] Hao hawana huko Akhera isipokuwa Moto wa Jahanamu wakiadhibika kwa joto lake, na yatawaondokea wao manufaa na yale mema waliyoyatenda, na matendo yao yatatanguka kwa kuwa hayakuwa yanakusudiwa Mwenyezi Mungu

    [17] Je, yule aliyekuwa kwenye hoja na uangalifu kutoka kwa Mola wake katika kile anachokiamini na anachokilingania kwa wahyi ambao ndani yake Mwenyezi Mungu Ameuteremsha ushahidi huu, na ukafuatiwa na hoja nyingine kutoka Kwake yenye kuutolea ushahidi, nayo ni Jibrili au ni Muhammad, rehema na amani ziwashukie, na ukatiliwa nguvu na dalili ya tatu kabla ya Qur’ani, nayo ni Taurati - Kitabu alichotemshiwa Mūsā chenye uongozi na rehema kwa waliokiamini- (je yeye) ni kama yule ambaye hamu yake ilikuwa ni maisha yenye kutoweka na pambo lake? Hao wanaiamini hii Qur’ani wanazifuata hukumu zake kivitendo. Na mwenye kuikanusha hii Qur’ani, miongoni mwa wale waliojikusanya kumpinga Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, basi malipo yake ni Moto, hapana budi atauingia. Basi usiwe na shaka juu ya jambo la Qur’ani na kuwa inatoka kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka baada ya dalili na hoja kulitolea ushahidi hilo. Na ujue kwamba Dini hii ndio ukweli unaotoka kwa Mola wako, lakini wengi wa watu hawaamini wala hawayatendi yale wanayoamrishwa. Huu ni muongozo unaowaenea ummah wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [18] Na hakuna yoyote aliye dhalimu zaidi kuliko yule aliyemzulia Mwenyezi Mungu urongo. Hao wataorodheshwa kwa Mola wao Siku ya Kiyama, ili Awahesabu kwa matendo yao. Na watasema waliohudhuria miongoni mwa Malaika na Manabii na wengineo, «Hawa ndio wale waliosema urongo kumsingizia Mola wao ulimwenguni. Mwenyezi Mungu Amewakasirikia wao na Amewalaani laana isiyokatika, kwa kuwa udhalimu walioufanya umekuwa ni sifa inayoambatana na wao

    [19] Hawa madhalimu ni wale ambao wanawazuia watu na njia ya Mwenyezi Mungu yenye kupelekea kumuubudu na wanataka njia hizi ziwe kombo ziambatane na matamanio yao na wao wanaikanusha Akhera, hawaamini kufufuliwa wa kulipwa

    [20] Makafiri hao hawakuwa ni wenye kumhepa Mwenyezi Mungu kwa kumkimbia, na hawakuwa na wasaidizi wa kuwazuia wao wasipata mateso ya Mwenyezi Mungu. Wataongezewa adhabu katika Jahanamu, kwa kuwa wao walikuwa hawawezi kuisikia Qur’ani kwa namna ya kuwafanya wanufaike au wazione alama za Mwenyezi Mungu katika ulimwengu kwa namana ya kuwafanya waongoke, kwani wao walikuwa wameshughulika na ukafiri ambao walikuwa wamedumu nao

    [21] Hao ndio wale waliopata hasara ya nafsi zao kwa kumzulia kwao Mwenyezi Mungu urongo na waliwaondokea wao wauungu waliokuwa wakiwazua na kudai kwamba wao watawaombea

    [22] Ukweli ni kwamba wao kesho Akhera ni wenye kapata hasara zaidi kibiashara, kwa kuwa wao waliacha daraja za Pepo na kuchukuwa mashimo ya Moto, kwa hivyo wakawa kwenye Moto wa Jahanamu. Huko ndiko kupata hasara waziwazi

    [23] Hakika wale ambao walimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafanya matendo mema, wakanyenyekea kwa Mwenyezi Mungu katika kila walichoamrishwa na kukatazwa. Hao ndio watu wa Peponi, hawatakufa humo wala hawatatoka kabisa

    [24] Mfano wa makundi mawili, ya ukafiri na Imani, ni mfano wa kipofu asiyeona na kiziwi asiyesikia na yule anayeona na kusikia: kundi la ukafiri haliioni haki likapata kuifuata wala halimsikii mlinganizi wa Mwenyezi Mungu likapata kuongoka kwa sababu yake. Ama kundi la Imani limishaziona hoja za Mwenyezi Mungu na limemsikia mlinganizi wa Mwenyezi Mungu na limemuitikia. Je, yanafanana makundi mawili haya? Kwani hamzingatii na mkafikiri

    [25] Hakika tulimtuma Nūḥ, kwa watu wake akasema kuwaambia, «Mimi ni muonyaji kwenu adhabu ya Mwenyezi Mungu, ni mwenye kuwabainishia yale niliyotumwa kwenu ya maamrisho ya Mwenyezi Mungu na makatazo yake

    [26] «Nawaamrisha kwamba msiabudu isipokuwa Mwenyezi Mungu. Mimi nawachelea nyinyi, mkitompwekesha Mwenyezi Mungu, Peke Yake, kwa Ibada, adhabu ya Siku yenye kuumiza.»

    [27] Wakasema wakubwa wa ukafiri miongoni mwa watu wake, «Wewe si Malaika bali wewe ni binadamu, inakuwaje wewe uletewe wahyi bila sisi? Na hatukuoni umefuatwa isipokuwa na watwevu wetu, na wao wamekufuata bila kufikiria wala kupima. Na sisi hatuwaoni nyinyi kuwa muna ubora wowote juu yetu, wa riziki wala mali, tangu mlipoingia kwenye dini yenu hii. Bali sisi tunaamini kwamba nyinyi ni warongo katika madai yenu

    [28] Nūḥ akasema, «Enyi watu wangu, iwapo mimi niko kwenye hoja iliyo wazi kutoka kwa Mola wangu katika yale niliyokuja nayo kutoka Kwake, itawafunukia nyinyi kwamba mimi niko kwenye haki inayotoka Kwake na kwamba Ameniletea rehema kutoka Kwake, nayo ni unabii na utume na kwamba Mwenyezi Mungu Amewafichia hayo kwa sababu ya ujinga wenu na kuhadaika kwenu. Basi je kwani inafaa niwalazimishe nayo kwa nguvu hali nyinyi mnaikanusha? Hatutafanya hivyo, lakini tunayategemeza mambo yenu kwa Mwenyezi Mungu ili Atoe uamuzi Anaoutaka kuhusu mambo yenu

    [29] Nūḥ, amani imshukiye, akaendelea kuwaambia watu wake, «Enyi watu wangu, siwaombi kwa kuwaita nyinyi kumpwekesha Mwenyezi Mungu, munipatie mali baada ya kuamini kwenu, kwani malipo ya ushauri wangu kwenu yako kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake. Na si shughuli yangu mimi kuwafukuza Waumini, kwani wao ni wenye kukutana na Mola wao Siku ya Kiyama. Lakini mimi nawaona nyinyi kuwa ni watu msiojua, kwa kuwa mnaniamrisha niwafukuze vipenzi vya Mwenyezi Mungu na niwaepushe na mimi

    [30] «Na enyi watu wangu, ni nani mwenye kunizuia mimi na Mwenyezi Mungu Akinitesa kwa kuwafukuza kwangu Waumini? Kwani hamyazingatii mambo mkayajua yenye nafuu zaidi kwenu na yenye kufaa zaidi

    [31] «Na wala siwaambii nyinyi kuwa mimi nina mahazina ya Mwenyezi Mungu, wala mimi siyajui yasiyoonekana, na mimi si mmoja kati ya Malaika, wala siwaambii hawa mnaowadharau miongoni mwa madhaifu wa Waumini kwamba Mwenyezi Mungu hatawapa malipo mema ya matendo yao. Mwenyezi Mungu, Peke Yake, ni Mjuzi kabisa kwa yaliyomo ndani ya vifua vyao na nyoyo zao. Na nikifanya hivyo, basi mimi wakati huo nitakuwa ni miongoni mwa wale wenye kujidhulumu wao wenyewe na kuwadhulumu wengineo»

    [32] Wakasema, «Ewe Nūḥ„ umelumbana na sisi na umezidisha katika malumbano yako kwetu, basi tuletee hiyo adhabu unayotuahidi, iwapo wewe ni miongoni mwa wakweli katika madai yako.»

    [33] Nūḥ, akasema kuwaambia watu wake, «Mwenyezi Mungu , Peke Yake, Ndiye Atakayewaletea nyinyi adhabu atakapo, na nyinyi si wenye kuiponyoka Akitaka kuwaadhibu, kwani Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, hakuna chochote chenye kumlemea katika ardhi wala katika mbingu

    [34] «Na hautawanufaisha nyinyi ushauri wangu na bidii yangu katika kuwalingania kwenye Imani, iwapo Mwenyezi Mungu Anataka kuwpoteza na kuwaangamiza. Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye mwenye kuwamiliki, na Kwake Yeye mtarejeshwa kesho Akhera kwa kuhesabiwa na kulipwa.»

    [35] Au je, wanasema hawa washirikina miongoni mwa watu wa Nūḥ, kwamba Nūḥ, amezua neno hili? Waambie, «Nikiwa nimemzulia urongo Mwenyezi Mungu hilo, basi ni juu yangu mimi, peke yangu, dhambi ya hilo; na nikiwa ni mkweli, basi nyinyi ndio wahalifu wenye dhambi, na mimi niko mbali na ukfiri wenu, ukanushaji wenu uhalifu wenu

    [36] Na Mwenyezi Mungu, Aliyetakata na sifa za upungufu na kutukuka, Alimletea wahyi Nūḥ„ amani imshukiye, ilipolazimika adhabu juu ya watu wake kwamba hawatamuamini Mwenyezi Mungu isipokuwa walioamini kabla ya hapo, «basi usisikitike, ewe Nūḥ„ juu ya yale waliokuwa wakiyafanaya

    [37] «Na utengeneze jahazi kwa maangalizi yetu na kwa amri yetu na msaada wetu, hali ya kuwa wewe uko kwenye utunzi wetu na hifadhi yetu, na usitake kwangu kuwapa muhula hawa waliojidhulumu nafsi zao, miongoni mwa watu wako, kwa ukafiri wao, kwani wao ni wenye kuzamishwa kwa mafuriko.» Katika hii aya pana kuthibitisha sifa ya 'ayn (jicho ) kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kwa namna inavyonasibiana na Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake

    [38] Na Nūḥ, akawa anatengeneza jahazi, na kila kundi la wakubwa wa watu wake likimpitia, humcheza shere. Nūḥ, aliwaambia, «Iwapo nyinyi mnatucheza shere leo, kwa ujinga wenu wa kutojua ukweli wa ahadi ya Mwenyezi Mungu, basi sisi tutawacheza shere nyinyi kesho wakati wa kuzama kama mnavyotucheza shere

    [39] Mtajua hapo, itakapokuja amri ya Mwenyezi mungu kwa hilo, ni yupi yule ambaye itamjia , hapa ulimwenguni, adhabu ya Mwenyezi Mungu yenye kumtweza na itamshukia, huko Akhera, adhabu ya daima isiyokatika.»

    [40] Mpaka ilipokuja amri yetu ya kuwaangamiza wao kama tulivyomuahidi Nūḥ, kwa hilo, na maji yakachimbuka kwa nguvu kutoka kwenye tanuri, mahala pa kuchomea mikate, ikiwa ni alama ya kuja adhabu, tulimuambia Nūḥ, «Beba ndani ya jahazi kila aina, miongoni mwa aina za wanyama wa kiume na wa kike, na uwabebe ndani yake watu wa nyumbani kwako, isipokuwa yule aliyetanguliwa na Neno kuwa wataadhibiwa katika wale wasiomuamini Mwenyezi Mungu kama mtoto wake na mke wake, na ubebe ndani yake aliyeamini pamoja na wewe katika watu wako.» Na hakuna aliyeamini pamoja na yeye isipokuwa wachache ingawa yeye alikaa na wao kwa muda mrefu

    [41] Nūḥ alisema kuwaambia walioamini pamoja na yeye, «Pandeni kwenye jahazi kwa jina la Mwenyezi Mungu. Kwa jina la Mwenyezi Mungu itatembea majini, na kwa jina la Mwenyezi Mungu itafika mwisho wa kwenda kwake na kutia nanga kwake. Hakika Mola wangu ni Mwingi wa kusamehe dhambi za mwenye kutubia na kurudi Kwake miongoni mwa waja Wake, ni Mwingi wa huruma kwao kwa kutowaadhibu baada ya kutubia

    [42] Nayo ikawa inatembea na wao kwenye mawimbi yanayopaa na kwenda juu mpaka yakawa kama majabali kwa urefu wake wa kwenda juu. Hapo Nūḥ alimwita mtoto wakewa kiume, na ambaye alikuwa yupo mahali kando na amejiepusha na Waumini, akamwambia, «Ewe mwanangu, panda na sisi kwenye jahazi na usiwe pamoja na wenye kumkanusha Mwenyezi Mungu, utakujazama.»

    [43] Mtoto wa Nūḥ akasema, «Nitakimbilia kwenye jabali nijihifadhi na maji na hilo litanizuia na kuzama. Nūḥ akamjibu, «Leo hakuna kitu chenye kuzuia amri ya Mwenyezi Mungu na hukumu Yake iliyoteremka kwa viumbe, ya gharika na maangamivu, isipokuwa yule aliyehurumiwa na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, basi amini na upande jahazini pamoja na sisi.» Hapo mawimbi makubwa yalitenganisha baina ya Nūḥ na mwanawe na akawa ni miongoni mwa waliogharikishwa wenye kuangamia

    [44] Akasema Mwenyezi Mungu kuiambia ardhi, baada ya watu wa Nūḥ kuangamia, «Ewe ardhi! Kunywa maji yako. Na ewe mbingu! Simamisha kunyesha mvua.» Na maji yakapungua na yakanywea, na amri ya Mwenyezi Mungu ikapitishwa ya kuangamia watu wa Nūḥ, na jahazi ikaegesha juu jabali la Jūdīy. Na hapo kukasemwa, «Kuwa mbali (na rehema ya Mwenyezi Mungu) ni kwa wale madhalimu waliokiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu na wasiamini.»

    [45] Na Nūḥ alimlingania Mola Wake kwa kumuomba na akasema, «Mola wangu, wewe umeniahidi kwamba utaniokoa, mimi na jamaa zangu, tusizame na tusiangamie, na hakika mototo wangu ni miongoni mwa watu wa nyumbani kwangu, na ahadi yako ndio kweli ambayo haibadiliki, na wewe ndiye hodari zaidi wa wenye kuhukumu na muadilifu wao zaidi.»

    [46] Mwenyezi Mungu Akasema, «Ewe Nūḥ, hakika yule mototo wako aliyeangamia si katika jamaa ambao nilikuahidi kuwa nitawaokoa. Hii ni kwa sababu ya ukafiri wake na kufanya kwake matendo yasiyokuwa mema. Na mimi nakukataza usiniombe jambo usiokuwa na ujuzi nalo. Mimi nakusihi usiwe ni miongoni mwa wajinga kwa kuniomba hilo.»

    [47] Akasema Nūḥ, «Ewe Mola wangu, Mimi najihami kwako na nataka hifadhi kukuomba kitu nisokuwa na ujuzi nacho, na usiponisamehe dhambi zangu na ukanihurumia kwa rehema zako,nitakuwa ni miongoni mwa wale waliojinyima hadhi zao na wakaangamia

    [48] Mwenyezi Mungu Akasema, «Ewe Nūḥ, Shuka kwenye ardhi kavu kutoka kwenye jahazi, kwa amani na salama zitokazo kwetu, na baraka ikishuka juu yako na juu ya ummah katika wale walioko na wewe. Na kuna umma na makundi miongoni mwa watu wa uovu ambao tutawastarehesha katika uhai wa kilimwengu mpaka ufike muda wao wa kuishi kisha iwapate wao kutoka kwetu adhabu iumizayo Siku ya Kiyama.»

    [49] Habari hiyo tuliyokuhadithia kuhusu Nūḥ na watu wake ni miongoni mwa habari za ghaibu zilizopita, ambazo tunakuletea wahyi juu yake, hukuwa ukizijua, wewe wala watu wako, kabla ya maelezo haya. Basi subiri juu ya ukanushaji wa watu wako na makero yao wanayokufanyia kama walivyosubiri Manabii huko nyuma. Na mwisho mwema wa duniani na Akhera ni wa waogopao wanaomcha Mwenyezi Mungu

    [50] Na tuliwamtumia watu wa kabila la 'Ād ndugu yao Hūd. Alisema kuwaambia, «Enyi watu wangu, muabuduni Mwenyezi Mungu, Peke Yake. Nyinyi hamuna mungu anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Yeye. Basi mtakasieni Yeye ibada. Kwani nyinyi hamkuwa, katika kumshirikisha kwenu Mwenyezi Mungu, isipokuwa ni warongo

    [51] «Enyi watu wangu, mimi siwaombi malipo yoyote, kwa haya niwalinganiyao ya kumtakasia Mwenyezi Mungu ibada na kuacha kuabudu masanamu,. Malipo yangu mimi ya kuwalingania nyinyi hayako juu ya yoyote isipokuwa Mwenyezi Mungu aliyeniumba. Basi hamtii akili mkatenganisha baina ya ukweli na upotofu

    [52] «Enyi watu wangu, takeni msamaha wa Mwenyezi Mungu kwa kumuamini Yeye, kisha mtubie Kwake kutokana na dhambi zenu. Kwani nyinyi mkifanya hivyo, Atawateremshia mvua yenye kufuatana iliyo nyinygi, hivyo basi mazuri yenu yatakuwa mengi na Atawaongezea nguvu juu ya nguvu mlizonazo kwa wingi wa watoto wenu na mfuatano wa neema juu yenu. Na msiyape mgongo yale ninayowalingania nyinyi kwayo mkawa ni wenye kuendelea juu ya makosa yenu.»

    [53] Wakasema, «Ewe Hūd, hukutujia na hoja zilizo wazi juu ya usahihi wa yale unayotuitia. Na sisi si wenye kuwaacha waungu wetu tunaowaabudu kwa sababu ya maneno yako. Na sisi si wenye kukuamini wewe katika hilo unalolidai

    [54] «Sisi hatusemi isipokuwa kwamba baadhi ya waungu wetu wamekutia wazimu kwa sababu ya kukataza kwako wasiabudiwe.» Akawaambia, «Mimi namshuhudisha Mwenyezi Mungu haya ninayoyasema na nawashuhudiza nyinyi kwamba mimi niko mbali na vile mnavyovishirikisha

    [55] badala ya Mwenyezi Mungu, miongoni mwa wale wafananishwao na Yeye na masanamu. Basi angalieni na mfanye bidii, nyinyi na hao mnaodai kati ya waungu wenu, kunipatia madhara, kisha msilicheleweshe hilo hata kitambo kidogo kiasi cha kupepesa jicho. Hivyo ni kwamba Hūd ana imani thabiti kwamba hayatampata yeye kutoka kwao wala kutoka kwa waungu wao madhara yoyote

    [56] «Mimi nimetegemea kwa Mwenyezi Mungu, Mola wangu na Mola wenu, Mmiliki wa kila kitu na Mwenye kukiendesha. Hakuna kitu chenye kunipata isipokuwa kwa amri Yake. Na Yeye Ndiye Muweza wa kila kitu, Hakuna kitu chochote kinachotambaa kwnye ardhi hii isipokuwa Mwenyezi Mungu Amekimiliki na kiko chini ya mamlaka Yake na uendeshaji Wake. Hakika Mola wangu Yuko kwenye njia iliyolingana sawa, kwa maana kwamba ni muadilifu katika hukumu Zake, sheria Zake na amri Zake, Anamlipa mwema kwa wema Wake na muovu kwa uovu wake

    [57] «Mkiyapa mgongo yale ninayowalingania kwayo ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtakasia ibada, basi nimeshaufikisha ujumbe wa Mola wangu kwneu na hoja ishasimama kwenu nyinyi, na Mwenyezi Mungu atawaangamiza kwa kuwa hamkumuamini, na Atawaleta watu wengine ambao watashika nafasi zenu katika majumba yenu na mali yenu, na ambao watamtakasia Mwenyezi Mungu ibada. Na nyinyi hamtamdhuru Yeye kitu chochote. Hakika Mola wangu amekidhibiti kila kitu na kukihifadhi; Yeye Ndiye Mwenye kunitunza msinifanyie ubaya

    [58] Na ilipokuja amri yetu kuwaadhibu watu wa Hūd, tulimuokoa Hūd na Waumini miongoni mwao kwa wema wetu juu yao na huruma, na tukawaokoa wao na adhabu kali Aliyoishukisha Mwenyezi Mungu kwa hao 'Ād, wakapambaukiwa na huku hakuna kionekanacho isipokuwa makazi yao

    [59] Hao ndio'Ād, walikanusha aya za Mwenyezi Mungu, wakaasi Mitume Wake na wakatii amri ya kila anayemfanyia kiburi Mwenyezi mungu asiyekubali haki wala kuinyoshea shingo

    [60] Wakafuatiwa, katika ulimwengu huu, na laana ya Mwenyezi Mungu, na wakafuatwa na hasira Zake Siku ya Kiyama. Jueni mtanabahi kwamba 'Ād walimkanusha Mola wao na wakawakanusha Mitume Wake. Jueni mtanabahi kwamba umbali na rehema ya Mwenyezi Mungu na maangamivu yatawashukia 'Ād, watu wa Hūd, kwa sababu ya ushirikina wao na kukanusha kwao neema ya Mola wao

    [61] Na tulimtuma kwenda kwa Thamūd ndugu yao Ṣāliḥ akasema kuwaambia, «Enyi watu wangu, muabuduni Mwenyezi Mungu, Peke Yake. Nyinyi hamuna mungu yoyote anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu. Basi mtakasieni ibada. Yeye Ndiye Aliyeanza kuwaumba kutokamana na ardhi, kwa kumuumba baba yenu Ādam kutokamana na hiyo, na akawafanya nyinyi ni wenye kuiimarisha. Hivyo basi, muombeni Awasamehe madhambi yenu, na rudini Kwake kwa kutubia kidhati. Hakika Mola wangu yuko karibu na yule anayemtakasia ibada na akawa na hamu ya kuja Kwake kwa kutubia, ni Mwenye kumuitikia anapomuomba.»

    [62] Tahamūd wakasema kumwambia Ṣāliḥ, «Kwa hakika, kabla ya neno hili ulilotwambia, tulikuwa tuna matumaini kwamba utakuwa ni kiongozi mwenye kusikizwa,. Je, unatukataza kuwaabudu waungu ambao baba zetu walikuwa wakiwaabudu? Hakika sisi tuko kwenye shaka yenye kutia wasiwasi juu ya mwito wako wa kutuita sisi tumuabudu Mwenyezi Mungu Peke Yake

    [63] Ṣāliḥ akasema kuwaambia watu wake, «Enyi watu wangu, iwapo niko kwenye hoja ya Mwenyezi Mungu na ukanijia mimi utume na hekima kutoka Kwake, niambieni mimi: ni nani atakayeniondolea adhabu ya Mwenyezi Mungu nikimuasi, nisiufikishe ujumbe na nisitoe ushauri mzuri kwenu? Hapo hamtaniogezea isipokuwa upotevu na kuwa mbali na wema

    [64] «Na enyi watu wangu, huyu ni ngamia wa Mwenyezi Mungu, Amemjaalia ni hoja na alama ya kuonesha ukweli wangu katika yale ninayowaitia. Basi muacheni ale katika ardhi ya Mawenyezi Mungu, kwani chakula chake hakiko juu yenu. Na wala msimguse kumchinja, kwani nyinyi mkifanya hivyo itawapata adhabu kutoka Kwake kwa muda mfupi baada kumchinja.»

    [65] Wakamkanusha na wakamchinja ngamia, hapo Ṣāliḥ akawaambia, «Stareheni na maisha yenu katika mji wenu kwa muda wa siku tatu, kwani adhabu ni yenye kuwashukia baada yake, na hiyo ni ahadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu isiyokanushika, haina budi kutukia.»

    [66] Basi amri yetu ilipokuja ya kuwaangamiza Thamūd, tulimuokoa Ṣāliḥ na walioamini pamoja na yeye na maangamivu kwa rehema kutoka kwetu. Na tuliwaokoa wao na unyonge wa Siku hiyo na udhalilifu wake. Hakika Mola wako, ewe Mtume, Ndiye Mwenye nguvu, Mwenye ushindi. Na miongoni mwa nguvu Zake na ushindi Wake ni kuwa Aliwaangamiza watu wenye kupita kiasi kwenye uasi na akawaokoa Mitume na wafuasi wao

    [67] Na ukelele wa nguvu uliwapata Thamūd walio madhalimu, hapohapo wakawa kwenye majumba yao ni wafu waliokauka na kuanguka kwa nyuso zao, hakuna anayetikisika

    [68] Kama kwamba wao, kwa haraka ya kuondoka kwao na kutoeka kwao, hawakuishi humo. Jueni mtanabahi kwamba Thamūd walikanusha aya za Mola wao na hoja Zake. Jueni mtanabahi kwamba kuwa mbali na kufukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu ni kwa hao Thamūd; ni upotevu ulioje na unyonge ulioje huo wao

    [69] Hakika Malaika walimjia Ibrāhīm, amani imshukiye, wakimpa yeye na mke wake bishara ya Isḥḥḥaq na Ya'qūb baada yake, wakasema, «Salām (amani)» Akasema kuwarudishia maamkuzi yao, «Salām (amani)» Hapo akaondoka haraka na akrudi na mwanang>ombe wa kuchoma aliyenona ili wao wale

    [70] <Alipoona Ibrāhīm kuwa mikono yao haifikikishwi kwenye yule mwanang>ombe aliyewaletea na kuwa wao hawamli, alikataa hilo kutoka kwao na akaingiwa na hisia ya uoga ndani ya moyo wake. Malaika wakasema, walipoona uoga uliomuingia Ibrāhīm, «Usiogope! Sisi ni Malaika wa Mola wako tumetumwa kwenda kwa watu wa Lūṭ kuwaangamiza

    [71] Na Sārah, mke wa Ibrāhīm, alikuwa amesimema nyuma ya pazia yuwasikia hayo maneno. Alicheka kwa kuyaonea ajabu aliyoyasikia. Hapo tukampa habari njema, kupitia kwa ndimi za Malaika, kwamba atazaa, kwa mume wake Ibrāhīm, mtoto atakayeitwa Isḥāq; na mtoto wake ataishi, na baada ya Isḥāq atakuwa na mjukuu kutoka kwake, naye ni Ya’qūb

    [72] Alipopewa bishara ya Isḥāq, Sārah alisema kwa kustaajabu, «Ee mimi ee! Vipi nitakuwa na mtoto na mimi ni mkongwe na huyu mume wangu yuko katika hali ya uzee na utu uzima? Kuzaa kwa mtu mfano wangu mimi na mfano wa mume wangu pamoja na ukuu wa myaka ni jambo la ajabu.»

    [73] Wajumbe walisema kumwambia , «Hivi wewe unaionea ajabu amri ya Mwenyezi Mungu na hukumu Yake? Rehema ya Mwenyezi Mungu na baraka Zake ziwashukie nyinyi, enyi watu wa nyumba ya unabii. Hakika Yeye, kutakata na kutukuka ni Kwake, ni mhimidiwa wa sifa na vitendo, ni Mwenye utukufu na ukubwa katika hizo.»

    [74] Ulipomuondokea Ibrāhīm uoga uliompata kwa wale wageni kutokula chakula, na ikamjia bishara njema ya Isḥāq na Ya’qūb, aliendelea kuwajadili Wajumbe wetu juu ya kile tulichowatuma cha kuwaadhibu watu wa Lūṭ na kuwaangamiza

    [75] Hakika Ibrāhīm ni mwingi wa uhalimu, hapendi uharakishaji wa adhabu, ni mwingi wa kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu na kumuomba, ni mwenye kutubia, anarejea kwa Mwenyezi Mungu katika mambo yake yote

    [76] Wajumbe wa Mwenyezi Mungu wakasema, «Ewe Ibrāhīm, uacha mjadala huu kuhusu mambo ya watu wa Lūṭ na kuwaombea huruma, kwani hakika ya mambo ni kwamba imithibiti juu yao adhabu na amri ya Mola wako aliyowapangia. Na wao, adhabu inayotoka Mwenyezi Mungu ni yenye kuwashukia, si yenye kuepushwa na wao wala kuzuiliwa..»

    [77] Na Malaika wetu walipomjia Lūṭ, aliudhika kwa kuja kwao na akaingiwa na hamu kwa hilo. Hivyo ni kwa kuwa yeye hakuwa anajua kwamba wao ni wajumbe wa Mwenyezi Mungu, akawachelea wasidhuriwe na watu wake na akasema, «Hii ni siku ya mtihani na shida.»

    [78] Watu wa Lūṭ wakamjia kwa haraka kutaka kufanya uchafu, na kabla ya kuja kwao walikuwa wanawendea wanaume kwa njia ya matamanio badala ya wanawake. Lūṭ akasema kuwaambia watu wake, «Hawa ni watoto wangu wa kike, waoeni. Wao niwasafi zaidi kwenu kuliko hayo mnayoyataka.» Aliwaita kuwa ni watoto wake wa kike sababu Nabii wa umma ana daraja ya baba kwao. «Basi muogopeni Mwenyezi Mungu na mjihadhari na mateso Yake, wala msinifedhehi kwa kuwakosea wageni wangu. Kwani hakuna mtu yoyote katika nyinyi aliye mzuri wa kupima mambo apate kuwakataza wanaotaka kufanya machafu akawzuia wao na hayo? Kumdhalilisha mgeni ni jambo la kutukanisha hakuna alifanyalo isipokuwa ni watu wa utwevu.»

    [79] Wakasema watu wa Lūṭ kumwambia yeye, «Umeshajua tangu mbeleni kwamba sisi hatuna haja ya wanawake wala matamanio. Na wewe unajua tulitakalo. Yaani, sisi hatutaki isipokuwa wanaume na hatuna hamu ya kuoa wanawake.»

    [80] Walipokataa isipokuwa ni kufanaya machafu, aliwaambia, «Lau mimi nina nguvu kwenu na nina wasaidizi pamoja na mimi, au niutemegee ukoo utakaonihami na nyinyi, ningaliwazuia nyinyi na hayo mnayoyataka.»

    [81] Malaika wakasema, Ewe Lūṭ, sisi ni wajumbe wa Mola wako, Ametutuma kuwaangamiza watu wako, na wao hawatakufikia. Basi toka kwenye kijiji hiki, wewe na watu wako (waliokuamini), katika kipindi kilichosalia cha usiku, na asizunguke nyuma yoyote katika nyinyi, ili asiione adhabu ikampata. Lakini mke wako aliyeenda kinyume chako kwa kukanusha na kufanya unafiki, kitampata yeye kile kitakachowapata watu wako cha maangamivu. Hakika maagano ya kuangamia kwao ni wakati wa asubuhi, nao ni wakati ambao ni karibu kufika.»

    [82] Basi amri yetu ilipokuja, ya adhabu kuwashukia, tuliifanya sehamu ya juu ya kijiji chao ambayo walikuwa wakiishi juu yake kuwa chini kwa kukigeuza. Na tuliwateremshia majiwe ya udongo ulio mgumu wenye nguvu, yamepangwa baadhi yake juu ya mengine na yamefuatana

    [83] yamewekwa alama huko kwa Mwenyezi Mungu kwa alama inayojulikana, hayafanani na majiwe yaliyo ardhini. Na hayakuwa majiwe haya ambayo Mwenyezi Mungu aliwateremshia watu wa Lūṭ, yako mbali na makafiri wa kikureshi kuwa watateremshiwa mfano wake. Katika haya kuna onyo kwa kila aliyeasi aliyeshindana na Mwenyezi Mungu

    [84] Na tulimtuma kwenda kwa watu wa Madyan ndugu yao Shu'ayb, akasema , «Enyi watu wangu, muabuduni Mwenyezi Mungu, Peke Yake. Nyinyi hamuna mungu yoyote anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu, basi mtakasieni ibada.. Wala msiwapunguzie watu haki zao katika vipimo vyao na mizani zao. Mimi nawaona nyinyi muko kwenye ukunjufu wa maisha, na mimi nawachelea, kwa sababu ya kupunguza vipimo na mizani, adhabu ya siku itakayowazunguka

    [85] «Na enyi watu wangu, timizeni vipimo vya vibaba na mizani kwa usawa Wala msiwapunguzie watu haki zao katika jumala ya vitu vyao. Wala msiende katika ardhi mkifanya mambo ya kumuasi Mwenyezi Mungu na kueneza uharibifu

    [86] «Kile kitakachosalia kwenu cha faida ya halali, baada ya kutimiza vipimo na mizani, kina baraka na ni chema kwenu kuliko kile mkichukuacho cha pato la haramu kwa njia ya kupunja na mfano wake. Iwapo nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu kikweli, basi fuateni amri Yake. Na mimi si mtunzi kwenu wa kuwahesabia matendo yenu.»

    [87] Wakasema, «Ewe Shu'ayb, je swala hii ambayo unaendelea nayo ndiyo inayokuamuru wewe kwamba sisi tuache masanamu na mizimu ambayo baba zetu wanaabudu, au kwamba sisi tujizuie tusitumie njia tuziwezazo za hila na vitimbi katika kuchuma mali yetu?» Wakasema kwa njia ya kumcheza shere, «Wewe ndiye mwenye akili na hodari wa mipango ya usimamizi wa mali.»

    [88] Akasema Shu'ayb, «Enyi watu wangu, Mwaonaje iwapo mimi niko kwenye njia iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu katika yale ninayowaitia ya kumtakasia Yeye ibada, na katika yale ninayowakataza ya kuharibu mali, na Akawa Ameniruzuku riziki ya ukunjufu ya halali iliyo nzuri? Na sitaki kuenda kinyume na nyinyi, nikafanya jambo nililowakataza; na sitaki, katika niwaamrishalo na niwakatazalo, isipokuwa ni kuwarakibisha kadiri ya uweza wangu na kujimudu kwangu. Na kuafikiwa kwangu, katika kuipata haki na kujaribu kuwarakibisha, kuko kwa Mwenyezi Mungu. Kwake Yeye, Peke Yake, nimejitegemeza, na Kwake Yeye narejea kwa kutubia na kuelekea

    [89] «Na enyi watu wangu, usiwapelekee uadui wenu kwangu na kunichukia na kuiacha Dini niliyonayo, kufanya ukakamavu na kuendelea na ukanushaji wa Mwenyezi Mungu mlionao. Kwani mkifanya hivyo, yatawapata nyinyi maangamivu kama yaliyowapata watu wa Nūḥ, au watu wa Hūd au watu wa Ṣāliḥ,. Na hawakuwa watu wa Lūṭ, na adhabu iliyowashukia ni mbali na nyinyi, si nchi waliyoishi wala zama walizokuwako

    [90] Na ombeni kutoka kwa Mola wenu msamaha wa dhambi zenu, kisha rudini kumtii na endeleeni juu yake. Hakika Mola wangu ni Mwingi wa rehema, ni Mwingi wa mapenzi na mahaba kwa aliyetubia na akarejea Kwake.» Katika hii aya, pana kuthibitisha sifa ya raḥmah (kurehemu) na mawaddah (kupenda) kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kama inavyonasibiana na Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake

    [91] Walisema, «Ewe Shu'ayb! Hatuyafahamu mengi unayotwambia, na sisi tunakuona wewe kuwa ni mnyonge kwetu, wewe si miongoni mwa watu wakubwa wala viongozi, na lau sisi si kuwastahi jamaa zako tungalikuua kwa kukupiga mawe.»- Na kundi la jamaa zake lilikuwa ni katika watu wanaofuata mila yao.- «Na wewe huna cheo wala heshima katika nafsi zetu.»

    [92] Akasema, «Enyi watu wangu! Kwani jamaa zangu ni wenye nguvu zaidi na ni watukufu zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu? Na mumeitupa amri ya Mola wenu, mkaiweka nyuma ya migongo yenu, mkawa hamjilazimishi kufuata amri Zake na hamjiepushi na makatazo Yake. Hakika Mola wangu ni kwa mnayoyafanya Ameyazunguka, hakuna chochote katika matendo yenu kinafichika Kwake hata kama kina uzito wa chungu mdogo, na Atawalipa kwa hizo kwa haraka au baadaye

    [93] «Na enyi watu wangu! Fanyeni mnaloliweza kwa njia yenu na namna yenu. Mimi ni mwenye kuendelea kufanya kwa njia yangu na nikitumia kile Mwenyezi Mungu Amenipa cha kuwalingania nyinyi kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Mtajua ni nani miongoni mwetu, itamjia adhabu yenye kumfanya mnyonge, na ni nani, miongoni mwetu, ni mrongo katika maneno yake: ni mimi au ni nyinyi? Na mngojee kitakachowashukia; mimi ni miongoni mwa wenye kungojea pamoja na nyinyi.» Hili ni onyo kali kwao

    [94] Na amri yetu ilipokuja ya kuwaangamiza watu wa Shu'ayb, tulimuokoa mjumbe wetu Shu'ayb na wale walioamini pamoja na yeye kwa rehema yetu. Na wale waliodhulumu walipatwa na ukulele kutoka mbinguni ukawaangamiza na wakawa wako majumbani mwao wamepiga magoti wakiwa ni wafu hawatikisiki

    [95] Kama kwamba wao hawakukaa kwenye nyumba zao wakati wowote. Jueni kwamba watu wa Madyan waliepushwa na rehema ya Mwenyezi Mungu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu aliwaangamiza watu wake na akawalaani, kama vile kina Thamūd walivyoepushwa na rehema Yake. Makabila mawili haya yalishirikiana katika kuwa mbali na rehema ya Mwenyezi Mungu na kuangamia

    [96] Hakika tulimtuma Mūsā na dalili zetu za upweke wetu na hoja inayomfahamisha mwenye kuiona na kuitia akilini, kwa moyo wenye siha, kwamba zinatoa dalili ya upweke wa Mwenyezi Mungu na urongo wa kila anayedai uola asiyekuwa Yeye, Aliyetakata na sifa za upungufu na kutukuka

    [97] Tulimtuma Mūsā kwa Fir'awn na wakubwa wa wafuasi wake na watukufu wa watu wake, Fir'awn akakanusha na akawaamuru watu wake wamfuate yeye, wakamtii yeye na wakaenda kinyume cha amri ya Mūsā. Na hakuna uongofu wowote wala muongozo mwema katika amri ya Fir'awn, ni ujinga mtupu, upotevu, ukanushaji na ujeuri

    [98] Fir'awn atatangulia akiwaongoza watu wake Siku ya Kiyama mpaka awatie Motoni. Ni mahali pabaya ambapo wao wataiangia

    [99] Na Mwenyezi Mungu Amewafuatishia laana katika ulimwengu huu, pamoja na adhabu Aliyowaharakishia ya kuzamishwa baharini. Na Siku ya Kiyama pia atawapa laana nyingine kwa kuwatia Motoni. Ni mabaya sana mambo yaliyokusanyika kwao na yakafuatana juu yao, ya adhabu ya Mwenyezi Mungu na laana ya duniani na Akhera

    [100] Haya tuliyokutajia wewe, ewe Mtume, ni miongoni mwa habari za watu wa miji ambayo tuliwaangamiza watu wake, twakupasha habari zake. Na miongoni mwa miji hiyo kuna iliyo na athari zilizosalia; na miongoni mwazo kuna ambazo athari zake zimefutika, hakuna chochote katika hizo kilichosalia

    [101] Hakukuwa kuwaangamiza wao ni bila ya sababu na dhambi zinazowafanya wastahili hayo, lakini walijidhulumu wenyewe kwa ushirikina wao na kuleta kwao uharibifu katika ardhi. Hawakuwapa nafuu wao hao waungu wao ambao walikuwa wakidai kuwa ni waungu na wakiwataka wawaondolee shida, wakati amri ya Mwenyezi Mungu ilipokuja ya kuwaadhibu wao. Na hao waungu wao hawakuwazidishia isipokuwa uvunjaji, maangamivu na hasara

    [102] Na kama nilivyowapatiliza kwa adhabu watu wa miji iliyodhulumu kwa kuenda kinyume na amri yangu na kuwakanusha Mitume wangu, nitawapatiliza wengineo miongoni mwa watu wa miji wakizidhulumu nafsi zao kwa kumkanusha Mwenyezi Mungu na kumuasi Yeye na kuwakanusha Mitume Wake. Hakika mapatilizo Yake ya mateso ni makali, yenye kuumiza, yaliyo magumu

    [103] Hakika katika kuwapatiliza watu wa miji iliyotangulia iliyodhulumu, ni mazingatio na mawaidha kwa anayeogopa mateso ya Mwenyezi Mungu na adhabu Yake huko Akhea. Siku hiyo ni ambayo watakusanywa watu wote ili wahesabiwe na walipwe, na wataishuhudia viumbe wote

    [104] Na hatuicheleweshi Siku ya Kiyama isipokuwa ni ukome muda uliyohesabiwa uliyo kwenye elimu yetu, hauzidi wala haupungui na kipimo chetu tulichoupimia kwa hekima yetu

    [105] Siku kitakapokuja Kiyama, hakuna nafsi itakayosema isipokuwa kwa idhini ya Mola Wake. Kati yao kuna shaqiyy (muovu) anayestahili adhabu na kuna sa'īd (mwema) aliyefadhiliwa kwa kupewa starehe

    [106] Ama wale waliokuwa waovu ulimwenguni kwa kuharibika akida yao na uovu wa vitendo vyao, basi Moto utakuwa ndio mahali pao pa kutulia; humo watakuwa na kutoa pumzi kutoka kwenye vifua kwa nguvu na kurudisha kwa shida, na sauti mbili hizo ni mbaya zaidi zilizopita kiasi

    [107] Watakuwa ni wenye kukaa humo milele muda wa kuweko mbingu na ardhi, hivyo basi adhabu yao haitakatika wala haitakoma, bali ni adhabu ya daima iliyotiliwa mkazo, isipokuwa iwapo Mola wako atataka, kwa kuwatoa waliompwekesha waliofanya maasia baada ya muda fulani wa kukaa kwao Motoni. Hakika Mola wako ni Mwenye kufanya Analolitaka

    [108] Na ama wale ambao Mwenyezi Mungu Amewaruzuku wema, wataingia Peponi wakae milele humo muda wa kuwako mbingu na ardhi, isipokuwa lile kundi ambalo Mwenyezi Mungu Atataka kulichelewesha, nalo ni lile la waliompwekesha Mwenyezi Mungu waliofanya maasia. Wao watasalia Motoni kwa kipindi fulani, kisha watatoka humo kwenda Peponi kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu na rehema Yake. Na Mwenyezi Mungu Atawapa watu wema hawa vipaji visizopunguzwa

    [109] Basi usiwe, ewe Mtume, katika shaka kuhusu ubatilifu wa vitu wanavyoviabudu washirikina hawa miongoni mwa watu wako. Wao hawaabudu, miongoni mwa masanamu, isipokuwa kama vile baba zao walikuwa wakiabudu huko nyuma. Na sisi ni wenye kuwatekelezea kile tulichowaahidi kikiwa kikamilifu kisichopunguzwa. Huu ni muelekezo kwa ummah wote, ingawa tamko lake limeelekezwa kwa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani ziwashukie

    [110] Na hakika tulimpa Mūsā Kitabu , nacho ni Taurati, wakatafautiana watu wake juu yake: baadhi yao walikiamini na wengine walikikanusha, kama walivyofanya watu wako kuhusu Qur'ani. Na lao si neno lililotangulia kutoka kwa Mola wako la kutowaharakishia adhabu viumbe Wake, ingaliwashukia wao duniani kwao hukumu ya Mwenyezi Mungu ya kuwaangamiza wenye kukanusha na kuwaokoa Waumini. Na makafiri wa watu wako, miongoni mwa mayahudi na washirikina, ewe Mtume, wako kwenye shaka inayowatia wasiwasi juu hii Qur'ani

    [111] Na hakika watu wote hao wanaotafautiana tuliokutajia habari zao , ewe Mtume, Mwenyezi Mungu Atawatekelezea malipo ya matendo yao Siku ya Kiyama, yakiwa mema watalipwa wema na yakiwa maovu watalipwa uovu. Hakika Mola wako , kwa wanayoyafanya hawa washirikina, ni Mtambuzi, hakuna kitendo chao chochote kinachofichamana Kwake. Katika hii pana kitisho na onyo kwao

    [112] Basi kumana msimamo, ewe Nabii, kama Alivyokuamurisha Mola wako, wewe na waliotubia pamoja nawe, wala msikipite kile Alichowaekea mpaka Mwenyezi Mungu. Hakika Mola wenu, kwa matendo yote mnayoyafanya, ni Muoni, hakuna kitu kinachofichika Kwake, na Atawalipa nyinyi kwa hayo

    [113] Wala msilemee upande wa hawa makafiri walio madhalimu, msije mkapatwa na Moto. Na hamna nyinyi msaidizi mwenye kuwanusuru na kusimamia mambo yenu isipokuwa Mwenyezi Mungu

    [114] Na tekeleza Swala, ewe Nabii, kwa njia ya ukamilifu katika ncha mbili za mchana: asubuhi na jioni, na katika nyakati za usiku. Kwani kufanya mema kunafuta dhambi zilizopita na kuondoa athari zake. Kuamrisha kusimamisha Swala na kueleza kwamba mema huondoa mabaya ni mawaidha kwa anayewaidhika nayo na akakumbuka

    [115] Na usubiri, ew Nabii, juu ya hiyo Swala na juu ya makero unayoyakuta kutoka kwa washirina wa watu wako, kwani Mwenyezi Mungu Hapotezi malipo ya walio wema katika matendo yao

    [116] Si ilikuwa wapatikane, miongoni mwa vizazi viliyopita kabla yenu, wasalia wa watu wazuri walio wema wanaowakataza makafiri waache ukafiri wao na kufanya uharibifu katika ardhi. Hawakupatikana katika hao isipokuwa wachache miongoni mwa walioamini na Mwenyezi Mungu akawaokoa na adhabu Yake Alipowapatiliza madhalimu. Na waliozidhulumu nafsi zao, miongoni mwa watu wa kila ummah uliopita, walifuata ladha za duniani na anasa zake walizostareheshwa, na wakawa wahalifu, wenye kudhulumu kwa kufuata kwao starehe walizokuwa nazo, ndipo adhabu ikathibiti juu yao. Katika hii aya pana mazingatio na mawaidha kwa wanaofanya maasia miongoni mwa Waislamu, kwa kuwa hawaepukani na udhalimu wa nafsi zao

    [117] Na hakuwa Mola wako, ewe Mtume, ni Mwenye kuuangamiza mji wowote miongoni mwa miji na hali watu wake ni wenye kufanya mambo mazuri katika ardhi, wenye kujiepusha na uharibifu na udhalimu; Yeye huwaangamiza wao kwa sababu ya udhalimu wao na uharibifu wao

    [118] Na lau Mola wako Alitaka, Angaliwafanya watu wote ni kundi moja, wako kwenye dini moja , nayo ni dini ya Uislamu. Lakini Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, hakutaka hivyo. Basi watu hawataacha kuendelea kutafautiana katika dini zao, na hayo ndiyo yanayoambatana na hekima Yake

    [119] Isipokuwa wale waliorehemewa na Mola wako, wakamuamini Yeye na wakawafuata Mitume Wake, kwani wao hawatafautiani juu ya kumpwkwesha Mwenyezi Mungu na yale ambayo Mitume wamekuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni matakwa ya Hekima Yake, Aliyetakata na sifa za upungufu na Akatukuka, kwamba Yeye Amewaumba wao wakiwa wametafautiana: kuna kundi ovu na kundi lema; na kila kundi limesahilishiwa kwa lile lililoumbiwa, na kwa hii ndipo agizo la Mwenyezi Mungu litatimia la kuwa Yeye Ataujaza, Moto wa Jahanamu, majini na binadamu waliomfuata Iblisi na askari wake na wasiongoke kwenye njia ya Imani

    [120] Na tunakupa habari, ewe Mtume, za Mitume waliokuwa kabla yako zenye kila unalohitajia la kuupa nguvu moyo wako ya kusimama imara ili kubeba majukumu ya Utume. Na umekujia wewe, katika sura hii na hahabri zilizomo, ufafanuzi wa haki ambayo wewe uko juu yake. Na yamekujia wewe, katika hii sura, mawaidha ya kuwafanya makafiri wakomeke na ukumbusho wa kuwafanya wenye kumuamini Mwenyezi mungu na Mitume Wake wakumbuke

    [121] Waambie, ewe Mtume, makafiri wasiokubali upweke wa Mwenyezi Mungu, «Fanyeni mnayoyafanya kwa namna yenu na mbinu zenu za kuupinga Ulinganizi na kumkera Mtume na wale waliomuitika, kwani sisi ni wenye kufanya kwa namna yetu mbinu zetu za kusimama imara juu ya Dini yetu na kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu

    [122] Na ungojeni mwisho wa jambo letu, na sisi tunangojea mwisho wa jambo lenu.» Katika hii pana onyo na kitisho kwao

    [123] Ni wa Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, ujuzi wa kila kisichoonekana mbinguni na ardhini. Na Kwake yanarejeshwa mambo yote Siku ya Kiyama. Basi muabudu Yeye, ewe Nabii, na umtegemezee mambo yako Kwake. Na Mola wako Hakuwa ni mwenye kughafilika na yale mnayoyafanya ya wema na uovu na Atamlipa kila mtu kwa matendo yake

    Yusufu

    Surah 12

    [1] Alif, Lām, Rā’. Maneno yametangulia juu ya herufi zilizokatwa na kutengwa mwanzo wa sura ya Al-Baqrah. Hizi ni aya za Kitabu kilichobainika kilicho wazi katika maana yake, mahalalisho yake, maharamisho yake na uongofu wake

    [2] Sisi tumekuteremshia Qur’ani kwa lugha ya Waarabu, huenda nyinyi, enyi Waarabu mkayatia akilini maana yake, mkayafahamu na mkatenda kulingana na uongofu wake

    [3] Sisi tunakusimulia wewe, ewe Mtume, visa vizuri zaidi kwa wahyi tuliyokuletea wa hii Qur’ani, na ingawa, kabla ya kukuteremshia, ulikuwa ni miongoni mwa walioghafilika nazo, hujui chochote kuhusu habari hizi

    [4] Kumbuka, ewe Mtume, kuwaambia watu wako neno la Yūsuf kumwambia babake, «Mimi nimeota usingizini kuona nyota kumi na moja, jua na mwezi, zote zikinisujudia.» Ndoto hii ilikuwa ni bishara ya cheo kikubwa, cha ulimwenguni na Akhera, alichofikia Yūsuf, amani imshukiye

    [5] Ya’qūb, amani imshukiye, alisema kumwambia mwanawe Yūsuf, «Ewe Mwanangu, usiwatajie ndugu zako ndoto hii, watakuhusudu, watakufanyia uadui na watafanya hila za kukuua, hakika Shetani kwa binadamu ni adui ambaye uadui wake uko waziwazi

    [6] «Na kama kama Alivyokuonesha Mola wako ndoto hii, pia Atakuteua na Atakufundisha uaguzi wa ndoto ambazo watu huziona usingizini, ujue matokeo yake ya uhakika, na atazitimiza neema zake kwako na kwa kizazi cha Ya’qūb, kama alivyozitimiza hapo nyuma kwa wazazi wako wawili, Ibrāhīm na Is’ḥāq, kwa kuwapa unabii na utume. Hakika Mola wako Anamjua yule Anayemteua miongoni mwa waja Wake, ni Mwingi wa hekima katika kuendesha mambo ya viumbe vyake

    [7] Hakika katika kisa cha Yūsuf na ndugu zake kuna mazingatio na dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu na hekima Yake kwa anyeuliza habari zao na akataka kuzijua

    [8] Waliposema ndugu zake Yūsuf wa kwa baba kuambiana wao kwa wao, «Hakika Yūsuf na ndugu yake wa kwa baba na mama wanapendwa zaidi na baba yetu kuliko sisi. Anawafanya wao bora juu yetu, na sisi ni kundi lenye idadi kubwa. Hakika baba yetu yuko makosani waziwazi, kwa kuwa amewafanya wao ni bora juu yetu bila ya sababu tunayoiyona yenye kupelekea kufanya hivyo

    [9] «Muueni Yūsuf! Au mtupeni kwenye ardhi isiyojulikana iliyo mbali na mji, hapo yatasafika kwenu mapenzi ya baba yenu na muelekeo wake kwenu, na hatageuka kwa wengine na kuacha kushughulika na nyinyi, na mtakuwa, baada ya kumuua Yūsuf au kumuepusha, ni wenye kutubia kwa Mwenyezi Mungu na kumuomba msamaha baada ya kosa lenu.»

    [10] Akasema mwenye kusema, miongoni mwa ndugu za Yūsuf, «Msimuue Yūsuf, na mtupeni ndani ya kisima ataokotwa na wapita njia miongoni mwa wasafiri, na hapo mtapumzika na yeye; na hakuna haja ya nyinyi kumuua, iwapo muna azma ya kulifanya hilo mnalolisema

    [11] wakasema ndugu zake Yūsuf, baada ya kuafikiana kumuepusha, «Ewe baba yetu, unani wewe hutufanyi sisi ni waaminifu juu ya Yūsufu pamoja na kuwa yeye ni ndugu yetu, na sisi tunamtakia wema na kumhurumia, tutamtunza na tutampa ushauri mzuri wa kidhati

    [12] «Tuachie awe na sisi kesho tutakapotoka kwenda kwenye malisho ya wanyama wetu, apate kutembea, apumbae, afurahike na acheze kwa kushindana na mfano wake miongoni mwa machezo yanayofaa. Na sisi ni wenye kumtunza na kila unalomuogopea.»

    [13] Ya’qūb alisema, «Hakika nafsi yangu itaniuma akiepukana na mimi na mkaenda na yeye malishoni. Na mimi nachelea asije akaliwa na mbwamwitu, hali mkiwa kwenye shughuli zenu mumeghafilika na yeye.»

    [14] Wakasema ndugu zake Yūsuf kumwambia baba yao, «Ikiwa mbwamwitu atamla na hali sisi ni kikundi chenye nguvu, sisi wakati huo tutakuwa ni wenye kupata hasara, hatuna wema wowote, na hakuna manufaa yoyote yanayotarajiwa kutoka kwetu.»

    [15] Hapo baba yao akawaachia wawe naye, walipokwenda na yeye na wakaamua kumtupa ndani ya kisima (na wakafanya hivyo) na hapo tukamletea wahyi Yūsuf, «Utawaambia ndugu zako mbeleni kuhusu kitendo chao hiki walichokufanyia na hali wao hawakitambui.»

    [16] Na wakaja ndugu zake Yūsuf kwa baba yao mwanzo wa usiku kipindi cha isha, huku wanalia na wanajionesha wana masikitiko na msiba

    [17] Wakasema, «Ewe baba yetu! Sisi tulikwenda tukawa tunashindana kukimbia na kurusha mishale, na tukamuacha Yūsuf kwenye vyombo vyetu na nguo zetu; na hatukufanya kasoro katika kumtunza, kwa kuwa tulimuacha mahali pa amani petu, na hatukumuacha isipokuwa kwa wakati mchache, mbwamwitu akamla. Na wewe hutatuamini, ingawa sisi ni wenye sifa ya ukweli, kwa sababu ya mapenzi yako makubwa kwa Yūsuf

    [18] Wakaja na kanzu yake ikiwa imerowa kwa damu ambayo si ya Yūsuf, ili iwe ni ushahidi juu ya ukweli wao, ikawa ni dalili ya urongo wao, kwa kuwa kanzu haikuchanika. Baba yao Ya’qūb, amani imshukiye, akawaaambia, «Mambo sivyo kama mlivyosema, bali ni nafsi zenu zenye kuamrisha uovu ziliwapambia jambo ovu kumfanyia Yūsuf, mkaliona ni zuri na mkalifanya. Basi nitasubiri subira nzuri isiyokuwa na malalamishi kwa kiumbe chochote, na namuomba Mwenyezi Mungu msaada wa kuweza kuubeba huo urongo mnaoupanga; sitegemei uwezo wangu wala nguvu zangu

    [19] Likaja kundi la wasafiri wakamtuma mwenye kuwatafutia maji, alipoiteremsha ndoo yake kisimani, Yūsuf aliishikilia. Hapo mchota maji alifurahi na akachangamka kwa kumuokota mtoto na akasema, «Ni bishara njema iliyoje! Huyu ni mtoto wa kiume mzuri.» Mchota maji na wenzake walimficha Yūsuf asijulikane na wasafiri wengine wasiwaoneshe, na wakasema, «Hii ni bidhaa tuumeinunua.» Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi mno wa wanayomfanyia Yūsuf

    [20] Na ndugu zake wakamuuza kwa wachota maji miongoni mwawasafiri kwa thamani chache ya dirhamu, na wakawa hawana haja na yeye, wanataka kuepukana na yeye. Hivyo ni kwa kuwa hawakijui cheo chake kwa Mwenyezi Mungu

    [21] Na wasafiri walipoondoka na Yūsuf kuelekea Misri, kiongozi wake alimnunua, naye ni waziri, na akamwambia mke wake, «Kaa naye vizuri na uyafanye mema makazi yake kwetu, huenda tukafaidika na utumishi wake, au tukamuweka hapa kwetu kama mtoto.» Na kama tulivyomuokoa Yūsuf na tukamfanaya kiongozi wa Misri kuwa na huruma na yeye, vilevile tulimmakinisha kwenye ardhi ya Misri na tulimfanya asimamie hazina zake, na ili tumfundishe kuagua ndoto na apate kujua kwa uaguze huo matukio ya wakati unaokuja. Na Mwenyezi Mungu ni Mshindi kwa jambo Lake, uamuzi Wake ni wenye kupita, hakuna Mwenye kuutangua, lakini wengi sana kati ya watu hawajui kwamba mambo yote yako kwenye mkono wa Mwenyezi Mungu

    [22] Yūsuf alipofikia umri wa kukamilika nguvu za ujana wake, tulimpa fahamu na elimu. Na mfano wa malipo haya tuliyomlipa Yūsuf kwa wema wake, tutawalipa walio wema kwa wema wao. Katika haya kauna kumliwaza Mtume, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye

    [23] Na mke wa yule kiongozi, ambaye Yūsuf alikuwa nyumbani kwake, alimtaka Yūsuf kwa upole na kubembeleza, kwa kuwa alimpenda sana na kwa ajili ya uzuri wake, na akamfungia milango na akasema kumwambia Yūsuf, «Njoo kwangu.» Akasema, «Najilinda kwa Mwenyezi Mungu na najihifadhi Kwake na kujihami kutokana na hayo unayoniitia ya kumfanyia hiana bwanangu aliyeyafanya mazuri mashukio yangu na akanikirimu. Sitamhini kwa watu wake. Hakika hafaulu anayedhulumu na akafanya mambo ambayo hatakiwi kuyafanya

    [24] Na nafsi yake ilivutika kufanya machafu, na Yūsuf nafsi yake ilipitiwa na mawazo ya kukubali, lau si yeye kuona alama miongoni mwa alama za Mola wake zenye kumkemea kufanya yale ambayo nafsi yake ilimzungumzia. Hakika tulimuonesha hilo, ili tumuepushiye baya na chafu katika mambo yake yote. Yeye ni miongoni mwa waja wetu waliosafishwa walioteulia kwa ujumbe na waliotakasa katika kumuabudu kwao Mwenyezi Mungu na kumpwekesha

    [25] Yūsuf alikimbilia mlangoni kutaka kutoka, na yeye (mke wa kiongozi) akafanya haraka kumshika na akamvuta nguo yake kwa nyuma ili kumzuia asitoke na akaipasua. Wakamkuta mumewe kwenye mlango, hapo akasema (mke wa Kiongozi), «Ni yapi malipo ya anayetafuta jambo baya kwa mke wako, isipokuwa ni afungwe au apewe adhabu yenye uchungu?»

    [26] Yūsuf akasema, «Yeye ndiye aliyetaka hilo kwangu. Na akatoa ushahidi mtoto wa mlezini katika jamaa zake(mke wa kiongozi) na akasema, «Iwapo kanzu yake imepasuka kwa mbele, basi mwanamke amesema kweli katika tuhma alizomfanyia na yeye (Yūsuf) ni miongoni mwa warongo

    [27] «Na iwapo nguo yake imeraruliwa kwa nyuma , basi mwanamke amesema urongo katika kauli yake, na yeye (Yūsuf) ni miongoni mwa wakweli.»

    [28] Yule mume alipoiona nguo ya Yūsuf imeraruliwa kwa nyuma alijua kwamba Yūsuf hana hatia na akasema kumwambia mke wake, «Urongo huu uliomtuhumu nao kijana huyu ni katika jumla ya vitimbi vyenu, enyi wanawake, kwani vitimbi vyenu ni vikubwa.»

    [29] Akasema kiongozi wa Misri, «Ewe Yūsuf! acha kutaja mambo yaliykuwa kutoka kwake na usimwambie yoyote. Na uombe msamaha wa dhambi zako kwa Mola wako, ewe mwanamke, iwapo wewe ni miongoni mwa wale waliofanya hatia kwa kumtaka Yūsuf kimapenzi bila ya yeye kutaka na kwa kumzulia urongo.»

    [30] Habari ziliwafikia wanawake mjini wakaizungumza kuhusu hizo na wakasema kwa njia ya kumpinga mke wa kiongozi, «Mke wa Bwana anajaribu kumtaka mtumwa wake na amwita amjie. Na mapenzi yake yamefikia kwenye ngozi ya moyo wake. Hakika sisi tunamuona yeye kuwa yuko kwenye upotevu waziwazi

    [31] Aliposikia mke wa Kiongozi kusengenya kwao na hila zao za kumtukana yeye, aliwatumia ujumbe na kuwaita kuja kumtembelea, na akatayarisha mito ya kutegemea na chakula cha kula, na akampa kila mmoja miongoni mwao kisu cha kukatia chakula kisha akasema kumwambia Yūsuf, «Jitokeze kwao.» Walipomshuhudia, walimuona ni kitu kikubwa chenye haiba, na wakashikwa na babaiko la uzuri wake na kuvutia kwake, wakajikata mikono yao katika hali ya kukata chakula kwa babaiko kuu na mshangao, na wakasema kwa kustaajabu, «Twajilinda na Mwenyezi Mungu! Huyu si binadamu!» kwa kuwa uzuri wake sio ule ujulikanao kwa wanadamu, «Huyu si mwingine isipokuwa ni mtukufu miongoni mwa Malaika.»

    [32] Mke wa kiongozi alisema kuwaambia wanawake waliojikata mikono yao, «Haya ndiyo yaliyowapata kwa kumuona yeye. Aliyefanya mpatikane na haya ni huyu kijana ambaye nyinyi mumenilaumu kusalitika naye. Kwa kweli nilimtaka na nikajaribu kumvutia ili anikubalie, akajizuia na akakataa. Na asipofanya ninachomuamuru mbeleni, atateswa kwa kutiwa jela na hapo atakuwa ni miongoni mwa wanyonge

    [33] Yūsuf akasema, akijilinda na shari lao na vitimbi vyao, «Ewe Mola wangu! Jela ni bora kwangu kuliko yale wanayoniitia ya kufanya machafu. Na usiponiepulia vitimbi vyao, nitalemea kwao na nitakuwa ni miongoni mwa wachache wa akili wenye kujifanyia madhambi kwa ujinga wao

    [34] Mwenyezi Mungu Akamkubalia Yūsuf maombi yake, akamwepushia kile alichotaka mke wa Kiongozi na marafiki zake kutoka kwake cha kumuasi Mwenyezi Mungu. Mwenyezi mungu Ndiye Mwenye kuyasikia maombi ya Yūsuf na maombi ya kila mwenye kuomba kati ya waja Wake, Ndiye Mwenye kuyajua matakwa yake, haja zake na kile kinachomfaa, na pia haja za viumbe Vyake vyote na yale yanayowafaa

    [35] Kisha ikamdhihirikia waziri na marafiki zake, baada ya kuziona dalili za kuwa Yūsuf hana hatia na amejiepusha na machafu, wamfunge mpaka muda fulani, mrefu au mfupi, ili kuzuia fedheha

    [36] Wakaingia jela pamoja na yeye vijana wawili. Mmoja wao akasema, «Mimi nimeota usingizini kwamba mimi nakamua zabibu ili ziwe pombe.» Na mwingine alisema, «Mimi nimeota kwamba nabeba mkate juu ya kichwa changu na ndege wanaula. Wakasema, «Tupe habari, ewe Yūsuf, uaguzi wa ndoto tulizoziota. Sisi tunakuona wewe ni miongoni mwa wale wanaofanya wema katika kuabudu kwao Mwenyezi Mungu na kuingiliana kwao na viumbe Wake.»

    [37] Yūsuf aliwaambia, «Hamtajiwa na riziki ya chakula kwa namna yoyote ile, isipokuwa mimi nitawapa tafsiri yake kabla ya kuwajia. Tafsiri hiyo nitakayowapa nyinyi wawili ni miongoni mwa yale niliyofundishwa na Mola wangu. Mimi nimemuamini na nimemtakasia ibada na nimejiepusha na dini ya wasiomuamini Mwenyezi Mungu wala kuamini kufufuliwa na kuhesabiwa

    [38] «Na nimefuata Dini ya baba zangu: Ibrāhīm, Is’ḥāq na Ya’qūb, ndipo nikaamuabudu Mwenyezi Mungu Peke Yake. Haikuwa kwetu sisi kumfanyia Mwenyezi Mungu mshirika katika kumuabudu. Kumpwekesha Mwenyezi Mungu huko, kwa kumhusu Yeye Peke Yake kwa ibada, ni miongoni mwa yale ambayo Mwenyezi Mungu Ametutunukia sisi na watu, lakini wengi zaidi wa watu hawamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema ya upwekeshaji wa Mwenyezi Mungu na Imani.»

    [39] Yūsuf akaendelea kusema kuwaambia vijana wawili waliokuwa na yeye jela, «Je, kuwaabudu waungu walioumbwa wa aina mbalimbali ni bora au ni kumuabudu Mwenyezi Mungu Aliye Mmoja, Mwenye kutendesha nguvu

    [40] «Nyinyi hamuabudu chochote kisichokuwa Mwenyezi Mungu isipokuwa ni majina yasiyokuwa na maana yoyote, mumeyafanya ni waola, nyinyi na baba zenu, kwa ujinga wenu na upotevu; Mwenyezi Mungu Hakuteremsha hoja au dalili yoyote juu ya usahihi wake. Hukumu ya haki ni ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Peke Yake, Asiye na mshirika. Yeye Ameamrisha kwamba msimwandame wala msimnyenyekee Asiyekuwa Yeye, na kwamba mumuabudu Yeye Peke Yake. Na hii ndiyo Dini iliyolingana sawa isiyokwenda kombo. Lakini wengi zaidi wa watu hawalielewi hilo, hawaujui uhakika wake

    [41] «Enyi marafiki wangu gerezani, haya uchukueni uaguzi wa ndoto zenu: ama yule aliyeona kwenye ndoto yake kuwa anakamua zabibu, yeye atatoka jela na atakuwa ni mwenye kuishughulikia pombe ya mfalme. Ama mwingine aliyeota kuwa anabeba mkate juu ya kichwa chake, yeye atasulubiwa na aachwe, na ndege waje wamle kichwa chake. Limeshapitishwa jambo ambalo mlikuwa mnaliuliza na limeshamalizwa.»

    [42] Hapo Yūsuf akamwambia yule aliyemjua kuwa ataokoka kati ya wale marafiki wake wawili, «Nitaje kwa bwanako mfalme na umwelezee kwamba mimi nimedhulumiwa, nimefungwa bila hatia.» Shetani akamsahaulisha mwanamume yule kumtajia mfalme hali ya Yūsuf, na kwa hivyo akakaa Yūsuf ndani ya jela myaka kadha

    [43] Na mfalme akasema, «Mimi niliona ndotoni, katika kulala kwangu, ngombe saba wanono wanaliwa na ngombe saba walioambata kwa kukonda, na niliona visuke saba vibichi na visuke saba vikavu. Enyi mabwana na wakubwa, nipeni habari ya ndoto hii, iwapo nyinyi ndoto mnaagua.»

    [44] Wakasema, «Ndoto yako hii ni mchanganyiko wa ndoto usiokuwa na tafsiri, na sisi hatukuwa ni wenye ujuzi kuagua ndoto namna hii.»

    [45] Hapo akasema yule aliyeokoka na kuuawa kati ya marafiki wawili wa Yūsuf ndani ya jela, na akakumbuka habari ya Yūsuf baada ya muda kupita, «Mimi nitawapa habari ya tafsiri ya ndoto hii. Nitumeni kwa Yūsuf nipate kuwaletea uaguzi wake.»

    [46] Alipofika yule mtu kwa Yūsuf alimwambia, «Yūsuf! Ewe mkweli sana! Tuagulie ndoto ya aliyeota ng’ombe saba wanono wanaliwa na ng’ombe saba waliokonda, na akaona masuke saba mabichi na mengine makavu. Natarajia nitarudi kwa mfalme na marafiki zake niwape tafsiri ya hiyo niliyokuuliza na ili wapate kujua cheo chako na utukufu wako.»

    [47] Yūsuf akasema kumwambia aliyemuuliza juu ya ndoto ya mfalme. «Uaguzi wa ndoto hii ni kwamba nyinyi mtaendelea kulima kwa bidii kwa myaka saba mfululizo ili mapato yawe mengi, basi kile mtakachokivuna kila mara kiwekeni akiba na mkiache kwenye masuke yake ili kihifadhike na kuingiwa na wadudu na ili kisalie kwa kipindi kirefu zaidi, isipokuwa kiasi kidogo cha nafaka mtakachokila

    [48] «Kisha itakuja, baada ya myaka ya neema, myaka yenye chaka kikali. Watu wa wakati huu watakula chakula mlichowahifadhia hapo nyuma, isipokuwa kichache mtakachokihifadhi na kukiweka akiba kiwe ni mbegu za kupandia mimea

    [49] «Kisha utakuja, baada ya myaka hii ya chaka, mwaka ambapo watu watanyeshezewa mvua, na hivyo basi Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Awaondolee shida, hapo wakamue matunda kwa wingi wa mavuno na neema.»

    [50] Mfalme akasema kuwaambia wasaidizi wake, «Mtoeni jela huyo mtu aliyeagua ndoto, na mleteni kwangu.» Yule aliyetumwa na mfalme alipomjia (Yūsuf) kumwita. Yūsuf alisema kumwambia, «Rudi kwa bwanako mfalme umtake awaulize wanawake walioijaruhi mikono yao juu ya uhakika wa mambo yao na habari zao na mimi, ili ukweli ufunuke kwa wote, na kutokuwa na hatia kwangu kuwe wazi, kwani Mola wangu ni Mjuzi zaidi wa mambo waliyoyapanga na waliyoyafanya, hakuna chochote kinachofichika Kwake katika hayo.»

    [51] Mfalme akasema kuwaambia wanawake walioijaruhi mikono yao. «Habari zenu ni zipi, mlipomtaka Yūsuf siku ya makaribisho? Kwani mliona chochote kutoka kwake chenye kutia shaka?» Wakasema, «Mwenyezi Mungu Atulinde! Hatujui chochote hata kidogo cha kumtia ila.» Hapo alisema mke wa Kiongozi, «Sasa umefunuka ukweli baada ya kufichika. Mimi ndiye niliyejaribu kumtia hatiani kwa kumbembeleza, na akakataa. Na yeye ni katika wakweli katika kila alilolisema

    [52] «Neno hilo nililolisema la kumwepushia Yūsuf tuhuma na kuikubalia makosa mimi mwenyewe ni kwa ajili mume wangu ajue kwamba mimi sikumfanyia hiana kwa kumzulia urongo na hayakutukia machafu kutoka kwangu pamoja na kuwa nilimtaka Yūsuf. Nimekubali hilo ili kuonyesha wazi kuwa mimi sina hatia wala yeye hana hatia na kwamba Mwenyezi Mungu Hawaafikii wala Hawaongozi wenye kufanya hiana katika uhaini wao.»

    [53] Akasema mke wa kiongozi,»Sijisafishi nafsi yangu, kwani nafsi inamwamrisha mtu sana kufanya maasia, kwa kutaka kupata utamu wa inavyopenda, isipokuwa yule ambaye Mwenyezi Mungu Amemhifadhi. Kwani Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe dhambi za waliotubia miongoni mwa waja Wake, ni Mwenye huruma nao sana.»

    [54] Mfalme, mtawala wa Misri, ilipomfikia habari kwamba Yūsuf hana hatia, alisema, «Mleteni kwangu nipate kumfanya ni miongoni mwa marafiki wangu wa kikweli na washauri wangu.» Yūsuf alipokuja, na mfalme akasema na yeye, akajua kwamba yeye hana hatia na kwamba ni muaminifu sana na ni mwenye tabia njema, alimwambia, «Wewe leo hapa kwetu una heshima kubwa na unaaminiwa kwa kila kitu.»

    [55] Yūsuf akataka kuwanufaisha waja na kueneza uadilifu baina yao, alimwambia mfalme, «Nifanye mimi kuwa msimamizi wa hazina za Misri, kwani mimi ni mshika hazina mwaminifu mwenye ujuzi na busara juu ya vitu ninavyosimamia.»

    [56] Na kama Mwenyezi Mungu Alivyomneemesha Yūsuf kwa kumtoa jela, Alimmakinisha katika nchi ya Misri akawa ashukia popote pale anapotaka. Mwenyezi Mungu Anampa rehema Zake Anayemtaka kati ya waja wake wachamungu, na Hayapotezi malipo ya yoyote aliyefanya matendo mema

    [57] Na kwa hakika malipo mema ya Akhera ni makubwa zaidi kuliko malipo ya duniani kwa wenye Imani na uchamungu ambao wanayaogopa mateso ya Mwenyezi Mungu na wanamtii Yeye katika maamrisho Yake na makatazo Yake

    [58] Nduguze Yūsuf walifika Misri, baada ya kushukiwa na ukame katika nchi yao, ili wachukue chakula kutoka huko. Wakaingia kwake na yeye, kwa nguvu ya akili yake ya kutambua na werevu wake, akawajua na wao wasimjue kwa muda mrefu uliopita na kwa kubadilika umbo lake

    [59] Yūsuf aliamuru wakirimiwe na wakaribishwe vizuri, kisha akawapa chakula walichotaka. Na walikuwa wamemwambia kwamba wana ndugu yao wa kwa baba ambaye hawakumleta pamoja nao, wakimaanisha ndugu yake Binyamin, akasema, «Nileteeni ndugu yenu wa kwa baba, kwani hamuoni kwamba mimi nimewapimia chakula vizuri na nimewakirimu kwa kuwakaribisha, na mimi ni mwema wa kuwakaribisha

    [60] «Na msiponijia na yeye, basi nyinyi hamtakua na chakula ambacho mimi nitawapimia, na msije kwangu.»

    [61] Wakasema, «Tutafanya bidii yetu kumkinaisha baba yake atuachie, na hatutaacha kufanya hivyo.»

    [62] Yūsuf aliwaambia watumishi wake, «Ichukueni thamani ya vitu vyao muiweke kwenye vyombo vyao kwa siri, kwa matarajio wapate kuiona watakapofika kwao na watambue vile sisi tulivyowakirimu ili wapate kurudi wakiwa na matumaini ya kupata vipewa vyetu.»

    [63] Waliporejea kwa baba yao walimsimulia yaliyokuwa ya ukarimu aliowafanyia huyo kiongozi, na wakasema, «Yeye hatatupatia kitu mbeleni isipokuwa iwapo ndugu yetu ambaye tulimuelezea kuhusu yeye atakuwa na sisi. Basi tuachie tuende na yeye tutaleta chakula kingi, na tunakuahidi kwamba tutamtunza.»

    [64] Baba yao akawaambia, «Vipi nitawaamini juu ya Binyāmīn, na nilishawaamini juu ya Yūsuf kabla yake, mkaahidi kumhifadhi na msilitekeleze hilo? Mimi siziamini ahadi zenu na utunzi wenu, lakini mimi nauamini utunzi wa Mwenyezi Mungu, Bora wa wenye kutunza na Mwenye huruma zaidi kuliko wenye huruma. Namtarajia Anirehemu, Amtunze na Amrudishe kwangu.»

    [65] Na walipofungua vyombo vyao walipata kwamaba thamani ya bidhaa waliyoitoa wamerudishiwa. Wakasema, «Ewe baba yetu! Tuombe nini zaidi ya hii? Hii ni thamani ya bidhaa zetu, Kiongozi ameturudishia, basi kuwa na utulivu kuhusu ndugu yetu na muache aende na sisi ili tupate kuwaletea watu wetu chakula kingi, tumtunze ndugu yetu na tupate kuongeza twesha ya ngamia kwa ajili yake. Kwani Kiongozi anampimia kila mtu twesha ya ngamia mmoja; na hilo ni jambo jepesi kwake.»

    [66] Ya’qūb, amani imshukiye, akasema kuwaambia, «Sitamuacha aende na nyinyi mpaka mchukue ahadi na mniapie kwa Mwenyezi Mungu kwamba mtamrudisha kwangu, isipokuwa iwapo mtashindwa nguvu msiweze kumuokoa. Basi walipompa ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa lile alilolitaka, Ya’qūb alisema, «Mwenyezi Mungu kwa tunalolinena Ndiye mtegemewa» Yaani, ushahidi Wake kwetu na utunzi Wake zinatutosha.»

    [67] Na akasema baba Yao kuwaambia wao,»Enyi wanangu mtakapoingia nchi ya Misri, msiingie kwa mlango mmoja, lakini ingieni kwa milango mbalimbali, ili msipatwe na jicho la husuda. Na mimi nikiwapa wasia huu, siwakingi na chochote Alichokiamua Mwenyezi Mungu kwenu. Hakuna uwamuzi wowote isipokuwa ni ule wa Mwenyezi Mungu Peke Yake, Kwake Yeye nimetegemea na nimeamini, na juu Yake Peke Yake waumini wanategemea.»

    [68] Na walipoingia kupitia milango mbalimbali, kama alivyowaamrisha baba yao, hilo halikuwa ni lenye kuwazuilia uamuzi wa Mwenyezi Mungu kwao, isipokuwa ilikuwa ni huruma ndani ya moya wa Ya’qūb juu yao wasipatikane na jicho la husuda. Na Ya’qūb ni mwenye ujuzi mkubwa wa mambo ya Dini yake aliyofundishwa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya wahyi, lakini wengi wa watu hawajui mwisho wa mambo na undani wake, na pia hawayajui anayoyajua Ya’qūb, amani imshukie, katika mambo ya Dini yake

    [69] Na walipoingia ndugu zake Yūsuf kwake, katika nyumba yake ya kukaribisha wageni, wakiwa pamoja na ndugu yake wa kwa baba na mama, Yusuif alimkumbatia nduguye wa kwa baba na mama na akamwambia kwa siri, «Mimi ni ndugu yako. Basi usihuzunike wala usiingiwe na dhiki kwa yale waliyonifanyia kipindi kilichopita.» Na akamuamuru alifiche jambo hilo kwao

    [70] Na alipowatayarishia Yūsuf na akawabebesha chakula ngamia wao, aliwaamuru watumishi wake wakakiweka kile chombo, ambacho alikua akiwapimia nacho watu, kwenye vyombo vya ndugu yake Binyamin kwa namna ambayo asitambue yoyote. Basi walipopanda kwenda zao, aliita mwenye kuita akisema, «Enyi wenye ngamia waliobebeshwa chakula, nyinyi ni wezi!»

    [71] Wakasema wana wa Ya’qūb, wakimwelekea yule aliyeita, «Ni kitu gani mnachokikosa?»

    [72] Yule aliyeita na waliokuwana yeye walisema, «Tumekikosa kipimio ambacho mfalme anapimia nacho. Na zawadi za mwenye kukileta ni twesha ya ngamia mmoja ya chakula.» Na yule aliyeita akasema, «Na mimi naidhamini na kuitolea ahadi hiyo twesha ya ngamia ya chakula.»

    [73] Ndugu zake Yūsuf wakasema, «Tunaapa kwa Mwenyezi Mungu, nyinyi mna uhakika kwa mliyoyashuhudia kutoka kwetu kwamba sisi hatukuja nchi ya Misri kufanya uharibifu, na si katika sifa zetu kuwa wezi.»

    [74] Wale waliopewa jokumu la kukitafuta kipimio walisema kuwaambia ndugu zake Yūsuf, «Ni ipi adhabu ya mwizi kwenu nyinyi, iwapo nyinyi ni warongo katika kauli yenu: ‘sisi si wezi’?»

    [75] Ndugu zake Yūsuf wakasema, «Malipo ya mwizi ni kwamba yule ambaye kitapatikana kilichoibiwa kwenye mzigo wa ngamia wake basi yeye ndiye malipo yake.» Yaani atakabidhiwa, kwa sababu ya wizi wake, kwa yule aliyemuibia awe mtumwa kwake.»Malipo mfano huu, nayo ni ya kufanywa mtumwa, tunawalipa wenye kufanya dhuluma kwa kuiba. Hii ndiyo dini yetu na mwendo wetu kuhusu wezi.»

    [76] wakarudi na ndugu zake Yūsuf kwake, akasimama mwenyewe kupekua mizigo yao. Akaanza na mizigo yao kabla ya mzigo wa ndugu yake, ili kuimarisha mpango wake wa kumfanya ndugu yake abakie pamoja na yeye, kisha akamalizikia kwenye vyombo vya ndugu yake na akakitoa chombo humo. Hivyo ndivyo tulivyomsahilishia Yūsuf mpango huu ambao ulimpelekea kumchukua ndugu yake kwenye mamlaka ya mfalme wa Misri. Kwani si katika dini yake kummiliki mwizi, isipokuwa kwamba matakwa ya Mwenyezi Mungu yamepelekea mipango hii na kutaka uamuzi kwenye sheria ya ndugu zake Yūsuf yenye hukumu ya mwizi kufanywa mtumwa. Tunawainua daraja tunaowataka ulimwenguni juu ya mwingine kama vile tulivyomuinua Yūsuf daraja. Na juu ya kila mwenye ujuzi kuna mjuzi zaidi kuliko yeye, mpaka ujuzi ukome kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Mjuzi wa yaliyofichika na yanayoonekana

    [77] Wakasema ndugu zake Yūsuf, iwapo huyu yuwaiba, ametangulia ndugu yake kuiba (wakimaanisha Yūsuf, amani imshukiye). Yūsuf akalificha hilo alilosikia la uzushi kutoka kwao ndani ya nafsi yake,na akauzungumzia moyo wake kwa kusema, «Nyinyi ni wabaya zaidi wa mahali kuliko huyo mliyomtaja, mliponifanyia njama zile zilizokua kutoka kwenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi wa sifa za urongo na uzushi mnazozitoa.»

    [78] Wakasema kwa njia ya kubembeleza na kutaka kuhurumiwa ili watekeleze ahadi ya baba yao, «Ewe kiongozi, hakika yeye ana mzazi wa kiume mkubwa wa myaka anayempenda na asiyeweza kuwa mbali na yeye. Kwa hivyo mchukue mmoja wetu badala ya Binyamin. Sisi tunakuona ni miongoni mwa watenda wema kwa vile unavotutendea sisi na wasiokuwa sisi.»

    [79] Yūsuf akasema, «Tunaomba hifadhi ya Mwenyezi Mungu na himaya Yake, tusiwe ni wenye kumchukua yoyote isipokuwa yule ambaye tulipata kipimio chetu kwake, kama mlivyoamua wenyewe. Kwani sisi tukifanya hayo ambayo mnataka tutakuwa ni miongoni mwa wanaohesabiwa kuwa ni waonevu.»

    [80] Walipokata tamaa ya kukubali kwake matakwa yao, walikaa kando na watu wakawa wanashauriana baina yao. Mkubwa wao kimyaka alisema, «Je hamjui kuwa baba yenu alichukuwa kwenu ahadi ya mkazo kuwa mtamrudisha ndugu yenu mpaka mshindwe, Na kabla ya tukio hili mlifanya kasoro kuhusu Yūsuf na mkamzungukia kinyume kwa hiana. Kwa hivyo sitaondoka kwenye ardhi ya Misri mpaka baba yangu aniamuru niondoke au Mola wangu Anihukumie niondoke na niweze kumchukua ndugu yangu. Na Mwenyezi Mungu ni Bora wa wanaohukumu na ni muadilifu zaidi wa wenye kutoa uamuzi baina ya watu

    [81] Rudini nyinyi kwa baba yenu, mpeni habari ya yaliyojiri na mwambieni, «Mwano Binyamin ameiba, na hatukushuhudia isipokuwa kwa lile ambalo tuna uhakika nalo. Kwani tumekiona kipimio kwenye mzigo wake, na hatukuwa na ujuzi wa ghaibu kuwa yeye ataiba tulipokuahidi kumrudisha.»

    [82] Waliporejea, wakampa habari baba yao yaliyotokea na wakamtaka ahakikishe yale waliyomwambia wakisema, «Na waulize, ewe baba yetu, watu wa Misri na wale waliokuwa pamoja na sisi kwenye msafara tuliorudi nao. Na sisi ni wakweli kwa yale tuliyokusimulia.»

    [83] Akawaambia, «Bali nafsi zenu zinazoamrisha mabaya ndizo zilizowapambia njama mlizozipanga, kama mlivyomfanyia Yūsuf. Basi uvumilivu wangu ni uvumilivu mzuri usio na babaiko wala ulalamishi. Kwani huenda Mwenyezi Mungu Akanirudishia wanangu watatu: Yūsuf, nduguye wa kwa baba na mama na ndugu yao mkubwa aliyebaki nyuma kwa sababu ya ndugu yake. Hakika Yeye Ndiye Mjuzi wa hali yangu , Ndiye Mwenye hekima katika uendeshaji mamboWake.»

    [84] Ya’qūb akawapa mgongo na asishughulike nao, ukiwa moyo wake umeingia dhiki kwa maneno waliyoyasema, na akasema, «Ewe hasara yangu juu ya Yūsuf!» Na macho yake yakawa meupe, kwa kuondoka weusi wake kwa masikitiko mengi. Moyo wake umejaa tele huzuni, lakini alikuwa akiificha sana

    [85] Wanawe wakasema, «Tunaapa kwa Mwenyezi Mungu, utendelea kumkumbuka Yūsuf na kuwa na huzuni nyingi juu yake mpaka ukaribie kuangamia au uangamie kikweli, basi ipumzishe nafsi yako.»

    [86] Ya’qūb akasema kuwajibu, «Simuonyeshi hamu yangu na masikitiko yangu isipokuwa Mwenyezi Mungu Peke Yake. Yeye Ndiye Mwenye kuondoa shida na matatizo. Na ninayajua, kuhusu rehema ya Mwenyezi Mungu na maliwazo Yake, mambo msiyoyajua.»

    [87] Ya’qūb akasema, «Enyi wanangu! Rudini Misri mpeleleze habari za Yūsuf na ndugu yake , wala msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu, kwani hawakati tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu isipokuwa wenye kuukanusha uwezo Wake, wenye kumkataa Yeye.»

    [88] Wakaenda Misri. Na walipoingia kwa Yūsuf walisema, «Ewe kiongozi, tumepatikana na ukame na ukavu, na tumekujia na thamani isiyokuwa nzuri na iliyo chache, basi tupe kwa hii thamani kiasi ulichokuwa ukitupa kabla kwa thamani nzuri. Na utunuku kwa kukubali kupokea thamani hii mbaya iliyo chache, na utulegezee juu ya hiyo thamani, hakika Mwenyezi Mungu Anawalipa wema wale wenye kuwasaidia wahitaji kwa mali zao.»

    [89] Aliposika maneno yao alilainika juu yao, akajitambulisha kwao na akasema, «Je, mnayakumbuka mabaya mliyomfanyia Yūsuf na ndugu yake mlipokuwa katika hali ya kutojua vile matendo yenu yataishia?»

    [90] Wakasema, «Je, kwa kweli wewe ni Yūsuf?»Akasema, «Ndio. Mimi ni Yūsuf na huyu ni ndugu yangu. Mwenyezi Mungu Ametukirimu, akatukusanya pamoja baada ya kupambanukana. Hakika Mwenye kumcha Mwenyezi Mungu na akavumilia shida, Mwenyezi Mungu hamuondolei malipo ya wema wake, Hakika atamlipa malipo mema zaidi.»

    [91] Wakasema, «Tunaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba Mwenyezi Mungu amekutukuza juu yetu na Amekufanya bora kwa elimu, upole na utukufu, ingawa sisi ni wakosa kwa yale tuliyokufanyia wewe na ndugu yako kwa kukusudia.»

    [92] Yūsuf akawaamia, «Hamlaumiwi leo; Mwenyezi Mungu Atawasamehe. Na Yeye ni Mwenye huruma zaidi ya wenye huruma kwa anayetubia dhambi zake na akarejea kwenye utiifu Kwake.»

    [93] Na alipowauliza kuhusu baba yake, walimpa habari ya kupofuka macho yake kwa kumlilia. Akawaambia, «Rudini kwa baba yenu mkiwa na kanzu yangu hii, mtupieni usoni mwake na macho yake yatarudi kuona, kisha waleteni kwangu watu wenu wote.»

    [94] Msafara ulipotoka nchi ya Misri wakiwa na ile kanzu, Ya’qūb alisema kuwaambia wale waliokuwa na yeye, «Mimi nasikia harufu ya Yūsuf, ingawa nyinyi mtanifanya ni mchache wa akili, mtanicheza shere na mtadai kwamba maneno haya yametoka kwangu bila ya fahamu.»

    [95] Waliohudhuria hapo kwake walisema, «Tunaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba wewe bado uko kwenye telezo lako la zamani la kumpenda Yūsuf na kwamba wewe hutamsahau.»

    [96] Alipokuja mwenye kumpa bishara Ya’qūb kwamba Yūsuf yuko hai, akaitupa kanzu ya Yūsuf usoni mwake akarudi Ya’qūb kuwa yuaona, akajawa na furaha na akawaambia waliokuwa hapo kwake, «Je, sikuwapa habari kwamba mimi nayajua kutoka kwa Mwenyezi Mungu msiyoyajua ya fadhila Zake, rehema Zake na ukarimu Wake.»

    [97] Wanawe wakasema, «Ewe baba yetu, tuombee Mola wako Atusamehe na Atusitirie dhambi zetu, hakika sisi tulikuwa wakosa katika yale tuliyomfanyia Yūsuf na ndugu yake.»

    [98] Ya’qūb akasema , «Nitamuomba Mola wangu Awasamehe dhambi zenu, kwani Yeye ni Mwingi wa kusamehe dhambi za waja Wake wanaotubia, ni Mwingi wa rehema kwao.»

    [99] Ya’qūb na watu wa nyumbani kwake wakatoka kuelekea Misri wakimkusudia Yūsuf. Walipofika kwake, Yūsuf aliwakumbatia wazazi wake wawili na akawaambia (wao wote), «Ingieni Misri kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu na hali mkiwa mko kwenye amani na mumeepukana na shida, ukame na kila zito.»

    [100] Akawakalisha wazazi wake wawili kwenye kitanda cha ufalme wake kwa njia ya kuwatukuza. Na wazazi wake na ndugu zake kumi na moja wakamsalimia kwa kumuinamia kwa kumwamkia na kumtukuza na sio kumuabudu na kumnyenyekea. Na hilo lilikuwa linaruhusiwa katika Sheria yao, na limeharamishwa katika Sheria yetu, kwa ajili ya kuziba njia inayopelekea kwenye ushirikina. Na Yūsuf akamwambia baba yake, «Kusujudu huku ndio uaguzi wa ndoto yangu niliyokusimulia kabla, katika udogo wangu, Mwenyezi Mungu Ameifanya ni kweli. Na amenifadhili aliponitoa jela na akawaleta nyinyi kutoka jangwani, baada ya Shetani kuharibu uhusiano wa undugu baina yangu mimi na ndugu zangu. Hakika Mola wangu ni Mpole wa kupitisha Analolitaka. Yeye Anayajua sana maslahi ya waja Wake, ni Mwingi wa hekima katika maneno Yake na vitendo Vyake.»

    [101] Kisha Yūsuf alimuomba Mola wake akisema, «Mola wangu! Umenipa ufalume wa Misri, na umnifundisha uaguzi wa ndoto na elimu nyinginezo. Ewe Muumba, na Mtengenezaji, mbingu na ardhi! Wewe Ndiye Msimamizi wa mambo yangu ulimwenguni na Akhera. Nifishe unichukue kwako nikiwa Muislamu na unikutanishe na waja wako wema miongoni mwa Manabii watenda mema na wasafiwa walioteuliwa.»

    [102] Hayo yaliyotajwa ya habari za Yūsuf ni miongoni mwa habari za ghaibu, tunakuelezea , ewe Mtume, kwa njia ya wahyi. Na hukuwako pamoja na ndugu zake Yūsuf walipompangia kumtia kisimani na wakamfanyia hila yeye na baba yake. Hii inaonesha dalili ya ukweli wako na kwamba Mwenyezi Mungu Anakuletea wahyi

    [103] Hawakuwa wengi wa washirikina miongoni mwa watu wako, ewe Mtume, ni wenye kukusadiki wala kukufuata, ingawa una pupa juu ya Imani yao. Basi usisikitike kwa hilo

    [104] Na hutaki kwa watu wako ujira ya kuwaongoa kwenye Imani. Na yale uliyotumwa nayo ya Qur’ani na uongofu ni mawaidha kwa watu wote wanajikumbusha kwayo na wanaongoka

    [105] Na dalili zenye kuonyesha upweke wa Mwenyezi Mungu na uwezo Wake ni nyinygi, zimeenea kwenye mbingu na ardhi, kama jua, mwezi, majabali na miti. Wanaziona lakini wamezipa mgongo, hawazifikirii na wala hawazingatii

    [106] Na hawa wenye kuzipa mgongo dalili za Mwenyezi Mungu hawakubali kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaumba, ni Mwenye kuwapa riziki, ni Muumba wa kila kitu na ni Mstahiki wa kuabudiwa isipokuwa katika hali ya kumshirikisha kwa kuabudu kwao masanamu na mizimu. Mwenyezi Mungu Ametukuka na kuepukana na hilo kabisa

    [107] Je, wana chochote kinachowafanya wameaminika isiwashukie wao adhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu yenye kuwaenea au iwajie wao Siku ya Kiyama ghafla na hali wao hawatambui wala hawana hisia na hilo

    [108] Waambie, ewe Mtume, «Hii ni njia yangu, ninaita kwenye kumuabudu Mwenyezi Mungu Peke Yake, nikiwa kwenye hoja inayotoka kwa Mwenyezi Mungu na uhakika, mimi na anayenifuata. Na ninamuepusha Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, na washirika na mimi si katika wale wanaomshirikisha pamoja na Mwenyezi Mungu mtu mwingine.»

    [109] Hatukuwatuma kabla yako, ewe Mtume, kwa watu isipokuwa wanaume miongoni mwao ambao tunawateremshia wahyi wetu, na wao ni miongoni mwa watu wa mijini, kwani hao wana uwezo zaidi wa kuuelewa ulinganizi na ujumbe, wawaamini wenye kuongoka kwenye haki na wawakanusha wenye kupotea njia yake. Basi si watembee katika ardhi wajionee ulikuwa vipi mwisho wa wakanushaji waliopita na ni maangamivu gani yaliyowashukia? Na malipo mema ya Nyumba ya Akhera ni bora kuliko dunia na vilivyomo ndani, kwa walioamini na wakamuogopa Mola wao. Basi hamfikirii mkazingatia

    [110] Na usiwe na haraka, ewe Mtume, ya kupata ushindi juu ya wanaokukanusha, kwani Mitume kabla yako hawakuwa wakijiwa na ushindi wa haraka kwa hekima tunayoijua. Ifikapo hadi ya Mitume kukata tamaa na watu wao na kuwa na hakika kwamba watu wao wamewakanusha na hakuna tamaa ya wao kuamini, ushindi utawajia wakati ambapo shida imezidi, basi hapo tuwaokoe tunaowataka kati ya Mitume na wafuasi wao. Na adhabu yetu haitorudishwa kutoka kwa Aliyefanya uhalifu na akmfanyia ujasiri Mwenyezi Mungu. Katika hili kuna kumliwaza Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [111] Kwa hakika kwenye habari za Mitume tulizokuelezea na mambo yaliyowakumba wenye kukanusha kuna mawaidha kwa wenye akili timamu. Hii Qur’ani haikuwa ni habari ya urongo iliyozuliwa, lakini tumeiteremsha ikiwa ni yenye kutolea ushahidi ukweli wa vitabu vilivyoteremshwa vilivyotangulia na kwamba vinatoka kwa Mwenyezi Mungu, na ikiwa ni ufafanuzi wa kila ambalo waja wanalihitaji la kuhalalishiwa na kuharamishiwa, linalopendeza na linalochukiza na mengineyo, na ikiwa ni muelekezo kutoka kwenye upotevu na ni rehema, kwa wenye Imani, ya kuzifanya nyoyo zao ziongoke, wapate kuyafuata kivitendo maamrisho na makatazo yaliyomo

    Ngurumo

    Surah 13

    [1] Alif, Lām, Mīm. Maelezo kuhusu herufi ziliokatwa na kutengwa yametangulia mwanzo wa sura ya Al-Baqarah. Hizi ni aya za Qur’ani zenye cheo kitukufu. Na Qur’ani hii uliyoteremshiwa, ewe Mtume, ndiyo haki, na sivyo kama vile wanavyosema washirikina kwamba wewe mwenyewe ndio uliyoileta. Pamoja na hili, wengi wa watu hawaiamini wala hawaifuati kivitendo

    [2] Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Ndiye Aliyeziinua mbingu saba kwa uweza Wake bila ya nguzo, kama vile ambavyo mnaziona, kisha akalingana - yaani akawa juu - ya Arshi kulingana kunakonasibiana na utukufu Wake na ukubwa Wake, na Akalidhalilisha jua na mwezi kwa manufaa ya waja, kila moja wapo ya viwili hivyo kinazunguka kwenye anga lake mpaka Siku ya Kiyama. Anapekesha, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, mambo ya ulimwenguni na Akhera, Anawafafanulia dalili zenye kuonyesha uweza Wake na kwamba yeye hakuna mungu isipokuwa Yeye, ili muwe na Imani ya kikweli kwa Mwenyezi Mungu na mjiyakinishe kurudi Kwake, mpate kuamini ahadi Yake ya thawabu na adhabu na mumtakasiye ibada Peke Yake

    [3] Na Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Ambaye Aliifanya ardhi iwe kunjufu iliyonyoshwa, Akaitayarisha kwa maisha yenu, Akayaweka humo majabali yenye kuithibitisha na mito ya nyinyi kunywa na kunufaika, Akaweka humo aina mbili za kila matunda, katika hayo kukawa kuna meupe na meusi, tamu na kali, na Akaufanya usiku ufinike mchana kwa giza lake. Hakika katika hayo yote pana mazingatio kwa wenye kuyafikiri wakawaidhika

    [4] Na kwenye ardhi kuna sehemu zinaopakana, kati ya hizo kuna zilizo nzuri zenye kuota mimea inayowafaa watu na kati ya hizo kuna kavu zenye chumvi zisizootesha chochote. Na katika ardhi nzuri kuna mashamba ya zabibu, na Amejaalia humo aina tafauti za makulima na mitende iliyokusanyika mahali pamoja na isiyokusanyika hapo, vyote hivyo viko katika mchanga mmoja na vinakunywa maji mamoja, isipokuwa vinatafautiana katika matunda, ukubwa, utamu na mengineyo: hili ni tamu na hili ni kali, na mengine ni bora kuliko mengine katika kula. Katika hilo kuna dalili kwa mwenye moyo unaoyaelewa maamrisho ya Mwenyezi Mungu na makatazo Yake

    [5] Ukiona ajabu , ewe Mtume, ya makafiri kutoamini baada ya dalili hizi, basi ajabu kubwa zaidi ni kusema kwao, «Je, tukifa na tukawa mchanga tutafufuliwa upya?» Hao ndio wenye kumkanusha Mola wao Aliyewafanya waweko kutoka kwenye hali ya kutokuwako. Na hao kutakuwa na minyororo kwenye shingo zao Siku ya Kiyama. Na hao wataingia Motoni na hawatatoka kabisa

    [6] Na wale wakanushaji wanakuharakisha uwaletee adhabu ambayo mimi sikuwaharakishia kabla ya kuamini Imani ambayo kwayo kunatarajiwa usalama na matendo mema. Na yashapita mateso ya wakanushaji kabla yao, kwa nini wao hawawi ni wenye kuwaidhika na wao? Hakika Mola wako ni Mwenye msamaha wa dhambi za watu waliotubia dhambi zao juu ya udhalimu wao, Atawafungulia mlango wa msamaha na Atawaita waingie, na huku wao wanazidhulumu nafsi zao kwa kumuasi Mola wao. Hakika Mola Wako ni Mkali wa mateso juu ya walioendelea kwenye ukafiri, upotevu na kumuasi Mwenyezi Mungu

    [7] Na makafiri wa Makkah wanasema, «Basi si ajiwe na miujiza inayoonekana kama fimbo ya Mūsā na ngamia wa Ṣāliḥ.» Na hilo haliko kwenye mkono wako, ewe Mtume; hukuwa wewe isipokuwa ni mwenye kuwafikishia na ni mwenye kuwatisha adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na kila ummah una mjumbe wa kuwaongoza kwenye njia ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka

    [8] Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Anakijua alichokibeba kila mwanamke ndani ya tumbo lake: ni cha kiume au ni cha kike, ni chema au ni kibaya. Na anakijua kile ambacho zao zinakipunguza kikazaliwa kimekufa au kabla ya kutimia myezi tisa au kikapita muda huo. Na kila kitu, chenye kuzidi au kupungua, kimekadiriwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kipimo kisichopitisha kiasi

    [9] Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyofichika na macho na yanayoonekana, Aliye Mkubwa wa dhati, majina na sifa , Aliye juu ya viumbe Vyake vyote kwa dhati Yake, uweza Wake na kutendesha nguvu Kwake

    [10] Analingana, katika ujuzi Wake Aliyetukuka, yule anayesirisha maneno, katika nyinyi, na anayedhihirisha. Na analingana Kwake yule anayefanya matendo yake kwa siri ndani ya giza la usiku na yule mwenye kuyafanya waziwazi kwenye mwangaza wa mchana

    [11] Na Mwenyezi Mungu Anayetukuka Ana Malaika wanaompitia binadamu, kundi baada ya kundi, mbele yake na nyuma yake, wanamhifadhi kwa amri ya Mwenyezi Mungu na kuyadhibiti yanayofanywa na yeye, mema au maovu. Hakika Mwenyezi Mungu , Aliyetakata na kutukuka, Hageuzi neema aliyowaneemesha watu mpaka wakiwa wao watayageuza yale waliyoamrishwa na Mola wao na wakamuasi. Na Mwenyezi Mungu Akiwatakia watu mitihani basi hakuna namna ya kuyakimbia, na hawana wao asiyekuwa Mwenyezi Mungu msimamizi yoyote wa kuyasimamia mambo yao, akawaletea yanayopendwa na akawakinga na yanayochukiwa

    [12] Yeye Ndiye Ambaye anawaonesha umeme, nao ni mwangaza unaong’aa kutoka ndani ya mawingu, mkawa mnaogopa msishukiwe na vimondo venye kuchoma kutokana na umeme huo, na pia mkawa mnatazamia mvua inyeshe. Na kwa uweza Wake, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, anayleta mawingu yanayobebeshwa maji mengi kwa ajili ya manufaa yenu

    [13] Na radi linamtakasia Mwenyezi Mungu sifa Zake njema, matakaso yanayoonyesha dalili kwamba linamnyenyekea Mola Wake. Na Malaika wanamwepusha Mola wao na kila la upungufu kwa kumuogopa kwao Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu Anatuma vimondo vyenye kuangamiza, Akawaangamiza kwavyo anaowataka kati ya viumbe vyake. Na makafiri wanabisha juu ya upweke wa Mwenyezi Mungu na uweza Wake kufufufua, na hali Yeye Ana uweza mwingi na nguvu na ujabari wa kuwatesa waliomuasi

    [14] Ni wa Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Peke Yake, ulinganizi wa tawhīd «Hapana mola isipokuwa Mwenyezi Mungu.» Haabudiwi wala haombwi isipokuwa Yeye. Na waungu ambao wao wanawaabudu badala ya Mwenyezi Mungu hawaitiki maombi ya mwenye kuwaomba. Na hali yao pamoja na hao waungu ni kama hali ya mwenye kiu anayenyosha vitanga vyake viwili vya mkono kwenye maji kutoka mbali ili yafike kwenye kinywa chake, yakawa hayafiki. Na maombi ya makafiri kwa hao waungu hayakuwa isipokuwa yako mbali na usawa, kwa kuwa wao wanamshirikisha wengine pamoja na Mwenyezi Mungu

    [15] Na Mwenyezi Mungu Peke Yake wanamsujudia, wakinyenyekea na kufuata, walioko mbinguni na ardhini wote, Waumini wanamsujudia na kumnyenyekea kwa ridhaa na hiari, na makafiri wanamnyenyekea kwa nguvu, kwa kuwa wao wanafanya kiburi kumuabudu na hali yao na maumbile yao yanawakanusha juu ya hilo. Na vivuli vya viumbe vinafuata utukufu wa Mwenyezi Mungu, vinatembea kulingana na matakwa Yake mwanzo wa mchana na mwisho wake

    [16] Waambie washirikina, ewe Mtume, «Ni nani muumba mbingu na ardhi na mwenye kuziendesha?» Sema, «Mwenyezi Mungu Ndiye Muuumba Mwenye kuziendesha. Na nyinyi mnalikubali hilo.» Kisha waambie ukiwalazimisha hoja, «Je, mnawafanya wasiokuwa Yeye ni waabudiwa wenu, na hali ya kuwa wao hawawezi kuzinufaisha nafsi zao au kuzidhuru, wacha kule kuwanufaisha nyinyi au kuwadhuru, na mkaacha kumuabudu mwenye kuwamiliki wao?» Waambie, «Kwani analingana kwenu nyinyi kafiri, ambaye ni kama kipofu, na Muumini, ambaye ni kama anayeona? Au kwani unalingana kwenu nyinyi ukafiri, ambao ni kama giza, na Imani, ambayo ni kama mwangaza? Au ni kwamba wale wasimamizi wao wanaowafanya ni washirika wa Mwenyezi Mungu wanaumba kama Anavyoumba, vikawatatiza viumbe vya washirika na viumbe vya Mwenyezi Mungu, ndipo wakaitakidi kwamba wao wanastahiki kuabudiwa?» Waambie, ewe Mtume, «Mwenyezi Mungu Aliyetukuka ni Muumba kila kilichoko ambacho hakikuwako; Yeye Ndiye Anayestahiki kuabudiwa Peke Yake na Yeye Ndiye Aliye mmoja Mwenye kutendesha nguvu Anayestahiki uungu na ibada, na sio masanamu na mizimu isiyodhuru wala kunufaisha.»

    [17] Kisha Mwenyezi Mungu Akapiga mfano wa ukweli na urongo kuwa ni kama maji Aliyoyateremsha kutoka juu, yakapita kwenye mabonde ya ardhi kwa kadiri ya udogo wake na ukubwa wake, mikondo ya maji ikabeba povu likiwa juu yake lisilo na faida. Na akapiga mfano mwingine wa madini ambayo watu huyachoma moto ili kuyayeyusha kutaka kutengeneza pambo, kama vile dhahabu na fedha, au kutaka manufaa ya kujinufaisha, kama vile shaba, ukatoka uchafu wake usio na faida kama ule uliokuwa pamoja na maji. Kwa mfano huu, Mwenyezi Mungu Apigia mfano ukweli na urongo. Urongo ni kama povu la maji, linapotea au linatupwa kwa kuwa halina faida, na ukweli ni kama maji safi na madini yaliyotakasika, yanasalia kwenye ardhi kwa kunufaika nayo. Kama Alivyowafafanulia nyinyi mifano hii, hivyo ndivyo Anavyoipiga kwa watu upate kufunuka wazi ukweli ujitenge na urongo, na uongofu ujitenge na upotevu

    [18] Pepo ni ya wenye kuamini ambao wanamtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na Moto ni wa wale ambao hawakumtii na wakamkanusha. Na lau walikuwa wanamiliki kila kilichoko ardhini na zaidi ya kama hiko pamoja nacho, wangalikitoa kwa kujikomboa nafsi zao na adhabu ya Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama, na hakingalikubaliwa kutoka kwao. Wao watafanyiwa hesabu kwa kila tendo baya walilolitenda. Na makazi yao ya kukaa ni Jahanamu, itakuwa ni tandiko kwao. Na tandiko baya mno ni hilo walilojitayarishia nafsi zao

    [19] Je, yule anayejua kwamba kile ulichokuja nacho, ewe Mtume, ndicho ukweli unaotoka kwa Mwenyezi Mungu na akauamini ni kama kipofu asiyeuona ukweli ambaye hakuamini? Hakika wanaowaidhika ni wenye akili timamu

    [20] ambao wanatekeleza ahadi ya Mwenyezi Mungu Ambayo Aliwaamrisha kwayo na wasiitangue ahadi ya mkazo ambayo walimuahidi nayo Mwenyezi Mungu

    [21] Nao ndio ambao wanawaunga wale ambao Mwenyezi Mungu Amewaamrisha wawaunge kama jamaa wa karibu na wahitaji, wanamtunza Mola wao na wanaogopa Asiwahesabu kwa madhambi yao yote na Asiwasamehe chochote katika hayo

    [22] Nao ndio ambao walivumilia udhia na kusimama juu ya utiifu na kujiepusha na uasi kwa kutafuta radhi za Mola wao, walitekeleza Swala kwa namna iliyotimia zaidi, walitekeleza Zaka za lazima za mali yao na matumizi yanayopendekezwa kwa siri na kwa dhahiri na wakawa wanaondoa baya kwa zuri lenye kulifuta. Hao wanaosifika kwa sifa hizi watakuwa na mwisho wenye kusifiwa huko Akhera

    [23] Mwisho wao ni mabustani ya Pepo ya 'Adn, watakaa humo, hawataondoka kutoka humo, na pamoja nao watakuwamo waliokuwa wema miongoni mwa mababa, wake na watoto waume kwa wake, na huku malaika waingia kwao kutoka kila mlango wakipongeza na kuingia Peponi

    [24] Malaika watawaambia, «Amani iwashukie, yakiwa ni maamkizi yenu peke yenu, na msalimike na kila baya kwa uvumilivu wenu katika kumtii Mwenyezi Mungu. Neema ya nyumba ya mwisho ni Pepo.»

    [25] Ama waovu, wamesifiwa kwa sifa kinyume na zile za Waumini. Wao ni wale ambao hawatekelezi ahadi za Mwenyezi Mungu kwa kumpwekesha, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, kwa ibada baada ya kujitukulia ahadi ya mkazo. Na wao ni wale wanaokata kile ambacho Mwenyezi Mungu amewaamrisha kukiunga kama vile kukata zao na mengineyo na wanafanya uharibifu katika ardhi kwa kufanya maasia. Hao waliosifiwa kwa sifa hizi mbaya watakalolipata ni kufukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu na watakuwa na mambo ambayo ni mabaya kwao ya adhabu kali katika Nyumba ya Akhera

    [26] Mwenyezi Mungu Peke Yake Anamkunjulia riziki Anayemtaka miongoni mwa waja Wake na Anambania Anayemtaka kati yao. Na makafiri waliufurahia ukunjufu duniani. Na dunia hii haikuwa ikilinganishwa na Akhera isipokuwa ni kitu kidogo cha kustarehe nacho, na kwa haraka sana kinaondoka

    [27] Na makafiri wanasema kwa kushindana, «Si ateremshiwe Muhammad miujiza inayoonekena kama miujiza ya Mūsā na 'Īsā. Waambie kwamba Mwenyezi Mungu Anampoteza Anayemtaka miongoni mwa washindani wasiotaka uongofu na haimfai miujiza na Anawaongoza kwenye dini Yake ya haki anayerejea Kwake na kutaka radhi Zake

    [28] Na Anawaongoza wale ambao nyoyo zao zimetulia kwa kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtaja zikapata utulivu. Jua utanabahi kwamba kumtii Mwenyezi Mungu, kumtaja na malipo mema kutoka Kwake yanafanya nyoyo zitulie na zipumbae

    [29] Wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafanya matendo mema watakuwa na furaha, kipumbazi cha jicho, hali nzuri na marejeo mema kwenye Pepo ya Mwenyezi Mungu na radhi Zake

    [30] Kama tulivyowatuma Mitume kabla yako, tulikutuma, ewe Mtume, katika ummah waliopita kabla yao ummah wa Mitume, ili uwasomee ummah huu Qur’ani iliyoteremshwa kwako, na hali ya watu wako ni kuukanusha upweke wa Mwingi wa rehema. Waambie, ewe Mtume, «Mwingi wa rehema Ambaye hamkumpwekesha na mkamfanya ni Mola mmoja Ndiye Mola wangu, Peke Yake; hakuna mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye. Kwake Yeye nimetegemea na nina imani, na Kwake Yeye ndio marejeo yangu na makimbilio yangu

    [31] Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anawarudi makafiri ambao walitaka kwamba Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ateremshiwe miujiza yenye kuonekana, kwakuwaambia, «Lau kulikuwa na Qur’ani itakayosomwa ikafanya majabali yaondoke mahali pake au ardhi ipasuke itoe mito au wafu wafufuke na waseme, kama walivyotaka kwako, hii Qur’ani ingalikuwa ndiyo yenye kusifika na hayo na si kitu kingine, na pia hawangaliamini.. Bali ni ya Mwenyezi Mungu amri juu ya miujiza na mengineyo. Kwani hawakujua Waumini kwamba lau Mwenyezi Mungu Anataka, watu wote wa ardhini wangaliamini bila ya miujiza? Na hawataacha makafiri kuendelea kuteremkiwa na mkasa kwa sababu ya ukafiri wao, kama kuuawa na kutekwa katika vita vya Waislamu, au kuteremkiwa na mkasa huo karibu na nyumba zao, mpaka ahadi ya Mwenyezi Mungu ije ya kuwapa ushindi juu yao. Hakika Mwenyezi Mungu Haendi kinyume na ahadi Yake

    [32] Na iwapo wameufanyia shere ulinganizi wako, ewe Mtume, basi kuna ummah kabla yako waliwafanyia shere Mitume wao. Basi usiwe na masikitiko, niliwapa muhula wale waliokufuru kisha nikawapatiliza kwa mateso yangu; na yalikuwa ni mateso makali

    [33] Je, Yule Anayesimamia kila nafsi Akiyadhibiti yale inayoyafanya, ni mwenye haki zaidi ya kuabudiwa au ni hivi viumbe visivyojiweza? Na wao, kwa ujinga wao walimfanyia Mwenyezi Mungu washirika miongoni mwa viumbe Wake wakawa wanawaabudu. Waambie, ewe Mtume, «Tajeni majina yao na sifa zao.» Na hawatapata kwenye sifa zao chochote cha kuwafanya wao wastahiki kuabudiwa. Au nyinyi mnampasha habari Mwenyezi Mungu kuwa Ana washirika katika ardhi Yake ambao Hawajui? Au mnawaita ni washirika kimaneno tu bila ya kuwa na hakika? Bali Shetani aliwapambia makafiri neno lao la ubatilifu na akawazuia njia ya Mwenyezi Mungu. Na yule ambaye Mwenyezi Mungu Hakumwafikia kuongoka basi hakuna yoyote mwenye kumuongoza na kumwafikia kwenye haki na uongofu

    [34] Makafiri hawa wenye kuzuia njia ya Mwenyezi Mungu watakuwa na adhabu ngumu katika maisha ya ulimwenguni kwa kuuawa, kutekwa na kuhiziwa. Na kwa hakika, adhabu yao huko Akhera ni nzito zaidi na ni kali zaidi, na hawatakuwa na kizuizi chenye kuwazuia wasipate adhabu ya Mwenyezi mungu

    [35] Sifa ya Pepo ambayo Mwenyezi Mungu Amewaahidi nayo wale wanaomuogopa na kwamba mito inapita chini ya miti yake na majumba yake ya fahari, Matunda yake hayamaliziki na kivuli chake hakiondoki. Malipo mema hayo ya Pepo ndio mwisho wa waliomuogopa Mwenyezi Mungu wakajiepusha na mambo ya kumuasi na wakatekeleza faradhi Zake. Na mwisho wa makafiri ni Moto

    [36] Na wale ambao tuliwapa Kitabu, miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara, yoyote kati yao mwenye kukuamini, kama 'Abdullāh bin Salām na Najashi, wanaifurahia Qur’ani uliyoteremshiwa kwa kuwa inaenda sambamba na kile walichonacho. Na miongoni mwa wale wanaojiweka pamoja kukupinga, kama Sayyid na 'Aqib: maaskofu wawili wa Najran , na Ka'b bin al-Ashraf, wanaokanusha baadhi ya yale uliyoteremshiwa. Waambie, «Mwenyezi Mungu Ameniamrisha nimuabudu Yeye Peke Yake na nisimshirikishe chochote. Nawaita watu wamuabudu, na Kwake Peke Yake ndio marejeo yangu na marudio

    [37] Na kama tulivyowateremshia Mitume Vitabu kwa lugha zao, tulikuteremshia wewe, ewe Mtume, Qur’ani kwa lugha ya Kiarabu, ili uitumie katika kuhukumu. Na lau ulifuata mapendeleo ya washirikina katika kumuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu, baada ya haki iliyokujia kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hutakuwa na msaidizi yoyote mwenye kukuhami na kuzuia adhabu ya Mwenyezi Mungu isikufikie

    [38] Na kumbuka waliposema, «Una nini, ewe Mtume, unaoa wanawake?» Hakika tulituma kabla yako Mitume kati ya wanadamu na kuwafanya wawe na wake na watoto. Na pia utaje waliposema, «Lau alikuwa ni Mtume angalituletea miujiza tuliyoitaka.» Haiko kwenye uwezo wa Mtume yoyote, kuleta miujiza ambayo watu wake waliitaka isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Kila jambo alilolihukumu Mwenyezi Mungu lina maandishi na wakati, Mwenyezi Mungu Ameliandika hapo Kwake, halitangulii wala halichelewi

    [39] Mwenyezi Mungu Anakifuta Akitakacho miongoni mwa hukumu na mengineyo, na Anakiacha kisalie Akitakacho miongoni mwa hizo kwa hekima fulani Anayoijua. Na Kwake kuna asili ya Kitabu, nacho ni Al-Lawh„ Al-Mah,fūd,: Ubao uliohifadhiwa ambao yamethibitishwa ndani yake kimaandishi hali za viumbe mpaka Siku ya Kiyama

    [40] Na tukikuonesha , ewe Mtume, baadhi ya mateso tuliyowaahidi maadui zako ya kuhizika na kuungulika ulimwenguni, basi hayo ni yale tuliyowaharakishia. Na tukikufisha kabla hujaona hayo, basi wajibu wako haukuwa isipokuwa ni kutekeleza ulinganizi, na hesabu na malipo ni juu yetu

    [41] Kwani hawaoni hawa makafiri kwamba sisi tunaijia ardhi na kuipunguza pambizoni mwake kwa kuwapa Waislamu ushindi wa kuiteka miji ya makafiri na kuishikanisha na miji ya Kiislamu? Na Mwenyezi Mungu Anaamua, hakuna Mwenye kuurudi uamuzi Wake na hukumu Yake. Na Yeye ni Mpesi wa kuhesabu, basi wasifanye haraka ya kutaka kuletewa adhabu, kwani kila lenye kuja liko karibu

    [42] Hakika wale waliokuwa kabla yao waliwapangia njama Mitume wao, kama vile hawa walivyokufanyia. Basi vitimbi vyote vina Mwenyezi Mungu, Anatangua vitimbi vyao na kuwarudishia wenyewe wapite patupu na wajute. Na Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu Kwake, Anakijua kile ambacho kila mtu anakichuma, chema au kibaya, na atalipwa kwa hicho. Na watajuwa makafiri, watakapofika kwa Mola wao, ni nanani atakuwa na mwisho mwema baada ya dunia hii. Huo ni wa wafuasi wa Mitume. Katika haya kuna onyo na tishio kwa makafiri

    [43] Na wenye kumkanusha Nabii wa Mwenyezi Mungu wanasema, «Ewe Muhammad, hukutumilizwa na Mwenyezi Mungu.» Waambie, «Inatosha kuwa Mwenyezi Mungu ni shahidi juu ya ukweli wangu na urongo wenu, na unatosha ushahidi wa wenye ujuzi wa Kitabu miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara kati ya wale waliouamini utume wangu na kwamba yale niliokuja nayo yanatoka kwa Mwenyezi Mungu na akaufuata ukweli na akatoa ushahidi huo waziwazi na asiufiche

    Ibrahimu

    Surah 14

    [1] Alif, Lām, Rā. Hii Qur’ani ni kitabu tulichokuletea wahyi ili uwatoe binadamu kutoka kwenye upotevu na upotovu kuwapeleka kwenye uongofu na mwangaza, kwa idhini ya Mola wao na taufiki Yake kwao, kwenye Uislamu ambao ndio njia ya Mwenyezi Mungu Mwenye kushinda Anayehimidiwa kwa kila hali

    [2] Mwenyezi Mungu Ambaye ni Vyake vilivyoko mbinguni na vya ardhini, kwa kuviumba, kuvimiliki na kuviendesha. Yeye Ndiye Ambaye ni lazima ibada Afanyiwe Yeye Peke Yake. Na wale waliogeuka na wasimuamini Mwenyezi Mungu na wasiwafuate Mitume Wake watapata maangamivu na adhabu kali Siku ya Kiyama

    [3] Na hawa wenye kugeuka wasimuamini Mwenyezi Mungu na wasimfuate Mtume Wake ndio wanaochagua maisha ya dunia yenye kutoeka na wanaacha Akhera yenye kusalia, wanawakataza watu kufuata dini ya Mwenyezi Mungu na wanaitaka iwe ni njia iliyopotoka ili iafikiane na mapendeleo yao. Hao waliosifiwa kwa sifa hizi wamo ndani ya upotevu wa kutoiona haki, wako mbali na njia zote za uongofu

    [4] Na hatukutuma Mitume kabla yako, ewe Nabii, isipokuwa kwa lugha ya watu wake, ili awafafanulie sheria ya Mwenyezi Mungu, ili Mwenyezi Mungu Apate kumpoteza Anayemtaka awe kando na uongofu na Amwongoze Anayemtaka kwenye ukweli. Na yeye Ndiye Mshindi katika ufalme Wake, ni Mwenye hekima Anayeyaweka mambo mahali pake kulingana na hekima

    [5] Na kwa hakika tulimtuma Mūsā kwa Wana wa Isrāīl na tukamsaidia kwa miujiza yenye kuonyesha ukweli wake na tukammpa amri awalinganie wao kwenye Imani, ili awatoe wao kutoka kwenye upotevu awatie kwenye uongofu na awakumbushe neema za Mwenyezi Mungu na mateso Yake katika wakati wake. Katika kukumbusha huku mambo hayo kuna dalili nyingi kwa kila mvumilivu sana juu ya utiifu wa Mwenyezi Mungu, kuyaepuka yaliyoharamishwa na Yeye na kuyakubali maandiko Yake, mwenye kushukuru sana, mwenye kusimama kutekeleza haki za Mwenyezi Mungu na anayemshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema Zake. Aina mbili hizi za watu zimetajwa mahsusi, kwa kuwa wao ndio wanaozingatia hizo dalili na hawaghafiliki nazo

    [6] Na watajie, ewe Mtume, watu wako kisa cha Mūsā pindi alipowaambia watu wake, «Tajeni neema ya Mwenyezi Mungu kwenu alipowaokoa kutokana na Fir'awn na wafuasi wake waliokuwa wakiwaonjesha adhabu kali zaidi, wakiwaua watoto wenu wa kiume, ili asitokee kati yao atakayeuvamia ufalme wa Fir'awn, na walikuwa wkiwaacha wanawake wenu kwa kutumika na kudharauliwa. Na katika misukosuko hiyo na kuokolewa huko ni mtihani mkubwa utokao kwa Mola wenu.»

    [7] Mūsā aliwaambia, «Na kumbukeni pindi Mola wenu alipowajulisha kwa kuwasisitiza kwamba mkimshukuru kwa neema Zake Atawazidishia nyongeza Zake, na mkikanusha neema ya Mwenyezi Mungu, Atawaadhibu adhabu kali.»

    [8] Na akawaambia, «Mkimkanusha Mwenyezi Mungu , nyinyi na watu wa ardhini, hamtamdhuru Mwenyezi Mungu kitu chochote. Kwani Mwenyezi mungu ni Mkwasi kutowahitajia viumbe Vyake, ni mstahiki wa kushukuriwa na kusifiwa, ni mshukuriwa kwa hali zote.»

    [9] Kwani haikuwajia, enyi ummah wa Muhammad, habari za ummah waliowatangulia: watu wa Nūḥ, watu wa Hūd, watu wa Ṣāliḥ na ummah waliokuja baada yao? Hakuna anayeidhibiti idadi yao isipokuwa Mwenyezi Mungu. Mitume wao waliwajia kwa hoja waziwazi, wakaiuma mikono yao kwa hasira na kwa kiburi cha kutoikubali Imani, na wakasema kuwaambia Mitume wao, «Sisi hatuyaamini mliyotuletea, na sisi tuko kwenye shaka yenye kutia wasiwasi juu ya yale unayotuitia kwayo ya kumuamini Mwenyezi Mungu na kumpwekesha.»

    [10] Mitume wao wakasema kuwaambia, «Je, pana shaka yoyote juu ya Mwenyezi Mungu na kuwa Yeye Ndiye Muabudiwa Peke Yake, na hali Yeye ni Muumba wa mbingu na ardhi na Mwenye kuzifanya zipatikane kutoka kwenye hali ya kutokuwako bila ya kuwa na mfano uliotangulia, na hali Yeye Anawaita kwenye Imani Apate kuwasamehe mliyoyatanguliza ya ushirikina na Awaepushie adhabu ya kumaliza kabisa, Awape nafasi ya kusalia ulimwenguni mpaka muda Aliyoupanga ambao ni kikomo cha nyakati za maisha yenu, Asiwaadhibu duniani? Wakawaambia Mitume wao, «Hatuwaoni nyinyi isipokuwa ni binadamu, hali zenu ni kama zetu, hamna ubora wowote juu yetu wa kuwafanya muwe Mitume. Mnataka kutuzuia kuviabudu vitu ambavyo baba zetu walikuwa wakiviabudu miongoni mwa masanamu na mizimu. Basi tuletee hoja iliyo wazi yenye kuonyesha usahihi wa yale mnayoyasema

    [11] Mitume waliposikia yale yaliyosemwa na watu wao waliwaambia, «Ni kweli kwamba sisi hatukuwa isipokuwa ni binadamu kama nyinyi, kama mlivyosema. Lakini Mwenyezi Mungu Anawafanyia wema Anaowataka miongoni mwa waja wake kwa kuwapa neema Zake na kuwateua kwa kuwapa utume Wake. Na hizo dalili waziwazi mlizozitaka, haiwezekani sisi kuwaletea isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na taufiki Yake. Na kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake wanategemea Waumini katika mambo yao yote

    [12] «Na vipi sisi tusimtegemee Mwenyezi mungu , na hali Yeye Ndiye Aliyetuongoza njia ya kuokoka na adhabu Yake kwa kufuata hukumu za dini Yake? Na sisi tutavumilia sana makero yenu kwetu kwa maneno maovu na mengineyo. Na kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake ni lazima Waumini wamtegemee Awapatie nusura ushindi juu ya maadui zao.»

    [13] Nyoyo za makafiri ziliingia dhiki kwa maneno ya Mitume na wakasema kuwaambia, «Hakika tutawatoa kutoka miji yetu mpaka mrudi kwenye dini yetu.» Mwenyezi Mungu Akatuma wahyi kwa Mitume kwamba Atawaangamiza wenye kukataa wenye kumkanusha Yeye na Mitume Wake

    [14] «Na tutaufanya mwisho mwema uwe ni wa Mitume na wafuasi wao kwa kuwakalisha kwenye ardhi ya makafiri baada ya kuwaangamiza. Kuwaangamiza huko na kuwakalisha Waumini ardhi yao ni jambo la uhakika kwa anayeogopa kisimamo chake mbele yangu Siku ya Kiyama na akaoogopa unyo langu na adhabu yangu.»

    [15] Mitume wakaelekea kwa Mola wao wakamuomba Awape ushindi juu ya maadui wao na Ahukumu baina yao, na Yeye Akawakubalia na Akamwangamiza kila mwenye kujiona asiyekubali haki, Asiyeiandama na Asiyetaka kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtakasia ibada

    [16] Mbele yake, huyu kafiri, patakuwa na Jahanamu, ataikuta na adhabu yake na atanyweshwa humo usaha na damu zinazotoka kwenye miili ya watu wa Motoni

    [17] Mwenye kiburi atajaribu kumeza usaha na damu na vinginevyo vinavyotiririka mara kwa mara kutoka kwa watu wa Motoni, na hataweza kuzimeza kwa uchafu wake, umoto wake na uchungu wake. Na adhabu kali ya kila aina itamjia kwenye kila kiungo katika mwili wake. Hatakuwa ni mwenye kufa akapumzika. Na baada ya adhabu hii atapatiwa adhabu nyingine yenye kuumiza

    [18] Hali ya matendo mazuri ya makafiri ulimwenguni, kama vile kufanya wema na kuunga zao, ni kama hali ya jivu lililopigwa na upepo wa nguvu katika siku yenye upepo mkali usiache hata alama yake. Hivyo ndivyo yatakavyokuwa matendo yao, hawatapata kwa matendo hayo kitu cha kuwanufaisha mbele ya Mwenyezi Mungu; kwani ukafiri umeyaondoa kama vile upepo ulivyoondoa jivu. Kushughulika huko na kufanya matendo mema huko bila ya msingi, ndio kupotea kuliko mbali na njia ya sawa

    [19] Je, hujui, ewe mwenye kwambiwa,- na makusudiwa ni watu kwa jumla- kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyepatisha mbingu na ardhi kwa namna thabiti yenye kuonyesha hekima Yake , na kwamba Yeye Hakuziumba kwa mchezo, bali ni kwa ajili ya kutolea ushahidi juu ya upweke Wake na ukamilifu wa uweza Wake, ili wamuabudu Peke Yake, na wasimshirikishe na kitu chochote? Basi Akitaka Atawaondoa na Awalete watu wasiokuwa nyinyi wanaomtii Mwenyezi Mungu

    [20] Na kuwaangamiza nyinyi na kuwaleta watu wengine wasiokuwa nyinyi si jambo lisilowezekana kwa Mwenyezi Mungu, bali ni jambo lilio pesi

    [21] Na watatoka viumbe kwenye makaburi yao na watajitokeza waziwazi Siku ya Kiyama kwa Mwenyezi Mungu Aliye Mmoja Mwenye kutendesha nguvu, ili Awahukumu baina yao. Hapo wafuasi watasema kuwaambia viongozi wao , «Sisi tulikuwa kwenu nyinyi ulimwenguni ni wafuasi, tukifuata amri zenu. Je, nyinyi ni wenye kututetea na kuizuia chochote miongoni mwa adhabu ya Mwenyezi Mungu kama mlivyokuwa mkituahidi? Viongozi watasema, «Lau Mwenyezi Mungu Alituongoza kwenye Imani tungaliwalekeza kwenye hiyo, lakini Yeye Hakutuafikia ndipo tukapotea na tukawapoteza. Ni sawa kwetu sisi na kwenu kuwa na babaiko au kuvumilia, kwani hatuna pa kukimbilia kuepukana na adhabu wala pa kupata uokozai

    [22] Shetani atasema baada ya Mwenyezi Mungu kuamua jambo Lake na kuwahesabu viumbe Vyake, na kuingia watu wa Peponi Peponi na watu wa Motoni Motoni, «Mwenyezi Mungu Aliwaahidi nyinyi ahadi ya kweli ya kufufuliwa na kulipwa, na mimi niliwaahidi ahadi ya urongo kwamba hakuna kufufuliwa wala kulipwa, nikakawaendea kinyume na ahadi yangu. Na mimi si kuwa na nguvu zozote za kuwalazimisha kunifuata, wala si kuwa na hoja. Isipokuwa mimi niliwaita kwenye ukafiri na upotevu mkanifuata. Basi msinilaumu, jilaumuni nyinyi wenyewe. Dhambi ni dhambi zenu wenyewe. Mimi si mwenye kuwaokoa na nyinyi si wenye kunokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Mimi nimejiepusha na jambo la nyinyi kunifanya mimi ni mshirika pamoja na Mwenyezi Mungu katika kutiiwa ulimwenguni. Hakika madhalimu, katika kuupa mgongo kwao ukweli na kuufuata urongo, watakua na adhabu kali iumizayo

    [23] Na wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafanya matendo mema, watatiwa ndani ya mabustani ya Pepo ambayo chini ya miti yake na majumba yake ya fahari inapita mito. Hawatatoka humo milele, kwa idhini ya Mola wao na uweza Wake na nguvu Zake. Watasalimiwa humo kwa salamu itokayo kwa Mwenyezi Mungu, Malaika Zake na Waumini

    [24] Kwani huoni, ewe Mtume, namna gani Mwenyezi Mungu alivolipiga mfano neno la tawhīd «Lā ilahā illā Allāh» wa mti mkubwa, nao ni mtende, ambao shina lake limejikita imara ndani ya ardhi na kilele chake kiko juu kimeelekea mbiguni

    [25] Unatoa matunda yake kila kipindi kwa idhini ya Mola wake. Namna hiyo ndivyo ulivyo mti wa Imani: msingi wake umejikita imara ndani ya moyo wa Muumini kiujuzi na kiitikadi, na tagaa zake za matendo mema na tabia za kuridhisha zinapaishwa juu kwa Mwenyezi Mungu, na malipo yake mema yanapatikana kila kipindi. Na Mwenyezi Mungu Anawapigia watu mfano ili wakumbuke na wawaidhike wapate kuzingatia

    [26] Na mfano wa neno ovu, nalo ni neno la ukafiri, ni kama mti muovu wa chakula na ladha, nao ni mti wa subili, uliong’olewa juu ya ardhi, kwa kuwa mizizi yake iko karibu na uso wa ardhi, hauna mizizi iliyojikita ndani wala hauna tagaa zenye kwenda juu. Hivo ndivyo kafiri alivyo, hana uthabiti wala hana wema na wala hakuna tendo lema lake lolote litakalopaishwa kwa Mwenyezi Mungu

    [27] Mwenyezi Mungu Anawathibitisha wale waloamini kwenye neno la ukweli lenye uimara nalo ni kukubali kwamba hakuna mola anayepasa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhaamad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwamba Atawathibitisha kwenye dini ya kweli aliyokuja nayo katika huu ulimwengu, Atawapa mwisho mwema wakati wa kufa, na Atawaongoza watoe jawabu ya sawa watakapoulizwa na Malaika wawili kaburini. Na Mwenyezi Mungu Atawapoteza madhalimu wasiuone usawa ulimenguni na Akhera. Na Mwenyezi Mungu Anafanya Analolitaka kwa kuwaafikia wenye kuamini na kutowaongoza wenye kukufuru na kuasi

    [28] Kwani hutazami, ewe mwenye kuambiwa (makusudio ni jumla ya wenye kuambiwa), hali ya wakanushaji miongoni mwa makafiri wa Kikureshi waliochagua kumkanusha Mwenyewzi Mungu badala ya kumshukuru kwa neema ya amani na kutumilizwa Nabii Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, kwao wao? Na kwa hakika waliwashukisha wafuasi wao nyumba ya maangamivu, waliposababisha kuwatoa wao kwenda Badr wakauawa, na mwisho wao ukawa ni nyumba maangamivu

    [29] nayo ni Moto wa Jahanamu ambao watauingia na wataungulika na joto lake. Na mahali pabaya pa kukaa na kutulia ni hapo penye makao yao

    [30] Na hawa makafiri walimfanya Mwenyezi Mungu ana washirika ambao waliwaabudu pamoja na Yeye, ili wawaepushe watu na Dini Yake. Waambie, «Stareheni katika maisha ya ulimwengu, kwani hayo ni upesi kuondoka, na marejeo yenu na kurudi kwenu ni kwenye adhabu ya Jahanamu.»

    [31] Waambie, ewe Mtume, waja wangu walioamini watekeleze Swala kwa namna yake inayotakikana na watoe sehemu ya mali tuliyowapa katika njia za heri, za lazima na za zinazopendekezwa, watoe kwa siri au waziwazi, kabla ya kuja Siku ya Kiyama ambayo haitafaa kitu fidia wala urafiki

    [32] Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi, Akazifanya zipatikane baada ya kutokuwako, Akateremsha mvua kutoka mawinguni Akaihuisha Ardhi kwa hiyo baada ya kuwa imekufa, Akawatolea nyinyi kutoka ndani ya ardhi vyakula vyenu, Akawadhalilishia majahazi yapate kuenda baharini kwa amri Yake kwa ajili ya manufaa yenu, Akawadhalilishia mito ili munywe nyinyi na wanywe wanyama wenu na kwa ajili ya mimea yenu na manufaa yenu mengine

    [33] Na Akawadhalilishia nyinyi jua na mwezi, haviachi kutembea kwake, ili maslahi yenu yatimie kwa viwili hivyo. Na Akwadhalilishia nyinyi usiku, ili mtulie humo na mpumzike, na mchana ili mtafute fadhila Zake na mpange maisha yenu

    [34] Na Akawapa nyinyi kila mlichomuomba. Na mkihesabu ili kujua idadi ya neema za Mwenyezi Mungu juu yenu, hamtaweza kuzihesabu na kudhibiti idadi yake wala kusimama itakikanavyo kushukuru kwa hizo kwa wingi wake na aina zake. Hakika Binadamu ni mwingi wa kujidhulumu nafsi yake, ni mwingi wa kukanusha neema za Mola wake

    [35] Na kumbuka, ewe Mtume, pindi Ibrāhīm aliposema akimuomba Mola Wake, baada ya kumfanyia makao mwanawe wa kiume, Isma'il, pamojaa na mamake, Hajar, kwenye bonde la Makkah, «Ewe Mola ijaalie Makkah ni mji wa amani, awe kila aliye humo yuko kwenye amani, na uniepushe mimi na wanangu na kuabudu masanamu

    [36] «Ewe Mola wangu! Masanamu wamesababisha kuwaepusha watu wengi na njia ya ukweli. Basi mwenye kunifuata mimi katika kumpwekesha Mwenyezi Mungu, yeye atakuwa kwenye Dini yangu na mwendo wangu, na mwenye kwenda kinyume na mimi, katika mambo ambayo si ya ushirikina, basi wewe ni Mwingi wa kusamehe dhambi za wenye kufanya madhambi, kwa fadhila zako, ni Mwingi wa huruma kwao, unamsamehe unayemtaka miongoni mwao

    [37] «Ewe Mola wetu! Mimi nimewafanya watoto wangu wakae kwenye bonde lisilo na mimea wala maji, penye ujirani na mji wako mtakatifu. Mola wetu! Mimi nimefanya hilo kwa amri Yako, ili wasimamishe Swala kwa namna yake itakikanayo, basi ifanye myoyo ya baadhi ya viumbe vyako ilemee kwao na ipendelee, na uwape riziki ya kila aina ya matunda wakiwa mahali hapa, ili wakushukuru kwa neema zako.» Mwenyezi Mungu Akakubali maombe yake

    [38] «Ewe Mola wetu! Hakika wewe unajua kila tunachokificha na tunachokionyesha. Na hakuna chochote chenye kupotea na kuwa nje ya ujuzi wa Mwenyezi Mungu miongoni mwa vilivyoko ardhini na mbinguini.»

    [39] Ibrāhīm anamsifu Mola wake na anasema, «Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu Aliyeniruzuku, pamoja na uzee wangu, wanangu wawili, Ismā'īl na Isḥāq, baada ya maombi yangu Anitunuku miongoni mwa wema, kwani Mola wangu ni mwenye kusikia maombi ya mwenye kumuomba; na mimemuomba na Hakuyapitisha patupu matarajio yangu

    [40] «Ewe Mola wangi! Nijaalie ni mwenye kuendelea kutekeleza Swala kwa njia ya ukamilifu zaidi na ujaalie katika kizazi changu wenye kuendelea nayo. Ewe Mola wetu! Na uyakubali maombi yangu na uikubali ibada yangu

    [41] «Ewe Mola wetu! Nisamehe iwapo yametukia kutoka kwangu mambo ambayo binadamu hawasalimiki nayo, na uwasamehe wazazi wangu wawili (Hapa ni kambla haijamfunukia kwamba baba yake ni adui wa Mwenyezi Mungu) na uwasamehe Waumini wote Siku ambayo watu watasimama kuhesabiwa na kulipwa..»

    [42] Na usidhani, ewe Mtume, kwamba Mwenezi Mungu ni mwenye kughafilika na yale wanayoyafanya madhalimu, ya kukukanusha wewe na Mitume wengine na kuwakera Waumini na maasia mengineyo. Kwa kweli, Anachelewsha kuwatesa mpaka Siku ngumu ambayo macho yao yatakodoka na hayatafumbika kwa kitisho cha yale yanayoyaona. Katika hii pana kumliwaza Mtume Muhammad, rehema na amani zimshukiye

    [43] Siku watakaosimama madhalimu kutoka makaburini mwao wakikimbilia kumwitika mlinganizi wakiinua vichwa vyao, hawaoni chote kwa kituko cha kisimamo, na hali nyoyo zao ni tupu hazina kitu ndani yake, kwa kicho kingi na kuogopa ktuko cha wanayoyaona

    [44] Na waonye, ewe Mtume, wale watu ambao wewe umetumilizwa kwao, adhabu ya Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama. Na hapo wale waliojidhulumu kwa kukanusha watasema, «Ewe Mola,wetu! Tupe muhula wa muda mchache, tutakuamini na tutawasadiki Mitume wako. Na wataambiwa kwa kujereshwa, «Je, hamkuapa katika uhai wenu kwamba hamtaondoka ulimwenguni kwenda Akhera, na msiamini kufufuliwa huku

    [45] «Na mkakaa kwenye makao ya makafiri waliopita waliojidhulumu nafsi zao, kama vile watu wa Hūd na Ṣāliḥ, na mkajua, kwa mlivyoona na mlivyombiwa, maangamivu tuliyowateremshia na tukawapigia mifano katika Qur’ani msizingatie?»

    [46] Na kwa kweli, washirikina walimpangia njama Mtume, rehema na amani zimshukie, za kumuua. Na vitimbi vyao vilikuwako kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuwa Yeye Amewazunguka. Na vitimbi vyao vikawarudia wenyewe. Na havikuwa vitimbi vyao ni vyenye kuondoa majabali wala vitu vinginevyo kwa udhaifu wake na unyonge wake. Na wao hawakumdhuru Mwenyezi Mungu, lakini walijidhuru wenyewe

    [47] Basi usidhanie, ewe Mtume, kwamba Mwenyezi Mungu Atakwenda kinyume na vile Alivyowaahidi Mitume Wake, kuwa Atawapa ushindi na Atawaangamiza wenye kuwakanusha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mshindi, hakuna kitu kinachomshinda kukifanya, ni Mwenye kuwalipiza maadui wake kwa kuwapa mateso makali kabisa. Maneno haya ingawa anaambiwa Nabii, rehema na amani zimshukie, yanaelekezwa kwa ummah wote

    [48] Na malipizo ya Mwenyezi Mungu ya kuwatesa maadui Wake Siku ya Kiyama yatakuwa kwenye siku ambayo itabadilishwa hii ardhi kwa ardhi nyingine nyeupe iliyotakata kama fedha, na vilevile zitatabadilishwa mbingu kwa nyingine, na watatoka viumbe makaburini mwao wakiwa hai wakiwa wamejitokeza kukutana na Mwenyezi Mungu Aliye Mmoja, Mwenye kutendesha nguvu, Aliyepwekeka kwa utukufu Wake, majina Yake, sifa Zake na matendo Yake na kulazimisha Kwake kila kitu

    [49] Na utawaona,ewe Nabii, waasi Siku ya Kiyama wamefungwa pingu, mikono yao miguu yao yamekutanishwa pamoja kwa minyonyoro, na hali wakiwa watwevu

    [50] Nguo zao ni za rojo la mafuta linalochomeka sana, na hapo moto utaziramba nyuso zao na kuzichoma

    [51] Mwenyezi Mungu Atawafanyia hayo yakiwa ni malipo yao kwa madhambi waliyoyachuma duniani. Na Mwenyezi Mungu Atamlipa kila binadamu kwa alilolitenda, baya au zuri. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mpesi wa kuhesabu

    [52] Hii Qur’ani tuliyokuteremshia, ewe Mtume, ni maelezo na ni tangazo kwa watu, kwa kuwashauri na kuwatisha, na ili wawe na yakini kwamba Mwenyezi Mungu ni Mola Mmoja, wapate kumuabudu, Peke Yake, Asiye na Mshirika, na wapate kuwaidhika kwayo wenye akili timamu

    Al Hijr

    Surah 15

    [1] (Alif, Lām, Rā) Yametangulia maelezo kuhusu herufi zilizokatwa na kutengwa. Hizo ni aya tukufu miongoni mwa aya za Kitabu kitukufu kilichoteremshwa kwa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye. Nazo ni aya za Qur’ani zenye kufafanua kweli kwa matamko mazuri zaidi na yaliyo wazi zaidi na yenye kuonyesha zaidi makusudio. Kitabu na Qur’ani ni kitu kimoja ; na hapa Mwenyezi Mungu Ameyakusanya pamoja majina mawili

    [2] Makafiri watatamani, watakapowaona Waumini walioasi wakitoka Motoni, lau wao walikuwa ni wenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu wakawa ni wenye kutoka kama wao

    [3] Waache, ewe Mtume, hao makafiri wapate kula na wastarehe na ulimwengu wao na iwashughulishe tamaa ya huo ulimwengu wasimtii Mwenyezi Mungu, watakuja kujua mwisho wa mambo yao ambayo ni hasara ya duniani na Akhera

    [4] Na wakiomba kuteremshiwa adhabu, kwa kukukanusha, ewe Mtume, basi sisi hatuuangamizi mji, isipokuwa uwapo wakati wa kuangamizwa umeshapangwa; hatutawaangamiza mpaka waufikie mfano wa wale waliowatangulia

    [5] Hakuna watu wowote watakaoupita muda wao uliowekwa wakauzidisha wala kuutangulia wakaupunguza

    [6] Na wenye kumkanusha Muhammad, rehema na amani zimshukie, walisema kwa njia ya shere, «Ewe yule ulioteremshiwa Qur’ani, ‘wewe umerukwa na akili.’

    [7] Si utuletee Malaika iwapo wewe ni mkweli wapate kutoa ushahidi kwamba Mwenyezi Mungu Amekutumiliza.»

    [8] Na Mwenyezi Mungu Akawajibu: Sisi hatuwateremshi Malaika isipokuwa kwa adhabu ambayo haina kucheleweshwa kwa asiyeamini na hawakuwa ni wenye kuachwa wakati Malaika watakapoteremka

    [9] Hakika sisi tumeiteremsha Qur’ani kwa Nabii Muhammad, rehema na amani zimshukiye, na hakika sisi tunachukua ahadi kuitunza isiongezwe, isipunguzwe wala sehemu yoyote katika hiyo isipotee

    [10] Na kwa hakika tulitumiliza kabla yako, ewe Mtume, Wajumbe kati ya makundi ya wa mwanzo

    [11] Hakuna Mjumbe yoyote aliwajia wao isipokuwa walikuwa wakimfanyia shere.Katika haya pana kumliwaza Mtume, rehema na amani zimshukie. Na kama walivyokufanyia hawa, hivyo ndivyo walivyofanyiwa Mitume kabla yako

    [12] Kama tulivyoutia ukafiri kwenye nyoyo za ummah waliotangulia kwa sababu ya kuwafanyia shere Mitume na kuwakanusha, hivyo ndivyo tunavyofanya kwenye nyoyo za washirikina miongoni mwa watu wako waliofanya uhalifu wa kumkanusha Mwenyezi Mungu na kuwakanusha Mitume Wake

    [13] hawauamini Ukumbusho ulioteremshwa kwako. Na umeshapita mwendo wa wamwanzo wa kuwaangamiza wakanushaji. Na hawa ni kama wao, wataangamizwa wenye kuendelea na ukafiri na ukanushaji miongoni mwao

    [14] Na lau tuliwafungulia makafiri wa Makkah mlango wa mbingu, wakaendelea kupanda kuingia ndani wapate kuyashuhudia yaliyomo mbinguni ya ajabau za ufalme wa Mwenyezi Mungu, hawangaliamini

    [15] na wangalisema, «Macho yetu yamerogwa mpaka tumekuwa tunaona tusiyoyaona. Sisi tumerogwa tu na Muhammad kwenye akili zetu.»

    [16] Na miongoni mwa dalili za uweza wetu ni kwamba sisi tumeweka kwenye uwingu wa karibu vituo ya sayari kushukia, ambayo kwayo zinajulikana njia, nyakati, urutuba na ukavu, na tumeupamba uwingu huu kwa nyota ili wenye kuziangalia wataamali na wazingatie

    [17] Na tumeuhifadhi uwingu huo na kila Shetani Aliyetolewa na aliyefukuzwa kutoka kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu ili asiufikie

    [18] Isipokuwa aliyetega sikio kusikiliza maneno ya watu wa juu baadhi ya nyakati, akafikiwa na sayari inayotoa mwangaza na kumchoma.Na huenda Shetani akamddokeza rafiki yake baadhi ya habari alizozisikia kwa kutegea kabla hajateketezwa na kimondo

    [19] Na ardhi tumeinyosha ikawa kunjufu, tukaweka juu yake majabali yenye kuiimarisha , tuakaotesha kila aina ya mimea ambayo waja wanaihitajia kwa kipimo kinachojulikana

    [20] Na tukawawekea nyinyi humo vitu mnavyovihitajia katika maisha yenu miongoni mwa makulima, wanyama, aina mbalimbali ya shughuli za kujipatia maisha na vinginevyo. Na tukawaumbia nyinyi watoto, watumishi na wanyama manaonufaika nao. Na riziki zao haziko juu yenu, bali ziko juu ya Mwenyezi Mungu Bwana wa viumbe vyote kwa wema utokao Kwake na ukarimu

    [21] Na hakuna chochote cha manufaa ya waja isipokuwa ziko kwetu hazina zake za kila aina, na hatukiteremshi isipokuwa kwa kadiri iliyowekewa mpaka, kama vile tutakavyo. Hazina zote ziko mkononi mwa Mwenyezi Mungu, Anampa Anayemtaka na Anamzuilia Anayemtaka, kulingana na rehema Yake kunjufu na hekima Yake kubwa

    [22] Na tunatuma upepo na tunaufanya uwe mtiifu kwetu uyajaze mawingu yabubujishe maji na yanyeshe na yanywesheze miti, hapo majani yake yafunguke na mafumba yake yajitokeze. Na mvua inabeba heri na nafuu na tunayateremsha maji yake tuliyowatayarishia nyinyi kwa ajili ya kunywa kwenu, ardhi yenu na wanayama wenu. Na nyinyi si waweza wa kuyahifadhi na kuyaweka akiba, lakini sisi tunawahifadhia kwa kuwahurumia na kuwafanyia hisani

    [23] Ndio sisi tunaompa uhai aliyekufa kwa kumpatisha kutoka kwenye hali ya kutokuwako, na tunamfisha aliyekuwa hai baada ya ajali yake kukoma. Na sisi ndio wenye kuirithi ardhi na walioko juu yake

    [24] Kwa hakika tunawajua walioangamia miongoni mwenu tangu Ādam, walio hai na watakaokuja mpaka Siku ya Kiyama

    [25] Na hakika Mola wako Ndiye Atakayewakusanya wao wahesabiwe na walipwe. Hakika Yeye ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji Wake mambo, ni Mwingi wa ujuzi, hakuna kinachofichika Kwake

    [26] Kwa hakika tulimuumba Ādam kwa udongo mkavu, ukigongwa unasikiwa sauti. Na udongo huu mkavu ni miongoni mwa udongo mweusi uliogeuka rangi yake na harufu yake kwa kipindi kirefu cha kukaa kwake

    [27] Na tulimuumba baba wa majini, naye ni Iblisi, kabla ya kuumbwa Ādam, kwa moto mkali sana, usio na moshi

    [28] Kumbuka, ewe Mtume, pindi Mola wako Aliposema kuwaambia Malaika, «Mimi nitamuumba mtu kutokana na udongo mkavu. Na udongo huu mkavu unatokana na udongo mweusi uliogeuka rangi

    [29] «Basi nitakapomtengeneza na kulikamilisha umbo lake na nikapuliza roho ndani yake, mwangukieni hali ya kusujudu,» sijida ya maamkizi na heshima na si sijida ya ibada

    [30] Na Malaika wote walisujudu kwa umoja wao, kama Alivyowaamrisha Mola Wao.. Hakuna yoyote kati yao aliyekataa

    [31] Lakini Iblisi alikataa kumsujudia Ādam pamoja na Malaika waliosujudu

    [32] Mwenyezi Mungu Akasema kumwambia Iblisi, «Una nini wewe kutosujudu pamoja na Malaika?»

    [33] Iblisi akasema akionyesha kiburi chake na uhasidi wake, «Hainasibiani na mimi nimsujudie mtu uliyempatisha kutokana na udongo mkavu, uliokuwa mweusi na uliogeuka.»

    [34] Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Akamwambia, «Basi toka Peponi, wewe ushafukuzwa na umeepushwa na kila jema

    [35] umeshukiwa na laana na umewekwa mbali na rehema yangu mpaka Siku ya kufufuliwa watu ili wahesabiwe na walipwe..»

    [36] Iblisi akasema, «Ewe Mola wangu! Nipatie muda mpaka siku ya wewe kuwafufua waja wako , nayo ni Siku ya Kiyama.»

    [37] Mwenyezi Mungu Akamwambia, «Wewe ni miongoni mwa wale niliowapa muda na kuchelewesha kuwaangamiza mpaka siku ambayo viumbe wote watakufa baada ya Mpulizo wa kwanza

    [38] na siyo mpaka siku ya Ufufuzi. Na alikubaliwa hilo kwa njia ya kulegezewa na kuachiliwa, na ni mtihani kwa binadamu na majini

    [39] Akasema Iblisi, «Mola wangu, kwa sababu ya vile ulivyonipoteza na kunipotosha nitawapambia vizazi vya Ādam kukuasi katika ardhi na nitawapoteza wote wasiione njia ya uongofu

    [40] isipokuwa waja wako ambao umewaongoa wakakutakasia ibada peke yako pasi na viumbe wako wengine.»

    [41] Akasema Mwenyezi Mungu , «Hii ni njia nyofu iliyolingana inayofikisha kwangu na kwenye Nyumba ya ukarimu wangu

    [42] Kwa kweli, wale waja wangu ambao wamenitakasia mimi sitakupatia uwezo juu ya nyoyo zao ili uwapoteze kwa uwezo huo na njia iliyonyoka. Lakini uwezo wako utakuwa ni juu ya yule aliyekuandama miongoni mwa wapotofu washirikina ambao wameukubali usimamizi wako na kukutii badala ya kunitii mimi.»

    [43] Hakika Moto mkali ndio agizo la Iblisi na wafuasi wake wote

    [44] Una milango saba , kila mlango uko chini ya mwengine. Kila mlango utakuwa na fungu na sehemu la wafuasi wa Iblisi kulingana na matendo yao

    [45] Hakika wale waliomcha Mwenyezi Mungu, kwa kuyafuata Aliyoyaamrisha na kujiepusha na aliyoyakataza.watakuwa kwenye mabustani ya Pepo na mito ipitayo

    [46] Wataambiwa, «Ingieni Mabustani haya mkiwa watulivu mumesalimika na kila ovu mumeaminika na kila adhabu

    [47] Na tutawaondolea yaliyomo ndani ya nyoyo zao ya chuki na uadui, wataishi Peponi wakiwa ndugu wapendanao, watakaa kwenye vitanda vikubwa na nyuso zao zitaelekeana katika hali ya kuungana na kupendana

    [48] Haitawapata humo tabu wala uchovu. Na wao ni wenye kusalia humo milele

    [49] Wapashe habari, ewe Mtume, waja wangu kwamba mimi ni mwenye kuwasamehe Waumini wenye kutubia, ni mwenye huruma kwao

    [50] na kwamba adhabu yangu ndiyo adhabu iumizayo yenye kutia uchungu kwa wasiotubia

    [51] Na wapashe habari, ewe Mtume, kuhusu wageni wa Ibrāhīm miongoni mwa Malaika ambao walimpa habari njema za kupata mwana na za kuangamia kwa jamaa za Lūṭ

    [52] Pindi walipoingia kwake na wakamwamkia kwa kusema, «Amani.» Hapo naye akawarudishia maamkizi ya amani. Kisha akwaletea chakula na wao wasikile, na hapo akasema, «Sisi ni wenye kicho na nyinyi.»

    [53] Malaika wakamwambia, «Usiwe na kicho. Sisi tumekuja kukupa habari njema kwamba utapata mwana atakayekuwa na ujuzi mwingi wa Dini, naye ni Is’ḥāq.»

    [54] Ibrāhīm akasema, huku yuwaona ajabu, «Mnanipa habari njema za kupata mwana na mimi nishakuwa mtu mzima, na mke wangu pia, ni kwa njia gani mnanipa habari njema hizo za kushangaza?»

    [55] Wakasema, «Tunakupa habari njema kwa kweli ambayo Mwenyezi Mungu Ametujulisha nayo. Basi usiwe miongoni mwa waliokata tamaa ya wewe kupata mwana.»

    [56] Ibrāhīm akasema, «Hakika hawakati tamaa na rehema za Mola wao isipokuwa walio na makosa waliojitenga na njia ya haki.»

    [57] Na akasema, «Ni jambo gani kubwa mlilolijia, enyi mliotumwa, kutoka kwa Mwenyezi Mungu?»

    [58] Wakasema, «Hakika Mwenyezi Mungu Ametutuma kuwaangamiza watu wa Lūṭ walio washirikina wapotofu

    [59] isipokuwa Lūṭ na watu wake waliomuamini, hao hatutawaangamiza na tutawaokoa wote

    [60] Ama yule mke wake aliye kafiri, tumepitisha kwa amri ya Mwenyezi Mungu kumwangamiza pamoja na watakaosalia kwenye adhabu.»

    [61] Basi walipofika kwa Lūṭ Malaika waliotumwa

    [62] Aliwaambia, «Kwa kweli, nyinyi ni watu msiojulikana na mimi.»

    [63] Wakasema, «Usiogope. Kwani hakika yetu sisi tumekujilia na adhabu ambayo jamaa zako walikuwa na shaka nayo na hawakuwa wakiikubali kuwa ni kweli

    [64] Na tumekujia na haki kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na kwa hakika sisi ni wasema kweli

    [65] Kwa hivyo, toka miongoni mwao , wakiwa pamoja na wewe watu wako waumini, baada ya kupita sehemu ya usiku. Na wewe nenda nyuma yao isije mmoja wao akasalia nyuma ikampata adhabu. Na jichungeni asije mmoja wenu akageuka na akatazama nyuma yake asije akaona adhabu na pia naye ikampata. Na kimbilieni kule ambako Amewaamrisha Mwenyezi Mungu, ili mpate kuwa mahali salama penye amani

    [66] Na tukampelekea wahyi Lūṭ kwamba watu wako(waliokukanusha) wataangamizwa wote, hakuna atakayesalia, pindi kutakapoanza kupambazuka

    [67] Na wakaja wakazi wa mji wa Lūṭ mpaka kwa Lūṭ pindi walipojua kwamba kwake kuna wageni, huku wana furaha na nderemo kwa wageni wake, ili wawachukue wafanye nao machafu

    [68] Lūṭ akawaambia, «Hawa ni wageni wangu, na wako kwenye himaya yangu, basi msiniaziri

    [69] na yaogopeni mateso ya Mwenyezi Mungu, wala msiwasumbue mkaniingiza kwenye unyonge na madharau kwa kuwaudhi wageni wangu.»

    [70] Watu wake wakasema, «Kwani sisi si tulikukataza kumkaribisha mgeni yoyote miongoni mwa walimwengu - na walikuwa wakiwakatia njia wasafiri - kwa kuwa sisi tunataka kufanya machafu na wao?»

    [71] Lūṭ akasema kuwaambia, «Hawa wanawake wenu ni mabinti zangu, waoeni iwapo mnataka kumaliza hamu zenu, wala msiyafanye mliyokatazwa na Mwenyezi Mungu ya kuwajia wanaume.» Amewaita hao wanawake kuwa ni mabinti zake, kwa kuwa Nabii wa ummah ana cheo cha baba kwao

    [72] Muumba Anaapa kwa Anayemtaka na kwa Anachokitaka. Ama muumbwa haifai kwake kuapa isipokuwa kwa jina la Mwenyezi mungu. Na Ameapa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kwa uhai wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, kwa kumtukuza kwa watu, kwamba watu wa Lūṭ wako kwenye sahau kali, wana shaka na wako kwenye ushindani

    [73] Walikuwa hivyo mpaka kilipowashukia kimondo cha adhabu katika kipindi cha kutoka jua

    [74] Hapo tulivipindua vijiji vyao tukavifanya juu yake kuwa chini yake, na tukawanyeshea mawe ya udongo uliokauka ulio mgumu

    [75] Kwa hakika, katika yale yaliyopwapata pana mawaidha kwa wenye kuangalia na kuzingatia

    [76] Na kwa hakika, vijiji vyao viko kwenye njia ya kudumu ambayo wasafiri wanaopitia huko wanaviona

    [77] Kwa hakika, katika kule kuwaangamiza kwetu pana ushahidi waziwazi kwa wenye kuamini na wenye kutenda matendo yanayoambatana na sheria za Mwenyezi Mungu

    [78] Na kwa hakika, wakazi wa mji uliozingirwa na miti, nao ni watu wa Shu'ayb, walikuwa ni wenye kuzidhulumu nafsi zao kwa kumkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume wao mtukufu

    [79] Hivyo basi tuliwaadhibu kwa mtetemeko na adhabu ya siku ya uvuli. Na kwa hakika, makazi ya watu wa Lūṭ na watu wa Shu'ayb yako katika njia iliyo wazi, watu wanayapitia katika safari zao na wanapata mazingatio

    [80] Na kwa hakika, walimkanusha Mtume Ṣāliḥ, amani imshukiye, watu wa bonde la Hijr, nao ni kina Thamūd, wakawa kwahilo ni wenye kuwakanusha Mitume wote. Kwani mwenye kumkanusha Mtume mmoja huwa amewakanusha Mitume wote, kwani wao wako kwenye Dini moja

    [81] Na tuliwapa watu wa Ṣāliḥ aya zetu zinazojulisha usahihi wa mambo ya haki ambayo amekuja nayo kwao Mtume Ṣāliḥ, na miongoni mwayo ni ngamia, waszingatie kwa aya hizo na wakawa ni wenye kujiweka mbali nazo na kuzipa mgongo

    [82] Na walikuwa wakiyachonga majabali na wakifanya humo majumba, na huku wao wanajiaminisha kwamba hayatawaangukia na hayataharibika

    [83] Kikawachukua wao kimondo cha adhabu kipindi cha kucha mapema

    [84] Na hazikuwatetea wao mali zao wala zile ngome kwenye mlilima ya mawe wala zile nguvu na heshima walizopewa

    [85] Na hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyoko baina yake isipokuwa kwa haki, zikiwa ni zenye kujulisha ukamilifu wa muumba wake na uweza Wake, na kwamba Yeye Ndiye Ambaye ibada yoyote haifai kufanyiwa isipokuwa Yeye, Peke Yake, Asiyekuwa na mshirika. Na ule wakati ambao Kiyama kitasimama hauna budi ni wenye kuja, ili kila mtu apate kulipwa kwa yale aliyoyatenda. Basi wasamehe, ewe Mtume, hao washirikina, usiwachukulie na uyaachilie mbali wanayoyatenda

    [86] Hakika Mola wako Ndiye Muumba wa kila kitu, Ndiye Anayekijua, kwa hivyo hakuna kitu chochote kinachomshinda wala kufichika Kwake katika ardhi wala mbinguni

    [87] Na kwa kweli tumekupa, ewe Mtume, ufunguo wa Qur,ani, nao ni hizo aya saba (za sura ya Fatiha) zinazokaririwa katika kila Swala, na tumekupa Qur,ani tukufu

    [88] Usiziangalie kwa macho yako mawili zile starehe za duniani ambazo tuliwastarehesha nazo makafiri aina mbalimbali, na usisikitike juu ya ukafiri wao, na uwanyenyekee wenye kumuamini MwenyeziMungu na Mtume wake

    [89] Na sema, «Mimi ndiye muonyaji mwenye kuyafunua wazi yale ambayo watu wanaongokea kwayo kwenye kumuamini Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu

    [90] Na ni mwenye kuwaonya nyinyi isije ikawapata adhabu kama ile Aliyoiteremsha Mwenyezi Mungu kwa wale walioigawanya Qur,ani, wakaiamini baadhi yake na wakaikanusha baadhi nyingine miongoni mwa Mayahudi, Wanaswara na makafiri wa Kikureshi

    [91] «Na wao ni wale walioifanya Qur’ani kuwa ni vigawannyo na mafungu.» Kati yao kuna wanaosema, ‘ni uchawi’ na kati yao kuna wanaosema, ‘ni ukuhani’ na kati yao kuna wanaosema yasiyokuwa hayo ili wawazuie watu kufuata uongofu

    [92] Naapa kwa Mola wako, tutawahesabu tena tutawahesabu Siku ya Kiyama, na tutawalipa tena tutawalipa wote kwa kuigawanya kwao Qur’ani, kwa kuzua kwao urongo, kuibadilisha, kuipotoa na yasiyokuwa hayo

    [93] ambayo wao walikuwa wakiyatenda ya kuabudu mizimu, maasia na madhambi. Na katika haya pana kuwatisha na kuwaonya wao wasidumu nayo haya matendo mabaya

    [94] Na utangaze waziwazi ulinganizi wa haki ambao Amekuamrisha nao Mwenyezi Mungu, wala usiwajali washirikina, kwani kwa kweli Amekutakasa Mwenyezi Mungu kutokana na hayo wanayoyasema

    [95] Sisi, kwa hakika, tumekutosheleza hao wacheza shere wenye kufanya dharau kati ya viongozi wa Kikureshi

    [96] ambao wameifanya mizimu na vinginevyo kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu. Basi watakuja kuujua mwisho wa vitendo vyao, hapa duniani na kesho Akhera

    [97] Na kwa kweli, tunaujua unyongekaji wa kifua chako, ewe Mtume, kwa yale wayasemayo washirikina kuhusu wewe na kuhusu ulinganizi wako

    [98] Kimbilia kwa Mola wako pindi unaponyongeka moyo wako, na uitakase dhati Yake kwa kumshukuru na kumsifu. Na uwe ni miongoni mwa wenye kuswali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na wenye kumuabudu, kwani kwa kweli hilo litakutosheleza na lile lenye kukutia kero

    [99] Na uendelee kumuabudu Mola wako muda wa uhai wako mpaka ikujie yakini isiyokuwa na shaka nayo ni kifu. Na Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, alitekeleza amri ya Mola Wake, kwani hakuacha kuendelea kumuabudu Mwenyezi Mungu mpaka ikamjia yakini ya kifo kutoka kwa Mola Wake

    Nyuki

    Surah 16

    [1] Kumekaribia kusimama Kiyama na kutoka amri ya Mwenyezi Mungu ya kuwaadhibu nyinyi, enyi makafiri, basi msiifanyie haraka adhabu kwa njia ya kuicheza shere ahadi ya Mtume kwenu. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Ameepukana na ushirika na washirikina

    [2] Mwenyezi Mungu Anawateremsha Malaika kuleta wahyi kwa amri Yake kwa anayemtaka miongoni mwa waja Wake waliotumilizwa kwamba watisheni watu na ushirikina na waambieni kwamba hapana wa kuabudiwa kwa haki isipokuwa mimi. Hivyo basi, nicheni kwa kutekeleza faradhi zangu na kunipwekesha kwa kuniabudu na kunitakasa

    [3] Ameziumba mbingu na ardhi kwa haki, ili waja kwa hizo wachukue ushahidi juu ya utukufu wa Muumba wa hizo na kwamba, Yeye Peke Yake, Ndiye Anayestahiki kuabudiwa, Ameepukana, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, na Ametukuka na ushirikina wao

    [4] Amemuumba binadamu kutokana na maji matwevu, akitahamaki ajiona ana nguvu na majivuno, na akawa mkali wa utesi na kumjadili Mola wake katika kukanusha kufufuliwa na mengineyo, kama vile kusema, «Ni nani atakayeihuisha mifupa iwapo imeoza.» Na akawa ni mwenye kumsahau Mwenyezi Mungu Aliyemuumba kutoka kwenye hali ya kutokuwako

    [5] Na wanyama miongoni mwa ngamia, ng’ombe na mbuzi, Mwenyezi Mungu Amewaumbia, enyi watu, na akajaalia joto katika sufi na manyoa yake, na manufaa mengine katika maziwa yake na ngozi zake na kuwatumia kwa kuwapanda na, wengine miongoni mwao, kuwala

    [6] Na muna, kwa wanyama hao, pambo linaloingiza furaha kwenu, pindi mnapowarudisha kwenye mazizi yao jioni na pindi mnapowatoa kukicha kuwapeleka malishoni

    [7] Na wanabeba wanyama hawa vyombo vyenu vizito kuvipeleka kwenye mji wa mbali ambao hamkuwa ni wenye kuufikia isipokuwa kwa usumbufu mwingi wa nafsi zenu na mashaka makubwa. Hakika Mola wenu ni Mpole, Mwenye huruma kwenu kwa kuwafanyia vitu mnavyovitaka kuwa vipesi. Hivyo basi kusifiwa ni Kwake na kushukuriwa

    [8] Na Amewaumbia farasi, nyumbu na punda, mpate kuwapanda na wawe ni pambo kenu nyinyi na maangalizi mazuri. Na Anawaumbia nyinyi aina mbalimbali za vipando na vinginevyo ambavyo nyinyi hamna ujuzi navyo, ili mzidi kumuamini na kumshukuru

    [9] Na ni juu ya Mwenyezi Mungu kuwaeleza njia iliolingana sawa ya kuwaongoa nyinyi, nayo ni Uislamu. Na miongoni mwa njia kuna iliyoenda kombo isiyofikisha kwenye uongofu, nayo ni kila njia iliyo kinyume na Uislamu miongoni mwa mila na itikadi. Na lau Angalitaka Mwenyezi Mungu kuwaongoza, basi Angaliwaongoza nyote kwenye Imani

    [10] Yeye Ndiye Aliyewateremshia mvua kutoka juu na Akawapatia nyinyi kwa hiyo mvua maji mnayokunywa na akawatolea kwa maji hayo miti ya nyinyi kuwalisha wanyama wenu, na yanarudi kwenu matumizi yake na manufaa yake

    [11] Anawatolea nyinyi kutoka kwenye ardhi, kwa maji haya mamoja, mazao mbalimbali: Anawatolea nyinyi kwayo mizaituni, mitende na mizabibu, na anawatolea nyinyi kwayo kila aina ya matunda, makubwa kwa madogo. Hakika katika hayo pana ushahidi waziwazi kwa watu wanaofikiri na wakazingatia

    [12] Na Amewadhalilishia usiku kwa mapumziko yenu, na mchana kwa maisha yenu, na Amewadhalilishia jua likawa na mwangaza, na mwezi ukawa na nuru, na ili mpate kujua miaka na hesabu na manufaa mengine yasiyokuwa hayo. Na nyota huko mbinguni zimedhalilishwa kwa ajili yenu kwa amri ya Mwenyezi Mungu, ili mjue nyakati, kuiva kwa matunda na mazao na pia kuongoka kwa nyota hizo kwenye giza. Hakika, katika kudhalilisha huko, kuna alama waziwazi kwa watu wanaotia mambo akilini mwao kuhusu Mwenyezi Mungu, hoja Zake na alama Zake

    [13] Na Amewadhalilishia vile Alivyowaumbia katika ardhi miongoni mwa vinavyotambaa humo na matunda na madini na visivyokuwa hivyo ambavyo vina rangi na manufaa mbalimbali. Hakika katika uumbaji huo na kutafautiana rangi na manufaa pana mazingatio kwa watu wanaowaidhika na wanaojua kwamba katika kuvidhalilisha vitu hivyi pana alama nyingi juu ya umoja wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na juu ya kumpwekesha kwa ibada

    [14] Na Yeye Ndiye Ambaye Amewadhalilishia bahari ili mpate kula nyama laini ya samaki mnaowavua, na mtoe humo pambo mnalolivaa kama lulu na marjani, na utaziona jahazi kubwa zinapasua uso wa maji zikienda na kurudi, na mnazipanda ili mtafute riziki ya Mwenyezi Mungu kwa kufanya biashara na kutafuta faida ndani yake. Kwani huenda nyinyi mkamshukuru Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kwa neema zake kubwa juu yenu na msimuabudu asiyekuwa Yeye

    [15] Na Ameyakitisha kwenye ardhi majabali ya kuithibitisha ili isije ikawayumbisha nyinyi, na Ameiweka humo mito ili mpate kunywa maji yake, na Amefanya humo njia nyingi ili mpate kuongoka kwa njia hizo kuzifikia sehemu mnazozikusudia

    [16] Na kwenye hiyo ardhi Ameweka alama ambazo kwa alama hizo mnajielekeza njia kipindi cha mchana, kama alivyoziweka nyota ili kujiongoza kwa nyota hizo kipindi cha usiku

    [17] Basi mnamfanya Mwenyezi Mungu Ambaye Anaviumba vitu hivyi na vinginevyo, katika kustahiki Kwake kuabudiwa Peke Yake, ni kama waungu wanaodaiwa ambao hawaumbi chochote? Basi hamukumbuki utukufu wa Mwenyezi Mungu mkamuabudu Yeye Peke Yake

    [18] Na mkijaribu kuzidhibiti neema za Mwenyezi Mungu kwenu, ili mjue idadi yake, hamuwezi kuzidhibiti kwa wingi wake na utafauti wake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, ni Mwenye huruma kwenu, kwani Anasamehe kasoro zenu za kutotekeleza ushukuru wa neema, wala Hazikati kwenu, kwa kukiuka kwenu mipaka, wala Hawaharakishii mateso

    [19] Na Mwenyezi Mungu, Aliyetakata na kila aina ya upungufu, Anayajua matendo yenu yote, sawasawa yale mnayoyaficha ndani ya nafsi zenu kati ya hayo na yale mnayoyafanya waziwazi mbele ya wengine, na Atawalipa kwayo

    [20] Na wale waungu ambao washirikina wanawaabudu hawaumbi chochote hata kama ni kidogo vipi. Hao ni viumbe ambazo washirikina wamevitengeneza kwa mikono yao. Vipi basi wataviabudu

    [21] Wote hao ni visiki, havina uhai, wala hawajui wakati ambao Mwenyezi Mungu Atawafufua wale wanaowaabudu. Na waungu hao pamoja na wanaowaabudu wote watatupwa Motoni Siku ya Kiyama

    [22] Mola wenu Ndiye Mstahiki wa kuabudiwa Peke Yake. Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu Mmoja Peke Yake, hivyo basi wale wasioamini kufufuliwa, nyoyo zao ni zenye kuukanusha upweke Wake, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, kwa kutoogopa mateso Yake. Kwa hivyo, wao wana ujeuri wa kutoikubali haki na kukataa kumuabudu Mwenyezi Mungu Peke Yake

    [23] Ni kweli kwamba Mwenyezi Mungu Anayajua wanayoyaficha ya itikadi, maneno na vitendo, na wanayoyaonyesha waziwazi katika hayo, na Atawalipa kwa hayo. Kwa kweli Yeye, Aliyeshinda na kutukuka, Hawapendi wanaofanya ujeuri wa kukataa kumuabudu na kumtii, na Atawalipa kwa hilo

    [24] Na pindi wanapoulizwa, hawa washirikina, kuhusu yale yaliyoteremshiwa Nabii Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, wanasema kwa urongo na uzushi, «Hakuleta isipokuwa visa vya waliotangulia na porojo zao.»

    [25] Mwisho wao utakuwa ni kuzibeba dhambi zao kamili Siku ya Kiyama, hawatasamehewa chochote, na watazibeba dhambi za wale waliowadanganya ili kuwaepusha na Uislamu, bila ya kupunguziwa dhambi zao. Jueni mtanabahi, ni ubaya ulioje wa dhambi watakazozibeba

    [26] Kabla ya washirikina hawa, makafiri waliwafanyia vitimbi Mitume wao, na kuifanyia vitimbi haki waliokuja nayo. Hapo amri ya Mwenyezi Mungu ililijia jengo lao kutoka kwenye asili yake na msingi wake, na sakafu ikawaangukia, na maangamivu yakawajia kwenye sehemu ambazo walijimakini kuwa ni za amani, kutoka mahali wasipodhania kuwa maangamivu yatawajia kutoka hapo

    [27] Kisha Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu Atawafedhehi na Atawafanya wanyonge kwa adhabu na Atasema, «Wako wapi washirika wangu miongoni mwa waungu mliowaabudu badala yangu ili wawatetee msipate adhabu, na hali mlikuwa mkiwapiga vita Manabii na Waumini na mkiwafanyia uadui kwa sababu ya waungu hao?» Wanavyuoni wachamungu watasema, «Hakika utwevu na adhabu ndani ya Siku hii zitawashukia wenye kumkanusha Mwenyezi Mungu na Mitume Wake

    [28] ambao Malaika watazichukua roho zao, na wao wako katika hali ya kuzidhulumu nafsi zao kwa kukanusha.» Hapo watajisalimisha kwenye amri ya Mwenyezi Mungu pindi wanapoyaona mauti, na watavikanusha vile walivyokuwa wakiviabudu badala ya Mwenyezi Mungu na watasema, «Hatukuwa tukifanya maasia yoyote.» Na wataambiwa, «Mnasema urongo! Kwa hakika, mlikuwa mkiyafanya. Mwenyezi Mungu Anayajua matendo yenu yote na Atawalipa kwayo.»

    [29] Ingieni milango ya Jahanamu. Hamtotoka humo milele. Na mahali hapo ni paovu pa kukaa wenye kiburi waliokataa kumuamini Mwenyezi Mungu, kumuabudu Yeye Peke Yake na kumtii

    [30] Na wanapoambiwa Waumini wenye kumuogopa Mwenyezi Mungu, «Ni kitu gani Alichokiteremsha Mwenyezi Mungu kwa Nabii Muhammad, rehema na amani zimshukie?» wanasema, «Mwenyezi Mungu Amemteremshia wema na uongofu.» Wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake hapa duniani na wakawalingania waja wa Mwenyezi Mungu kwenye Imani na matendo mema, watapata heshima kubwa ya kupewa ushindi duniani na riziki kunjufu. Na nyumba ya Akhere ni bora kwao na ni kubwa kuliko vile walivyopewa duniani. Na nyumba yenye neema zaidi ya wale wachamungu wenye kumuogopa Mwenyezi Mungu ni Akhera

    [31] Makazi yao ni mabustani ya Pepo ya Milele, watatulia humo, hawatatoka humo kabisa, mito itakuwa ikipita chini ya miti yake na majumba yake ya fahari. Watakuwa na kila kinachotamaniwa na nafsi zao. Kwa mfano wa malipo haya mazuri, Mwenyezi Mungu Atawalipa wachamungu wenye kumuogopa

    [32] ambao Malaika watazichukua roho zao, na hali nyoyo zimetakasika na ukafiri. Malaika watawaambia, «Amani iwe juu yenu, Maamkizi yenu peke yenu , na muokoke na kila ovu, ingieni Peponi kwa yale mliyokuwa mkiyafanya ya kumuamini Mwenyezi Mungu na kufuata amri Yake.»

    [33] Washirikina hawangojei isipokuwa wajiwe na Malaika wazichukue roho zao wakiwa katika hali ya ukafiri, au ije ya amri ya Mwenyewzi Mungu na adhabu ya haraka ya kuwaangamiza. Na kama walivyokanusha hawa, walikanusha makafiri kabla yao, Mwenyezi Mungu Akawaangamiza. Wala Mwenyezi Mungu Hakuwadhulumu kwa kuwaangamiza na kuwaadhibu, lakini wao ndio waliokuwa wakizidhulumu nafsi zao kwa mambo yaliyowafanya wastahili kuadhibiwa

    [34] Basi yaliwateremkia mateso ya madhambi yao ambayo waliyatenda na ikawazingira wao adhabu ambayo walikuwa wakiifanyia shere

    [35] Na washirikina walisema, «Lau kama Mwenyezi Mungu Alitaka tumuabudu Yeye Peke Yake, hatungalimuabudu yoyote asiyekuwa Yeye, sisi wala baba zetu kabla yetu, wala hatungaliharamisha chochote Asichokiharamisha». Ni hoja kama hizi za kipotofu walizozitumia makafifiri waliopita. Na wao ni warongo, kwani Mwenyezi Mungu Aliwaamrisha na Akawakataza na Akawawezesha kuyasimamia Aliyowakalifisha nayo, na Akawapa nguvu na matakwa yanayotokamana na vitendo vyao. Kwa hivyo, kujenga hoja kwao wakitegemea mapitisho ya Mwenyezi Mungu na makadirio Yake ni ubatilifu mkubwa baada ya kuonywa kwao na Mitume. Na Mitume wenye kuwaonya hawana la zaidi isipokuwa kuufikisha ujumbe ulio wazi waliokalifishwa nao

    [36] Kwa hakika tulipeleka kwa kila ummah uliopita mjumbe wa kuwaamrisha wao kumuabudu Mwenyezi Mungu na kumtii Peke Yake, na kuacha kumuabudu asiyekuwa Yeye miongoni mwa Mashetani, mizimu, wafu na vinginevyo kati ya vile vinavyotegemewa badala ya Mwenyezi Mungu. Basi wakawa miongoni mwao wale ambao Mwenyezi Mungu aliwaongoa wakafuata njia ya Mitume, na kati yao wakapatikana wakaidi waliofuata njia za upotofu, hapo ikapasa kwao upotevu na Mwenyezi Mungu Asiwaafikie. Basi tembeeni katika ardhi na mjionee kwa macho yenu vipi yalivyokuwa marejeo ya hawa wakanushaji na maangamivu yaliyowashukia, mpate kuzingatia

    [37] Utakapofanya bidii yako ya mwisho, ewe Mtume, kuwaongoa hawa washirikina, basi jua kwamba Mwenyezi Mungu Hamuongozi Anayepotosha, na hawana wao yoyote asiyekuwa Mwenyezi Mungu atakayewaokoa na kuwazuilia adhabu Yake

    [38] Na hawa washirikina waliapa kwa Mwenyezi Mungu viapo vizito kwamba Mwenyezi Mungu Hatamfufua aliyekufa baada na kumalizika na kutawanyika. Kwani, Atawafufufa Mwenyezi Mungu kwa lazima, hiyo ni ahadi ya kweli Aliyojilazimisha nayo, lakini wengi wa watu hawaujui uweza wa Mwenyezi Mungu wa kufufua, ndio maana wanaukanusha

    [39] Mwenyezi Mungu Atwafufua waja wote, ili awafunulie ukweli wa Ufufuzi ambao wametafautiana juu yake, na ili makafiri wenye kuukanusha wapate kujua kwamba wao wako kwenye ubatilifu na kwamba wao ni warongo pindi walipoapa kwamba hakuna kufufuliwa

    [40] Hakika jambo la kufufua ni pesi kwetu. Kwani sisi tutakapo kitu, tunakiambia «Kuwa» ukitahamaki kimeshakuwa na kimeshapatikana

    [41] Na wale walioacha makao yao kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na wakahama baada ya matukio ya kudhulumiwa, tutawakalisha duniani makao mema. Na malipo ya Akhera ni makubwa zaidi, kwani malipo yao huko ni Pepo. Lau wale waliosalia nyuma wakaacha kugura wanayajuwa, ujuzi wa uhakika, yale yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ya malipo na thawabu kwa wale wanaogura katika njia Yake, hangalisalia nyuma yoyote katika wao

    [42] Hawa wenye kugura katika njia ya Mwenyezi Mungu ndio waliovumilia juu ya amri ya Mwenyezi Mungu na makatazo Yake na juu ya makadirio Yake yenye uchungu, na kwa Mola wao Peke Yake wanategemea, ndipo wakastahiki cheo hiki kikubwa

    [43] Na hatukuwatuma kwa waliotangulia kabla yako, ewe Mtume, isipokuwa Mitume miongoni mwa wanaume, sio Malaika, tunaowaletea wahyi. Na iwapo nyinyi, enyi washirikina wa Kikureshi, hamliamini hilo, basi waulizeni waliopewa vitabu vilivyopita, watawapa habari kwamba Manabii walikuwa ni binadamu, mkiwa hamjui kwamba wao ni binadamu. Aya hii inakusanya kila suala kati ya masuala ya Dini, iwapo mtu hana ujuzi nalo amuulize anayelijua miongoni mwa wanavyuoni waliovama katika elimu

    [44] Na tuliwatuma Mitume waliotangulia wakiwa na dalili waziwazi na vitabu vya mbinguni. Na tumekuteremshia wewe, ewe Mtume, Qur’ani upate kuwafunulia watu maana yake na hukumu zake zilizofichika, na ili wapate kuizingatia na waongoke kwayo

    [45] Je, wanajiaminisha wale makafiri wanaopanga vitimbi kwamba Mwenyezi Mungu Hatawadidimiza ndani ya ardhi kama Alivyomfanya Qarun au kwamba adhabu haitawafikia kutoka mahali wasipopadhania na wasipopatarajia

    [46] au adhabu haitawapata hali wakiwa wanazunguka kwenye safari zao na shughuli zao? Wao si wenye kumtangulia Mwenyezi Mungu wala kumponyoka wala kuokoka na adhabu Yake, kwani Yeye Ndiye Mwenye nguvu Ambaye hakuna chenye kumuelemea

    [47] Au Mwenyezi Mungu Awapatilize kwa upungufu wa mali na watu na matunda au katika hali ya kuogopa kwao Asiwatie mkononi. Kwani Mola wenu ni Mpole kwa waja Wake, ni Mwenye huruma kwao

    [48] Je, kwani makafiri hawa wamekuwa vipofu wakawa hawaangalii vitu venye vivuli Alivyoviumba Mwenyezi Mungu, kama vile majabali na miti ambayo vivuli vyake vinapinduka, mara nyingine upande wa kulia na mara nyingine upande wa kushoto, kufuatia mwendo wa jua kipindi cha mchana na mwendo wa mwezi kipindi cha usiku.Vyote hivyo ni vyenye kuunyenyekea ukuu wa Mwenyezi Mungu na utukufu Wake. Navyo viko chini ya uendeshaji Wake, mipango Yake na utendeshaji nguvu Wake

    [49] Na vinamsujudia Mwenyezi Mungu Peke Yake vyote vilivyo mbinguni na vilivyo ardhini, miongoni mwa vinavyotambaa. Na Malaika wanamsujudia Mwenyezi Mungu, na wao hawafanyi ujeuri kwa kukataa kumuabudu Yeye. Na Amewahusu Malaika kwa kuwataja baada ya kuwakusanya pamoja na viumbe wengine, kutokana na utukufu wao, ubora wao na wingi wa kuabudu kwao

    [50] Hao Malaika wanamuogopa Mola wao Ambaye Yuko juu yao kwa dhati Yake, utendeshaji nguvu Wake na ukamilifu wa sifa Zake, na wanafanya wanayoamrishwa ya kumtii Mwenyezi Mungu. Katika aya hii pana kuthibitisha sifa ya kuwa Mwenyezi Mungu Yuko juu ya viumbe vyake vyote, kama inavyonasibiana na utukufu Wake na ukamilifu Wake

    [51] Na Alisema Mwenyezi Mungu kuwaambia waja Wake, «Msiabudu waungu wawili, kwani muabudiwa wenu ni Mola Mmoja. Basi niogopeni mimi na sio mwingine asiyekuwa mimi.»

    [52] Na ni vya Mwenyezi Mungu, Peke Yake, vyote vilivyoko mbinguni na ardhini, kwa kuviumba, kuvimiliki na kuviendesha. Na ibada inaelekezwa Kwake PekeYake, na pia kutiiwa na kutakaswa daima. Basi je, inafaa kwenu nyinyi mumuogope asiyekuwa Yeye na mumuabudu

    [53] Na neema yoyote mliyonayo ya uongofu au afya ya mwili, ukunjufu wa riziki na watoto na yasiyokuwa hayo, inatoka kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake, Yeye Ndiye Mwenye kuwaneemesha nayo. Kisha yanapowapata magonjwa, matatizo na ukame, basi ni kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake mnalia kwa maombi

    [54] Kisha Anapowaondolea matatizo na magonjwa, kitahamaki linatoka kundi la watu miongoni mwenu wakawa wanawafanya asiyekuwa Yeye kuwa ni washirika pamoja na Yeye na wategemewa

    [55] Ili wapate kuzikanusha neema zetu kwao, na miongoni mwazo ni kuondolewa matatizo. Basi jistarehesheni na ulimwengu wenu, nao mwisho wake ni kutoweka, hapo mtajua mwisho wa ukanushaji wenu na uasi wenu

    [56] Na miongoni mwa uovu wa matendo yao ni kwamba wao wanawatengea masanamu waliowafanya ni waungu, wasiojua chochote na wasionufaisha wala kudhuru, sehemu ya mali zao walizoruzukiwa na Mwenyezi Mungu ili kujisongeza kwao. Ninaapa kwa Mwenyezi Mungu! Mtaulizwa tena mtaulizwa Siku ya Kiyama kuhusu yale ya urongo ambayo mlikuwa mkimzulia Mwenyezi mungu

    [57] Na makafiri wanamsingizia Mwenyezi Mungu kuwa ana watoto wa kike na huwa wakisema, «Malaika ni watoto wa kike wa Mwenyezi Mungu». Ameepukana Mwenyezi Mungu na neno lao. Na wanajichukulia wao wenyewe watoto wa kiume wanaowapenda

    [58] Na pindi anapokuja mwenye kumpasha habari mmoja wao ya kuzaliwa mtoto wa kike, uso wake hapohapo unageuka mweusi, kwa kuyachukia aliyoyasikia, na akajawa na hasira na huzuni

    [59] Anajificha kwa kuchukia asionekane na watu wake, akiona aibu na kuingiwa na huzuni kwa habari iliyomchukiza ya kuzaliwa mtoto wa kike, huku akiwa ametunduwaa juu ya tukio la mtoto huyo aliyezaliwa: je, amuache kuishi kwenye hali ya unyonge na utwevu au amzike mchangani akiwa hai? Jueni mtanabahi kwamba ni uamuzi mbaya mno wanaouamua ya kuwafanya watoto wa kike ni wa Mwenyezi Mungu na watoto wakiume ni wao

    [60] Wale wasioiamini Akhera na wasiofanya matendo ya kuwafaa huko wana sifa mbaya za ulemevu, uhitaji, ujinga na ukafiri, na Mwenyezi Mungu Ana sifa tukufu za ukamilifu, kujitosheleza na viumbe Vyake. Na Yeye Ndiye Mshindi katika mamlaka Yake, ni Mwenye hekima katika uendeshaji Wake

    [61] Lau kwamba Mwenyezi Mungu Anawapatiliza watu kwa ukafiri wao na uzushi wao, Hangalimuacha juu ya ardhi mtu yoyote mwenye kutembea, lakini Anawabakisha mpaka wakati uliopanagwa, nao ni mwisho wa muda wao wa kuishi, basi utakapofika wakati wao wa kuondoka duniani, hawatacheleweshwa nao hata muda mchache wala hawatatangulia

    [62] Na miongoni mwa maovu yao, ni kwamba wao wanawafanya ni wa Mwenyezi Mungu watoto wa kike ambao wao wenyewe wanawachukia. Na ndimi zao zinasema urongo kwamba wao watakuwa na mwisho mwema. Kwa kweli, wao watakuwa na Moto na wao ni wenye kuachwa humo na kusahauliwa

    [63] Naapa kwa Mwenyezi Mungu, hakika tumewapeleka Mitume kwa makundi ya watu kabla yako, ewe Mtume, Shetani akawapambia matendo waliyoyafanya ya ukafiri, ukanushaji na kuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Yeye anasimamia kazi ya kuwapoteza wao ulimwenguuni, na hao wenye kupotezwa, watakuwa na adhabu kali yenye kuumiza kesho akhera

    [64] Na hatukukuteremshia Qur’ani, ewe Mtume, isipokuwa ni uwafunulie watu wazi yale ambayo walikuwa wakitafautiana juu yake, ya dini na hukumu, ili hoja zisimame kwao kwa maelezo yako ambayo hayauachii upotofu njia ya kuingia nyoyoni. Na kwa kuwa Qur’ani ni uongofu, haitoi nafasi ya kutunduwaa, nayo ni rehema kwa Waumini katika kufuata kwao uongofu na kujiepusha kwao na upotevu

    [65] Na Mwenyezi Mungu Ameteremsha mvua kutoka mawinguni, na Akatoa kwa mvua hiyo mimea kutoka ardhini baada ya kuwa kame na kavu. Hakika katika kuteremsha mvua na kuotesha mimea pana ushahidi juu ya uweza wa Mwenyezi Mungu wa kufufua, na pia pana ushahidi juu ya upweke Wake kwa watu wanaosikia, wanaozingatia, wanaomtii Mwenyezi Mungu na wanaomuogopa

    [66] Kwa kweli muna nyinyi, enyi watu, mazingatio katika wanyama howa, nao ni ng’ombe, ngamia na mbuzi na kondoo. Kwani mumeshuhudia kwamba sisi tunawanywesha kutoka kwenye nyato zao maziwa yanayotoka kati ya choo, kilicho ndani ya tumbo, na damu yakiwa yamesafishika na kila uchafu, yenye ladha, hayamkeri mwenye kuyanywa

    [67] Na miongoni mwa neema zetu kwenu ni yale matunda ya mitende na mizabibu mnayoyachukuwa mkayatengeneza pombe yenye kulewesha - na hii na kabla haijaharamishwa- na chakula kizuri. Hakika katika hayo yaliyotajwa pana ushahidi juu ya uweza wa Mwenyezi Mungu kwa watu wenye kuzitia akilini hoja hizo wakazizingatia

    [68] Na Mola wako, ewe Mtume, Aliwapa nyuki ufunzi kwamba jifanyieni nyumba kwenye majabali, kwenye miti na kwenye nyumba na sakafu zinazojengwa na watu

    [69] Kisha kuleni katika kila tunda mnalolipenda na mzifuate njia za Mola wenu mlizotayarishiwa ili kutafuta riziki majabalini na kati ya miti. Na Mwenyezi Mungu Amewasahilishia njia hizo, hamupotei katika kurudi hata kama ni mbali. Inatoka kwenye matumbo ya nyuke asali yenye rangi tafauti: nyeupe, manjano, nyekundu na nyiginezo. Na kwenye hiyo asali pana tiba ya magonjwa ya watu. Hakika katika hayo wanayoyafanya nyuki pana ushahidi wenye nguvu juu ya uweza wa Muumba wao kwa watu wanaofikiria na wakazingatia

    [70] Na mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Amewaumba, kisha Atawafisha katika mwisho wa umri wenu. Na kati yenu kuna wale ambao watafikia umri muovu, nao ni ukongwe, kama alivyokuwa uchangani mwake, hajui chochote ambacho alikuwa akikijua. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, ni muweza, ujuzi Wake na uweza wake vimezunguka kila kitu. Mwenyezi Mungu Aliyemrudisha mwanadamu kwenye hali hii ni muweza wa kumfisha kisha kumfufua

    [71] Mwenyezi Mungu Amewafanya bora baadhi yenu kuliko wengine katika riziki Aliyowapa ulimwenguni: katika nyinyi kuna tajiri na katika nyinyi kuna masikini, katika nyinyi kuna anayemiliki na katika nyinyi kuna anayemilikiwa, wenye kumiliki hawawapi wenye kuwamilikiwa kile Alichowapa Mwenyezi Mungu cha kuwafanya wawe na kiwango cha mali sawa na wao. Basi iwapo hawaliridhii hilo kwenye nafsi zao, ni kwa nini wanaridhika kumfanya Mwenyezi Mungu kuwa Ana washirika miongoni mwa watumwa Wake? Kwa kweli huu ni udhalimu mkubwa kabisa na ukanushaji mkubwa kabisa wa neema za Mwenyezi mungu

    [72] Na Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Amewaumba wake kutokana na na nyinyi ili nafsi zenu ziliwazike na wao, na amewapa kutokana nao watoto, na kutokana na kizazi chao wajukuu, na Amewaruzuku vyakula vizuri miongoni mwa matunda, nafaka, nyama na visivyokuwa hivyo. Je, kwani wanauamini upotofu wa uungu wa washirika wao na wanazikanusha neema za Mwenyezi Mungu zisizohesabika na hawamshukuru kwa kumpwekesha Yeye Peke Yake, Aliyetukuka na kuwa juu, kwa ibada

    [73] Na washirikina wanaabudu masanamu ambayo hayana mamlaka ya kuwapa riziki itokayo mbinguni kama mvua wala itokayo ardhini kama mazao. Wao hawamiliki kitu chochote wala hapana uezekano wowote kwa wao kukimiliki, kwani wao hawawezi

    [74] Na mjuapo kwamba masanamu na mizimu havinufaishi, basi msimfanye Mwenyezi Mungu Ana ambao ni kama Yeye wenye kufanana na Yeye miongoni mwa viumbe Wake mkawa mnawashirikisha wao pamoja na Yeye katika ibada. Hakika Mwenyezi Mungu Anayajua mnayoyafanya, na nyinyi mumeghafilika hamjui makosa yenu na ubaya wa mwisho wenu

    [75] Na Mwenyezi Mungu Amepiga mfano, Akafafanua kwa mfano huo ubatilifu wa itikadi ya washirikina. Mfano wenyewe ni wa mtu aliyemilikiwa asiyeweza kujipitishia jambo asiyemiliki chochote, na mtu mwingine aliye huru, mwenye mali ya halali ambayo Mwenyezi Mungu Amemruzuku, anayemiliki kupitisha atakalo katika mali hayo, akawa anapeana kwa siri na kwa dhahiri. Je, kuna yoyote mwenye akili atakayesema kwamba watu wawili hawa wako sawa? Hivyo ndivyo Alivyo Mwenyezi Mungu Anayemiliki na Anayepitisha. Yeye Hafanani na viumbe Vyake na watumwa wake. Basi vipi mtasawazisha baina yao? Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Peke Yake. Yeye Ndiye Anayestahiki kushukuriwa na kusifiwa. Lakini wengi wa washirikina hawajui kwamba sifa njema na neema ni za Mwenyezi mungu na kwamba Yeye, Peke Yake, Ndiye Anayestahiki kuabudiwa

    [76] Na Mwenyezi Mungu Amepiga mfano mwingine wa ubatilifu wa ushirikina. Mfano wenyewe ni wa watu wawili, mmoja wao ni bubu kiziwi, haelewi wala haelezi, hawezi kujinufaisha yeye mwenyewe wala wengine, naye ni mzigo mzito kwa anyesimamia mambo yake na kumwangalia kwa mahitaji yake, akimtuma kwa jambo lolote alitekeleze hafaulu wala hamletei jambo lolote zuri. Na mtu mwengine ana hisia zilizo sawa, anajinufaisha yeye na wengine, anaamuru utunzaji wa haki, na yeye yuko kwenye njia iliyo wazi isiyopotoka. Je, watu wawili hawa wanalingana katika maoni ya wenye akili? Basi vipi mtasawazisha baina ya sanamu kiziwi na Mwenyezi Mungu Muweza Mwenye kuneemesha kila zuri

    [77] Ni wa Mwenyezi Mungu, Aliyetakata na kutukuka, ujuzi wa mambo yasiyoonekana ya mbinguni na ardhini. Na jambo la Kiyama halikuwa, kwa uharaka wa kuja kwake, isipokuwa ni kama mtazamo wa haraka wa jicho au ni haraka zaidi kuliko huo. Hakika Mwenyezi Mungu kwa kila jambo ni Muweza

    [78] Na Mwenyezi Mungu , Aliyetakata na kutukuka, Amewatoa nyinyi kutoka kwenye matumbo ya mama zenu baada ya kipindi cha mimba, hali hamtambui chochote kilichoko pambizoni mwenu, na akawapatia sababu za kutambua miongoni mwa mashikio ya kusikia na macho ya kuonea na nyoyo, huenda nyiyi mkamshukuru Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kwa neema hizo na mukampwekesha, Aliyeshinda na kutukuka, kwa ibada

    [79] Je, hawakutazama washirikina kuwaangalia ndege walivyoendeshwa na kuwezeshwa kuruka angani, baina ya mbingu na ardhi, kwa amri ya Mwenyezi Mungu? Hakuna anaowazuia wasianguke isipokuwa Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, kwa kuwa amewaumbia mbawa na mikia na Akawawezesha kuruka. Hakika katika huko kuendeshwa na kuzuiliwa kuna alama za ushahidi kwa wale wanaoziamini dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu

    [80] Mwenyezi Mungu, Aliyetakata na sifa za upungufu, Amewapatia nyinyi mapumziko na utulivu kwenye nyumba zenu pamoja na watu wenu mkiwa mijini, na Amewapatia nyinyi mahema na mindule ya ngozi za wanyama- howa, ambayo ni sahali kwenu mkiwa safarini, na ambayo ni sahali kwenu kuisimamisha pale mkaapo baada ya safari, na Amewapatia nyinyi kutokana na manyoya ya kondoo, manywele ya ngamia na nwyele za mbuzi vyombo vya matumizi yenu ya kuvaa, kujifinika, kutandika na pambo la nyinyi kujifurahisha kwalo mpaka kipindi kilichotajwa na wakati ujulikanao

    [81] Na Mwenyezi Mungu Amewaptia miti na vinginevyo vya kuwaletea vivuli, na amewafanyia kwenye majabali na pango sehemu za kuhamia mnapohitajia, na Amewafanyia nguo kutokana na pamba na sufi na vinginevyo za kuwahifadhi na joto na baridi, na Amewaumbia chuma cha nyinyi kujikinga na silaha za kudunga za maadui wenu na madhara yao katika vita vyenu na wao. Kama vile Alivyowaneemesha kwa neema hizi, atawakamilishia neema Zake kwenu kwa kuwafafanulia wazi Dini ya haki, ili mjisalimishe kwa amri ya Mwenyezi Mungu, Peke Yake, na msimshirikishe na kitu chochote katika ibada Yake

    [82] Wakikupa mgongo, ewe Mtume, baada ya kuziona hizi aya, basi usisikitike. Kwani jukumu lako ni kuufikisha ujumbe uliotumwa nao waziwazi, ama kuongoa ni kwetu sisi

    [83] Washirikina hawa wazijua neema za Mwenyezi Mungu juu yao za kutumilizwa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwao, kisha wanaukanusha utume wake. Na wengi wa watu wake ni wale wanaoukanusha utume wake na sio wanaoukubali

    [84] Na wakumbushe, ewe Mtume, yale yatakayokuwa Siku ya Kiyama, tutakapowaletea kila kundi la watu Mtume wao akitolea ushahidi Imani ya walioamini miongoni mwao na ukanushaji wa wenye kukanusha. Kisha hao waliokanusha hawatapewa nafasi ya kuomba msamaha kwa waliyoyafanya, na hawatatakiwa kumridhisha Mola wao kwa kutubia na kufanya matendo mema, kwani wakati wa hilo ushapita

    [85] Na wale waliokanusha watakapoishuhudia adhabu ya Mwenyezi huko Akhera, basi hawatapunguziwa chochote katika hiyo adhabu, hawatapewa muhula wala hawatacheleweshwa

    [86] Na wale waliokanusha watakapowaona Siku ya Kiyama waungu wao waliokuwa wakiwaabudu pamoja na MwenyeziMungu watasema, «Mola wetu! Hawa ndio washirika wetu tuliokuwa tukiwaabudu badala yako.» Hapo waungu hao watatamka kuwakanusha wale waliowaabudu na watasema, «Hakika nyinyi, enyi washirikina, ni warongo, mlipotufanya sisi ni washirika wa Mwenyezi Mungu na mkatuabudu pamoja na Yeye. Sisi hatukuwaamuru hilo, wala hatukudai kwamba sisi tunastahiki uungu, lawama ni juu yenu.»

    [87] Na hiyo Siku ya Kiyama, washirikina wataonyesha kusalimu amri na unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu, na yatawapotea yale ya urongo waliokuwa wakiyazua na kwamba waungu wao watawaombea

    [88] Wale ambao waliukanusha upweke wa Mwenyezi Mungu na unabii wako, ewe mtume, na wakakukanusha wewe, wakawakataza wengine wasimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, tutawazidishia adhabu juu ya ukanushaji wao na adhabu juu ya kuwazuia watu kuifuata haki. Na hili ni kwa sababu ya kukusudia kwao kufanya uharibifu na kuwapoteza waja kwa ukafiri na uasi

    [89] Na kumbuka, ewe Mtume, pindi tutakapomleta, Siku ya Kiyama, katika kila ummah miongoni mwa ummah zote, shahidi juu yao: naye ni Mtume ambaye Mwenyezi Mungu Alimpeleka kwao anayetokana na wao wenyewe na kwa lugha yao, na tukakuleta wewe, ewe Mtume, ukiwa ni shahidi juu ya ummah wako. Na kwa kweli, tumekuteremshia Qur’ani ikiwa na ufafanuzi wa kila jambo linalohitajia maelezo, kama hukumu za halali na haramu, malipo mema na mateso na yasiyokuwa hayo, na ili iwe ni uongofu wenye kutoa kwenye upotevu, na ni rehema kwa atakayeiamini na kuifuata kivitendo, na iwe ni bishara njema kwa Waumini kwamba watakuwa na mwisho mwema

    [90] Hakika Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Anawaamrisha waja Wake ndani ya Qur’ani hii wawe waadilifu, wafanye usawa katika kutunza haki Yake, kwa kumpwekesha Yeye na kutomshirikisha, na haki ya waja Wake, kwa kumpa haki yake kila mwenye haki. Na Anaamrisha kufanya wema katika kutekeleza haki Yake, kwa kumuabudu na kutekeleza faradhi Zake kwa namna ilivyopasishwa na Sheria, na kuwafanyia wema viumbe Wake katika maneno na vitendo. Na Anaamrisha kuwapa walio na ukaribu wa ujamaa kitu cha kuwaunga na kuwatendea wema. Na Anakataza kila ambalo ni ovu, likiwa ni neno au ni tendo, na ambalo Sheria inalipinga na haikubaliani nalo la ukafiri na maasia, na kuwadhulumu watu na kuwafanyia maonevu. Na Mwenyezi Mungu, kwa maamrisho haya na makatazo haya, Anawaidhia na kuwakumbusha mwisho mbaya, ili mzikumbuke amri za Mweneyzi Mungu na mnufaike nazo

    [91] Na jilazimisheni kutekeleza kila ahadi mliyojilazimisha nayo juu ya nafsi zenu, baina yenu nyinyi na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, au baina yenu na watu katika yale yasiyoenda kinyume na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunnah ya Nabii Wake. Wala msirudi nyuma kwenye viapo mlivyovitilia mkazo, na hali mlimfanya Mwenyezi Mungu Ndiye mdhamini na msimamizi mlipomuahidi. Hakika Mwenyezi Mungu Anayajua mnayoyafanya na Atawalipa kwayo

    [92] Wala msirudi nyuma kwenye ahadi zenu, ukawa mfano wenu ni kama wa mwanamke aliyefuma mfumo akautengeneza vizuri kisha akaufumua, Mnavifanya viapo vyenu mlivyoviapa wakati wa makubaliano kuwa ni udanganyifu kwa mliyopatana naye, mkawa mnazivunja ahadi zenu mnapopata kundi la watu wenye mali kuliko wale mlioahidiana nao. Kwa hakika, Mwenyezi Mungu Anawapa mtihani kwa kuwaamrisha nyinyi mtekeleze ahadi na kuwakataza nyinyi msizivunje. Na ili Apate kuwaeleza, Siku ya Kiyama, yale ambayo mlikuwa mkitafautiana kwayo kuhusu kumuamini Mwenyezi Mungu na kuuamini unabii wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [93] Na lau Mwenyezi Mungu angalitaka angaliwaafikia nyote Akawafanya muwe kwenye muelekeo mmoja, nao ni Uislamu na Imani, na Angaliwalazimisha nao. Lakini Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Anampoteza Anayemtaka, kati ya wale ambao Yeye Alijua kuwa walichagua upotevu, Asimuongoze kwa uadilifu Wake. Na Anamuongoza Anayemtaka, kati ya wale ambao Yeye Alijua kuwa wao walichagua haki, Akampa muelekeo kwa wema Wake. Na Mwenyezi Mungu Atawauliza nyinyi nyote, Siku ya Kiyama, yale ambayo mlikuwa mkiyafanya ulimwenguni kati ya yale Aliyowaamrisha nayo na Aliyowakataza, na Atawalipa nyinyi kwa hayo

    [94] Wala msifanye , kati ya viapo mnavyoviapa, udanganyifu kwa wale mliowaapia, mkaja kuangamia baada ya kuwa kwenye amani. Ni kama yule ambaye nyayo zake ziliteleza baada ya kuwa zimekita. Na mtaonja adhabu ya kuwaudhi ulimwenguni kwa vile mlisababisha kuwakataza wengine na Dini hii kwa ukiukaji ahadi waliouona kutoka kwenu, na huko Akhera mtapata adhabu kubwa

    [95] Na wala msivunje ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa kuchukua badala yake kitu kidogo cha starehe ya duniani. Hakika malipo mema yaliyoko kwa Mweneyzi Mungu ya utekelezaji ahadi ni bora kwenu kuliko thamani hii ndogo. Basi iwapo nyinyi ni watu mnaojua, zingatieni tafauti iliyopo baina ya mazuri mawili haya: ya ulimwenguni na ya Akhera

    [96] Hayo mliyonayo, miongoni mwa taka za kilimwengu, yataondoka na yale yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu, ya riziki na thawabu, hayataondoka. Na wale waliohimili kubeba mazito ya Sheria waliyotakiwa wayabebe, miongoni mwayo ikiwa ni utekelezaji ahadi, tutawalipa malipo mazuri zaidi ya matendo yao mema: tutawapa zaidi kwa matendo yao madogo kama tutakavyowapa zaidi kwa matendo yao makubwa kwa ukarimu wetu

    [97] Mwenye kufanya tendo zuri, akiwa ni mwanamume au ni mwanake, na huku ni mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake , basi tutampa maisha mema yenye utulivu duniani hata kama ni mchache wa mali, na tutawalipa huko Akhera thawabu zao kwa uzuri zaidi ya walivyofanya duniani

    [98] Na pindi ukitaka, ewe Muumini, kusoma chochote katika Qur’ani, basi jilinde kwa Mwenyezi Mungu na Shari la Shetani aliyefukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu kwa kusema, «A'ūdhu bi- Llāhi min ash-Shayttān ar-Rajīm»(Najilinda kwa Mwenyezi Mungu na Shetani Aliyefukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu)

    [99] Kwa hakika, Shetani hana uwezo wa kuwasaliti wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wanaomtegemea Mola wao

    [100] Uwaezo wake wa kusaliti ni juu ya wale waliomfanya yeye ni msaidizi wao na wakamtii na wale ambao wao, kwa sababu ya kumtii yeye, wanamshirikisha Mwenyezi Mungu Aliyetukuka

    [101] Na tunapoibadilisha aya kwa aya nyingine, na Mwenyezi Mungu Mwenye kuumba ni Anayajua zaidi maslahi ya viumbe Wake kwa hukumu Anazoziteremsha katika nyakati mbalimabali, makafiri wanasema, «Hakika yako wewe, Ewe Muhammad, ni mrongo mwenye kumzulia Mwenyezi Mungu Asiyoyasema.» Na Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amni zimshukiye, si kama wanavyodai. Lakini wengi wao hawana ujuzi juu ya Mola wao wala kuhusu Sheria Yake na hukumu Zake

    [102] Waambie, ewe Mtume, Qurani haikuzuliwa na mimi, bali aliyeiteremsha ni Jibrili kutoka kwa Mola wako kwa ukweli na uadilifu ili kuwafanya Waumini wawe imara, kuwaongoza wao kutoka kwenye upotevu , na kuwapa bishara njema wale waliojisalimisha na kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu, Bwana wa viumbe wote

    [103] Na kwa hakika tunajua kuwa washirikina wanasema kwamba Nabii anapokea Qur’ani kutoka kwa kiumbe miongoni mwa wanadamu. Wamesema urongo! Kwani ulimi wa yule waliomsingizia kuwa amemfundisha Nabii, rehema na amani zimshukie, si wa Kiarabu usiyotasua, na hii Qur’ani ni kwa lugha ya Kiarabu, imefikia upeo wa ufafanuzi na ubainifu

    [104] Hakika hao makafiri wasioiamini Qur’ani, Mwenyezi Mungu Hatawaelekeza kuipata haki, na Siku ya Akhera watakuwa na adhabu kali iumizayo

    [105] Kwa hakika wanaozua urongo ni wale wasiomuamini Mwenyezi Mungu na aya Zake, na wao ndio warongo kwa neno lao hilo. Ama Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, anayemuamini Mola wake na kumnyenyekea, haiwezekani kwake yeye kumkanusha Mwenyezi Mungu na kumsingizia Asiyoyasema

    [106] Hakika wanaozua urongo ni wanaotamka neno la ukafiri na akaritadi baada ya kuamini. Hao itawashukia wao hasira kutoka kwa Mwenyezi Mungu, isipokuwa yule aliyelazimishwa kutamaka maneno ya ukafiri na akayatamka kwa kuchelea kuangamia, hali moyo wake umejikita kwenye Imani, basi huyo hana lawama. Lakini mwenye kutamka ukafiri na moyo wake ukatulia juu yake, hao watashukiwa na hasira kali kutoka kwa Mwenyezi Munngu na watapata adhabu kubwa

    [107] Hiyo ni kwa sababu ya kuchagua kwao dunia na pambo lake na kuifanya kwao hiyo dunia kuwa ni bora kuliko Akhera na malipo yake na kwamba Mwenyezi Mungu Hawaongozi makafiri wala hawaelekezi kwenye haki na usawa

    [108] Hao ndio wale ambao Mwenyezi Mungu Amewapiga muhuri nyoyo zao kwa ukafiri na ufadhilishaji dunia juu ya Akhera, hazitafikiwa na nuru ya uongofu, na Amewafanya viziwi masikio yao kutozisikia aya za Mwenyezi Mungu , kusikia kwa kuzingatia, na Amewafanya vipofu macho yao wasizione hoja zinazojulisha uungu wa Mwenyezi Mungu , na hao ndio wenye kughafilika na ile adhabu Aliyowaandalia Mwenyezi Mungu

    [109] Ni kweli kabisa kwamba wao, huko Akhera, ndio wenye hasara wenye kuangamia, waliotumia maisha yao kwa mambo yaliyopelekea kuadhibiwa na kuangamizwa

    [110] Kisha Mola wako, kwa wale waliofanywa wanyonge ndani ya Makkah na wakaadhibiwa na washirikina mpaka wakakubali matendo yao kijuujuu, wakawafitini kwa kutamka yanayowaridhi, na hali nyoyo zao zimetulia katika Imani, na ilipowezekana kwao kujiokoa waligura kwenda Madina kisha wakapigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na wakavumilia mashaka ya majukumu, hakika Mola wako , baada ya kutubia kwao ni Mwenye kuwasamehe , ni Mwenye kuwarehemu

    [111] Na wakumbushe wao, ewe Mtume, Siku ya Kiyama pindi itakapokuja kila nafsi ikijitetea yenyewe na kutoa nyudhuru za kila aina, na hapo Mwenyezi Mungu Ailipe kila nafsi malipo ya ilichokifanya bila ya kuidhulumu. Hatawaongezea mateso wala hawatapunguzia malipo yao

    [112] Na Mwenyezi Mungu Amepiga mfano wa mji wa Makkh. Ulikuwa uko kwenye salama ya kutofanyiwa uadui, utulivu kutokana na dhiki za maisha na unajiliwa na riziki zake kwa uzuri na usahali kutoka kila upande, wakazi wake wakazikanusha neema za Mwenyezi Mungu kwao, wakamshirikisha na wasimshukuru, hapo Mwenyezi Mungu Akawatesa kwa njaa na kicho kwa kuviogopa vikosi vya Mtume, reheme ya Mwenyezi Mungu na amni zimshukiye, na majeshi yake yaliyokuwa yakiwatisha, na hili ni kwa sababu ya ukafiri wao na vitendo vyao vya ubatilifu

    [113] Hakika Mwenyezi Mungu Alipeleka kwa watu wa Makkah Mtume miongoni mwao, yeye ni Nabii Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wanaijua nasaba yake, ukweli wake na uaminifu wake, wasiyakubali yale aliyowajia nayo na wasimuamini. Hapo iliwapata adhabu ya shida, njaa, kicho na kuuawa wakuu wao huko Badr na hali wao ni madhalimu wa nafsi zao kwa kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kuwazuia watu njia Yake

    [114] Basi kuleni, enyi Waumini, miongoni mwa vile ambavyo Mwenyezi Mungu Amewaruzuku na Akavifanya ni halali nzuri kwenu. Na shukuruni neema za Mwenyezi Mungu kwenu, kwa kuzitambua na kuzitumia katika kumtii Mwenyezi Mungu, iwapo nyinyi, kikweli, ni wenye kuandama amri Yake, ni wenye kusikia na kumtii Yeye, mnamuabudu Yeye Peke Yake, Asiye na mshirika

    [115] Hakika Amewaharamishia mfu wa mnyama, damu yenye kutiririka kutoka kwa mnyama aliechinjwa pale achinjwapo, nyama ya nguruwe na mnyama aliyechinjiwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Lakini yoyote Aliyelazimika kula chochote kati ya vitu hivi vilivyoharamishwa, kwa dharura ya kuogopa kufa, na hali yeye si dhalimu wala si mkiukaji mpaka ya dharura, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kumsamehe na ni Mwenye huruma naye, Hatamtesa kwa kwa kitendo alichokifanya

    [116] wala msiseme, enyi washirikina, urongo unaotolewa na ndimi zenu: «hii ni halali» juu ya kitu kilichoharamishwa «na hii ni haramu» juu ya kitu kilichohalalishwa, ili kumzulia Mwenyezi Mungu urongo kwa kumnasibishia uhalalishaji na uharamishaji. Hakika wale wanaomzulia Mwenyezi Mungu urongo hawatafaulu kupata wema wowote ulimwenguni wala Akhera

    [117] Starehe walionayo duniani na starehe yenye kuondoka na ni chache. Na huko Akhera watapata adhabu iumizayo

    [118] Na Mayahudi tuliwaharamishia vile vitu tulivyokupa habari zake, ewe Mtume, kabla, navyo ni kila mnyama mwenye kucha na mafuta ya ng’ombe, mbuzi na kondoo, isipokuwa kile kilichobebwa na migongo yao au matumbo yao au kilichotangamana na mifupa. Na sisi hatukuwadhulumu wao , lakini wao walikuwa ni wenye kuzidhulumu nafsi zao kwa kukanusha na kufanya uadui, ndipo wakastahili kuharamishiwa kwa njia ya kutiwa adabu

    [119] Kisha hakika Mola wako, kwa wale waliofanya maasia, kwa kutojua mwisho wake na kwamba yanapasisha hasira za Mwenyezi Mungu - kwani kila anayemuasi Mwenyezi Mungu, kwa kukosea au kwa kusudia, huwa ni mjinga kwa mtazamo huu, hata kama anajua kuwa ni haramu-, kisha wakarudi kwa Mwenyezi Mungu na kuyaepuka yale madhambi waliokuwa wakiyafanya na wakazitengeneza nafsi zao na matendo yao, hakika Mola wako, baada ya kutubia kwao na kutengenea kwao, ni Mwenye kuwasamehe, ni Mwenye huruma kwao

    [120] Hakika Ibrāhīm alikuwa kiongozi katika mema, na alikuwa mtiifu mnyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu, haendi kombo na Uislamu, ni mwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu, si mwenye kumshirikisha

    [121] Na alikuwa ni mwenye kuzishukuru neema za Mwenyezi Mungu kwake. Mwenyezi Mungu Alimchagua kwa ujumbe Wake na Akamuongoza kwenye njia iliyolingana sawa, nayo ni Uislamu

    [122] Na tulimpa ulimwenguni neema nzuri ya kusifiwa na watu waliokuja nyuma yake, kufuatwa na kuwa na watoto wema. Na yeye, mbele ya Mwenyezi Mungu, huko Akhera, ni miongoni mwa watu wema wenye daraja za juu

    [123] Kisha tukakuletea wahyi, ewe Mtume, kwamba uifuate dini ya Uislamu kama alivyoifuata Ibrāhīm na kwamba ulingane juu yake na usiiyepuke, kwani Ibrāhīm hakuwa ni miongoni mwa wale wanaowashrikisha wengine pamoja na Mwenyezi Mungu

    [124] Mwenyezi Mungu Ameufanya utukuzaji wa siku ya Jumamosi, kwa kuitenga kwa kufanya ibada ndani yake, kwa Myahudi ambao walitafautiana na Nabii wao juu yake, na wakaiteua badala ya siku ya Ijumaa ambayo waliamrishwa waitukuze. Hakika Mola wako , ewe Mtume, ni Mwenye kuhukumu baina ya wale waliotafautiana na Nabii wao Siku ya Kiyama na kumlipa kila mmoja kwa yale anayofaa kuyapata

    [125] Lingania, ewe Mtume, wewe na aliyekufuata, kwenye Dini ya Mola wako na njia Yake iliyolingana sawa kwa kutumia hekima ambayo Mwenyezi Mungu alikuletea wahyi nayo ndani ya ya Qur’ani na Sunnah. Na uwazungumzie watu kwa njia inayolingana na wao, uwape nasaha kwa njia nzuri yenye kuwavutia kwenye kheri na kuwakimbiza wajiepushe na shari, na ujadiliane na wao kwa njia nzuri za kujadiliana za utaratibu na upole, kwani si juu yako isipokuwa ni kufikisha ujumbe, na ushafikisha. Ama kuwafanya waongoke, hilo ni juu ya Mwenyezi Mungu Peke Yake. Yeye Ndiye Anayemjua zaidi yule aliyepotea na akaiyepuka njia Yake, na Yeye Anawajua zaidi walioongoka

    [126] Na mkitaka kuwalipiza kisasi, enyi Waumini, wale waliowafanyia uadui, msiongeze zaidi ya vile walivyowafanya. Na mkisubiri, basi hilo ni bora kwenu nyinyi ulimwenguni, kwa kupewa ushindi, na kesho Akhera, kwa kupewa malipo makubwa

    [127] Na vumilia, ewe Mtume, kwa maudhi yanayokupata katika njia ya Mwenyezi Mungu mpaka ikujie faraji, na hakukuwa huku kuvumilia kwako isipokuwa ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kwani Yeye Ndiye mwenye kukusaidia na kukupa uthabiti, na usisikitike juu ya wale wanaoenda kinyume na wewe na wasiitikie ulinganizi wako, wala usiwe na usijitie dhiki za moyo kutokana na hila zao na vitimbi vyao, kwani hilo litawarudia wao wenyewe kwa shari na mateso

    [128] Kwa hakika Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, kwa taufiki Yake, msaada Wake, upaji nguvu Wake na nusura Yake Yuko pamoja na waliomcha kwa kuyafuata Aliyoyaamrisha na kuyaepuka Aliyoyakataza; na yuko pamoja na wale wanatenda wema, kwa kutekeleza faradhi Zake na kusimama kutimiza haki Zaka na kujilazimisha kumtii, kwa kuwapa msaada Wake, uongozi Wake na nusura Yake

    Safari ya Usiku

    Surah 17

    [1] Mwenyezi Mungu Anajisifu na kujitukuza kwa uweza Wake juu ya yasiyowezekana na yoyote isipokuwa Yeye, hapana Mola isipokuwa Yeye, hapana Mlezi isipokuwa Yeye. Yeye Ndiye ambaye Aliyempeleka mja Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, kipindi cha usiku, kwa mwili wake na roho yake, katika hali ya kuangaza na siyo ya kulala, kutoka msikiti wa Ḥarām Uliyoko Makkah, kwenda msikiti wa Aqṣā uliyoko Bayt al- Maqdis, ambao Mwenyezi Mungu Amezibariki sehemu zinazouzunguka kwa matunda, nafaka na vinginevyo, na Akaufanya ni mahali pa Manabii wengi, ili ajionee maajabu ya uweza wa Mwenyezi Mungu na dalili za upweke Wake. Hakika Mwenyezi Mungu, Aliyetakata na kutukuka, Ndiye Mwenye kuzisikia sauti zote, Ndiye Mwenye kukiona kila cha kuonekana, na Atampa kila mmoja anachofaa kupata duniani na Akhera

    [2] Na kama Mwenyezi Mungu Alivyomtukuza Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, kwa kumpeleka safari hiyo ya usiku, Alimtukuza Mūsā, amani imshukiye, kwa kumpa Taurati na Akaifanya ni yenye kuufafanua ukweli na kuwaongoza Wana wa Isrāīl na Akaifanya ni yenye kukusanya makatazo kwao ya kumfanya asiyekuwa Mwenyezi Mungu kuwa ni mtegemewa au ni muabudiwa wakawa wamtegemezea mambo yao

    [3] Enyi kizazi cha wale tuliowaokoa na tukawabeba pamoja na Nūḥ katika jahazi, msimshirikishe Mwenyezi Mungu katika kumuabudu, na kuweni ni wenye kushukuru neema Zake na ni wenye kumfuata Nūḥ, amani imshukiye, kwani yeye alikuwa ni mja mwenye kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa moyo wake, ulimi wake na viungo vyake

    [4] Na tuliwapasha habari Wana wa Isrāīl katika Taurati ambayo waliteremshiwa kwamba yeye hapana budi itatukia kutoka kwao uharibifu mara mbili katika Bayt al- Maqdis na sehemu zinazofuatia kwa kudhulumu, kuua Manabii, kufanya kiburi, kupita kiasi na kufanya uadui

    [5] Ukitukia kutoka kwenu uharibifu wa kwanza, tutawasaliti nyinyi na waja wetu wenye ushujaa na nguvu kali, watawashinda, watawaua na watawafukuza, hapo wazunguke kwenye nyumba zenu wakifanya uharibifu. Hiyo ilikuwa ni ahadi isiyokuwa na budi kutukia kwa kupatikana sababu zake kutoka kwenu

    [6] Kisha tukawarudishia ushindi, enyi wana wa Isrāīl, na kuwa juu ya maadui zenu waliowasaliti, na tukawazidishia riziki zenu na watoto wenu na tukawapa nguvu na tukawafanya muwe wengi wa idadi kuliko adui yenu. Hiyo ni kwa sababu ya wema wenu na unyenyekevu wenu kwa Mola wenu

    [7] Mkifanya matendo yenu na maneno yenu kuwa mazuri,basi mimejifanyia vizuri nyinyi wenyewe, kwa kuwa malipo ya hayo yatarudi kwenu; na mkifanya vibaya, basi mateso ya hayo ni yenye kuwarudia nyinyi. Na utakapofika wakati wa uharibifu wa pili, tutawasaliti maadui wenu mara nyingine, ili wawadhalilishe na wawashinde na idhihiri athari ya udhalilifu na utwevu kwenye nyuso zenu na wawaingilie kwenye Bayt al Maqdis waiharibu kama walivyoiharibu mara ya kwanza na wavunjevunje kila kilichoko chini ya mikono yao uvunjaji kamili

    [8] Inatarajiwa kuwa Mola wenu, enyi Wana wa Isrāīl, Atawarehemu baada ya kuwatesa, mkitubia na mkatengenea, na mkirudi kufanya uharibifu na maonevu, tutarudi kuwatesa na kuwadhili. Na tumeufanya moto wa Jahanamu, kwenu na kwa makafiri kwa jumla, ni gereza ambalo hakuna kutoka humo kabisa. Katika aya hii na ile kabla yake pana onyo kwa ummah huu dhidi ya kufanya maasia ili lisiwapate lile lililowapata Wana wa Isrāīl, basi mipango ya Mwenyezi Mungu ni mimoja, haina kubadilika wala kugeuka

    [9] Hii Qur’ani tuliyoiteremsha kwa mja wetu Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, inawaongoza watu kwenye njia nzuri kabisa nayo ni mila ya Kiislamu, na inawapa bishara njema Waumini, wanaofanya yale ambayo Mwenyezi Mungu Amewaamrisha kwayo na wanaokomeka na yale ambayo Amewakataza nayo, kwamba watakuwa na malipo makubwa

    [10] na kwamba wale ambao hawaamini Nyumba ya Akhera na malipo yaliyoko huko, tumewatayarishia adhabu yenye kuumiza ndani ya Moto

    [11] Na binadamu wakati mwingine hujiapiza mabaya nafsi yake au mtoto wake au mali yake awapo na hasira kama vile anavyoomba mema. Hii ni kwa sababu ya ujinga wa mwanadamu na pupa lake. Na miongoni mwa rehema ya Mwenyezi Mungu kwake ni kwamba Yeye Anayakubali maombi yake mema na sio mabaya na kwamba Yeye anajua kuwa yeye hakukusudia kutaka hilo. Hakika binadamu ana tabia ya kuwa na pupa sana

    [12] Na tumefanya usiku na mchana kuwa ni alama mbili zenye kuonyesha upweke wetu na uweza wetu, tukaifuta alama ya usiku, nayo ni mwezi, na tukaifanya alama ya mchana, nayo ni jua, ni yenye mwangaza, ili binadamu apate kuona kwenye mwangaza wa mchana namna ya kupekesha mambo ya maisha yake na ili aingie kwenye utulivu na mapumziko wakati wa usiku, na ili watu wajue, kwa kupishana mchana na usiku, idadi ya miaka na hesabu ya miezi na siku, wakaweka juu ya hiyo mipango wanayoitaka ya maslahi yao. Na kila kitu tumekifafanua ufafanuzi wa kutosha

    [13] Na kila binadamu Mwenyezi Mungu Anayajaalia yale anayoyatenda, yawe mema au maovu, ni yenye kuwa na yeye wakati wote, hatahisabiwa kwa matendo ya mtu mwingine, wala mwingine hatahesabiwa kwa matendo yake yeye. Na Mwenyezi Mungu Atamtolea , Siku ya Kiyama, kitabu kilichoandikwa ndani yake yale aliyoyatenda; atakiona kimefunguliwa mbele yake

    [14] Ataambiwa, «Soma kitabu cha matendo yako.» Hapo atasoma, hata kama hakuwa akijua kusoma ulimwenguni, «Leo nafsi yako itakutosheleza kuwa ni yenye kukuhesabia matendo yako, upate kujua malipo yake.» Huu ni miongoni mwa uadilifu na uchungaji haki mkubwa kabisa kwamba mja aambiwe, ‘jihesabu nafsi yako, kwani inatosha kuwa ni yenye kukuhesabu. ’

    [15] Mwenye kuongoka akafuata njia ya haki, basi malipo mema yake yatamrudia yeye peke yake; na mwenye kupotoka akafuata njia ya ubatilifu, basi mateso ya kufanya hivyo yatamrudia yeye peke yake; na hakuna nafsi yoyote iliyofanya dhambi itabeba makosa ya nafsi nyingine iliyofanya dhambi. Na Mwenyezi Mungu Hatamuadhibu yoyote isipokuwa baada ya kumsimamishia hoja kwa kutuma Mitume na kuteremsha Vitabu

    [16] Na tukitaka kuwaangamiza watu wa mji kwa udhalimu wao, tunawaamrisha wenye gogi wao wamtii Mwenyezi Mungu, wampwekeshe na wawaamini Mitume Wake, na wasokuwa wao wako nyuma yao kwa kuwafuata, wakaasi amri ya Mola wao na wakawakanusha Mitume Wake, hapo likapasa juu yao neno la adhabu ambalo hakuna namna ya kurudishwa, na tukawamaliza kwa maangamivu yaliyotimia

    [17] Na ni wengi tuliowaangamiza miongoni mwa watu waliokanusha Mitume wao baada ya Nabii wa Mwenyezi Mungu, Nūḥ. Na inatosha kwamba Mola wako, ewe Mtume, ni Mjuzi wa matendo yote ya waja Wake, hakifichamani Kwake chochote chenye kufichamana

    [18] Yoyote ambaye matakwa yake ni ulimwengu huu wa sasa na akaushughulikia huo peke yake, asiiamini Akhera na asifanye matendo ya kumfaa huko, Mwenyezi Mungu Atamharakishia, hapa ulimwenguni, Anayoyataka Mwenyezi Mungu na kuyapendelea miongoni mwa yale aliyoyaandika kwenye Ubao Uliohifadhiwa (Al- Lawḥ Al-Mahfūḍ) kisha Mwenyezi Mungu Atamjaalia huko Akhera moto wa Jahanamu, atauingia akiwa ni mwenye kulaumiwa, ni mwenye kufukuzwa kwenye rehema Yake Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka. Hiyo ni kwa sababu ya kutaka kwake ulimwengu na kujishughulisha nao bila ya Akhera

    [19] Na yoyote aliyekusudia kwa matendo yake mema kupata malipo ya Nyumba ya Akhera yenye kusalia na akajishughulisha nayo kwa kumtii Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, na hali yeye ni mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu na kuamini thawabu Zake na malipo Yake makubwa, basi hao matendo yao ni yenye kukubaliwa ni yenye kuhifadhiwa kwa ajili yao mbele ya Mola wao na watapata malipo yake

    [20] Kila kundi, miongoni mwa wenye kuufanyia kazi ulimwengu wenye kumalizika na wenye kuifanyia kazi Akhera yenye kusalia, tunalipatia riziki yetu: tunawaruzuku Wauminiu na makafiri ulimwenguni. Kwani riziki inatokana na vipawa vya Mola wako kwa wema Wake; na vipawa vya Mola wako hanyimwi mtu yoyote, awe ni Muumini au ni kafiri

    [21] Taamali, ewe Mtume, vile Mwenyezi Mungu Alivyowatukuza baadhi ya watu juu ya wengine ulimwenguni kiutajiri na kimatendo. Na Akhera in daraja kubwa zaidi kwa Waumini na ina matukuzo makubwa zaidi

    [22] Usimfanye, ewe mwanadamu, pamoja na Mwenyezi Mungu mshirika yoyote katika ibada Yake, kwani ukifanya hivyo utarudi uwe ni mwenye kutukanika na kuhizika

    [23] Na Mola wako, ewe mwanadamu, Ameamrisha na kulazimisha na kupasisha Apwekeshwe, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, kwa kuabudiwa Peke Yake, na Ameamrisha kuwafanyia wema baba na mama, hasa wakiwa katika hali ya ukongwe: usione dhiki wala uzito kwa jambo lolote ulionalo kwa mmoja wao au kwa wao wawili, wala usiwasikizishe neno baya, hata kama ni sauti ya kuonesha kutoridhika ambayo ni neno baya la daraja ya chini kabisa, wala usiwafanyie tendo baya, lakini kuwa mpole kwao na uwaambie wao daima maneno mapesi yenye ulaini

    [24] Na uwe, kwa mamako na babako, mdhalilifu na mnyenyekevu kwa kuwahurumia, na umuombe Mola wako awarehemu kwa rehema Zake kunjufu wakiwa hai na wakiwa wamekufa, kama walivyovumilia juu ya kukulea ulipokuwa mdogo usiokuwa na uwezo wala nguvu

    [25] Mola wenu, enyi watu, ni Mjuzi zaidi wa mazuri na mabaya yaliyomo ndani ya nyoyo zenu. Iwapo matakwa yenu na makusudio yenu ni kumridhisha Mwenyezi Mungu na kujikaribisha Kwake, basi Yeye, kutakata na sifa mbaya ni Kwake, kwa wenye kurejea Kwake katika nyakati zote ni Mwingi wa kusamehe. Basi yoyote yule ambaye Mwenyezi Mungu Amejua kwamba hakuna katika moyo wake isipokuwa ni kurejea Kwake na kumpenda, Yeye Atamsamehe na Atamghufiria yatakayotukia miongoni mwa madhambi madogo yanayolingana na tabia za kibinadamu

    [26] Na umfanyie wema kila mwenye ukaribu wa ujamaa na wewe, na umpe haki yake ya wema na hisani, na umpe masikini mwenye uhitaji na msafiri aliyeepukana na watu wake na mali yake, na usitumie mali yako katika njia isiyokuwa ya kumtii Mwenyezi Mungu au kwa njia ya kupita kiasi na ufujaji

    [27] Hakika wale wenye kupita kiasi katika matumizi na wenye kutoa mali yao katika kumuasi Mwenyezi Mungu wanafanana na Mashetani kwenye uovu, uharibifu na maasia, na Shetani ni mwingi wa kukufuru, ni mkanushaji sana neema za Mola wake

    [28] Na ukiwaepuka hawa ambao uliamrishwa uwape, kwa kuwa hakuna kitu cha kuwapa, kwa kungojea riziki kutoka kwa Mola wako, basi waambie maneno laini ya upole kama vile kuwaombea dua awatajirishe na awape riziki kunjufu, na uwaahidi kwamba Mwenyezi Mungu Akiyafanya mambo ya riziki kuwa mapesi kwa wema Wake basi wewe utawapatia nao

    [29] Wala usiuzuie mkono wako kutumia katika njia njema, ukaidhiki nafsi yako na watu wako na wahitaji, na wala usipite kiasi katika matumizi ukatoa zaidi ya uwezo wako, kwani ukifanya hivyo utaketi hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa, kwani watu watakulaumu na watakutukana, na ni mwenye kujuta juu ya ufujaji wako na mali yako kupotea

    [30] Hakika Mola wako nawakunjulia riziki baadhi ya watu na Anawabania wengine kulingana na ujuzi Wake na hekima Yake, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake. Yeye Ndiye Mwenye kuyaona mambo ya ndani ya waja Wake, hakuna chochote katika hali zao kilicho nje ya ujuzi Wake

    [31] Na mkijua kwamba riziki iko kwenye mkono wa Mwenyezi Mungu, kutkata na sifa za upungufu ni Kwake, basi msiwaue watoto wenu kwa kuchelea umasikini, kwani Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Mwenye kuwaruzuku waja Wake, Anawruzuku wana kama Anavyowaruzuku wazazi. Hakika kuua watoto ni dhambi kubwa

    [32] Wala msikaribie uzinifu na mambo yanayopelekea huko ili msiingie ndani yake, hakika hilo ni tendo baya sana, na njia mbaya zaidi ni njia ya tendo hilo

    [33] Wala msiiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu Ameharamisha kuuawa, isipokuwa kwa haki ya kisharia, kama kisasi au kumpiga mawe mzinifu aliyeingia kwenye hifadhi ya ndoa au kumuua aliyeritadi. Na mwenye kuuawa pasi na haki ya kisheria, basi tumempa msimamizi wa mambo yake , awe ni mrithi au ni hakimu, uwezo wa kutaka muuaji auawe au kutaka dia. Na haifai kwa msimamizi wa mambo ya aliouawa kupita mpaka wa Mwenyezi Mungu katika kuchukua kisasi, kama vile kuua watu wawili au wengi kwa mmoja au kumua muuaji kwa njia ya kumtesa. Mwenyezi Mungu ni Mwenye kumsaidia msimamizi wa aliyeuawa juu ya aliyeua mpaka aweze kumuua kwa njia ya kisasi

    [34] Wala msitumie mali ya watoto waliofiliwa na wazazi wao nao wako chini ya miaka ya kubaleghe na wakawa wako chini ya usimamizi wenu, isipokuwa kwa njia ambayo ni nzuri kwao, nayo ni kuyazalisha na kuyakuza, mpaka afikie mtoto yatima miaka ya kubaleghe na utumiaji mzuri wa mali. Na timizeni utekelezaji wa kila ahadi mliyojilazimisha nayo, kwani Mwenyezi Mungu Atamuuliza mwenye kuweka ahadi kuhusu hiyo ahadi Siku ya Kiyama, Atamlipa akiitimiza na kuitekeleza na Atamtesa akienda kinyume nayo

    [35] Na timizeni kipimo wala msikipunguze mnapowapimia wasiokuwa nyinyi, na mfanye mizani ya sawa, kwani kufanya uadilifu katika upimaji wa vibaba na mizani ni bora kwenu nyinyi ulimwenguni na kuna mwisho mwema mbele ya Mwenyezi Mungu kesho Akhera

    [36] Na usiyafuate, ewe binadamu, usiyoyajua, lakini hakikisha na uthibitishe. Hakika ya biadamu ni mwenye kuulizwa juu ya yale ambayo alitumia masikizi yake, maangalizi yake na moyo wake kuyafikia. Basi akivitumia vitu hivyo katika wema atapata malipo mema na akivitumia katika uovu atapata mateso

    [37] Na usitembee ardhini kwa kujigamba na kujivuna, kwani wewe hutaipasua ardhi kwa kutembea juu yake kwa namna hiyo na hutaifikia milima katika urefu kwa kujigamba kwako, kujivuna kwako na kutakabari kwako

    [38] Yote yaliyotangulia kutajwa, ya maamrisho na makatazo, Mwenyezi Mungu Anayachukia mabaya yake na hayaridhii kwa waja wake

    [39] Hayo tuliyoyaeleza na kuyafafanua kati ya hizi hukumu tukufu za kuamrisha matendo mema na kukataza tabia duni, ni miongoni mwa yale tuliyokutumia wahyi nayo. Na usimfanye, ewe binadamu, pamoja na Mwenyezi Mungu yoyote kuwa ni mshirika Wake katika kumuabudu, ukaja kutiwa ndani ya moto wa Jahanamu, hali ukilaumiwa na nfsi yako na watu, na ukawa ni mwenye kufukuzwa na kuepushwa na kila kheri

    [40] Je, kwani Amewahusu nyinyi Mola wenu, enyi washirikina, kwa kuwapa watoto wa kiume na Yeye Akajichukulia kutokana na Malaika watoto wa kike? Neno lenu hili ni upeo wa ubaya na linachukiza sana, halinasibiani na Mwenyezi Mungu, kuepukana na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake

    [41] Hakika tumeelza katika hii Qur’ani aina mbalimbali za hukumu, mifano na mawaidha, ili watu wapate kuwaidhika na kuzingatia yanayowafaa wayachukue na yenye kuwadhuru wayaache. Na haya maelezo na ufafanuzi hayawaongezei madhalimu isipokuwa kuwa mbali na haki na kughafilika kutia mambo akilini na kuzingatia

    [42] Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina, «Lau kulikuwa na waungu wengine pamoja na Mwenyezi Mungu, basi wangalitafuta waungu hao njia ya kushindana na Mwenyezi Mungu Mwenye 'Arshi iliyo kubwa.»

    [43] Mwenyezi Mungu Ameepukana na kutakata na hayo wanayoyasema washirikina, na Ametukuka utukufu mkubwa

    [44] Zinamtakasa Yeye, kutakata ni Kwake, mbingu saba na ardhi na viumbe wote waliyo humo. Na kila kitu kilichoko katika ulimwengu huu kinamuepusha Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na sifa za upungufu, maepusho yanayofungamana na kumsifu na kumshukuru, kutakata ni Kwake, lakini nyinyi,enyi watu, hamtambui hilo. Kwa kweli, Yeye ni Mpole kwa waja Wake, hawaharakishii adhabu wanaomuasi, ni Mwingi wa msamaha kwao

    [45] Na usomapo Qur’ani wakaisikia hawa washirikina, tunaweka baina yako wewe na hawa wasioiamini Akhera pazia yenye kusitiri ili kuziziba akili zao wasiifahamu Qur’ani, ikiwa ni mateso kwao kwa ukafiri wao na kukanusha kwao

    [46] Na tumeweka juu ya nyoyo za washirikina vifiniko, wasipate kuifahamu Qur’ani, na tumejaalia uziwi ndani ya mashikio yao, wasipate kuisikia. Na umtajapo Mola wao katika Qur’ani uwalinganiapo kwenye kumpwekesha Yeye na ukatazapo kushirikishwa, wao hurudi kinyumenyume kwa kuyakimbia maneno yako, kwa kutakabari na kujiona kuwa ni wakubwa mno wa kutofaa kumpwekesha Mwenyezi Mungu, Peke Yake, katika kumuabudu

    [47] Sisi tunayajua zaidi yale wanayoyasikiliza viongozi wa Kikureshi pale wakusikilizapo na hali nia zao ni mbovu. Kusikiliza kwao si kwa ajili ya kutaka kuogoka na kuikubali haki. Na sisi tunajua kule kunong’onezana kwao wanaposema, «Hamumfuati isipopkuwa ni mwanamume aliyerogwa na akili yake ikabadilika.»

    [48] Fikiri, ewe Mtume, kwa kulionea ajabu neno lao kwamba Muhammad ni mchawi mshairi mwenye wazimu. Hivyo basi wamekiuka mpaka na wamepotoka na hawakuongokea njia ya haki na usawa

    [49] Wasirirkina walisema wakikanusha kwamba wataumbwa umbo jipya baada ya mifupa yao kuoza na kuwa mbalimbali, «Je, sisi tutafufuliwa ufufuzi mpya Siku ya Kiyama?»

    [50] Waambie, ewe Mtume, kwa njia ya kuwafanya washindwe, «Kuweni na nguvu na ugumu kama mawe au chuma mkiweza hilo

    [51] Au kuweni umbo lolote kubwa ambalo akili zenu zaliona kuwa liko mbali na uhakika.» Na watasema kwa kukanusha, «Ni nani atakayeturudisha kwenye uhai baada ya kufa?» Waambie, «Atakayewarudisha na kuwarejesha ni Mwenyezi Mungu Aliyewaumba kutoka kwenye hali ya kutokuwako mara ya kwanza.» Na wasikiapo majibu haya watatikisa vichwa vyao kwa njia ya shere, huku wakiona ajabu na watasema, wakiliona jambo hilo kuwa ni mbali kukubalika, «Ufufuzi huu utatukia lini?» Sema, «Ni lipi linalowajulisha kwamba Ufufuzi huu, mnaoukanusha na mnaouona kuwa uko mbali, huenda ukawa ni wenye kutukia kipindi cha karibu?»

    [52] Siku Atakapowaita Muumba wenu mtoke kwenye makaburi yenu na mkaitika amri ya Mwenyezi Munguna na mkaiyandama, na shukrani ni Zake kwa kila namna, na mkadhani, kwa kituko cha Siku ya Kiyama na kwa kipindi kirefu cha kukaa kwenu Akhera, kwamba nyinyi hamkukaa duniani isipokuwa muda mchache

    [53] Na waambie waja wangu Waumini waseme, katika mazungumzo yao na kushauriana kwao wao kwa wao, maneno mazuri, kwani wao wakitofanya hivyo Shetani atatia ugomvi, uharibifu na utesi baina yao. Hakika Shetani kwa binadamu ni adui aliyeudhihirisha uadui

    [54] Mola wenu Anawajua nyinyi zaidi, enyi watu, Akitaka Atawarehemu Awaafikie kwenye Imani au Akitaka atawafisha kwenye ukafiri kisha Awaadhibu. Na hatukukutumiliza, ewe Mtume, uwe ni muwakilishi juu yao, unayapanga mambo yao na unawalipa kwa matendo yao, jukumu lako ni kuyafikisha uliyotumilizwa kwayo na kuieleza njia iliyolingana sawa

    [55] Na Mola wako, ewe Mtume, Anawajua zaidi walioko mbinguni na ardhini, na tumewafadhilisha baadhi ya Mitume juu ya wengine kwa matukufu, wingi wa wafuasi na kuwateremshia Vitabu, na Dawud, amani imshukiye, tumempa Zaburi

    [56] Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina wa Makkah, «Hawa masanamu mnaowaita wawaondolee shida hawawezi hilo wala hawawezi kuiyepusha kwenu nyinyi kuipeleka kwa wengine, na pia hawawezi kuigeuza kutoka namna ilivyo kuifanya namna nyingine, Mwenye kuweza hilo ni Mwenyezi Mungu Peke Yake.» Aya hii inakusanya kila anayeombwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, miongoni mwa Manabii, watu wema na wasiokuwa hao, kwa tamko la istighāthah (kutaka uokozi) au du'a’ (maombi) au mfano wake, kwani hapana mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu

    [57] Hao ambao washirikina wanawaomba, miongoni mwa Manabii, watu wema na Malaika, wao wenyewe wanashindana kujiweka karibu na Mola wao kwa matendo mema wanayoyaweza, wanatarajia rehema Yake na wanaogopa adhabu Yake. Hakika adhabu ya Mola wako ndiyo ambayo inatakikana kwa waja wawe na hadhari nayo na waiogope

    [58] Na Mwenyezi Mungu Anawaonya wanaokufuru kwamba hakuna mji wowote wenye kukufuru na kukanusha Mitume isipokuwa mateso Yake yataushukia kwa maangamivu hapa duniani kabla ya Siku ya Kiyama au kwa adhabu kali juu ya watu wake. Hayo ni maandishi Aliyoyaandika Mwenyezi Mungu na hukumu Aliyoipitisha, hapana budi kujiri, nayo imeandikwa kwenye Al-Lawḥ Al-Mahfūḍ (Ubao Uliohifadhiwa)

    [59] Hakuna kilichotuzuia kuteremsha miujiza ambayo washirikina waliitaka isipokuwa ni kwamba ummah waliowatangulia waliikanusha, Mwenyezi Mungu Aliwajibu kwa waliyotaka wakakanusha na wakaangamia. Na tuliwapa Thamūd, nao ni watu wa Ṣāliḥ, miujiza iliyo wazi, nayo ni ngamia, wakaikanusha na tukawaangamiza. Na huku kutuma kwetu Mitume wakiwa na alama, mazingatio na miujiza tuliyoipitisha kwenye mikono yao, hakukuwa isipokuwa ni kuwatisha waja wapate kuzingatia na wakumbuke

    [60] Kumbuka, ewe Mtume, pindi tulipokwambia kwamba Mola wako Amewazunguka watu kwa ujuzi na uweza. Na hatukuijaalia ndoto tuliyokuonyesha waziwazi usiku wa isrā’ (kwenda Bayt al- Maqdis) na mi'rāj (kupaa kwenda mbinguni) miongoni mwa maajabu ya viumbe isipokuwa ni kuwatahini watu. Na tunawatisha washirikina kwa aina mbalimbali za adhabu na miujiza, lakini kuwatisha huko hakuwaongezei isipokuwa ni kuendelea zaidi kwenye ukafiri na upotevu

    [61] Na ukumbuke neno tulilowaambia Malaika wamsujudie Ādam kwa kumwamkia na kumuhishimu, wakamsujudia wote isipokuwa Iblisi, alifanya kiburi na akakataa kusujudu, na huku akisema kwa njia ya kupinga na kujiona, «Je, nimsujudie huyu dhaifu aliyeumbwa kwa udongo?»

    [62] Iblisi akasema akionesha ujasiri wake na ukafiri kwa Mwenyezi Mungu, «Unamuona kiumbe huyu uliyemfadhilisha juu yangu? Ukinibakisha hai mpaka Siku ya Kiyama nitawatawala wale wanaozalikana na yeye kwa kuwapoteza na kuwaharibu isipokuwa wale waliotakaswa katika Imani, nao ni wachache.»

    [63] Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Akasema Akimuonya Iblisi na wafuasi wake, «Enda! Yoyote mwenye kukufuata miongoni mwa kizazi cha Ādam, basi mateso yako na mateso yao ndani ya moto wa Jahanamu ni mengi

    [64] «Na uwalaghai wale unaoweza kuwalaghai miongoni mwao kwa kuwaita kuniasi, na uwakusanyie askari zako unaowaweza, kati ya kila aliye juu ya kipando na anayetembea kwa miguu, na ujishirikishe nao katika mali yao wanayoyachuma kwa njia za haramu, na ujishirikishe nao katika watoto wao kwa kuwapambia uzinifu na uasi na kwenda kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu mpaka uenee uchafu na uharibifu, na uwaahidi wafuasi wako, miongoni mwa wale wanaozalikana na Ādam, ahadi za urongo, na kila ahadi za Shetani ni ubatilifu na udanganyifu

    [65] «Hakika waja wangu Waumini waliyotakaswa ambao walinitii, wewe huna uwezo wa kuwapoteza.» Na inatosha kuwa Mola wako , ewe Mtume, kuwa Ndiye Mwenye kuwalinda na kuwahifadhi Waumini kutokana na vitimbi vya Shetani na udanganyifu wake

    [66] Mola wenu, enyi watu, Ndiye Anayewaendeshea vyombo vya kusafiria baharini ili mtafute riziki ya Mwenyezi Mungu katika safari zenu na biashara zenu. Hakika Mwenyezi Mungu , kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, ni Mwingi wa huruma kwa waja Wake

    [67] Na mkipatikana na shida baharini mkakaribia kuzama na kuangamia, wanapotea kwenye akili zenu wale waungu ambao mlikuwa mkiwaabudu, na mkamkumbuka Mwenyezi Mungu Muweza, Peke Yake, Awasaidie na Awaokoe, hapo mnamtakasia katika kutaka msaada na uokzi, na Yeye Anawasaidia na Anawaokoa. Anapowaokoa kwa kuwaegesha kwenye nchi kavu, mnageuka mkaacha Imani, kumtakasia Mwenyezi Mungu na matendo mema. Na huu ni katika ujinga wa binadamu na ukafirir wake, kwani binadamu ni mkanushaji sana neema za Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka

    [68] Je, mumeghafilika, enyi watu, na adhabu ya Mwenyezi Mungu, ndipo mkajiaminisha kwamba ardhi haitawaporomokea ikawadidimiza au kwamba Mwenyezi Mungu Hatawanyesheza mvua ya mawe itokayo juu iwaue kisha msipate yoyote wa kuwalinda na adhabu Yake

    [69] Au mumejiaminisha, enyi watu, kwamba Mola wenu, na hali nyinyi mumemkanusha, hatawarudisha baharini mara nyingine kisha akawaletea kimbunga kikali chenye kuvunjavunja kila kitu kinachokifikia, kikaja kikawazamisha kwa ukanushaji wenu, kisha msipate kitu chochote cha madai au malalamiko juu yetu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu kitu chochote hata wizani wa chungu mdogo

    [70] Kwa hakika tumewatukuza watu wa kizazi cha Ādam kwa akili na kuwapelekea Mitume, na tukawadhalilishia vilivyoko ulimwenguni vyote: tukawadhalilishia wanyama barani wa kuwapanda na vyombo baharini vya kuwabeba, tukawaruzuku vilaji na vinywaji vizuri na tukawapa daraja kubwa juu ya viumbe wengi

    [71] Na kumbuka, ewe Mtume, Siku ya Kufufuliwa, kwa njia ya kutoa bishara na kuogopesha, pindi Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na ktukuka, Atakapoliita kila kundi la watu pamoja na kiongozi wao ambaye walikuwa wakimfuata ulimwenguni. Basi aliyekuwa mwema kati yao , na akapewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, hawa watasoma kitabu cha mema yao wakiwa katika hali ya kufurahika na kuterema, na kamwe hawatapunguziwa chochote katika malipo ya matendo yao mazuri, hata kama ni kadiri ya uzi unaokuwa kwenye mpasuko wa koko ya tende

    [72] Na aliyekuwa kipofu wa moyo, katika ulimwengu huu, wa kutoziona dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu, asiyaamini yale aliyokuja nayo Mtume Muhammad, rehema na amani zimshukiye, basi yeye, Siku ya Kiyama, atakuwa kipofu zaidi wa kutoiona njia ya Peponi na atapotea zaidi njia ya uongofu na usawa

    [73] Na kwa hakika washirikina walikaribia kukuepusha, ewe Mtume, na Qur’ani Aliyokuteremshia Mwenyezi Mungu ili utuzulie isiyokuwa hiyo tuliyokuletea wahyi nayo. Na lau ulifanya walivyotaka, wangalikufanya ni kipenzi msafiwa

    [74] Na lau si sisi kukuimarisha kwenye haki na kukuhifadhi usikubaliane nao, ungalikaribia kuelemea kwao kidogo katika yale waliyokushauri kwa nguvu za udanganyifu wao na wingi wa hila zao na kuwa na hamu kwako waongoke

    [75] Na lau ulielemea, ewe Mtume, upande wa hawa washirikina maelemeo madogo katika yale waliyotaka kwako, basi tungalikuonjesha mara mbili zaidi ya adhabu ya duniani na mara mbili zaidi ya adhabu ya baada ya kufa kesho Akhera, hivyo ni kwa ajili ya kutimia neema ya Mwenyezi Mungu kwako na ukamilifu wa kumjua Mola wako, kisha hutampata yoyote mwenye kukuepushia adhabu yetu

    [76] Na makafiri walikaribia kukutoa Makkah kwa kukukera, na lau walikutoa huko hawangalikaa huko baada yako isipokuwa muda mchache, hadi iwashukie adhabu ya ulimwenguni

    [77] Huo ndio mwendo uliowekwa na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, katika kuwaangamiza watu wanaomtoa Mtume wao kutoka kwao, na hutapata mabidiliko kwenye mwendo wetu, kwani hatuendi kinyume na ahadi yetu

    [78] Simamisha Swala itimie kuanzia kipindi cha kupinduka jua wakati wa mchana mpaka kipindi cha usiku. Inaingia hapa Swala ya Adhuhuri, Alasiri, Magharibi na Isha. Na simamisha Swala ya Alfajiri na urefushe kisomo chake, kwani Swala ya Alfajiri inahudhuriwa na Malaika wa usiku na Malaika wa mchana

    [79] Na inuka, ewe Nabii, kutoka kwenye usingizi sehemu ya usiku, usome Qur’ani katika Swala ya usiku, ipate kuwa, hiyo Swala ya usiku, ni nyongeza kwako katika utukufu wa cheo na kupandishiwa daraja. Huenda Mwenyezi Mungu Akakuleta uwe ni mwenye kuwashufaia watu Siku ya Kiyama, ili Mwenyezi Mungu Awarehemu kwa kuwaondolea waliokuwa nayo, na usimame kisimamo ambacho watakushukuru kwacho wa mwanzo na wa mwisho

    [80] Na useme, «Mola wangu! Nitia matio mazuri katika jambo lililo lema kwangu na unitoe matoko mazuri kwenye mambo yaliyo mabaya kwangu, na unipatie hoja thabiti kutoka kwako yenye kuniokoa na wote wanaoenda kinyume na mimi.»

    [81] Na useme, ewe Mtume, kuwaambia washirikina, «Uislamu umekuja na ushirikina umeondoka. Kwani ubatilifu hauna kusalia wala kujikita, na ukweli ndio wenye kuimarika na kusalia ambao hauondoki.»

    [82] Na tunateremsha miongoni mwa aya za Qur’ani yanayopoza magonjwa ya nyoyo kama shaka , unafiki na ujinga, na yanayopoza miili kwa kujizungua nayo, na yanayokuza Imani ambayo ni sababu ya kufaulu kupata rehema ya Mwenyezi Mungu. Na hii Qur’ani haiwaongezei makafiri wanapoisikia isipokua ukafiri na upotevu, kwa kuikanusha kwao na kutoiamini

    [83] Na tunapompa mwanadamu, vile alivyo, neema ya mali na afya na mfano wa hizo, anageuka na kujiweka mbali na kumtii Mwenyezi Mungu, na akipatikana na shida ya ufukara au ugonjwa huwa ni mwenye kukata tamaa, kwa kuwa yeye haamini kuwa atapata nyongeza njema za Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, isipokuwa yule ambaye Mwenyezi Mungu Amemuhifadhi katika hali yake ya raha na ya shida

    [84] Sema, ewe Mtume, kuwaambia watu, «Kila mmoja miongoni mwenu anatenda kulingana na hali zinazonasibiana na yeye , na Mola wenu ni Mjuzi zaidi wa yule aliyeongoka zaidi njia ya haki.»

    [85] Na makafiri wanakuuliza juu ya uhakika wa roho kwa njia ya ushindani, basi wajibu kwamba uhakika wa roho na hali zake ni katika mambo ambayo Mwenyezi Mungu Ameufanya ujuzi wake uweko Kwake. Na hamukupewa ujuzi, nyinyi na watu wote, isipokuwa kitu kichache

    [86] Na lau tulitaka kuifuta Qur’ani moyoni mwake, tungaliliweza hilo, na hungalimpata mwenye kukuhami ambaye atatuzuia kufanya hivyo au akurudishie Qur’ani

    [87] Lakini Mwenyezi Mungu Alikurehemu, Akaithibitisha moyoni mwako, hakika wema Wake juu yako ni mkubwa. Yeye Amekupa hii Qur’ani tukufu, Al-Maqām al-Maḥmūd (Kisimamo Kishukuriwacho) na mengineyo miongoni mwa yale ambayo Hakumpa yoyote katika viumbe

    [88] Sema, «Lau wataafikiana majini na binadamu kujaribu kuleta mfano wa hii Qur’ani yenye kuelemea, hawataweza kuileta, hata kama watashirikiana na kusaidiana kufanya hivyo.»

    [89] Na tumewafafanulia watu katika hii Qur’ani kila aina ya mfano unaopasa kuzingatiwa, kwa njia ya kuwasimamishia hoja, ili waifuate na waitumie, lakini wengi wa watu walikataa isipokuwa ni kuipinga haki na kuzikanusha hoja za Mwenyezi Mungu na dalili Zake

    [90] Na Qur’ani ilipowaelemea washirikina na ikawashinda, waliingia kutaka miujiza kulingana na mapendeleo yao wakasema, «Hatutakuamini, ewe Muhammad, na hatutafanya vile unavyosema mpaka utupasulie kwenye ardhi ya Makkah chemchemu ya maji yenye kupita

    [91] «Au uwe na shamba lenye aina za mitende na mizabibu, na uifanye mito ni yenye kupita kati yake kwa wingi

    [92] «Au uiangushe mbingu juu yetu iwe vipande-vipande kama ulivyodai, au utuletee Mwenyezi Mungu na Malaika Wake tuwaone wametukabili waziwazi

    [93] «Au uwe na nyumba ya dhahabu, au upande daraja za kukupaisha mbinguni, na hatutaamini kupaa kwako mpaka urudi ukiwa na kitabu kitokacho kwa Mwenyezi Mungu kilichofunguliwa tusome ndani yake kwamba wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kikweli.» Sema, ewe Mtume, kwa kushangaa juu ya ushindani wa makafiri hawa, «Kutakata na sifa za upungufu ni kwa Mola wangu! Kwani mimi ni nani, isipokuwa ni mja miongoni mwa waja Wake mwenye kufikisha ujumbe Wake? Basi vipi mimi nitaweza kuyafanya mnayoyataka?»

    [94] Na hakuna kilichowazuia makafiri kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na kuwatii, pindi ulipowajia wao ufafanuzi wa kutosha kutoka kwa Mwenyezi Mungu, isipokuwa ni kule kusema kwao kwa ujinga na kwa njia ya kukanusha, «Je, kwani Mwenyezi Mungu Ametumiliza Mtume miongoni mwa jinsi ya binadamu?»

    [95] Waambie, ewe Muhammad, ukiwarudi washirikina kule kukanusha kwao kuwa Mtume ni miongoni mwa wanadamu, «Lau juu ya hii ardhi kulikuwa na Malaika wanatembea kwa kujituliza, tungaliwapelekea mtume miongoni mwa jinsi yao,» lakini watu wa ardhi ni wanadamu, basi mtume wa kupelekewa inatakiwa awe ni miongoni mwa jinsi yao, ili iwezekane kwao kuzungumza naye na kufahamu maneno yake

    [96] Waambie, «Inatosha kuwa Mwenyezi Mungu ni shahidi baina yangu mimi na nyinyi juu ya ukweli wangu na uhakika wa unabii wangu. Hakika Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, ni Mtambuzi wa hali za waja Wake ni Muoni wa matendo yao, na Atawalipa kwa hayo.»

    [97] Na yoyote yule ambaye Mwenyezi Mungu Anamuongoza ndiye mwenye kuongoka kwenye haki, na yoyote yule ambaye Yeye Anampoteza, Akamdhili na Akamuachia yeye na nafsi yake basi huyo hakuna mwenye kumuongoza badala ya Mwenyezi Mungu. Hawa wapotevu Mwenyezi Mungu Atawafufua Siku ya Kiyama na Awakusanye kwa nyuso zao hali wakiwa hawaoni wala hawatamki wala hawasikii. Mwisho wao ni moto wa Jahanamu wenye kuwaka, kila kutuliapo kuwaka kwake na kuzimika mroromo wake, tunawazidishia moto wenye kuwaka na kuroroma

    [98] Adhabu hii iliyosifiwa ni mateso kwa washirikina kwa sababu ya kukanausha kwao aya za Mwenyezi Mungu na hoja Zake, kukanusha kwao Mitume Wake waliowaita kumuabudu Yeye na kule kusema kwao kwa njia ya kukataa, waamrishwapo kuamini kuwa kuna Ufufuzi, «Tutakapokufa na tukawa mifupa iliyochakaa na vipande vilivyotengeka mbalimbali, je tutafufuliwa baada yake hali ya kuwa ni viumbe vipya?»

    [99] Je, kwani wameghafilika hawa washirikina, wasiangalie na kujuwa kwamba Mwenyezi Mungu, Aliyeumba mbingu na ardhi na viumbe vilivyomo ndani yake bila ya mfano uliotangulia, ni muweza wa kuumba mfano wao baada ya kumalizika kwao? Mwenyezi Mungu Amewaekea washirikina hawa wakati maalumu wa kufa kwao na kuadhibiwa, hapana shaka wakati huo utawafikia. Na pamoja na uwazi wa haki na dalili Zake walikataa washirikina isipokuwa ni kuikanusha Dini ya Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka

    [100] Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Lau nyinyi mnamiliki hazina za rehema ya Mola wangu ambazo hazimaliziki wala hazitoeki, basi mungalizifanyia ubahili msitoe katika hizo kuwapa wengine kwa kuchelea zisimalizike mkawa mafukara.» Na ni katika tabia ya binadamu kuwa yeye ni mgumu wa kile kilicho mkononi mwake, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu

    [101] Na hakika tulimpa Mūsā miujiza tisa iliyo waziwazi, yenye kutolea ushahidi wa ukweli wa unabii wake, nayo ni fimbo, mkono, ukame, upungufu wa matunda, mafuriko, nzige, chawa, vyura na damu. Basi waulize Mayahudi, ewe Mtume, suala la kuthibitisha, pale Mūsā alipowajia mababu zao na miujiza iliyo wazi, Fir'awn akasema kumwambia Mūsā, «Mimi nadhani, ewe Mūsā, kwamba wewe ni mchawi uliodanganywa na kutekwa akili yako kwa vitendo hivyo vya ajabu unavyovileta.»

    [102] Mūsā akamjibu, «Umeshajua kwa yakini, ewe Fir'awn, kwamba hakuiteremsha miujiza hiyo tisa yenye kuutolea ishahidi unabii wangu isipokuwa Mola wa mbingu na ardhi, ipate kuwa ni dalili ambazo wenye busara watazitumia kuonyesha upweke wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka katika uola Wake na uungu Wake, na mimi nina yakini kwamaba wewe, ewe Fir'awn, ni mwenye kuangamia, kulaaniwa na kushindwa.»

    [103] Hapo Fir'awn akataka kumbabaisha Mūsā na kumtoa pamoja na Wana wa Isrāīl kwenye ardhi ya Misri, tukamuanagamiza baharini yeye na askari waliokuwa pamoja na yeye kwa kuwatesa

    [104] Na tukasema, baada ya kuangamia Fir’awn na askari wake, kuwaambia Wana wa Isrāīl, «Kaeni ardhi ya Sham. Na itakapo kuja Siku ya Kiyama, tutawaleta nyote kutoka makaburini mwenu kufika kwenye kisimamo cha kuhesabiwa.»

    [105] Na tumemteremshia Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, hii Qur’ani ili kuwaamrisha waja, kuwakataza, kuwalipa mema na kuwaadhibu; na imeteremka kwa ukweli, uadilifu na utunzi isibadilishwe na isigeuzwe. Na hatukukutumiliza wewe, ewe Mtume, isipokuwa ni uwabashirie Pepo waliotii na uwatishe na Moto walioasi na kukanusha

    [106] Na tumekuteremshia, ewe Mtume, Qur’ani tuliyoieleza, tukaipanga na kuifafanua ikawa ni yenye kutenganisha baina ya uongofu na upotevu na ukweli na ubatilifu, ili upate kuwasomea watu kwa umakinifu na upole; na tumeiteremsha mafungu-mafungu kidogo-kidogo kulingana na matukio ya wakati na mahitaji yake

    [107] Sema, ewe Mtume, uwaambie hawa wakanushaji, «Iaminini Qur’ani au msiiamini, kwani kuiamini kwenu hakuiongezei ukamilifu, na kuikanusha kwenu hakuifanyi iwe na upungufu, kwani wanavyuoni waliopewa Vitabu vilivyotangulia kabla ya Qur’ani na wakajua uhakika wa wahyi, wanaposomewa Qur’ani wananyenyekea na wanamsujudia Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa nyuso zao kwa kumtukuza na kwa kumshukuru

    [108] Na wanasema, hawa waliopewa ujuzi, wanapoisikia Qur’ani, «Kuepukana na kutakasika ni kwa Mola wetu na kila sifa wanazompa washirikina; halikuwa agizo la Mwenyezi Mungu Aliyetukuka isipokuwa ni lenye kutukia kikweli.»

    [109] Na hapo hawa wanapomoka hali ya kusujudu kwa nyuso zao, huku wakilia kwa kuathirika na mawaidha ya Qur’ani. Na kule kuisikia Qur’ani na mawaidha yake kunawafanya wazidi kuinyenyekea amri ya Mwenyezi Mungu na kuunyenyekea uweza Wake mkubwa

    [110] Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina wa watu wako waliokupinga kutumia kwako neno la Yā Allāh , Yā Raḥmān, katika maombi, «Muombeni Allāh (Mwenyezi Mungu) au muombeni Raḥmān (Mwingi wa rehema), kwani kwa majina yoyote yake mkimuomba huwa mnamuomba Mola Mmoja, kwa kuwa majina Yake yote ni mazuri. Wala usidhihirishe kisomo katika Swala yako wakakusikia washirikina, wala usisome kwa siri wasikusikie masahaba zako, na uwe kati na kati baina ya kudhihirisha na kusirisha.»

    [111] Na useme, «Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu, ukamilifu na sifa njema ni Zake, Aliyeepukana na mwana na mshirika katika uungu Wake. Na Mwenyezi Mungu Hana msaidizi yoyote kati ya viumbe vyake, Yeye Ndiye Mkwasi na Ndiye Mwenye nguvu., na wao ndio mafukara wanaomhitajia.» Na umtukuze matukuzo yaliyotimu, kwa kumsifu, kumuabudu Peke Yake bila ya mshirika, na kumtakasia Dini yote.»

    Pango

    Surah 18

    [1] Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, kwa kuwa Ana sifa ambazo zote ni sifa za ukamilifu na kwa kuwa ana neema zilizo wazi na zilizofichika, za kidini na za kidunia, Ambaye Alifanya wema Akamteremshia mja Wake na Mtume Wake Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, Qur’ani na Asiifanye iwe na kitu chochote cha kupotoka na haki

    [2] Mwenyezi Mungu Ameifanya kuwa ni Kitabu kilicholingana kisicho na tafauti ndani yake wala mgongano, ili Awaonye makafiri na adhabu kali itokayo Kwake, na Awape bishara njema wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wanaofanya matendo mema, kwamba wao watakuwa na malipo mengi, nayo ni Pepo

    [3] watakaa kwenye starehe hiyo, hawataiepuka milele

    [4] Na awaonye kwayo washirikina waliosema, «Mwenyezi Mungu Amejifanyia mtoto.»

    [5] Hawa washirikina hawana ujuzi wowote wa kile wanchokidai kwamba Mwenyezi Mungu Amejifanyia mtoto, vilevile wale waliopita kabla yao ambao wao wamewaiga, hawakuwa na ujuzi huo. Ni makubwa sana maneno haya mabaya yanayotoka kwenye vinywa vyao. Wao hawasemi isipokuwa urongo

    [6] Huenda wewe, ewe Mtume, ukajiangamiza nafsi yako kwa majonzi na masikitiko baada ya watu wako kukuepuka na kukupa mgongo, iwapo hawataiamini hii Qur’ani na kuifuata kivitendo

    [7] Hakika sisi tumevifanaya vilivyoko juu ya uso wa ardhi viwe ni pambo lake na ni manufaa kwa watu wake, ili tuwatahini ni nani kati yao aliye mzuri zaidi wa vitendo vya utiifu kwetu na ni nani kati yao aliye mbaya zaidi wa kufanya maasia, na tutamlipa kila mtu anachostahiki

    [8] Na sisi, dunia imalizikapo, ni wenye kuvifanya vilivyoko juu ya ardhi, kati ya hilo pambo, viwe mchanga usio na mimea

    [9] Usidhani kwamba kisa cha watu wa pangoni (asḥāb al-kahf) na ubao ulioandikwa majina yao ni jambo geni la ajabu miongoni mwa alama zetu. Kuumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ni jambo la ajabu zaidi kuliko hilo

    [10] Kumbuka, ewe Mtume, pindi walipohamia vijana Waumini kwenye pango kwa kuchelea wasiteswe na watu wao na kulazimishwa kuabudu masanamu, na wakasema, «Mola wetu! Tupe rehema kutoka kwako, ambayo kwayo ututhibitishe na utuhifadhi na shari, na utusahilishie njia ya sawa yenye kutupelekea kufanya matendo unayoyapenda, tuwe waongofu na tusiwe wapotevu.»

    [11] Hapo tukawalaza usingizi mrefu, na wakasalia kwenye pango miaka mingi

    [12] Kisha tukawaamsha kutoka kwenye usingizi wao ili tuwaonyeshe watu tuliyoyajua hapo kale ipate kupambanuka ni lipi kati ya makundi mawili, yanayobishana juu ya kipindi cha kukaa kwao, limedhibiti zaidi katika kuhesabu: je, walikaa siku moja au mbili au walikaa muda mrefu

    [13] Sisi tunakuhadithia, ewe Mtume, habari yao kwa ukweli. Watu wa pango ni vijana waliomuamini Mola wao na wakafuata amri Zake, na tukawazidishia uongofu na uimara katika haki

    [14] Na tukazipa nguvu nyoyo zao kwa Imani na tukazikaza nia zao kwa hiyo Imani, waliposimama mbele ya mfalme kafiri, huku naye akiwalaumu kwa kuacha ibada ya masanamu, na wakamwambia, «Mola wetu tunayemuabudu ni Mola wa mbingu na ardhi, hatutaabudu waungu wengine, na tukisema lingine lisilokuwa hili tutakuwa tumesema neno la udhalimu lililo mbali na haki.»

    [15] Kisha wakaambiana wao kwa wao, «Watu wetu hawa wamewachukua wasiokuwa Mwenyezi Mungu wakawafanya ni wauungu, basi si watuletee ushahidi waziwazi kuwa hao wafaa kuabudiwa? Hakuna yoyote aliye dhalimu zaidi kuliko yule aliyemzulia Mwenyezi Mungu urongo kwa kudai kuwa Ana mshirika katika kuabudiwa

    [16] Na mlipotengana na watu wenu kwa ajili ya dini yenu na mkawaacha waungu wanaowaabudu isipokuwa kumuabudu Mungu Mmoja, basi hamieni kwenye pango iliyoko jabalini mpate kumuabudu Mola wenu Peke Yake, hapo Mwenyezi Mungu Atawakunjulia rehema Yake ambayo kwayo Atawapa sitara ya dunia na Akhera na Atawafanyia njia za maisha ziwe pesi mnufaike nazo katika maisha yenu

    [17] Walipofanya hivyo, Mwenyezi Mungu Aliwatia usingizi wakalala na Akawahifadhi. Na utaliona jua, ewe mwenye kuwatazama wao, linapochomoza upande wa mashariki linapenyeza pale walipo upande wa kulia, na linapozama linawaacha upande wa kushoto, na hali wao wako kwenye sehemu kunjufu ndani ya pango, joto la jua haliwasumbui na hewa haiwakatikii. Hayo tuliyowafanyia vijana hawa ni miongoni mwa dalili za uweza wa wa Mwenyezi Mungu. Basi yoyote yule ambaye Mwenyezi Mungu Atamuafikia kuongoka kwa aya Zake, yeye ndiye mwenye kuongoka, na yoyote ambaye Hatamuafikia hilo, hutapata yoyote wa kumsaidia na kumuongoza kuifikia haki, kwani kuafikiwa na kutoafikiwa viko mikononi mwa Mwenyezi Mungu

    [18] Na utadhani, ewe mwenye kutazama, kwamba watu wa pangoni wako katika hali ya kuangaza, na mambo yalivyo ni kuwa wao wamelala, na sisi tunawaangalia kwa kuwatunza, tunawageuza na wao wamelala, mara nyingine ubavu wa kulia na mara nyingine ubavu wa kushoto, ili ardhi isiwale, na mbwa wao aliyekuwa amefuatana nao ameinyosha miguu yake ya mbele kwenye ukumbi wa pango. Lau uliwashuhudia ungaligeuka kukimbia na unagalijawa na kicho kwa kuwaogopa

    [19] Na kama tulivyowalaza na tukawahifadhi muda huu mrefu, tuliwaamsha kutoka kwenye usingizi wao kama vile walivyokuwa bila kubadilika, ili waulizane wao kwa wao, «Ni muda gani tulikaa tukiwa tumelala hapa?» Baadhi yao wakasema, «Tumekaa siku moja au sehemu ya siku.» Na wengine ambao mambo yaliwachanganyikia walisema, «utegemezeni ujuzi wa hilo kwa Mwenyezi Mungu, kwani Mola wenu ni Mjuzi zaidi wa kipindi mlichokikaa, basi mtumeni mmoja wenu na pesa zenu hizi za fedha aende mjini kwetu aangalie ni mtu gani hapo mjini mwenye chakula kizuri zaidi na cha halali, na awaletee chakula kutoka kwake, na ajifichefiche akiwa na muuzaji katika kununua kwake ili tusigundulike na mambo yetu yakafichuka, na msijulikane kabisa na mtu yoyote

    [20] Kwa hakika watu wenu wakiwagundua mulipo watawapiga mawe wawaue au watawarudisha kwenye dini yao muwe makafiri, na mkifanya hivyo basi hamtafaulu kabisa kupata matakwa yenu ya kuingia Peponi

    [21] Na kama vile tulivyowalaza miaka mingi na tukawaamsha baada yake, tuliwafanya wajulikane na watu wa zama hizo baada ya muuzaji kuzigundua aina ya dirhamu alizozileta yule aliyetumwa na wao, ili watu wapate kujua kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ya Ufufuzi ni kweli na kwamba Kiyama hakina shaka ni chenye kuja. Kitahamaka hao waliowagundua watu wa Pango wakawa ni wenye kushindana kuhusu jambo la Kiyama: kuna waliolikubali na kuna waliolipinga. Na Mwenyezi Mungu Akajaalia kule kuwagundua watu wa Pango ni hoja kwa Waumini juu ya makafiri. Na baada ya mambo yao kugnuduliwa na wakafa, lilisema kundi moja la wale waliowagundua, «Jengeni kwenye mlango wa pango jengo la kuwasitiri kisha muwawache na mambo yao, Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa hali yao.» Na wakasema wale wenye kusikizwa maneno yao na wenye uwezo miongoni mwao, «Tutatengeneza mahali pao hapo msikiti wa kufanya ibada.» Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, alikataza kuyafanya makaburi ya Manabii na watu wema kuwa misikiti, na alimlaani mwenye kufanya hivyo katika nyasia zake za mwisho kwa umati wake. Pia alikataza kabisa kujenga juu ya makaburi na kuyajengea na kuandika juu yake, kwani yote hayo ni miongoni mwa upitaji kiasi unaopelekea kuwaabudu waliomo ndani

    [22] Watasema baadhi ya Watu wa Kitabu wenye kujishughulisha na mambo yao kwamba wao ni watatu na wa nne wao ni mbwa wao, na kundi lingine litasema kwamba wao ni watano na wa sita wao ni mbwa wao. Maneno ya makundi mawili haya ni maneno ya kudhania bila dalili yoyote. Na kundi la tatu litasema kwamba wao ni saba na wa nane wao ni mbwa wao. Sema, ewe Mtume, «Mola wangu Ndiye Mjuzi kabisa wa idadi yao,» hakuna anayeijua idadi yao isipokuwa ni wachache kati ya viumbe Wake. Basi usibishane na Watu wa Kitabu kuhusu idadi yao isipokuwa ubishi wa juu-juu usiokuwa na undani kwa kuwasimulia yale ambayo Mwenyezi Mungu amekuletea wahyi nayo, na usiulize kuhusu idadi yao na hali zao kwani wao hawalijui hilo

    [23] Na usiseme juu ya kitu chochote unachoazimia kukifanya, «Mimi nitafanya kitu hiko kesho.»

    [24] Isipokuwa ufungamanishe neno lako na matakwa ya Mwenyezi Mungu na useme, «Mwenyezi Mungu Atakapo.» Na mkumbuke Mola wako unaposahau kwa kusema, «Mwenyezi Mungu Atakapo.» Na kila unaposahau, mtaje Mwenyezi Mungu, kwani kumtaja Mwenyezi Mungu huondosha kusahau, na useme, «Matarajio ni kwamba Mola wangu Aniongoze njia ya karibu zaidi yenye kufikisha kwenye uongofu na ya sawa

    [25] Na vijana hao walikaa wakiwa wamelala ndani ya pango yao muda wa miaka mia tatu na siku tisa kwa hesabu ya kimwezi

    [26] Na ukiulizwa, ewe Mtume, kuhusu muda wa kukaa kwao kwenye pango, na wewe huna ujuzi wa hilo na hukupata wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, basi usisongee mbele kwa lolote kuhusu jambo hilo, isipokuwa sema,»Mwenyezi Mungu Ndiye Mjuzi zaidi wa muda wa kukaa kwao. Ni wake Yeye ujuzi wa visivyoonekana vya mbinguni na ardhini, ni kuona kulioje Kwake na kusikia kulioje!» Yaani : uonee ajabu ukamilifu wa kuona Kwake na wa kusikia Kwake na wa kukizunguka Kwake kila kitu. Viumbe hawana yoyote mwingine isipokuwa Yeye wa kusimamia mambo yao, na Hana mshirika katika uamuzi Wake, hukumu Yake na sheria Zake, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake

    [27] Na usome Qur’ani, ewe Mtume, ambayo Mwenyezi Mungu Amekuletea wahyi nayo, kwani hiyo Qur’ani ni Kitabu ambacho hakuna mwenye kuyageuza maneno yake kwa kuwa ni ya kweli na ya uadilifu, na hutapata isipokuwa kwa Mola wako mahala pa wewe kuhamia wala pa kujilinda

    [28] Na uvumilie nafsi yako, ewe Mtume, pamoja na Masahaba wako miongoni mwa Waumini masikini wanaomuabudu Mola wao Peke Yake na kumuomba Yeye kucha na kutwa, wakiomba kupata radhi Zake, ukae mamoja nao na utangamane nao, na usiuepushe uso wako na wao kuwaangalia wasiokuwa wao miongoni mwa makafiri kwa kutaka kujistarahesha na pambo la uhai wa kilimwengu. Na usimtii yule tulioufanya moyo wake ughafilike kututaja na akafadhilisha kufuata matamanio yake juu ya kumtii Mola Wake na mambo yake yakawa, katika matendo yake yote, yamepotea na kuangamia

    [29] Na usme kuwaambia hawa walioghafilika, «Haya niliyowaletea ndio ukweli utokao kwa Mola wenu. Basi yoyote kati yenu atakye kuamini na akafanya matendo yanayolingana na hiyo Imani, na afanye kwani hilo ni bora kwake, na mwenye kutaka kukanusha na akanushe kwani atakua hakumdhulumu yoyote isipokuwa nafsi yake mwenyewe. Hakika sisi tumewatayarishia makafiri Moto mkali ambao kuta lake limwazunguka. Na makafiri hawa wakitaka msaada Motoni wapatiwe maji kwa vile kiu ilivyo kali, wataletewa maji kama mafuta machafu yaliyo moto sana yanayochoma nyuso zao. Ni kibaya kilioje kinywaji hiki ambacho hakiondoi kiu yao bali kinaizidisha na ni ubaya ulioje wa Moto kuwa ndio mashukio yao na makazi. Katika haya pana onyo na tishio kali kwa yoyote mwenye kuipa mgongo haki na asiuamini utume wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, na asifanye vitendo vinavyolingana na Imani hiyo

    [30] Hakika wale waliomuamini Mwenyezi MUngu na Mtume Wake na wakafanya matendo mema watakuwa na malipo makubwa kabisa. Sisi hatupotezi malipo yao wala hatutawapunguzia kwa matendo mazuri waliyoyafanya

    [31] Hao walioamini watakuwa na mabustani ya Peponi, watakaa humo daima, ambapo mito yenye maji tamu itakuwa ikipita chini ya vyumba vyao na nyumba zao. Watapambwa humo kwa vikuku vya dhahabu, na watavaa nguo za rangi ya kijani zilizofumwa kwa hariri nyembamba na nzito. Watategemea wakiwa humo kwenye vitanda vilivopambwa kwa pazia nzuri. Neema ya malipo ni malipo yao, na Pepo ni nzuri kuwa ni mashukio yao na mahali pao

    [32] Wapigie, ewe Mtume, makafiri wa watu wako mfano wa wanaume wawili miongoni mwa ummah waliopita : mmoja wao ni Muumini na mwingine ni kafiri, na yule kafiri tulimfanya awe na mashamba mawili ya mizabibu tuliyoizungusha na mitende mingi, na tukaotesha kati yake makulima mengi ya sampuli mbalimbali yenye manufaa

    [33] Kila mojawapo ya yale mashamba mawili lilikuwa limetoa matunda yake na halikupunguza kitu katika utoaji wake, na tulipasua mto baina yao ili kuyanosheza kwa usahali na upesi

    [34] Na mwenye hayo mashamba mawili alikuwa na matunda na mali mengine, hapo akasema kumwambia mwenzake akimjadili katika mazungumzo, na huku amejawa na majivuno, «Mimi ni mwingi wa utajiri kuliko wewe na nina wasaidizi wenye nguvu zaidi wenye kunihami.»

    [35] Na akaingia shambani kwake , na hali amejidhulumu nafsi yake kwa kukanusha kufufuliwa na kuwa na shaka kwake juu ya kusimama Kiyama, yakampendeza matunda yake na akasema, «Siamini kwamba shamba hili litaangamia muda wa maisha

    [36] na siamini kwamaba Kiyama ni chenye kutukia, na kikitukia kwa kukisia tu, kama unavyodai ewe mwenye kuamini, na nikarudishwa kwa Mola wangu, basi huko Kwake nitapata bora zaidi kuliko shamba hili nirudishiwe na nirejeshewe, kwa ajili ya utukufu wangu na cheo changu Kwake.»

    [37] Mwenzake Muumini akamwambia, huku akimjadili kwa kumuwaidhia, «Vipi wewe utamkanusha Mwenyezi Mungu Aliyekuumba kwa mchanga kisha kwa tone la manii kisha Akakusawazisha kwa kukufanya binadamu mwenye kimo kilicholingana na umbo?» Katika aya hii pana dalili ya kwamba mwenye uweza wa kuanzisha kuumba viumbe ni muweza wa kuwarudisha

    [38] «Lakini mimi sisemi maneno hayo yako yanayoonyesha ukafiri wako. Kwa kweli, mimi nasema ‘Mwenye kuneemesha na kufanya hisani ni Mwenyezi Mungu Mola wangu Peke Yake, na mimi simshrikishi yeye katika kumuabudu na yoyote asiyekuwa Yeye

    [39] «Kwani si ingalikuwa afadhali, ulipoingia kwenye shamba lako na likakupendeza, kama ulimshukuru Mwenyezi Mungu na ukasema, ‘Haya ni yale Aliyenitakia Mwenyezi Mungu, sina nguvu ya kuyapata isipokuwa ni kwa Mwenyezi Mungu.’ Iwapo waniona mimi kuwa ni mchache wa mali na watoto kuliko wewe

    [40] basi Mwenyezi Mungu huenda Akanipa mimi bora zaidi kuliko shamba lako, na Akakuondolea hiyo neema kwa ukafiri wako, na akailetea shamba yako adhabu kutoka mbinguni ikawa ni ardhi tupu iliyo kavu ambayo nyayo haziwezi kuthibiti juu yake wala hakuna mmea unaoota

    [41] au maji yake ya kuinyosheza yazame ardhini na kukauka usiwezi kuyatoa.»

    [42] Yakawa ni kweli yale maneno ya yule Muumini, na shamba likaharibika na vilivyomo ndani vikaangamia, akawa yule kafiri anageuza vitanga vyake vya mikono huku na huku kwa kulilia hasara na majuto kwa gharama aliyoitoa pale, na hali mitiyake imeanguka chini baadhi yake iko juu ya mingine, na akawa yuwasema, «Natamani lau nilizitambua neema za Mwenyezi Mungu na uweza Wake na sikumshirikisha Mwenyezi Mungu na yoyote.» Na haya ni majuto yake wakati ambapo majuto hayamfalii kitu

    [43] Na hakuwa na kundi la watu, kati ya wale ambao alijifahiri nao, wenye kumtetea na adhabu ya Mwenyezi Mungu yenye kumshukia, wala hakuwa ni mwenye kujitetea kwa nafsi yake na nguvu zake

    [44] Katika shida kama hizi mategemeo na usaidizi huwa uko kwa Mwenyezi Mungu wa haki. Yeye ni bora wa kulipa mema na ni bora wa kuwapa mwisho mwema wale waliyoko hifadhini Mwake

    [45] Na wapigie watu, ewe Mtume, hasa wale wenye kujiona kati yao, mfano wa hali ya ulimwengu, ambao wameghurika nao, kwa uzuri wake na upesi wa kuondoka kwake, kwamba ni kama maji aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu kutoka juu ambayo kwayo mimea ikatoka kwa idhini Yake na ardhi ikageuka ikawa rangi kijani. Na usipite isipokuwa muda mchache kitahamaka mimea hii ikawa imevunjikavunjika inarushwa na upepo kila upande. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza mkubwa juu ya kila kitu

    [46] Mali na watoto ni uzuri na nguvu za ulimwengu huu wenye kumalizika. Na matendo mema, hasa kuleta tasbihi (kusema Subḥāna-llāh), tahmidi (kusema Alḥmdu li-llāh), takbiri (kusema Allāh Akbar) na tahlili(kusema Lā ilāha illa-llāh) yana malipo mazuri zaidi kuliko mali na wana. Matendo haya mema ndio bora zaidi kwa mtu kutarajia malipo mema kutoka kwa Mola wake na akapata kwayo huko Akhera yale ambayo alikuwa akiyatazamia duniani

    [47] Wakumbushe Siku tutakapoyaondoa majabali kutoka mahali pake, na ukaiona ardhi waziwazi haina vya kuifinika miongoni mwa viumbe vilivyokuwa juu yake, na tukawakusanya wa mwanzo na wa mwisho kwenye kisimamo cha kuhesabiwa, tusimuache yoyote miongoni mwao

    [48] Na hapo watahudhurishwa wote kwa Mola wako wakiwa wamejipanga safu, hakuna yoyote kati yao anayefichwa, na hapo Awaambie «Tumewafufua na mumetujia mkiwa peke yenu, hakuna mali pamoja na nyinyi wala watoto, kama vile tulivyowaumba mara ya kwanza. Bali mlifikiria kwamba hatutawaekea nyinyi wakati wa kuwafufua na kuwalipa kwa matendo yenu.»

    [49] Na kitawekwa kitabu cha matendo ya kila mtu kuliani kwake au kushotoni kwake, hapo utawaona waasi wameingiwa na kicho kwa yaliyomo ndani kwa sababu ya mambo ya uhalifu waliyoyafanya, na watasema watakapokiangalia, «Ewe maangamivu yetu! Kina nini kitabu hiki hakikuacha dogo wala kubwa isipokuwa kimelisajili?» Na watayakuta yote waliyoyafanya ulimwenguni yako mbele yao yamesajiliwa. Na Mola wako Hamdhulumu yoyote hata kadiri ya chungu mdogo. Mtiifu hatapunguziwa malipo yake mema, na muasi hataongezewa mateso yake

    [50] Na kumbuka pale tulipowaamrisha Malaika kumsujudia Ādam, kimaamkizi na sio kiibada, na tukamwamrisha Iblisi vile tulivowaamrisha Malaika. Hapo Malaika wote walisujudu, lakini Iblisi aliyekuwa ni miongoni mwa majini, alitoka nje ya utiifu wa Mwenyezi Mungu na asisujudu kwa kiburi na wivu. Basi mnamfanya yeye, enyi watu, na waliozalikana na yeye kuwa ni wasaidizi wenu, mkawa mnawatii na mnaacha kunitii mimi, na hali yeye ni adui yenu aliye mtesi mno? Ni ubaya ulioje wa madhalimu kumtii Shetani badala ya kumtii Mwingi wa rehema

    [51] Sikumleta Iblisi na kizazi chake, ambao nyinyi mnawatii, katika uumbaji wa mbingu na ardhi, nikataka msaada wao kuziumba, wala sikuwashuhudisha baadhi yao uumbaji wa wengine. Bali mimi nilipwekeka katika kuumba zote hizo bila msaidizi wala mwenye kutilia nguvu, na sikuwa ni mwenye kuwafanya wapotezaji miongoni mwa Mashetani na wengineo kuwa ni wasaidizi, basi vipi nyinyi mnawapatia haki yangu na mnawafanya wao ni wategemewa wenu badala yangu na hali mimi ndiye muumba wa kila kitu

    [52] Na wakumbushe pindi Atakaposema Mwenyezi Mungu kuwaambia washirikina Siku ya Kiyama, «Waiteni washirika wangu ambao mlikuwa mnadai kwamba wao ni washirika wangu katika ibada, wapate kuwaokoa na mimi leo.» Hapo wakaomba uokozi wao, na wao wasiwaokoe, na tukaweka baina ya wenye kuabudu na waabudiwa kitu cha kuwaangamiza katika moto wa Jahanamu wawe wote ni wenye kuangamia humo

    [53] Na hao wahalifu wakaushuhudia Moto, na wakawa na yakini kwamba wao hapana budi ni wenye kuingia humo na wasipate njia yoyote ya kupitia ili kujiepusha nao

    [54] Kwa hakika tumeeleza na kufafanua katika hii Qur’ani aina nyingi ya mifano ili waaidhike na waamini. Na mwanadamu ni mwingi wa utesi na ubishi miongoni mwa viumbe

    [55] Na hakuna kilichowazuia watu kuamini, alipowajia Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, akiwa na Qur’ani, na kumuomba maghufira Mola wao kwa kutaka Awasamehe, isipokuwa ni kule kushindana kwao na Mtume, kutaka kwao wajiwe na mwendo wa Mwenyezi Mungu wa kuwaangamiza watu waliopita kabla yao au wapatikane na adhabu ya Mwenyezi Mungu waziwazi

    [56] Na hatuwatumilizi Mitume kwa watu isipokuwa wawe ni wenye kuwabashiria Pepo wenye Imani na matendo mema na kuwatisha na Moto wenye kukanusha na kuasi. Na pamoja ya kuwa haki ifunushie wazi, wale waliokanusha wanagombana na mitume wao kiubatili kwa njia ya upotufu, ili wapate kuiondoa, kwa ubatilifu wao, haki aliyokuja nayo Mtume, na wamekifanya kitabu changu, hoja zangu na adhabu ambayo walionywa nayo kuwa ni shere na ni kitu cha kufanyiwa mzaha

    [57] Na hakuna yoyote aliye mwingi wa udhalimu kuliko yule aliyepewa mawaidha ya aya za Mola wake zilizo wazi akazipuuza na akaendelea kwenye ubatilifu wake na akasahau matendo mabaya yaliyotangulizwa na mikono yake miwili asirudi nyuma. Sisi tumeweka vifiniko juu ya nyoyo zao ndipo wasiifahamu Qur’ani na wasiufikie wema uliyomo, na tumefanya ndani ya mashikio yao kitu kinachofanana na uziwi ndipo wasiisikie na wasinufaike nayo, na ukiwaita kwenye Imani hawatakuiitika na hawataongoka kuifuata kabisa

    [58] Na Mola wako Ndiye Mwenye kusamehe dhambi za waja Wake wanapotubia, Ndiye Mwenye kuwarehemu. Lau Awatesa hawa wenye kuzipa mgongo aya Zake kwa madhambi na makosa waliyoyatenda, Angaliwaharakishia adhabu, lakini Yeye, Aliyetukuka, ni Mpole, Haharakishi kutesa. Lakini wana kipindi walichowekewa cha wao kulipwa kwa matendo yao, hawana njia ya kuepukana nacho wala kuhepa

    [59] Vijiji hivyo vilivyo karibu na nyinyi, kama vijiji vya watu wa Nūḥ„ Ṣāliḥ„ Lūṭ, na Shu'ayb, tuliviangamiza watu wake walipodhulumu kwa kukufuru, na tuliwawekea wakati na muda maalumu wa kuwaangamiza; walipoufikia adhabu iliwajia na Mwenyezi Mungu Akawaangamiza kwayo

    [60] Na kumbuka pindi Mūsā alipomwambia mtumishi wake, Yūsha' bin Nūn, «Sitaacha kuendelea kutembea mpaka nifike kwenye makutaniko ya bahari mbili au niende kipindi kirefu mpaka nifike kwa mja mwema nipate kujifunza kwake elimu nisiokuwa nayo.»

    [61] Wakajibidiisha kwenda, na walipofika kwenye makutano ya bahari nmbili walikaa penye jiwe la manga, na wakamsahau samaki wao ambaye Mūsā aliamuru achukuliwe kiwe ni chakula chao. Yūsha' alimbeba kikapuni, kitahamaka amekua hai na akawa anajisingirisha kuingia baharini, na akajifanyia njia iliyo wazi

    [62] Walipoondoka pale mahali walipomsahau samaki, na Mūsā akahisi njaa, alimwambia mtumishi wake, «tuletee chakula chetu cha mwanzo wa mchana, hakika tumechoka kwenye safari yetu hii.»

    [63] Mtumishi wake akamwambia, «Unakumbuka tuliposhukia kwenye jiwe ambapo tulipumzika? Nilisahau kukwambia habari ya yule samaki, na hakuna aliyenisahaulisha isipokuwa ni Shetani. Na yule samaki, aliyekuwa mekufa, uhai umemrudia, akajirusha baharini na akajitolea njia ya kwendea, na mambo yake ni yenye kustaajabiwa

    [64] Mūsā akasema, «Yaliyotokea ndiyo ambayo tulikuwa tukiyataka, kwani hiyo ni alama yangu ya mahali pa mja mwema.» Hapo wakarudi wakizifuata alama za nyayo zao mpaka wakakoma kwenye jiwe

    [65] Wakamkuta mja mwema miongoni mwa waja wetu ambaye ni al-Khaḍir, amani imshukiye- naye ni Nabii, miongono mwa Manabii wa Mwenyezi Mungu, ambaye Mwenyezi Mungu Amemfisha, tuliyempa rehema kutoka kwetu na tukamfundisha elimu kubwa itokayo kwetu

    [66] Mūsā akamsalimia na akamwambia, «Je, utaniruhusu nikufuate, unifundishe elimu ambayo Mwenyezi Mungu Amekufudisha kadiri ya mimi kujiongoza nayo na kunufaika

    [67] Al-Khiḍir akawmwambia, «Hakika wewe , ewe Mūsā, hutaweza kuvumilia kunifuata na kuwa na mimi

    [68] Na utakuwa na uvumilivu kwa nitakalolifanya miongoni mwa mambo yaliyofichika kwako ambayo Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Alinifundisha

    [69] Mūsā akamwambia, «Utanikuta, Mwenyezi Mungu Akitaka, ni mwenye kuvumilia kwa nitakayoyaona kwao, na sitaenda kinyume na amri yako yoyote utakayoniamrisha

    [70] Al-Khiḍr akakubali na akamwambia, «Ukifuatana na mimi usiniulize juu ya chochote usichokikubali mpaka nikupe maelezo yake yaliyofichika kwako bila ya wewe kuuliza.»

    [71] Wakatoka kwenda kwenye ufuo wa pwani, ikawapita mashua, wakawataka wenyewe wapande na wao. Walipopanda Al-Khiḍr aliukoboa ubao kutoka kwenye mashua na akaitoboa tundu. Mūsā akamwambia,»Umeitoboa mashua ili uwazamishe wenyewe, na hali wao walituchukua bila malipo? Kwa hakika umefanya jambo baya.»

    [72] Al-Khiḍr akamwambia, «Nilisema tangu mwanzo, ‘Hakika wewe hutoweza kuvumilia kuandamana na mimi.’»

    [73] Mūsā akasema akitoa udhuru, «usinichukulie kwa kusahau sharti yako juu yangu wala usinikalifishe mashaka ya kujifunza kwako, na amiliana na mimi kwa usahali na upole.»

    [74] Al-Khiḍr akakubali udhuru wake. Kisha wakatoka mashuani, na walipokuwa wanatembea kwenye ufuo wa pwani, ghafla wakamuona mvulana yuwacheza na wenzake, na Al-Khiḍr akamuua. Mūsā akamlaumu kwa nguvu na akasema, «vipi umeiua nafsi safi isyokuwa na kosa, isiyofikia umri wa kubeba majukumu, na haijaua mtu mpaka istahili kuuawa? Kwa hakika umefanya jambo baya sana.»

    [75] Akasema Al-Khiḍr kumwambia Mūsā kwa kumlaumu na kumkumbusha, «Je, sikukwambia kuwa wewe hutoweza kuvumilia pamoja na mimi kwa matendo unayoyaona kutoka kwangu katika yale ambayo hayakuzungukwa na ujuzi wako?»

    [76] Mūsā akamwambia, «Nikikuuliza kitu baada ya mara hii, niache na usifuatane na mimi, utakuwa ushapata sababu kuhusu mimi na hutakuwa umefanya kasoro, kwa kuwa ulinambia kwamba mimi sitaweza kuvumilia pamoja na wewe.»

    [77] Mūsā akaenda na Al-Khiḍr mpaka wakafika kwa watu wa kijiji, wakataka wapewe chakula kwa njia ya makaribisho. Watu wa kijijini walikataa kuwakaribisha. Kisha wao wawili walipata hapo ukuta ulioinama uliokaribia kuanguka, Al-Khiḍr akaulinganisha mpaka ukawa uko sawa. Mūsā akamwambia, «Lau ungalitaka ungalichukua kwa kazi hii malipo ukayatumia kujipatia chakula chetu kwa kuwa wao hawakutukaribisha.»

    [78] Al-Khiḍr akamwambia Mūsā, «Huu ndio wakati wa kupambanukana mimi na wewe. Nitakuelezea habari ya matendo yangu niliyoyafanya ambayo wewe ulinipinga nayo na ambayo hukuweza kuwa na uvumilivu wa kutoyauliza na kutonipinga mimi kuhusu hayo

    [79] «Ama mashua ambayo nilitoboa tundu, ilikuwa ni ya watu masikini wanaofanya kazi baharini wakiwa ndani yake wakijitafutia riziki, nikataka kuitia kombo kwa kuitoboa, kwa kuwa mbele yao kulikuwa na mfalme anayechukuwa kila mashua nzuri kwa kuwanyang’anya wenyewe

    [80] Na ama mvulana niliyemuua alikuwa, katika ujuzi wa Mwenyezi Mungu, ni kafiri, na babake na mamake walikuwa Waumini, tukaogopa lau huyu mvulana ataendelea kuishi atawatia wazazi wake kwenye ukafiri na udhalimu wenye kupita kiasi kwa kumpenda kwao au kwa kumuhitajia

    [81] «Tukataka Mwenyezi Mungu Ampe badala yake aliyetengenea zaidi kwa wema , dini na utiifu kwa wao wawili

    [82] «Na ama ukuta nilioulinganisha, baada ya kuwa umeinama, mpaka ukawa sawa, ulikuwa ni wa wavulana wawili mayatima hapo kijijini, na chini yake kulikuwa na hazina yao ya dhahabu na fedha, na baba yao alikuwa mtu mwema, Mola wako Akataka wawe wakubwa, wapate nguvu na waitoe hazina yao kwa rehema itokayo kwa Mola wako. Na mimi sikuyafanya yote haya, ewe Mūsā, kwa amri yangu na kivyangu, kwa hakika nimeyafanya kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Hayo niliyokueleza sababu zake ndiyo mwisho wa mambo ambayo hukuweza kuyavumilia kwa kuacha kuyauliza na kunipinga kwayo.»

    [83] Na hawa washiriikina wa watu wako wanakuuliza, ewe Mtume, kuhusu habari ya Dhulqarnain, mfalme aliye mwema, waambie, «Nitawapa habari kuhusu yeye ya kuwaachia kumbukumbu mupate kuikumbuka na kuizingatia.»

    [84] Sisi tulimpa udhibiti katika ardhi na tukampa sababu na njia za kila kitu za kufikia ayatakayo ya kukomboa miji nakuwashinda maadui na yasiyokuwa hayo

    [85] Akazifuata hizo sababu na njia kwa bidii na juhudi

    [86] Mpaka alipofika Dhulqarnain upande wa jua la kuchwa, alilikuta jua kwa vile alivyoliona kama kwamba linakuchwa ndani ya chemchemu ya maji moto yenye udongo mweusi, na akawakuta watu upande huo wa jua la kuchwa. Tulisema, «Ewe Dhulqarnain! Ima uwaadhibu kwa kuwaua au kwa linginelo, iwapo hawatakubali upweke wa Mwenyezi Mungu au uwatendee wema uwafundishe uongofu na uwaonyeshe usawa.»

    [87] Dhulqarnain akasema, «Ama yule aliyeidhulumu nafsi yake miongoni mwao na akamkanusha Mola wake, basi tutamuadhibu ulimwenguni kisha atarudi kwa Mola wake Amuadhibu adhabu kubwa katika moto wa Jahanamu

    [88] «Na ama aliyemuamini Mola wake miongoni mwao, akamkubali, akampwekesha na akafanya matendo ya utiifu Kwake, basi atapata Pepo ikiwa ni malipo kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na tutamfanyia wema na tutasema naye kwa upole na tutaamiliana naye kwa usahali.»

    [89] Kisha Dhulqarnain akarudi akaelekea upande wa Mashriki akifuata njia na sababu alizompa Mwenyezi Mungu

    [90] Mpaka alipofika upande wa kutoka jua alilikuta hilo jua linawatokea watu wasiokuwa na mjengo ya kuwasitiri wala miti ya kuwapatia kivuli cha kuwakinga na jua

    [91] Hivyo basi ujuzi wetu umeyazunguka mema aliyokuwa nayo na sababu kubwa alizokuwa nazo popote alipoelekea na kuenda

    [92] Kisha akaenda Dhulqarnain akifuata njia na sababu tulizomtunukia

    [93] Mpaka alipofika baina ya majabali mawili yaliyozuia vilivyo nyuma yake, aliwakuta hapo watu wasiokaribia kuelewa maneno ya wasiokuwa wao

    [94] Wakasema, «Ewe Dhulqarnain, kwa hakika, Ya’jūj na Ma’jūj - nao ni binadamu wa mataifa mawili makubwa- wanafanya uharibifu katika ardhi kwa kuangamiza mazao ya ukulima na vizazi, basi je, tukupatie ujira na tukukusanyie mali ili utuwekee kizuizi baina yetu na wao chenye kupambanua baina yetu na wao?»

    [95] Dhulqarnain akasema, «Haya Aliyonipa Mwenyezi Mungu ya ufalme na udhibiti wa mambo, ni bora kwangu mimi kuliko mali yenu, basi nisaidieni kwa nguvu zenu niwafanyie kizuizi baina yenu na wao.»

    [96] «Nipeni vipande vya chuma» Walipkuja navyo, wakaviweka na wakavipanga karibu baina ya yale majabali mawili, aliwaambia wanaofanya kazi, «Washeni moto.» Na kilpogeuka chuma kuwa moto alisema, «Nipatieni shaba iliyodeuka niimimine juu yake.»

    [97] Hawakuweza Ya’jūj na Ma’jūj kupanda juu ya kile kizuizi kwa kuwa kilikuwa kirefu na kinateleza, na hawakuweza kukitoboa kwa chini yake kwa umbali wa upana wake na ugumu wake

    [98] Dhulqarnain akasema, «Hiki nilichokijenga cha kuzuia uharibifu wa Ya’jūj na Ma’jūj ni rehema kwa watu itokayo kwa Mola wangu, na ahadi ya Mwenyezi Mungu itakapokuja ya kutoka Ya’jūj na Ma’jūj, Atakifanya kigongeke- gongeke kivunjike na kiwe sawa na ardhi, na ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli.»

    [99] Na tutawaacha Ya’jūj na Ma’jūj, siku ya kuwajia ahadi yetu, watangamane wao kwa wao na wachanganyike kwa wingi wao, na Pembe ya Ufufuzi itapulizwa na tutawakusanya viumbe wote ili wahesabiwe na walipwe

    [100] Na tutauhudhurisha moto wa Jahanamu kwa makafiri na tutaudhihirisha kwao waushuhudie, ili tuwaoneshe ubaya wa mwisho wao

    [101] Wale ambao macho yao ulimwenguni yalikuwa yamefinikwa na kutonikumbuka, hayazioni dalili zangu, na walikuwa hawawezi kustahamili kuzisikia hoja zangu zenye kupelekea kuniamini mimi na Mtume wangu

    [102] Je, walidhani walionikanusha kuwa watawafanya waja wangu kuwa ni waungu badala yangu, wawe ni wategemewa wao? Kwa hakika tumewatayarishia wenye kukanusha moto wa Jahanamu uwe ndio mashukio yao

    [103] Waambie watu, ewe Mtume, kwa kuwaonya: Je, tuwapashe habari ya watu wenye vitendo vya hasara zaidi

    [104] Wao ni wale ambao matendo yao yalipotea katika maisha ya ulimwengu- nao ni washirikina wa watu wako na wengineo kati ya wale waliopotea njia ya sawa wasiwe kwenye uongofu wala usawa- na hali wao wanadhania kuwa wanayatengeneza matendo yao

    [105] Hao ndio waliopata hasara zaidi kivitendo, ndio wao waliozikataa aya za Mola wao na wakazikanusha na wakapinga kuwa watakutana na Yeye Siku ya Kiyama, hivyo basi matendo yao yakabatilika kwa sababu ya ukafiri wao na kwa hivyo hatutawajali chochote Siku ya Kiyama

    [106] Malipo hayo waliyoandaliwa kwa kubatilika matendo yao, ni moto wa Jahanamu, kwa sababu ya kumkanusha kwao Mwenyezi Mungu na kuzifanyia kwao shere na mchezo aya Zake na hoja za Mitume Wake

    [107] Hakika wale walioniamini, wakawakubali Mitume wangu na wakafanya mema watapata Pepo ya juu kabisa, ya kati na kati na yenye mashukio bora kabisa

    [108] Hali ya kukaa milele humo, hawatataka kuepukana nayo kwa kuwa na hamu nayo na kuipenda

    [109] Sema, ewe Mtuume, «Lau maji ya bahari yalikuwa wino wa kalamu za kuandikia maneno ya Mwenyezi Mungu yanayokusanya elimu Yake, hukumu Zake na yale Aliyowatumia wahyi Malaika Wake na Mitume Wake, yangaliisha maji ya bahari kabla maneno ya Mwenyezi Mungu hayajaisha, hata kama tulikuja na bahari nyingine za kuongezea mfano wa bahari hiyo. Katika aya hii pana kuthibitisha kikweli sifa ya kusema kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kama kunakonasibiana na utkufu Wake na ukamilifu Wake.»

    [110] Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Kwa kweli, mimi ni binadamu kama nyinyi, ninaletewa wahyi kutoka kwa Mola wangu kwamba mola wenu ni Mola Mmoja. Basi yoyote anayekuwa ni mwenye kuiyogopa adhabu ya Mola wake na ana matumaini kupata malipo yake mazuri Siku ya Kiyama, na atende matendo mema kwa ajili ya Mola wake yenye kuafikiana na sheria Yake, na asimshirikishe yoyote pamoja na Yeye katika ibada.»

    Maryam

    Surah 19

    [1] «Kāf, Hā, Yā, 'Ayn, Ṣād» Yametangulia maelezo kuhusu herufi za mkato kama hizi katika mwanzo wa sura ya Al-Baqarah

    [2] Huu ni utajo wa rehema ya Mola wako kwa mja wake Zakariyyā. Tutakupasha habari yake , kwani pana mazingatio ndani yake kwa wenye kuzingatia

    [3] Pindi alipomuomba Mola wake kwa siri, ili yawe ni maombi makamilifu zaidi na yenye kutimia katika kumtakasia Mwenyezi Mungu na yawe ni yenye matarajio zaidi ya kujibiwa

    [4] Akasema, «Mola wangu! Mimi nimezeeka na mifupa yangu imedhoofika na nywele nyeupe zimeenea kichwani, na sikuwa huko nyuma nimekataliwa kujibiwa maombi

    [5] «Na mimi ninaogopa kwamba jamaa zangu wa karibu na wenye kusimama na mimi wasije, baada ya kufa kwangu, wakaacha kuisimamia Dini yako vile inavyotakikana isimamiwe na wakaacha kuwalingania waja wako kuwaleta kwako, na mke wangu ni tasa hazai, basi nitunukie kutoka kwako mtoto awe ni mrithi na msaidizi

    [6] «Atakayeurithi unabii wangu na unabii wa kizazi cha Ya’qūb, na umfanye mtoto huyu kuwa ni mwenye kuridhiwa na wewe na waja wako.»

    [7] Ewe Zakariyyā! Sisi tunakupa bishara ya kukubaliwa maombi yako. Tumekutunukia mtoto wa kuime, jina lake ni Yaḥyā, hatujampatia jina hili yoyote kabla yake

    [8] Zakariyyā alisema kwa kushangaa, «Mola wangu! Vipi nitakuwa na mtoto wa kiume na hali mke wangu ni tasa hazai, na mimi nimefikia upeo wa ukongwe na ulaini wa mifupa.»

    [9] Malaika akasema kumjibu Zakariyyā juu ya kile alichokionea ajabu, «Mambo ni kama unavyosema kuwa mke wako ni tasa na kuwa wewe umefikia upeo wa uzee, lakini Mola wako Amesema, ‘Kumuumba Yah,yā kwa namna hii ni jambo sahali na pesi kwangu.’» Kisha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Alimtajia Zakariyyā jambo la ajabu zaidi kuliko lile aliloliuliza akasema, «Na nimekuumba wewe kabla ya Yah,yā na hukuwa ni kitu chenye kutajika wala kilichoko.»

    [10] Zakariyyā akasema kutaka kujituliza zaidi, «Mola wangu! Nipe alama ya kwamba kile ambacho Malaika wamenibashiria nacho kishapatikana.» Akasema, «Alama yako ni kutoweza kusema na watu kwa muda wa masiku matatu na michana yake na hali wewe ni mzima mwenye afya.»

    [11] Zakariyyā akawajia watu wake kutoka mahali pake pa kuswali, napo ni mahali alipobashiriwa kuwa atapata mtoto, na akawashiria wamtakase Mwenyezi Mungu asubuhi na jioni kwa kumshukuru Yeye Aliyetukuka

    [12] Alipozaliwa Yah,yā na akafikia umri wa kufahamu maneno, Mwenyezi Mungu Alimuamuru aichukue Taurati kwa bidii na jitihada kwa kusema, «Ewe Yah,yā! lchukue Taurati kwa bidii na jitihada kwa kuyahifadhi matamko yake na kuyafahamu maneno yake na kuitumia, na tulimpa busara na ufahamu mzuri ilhali yeye ni mdogo wa miaka

    [13] Na tulimpa rehema na mapenzi kutoka kwetu na kusafika na madhambi. Na alikuwa ni muogopaji Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na ni mtiifu Kwake, mtekelezaji yale Aliyoyalazimisha na ni mwenye kujiepusha na yale Aliyoyaharamisha

    [14] Na alikuwa mtiifu kwa wazazi wake wawili, na hakuwa ni mwenye kiburi cha kutomtii Mola wake na kutowatii wazazi wake wawili

    [15] Na salamu itokayo kwa Mwenyezi Mungu imshukie Yah,yā na amani iwe na yeye siku alipozaliwa na siku atakapokufa na siku atakapofufuliwa hali ya kuwa hai

    [16] Na utaje, ewe Mtume, katika hii Qur’ani habari ya Maryam alipojiweka mbali na watu wake, akajifanyia mahali upande wa Mashariki kando na wao

    [17] Akaweka kizuizi chenye kumsitiri na jamaa zake na watu wengine, hapo tukampelekea Malaika Jibrili akajjitokeza kwake katika sura ya binadamu aliyetimia umbo

    [18] Maryam akasema kumwambia, «Mimi najilinda kwa Mwenyezi Mungu na wewe usinifanye ubaya, iwapo wewe ni miongoni mwa wanaomcha Mwenyezi Mungu.»

    [19] Malaika akawmambia, «Kwa hakika, mimi ni mjumbe wa Mola wako, Amenituma kwako nikutunuku mtoto wa kiume aliyesafika na madhambi.»

    [20] Maryam akamwambia Malaika, «Vipi mimi niwe na mtoto wa kiume, na hakuna binadamu aliyenigusa kwa ndoa ya halali, na mimi sikuwa mzinifu?»

    [21] Malaika akasema kumwambia, «Mambo ni hivyo kama unavyoeleza kwamba hakuna binadamu aliyekugusa na hukuwa mzinifu, lakini Mola wako Amesema, ‘Jambo hili kwangu ni pesi, na ili mtoto huyu awe ni alama kwa watu yenye kuonesha uweza wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, na awe ni rehema itakayotokana na sisi kwake yeye, kwa mamake na kwa watu.’» Na kupatikana kwa Īṣā kinamna hii lilikuwa ni jambo lililokadiriwa katika Ubao uliohifadhiwa, basi hapana budi lifanyike

    [22] Maryam akabeba mimba ya mtoto wa kiume baada ya Jibrili kupuliza kwenye mwanya wa kanzu yake, na pulizo hilo likafika kwenye uzao wake, na kwa sababu hiyo mimba ikaingia, na akaenda nayo mahali mbali na watu

    [23] Na uchungu wa mimba ukamfanya aende kwenye kigogo cha mtende, hapo akasema, «Natamani kama nilikufa kabla ya siku ya leo na nikawa kitu kisichojulikana, kisichotajwa na kisichotambulika ‘ni nani mimi?.’»

    [24] Jibrili au 'Īsā akamwita na kumwambia, «usisikitike, kwani Mola wako amekufanyia chini yako mkondo wa maji

    [25] «Na ukitikise kigogo cha mtende, zitakuangukia tende mbivu laini zitokazo mtini

    [26] «Basi zile hizo tende mbivu na unywe maji na ujifurahishe kwa huyo mtoto mwenye kuzaliwa. Na umuonapo yoyote miongoni mwa watu, akakuuliza juu ya jambo lako, mwambie, ‘Mimi nimejilazimisha nafsi yangu kwa Mwenyezi Mungu ninyamaze, sitatasema na mtu leo.’» Kunyamaza kimya kulikuwa ni ibada katika Sheria yao, na haikuwa hivyo katika Sheria ya Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [27] Hapo Maryam aliwajia watu wake, na yeye amembeba mtoto wake, akitokea mahali mbali. Walipomuona namna hiyo, walisema kumwambia, «Ewe Maryam! Umeleta jambo kubwa ulilolizua

    [28] «Ewe dada ya mtu mwema Hārūn! Babako hakuwa ni mtu mbaya anayefanya machafu, na mamako hakuwa ni mwanamke mbaya anayefanya umalaya.»

    [29] Maryama akashiria kwa mwanawe Īsā ili wamuulize na waseme naye. Wakasema kwa kumpinga, «Vipi tutasema na ambaye bado yuko mlezini aliye mchanga wa kunyonya?»

    [30] Īsā akasema, na yeye yuko katika hali ya uchanga wa kuwa mlezini yuwanyonya, «Mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu, Ameamua kunipatia Kitabu, nacho ni Injili, na amenifanya Nabii

    [31] «Na Amenifanya niwe na wingi wa wema na manufaa popote nipatikanapo, na ameniusia kutunza Swala na kutoa Zaka muda wa mimi kuwa hai

    [32] «Na Amenifanya mimi niwe mwenye kumtendea wema mamangu, na hakunifanya ni mwenye kujiona wala ni mbaya mwenye kumuasi Mola wangu

    [33] «Na salamu na amani ziko juu yangu mimi siku niliyozaliwa, siku nitakapokufa na siku nitakapofufuliwa nikiwa hai siku ya Ya Kiyama.»

    [34] Huyo tuliyokuhadithia, ewe Mtume, sifa zake na habari zake ndiye Īsā mwana wa Maryam pasina shaka, hali ya kuwa yeye ni neno la haki ambalo Mayahudi na Wanaswara walilifanyia shaka

    [35] Haikuwa kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, wala hainasibiani na Yeye kujichukulia mtoto miongoni mwa waja wake na viumbe vyake, Ameepukana na kutakasika na hilo; Akiamua jambo lolote, miongoni mwa mambo, na Akalitaka liwe, dogo au kubwa, halimkatalii, kwa hakika Yeye Analiambia, «Kuwa» na likawa kama alivyolitaka liwe

    [36] Na Īsā aliwaambia watu wake, «Na hakika ya Mwenyezi Mungu, Ambaye nawalingania nyinyi Kwake, ni Mola wangu na Mola wenu, basi muabuduni Yeye Peke Yake Asiye na mshirika, kwani mimi na nyinyi tuko sawa katika uja na kumnyenyekea Yeye. Hii ndio njia isiyo na kombo

    [37] Mapote ya watu wa Kitabu walitafautiana baina yao kuhusu mambo ya Īsā, amani imshukiye, kati yao kuna wanaopita kiasi katika kumtukuza nao ni Wanaswara, kati yao kuna waliosema kuwa yeye ni Mwenyezi Mungu, kati yao kuna waliosema kuwa yeye ni mwana wa Mwenyezi Mungu, kati yao kuna waliosema kuwa yeye ni mmoja kati ya waungu watatu, Ametukuka Mwenyezi Mungu na kuwa mbali na hilo wanalolisema, na kati yao kuna waliomwepuka, nao ni Mayahudi, na wakasema kwamba yeye ni mchawi na wakasema kwamba yeye ni mwana wa Yūsuf aliyekuwa seremala. Basi maangamivu ni ya waliokanusha kuwa wataishuhudia siku yenye vituko vikubwa, nayo ni Siku ya Kiyama

    [38] Ni makali yalioje yatakuwa masikizi yao na macho yao Siku ya Kiyama, siku watakayokuja kwa Mwenyezi Mungu , wakati ambapo hilo halitawafaa! Lakini madhalimu leo, katika dunia hii, wametoka nje ya haki waziwazi

    [39] Na uwaonye watu, ewe Mtume, Siku ya Majuto, wakati wa hukumu kutolewa, na mauti yaletwe kama kwamba ni kondoo mzuri, achinjwe hapo na na uamuzi utolewe baina ya viumbe, na hapo watu wa Imani waende Peponi na watu wa ukafiri waende Motoni, na hali wao leo katika dunia hii wameghafilika na yale ambayo walionywa nayo, hivyo basi hawaamini wala hawafanyi matendo mema

    [40] Sisi ndio tutakaoirithi ardhi na walio juu yake kwa kutoeka kwao na kusalia kwetu baada yao, na uamuzi wetu kupitishwa kwao. Na kwetu sisi ndio mwisho wao na kuhesabiwa kwao, na hapo tuwalipe kwa matendo yao

    [41] Na uwatajie, ewe Mtume, watu wako katika hii Qur’ani kisa cha Ibrahīm, amani imshukiye; kwa hakika yeye alikuwa ni mkweli mkubwa na ni miongoni mwa Manabii wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, wenye daraja za juu

    [42] Aliposema kumwambia babake, Āzar, «Ewe baba yangu! Ni kwa jambo gani unaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, masanamu wasiosikia, wasioona na wasioweza kuzuia chochote kisikufike

    [43] «Ewe baba yangu! Hakika Mwenyezi Mungu Amenipa ujuzi ambao hakukupa, basi nikubalie na unifuate kwa yale ninayokuitia kwayo, nikuongoze kwenye njia ya sawa ambayo hutapotea ukiifuata

    [44] «Ewe baba yangu! Usimtii Shetani ukawaabudu hawa masanamu, kwani Shetani anaenda kinyume na Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema, anakuwa na kiburi kumtii Mwenyezi Mungu

    [45] «Ewe baba yangu! Mimi ninaogopa usije ukafa kwenye ukafiri wako, ikakupata adhabu ya Mwingi wa rehema na ukawa ni rafiki wa Shetani ndani ya Moto.»

    [46] Baba yake Ibrāhīm akasema kumwambia mwanawe,»Kwani wewe umegeuka na kukataa kuabudu waungu wangu, ewe Ibrāhīm» Basi usipokomeka kuwatukana, nitakuua kwa kukupiga mawe. Na niondokee, usikutane na mimi wala usiseme na mimi kwa kipindi cha muda mrefu.»

    [47] Ibrāhīm alisema kumwambia baba yake, «Amani juu yako kutoka kwangu, halitakufikia kutoka kwangu jambo unalolichukia, na nitakuombea Mwenyezi Mungu uongofu na msamaha. Hakika Mola wangu ni Mwingi wa huruma ni Mpole kwangu kulingana na hali yangu, nikimuomba Ataniitikia

    [48] «Na nitawaepuka nyinyi na waungu wenu mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Na nitamuomba Mola wangu kwa kumtakasia, nikiwa na matumaini kuwa sitapita patupu kwa kumuomba Mola wangu Asinipe ninachomuomba.»

    [49] Na alipowaepuka wao na waungu wao wanaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, tulimruzuku, miongoni mwa watoto tuliomruzuku, Ish,āq na Ya'ūb mwana wa Ish,āq na tukawafanya wawaili hao kuwa Manabii

    [50] Na tukawatunukia wao wote rehema zetu zikiwa ni nyongeza zisizohesabika, na tukawajaalia watajike vizuri na wasifiwe kwa sifa njema zenye kubaki kwa watu

    [51] Na utaje katika Qur’ani, ewe Mtume, kisa cha Mūsā, amani imshukiye. Kwa hakika, yeye alikuwa ni mteule aliyesafishwa, na alikuwa ni Mtume na ni Nabii miongoni mwa Mitume waliokuwa na uthabiti

    [52] Na tulimuita upande wa jabali la Ṭūr Sīnā’ kuliani kwake (Mūsā), na tukamleta karibu na tukamtukuza kwa kusema na yeye. Katika hii pana kuthibitisha sifa ya kusema kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kama inavyonasibiana na utukufu Wake na ukamilifu Wake

    [53] Na tulimtunukia Mūsā, kutokana na rehema zetu, ndugu yake Hārūn akawa Nabii mwenye kumtilia nguvu na kumsaidia

    [54] Na utaje, ewe Mtume, katika hii Qur’ani habari ya Ismāīl, amani imshukiye. Yeye alikuwa ni mkweli katika ahadi, hakuahidi kitu isipokuwa hukitekeleza, na alikuwa ni Mtume na ni Nabii

    [55] Na alikuwa akiwaamrisha watu wake kusimamisha Swala na kutoa Zaka, na alikuwa kwa Mola wake, Aliyeshinda na kutukuka, ni mwenye kuridhiwa

    [56] Na utaje, ewe Mtume, katika hii Qur’ani habari ya Idris, amani imshukiye. Yeye alikuwa ni mkweli mkubwa katika maneno yake na vitendo vyake, ni Nabii aaliyeletewa wahyi

    [57] Na tukauinua utajo wake kwa viumbe wote na cheo chake kwa wale waliosongezwa karibu. Akawa ni mwenye utajo wa juu na, ni mwenye cheo cha juu

    [58] Hawa niliokusimulia habari zao, ewe Mtume, ni wale ambao Mwenyezi Mungu Amewaneemesha kwa nyongeza Zake na taufiki Yake, Akawafanya ni Mitume miongoni mwa kizazi cha Ādam, na miongoni mwa kizazi cha wale tuliowabeba pamoja na Nūḥ, katika jahazi, na miongoni mwa kizazi cha Ibrāhīm, na miongoni mwa kizazi cha Ya’qūb, na miongoni mwa wale tuliowaongoza kwenye Imani na tukawateua kwa utume na unabii. Wasomewapo aya za Mwingi wa rehema zinazokusanya upweke Wake na hoja Zake wanajipomosha chini hali ya kumsujudia Mwenyezi Mungu kwa kunyenyekea na kujidhalilisha , na wanalia kwa kumcha Yeye, kutakata ni Kwake na kutukuka ni Kwake

    [59] Wakaja, baada ya hawa walioneemeshwa, wafuasi wabaya, waliacha Swala kabisa au waliitoa nje ya wakati wake au waliacha nguzo zake na mambo yake ya lazima na wakafuata yanayolingana na kunasibiana na matamanio yao. Basi hao watapata shari na upotevu na kupita patupu ndani ya Jahanamu

    [60] Lakini aliyetubia dhambi zake miongoni mwao, akamuamini Mola wake na akafanya mema kusadikisha toba yake, hao Mwenyezi Mungu Atakubali toba yao, na wataingia Peponi pamoja na Waumini, na hawatapunguziwa chochote katika matendo yao mema

    [61] Pepo yenye mabustani ya milele na makazi ya daima, nayo ni ile ambayo Mwingi wa rehema Aliwaahidi waja Wake na kuifanya wasiione, nao wakaiamini bila ya kuwa wameiona. Hakika agizo la Mwenyezi Mungu kwa waja Wake la hii Pepo ni lenye kuja, hapana budi

    [62] Watu wa Peponi hawatasikia maneno ya batili humo, lakini watasikia ‘salamu’ ikiwa ndio maamkizi yao. Na watapata riziki yao humo ya chakula na kinywaji daima, kila wanapotaka, asubuhi na jioni, haina kiasi wala hadi maalumu

    [63] Hiyo ndiyo Pepo inayosifiwa kwa sifa hizo, hiyo ndiyo ambayo tutairithisha na kuitoa kuwapa waja wetu wanaotucha kwa kufuata amri zetu na kujiepusha na makatazo yetu

    [64] Na useme, ewe Jibrili, kumwambia Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, «Sisi, Malaika, hatuteremki kutoka mbinguni kuja ardhini isipokuwa kwa amri ya Mola wako kwetu, ni Yake yaliyoko mbele yetu yanayotukabili ya mambo ya Akhera na yale yaliyoko nyuma yetu yaliyopita katika ulimwengu na yale yaliyoko baina ya ulimwengu na Akhera. Amri yote ni Yake ya mahali na wakati. Na hakuwa Mola wako ni Mwenye kusahau kitu chochote miongoni mwa vitu

    [65] «Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wa mbingu na ardhi na vilivyoko baina yake, Ndiye Mmiliki, Muumba na Mwendeshaji wa hivyo vyote, basi muabudu Yeye Peke Yake, ewe Nabii, na uvumilie katika kumtii, wewe na waliokufuata, Hana mfano Wake kitu chochote katika dhati Yake, sifa Zake na vitendo Vyake.»

    [66] Na binadamu kafiri anasema, kwa kukanusha kufufuliwa baada ya kufa, «Je mimi nikifa na nikamalizika, kweli nitatolewa kwenye kaburi langu nikiwa hai?»

    [67] Vipi binadamu huyu kafiri amejisahau nafsi yake? Kwani hakumbuki kwamba sisi tulimuumba mara ya kwanza na hakuwa ni kitu kilichoko

    [68] Naapa kwa Mola wako, ewe Muhammad, tutawakusanya hawa wenye kukanusha kufufuliwa Siku ya Kiyama pamoja na Mashetani, kisha tutawaleta wote kando ya moto wa Jahanamu wakiwa wamepiga magoti, kwa ukubwa wa misukosuko ambayo wamo ndani yake, hali ya kuwa hawawezi kusimama

    [69] Kisha tutawachukua, katika kila pote, wale wakiukaji amri zaidi na wenye kumuasi Mwenyezi Mungu zaidi, tuanze kuwaadhibu

    [70] Kisha sisi ni tunawajua zaidi wale wanaostahili kuingia Motoni na kuadhibika kwa joto lake

    [71] Na hakuna katika nyinyi, enyi watu, yoyote isipokuwa ataufikia huo Moto kwa kupita juu Ṣirāṭ (Njia) iliyotandikwa juu ya daraja la moto wa Jahanamu, kila mmoja kulingana na matendo yake. Hilo ni jambo lenye kuwa kwa lazima, Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Amepitisha na Ameamua kwamba halina budi kuwa, hakuna namana ya kuliepuka

    [72] Kisha tutawaokoa wale ambao walimcha Mola wao kwa kumtii na kujiepusha na kumuasi na tuwaache Motoni wale waliojidhulumu nafsi zao katika hali ya kupiga magoti

    [73] Na watu wakisomewa aya zetu zilizoteremshwa zilizo wazi, wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu wanasemakawaambia Waumini, «Ni pote gani kati yetu na nyinyi lenye mashukio bora zaidi na makalio mazuri zaidi?»

    [74] Na ni mara nyingi tumewaangamiza ummah kabla ya hawa watu wako, ewe Mtume, waliokuwa na vitu vingi kuliko walivyokuwa navyo watu wako na mandhari ya kupendeza zaidi

    [75] Sema, ewe Mtume, kuwaambia wao, «Aliyekuwa amepotea njia ya haki asiyeifuata njia ya uongofu, Mwenyezi Mungu Atampa muhula na Atamnyoshea katika ule upotevu wake, mpaka atakapoyaona kwa yakini yale aliyoyaahidi Mwenyezi Mungu : ima adhabu ya haraka ulimwenguni au kusimama saa ya Kiyama, hapo atajuwa ni nani aliyopo na aliyetulia mahali pabaya na aliye mnyonge wa nguvu na askari

    [76] Na Mwenyezi Mungu Anawaongezea waja Wake, walioongoka katika dini Yake, uongofu juu ya uongofu walionao kwa yale yanayowapitia mara kwa mara ya kuyaamini malazimisho ya Mwenyezi Mungu na kuyafuata kivitendo. Na matendo mema yaliyosalia yana malipo bora kwa Mwenyezi Mungu kesho Akhera, na yana matokeo bora na mwisho mwema

    [77] Je ushajua, ewe Mtume, na ukaona ajabu kuhusu huyu kafiri, Al-'Ās bin Wail na walio mfano wake? Kwani yeye alizikufuru aya za Mwenyezi Mungu, akazikanusha na akasema, «Nitapatiwa-nitapatiwa huko Akhera mali na watoto.»

    [78] Je, amechungulia ghaibu akaona kuwa yeye atakuwa na mali na watoto, au ana ahadi juu ya hilo kutoka kwa Mwenyezi Mungu

    [79] Mambo siyo kama vile alivyodai yule kafiri, kwani yeye hana ujuzi wala hakupewa ahadi. Tutatayaandika anayoyasema ya urongo na uzushi juu ya Mwenyezi Mungu, na huko Akhera tutamuongezea aina mbali mbali za mateso, kama alivyojiongezea upotovu na upotevu

    [80] Na tutamrithi mali yake na watoto wake, na atatujia Siku ya Kiyama akiwa peke yake, hana mali wala watoto

    [81] Na washirikina wamewachukua waungu wanaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ili wawatetee na wajipatie nguvu kwao

    [82] Mambo sivyo kama wanavyodai. Hawa waungu hawatakuwa ni nguvu kwao, lakini waungu hawa watawaruka huko Akhera kuwa waliwaabudu wao na watakuwa ni wenye kusaidia katika kuteta na wao na kuwakanusha , kinyume na vile walivyodhania juu yao

    [83] Je, huoni, ewe Mtume, kwamba sisi tumewasaliti Mashetani juu ya wenye kumkanusha Mwenyezi Mungu na Mitume Wake, ili wawapoteze na wawaondoe kutoka kwenye utiifu kuwapeleka kwenye uasi

    [84] Basi usiwafanyie haraka, ewe Mtume, kwa kutaka adhabu iwashukie hawa makafiri, kwa kweli sisi tunahesabu umri wao na matendo yao hesabu isiyo na kasoro wala ukawiaji

    [85] Siku ambayo tutawakusanya wachamungu kwa Mola wao Mwenye huruma na wao, wakiwa makundi ya watu wenye kukirimiwa

    [86] na tutawaongoza wenye kumkanusha Mwenyezi Mungu kwa kuwasuta kwa nguvu kuwapeleka Motoni, wakitembea kwa miguu, wakiwa na kiu

    [87] Makafiri hawa hawatakuwa na uwezo wa kumuombea yoyote. Watakaokuwa na uwezo huo ni wale waliochukua ahadi ya hilo mbele ya Mwingi wa rehema, nao ni wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake

    [88] Na hawa makafiri walisema, «Mwenyezi Mungu amejifanyia mtoto.»

    [89] Kwa hakika mumeleta, enyi hao wenye kusema, kwa kusema neno hili, jambo kubwa lililo baya

    [90] Zakaribia mbingu kupasuka kwa ubaya mkubwa wa neno hilo, ardhi kuvunjika vipande-vipande ma majabali kuanguka kwa nguvu kwa kukasirika kwa ajili ya Mwenyezi Mungu

    [91] kwa kumnasibishia mtoto, Mwenyezi Mungu Ametukuka na jambo hilo kutukuka kukubwa sana

    [92] Haifai kwa Mwenyezi Mungu na hainasibiani na Yeye Awe na mtoto, kwani kuwa na mtoto ni dalili ya upungufu na mahitajio, na Mwenyezi Mungu Ndiye Mkwasi Mwenye kuhimidiwa Aliyeepushwa na sifa zote za upungufu

    [93] Hakuna aliye mbinguni, miongoni mwa Malaika, wala aliye ardhini, miongoni mwa binadamu na majini, isipokuwa atamjia Mola wake Siku ya Kiyama akiwa ni mja mdhalilifu mnyenyekevu mwenye kukubali uja wake Kwake

    [94] Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Amewadhibiti viumbe Wake wote na Ameijua idadi yao, hakuna yoyote miongono mawao mwenye kufichika na Yeye

    [95] Na kila mtu, miongoni mwa viumbe, atamjia Mola wake, Siku ya Kiyama, hali ya kuwa hana mali wala watoto pamoja na yeye

    [96] Hakika wale waliomuamini Mwenyezi Mungu, wakawafuata Mitume Wake na wakatenda mema kulingana na sheria Yake, Mwingi wa rehema Atatia katika nyoyo za waja Wake mahaba ya kuwapenda

    [97] Hakika sisi tumeirahisisha hii Qur’ani katika ulimi wako wa Kiarabu, ewe Mtume, ili uwape bishara wachamungu, miongoni mwa wafuasi wako, na uwaonye kwayo wakanushaji wenye utesi sana kwa njia isiyofaa

    [98] Na mara nyingi tumewaangamiza ummah waliotangulia kabla ya watu wako, humuoni yoyote miongoni mwao na husikii sauti yao, basi hivyo ndivyo watakavyokuwa makafiri wa watu wako, tutawaangamiza kama tulivyowaangamiza waliotanguli kabla yao. Katika hii pana onyo na agizo la kuwaangamiza wakanushaji wenye ushindani wa ubatilifu

    Twa Ha

    Surah 20

    [1] «Ṭā, Hā» Yametangulia maelezo kuhusu herufi za mkato mwanzo wa sura ya Al -Bqarah

    [2] Hatukuiteremsha Qur’ani kwako, ewe Mtume, ujisumbue kwa jambo usiloliweza kulifanya

    [3] Lakini tumeiteremsha iwe ni mawaidha, ili ajikumbushe nayo mwenye kuogopa adhabu ya Mwenyezi Mungu apate kujikinga nayo kwa kutekelaza faradhi na kujiepusha na mambo ya haramu

    [4] Hii Qur’ani ni teremsho kutoka kwa Mwenyezi Mungu Ambaye Ameumba ardhi na mbingu zilizo juu

    [5] Mwingi wa rehema, juu ya 'Arsh Amelingana, yaani Amekuwa juu na Ameangatika, kulingana kunakonasibiana na utukufu Wake na ukubwa Wake

    [6] Ni Vyake vilivyoko mbinguni na vilivyoko ardhini na vilivyoko baina yake na vilivyoko ndani yake, kwa kuviumba, kuvitamalaki na kuviendesha

    [7] Na ukitoa sauti, ewe Mtume, katika kusema ukaifanya ya juu au ya chini, basi hakuna chochote kinachofichika kwa Mwenyezi Mungu, Anajua siri na kilichofichika zaidi kuliko siri katika vitu ambavyo nafsi yako inakuzungumzia

    [8] Mwenyezi Mungu Ambaye hakuna muabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye, ni Yake Peke Yake majina yaliyokamilika katika uzuri

    [9] Na je, imekujia, ewe Mtume, habari ya Mūsā bin ‘Imrān, amani imshukie, katika kurudi kwake kutoka Madyan na kuelekea Misri

    [10] Alipouona moto usiko umewashwa, akasema kuwaambia watu wa nyumbani kwake, «Ngojeni! Mimi nimeuona moto, huenda nikawaletea kinga cha moto mkapata kujitoa ubaridi na mkawasha moto mwingine kwa kinga hiko, au nikapata mtu wa kutuongoza njia.»

    [11] Mūsā alipoufikia ule moto, Mwenyezi Mungu Alimuita, «Ewe Mūsā

    [12] Mimi ni Mola wako, vua viatu vyako, wewe sasa uko kwenye bonde la Tuwā nililolipa baraka. Hivyo ni ili ajiandae kusema na Mola wake

    [13] Na mimi nimekuteua , ewe Mūsā, kwa ujumbe wangu, basi sikiliza yale unayoletewa ya wahyi kutoka kwangu

    [14] Mimi Ndiye Mwenyezi Mungu, hakuna mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa mimi, sina mshirika, basi niabudu mimi na usimamishe Swala ili unikumbuke ndani yake

    [15] Hakika Kiyama ambacho watu hapo watafufuliwa hapana budi ni chenye kutukia. Nakaribia kukificha kwangu mimi mwenyewe, basi ni vipi atakijua mtu yoyote miongoni mwa viumbe. Hivyo ni apate kulipwa kila mtu kwa alilolitenda ulimwenguni, liwe zuri au baya

    [16] Basi asikuepushe, ewe Mūsā, na kukiamini na kujitayarisha nacho, asiyekikubali kuwa kitatukia na asiyetenda ya kumfaa huko na akayafuata matamanio ya nafsi yake na akakikanusha, kwani ukifanya hivyo utaangamia

    [17] Na ni nini hii iliyo kwenye mkono wako wa kulia, ewe Mūsā

    [18] Akasema Mūsā, «Hii ni ni fimbo yangu, naitegemea katika kwenda na ninapigia miti ili mbuzi wangu walishe majani yake yanayoanguka na pia nina maslahi nayo mengine.»

    [19] Mwenyezi Mungu Akamwambia Mūsā, «Itupe fimbo yako!»

    [20] Mūsā akaitupa chini, ikageuka kwa amri ya Mwenyezi Mungu ikawa nyoka anayetembea, na Mūsā akaona jambo kubwa na akazunguka kukimbia

    [21] Mwenyezi Mungu Akasema kumwambia Mūsā, «Mshike huyo nyoka na usimuogope, tutamrudisha kuwa fimbo vile alivyokuwa mwanzo

    [22] Na ukumbatie mkono wako kwenye ubavu wako chini ya shina la mkono utatoka hali ni mweupe kama barafu bila ya kuwa na mbalanga, ili iwe ni alama nyingine

    [23] Tumefanya hivyo ili kukuonesha , ewe Mūsā, dalili zetu kubwa zenye kutolea ushahidi uweza wetu, ukubwa wa ufalme wetu na usahihi wa utume wako

    [24] Enda, ewe Mūsā, kwa Fir'awn, kwa kuwa yeye amepitisha kipimo chake na ametoka kwenye utiifu wa Mola wake, umuite kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumuabudu

    [25] Mūsā akasema, «Ewe Mola wangu! Nikunjulie kifua changu

    [26] nirahisishie mambo yangu

    [27] na nifungulie ulimi wangu uwe na ufasaha wa matamshi

    [28] ili waelewe maneno yangu

    [29] Na unipatie msaidizi miongoni mwa watu wangu

    [30] naye ni Hārūn ndugu yangu

    [31] Nitilie nguvu kwa yeye na uuthibitishe mgongo wangu kwa ajili yake

    [32] Na umshirikishe na mimi katika unabii na ufikishaji ujumbe

    [33] Tupate kukuepusha na kila sifa ya upungufu na tukutakase kwa wingi

    [34] na tukutaje kwa wingi na tukushukuru

    [35] Kwa hakika, wewe ni mwenye kutuona, hakuna chochote kinachofichika kwako miongoni mwa vitendo vyetu.»

    [36] Mwenyezi Mungu Akasema, «Nishakupa kila ulichokiomba, ewe Mūsā

    [37] «Na tulikupa , ewe Mūsā, kabla ya neema hii, neema nyingine ulipokuwa ni mtoto wa kunyonya tukakuokoa na unyanyasaji wa Fir'awn

    [38] «Na hilo ni pale tulipomfahamisha mamako kwa kumtia mawazo kwamba

    [39] muweke mwanao, Mūsā, baada ya kuzaliwa, katika sanduku, kisha ulitie kwenye mto wa Nail. Hapo mto wa Nail utalipeleka hadi ufuoni, na hapo Fir'awn atalichukua, adui yangu na adui yake (huyo aliyomo sandukuni). Na nikayaingiza mapenzi kwako kutoka kwangu, ukawa kwa hilo, ni mwenye kupendwa na waja, na ili ulelewe chini ya uangalizi wangu na ulinzi wangu. Kwenye aya hii kuna kuthibitisha sifa ya jicho ('ayn) kwa Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, kama inavyonasibiana na utukufu Wake na ukamilifu Wake

    [40] «Na pia tulikuneemesha pindi alipokwenda dadako kufuatilia mambo yako, kisha akasema akiwaambia waliokuchukua, ‘Je, niwajulishe nyinyi yule anayeweza kuwalelea na kuwanyonyeshea?’ Basi tukakurudisha kwa mamako baada ya kwamba ulikuwa kwenye mikono ya Fir'awn ili nafsi yake itulie kwa kuokoka kwako na kuzama na kuuawa na asiwe na masikitiko ya kukukosa. Na ulimuua mtu wa kabila la Kibti kimakosa tukakuokoa na makero ya kitendo chako hiko na kuogopa kuuawa. Na tulikuonja maonjo mengi, ukatoka kwa kuogopa ukaenda kwa watu wa Madyan, ukaketi kwao miaka mingi, kisha ukaja kutoka Madyan katika kipindi tulichokipanga kwa kukutumiliza, kuja kulikofikiana na mpango wa Mwenyezi Mungu na matakwa Yake. Na mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu Mwingi wa baraka Aliyetukuka

    [41] «Nimekupa neema hizi, ewe Mūsā, zikiwa ni chaguo langu kwako na uteuzi ili ubebe utume wangu na ufikishe ujumbe wangu na usimame kutekeleza maamrisho yangu na makatazo yangu

    [42] «Enda, ewe Mūsā, wewe na ndugu yako Hārūn, ukiwa na aya zangu zinazoonyesha uungu wangu na ukamilifu wa uweza wangu na ukweli wa utume wako, wala msiwe wanyonge katika kuendeleza utajo wangu

    [43] Endeni, mkiwa pamoja, kwa Fir'awn, kwa kuwa yeye amekiuka mipaka katika ukafiri na udhalimu

    [44] na mumwambie maneno laini, kwani huenda akakumbuka au akamuogopa Mola wake.»

    [45] Mūsā na Hārūn wakasema, «Ewe Mola wetu! Sisi tunaogopa asije akakimbilia kutuadhibu au akajitolea kuipinga haki asiikubali.»

    [46] Mwenyezi Mungu Akasema kumwambia Mūsā na Hārūn, «Msimuogope Fir'awn, kwani mimi niko na nyinyi, nasikia maneno yenu na naona vitendo vyenu

    [47] Basi endeni kwake na mumwambie, ‘Sisi ni wajumbe wawili kutoka kwa Mola wako kwamba uwaache Wana wa Isrāīl na usiwakalifishe matendo wasiyoyaweza. Kwa hakika tumekujilia na ushahidi wa kimiujiza kutoka kwa Mola wako wenye kuonesha ukweli wetu katika ulinganizi wetu. Na kusalimika na adhabu ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ni kwa mwenye kuufuata uongofu Wake

    [48] Mola wako Ametuletea wahyi kwamba adhabu Yake itamshukia aliyekanusha na akaupa mgongo ulinganizi Wake na sheria Yake.’»

    [49] Fir'awn akawaambia wote wawili kwa njia ya kukanusha, «Basi ni nani Mola wenu, ewe Mūsā?»

    [50] Mūsā akamwambia, «Mola wetu ni Yule Ambaye Alikipa kila kitu umbile linalokifaa kulingana na uzuri wa utengezaji Wake kisha akamuongoza kila kiumbe uongofu kamili wa kunufaika kwa kile alichomuumbia Mwenyezi Mungu.»

    [51] Fir'awn akasema kumwambia Mūsā kwa njia ya kukosoa na kuteta, «Mambo yalikuwa vipi kwa ummah waliopita? Na ni vipi habari za kame zilizopita, kwani wao wametutangulia katika ukanushaji na ukafiri?»

    [52] Mūsā alisema kumwambia Fir'awn, «Hilo uliloliuliza halimo kwenye yale tunayoyazungumza, isipokuwa ujuzi wa watu wa hizo kame na mambo waliyoyafanya iko kwa Mola wangu kwenye Kitabu Kilichohifadhiwa (Al-Lawh (al-Mah,fūd) na mimi sina ujuzi nalo. Na Mola wangu Hapotei kwenye vitendo Vyake na hukumu Zake na Hasahau chochote Alichokijua katika hivyo

    [53] Yeye Ndiye Ambaye Amewafanyia ardhi nyepesi ili mnufaike nayo, na Amewatolea kwenye ardhi hiyo njia nyingi, na Ameteremsha kutoka juu mvua, akaitoa kwayo aina tafauti za mimea

    [54] Kuleni, enyi watu, miongoni mwa vizuri tulivyowaoteshea, na muwalishe wanyama howa wenu na wa mstuni. Kwa kweli, katika yote yaliyotajwa pana alama nyingi za uweza wa Mwenyezi Mungu na ni ulinganizi wa umoja Wake na kumpwekesha Yeye kwa kumuabudu kwa wenye akili timamu

    [55] Kutoka kwenye ardhi tumewaumba nyinyi, enyi watu, na humo tutawarudisha baada ya kufa, na kutoka humo tutawatoa mkiwa hai ili muhisabiwe na mulipwe

    [56] Na kwa kweli, tulimuonyesha Fir'awn dalili zetu na hoja zetu zote zenye kujulisha uungu wetu na uweza wetu na ukweli wa ujumbe wa Mūsā, akazikanusha na akakataa kuikubali haki

    [57] Fir'awn akasema, «Je, ewe Mūsā, umetujia ili upate kututoa majumbani mwetu kwa uchawi wako huu

    [58] «Basi tutakuletea uchawi mfano wa uchawi wako. Weka wakati maalumu kati yetu na wewe, ambao sisi tusiende kinyume nao na pia wewe usiende kinyume nao, katika mahali palipolingana palipo sawa kati yetu na wewe.»

    [59] Mūsā akasema kumwambia Fir'awm, «Ahadi yenu ya mkusanyiko ni suku ya sikukuu, pindi watu watakapojipamba na kukusanyika kutoka kila sehemu na upande kipindi cha asubuhi.»

    [60] Hapo Fir'awn aliyapa mgongo hali ya kuyapuuza yale ya ukweli aliyoletewa na Mūsā na akawakusanya wachawi wake, na baada yake akaja katika kipindi cha mkusanyiko

    [61] Mūsā akasema kuwaambia wachawi wa Fir'awn akiwapa mawaidha, «Jihadharini, msimzulie Mwenyezi Mungu urongo, Asije Akawamaliza nyinyi kwa adhabu itokayo Kwake na Akawaondoa kabisa. Na kwa kweli, amepata hasara mwenye kumzulia Mwenyezi Mungu urongo.»

    [62] Hapo wachawi walivutana na wakizungumza kwa siri kuhusu mambo yao. Walisema, «Kwa kweli, Mūsā na Hārūn ni wachawi

    [63] wanataka kuwatoa nyinyi nchini mwenu kwa uchawi wao na kuuondoa mfumo mkubwa mnaoushikilia wa uchawi

    [64] Basi vithibitisheni vitimbi vyenu na muwe na nia moja juu ya hilo pasi na kutengana kati yenu, kisha njooni mkiwa ni safu moja na mvirushe vilivyomo mikononi mwenu kwa mara moja ili muyashangaze macho ya watu na muushinde uchawi wa Mūsā na ndugu yake. Na kwa kweli, leo amepata matakwa yake yule atakayekuwa juu ya mwenzake akamshinda na akambana.»

    [65] Wachawi wakasema, «Ewe Mūsā! Ima uirushe fimbo yako mwanzo au tuanze sisi kuvirusha tulivyonavyo.»

    [66] Mūsā aliwaambia, «Basi rusheni nyinyi mwanzo hivyo mlivyonavyo.« Hapo wakazirusha kamba zao na fimbo zao

    [67] na ikamsawirikia Mūsā kuwa zile ni nyoka wanatembea na akaingiwa na kicho rohoni mwake

    [68] Mwenyezi Mungu Akamwambia Mūsā wakati huo, «Usiogope chochote, kwani wewe ndiye uliye juu ya hawa wachawi na uliye juu ya Fir'awn na askari wake, na utawashinda

    [69] «Na irushe fimbo yako iliyoko kwenye mkono wako wa kulia, itazimeza kamba zao na fimbo zao, kwani walichokifanya mbele yako si chochote isipokuwa ni vitimbi vya mchawi na kiinimacho cha uchawi. Na hafaulu mchawi kwa uchawi wake popote anapokuwa.»

    [70] Hapo Mūsā aliirusha fimbo yake, ikavimeza walivyovifanya, haki ikajitokeza na hoja ikasimama juu yao. Hapo wachawi walijitupa chini wakiwa katika hali ya kusujudu na wakasema, «Tumemuamini Mola wa Hārūn na Mūsā. Lau huu ulikuwa ni uchawi hatungalishindwa.»

    [71] Fir'awn akasema kuwaambia wachawi, «Mumemkubali vipi Mūsā, mkamfuata na mkamtambua kabla sijawaruhusu kufanya hivyo? Kwa kweli, Mūsā ndiye mkubwa wenu aliyewafundisha uchawi, kwa hivyo mumemfuata. Basi nitaikatakata mikono yenu na miguu yenu kinyume: mkono wa upande huu na mguu wa upande mwingine, na nitawasulubu kwa kuifunga miili yenu kwenye vigogo vya mitende. Na hapo mtajua, tena mtajua, enyi wachawi, ni yupi kati yetu, ni mimi au Mola wa Mūsā, mwenye adhabu kali zaidi na yenye kudumu zaidi kuliko mwingine?»

    [72] wachawi wakasema kumwambia Fir'awn,« Hatutakutanguliza wewe tukakusikiliza na tukaifuata dini yako juu ya yale aliyotuletea Mūsā yaliyo waziwazi yanayojulisha ukweli wake na ulazima wa kumfuata na kumtii Mola wake. Na hatutautanguliza uola wako wa kujipangia juu ya uola wa Mwenyezi Mungu Aliyetuumba. Basi fanya kile utakachotufanya. Ukweli ni kwamba utawala wako ni hapa katika maisha ya duniani. Na utakachokifanya kwetu si kitu isipokuwa ni adhabu itakayokoma kwa kukoma dunia hii

    [73] «Kwa kweli, sisi tumemuamini Mola wetu, tumemkubali Mtume Wake na tumeyatumia aliyokuja nayo ili Mola wetu Atusamehe dhambi zetu na yale uliyotulazimisha nayo ya kufanya uchawi wa kupingana na Mūsā. Na Mwenyezi Mungu ni bora kwetu kuliko wewe, ewe Fir'awn, kwa kumlipa aliyemtii na ni mwenye adhabu ya kudumu zaidi kwa anayemuasi na kuenda kinyume na amri Yake.»

    [74] Ukweli wa mambo ni kwamba mwenye kumjia Mola wake hali ya kuwa amemkanusha, basi atapata moto wa Jahanamu atakaoteswa nao; hatakufa humo akapumzika wala hataishi maisha ambayo atayafurahia

    [75] Na mwenye kumjia Mola wake hali ya kuwa amemuamini na ametenda matendo mema, basi atapata daraja za juu

    [76] katika mabustani ya Pepo ya kukaa daima ambayo mito inapita chini ya miti yake, wakiwa ni wenye kukaa humo milele. Neema hiyo ya daima ni malipo kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa mwenye kujisafisha nafsi yake na uchafu, uovu na ushirikina, na akamuabudu Mwenyezi Mungu, Peke Yake, akamtii na akajiepusha na matendo ya kumuasi na akakutana na Mola wake na huku hamshirikishi yoyote kati ya viumbe Vyake katika kumuabudu

    [77] Na kwa hakika tulimpelekea wahyi Mūsā tukamwambia, «Toka Misri usiku ukiwa pamoja na waja wangu miongoni mwa Wana wa Isrāīl, na uwatolee njia kavu baharini, bila kumuogopa Fir'awn na askari wake kuwa watawaandama na kuwakuta na bila ya kuogopa kuzama

    [78] Basi Mūsā alikwenda usiku pamoja na Wana wa Isrāīl akavuka nao kwenye njia ya bahari, hapo Fir'awn pamoja na askari wake wakawafuata, maji yakawafinika, kwa namna ambayo hakuna anayoijua isipokuwa Mwenyezi Mungu, na wote walizama isipokuwa Mūsā na watu wake

    [79] Na aliwapoteza Fir'awn watu wake kwa ukafiri aliyowapambia na ukanushaji, na hakuwafanya waandame njia ya uongofu

    [80] Enyi Wana wa Isrāīl, kumbukeni tulipowaokoa na adui yenu Fir'awn na tukafanya agano lenu ni upande wa kulia wa jabali la Tūr ili muteremshiwe Taurati, na tutukawateremshia jangwani vitu vya nyinyi kuvila vinavyofanana na gundi vyenye utamu wa asali, na ndege wanaofanana na tomboro

    [81] Kuleni riziki yetu nzuri na msifanye uadui kwa kuoneana nyinyi kwa nyinyi, kwani mkifanya hivyo hasira zangu zitawashukia, na yoyote mwenye kushukiwa na hasira zangu, basi yeye ameangamia na amepata hasara

    [82] Na mimi ni Mwingi wa kusamehe kwa anayetubia kutokana na dhambi zake na ukanushaji wake, akaniamini mimi na akafanya matendo mema kisha akaongoka kufuata njia ya ukweli na akasimama imara juu yake

    [83] Na ni kitu gani kilichokuharakisha, ewe Mūsā, ukawatangulia watu wako kwenda upande wa kulia wa jabali la Tūr na ukawaacha nyuma yako

    [84] Akasema, «Wao wako nyuma yangu watanifikia. Na nimewatangulia kuja kwako, ewe Mola wangu, ili uridhike na mimi.»

    [85] Mwenyezi Mungu akasema kumwambia Mūsā, «Hakika sisi tumewatahini watu wako, baada ya wewe kuwaepuka, kwa kuabudu kigombe, na Sāmirīy amewapoteza.»

    [86] Hapo Mūsā akarudi kwa watu wake akiwa ni mwenye hasira na masikitiko na akawaambia, «Enyi watu wangu, Si Mwenyezi Mungu Amewaagiza agizo zuri la kuiteremsha Taurati? Kwani hiyo ahadi imepitiwa na kipindi kirefu mkaona kuwa agizo limechelewa au mlitaka kufanya jambo ambalo kwalo zitawashukia hasira kutoka kwa Mola wenu ndipo mkaenda kinyume na agizo langu nililowaahidi, mkaabudu kigombe na mkaacha kujilazimisha na amri zangu

    [87] Wakasema, «Ewe Mūsā, sisi hatukwenda kinyume na agizo lako la kutuchagua, lakini sisi tulibebeshwa mizigo mizito ya pambo la watu wa Fir'awn, tukaitupa kwenye shimo lenye moto kwa amri ya Sāmirīy, na pia Sāmirīy alitupa mchanga aliokuwa nao wa kwato za farasi wa Jibrili, amani imshukiye.»

    [88] Hivyo basi Sāmirīy aliwatengenezea Wana wa Isrāīl kutokana na dhahabu kigombe ambacho ni mwili unaotoa sauti ya ng’ombe. Hapo wakasema waliofitinika nacho , «Huyu ndiye mola wenu na mola wa Mūsā aliyemsahau na kughafilika naye

    [89] Je, hawaoni hawa walioabudu kigombe kwamba hicho hakianzi kusema nao wala hakiwapi jawabu na hakiwezi kuwaondolea madhara wala kuwaletea manufaa

    [90] Kwa kweli, Hārūn aliwaambia Wana wa Isrāīl kabla Mūsā hajarudi kuwajia, «Enyi watu wangu, hakika nyinyi mumetahiniwa na huyu kigombe, ili aonekana wazi mwenye Imani miongoni mwenu apate kujitenga na mwenye kukanusha. Kwa hakika Mola wenu ni Al-Rahmān (Mwingi wa Rehema) si mwingine. Basi nifuateni katika lile ninalowaitia la kumuabudu Mwenyezi Mungu na muitii amri yangu katika kufuata sheria Yake.»

    [91] Walisema wenye kuabudu kigombe miongoni mwao, «Hatutaacha kusimama kukiabudu kigombe mpaka Mūsā arudi kwetu.»

    [92] Mūsā akasema kumwambia ndugu yake Hārūn, «Ni jambo gani lililokuzuia ulipowaona wamepotea na kuwa kando na Dini yao

    [93] usinifuate ukawa na mimi na ukawaacha? Je, umeasi amri yangu niliyokuamrisha kwayo ya kushika mahali pangu na kutengeneza baada ya mimi kuondoka

    [94] Kisha Mūsā alishika ndevu za Hārūn na kichwa chake akawa amvuta upande wake. Hārūn akamwambia, «Ewe mwana wa mamangu, usinishike ndevu zangu wala nywele za kichwa changu! Mimi niliogopa, lau niliwaacha na nikakutana na wewe, usije ukasema, «Umewagawanya Wana wa Isrāīl na hukutunza wasia wangu wa kukaa nao vizuri.»

    [95] Mūsā akasema kumwambia Sāmirīy, «Una jambo gani, ewe Sāmirīy? Na ni lipi lililokupelekea kufanya hilo ulilolifanya

    [96] Sāmirīy akasema, «Nilimuona ambaye hawakumuona, naye ni Jibrili, amani imshukiye, juu ya farasi, wakati walipotoka baharini na Fir'awn akazamishwa na askari wake, hapo niliteka kwa kitanga changu cha mkono mchanga wa athari ya kwato za farasi wa Jibrili nikaurusha kwenye pambo ambalo kwalo nimetengeneza kigombe, kikawa ni kigombe chenye mwili, chenye kutoa sauti ya ng’ombe, na kikawa ni kisirani na mtihani. Kufanya hivyo ndivyo nafsi yangu inayoamrisha maovu ilivyonipambia.»

    [97] Mūsā akasema kumwambia Sāmirīy, «Basi enda! Mateso yako katika uhai wa duniani ni uishi ukiwa umetengwa na umwambie kila mtu, ‘ Sigusi wala siguswi’, na una agizo huko Akhera la wewe kuadhibiwa na kuteswa, Mwenyezi Mungu Hataenda kinyume na agizo hilo na utalikuta. Na muangalie muabudiwa wako ambaye umesimama kumuabudu, tutamchoma kwa moto kisha tutampeperusha baharini achukuliwe na upepo kusiwe na athari yake yoyote yenye kusalia

    [98] Kwa kweli, mola wenu, enyi watu, ni Mola Mmoja Ambaye hakuna muabudiwa isipokuwa Yeye, ujuzi Wake umeenea kila kitu

    [99] Na kama tulivyokusimulia, ewe Mtume, habari za Mūsā na Fir'awn na watu wao, tunakupa habari za waliokutangulia wewe. Na tumekuletea hii Qur’ani kutoka kwetu iwe ni ukumbusho kwa mwenye kujikumbusha

    [100] Mwenye kuipa mgongo hii Qur’ani, asiiamini na asiitumie, atakuja Siku ya Kiyama akiwa amebeba dhambi kubwa

    [101] Hao watakaa milele kwenye adhabu, na utawakera mzigo huo mzito wa madhambi kwa kuwa umewatia Motoni

    [102] Siku Malaika watakapovuvia kwenye pembe ili kutoa ukulele wa kufufuliwa na tuwaongoze makafiri siku hiyo wakiwa rangi ya buluu, miili yao imegeuka na pia macho yao kwa matukio makubwa yaliyojiri

    [103] Huku wakinong’onezana baina yao na wakiambiana wao kwa wao, «Hamkukaa kwenye uhai wa ulimwenguni isipokuwa siku kumi

    [104] Sisi ni wajuzi zaidi kwa wanayoyasema na wanayoyaficha pindi anaposema mjuzi wao zaidi na mwenye akili nyingi miongoni mwao, «Hamkuishi isipokuwa siku moja,» kwa ufupi wa kipindi cha duniani watakaouhisi ndani ya nafsi zao Siku ya Kiyama

    [105] Na wanakuuliza watu wako, ewe Mtume, kuhusu hatima ya majabali Siku ya Kiyama. Basi waambie, «Mola wangu Atayaondoa mahali pake na atyafanya ni vumbi lililopeperushwa

    [106] «Aiwache ardhi wakati huo imetandazika, imelingana na imekuwa kavu haina mimea

    [107] Mwenye kuiangalia haoni, kwa kulingana kwake, mbeteko wala muinuko wala mteremko

    [108] Katika siku hiyo, watu wataifuata sauti ya mlinganizi kuelekea kwenye kisimamo cha Kiyama, hakuna njia ya kuepuka ulinganizi wa mwenye kulingania, kwani huo ni haki na kweli kwa viumbe wote. Hapo sauti zitatulia kwa kumnyenyekea Mwingi wa rehema, hutasikia kutoka kwao isipokuwa sauti ya ndani isiyosikika

    [109] Katika siku hiyo, hayatamfaa maombezi kiumbe yoyote, mpaka iwapo Mwingi wa rehema Ataruhusu na Ataridhika na mwenye kuombewa, na hiyo haiwi isipokuwa kwa mwenye Imani mwenye ikhlasi

    [110] Anayajuwa mambo ya Kiyama yaliyoko mbele ya watu na mambo ya dunia yaliyoko nyuma yao, na viumbe Vyake hawamzunguki kwa kumjua, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake

    [111] Na nyuso za viumbe zitamnyenyekea na kumdhalilikia mwenye kuziumba, Mwenye kila maana ya uhai mkamilifu kama inavyonasibiana na utukufu Wake, Ambaye Hafi , Anayesimama kuendesha kila kitu, Aliye Mkwasi wa kutomuhitajia asiyekuwa Yeye. Kwa kweli, amepata hasara Siku ya Kiyama mwenye kumfanya ni mshirika wa Mwenyezi Mungu yoyote kati ya viumbe Vyake

    [112] Na mwenye kufanya matendo mema na hali yeye anamuamini Mola wake, hataogopa maonevu ya kuongezwa maovu yake wala unyanyasaji wa kupunguziwa mema yake

    [113] Na kama tulivyowapendekezea wenye Imani kufanya matendo mema na tukawaonya makafiri kuendelea kwenye maasia yao na ukanushaji wao aya zetu, tuliiteremsha hii Qur’an kwa lugha ya Kiarabu wapate kuielewa. Na tumefafanua ndani yake aina za maonyo kwa matarajio wamuogope Mola wao, au hii Qur’ani iwaletee ukumbusho wapate kuwaidhika na kuzingatia

    [114] Ameepukana Mwenyezi Mungu, kutakata ni Kwake, na Amekuwa juu na ametakasika na kila upungufu, Aliye Mfalme Ambaye mamlaka Yake yamemtendesha nguvu kila mfalme na mjeuri, Mwenye kuendesha kila kitu, Ambaye Yeye Ndiye ukweli, na agizo Lake ni kweli, na onyo Lake ni kweli, na kila kitu kinachotoka Kwake ni kweli. Na usifanye haraka, ewe Mtume, ya kushindana na Jibrili katika kuipokea Qur’ani kabla hajaimaliza, na useme, «Mola wangu! Niongezee elimu juu ya ile uliyonifundisha.»

    [115] Na kwa hakika tulimuusia Ādam kabla hajakula kutoka kwenye ule mti, asile kutoka kwenye mti huo na tukamwambia kwamba Iblisi ni adui yako na mke wako, basi wasiwatoe nyinyi wawili kutoka Peponi, mkajasumbuka wewe na mke wako duniani. Basi Shetani akamshawishi, naye akamtii na akausahau wasia. Na hatukumpata na nia ya nguvu yenye kumfanya aitunze ile amri aliyopewa

    [116] Na kumbuka, ewe Mtume, pindi tuliposema kuwaambia Malaika, «Msujudieni Ādam sijida ya maamkizi na kutoa heshima, nao wakatii na wakasujudu, lakini Iblisi alikataa kusujudu

    [117] Tukasema, «Ewe Ādam! Kwa hakika, huyu Iblisi ni adui yako na mke wako, basi jihadharini naye na msimtii kwa kuniasi mimi, asije akawatoa Peponi ukasumbuka ukitolewa humo

    [118] Hakika yako wewe, ewe Ādam, una neema ya kula kwenye Pepo hii na hutashikwa na njaa, na pia kuvaa na hutakaa tupu

    [119] na una neema ya kutoshikwa na kiu katika hii Pepo na kutopatwa na joto la jua

    [120] Hapo Shetani akamshawishi Ādam na akamwambia, «Je, nikushauri kwa kukuonesha mti ambao lau utakula kutoka mti huo utakaa milele na hutakufa na utakuwa na ufalme usiokoma na usiokatika

    [121] Basi Ādam na Ḥawwā’ wakala kutoka kwenye mti ambao Mwenyezi Mungu Aliwakataza nao, na papo hapo tupu zao zikafunuka, na kabla ya hapo zilikuwa zimesitiriwa na macho yao hayazioni. Hapo wakawa wanakata majani ya miti ya Peponi na kujiambisa nayo ili kufinika tupu zao zilizowafunuka. Na Ādam alienda kinyume na amri ya Mola wake na akapotea kwa kula kutoka kwenye mti ambao Mwenyezi Mungu Alimkataza asiukaribie

    [122] Kisha Mwenyezi Mungu Akamteua Ādam, Akamkaribisha, Akaikubali toba yake na Akamuongoza njia njema ya kuifuata

    [123] Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Akamwambia Ādam na Ḥawwā’ «Shukeni kutoka kwenye Pepo muende ardhini nyote pamoja na Iblisi, kwani nyinyi na yeye ni maadui. Mtakapojiwa na uongofu na maelezo kutoka kwangu, basi mwenye kufuata uongofu wangu na maelezo yangu na akayatumia yote mawili, yeye atakuwa amefuata usawa duniani na ataongoka, na hatasumbuka huko Akhera kwa kuteswa na Mwenyezi Mungu

    [124] Na mwenye kuupa mgongo utajo wangu ambao ninamkumbusha nao, atakuwa na maisha ya dhiki na usumbufu katika uhai wa kilimwengu, hata kama inaonekana kuwa yeye ni miongoni mwa watu wa utajiri na nafasi, na kaburi yake itambana na aadhibiwe humo, na tutamfufua Siku ya Kiyama akiwa kipofu wa kutoona na wa hoja

    [125] Atasema huyo mwenye kuupa mgongo utajo wa Mwenyezi Mungu , «Mola wangu! Kwa nini umenifufua nikiwa kipofu na hali nilikuwa nikiona duniani?»

    [126] Mwenyezi Mungu Atasema kumwambia, «Nimekufufua ukiwa kipofu, kwa kuwa wewe zilikujia aya zetu zikiwa na hoja waziwazi, ukazipa mgongo na usiziamini. Na kama ulivyoziacha ulimwenguni, basi leo vilevile utaachwa Motoni

    [127] «Hivyo ndivyo tutakavyomtesa, kwa mateso ya hapa duniani, yule aliyepita kiasi katika kujidhulumu nafsi yake akamuasi Mola wake na asiziamini aya zake. Na kwa kweli, adhabu ya kesho Akhera waliyoandaliwa ina uchungu mkali zaidi na inadumu na kujikita zaidi, kwa kuwa haikatika na haimaliziki.»

    [128] Kwani haukuwaongoza watu wako kwenye njia ya sawa, Ewe mtume, ule wingi watu waliokanusha kabala yao tuliowaangamiza na hali wao wanatembea kwenye nyumba zao na wanaziona athari za kuangamia kwao? Kwa hakika, katika wingi wa watu hao na mabaki ya adhabu waliyopewa pana mazingatio na mawaidha kwa wenye akili za kuelewa

    [129] Na lau si neno litokalo kwa Mola wako na muda uliotajwa mbele Yake, wangalipata maangamivu yenye kulazimiana na wao hapa ulimwenguni, kwa kuwa wao wanastahili kuyapata kwa sababu ya ukafiri wao

    [130] Basi vumilia, ewe Mtume, juu ya yale wanayoyasema wakanushaji kuhusu wewe ya sifa mbaya na urongo, umtakase Mola wako kwa kumshukuru katika Swala ya alfajiri kabla jua halijachomoza, na katika Swala ya alasiri kabla ya jua kuzama, na katika Swala ya ishai nyakati za usiku, na umtakase Mola wako kwa kumshukuru katika Swala ya adhuhuri, kwani kipindi chake kiko nchani mwa nusu ya kwanza ya mchana na nusu ya pili, na katika Swala ya magaribi, ili ulipwe kwa matendo haya kwa namna ambayo utaridhika nayo

    [131] Na usivitazame vitu ambavyo tumewastarehesha navyo hawa washirikina na wanaofanana na wao miongoni mwa aina ya starehe. Kwani hivyo ni pambo lenye kuondoka katika uhai huu wa kilimwengu. Tumewastarehesha navyo,ili tuwatahini navyo. Na riziki ya Mola wako na malipo yake ni bora kwako kuliko hivyo tulivyowastarehesha navyo na ni vya kudumu zaidi, kwani havina kukatika wala kumalizika

    [132] Na waamrishe watu wako, ewe Nabii, kuswali na ujisubirishe nayo. Sisi hatutaki kutoka kwako mali, kwani sisi ndio tunaokuruzuku na kukupa. Na mwisho mwema ulimwenguni na Akhera ni wa wachajimungu

    [133] Na walisema wenye kukukanusha, ewe Mtume, «Basi si utuletee alama itokayo kwa Mola wako yenye kuonesha ukweli wako?» Kwani hikuwajia hii Qur’ani yenye kuisadukisha haki iliyomo kwenye Vitabu vilivyopita?»

    [134] Na lau sisi tuliwaangamiza wenye kukanusha kwa adhabu kabla hatujawapelekea Mtume na kuwateremshia Kitabu, wanagalisema, «Mola wetu! Si utuletee Mtume kutoka kwako tupate kumuamini na tufuate aya zako na Sheria yako, kabla ya sisi kudhalilika na kuhizika kwa adhabu yako.»

    [135] Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, «Kila mmoja kati yetu sisi na nyinyi anagojea matukio ya ulimengu na ni nani atakayepata ushindi na kufaulu. Basi ngojeni, mtajua ni watu gani walioko kwenye njia iliyokaa sawa na nani, kati yetu sisi na nyinyi, aliyeongoka kwenye haki.»

    Manabii

    Surah 21

    [1] Umekaribia wakati wa kuhesabiwa watu juu ya matendo waliyoyatanguliza, pamoja na hivyo, makafiri wanaishi wakiwa kwenye hali ya kupumbaa, wameghafilika na uhakika huu, wakiwa kwenye hali ya kulipa mgongo onyo hili

    [2] Hakuna kitu chochote katika Qur’ani chenye kuteremka, kinachosomwa kwao na chenye kuwakumbusha upya, isipokuwa huwa wakikisikia wakiwa katika hali ya kucheza na kufanya shere

    [3] Nyoyo zao zimeghafilika na Qur’ani, zimeshughulika na ubatilifu wa dunia na matamanio yake, hawayafahamu yaliyomo ndani yake. Lakini madhalimu miongoni mwa Makureshi wamejikusanya pamoja juu ya jambo lililofichika, nalo ni kueneza yale ambayo kwayo wanawazuia watu kumuamini Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa kuwa yeye ni binadamu mfano wao, hatafautiani na wao katika kitu chochote, na kwamba Qur’ani aliyoileta ni uchawi. (Wanawaambia kwa kusema) «Vipi mutakuja kwake na mumfuate na hali kwamba mnaona kwamba yeye ni binadamu kama nyinyi?»

    [4] Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, analirudisha kila jambo kwa Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, akasema, «Mola wangu Analijua jambo la mbinguni na la ardhini na Anayajua maneno yenu mnayoyasema kwa siri, na Yeye Ndiye Mwenye kuyasikia maneno yenu, Ndiye Mwenye kuzijua hali zenu.» Katika hiya pana tishio kwao na onyo

    [5] Lakini makafiri wameikanusha Qur’ani: kuna wanaosema kwamba ni mchanganyiko wa ndoto zisizo na ukweli, kuna wanaosema kwamba ni uzushi na urongo na si wahyi na kuna wanaosema kwamba Muhammad ni mshairi na kwamba haya ambayo amekuja nayo ni mashairi, na akiwa anataka tumuamini basi na atuletee miujiza yenye kuonekana kama vile ngamia wa Ṣāliḥ na miujiza ya Mūsā na 'Īsā na yale ambayo walikuja nayo Mitume kabla yake

    [6] Hakuna mji wowote ulioamini kabala ya makafiri wa Makkah ambao watu wake walitaka miujiza kutoka kwa Mtume wao na ikatokea kweli, bali walikanusha na tukawaangamiza. Basi je, makafiri wa Makkah wataamini iwapo itakuwa miujiza waliyoitaka? Sivyo, wao hawataamini

    [7] Na hatukuwatumiliza kabla yako , ewe Mtume, isipokuwa wanaume wa kibinadamu ambao tunawaletea wahyi, na hatukuwatumiliza Malaika. Basi waulizeni, enyi watu wa Makkah, wenye ujuzi wa vitabu vilivyoteremshwa huko nyuma iwapo hamjui hilo

    [8] Na hatukuwafanya wale Mitume kabla yako wawe nje ya tabia ya binadamu, wasihitaji chakula na kinywaji, na hawakuwa ni wenye kukaa milele wakawa hawafi

    [9] Kisha tuliwatimizia Manabii na wafuasi wao yale tuliyowaahidi ya ushindi na kuokolewa, na tukawaangamiza wenye kuzionea nafsi zao kwa kumkanusha kwao Mola wao

    [10] Kwa kweli tumekuteremshia hii Qur’ani; ndani yake kuna enzi yenu na utukufu wenu katika ulimwengu na Akhera iwapo mtajikumbusha nayo. Je, hamuyafahamu yale ambayo kwayo niliwatukuza nyinyi juu ya wasiokuwa nyinyi

    [11] Na kuna miji mingi ambayo watu wake walikuwa madhalimu kwa kukanusha kwao yale ambayo Mitume wao walikuja nayo. Ndipo tukawaangamiza kwa adhabu iliyowamaliza wote, na tukafanya wapatikane watu wengine wasiokuwa wao

    [12] Walipoiyona, madhalimu hawa, adhabu yetu kali ikiwashukia na wakaziona ishara zake, wakitahamaki wakawa wanakimbia kwa haraka kutoka mjini mwao

    [13] Wakaitwa wakiwa katika hali hii na kuambiwa, «Msikimbieni, na rudini kwenye ladha zenu na starehe zenu katika ulimwengu wenu wenye kupumbaza na nyumba zenu zilizojengwa, kwani huenda mkaulizwa jambo kuhusu ulimwengu wenu. Na hiyo ni kwa njia ya kuwafanyia shere na ubishi.»

    [14] Hawakuwa na majibu yoyote isipokuwa ni kukubali makosa yao na kusema, «Ee maangamivu yetu! Tumejidhulumu nafsi zetu kwa ukafiri wetu.»

    [15] Yaliendelea maneno hayo - nayo ni yale ya kujiapiza wenyewe maangamivu na kukubali kuwa wamejidhulumu wenyewe- kuwa ndiyo mwito wao wanaoukariri mpaka tukawafanya kama mimea ya ukulima iliyovunwa, wakiwa wametulia hawana uhai. Basi kuweni na hadhari, enyi mnaoambiwa, na kuendelea kumkanusha Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, isije ikawashukia nyinyi yale yaliyowashukia watu waliopita kabla yenu

    [16] Na hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyoko baina yake kwa upuuzi na ubatilifu, lakini ni kwa kusimamisha hoja juu yenu, enyi watu, na ili mzingatie kwa hayo yote mpate kujua kwamba Yule Aliyeziumba hizo mbingu na ardhi hafanani na chochote, na hakuna anayefaa kuabudiwa isipokuwa Yeye

    [17] Lau tulitaka kujifanyia kipumbazi cha mtoto au mke tungalikifanya kutoka kwetu, na sio kwenu. Hatukuwa ni wenye kufanya hilo kwa kuwa ni muhali kwetu kuwa na mtoto au mke

    [18] bali tunaisukuma haki na tunaifafanua, na hapo urongo unapomoka, na punde si punde unaondoka na kupotea. Na nyinyi, enyi washirikina, mtapata adhabu huko Akhera kwa kumsifu kwenu Mola wenu kwa sifa zisizonasibiana na Yeye

    [19] Ni milki ya Mweyezi Mungu, Aliyetakasika na sifa za upungufu, kila aliye mbinguni na ardhini. Na wale Malaika walioko mbele Yake hawafanyi kiburi kumuabudu Yeye wala hawachoki kufanya hivyo. Basi vipi itafaa Ashirikishwe na kitu ambacho ni mja wake na kiumbe chake

    [20] Wao (hao Malaika) wanamtaja Mwenyezi Mungu na wanamtakasa daima, hawadhoofiki wala hawachoki

    [21] Itakuwa sawa vipi kwa washirikina kujifanyia waungu walemevu kutoka ardhini wasioweza kuhuisha wafu

    [22] Lau mbinguni na ardhini kulikuwa na waungu wasiokuwa Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, wenye kuyaendesha mambo yake, ungaliharibika mpango wake. Basi Mwenyezi Mungu, Bwana wa 'Arsh, Ameepukakana na sifa za upungufu na Ametakasika na kila sifa ambayo wakanushaji makafiri wanamsifu nayo ya urongo, uzushi na kila aibu

    [23] Miongoni mwa dalili za kupwekeka Kwake, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, kwa kuumba na kustahiki kuabudiwa ni kwamba Yeye Haulizwi kuhusu uamuzi Wake kwa viumbe Wake na kwamba viumbe Wake wote ndio wenye kuulizwa kuhusu matendo yao

    [24] Je, hawa washirikina waliwafanya wasiokuwa Mwenyezi Mungu kuwa ni waungu wanaonufaisha na kudhuru na wanaohuisha na kufisha? Sema, ewe Mtume, kuwaambia wao, «Leteni dalili zenu mlizonazo juu ya hao mliowafanya waungu.» Kwani hakuna, ndani ya Qur’ani niliyokuja nayo wala ndani ya Vitabu vilivyotangulia, dalili yoyote ya yale mliyoyafuata.» Na wao hawakushirikisha isipokuwa ni kwa sababu ya ujinga wao na kuigiza, kwa hivyo wao ni wenye kuupa mgongo ukweli na ni wenye kuukataa

    [25] Na hatukutumiliza kabla yako, ewe Mtume, mjumbe yoyote isipokuwa tunampatia wahyi kwamba hapana mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu. Basi mtakasieni ibada Yeye Peke Yake

    [26] Na washirikina walisema, «Mwenyezi Mungu Amejifanyia mtoto» kwa madai yao kwamba Malaika ni watoto wa kike wa Mwenyezi Mungu. Ametakasika Mwenyezi Mungu na hilo! Malaika ni waja wa Mwenyezi Mungu waliokurubishwa waliohusishwa kwa kupewa matukufu

    [27] na wao kwa utiifu wao mzuri hawasemi isipokuwa lile ambalo Mola wao Amewaamrisha kwalo, na hawafanyi tendo lolote mpaka Awaruhusu

    [28] Na hakuna tendo lolote miongoni mwa matendo ya Malaika, lililopita au linalofuatia, isipokuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Analijua na anawahesabia kwalo. Na hawatangulii kumuombea yoyote isipokuwa yule ambaye Mwenyezi Mungu Ameridhika wamuombee. Na wao kwa kumuogopa Mwenyezi Mungu wana hadhari ya kuenda kinyume na maamrisho Yake na makatazo Yake

    [29] Na yoyote miongoni mwa Malaika atakayedai kwamba yeye ni mungu pamoja na Mwenyezi Mungu, kwa kukadiria, basi malipo yake ni moto wa Jahanamu. Na mfano wa malipo hayo ndivyo tunavyomlipa kila dhalimu mshirikina

    [30] Kwani hawakujua hawa ambao wamekufuru kwamba mbingu na ardhi zilikuwa zimeshikana, hakuna kipambanuzi baina yao, hakuna mvua kutoka juu wala mimea kutoka kwenye ardhi, kisha tukazipambanua kwa uweza wetu, tukateremsha mvua kutoka juu na tukatoa mimea kutoka kwenye ardhi na tukajaalia kutokana na maji kila kitu chenye uhai. Basi je hawaamini hawa wakanushaji, wakayasadiki wanayoyaona na wakamuhusuMwenyezi Mungu tu kwa ibada

    [31] Na tumeumba kwenye ardhi majabali yenye kuituliza isitikisike na tumetoa, kwenye hayo majabali, njia kunjufu, ili viumbe waongoke kwenye njia za kujitafutia maisha yao na kumpwekesha Muumba wao

    [32] Na tumeifanya mbingu ni sakafu ya ardhi, haiinuliwi na nguzo, nayo imetunzwa, haianguki wala haipenywi na mashetani. Na makafiri wameghafilika na kupumbaa kutozizingatia alama za mbnguni (Jua, mwezi na nyota) na kutozifikiria

    [33] Na mwenyezi Mungu , Aliyetukuka, Ndiye Aliyeumba usiku ili watu wapate kutulia, na mchana ili wapate kutafuta maisha. Na Ameumba jua, likiwa ni alama ya mchana, na mwezi, ukiwa ni alama ya usiku. Na kila kimojawapo ya hivyo viwili kina njia ya kupitia na kuogelea hakiendi kando nayo

    [34] Hatukumfanya mwadamu yoyote kabla yako, ewe Mtume, asalie duniani milele. Basi ufapo wewe, kwani wao wana matumaini ya kuishi daima baada yako? Hili haliwi. Katika aya hii pana dalili kwamba Al-Khadhir, amani imshukie, ameshakufa, kwa kuwa yeye ni mwanadamu

    [35] Kila nafsi ni yenye kuonja kifo hapana budi namna utakavyorefuka umri wake duniani. Na kuweko kwake maishani hakukuwa isipokuwa ni mtihani wa majukumu ya maamrisho na makatazo na mabadiliko ya hali, mazuri na mabaya, kisha baada ya hapo kuna kurudi na kurejea kwa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, ili kuhesabiwa na kulipwa

    [36] Na makafiri wanapokuona, ewe Mtume, wanakuashiria kwa kukufanyia shere, huwa wakiambiana wao kwa wao, «Je, ni huyu yule mtu anayewatukana waungu wenu?» Wao wamemkanusha Mwingi wa rehema na wamezikanusha neema Zake na yale Aliyoyateremsha ya Qur’ani na uongofu

    [37] Ameumbwa mwanadamu akiwa na pupa, anayafanyia haraka mambo na anakuwa na pupa yawe. Na kwa kweli, Makureshi waliifanyia haraka adhabu na wakaona kuwa imechelewa kutokea., Mwenyezi Mungu Akawaonya kwamba Atawaonesha adhabu waliyoifanyia haraka, basi wasimuombe Mwenyezi Mungu awaharakishie na awaletee kwa upesi

    [38] Na makafiri wanasema, wakiifanyia haraka adhabu kwa njia ya shere, «Ni lini itapatikana ile unayotuonya nayo, ewe Muhammad, iwapo wewe na aliyekufuata wewe ni miongoni mwa wakweli.»

    [39] Lau makafiri wanajua watakayoyakuta watakapokuwa hawawezi kuzilinda nyuso zao na migongo yao na Moto na wasiipate wenye kuwanusuru, hawangalibaki kwenye ukafiri wao na hawangaliifanyia haraka adhabu yao

    [40] Hakika Kiyama kitawajia ghafla, hapo wataduwaa na watakuwa na kicho kikubwa na hawataweza kuizuia adhabu isiwapate, na hawatapewa nafasi ya kutubia wala kutoa udhuru

    [41] Mitume kabla yako, ewe Mtume, walifanyiwa shere, ikawafikia wale waliokuwa wakiifanyia shere adhabu ambayo walikiifanyia dhihaka na kejeli

    [42] Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa wanaoifanyia haraka adhabu, «Hakuna anayewahifadhi na kuwalinda na adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwashukia , usiku wenu au mchana wenu, katika kulala kwenu au kuangaza kwenu?» Bali wao wamepumbaa na wameghafilika na Qur’ani na mawaidha

    [43] Je wao wanao waungu wenye kuwazuia wao na adhabu yetu? Kwa hakika, waola wao hawawezi kujinusuru wenyewe, vipi wataweza kuwanusuru wenye kuwaabudu? Na wao hawatanusuriwa kutokana na sisi

    [44] Kwa hakika makafiri na baba zao walighurika na muhula waliopewa kwa kile walichokiona cha mali, watoto na maisha marefu, ndipo wakajikita kwenye ukafiri wao wasiepukane nao, na wakadhani kwamba wao hawataadhibiwa. Kwa kweli, wameghafilika na mpango uliopita, kwani Mwenyezi Mungu anaipunguza ardhi kwenye pambizo zake kwa adhabu Anayoiteremsha kwa washirikina kila sehemu na kushindwa. Je, makafiri wa Makkah Wana nafasi ya kutoka nje ya uwezo wa Mwenyezi Mungu au kukataa kufa

    [45] Sema, ewe Mtume, kuwaambia wale uliotumilizwa kwao, «Siwatishii adhabu ya Mwenyezi Mungu isipokuwa ni kwa wahyi wa Mwenyezi Mungu,» nao ni Qur’ani. «Lakini makafiri hawasikii yale wanayosomewa masikizi ya kuzingatia wanapoonya, na kwahivyo hawafaidiki nayo.»

    [46] Lau liliwapata makafiri fungu la adhabu ya Mwenyezi Mungu wangalijua mwisho wa kukanusha kwao na wangalilikabili hilo kwa kujiapiza maangamivu kwa sababu ya kujidhulumu kwao nafsi zao kwa kumuabudu kwao asiyekuwa Mwenyezi Mungu

    [47] Na Mwenyezi Mungu Ataiweka Mizani ya uadilifu kwa ajili ya Hesabu katika siku ya Kiyama. Hawatadhulumiwa hawa wala wengine kitu chochote, hata kama ni kitendo, kizuri au kibaya, cha kadiri ya chungu mdogo, kitazingatiwa katika hesabu ya mwenyewe. Na inatosha kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyadhibiti matendo ya waja Wake na ni Mwenye kuwalipa kwayo

    [48] Kwa hakika, tulimpa Mūsā na Hārūn hoja na ushindi juu ya maadui wao na pia Kitabu, nacho ni Taurati, ambacho kwacho tumepambanua baina ya ukweli na urongo, na ambacho ni nuru ambayo kwayo wanajioongoza wachamungu wenye kuogopa adhabu ya Mola wao

    [49] Na wao ni wenye kicho na hofu kwa kuuogopa wakati Kiyama kitasimama

    [50] Na hii Qur’ani ambayo Mwenyezi Mungu Ameiteremsha kwa Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukliye, ni ukumbusho kwa anayejikumbusha nayo na akatekeleza amri Zake na akajiepusha na makatazo Yake, ina kheri nyingi na manufaa makubwa. Je, mnaikanusha na hali ina upeo wa uwazi na ufunuzi

    [51] Kwa hakika, tulimpa Ibrāhīm uongofu wake ambao yeye aliwalingania watu waufuate kabla ya Mūsā na Hārūn. Na sisi tulikuwa tunajua kwamba yeye anastahiki hilo

    [52] Pindi aliposema kumwambia babake na watu wake, «Ni masanamu gani hawa mliowatengeneza kisha mkakaa kuwaabudu na mkajilazimisha nao.»

    [53] Wakasema, «Tuliwapata baba zetu wakiwaabudu, na sisi tunawaabudu kwa kuwaiga wao.»

    [54] Ibrāhīm akawaambia, «Kwa hakika nyinyi na wazee wenu, kwa kukuwaabudu kwenu hawa masanamu, muko mbali waziwazi na haki.»

    [55] Wakasema, «Je, neno hili ambalo umekuja nalo kwetu ni la usawa na ukweli, au neno lako ni la mtu anayefanya mzaha na shere, hajui analosema?»

    [56] Ibrāhīm, rehema na amani zimshukie, akasema, «Bali Mola wenu Ambaye ninawalingania mumuabudu Ndiye Mola wa mbingu na ardhi Ambaye Ameziumba, na mimi ni mwenye kulitolea ushahidi hilo

    [57] «Na ninaapa kwa Mwenyezi Mungu, nitawachimba masanamu wenu niwavunjevunje baada ya nyinyi kuondoka kwenda zenu na kuwaacha.»

    [58] Hapo Ibrāhīm akawavunjavunja masanamu akawafanya vipande- vipande vilivyo vidogo na akamuacha mkubwa wao, ili watu wake wapate kumrudia kumuuliza, na ili ulemevu wao na upotevu wao upate kujulikana waziwazi, na ili hoja isimame kwao

    [59] Na watu wakarudi na wakawaona masanamu wao wamevunjwa- vunjwa na wametwezwa. Hapo wakaulizana wao kwa wao, «Ni nani aliyefanya haya kwa waungu wetu? Huyo, kwa kweli, ni dhalimu kwa kuwa na ujasiri juu ya waungu wanaostahiki kuheshimiwa na kutukuzwa.»

    [60] Hapo wale waliomsikia Ibraim akiapa kwamba atawachimba masanamu wao, «Tulimsikia kijana akiwataja kwa ubaya, anaitwa Ibrāhīm.»

    [61] Viongozi wao wakasema, «Mleteni Ibrāhīm mbele ya watu aonekane, wapate kushuhudia kukubali kwake makosa ya aliyoyasema, ili iwe ni hoja dhidi yake.»

    [62] Ibrāhīm akaletwa, na wakamuuliza kwa njia ya kumpinga, «Je, ni wewe uliowavunjavunja waungu wetu?» Wakikusudia masanamu wao

    [63] Ibrāhīm akalipata alitakalo la kuonesha wazi upumbavu wao na huku wakiona, akasema, «Aliyewavunjavunja ni huyu sanamu mkubwa, waulizeni hilo waungu wenu mnaowadai iwapo watasema au watawapa majibu.»

    [64] Hapo wakatahayari na ukawafunukia wazi upotevu wao, vipi wanawaabudu na ilhali wao wanashindwa kujitetea wenyewe kitu chochote wala kuwajibu mwenye kuwauliza? Na wakakubali wenyewe kuwa wamefanya udhalimu na ushirikina

    [65] Punde si punde ukakamavu wao uliwarudia baada ya kushindwa hoja, wakageuka kurudi kwenye ubatilifu wao na wakatumia hoja dhidi ya Ibrāhīm ambayo ni hoja dhidi yao wakasema, «Vipi tutawauliza na hali wewe unajua kuwa hawa hawasemi?»

    [66] Ibrāhīm akasema kwa njia ya kudharau jambo la kuabubudu masanamu, «Vipi mnaabudu masanamu wasionufaisha wanapoabudiwa wala kudhurisha wanapoachwa

    [67] Ubaya ni wenu na ni wa waungu wenu mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka. Kwani hamutii akili mkajua uovu wa haya mliyonayo?»

    [68] Ilipopomoka hoja yao na ukweli ukajitokeza, waliamua kutumia uwezo wao na wakasema, «Mchomeni Ibrāhīm kwa moto mkionesha hasira kwa ajili ya waungu wenu, iwapo nyinyi ni wenye kuwasaidia basi washeni moto mkubwa na mumtupe ndani yake.»

    [69] Mwenyezi Mungu Akamsaidia Mtume Wake na Akauambia moto, «Kuwa baridi na salama kwa Ibrāhīm!» Hivyo basi asiipate na udhia wala asifikiwe na jambo la kuchukiza

    [70] Na wale watu walimtakia Ibrāhīm maangamivu na Mwenyezi Mungu Akavitangua vitimbi vyao na Akawafanya wao wawe ni wenye kushindwa na kuwa chini

    [71] Na tukamuokoa Ibrāhīm na Lūṭ ambaye alimuamini kutoka 'Irāq na tukawatoa huko hadi Shām ambako tulikubariki kwa kheri nyinygi, na huko kulikuwa na Manabaii, rehema na amani ziwashukie, wengi zaidi

    [72] Na Mwenyezi Mungu Alimneemesha Ibrāhīm kwa kumtunuku Isḥāq alipomuomba, na zaidi ya hilo Alimtunuku, kutokana na Isḥāq, Ya'qūb. Na kila mmoja kati ya Ibrāhīm na Isḥāq na Ya'qūb Mwenyezi Mungu Alimjaalia kuwa mwema na mtiifu Kwake

    [73] Na tukamfanya Ibrāhīm, Isḥāq na Ya'qūb kuwa viongozi wa watu, wanawalingania wamuabudu Yeye na kumtii kwa idhini Yake Aliyetukuka, na tuliwaletea wahyi kufanya mema ya kuzifuata kivitendo sheria za Manabii, kusimamisha Swala kwa njia zake na kutoa Zaka. Na wao walizifuata amri hizo na walikuwa watiifu kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake bila Mwingine

    [74] Na tulimpa Lūṭ unabii, kufanya uamuzi baina ya watesi na ujuzi wa amri za Mwenyezi Mungu na Dini Yake. Na tulimuokoa na kijiji chake Sadūm ambacho watu wake walikuwa wakifanya mambo machafu. Wao, kwa sababu ya machafu na maovu ambayo watu wa uovu na uchafu wakiyatenda, walikuwa nje ya utiifu wa Mwenyezi Mungu

    [75] Na Mwenyezi Mungu Akamkamilishia nema, Akamtia ndani ya rehema Yake kwa kumuokoa na kile kilichowafikia watu wake kwa kuwa yeye alikuwa ni miongoni mwa wale wanaofanya matendo ya utiifu Kwake

    [76] Na mkumbuke Nūḥ, ewe Mtume, alipomuita Mola Wake kabla yako na kabla ya Ibrāhīm na Lūṭ, tukaitika mwito wake na tukamuokoa, yeye na watu wake waliomuamini, na makero makubwa

    [77] Na tukamnusuru na vitimbi vya watu waliozikanusha alama zetu zenye kuonesha ukweli wake. Kwa haki, wao walikuwa ni watu wa ubaya, na hivyo basi tuliwazamisha wote kwa mafuriko

    [78] Na kumbuka Nabii wa Mwenyezi Mungu Dāwūd na mwane Sulaiman, ewe Mtume, walipotoa uamuzi juu ya kesi iliyoletwa na wagonvi wawili, kondoo wa mmoja wao waliharibu mimea ya mwingine, walienea kwenye mimea hiyo kipindi cha usiku wakaiharibu. Dāwūd alitoa uamuzi kwamba wale kondoo wawe ni milki ya mwenye mimea wakiwa ni badala ya mimea yake iliyoharibiwa, kwa kuwa thamani ya viwili hivyo ni sawa. Na sisi tuliushuhudia uamuzi wao, haukufichamana kwetu

    [79] Tukamfahamisha Sulaymān kuzingatia maslahi ya pande mbili na kufanya uadilifu, akatoa uamuzi kwamba yule mwenye kondoo ashughulike kutengeneza mimea iliyoharibika na kumalizika kwa muda maalumu ambapo katika muda huo yule mwenye mimea ajifaidishe kwa manufaa ya kondoo, kama vile maziwa, sufi na mfano wake, na baadaye kondoo warudi kwa mwenyewe na mimea irudi kwa mwenyewe, kwa kuwa thamani ya mimea iliyoharibiwa inalingana na manufaa ya wale kondoo. Na kila mmoja kati ya Dāwūd na Sulaymān tulimpa busara na ujuzi. Na tulimfanyia Dāwūd wema wa kumdhalilishia majabali yakawa yanaleta tasbihi anapoleta tasbihi, na vilevile ndege wakawa wanaleta tasbihi, na sisi tulikuwa ni wenye kulifanya hilo

    [80] Na Mwenyezi Mngu Alimhusu Dāwūd, amani imshukiye, kwa kumfundisha kutengeneza nguo za kivita, akizifanya kwa kutunga vikuku vilivyoshikamana, kurahisisha harka ya mwili, ili kuwakinga wapiganaji wasiathiriwe na silaha wanazopigwa. Je, nyinyi ni wenye kushukuru neema ya Mwenyezi Mungu kwenu kupitia kwa mkono wa mja Wake Dāwūd

    [81] Na tulimdhalilishia Sulaymān upepo wenye kuvuma kwa kasi ukimchukua yeye na walio pamoja naye, ukawa unapita kwa amri yake kuelekea ardhi ya Bayt al-Maqdis iliyoko Shām amabayo tuliibariki kwa kheri nyingi. Na ujuzi wetu umeenea vitu vyote

    [82] Na tulimdhalilishia Sulaymān, kati ya mashetani, mashetani ambao alikuwa akiwatuma kufanya yale ambayo wasiokuwa wao wanashindwa nayo, walikuwa wakipiga mbizi baharini wakimtolea lulu na johari, na walikuwa wakimtengenezea vitu avitakavayo kwao, hawakuwa wakiweza kukataa kufanya ayatakayo kutoka kwao. Mwenyezi Mungu Amewahifadhi kwa nguvu Zake na enzi Yake , kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake

    [83] Na kumbuka, ewe Mtume, mja wetu Ayyūb, tulipomtahini kwa madhara na ugonjwa mkubwa mwilini mwake, na akakosa watu wake, mali yake na watoto wake, akasubiri kwa kutaka thawabu, na akamlingania Mola wake, Aliyetukuka na kushinda, kwa kumuomba, «Mimi nimepatikana na madhara, na wewe Ndiye Mwenye huruma kuliko wenye huruma, basi niepushie nayo!»

    [84] Hapo tukayakubali maombi yake, tukamuondolea matatizo na tukamrudishia alichokikosa miongoni mwa wake, watoto na mali mara mbili zaidi. Tulimfanyia hayo kwa huruma itokayo kwetu na ili awe ni kiolezo kwa kila mwenye kuvumilia mitihani, mwenye matumaini ya kupata rehema ya Mola wake na mwenye kumuabudu

    [85] Na kumbuka Ismā'īl, Idrīs na Dhulkifl. Wote hao ni miongoni mwa wavumilivu katika kumtii Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, katika kujiepusha na kumuasi na juu ya makadirio Yake, na kwa hivyo walistahiki kutajwa kwa sifa nzuri

    [86] Na tukawatia ndani ya rehema yetu. Kwa hakika wao ni miongoni mwa wale ambao imetengenea ndani yao na nje yao, wakamtii Mwenyezi Mungu na wakafanya matendo yanayolingana na maamrisho Yake

    [87] Na kumbuka kisa cha mtu wa chewa, naye ni Yūnus mwana wa Mattā, amani imshukie, Mwenyezi Mungu Alimtumiliza kwa watu wake, akawalingania wasimuamini, akawaonya kuwa wataadhibiwa, lakikni hawakurudi nyuma. Na asiwavumilie kama vile Mwenyezi Mungu Alivyomuamrisha na akaondoka kutoka kwao akiwa na hasira juu yao, akiwa amebanwa na kifua kwa kuasi kwao. Na akadhani kwamba Mwenyezi Mungu Hatampa dhiki na kumuadhibu kwa ukiukaji huu. Mwenyezi Mungu Akamtahini kwa dhiki nyingi na kifungo na akamezwa na tewa baharini, na akamlingania Mola wake kwa kumuomba katika magiza ya usiku, bahari na tumbo la tewa hali ya kutubia na kukubali ukiukaji wake kwa kuacha kuwavumilia watu wake, huku akisema, «Hapana muabudiwa kwa haki isipokuwa wewe! Kutakasika na sifa za upungufu ni kwako! kwa hakika mimi nimekuwa miongoni mwa wenye kudhulumu!»

    [88] Basi hapo tukamkubalia maombi yake na tukamuondolea unguliko la shida. Na hivyo ndivyo tunavyowaokoa wakweli wenye kuzifuata sheria zetu kivitendo

    [89] Na kumbuka, ewe Mtume, kisa cha mja wa Mwenyezi Mungu Zakariyya alipomuomba Mola wake Amtunukie wana, wakati umri wake ulipokuwa mkubwa, kwa kusema, «Mola wangu! Usiniache pweke ni siwe na mwana! Basi nitunuku mrithi wa kusimamia mambo ya Dini kwa watu baada yangu mimi, na wewe Ndiye bora wa wenye kusalia na bora wa wenye kusimamia mambo yangu baada yangu kwa uzuri!»

    [90] Tukamkubalia maombi yake na tukamtunuku yeye, akiwa katika hali ya uzee, mwanawe Yaḥyā, na tukamfanya mke wake ni mwema wa tabia na ni mwenye kufaa kushika mimba na kuzaa baada ya kuwa tasa. Kwa kweli, wao walikuwa wakiikimbilia kila kheri, na wakituomba wakitumai kupata mazuri yaliyoko kwetu wakiogopa mateso yetu na walikuwa wadhalilifu na wanyonge kwetu

    [91] Na kumbuka, ewe Mtume, kisa cha Maryam binti ya 'Imran aliyeihifadhi tupu yake na haramu na asifanye uzinifu katika maisha yake. Mwenyezi Mungu Akamtuma Jibrili, amani imshukiye, kwake akapuliza katika mfuko wa kanzu yake, na ule mpulizo ukafika kwenye uzao wake, na Mwenyezi Mungu akamuumba Al-Masīḥ 'Īsā, amani imshukie. Hivyo basi akabeba mimba yake bila ya mume, na kwa ajili hiyo akawa , yeye na mwanawe, ni alama ya uweza wa Mwenyezi Mungu na mazingatio kwa viumbe mpaka kusimama Kiyama

    [92] Manabii hawa wote, dini yao ni moja, nayo ni Uislamu. Nao ni kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu kwa kwa kuwa mtiifu na kumpwekesha Yeye kwa ibada. Na Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Ndiye Bwana wa viumbe, basi muabuduni, enyi watu, Peke Yake, Asiye na mshirika

    [93] Lakini watu walitafautiana juu ya Mitume wao, na wengi wa wafauasi wao katika dini walipambanukana wakawa ni makundi na mapote, wakaabudu viumbe na matamanio. Na wote hao ni wenye kurejea kwetu na ni wenye kuhesabiwa juu ya yale waliyoyafanya

    [94] Basi Mwenye kujilazimisha kumuamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake na akafanya awezayo ya matendo mema kwa kumtii Mwenyezi Mungu na kumuabudu. Kwani Mwenyezi Mungu Hayapotezi matendo Yake wala Hayabatilishi, bali Anayaongeza yote hayo mara nyingi, na atayakuta aliyoyatenda kwenye Kitabu chake siku atakayofufuliwa baada ya kufa kwake

    [95] Haiwezekani kwa watu wa miji tuliyoiangamiza, kwa sababu ya ukanushaji wao na dhulma zao, kurudi duniani kabla ya Siku ya Kiyama ili kurakibisha kasoro zao ambazo walikuwa nazo

    [96] Basi pindi kitakapofunguliwa kizuizi cha Ya’jūj na Ma’jūj, na wakatoka kwenye ardhi za juu wakaenea kwenye pande zake kwa haraka

    [97] hapo Siku ya Kiyama itakuwa imekaribia na vituko vyake vitajitokeza, na hapo utayaona macho ya makafiri yamekodoka hayapepesi kwa kibabaiko kikali, huku wakiwa wanajiapiza maangamivu kwa majuto wakisema, «Ee ole wetu! Kwa hakika tulikuwa tumeghafilika na Siku hii na kujiandalia nayo na kwa hivyo tulikuwa madhalimu.»

    [98] Kwa hakika, nyinyi, enyi makafiri, na vitu ambavyo mlikuwa mkiviabudu badala ya Mwenyezi Mungu, miongoni mwa masanamu, na wale walioridhia muwaabudu, kati ya majini na binadmu, ni viwashio vya moto wa Jahanamu na ni kuni zake, nyinyi na wao humo mtaingia

    [99] Lau hawa ambao mliwaabudu badala ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka walikuwa ni waungu wanaostahiki kuabudiwa, hawangaliingia moto wa Jahanamu pamoja na nyinyi, enyi washirikina. Kwa hakika, wote hao, waabudu na waabudiwa, ni wenye kukaa milele ndani ya moto wa Jahanamu

    [100] Hawa wenye kuadhibiwa Motoni wataona uchungu unaooneshwa na mlio wa sauti zao ambapo pumzi zao zinatoka kwa nguvu sana kutoka kwenye vifua vyao. Na wao wakiwa Motoni hawasikii kwa ukali wa adhabu wanayopewa

    [101] Kwa hakika, wale ambao kimetangulia kwetu sisi kitangulizi chema katika ujuzi wetu kuwa watakuwa ni watu wa Peponi, hao wataepushwa na Moto, hawataungia wala hawatakuwa karibu nao

    [102] Hawatasikia sauti ya mroromo wake na kuchomeka kwa miili humo, kwani wameshakaa kwenye nyumba zao huko Peponi na wamekuwa ni wenye kukaa makao ya milele katika starehe na ladha zake zinazotamaniwa na nafsi zao

    [103] Hakiwatishi wao kituko kikubwa Siku ya Kiyama, bali Malaika watawapa bishara njema kwa kuwaambia, «Hii ndiyo siku yenu mlioahidiwa maandalizi mema kutoka kwa Mwenyezi Mungu na thawabu nyingi.»

    [104] Siku ambayo tutaikunja mbingu kame vile ukurasa unaokunjiwa maandishi yaliyomo ndani na tutawafufua viumbe kama vile walivyokuwa mwanzo walipozaliwa na mama zao. Hiyo ndiyo ahadi ya Mwenyezi Mungu isiyokwenda kinyume. Tumeliahidi hilo ahadi ya kweli tuliyojilazimisha nayo. Hakika sisi daima ni wenye kufanya tunaloahidi

    [105] Na kwa hakika, tuliandika kwenye vitabu vilivyoteremshwa, baada ya kuwa yashaandikwa katika Ubao Uliohifadhiwa, kwamba ardhi watairithi waja wa Mwenyezi Mungu walio wema, wale wanaosimama imara kwa yale waliyoamrishwa na wakajiepusha na yale waliyokatazwa, nao ni ummah wa Muhammad, rehema na amani ya Mwenyezi Mungu zishukiye

    [106] Kwa hakika, kwenye mawaidha haya yanayosomwa pana mazingatio ya kutosha kwa watu wenye kumuabudu Mwenyezi Mungu kwa namna Aliyowaekea na Anayoiridhia kutoka kwao

    [107] Na hatukukutumiliza , ewe Mtume, isipokuwa ni rehema kwa watu wote. Mwenye kukuamini atakuwa mwema na ataokoka, na asiyeamini atapita patupu na atapata hasara

    [108] Sema, «Kile nilicholietewa wahyi na nikatumilizwa kwacho ni kwamba mola wenu Anayestahiki kuabudiwa, Peke Yake, ni Mwenyezi Mungu. Basi jisalimisheni Kwake na mnyoshe shingo zenu kwa kumuabudu.»

    [109] Basi hawa wakiupuka Uislamu waambie, «Ninawafikishia nyote kile ambacho Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Amenitumia wahyi nacho. Mimi na nyinyi tuko sawa katika kuyajua yale ninayowaonya nayo na kuwatahadharisha, na mimi sijui, baada ya hapo, ni lini adhabu mliyoagiziwa itawashukia?»

    [110] Kwa hakika Mwenyezi Mungu Anayajua mnayoyadhihirisha miongoni mwa maneno yenu na mnayoyaficha ndani ya nyoyo zenu, na Atawahesabu kwayo

    [111] Na sijui huenda kukawa kule kucheleweshwa adhabu mliyoitaka iwajie kwa haraka ni mavuto na mtihani kwenu, na ili mjistareheshe ulimwenguni mpaka muda ukome, mpate kuzidisha ukafiri, kisha hiyo iwe ni sababu ya nyinyi kupata mateso makubwa zaidi

    [112] Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, akasema,» Mola wangu! Amua baina yetu na watu wetu walioukanusha Uamuzi wa haki, na tunamuomba Mola wetu Mwingi wa rehema, tunataka msaada Wake tuzibatilishe sifa mnazombandika, enyi makafiri, za ushirikina na ukanushaji na uzushi na juu ya maonyo mnayotuonya kuwa mtakuwa na nguvu na ushindi

    Hija

    Surah 22

    [1] Enyi watu! Tahadharini na mateso ya Mwenyezi Mungu, kwa kufuata amri zake na kuepuka makatazo yake, kwani vituko vitakavyotokea pindi kisimamapo Kiyama na mtetemeko mkubwa wa ardhi utakaofanya pambizo zake zipasukepasuke, ni jambo kubwa ambalo hakuna mwenye kulikadiria wala kulifikia vile litakavyokuwa, wala kujua namna yake isipokua Mola wa viumbe wote

    [2] Siku mtakapokiona Kiyama kimesima, mama atamsahau mtoto wake mchanga aliyempa titi lake kunyoya kwa shida iliyomshukia, mwenye mimba ataharibu mimba yake kwa babaiko na akili za watu zitapotea watakuwa ni kama walevi kwa tukio hilo kubwa na babaiko na hali wao si walevi wa pombe, lakini ni ukali wa adhabu ndio uliowapoteza akili zao na hisia zao

    [3] Na baadhi ya vichwa vya ukafiri miongoni mwa watu wanaleta utesi na wanatilia shaka uweza wa Mwenyezi Mungu wa kufufua, kwa ujinga wao wa kutojua uhakika wa uweza huu na kwa kumfuata kila shetani mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mitume Wake kati ya viongozi wa upotevu

    [4] Mwenyezi Mungu amehukumu na kukadiria juu ya huyu Shetani kwamba yeye ampoteze kila mwenye kumfuata na asimuongoze kwenye ukweli, bali amuandamishe njia ya kupelekea kwenye adhabu ya Jahanamu uliowashwa, ikiwa ni malipo ya kumfuata kwake huyo Shetani

    [5] Enyi watu, mkiwa muna shaka ya kuwa Mwenyzi Mungu atawafufua wafu, basi sisi tumemuumba baba yenu Adam kutokana na mchanga kisha kizazi chake kikazaana kutokana na nutfah, nayo ni manii ambayo mwanamume anayarusha kwenye uzao wa mwnamke, yakageuka kwa uweza wa Mwenyezi Mungu yakawa 'alaqah, nalo ni pande la damu nyekundu iliyo nzito, kisha yakawa mudghah, nacho ni kinofu kidogo cha nyama cha kuweza kutafunika, mara nyingine kikawa kitaumbwa, yaani kiumbike kikamilifu mpaka kifikiye hadi ya kutoka kwa mtoto akiwa hai, na mara nyingine kisiumbike kikamilifu kikatoka kabla ya kutimia, ili tuwafafanulie ukamilifu wa uweza wetu wa kupelekesha miongo ya uumbaji. Na tunakibakisha kwenye zao tunachokitaka, nacho ni kile kinachoendelezwa kuumbwa kwake mpaka wakati wa kuzaliwa kwake na itimie ile miongo ya kuzaliwa wana wa matumboni wakiwa wadogo, wakuwe mpaka wafikie umri wa kuwa na nguvu, nao ni wakati wa ubarobaro na nguvu na kukamilika akili. Na baadhi ya watoto huenda wakafa kabla ya hapo, na baadhi yao wanakuwa mpaka wanafikisha miaka ya ukongwe na udhaifu wa akili, akawa huyu aliyezeeka hajui kitu alichokuwa akikijua kabla ya hapo. Na utaiyona ardhi ni kavu, imekufa haina mimea yoyote, tuyateremshapo maji juu yake, inatikisika kwa mimea ikawa inafunguka, inachepuza, inanyanyuka na kuongezeka kwa kutosheka na maji na ikaotesha kila aina ya mimea mizuri yenye kuwafurahisha wenye kuangalia

    [6] Hayo yaliyotangulia kutajwa, miongoni mwa alama za uweza wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, ndani yake pana dalili ya kukata kwamba Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kutakasika, Ndiye Mola Mwenye kuabudiwa kwa haki Ambaye hakuna anayefaa kuabudiwa isipokuwa Yeye, na Yeye Ndiye Mwenye kuwahuisha wafu, na Yeye ni Muweza wa kila kitu

    [7] Na kwamba wakati wa ufufuzi ni wenye kuja, hilo halina shaka, na kwamba Mwenyezi Mungu Atawafufua wafu kutoka makaburini mwao ili Awahesabu na Awalipe

    [8] Miongoni mwa makafiri kuna wenye kujadili kwa njia ya ubatilifu kuhusu Mwenyezi Mungu na kuhusu kumpwekesha Yeye na kuhusu kumteua Kwake Mitume wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kuhusu kuteremsha Kwake Qur’ani. Kujadili huko ni bila ya ujuzi, ufafanuzi wala kitabu kitokacho kwa Mwenyezi Mungu chenye ushahidi na hoja iliyo wazi

    [9] hali akiipotoa shingo yake kwa kiburi na akiupa mgongo ukweli, ili awazuie wengine wasiingie kwenye Dini ya Mwenyezi Mungu. Basi huyo atapata hizaya ulimwenguni kwa kuangamia na mambo yao kufedheheka; na Siku ya Kiyama tutamchoma kwa Moto

    [10] Na ataambiwa, «Adhabu hiyo ni kwa sababu ya maasia uliyoyafanya na makosa uliyoyachuma, na Mwenyezi Mungu Hamuadhibu yoyote pasi na dhambi.»

    [11] Miongoni mwa watu kuna anayeingia kwenye Uislamu kwa udhaifu na shaka, akawa anamuabudu Mwenyezi Mungu juu ya shaka na ukosefu wa uamuzi, ni kama yule anayesimama kwenye ukingo wa jabali au ukuta, hawi thabiti katika kusimama kwake, huifungamanisha Imani yake na ulimwengu wake: akiishi katika hali ya afya na ukunjufu huendelea kwenye ibada yake, na akipatikana na mitihani ya tabu na shida huyanasibisha hayo na Dini yake, na kwa hivyo huiacha. Ni kama yule anayegeuka kwa uso wake baada ya kulingana sawa, hivyo basi akapata hasara ya ulimwengu, kwani kukufuru kwake hakugeuzi chochote alichokadiriwa katika ulimwengu wake, na akapata hasara ya Akhera kwa kuingia Motoni, na hiyo ni hasara inayoonekana waziwazi

    [12] Huyo aliyepata hasara anakiabudu kitu, badala ya Mwenyezi Mungu, kisichomdhuru lau akikiwacha wala kumnufaisha akikiabudu. Huko ndiko kupotea kulioko mbali na haki

    [13] Anamubudu ambaye madhara yake ya hakika yako karibu zaidi kuliko manufaa yake, ni ubaya ulioje wa muabudiwa huyo kuwa ni muokozi na ni ubaya uilioje wake kuwa ni wakutangamana naye

    [14] Hakika Mwenyezi Mungu Atawatia, wale ambao walimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakajikita katika hiyo Imani na wakafanaya mema, kwenye mabustani ya Pepo ambayo inapata mito chini ya majumba yake ya fahari na miti yake. Hakika Mwenyezi Mungu Anafanya Analolitaka la kuwapa malipo mazuri wenye kumtii kwa ukarimu Wake na kuwatesa wenye kumuasi kwa uadilifu Wake

    [15] Yoyote yule anayeitakidi kwamba Mwenyezi Mungu Aliyetukuka hatamsaidia Mtume Wake kwa kumpa ushindi ulimwenguni kwa kuipa nguvu Dini yake na huko Akhera kumtukuza daraja yake na kumuadhibu aliyemkanusha, basi anyoshe kamba aifunge kwenye sakafu ya nyumba yake kisha ajitie kitanzi kisha aikate hiyo kamba, kisha aangalie iwapo hilo litamuondolea hasira alizonazo ndani ya nafsi yake. Mwenyezi Mungu ni Mwenye kumnusuru Nabii Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, hapana budi

    [16] Na kama Alivyosimamisha Mwenyezi Mungu hoja, miongoni mwa dalili za uweza Wake, juu ya makafiri kuhusu ufufuzi, vilevile Aliiteremsha Qur’ani, ambayo aya zake ziko wazi katika matamshi yake na maana yake na ambayo kwayo Mwenyezi Mungu Anamuongoza anayemtaka aongoke. Kwani hakuna Mwenye kuongoa isipokuwa Yeye

    [17] Hakika wale waliomumini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, na Mayahudi na Sābiūn (watu waliobaki kwenye maumbile yao na hawana dini wanayoifuata) na Wanaswara na Majūs (wnaoabudu moto) na wale walioashirikisha (wanaoabudu masanamu), Mwenyezi Mungu Atapambanua baina yao wote, Siku ya Kiyama, Awatie Waumini Peponi na Awatie makafiri Motoni, Mwenyezi Mungu juu ya kila kitu ni Shahidi, Anayashuhudia matendo yote ya waja, Anayadhibiti na Anayahifadhi, Na Atamlipa kila mtu kile anachostahili, malipo yanayolingana na matendo waliokuwa wakiyafanya

    [18] Je hujui, ewe Mtume, kwamba Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, wanamsujudia Yeye, katika hali ya kunyenyekea na kufuata amri, Malaika walioko mbinguni, viumbe walioko ardhini, jua, mwezi, majabali, miti na wanyama? Na wanamsujudia Mwenyezi Mungu, kwa kutii na kwa hiari, watu wengi, nao ni Waumini. Na kuna watu wengi imepasa adhabu juu yao, na kwa hivyo wao ni watwevu. Na yoyote yule ambaye Mwenyezi Mungu Amemtweza hakuna yoyote wa kumtukuza. Hakika Mwenyezi Mungu Anafanya kwa viumbe vyake Atakalo kuambatana na hekima Yake

    [19] Haya ni mapote mawili ya watu, wametafautiana kuhusu Mola wao: watu wa Imani na watu wa ukafiri, kila mmoja anadai kuwa yeye yuko kwenye usawa. Wale waliokufuru watazungukwa na adhabu yenye sura ya nguo za Moto walizopatiwa wazivae, zitaichoma miili yao na yatamiminwa juu ya vichwa vyao maji yaliyofikia upeo wa ukali

    [20] hapo yateremke ndani ya matumbo yao na viyayuke vilivyomo ndani yake mpaka yapenyeze kwenye ngozi zao yazichome na zitoke na kuanguka

    [21] Na Malaika watawapiga vichwa vyao kwa nyundo za chuma

    [22] Na kila wakijaribu kutoka Motoni, kwa sababu ya makero na mateso walionayo, watarudishwa adhabuni na wataambiwa, «Onjeni adhabu ya Moto unaochoma.»

    [23] Hakika Mwenyezi Mungu Atawatia watu wa Imani na matendo mema kwenye mabustani ya Pepo ambayo starehe yake ni ya daima, inapita mito chini ya miti yake, watapambwa humo kwa makuku ya dhahabu na kwa lulu; na nguo zao za kawaida Peponi ni hariri kwa wanawake na kwa wanaume

    [24] Kwa hakika, Mwenyezi Mungu Aliwaongoza ulimwenguni kwenye neno zuri: tamshi la kumpwekesha Mwenyezi Mungu, kumshukuru na kumsifu, na huko Akhera wamshukuru Mwenyezi Mungu kwa mwisho mwema, kama vile Alivyowaongoza kabla ya hapo kufuata njia ya Uislamu inayosifiwa inayofikisha Peponi

    [25] Hakika wale waliomkufuru Mwenyezi Mungu na wakayakanusha yale ambayo alikuja nayo Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wakawazuia wengine kuingia kwenye Dini ya Mwenyezi Mungu, wakamzuia Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, pamoja na waumini katika mwaka wa Ḥudaybiyah wasiingie Msikiti wa Ḥarām tulioufanya ni wa Waumini wote, wanaokaa hapo na wanaokuja kuukusudia, hao watapata adhabu kali yenye kuumiza. Na yoyote anayetaka, ndani ya Msikiti wa Ḥarām, kuenda kombo na haki kwa njia ya udhalimu na akamuasi Mwenezi Mungu humo ndani, basi tutamuonjesha adhabu kali yenye kuumiza

    [26] Taja, ewe Nabii, pindi tulipomuelezea Ibrāhīm, amani imshukiye, mahali pa Nyumba, tukamtayarishia yeye mahali hapo, na palikua hapajulikani. Na tulimuamrisha aijengi juu ya misingi ya kumcha Mwenyezi Mungu na kumpwekesha na aisafishe na ukafiri na mambo ya uzushi na uchafu, ili iwe ni mahali pakunjufu kwa wenye kuizunguka kwa kutufu na wenye kuswali hapo

    [27] na uwajulishe watu, ewe Ibrāhīm, uwajibu wa Hija juu yao, watakujia kwa kila namna zao, wakiwa wanatembea kwa miguu na wakiwa wanapanda, miongoni mwa ngamia, kila aliyeambata matumbo kwa kutembea na kufanya kazi na sio kwa udhaifu. Watakuja kutoka njia ya mbali

    [28] ili kuyahudhuria yenye kuwafaa ya kusamehewa dhambi zao, kulipwa thawabu za utekelezaji wa ibada yao ya Hija na utiifu wao, kujipatia mapato katika biashara zao na mengine yasiokuwa hayo. Na ili wataje jina la Mwenyezi Mungu kwa kuchinja wanyama ambao kwao wanajisongeza karibu na Mwenyezi Mungu, miongoni mwa ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo, katika siku maalumu: nazo ni siku ya kumi ya Mfungotatu na siku tatu baada yake, kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema Zake. Na wao wameamrishwa kwa kupendekezewa kula katika vichinjwa hivi na kumlisha kutokana nazo masikini ambaye umasikini wake umembana

    [29] Kisha wale mahujaji wakamilishe matendo ya ibada yaliyosalia ya kujifungua na kutoka kwenye kifungo cha ibada yao ya Hija, nako ni kwa kuondoa uchafu uliokusanyika kwenye miili yao, kukata kucha zao na kunyoa nywele zao, na watekeleze yale waliyojilazimsha nafsi zao ya kuhiji na kufanya Umra na kuchinja wanyama wa tunu, na waitufu kwa kuizunguka Nyumba huru ya kale ambayo Mwenyezi Mungu Ameikomboa isitawaliwe kimabavu na watu wasioijali, nayo ni Alkaba

    [30] Hiyo Aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu ya kuondoa uchafu, kutekeleza nadhiri na kuitufu Nyumba ndiyo Aliyoyapasisha Mwenyezi Mungu, basi yatukuzeni. Na yoyote mwenye kuyatukuza Aliyoyatakasa Mwenyezi Mungu, na miongoni mwayo ni matendo Aliyoyawekea ibada ya Hija kwa kuyatekeleza kikamilifu kwa kumtakasia Mwenyezi Mungu, basi hilo ni bora zaidi kwake, ulimwenguni na Akhera. Na Mwenyezi Mungu Amewahalalishia nyinyi kula wanyama-howa isipokuwa kile Alichokiharamisha kwenu katika kile mnachosomewa ndani ya Qur’ani miongoni mwa mizoga na mengineyo, basi kiepukeni. Katika hili pana kubatilisha kile ambacho Waarabu walikuwa wakikiharamisha cha baadhi ya wanyama-howa. Na jiekeni mbali na uchafu ambao ni masanamu na urongo wa kumzulia Mwenyezi Mungu

    [31] Hali ya kulingana sawa kwa Mwenyezi Mungu juu ya kumtakasia matendo, kumuelekea Yeye kwa kumuabudu Yeye Peke Yake na kumpwekesha kwa utiifu na kumuepuka kila asiyekuwa Yeye kwa kukataa ushirikina, kwani mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu chochote, mfano wake- katika kuwa mbali kwake na uongofu na katika kuangamia kwake na kuanguka kwake kutoka kwenye kilele cha Imani hadi kwenye shimo la ukafiri na wakawa Mashetani wanamnyakuwa kutoka kila upande - ni kama mfano wa mtu aliyeanguka kutoka mbinguni, ima ndege watamnyakuwa na kumkatakata viungo vyake au kimbunga kikali cha upepo kitamchukua kimtupe mahali mbali sana

    [32] Hayo ndiyo Aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu ya kumpwekesha na kumtakasia ibada. Na yoyote mwenye kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu na akayatukuza mambo makubwa ya Dini, na miongoni mwayo ni matendo ya Hija na sehemu zake na wanyama wanaochinjwa huko, kwa kuchagua walio wazuri na walio wanono, basi kutukuza huko ni katika vitendo vya wenye nyoyo zenye kusifika kwa kumcha Mwenyezi Mungu na kumuogopa

    [33] Muna nyinyi, katika wanyama hawa wa kutolewa tunu, manufaa ya nyinyi kunufaika nayo miongoni mwa sufi, maziwa, kipando na megineyo ambayo hayawadhuru hao wanyama mpaka wakati wa kuchinjwa huko kwenye Nyumba ya kale, nako ni eneo lote takatifu

    [34] Na kila kundi lenye kuamini lililotangulia, tumelifanyia mambo ya ibada ya kuchinja na kumwaga damu, hayo ni kwa ajili wapate kutaja jina la Mwenyezi Mungu Aliyetukuka wakati wa kuchinja kile tulichowaruzuku cha hawa wanyama-howa na wamshukuru. Basi Mola wenu, enyi watu, ni Mola Mmoja, Yeye ni Mwemyezi Mungu. Hivyo basi iandameni amri Yake na amri ya Mtume Wake. Na uuwape bishara njema, ewe Mtume, wale wanyenyekevu waliosalimu amri kwa Mola wao, kwamba watapata kheri mbili: ya ulimenguni nay a Akhera

    [35] Wanyenyekevu hawa wenye kujinyongesha (kwa Mwenyezi Mungu) miongoni mwa sifa zao ni kwamba wao Atajwapo Mwenyezi Mungu Peke Yake, wanaiyogopa adhabu Yake na wanakuwa na hadhari wasimuasi, na wakipatikana na shida na matatizo, wanasubiri juu ya hayo wakiwa na matumaini kupata malipo mema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, wanatekeleza Swala kikamilifu, na wao pamoja na hayo wanatoa, katika kile Alichowaruzuku Mwenyezi Mungu, katika mambo yanayowapasa ya Zaka, matumizi ya watoto na kila ambaye matumizi yake yanawalazimu, katika njia ya Mwenyezi Mungu na katika matumizi yanayopendekezwa yasio ya lazima

    [36] Na tumewafanyia nyinyi kule kuchinja ngamia ni miongoni mwa alama za Dini na mambo yake makubwa. Ili mpate kujisongeza karibu na Mwenyezi Mungu kwayo. Katika hao nyinyi, enyi wenye kujisongeza karibu naye, muna kheri katika manufaa yake ya kula, kutoa sadaka na kupata malipo ya thawabu. Basi semeni mnapowachinja, «Bismillāh» (kwa jina la Mwenyezi Mungu). Na ngamia huchinjwa akiwa amesimama, miguu yake mitatu imepangwa na mmoja umefungwa, basi akianguka kwa mbavu zake, huwa amekuwa halali kumla. Wale waliomchinja kwa ajili ya ibada na wale kitu katika mnyama huyo na wamlishe kutokana naye aliyekinai, naye ni muhitaji asiyeomba kwa kujihifadhi, na muhitaji anayeomba kumaliza haja yake. Hivi ndivyo Alivyowadhalilishia Mwenyezi Mungu ngamia, huenda mukamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwadhalilishia

    [37] Hazitamfikia Mwenyezi Mungu nyama za vichinjwa hivyi wala damu zake kitu chochote, kitakachomfikia Yeye ni kule kumtakasia kwenu katika hivyo na kuwa lengo lake ni radhi za Mwenyezi Mungu Peke Yake. Hivyo basi Amewadhalilishia nyinyi, enyi wenye kujikurubisha, ili mumtukuze Mwenyezi Mungu na mumshukuru kwa kuwaongoza kwenye haki, kwani Yeye Anastahiki hilo. Na uwape bishara njema, ewe Nabii, wenye kufanya wema kwa kumuabudu Mwenyezi Mungu Peke Yake na kuwafanyia wema viumbe vyake, kupata kila lema na kufaulu

    [38] Hakika Mwenyezi Mungu Anawalinda Waumini na uadui wa makafiri na vitimbi vya waovu, kwani Yeye, Aliyeshinda na kutukuka, Hampendi kila mwingi wa hiana wa amana ya Mola wake, mwingi wa kukanusha neem Zake

    [39] Waislamu, mwanzo wao, walikuwa wamekatazwa kupigana na makafiri, wameamrishwa kuvumilia maudhi yao. Maudhi ya washirikina yalipofikia upeo wake na Mtume akatoka Makkah hali ya kugura kwenda Madina na Uislamu ukawa na nguvu, Mwenyezi Mungu Aliwaruhusu Waislamu kupigana kwa sababu hiyo ya maonevu yaliyowashukia na uadui. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwanusuru na kuwadhalilisha maadui wao

    [40] Wale ambao walilazimishwa kutoka majumbani mwao, si kwa lolote isipokuwa ni kwa kuwa wamesilimu na wamesema, «Mola wetu ni Mwenyezi Mngu Peke Yake.» Na lau si mpango Aliouiweka Mwenyezi Mungu wa kuondoa maonevu ambayo kwayo wananufaika watu wa dini zote zilizoteremshwa na kuurudisha ubatilifu kwa kuruhusu kupigana, haki ingalishindwa katika kila ummah, ardhi ingaliharibiwa, sehemu za ibada zingalivunjwa, miongoni mwa mindule ya watawa, makanisa ya Wanaswara, majumba ya ibada ya Mayahudi na misikiti ya Waislamu ambayo Wanaswali ndani yake, na wanamtaja Mwenyezi Mungu humo kwa wingi. Na mwenye kufanya bidii kuitetea Dini ya Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu Atamnusuru juu ya adui yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Asiyeshindwa, ni Mshindi Asiyefikiwa, Amewatendesha nguvu viumbe na Amezishika paa za nyuso zao

    [41] Wale tuliowaahidi kuwa tutawanusuru ndio wale tukiwapa utulivu kwenye ardhi na kuwatawalisha humo kwa kuwapa ushindi juu ya adui wao, wanasimamisha Swala kwa kuiitekeleza kwa nyakati zake kwa namna zake, wanatoa Zaka za mali zao kuwapa wastahiki wake, wanaamrisha kila ambalo Mwenyezi Mungu Ameliamrisha la haki Zake na haki za waja Wake na wanakataza kila ambalo Mwenyezi Mungu Amelikataza na Mtume Wake. Na ni wa Mwenyezi Mungu Peke Yake mwisho wa mambo yote, na mwisho mwema ni wa uchamungu

    [42] Na wakikukanusha watu wako, ewe Mtume, basi wamewatangulia wao katika kukanusha Mitume wao watu wa Nūḥ,' Ād, Thamūd

    [43] na watu wa Ibrāhīm na watu wa Lūṭ

    [44] na watu wa Madyan waliomkanusha Shu'ayb na pia Fir'awn na watu wake walimkanusha Mūsā. Sikuwaharakishia ummah hao mateso, bali niliwapa muda kisha kila mmoja wa hao niliupatiliza kwa adhabu. Ilikuwaje vile nilivyowakataza wao ukafiri wao na ukanushaji wao na nilivyowabadilishia neema waliokuwa nayo kwa adhabu na maangamivu

    [45] Ni miji mingi iliyojidhulumu kwa ukafiri wake, tuliwaangamiza watu wake, nyumba zao zikavunjwa zikawa ziko tupu hazina wakazi wake, visima vyake vikawa havichotwi maji na majumba yake ya fahari yaliyo marefu yaliyopambwa hayakuwakinga watu wake na adhabu kali

    [46] Si watembee hao wakanushaji wa Makureshi kwenye ardhi wajionee athari za walioangamizwa, wafikirie kwa akili zao na wazingatie na wasikie habari zao kusikia kwa mazingatio wapate kuwaidhika? Kwani upofu si upofu wa macho, hakika ya upofu wenye kuangamiza ni upofu wa busara wa kutoijua haki na kutozingatia

    [47] Na makafiri wa Kikureshi, kwaujinga wao, wanakuharakisha, ewe Mtme, uwaletee adhabu ambayo uliwaonya nayo baada ya kuwa wakakamavu juu ya ukafiri. Mwenyezi Mungu Hataenda kinyume na ahadi yake ya adhabu aliyowaonya nayo, haina budi kutuka. Na hapa duniani Aliwaharakishia hiyo, siku ya vita vya Badr. Na siku moja miongoni mwa siku mbele ya Mwenyezi Mungu ni kama miaka alfu moja mnazozihesbu katika miaka duniani

    [48] Kuna miji mingi ilikuwa kwenye udhalimu, kwa ukakamavu wa watu wake juu ya ukafiri, nikawapa muda , na sikuwaharakishia adhabu na kwa hivyo wakaghurika, kisha nikawachukuwa kwa kuwaadhibu katika hii dunia, na ni kwangu ndio marejeo yao baada ya kuangamia kwao nitawapa adhabu wanayostahili

    [49] Sema, ewe Mtume, «Enyi watu! Mimi si kuwa isipokuwa ni muonyaji kwenu mwenye kumfikishia Mwenyezi Mungu ujumbe Wake

    [50] Basi wale wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na imani hiyo ikajikita kwenye nyoyo zao na wakafanya matendo mema, watapata msamaha wa dhambi zao kutoka kwa Mola wao na sitara ya kufinika matendo ya uasi yaliyotokana na wao na riziki nzuri isiyokatika nayo ni Pepo

    [51] Na wale wenye kujitahidi kufanya vitimbi ili kuzitangua aya za Qur’ani kwa kuzikanusha hali ya kuwa ni watesi na washindani, basi hao ndio watu wa Moto wenye kuwaka, wataungia na watasalia humo milele.»

    [52] Na hatukuwatumiliza kabla yako wewe, ewe Mtume, Mtume yoyote wala Nabii isipokuwa asomapo kitabu cha Mwenyezi mungu, Shetani anatia katika kisomo chake wasiwasi na tashwishi, ili kuwazuilia watu kufuata kile anachokisoma. Lakini Mwenyezi Mungu Anatangua vitimbi vya Shetanai, Anauondoa ushawishi wake na Anathibitisha aya Zake zilizo wazi. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyokuwa na yatakayokuwa, hakuna kinachofichika Kwake chochote, ni Mwingi wa hekima katika makadirio Yake na amri Zake

    [53] Na hakikua kitendo hiki kutoka kwa Shetani isipokuwa Mwenyezi Mungu Akifanye ni mtihani kwa wale ambao ndani ya nyoyo zao muna shaka na unafiki na kwa wale washirikina washupavu wa nyoyo ambao haliathiri kwao kemeo lolote. Na kwa hakika, madhalimu miongoni mwa hawa na wale wako kwenye uadui mkubwa na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na upingaji haki ulio mbali na usawa

    [54] Na ili wapate kujua wenye elimu ambao wanapambanua, kwa ujuzi wao, baina ya ukweli na urongo kwamba Qur’ani tukufu ndio haki iliyoteremka juu yako, ewe Mtume, kutoka kwa Mwenyezi Mungu, haina udanganyifu ndani yake na hakuna njia yoyote ya Shetani kuifikia, na kwa hiyo imani yao inaongezeka na nyoyo zao zinainyenyekea. Na hakika ya Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaongoa wale walioiamini na wakamuamini Mtume Wake kwenye njia ya haki iliyo wazi, nayo ni Uislamu, na Atawaokoa kwayo na upotevu

    [55] Na hawataacha makafiri wenye kukanusha kuendelea kuwa kwenye shaka juu ya Qur’ani uliokuja nayo mpaka Kiyama kiwajie kwa ghafula na hali wao wako juu ya ukanushaji wao, au iwajie wao adhabu ya Siku isiyokuwa na wema ndani yake, nayo ni Siku ya kiyama

    [56] Ufalume na mamlaka katika Siku hii ni ya Mwenyezi Mungu Peke Yake, na Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Ataamua baina ya Waumini na makafiri. Wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafanya matendo mema, ni zao wao starehe za daima kwenye mabustani ya Pepo

    [57] Na wale walioukataa upwekwe wa Mwenyezi Mungu, wakawakanusha Mitume Wake na wakazipinga aya za Qur’ani, basi hao watapata adhabu yenye kuwafanya wanyonge na kuwatweza ndani ya moto wa Jahanamu

    [58] Na wale waliyotoka majumbani mwao kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu na kuinusuru Dini Yake, yoyote kati yao atakayeuawa akiwa katika hali ya kupigana na makafiri, na yoyote kati yao atakayekufa bila kupigana, Mwenyezi Mungu Atawaruzuku Pepo na starehe zake zisizokatika wala kuondoka. Na kwa hakika, Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Ndiye Mbora wa wenye kuruzuku

    [59] Atawatia Mola wao tena Atawatia mahali pa kuingia ambapo watapapenda, napo ni Peponi. Na kwa hakika Mwenyezi Mungu Anamjua sana yule anayetoka katika njia Yake na mwenye kutoka kwa ajili ya ulimwengu, ni Mpole kwa wale waliomuasi hawafanyii haraka kuwatesa

    [60] Hilo ni jambo tulilokusimulia la kuwatia Peponi waliogura(katika njia ya Mwenyezi Mungu), na mwenye kufanyiwa uadui na kuonewa basi yeye ameruhusiwa kupambana na huyo mhalifu kwa kitendo kama chake, na atakuwa hana makosa. Na akirudi yule mhalifu kumuonea na akafanya udhalimu, basi Mwenyezi Mungu Atampa ushindi yule mdhulumiwa aliyeonewa, kwani haifai afanyiwe uadui kwa kuwa amejilipizia. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehefu ni Mwingi wa kughofiria, Anasamehe dhambi za wenye kukosea, hawafanyii haraka kuwatesa na anazifinika dhambi zao

    [61] Huyo Aliyewaekea hukumu hizo za uadilifu Ndiye wa kweli, na Yeye Ndiye Muweza waAlitakalo. Na katika uweza Wake ni kwamba Yeye Anaziingiza saa za usiku zipunguazo kwenye saa za mchana, na anaziingiza saa za mchana zipunguazo kwenye saa za usiku na kwamba Mwenyezi Mungu ni Msikizi wa kila sauti, ni Muoni wa kila kitendo, hakifichiki kitu chochote Kwake

    [62] Hayo ni kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye Mola wa haki Ambaye hapana yoyote Anayepasa aabudiwe isipokuwa Yeye na kwamba vile wanavyoviabudu washirikina miongoni mwa masanamu na waungu-bandia wanaodaiwa kufanana na Yeye ndio batili wasionufaisha wala kudhuru, na kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye Aliye juu ya viumbe vyake kwa dhati, cheo na utendeshaji nguvu, Ndiye Aliyejiepusha na wanaodaiwa kufanana na Yeye na kuwa wendani Wake, Aliye Mkuu katika dhati Yake, majina Yake na sifa Zake. Yeye ni Mkubwa kuliko kila kitu

    [63] Je, huoni, ewe Mtume, kwamba Mwenyezi Mungu Ameteremsha mvua kutoka mbinguni, ardhi ikawa kijani kwa mimea iliyomea? Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma na upole kwa waja Wake kwa kuitoa mimea kutoka ardhini kwa maji hayo, ni mtambuzi wa mambo yanayowafaa

    [64] Ni vya Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, vilivyoko ardhini na mbinguni, kwa kuviumba, kuvimiliki na kuwa chini ya usimamizi wake, kila kimoja kati ya hizo kinahitajia uendeshaji Wake na maneemesho Yake. Na hakika Mwenyezi Mungu Ndie Aliye Mkwasi ambaye Hahitajii kitu chochote, Anayeshukuriwa kwa kila namna

    [65] Je, huoni kwamba Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Amewadhalilishia vilivyoko ardhini miongoni mwa vitu vitambaavyo na wanyama na nafaka na matunda na vitu visivyo na roho, kwa ajili ya kipando chenu, chakula chenu na manufaa yenu, kama Alivyowadhalilishia mashua zinazotembea baharini kwa uweza Wake na amri Yake, ziwabebe nyinyi na vyombo vyenu ziwafikishe kwenye miji na sehemu mzitakazo na kwamba Yeye Ndiye Anayeizuia mbingu na kuitunza, ili isianguke juu ya ardhi ikawaangamiza walioko juu yake isipokuwa kwa idhini Yake, Aliyetakasika na kila sifa za upungufu, kuwa hilo lifanyike, ili Awarehemu watu rehema kunjufu katika mambo yao ya hivi sasa hapa duniani na ya baadaye kesho Akhera? Na miongoni mwa rehema Zake ni vitu hivi Alivowadhalilishia na vinginevyo kwa fadhila Zake juu yao

    [66] Na Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu Aliyewapa uhai kwa kuwafanya mupatikane kutoka kwenye hali ya kutokuwako, kisha Atawafisha umri wenu ukomapo, kisha Atawahuisha kwa kuwafufua ili Awahesabu kwa matendo yenu. Hakika mwanadamu ni mwingi wa kukataa alama zenye kuonyesha uweza wa Mwenyezi Mungu na upweke Wake

    [67] Kila watu miongoni mwa jinsi za watu waliopita tumewaekea sheria na ibada tuliowaamrisha wao kwazo, na wao ni wenye kuzitumia, basi wasikufanyie ushindani, ewe Mtume, hao washirikina wa Kikureshi kuhusu Sheria yako na yale Aliyokuamrisha Mwenyezi Mungu katika matendo ya Hija na aina zote za ibada. Na ulinganie kwenye kumpwekesha Mola wako na kumtakasia ibada na kufuata amri Yake. Hakika wewe uko kwenye Dini iliyolingana sawa, isiyokuwa na mapindi

    [68] Na wakishikilia kujadiliana na wewe kwa njia ya ubatilifu kuhusu yale unayowalingania nayo, usijadiliane na wao, bali waambie, «Mwenyezi Mungu ni mjuzi zaidi wa mnayoyafanya ya ukafiri na kukanusha,» kwani wao wanafanya inadi na kiburi

    [69] Mwenyezi Mungu Atahukumu kati ya Waislamu na makafiri Siku Ya Kiyama katika tafauti zao kuhusu dini. Katika aya hii pana adabu nzuri ya kuwarudi wanaofanya mjadala kwa njia ya ujeuri na kiburi

    [70] Je, hujui, ewe Mtume, kwamba Mwenyezi Mungu anavijua vilivyomo mbinguni na ardhini ujuzi kamili Aliouthibitisha katika Ubao Uliohifadhiwa? Ujuzi huo ni jambo sahali kwa Mwenyezi Mungu Ambaye hakuna kitu kinachomshinda

    [71] Na makafiri wa Kikureshi wanashikilia kumshirikisha Mwenyezi Mungu pamoja na kuwa ubatilifu wa waliyonayo uko waziwazi. Wao wanawaabudu waungu ambao haukuteremka, kwenye kitabu chochote miongoni mwa vitabu vya Mwenyezi Mungu, ushahidi kuwa wao wanafaa kufanyiwa ibada, na wao (hao waungu) hawajui chochote kuhusu yale waliyoyazua (hao makafiri) na kumsingizia Mwenyezi Mungu, hakika hilo ni jambo ambalo kwalo wamewafuata baba zao bila dalili yoyote. Basi kitakapokuja kipindi cha kuhesabiwa huko Akhera, hawa washirikina hawatakuwa na msaidizi mwenye kuwanusuru au kuwakinga na adhabu

    [72] Na pindi zinaposomwa kwa washirikina aya za Qur’ani zilizo wazi, utauona uchukivu waziwazi kwenye nyuso zao, wanakaribia kuwapiga Waumini wanaowalingania kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kuwasomea aya Zake. Basi waambie, ewe Mtume, «je, si niwape habari ya kitu chenye kuchukiza zaidi kwenu kuliko kuisikia haki na kuwaona walinganizi wake? Ni Moto ambao Mwenyezi Mungu Ameutayarisha kwa makafiri huko Akhera. Na mahali pabaya zaidi pa mtu kuishia ni hapo.»

    [73] Enyi watu! Kumepigwa mfano, usikilizeni na muuzingatie: Kwa hakika, masanamu na wanaodaiwa kufanana na Mwenyezi Mungu mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, hawatoweza lau wakikusanya kuumba nzi mmoja, basi itakuaje kuumba kikubwa zaidi? Wala hawawezi kukirudisha kitu alichokinyakua nzi kutoka kwao, Je kuna kuelemewa zaidi kuliko huko? Vyote viwili pamoja ni vinyonge: amedhoofika mtaka kurudisha kitu kilichochukuliwa na nzi kutoka kwake, naye ni yule muabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu, na pia amedhoofika mtakwa, naye ni nzi. Basi vipi hawa masanamu na wanaofanywa kuwa wanafanana na Mwenyezi Mungu watafanywa ni waungu, ilhali wao wako kwenye udhaifu huu

    [74] Hawa washirikina hawakumtukuza Mwenyezi Mungu vile Anavyostahiki kutukuzwa, kwa kuwa wao wamemfanya kuwa Ana washirika, na hali Yeye Ndiye Mwenye nguvu Aliyeumba kila kitu, Ndiye Mshindi Asiyeshindwa

    [75] Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Anateua, miongoni mwa Malaika, wajumbe kuwatuma kwa Manabii Wake, na Anateua kutokana na watu, wajumbe wakufikisha jumbe Zake kwa viumbe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia maneno ya waja Wake, Mwenye kuviona vitu vyote na yule anayemteua kwa utume miongoni mwa viumbe Wake. Na Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake

    [76] Anayajua yaliyo mbele ya Malaika wake na Mitume Wake kabla hajawaumba, na Anayajua yenye kuwa baada ya kutoweka kwao. Na kwa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, yanarejea mambo yote

    [77] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, rukuuni na sujuduni katika Swala zenu na muabuduni Mola wenu, Peke Yake, Asiye na mshirika, na fanyeni wema ili mufuzu

    [78] na zipigeni jihadi nafsi zenu, na simameni, kisimamo kikamilifu, kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu, na waiteni viumbe kwenye njia Yake, na piganeni jihadi kwa mali zenu, ndimi zenu na nafsi zenu, hali ya kumtakasia nia Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, kwa hayo, hali ya kuzisalimisha Kwake nyoyo zenu na viungo vyenu. Yeye Amewateua muibebe hii Dini. Na Amewapa neema kwa kuifanya Sheria Yake kuwa sahali, haina dhiki wala mikazo katika Amri zake na hukumu zake kama vile ilivyokuwa kwa baadhi ya ummah kabla yenu. Mila hii yenye usahali ndio Mila ya baba yenu Ibrāhīm. Na Mwenyezi Mungu Amewaita nyinyi Waislamu tangu nyuma kwenye Vitabu vilivyoteremshwa vilivyotangulia na katika hii Qur’ani. Na Amewahusu nyinyi kwa chaguo hili, ili mwisho wa Mitume, Mhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, awe shahidi wenu kuwa amewafikishia ujumbe wa Mola wake, na ili muwe ni mashahidi wa ummah wengine kuwa Mitume wao waliwafikishia kwa habari mlizopewa na Mwenyezi Mungu katika Kitabu Chake. Basi jibidiisheni kujua thamani ya neema hii mupate kuishukuru, na mujilazimishe kufuata maamrisho ya Dini ya Mwenyezi Mungu kwa kutekeleza Swala kwa nguzo zake na sheruti zake na kutoa Zaka za faradhi, na muingie kwenye himaya ya Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, na mumtegemee Yeye, kwani yeye Ndiye Mbora wa kutegemewa kwa mwenye kumtegemea na ni Mbora wa kunusuru kwa anayeomba nusura Yake

    Waumini

    Surah 23

    [1] Kwa hakika wamefaulu wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, wenye kuzitumia sheria Zake

    [2] Wale ambao miongoni mwa sifa zao ni kwamba wao ni wanyenyekevu kwenye Swala zao, nyoyo zinajishughulisha na hiyo Swala tu na viungo vyao vimetulia kwayo

    [3] Na wale ambao wanaacha kila lisilo na wema ndani yake, la maneno na la vitendo

    [4] Na wale ambao wanazitakasa nafsi zao na mali zao kwa kutoa Zaka za aina mbalimbali za mali zao

    [5] Na wale ambao wanazihifadhi tupu zao kwa kuziepusha na mambo Al;iyoyafanya haramu Mwenyezi Mungun ya uzinifu, ulawiti na machafu mengine

    [6] Isipokuwa kwa wake zao au wajakazi waliomilikiwa na mikono yao ya kulia. Hao, Waumini hawana lawama wala makosa kuwaingilia na kujistarehesha nao, kwa kuwa Mwenyezi Mungu Amewahalalishia

    [7] Basi mwenye kutaka kujistarehesha na asiyekuwa mkewe au mjakazi wake, huyo ni miongoni mwa wenye kuikiuka halali na kuijia haramu na atakuwa amejiorodhesha nafsi yake kwenye mateso ya Mwenyezi Mungu na hasira Zake

    [8] Na wale ambao wanavitunza vitu vyote walivyoaminiwa nazo na wanatekeleza ahadi zao zote

    [9] Na wale ambao daima wanazitekeleza Swala zao kwa nyakati zake na kwa namana iliyowekwa na Sheria iliyokuja kutoka kwa Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye

    [10] Hao ndio Waumini wenye kuirithi Pepo

    [11] Ambao watairithi Pepo ya juu kabisa na ya kati na kati, nayo ndiyo yenye mashukio bora zaidi kuliko zote, wao humo watakaa milele, neema zao hazitakatika wala hazitaondoka

    [12] Na kwa hakika tulimuumba Ādam kutokana na udongo uliochukuliwa kutoka ardhi yote

    [13] Kisha tukawaumba watoto wake wakiwa ni wenye kuzaana kutokana na tone la maji: nalo ni manii ya wanaume, yanatoka kwenye migongo yao na yanatulia ndani ya zao za wanawake

    [14] Kisha tukaliumba hilo tone kwa kuligeuza kulifanya pande la damu iliyo nyekundu, kisha tukaliumba pande la damu kwa kuligeuza kulifanya kinofu cha nyama kadiri ya kutafunika baada ya siku arubaini, na tukakiumba kinofu cha nyama kilicho laini kwa kukigeuza kukifanya mifupa, na tukaivisha nyama ile mifupa, kisha tukamfanya ni kiumbe kingine kwa kuvuvia roho ndani yake. Ametukuka Mwenyezi Mungu Mwenye kheri nyingi Ambaye Ametengeneza umbo la kila kitu

    [15] Kisha nyinyi, enyi binadamu, baada ya vipindi vya maisha na umri kukoma, mtakufa

    [16] Kisha nyinyi, baada ya kufa na dunia kumalizika, mtafufuliwa mkiwa hai kutoka makaburini mwenu muhesabiwe na mlipwe

    [17] Kwa hakika tuliziumba juu yenu mbingu saba, moja juu ya nyingine, na hatukuwa tumeghafilika na viumbe, hatughafiliki na kiumbe wala hatumsahau

    [18] Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji kwa kadiri ya mahitaji ya viumbe, na tumeifanya ardhi kuwa ni mahali pa kutulia haya maji, na sisi niwaweza wa kuyaondoa maji haya yaliyotulia. Katika haya pana kitisho na onyo kwa wenye udhalimu

    [19] Tukawafanyia kwa maji haya mashamba ya mitende na mizabibu, mukawa nayo nyinyi kutokana na mashamba hayo matunda ya aina nyingi na sampuli mbalimbali, na katika hayo munakula

    [20] Na tukawatolea nyinyi kwa maji hayo mizaituni ambayo inatoka kandokando ya jabali la Tūr Ṣīnā’ ambao unakamuliwa mafuta ya kujipaka na kutumia kwa chakula

    [21] Na nyinyi, enyi watu, muna mazingatio katika ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo ya kulizingatia namna ya kuumbwa kwao. Tunawanywesha maziwa yanayotoka matumboni mwao. Na munayo nyinyi kutokana nao manufaa mengine mengi kama sufi na ngozi na mfano wa hivyo, na miongoni mwao mnakula

    [22] Na juu ya ngamia na majahazi, katika nchi kavu na baharini munabebwa

    [23] Kwa hakika, tulimtumiliza Nūḥ kwa watu wake kuwalingania kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu, (alipokwenda) akawaambia, «Muabuduni Mwenyezi Mungu peke Yake, nyinyi hamuna muabudiwa yoyote isipokuwa Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu, basi mtakasieni ibada. Kwani nyinyi hamuiogopi adhabu yake?»

    [24] Basi wale waheshimiwa wa watu wake walimkanusha na wakasema kuwaambia watu wa kawaida wao, «Yeye ni mwanadamu kama nyinyi, hana ubora wowote wa kutafautiana na nyinyi, na hataki kwa maneno yake isipokuwa uongozi na utukufu juu yenu, na lau Mwenyezi Mungu Alitaka kutuletea mtume, Angalimtuma Malaika kwetu, hatujasikia mfano wa hili kwa watu waliotutangulia miongoni mwa mababa na mababu. Na huyu Nūh

    [25] hakuwa isipokuwa ni mwanamume aliyeshikwa na wazimu, basi ngojeeni mpaka atakapopata fahamu auache ulinganizi wake au afe mupumzike na yeye.»

    [26] Nūḥ akasema, «Mola wangu! Niokoe na watu wangu kwa sababu ya kunikanusha mimi kwa yale niliyowafikishia ya ujumbe wako.»

    [27] Hapo tukamletea wahyi na kumwambia, «Tengeneza jahazi chini ya uangalizi wetu na amri yetu kwako na usaidizi wetu, na wewe uko kwenye utunzi wetu na hifadhi yetu. Basi amri yetu itakapokuja ya kuwaadhibu watu wako kwa kuwazamisha, na mafuriko yakaanza, na maji yakatembuka kwa nguvu kwenye tanuri, napo ni mahali pa kuchomea mikate, ikiwa ni alama ya kuja kwa adhabu, hapo basi watie ndani ya jahazi, kati ya kila kilicho hai, kiume na kike, ili kizazi kisalie. Na uwatie watu wako pia, isipokuwa yule aliyestahili kuadhibiwa kwa ukafiri wake, kama mke wako na mwano wa kiume, na usiniombe kuokolewa watu wako waliodhulumu, kwani wao hapana budi ni wenye kuzamishwa. Na katika aya hii pana kuthibitisha sifa ya jicho kwa Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, kama inavyonasibiana na Yeye, Aliyetukuka, bila kufananisha wala kulifanya liko namna gani

    [28] ‘’Basi ukiwa juu ya jahazi na ukatulia humo wewe na walio pamoja na wewe, mukiwa mumesalimika na kuzama, sema, ‘Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu Aliyetuokoa na watu makafiri.’»

    [29] Na useme, «Mola wangu! Nifaniye wepesi uteremkaji uliobarikiwa wenye amani, na wewe ndiye bora wa wenye kuteremsha.» Katika hili pana mafunzo kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, kwa waja Wake wasome dua hii wateremkapo mahali

    [30] Kwa hakika, katika kuwaokoa Waumini na kuwaangamiza makafiri, pana dalili wazi zakuonesha ukweli wa Mitume wa Mwenyezi Mungu katika yale waliokuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na sisi ni wenye kuwapa mtihani watu kwa kuwapelekea Mitume kwao kabla mateso hayajawashukia

    [31] Kisha tukawaleta baada ya watu wa Nūḥ kizazi kingine, nacho ni kile cha watu wa kabila la ‘Ād

    [32] Tukampeleka kwao Mtume miongoni mwao, naye ni Hūd, amani imshukiye, akawaambia, «Muabuduni Mwenyezi Mungu, Peke Yake, hamuna muabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye. Je, hamuogopi mateso Yake mtakapomuabudu asiyekuwa Yeye?»

    [33] Watukufu na viongozi waliomkufuru Mwenyezi Mungu miongoni mwa watu wake na waliokataa kuwa kuna maisha ya Akhera na zikawafanya wakiuke mipaka zile neema walizoneemeshwa ulimwenguni za maisha ya anasa za kupindukia, «Huyu anayewaita mumpwekeshe Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, si lolote isipokuwa ni mwanadamu kama nyinyi, anakula chakula cha aina mnachokula nyinyi, na anakunywa aina ya kinywaji mnachokunywa

    [34] «Na lau mtamfuata binadamu kama nyinyi, basi nyinyi mtakuwa wakati huo ni wenye kupata hasara kawa kuwaacha waungu wenu na kumfuata yeye

    [35] «Vipi mtayaamini yale anayowaahidi kwamba nyinyi mkifa na mkawa mchanga na mifupa iliyovunjika vipande-vipande, kuwa mtatolewa kutoka kwenye makaburi yenu mkiwa hai

    [36] «Kwa hakika, liko mbali sana hilo mnaloahidiwa, enyi watu, la kwamba nyinyi mtatolewa makaburini mwenu mkiwa hai baada ya kufa kwenu

    [37] «Maisha yetu ni ya hapa duniani tu, wazazi wanakufa na watoto wanaishi. Na sisi si wenye kutolewa tukiwa hai mara nyingine

    [38] «Na huyu, Anayewalingania kwenye Imani, hakuwa isipokuwa ni mtu amemzulia Mwenyezi Mungu urongo. Na sisi si wenye kuyaamini anayoyasema.»

    [39] Hapo Mtume wao Alimuomba Mola wake akisema, «Ewe Mola wangu! Ninusuru juu yao kwa kuwa wamenikanusha.»

    [40] Mwenyezi Mungu Akasema Akiyakubali maombi yake, «Kwa muda mchache watakuwa ni wenye kujuta.» Yaani, baada ya kipindi cha muda mchache watakuwa na majuto hao wakanushaji.»

    [41] Hawakupitiwa na muda, uliwajia wao ukelele mkali pamoja na upepo ambao kwa upepo huo Mwenyezi Mungu Aliwaangamiza, wakafa wote na wakawa ni kama takataka za mtiririko wa maji zinazoelea juu ya maji. Basi maangamivu ni ya hawa madhalimu, na kuwa mbali na rehema ya Mwenyezi Mungu ni kwao. Kwa hivyo, na wajihadhari wenye kusikia, wasije wakawakanusha Mitume wao, ikawashukia wao adhabu ilyowashukia waliowatangulia

    [42] Kisha tukawaleta, baada ya hawa waliokanusha, ummah na viumbe wengine, kama watu wa Lūṭ, Shu'ayb, Ayyūb na Yūnus, rehema za Mwenyezi Mungu na amani Yake ziwashukie

    [43] Hautangulii ummah wowote, miongoni mwa ummah hawa wanaokanusha Mitume wao, muda uliowekewa kuangamia kwake, wala hauchelewi

    [44] Kisha tukawapeleka Mitume wetu waende kwa ummah hao, wakifuatana: hawa baada wengine. Na kila Mtume akiwalingania watu wake, wanamkanusha. Basi tukawafuatisha, kundi baada ya kundi, kwa kuwaangamiza na kuwamaliza, na hakuna kilichosalia isipokuwa ni habari za kuangamia kwao.Na tukazifanya habari hizo ni maneno ya kuzungumzwa na watu waliokuja baada yao, wakizichukuwa kuwa ni mazingatio. Basi maangamivu na kuepushwa na kila kheri ni kwa watu wasiowaamini Mitume wala kuwatii

    [45] Kisha tukampeleka Mūsā na ndugu yake Hārūn kwa alama zetu tisa, nazo ni fimbo, mkono, nzige, chawa, vyura, damu, mafuriko, shida za maisha na upungufu wa matunda, zikiwa ushahidi uliyo wazi wenye kuzishinda nyoyo, zipate kulainika kwa alama hizo nyoyo zaWaumini, na isimame hoja juu ya washindani. Tuliwapeleka wao wawili

    [46] kwa Fir'awn, hakimu wa Misri, na watukufu wa watu wake ambao walifanya kiburi wakakataa kumuamini Mūsā na ndugu yake. Na wao walikuwa ni watu wanaojiona bora kuliko watu wengine na walikuwa wakiwanyanyasa kwa kuwadhulumu

    [47] Wakasema, «Je, tuwaamini watu wawili kama sisi, na jamaa zao Wana wa Isrāīl wako chini ya amri yetu, wanatutii na wanajidhalilisha kwetu.?»

    [48] Basi wakawakanusha katika yale waliyokuja nayo, wakawa ni wenye kuangamizwa kwa kuzamishwa baharini

    [49] Hakika tulimletea Mūsā Taurati, ili watu wake wajiongoze nayo kwenye haki

    [50] Na tulimjaalia Īsā mwana wa Maryam na mamake ni alama yenye kuonesha uweza wetu, kwani tulimuumba bila ya baba, na tulimfanyia makao kwenye ardhi iliyopo mahali pa juu palipolingana ili apate utulivu juu yake, penye urutuba na maji yapitayo yanayoonekana waziwazi kwa macho

    [51] Enyi Mitume! Kuleni riziki ya halali na fanyeni matendo mema, kwani mimi kwa mnayoyafanya ni mjuzi, hakuna kitu chochote chenye kufichika kwangu katika matendo yenu. Wanaohutubiwa katika aya hii ni Mitume wote kwa jumla, amani iwashukie, na wafuasi wao. Na katika aya pana dalili kwamba kula halali inasaidia kufanya matendo mema na kwamba mwisho wa haramu ni mbaya na miongoni mwa ubaya wake ni kurudishwa dua kwa kutokubaliwa

    [52] Na kwa hakika Dini yenu, enyi Mitume, ni Dini moja, nayo ni Uislamu, na mimi ni Mola wenu niogopeni kwa kufuata maamrisho yangu na kujiepusha na makatazo yangu

    [53] Na wafuasi walipambanukana katika dini wakawa makundi na mapote, wakaifanya dini yao kuwa dini nyingi baada ya kuamrishwa wajikusanye pamoja. Kila kundi linajigamba kwa maoni yake, linadai kuwa kundi hilo liko kwenye haki na lingine liko kwenye batili. Katika haya pana onyo la kujiweka kwenye makundi na kupambanukana katika Dini

    [54] Basi waache , ewe Mtume, kwenye upotevu wao na ujinga wao wa kutoijua haki hadi pale adhabu itakapowashukia

    [55] Kwani wanadhani hawa makafiri kwamba yale tunayowapa ya mali na watoto ulimwenguni ni mazuri waliyoharakishiwa na kwamba wao wanastahiki hayo

    [56] Hakika tunawaharakishia haya mazuri kwa kuwatahini na kwa kuwavuta kidogo kidogo, lakini wao hawalihisi hilo

    [57] Hakika wale ambao kwa kumcha Mola wao wanayaogopa na kujitahadhari na yale Aliyowaogopesha nayo Mwenyezi Mungu Aliyetukuka

    [58] Na wale ambao wao wanaziamini aya za Mwenyezi Mungu katika Qur’ani na wanazitumia

    [59] Na wale ambao wao wanaitakasa ibada kwa Mwenyezi Mungu , Peke Yake, na hawamshirikishi na Yeye mwingine asiyekuwa Yeye

    [60] Na wale wanaojibidiisha kufanya matendo ya kheri na wema, mioyo yao ina kicho cha kuogopa yasikubaliwe matendo yao na yasiwaokoe na adhabu ya Mola wao warejeapo Kwake kwa kuhesabiwa

    [61] Hao wanaojibidiisha kutii, dasturi yao ni kukimbilia kufanya kila kitendo chema, na wao kwa kuyaendea mambo mema ni wenye kutangulia

    [62] Hatumlazimishi mja yoyote miongoni mwa waja wetu isipokuwa kile kinachomkunjukia kukifanya, na matendo yao yamesajiliwa kwetu ndani ya Kitabu cha kudhibiti matendo, ambacho Malaika watakiinua, kitakachosema ukweli juu yao, na hakuna yoyote kati yao Atakayedhulumiwa

    [63] Lakini nyoyo za makafiri ziko kwenye upotevu uliowafinika, zimejiepusha na Qur’ani na yaliyomo ndani yake. Na wao, pamoja na ushirikina wao, wana matendo mabaya, Mwenyezi Mungu Anawapa muhula wayafanye, ili ziwapate wao hasira za Mwenyezi Mungu na mateso Yake

    [64] Mpaka tutakapowashika wenye gogi na kiburi miongoni mwao kwa adhabu yetu, hapo ndipo watainua sauti zao wakinyenyekea na wakiomba waokolewe

    [65] Na hapo waambiwe, «Msipige kelele wala msiombe kuokolewa leo! Nyinyi hamuwezi kuziokoa nafsi zenu, na hakuna yoyote atakayewaokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu

    [66] «Zilikuwa aya za Qur’ani zikisomwa kwenu, ili mupate kuziamini, na mlikuwa mnazikimbia hamtaki kuzisikia na kuzikubali na kuzitumia, kama anavyofanya mwenye kurudi nyuma kwa kule kurudi kwake nyuma

    [67] «Mnalifanya hilo na huku mnawaonesha watu kiburi pasi na haki kwa sababu ya Nyumba ya Mwenyezi Mungu tukufu. Mnasema, ‘Sisi ni watu wa Nyumba hiyo, hatushindwi tukiwa hapo,’ na mnakesha mkiwa kando-kando yake kwa maneno maovu.»

    [68] Kwani hawayafikirii yaliyomo ndani ya Qur’ani wakapata kujua ukweli wake au limewazuia wao kuamini kwa kuwa wamejiwa na Mtume na kitabu ambacho mfano wake hakikuwajia baba zao wa mwanzo, wakakikanusha kwa ajili hiyo na wakakipa mgongo

    [69] Au limewazuia wao kuifuata haki kwa kuwa Mtume wao, Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, hajulikani kwao na kwa hivyo wanamkataa

    [70] Au wanamdhania kuwa ni mwendawazimu? Kwa hakika wamedanganya. Ukweli ni kuwa amewajia na Qur’ani, upwekeshaji Mwenyezi Mungu na dini ya kweli. Na wengi wao wanaichukia haki kwa uhasidi na uadui

    [71] Lau kama Mwenyezi Mungu Angaliwawekea sheria inayolingana na mapendeleo yao, zingaliharibika mbingu na ardhi na vilivyomo humo. Bali tumewaletea yale ambayo ndani yake muna alama za nguvu yao na utukufu wao, nayo ni Qur’ani, na wao wanaipa mgongo

    [72] Au limewazuia wao kukuamini kwa kuwa wewe, ewe Mtume, unawaomba malipo juu ya ulinganizi wako kwao, hivyo basi wakafanya ubahili? Hukufanya hivyo, kwa kuwa zile thawabu zilizoko kwa Mwenyezi Mungu na vipewa ni bora zaidi. Na Yeye ni bora wa wanaoruzuku, hakuna awezaye kuruzuku kama Yeye Anavyoruzuku, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake

    [73] Kwa hakika wewe, ewe Mtume, unawalingania watu wako na wengineo kwenye Dini iliyolingana sawa, nayo ni Dini ya Uislamu

    [74] Na kwa hakika, wale ambao hawaamini kufufuliwa na kuhesabiwa wala hawayafanyii kazi hayo mawili, basi hao wamepotoka kando ya njia ya Dini iliyonyoka, nayo ni dini ya Uislamu

    [75] Na lau tungaliwahurumia na tukawaaondolea ukame na njaa, wangaliendelea kwenye ukafiri na ushindani, wakiwa katika hali ya kuduwaa na kukosa muelekeo

    [76] Na kwa hakika, tuliwajaribu wao kwa kuwaonja kwa aina mbalimbali za mikasa, pamoja na hivyo wasimnyenyekee Mola wao na wasimuombe kwa unynyekevu wakati wa kushukiwa na hiyo mikasa

    [77] Mpaka tulipowafungulia juu yao mlango wa adhabu kali huko Akhera, wakitahamaki wamo ndani yake, wamekata tamaa kupata kheri yoyote, wamechanganyikiwa hawajui wafanye nini

    [78] Na yeye Ndiye Aliyewaumbia masikizi ya kuvisikia venye kusikika, na macho ya kuviona venye kuonekana, na nyoyo ili muelewe. Pamoja na hayo, shukrani zenu kwa hizi neema za mfululizo juu yenu bado ni chache hata hazitajiki

    [79] Na yeye Ndiye Aliyewaumba watu wote katika ardhi, na Kwake Yeye mtakusanywa baada ya kufa kwenu, na hapo Atawalipa kwa mliyoyatenda, mema au maovu

    [80] Na Yeye , Peke Yake, Ndiye Anayehuisha kutoka katia hali ya kutokuweko, na Ndiye Atakayefisha baada ya uhai. Na ni kwake Yeye kufuatana usiku na mchana na pia kupishana. Basi hamuuweki akilini mwenu uweza Wake na upweke Wake

    [81] Lakini makafiri hawakuamini kuwa kuna kufufuliwa, lakini waliyakariri maneno ya wakale wao wakanushaji

    [82] walisema «Ati tutakapokufa na miili yetu ikatangamana na mchanga wa ardhi pamoja na mifupa yetu tutafufuliwa mara nyingine? Hili haliwi wala haliingii akilini.»

    [83] Yameshasemwa maneno haya kuambiwa wazee wetu kitambo, kama vile unavyotuambia, ewe Muhammad, hatukuyaona kuwa yana uhakika. Hayakuwa haya isipokuwa ni porojo za watu wa kale

    [84] Waambie, «Ni ya nani Ardhi hii na walio ndani yake iwapo muna ujuzi?»

    [85] Watakubali kwa lazima kwamba ni ya Mwenyezi Mungu, Yeye Ndiye Muumba wake na Ndiye Mwenye kuimiliki. Waambie, «Je, haliwi hilo kwenu ni lenye kuwafanya mukumbuke kuwa Yeye ni Muweza wa kuwafufua wafu na kuwarudishia uhai?»

    [86] Sema, «Ni nani Mola wa mbingu saba na Mola wa ‘Arsh iliyo kubwa, ambayo ndiyo kiumbe kikubwa kabisa na kilichoko juu kabisa?»

    [87] Watasema kwa lazima kuwa hizo ni milki ya Mwenyezi Mungu. Basi waambie, «Mbona hamuogopi adhabu ya Mwenyezi Mungu mnapomuabudu asiyekuwa Yeye?»

    [88] Sema, «Ni nani mmiliki wa kila kitu? Na ni nani Ambaye mkononi Mwake kuna hazina za kila kitu? Na ni nani Anayempa himaya mwenye kutaka himaya Yake, ambapo hakuna anayeweza kumhami na kumlinda yule ambaye Mwenyezi Mungu Anataka kumuangamiza wala hakuna anayekinga shari Aliyoikadiria Mwenyezi Mungu, iwapo mnalijua hilo?»

    [89] Watajibu kuwa hayo yote ni ya Mwenyezi Mungu. Sema uwaambie, «Vipi zinaondoka akili zenu na mnadanganywa na mnaepushwa njia ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtii na kuyaamini mambo ya kufufuliwa na kurudishiwa uhai?»

    [90] Ilivyo ni kwamba tumewaletea wakanushaji hawa ukweli wa yale tuliyompeleka kwayo Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie. Na kwa hakika wao ni warongo kwenye ushirikina wao na ukanushaji wao kufufuliwa

    [91] Mwenyezi Mungu Hakujifanyia mwana, na hakukuwa pamoja na Yeye muabudiwa mwingine, kwani kama kungalikuwa huko kuna waabudiwa zaidi ya mmoja pamoja na Yeye, basi kila muabudiwa angalijitenga na alivyoviumba na kungalikuwa na ushindani kati yao kama ilivyo kwa watawala wa ulimwnguni. Hapo mpango wa ulimwengu ungaliharibika. Ametakasika Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kuepukana na sifa wanazompa za kuwa Yeye ana mshirika au mwana

    [92] Yeye, Peke Yake, Ndiye Anayejua yanayofichika kwa viumbe vyake na wanayoyaona. Basi Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ameepukana na mshirika ambaye wanadai kuwa Anaye

    [93] Sema, ewe Mtume, «Mola wangu! Unioneshapo kwa hawa washirikina ile adhabu yako uliyowaonya nayo

    [94] basi usiniangamize kwa ile uliyowaangamiza nayo. Na uniokoe na adhabu yako na hasira zako. Usiniweke pamoja na watu washirikina na madhalimu. Bali niingize kwa wale uliokuwa radhi nao.»

    [95] Na kwa hakika sisi tunaweza kukuonesha yale tunayowaahidi ya adhabu

    [96] Pindi wanapokufanyia ubaya maadui zako, ewe Mtume, kwa maneno au vitendo, basi usiwalipe ubaya, lakini uondoshe ubaya wao kwa kuwafanyia wema. Sisi tunayajua mno yale wanayokubandika washirikina ya sifa za ushirikina na kukukanusha, na Atawalipa kwa hayo malipo maovu mno

    [97] Na useme, ewe Nabii, «Mola wangu! Najilinda kwako na upotezaji wa Mashetani unaoupelekea kwenye ubatilifu na uharibifu na kuzuia watu wasiifuate haki

    [98] Na ninajilinda kwako, ewe Mola wangu, na kuingiliwa na wao kwenye mambo yangu.»

    [99] Mwenyezi Mungu Anawatolea habari makafiri au waliokiuka mipaka ya amri Yake, Aliyetukuka, walioko kwenye hali ya kusongwa na kifo, mauti yalipowafikia na wakaishuhudia adhabu waliyoandaliwa, hapo huwa akisema kila mmoja wao, «Mola wangu! Nirudisha ulimwenguni

    [100] «Huenda mimi nikayarekebisha yale niliyoyapoteza ya imani na utiifu.» Hatolipata hilo, kwani hatakubaliwa hilo aliloliomba wala hatapewa muhula. Hilo ni neno tu atalisema. Ni neno lisilomnufaisha, na yeye kwa neno hilo si mkweli, kwani lau angalirudishwa ulimwenguni angaliyarudia yale aliyokatazwa. Na Wenye kufa watasalia kwenye kizuizi na kitengo kilichoko kati ya Akhera na duniani mpaka Siku ya kufufuliwa na kukusanywa

    [101] Basi Siku ya Kiyama itakapokuwa, na Malaika anayehusika akavivia kwenye baragumu, na watu wakafufuliwa kutoka makaburini mwao, hapo hakuna kujigamba kwa nasaba kama walivyokuwa wakijigamba nazo duniani wala hapana yoyote atakayemuuliza yoyote

    [102] Basi yule ambaye mema yake yatakuwa mengi na zikawa nzito kwayo mizani za matendo yake Siku ya kuhesabiwa, basi hao ndio wenye kufaulu kupata Pepo

    [103] Na yule ambaye mema yake yatakuwa machache kwenye mizani na maovu yake yatakuwa mengi zaidi, na kubwa zaidi ya hayo maovu ni ushirikina, basi hao ndio ambao wamepita patupu na wakaziangamiza nafsi zao kwenye moto wa Jahanamu, watasalia humo milele

    [104] Moto huo utaunguza nyuso zao, na wao humo watakuwa ni wenye kufinya nyuso, midomo yao imekauka na meno yao yamejitokeza nje

    [105] Wataambiwa, «Je, hamkuwa mkisomewa aya za Qur’ani huko duniani, mkawa mnazikanusha?»

    [106] Wakikubali kuwa Mitume wao waliwapelekea ujumbe na wakawaonya, watasema Siku ya Kiyama, «Mola wetu! Raha zetu, na pia matamanio yetu yalikadiriwa kwetu kwenye ujuzi wako uliotangulia, zilitutawala na kwa hivyo tukawa, katika matendo yetu, ni wenye kupotea na kuwa kando ya njia ya uongofu

    [107] «Mola wetu! Tutoe Motoni na uturudishe duniani. Na huko, tukirudi upotevuni, basi kwa kweli sisi ni madhalimu tunastahili kuadhibiwa.»

    [108] Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, Atawaambia, «Kaeni Motoni mkiwa wanyonge wala msiseme na mimi.» Hapo yatakatika maombi yao na matumaini yao

    [109] «Kulikuwa na kundi la waja wangu, nao ni Waumini, wakiomba kwa kusema, ‘Mola wetu! Tumeamini, basi yasitiri madhambi yetu na uturehemu, na wewe ndiye bora wa kurehemu.’

    [110] «Mkajishughulisha kuwacheza shere, mpaka mkasahau kumtaja Mwenyezi Mungu na mkasalia kwenye ukanushaji wenu, na kwa kweli mlikuwa mkiwacheka kwa shere na dharau

    [111] «Mimi nilililipa kundi hili la waja wangu Waumini kwa kuwafanya wafuzu kupata Pepo kwa sababu ya uvumilivu wao juu makero na utiifu kwa Mwenyezi Mungu»

    [112] Na watu waovu wataulizwa wakiwa Motoni, «Mlisalia miaka mingapi ulimwenguni? Na mlipoteza mangapi huko ya kumtii Mwenyezi Mungu?»

    [113] Watasema kwa kituko cha Kisimamo na ukali wa adhabu, «Tulikuwa huko kwa siku moja au sehemu ya siku. Waulize washika hesabu wenye kuhesabu miezi na siku.»

    [114] Hapo Atawaambia «Hamkuketi isipokuwa kipindi kichache, na lau mlivumilia juu ya kumtii Mwenyezi Mungu mungalifaulu kuipata Pepo, kama mungalikuwa na ujuzi wa hilo.» Hivyo ni kwamba kipindi cha kukaa kwao duniani ni kichache sana kulingana na kipindi cha kukaa kwao Motoni milele

    [115] Je, mlidhania, enyi viumbe, ya kwamba sisi tuliwaumba nyinyi mkiwa mumepuuzwa: hakuna maamrisho wala makatazo wala malipo mema wala mateso, na kwamba nyinyi hamtorudishwa kwetu Akhera kwa Hesabu na Malipo

    [116] Ametukuka Mwenyezi Mungu Aliye Mfalme, Anayepelekesha kila kitu, Ambaye Yeye ni Kweli, ahadi Yake ni kweli na onyo Lake ni kweli na kila kitu kutoka Kwake ni kweli. Ametakasika na kuwa Ataumba kitu kwa upuuzi au pasi na maarifa. Hapana mola isipokuwa Yeye, Mola wa ‘Arsh tukufu ambayo ndicho kiumbe kikubwa kuliko vyote

    [117] Na yoyote atakayeabudu, pamoja na Mwenyezi Mungu Aliyepwekeka, mungu mwingine, asiyekuwa na hoja yoyote juu ya ustahiki wake kuabudiwa. Basi kwa kweli malipo yake juu ya kitendo chake hicho kiovu yako mbele ya Mola wake huko Akhera. Ukweli ni kwamba hakuna kufuzu wala kuokoka kwa makafiri Siku ya Kiyama

    [118] Na useme, ewe Nabii, «Mola wangu! Samehe madhambi na urehemu. Na wewe ndiye bora wa anayemrehemu mwenye dhambi, akaikubali toba yake na asimtese kwa dhambi zake

    Nuru

    Surah 24

    [1] Hii ni sura kubwa miongoni mwa sura za Qur’ani, tumeiteremsha na tumelazimisha kuzifanyia kazi hukumu zake, na tumeteremsha ndani yake hoja nyingi zilizo waziwazi ili mupate kujikumbusha, enyi Waumini, kwa aya hizi zilizo waziwazi na muzitumie

    [2] Mzinifu mwanamume na mzinifu mwanamke ambao hawajawahi kuoa au kuolewa, adabu ya kila mmoja kati yao ni kupigwa mboko mia moja. Na imethibiti katika Sunnah (mapokezi kutoka kwa Mtume) kwamba pamoja na mboko hizi, ahamishwe kwa kipindi cha mwaka mmoja. Wala kusiwafanye nyinyi kule kuwahurumia kuacha kuwatia adabu hiyo au kuipunguza, iwapo munamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na munazifuata kivitendo hukumu za Kiislamu. Na waihudhurie adabu hiyo kikundi cha Waumini kwa kuwaumbua na iwe ni kitisho, mawaidha na mazingatio

    [3] Mwanamume mzinifu haridhiki isipokuwa kumuoa mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina asiyekubali uharamu wa uhalifu wa uzinifu, na mwanamke mzinifu haridhiki isipokuwa kuolewa na mwanamume mzinifu mwanamume mshirikina asiyekubali uharamu wa uzinifu. Ama wanaume na wanawake wanaojizuia na uzinifu, wao hawaridhiki na hilo, na ndoa hiyo imeharamishwa kwa Waumini. Na huu ni ushahidi wazi wa uharamu wa kumuoa mwanamke mzinifu mpaka atubie, vilevile uharamu wa kumuoza mwanamume mzinifu mpaka atubie

    [4] Na wale wanaowatuhumu watu waliojihifidhi, miongoni mwa wanaume na wanawake, kwa uchafu wa uzinifu pasi na kushuhudia pamoja na wao mashahidi wanne waadilifu, basi wapigeni mboko themanini na msiwakubalie ushahidi mwingine wowote kabisa, na hao ndio waliotoka nje ya utiifu wa Mwenyezi Mungu

    [5] Lakini mwenye kutubia, akajuta, akarudi nyuma katika tuhuma yake na akatengeneza matendo yake, kwa kweli Mwenyezi Mungu Atamsamehe dhambi zake, Atamuonea huruma na Ataikubali toba yake

    [6] Na wale wanaowatuhumu wake zao kwa uzinifu, na wakawa hawana mashahidi wa kutilia nguvu tuhuma yao isipokuwa wao wenyewe, basi ni juu ya mmoja wao hao wenye kutuhumu, atoe ushahidi mbele ya kadhi mara nne kwa kusema, «Ninashuhudia kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba mimi ni mkweli katika lile la uzinifu ambalo nimemtuhumu mke wangu kwalo.»

    [7] Na aongeze kwenye ushahidi wa tano kujiapiza nafsi yake kuwa inastahili kupata laana ya Mwenyezi Mungu iwapo yeye ni mrongo katika maneno yake hayo

    [8] Na kwa ushahidi wake huu, itapasa kwa yule mke aliyetuhumiwa kutiwa adabu ya uzinifu, nayo ni kupigwa mawe mpaka kufa. Na haitamuepukia adabu hii mpaka atoe ushahidi wa kupinga ule ushahidi wa mumewe, mara nne kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba mumewe ni mrongo katika madai yake kuwa yeye amezini

    [9] Na aongeze katika ushahidi wake wa mara ya tano kwa kujiapiza kuwa anapaswa kushukiwa na hasira za Mwenyezimngu iwapo mumewe ni mkweli katika madai yake kuwa yeye amezini. Na katika hali hii watatenganishwa baina ya wao wawili

    [10] Na lau kama si wema wa Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema Zake kwenu, enyi Waumini, kwa mapitisho haya ya kisheria kwa waume na wake, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuitikia toba kwa aliyetubia miongoni mwa waja wake ni Mwingi wa hekima katika sheria Zake na maongozi Yake, basi yangalimpata mmoja wa wale wawili wanaolaaniana yale aliyojiapiza

    [11] Kwa hakika, wale waliokuja na urongo mbaya kabisa, nao ni kumsingizia Mama wa Waumini 'Aishah, radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie, kuwa amefanya kitendo kichafu, ni kikundi cha watu wanaohusiana na nyinyi, enyi kongamano la Waislamu. Msidhanie maneno yao ni shari kwenu, ilivyo ni kuwa maneno yao ni kheri kwenu, kwa kuwa yalitokamana na maneno hayo kutakaswa Mama wa Waumini na uchafu, kusafika kwake na kuukuza utajo wake, kuzipandisha daraja, kuyafuta maovu na kuwasafisha Waumini. Kila mmoja aliyouzungumza urongo huo atapata malipo ya kitendo chake cha dhambi. Na yule aliyebeba jukumu kubwa zaidi katika uzushi huo, naye ni 'Abdullāh bin Ubayy bin Salūl, kiongozi wa wanafiki, Mwenyezi Mungu Amlaani, atakuwa na adhabu kubwa huko Akhera, nayo ni kukaa milele wakati waliposikia uzushi huo, nayo nikumuepushia kile ambacho hao (wazushi) walimsngizia nacho na kusema, «Huu ni urongo waziwazi juu ya 'Aishah, radhi za Mwenyezi Mungu zimshukuie

    [12] Si ingalikuwa bora kwa Waumini wanaume na wanawake wadhaniane kheri wao kwa wao pindi walikposikia uzushi huo, kuwa yale waliyosingiziwa hawanayo, na waseme, «Huu ni urongo ulio wazi» juu ya ‘Aishah, radhi za Mwenyezi Mungu zimfikie

    [13] Si ingalikuwa walete mashahidi waadilifu wanne kuthibitisha maneno yao waliyoyasema. Na kwa kuwa hawakulifanya hilo, basi wao ni warongo mbele ya Mwenyezi Mungu

    [14] Na lau kama si wema wa Mwenyezi Mungu kwenu na rehema Zake, kwa kuwa wema Wake umewakusanya nyinyi katika Dini yenu na Akhera yenu, Asifanye haraka kuwaadhibu na aikubali toba ya mwenye kutubia miongoni mwenu, basi inagaliwapata adhabu kali kwa sababu ya maneno ya uvumi mliyojihusisha nayo

    [15] Kipindi mlichokuwa mnaupokea uzushi na mnaueneza kwa midomo yenu, nao ni yale maneno ya urongo na ambayo hamuna ujuzi nao. Na mambo mawili haya yameharamishwa: kusema maneno ya urongo na kusema bila ya ujuzi. Na mnadhani kuwa hilo ni jambo dogo, nalo ni kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Katika haya pana makemeo bayana juu ya kupuuza makatazo ya uenezaji ubatilifu

    [16] Mbona hamukusema mlipousikia uzushi huo, «Haifai kwetu kuusema urongo huu. Kutakasika ni kwako, ewe Mola, kuyasema hayo juu ya mke wa Mtume wako Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie. Huu ni urongo uliobeba mzigo mkubwa wa madhambi.»

    [17] Mwenyezi Mungu Anawakumbusha na Anawakataza msirudie kitendo hiki cha kusingizia urongo, iwapo nyinyi ni wenye kumuamini Yeye

    [18] Na Anawafafanulia nyinyi aya zinazokusanya hukumu za kisheria na mawaidha. Na Mwenyezi Mungu Anayajua sana matendo yenu, ni Mwenye hekima katika sheria Zake na uendeshaji Wake

    [19] Kwa hakika,wale wanaopenda kuenea machafu kwa Waislamu, ya tuhuma za uzinifu au jambo lolote baya, watapata adhabu kali ulimwenguni, kwa kupigwa mboko, na mengineyo miongoni mwa mitihani ya kilimwengu, na watapata adhabu ya Motoni huko Akhera wakiwa hawakutubia. Na Mwenyezi Mungu, peke Yake, Ndiye Anayejua urongo wao na Ndiye Anayeyajua maslahi ya waja wake na mwisho wa mambo , na nyinyi hamyajui hayo

    [20] Na lau kama si wema wa Mwenyezi Mungu juu ya wale waliohusika kwenye tukio la uzushi na rehema zake kwao na kwamba Mwenyezi Mungu Anawahurumia waja Wake Waumini huruma kunjufu katika yale wanaokuwa na pupu nayo (ya ulimwengu) na yale wanayoyasubiri (ya Akhera), hangalizifunua wazi hukumu hizi na mawaidha na Angalifanya haraka kumuadhibu yule aendaye kinyume na amri Yake

    [21] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazitekeleza sheria Zake, msiziandame njia za Shetani. Na yoyote anayefuata njia za Shetani, basi (huyo Shetani) anamuamrisha vitendo viovu na vichafu. Na lau si wema wa Mwenyezi Mungu kwa Waumini na rehema zake kwao, hanagalitakasika yoyote katika wao kabisa na uchafu wa madhambi yake. Lakini Mwenyezi Mungu, kwa wema wake, Anamtakasa Anayemtaka. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasikia maneno yenu , ni Mjuzi wa nia zenu na matendo yenu

    [22] Wala wasiape watu wema katika Dini na wakunjufu wa mali kuacha kuwaunga watu wao wa karibu wasiokuwa na kitu na wahitaji na wageni waliogura makwao na kuwanyima matumizi kwa sababu kuna kosa walilifanya. Basi na wayasamehe maovu yao wala wasiwatese. Kwani nyinyi hamupendi Mwenyezi Mungu Awasamehe? Basi wasameheni. Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwasamehe waja Wake, ni Mwenye huruma kwao. Katika haya pana mahimizo juu ya kusamehe na kusahau kabisa, hata kama mtu atatendewa uovu

    [23] Kwa kweli wale wanaowasingizia kitendo cha uzinifu wanawake wenye kujihifadhi, wasiofikiria machafu na walio Waumini ambao halijawapitia jambo hilo kwenye nyoyo zao, hao ni wenye kufukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu , duniani na Akhera, na watapata adhabu kubwa kwenye moto wa Jahanamu. Kwenye aya hii kuna ushahidi juu ya ukafiri wa mwenye kumtukana au kumtuhumu mke yoyote kati ya wake za Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa jambo ovu lolote

    [24] Hiyo ndiyo adhabu ya Siku ya Kiyama, siku ambayo ndimi zao zitatoa ushahidi kinyume na wao kwa yale ambayo hizo ndimi zimeyatamka, na itazungumza mikono yao na miguu yao kuhusu yale ambayo hiyo mikono na miguu iliyatenda

    [25] Katika siku hiyo, Mwenyezi Mungu Atawalipa malipo yao kamili juu ya matendo yao kwa usawa, na watajua kwenye mkusanyiko huo mkubwa wa kisimamo kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye Ukweli ulio wazi, Ambaye Yeye ni kweli, ahadi yake ni ya kweli, makemeo yake ni kweli na kila kitu kitokanao na yeye ni kweli, Ambaye hamdhulumu yoyote chochote hata kama ni kadiri ya uzani wa chungu mdogo

    [26] Kila kiovu miongoni mwa wanaume na wanawake, maneno na vitendo, kinalingana na kiovu na kinaoana nacho. Na kila kizuri miongoni mwa wanaume na wanawake, maneno na vitendo, kinalingana na kizuri na kinaoana nacho. Na wanaume wazuri na wanawake wazuri ni wenye kutakaswa na uovu wanaowasingizia nao wale waovu. Watapata kutoka kwa Mwenyezi Mungu msamaha utakaoyafinika madhambi yote na riziki njema Peponi

    [27] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazitumia sheria Zake, msiingie kwenye nyumba zisizokuwa zenu, mpaka muwatake ruhusa wenyewe ya kuingia na muwaamkie. Na matamshi ya maamkizi hayo yatokayo kwenye Sunnah ni, «Assalāmu ‘alaikum. Je, niingie?» Kutaka ruhusa huko ni bora kwenu nyinyi. Huenda mkazikumbuka, kwa kufanya kwenu hivyo, amri za Mwenyezi Mungu na mkapata kumtii

    [28] Na iwapo hamtampata mtu kwenye nyumba za watu wengine, basi msizingie mpaka aweko mwenye kuwaruhusu. Asiporuhusu na akasema, «rudini,» basi rudini, wala msisisitize kutaka kuruhusiwa, kwani kurudi wakati huo ni jambo zuri zaidi kwenu, kwani mwanadamu ana nyakati na hali ambazo hapendi kwenye hali hizo kuonekana na mtu mwingine. Na Mwenyezi Mungu kwa mnayoyatenda ni Mjuzi na Atamlipa kila mtendaji kitendo chake

    [29] Lakini hapana ubaya kwenu kuiingia , bila ya kubisha hodi, nyumba ambazo hazikuwekwa kuwa ni makazi ya watu maalumu wajulikanao isipokuwa ziwe ni maliwazo kwa wenye kuzihitajia, kama nyumba zilizowekwa kuwa ni sadaka kwa mpita njia kwenye njia ya wasafiri na zisokuwa hizo katika huduma. Basi ndani ya nyumba hizo muna manufaa na mahitaji ya wenye kuyaingia, kwani kubisha kwenye hali hiyo ni usumbufu. Na Mwenyezi Mungu Anazijua hali zenu zilizo waziwazi na za zilizofichika

    [30] Sema, ewe Nabii, uwaambie Waumini wanaume wayainamishe macho yao kutoangalia vitu visivyohalali kwao miongoni mwa wanawake na tupu, na wazilinde tupu zao na vile Alivyovifanya haramu Mwenyezi Mungu miongoni mwa uzinifu, ulawiti, kufunua tupu na mfano wa hayo. Kufanya hivyo ni usafi zaidi kwao. Kwa hakika, Mwenyezi Mungu ni Mtambuzi wa wanayoyafanya katika yale Anayowaamrisha na kuwakataza

    [31] Na useme kuwaambia Waumini wanawake wayainamishe macho yao kutoyaangalia yasiokuwa halali kwao miongoni mwa tupu, na wazilinde tupu zao na yale Aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu, wala wasionyeshe waziwazi pambo lao kwa wanaume, bali wajipinde kulificha pambo lao isipokuwa nguo za juu ambazo imezoeleka kuzivaa, iwapo hakuna kwenye nguo hizo kivutio cha kupelekea kufitinika nao, na waviangushe vifiniko vya vichwa vyao kwenye uwazi wa sehemu za juu za nguo zao kwenye sehemu za vifua vyao huku wamezifinika nyuso zao ili sitara yao itimie. Na wasiuonyeshe urembo uliofichika isipokuwa kwa waume zao, kwani wao wanaona kutoka kwao wasiyoyaona wengine. Na sehemu ya urembo huo, kama uso, shingo, mikono miwili na sehemu za begani za mikono, zinafaa kuonekana na baba zao au baba za waume zao au watoto wao au watoto wa waume zao au ndugu zao au watoto wa ndugu zao wa kiume, au watoto wa dada zao au wanawake wenzao, walio Waislamu na sio makafiri, au watumwa waliowatawala au wafuasi kati wanaume ambao hawana malengo wala haja ya wanawake, kama vile mapite wanaowafuata watu kwa sababu ya kula au kunywa tu, au watoto wadogo ambao hawana ujuzi wowote wa mambo yanayohusiana na tupu za wanawake na ambao bado hawana matamanio. Na wasipige miguu yao, hao wanawake, wanapotembea ili kuwasikilizisha watu mapambo yao yaliyofichika, kama vikuku(vinavovawa miguuni kama pambo) na mfano wake. Na rudini, enyi Waumini, kwenye kumtii Mwenyezi Mungu katika yale Aliyowaamrisha kwayo kati ya sifa hizi nzuri na tabia njema, na yaacheni yale ambayo walikuwa nayo watu wa zama za ujinga ya tabia na sifa mbovu kwa matarajio mufaulu kuzipata kheri mbili: ya ulimwenguni na ya Akhera

    [32] Na waozeni, enyi Waumini, wanaume wasiokuwa na wake na wanawake wasiokuwa na waume, miongoni mwa waungwana na walio wema kati ya watumwa wenu na wajakazi wenu. Iwapo anayetaka kuoa kwa kujihifadhi ni masikini mwenye uhitaji, Mwenyezi Mungu Atamtosheleza kutokana na ukunjufu wa riziki Yake. Na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu, ni Mwingi wa kheri, ni Mkuu wa fadhila na ni Mjuzi mno wa nyenendo za waja Wake

    [33] Na wale wasiokuwa na uwezo wa kuoa kwa ufukara wao au kwa jambo lingine, basi na wajizoeze uvumilivu wa kutoyafanya Aliyoyakataza Mwenyezi Mungu, mpaka Mwenyezi Mungu Awatosheleze kwa wema Wake na Awasahilishie kuoa. Na wale wanaotaka kujikomboa na utumwa na ujakazi kwa kufanya mkataba na mabwana zao kwa kutoa kiasi maalumu cha pesa wawapatie, basi ni juu ya hao wamiliki wao waandikiane mapatano na wao kwa hilo, iwapo watajua kuwa kuna wema ndani yao ya uongofu, uwezo wa kujitafutia pesa na wema wa Dini. Na ni juu yao, hao wamiliki, wawape pesa, hao watumwa wao, au wawasamehe sehemu ya pesa walioandikiana. Na haifai kwenu kuwalazimisha wajakazi wenu kufanya uzinifu kwa lengo la kutaka kupata pesa. Na vipi litapatikana kwenu hilo na huku wao wenyewe wanataka kujilinda na uchafu huo, na nyinyi mnawakatalia hilo? Katika haya, pana kuonesha ubaya wa kitendo kiovu walichokifanya. Na yoyote mwenye kuwalazimisha wao kufanya uzinifu, basi Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, baada ya kuwalazimisha wao, ni mwenye kuwasamehe (hao waliolazimishwa) na kuwaonea huruma, na dhambi ni kwa yule Aliyewalazimisha

    [34] Na kwa hakika tumewateremshia, enyi watu, aya za Qur’ani zikiwa ni dalili wazwazi za kuonesha haki, na ni mfano wa matukio ya ummah uliopita wa Waumini kati yao na makafiri na yaliyowapitia ya kuwafaa na kuwadhuru ambayo ni mfano na mazingatio kwenu na ni mawaidha ya kuwaidhika mwenye kumcha Mwenyezi Mungu na kujihadhari na adhabu Yake

    [35] Mwenyezi Mungu ni Nuru ya mbinguni na ardhini, Anaendesha mambo humo na Anawaongoza watu wake. Kwa hivyo, Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, ni Nuru, na pazia Yake ni Nuru. Kwayo zimeng’ara mbingu na ardhi na vilivyomo ndani. Na kitabu cha Mwenyezi Mungu na uongofu wake ni nuru kutoka Kwake, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake. Na lau si nuru Yake yeye Aliyetukuka, lingalishikamana giza na kupandana, hili juu ya lingine. Mfano wa nuru Yake ambayo inaongoza kupeleka Kwake, nayo ni Imani na Qura’ni ndani ya moyo wa mwenye kuamini, ni kama kishubaki, nacho ni kidirisha ukutani kisichoonyesha upande wa pili, kwenye kidirisha kuna taa, ambapo hapo kidirisha kinakusanya nuru ya ile taa, zote zikawa mwangaza wake ni mmoja. Na taa hiyo iko kwenye kiyoo, kama kawamba kiyoo hiko kwa usafi wake ni nyota ing’arao kama duri. Taa hiyo inawashwa kwa mafuta ya mti uliobarikiwa, nao ni mzaituni, si wa upande wa mashariki tu usiopatwa na jua mwisho wa mchana, wala si wa magharibi tu usiopatwa na jua mwanzo wa mchana, isipokuwa uko katikati kwenye sehemu ya ardhi, haukuelekea Mashariki wala Magharibi. Yanakaribia mafuta yake kwa usafi wake kuwaka yenyewe bila ya kuguswa na moto, na pindi yakiguswa na moto hung’ara mn’garo mkali mno, nuru juu ya nuru. Hiyo ni nuru kutokana na mwangaza utokao kwenye mafuta, ulioko juu ya nuru itokanayo na kuwasha moto. Basi huo ndio mfano wa uongofu, huwa unang’ara ndani ya moyo wa mwenye Imani. Na Mwenyezi Mungu Anamuongoza na kumuelekeza kuifuata Qur’ani Amtakaye, na Anawapigia watu mifano ili wapate kuifahamu mifano yake na hekima zake. Na Mwenyezi Mungu kwa kila kitu ni Mjuzi mno na hakuna chochote kinachofichamana Kwake

    [36] Nuru hii inayong’ara kwenye misikiti ambayo Mwenyezi Mungu Ameamrisha itukuzwe, ijengwe na jina Lake litajwe humo kwa kusoma Kitabu Chake na kuleta tasbihi (subhān Allāh) na kuleta tahlili (Allāh Akbar) na yasiyokuwa hayo katika aina mbalimbali za kumtaja. Wanaswali kwenye misikiti hiyo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu asubuhi na jioni

    [37] Wanaume ambao hawapumbazwi na ununuzi wala uuzaji na jambo la kumtaja Mwenyezi Mungu, kusimamisha Swala na kutoa Zaka kwa anayestahiki kupewa; wanaiogopa Siku ya Kiyama ambayo nyoyo zinageukageuka baina ya matumaini ya kuokoka na kicho cha kuangamia, na macho yatakuwa yanageukageuka yanatazama ni mwisho gani yataishia

    [38] Ili Mwenyezi Mungu Awape malipo mema ya matendo yao mazuri zaidi na Awaongezee kutokana na wema Wake. Na Mwenyezi Mungu Anamruzuku Anayemtaka bila kumhesabia, bali Anampa malipo ambayo matendo yake mema hayakuyafikia, na pasi na hesabu wala kipimo

    [39] Na wale waliomkanusha Mola wao na wakawafanya warongo Mitume Wake, matendo yao waliyoyategemea kuwa yatawafaa huko Akhera, kama kuunga kizazi, kuwaacha huru mateka na yasiyokuwa hayo, yatakuwa ni kama mangati, nayo ni yale yanayoonekana kama maji juu ya ardhi tambarare kipindi cha mchana cha jua kali, mwenye kiu akiyaona anadhani ni maji, na akiyajia hakuti kuwa ni maji. Basi kafiri anadhani kwamba matendo yake yatamfaa, na ifikapo Siku ya Kiyama atakuta kuwa hayana malipo mema, na hapo atamkuta Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Anamngojea Ampe malipo ya matendo yake kikamilifu. Na Mwenyezi Mungu ni Mpesi wa kuhesabu. Basi wajinga wasione kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu imekawia kuwa, kwani hiyo hapana budi kuja kwake

    [40] Au matendo yao yawe mfano wa giza ndani ya bahari yenye kina, juu yake kuna mawimbi, na juu ya mawimbi kuna mawimbi mengine, na juu ya mawimbi hayo kuna mawingu mazito. Hilo ni giza kubwa sana, giza juu ya giza, pindi atowapo mkono wake mtazamaji, kamwe hakaribii kuuona kwa ukubwa wa giza. Limerundikana kwa makafiri giza la ushirikina, upotevu na uharibifu wa matendo. Na yule ambaye Mwenyezi Mungu Hakumpatia nuru itokamanayo na Kitabu Chake na mwendo wa Mtume Wake, basi huyo hana wa kumuongoza

    [41] Kwani hukujua, ewe Mtume, kwamba Mwenyezi Mungu vinamtakasa Yeye viumbe vilivyoko mbinguni na ardhini. Na ndege wamezikunjua mbawa zao huko juu angani wanamtakasa Mola wao? Kila kiumbe, Mwenyezi Mungu Amemfundisha namna ya kumswalia na ya kumtakasa. Na Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Anayaona anayoyafanya kila mwenye kuabudu na kutakasa, hakuna chochote kinachofichika Kwake Yeye kuhusu hayo, na Atawalipa kwa hayo

    [42] Ni wa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, ufalme wa mbinguni na ardhini. Ndiye Mwenye utawala wa hizo zote. Na Kwake Yeye ndio marejeo Siku ya Kiyama

    [43] Kwani hukuona kwamba Mwenyezi Mungu, Aliyetakata na kutukuka, Anayapeleka mawingu pale Anapopataka, kisha Anayakusanya baada ya kuwa mbalimbali, kisha anayafanya yapandane na yarundikane, kisha Anaiteremshe mvua kutoka kwenye mrundiko huo? Na Anateremsha, kutoka kwenye mawingu yanayofanana na milima ya mawe kwa ukubwa wake, mvua ya barafu, Akaipeleka kwa amtakaye kati ya waja Wake na Akaiyondosha kwa Amtakaye kati yao kuambatana na hekima Yake na mpango Wake. Unakaribia mwangaza wa umeme huo umemetekao huko mawinguni, kwa ukali wake, kuyapofua macho ya wenye kuutazama

    [44] Na miongoni mwa ushahidi wa kutolea dalili uweza wa Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, kwamba Yeye Anaugeuza usiku na mchana kwa kuja mmoja wapo baada ya mwingine na kutafautiana kwao kwa urefu na ufupi. Katika hilo pana ushahidi kwa mtu mwenye busara na kuizingatia

    [45] Na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Amekiumba kila kitambaacho ardhini kutokana na maji, kwani maji ndio asili ya kuumbwa kwake. Na miongoni mwa vitambaavyo kuna anayetembea kwa matumbo yake kama vile nyoka na mfano wake, na katika hao kuna anayetembea kwa miguu miwli kama binadamu, na miongoni mwao kuna anayetembea kwa miguu minne kama wanyama na mfano wake. Na Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Anaumba anachotaka, na Yeye ni Muweza wa kila kitu

    [46] Na kwa hakika tumeteremsha katika Qur’ani vitambulisho vilivyo waziwazi venye kuongoza kwenye haki. Na Mwenyezi Mungu Anamuongoza na kumuelekeza Anayemtaka katika waja wake kwenye njia iliyolingana sawa, nayo ni Uislamu

    [47] Na wanafiki wanasema, «Tumemuamuni Mwenyezi Mungu na yale ambayo amekuja nayo Mtume na tumezitii amri zao.» Kisha vinatoka vikundi kati yao, baada ya hapo, vikayapa mgongo hayo, visiukubali uamuzi wa Mtume. Basi hao hawakuwa ni Waumini

    [48] Na wanapoitwa, wanapokuwa kwenye ugomvi baina yao, kwenye hukumu iliyo ndani ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu na waje kwa Mtume ili afanye uamuzi kati yao, ghafula hujitokeza kikundi kati yao kikajiepusha na kikawa hakikubali hukumu ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, pamoja na kuwa hiyo ndiyo haki isiyo na shaka

    [49] Na iwapo haki iko upande wao, basi wao wanakuja kwa Nabii, rehema na amani zimshukie, wakiwa watiifu na kuwa tayari kuiandama hukumu yake, kwa kutambua kwao kwamba yeye atatoa uamuzi wa haki

    [50] Je, sababu ya kupa mgongo kwao ni ule ugonjwa wa unafiki ulio ndani ya nyoyo zao au wanaushuku unabii wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie? Au sababu ni kuchelea kwao isije ikawa hukumu ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake ni ya maonevu? Ukweli ni kwamba wao hawaogopei maonevu, isipokuwa kiini hasa ni kwamba wao wenyewe ndio madhalimu walio waovu

    [51] Ama Waumini wa kweli, msimamo wao ni kwamba wanapoitwa kwenda kuhukumiwa, katika ugomvi ulio kati yao, na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na hukumu ya Mtume Wake, wanakubali uamuzi unaotolewa na wanasem, «Tumesikia tulioambiwa na tumemtii aliyetuita kwenye hilo.» Na hao ndio waliofaulu wenye kufuzu kupata matakwa yao kwenye mabustani ya Pepo yenye neema

    [52] Na mwenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake katika kufuata maamrisho na kujiepusha na makatazo na akaogopa mwisho mbaya wa uasi na akajihadhari na adhabu ya Mwenyezi Mungu, basi hao ndio wenye kufuzu kupata neema Peponi

    [53] Na wanafiki waliapa kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, kwa upeo wa juhudi yao, viapo vizito, «Ukituamrisha, ewe Mtume, kutoka kwenda kwenye jihadi pamoja na wewe, tutatoka tena tutatoka» Sema uwaambie, «Msiape viapo vya urongo, kwani utiifu wenu unajulikana kuwa ni wa ulimini tu. Kwa kweli Mwenyezi Mungu Anayatambua mnayoyafanya, na Atawapa malipo yake

    [54] Na useme, ewe Mtume, kuwaambia watu, «Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume.» Na wakipa mgongo, basi jukumu la Mtume ni kufanya aliyoamrishwa ya kuufikisha ujumbe, na ni jukumu la watu wote kuyafanya waliyoamrishwa ya kufuata. Na mkimtii yeye mtaongoka. Na jukumu la Mtume ni kuufikisha ujumbe wa Mola wake mafikisho yaliyo wazi

    [55] Mwenyezi Mungu Amewaahidi walioamini miongoni mwenu na wakafanya matendo mema kwamba atawarithisha ardhi ya washirikina na atawafanya ni wasimamizi wa hiyo ardhi, kama alivyofanya kwa waliokuja kabla yao kati ya wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake, na Aifanye Dini yao ambayo Ameridhika nayo na Akawachagulia, nayo ni Uislamu, ni Dini yenye ushindi na uthabiti, na Azigeuze hali zao kwa kuwaondolea kicho na kuwaletea amani, iwapo watamuabudu Mwenyezi Mungu, Peke Yake, na watasimama imara kwa kumtii, na wasimshirikishe na kitu chochote. Na Mwenye kukanusha baada ya hilo la kupewa usimamizi, amani, uthabiti na utawala kamili, na akakanusha neema za Mwenyezi Mungu, basi hao ndio waliotoka nje ya utiifu kwa Mwenyezi Mungu

    [56] Na isimamisheni Swala kwa kuitimiza, na toeni Zaka kuwapa wanaostahiki kupewa na mumtii Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa kutarajia Mwenyezi Mungu Awarehemu

    [57] Msidhani tena msidhani kwamba wale waliokufuru wanamshinda Mwenyezi Mungu katika ardhi, kwani Yeye ni Muweza wa kuwaangamiza, na marejeo yao, huko Akhera ni Motoni. Na ni mabaya sana marejeo haya na mwisho huu. Maneno haya ni maelekezo kwa ummah wote, ingawa anayeambiwa hapa ni Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [58] Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifanyia kazi sheria Zake! Waamrisheni watumwa wenu, wajakazi wenu na watoto waungwana mabao umri wao haujafikia wa kubaleghe waombe ruhusa wakitaka kuingia kwenu katika nyakati za mapumziko yenu na kuvua nguo zenu: kabla ya Swala ya Alfajiri, kwa kuwa huo ni wakati wa kuvua nguo za kulalia na kuvaa nguo za baada ya kuamka, na wakati wa kuvua nguo kwa mapumziko ya kipindi cha mchana wakati wa jua kali, na baada ya Swala ya Isha, kwa kuwa huo ni wakati wa kulala. Nyakati tatu hizi ni za kujifunua na kujiacha wazi na kunapungua kujisitiri. Lakini katika nyakati sizokuwa hizo, si makosa wakiingia bila ya idhini, kwa kuwa wao wanahitaji kuingia kwenu, wao ni wa kuingia na kutoka mara kwa mara kwa kutumika, na kwa kuwa dasturi iliyozoeleka ni kuwa nyinyi mnatembeleana nyakati hizi kwa kutimiza haja zenu zenye maslahi kwenu. Na kama Alivyowafafanulia Mwenyezi Mungu hukumu za kutaka ruhusa (ya kuingia majumbani), Anawafafanulia aya Zake, hukumu Zake, hoja Zake na Sheria za Dini Yake. Na Mwenyezi Mungu Anayajua sana yanayowafaa viumbe Wake, ni Mwingi wa hekima katika upelekeshaji Wake mambo yao

    [59] Na pindi watoto wanapofikia miaka ya kubaleghe na kukalifishwa hukumu za kisheria, ni juu yao watake ruhusa wakitaka kuingia nyakati zote kama wanavyotaka ruhusa watu wazima. Na kama Mwenyezi Mungu Anavyowafafanulia adabu za kutaka ruhusa (kuingia majumbani), vilevile Anawafafanulia Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, aya Zake. Na Mwenyezi Mungu Anayajua sana yanayowafaa waja Wake, ni Mwingi wa hekima katika sheria Zake

    [60] Na wanawake wakongwe ambao wamejikalia hawajistareheshi na hawana matamanio kwa sababu ya uzee wao, hawana hamu ya kuolewa na wanaume wala wanaume hawana hamu nao. Wanawake hawa hawana makosa kujitanda sehemu ya nguo zao kama vile shuka, bila kuonesha pambo wala kujirembesha. Na kuvaa kwao nguo hizi, kwa kujisitiri na kujihifadhi, ni uzuri kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Msikizi wa maneno yenu, ni Mjuzi wa nia zenu na matendo yenu

    [61] Hawana dhambi watu wenye nyudhuru miongoni mwa vipofu, viguru na wagonjwa, kuyaacha mambo ya lazima ambayo hawawezi kuyatekeleza, kama kupigana jihadi na mfano Wake katika vitu ambavyo vinahitajia kwa kipofu awe huona na kiguru awe mzima na mgonjwa awe na afya nzuri. Na nyinyi, enyi Waumini, hamuna makosa kula kwenye majumba ambayo ndani yake kuna wake zenu na watoto wenu, na hapa yanaingia majumba ya watoto, au majumba ya baba zenu au mama zenu au ndugu zenu wa kiume au dada zenu au ami zenu au mashangazi zenu au wajomba zenu au mama zenu wadogo au kwenye nyumba ambazo mliwakilishwa kuzisimamia wakati wenyewe hawapo kwa ruhusa yao au kwenye nyumba za marafiki. Hakuna makosa yoyote kwenu kula mkiwa pamoja au mbalimbali. Na muingiapo kwenye nyumba zinazokaliwa au zisizokaliwa, amkianeni nyinyi kwa nyinyi kwa maamkizi ya Kiislamu, nayo ni «As-salāmu ‘alaikum wa rahmatullāhi wa barakātuh, au As-salāmu ‘alainā wa ‘alā ‘ibādillāhi-s-sālihīn, iwapo hakuna yoyote. Maamkizi haya Mwenyezi Mungu Ameyaweka, nayo yana baraka, yanakuza kusafiana nia na kupendana, ni mazuri yanayopendeza kwa mwenye kuyasikia. Na kwa mfano wa ufafanuzi huu anawafafanulia Mwenyezi Mungu alama za Dini Yake na aya Zake, ili mzifahamu na mzitumie

    [62] Kwa hakika Waumini kikwelikweli ni wale ambao Wamemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakazitumia sheria Zake, na wakiwa wapo pamoja na Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, katika jambo ambalo amewakusanya kwalo la maslahi ya Waislamu, hawaondoki mpaka wamuombe ruhusa. Kwa hakika wale wanaokuomba ruhusa, ewe Nabii, ndio wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake kikweli. Basi wakikuomba ruhusa kwa baadhi ya haja zao, mruhusu unayemtaka miongoni mwa wale waliokuomba ruhusa kuondoka kwa udhuru, na uwaombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu, kwani Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe dhambi za waja Wake wenye kutubia, ni mwingi wa huruma kwao

    [63] Msiseme, enyi Waumini, mnapomuita Mtume wa Mwenyezi Mungu, «Ewe Muhammad!» wala «Ewe Muhammad bin Abdillah!» kama wanavyosema hivyo baadhi yenu kuwaambia wengine. Lakini mtukuzeni na mseme, «Ewe Nabii wa Mwenyezi Mungu! Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu!» Kwa kweli Mwenyezi Mungu Anawajua wale wanaoondoka kutuka kwenye kikao cha Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa siri, bila ya ruhusa yake, wakisaidiana kujificha. Basi na wajihadhari wanaoenda kinyume na amri Yake wasije wakashukiwa na janga na shari au adhabu yenye uchungu iumizayo

    [64] Jueni mtanbahi kwamba ni vya Mwenyezi Mungu vilivyoko mbinguni na ardhini, kwa kuviumba, kuvimiliki, kuvifanya vimdhalilikie. Ujuzi Wake umevizunguka vyote ambavyo muko navyo. Na Siku ya Akhera, ambayo waja watarejea Kwake, Atawapa habari ya matendo yao, na Atawalipa kwayo. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu, hayafichamani Kwake Yeye matendo yao na hali zao

    Kipambanuzi

    Surah 25

    [1] Ni kubwa mno baraka za Mwenyezi Mungu na ni mengi sana mema Yake na ni kamilifu sifa Zake, Aliyetakasika na kutukuka, Ambaye Ameiteremsha Qur’ani, yenye kupambanua baina ya ukweli na ubatilifu, kwa mja Wake Muhammad, rehemea ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ili awe ni mjumbe kwa binadamu na majini na awe muonyaji wa adhabu ya Mwenyezi Mungu kwao

    [2] Ambaye Ana ufalme wa mbingu na ardhi, Hakujifanyia mtoto na hakuwa na mshirika katika ufalme Wake. Na Yeye Ndiye Aliyeumba kila kitu, Akakisawazisha kulingana na umbo linalonasibiana nacho na inavyotakikana kulingana na hekima Yake, pasi na kupungua wala kwenda kombo

    [3] Na washirikina wa kiarabu walitengeneza waungu, wasiokuwa Mwenyezi Mungu. Waungu hao hawawezi kuumba chochote, na Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyewaumba wao na wenye kuwaabudu, wala hawana uwezo wa kuzuia madhara wala kujiletea manufaa, wala hawawezi kukifisha kilicho hai wala kukihuisha kilichokufa au kumfufua yoyote, miongoni mwa wafu, akiwa hai kutoka kaburini mwake

    [4] Na wenye kumkanusha Mwenyezi Mungu walisema kwamba hii Qur’ani ni urongo tu na ni uzushi uliofanywa na Muhammad na akasaidiwa na watu wengine. Kwa hakika wamefanya udhalimu mbaya sana na wameleta uzushi wenye kuchukiza, kwani Qur’ani haikuwa inamkinika kwa binadamu yoyote kuizua

    [5] Na walisema kuhusu Qur’ani, «Hiyo ni hadithi za wakale katika vitabu vyao, na Muhammad amezinakili. Basi hizo anasomewa asubuhi na jioni,»

    [6] Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Kwa hakika Aliyeiteremsha Qur’ani ni Mwenyezi Mungu Ambaye ujuzi Wake umevizunguka vilivyoko mbinguni na ardhini. Kwa hakika Yeye ni Msamehefu sana kwa waliotubia kutokana na madhambi na maasia, ni Mwenye huruma kwao kwa kuwa hakufanya haraka ya kuwatesa.»

    [7] Na walisema washirikina, «Ana nini huyu anayedai kwamba yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (wakimkusudia Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie), anakula chakula kama sisi na aenda sokoni kutafuta riziki? Basi si angalimtuma Malaika awe naye ashuhudilie ukweli wake

    [8] au imshukie kutoka mbinguni kanzi ya mali, au awe na shamba kubwa ambalo yeye anakula matunda yake.» Na wakaendelea kusema, hawa madhalimu wenye kukanusha, «Mumfuatao nyinyi si mwingine isipokuwa ni mtu aliyefanyiwa uchawi ulioathiri akili yake.»

    [9] Tazama, ewe Mtume, namna walivyosema, hawa wakanushaji, juu yako maneno hayo ya ajabu yanayofanana na mifano kwa ugeni wake, ili wafikie kukukanusha, kwa hivyo wakawa mbali na haki, na kwa hivyo hawapati njia ya kuifikia (hiyo haki) ili wayarakibishe maneno waliyoyasema kuhusu wewe, ya urongo na uzushi

    [10] Ni kubwa mno baraka za Mwenyezi Mungu, na ni mengi sana mema Yake, Ambaye Akitaka Atakufanyia mema zaidi kuliko yale waliotamani uwe nayo, Angalikufanyia, ulimwenguni, mashamba mengi ambayo kati yake inapita mito, na Akufanye uwe na majumba makubwa ya fahari

    [11] Na hawakukanusha, kwa kuwa unakula chakula na unaenda sokoni, lakini wameikanusha Siku ya Kiyama na malipo yake yaliyoko. Na tumewatayarishia waliokikanusha Kiyama Moto mkali, watachomwa nao

    [12] Moto huo ukiwaona hawa wakanushaji Siku ya Kiyama, kutoka mahali mbali, watasikia sauti ya kuchemka kwake na mkoromo wake kwa ukali wa hasira zake kwao

    [13] Na pindi wakitupwa kutoka mahali pembamba sana pa moto wa Jahanamu, ikiwa mikono yao imeshikanishwa na minyonyoro kwenye shingo zao, hapo watajiapiza kuangamia ili wajiokoe nayo

    [14] Hapo wataambiwa kwa kukatishwa tamaa, leo msjiiombee maangamivu mara moja, lakini jiombeeni mara nyingi, kwani hilo halitawaongezea isipokuwa makero, hakuna maokozi kwenu

    [15] Sema uwaambie, ewe Mtume, «Je, Moto huu mliosifiwa ni bora au ni Pepo ya neema za milele walioahidiwa wenye kuiogopa adhabu ya Mwenyezi Mungu, ambayo itakuwa yao ikiwa ni malipo ya matendo yao na ni mahali watakapoishia huko Akhera

    [16] Hawa wenye utiifu watavipata wanavyovitamani vya ladha za neema, starehe yao humo ni ya daima, na kuingia kwao humo ilikuwa ni ahadi ya Mola wako, ewe Mtume, yenye kuombwa, kwa kuwa waja wema wa Mwenyezi Mungu wanamuomba (hiyo Pepo). Na Mwenyezi Mungu Haendi kinyume na ahadi Yake

    [17] Na Siku ya Kiyama, Mwenyezi Mungu Atawakusanya washirikina na vile ambavyo walikuwa wakiviabudu badala Yake. Hapo awaambie waabudiwa, «Je, ni nyinyi mliowapoteza njia ya haki waja wangu hawa, au ni wao wenyewe waliopotea njia wakawaabudu nyinyi?»

    [18] Hapo waabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu watasema, «Kutakasika ni kwako, ewe Mola wetu! Tunajiepusha na kitendo walichokifanya hawa. Haipasii kwetu sisi kuwategemea wasaidizi wa kutusaidia isipokuwa wewe. Lakini wewe uliwasterehesha hawa washirikina na baba zao kwa mali na afya nzuri, mpaka wakasahau utajo wako wakakushirikisha, na wakawa ni watu walioangamia walioghilibiwa na ubaya na hizaya.»

    [19] Hapo waambiwe washirikina, «Kwa kweli, wamewakanusha nyinyi, hawa mliowaabudu kwenye madai yenu juu yao. Enyi hawa, nyinyi hamuwezi kuzikinga nafsi zenu na adhabu wala kuziokoa. Na mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, akajidhulumu nafsi yake, akamuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu na akafa katika hali hiyo, mwenyezi Mungu Atamuadhibu adhabu kali

    [20] Na hatukumtumiliza yoyote kabla yako, ewe Mtume, miongoni mwa Mitume wetu, isipokuwa walikuwa binadamu, wanaokula chakula na wanaoenda sokoni. Na tumewafanya baadhi yenu, enyi watu, ni maonjo na mtihani kwa wengine, kwa uongofu na upotevu, utajiri na umasikini, uzima na ugonjwa. Basi je, mtavumilia msimame imara juu ya yale ambayo Mwenyezi Mungu Amewalazimisha nayo na mumshukuru ili Mola wenu awape malipo mema au hamtavumilia mustahili kuteswa? Na Mola wako, ewe Mtume, Anamuona anayepapatika au anayevumilia, na anayekanusha au anayeshukuru

    [21] Na walisema wale ambao hawatarajii kukutana na Mola wao baada ya kufa kwao kwa kuwa wanamkanusha, «Si angalau tuteremshiwe Malaika watueleze kwamba Muhammad ni mkweli au tumuone Mola wetu waziwazi Atuelezee habari ya ukweli wake juu ya utume wake.» Kwa kweli wamejiona nafsi zao na wamefanya kiburi kwa kuwa wamefanya ujasiri kusema hili na wamepita mpaka katika ujeuri wao na ukafiri wao

    [22] Siku watakapowaona Malaika wakati wa kufa kwao, na wakiwa ndani ya makaburi yao na Siku ya Kiyama, kwa sura ambazo sizo zile walizozitaka, sio kuwapa bishara ya Pepo, lakini kuwaambia, «Mwenyezi Mungu Ameifanya Pepo ni mahali palipoharamishwa kwenu.»

    [23] Hapo tutayaleta yale waliyoyafanya yanayoonekana kuwa ni mazuri na ya kidini, tuyafanye ni yenye kubatilika na kupotea. Hayatawanufaisha na yatakuwa ni kama vumbi linalorushwa, nalo ni lile vumbi lembamba linaloonekana kwenye mwangaza wa jua. Hivyo ni kwamba matendo mema hayawi na manufaa yoyote huko Akhera isipokuwa mwenye kuyafanya awe na imani ya kumuamini Mwenyezi Mungu na kumtakasia na kumfuata Mtume Wake Muhammd, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [24] Watu wa Peponi, Siku ya Kiyama, watakuwa na mahali pa kutulia bora zaidi kuliko watu wa Motoni, na watakuwa na mashukio mazuri kabisa. Raha yao imekamilika na starehe yao haitatangamana na chochote kile chenye kuharibu

    [25] Ikumbuke, ewe Mtume, Siku hiyo ambayo mbingu zitapasuka-pasuka, na katika mwanya wa pasuko hizo yajitokeza mawingu meupe yaliyo membamba, na Siku hiyo Mwenyezi Mungu Awateremshe Malaika wa mbinguni wawazunguke viumbe katika Mkusanyiko, na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, Aje kufanya uamuzi baina ya waja kwa namna inayonasibiana na utukufu Wake

    [26] Mamlaka ya kikweli katika Siku hii ni ya Mwingi wa rehema Peke Yake bila mwingine. Na Siku hii itakuwa ngumu kwa makafiri kwa mateso yatakayowapata na adhabu kali

    [27] Na ikumbuke, ewe Mtume, Siku ambayo mwenye kujidhulumu nafsi yake ataiuma mikono yake kwa majuto na unguliko kwa kusema, «Laiti mimi niliandamana na Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na nikamfuata katika kuufanya Uislamu kuwa ni njia ya Peponi,»

    [28] na atasema kwa maunguliko, «Laiti mimi sikumfanya fulani kuwa ni rafiki wa kumfuata na kumpenda

    [29] Amenipoteza rafiki huyu na kuniepusha na Qur’ani baada ya kunijia» Na Shetani aliyefukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu amekuwa daima ni mwenye kumtupa mwanadamu. Katika aya hizi kuna onyo kwamba rafiki mbaya asifuatwe, kwani yeye huenda akawa ni sababu ya kumtia, yule anayefuatana na yeye, Motoni

    [30] Na Mtume atasema akishtakia matendo ya watu wake, «Ewe Mola wangu! Kwa kweli watu wangu wameiacha hii Qur’ani na wameigura, wameendelea sana katika kuipa mgongo na kuacha kuizingatia na kuitumia na kuifikisha. Katika aya hii pana kitisho kikubwa kwa anayeigura Qur’ani na asiitumie

    [31] Na kama tulivyokufanya, ewe Mtume, uwe na maadui miongoni mwa wahalifu watu wako, tulimfanya kila Nabii, miongoni mwa Manabii, awe na adui kati ya wale wahalifu wa watu wake. Basi vumilia kama walivyovumilia. Na inatosha kuwa Mola wako ni Mwenye kuongoa, ni Mwenye kuilekeza, ni Mwenye kuonyesha njia na ni Mwenye kutoa msaada wa kukusaidia wewe dhidi ya maadui zako.Katika haya pana maliwazo kwa Nabii Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye

    [32] Na Waliokanusha walisema, «Si hii Qur’ani ateremshiwe Muhammad kwa mara moja» kama ilivyokuwa Taurati, Injili na Zaburi? Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Akasema «Tumeiteremsha ikiwa hivyo, sehemu-sehemu, ili kuutia nguvu moyo wako na ili wewe uzidi utulivu, upate kuielewa na kuibeba, na tumeifunua wazi kwa kuithibitisha na kwa kuileta polepole.»

    [33] Na hawakujii, ewe Mtume, hawa washirikina na hoja yoyote au utata wowote isipokuwa tutakuletea majibu ya ukweli na ufafanuzi wake mzuri zaidi

    [34] Hao makafiri ndio watakaoburutwa kwa nyuso zao hadi kwenye Moto wa Jahanamu. Hao ndio wenye mashukio mabaya kabisa miongoni mwa watu na ndio walioko mbali kabisa na njia ya haki

    [35] Na kwa hakika, tulimpelekea Mūsā Taurati, tukamfanya ndugu yake Hārūn kuwa ni msaidizi wake

    [36] na tukawaambia wao wawili,»Endeni kwa Fir’awn na watu wake waliozikanusha dalili za uola wetu na uungu wetu.» Basi wakawaendea na wakawalingania wamuamini Mwenyezi Mungu, wamtii na wasimshirikishe. Wakawakanusha, na kwa hivyo tukawaangamiza maangamivu makubwa

    [37] Na tuliwazamisha watu wa Nūḥ kwa mafuriko walipomkanusha. Na mwenye kumkanusha Mtume yoyote huwa amewakanusha Mitume wote. Na tulikufanya kule kuwazamisha ni mazingatio kwa watu. Na tutawapatia wao na wale waliofuata njia yao katika kukanusha, Siku ya Kiyama, adhabu yenye kuumiza

    [38] Na tuliwaangamiza hao ‘Ād, watu wa Hūd, na Thamūd, watu wa Ṣāliḥ, na watu wa Kisimani na watu wengine wengi waliokuwako baina ya watu wa Nūḥ, kina ‘Ād, kina Thamūd na watu wa Rass(hapo kisimani) hakuna awajuao isipokuwa Mwenyezi Mungu

    [39] Na ummah wote hao tuliwabainishia hoja na kuwafafanulia dalili na tukawaondolea nyudhuru (za kutojua). Pamoja na hivyo, hawakuamini, na kwa ajili hiyo tuliwapa maangamivu kwa kuwaadhibu

    [40] Na washirikina wa Makkah walikuwa wakikipitia kijiji cha watu wa Lūṭ katika safari zao, nacho ni kijiji cha Sadūm ambacho kiliangamizwa kwa mawe kutoka mbinguni, wasizingatie kwa hilo, bali walikuwa hawatazamii kuwa kuna marejeo Siku ya Kiyama ambapo wao watalipwa

    [41] Na wakuonapo hao wakanushaji, ewe Mtume, wanakufanyia shere wakisema, «Je, ni huyu yule anayedai kwamba Mwenyezi Mungu Amemtumiliza kuwa ni mjumbe kwetu

    [42] Yeye amekaribia kutuepusha na kuwaabudu masanamu wetu kwa hoja zake za nguvu na ufasaha wake, lau hatungalisimama imara juu ya kuwaabudu.» Na watajuwa, watakapoiona adhabu wanayoistahili, ni nani aliyepotoka zaidi kidini: ni wao au ni Muhammad

    [43] Mwangalie, ewe Mtume, kwa kumuonea ajabu yule aliyeyatii matamanio yake kama kumtii Mwenyezi Mungu. Je, wewe utakuwa ni mwenye kumtunza mpaka umrudishe kwenye Imani

    [44] Au unadhani kwamba wengi wao wanazisikia aya za Mwenyezi Mungu, kusikia kwa kuzingatia, au wanayaelewa yaliyomo ndani yake? Hawakuwa isipokuwa ni kama wanyama, katika kutonufaika kwa wanayoyasikia, bali wao wamepotea njia zaidi kuliko hao wanyama

    [45] Kwani huoni vipi Mwenyezi Mungu Alivyokinyosha kivuli kuanzia kutokea alfajiri mpaka kutokea jua? Na lau Mwenyezi Mungu Alitaka Angalikifanya kisimame na kitulie, kisiondolewe na jua kisha tungalilifanya jua kuwa ni alama ambayo kwa hali zake inachukuliwa dalili ya hali za kivuli

    [46] Kisha kivuli kinapotea kidogo- kidogo, kila kunapoongezeka kupaa juu kwa jua ndipo kunapoongezeka kupungua kwake. Hilo ni miongoni mwa dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu, ukubwa Wake na kwamba Yeye Peke Yake Ndiye Anayestahiki kuabudiwa, si mwengine

    [47] Na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Ndiye Aliyewawekea usiku kuwa ni wenye kuwasitiri nyinyi kwa giza lake, kama vile mavazi yanavyowasitiri. Na Amewawekea usingizi kuwa ni raha ya miili yenu, ndani yake mnatulia na mnapumzika. Na Amewawekea mchana ili mtapakae kwenye ardhi na mtafute maisha yenu

    [48] Na Yeye Ndiye Aliyezituma pepo zinazobeba mawingu, zenye kuwabashiria watu mvua ikiwa ni rehema kutoka Kwake; na tumeyateremsha kutoka mbinguni maji ya kujisafisha nayo

    [49] ili tutoe kwayo mimea mahali pasipo na mimea, ipate kuhuika ardhi ya ukame baada ya kuwa imekufa (kwa ukavu), na ili tuwanyweshe maji hayo wanyama howa na watu miongoni mwa viumbe vyetu vyingi

    [50] Na hakika tunateremsha mvua juu ya sehemu ya ardhi bila ya nyingine, ili wale walioteremshiwa mvua wapate kukumbuka neema ya Mwenyezi Mungu juu yao na wamshukuru, na ili wale walionyimwa mvua wafanye haraka kutubia kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, Apate kuwarehemu wao na kuwanywesha. Lakini wengi wa watu wanakataa isipokuwa ni kukanusha neema zetu juu yao, kama neno lao wanalolisema, «tumeletewa mvua kwa sababu ya nyota kadha na kadha.»

    [51] Na lau tungalitaka tungalimpeleka muonyaji katika kila mji, wa kuwalingania wao kwa Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, na kuwaonya wao adhabu Yake. Lakini tumekufanya wewe, ewe Mtume, ni mwenye kupelekwa kwa watu wote wa ardhini, na tumekuamrisha wewe uwafikishie hii Qur’ani

    [52] Basi usiwatii makafiri kwa kuacha kitu chochote kile ambacho umetumilizwa nacho. Lakini fanya bidii yako katika kuufikisha ujumbe na upigane jihadi na wenye kuikanusha hii Qur’ani, kupigana jihadi kukubwa kusikochanganyika na udhaifu

    [53] Na Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyezichanganya bahari mbili: ya tamu yenye ladha nzuri, na ya chumvi yenye uchumvi mwingi, na Akaweka baina ya hizo mbili kizuizi chenye kuzuia kila mojawapo ya hizo isiiharibu nyingine na pingamizi ili mojawapo isiifikie nyingine

    [54] Na Yeye Ndiye Aliyeumba kizazi cha kiume na kike kutokamana na manii ya mwanamume, na kutokana na hayo ukapatikana ujamaa wa kinasaba na ujamaa wa ukwe. Na Mola wako ni Mwenye uweza wa kuumba Anachotaka

    [55] Na pamoja na dalili hizi za uweza wa Mwenyezi Mungu na wema Wake kwa viumbe Wake, makafiri wanaabudu, badala ya Mwenyezi Mungu, kitu ambacho hakiwanufaishi wakikiabudu wala hakiwadhuru wakiacha kukiabudu. Na kafiri ni msaidizi wa Shetani juu ya Mola wake, kwa kufanya ushirikina katika ibada ya Mwenyezi Mungu, na ni mwenye kumpa nguvu huyo Shetani juu kumuasi Mwenyezi Mungu

    [56] Na hatukukutumiliza wewe, ewe Mtume, isipokuwa uwe ni mwenye kuwabashiria Waumini Pepo na mwenye kuwaonya makafiri na Moto

    [57] Waambie, «Sitaki kutoka kwenu, kwa kufikisha ujumbe, malipo yoyote. Lakini mwenye kutaka kuongoka na kufuata njia ya haki inayompeleka kwa Mola wake na kutumia katika mambo Anayoyaridhia, mimi sitawalazimisha hilo, isipokuwa hilo, kwa kweli, ni bora kwa maslahi ya nafsi zenu.»

    [58] Na jitegemeze kwa Mwenyezi Mungu Ambaye Ana uhai uliokamilika kwa namna zote, kama inavyonasibiana na utukufu Wake, Ambaye hafi, na umtakase na sifa za upungufu. Na inatosha kuwa Mwenyezi Mungu ni Mtambuzi wa madhambi ya viumbe Vyake. Hakuna chochote kinachofichika Kwake katika hayo. Na Atawahesabia na Atawalipa kwa hayo

    [59] Aliyeumba mbingu na ardhi na vilivyoko baina yake kwa Siku sita, kisha akalingana juu ya '“Arsh - yaani Akawa juu na Akaangatika- kulingana kunakonasibiana na utisho Wake, Yeye Ndiye Mwingi wa rehema. Basi muulize, ewe Mtume, Mtambuzi kuhusu Yeye. Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika, Anajikusudia Mwenyewe Aliyetukuka, kwani Yeye Ndiye Anayejua sifa Zake, ukuu Wake na utukufu Wake. Na hakuna yoyote, katika binadamu, anayemjua zaidi Mwenyezi Mungu wala anayetambua habari Zake zaidi kuliko mja Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye

    [60] Na wakiambiwa makafiri, «Msujudieni Al-Raḥmān (Mwingi wa rehema) na muabuduni,» wanasema, «Hatumjui Al-Raḥmān (Mwingi wa rehema). Je, tukisujudie kila unachotuamrisha kukisujudia kwa kutii amri yako?» Basi hilo la kuwaita wao kumsujudia Al-Raḥmān (Mwingi wa rehema) linawaongezea wao kuikimbia imani na kuwa mbali nayo

    [61] Ni kubwa baraka za Mwingi wa rehema na ni nyingi kheri Zake Aliyeziweka mbinguni nyota kubwa pamoja njia zake, na akaliweka, katika hizo mbingu, jua linalotoa mwangaza na mwezi unaong’ara

    [62] Na Yeye Ndiye Aliyefanya usiku na mchana vipishane, kimoja baada ya kingine, kwa anayetaka kuzingatia hilo kwa kumuamini Mwenyezi Mungu, Mpelekeshaji mambo na Muumbaji au anayetaka kumshukuru Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa neema Zake na mema Yake

    [63] Na waja wa Mwingi wa rehema walio wema ni wale ambao wanatembea juu ya ardhi kwa utulivu wakiwa wanyenyekevu; na wajinga mafidhuli wanaposema nao maneno ya kuwaudhi wanawapa majibu mazuri na wanasema nao maneno ya kuwafanya wasalimike na dhambi na (pia wasalimike na) kukabiliana na mjinga kwa ujinga wake

    [64] Na ambao wanaswali usiku kwa wingi wakimtakasia Mola wao wakiwa ndani ya Swala na wakijidhalilisha Kwake kwa kusujudu na kusimama

    [65] Na ambao, pamoja na kujibidiisha kufanya ibada, wanamuogopa Mola wao na kwa hivyo wanamuomba Awaokoe na adhabu ya Jahanamu, kwani adhabu yake inalazimiana na muadhibiwa

    [66] Kwa hakika moto wa Jahanamu ni mahali pabaya pa kutulia na kukaa

    [67] Na ambao wakitumia mali zao hawapitishi kipimo katika kutoa wala hawabani katika matumizi, na kutumia kwao huwa kuko kati na kati baina ya kupitisha kipimo na kubana

    [68] Na ambao wanampwekesha Mwenyezi Mungu na hawamuombi wala kumuabudu mola asiyekuwa Yeye, wala hawaiui nafsi ambayo Mwenyezi Mungu Ameharamisha kuuawa isipokuwa kwa kitu kinachopasisha kuuawa, kama vile kukufuru baada ya kuamini au kuzini baada ya ndoa au kumuua mtu kwa uadui, wala hawazini bali wanazihifadhi tupu zao isipokuwa kwa wake zao au wale ambao mikono yao ya kulia imemiliki. Na mwenye kuyafanya madhambi haya makubwa atakuta mateso huko Akhera

    [69] Ataongezewa adhabu maradufu Siku ya Kiyama na ataketi milele akiwa mdhalilifu mnyonge. Onyo la kukaa milele ni kwa wale wanaoyafanya yote hayo au ni kwa yule aliyemshirikisha Mwenyezi Mungu

    [70] Lakini mwenye kutubia kutokana na madhambi haya toba ya dhati na akaamini imani ya kukata yenye kuambatana na matendo mema, basi hao Mwenyezi Mungu Atawafutia makosa yao na Atawaweka mahali Pake mema, kwa sababu ya kutubia kwao na kujuta kwao. Na kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe kwa anayetubia, ni Mwingi wa rehema kwa waja Wake kwa kuwa Amewaita watubie baada ya kushindana na Yeye kwa kufanya maasia makubwa kabisa

    [71] Na yoyote anayetubia kwa madhambi aliyoyafanya na akafanya matendo mema, basi yeye, kwa hilo, atakuwa amerudi kwa Mwenyezi Mungu kisawasawa, na hapo Mwenyezi Mungu Ataikubali toba yake na Atazifuta dhambi zake

    [72] Na ambao hawatoi ushahidi wa urongo wala hawahudhurii vikao vyake, na wapitapo kwa watu wa ubatilifu na ulaghai bila ya kukusudia wanapita hali ya kupa mgongo na kupinga, wanajiepusha nao (huo ubatilifu na ulaghai) na hawauridhii kwa wengine

    [73] Na ambao wakipewa mawaidha kwa aya za Qur’ani na dalili za upweke wa Mwenyezi Mungu hawajighafilishi nazo wakawa kama ambao ni viziwi hawakuzisikia na vipofu hawakuziona, lakini nyoyo zao zinazielewa na akili zao zinafunguka kuzikubali, na basi hapo wanajipomosha kwa Mwenyezi Mungu hali ya kusujudu na kutii

    [74] Na ambao wanamuomba Mwenyezi Mungu Aliyetukuka wakisema, «Mola wetu! Tutunukie miongoni mwa wake zetu na wana wetu cha kutuliza macho yetu na chenye maliwazo na furaha kwetu, na utufanye ni kiigizo chema kwa wachamungu kutuiga.»

    [75] Hao waja wa Mwingi wa rehema, waliosifika kwa sifa zilizopita, watalipwa majumba ya Peponi ya juu kabisa, kwa rehema ya Mwenyezi Mungu na kwa sababu ya uvumilivu wao juu ya kufanya matendo ya utiifu, na watalakiwa humo Peponi kwa maamkizi na salamu kutoka kwa Malaika, na watakuta maisha mema na kusalimika na maafa

    [76] hali ya kukaa milele humo bila ya kufa. Ni nzuri mno hiyo Pepo kuwa ni mahali pa wao kutulia na makao ya wao kukaa, hawatataka kuondoka hapo

    [77] Mwenyezi Mungu Anatoa habari kuwa Yeye hawajali watu wala hashughuliki nao lau si wao kumlingania Yeye ulinganizi wa ibada na ulinganizi wa maombi. Hakika yenu nyinyi, enyi makafiri, mumekanusha, na ukanushaji wenu utapelekea mupate adhabu yenye kuwa na nyinyi kama vile mwenye kudai anavyokuwa na mdaiwa wake, na Atawaangamiza duniani na Akhera

    Washairi

    Surah 26

    [1] «Ṭā, Sīn, Mīm.» Yametangulia maelezo kuhusu herufi za mkato mwanzo wa sura ya Al-Baqarah

    [2] Hizi ni aya za Qur’ani yenye kufafanua kila kitu, yenye kupambanua baina ya uongofu na upotevu

    [3] Huenda wewe, ewe Mtume, kwa kuwa una hamu sana ya kutaka wao waongoke, ukajiangamiza mwenyewe kwa kuwa wao hawakukuamini na hawakufuata kimatendo uongofu wako. Basi usifanye hivyo

    [4] Tukitaka tutawateremshia wakanushaji, miongoni mwa watu wako, miujiza itokayo mbinguni yenye kuwaogopesha itakayowalazimisha wao kuamini, na hapo shingo zao ziwe zimenyongeka na kudhalilika. Lakini hatukutaka hilo, kwani Imani yenye kunufaisha ni kuyaamini yaliyoghibu kwa hiyari

    [5] Na hauwajii washirikina hawa ukumbusho, kutoka kwa Mwingi wa rehema unaoanzwa kuteremshwa, kitu baada ya kitu, wenye kuwaamrisha na kuwakataza na kuwakumbusha Dini ya kweli, isipokuwa wanaupa mgongo na hawaukubali

    [6] Kwa hakika washaikanusha Qur’ani na washaifanyia shere, basi zitawajia wao habari za jambo ambalo walikuwa wakilifanyia shere na dharau, na itawashukia wao adhabu ikiwa ni malipo ya kumuasi Mola wao

    [7] Je, wanakanusha na hali wao hawakuiangalia ardhi ambayo ndani yake tumeotesha kila aina nzuri ya mimea ambayo hakuna awezae kuiyotesha isipokuwa Mola wa viumbe vyote

    [8] Kwa hakika, katika kuitoa mimea kwenye ardhi ni dalili wazi ya ukamilifu wa uweza wa Mwenyezi Mungu, na wengi wa watu hawakuwa ni wenye kuamini

    [9] Na kwa hakika Mola wako Ndiye Mshindi wa kila kiumbe, ni Mwenye kurehemu Ambaye rehema Yake imeenea kila kitu

    [10] Na wakumbushe watu wako, ewe Mtume, pindi Mola wako Alipomuita Mūsā kuwa awaendee watu madhalimu

    [11] nao ni watu wa Fir’awn na uwaambie wayaogope mateso ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na waache ukafiri na upotevu walionao

    [12] Mūsā akasema, «Mola wangu! Mimi ninaogopa wasije wakanikanusha juu ya utume

    [13] na moyo wangu ukaingia kero kwa kunikanusha, na ulimi wangu usiwe na ufasaha wa kulingania. Basi mtume Jibrili aende na wahyi kwa ndugu yangu Hārūn, ili anisaidie na aniamini kwa ninayoyasema, na awafafanulie kile ninachowaambia, kwani yeye ana ufasaha zaidi wa matamshi kuliko mimi

    [14] Na watanishika na kosa la kumuua mwanamume wa jamii ya Qibṭī miongoni mwao, na kwa hivyo ninaogopa wasiniue kwa ajili yake.»

    [15] Mwenyezi Mungu Akamwambia Mūsā, «Sivyo hivyo! Hawatakuua. Na nimekubali matakwa yako juu ya Hārūn. Basi endeni mkiwa na miujiza yenye kuonyesha ukweli wenu. Sisi tuko pamoja na nyinyi kwa ujuzi, utunzi na usaidizi tunasikiliza

    [16] Mjieni Fir’awn na mumwambie, «Sisi tumetumwa kwako na kwa watu wako kutoka kwa Mola wa viumbe wote

    [17] kwamba uwaache Wana wa Isrāīl waende na sisi.»

    [18] Fir’awn akasema kumwambia Mūsā kwa kumsimanga, «Je, hatukukulea kwenye majumba yetu ukiwa mchanga, ukakaa kwenye utunzi wetu miaka (mingi) katika umri wako

    [19] ukafanya tendo la jinai kwa kumuua mwanamume miongoni mwa watu wangu, ulipompiga na ukamsukuma, na wewe ni miongoni mwa wakanushaji neema zangu na kukataa uola wangu

    [20] Mūsā akasema kumjibu Fir’awn, «Nilifanya uliyoyataja kabla Mwenyezi Mungu Hajaniletea wahyi na kunitumiliza kama Mtume

    [21] ndipo nilitoka kwenu kwa kukimbia kuelekea Madyan nilipoogopa usije ukaniua kwa nililolifanya bila kukusudia, Na Mola wangu Akanitunuku unabii na elimu na Akanifanya ni miongoni mwa Mitume

    [22] Na kwani huko kulelewa nyumbani kwako unakuona ni neema kutoka kwako juu yangu, na hali wewe umewafanya Wana wa Isrāīl ni watumwa , unawachinja wana wao wa kiume na unawaachilia wanawake wao ili watumwe na wadharauliwe?»

    [23] Fir’awn akamwambia Mūsā, «Na huyo Mola wa viumbe wote Ambaye unadai kwamba wewe ni mjumbe Wake, ni kitu gani?»

    [24] Mūsā akasema, «Yeye ni Mmiliki na Mwenye kuipelekesha mbingu na ardhi na vilivyoko baina ya viwili hivyo. Iwapo nyinyi mna yakini na hilo, basi aminini.»

    [25] Fir’awn akasema kuwaambia walioko pambizoni mwake miongoni mwa watukufu wa watu wake, «Je, hamusikii maneno ya Mūsā ya ajabu kwamba kuna mola asiyekuwa mimi?»

    [26] Mūsā akasema, «Mola Ambaye mimi nawalingania nyinyi Kwake ni Yule Aliyewaumba nyinyi na Aliyewaumba wa mwanzo. Basi vipi nyinyi mnamuabudu ambaye ni kiumbe kama nyinyi na yeye ana mababa waliotoeka kama mababa zenu?»

    [27] Fir’awn akasema kuwaambia wale watu wake makhsusi akiwapandisha ghadhabu zao, kwa kuwa Mūsā amemkanusha yeye, «Kwa kweli, huyu mjumbe wenu aliyeletwa kwenu ni mwendawazimu , asema maneno yasiyofahamika.»

    [28] Mūsā akasema, «Mola wa Mashariki na Magharibi na vilivyoko baina ya viwili hivyo, na vilivyomo ndani yake vya mwangaza na giza. Hili linapelekea kuwa ni lazima kumuamini Yeye Peke Yake, iwapo nyinyi ni miongoni mwa watu wa akili na kuzingatia.»

    [29] Fir’awn akamwambia Mūsā kwa kumtisha, «Ukichukua mwingine aseyekuwa mimi ukamfanya ni mola nitakufunga jela pamoja na wale niliowafunga.»

    [30] Mūsā akasema, «Je, utanifanya mimi ni miongoni mwa wafungwa jela, hata nikikuletea hoja ya kukata ambayo kwa hiyo utabainika ukweli wangu?»

    [31] Fir’awn akasema, «Basi ilete ikiwa wewe ni miongoni mwa wakweli katika madai yako.»

    [32] Hapo Mūsā akaitupa fimbo yake na ikageuka kuwa nyoka wa kikweli, si kiinimacho kama wanavyofanya wachawi

    [33] Na akautoa mkono wake kwenye uwazi wa kanzu yake uliofunguliwa kifuani au chini ya kwapa lake, na papo hapo ukawa mweupe kama barafu, na sio weupe wa mbalanga, ukawashangaza waangaliaji

    [34] Fir’awn akasema kuwaambia watukufu wa watu wake, kwa kuogopa wasije wakaamini, «Kwa kweli Mūsā ni mchawi hodari

    [35] Anataka kuwatoa nyinyi, kwa uchawi wake, kwenye ardhi yenu. Basi mnatoa shauri gani kuhusu yeye nipate kuyafuata maoni yenu?»

    [36] Watu wake wakamwambia, «Msubirishe Mūsā na Hārūn, na utume askari mijini wawakusanye wachawi

    [37] Watakujia na kila anayejua uchawi na akawa hodari kuufahamu.»

    [38] Wakakusanywa wachawi, na wakapangiwa wakati maalumu, nao ni wakati wa mchana wa siku ya Pambo ambayo wanajitenga na shughuli zao, na wanajikusanya na kujipamba, ili wakutane na Mūsā

    [39] na wawahimize watu kujumuika kwa matarajio kwamba ushindi uwe ni wa wachawi

    [40] Sisi tunatarajia ushindi uwe ni wa wachawi ili tujikite kwenye dini yetu

    [41] Na wachawi walipomjia Fir’awn walimwambia, ‘Je, sisi tutakuwa na malipo ya mali au heshima ikiwa tutakuwa ni wenye kumshinda Mūsā?»

    [42] Fir’awn akasema, «Ndio, nyinyi mtapata kwangu malipo mnayoyataka, na nyinyi hapo mtakuwa ni miongoni mwa wenye kusogezwa karibu na mimi.»

    [43] Mūsā akasema kuwaambia wachawi, akitaka kuutangua uchawi wao na kuonyesha kuwa kile alichokileta si uchawi, «Tupeni mtakavyovitupa vya uchawi.»

    [44] Basi wakatupa kamba zao na fimbo zao, na zikawadhihirikia watu kwenye akili zao kuwa ni nyoka wanaotembea, na wakaapa kwa enzi ya Fir’awn kwa kusema, «Sisi ni wenye kushinda.»

    [45] Hapo akaitupa Mūsā fimbo yake, na papo hapo ikawa ni nyoka mkubwa, akawa anavimeza vile vilivyotokana na wao, hao wachawi, vya uzushi na bandia

    [46] Waliposhuhudia hilo na wakajua kuwa halitokani na udanganyifu wa wachawi, walimuamini Mwenyezi Mungu na wakamsujudia

    [47] na wakasema, «Tumemuamini Mola wa viumbe vyote

    [48] Mola wa Mūsā na Hārūn.»

    [49] Fir’awn akasema kuwaambia wachawi kwa kukataa, «Mumemkubali Mūsā bila ya idhini yangu!» Na akasema akiashiria kuwa kitendo cha Mūsā ni uchawi, «Yeye ni mkubwa wenu aliyewafundisha nyinyi uchawi, basi mtayajua mateso yatakayowafikia. Nitaikata mikono yenu na miguu yenu kitafauti: kwa kuukata mkono wa kulia na mguu wa kushoto au kinyume chake, na nitawasulubu nyote.»

    [50] Wachawi walisema kumwambia Fir’awn, «Hakuna madhara ya duniani yatakayotupata, kwa kweli sisi ni wenye kurudi kwa Mola wetu, Atupe neema ya kuendelea

    [51] Sisi tunataraji Mola wetu Atusamehe makosa yetu ya ushirikina na mengineyo kwa kuwa sisi ndio Waumini wa mwanzo katika watu wako.»

    [52] Na Mwenyezi Mungu Akampelekea wahyi Mūsā, amani imshukie, kwamba, «Enda usiku pamoja na walioamini miongoni mwa Wana wa Isrāīl, ili Fir’awn na askari wake, ambao watawafuata nyinyi, wasije wakawafikia kabla ya kufika kwenu baharini.»

    [53] Fir’awn akawatuma askari wake, alipopata habari kwamba Wana wa Isrāīl wameenda usiku, wakusanye jeshi lake kutoka miji ya utawala wake

    [54] Fir’awn akasema, «Kwa kweli, Wana wa Isrāīl waliokimbia pamoja na Mūsā ni pote twevu lenye idadi ndogo

    [55] Na wao wamevijaza hasira vifua vyetu kwa kuwa wameenda kinyume na dini yetu na wametoka bila ya idhini yetu

    [56] na sisi sote tuko macho, tuko tayari nao.»

    [57] Mwenyezi Mungu Akamtoa Fir’awn na watu wake kwenye ardhi ya Misri yenye mabustani, mabubujiko ya maji

    [58] hazina za mali na majumba mazuri

    [59] Na kama tulivyowatoa, tuliwapatia nyumba hizo Wana wa Isrāīl baada yao wao

    [60] Hivyo basi Fir’awn na askari wake walimkuta Mūsā na waliokuwa pamoja na yeye wakati wa kuchomoza jua

    [61] Yalipoonana makundi mawili, watu wa Mūsā walisema, «Kwa hakika jumuiko la Fir’awn ni lenye kutufikia na kutuangamiza.»

    [62] Mūsā alisema kuwaambia, «Sivyo! Mambo si kama mlivyotaja. Hamtafikiwa. Kwa hakika Mwenyezi Mungu Yupo na mimi kwa msaada, Ataniongoza njia ya kuokoka mimi na kuokoka nyinyi.»

    [63] Hapo tukampelekea wahyi Mūsā kwamba, «Piga bahari kwa fimbo yako!» Akapiga. Na bahari ikapasuka njia kumi na mbili kwa idadi ya kabila za Wana wa Isrāīl. Na kila kipande kilichojitenga na bahari ni kama jabali kubwa

    [64] Na tulimsogeza karibu Fir’awn na watu wake mpaka wakaingia baharini

    [65] Na tukamuokoa Mūsā na waliokuwa pamoja na yeye wote. Bahari ikaendelea kuachana kwake (kwa ule mpasuko) mpaka wakavuka kwenye nchi kavu

    [66] Kisha tukamzamisha Fir’awn na waliokuwa pamoja na yeye kwa kuifanya bahari iwafinike baada ya wao kuingia ndani wakimfuata Mūsā na watu wake

    [67] Kwa hakika, katika hilo lililotukia pana mazingatio ya ajabu yenye kuonyesha dalili ya uweza wa Mwenyezi Mungu. Na wengi wa wafuasi wa Fir’awn hawakuwa ni wenye kuamini, pamoja na alama hii yenye kushinda

    [68] Na hakika ya Mola wako Ndiye Mshindi, Ndiye Mwenye kurehemu. Kwa nguvu Zake na ushindi Amewaangamiza makafiri wakanushaji, na kwa rehema Yake Amemuokoa Mūsā na waliokuwa pamoja na yeye wote

    [69] Na wasimulie makafiri, ewe Mtume, habari ya Ibrāhīm

    [70] alipomwambia babake na watu wake, «Mnaabudu kitu gani?»

    [71] Wakasema, «Tunaabudu masanamu, tunaketi na kuendelea kuwaabudu.»

    [72] Akasema Ibrāhīm akiwatanabahisha uharibifu wa njia yao, «Kwani wanasikia maombi yenu mnapowaomba

    [73] Au wanawapatia manufaa mkiwaabudu? Au wanawafanya mupate madhara mkiacha kuwaabudu?»

    [74] Wakasema, «Haliwi lolote katika hayo, lakini tuliwakuta mababa zetu wakiwaabudu, na sisi tukawaiga katika yale ambayo walikuwa wakiyafanya.»

    [75] Ibrāhīm akasema, «Je, mumefikiria kuvitia akilini hivyo mnavyoviabudu, miongoni mwa masanamu yasiyosikia wala kunufaisha wala kudhuru

    [76] nyinyi na mababa zenu waliowatangulia

    [77] Kwani hao mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni maadui zangu. Lakini Mola wa viumbe wote na Mmiliki wa mambo yao, Yeye Peke Yake Ndiye ninayemuabudu

    [78] Yeye Ndiye Aliyeniumba kwa sura nzuri zaidi. Yeye ananiongoza kwenye maslahi ya dunia na Akhera

    [79] Na Yeye Ndiye Anayenineemesha kwa chakula na kinywaji

    [80] Na nikipatikana na ugonjwa, Yeye Ndiye Anayeniponyesha na kuniondolea

    [81] Na Yeye Ndiye Atakayenifisha duniani kwa kuichukua roho yangu, kisha Atanihuisha Siku ya Kiyama, hakuna awezaye hilo isipokuwa Yeye

    [82] Na Ambaye ninatarajia Atanisamehe dhambi zangu Siku ya Malipo.»

    [83] Ibrāhīm akasema akimuomba Mola wake, «Mola wangu! Nitunukie elimu na fahamu, na unikutanishe na watu wema, na unikusanye mimi na wao Peponi

    [84] «Na unifanye niwe na sifa nzuri na utajo mwema kwa wale watakaokuja baada yangu mpaka Siku ya Kiyama

    [85] «Na unifanye mimi niwe miongoni mwa waja wako utakaowarithisha starehe za Peponi.»

    [86] Hii ni dua ya Ibrāhīm, amani imshukiye, ya kumuomba Mwenyezi Mungu Amuokoe babake na upotevu na Ampe uongofu, ili Amghufirie na Amsamehe, kama Ibrāhīm alivyomuahidi babake kumuombea Mungu, na ilipomfunukia kuwa yeye ni mwenye kuendelea kwenye ukafiri na ushirikina mpaka afe alijiepusha naye

    [87] «Na usinipe unyonge Siku hiyo, ambayo watu watatoka makaburini ili wahesabiwe na walipwe

    [88] Siku ambayo mali na watoto havitamfaa yoyote miongoni mwa waja

    [89] isipokuwa yule aliyemjia Mwenyezi Mungu kwa moyo uliyosalimika na ukafiri, unafiki na uovu.»

    [90] Na Pepo itasogezwa karibu kwa wale waliojiepusha na ukafiri na matendo ya uasi na wakamuelekea Mwenyezi Mungu kwa kumtii

    [91] Na Moto utaonyeshwa waziwazi kwa makafiri ambao walipotea njia ya uongofu na wakayafanyia ujasiri yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu na wakawakanusha Mitume Wake

    [92] Na wataambiwa kwa kulaumiwa, «Wako wapi waungu wenu ambao mlikuwa mkiwaabudu

    [93] badala ya Mwenyezi Mungu na mkidai kwamba wao watawaombea leo? Je, watawanusuru na wawazuilie adhabu isiwafikie au watajinusuru kwa kuikinga adhabu isiwafikie?» Hakuna chochote katika hayo

    [94] Hapo watakusanywa na watupwe kwenye Jahanamu kwa vichwa vyao, mara baada ya nyingine mpaka watakapotulia humo: wao, wale waliowapoteza

    [95] na wasaidizi wa Iblisi waliowapambia shari; hakuna yoyote kati yao atakayeponyoka

    [96] Watasema wakikiri makosa yao, na huku wanagombana, ndani ya Jahanamu, na wale waliowapoteza wao

    [97] «Tunaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba sisi, duniani, tulikuwa kwenye upotevu ulio waziwazi, haukuwa umefichika

    [98] tulipowafanya nyinyi kuwa ni sawa na Mola wa viumbe wote, Anayestahiki kuabudiwa, Peke Yake

    [99] Na hakuna kilichotutia kwenye mwisho huu mbaya isipokuwa ni wahalifu ambao walitulingania tumuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu

    [100] «Hapana yoyote wa kutuombea na kututoa kwenye adhabu

    [101] wala mwenye kutupenda kikweli na kutuhurumia

    [102] «Tunatamani tupatiwe fursa ya kurudi ulimwenguni tupate kuwa miongoni mwa wenye kuamini na kuokolewa.»

    [103] Hakika katika habari ya Ibrāhīm iliyotangulia kuna mazingatio kwa mwenye kuzingatia. Na wengi wenye kuisikia habari hii hawakuwa ni wenye kuamini

    [104] Na kwa hakika, Mola wako Ndiye Mshindi Aliye Muweza wa kuwalipiza wakanushaji, Ndiye Mwenye kuwarehemu waja Wake Waumini

    [105] Waliukanusha watu wa Nūḥ ujumbe wa Nabii wao. Wakawa, kwa kufanya hivyo, ni wakanushaji wa Mitume wote, kwa kuwa kila Mtume anaamrisha kuwaamini Mitume wote

    [106] Kumbuka pindi aliposema kuwaambia wao ndugu yao Nūḥ, «Je, hamumuogopi Mwenyezi Mungu kwa kuacha kumuabudu asiyekuwa Yeye

    [107] Mimi kwenu nyinyi ni Mtume muaminifu katika yale ninayowafikishia

    [108] Basi ifanyeni Imani kuwa ndio kinga yenu na adhabu ya Mwenyezi Mungu, na nitiini mimi katika yale ninayowaamrisha ya kumuabudu Yeye Peke Yake

    [109] na sitaki kutoka kwenu malipo yoyote ya kuufikisha ujumbe, malipo yangu hayako juu ya yoyote isipokuwa Mola wa viumbe wote, Mwenye kuendesha mambo ya viumbe Vyake

    [110] Basi jihadharini na mateso Yake na mnitii mimi kwa kufuata amri Zake na kujiepusha na makatazo Yake.»

    [111] Watu wake wakamwambia, «Vipi tutakuamini na tutakufuata na hali hao waliokufuata ni watu wanyonge na wale wa hali ya chini miongoni mwao?»

    [112] Nūḥ, amani imshukie, aliwajibu kwa kusema, «Sikupewa jukumu la kujua matendo yao. Jukumu nililopewa ni kuwalingania wao kwenye Imani. Na linalozingatiwa ni Imani, na sio cheo, ukoo, kazi na ujuzi wa sanaa

    [113] «Hesabu yao, ili walipwe kwa matendo yao na yaliyomo ndani ya nafsi zao, ni juu ya Mola wangu Anayeona na kujua siri zote. Lau mnatambua hilo hamngalisema maneno haya

    [114] «Na mimi si mwenye kuwafukuza wale wanaouamini ulinganizi wangu, namna itakavyokuwa hali yao, kwa kufuata matakwa yenu, ili mniamini

    [115] Mimi sikuwa isipokuwa ni mwonyaji ambaye onyo lake liko wazi.»

    [116] Hapo watu wa Nūḥ waliacha kubishana na wakaamua kutoa vitisho, hivyo basi wakamuambia, «Usiporudi nyuma, ewe Nūḥ, ukaacha huo ulinganizi wako, utakuwa ni miongoni mwa wenye kuuawa kwa kupigwa mawe.»

    [117] Nūḥ aliposikia neno lao hili, alimuomba Mola wake kwa kusema, «Mola wangu! Kwa hakika watu wangu wameamua kuendelea kunikanusha

    [118] basi amua baina yangu na wao uamuzi wa kumwangamiza mwenye kukataa kukupwekesha na akamkanusha Mtume wako. Na uniokoe mimi, na Waumini walio pamoja na mimi, na adhabu utakayowaadhibu makafiri.»

    [119] Basi tukamuokoa na wale walio pamoja na yeye katika jahazi iliyojazwa aina mbalimabali za viumbe alivyovibeba pamoja na yeye

    [120] Kisha tukawazamisha, baada ya kumuokoa Nūḥ na wale waliokuwa pamoja na yeye, wale waliosalia kati ya wale ambao hawakuamini na wakaukataa ushauri aliyowapa

    [121] Hakika katika maelezo ya Nūḥ na yale yaliyokuwa ya kuokolewa Waumini na kuangamizwa wakanushaji ni alama na ni zingatio kubwa kwa waliokuja baada yao. Na wengi wa wale waliokisikia kisa hiki hawakuwa ni wenye kumuamini Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na sheria Zake

    [122] Na kwa kweli Mola wako Ndiye Mshindi katika kuwatesa waliomkanusha na wakaenda kinyume na amri Yake, Mwenye rehema kwa waja Wake walioamini

    [123] Walimkanusha watu wa kabila la ‘Ād Mtume wao Hūd, amani imshukiye, na kwa hivyo wakawa ni wakanushaji wa Mitume wote, kwa kuwa ulinganizi wao ni mmoja katika misingi yake na malengo yake

    [124] Alipowaambia ndugu yao Hūd, «Je, hamumchi MwenyeziMungu mukamtakasia ibada

    [125] Mimi nimetumwa kwenu niwaongoze na niwaonyeshe njia, ni mtunzi wa ujumbe wa Mwenyezi Mungu, ninaufikisha kwenu kama Alivyoniamrisha Mola wangu

    [126] Basi iogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu na mnitii mimi katika kile ninachowaitia nyinyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu

    [127] na sitaki kutoka kwenu, kwa kuwaongoza nyinyi kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu, aina yoyote ya malipo. Malipo yangu hayako juu ya yoyote isipokuwa Mola wa viumbe wote

    [128] «Je mnajenga kila mahali palipoinuka jengo refu mkawa mnatazama kutoka hapo na mnawacheza shere wapita njia? Huo ni upuuzi na upitaji kiasi, na hauwaletei nyinyi faida yoyote katika dini au katika dunia

    [129] Na mnafanya majumba imara na ngome zilizojengwa madhubuti, kama kwamba nyinyi mtakaa milele duniani na hamtakufa

    [130] Na mnapomshika mtu kwa nguvu na mkamakinika kumuua au kumpiga, basi mnalifanya hilo kwa kutendesha nguvu hali ya kufanya maonevu

    [131] «Basi muogopeni Mwenyezi Mungu na mkifuate kile ninachowalingania, kwani hilo lina nafuu zaidi kwenu

    [132] na mcheni Mwenyezi Mungu Aliyewapa aina mbalimbali za neema zisizofichika kwenu

    [133] Amewapa wanyama hawa: ngamia ng’ombe, mbuzi na kondoo, na Amewapa watoto

    [134] na Amewapa mabustani yenye matunda, na Amewatolea maji kwenye chemchemi zinazopita

    [135] Hūd, amani imshukiye, akasema akiwatahadharisha wao, «Mimi ninaogopa , mkiendelea na yale mliyo nayo ya ukanushaji, uonevu na kuzikufuru neema, asije Mwenyezi Mungu Akawateremshia nyinyi adhabu katika Siku ambayo shida yake ni kubwa kwa kitisho cha adhabu yake

    [136] Wakamwambia, «Ni sawa kwetu kutukumbusha, kututisha na kuacha kufanya hivyo, hatutakuamini

    [137] Na wakasema, «Haikuwa dini hii tuliyonayo isipokuwa ni dini ya watu wa mwanzo na desturi zao

    [138] na sisi si wenye kuadhibiwa kwa tunalolifanya katika yale ambayo unatuonya nayo ya adhabu.»

    [139] Wakaendelea kumkanusha, na Mwenyezi Mungu Akawaangamiza kwa upepo wa baridi ulio mkali. Kwa hakika, katika kuangamiza huko kuna mazingatio kwa wanaokuja baada yao, na hawakuwa wengi wao, wale waliokisikia kisa chao, ni wenye kukuamini wewe

    [140] Hakika Mola wako Ndiye Mwenye nguvu, Mshindi kwa anayoyataka ya kuwaangamiza wakanushaji, Mwenye huruma kwa Waumini

    [141] Watu wa kabila la Thamūd waliukanusha ujumbe wa Mtume wao Ṣāliḥ na wakaukanusha mwito wake wa kumpwekesha Mwenyezi Mungu, na kwa hivyo wakawa wamewakanusha Mitume wote, kwa kuwa wao wote wanalingania kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu

    [142] Pindi alipowaambia wao ndugu yao Ṣāliḥ»Je, hamuogopi mateso ya Mwenyezi Mungu, mkampwekesha kwa ibada

    [143] Mimi nimetumilizwa kwenu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ni mwenye kuutunza ujumbe huu kama nilivyoupokea kutoka kwa Mwenyezi Mungu

    [144] Basi jihadharini na mateso Yake, Aliyetukuka, na fuateni kile nilichowalingania mkifuate

    [145] Na mimi sitaki malipo kwa kuwashauri na kuwaongoza, malipo yangu hayako isipokuwa kwa Mola wa viumbe wote

    [146] «Je, Awaache Mola wenu katika starehe mlizonazo, hali ya kuwa mumetulia katika dunia hii mkiwa mumesalimika na adhabu na kuondoka na kufa

    [147] Mkiwa kwenye mabustani yenye matunda, chemchemi zinazopita

    [148] nafaka nyingi na mitende ambayo matunda yake yamestawi, yamelainika na yameiva

    [149] na mnachonga kutoka kwa majabali majumba hali ya kuwa ni wamahiri wa kuyachonga, mkiwa na kiburi na majivuno.»

    [150] Basi ogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu na mkubali ushauri wangu

    [151] na msiandame amri ya wenye kuzidhulumu nafsi zao, waliokolea katika kumuasi Mwenyezi Mungu

    [152] waliozoea kufanya uharibifu kwenye ardhi, uharibifu usiotengenezeka

    [153] Watu wa Thamūd walimwambia Nabii wao Ṣāliḥ, «Wewe hukuwa isipokuwa ni miongoni mwa wale waliofanyiwa uganga wa uchawi mwingi, mpaka uchawi ukaathiri akili yako

    [154] Hukuwa wewe isipokuwa ni mmoja wa wanadamu unaofanana na sisi katika ubinadamu, basi vipi utakuwa tafauti na sisi kwa utume? Basi leta hoja wazi inayoonyesha kuwa utume wako umethibiti, iwapo wewe ni mkweli katika madai yako kwamba Mwenyezi Mungu Amekutumiliza kwetu.»

    [155] Ṣāliḥ akasema kuwaambia- na hapo alikuwa amewaletea ngamia ambaye Mwenyezi Mungu alimtolea kwenye jiwe-, «Huyu ni ngamia wa Mwenyezi Mungu. Yeye ana hisa ya maji siku maalumu, na nyinyi mna hisa ya maji kwa siku nyingine. Haifai kwenu nyinyi kunywa siku ile ambayo ni hisa yake, na yeye hatakunywa siku ambayo ni hisa yenu

    [156] Na msimguse kwa kitu chochote cha kumdhuru, kama kipigo au mauaji au mfano wake, kwani mkifanya hivyo, Mwenyezi Mungu Atawaangamiza nyinyi kwa adhabu ya Siku ambayo shida yake ni kubwa kwa sababu ya papatiko litakalotukia Siku hiyo na shida

    [157] Basi wakamchinja ngamia, wakawa ni wenye kujuta kwa walilolifanya walipokuwa na uhakika kuwa watashukiwa na adhabu, na majuto yao yasiwafae kitu

    [158] Basi adhabu ya Mwenyezi Mungu ikawashukia, ile ambayo Ṣāliḥ, amani imshukiye, aliwaahidi nayo, na ikawaangamiza. Kwa hakika, katika kuwaangamiza watu wa Thamūd pana mazingatio kwa mwenye kuuzingatia mwisho huu; na wengi wao hawakuwa ni wenye kuamini

    [159] Na kwa hakika Mola wako Ndiye Mshindi, Mwenye kutendesha nguvu, Mwenye kuwatesa maadui Wake, Mwenye huruma kwa walioamini miongoni mwa viumbe Wake

    [160] watu wa Lūṭ waliukanusha utume wake, wakawa kwa hilo ni wakanushaji wa Mitume waliosalia, kwa kuwa lile walilolileta la kumpwekesha Mwenyezi Mungu na misingi ya Sheria ni moja

    [161] Pindi ndugu yao Lūṭ alipowaambia, «Je, hamuogopi adhabu ya Mwenyezi Mungu

    [162] Mimi ni mjumbe kutoka kwa Mola wenu aliye muaminifu juu ya utekelezaji wa ujumbe Wake kwenu

    [163] Basi jihadharini na mateso ya Mwenyezi Mungu kwa kumkanusha kwenu mjumbe Wake, na nifuateni mimi katika yale ninayowalingania

    [164] Na siwaombi malipo yoyote juu ya ulinganizi wangu wa kuwaongoza, malipo yangu hayako isipokuwa kwa Mola wa viumbe wote

    [165] «Mnawaingilia binadamu wanaume

    [166] na mnawaacha wake zenu ambao Mwenyezi Mungu Amewaumbia nyinyi ili mstarehe na mzaane? Lakini nyinyi ni watu, kwa uasi huu, wenye kuyakiuka yale ambayo Mwenyezi Mungu Amewaruhusu ya halali na kuyaendea ya haramu.»

    [167] Watu wa Lūṭ wakasema, «Usipoacha, ewe Lūṭ, kutukataza kuwajia wanaume na kukichafua kitendo hicho (cha kuwajia wanaume), utakuwa ni miongoni mwa wenye kufukuzwa kutoka miji yetu.»

    [168] Lūṭ akasema kuwaambia wao, «Mimi ni miongoni mwa wale wanaokichukia sana kitendo chenu mnachokifanya cha kuwajia wanaume.»

    [169] Kisha Lūṭ akamuomba Mola wake, alipokata tamaa kuwa watamsikiliza, alisema, «Mola wangu! Niokoe mimi na uwaokoe jamaa zangu na kile wanachokifanya watu wangu cha uasi huu mchafu na (utuokoe na) adhabu yako itakayowapata.»

    [170] Basi tukamuokoa yeye na watu wa nyumbani kwake na wale wote walioukubali ulinganizi wake

    [171] isipokuwa mkongwe miongoni mwa watu wa nyumbani kwake, naye ni mke wake ambaye hakushirikiana na wao katika kuamini, hivyo basi akawa ni mwenye kusalia kwenye adhabu na maangamivu

    [172] Kisha tukawaangamiza wasiokuwa wao, miongoni mwa makafiri, kuwaangamiza kukubwa

    [173] na tukawateremshia wao mawe kutoka juu kama mvua yakawaangamiza. Ilikuwa mvua mbaya sana ya wale walioonywa na Mitume wao na wasiwakubalie. Kwa hakika, wao wameteremshiwa aina mabaya zaidi za maangamivu na uvunjaji

    [174] Kwa hakika, katika mateso hayo yaliyowateremkia watu wa Lūṭ pana mazingatio na mawaidha ya kuwafanya wenye kukanusha wawaidhike. Na wengi wao hawakuwa ni wenye kuamini

    [175] Na kwa kweli Mola wako Ndiye Mshindi Mwenye nguvu ya kuweza kuwashurutisha wakanushaji, Mwenye huruma kwa waja Wake wema

    [176] Walimkanusha watu wa nchi yenye miti iliyoshikana Mtume wao Shu’ayb kuhusu utume wake, na kwa hivyo waliukua wamekanusha jumbe zote za Mitume

    [177] Alipowaambia wao Shu’ayb, «Je, hamuogopi kuwa Mwenyezi Mungu Atawatesa kwa ushirikina wenu na kufanya kwenu matendo ya uasi

    [178] Mimi nimetumilizwa kwenu kutoka kwa Mwenyezi Mungu niwaongoe, ni mtunzi wa kile alichoniletea mimi Mwenyezi Mungu cha wahyi wa utume

    [179] Basi yaogopeni mateso ya Mwenyezi Mungu na mkifuate kile ninachowaitia cha uongofu wa Mwenyezi Mungu mupate kuongoka

    [180] Na sitaki kwenu, kwa kule kuwalingania kwangu kwenye kumuamini Mwenyezi Mungu, malipo yoyote. Malipo yangu hayako isipokuwa kwa Mola wa viumbe wote.”

    [181] Shu’ayb akaendelea kuwaambia- na walikuwa wakipunguza vipimo na mizani-, «Watimizieni watu vipimo kwa kuwakamilishia, na msiwe ni kati ya wale wanaowapunja watu haki zao

    [182] na mpime kwa mizani ya uadilifu iliyolingana sawa

    [183] na msiwapunje watu chochote katika haki zao kwenye vipimo au mizani au vinginevyo, na msizidishe uharibifu katika ardhi kwa kufanya ushirikina, kuua, kunyang’anya, kuwatisha watu na kutekeleza vitendo vya uasi

    [184] «Na jihadharini na mateso ya Mwenyezi Mungu Aliyewaumba na Akawaumba watu wa mataifa yaliyowatangulia.»

    [185] Wakasema, «Ukweli ni kwamba wewe, ewe Shu’ayb, ni miongoni mwa wale waliopatwa na uchawi ukawashika sana ukawaondoa akili zao

    [186] Na wewe hukuwa isipokuwa ni mfano wetu sisi katika ubinadamu, basi vipi utahusika peke yako kwa utume bila ya sisi? Na kwa kweli, dhana yetu kubwa kuhusu wewe ni kuwa wewe ni miongoni mwa warongo katika kile unachokidai cha utume

    [187] Iwapo wewe ni mkweli katika madai yako ya utume, basi muombe Mwenyezi Mungu Atuangushie vipande vya adhabu kutoka mbinguni vitumalize.»

    [188] Shu’ayb akawaambia wao, «Mola wangu Anayajua zaidi yale mnayoyafanya ya ushirikina na uasi na mateso mnayostahili.»

    [189] Wakaendelea kumkanusha, likawapata wao joto kali, wakawa wanatafuta mahali pa hifadhi ili wajifinike. Kikawafinika kiwingu, kikawapatia ubaridi na upepo laini, na walipokusanyika chini yake, moto uliwawakia na ukawachoma, basi hapo yakawa maangamivu yao wote katika siku yenye kitisho kikali

    [190] Hakika katika mateso hayo yaliyowashukia kuna ushahidi wazi juu ya uweza wa Mwenyezi Mungu katika kuwapatiliza wakanushaji kwa adhabu na kuna mazingatio kwa mwenye kuzingatia. Na hawakuwa wengi wao ni wenye kuamini na kuwaidhika kwa hayo

    [191] Na kwa hakika, Mola wako, ewe Mtume, Ndiye Yeye Aliye Mshindi katika kuwatesa Kwake wale Anaowatesa miongoni mwa maadui Wake, Ndiye Anayewarehemu waja Wake wanaompwekesha

    [192] Na kwa hakika, hii Qur’ani ambayo ndani yake zimetajwa habari hizi za kweli imeteremshwa na Muumba viumbe na Mmiliki wa mambo yote

    [193] Jibrili muaminifu ameshuka nayo

    [194] akakusomea mpaka ukaikusanya moyoni mwako, kwa kuihifadhi na kuielewa, upate kuwa ni mmoja wa wajumbe wa Mwenyezi Mungu wenye kuwafanya watu wao waogope mateso ya Mwenyezi Mungu, upate kuwaonya, kwa Teremsho hili, binadamu na majini wote

    [195] Ameshuka nayo Jibrili kwako kwa lugha ya Kiarabu yenye maana yaliyo wazi, yenye ushahidi unaoonekena, ikikusanya kile wanachokihitajia cha kutengeneza mambo ya Dini yao na dunia yao

    [196] Na kwa hakika, utajo wa hii Qur’ani umethibitishwa katika Vitabu vya Manabii waliotangulia, vimeibashiri na kukubali kuwa ni ya kweli

    [197] Je, haiwatoshi hawa kuwa ni ushahidi kwamba wewe ni mtume wa Mwenyezi Mungu na kwamba Qur’ani ni kweli kuwa wasomi wa Wana wa Isrāīl wana ujuzi wa usahihi wa hilo na wale walioamini miongoni mwao kama ‘Abdullāh bin Sallām

    [198] Na lau tungaliiteremsha Qur’ani kwa baadhi ya wale wasiozungumza lugha ya Kiarabu

    [199] wakawasomea makafiri wa Kikureshi kisomo cha Kiarabu kilicho sawa, wangaliikanusha pia na wangalizua sababu ya ukanushaji wao

    [200] Hivyo ndivyo tulivyotia ndani ya nyoyo za wahalifu kuikanusha Qur’ani na hilo likawa limejikita ndani ya hizo nyoyo

    [201] na hii ikawa ni sababu ya udhalimu wao na uhalifu wao. Basi hapana njia ya wao kubadilika kwa kuyaacha waliyonayo ya kuikanusha Qur’ani mpaka waishuhudie adhabu kali walioahidiwa

    [202] Hapo adhabu iwashukie ghafla na hali wao hawajui kuja kwake kabla ya hapo

    [203] na hapo waseme, watakaposhtushwa nayo, kwa majuto ya Imani iliyotupita tukaikosa, «Je, sisi ni wenye kupatiwa nafasi na kucheleweshwa tupate kutubia kwa Mwenyezi Mungu ushirikina wetu na tuyapatilize yaliyotupita?»

    [204] Je, hawa wamedanganyika na kule kuwapa muhula kwangu ndipo wakawa wanataka kuteremka adhabu kwa haraka juu yao kutoka mbinguni

    [205] Je, umejua, ewe Mtume, lau tungaliwastarehesha kwa uhai wa miaka mingi kwa kuwacheleweshea muda wao wa kuishi

    [206] kisha iwashukie adhabu ilioahidiwa

    [207] Hakutawafaa kitu kule kustarehe kwao kwa umri mrefu na maisha mazuri wasipotubia kutokana na ushirikina wao. Basi adhabu ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuwashukia hivi karibuni (ulimwenguni) au baadaye (huko Akhera)

    [208] Na hatukuuangamiza mji wowote, miongoni mwa miji katika mataifa yote, isipokuwa baada ya kuwatumiliza Mitume kwao wawaonye

    [209] ili wawe ni makumbusho kwao na uzindushi wa yale yenye uokofu kwao. Na hatukuwa ni wenye kudhulumu kwa kuwaadhibu watu kabla ya kuwapelekea Mtume

    [210] Na Qur’ani hawakuiteremsha mashetani kwa Muhammad, kama wanavyodai makafiri

    [211] na hilo halifai kutoka kwao na wala hawaliwezi

    [212] kwa kuwa wao ni wenye kuzuiliwa kuisikiliza Qur’ani kutoka mbinguni, ni wenye kupigwa na vimondo

    [213] Hivyo basi usiabudu, pamoja na Mwenyezi Mungu, muabudiwa yoyote asiyekuwa Yeye, ufanyapo hivyo utateremkiwa na adhabu ile iliyowashukia hawa walioabudu, pamoja na Mwenyezi Mungu, asiyekuwa Yeye

    [214] Na watahadharishe, ewe Muhammad, watu wako wa karibu, ukianzia na wale walio karibu na wewe zaidi, isije adhabu yetu ikawashukia

    [215] Na uwe laini wa mwenendo na maneno, kwa unyenyekevu na huruma, kwa yule ambaye imekufunukia kutoka kwake kuitika mwito wako

    [216] Basi wakienda kinyume na amri yako na wasikufuate, jiepushe na vitendo vyao na yale waliyonayo ya ushirikina na upotevu

    [217] Na Umuachie jambo lako Mwenyezi Mungu, Aliye Mshindi Ambaye hakuna wa kushindana na Yeye wala wa kumlazimisha, Mwenye kurehemu Ambaye Hawaachi wenye kumtegemea

    [218] Na Ambaye Anakuona unaposimama kuswali ukiwa peke yako ndani ya usiku

    [219] Na Anaona vile unavyogeuka, pamoja na wenye kumsujudia katika Swala zao wakiwa na wewe, ukiwa katika hali ya kusimama, kurukuu na kusujudu na kuketi

    [220] Hakika Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Anayesikia kusoma kwako na kumtaja kwako, Ndiye Anayejua nia yako na matendo yako

    [221] Je, niwapashe habari, enyi watu, ni nani ambaye mashetani wanamshukia

    [222] Wanamshukia kila mwingi wa urongo, mwingi wa madhambi miongoni mwa makuhani

    [223] Mashetani wanasikiliza kwa kuiba, wanayanyakuwa maneno kutoka sehemu za juu wakawatupia makuhani na wale wanaokuwa na mwenendo wao miongoni mwa watu wenye matendo mabaya. Na wengi wa hawa ni warongo, kwani mmoja wao husema kweli katika neno moja na akaongeza juu yake maneno mia moja ya urongo

    [224] Na washairi, mashairi yao yanasimama juu ya ubatilifu na urongo, na wanafuatana na wao wapotevu waliopotoka kama wao

    [225] Kwani huoni, ewe Nabii, kwamba wao wanaenda kama mtu aliyekosa mwelekeo, wanavama ndani ya kila aina ya fani za urongo, uzushi, uvunjaji heshima, kutukana nasaba na kuwataja vibaya wanawake waliojihifadhi

    [226] na kwamba wao wanayasema wasiyoyatenda, wanapita mipaka katika kuwasifu watu wa ubatilifu na wanawatia kasoro watu wa haki

    [227] Mwenyezi Mungu amewavua, kati ya hao washairi, wale washairi walioongoka kwa kuamini na kufanya matendo mema, na wakamtaja Mwenyezi Mungu kwa wingi, wakatunga mashairi juu ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, na kumsifu Yeye, Mwenye utajo mtukufu, na kumtetea Mtume Wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wakasema maneno ya busara yenye mawaidha na adabu nzuri, na wakaunusuru Uislamu wakawa wanamtukana anayeutukana au anayemtukana Mtume wake kwa kuwarudi washairi makafiri. Na watajua wale waliozidhulumu nafsi zao kwa ushirikina na matendo ya uasi, wakawadhulumu wasiokuwa wao kwa kuwanyima haki zao au kuwafanyia uadui au tuhuma za urongo, ni marejeo gani ya shari na maangamivu watakayorejea. Kwa kweli, hayo ni mageuko mabaya. Tunamuomba Mwenyezi Mungu salama na afya

    Chumvi

    Surah 27

    [1] «Tā Sīn» Yametangulia maelezo kuhusu herufi zilizokatwa na kutengwa katika mwanzo wa sura ya Al-Baqarah. Hizi ni aya za Qur’ani, nazo ni aya za Kitabu kitukufu zenye maana yaliyofunuka wazi zenye ushahidi waziwazi wa kuonyesha elimu zilizomo, hekima na Sheria

    [2] Nazo ni aya zenye kuongoza kwenye njia ya kufuzu duniani na Akhera, na zinatoa bishara ya malipo mazuri kwa Waumini walioziamini na wakaongoka kwa uongofu wake

    [3] Ambao wanasimamisha Swala tano zilizotimia nguzo, zilizokamilika masharti, na wanatekeleza Zaka za lazima kwa wanaostahiki kupewa, na wao wanaamini kwa yakini maisha ya Akhera na yaliyomo ndani yake ya malipo mema na mateso

    [4] Hakika ya wale wasioamini nyumba ya Akhera na hawafanyi matendo ya kuwafaa huko, tutawapambia wao matendo yao mabaya wayaone ni mazuri, na wao watakuwa wakizunguka kwenye matendo hayo wakiwa wameduwaa

    [5] Hao ndio watakaopata adhabu mbaya duniani, kwa kuuawa, kutekwa, kudhalilika na kushindwa. Na wao huko Akhera watakuwa ni wenye hasara kubwa zaidi

    [6] Na kwa hakika wewe , ewe Mtume, unapewa Qur’ani kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwingi wa hekima katika kuumba Kwake na upelekeshaji Wake Ambaye Amekizunguka kila kitu kwa kukijua

    [7] Taja habari ya Mūsā aliposema kuwaambia watu wa nyumbani kwake katika safari yake kutoka Madyan kwenda Misri, «Mimi nimeuona moto. Nitawajia kutoka huko na habari ya kutuonyesha njia, au nitawajia na kinga cha moto mupate mvuke wake mjihami na baridi

    [8] Mūsā alipoujia moto, Mola wake Alimwita na akampa habari kwamba hapa ni mahali Alipopatakasa Mwenyezi Mungu na Akapabariki na Akapafanya ni mahali pa kusema na Mūsā na kumtumiliza, na kwamba Mwenyezi Mungu Amewabariki waliopo motoni na waliopo pambizoni mwake miongoni mwa Malaika, na kumtakasa Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe, kwa kumuepusha na sifa zisizonasibiana na Yeye

    [9] «Ewe Mūsā! Hakika yangu mimi ni Mwenyezi Mungu ninayestahiki kuabudiwa peke yangu, ni Mshindi Mwenye nguvu wa kuwaadhibu maadui zangu, niliye na hekima katika upelekeshaji wa viumbe vyangu

    [10] Na itupe fimbo yako!» Akaitupa ikawa nyoka. Alipoiona inatikisika kwa ulaini kama vile nyoka mwepesi anavyojitikisa, alizunguka kukimbia na asiirudie. Hapo Mwenyezi Mungu Akamtuliza kwa neno Lake, «Ewe Mūsā! Usiogope. Hakika mimi hawaogopi mbele yangu wale niliowatuma na ujumbe wangu

    [11] Isipokuwa yule aliyepitisha mpaka kwa kufanya dhambi kisha akatubia, akabadilisha toba njema baada ya dhambi baya, kwani mimi ni mwenye kumsamehe ni mwenye kumrehemu.» Basi asikate tamaa mtu yoyote na rehema ya Mwenyezi Mungu na msamaha Wake

    [12] «Na utie mkono wako kwenye uwazi wa kanzu yako uliofunuliwa kifuani, utatoka ukiwa mweupe kama barafu, bila ya kuwa na mbalanga, ikiwa ni moja ya miujiza tisa, nayo, pamoja na huo mkono, ni fimbo, miaka ya ukame, upungufu wa matunda, mafuriko, nzige, chawa, vyura na damu, ili kukupa nguvu wewe katika ujumbe wako utakaoupeleka kwa Fir’awn na watu wake. Hakika wao walikuwa ni watu waliotoka nje ya amri ya Mwenyezi Mungu na kumkanusha.»

    [13] Miujiza hii ilipowajia, hali ya kuwa imefunuka wazi, inamfanya mwenye kuitazama auone uhakika wa yale inayoyatolea ushahidi, walisema, «Huu ni uchawi uliofunuka waziwazi.»

    [14] Na waliikanusha, Fir’awn na watu wake, miujiza tisa yenye kuonyesha wazi ukweli wa Mūsā katika unabii wake na ukweli wa ulinganizi wake, na walikanusha kwa ndimi zao kuwa inatoka kwa Mwenyezi Mungu, na hali wana yakini nayo ndani ya nyoyo zao, kwa kuifanyia uadui haki na kuwa na kiburi cha kutoikubali. Basi angalia , ewe Mtume, ulikuwa vipi mwisho wa wale waliozikanusha aya za Mwenyezi Mungu na wakafanya uharibifu kwenye ardhi? Mwenyezi Mungu aliwazamisha baharini. Na katika hilo kuna mazingatio kwa anayezingatia

    [15] Na kwa kweli, tulimpa Dāwūd na Sulaymān elimu wakaitumikia na wakasema, ‘Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu Aliyetufanya bora kuliko wengi miongoni mwa waja Wake Waumini. Katika hii aya kuna dalili ya utukufu wa elimu na daraja ya juu ya wenye elimu

    [16] Na Sulaymān alimrithi baba yake Dāwūd unabii na elimu. Na alisema Sulaymān kuwaambia watu wake, «Enyi watu! Tumefundishwa na kufahamishwa maneno ya ndege, na tumepewa kila kitu kinachohitajika. Kwa hakika, huu ambao Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Ametupa ndio wema ulio waziwazi ambao Anatufadhilisha nao juu ya wasiokuwa sisi

    [17] Na akakusanyiwa Sulaymān askari wake miongoni mwa majini, binadamu na ndege katika matembezi yao. Na wao, pamoja na wingi wao, hawakua wamepuuzwa, bali palikuwa, juu ya kila jinsi, mwenye kuwasimamia wa mwanzo wao kwa wa mwisho wao ili wasimame wote wakiwa wamejipanga

    [18] Mpaka walipofika kwenye bonde la chungu, alisema chungu mmoja «Enyi chungu! Ingieni kwenye makazi yenu ili Sulaymān na askari wake wasije wakawaua na hali wao hawajui hilo.»

    [19] Akatabasamu akicheka kwa neno la huyu chungu, kwa kufahamu kwake na kuwa na akili ya kuwaonya chungu, na akatambua neema ya Mwenyezi Mungu juu yake. Hapo akaelekea Kwake akiomba, «Mola wangu! Nipe muelekeo na uniafikie nishukuru neema zako ulizonineemesha mimi na wazazi wangu wawili, na nifanye matendo mema ambayo wewe utaridhika nayo kutoka kwangu na unitie, kwa rehema zako, ndani ya starehe ya Pepo yako pamoja na waja wako wema ambao uliridhika na matendo yao

    [20] Na akakagua Sulaymān hali ya ndege waliofanywa watiifu kwake na hali ya wale wasiokuweko miongoni mwao, na kulikuwa hapo kwake kuna ndege anayetambulikana na kujulikana aina ya hud-hud asimpate hapo. Akasema, «Kwa nini mimi simuoni yule hud-hud nimjuwae? Je, kuna kitu kilichomfanya afichike nisimuone? Au huyu ni miongoni mwa wale ambao hawapo hapa kwangu, ndio nisimuone kwa kuwa hayupo?» Ilipofunuka wazi kuwa hayupo

    [21] alisema, «Nitamuadhibu hud-hud huyu adhabu kali kwa kumtia adabu ya kutokuweko kwake, au nitamtesa kwa kumchinja kwa kitendo alichokifanya kwa kuwa aliharibu nidhamu aliyowekewa aifuate, au ni lazima anijie na hoja iliyo wazi ya sababu ya kughibu kwake

    [22] Akakaa hud-hud muda usio mrefu kisha akahudhuria, na Sulaymān akamlaumu juu ya kughibu kwake na kutokuwako kwake. Hud-hud akamwambia, «Nimejua jambo usilolijuwa kikamilifu, na nimekujia kutoka mji wa Saba’ na habari ya jambo muhimu sana, na mimi nina yakina nalo

    [23] «Mimi nimemkuta mwanamke anawatawala watu wa Saba ’, na amepatiwa kila kitu katika mahitaji ya utawala wa kidunia, na ana kitanda cha heshima kubwa anakalia juu yake kuendesha mambo ya ufalme wake

    [24] «Nimemkuta Yeye na watu wake wanaabudu jua, wakiacha kumuabudu Mwenyezi Mungu. Na Shetani Amewapambia matendo yao mabaya waliokuwa wakiyafanya, akawaepusha na kumuamini Mwenyezi Mungu na kumpwekesha, hivyo basi wao hawaongoki kuelekea kwa Mwenyezi Mungu, kumpwekesha na kumuabudu Peke Yake.»

    [25] Shetani amewapambia hilo, ili wasimsujudie Mwenyezi Mungu Ambaye Anakitoa kilichofichwa na kufinikwa mbinguni na ardhini miongoni mwa mvua, mimea na visivyokuwa hivyo, na Anayajua mnayoyafanya kwa siri na mnayoyafanya kwa dhahiri

    [26] Mwenyezi Mungu, Ambaye hakuna muabudiwa anayestahiki ibada isipokuwa Yeye, ni Mola wa ‘Arsh iliyo kubwa ambayo ni kubwa kuliko viumbe vyote

    [27] Sulaymān alisema kumwambia hud-hud, «Tutaichunguza habari uliyotuletea tujue: unasema kweli katika hiyo au umekuwa ni katika warongo ndani yake

    [28] Enda na barua yangu hii kwa watu wa Saba’ uwapatie, kisha jiepushe kando na wao ukiwa karibu nao mahali unapoweza kusikia maneno yao na uyatie akilini maneno yatakayopitika baina yao.»

    [29] Hud-hud alienda akamrushia malkia ile barua. Papo hapo akaisoma na akawakasunya watukufu wa watu wake, na akamsikia akisema, «Mimi nimefikiwa na barua tukufu yenye cheo kutoka kwa mtu mkubwa wa cheo.»

    [30] Kisha akayaeleza yaliyomo ndani akasema, «Hiyo inatoka kwa Sulaymān, nayo imeanza na ‘Bi ism Allāh al-Rahmān al-Rahīm» (Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwenye kuwarehemu wema na waovu ulimwenguni, Mwenye kuwarehemu wema watupu kesho Akhera)

    [31] Msifanye kiburi wala msijifanye wakubwa mkakataa kuyakubali haya ninayowalingania. Na njooni kwangu mkiwa ni wenye kukubali upweke wa Mwenyezi Mungu na kujisalimisha Kwake kwa utiifu.»

    [32] Akasema, «Enyi watukufu! Nipeni shauri kuhusu jambo hili. Sikuwa mimi ni mwenye kuamua jambo isipokuwa mbele yenu na kwa ushauri wenu.»

    [33] Wakasema kumjibu ,»Sisi ni wenye nguvu wa idadi na silaha, na ni watu wa utetezi na ushujaa katika vita vikali, na uamuzi ni wako, na wewe ndiye mwenye maoni, basi fikiria unatuamrisha nini. Sisi ni wenye kusikiliza maneno yako na ni watiifu kwako.»

    [34] Akasema akiwatahadharisha kukabiliana na Sulaymān kwa uadui na akiwaelezea mwisho mbaya wa kupigana, «Kwa hakika, wafalme wakiingia na majeshi yao kwenye mji kwa nguvu na ushindi, wanauharibu, wanawafanya watukufu wake kuwa wanyonge, wanauwa na wanachukua mateka. Na hii ndiyo desturi yao inayoendelea na inayojikita ili kuwafanya watu wawaogope

    [35] Na mimi nitamtumia Sulaymān tunu iliyokusanya mali ya thamani ili kufanya urafiki naye kwayo, na nitangojea watarudi na nini hao wajumbe.»

    [36] Mjumbe wa malkia alipokuja na tunu kwa Sulaymān, alisema Sulaymān, akilikataa hilo na akizungumzia neema za Mwenyezi Mungu juu yake, «Mnanipatia mali ili kuniridhisha? Yale aliyonipa Mwenyezi Mungu ya unabii, ufalme na mali mengi ni mazuri zaidi na ni bora zaidi kuliko hayo Aliyowapa nyinyi, bali nyinyi ndio mnaofurahia tunu mnayotunukiwa, kwa kuwa nyinyi ni watu wa kuonyeshana kwa kujifahiri na dunia na kuipapia kwa wingi.»

    [37] Na Sulaymān, amani imshukiye, akasema kumwambia mjumbe wa watu wa Saba’, «Rejea kwao, kwani naapa kwa Mwenyezi Mungu, tutawajia wao na askari wasioweza kupambana nao na kukabiliana nao, na tutawatoa kutoka nchini mwao wakiwa wadhalilifu, hali ya kuwa wanyonge wenye kudharauliwa, iwapo hawatafuata Dini ya Mwenyezi Mungu Peke Yake na hawataacha kumuabudu asiyekuwa Yeye.»

    [38] Sulaymān akasema akiwahutubia wale ambao Mwenyezi Mungu Amemdhalilishia miongoni mwa majini na binadamu, «Ni nani kati yenu ataniletea kitanda cha ufalme wake kabla hawajanijia wakiwa katika hali ya kufuata na kutii?»

    [39] Akasema afriti wa kijini mwenye nguvu na ukali, «Mimi nitakuletea kabla hujainuka kutoka kwenye kikao chako hiki unachokaa kuhukumu baina ya watu. Na mimi ni mwenye nguvu na uwezo wa kukibeba, ni muaminifu wa kuvitunza vilivyomo ndani yake, nitakuja nacho kama kilivyo, sikipunguzi kitu chake chochote wala sikigeuzi.»

    [40] Akasema yule ambaye alikuwa na ujuzi kutoka kwenye Kitabu, «Mimi nitakuletea hiko kitanda kabla ya kupepesa macho yako yanapogeuka kuangalia kitu.» Sulaymān akamruhusu, naye akamuomba Mwenyezi Mungu na akakileta kitanda cha kifalme. Alipokiona Sulaymān kimehudhurishwa mbele yake na kimethibiti alisema, «Huu ni miongoni mwa wema wa Mola wangu Aliyeniumba na akaumba ulimwengu wote ili kunitahini mimi nitalishukuru hilo kwa kutambua neema Yake Aliyetukuka au nitakufuru kwa kuacha kushukuru? Na mwenye kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema Zake, nafuu ya hilo itamrudia yeye mwenyewe, na mwenye kukanusha neema na akaacha kushukuru, basi hakika Mola wangu Ametosheka Hahitajii shukrani yake, ni Karimu ambaye kheri Yake inamuenea hapa duniani mwenye kushukuru na mwenye kukufuru, kisha Atawahesabu huko Akhera na awalipe

    [41] Sulaymān akasema kuwaambia walioko mbele yake, «Kibadilisheni kitanda cha ufalme wake ambacho anakaa juu yake kwa namna ya yeye kutokitambua akikiona, tuone: ataelekezeka kukijua au atakuwa ni kati ya wale wasioelekezeka?»

    [42] Alipokuja malkia wa Saba ’.kwa Sulaymān kwenye kikao chake aliambiwa, «je, kitanda cha ufalme wako kiko hivi?» Akasema, «Hicho kinafanana nacho.» Ikambainikia Sulaymān kuwa amejibu jawabu la sawa na ameshajua uweza wa Mwenyezi Mungu na usahihi wa unabii wa Sulaymān , amani imshukiye. Na tulipewa elimu ya kumjua Mwenyezi Mungu na kujuwa uweza Wake kabla yake yeye, na tulikuwa ni wenye kuifuata amri ya Mwenyezi Mungu ni wenye kuifuata dini ya Uislamu.»

    [43] Na kilimzuia yeye kumuabudu Mwenyezi Mungu Peke Yake kile alichokuwa akikiabudu badala ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka,. Kwa hakika yeye alikuwa ni kafiri na alikulia kati ya watu makafiri na akaendelea kwenye dini yao, isipokuwa hivyo, yeye ana werevu na busara ya kuijua haki na kuipambanua na batili, lakini itikadi za ubatilifu zinaondoa nuru ya moyo

    [44] Akaambiwa, «Ingia kwenye jumba.» na ukumbi wake ulikuwa wa ukoa, chini yake palikuwa na maji. Alipouona ukumbi alidhania ni maji yanayopiga mawimbi, na akafunua miguu yake ili kuingia majini. Sulaymān akamwambia, «Huo ni ukumbi laini wa ukoa ulio safi na maji yako chini yake.» Akatambua ukubwa wa ufalme wa Sulaymān na akasema, «Mola wangu! Nimeidhulumu nafsi yangu kwa ushirikina niliokuwa nao, na nimesalimu amri kwa kumfuata Sulaymān kwa kuingia kwenye dini ya Mola wa viumbe wote.»

    [45] Hakika tulimtumiliza kwa watu wa Thamūd ndugu yao Ṣāliḥ kwamba: Mpwekesheni Mwenyezi Mungu na musimchukue mungu mwingine mukamuabudu pamoja na Yeye. Alipowajia Ṣāliḥ kuwalingania kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumuabudu Peke Yake, watu wake walikuwa mapote mawili: mojawapo ya mapote mawili lilimuamini na lingine liliukanusha ulinganizi wake, kila mmoja kati ya watu wa mapote hayo mawili alikuwa akidai kwamba haki iko pamoja na yeye

    [46] Ṣāliḥ alisema kuliambia pote lililokanusha, «Kwa nini mnaharakisha ukanushaji na kufanya matendo mabaya ambayo yatawaletea adhabu na mnachelewesha kuamini na kufanya matendo mema ambayo yatawaletea malipo mazuri? Si mutake msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu mwanzo na mtubie kwake kwa matumaini ya kurehemewa.»

    [47] Wakasema watu wa Ṣāliḥ kumwambia, «Tumepata ukorofi kwa sababu yako wewe na watu walioko na wewe kati ya wale walioingia katika dini yako.» Ṣāliḥ aliwaambia, «Wema Anaowapatia Mwenyezi Mungu au uovu, basi hua umekadiriwa kwenu na Mwenyezi Mungu na Atawapa malipo yake. Bali nyinyi ni watu ambao mtapewa mtihani wa mambo ya furaha na maudhiko na mema na maovu

    [48] Na katika mji wa Ṣāliḥ, nao ni mji wa Ḥijr, ulioko Kaskazini magharibi ya bara Arabu, kulikuwa na wanaume tisa, shughuli yao ni kufanya uharibifu katika ardhi usiochanganyika na wema wowote wa kutengeneza

    [49] Watu tisa hawa wakaambiana wao kwa wao, «Apianeni kwa Mwenyezi Mungu, kila mmoja awaapie wengine:’Tunaapa tutamjia Ṣāliḥ kwa ghafla, kipindi cha usiku, tumuue yeye na tuwaue watu wake kisha tutamuambia atakayesimama kutaka kisasi cha damu yake miongoni mwa jamaa zake: ‘Hatukushuhudia kuuawa kwao.’ Na sisi tutakuwa ni wakweli kwa tuliyoyasema.»

    [50] Basi wakazipanga hila hizi za kumuangamiza Ṣāliḥ na watu wake kwa kuwafanyia vitimbi, tukamuokoa Nabii wetu Ṣāliḥ, amani imshukie, na tukawapatiliza kwa mateso kwa ghafla na hali wao hawatazamii vitimbi vyetu kwao kama malipo ya vitimbi vyao

    [51] Basi tazama , ewe Mtume, mtazamo wa mazingatio, mwisho wa njama za ukatili za kundi hili kumfanyia Nabii wao Ṣāliḥ. Sisi tuliwaangamiza wao na watu wao wote

    [52] Hayo ni makazi yao, yako matupu, hakuna yoyote ndani yake. Mwenyezi Mungu Amewaangamiza kwa sababu ya wao kuzidhulumu nafsi zao kwa ushirikina na kumkanusha Nabii wao. Kwa kweli, katika uvunjaji huo na uangamizaji pana mawaidha kwa watu wanaokijua kile tulichowafanya. Na huu ndio mwendo wetu kwa wenye kuwakanusha Mitume

    [53] Na tukamuokoa, na yale maangamivu yaliyowafika kina Thamūd, Ṣāliḥ na waliomuamini waliokuwa wakijikinga, kwa Imani yao, na adhabu ya Mwenyezi Mungu

    [54] Na mkumbuke na umtaje Lūṭ, aliposema kuwaambia watu wake, «Hivi nyinyi mnaleta kitendo ambacho ni upeo wa ubaya, nanyi mnajua ubaya wake

    [55] Hivi nyinyi mnawajia wanaume kwenye tupu zao za nyuma kwa matamanio badala ya wanawake? Bali nyinyi ni watu msiojua haki ya Mwenyezi Mungu juu yenu, ndipo mkaenda kinyume na amri Yake na mkamuasi Mtume Wake kwa kitendo chenu kibaya ambacho hakuwatangulia nacho yoyote katika viumbe.»

    [56] Watu wa Lūṭ hawakuwa na jawabu la kumpa isipokuwa ni kuambiana wao kwa wao, «Watoeni wafuasi wa Lūṭ kwenye mji wenu, kwani wao ni watu wanaojiepusha na kuwajilia wanaume.» Waliwaambia hilo kwa njia ya kuwafanyia shere

    [57] Tukamuokoa Lūṭ na watu wake waliomfuata na adhabu ambayo itawashukia watu wa Lūṭ waliomkanusha, isipokuwa mkewe tuliomkadria kuwa ni mwenye kusalia kwenye adhabu mpaka aangamie pamoja na wenye kuangamia, kwa kuwa yeye alikuwa ni msaidizi wa watu wake kwa matendo yao mabaya na alikua akiridhika nayo

    [58] Na tukawateremshia kutoka mbinguni mvua ya mawe ya udongo yenye kuangamiza. Ilikuwa mbaya mno mvua ya hao walioonywa ambao hoja iliwasimamia

    [59] Sema, ewe Mtume, «Sifa njema na shukrani ni za Mewenyezi Mungu, na amani kutoka Kwake na usalama ziwashukie waja Wake Aliowateua kwa kuwapa utume.» Kisha waulize washirikina wa watu wako, «Je, Mwenyezi Mungu Anayemiliki kunufaisha na kudhuru ni bora au ni yule wanayemshirikisha badala Yake kati ya wale wasiojimilikia wenyewe wala kuwamilikia wengine nafuu yoyote wala madhara yoyote?»

    [60] Na waulize wao , «Ni nani aliyeumba mbingu na ardhi na Akawateremshia maji kutoka mbinguni, Akaotesha kwa hayo maji mabustani yenye mandhari mazuri?» Hamkuwa nyinyi ni wenye kuipanda miti yake lau si Mwenyezi Mungu kuwateremshia maji kutoka mbinguni. Kumuabudu Mwenyezi Mungu ndio ukweli na kumuabudu asiyekuwa Yeye ndio urongo. Je, kuna muabidiwa pamoja na Mwenyezi Mungu alifanya vitendo hivi mpaka aabudiwe pamoja na Yeye na ashirikishwe na Yeye? Bali washirikina hawa ni watu wanapotoka na njia ya haki na Imani ndio wakamfanya Mwenyezi Mungu ni sawa na asiyekuwa Yeye katika kuabudiwa na kutukuzwa

    [61] Je, kuviabudu vile mnavyovishirikisha na Mola wenu ni bora au Yule Aliyewafanyia ardhi kuwa ni mahali pa kutulia, Akaitoa mito kati yake, Akaiwekea majabali yaliyojikita na Akaweka kizuizi baina ya bahari mbili, ya tamu na chumvi, ili mojawapo isiiharibu nyingine? Je kuna muabudiwa yoyote pamoja na Mwenyezi Mungu alifanya hilo hata mumshirikishe na Yeye katika kuabudu kwenu? Bali wengi wa hawa washirikina hawajui kadiri ya ukubwa wa Mwenyezi Mungu, hivyo basi wanamshirikisha Yeye kwa kuiga na kwa udhalimu

    [62] Je, kuviabudu vile mnavyovishirikisha na Mwenyezi Mungu ni bora au Yule Anayemjibu mwenye shida anapomuomba, Anayemuondolea maovu yaliyomshukia na Anayewafanya nyinyi ni wenye kushikilia nafasi za waliowatangulia nyinyi katika ardhi? Je, kuna muabudiwa yoyote pamoja na Yeye Anayewaneemesha neema hizi? Ni uchache sana kwenu nyinyi kukumbuka na kuzingatia, na kwa hivyo, mlimshirikisha Mwenyezi Mungu na mwingine katika kumuabudu

    [63] Je, kuviabudu vile mnavyomshirikisha navyo Mwenyezi Mungu ni bora au Yule Anayewaongoza katika giza la bara na bahari mnapopotea na njia ikawa na giza kwenu, Ambaye Anapeleka upepo wenye kutoa bishara njema ya kile ambacho Mwenyezi Mungu Anawarehemu waja Wake kwacho, nacho ni mvua yenye kuhuisha ardhi iliyokufa? Je, kuna muabudiwa yoyote pamoja na Mwenyezi Mungu anayewafanyia chochote katika hayo mkamuomba badala yake? Ameepukana Mwenyezi Mungu na kutakasika na hivyo ambavyo wao wanamshirikisha navyo asiyekuwa Yeye

    [64] Na waulize wao: Ni nani anayeanzisha kuumba viumbe, kisha anaviondosha akitaka, kisha anavirudisha? Na ni nani anayewaruzuku nyinyi kutoka mbinguni kwa kuiteremsha mvua? Na ni nani anayehuisha ardhi kwa kuotesha mimea na vinginevyo? Je, kuna muabudiwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu anafanya hayo? Sema, Leteni hoja yenu iwapo nyinyi ni wakweli katika madai yenu kwamba Mwenyezi Mungu Ana mshirika katika mamlaka Yake na ibada Yake.»

    [65] Sema, ewe Mtume, kuwaambia wao, «Hakuna yoyote ajuwaye, mbinguni wala ardhini, jambo lolote lililofichika ambalo Mwenyezi Mungu Amejihusisha Mwenyewe kulijua. Na wao hawajui ni lini watafufuliwa kutoka makaburini mwao wakati wa Kiyama kusimama.»

    [66] Bali ujuzi wao wa Kiyama utakamilika huko Akhera, huko watakuwa na yakini juu ya Nyumba ya Akhera na vituko vilivyomo watakapoishuhudia. Na wao walipokuwa duniani walikuwa na shaka nayo, bali akili zao zilikuwa zimepofuka hawaiyoni

    [67] Na walisema wale waliokanusha upweke wa Mwenyezi Mungu, «Je, sisi na wazazi wetu tutafufuliwa, tukiwa hai kama tulivyo, baada ya kufa kwetu, baada ya sisi kuwa mchanga

    [68] Tuliahidiwa kufufuliwa huku, sisi na wazazi wetu, hapo kabla(tulipokuwa duniani) hatukuuona uhakika wake wala kutokea kwake. Hatukuona ahadi hii isipokuwa ni hadithi za urongo zilizozuliwa na kuandikwa na watu wa kale ndani ya vitabu vyao

    [69] Waambie, ewe Mtume, hawa wakanushaji, «Tembeeni kwenye ardhi mziangalie nyumba za wahalifu waliokuwa kabla yenu muone ulikuwa vipi mwisho wa wenye kuwakanusha Mitume? Mwenyezi Mungu Aliwaangamiza kwa ukanushaji wao, na Mwenyezi Mungu Atawafanya nyinyi kama wao iwapo hamtaamini.»

    [70] Usiwe na masikitiko juu ya kukupa mgongo kwao, hao washirikina, na kukukanusha, na usiwe na dhiki moyo wako juu ya vitimbi vyao wanavyokufanyia, kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kukupa ushindi juu yao

    [71] Na washirikina wa watu wako, ewe Mtume, wanasema «Itakuwa lini ahadi hii ya adhabu mnayotuahidi kwayo, wewe na wafuasi wako, mkiwa nyinyi ni wakweli katika yale mnayotuahidi?»

    [72] Waambie, ewe Mtume, «Huenda yakawa ni karibu kwenu baadhi ya yale mnayoyafanyia haraka ya adhabu ya Mwenyezi Mungu.»

    [73] Na hakika ya Mola wako ni Mwenye nyongeza za wema kwa watu, kwa kuacha kuwaharakishia wao adhabu kwa kumuasi kwao Yeye na kumkanusha. Lakini wengi wao hawamshukuru kwa hilo wakamuamini na wakamtakasia ibada

    [74] Na kwa hakika, Mola wako ni Yeye Anayekijua kile ambacho vifua vyao vinakificha na kile ambacho vinakifichua wazi

    [75] Na hakuna kitu chochote kilichofichika na macho ya viumbe, kilichoko mbinguni na ardhini,isipokuwa kiko kwenye Kitabu kilicho waziwazi kilichoko kwa Mwenyezi Mungu. Kitabu hiko kimevizunguka vyote vilivyokuwa na vitakavyokuwa

    [76] Kwa hakika, hii Qur’ani inawapa Wana wa Isrāīl habari ya ukweli katika mambo mengi zaidi ambayo wao wametafautiana juu yake

    [77] Na kwa hakika, hii Qur’ani ni uongofu kutoka kwenye upotevu na ni rehema inayotoa kwenye adhabu kwa mwenye kuiamini na akajiongoza kwa uongofu wake

    [78] Hakika Mola wako Anahukumu baina ya wanaotafautiana, miongoni mwa Wana wa Isrāīl na wasiokuwa wao, kwa uamuzi wake kati yao. Akamlipiza kwa kumtesa mtenda makosa na kumlipa mema mtenda wema. Na Yeye Ndiye Mwenye nguvu Anayeshinda, uamuzi Wake haurudishwi, Aliye Mjuzi, kwa hivyo ukweli na urongo hazimchanganyikii

    [79] Jitegemeze, ewe Mtume, katika mambo yako yote kwa Mwenyezi Mungu na uwe na imani Kwake, kwani Yeye ni Mwenye kukutosha. Hakika wewe uko kwenye njia iliyo wazi isiyokuwa na shaka

    [80] Hakika yako wewe, ewe Mtume, huwezi kumsikilizisha haki yule ambaye Mwenyezi Mungu Amepiga mhuri juu ya moyo wake Akaufisha, na humsikilizishi ulinganizi wako yule ambaye Mwenyezi Mungu Ameyafanya masikizi yake kuwa kiziwi asiisikie haki, pindi wanapogeuka kukupa mgongo wewe. Kwani kiziwi hasikii ulinganizi akiwa amekuelekea, basi itakuwa vipi akiwa katika hali ya kupa mgongo na kugeuka

    [81] Na wewe, ewe Mtume, hukuwa ni mwenye kuongoa kutoka kwenye upotevu yule ambaye Mwenyezi Mungu Amemfanya kipofu asiuone uongofu na unyofu. Na haimkini kwako wewe umsikilizishe isipokuwa yule anayeziamini aya zetu, basi hao ni wenye kusalimu amri, watiifu na wenye kuyakubali yale ninayowalingania wao

    [82] Na itakapopasa adhabu juu yao, kwa sababu ya kuvama kwao ndani ya madhambi na uasi na kuzipa mgongo kwao sheria za Mwenyezi Mungu na hukumu Zake mpaka wakawa ni miongoni mwa wabaya wa viumbe vyake, tutawatolea wao, katika kipindi cha mwisho wa zama, alama, miongoni mwa alama kubwa za Kiyama, nayo ni Mnyama atakayesema na wao kwamba watu wanaokanusha kufufuliwa ni wakanushaji wa Qur’ani na Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, hawaaamini wala hawafanyi matendo mema

    [83] Na siku tutakayokusanya- Siku ya Ufufuzi- katika kila jamii, kundi la watu, miongoni mwa wale wanaozikanusha aya zetu na hoja zetu, watazuiliwa wa mwanzo wao wachanganywe na wa mwisho wao, wapate kukusanyika wote, kisha waongozwe hadi pale pa kuhesabiwa

    [84] Mpaka litakapokuja, miongoni mwa kila jamii, pote la wale wanaozikanusha aya zetu na wakakusanyika, Mwenyezi Mungu Atasema, «Je, mumezikanusha aya zangu nilizoziteremsha kwa Mitume wangu na alama nilizozisimamisha zenye kuonyesha upweke wangu na ustahiki wangu peke yangu kuabudiwa na hali nyinyi hamkuwa na ujuzi wa kutosha kuwa ni batilifu, hata iwafanye mzipe mgongo na mzikanushe au ni kitu gani mlikuwa mkifanya?»

    [85] Hapo lithibiti juu yao neno la adhabu kwa sababu ya udhalimu wao na ukanushaji wao, na watakuwa hawatamki neno lenye hoja ya wao kujitetea nafsi zao ili kujiepushia adhabu kali iliyowashukia

    [86] Je, hawakuona hawa wakanushaji wa aya zetu kwamba sisi tumeufanya usiku ni kipindi cha wao kutulia ndani yake na kulala, na mchana ni kipindi cha wao kuona ili waende kutafuta maisha yao? Hakika katika kuvipelekesha hivyo viwili kuna ushahidi kwa watu wanaoamini ukamilifu wa uweza wa Mwenyezi Mungu, upweke Wake na ukubwa wa neema Zake

    [87] Na kumbuka, ewe Mtume, siku ambayo Malaika atakapovuvia kwenye pembe, hapo wababaike walioko mbinguni na ardhini babaiko kubwa sana kwa kituko cha Mvuvio huo, isipokuwa yule aliyevuliwa na Mwenyezi Mungu kati ya wale Aliyowakirimu na Akawahifadhi na hilo babaiko. Na viumbe wote watamjia Mwenyezi Mungu wakiwa wanyonge watiifu

    [88] Na utayaona majabali ukidhania kuwa yamesimama na yametulia na hali yanatembea mwendo wa kasi kama vile yanavyotembea mawingu yanayopelekwa na upepo. Na huu ni katika utengenezaji wa Mwenyezi Mungu Ambaye Ametengeneza uumbaji wa kila kitu na Akaufanya mzuri madhubuti. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtambuzi wa mnayoyafanya, enyi watu, yawe mazuri au mabaya na Atawalipa kwa hayo

    [89] Mwenye kuja na upwekeshaji wa Mwenyezi Mungu na kumuamini na kumuabudu Peke Yake na matendo mema Siku ya Kiyama, basi Atakuwa na malipo mema makubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, yatakaokuwa mema na bora zaidi, nayo ni Pepo. Na wao, Siku ya babaiko kubwa, watakuwa kwenye amani

    [90] Na mwenye kuja na ushirikina na matendo mabaya yanayochukiza, basi malipo yao ni awatupe Motoni Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama. Na wataambiwa kwa kulaumiwa, «Je, mtalipwa isipokuwa kile mliokuwa mkikifanya duniani?»

    [91] Sema, ewe Mtume, kuwaambia watu, «Hakika nimeamrishwa nimuabudu Mola wa mji huu, nao ni Makkah, ambao Ameuharamisha kwa viumbe wake wasimwage humo damu iliyo haramu kuimwaga au kumdhulumu yoyote ndani yake au kuwinda viindwa vyake au kukata mti wake. Na ni Chake Yeye kila kitu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake. Na nimeamrishwa nimuabudu Yeye Peke Yake, na sio mwingine, na niwe mtiifu Kwake

    [92] na niwasomee watu Qur’ani, basi mwenye kuongoka kuyajua yaliyomo ndani yake na akayafuata niliokuja nayo, wema wa hilo na malipo yake yatamfaa mwenyewe. Na mwenye kupotea akapotoka na njia ya haki, basi wewe sema, «Mimi ni muonyaji kwenu, nawaonya na adhabu ya Mwenyezi Mungu na mateso Yake iwapo hamtaamini, kwani mimi ni mmoja wa Mitume waliowaonya watu wao, na uongofu wa aina yoyote hauko mikononi mwangu

    [93] Na sema, ewe Mtume, «Sifa nzuri ni za Mwenyezi Mungu, atawaonyesha alama Zake ndani ya nafsi zenu na kwenye mbingu na ardhi, na mtazijua ujuzi wenye kuwaonyesha haki na kuwafafanulia ubatilifu. Na Mola wako si mwenye kughafilika na hayo mnayoyafanya na Atawalipa nyinyi kwa hayo

    Visa

    Surah 28

    [1] Ṭā, Sīn, Mīm. (Yametangulia maelezo kuhusu herufi ziliokatwa na kutengwa mwanzo wa sura ya Al-Baqarah)

    [2] Hizi ni aya za Qur’ani niliyokuteremshia, ewe Mtume, yenye kufafanua kila kile ambacho waja wanakihitajia katika ulimwengu wao na Akhera yao

    [3] Tunakusimulia wewe habari ya Mūsā na Fir’awn kwa ukweli (ili wazingatie wale) watu wanaoiamini hii Qur’ani na wakubali kwamba inatoka kwa Mwenyezi Mungu na wafanye matendo yanayoambatana na uongofu wake

    [4] Hakika Fir’awn alifanya kiburi na akapita mipaka katika nchi, akawafanya watu wake kuwa ni makundi tafauti-tafauti, akawa analinyongesha kundi moja ya hayo, nalo ni lile la Wana wa Isrāīl, akawa anawaua watoto wao wa kiume na anawabakisha wanawake wao kwa kutumika na kudharauliwa, Hakika yeye alikuwa ni miongoni mwa waharibifu katika ardhi

    [5] Na tunataka kuwafadhili wale ambao Fir'awn aliwafanya wanyonge nchini, tuwafanye ni viongozi katika wema na ni wenye kuulingania, na tuwafanye wao wairithi nchi baada ya kuangamia Fir'awn na watu wake

    [6] Na tuwape uthabiti katika nchi na tumfanye Fir’awn, Hāmān na askari wao waone, kutoka kundi hili linalonyongeshwa kile walichokuwa wakikiogopa cha kuangamia kwao na kuondoka ufalme wao na kuwatoa wao kwenye nyumba zao kwa mkono wa mzaliwa wa Wana wa Isrāīl

    [7] Na tukampa mawazo mamake Mūsā alipomzaa na akamuogopea asije Fir'awn akamchinja kama anavyowachinja watoto wa wana wa Isrāīl kwamba «mnyonyeshe ukiwa mtulivu, na pindi uogopapo kujulikana mambo yake, muweke sandukuni na ulitupe kwenye mto wa Nail bila ya kuogopa kwamba fir'awn na watu wake watamuua na bila ya kuwa na masikitiko ya kuepukana na yeye, hakika sisi tutamrudisha kwako na tutamtumiliza kuwa Mtume.»

    [8] Hapo akamuweka sandukuni na akalitupa kwenye mto wa Nail, na wafuasi wa Fir'awn wakalipata na wakalichukua, na mwisho wake ukawa vile Alivyokadiria Mwenyezi Mungu kuwa Mūsā awe ni adui yao kwa kuwa kinyume na dini yao, na awatie kwenye huzuni ya kuzamishwa na kuondokewa na ufalme wao mikononi mwake. Kwa hakika, Fir'awn na Hāmān na wasaidizi wao walikuwa wafanyaji makosa washirikina

    [9] Na mke wa Fir'awn alipomuona , Mwenyezi Mungu Alimtia mapenzi moyoni mwake na akasema kumwambia Fir'awn, «Mtoto huyu atakuwa chimbuko la furaha kwangu mimi na wewe, Msimuue kwani huenda tukapata kheri kutoka kwake au tumfanye ni mtoto wetu» na hali Fir'awn na jamaa wa nyumbani kwake hawafahamu kwamba maangamivu yao yatatokana mikononi mwake

    [10] Na kifua cha mamake Mūsā kikawa hakijishughulishi na kitu chochote duniani isipokuwa hamu ya Mūsā na kumtaja, na alikaribia kudhihirisha kuwa yule ni mwanawe lau si sisi kumthibitisha, naye akavumilia asilidhihirishe hilo, ili awe ni miongoni mwa wenye kuamini ahadi ya Mwenyezi Mungu na mwenye kuwa na yakini nayo

    [11] Na akasema mamake Mūsā kumwambia nduguye wa kike alipomtupa mtoni, «Fuata athari za Mūsā uone atafanywa nini? Akafuata athari zake na akamuona kwa mbali na hali watu Fir'awn hawajui kwamba yeye ni dadake na kwamba yeye afuatilia habari zake

    [12] Na tulimzuia Mūsā asinyonye kutoka kwa wanyonyeshaji kabla hatujamrudisha kwa mamake, hapo dadake akasema, «Je, ni waonyeshe watu wa nyumba ambao watamlea na kumnyonyesha vizuri na ambao watakuwa na huruma naye? Wakamkubalia hilo

    [13] Basi tukamrudisha Mūsā kwa mamake, ili jicho lake litulie kwake na tukamtekelezea ahadi yetu kwake, kwa kuwa alirudi kwake akiwa amesalimika na kuuawa na Fir'awn, na ili asihuzunike kwa kuepukana naye, na ajue kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli, ile Aliyowaahidi kuwa atawarudishia na Amfanye ni miongoni mwa Mitume. Hakika Mwenyezi Mungu Haendi kinyume na ahadi Yake, lakini wengi wa washirikina hawajui kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli

    [14] Na Alipofikia Mūsā umri wa kuwa na nguvu na ikakamilika akili yake, tulimpa busara na elimu ya kujulia hukumu za Sheria. Na kama tulivyompa Mūsā malipo mema kwa utiifu wake na wema wake, tunampa malipo mema mwenye kufanya wema miongoni mwa waja wetu

    [15] Na Mūsā aliingia mjini kwa kujificha wakati ambapo watu wake walikuwa wako katika hali ya kughafilika, akawapata humo watu wawili wanapigana, mmoja wao ni katika wana wa Isrāīl jamaa za Mūsā na mwingine ni katika jamaa za Fir’awn. Basi yule aliyekuwa ni katika jamaa ya Mūsā alitaka msaada dhidi ya yule Aliyekuwa katika maadui zake, hapo Mūsā akampiga kofi na akafa. Mūsā akasema alipomuua, «Huu ni katika ushawishi wa Shetani aliyenipandisha hasira zangu mpaka nikampiga huyu akafa. Hakika ya Shetani ni adui ya mwanadamu ni mwenye kupoteza njia ya uongofu, ni mwenye uadui wa waziwazi.» Kitendo hiki cha Mūsā kilikuwa kabla ya kupewa unabii

    [16] Mūsā akasema, «Mola wangu! Mimi nimejidhulumu nafsi yangu kwa kumuua mtu ambaye hukuniamuru kumuua, basi nisamehe dhambi hilo.» Na Mwenyezi Mungu Akamsamehe. Kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe sana dhambi za waja Wake, ni Mwenye huruma nao sana

    [17] Mūsā akasema, «Mola wangu! Kwa vile ulivyonineemesha kwa toba, msamaha na neema nyingi, sitakuwa mwenye kumsaidia yoyote kufanya uasi wake na uhalifu wake

    [18] Hivyo basi Mūsā akaingiwa na kicho akiwa kwenye mji wa Fir’awn, anatafuta habari zinazozungumzwa na watu kuhusu yeye na yule mtu aliyemuua, hapo akamuona yule mtu wake wa jana akipigana na Mmisri mwingine na akimtaka amsaidie. Mūsā alimwambia, «Kwa kweli, wewe ni mwingi wa upotofu, ni mpotevu waziwazi.»

    [19] Basi alipotaka Mūsā kumshika Mmisri kupambana naye, alisema, «Je, unataka kuniua mimi kama ulivyomuua mtu jana? Hutaki isipokuwa kuwa jeuri katika nchi, na hutaki kuwa ni miongoni mwa wale wanaofanya upatanishi kati ya watu.»

    [20] Na akaja mtu mbiombio kutoka mwisho wa mji, akasema, «Ewe Mūsā! Kwa hakika wale watukufu wa jamii ya Fir’awn wanafanya njama ya kukuua na wanashauriana juu ya hilo, basi toka. Kwani mimi ni kati ya wale wanaokupa ushauri mzuri na wanaokupendelea wema.»

    [21] Hapo Mūsā akautoka mji wa Fir'awn akiwa katika hali ya kuogopa, akitazamia kukamatwa na wale wanaomtafuta, na akamuomba Mwenyezi Mungu Amuokoe na watu madhalimu

    [22] Na alipokusudia kuelekea nchi ya Madyan, na akatoka nje ya utawala wa Fir'awn, alisema, «Nina matumaini kwamba Mola wangu Ataniongoza njia nzuri ya kuelekea Madyan.»

    [23] Alipoyafikia maji ya Madyan, alilikuta hapo kundi la watu wanawapa maji wanyama wao, na akawakuta, kando ya kundi hilo, wanawake wawili wamejitenga na watu na wamewazuilia wanyama wao na pale penye maji, kwa kushindwa kwao na udhaifu wao wa kutoweza kubanana na wanaume, na wanangojea mpaka wanyama wa watu waondoke kwenye maji kisha hapo wawapatie wanyama wao maji. Mūsā, amani imshukiye, alipowaona aliwaonea huruma, kisha alisema kuwaambia, «Muna nini nyinyi?» wakasema, «Hatuwezi kubanana na wanaume, na hatuchoti maji mpaka watu wamalize kuchota, na baba yetu ni mzee sana hawezi kuwachotea maji wanyama wake kwa udhaifu wake na uzee wake.»

    [24] Basi Mūsā akawachotea maji wanyama wa wale wanawake wawili, kisha akageuka kwenda kwenye kivuli cha mti kujifinika nacho na akasema, «Mola wangu! Hakika mimi ni mhitaji wa wema wako wowote ule utakaoniletea,» kama vile chakula. Na njaa ilikuwa imemshika sana

    [25] Hapo akaja mmoja wa wale wanawake wawili aliyewachotea maji akitembea na huku yuwaona haya akasema, «Baba yangu anakuita ili akupe malipo ya maji uliyotuchotea.» Na Mūsā akaenda na yeye hadi kwa baba yake. Alipomjia baba yake na akamsimulia habari zake yeye pamoja na Fir’awn na watu wake, yule baba wa mwanamke alisema, «Usiogope! Umeokoka na watu madhalimu, nao ni Fir'awn na watu wake, kwani wao hawana mamlaka yoyote nchini kwetu.»

    [26] Akasema mmoja wa wanawake wawili kumwambia baba yake, «Ewe baba yangu! Muajiri yeye akuchungie wanyama wako, kwani mtu bora wa wewe kumuajiri kwa kuchunga ni yule aliye na nguvu ya kuwalinda wanyama wako, aliye muaminifu ambaye huchelei kuwa atakufanyia hiana katika amana unayompatia.»

    [27] Mzee akasema kumwambia Mūsā, «Mimi nataka kukuoza mmoja wa mabinti wangu hawa wawili, kwa sharti uwe muajiriwa wangu wa kuwachunga wanyama wangu kwa kipindi cha miaka minane. Na ukikamilisha miaka kumi, basi hiyo ni hisani yako. Na mimi sitaki kukusumbua kwa kuifanya miaka kumi. Utanikuta mimi, Mwenyezi Mungu Akitaka, ni miongoni mwa watu wema, katika uzuri wa tangamano na utekelezaji ahadi wa ninayoyasema

    [28] Mūsā akasema, «Hilo ulilolisema lisimame kuwa ndio ahadi baina yangu mimi na wewe, muda wowote wa vipindi viwili nitakaa kazini, nitakuwa nimekutekelezea, na sitatakiwa kuengeza juu yake, na Mwenyezi Mungu, kwa tunayoyasema, ni Mtegemewa, ni Mtunzi, Anatuona na Anakijua kile tulichofanya mapatano juu yake.»

    [29] Basi Nabii wa Mwenyezi Mungu Mūsā, amani imshukiye, alipomtekelezea mwenzake kipindi cha miaka kumi, nao ni muda mkamilifu zaidi wa vile vipindi viwili, na akaenda na watu wa nyumbani kwake kuelekea Misri, aliona moto upande wa jabali la Ṭūr. Mūsā alisema kuwaambia watu wa nyumbani kwake, «Subirini na mngojee. Mimi nimeona moto. Huenda nikawaletea habari kutoka kule, au nikawaletea kinga cha moto mkapata kujiotesha nacho.»

    [30] Basi Mūsā alipoujia moto, Mwenyezi Mungu Alimuita kutoka upande wa bonde la mkono wa kulia wa Mūsā, katika ardhi iliyobarikiwa ya upande wa mti kwamba: «Ewe Mūsā! Mimi Ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe wote,»

    [31] na kwamba: «itupe fimbo yako!» Na Mūsā akaitupa, ikageuka kuwa nyoka anayetembea kwa haraka. Alipoiona inatetemeka kama kwamba ni nyoka kama walivyo nyoka wengine, aligeuka kumkimbia na asizunguke kwa kuogopa. Na hapo Mola wake Alimuita, «Ewe Mūsā! Nielekee mimi, na usiogope! Wewe ni miongoni mwa wenye kuaminika na kila lenye kuchukiza

    [32] «Tia mkono wako kwenye uwazi wa kanzu yako uliofunguliwa kifuani na uutoe, utatoka kuwa mweupe, kama barafu, ambao si wa ugonjwa wala mbalanga, na ujikumbatie kwa mikono yako ili usalimike na kicho. Hivi viwili nilivyokuonesha, ewe Mūsā, vya fimbo kugeuka nyoka na kuufanya mkono wako kuwa mweupe na wenye kung’ara, si kwa ugonjwa wala mbalanga, ni dalili mbili kutoka kwa Mola wako, uende nazo kwa Fir’awn na watukufu wa watu wake.» Hakika Fir’awn na viongozi walio karibu naye walikuwa ni wakanushaji

    [33] Mūsā akasema, «Mola wangu! Mimi nimemuua mtu wa jamii ya Fir’awn, basi naogopa wasije wakaniua

    [34] Na ndugu yangu, Hārūn, ana ufasaha zaidi wa matamshi kuliko mimi, basi mtume yeye pamoja na mimi awe msaidizi wangu, ataniamini na atawafafanulia wao yale ninayowaambia. Mimi ninachelea wasije wakanikanusha mimi kwa maneno yangu nitakayowaambia kwamba mimi nimetumilizwa kwao.»

    [35] Mwenyezi Mungu Akamwambia Mūsā, «Tutakupa nguvu kwa ndugu yako, na tutawapa nyinyi wawili hoja juu ya Fir’awn na watu wake wasiweze kuwafikia nyinyi kwa ubaya wowote. Nyinyi wawili na wale wenye kuwaamini nyinyi ndio mtakaopewa ushindi juu ya Fir’awn na watu wake kwa sababu ya aya zetu na ukweli unaoonyeshwa na hizo aya.»

    [36] Mūsā alipomjia Fir’awn na viongozi wa mamlaka yake na aya zetu na hoja zetu zenye kushuhudilia ukweli wa yale aliyokuja nayo kutoka kwa Mola wake, walimwambia Mūsā, «Hili ulilotujia nalo si chochote isipokuwa ni uchawi uliouzua kwa urongo na ubatilifu. Na hatujawahi kusikia jambo hili unalotuitia kwalo kutoka kwa wale waliotutangulia waliopita kabla yetu.»

    [37] Na Mūsā alisema kumwambia Fir’awn, «Mola wangu Anamjua zaidi aliye kwenye sawa kati yetu, aliyekuja na uongofu kutoka Kwake, na yule atakayekuwa na mwisho wa kushukuriwa katika Nyumba ya Akhera. Kwa hakika, madhalimu hawatayapata matakwa yao.»

    [38] Na Fir’awn akasema kuwaambia watukufu wa watu wake, «Enyi viongozi! Mimi sijui kwamba nyinyi muna mola isipokuwa mimi anayestahiki kuabudiwa. Basi, ewe Hāmān! Niwashie moto juu ya udongo mpaka ushikane, na unijengee jengo lenye urefu wa kuelekea juu, kwani huenda nikamchungulia muabudiwa wa Mūsā ambaye yeye anamuabudu na anawaita watu wamuabudu. Na mimi ninadhani kuwa yeye ni miongoni mwa warongo katika hayo anayoyasema.»

    [39] Na Fir’awn na askari wake walifanya kiburi katika nchi ya Misri bila ya haki kwa kukataa kumuamini Mūsā na kumfuata katika lile alilowaitia na wakadhani kwamba baada ya kufa kwao hawatafufuliwa

    [40] Tukamchukua Fir’awn na askari wake tukawatupa wote baharini na tukawazamisha. Basi angalia, ewe Mtume, ulikuwa vipi mwisho wa hawa waliojidhulumu wenyewe wakamkanusha Mola wao

    [41] Na tumemfanya Fir’awn na watu wake ni wenye kuongoza kwenye njia ya motoni, wakifuatwa na watu wa ukafiri na uasi. Na Siku ya Kiyama hawataokolewa. Hiyo ni kwa sababu ya ukafiri wao na kuwakanusha kwao Mitume wa Mola wao na kuendelea kwao kufanya hivyo

    [42] Na tukamfuatilizia Fir’awn na watu wake laana na hasira kutoka kwetu juu yao. Na Siku ya Kiyama, wao watakuwa ni miongoni mwa wale ambao matendo yao yalikuwa yamechafuka, wale watakaowekwa mbali na rehema ya Mwenyezi Mungu

    [43] Na hakika tulimpa Mūsā Taurati baada ya kuwaangamiza ummah waliokuwa kabla yake, kama vile watu wa Nūḥ, ‘Ād, Thamūd, na watu wa Lūṭ na watu wa Madyan, hali ya kuwa Taurati ina hoja kwa Wana wa Isrāīl ambazo kwa hizo wanayaona yale yanayowafaa na yanayowadhuru, na ndani yake kuna rehema kwa wanaoifuata Taurati kivitendo. Huenda wao wakazikumbuka neema za Mweyezi Mungu juu yao, wakamshukuru kwa hizo na wasimkanushe

    [44] Na hukuwako, ewe Mtume, upande wa jabali la jua la kuchwa wa Mūsā, tulipombebesha maamrisho yetu na makatazo yetu, na hukuwa ni kati ya wale waliolishuhudia hilo mpaka kusemwe kwamba habari hii imekufikia kwa njia hii

    [45] Lakini sisi tuliwaumba watu baada ya Mūsā, wakakaa kwa muda mrefu, wakasahau ahadi ya Mwenyezi Mungu, wakaacha amri yake. Wala hukuwa ni miongoni mwa wakazi wa mji wa Madyan ukiwasomea kwao Kitabu chetu, na kwa hivyo ikakujia habari yao na ukaisimulia. Lakini habari uliokuja nayo kuhusu Mūsā ni wahyi na ni ushahidi wa utume wako

    [46] Na hukuwako, ewe Mtume, upande wa jabali la Tūr tulipomuita Mūsā, na hukushuhudia lolote katika hayo. Lakini sisi tulikutumiliza ukiwa ni rehema kutoka kwa Mola wako, ili uwaonye watu ambao hawakujiwa na muonyaji kabla yako, huenda wao wakakumbuka wema uliokuja nao wakaufuata na uovu ulioukataza wakajiepusha nao

    [47] Na lau si adhabu iteremke kwa hawa makafiri kwa sababu ya ukafiri wao, kisha waseme, «Si mwanzo utuletee Mtume kwetu, tupate kuzifuata aya zako zilizoteremshwa kwenye Kitabu chao na tuwe ni miongoni mwa wenye kukuamini»

    [48] Na alipowajia Muhammad watu hawa akiwa ni muonyaji kwao walisema, «Si apewe, huyu aliyetumilizwa kwetu, mfano wa kile alichopewa Mūsā, cha miujiza inayoonekana na Kitabu kilichoteremshwa mara moja.» Waambie, ewe Mtume, «Je, si Mayahudi walikikanusha kile alicholetewa Mūsā hapo kabla? Walisema kwamba ndani ya Taurati na Qur’ani kuna aina mbili za uchawi zilizosaidiana katika uchawi utokanao na hivyo viwili, na wakasema, «Sisi ni wenye kuvikanusha vyote viwili.»

    [49] Waambie hawa, ewe Mtume, «Basi Leteni kitabu kinachotoka kwa Mwenyezi Mungu ambacho ni cha sawa zaidi kuliko Taurati na Qur’ani, nipate kukifuata mkiwa nyinyi ni wakweli katika madai yenu.»

    [50] Wasipokuitikia kwa kuleta Kitabu, na hawakusaliwa na hoja yoyote, basi ujue kwamba wao wanafuata matamanio yao. Na hakuna yoyote aliye mpotevu zaidi kuliko yule aliyefuata matamanio yake bila ya kuwa na uongofu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu Hawaafikii kuifikilia haki watu madhalimu walioenda kinyume na amri ya Mwenyezi Mungu na wakakiuka mipaka Yake

    [51] Na kwa hakika, tuliifafanua na kuieleza Qur’ani kwa kuwaonea huruma watu wako, ewe Mtume, huenda wao wakakumbuka na wakawaidhika nayo

    [52] Wale ambao tuliwapa Kitabu kabla ya Qur’ani, nao ni Mayahudi na Wanaswara ambao hawakugeuza, wanaiamini Qur’ani na wanamuamini Muhammad, rehema na amani zimshukiye

    [53] Na pindi isomwapo hii Qur’ani kwa wale tuliowapa Kitabu wanasema, «Tumeiamini na tumeifuata kivitendo, hiyo ni haki itokayo kwa Mola wetu, hakika sisi tulikuwa, kabla haijateremka, ni Waislamu wenye kumpwekesha, kwani Dini ya Mwenyezi Mungu ni moja, nayo ni Uislamu.»

    [54] Hawa ambao sifa zao zimetangulia, watapewa malipo ya matendo yao mema mara mbili: ya kukiamini Kitabu chao na kuiamini kwao Qur’ani kwa vile walivyosubiri. Na miongoni mwa sifa zao ni kwamba wao wanalikinga baya kwa zuri, na katika kile tunachowaruzuku wanatumia katika njia ya uzuri na wema

    [55] Na wanaposikia, watu hawa, maneno ya ubatilifu, hawayapulikizi, na wanasema, «Sisi tuna matendo yetu tusiyoyaepuka, na nyinyi muna matendo yenu msiyoyaepuka. Sisi hatujishughulishi kuwarudi nyinyi, na hamtasikia kutoka kwetu isipokuwa mema, na hatutasema na nyinyi kulingana na ujinga wenu, kwa kuwa sisi hatutaki njia ya wajinga na hatuipendi.» Na haya ni miongoni mwa maneno mazuri zaidi ambayo walinganizi kwa Mwenyezi Mungu wanayasema

    [56] Wewe, ewe Mtume, humuongoi, uongofu wa kumuafikia, unayependa aongoke. Lakini hilo liko kwenye mkono wa Mwenyezi Mungu, Anamuongoa Anayemtaka kumuongoa kwenye Imani na kumuafikia aifuate. Na Yeye Ndiye Anayemjua zaidi anayefaa kuongoka, hivyo basi Anamuongoa

    [57] Na makafiri wa Makkah wanasema, «Tukiifuata haki uliyotuletea na tukajiepusha na wategemewa na waungu, tutanyakuliwa kutoka kwenye ardhi yetu kwa kuuawa na kutekwa na kuporwa mali.» Kwani hatukuwafanya wao wamakinifu ndani ya mji wa amani, ambao ndani yake tumeharamisha umwagaji damu na ambao yanaletwa huko matunda ya kila aina yakiwa ni riziki kutoka kwetu? Lakini wengi wa hawa washirikina hawajui kadiri ya neema hizi kwao, wakapata kumshukuru Aliyewaneemesha wao kwazo na wakamtii

    [58] Na wengi miongoni mwa watu wa miji tuliwaangamiza yalipowapumbaza wao maisha yao yakawashughulisha wasiwaamini Mitume, kwa hivyo wakakufuru na wakapita kiasi. Basi hayo ndio majumba yao, hayakukaliwa baada yao isipokuwa machache katika hayo. Na sisi daima ndio wenye kuwarithi waja: tunawafisha, kisha wanarejea kwetu tukawalipa kwa matendo yao

    [59] Na hakuwa Mola wako, ewe Mtume, ni mwenye kuiangamiza miji iliyo pambizoni mwa Makkah katika zama zako mpaka Atumilize kwenye kilele cha miji hiyo, nacho ni Makkah, Mtume atakayewasomea wao aya zetu. Na hatukuwa ni wenye kuiangamiza miji isipokuwa na watu wake wanajidhulumu wenyewe kwa kumkanusha Mwenyezi Mungu na kumuasi, basi wao kwa hivyo wanastahili mateso na adhabu

    [60] Na chochote kile mlichopewa, enyi watu, cha mali na watoto, basi hayo ni starehe ya nyinyi kustarehe nayo katika maisha haya ya kilimwengu na ni pambo la kujipamba nalo. Na yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu, yaliyowekewa watu walio watiifu Kwake na wenye kumtegemea, ni bora zaidi na ni yenye kusalia zaidi, kwani hayo ni ya daima yasiyomalizika. Basi nyinyi hamuwi na akili, enyi watu, ya kuzingatia kwayo, mkajua lema na ovu

    [61] Je, yule tuliyomuahidi Pepo, miongoni mwa viumbe wetu, kwa sababu ya kututii, akawa ni mwenye kupata alichoahidiwa na ni mwenye kukifikia, ni kama yule tuliyempa, katika uhai wa kilimwengu, starehe zake, naye akastarehe nazo na akaipa mbele ladha ya karibu kuliko ile ya baadaye, kisha yeye akawa ni mwenye kuhudhurishwa Siku ya Kiyama ili ahesabiwe na alipwe? Makundi mawili haya hayalingani. Basi mwenye akili ajichagulie nafsi yake kile kilicho bora kuchagua, nacho ni kule kumtii Mwenyezi Mungu na kutafuta radhi Zake

    [62] Na siku ambayo Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, Atakapowaita wale waliomshirikisha Yeye wategemewa na masanamu ulimwenguni, awaambie, «Wako wapi washirika wangu ambao nyinyi mlikuwa mkidai kuwa wao ni washirika wangu?»

    [63] Watasema wale ambao imethibiti kwao adhabu, nao ni walinganizi wa ukafiri, «Mola wetu! Hawa ndio tuliowapoteza. Tuliwapoteza kama tulivyopotea sisi. Tumejiepusha kwako na urafiki wao na uokoaji wao. Hawakuwa ni sisi wanaotuabudu, Hakika ni kwamba wao walikuwa wakiwaabudu mashetani.»

    [64] Na wataambiwa, Siku ya Kiyama, wale wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, «Waiteni washirika wenu ambao mlikuwa mkiwaabudu badala ya Mwenyezi Mungu.» Na wao wakawaita na wasiwajibu. Na wakaiona wazi adhabu, na lau wao wangalikuwa ni waongofu ulimwenguni, hawangaliadhibiwa.»

    [65] Na siku ambayo Mwenyezi Mungu Atawaita hawa washirikina na aseme, «Mliwajibu vipi Mitume katika yale tuliyowatuma wao kwenu?»

    [66] Hapo hoja zao zote zitafichika, wasijue ni hoja ipi waitumie. Wao hawatoulizana wao kwa wao kuhusu hoja za kuzitumia, maswali yenye nafuu

    [67] Ama yule aliyetubia kati ya washirikina na akamtakasia Mwenyezi Mungu ibada na akafanya matendo yanayoambatana na amri Yake na Mtume Wake, yeye ni katika wale wanaofuzu katika Nyumba Mbili

    [68] Na Mola wako anaumba anachokitaka kukiumba, na anamteua awe karibu na Yeye Anayemtaka katika viumbe wake. Na hakuna yoyote mwenye chochote cha amri na uteuzi. Kwa hakika, hilo ni la Mwenyezi Mungu Peke Yake, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Ametukuka na kuepukana na ushirikina wao

    [69] Na Mola wako anayajua yale yanayofichwa na vifua vya waja Wake na yale wanayoyafanya waziwazi

    [70] Na Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu Ambaye hapana muabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye. Ni Zake sifa njema na shukrani katika ulimwengu na Akhera. Na ni Wake uamuzi baina ya waja Wake. Na Kwake mutarudishwa baada ya kufa kwenu, muhesabiwe na mulipwe

    [71] Sema, ewe Mtume, «Nipeni habari, enyi watu, iwapo Mwenyezi Mungu Angaliwaekea usiku wa daima mpaka Siku ya Kiyama, ni mungu gani asiyekuwa Mwenyezi Mungu angaliwaletea mwangaza wa nyinyi kupata kuona? Basi kwani nyinyi hamsikii kwa namna ya kufahamu na kukubali?»

    [72] Waambie, «Nipeni habari iwapo Mwenyezi Mungu Angaliwaekea mchana wa daima mpaka Siku ya Kiyama, ni mungu gani asiyekuwa Mwenyezi Mungu angaliwaletea usiku wa nyinyi kutulia na kupumzika ndani yake? Basi hamuoni kwa maangalizi yenu kule kupishana kwa usiku na mchana?»

    [73] Na miongoni mwa rehema Yake kwenu, enyi watu, ni kuwafanyia usiku na mchana Akatafautisha baina ya viwili hivi, Akaufanya huu usiku kuwa ni giza, ili mutulie humo na miili yenu ipumzike. Na Akawafanyia mchana kuwa ni mwangaza, ili mutafute maisha yenu na ili mumshukuru Yeye kwa kuwapa nyinyi neema zake hizo

    [74] Na Siku ambayo Mwenyezi Mungu Atawaita hawa washirikina Awaambie, «Wako wapi washirika wangu ambao mulikuwa mukidai duniani kwamba wao ni washirika wangu?»

    [75] Na tutamtoa kwenye kila ummah, miongoni mwa ummah zenye kukanusha, shahidi, naye ni Nabii wao, atakayetoa ushahidi juu ya yaliyopita duniani ya ushirikina wao na ukanushaji wao Mitume wao. Tukaziambia ummah hizo zilizokanusha Mitume wake na yale waliyoyaleta kutoka kwa Mwenyezi Mungu, «Leteni hoja yenu juu ya kile mlichomshirikisha nacho Mwenyezi Mungu.» Wakati huo watajua kuwa hoja nzuri ni ya Mwenyezi Mungu juu yao, kuwa haki ni ya Mwenyezi Mungu, na kitawaondokea kile walichokuwa wakimzulia Mola wao kisiwanufaishe hiko, bali kiwadhuru na kiwafikishe kwenye Moto wa Jahanamu

    [76] Hakika Qārūn alikuwa ni miongoni mwa watu wa jamii ya Mūsā, rehema na amani zimshukiye, akakiuka mpaka wake katika kuwa na kiburi na ujabari juu yao. Na tulimpa Qārūn mahazina mengi ya mali, mpaka ikafikia kiwango cha kuwa funguo zake zinawaelemea idadi kubwa ya watu wenye nguvu kuzibeba. Walipomuambia watu wake, «Usifanye kiburi ukawa na gogi la furaha kwa mali uliyonayo. Hakika Mwenyezi Mungu Hawapendi kati ya waja wake wale wenye kiburi ambao hawamshukuru Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kwa kile Alichowapa

    [77] «Na utafute, kwa mali Aliyokupa Mwenyezi Mungu, malipo mema ya Nyumba ya Akhera, kwa kufanyia mambo ya kumtii Mwenyezi Mungu duniani, na usiache fungu lako la duniani la kustarehe humo kwa halali bila kupita kiasi, na uwafanyie watu hisani kwa kuwapa sadaka kama vile Mwenyezi Mungu Alivyokufanyia hisani kwa kukupa mali mengi haya, na usitafute kile Alichokiharamisha Mwenyezi Mungu cha kuwadhulumu watu wako, kwani hakika Mwenyezi Mungu Hawapendi waharibifu, na Atawalipa kwa matendo yao mabaya.»

    [78] Akasema Qārūn kuwaambia watu wake waliomuwaidhia, «Kwa hakika, mahazina haya ya mali nimeyapata kutokana na ujuzi na uwezo.»Kwani Qārūn hajui kwamba Mwenyezi Mungu ameshawaangamiza ummah wengi kabla yake yeye waliokuwa na nguvu zaidi za kushinda na ukusanyaji zaidi wa mali? Na hawataulizwa wahalifu kuhusu dhambi zao, kwa kuwa Mwenyezi Mungu Anazijua, isipokuwa wataulizwa maulizo ya kuwalaumu na kuwasimanga. Na Atawatesa Mwenyezi Mungu kulingana na ujuzi Wake kuhusu wao

    [79] Basi akatoka Qārūn akiwa kwenye pambo lake, akitaka kwa kufanya hivyo kuonyesha ukubwa wake na wingi wa mali yake. Na walipomuona wale wanaotaka pambo la uhai wa kilimwengu walisema, «Tunatamani lau sisi tungalipatiwa mfano wa kile alichopatiwa Qārūn, cha mali, pambo na heshima. Kwa kweli, Qārūn ni mwenye sehemu kubwa ya dunia.»

    [80] Na wakasema, wale waliopewa elimu ya kumjua Mwenyezi Mungu na Sheria Yake na wakijua uhakika wa mambo, kuwaambia wale waliosema, «Tunatamani tuwe na mfano wa kile alichopatiwa Qārūn», «Ole wenu! Muogopeni Mwenyezi Mungu na mumtii. Malipo mema ya Mwenyezi Mungu ni bora, kwa aliyemuamini Yeye na Mitume Wake na akafanya matendo mema, kuliko kile alichopatiwa Qārūn. Na haupokei ushauri huu na akaafikiwa kuufuata na kuufanyia kazi isipokua yule anayepigana jihadi na nafsi yake, anayevumilia katika kumtii Mola wake na anayejiepusha na mambo ya kumuasi

    [81] Basi tukamdidimiza Qārūn pamoja na nyumba yake ndani ya ardhi. Na hakuwa na askari wa kumuokoa badala ya Mwenyezi Mungu, na hakuwa ni mwenye kujikinga na Mwenyezi Mungu yatakapomshukia mateso Yake

    [82] Na wale waliotamani kuwa kama yeye jana yake wakawa wanasema, wakiwa na uchungu, wenye kuzingatia na wenye kuiogopa adhabu isiwashukie, «Hakika Mwenyezi Mungu Anamkunjulia riziki Anayemtaka miongoni mwa waja Wake, na Anambania Anayemtaka miongoni mwao. Lau si Mwenyezi Mungu kutuneemesha kwa kutotuadhibu kwa tulilolisema, Angalitudidimiza sisi ardhini kama Alivyomfanya Fir’awn. Kwani hujui kwamba makafiri hawafaulu, hapa duniani wala Akhera

    [83] Hiyo ndiyo Nyumba ya Akhera. Tumewapatia, ile starehe yake, wale ambao hawataki kuifanyia kiburi haki hapa duniani wala kufanya uharibifu humo. Na mwisho wenye kushukuriwa, nayo ni pepo, ni wa yule aliyejikinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu na akafanya mema na akaacha mambo yaliyoharamishwa

    [84] Mwenye kuja, Siku ya Kiyama, na utakasaji wa Mwenyezi Mungu Mmoja na matendo mema yanayolingana na Sheria ya Mwenyezi Mungu, basi yeye atakuwa na malipo makubwa yenye kheri zaidi kuliko kile alichokifanya. Na kheri hiyo ni Pepo na starehe ya daima. Na mwenye kuja na matendo mabaya, hawatalipwa hao waliofanya maovu kwa matendo yao, isipokuwa yale waliokuwa wakiyafanya

    [85] Hakika Yule Aliyekuteremshia wewe, Qur’ani, ewe Mtume, na akakulazimisha wewe uifikishe na ushikamane nayo, ni Mwenye kukurudisha kule ulikotoka, nako ni Makkah. Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Mola wangu Anamjua zaidi yule aliyeleta uongofu na yule ambaye ameenda nje ya haki waziwazi.»

    [86] Na hukuwa ukitarajia, ewe Mtume, kuteremkiwa na Qur’ani, lakini Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Alikurehemu Akakuteremshia. Basi mshukuru Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kwa neema Zake, na usiwe ni mwenye kuwasaidia watu wa ushirikina na upotevu

    [87] Na wasikuepushe wewe washirikina hawa na ufikishaji aya za Mola wako na hoja Zake baada ya kuwa Amekuteremshia kwako, na ufikishe ujumbe wa Mola wako, na usiwe ni miongoni mwa washirikina katika kitu chochote

    [88] Wala usiabudu, pamoja na Mwenyezi Mungu, muabudiwa mwingine. Hapana muabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu. Kila kitu ni chenye kuangamia na kutoeka isipokuwa uso Wake. Uamuzi ni Wake. Na Kwake Yeye mutarudishwa baada ya kufa kwenu ili muhesabiwe na mulipwe. Katika aya hii kuna kuthibitisha sifa ya uso wa Mwenyezi Mungu, aliyetukuka, kama inavyonasibiana na ukamilifu Wake, ukubwa Wake na utukufu Wake

    Buibui

    Surah 29

    [1] «Alif, Lām, Mīm.» Yametangulia maelezo juu ya herufi zilizokatwa na kutengwa mwanzo wa sura ya Al-Baqarah

    [2] Je wanadhani watu kwamba wakisema «Tumeamini» Mwenyezi Mungu Atawaachilia bila ya kuwajaribu wala kuwatahini

    [3] Kwa hakika, tuliwajaribu wale waliokuwa kabla yao miongoni mwa ummah mbalimbali na tukawatahini kwa Mitume wetu tuliowatumiliza kwao. Basi hakika ni kwamba Mwenyezi Mungu Atawajua, ujuzi wa kujitokeza nje kwa viumbe, ukweli wa wale wakweli katika Imani yao na urongo wa warongo, ili Alipambanue kila kundi na lingine

    [4] Je, kwani wanadhani wale wanaofanya mambo ya uasi, ya ushirikina na mengineyo, kuwa watatushinda wajikwepeshe na sisi tusiwaweze? Ni uamuzi mbaya mno wanaouamua

    [5] Yoyote mwenye kuwa na matumaini ya kukutana na Mwenyezi Mungu na akawa na matarajio ya kupata malipo Yake mema, basi muda Aliouweka Mwenyezi Mungu wa kuwafufua viumbe Wake ili wahesabiwe na walipwe ni wenye kuja hivi karibuni. Na Yeye Ndiye Msikizi wa maneno, Mjuzi wa vitendo

    [6] Na mwenye kupigana jihadi katika njia ya kuinua neno la Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, na akapigana jihadi na nafsi yake kwa kuisukuma ifanye vitendo vya utiifu, basi anapigana jihadi kwa maslahi ya nafsi yake. Kwa kuwa yeye anafanya hilo kwa kutaka thawabu ya kupigana kwake jihadi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Hana haja ya matendo mema ya waja Wake, kwani mamlaka ni Yake, uumba na mapitisho

    [7] Na wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafanya matendo mema, kwa hakika tutawafutia makosa yao na tutawalipa kwa matendo yao mema, mazuri zaidi ya yale waliokuwa wakiyafanya

    [8] Na tumemsihi binadamu awatendee wema wazazi wake wawili na awe mwema kwao wa maneno na vitendo. Na wakikusukuma kwa bidii, ewe binadamu, umshirikishe mwingine na mimi katika ibada yangu, basi usifuate amri yao. Matakwa ya kuwa Mwenyezi Mungu ashirikishwe yanashikanishwa na matakwa ya kuwa vitendo vingine vya maasia vifanywe. Kwani hakuna kutiiwa kiumbe namna atakavyokuwa katika jambo la kumuasi Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kama lilivyothibiti hilo kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye. Kwangu mimi ndio mwisho wenu, Siku ya Kiyama, na huko niwape habari ya matendo mema na mabaya ambayo mlikuwa mkiyafanya duniani na niwalipe kwa hayo

    [9] Na wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wakafanya matendo mema, tutawatia Peponi wakiwa ni katika jumla ya waja wa Mwenyezi Mungu wema

    [10] Na miongoni mwa watu, kuna anayesema, «Tumemuamini Mwenyezi Mungu.» Na afanyiwapo udhia na washirikina huwa akipapatika kutokana na mateso yao na makero yao, kama anavyopapatika kutokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu na asivumilie makero yake, akaritadi na akaiacha Imani yake. Na lau waja ushindi kutoka kwa Mola wako, ewe Mtume, kwa watu wenye kumuamini, watasema hawa wenye kuritadi kuiacha Imani yao, «Sisi tulikuwa pamoja na nyinyi, enyi Waumini, tukiwasaidia dhidi ya maadui wenu.» Je, si Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi kuliko yoyote wa kuyajua yaliyomo ndani ya vifua vya viumbe wake wote

    [11] Na Atawajua Mwenyezi Mungu, tena atawajua, ujuzi wenye kujitokeza kwa viumbe, wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakazifuata Sheria Zake kivitendo, na Atawajua, tena Atawajua, wanafiki, ili Alipambanue kila kundi na lingine

    [12] Na wanasema wale waliokataa upweke wa Mwenyezi Mungu miongoni mwa Makureshi, na wasiliamini onyo la Mwenyezi Mungu na ahadi Yake, kuwaambia wale waliomuamini Mwenyezi Mungu miongoni mwao na wakafuata Sharia Zake kivitendo, «Iacheni Dini ya Muhammad, na fuateni dini yetu, kwani sisi tutayabeba makosa yenu,» na wao si wenye kubeba chochote katika dhambi zao. Kwa kweli, wao ni warongo kwa yale waliyoyanena

    [13] Na wataibeba, tena wataibeba, washirikina hawa mizigo ya nafsi zao na madhambi yake na mizigo ya wale waliowapoteza na wakawazuia wasiifuate njia ya Mwenyezi Mungu pamoja na mizigo yao wenyewe, bila ya wale waliowafuata nyinyi kupunguziwa mizigo yao kitu chochote. Na wataulizwa, tena wataulizwa, Siku ya Kiyama, kuhusu yale ya urongo waliokuwa wakiyazua

    [14] Na hakika tulimtumiliza Nūḥ kwa watu wake, akakaa kwao miaka elfu moja kasoro miaka hamsini, akiwaita kwenye upwekeshaji wa Mwenyezi Mungu na akiwakataza ushirikina, na wao wasimuitikie. Mwenyezi Mungu Akawaangamiza kwa mafuriko, na wao wako katika hali ya kujidhulumu wenyewe kwa ukafiri wao na kupita kiasi kwao katika uasi

    [15] Hivyo basi tukamuokoa Nūḥ na waliomfuata miongoni mwa wale waliokuwa naye jahazini. Na tukalifanya hilo kuwa ni mazingatio na mawaidha kwa viumbe wote

    [16] Mkumbuke na umtaje, ewe Mtume, Ibrāhīm, amani imshukie, alipowalingania watu wake kwamba: mtakasieni Ibada Mwenyezi Mungu Peke Yake, na muogope hasira Zake kwa kutekeleza faradhi Zake na kujiepusha na vitendo vya kumuasi. Hilo ni bora kwenu ikiwa mnakijua kilicho chema kwenu kutokana na kilicho kibaya kwenu

    [17] Hamuabudu, enyi watu, badala ya Mwenyezi Mungu isipokuwa masanamu na mnazua urongo kwa kuwaita wao waungu. Kwa hakika, hawa masanamu wenu mnaoaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, hawawezi kuwaruzuku nyinyi kitu chochote, basi tafuteni riziki kwa Mwenyezi Mungu na sio kwa masanamu wenu na mumtakasie ibada na shukrani kwa kuwaruzuku. Ni kwa Mwenyezi Mungu mtarudishwa baada ya kufa kwenu, na hapo awalipe kwa yale ambayo mlifanya

    [18] Na mkimkanusha, enyi watu, Mtume wetu Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, katika kile alichowalingania mkifuate cha kumuabudu Mwenyezi Mungu Peke Yake, basi kuna makundi ya watu kabla yenu waliowakanusha Mitume wao katika kile walichowaitia, na kwa hivyo zikawashukia hasira za Mwenyezi Mungu. Na Mtume Muhammad hana jukumu lingine isipokuwa ni kuwafikishia nyinyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu ujumbe Wake ufikishaji wenye uwazi, na ashafanya hilo

    [19] Kwani hawa hawajui ni vipi Mwenyezi Mungu Anaanzisha uumbaji viumbe kutoka katika hali ya kutokuwako, kisha Atawarudisha baada ya kutoweka kwao, kama alivyoanzisha mara ya kwanza uumbaji mpya na kwamba kulifanya hili si jambo lisilowezekana na Yeye? Hakika hilo kwa Mwenyezi Mungu ni lepesi kama lilivyokuwa lepesi lile la kuanzisha uumbaji wake

    [20] Sema, ewe Mtume, kuwaambia wenye kukanusha kufufuliwa baada ya kufa, «Endeni katika ardhi, muangalie namna Mwenyezi Mungu Alivyoanzisha uumbaji na Asielemewe kuuanzisha hapo mwanzo?» Hivyo basi Hataelemewa na kule kuuanzilisha upya uanzilishaji mwingine. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu, hakuna jambo lolote Alitakalo linalomshinda

    [21] Anamuadhibu Anayemtaka kati ya viumbe Vyake kwa makosa waliyoyafanya siku za uhai wao, na Anawarehemu Anaowataka miongoni mwao, kati ya wale waliotubia, wakaamini na wakafanya matendo mema. Na Kwake Yeye mtarejeshwa muhesabiwe na mulipwe kwa mliyoyafanya

    [22] Na hamkuwa nyinyi, enyi watu, ni wenye kumshinda Mwenyezi Mungu katika ardhi wala katika mbingu iwapo mtamuasi. Na nyinyi hamuna badala ya Mwenyezi Mungu mtegemewa yoyote wa kuyasimamia mambo yenu, wala msaidizi wa kuwaokoa nyinyi na Mwenyezi Mungu iwapo Anawatakia mabaya

    [23] Na wenye kukanusha hoja za Mwenyezi Mungu na kupinga dalili Zake, hao hawatakuwa na matarajio ya rehema yangu huko Akhera watakapoishuhudia adhabu iliyoandaliwa kwao, na wao watakuwa na adhabu yenye uchungu na iumizayo

    [24] Basi jawabu ya watu wa Ibrāhīm haikuwa isipokuwa ni kuambiana wao kwa wao, «Muueni au mchomeni kwa moto!» Wakamtupa motoni, na Mwenyezi Mungu Akamuokoa nao, na akaufanya kuwa ni baridi na salama kwake. Hakika katika kumuokoa kwetu Ibrāhīm kutokana na moto pana dalili na hoja kwa watu wanaomuamini Mwenyezi Mungu na kufanya matendo yanayoambatana na Sheria Yake

    [25] Na Akasema Ibrāhīm kuwaambia watu wake, «Enyi watu wangu! Kwa hakika, nyinyi mumewaabudu waungu wa ubatilifu, mumewafanya wao ni waabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu, mnapendana juu ya kuwaabudu na mnajipendekeza kwa kuwatumikia. Kisha, Siku ya Kiyama, baadhi yenu watajiepusha na wengine na mtalaaniana nyinyi kwa nyinyi, na mwisho wenu ni Moto, na hamtakuwa na msaidizi wa kuwazuia kuuingia

    [26] Lūṭ akamuamini Ibrāhīm na akaufuata mwenendo wake. Na Ibrāhīm akasema, «Mimi nitaiwacha nchi ya watu wangu na nitaenda kwenye ardhi iliyobarikiwa, nayo ni Shām, kwani Mwenyezi Mungu ni Mshindi Asiyeshindwa ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji mambo Wake

    [27] Na tukamtunukia yeye Isḥāq, mtoto wake, na Y'qub, mtoto wa mtoto wake. Na tukawafanya, katika kizazi chake, Mitume na tukawaletea Vitabu. Na tukampa yeye malipo mema ya mitihani aliyoipata kwa ajili yetu, nayo ni kutajwa vizuri na kuwa na wana wema duniani. Na kwa hakika, yeye huko Akhera ni miongoni mwa watu wema

    [28] Mkumbuke na umtaje Lūṭ, ewe Mtume, alipowaambia watu wake, «Kwa hakika, nyinyi mnaleta kitendo kichafu, hakuna yoyote katika viumbe aliyetangulia kukifanya

    [29] Je, ni vipi nyinyi mnawajilia wanaume kupitia sehemu zao za nyuma, mnavamia njia za wasafiri kwa kitendo chenu kiovu na mnafanya vitendo vibaya kwenye mabaraza yenu, kama vile kuwacheza shere watu, kuwarushia mawe wapita njia na kuwakera kwa maneno na vitendo kwa namna isiyofaa?» Katika haya kuna tangazo kwamba haifai watu kukusanyika juu ya jambo baya ambalo Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wamelikataza. Watu wa Lūṭ hawakuwa na jawabu la kumpa isipokuwa ni kusema, «tuletee adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwa wewe ni miongoni mwa wakweli katika hayo unayoyasema na ni miongoni mwa watekelezaji katika ahadi unayoitoa.»

    [30] Akasema, «Mola wangu! Nipe ushindi juu ya watu waharibifu kwa kuwateremshia adhabu, kwa kuwa wameuzua uchafu huu na wameendelea nao» Na Mwenyezi Mungu Akaikubali dua yake

    [31] Na Malaika walipomjia Ibrāhīm na habari ya furaha itokayo kwa Mwenyezi Mungu ya (kuzaliwa) Isḥāq, na nyuma ya Isḥāq ni mwanawe, Ya’qūb, walisema wale Malaika, «Sisi ni wenye kuwaangamiza watu wa kijiji cha watu wa Lūṭ, nacho ni Sadūm, kwa kuwa watu wake wamekuwa ni wenye kujidhulumu wenyewe kwa kumuasi Mwenyezi Mungu.»

    [32] Akasema Ibrāhīm kuwaambia Malaika, «Huko kuna Lūṭ, na yeye si miongoni mwa madhalimu.» Malaika wakasema, «Sisi tunamjua zaidi aliye huko. Tutamuokoa, yeye na watu wa nyumbani kwake, na maangamivu yatakayowashukia watu wa kijiji chake, isipokuwa mke wake atakayesalia kwenye maangamivu

    [33] Na Malaika walipomjia Lūṭ, hilo lilimkera, kwa kuwa yeye aliwadhania ni wageni wanadamu na akaingiwa na masikitiko kwa kuwako kwao kwa kuwa ajua ubaya wa kitendo cha watu wake, na wao wakamwambia, «Usituogopee, kwani watu wako hawatatufikia. Na wala usiwe na masikitiko kwa kuwa tunakupasha habari kuwa sisi ni wenye kuwaangamiza wao. Sisi ni wenye kukuokoa wewe na hiyo adhabu itakayowashukia watu wako na ni wenye kuwaokoa watu wa nyumbani kwako pamoja nawe isipokuwa mke wako, kwani yeye ni mwenye kuangamia akiwa na wale wenye kuangamia katika watu wake

    [34] «Sisi ni wenye kuwateremshia watu wa kijiji hiki adhabu kutoka mbinguni kwa sababu ya kumuasi kwao Mwenyezi Mungu na kufanya kwao machafu.»

    [35] Na tulizibakisha, katika nyumba za watu wa Lūṭ, athari zilizo wazi kwa watu wanaoelewa mambo ya kuwapa mazingatio na kunufaika kwayo

    [36] Na tulimtumiliza, kwa watu wa Madyan, ndugu yao, Shu'ayb. Akawaambia, «Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu Peke Yake, na mumtakasie Ibada, kwani nyinyi hamuna Mola isipokuwa Yeye. Na kuweni na matarajio mema, kwa ibada mnazofanya, kupata malipo mazuri ya Siku ya Akhera, na msifanye uharibifu na maasia kwa wingi, na msijikite juu ya hayo. Lakini tubieni kwa Mwenyezi Mungu kwa makosa hayo na mrudi Kwake

    [37] Wakamkanusha Shu'ayb watu wa Madyan kwa yale aliyokuja nayo ya utume kutoka kwa Mweyezi Mungu, basi wakapatikana na msukosuko mkali, wakawa wamelala chini kwenye nyumba zao hali ya kuwa wameangamia

    [38] Na tukawaangamiza kina 'Ād na Thamūd, na yameshaonekana na nyinyi magofu ya nyumba zao, vile yalivyokuwa matupu, hayana mtu yoyote katika wakazi wake, na vile mateso yetu yalivyowashukia wao wote. Na Shetani aliwapambia wao matendo yao maovu, na kwa hivyo akawazuia wasiifuate njia ya Mwenyezi Mungu na njia ya kumuamini Yeye na Mitume Wake, na walikuwa wakijiongoza kuona njia katika ukafiri wao na upotevu wao wakijifurahisha nayo, wakidhani kwamba wao wako kwenye uongofu na usawa, ilhali wao wamezama kwenye upotevu

    [39] Na tulimuangamiza Qārūn, Fir'awn na Hāmān. Na wote hao Mūsā aliwajia na dalili waziwazi, wakajifanya wakubwa katika ardhi na wakafanya kiburi humo. Na hawakuwa wao ni wenye kutuponyoka, bali sisi tulikuwa tuna uweza juu yao

    [40] Kila mmoja, kati ya hao waliotajwa, tulimkamata kwa dhambi zake: kati yao kuna wale tuliyowatumia mawe ya udongo ulioshikana, nao ni watu wa Lūṭ, na kati yao kuna waliopatwa na ukelele, nao ni watu wa Ṣāliḥ na watu wa Shu'ayb , na kati yao kuna tuliowadidimiza ardhini kama vile Qārūn, na katika wao kuna tuliowazamisha majini, nao ni watu wa Nūḥ na Fir'awn na jamaa zake. Na Mwenyezi Mungu hakuwa ni Mwenye kuwaangamiza hawa kwa dhambi wengine akawa ni mwenye kuwadhulumu kwa kuwaangamiza wao bila kustahili, lakini wao walikuwa wakijidhulumu wenyewe kwa kujistarehesha kwa neema za Mola wao na kumuabudu asiyekuwa Yeye

    [41] Mfano wa wale waliowafanya masanamu ni wategemewa badala ya Mwenyezi Mungu, wakawa wanatarajia msaada wao, ni kama mfano wa buibui aliyejitengenezea nyumba ili imuhifadhi, isimfalie kitu alipokuwa na haja nayo. Hivyo basi ndivyo walivyo hawa washirikina, hawakuwafalia kitu wale waliowachukuwa kuwa ni wasaidizi wao badala ya Mwenyezi Mungu. Na kwa hakika, nyumba iliyo dhaifu zaidi ni nyumba ya buibui, na lau wao wangalikuwa wakilijua hilo hawangaliwafanya wao ni wasaidizi wenye kutegemewa badala ya Mwenyezi Mungu, kwani wao hawawanufaishi wala hawawadhuru

    [42] Hakika Mwenyezi Mungu Anavijua vile wanavyomfananisha navyo washirikina na kumshirikisha navyo, na kwamba hivyo , kwa hakika, si kitu chochote, bali ni majina tu waliyoyaita, havinufaishi wala havidhuru. Na Yeye Ndiye Mshindi Mwenye uweza wa kuwatesa waliomkufuru, Ndiye Mwenye hekima katika uendeshaji mambo Wake na utengenezaji Wake

    [43] Na mifano hii tunawapigia watu , ili wanufaike nayo na wajifunze kwayo. Na hawaielewi isipokuwa wale wanaomjua Mwenyezi Mungu na kuzijua aya Zake na Sheria Zake

    [44] Mwenyezi Mungu Ameumba mbingu na ardhi kwa uadilifu na usawa. Hakika katika uumbaji Wake huo kuna ushahidi mkubwa, kwa wanaoamini, wa uweza Wake na kupwekeka kwake kwa uungu. Na Amewahusu Waumini kwa kuwataja kwa kuwa wao ndio wanaonufaika na huo ushahidi

    [45] Isome hii Qur’ani iliyoteremshwa kwako, na uifuate kivitendo, na utekeleze Swala kwa mipaka yake, kwani utunzaji wa Swala unamkataza mtu kuingia kwenye vitendo vya uasi na makatazo. Hivyo ni kwamba mwenye kuzitimiza nguzo zake na masharti yake, moyo wake unang’ara, Imani yake inazidi, hima yake ya kufanya mema inapata nguvu na matamanio yake ya kufanya mabaya yanapungua au yanaondoka. Na kwa hakika, kumtaja Mwenyezi Mungu katika Swala na isiyokuwa Swala ni jambo kubwa na bora kuliko kitu chochote. Na Mwenyezi Mungu Anayajua mnayoyatenda ya uzuri na ubaya, hivyo basi Atawalipa kwa hayo malipo makamilifu zaidi na yanayotosha zaidi

    [46] Na wala msijadiliane, enyi Waumini, na Mayahudi na Wanaswara isipokuwa kwa njia nzuri na maneno mazuri na kulingania kwenye haki kwa njia sahali yenye kupelekea kwenye lengo hilo, isipokuwa wale ambao wamekaa kando na haki wakafanya ushindani na kiburi na wakatangaza vita juu yenu, basi hao piganeni nao kwa upanga mpaka waamini au watoe jizia (kodi maalumu) kwa mkono na wao wakiwa katika hali ya unyonge. Na semeni, «Tumeiamini Qur’ani iliyoteremshwa kwetu, na tumeiamini Taurati na Injili ambazo mliteremshiwa, na Mola wetu na Mola wenu ni Mmoja Hana mshirika Wake katika uungu Wake, wala katika sifa Yake ya kuwa ni Mola, wala majina Yake na sifa Zake. Na sisi ni wenye kunyenyekea na kujifanya wanyonge Kwake kwa kumtii katika yale Aliyotuamrisha na Aliyotukataza

    [47] Na kama tulivyowateremshia Kitabu, ewe Mtume, wale Mitume waliokuwa kabla yako, vilevile tumekuteremshia Kitabu hiki chenye kusadikisha Vitabu vilivyotangulia. Basi wale tuliyowapa Kitabu miongoni mwa Wana wa Isrāīl wakamjua vile inavyotakikana wamjue, wanaiamini Qur’ani. Na kati ya hawa Warabu wa Kikureshi kuna wanaomuamini. Na hawaikanushi Qur’ani au kuzifanyia shaka dalili zake na hoja zake zenye ushahidi uliyo wazi isipokuwa makafiri ambao mienendo yao ni kukataa na kufanya ushindani

    [48] Na miongoni mwa miujiza yako iliyo wazi, ewe Mtume, ni kuwa wewe hukusoma kitabu wala hukuandika herufi zozote kwa mkono wako wa kulia kabla ya hii Qur’ani kukuteremkia, na hali wao wanalijua hilo. Na lau ungalikuwa ni mwenye kusoma au kuandika kabla hujaletewa wahyi wangalilifanyia shaka hilo hao wapotofu na wangalisema, «Amejifunza hiyo (Qur’ani) au ameinakili kutoka kwenye vitabu vilivyotangulia.»

    [49] Lakini Qur’ani ni aya zilizofunuka zilizo wazi katika kuutolea ushahidi ukweli, wanavyuoni wanaihifadhi. Na hawazikanushi aya zetu na kuzikataa isipokuwa washindani wanaoijua haki na kuiepuka

    [50] Na washirikina walisema, «Si ateremshiwe Muammad dalili na hoja kutoka kwa Mola wake, kama vile ngamia wa Ṣāliḥ na fimbo ya Mūsā!» Waambie, «Jambo la miujiza hii liko kwa Mwenyezi Mungu, Akitaka Ataiteremsha na Akitaka Ataizuia. Na hakika ni kwamba mimi ni muonyaji, ninawatahadharisha na ukali wa adhabu Yake na mateso Yake, na ni mwenye kuwaonyesha njia ya haki na batili.»

    [51] Kwani haikuwatosha washirikina hawa ili wajue ukweli wako, ewe Mtume, kuwa sisi tumekuteremshia Qur’ani inayosomwa kwao? Hakika katika hii Qur’ani kuna rehema kwa Waumini, ulimwenguni na Akhera, na kuna ukumbusho wa kujikumbusha nao wa mazingatio na mawaidha

    [52] Sema, «Inatosha kuwa Mwenyezi Mungu ni Shahidi baina yangu mimi na nyinyi juu ya ukweli wangu wa kuwa mimi ni Mtume Wake, na juu ya kunikanusha kwenu mimi na kuirudisha kwenu haki niliyokuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Anavijuwa vilivyomo mbinguni na ardhini», hakuna kinachofichamana na Yeye chochote kile kilichoko ndani ya hivyo viwili. Na wale waliouamini urongo na wakamkanusha Mwenyezi Mungu, pamoja na kuwepo dalili hizi zilizo wazi, hao ndiyo wenye hasara ulimwenguni na Akhera

    [53] Na wanakuharakisha, ewe Mtume, hawa washirikina wa watu wako uwaletee adhabu kwa kukufanyia shere. Na lau si Mwenyezi Mungu kuwa Amewawekea wakati wa kuadhibiwa wao duniani usiotangulia wala kuchelewa, ingaliwajia wao adhabu pale walipoitaka. Na kwa hakika itawajia ghafula na hali wao hawaitambui wala kuihisi

    [54] Wanakuharakisha uwaletee adhabu ulimwenguni, na hali hiyo ni yenye kuwajia hapana budi, ima hapa ulimwenguni au huko Akhera. Na kwa hakika adhabu ya Jahanamu huko Akhera ni yenye kuwazunguka, hawana makimbilio nayo

    [55] Hiyo Siku ya Kiyama, adhabu ya Jahanamu itawafinika makafiri upande wa juu ya vichwa vyao na upande wa chini ya nyayo zao. Hivyo basi Moto utawazunguka pande zao zote, na Mwenyezi Mungu Atasema kuwaambia wakati huo, «Onjeni malipo ya yale mliokuwa mkiyafanya ulimwenguni, ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kufanya uhalifu na madhambi

    [56] «Enyi waja wangu mlioamini! Iwapo muna shida ya kudhihirisha Imani na ibada ya Mwenyezi Mungu Peke Yake, basi hamieni kwenye ardhi ya Mwenyezi Mungu iliyo kunjufu na munitakasie ibada mimi peke yangu.»

    [57] Kila nafsi iliyo hai ni yenye kuonja kifo, kisha kwetu sisi mtarejea muhesabiwe na mulipwe

    [58] Na wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafanya matendo mema waliyoamrishwa kwayo, tutawatayarishia katika Pepo vyumba vilivyo juu, ambavyo chini yake inapita mito, hali ya kukaa humo milele.Neema ya malipo ya wenye kufanya utiifu kwa Mwenyezi Mungu ni Vyumba hivi vilivyoko ndani ya Mabustani ya starehe

    [59] Mabustani hayo yaliyotajwa ni ya Waumini waliovumilia katika kumuabudu Mwenyezi Mungu, wakashikamana na dini yao na wakawa wanamtegemea Mwenyezi Mungu katika riziki zao na kupigana jihadi na maadui wao

    [60] Ni viumbe vingapi vitambaavyo visivyojiwekea akiba ya chakula chao cha kesho, kama vile mwanadamu anavyofanya. Basi Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kuwa juu, Anaviruzuku kama Anavyowaruzuku nyinyi. Na Yeye ni Msikizi wa maneno yenu, ni Mjuzi wa vitendo vyenu na mawazo ya nyoyo zenu

    [61] Na ukiwauliza, ewe Mtume, hao washirikina,»Ni nani aliyeumba mbingu na ardhi kwa mpango huu mzuri na akalidhalilisha jua na mwezi?» Watasema, «Aliyeviumba hivyo ni Mwenyezi Mungu Peke Yake.» Basi vipi wao watapotoshwa waache kumuamini Mwenyezi Mungu, Muumba na Muendeshaji wa kila kitu, na wakawa wanamuabudu asiyekuwa Yeye? Basi uonee ajabu uzushi wao na urongo wao

    [62] Mwenyezi Mungu, aliyetakasika na kuwa juu, Anampanulia riziki Anayemtaka na Anawabania wengine katika wao, kwa kuwa Anayajua yanayowafaa waja Wake. Hakika Mwenyezi Mungu kwa kila jambo, katika hali zenu na mambo yenu, ni Mjuzi, hakuna chochote kinachofichamana Kwake

    [63] Na ukiwauliza, ewe Mtume, hao washirikina, «Ni nani anayeteremsha maji kutoka mawinguni, yakaotesha mimea juu ya ardhi baada ya kuwa imekauka?» watakwambia huku wakikubali, «Mwenyezi Mungu Peke Yake Ndiye Anayeyateremsha hayo.» Sema, «Shukrani ni za Mwenyezi Mungu Aliyedhihirisha hoja yako kwao. Lakini wengi wao hawafahamu yanayowafaa wala yanayowadhuru, na lau waelewa hawangalimshirikisha Mwenyezi Mungu na Mwengine

    [64] Na haukuwa uhai huu wa ulimwengu isipokuwa ni pumbao na mchezo wa kuzifanya nyoyo zipumbae na miili icheza, kwa sababu ya pambo na matamanio, kisha yanaondoka haraka. Na kwa hakika, nyumba ya Akhera ndiyo uhai wa kikweli na wa daima usikokuwa na kifo ndani yake. Lau watu wanalijua hilo hawangalifadhilisha nyumba ya kutoweka juu ya Nyumba ya kusalia

    [65] Na wanapopanda makafiri kwenye majahazi baharini, na wakaogopa kuzama, wanampwekesha Mwenyezi Mungu na kumtakasia dua wakati wa shida yao. Na Anapowaokoa akawafikisha kwenye nchi kavu, na shida ikawaondokea, wanarudi kwenye ushirikina wao. Hakika yao wao, kwa kufanya hivi, wanagongana, wanampwekesha Mwenyezi Mungu kipindi cha shida na wanamshirikisha kipindi cha raha

    [66] Na kushirikisha kwao baada ya sisi kuwaneemesha kwa kuwaokoa na bahari, ni ili iwe mwisho wake ni kuzikanusha zile tulizowaneemesha katika nafsi zao na mali zao na ili wakamilishe kujistarehesha kwao katika hii dunia. Basi wataujua uharibikaji wa matendo yao na kile Alichowaandalia wao Mwenyezi Mungu cha adhabu kali Siku ya Kiyama. Na katika hilo pana onyo na tahadharisho kwao

    [67] Kwani hawakushuhudia makafiri wa Makkah kwamba Mwenyezi Mungu Amewawekea Makkah kuwa ni mahali patakatifu penye amani, watu wake wanapata amani humo ya nafsi zao na mali zao, hali watu walio pambizoni mwake, nje ya eneo takatifu, wananyakuliwa hawana amani? Je, ni ushirikina wanaouamini na ni neema ya Mwenyezi Mungu Aliyowahusu wao nayo, wanayoikanusha, wakawa hawamuabudu Yeye, Peke Yake, bila mwingine

    [68] Hakuna yoyote aliye na udhalimu mkubwa kuliko yule aliyemkanusha Mwenyezi Mungu na akamnasibishia Mwenyezi Mungu upotevu alio nao na ubatilifu, au akaikanusha haki ambayo Mwenyezi Mungu Amemleta nayo Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie. Hakika ndani ya Moto ni makao ya aliyemkanusha Mwenyezi Mungu na akaukataa upweke Wake na akamkanusha Mtume Wake Muhammad,rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [69] Na Waumini waliopigana jihadi na maadui wa Mwenyezi Mungu, nafsi na Shetani na wakavumilia kwenye misukosuko na makero katika njia ya Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu Atawaongoa kwenye wema na kuwasimamisha imara juu ya njia iliyolingana sawa. Na yoyote ambaye sifa yake ni hii, basi yeye amejifanyia wema nafsi yake na amewafanyia wema wengine. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kuwa juu, Yupo pamoja na wale viumbe wake waliofanya wema, kwa kuwapa ushindi, kuwatilia nguvu, kuwahifadhi na kuwaongoza

    Warumi

    Surah 30

    [1] «Alif, Lām, Mīm» Yametangulia maelezo kuhusu herufi zilizokatwa- katwa na kutengwa mwanzo wa sura ya Al-Baqarah

    [2] Wafursi waliwashinda Warumi

    [3] katika sehemu za karibu za ardhi ya Shamu kuelekea Uajemi. Na Warumi watawashinda Wafursi

    [4] katika kipindi kisichopita miaka kumi na kisichopungua miaka mitatu. Ni ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, amri yote kabla ya ushindi wa Warumi na baada yake. Na siku hiyo ambayo Warumi watapata ushindi juu ya Wafursi Waumini wataifurahia nusura ya Mwenyezi Mungu kwa Warumi juu ya Wafursi

    [5] Na Mwenyezi Mungu, Kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Anamsaidia Anayemtaka na Anaacha kumsaidia Anayemtaka. Na Yeye Ndiye Mshindi Ambaye hakuna wa kushindana naye, Ndiye Mwenye kumrehemu Anayemtaka miongoni mwa viumbe Vyake. Na hilo lilithibitika, na Warumi waliwashinda Wafursi baada ya miaka saba, na Waislamu wakafurahi kwa hilo, kwa kuwa Warumi walikuwa ni watu wa Kitabu ingawa wamekipotosha

    [6] Mwenyezi Mungu Amewaahidi Waumini, ahadi ya kukata isiyoenda kinyume, kuwapa ushindi Warumi juu ya Wafursi wenye kuabudu masanamu. Lakini wengi wa makafiri wa Makkah hawajui kwamba kile Alichokiahidi Mwenyezi Mungu ni kweli

    [7] Wanayoyajua wao ni mambo yaliyofunuka wazi ya dunia na pambo lake, na wao kuhusu mambo ya Akhera na yale yanayowafaa huko wameghafilika, hawayafikirii

    [8] Kwani hawakufikiri, hawa wakanushaji Mitume wa Mwenyezi Mungu na kukutana na Yeye, vile Mwenyezi Mungu Alivyowaumba, na kuwa wao Amewaumba na hawakuwa kitu chochote? Mwenyezi Mungu hakuumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake isipokuwa ni kwa ajili ya kusimamisha uadilifu, malipo mema na mateso na kutolea ushahidi upweke Wake na uweza Wake. Na kwa muda uliotajwa wa kukomea kwake nao ni Siku ya Kiyama. Na kwa hakika, wengi wa watu ni wenye kukataa na kukanusha kwa ujinga wao wa kutojua kuwa marejeo yao ni kwa Mwenyezi Mungu baada ya kutoweka kwao na kwa kughafilika kwao na Akhera

    [9] Basi si waende hawa wanaomkanusha Mwenyezi Mungu, wanaoghafilika na Akhera, mwendo wa kufikiria na kuzingatia, wakapata kuona yalikuwa namna gani malipo ya ummah waliowakanusha Mitume wa Mwenyezi Mungu, kama vile kina ‘Ād na Thamūd? Hakika walikuwa wana nguvu zaidi kuliko wao kimiili na wana uwezo zaidi wa kustarehe na maisha, kwa kuwa waliilima ardhi na kuipanda mimea, na wakajenga majumba ya fahari na wakayakalia, hivyo basi waliuamirisha ulimwengu wao kuliko vile watu wa Makkah walivyouamirisha ulimwengu wao, na kusiwafalie kitu kule kuamirisha kwao wala urefu wa maisha yao. Na Mitume wao waliwajia na hoja waziwazi na dalili zenye kung’ara, wakawakanusha na Mwenyezi Mungu Akawaangamiza. Na Hakuwadhulumu kwa huko kuwaangamiza, isipokuwa wao wenyewe walijidhulumu wenyewe kwa kufanya ushirikina na kuasi

    [10] Kisha ulikuwa mwisho wa waovu, miongoni mwa madhalimu na makafiri, ni mbaya zaidi na muovu zaidi, kwa kumkanusha kwao Mwenyezi Mungu na kuzifanyia shere aya Zake ambazo Aliziteremsha kwa Mitume Wake

    [11] Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Ndiye Aliyepwekeka kwa kuanzisha uumbaji viumbe vyote. Na Yeye Ndiye Anayeweza, Peke Yake, kuvirudisha mara nyingine, kisha Kwake Yeye watarejea viumbe wote, Amlipe aliye mwema kwa wema wake na aliye mbaya kwa ubaya wake

    [12] Na Siku ambayo Kiyama kitasimama wahalifu watakata tamaa ya kuokoka na adhabu, na utawapata wao mshangao utakaokata hoja zao

    [13] Na washirikina , Siku hiyo, hawatokuwa na waombezi kati ya waungu wao waliokuwa wakiwaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, bali wao, hao waungu, watajiepusha nao na wao watajiepusha nao. Maombezi ni ya Mwenyezi Mungu Peke Yake, na hayatafutwi kutoka kwa mwingine

    [14] Na Siku ambayo Kiyama kitasimama, watatengana watu wa Imani na watu wa ukafiri

    [15] Ama waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, wenye kufanya matendo mema, watakuwa Peponi ambapo watakirimiwa, watafurahishwa na wataneemeshwa

    [16] Na ama wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu na wakayakanusha yale waliyokuja nayo Mitume na wakakanusha kufufuliwa baada ya kufa, basi hao watakaa adhabuni, ikiwa ni malipo ya kile walichokikanusha ulimwenguni

    [17] Basi, enyi waumini, Mtakaseni Mwenyezi Mungu na mumuepushe na mshirika, mke na mtoto, na msifuni kwa sifa za ukamilifu kwa ndimi zenu, na mlithibitishe hilo kwa viungo vyenu vyote muingiliwapo na wakati wa jioni, na muingiliwapo na wakati wa asubuhi, na wakati wa usiku na wakati wa mchana

    [18] Na ni Zake Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, shukrani na sifa njema katika mbingu na ardhi, na usiku na mchana

    [19] Mwenyezi Mungu Anakitoa kilicho hai kutokana na kilichokufa, kama vile binadamu kutokana na tone la manii na ndege kutokana na yai, na Anakitoa kilichokufa kutokana na kilicho hai, kama vile tone la manii kutokana na binadamu na yai kutokana na ndege. Na Anahuisha ardhi kwa mimea baada ya kukauka na kuwa kavu. Na kwa namna hii ya kuhuisha mtatoka , enyi watu, makaburini mwenu mkiwa hai ili muhesabiwe na mulipwe

    [20] Na miongoni mwa alama za Mwenyezi Mungu zinazoonyesha ukubwa wake na ukamilifu wa uweza Wake, ni kuwa Alimuumba baba yenu Ādam kutokana na mchanga, kisha nyinyi binadamu mnaenea kwenye ardhi kwa kuzaliana mnatafuta fadhila za Mwenyezi Mungu

    [21] Na miongoni mwa alama zenye kuonyesha ukubwa Wake na ukamilifu wa uweza wake ni kuwa Amewaumba wake kwa ajili yenu kutokana na jinsi yenu, enyi wanaume, ili nafsi zenu zijitulize kwao na ziburudike, na Akatia mapenzi na huruma baina ya mwanamke na mumewe. Hakika katika uumbaji huo wa Mwenyezi Mungu pana alama zenye kuonyesha uweza wa Mwenyezi Mungu na kupwekeka Kwake kwa watu wenye kufikiria na kuzingatia

    [22] Na miongoni mwa dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu ni uumbaji mbingu na kuwa juu kwake bila ya nguzo, na uumbaji ardhi ikiwa imekunjuka na kupanuka, na kutafautiana lugha zenu na kuwa mbalimbali rangi zenu. Hakika katika hayo kuna mazingatio kwa kila mwenye elimu na busara

    [23] Na miongoni mwa dalili za uweza huu ni kuwa Mwenyezi Mungu Amewawekea usingizi uwe ni mapumziko kwenu ya usiku au mchana, kwani katika kulala yanapatikana mapumziko na kuondokewa na machovu, na Amewawekea mchana ambapo ndani yake mnaenda huku na kule kutafuta riziki. Hakika katika hayo kuna dalili ya ukamilifu wa uweza wa Mwenyezi Mungu na upitishaji matakwa Yake kwa watu wanaosikia mawaidha usikiaji wa kutia akilini, kufikiria na kuzingatia

    [24] Na miongoni mwa dalili za uweza Wake, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake ni kuwaonyesha umeme, mkaogopa vimondo na mkawa na matumaini ya mvua, na Anateremsha mvua kutoka mawinguni ikahuisha ardhi baada ya kuwa katika hali ya ukame na ukavu. Hakika katika hayo kuna dalili ya ukamilifu wa uweza wa Mwenyezi Mungu na ukubwa wa hekima Yake na wema Wake kwa kila Mwenye akili ya kujiongoza

    [25] Na miongoni mwa alama Zake zenye kuonyesha uweza Wake ni kuwa mbingu na ardhi zinasimama, zinatulia na zinajikita kwa Amri Yake, zisitikisike na mbingu isianguke juu ya ya ardhi, kisha Mwenyezi Mungu Atakapowaita nyinyi kwenye kufufuliwa Siku ya Kiyama, muda si muda mtajikuta mnatoka makaburini kwa haraka

    [26] Ni wa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, wote waliyoko mbinguni na ardhini, miongoni mwa Malaika, binadamu, majini, wanyama, mimea na visivyo na uhai, wote hao wanafuata amri Yake wanaunyenyekea ukamilifu Wake

    [27] Na ni Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Anayeanzisha uumbaji viumbe kutoka kwenye hali ya kutokuwako, kisha Atawarudisha wakiwa hai baada ya kufa. Na kuwarudishia viumbe uhai baada ya kufa ni rahisi kwa Mwenyezi Mungu kuliko kuanzisha kuwaumba, na yote mawili ni rahisi Kwake. Na ni ya Mwenyezi Mungu sifa ya hali ya juu katika kila anachosifiwa, Hakuna chochote mfano Wake, na Yeye Ndiye Mwenye kusikia, Ndiye Mwenye kuona, Na Yeye Ndiye Mshindi Asiyeshindwa, Ndiye Mwingi wa hekima katika maneno Yake na vitendo Vyake na uendeshaji mambo ya viumbe Vyake

    [28] Mwenyezi Mungu Amewapigia mfano, enyi washirikina, utokao na nafsi zenu: Je kuna yoyote, kati ya watumwa wenu na wajakazi wenu, anayeshirikiana na nyinyi katika riziki yenu na mkaona kuwa nyinyi na wao muko sawa katika hiyo, ikawa mnawaogopa wao kama mnavyowaogopa waungwana washirika katika ugawaji wa mali zenu? Nyinyi hamtaridhika na hilo, basi vipi mtaridhika na hilo upande wa Mwenyezi Mungu kwa kumfanya kuwa Ana mshirika miongoni mwa viumbe Vyake? Kwa mfano wa ufafanuzi huu, tunawafafanulia ushahidi na hoja watu wenye akili timamu ambao watanufaika nao

    [29] Bali washirikina walifuata matamanio yao kwa kuwaiga wazazi wao bila ujuzi wowote, wakashirikiana nao katika ujinga na upotevu. Na hakuna yoyote anayeweza kumuongoza yule ambaye Mwenyezi Mungu Amempoteza kwa sababu ya kuendelea kwake kwenye ukafiri na ukaidi. Na hawa hawana wasaidizi wa kuwaokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu

    [30] Basi simamisha uso wako, ewe Mtume, wewe na waliokufuata na uendelee kwenye msimamo wa dini ambayo Mwenyezi Mungu Amekuwekea, nayo ni Uislamu ambao Mwenyezi Mungu Ameifanya ilingane na maumbile ya watu. Basi kuendelea kwenu kubaki kwenye Uislamu, na kushikamana kwenu nao ni kushikamana na umbile la Mwenyezi Mungu la kumuamini Mwenyezi Mungu Peke Yake. Hapana ugeuzaji wa uumbaji wa Mwenyezi Mungu na Dini Yake, kwani hiyo ndiyo njia iliyonyoka yenye kupelekea kwenye radhi za Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe wote, na Pepo Yake. Lakini wengi wa watu hawajui kuwa yale niliyokumrisha nayo, ewe Mtume, ndiyo Dini ya haki na si nyigine

    [31] Na muwe ni wenye kurejea kwa Mwenyezi mungu kwa kutubia na kumtakasia matendo mema. Na muogopeni Yeye kwa kufanya maamrisho na kujiepusha na makatazo, na msimamishe Swala kikamilifu kwa nguzo zake na mambo yake yanayopasa na sharti zake, na msiwe ni miongoni mwa wenye kumshirikisha mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu katika ibada

    [32] Na msiwe ni miongoni mwa washirikina na watu wa (kufuata) matamanio na mambo ya uzushi, walioibadilisha dini yao na wakaigeuza kwa kuchukuwa baadhi yake na kuacha baadhi yake kwa kufuata matamanio yao, wakawa ni makundi na mapote, wanafuata mikao ya viongozi wao na vyama vyao na maoni yao, wanasaidiana wao kwa wao katika batili, kila watu wa kundi wanashangilia na kufurahia mkao wao, wanajihukumia wenyewe kuwa wao wako kwenye haki na wasiokuwa wao wako kwenye ubatilifu

    [33] Na yakiwapata watu matatizo na misukosuko wanamuomba Mola wao, hali ya kumtakasia, Awaondolee mashaka, na Anapowarehemu na Akawaondolea mashaka, punde si punde linatoka pote la watu kati yao wakarudi kwenye ushirikina mara nyingine wakamuabudu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu

    [34] Ili wakanushe kile tulichowapa na kuwaneemesha kwacho cha kutatuliwa matatizo na kuondolewa shida. Basi stareheni, enyi washirikina, kwa neema na ukunjufu katika dunia hii, mtakijua mtakachokikuta cha adhabu na mateso

    [35] Au tuliwateremshia hawa washirikina hoja yenye kutoa mwangaza na kitabu kisicho na shaka kitamke kueleza usahihi wa ushirikina wao na ukanushaji wao Mwenyezi Mungu na aya Zake

    [36] Na tunapowaonjesha watu neema itokayo kwetu ya afya, uzima na mafanikio, wanafurahia hilo furaha ya kiburi na majivuno, na sio furaha ya shukrani. Na yakiwapata wao magonjwa, umasikini, kuogopa na dhiki kwa sababu ya dhambi zao na maasia yao, ghafula wao wanakata tamaa kuwa hayo yatawaondokea. Na hii ni tabia ya wengi wa watu katika hali ya neema na matatizo

    [37] Kwani hawajui kwamba Mwenyezi Mungu Anamkunjulia riziki Anayemtaka kwa kumjaribu: atashukuru au atakufuru? Na (kwani hawajui kwamba Yeye) Anambania riziki Anayemtaka kwa kumjaribu: je atavumilia au atababaika? Hakika katika kukunjulia na kubania kuna alama (za utendakazi wa Mwenyezi Mungu) kwa watu wanaomuamini Mwenyezi Mungu na wanaojua hekima ya Mwenyezi Mungu na rehema Yake

    [38] Basi mpe , ewe mwenye kuamini, jamaa yako wa karibu haki yake ya kuunga kizazi na sadaka na mambo mengine ya wema. Na mpe masikini na mwenye uhitaji aliyekatikiwa na njia (kwa kuishiwa na pesa akiwa safarini) Zaka na sadaka. Kwani kutoa huko ni bora kwa wale wanaoukusudia kupata radhi ya Mwenyezi Mungu kwa matendo yao mema. Na wanaofanya matendo haya na megineyo miongoni mwa matendo mema, wao ndio wenye kufaulu kupata malipo ya Mwenyezi Mungu, ndio wenye kuokoka na mateso Yake

    [39] Na mkopo wowote wa pesa mnaoutoa kwa makusudio ya riba, na kutaka kuzidisha mkopo huo ili kupatikane ongezeko katika mali ya watu, basi mbele ya Mwenyezi Mungu hayaongezeki, bali Anayaondolea baraka na kuyabatilisha. Na Zaka na sadaka mnazotoa kuwapatia wastahiki kwa kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu na kutaka malipo yake, basi hiki ndicho ambacho Mwenyezi Mungu Anakikubali na Atawaongezea mara nyingi zaidi

    [40] Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Ndiye Aliyewaumba nyinyi, enyi watu, kisha Akawapa riziki katika uhai huu, kisha Atawafisha muda wenu ukomapo, kisha Atawafufua kutoka makaburini mkiwa muko hai mpate kuhesabiwa na kulipwa. Je kuna yoyote miongoni mwa washirika wenu anayefanya chochote katika hayo? Ameepukana Mwenyezi Mungu na Ametakasika na ushirikina wa hawa wenye kumshirikisha

    [41] Uharibifuumejitokezabaranina baharini, kama vile ukame, uchache wa mvua, wingi wa magonjwa na majanga, kwa sababu ya maasia yanayofanywa na binadamu, hivyo basi Awapatie adhabu kwa baadhi ya matendo waliyoyatenda ulimwenguni wapate kutubia kwa Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa na upungufu ni Kwake, na warudi nyuma waache maasia na matendo yao yatengenezeke na mambo yao yalingane sawa

    [42] Sema, ewe Mtume, kuwaambia wenye kuyakanusha uliyokuja nayo, «Tembeeni kwenye sehemu za ardhi matembezi ya kuzingatia na kutia mambo akilini, na mtazame vile ulivyokuwa mwisho wa ummah waliopita wenye kukanusha, kama vile watu wa Nūḥ, ‘Ād na Thamūd, mtakuta kwamba mwisho wao walioishia ulikuwa mbaya zaidi na kikomo hiko walichokomea kilikuwa kibaya zaidi, kwani wengi wao walikuwa ni wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu

    [43] Basi elekeza uso wako, ewe Mtume, upande wa Dini iliyonyoka, nayo ni Uislamu, hali ya kutekeleza maamrisho yake na kujiepusha makatazo yake. Na ushikamane nayo kabla Siku ya Kiyama haijaja, kwani ijapo Siku hiyo, ambayo hakuna anayeweza kuirudisha, viumbe watapambanuka wakiwa makundi- makundi yalio tafauti ili waoneshwe matendo yao

    [44] Mwenye kukanusha basi mateso ya ukanushaji wake yatamshukia yeye, nayo ni kukaa milele Motoni. Na mwenye kuamini na akafanya matendo mema basi hao wanajitayarishia wenyewe makao ya Peponi, kwa sababu ya kushikamana kwao na utiifu wa Mola wao

    [45] Hivyo basi Mwenyezi Mungu Awalipe wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafanya matendo mema kwa fadhila Zake na wema Wake, hakika Yeye Hawapendi wakanushaji kwa kuwa Ana hasira na ghadhabu juu yao

    [46] Na miongoni mwa alama za Mwenyezi Mungu zenye kuonyesha kuwa Yeye ndiye Mungu wa kweli Peke Yake, Asiye na Mshirika, na kuwa Ana uweza mkubwa, ni kule kutuma upepo mbele ya mvua ukiwa ni wenye kuleta habari njema, kwa kuyasukuma mawingu, hapo nafsi zikaingiwa na furaha kwa hilo, ili awaonjeshe rehema Yake kwa kuwateremshia mvua ambayo kwayo miji inahuika na pia waja, na ili jahazi zitembee baharini kwa amri Yake na matakwa Yake, na ili mtafute fadhila Zake kwa kufanya biashara na megineyo. Mwenyezi Mungu Amefanya hayo yote ili mzishukuru neema Zake na mmuabudu Yeye Peke Yake

    [47] Kwa hakika tuliwatuma kabla yako wewe, ewe Mtume, Mitume waende kwa watu wao kwa kubashiria na kuonya, wawaite kwenye upwekeshaji (wa Mwenyezi Mungu) na wawatahadharishe na ushirikina. Wakawajia na miujiza na hoja zenye mwangaza, na wengi wao wakamkanusha Mola wao, na kwa hivyo tukawatesa wale waliotenda mabaya miongoni mwao, tukawaangamiza na tukawapa ushindi wafuasi wa Mitume. Na hivyo ndivyo tunavyowafanya wenye kukukanusha wanapoendelea kukukanusha na wasiamini

    [48] Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Anayetuma upepo ukayasukuma mawingu yaliyojaa maji, na Mwenyezi Mungu Akayasambaza mbinguni vile Anavyotaka, Akayafanya ni vipande vilivyotenganika mbalimbali, hapo ukaiona mvua inatoka mawinguni. Na Aipelekapo Mwenyezi Mungu kwa waja wake, ghafla utawakuta wameingiwa na bashasha na wanafurahi kwa kuwa Mwenyezi Mungu Amewaletea hiyo

    [49] Na ingawa wao kabla ya kuteremka mvua walikuwa katika hali ya kukata tamaa na kutokuwa na matumaini kwa sababu ya kutonyeshewa na mvua

    [50] Basi Tazama, ewe mwenye kuangalia, mtazamo wa kutia akilini na kuzingatia, athari za mvua kwenye mimea, nafaka na miti, ujionee vipi Mwenyezi Mungu Anaipa uhai ardhi baada ya kuwa imekufa, Akaiotesha mimea na nyasi? Hakika Yule aliyeweza kuihuisha ardhi hii Ndiye Atakayehuisha wafu, na Yeye juu ya kila kitu ni Muweza, hakuna kinachomshinda

    [51] Na tukiupeleka kwenye mashamba yao ya nafaka na mimea yao upepo wenye kuharibu, wakaiona mimea yao imeharibika kwa upepo huo, ikawa imekuwa rangi ya manjano baada ya kuwa rangi ya kijani, wangalikaa baada ya kuiona wakimkufuru Mwenyezi Mungu na kuzikanusha neema Zake

    [52] Kwa hakika wewe, ewe Mtume, humsikilizishi yule ambaye moyo wake umekufa au mashikio yake yamezibana yakawa hayaisikii haki. Basi usibabaike wala usisikitike kwa kukataa kukuamini hawa washirikina, kwani wao ni kama viziwi na wafu, hawasikii wala hawahisi hata kama wako mbele yako, basi itakuwa vipi iwapo hawako na wewe na wamekupa mgongo

    [53] Na hukuwa wewe, ewe mtume, ni mwenye kumuongoza yule aliyefanywa kipofu na Mwenyezi Mungu asiione njia ya uongofu. Utakayemsikilizisha akanufaika kwa kusikia si mwingine isipokuwa yule anayeziamini aya zetu, basi hao ni wenye kuandama na kufuata amri ya Mwenyezi Mungu

    [54] Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Ndiye Ambaye Amewaumba kwa maji ya udhaifu na unyonge, nayo ni tone la manii, kisha akaleta, baada ya udhaifu wa utoto, nguvu za utu uzima, kisha akaleta, baada ya nguvu hizi, udhaifu wa uzee na ukongwe. Anaumba Anachotaka cha udhaifu na nguvu. Na Yeye Ndiye Mjuzi wa viumbe Vyake, Ndiye Muweza wa kila kitu

    [55] Na siku kitakapokuja Kiyama na Atakapo Mwenyezi Mungu kuwafufua viumbe kutoka makaburini mwao, wataapa washirikina kwamba hawakukaa duniani isipokuwa kipindi kifupi cha wakati. Watasema urongo katika kiapo chao kama walivyokuwa wakisema urongo duniani na wakiikataa haki ambayo Mitume walikuja nayo

    [56] Na watasema wale waliopewa elimu na imani ya Mwenyezi Mungu, miongoni mwa Malaika, Mitume na Waumini, «Mlikuwa mmekaa katika kile Alichokiandika Mwenyezi Mungu, kutokana na ujuzi Wake uliotangulia, kuanzia siku mliyoumbwa mpaka mkafufuliwa. Basi hii ndio Siku ya Ufufuzi, lakini nyinyi mlikuwa hamjui, ndipo mkaikataa duniani na mkaikanusha.»

    [57] Basi Siku ya Kiyama, hazitawafaa madhalimu nyudhuru zao wazitowazo, na hawatatakiwa wamridhishe Mwenyezi Mungu kwa kutubia na kutii, isipokuwa watateswa kwa makosa yao na maasia yao

    [58] Hakika tuliwafafanulia watu, katika hii Qur’ani, kila mfano ili kuwasimamishia hoja na kuthibitisha kuwa Mwenyezi Mungu ni Mmoja, Aliyetukuka na kuwa juu. Na lau ungaliwajia na hoja yoyote yenye kuonyesha ukweli wako, wale waliokukanusha wangalisema kukwambia, «Hamkuwa nyinyi, ewe Mtume na wafuasi wako, isipokuwa ni warongo katika yale mambo mnayotuletea.»

    [59] Mfano wa muhuri huu, Mwenyezi Mungu Anapiga muhuri juu ya nyoyo za wasioujua uhakika wa kile unachowaletea, ewe Mtume, kutoka kwa Mwenyezi Mungu kutokana na mazingatio haya na miujiza iliyo waziwazi

    [60] Basi vumilia, ewe Mtume, kwa yale yanayokupata ya makero ya watu wako kwako na kukukanusha kwao, kwani ahadi ya Mwenyezi Mungu kwako ya ushindi, uthabiti na malipo mema ni kweli isiyo na shaka. Na wasikubabaishe wakakuweka kando na Dini yako wale wasiokuwa na yakini ya Agizo (la Siku ya Kiyama) na wasioamini kufufuliwa na malipo

    Luqman

    Surah 31

    [1] «Alif, Lām, Mīm» Yametangulia maelezo kuhusu herufi zilizokatwa na kutengwa mwanzo wa sura ya Al-Baqrah

    [2] Aya hizi ni aya za Qur’ani yenye hekima kubwa

    [3] Aya hizi ni uongofu na ni rehema kwa waliofanya vizuri kuyafiuata kivitendo yale yaliyoteremshwa katika Qur’ani na aliyowaamrisha kwayo Mtume wao Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [4] Wanaotekeleza Swala kikamilifu kwa nyakati zake na wanaotoa Zaka zilizo lazima juu yao kwa wanaostahiki kupewa. Na hali wao wana yakini kuwa kuna kufufuliwa na kulipwa Akhera

    [5] Hao wanaosifika kwa sifa zilizotangulia wako kwenye ubainifu na nuru kutoka kwa Mola wao, na wao ndio wenye kufaulu ulimwenguni na Akhera

    [6] Na miongoni mwa watu kuna anayenunua maneno ya pumbao, nayo ni kila chenye kumpumbaza mtu na utiifu wa Mwenyezi Mungu, ili awapoteze watu na njia ya uongofu wafuate njia ya matamanio na azifanye aya za Mwenyezi Mungu kuwa ni shere, basi hao watakuwa na adhabu yenye kuwadhalilisha na kuwatweza

    [7] Na anaposomewa aya za Qur’ani anaupa mgongo utiifu wa Mwenyezi Mungu na anafanya kiburi bila kuzingatia, kama kwamba yeye hakusikia kitu, kama kwamba kwenye mashikio yake kuna uziwi. Na yoyote ambaye hali yake ni hii, mpe bishara, ewe Mtume, ya adhabu kali yenye kuumiza humo Motoni Siku ya Kiyama

    [8] Hakika wale waliomuamini mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakatenda mema waliyoamrishwa, hao wana starehe ya daima ndani ya mabustani ya Peponi

    [9] Na uhai wao katika mabustani hayo ya Peponi ni uhai wa milele, haukatiki wala haumaliziki, Mwenyezi Mungu Amewaahidi hilo ahadi ya kweli. Na Yeye , kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Haendi kinyume na ahadi Yake. Na Yeye ni Mshindi katika amri Yake, ni Mwenye hekima katika uendeshaji mambo Wake

    [10] Ameumba mbingu, Akaziinua bila ya nguzo kama mnavyoziona. Na Ameweka ndani ya ardhi majabali yaliyojikita, ili zisipate kutikisika na kutetemeka yakaharibika maisha yenu. Na Ameeneza kwenye ardhi aina mbalimbali za wanyama. Na tumeteremsha kutoka mawinguni mvua, tukaotesha kwayo kwenye ardhi kila aina ya mimea mizuri yenye nafuu yenye mandhari mazuri

    [11] Na vyote mnavyovishuhudia ni viumbe vya Mwenyezi Mungu, basi nionesheni, enyi washirikina, imeumba nini hiyo miungu yenu mnayoiabudu badala ya Mwenyezi Mungu? Bali washirikina wameenda kando na haki na msimamo wa sawa waziwazi

    [12] Na kwa hakika tulimpa mja mwema miongoni mwa waja wetu , naye ni Luqman, busara, nayo ni ufahamu wa Dini, akili na usawa wa maneno, na tulimwambia, «Zishukuru neema za Mwenyezi Mungu juu yako. Na Mwenye kumshukuru Mola wake, faida yake itamrudia mwenyewe, na Mwenye kukanusha neema Zake, basi Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Hahitaji kushukuriwa, ni Zake Yeye shukrani na sifa njema kwa kila hali

    [13] Na kumbuka na utaje, ewe Mtume, ushauri wa Luqman kwa mwanawe alipomuambia kwa kumwaidhia, «Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu ukajidhulumu nafsi yako, hakika ushirikina ni dhambi kubwa na ovu kabisa la madhambi makubwa.»

    [14] Na tulimuamuru binadamu kuwatendea wema wazazi wake wawili na kuwafanyia hisani, Mamake alimbeba tumboni, shida juu ya shida, na mimba yake na kumaliza kunyonya kwake ni ndani ya kipindi cha miaka miwili, na tukamwambia, «Mshukuru Mwenyezi Mungu kisha uwashukuru wazazi wako, kwangu mimi ndio marejeo nipate kumlipa kila mmoja kwa anachostahili

    [15] «Na wakikusukuma kwa bidii wazazi wako wawili, ewe mtoto mwema, ili unishirikishe mimi na mwingine katika kuniabudu katika kitu ambacho huna ujuzi nacho, au wakakuamuru ufanye jambo miongoni mwa mambo ya kumuasi Mwenyezi Mungu basi usiwatii, kwani hakuna kutiiwa kiumbe kwa kuasiwa Muumba. Na suhubiana nao ulimwenguni kwa wema katika mambo mema yasiyo na madhambi. Na ufuate, ewe mwana mwenye Imani, njia ya aliyetubu kutokana na dhambi zake, akarudi kwangu na akamuamini Mtume wangu Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie. Kisha ni kwangu mimi marejeo yenu, niwape habari ya yale mliokuwa mkiyafanya duniani na nimlipe kila mtenda kwa matendo yake

    [16] «Ewe mwanangu! Jua kwamba uovu au wema uwapo ni kadiri ya chembe ya hardali, nayo ni ile iliyo upeo wa udogo, iliyo ndani ya jabali au iliyo mahali popote, mbinguni au ardhini, Mwenyezi Mungu Ataileta Siku ya Kiyama na Ataihesabu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja Wake, ni Mtambuzi wa matendo yao

    [17] «Ewe mwanangu! Simamisha Swala kikamilifu kwa kutimiza nguzo zake, sharti zake na mambo ya lazima yake, na uamrishe mema na ukataze maovu, na ujue kwamba nyasia hizi ni miongoni mwa mambo Aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu ambayo inatakiwa kuyafanyia pupa

    [18] «Na usizungushe uso wako ukauepusha na watu unaposema na wao au wanaposema na wewe, kwa kuwadharau na kuwafanyia kiburi, wala usitembee kwenye ardhi baina ya watu kwa kujigamba na kujivuna. Hakika Mwenyezi Mungu Hampendi kila mwenye kiburi, mwenye kujifahiri katika nafsi yake, pambo lake na maneno yake

    [19] «Na unyenyekee katika kwenda kwako na uishukishe chini sauti yako usiipandishe juu, kwani sauti mbaya zaidi na inayochukiza zaidi ni sauti ya punda wanaojulikana kwa upumbavu wao na sauti zao za juu.»

    [20] Kwani hamuoni, enyi watu, kuwa Mwenyezi Mungu amewadhalilishia vilivyoko mbinguni miongoni mwa jua, mwezi, mawingu na vinginevyo, na vilivyoko ardhini miongoni mwa wanyama, miti, maji na vinginevyo visivyodhibitika, na Akaeneza kwenu neema Zake za nje juu ya miili na viungo, na za ndani, kwenye akili na nyoyo, na zile Alizowawekea katika zile msizozijua? Na miongoni mwa watu kuna anayefanya ushindani juu ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtakasia ibada bila ya hoja wala ubainifu wala kitabu chenye kubainisha kinachofafanua uhakika wa madai yako

    [21] Na wakiambiwa hawa wenye kufanya ushindani juu ya kumuwahidisha Mwenyezi Mungu na kumpwekesha kwa ibada, «Fuateni yale Ailiyoyateremsha Mwenyezi Mungu kwa Nabii Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie,» wanasema, «Bali tutafuata yale tuliyowapata wazazi wetu wako nayo ya ushirikina na kuabudu masanamu.» Je, wanafanya hayo hata kama Shetani anawaita wao, kwa kuwapambia wao matendo yao mabaya na ukanushaji wao Mwenyezi Mungu, kwenye adhabu ya Moto unaowaka

    [22] Na mwenye kumtakasia Mwenyezi Mungu ibada yake na kumkusudia kwake Mola wake Aliyetukuka, na akawa mwema katika maneno yake, mwenye kutengeneza matendo yake, basi huwa ameshikamana na kamba yenye kufikisha kwenye radhi za Mwenyezi Mungu na Pepo Yake. Na kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake yanakuwa mambo yote, Akamlipa aliye mwema kwa wema wake na aliye mbaya kwa ubaya wake

    [23] Na mwenye kukanusha, usimsikitikie, ewe Mtume, wala usiwe na huzuni, kwa kuwa wewe umetekeleza wajibu wako wa ulinganizi na ufikishaji, kwetu sisi ndio marejeo yao na mwisho wao Siku ya Kiyama, tuwapashe habari ya matendo yao maovu waliyoyafanya duniani, kisha tuwalipe kwa hayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yale ambayo nyoyo zao zinayaficha, ya kumkanusha Mwenyezi Mungu na kufadhilisha kumtii Shetani

    [24] Tutawastarehesha wao kwenye ulimwengu huu wenye kutoweka kwa muda mchache, kisha Siku ya Kiyama tutawawapeleka kwa nguvu na kuwaongoza kwenye adhabu yenye kitisho, nayo ni adhabu ya Jahanamu

    [25] Na lau unawauliza, ewe Mtume, hawa wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, «Ni nani aliyeumba mbingu na ardhi?» Watasema, «Ni Mwenyezi Mungu.» Basi wanaposema hilo, waambie, «Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu Aliyeonyesha ushahidi kutoka kwenu nyinyi wenyewe.» Lakini wengi wa hawa washirikina hawaangalii wala hawazingatii ni nani anayestahiki kusifiwa na kushukuriwa , kwa hivyo ndivyo wakamshirikisha mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu

    [26] Ni vya Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, vyote vilivyoko mbinguni na ardhini kwa kuvimiliki, kuvifanya vifuate amri, kuvipatisha na kuvipangia mambo yake, hivyo basi hakuna anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu Ndiye Mkwasi Anayejitosheleza mwenyewe Asiyehitaji viumbe Vyake. Ni Zake Yeye shukrani na sifa njema kwa kila namna

    [27] Na lau miti ya ardhi yote ingalichongwa ikafanywa kalamu na bahari ikawa ni wino wake, na zikaongezwa juu yake bahari saba, na yakaandikwa, kwa kalamu hizo na wino huo, maneno ya Mwenyezi Mungu yatokanao na ujuzi wake na hukumu Zake na yale ambayo Amewaletea wahyi Malaika Wake na Mitume Wake, zingalivunjika- vunjika kalamu hizo na ungaliisha wino huo, na hayangaliisha maneno ya Mwenyezi Mungu yaliyotimia ambayo hakuna mwenye kuyazunguka kiujuzi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mshindi Mwenye nguvu katika kuwatesa wanaomshirikisha, ni Mwingi wa hekima katika kuendesha mambo ya viumbe Vyake. Katika aya hii pana kumthibitishia Mwenyezi Mungu Aliyetukuka sifa ya Maneno kikweli, kama inavyonasibiana na utukufu Wake na ukamilifu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake

    [28] Hakukuwa kuwaumba nyinyi, enyi watu, na kuwafufua Siku ya Kiyama, vile ilivyo nyepesi na rahisi, isipokuwa ni kama kuumba nafsi moja na kuifufua. Hakika Mwenyezi Mungu Anayasikia maneno yenu, Anayaona matendo yenu, na Atawalipa kwa hayo

    [29] Kwani huoni kwamba Mwenyezi Mungu Anazichukua baadhi ya saa za usiku, hivyo basi mchana ukarefuka na usiku ukawa mfupi, na Anazichukua baadhi ya saa za mchana, hivyo basi usiku ukarefuka na mchana ukawa mfupi, na Amewadhalilishia jua na mwezi, kila mojawapo ya hivyo viwili kinatembea kwenye mzunguko wake hadi wakati maalumu uliopangiwa, na kwamba Mwenyezi Mungu Anayaona matendo yote ya viumbe, yawe mema au mabaya, hakuna chochote kati ya hivyo kinachofichamana Kwake

    [30] Yote hayo ni miongoni mwa ukubwa wa uweza Wake. Mpate kujua na mkubali kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye wa kweli katika dhati Yake na sifa Zake na matendo Yake, na kuwa vile wanavyoviomba visivyokuwa Yeye ndio vya urongo, na kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyetukuka, kwa dhati Yake, uweza Wake na kutendesha nguvu Kwake, Aliye juu ya viumbe Vyake vyote, Aliye Mkubwa juu ya kila kitu, na kila kisichokuwa Yeye kinanyenyekea Kwake, Yeye Peke Yake Ndiye Anayestahiki kuabudiwa, na si mwingine

    [31] Kwani huoni, ewe mtazamaji, kwamba majahazi yanayotembea baharini kwa amri ya Mwenyezi Mungu ni neema itokayo Kwake kwa viumbe Wake, Apate kuwaonyesha utendakazi Wake na hoja Zake kwenu za kuwafanya nyinyi mzingatie? Hakika katika kupitisha majahazi baharini kuna dalili nyingi kwa kila mvumilivu sana wa kuyaepuka yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu na katika kumtii Yeye na kuyavumilia mambo yaliyokadiriwa na Yeye, mwingi wa kushukuru neema Zake

    [32] Na washirikina wanapopanda majahazini na mawimbi makubwa yakawazunguka pambizoni mwao kama vile mawingu na majabali, huingiwa na hofu na babaiko la kuogopa kuzama, na hapo wanamkimbilia Mwenyezi Mungu na wanamtakasia dua zao, na Anapowaokoa Akawafikisha kwenye bara, kati yao kutakua na mtu wa kati na kati asiyemshukuru Mwenyezi Mungu kikamilifu, na kati yao kutakuwa na mwenye kukanusha neema za Mwenyezi Mungu na kuzikataa. Na hakanushi aya zetu na hoja zetu zenye kutolea ushahidi ukamilifu wa uweza wetu na upweke wetu isipokuwa kila mwingi wa kuvunja ahadi, mwingi wa kukataa neema za Mwenyezi Mungu juu Yake

    [33] Enyi watu! Mcheni Mola wenu na mtiini kwa kufuata maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake, na jihadharini na Siku ya Kiyama ambayo mzazi hatamfalia kitu mwane, wala mwana hatamfalia kitu babake. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli haina shaka, basi msihadaike na uhai wa duniani na pambo lake, ukawafanya msahau uhai mwingine. Na asiwahadae nyinyi yoyote mwenye kuhadaa miongoni mwa mashetani wa kibinadamu na wa kijini

    [34] Hakika Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Anajuwa ni lini Kiyama kitasimama. Na Yeye Ndiye Anayeteremsha mvua kutoka mawinguni, hakuna awezae hilo yoyote isipokuwa Yeye. Na Anajua vilivyomo ndani ya vizazi vya wanawake. Na Anajua kitakachotendwa na kila mtu wakati ujao. Na hakuna nafsi inayojua itakufa wapi. Ni Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Peke Yake Ndiye Anayehusika kwa kujua hayo yote. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtambuzi, Ameyazunguka mambo ya nje na ya ndani, hakuna chochote katika hayo kinachofichamana Kwake

    Sujida

    Surah 32

    [1] «Alif, Lām, Mīm» Yametangulia maelezo kuhusu herufi zilizokatwa na kutengwa mwazo wasua ya Al-Baqarah

    [2] Hii Qur’ani aliyokuja nayo Mtume Muhammad, rehema na amani zimshukie, haina shaka kuwa imeteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe wote

    [3] Kwani je, wanasema washirikina kuwa Muhammad Ameizua Qur’ani? Wamesema urongo, bali hiyo Qur’ani ndiyo ukweli uliothibiti ulioteremshwa kwako, ewe Mtume, kutoka kwa Mola wako, ili uwaonye nayo watu ambao hawakujiwa na muonyaji kabla yako wewe, huenda wao wakaongoka: wakaijua haki, wakaiamini, wakaitanguliza na wakakuamini wewe

    [4] Mwenyezi Mungu Ndiye Ambaye aliumba mbingu na ardhi na vilivyoko baina yake kwa Siku sita kwa hekima Anayoijua. Na Yeye ni Muweza wa kuziumba kwa neno «Kuwa» na likawa, kisha Akalingana, Kutakasika na kuwa juu ni Kwake - nako ni kuwa juu na kunyanyuka- juu ya ‘Arsh Yake , kulingana kunakonasibiana na utukufu Wake, hakusemwi kuko namna gani wala hakufananishwi na vile binadamu wanavyolingana. Hamna nyinyi, enyi watu, mtegemewa wa kumtegemezea mambo yenu, au muombezi wa kuwaombea nyinyi mbele ya Mwenyezi Mungu, ili muokoke na adhabu Yake. Basi kwani nyinyi hamwaidhiki na mkafikiria, enyi watu, mkampwekesha Mwenyezi Mungu kwa uungu na mkamtakasia ibada

    [5] Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anaendesha mambo ya viumbe kutoka mbinguni hadi ardhini, kisha mambo hayo yanapanda kwa Mwenyezi Mungu pamoja na mapelekesho kwa kipindi cha siku moja ambayo kadiri yake ni miaka elfu moja ya siku za duniani mnazozihesabu

    [6] Huyo Muumbaji Mwenye kuendesha mambo ya viumbe ni Mjuzi wa kila kinachofichamana na macho, miongoni mwa mambo yanayohifadhiwa na vifua na kufichwa na nafsi, na ni Mjuzi wa vitu vinavyoonekana na macho, na Yeye Ndiye Mwenye nguvu, Ndiye Mwenye kushinda Asiyeshindwa, Ndiye Mwenye kuwarehemu waja Wake Waumini

    [7] Mwenyezi Mungu Ndiye Ambaye Ametengeneza uumbaji wa kila kitu, na Alianza kumuumba binadamu, naye ni Ādam, kwa udongo

    [8] Kisha Akavifanya vizazi vya Ādam vizalikane na tone dhaifu lililo dogo na twevu

    [9] Kisha Aliukamilisha uumbaji wa binadamu na Akaufanya upendeze na Akalifanya zuri umbo lake, na Akapuliza ndani yake roho Yake kwa kumtuma Malaika kwake ili apulize roho, na Akawapa nyinyi, enyi watu, neema ya masikizi na maangalizi ya kupambanua sauti, rangi, vitu na watu, na neema ya akili ya kupambanua jema na baya na lenye kunufaisha na kudhuru. Ni kuchache kule kumshukuru kwenu Mola wenu kwa neema Alizowapatia

    [10] Na wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu wenye kukanusha kufufuliwa wamesema, «Je, itakapokuwa mchanga nyama yetu na mifupa yetu, je, tutafufuliwa tuwe umbo lingine?» huku wakiona kuwa hilo liko mbali kutokea na huku hawataki kuifikia haki. Na hilo kwao ni udhalimu na ushindani, hii ni kwamba wao wanakanusha kukutana na Mola wao Siku ya Kiyama

    [11] Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina hawa, «Atakayewafisha nyinyi ni Malaika wa kifo aliyewakilishwa kwenu, atakayezichukua roho zenu utakapokoma muda wenu wa kuishi, na hamtachelewa hata nukta moja, kisha mtarudishwa kwa Mola wenu, Awalipe kwa matendo yenu, yakiwa ni mema Awalipe wema na yakiwa maovu Awalipe uovu

    [12] Na lau ungaliona, ewe mhutubiwa, pindi wahalifu waliokanusha kufufuliwa wakiwa wameviinamisha vichwa vyao mbele ya Mola wao kutokana na hizaya na aibu huku wanasema, «Mola wetu! Tumeyaona machafu yetu na tumesikia kutoka kwako ukweli wa yale waliokuwa Mitume wako wakituamrisha duniani, na tumeshatubia kwako, basi turudishe duniani ili tufanye matendo ya utiifu kwako. Sisi tushayaamini sasa yale tuliokuwa tukiyakanusha ya kuwa wewe ni mmoja na kwamba wewe utawafufua walio makaburini. Na lau ungaliyaona, ewe mhutubiwa, haya yote ungaliona jambo kubwa na janga zito

    [13] Na lau tungalitaka tungaliwapa washirikina hawa uongofu wao na Angaliwaonyesha njia ya Imani, lakini limethibiti neno linalotoka kwangu na limepasa kwamba nitaujaza, moto wa jahanamu, watu wote wa aina mbili, ya kijini na kibanadamu, wenye kukufuru na kuasi, kwa kuwa walichagua upotevu na kuacha uungofu

    [14] Wataambiwa washirikina hawa kwa njia ya kulaumiwa, watakapoingia Motoni, «Basi onjeni adhabu kwa sababu ya kughafilika kwenu na Akhera na kujiingiza kwenu kwenye ladha za dunia, sisi tutawaacha kwenye adhabu leo, na onjeni adhabu ya moto wa Jahanamu isiyomalizika kwa yale mliokuwa mkiyafanya duniani ya kumkanusha Mwenyezi Mungu na kumuasi.»

    [15] Kwa kweli, wanaoziamini aya za Qur’ani na kuzifuata kivitendo ni wale ambao wanapowaidhiwa nazo au wanaposomewa, wanamsujudia Mola wao kwa kumnyenyekea na kumtii na wanamtakasa Mwenyezi Mungu kwa kumsifu katika kusujudu kwao, na hali wao hawaoni kiburi wakaacha kumsujudia na kumtakasa na kumuabudu Yeye Peke Yake Asiyekuwa na mshirika

    [16] Mbavu za hawa wanaoziamini aya za Mwenyezi Mungu zinajiepusha na magodoro ya kulalia, wakiswali kwa Mola wao swala ya usiku, wakimuomba kwa kuogopa adhabu na kutarajia malipo mema, na katika kile tulichowaruzuku wanatumia katika kumtii Mwenyezi Mungu na katika njia Yake

    [17] Hakuna nafsi yoyote inayoyajua yale aliyowawekea Mwenyezi Mungu hawa Waumini ya kutuliza macho na kufurahisha moyo, yakiwa ni malipo yao kwa matendo yao mema

    [18] Je, Yule Aliyekuwa mtiifu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, mwenye kuamini agizo lake la kuwalipa mema wema wenye kufanya mema na kuwalipa ubaya wenye kufanya mabaya, ni kama yule aliyemkanusha Mwenyezi Mungu na Mitume Yake na akaikanusha Siku ya Kiyama? Hawalingani mbele ya Mwenyezi Mungu

    [19] Ama wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na wakayafanya yale waliyoamrishwa kwayo, basi malipo yao ni mabustani ya Pepo watashukia huko na watakaa kwenye starehe zake wakiandaliwa, yakiwa malipo yao kwa yale waliokuwa wakiyafanya ulimwenguni ya utiifu Kwake

    [20] Na ama wale waliotoka nje ya utiifu kwa Mwenyezi Mungu na wakafanya matendo ya kumuasi, basi mahali pao pa kutulia ni moto wa Jahanamu, kila wakitaka kutoka wanarudishwa ndani. Na wataambiwa, kwa kulaumiwa na kukaripiwa, «Onjeni adhabu ya Moto ambayo mlikuwa mkiikanusha ulimwenguni.»

    [21] Na tutawaonjesha, tena tutawaonjesha, hawa waasi wenye kukanusha adhabu ndogo ya matatizo, shida na misiba ya duniani kabla ya adhabu kubwa zaidi Siku ya Kiyama, ambako wataadhibiwa ndani ya moto wa Jahanamu, huenda wao wakarejea na wakatubia dhambi zao kwa Mola wao

    [22] Hakuna hata mmoja aliye dhalimu zaidi wa nafsi yake kuliko yule aliyekumbushwa dalili za Mwenyezi Mungu kisha akazipa mgongo zote, asiwaidhike kwa mawaidha yake, bali akayafanyia kiburi. Hakika sisi ni wenye kuwatesa wale wahalifu waliozipa mgongo aya za Mwenyezi Mungu na hoja Zake na wasinufaike nazo

    [23] Hakika tulimletea Mūsā Taurati kama tulivyokuletea wewe, ewe Mtume, Qur’ani. Basi usiwe na shaka ya kukutana na Mūsā usiku wa Isrā’ (safari ya kwenda Bayt al- Maqdis) na Mi’rāj (safari ya kwenda mbinguni), na tukaifanya Taurati ni uongofu kwa Wana wa Isrāīl, Unawalingania kwenye haki na kwenye njia iliyonyoka

    [24] Na tuliwafanya, miongoni mwa Wana wa Isrāīl, ni waongozi na walinganizi kwenye wema, watu wanawafuata na wao wanawalingania kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumuabudu Peke Yake na kumtii. Na walipata daraja hii ya juu waliposubiri juu ya amri za Mwenyezi Mungu, kuyaacha makemeo Yake na kuwalingania na kuvumilia makero katika njia Yake, na walikuwa wanaziamini kikweli aya za mwenyezi Mungu na hoja Zake

    [25] Hakika Mola wako, ewe Mtume, Atatoa uamuzi baina ya Waumini na makafiri miongoni mwa Wana wa Isrāīl na wasiokuwa wao Siku ya Kiyama kwa uadilifu katika yale waliotafautiana juu yake miongoni mwa mambo ya dini, na Atamlipa kila binadamu kwa matendo yake kwa kuwatia watu wa Peponi Peponi na watu wa Motoni Motoni

    [26] Kwani haikuwabainikia hawa wenye kumkanusha Mtume ni mara ngapi tuliwaangamiza ummah waliotangulia kabla yao na huku wanatembea kwenye makazi yao, wakawa wanayaona waziwazi, kama vile watu wa Hūd, Ṣāliḥ na Lūṭ? Hakika katika hayo kuna alama na mawaidha ya kutolea ushahidi ukweli wa Mitume waliowajia na urongo wa ushirikina walionao. Basi kwani hawasikii, hawa wenye kuwakanusha Mitume, mawaidha ya Mwenyezi Mungu na dalili Zake wakapata kunufaika nayo

    [27] Kwani hawakuona wenye kukanusha kufufuliwa baada ya kufa kwamba sisi tunayapeleka maji kwenye ardhi kavu iliyo ngumu ambayo haina mimea, tukatoa kwa maji hayo mimea yenye rangi mbalimbali yenye kuliwa na wanyama wao na miili yao ikapata chakula cha kuwafanya wao waishi kwayo? Kwani hawazioni neema hizi kwa macho yao wakajua kwamba Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwahuisha wafu na kuwafufua kutoka makaburini mwao

    [28] Hawa washirikina wanaifanyia haraka adhabu, wanasema, «Ni lini hukumu hii ya kutuadhibu, kama mnavyodai, ambayo itaamua baina yetu na nyinyi, iwapo nyinyi ni wakweli katika madai yenu?»

    [29] Waambie, ewe Mtume, «Siku ya hukumu ambayo mtateswa na mtashuhudia kifo, makafiri hakutawafaa kuamini kwao, wala hawatacheleweshwa ili watubie na warudie.»

    [30] Basi wape mgongo, ewe Mtume, hawa washirikina, na usiujali ukanushaji wao, na ungojee vile Mwenyezi Mungu Atawafanya. Hakika wao ni wenye kungojea na kutaraji mpatikane na ubaya. Basi Mwenyezi Mungu Atawapa hizaya na Atawadhalilisha na Akupe ushindi juu yao. Na Mwenyezi Mungu Ashalifanya hilo, sifa njema ni Zake na wema ni Wake

    Washirika

    Surah 33

    [1] Ewe Nabii! Endelea daima kwenye kumcha Mwenyezi Mungu kwa kuyafanya maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake, na waumini wakufuate kwa kuwa wao wanahitajia hilo zaidi kuliko wewe, na usiwatii makafiri na watu wa unafiki. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu, ni Mwenye hekima katika uumbaji Wake, amri Zake na uendeshaji mambo Wake

    [2] Na uyafuate yale uliyoletewa wahyi kutoka kwa Mola wako, ya Qur’ani na Sunnah. Hakika Mwenyezi Mungu Anayaona mnayoyafanya na ni Mwenye kuwalipa kwa hayo, hakuna kitu kinachofichamana Kwake katika hayo

    [3] Na umtegemee Mola wako, na umuachie Yeye mambo yako, na Yeye Anatosha kuwa Mtunzi kwa anayemtegemea na kurudia Kwake

    [4] Mwenyezi Mungu hakumfanya yoyote miongoni mwa wanadamu awe na nyoyo mbili kifuani mwake, na hakuwafanya wake wenu mnaojiharamisha nao kwa njia ya ẓihār kama vile uharamu wa mama zenu. (Ẓihār ni mwanamume kumwambia mkewe, ‘Wewe ni haramu kwangu kama vile mgongo wa mamangu.’ Na hii ilikuwa ni talaka katika kipindi cha ujinga (kabla ya kuja Uislamu) na Mwenyezi Mungu Akabainisha kwamba mke hawi mama kwa namna yoyote. Na Mwenyezi Mungu Hakuwafanya watoto wa kubandika kuwa ni wana katika sheria. Bali ufananishaji na mgongo na ubandikaji wana, viwili hivyo havina uhakika katika uharamishaji wa milele, kwani mke aliyefananishwa na mgongo wa mama hawi ni kama mama katika uharamu, na nasaba haithubutu kwa kujibandika wana kwa mtu kusema kuhusu mwana wa kubandika, «Huyu ni mwanangu». Kwani haya ni maneno ya mdomo yasiyo na ukweli na hayazingatiwi. Na Mwenyezi Mungu Anasema haki na Anawabainishia waja Wake njia Yake na Anawaongoza njia ya uongofu

    [5] Wale mnaodai kuwa ni wana wenu wanasibisheni na baba zao, hilo ni jambo la uadilifu zaidi na la sawa zaidi kwa Mwenyezi Mungu. Mkiwa hamuwajui baba zao wa kihakika, basi hapo waiteni kwa undugu wa Dini ambayo inawakusanya nyinyi na wao, kwani wao ni ndugu zenu katika Dini na pia ni marafiki zenu. Na nyinyi hamna dhambi kwa makosa mliyoyafanya bila kukusudia, lakini Mwenyezi Mungu Atawapatiliza mkifanya hilo kwa kusudi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa aliokosea, ni Mwingi wa rehema kwa mwenye kutubia dhambi Zake

    [6] Nabii Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ni bora kwa Waumini na ni karibu na wao zaidi kuliko nafsi zao katika mambo ya dini na dunia. Na heshima ya wake za Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa ummah wake, kama vile heshima ya mama zao, haifai kuwaoa wake za Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, baada yake. Na wenye ujamaa wa ukaribu, miongoni mwa Waislamu, baadhi yao wana haki zaidi ya kuwarithi wengine katika hukumu ya Mwenyezi Mungu na sheria Yake kuliko kurithi kwa (misingi ya) Imani na uhamiaji. (Waislamu hapo mwanzo wa Uislamu walikuwa wakirithiana kwa misingi ya hijrah (uhamiaji) na Imani au Dini na si kwa kizazi, kisha hilo likaondolewa kwa aya ya urathi), isipokuwa iwapo nyinyi, enyi Waislamu, mtawafanyia wema kwa kuwahami, kuwafanyia wema, kuwaunga na kuwaachia wasia wa kuwafaidisha. Hukumu hii iliyotajwa imekadiriwa, imeandikwa kwenye Ubao uliyohifadhiwa, basi ni lazima kwenu muifuate kivitendo. Ndani ya aya hii pana ulazima wa kuwa Mtume, rehema na amani zimshukie, awe ni mwenye kupendwa zaidi na mja kuliko nafsi yake, na ulazima wa kumfuata yeye kikamilifu. Na ndani yake pana ulazima wa kuwaheshimu mama za Waumini, wake za Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kwamba mwenye kuwatukana atarudi na hasara

    [7] Na kumbuka utaje, ewe Nabii, tulipochukua kutoka kwa Manabii ahadi ya mkazo kutekeleza ujumbe, na tukachukua ahadi kutoka kwako, na kutoka kwa Nūḥ, Ibrāhīm, Mūsā na Īsā mwana wa Maryam (nao ndio Mitume wenye nyoyo thabiti, katika kauli iliyo mashuhuri), na tukachukua kutoka kwao ahadi ya mkazo ya kufikisha ujumbe na kutekeleza amana na kuaminiana wao kwa wao

    [8] Mwenyezi Mungu Alichukua ahadi hiyo kutoka kwa Mitume hao, ili Apate kuwauliza waliotumwa vile walivyojibiwa na ummah wao, ili Mwenyezi Mungu Awalipe Pepo wenye kuamini. Na Amewaandalia makafiri, Siku ya Kiyama, adhabu kali ndani ya Jahanamu

    [9] Enyi Waumini! Ikumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Aliyowaneemesha nyinyi katika Madina siku ya vita vya Makundi (Aḥzāb), navyo ndivyo vita vya Shimo (Khandaq), walipojikusanya dhidi yenu washirikina kutoka nje ya Madina, na Mayahudi na wanafiki wakiwa ndani ya Madina na pambizoni mwake, wakawaviringa nyinyi, hapo tukayatumia yale makundi upepo mkali uliong’oa mahema yao na kuvirusha vyungu vyao, na tukawatumia Malaika kutoka mbinguni msiowaona, hapo basi nyoyo zao zikaingia kicho. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona mnayoyatenda, hakuna chochote kinachofichamana kwake katika hayo

    [10] Kumbukeni pindi walipowajia kwa juu yenu kutoka sehemu ya juu ya bonde lilioko upande wa mashariki na kwa chini yenu kutoka sehemu ya kati ya bonde lilioko upande wa magharibi, na pindi macho yalipokodoka kwa kuduwaa sana na kushutuka, na nyoyo zikafika kwenye magorombo (ya koo) kwa kitisho kikali, na wanafiki wakajawa na ukataji tamaa na uvumi ukazidi, na mkawa mnamdhania Mwenyezi Mungu dhana mbaya ya kuwa Yeye Hataiokoa Dini Yake na Hatalikuza jina Lake

    [11] Katika msimamo huo mgumu, Imani za Waumini zilijaribiwa na watu wakakaguliwa, na akajulikana mnafiki kwa kutengwa na Muumini, na wakasukikasukika msukosuko mkali kwa kuingiwa na kicho na babaiko, ili Imani yao ibainike na yakini yao izidi

    [12] Na pindi waliposema wanafiki na wale ambao ndani ya nyoyo zao mna shaka, nao ni wale madhaifu wa Imani, «Ahadi ya Mwenyezi Mungu Aliyotuahidi ya kupata ushindi na utulivu, haikuwa isipokuwa ni maneno ya urongo na udanganyifu, basi msimuamini.»

    [13] Na kumbuka, ewe Nabii, neno la kipote cha wanafiki wakiwaita Waumini miongoni mwa watu wa Madina, «Enyi watu wa Yathrib (nalo ni jina la zamani la Madina), ‘Msikae kwenye vita ambavyo mtashindwa, rudini majumbani mwenu ndani ya Madina’» Na pote lingine la wanafiki linamuomba ruhusa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kurudi majumbani mwao kwa kisingizio kuwa hayako imara, na kwa hivyo wanayaogopea, na ukweli ni kwamba hayo si hivyo, na lengo lao halikuwa isipokuwa ni kukimbia vita

    [14] Na lau jeshi la makundi lingaliingia Madina kupitia pambizoni mwake, kisha wakatakwa hawa wanafiki wamshirikishe Mwenyezi Mungu na warudi kutoka kwenye Uislamu, wangalilikubali hilo kwa haraka, na hawangalichelewesha kurudi kwenye ushirikina isipokuwa kwa muda mchache

    [15] Na kwa hakika, wanafiki hawa walimuahidi Mwenyezi Mungu kupitia kwa Mtume Wake kabla ya vita vya Shimo (Khandaq) kuwa hawatakimbia watakapohudhuria vita na hawatachelewa watakapoitwa kwenda Jihadi, lakini wao walihini ahadi yao. Na Mwenyezi Mungu Atawahesabu kwa hilo na Atawauliza kuhusu ahadi hiyo. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu itaulizwa na itahesabiwa

    [16] Sema, ewe Nabii, kuwaambia hawa wanafiki, «Kukimbia kwenu vitani kwa kuogopa kufa au kuuawa, huko hakutachelewesha muda wenu wa kuishi katika dunia hii, na mkikimbia hamtastarehe katika dunia hii isipokuwa kwa kadiri ya umri wenu uliowekewa kikomo, nacho ni muda mchache sana ukilinganishwa na Akhera.»

    [17] Sema, ewe Nabii, kuwaambia wao, «Ni nani Atakayewazuia na Mwenyezi Mungu Au Atakayewaokoa na adhabu Yake Akiwa Anawatakia ubaya au Akiwa Anawatakia rehema?» Na hakika Yeye Ndiye Mpaji, Mzuiliaji, Mwenye kudhuru, Mwenye kunufaisha? Na hawatapata hawa wanafiki, isipokuwa Mwenyezi Mungu, msaidizi wa kuwasaidia wala mnusuru wa kuwapa ushindi

    [18] Hakika Mwenyezi Mungu Anawajua wale wenye kuwavunja watu moyo wasipigane jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, na wenye kuwaambia ndugu zao, «Njooni mjiunge na sisi na muacheni Muhammad! Msihudhurie vitani pamoja na yeye.» Kwani sisi tunachelea msije mkaangamia anapoangamia yeye. Na wao, pamoja na uvunjaji moyo wao huu, hawaji vitani isipokuwa kwa tukizi, kwa kujionyesha na kutaka kusikika na kuogopa fedheha

    [19] Wanawafanyia nyinyi, enyi Waumini, ugumu wa mali, nafsi, juhudi na mapenzi kwa uadui na chuki walizonazo ndani ya nafsi zao, kwa kupenda kuishi na kuogopa kufa. Na vita vikisimama huwa wakiogopa kuangamia, na utawaona wanakuangalia, macho yao yanazunguka kwa kuwa akili zao zimeondoka kwa kuogopa na kukimbia kuuawa, kama vile macho ya mtu aliyekaribia kufa yanavyozunguka. Na vita vinapomalizika na hofu kuondoka wanawarushia nyinyi matamshi makali yenye kukera. Na utawakuta wao, zinapogawiwa ngawira, ni wachoyo na ni mahasidi. Hao hawakuamini kwa nyoyo zao ndipo Mwenyezi Mungu Akawaondolea thawabu za matendo yao, na hilo kwa Mwenyezi Mungu ni jepesi

    [20] Wanafiki wanadhani kwamba mapote ya watu ambao Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Aliwafanya washindwe, hawakuondoka kwenda zao, hivyo ni kwa sababu ya kicho na uoga. Na lau hayo mapote yangalirudi Madina wangalitamani wanafiki hao kuwa wao hawako Madina, wako pamoja na mabedui wa jangwani wantafuta habari zenu na wanauliza kuhusu wana wenu wakiwa mbali. Na lau wangalikuwa wako na nyinyi hawangalipigana pamoja na nyinyi isipokuwa kidogo, kwa uoga wao mwingi, unyonge wao na uchache wa Imani yao

    [21] Hakika yenu nyinyi, enyi Waumini, mna mfano mwema wa kuiga katika maneno ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, matendo yake na mwenendo wake. Basi jilazimisheni na mwenendo wake, kwani anaoufuata na kuuiga ni yule anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, Akamtaja Mwenyezi Mungu na kumuomba msamaha kwa wingi na akamshukuru kwa kila namna

    [22] Na Waumini walipoyashuhudia mapote ya watu waliojikusanya pambizoni mwa mji wa Madina na wakauzunguka, walikumbuka kwamba ahadi ya ushindi imekaribia na wakasema, «Haya ndiyo yale Aiyotuahidi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake ya maonjo, shida na (kisha) ushindi. Mwenyezi Mungu Alitekeleza ahadi Yake na Mtume Wake alisema kweli katika bishara njema aliyoitoa. Na hakukuwaongezea kule kuyatazama yale mapote isipokuwa kumuamini Mwenyezi Mungu na kujisalimisha na uamuzi Wake na kufuata amri Yake

    [23] Miongoni mwa Waumini kuna wanaume waliotekeleza ahadi zao walizomuahidi Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na wakasubiri juu ya shida, madhara na wakati wa vita. Kati yao kuna aliyetekeleza nadhiri akafa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu au akafa juu ya ukweli na utekelezaji ahadi, na kati yao kuna anayengojea mojawapo ya mema mawili, ushindi au kufa shahidi, na hawakuigeuza ahadi ya Mwenyezi Mungu wala hawakuitangua wala hawakuibadilisha kama vile wanafiki walivyogeuza

    [24] Ili Mwenyezi Mungu Awalipe mema watu wa ukweli kwa ukweli wao na kujitolea kwao, nao ni Waumini, na ili Awaadhibu wanafiki Akitaka kuwaadhibu, kwa kutowapa taufiki ya kutubia toba ya kidhati kabla ya kufa, hivyo basi wafe kwenye ukafiri na wastahili Moto, au Awape taufiki ya kutubia na kurejea, kwani Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe dhambi za wenye kuzidhulumu nafsi zao, ni Mwingi wa huruma kwao kwa kuwapa taufiki ya kutubia toba ya kidhati

    [25] Na Akayarudisha Mwenyezi Mungu mapote ya ukafiri kutoka Madina yakiwa yamepita patupu, yamepata hasara na yamejawa na hasira, hayakupata kheri yoyote duniani wala Akhera, na Mwenyezi Mungu Akawatosheleza Waumini (wasilazimike) kupigana kwa kuwasaidia kwa sababu Alizowatolea. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Hashindwi wala Halazimishwi, ni Mshindi katika ufalme Wake na mamlaka Yake

    [26] Na Mwenyezi Mungu Akawateremsha Mayahudi wa Banū Qurayẓah kutoka kwenye ngome zao kwa kuwa waliyasaidia Mapote katika kupigana na Waislamu, na Akatia hofu ndani ya nyoyo zao wakashindwa, mkawa mnaua kundi katika wao na mnateka kundi lingine

    [27] Na Akawamilikisha nyinyi, enyi Waumini, ardhi yao, makazi yao na mali yao yanayohamishika kama vile pambo, silaha na wanyama na yasiyohamishika kama vile mashamba, nyumba na ngome zilizojikita. Na Akawarithisha ardhi ambayo hamkuweza kuikanyaga kabla ya hapo. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu, hakuna kinachomshinda

    [28] Ewe Nabii! Waambie wake zako waliojikusanya mbele yako wakitaka kwako ongezo la matumizi, «Mkiwa mnataka maisha ya kilimwengu na pambo lake, basi njooni niwastareheshe kwa kitu kichache cha kilimwengu nilicho nacho na niwatenge bila ya kuwadhuru wala kuwaudhi

    [29] «Na mkiwa mnataka radhi ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na yale aliyowaandalia Mwenyezi Mungu katika Nyumba ya Akhera, basi vumilieni juu ya hali mliyonayo, na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, kwani hakika Mwenyezi Mungu Amewaandalia walio wema katika nyinyi malipo makubwa.» (Na walimchagua Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na yale Aliyowaandalia Mwenyezi Mungu katika Nyumba ya Akhera)

    [30] Enyi wake za Mtume! Yoyote miongoni mwenu Atakayefanya maasia yaliyo wazi ataongezewa adhabu mara mbili zaidi.( Na kwa kuwa cheo chao ni cha juu, imenasibiana na cheo hicho Mwenyezi Mungu Alifanye dhambi linalotokana na wao liwe zito, ili kuhifadhi heshima yao na heshima ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, Na kuadhibu huko ni rahisi kwa Mwenyezi Mungu)

    [31] Na mwenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake kati yenu na akafanya matendo Aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu , tutampa malipo mema ya matendo yake mara mbili zaidi ya malipo ya asiyekuwa yeye kati ya wanawake wengine, na tumemuandalia yeye riziki nzuri, nayo ni Pepo

    [32] Enyi wake wa Nabii! Nyinyi, katika utukufu na cheo, si kama wanawake wasiokuwa nyinyi iwapo mtafanya matendo ya utiifu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mtajiepusha na mambo ya kumuasi yeye. Basi msizungumze na wanaume wa kando kwa sauti nyororo yenye kumtia tamaa mwanamume ambaye kuna ubaya ndani ya moyo wake na ugonjwa wa kutamani haramu, (Hii ni adabu ya lazima kwa kila mwanamke Anayemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho.) na semeni maneno yaliyo mbali na shaka yasiyokatazwa na Sheria

    [33] Najilazimisheni kuwa majumbani mwenu, na msitoke humo isipokuwa kwa mahitaji, na msionyeshe uzuri wenu kama vile wanawake wa kipindi cha ujinga wa mwanzo walivyokuwa wakifanya, katika zama zilizotangulia Uislamu. Na maneno haya wanaambiwa wanawake wa kila zama. Na tekelezeni, enyi wake wa Nabii, Swala kwa ukamilifu katika nyakati zake, na toeni Zaka kama Alivyoamrisha Mwenyezi Mungu, na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake katika maamrisho yao na makatazo yao. Hakika si lingine Mwenyezi Mungu Amewausia haya ili Awasafishe nyinyi na Awaondolee udhia na ubaya enyi watu wa nyumba ya Nabii!, ambao miongoni mwao ni wake zake na wanaozalikana na yeye, rehema na amani zimshukie, na Azitakase nafsi zenu upeo wa kuzitakasa

    [34] Na yatajeni yale yanayosomwa ndani ya majumba yenu, ya Qur’ani na hadithi za Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiena muyafanyie kazi na muyape cheo ambacho yanastahiki., kwani hayo ni miongoni mwa neema za Mwenyezi Mungu kwenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole kwenu, kwa kuwa Amewaweka majumbani ambako aya za Mwenyezi Mungu zinasomwa na Sunnah, ni Mtambuzi wa kuwatambua nyinyi kwa kuwachagua muwe wake wa Mtume Wake

    [35] Hakika wale wanaume na wanawake wenye kufuata amri za Mwenyezi Mungu, na wanaume na wanawake wenye kuamini, na wanaume na wanawake wenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na wakweli wa kiume na wa kike, na wanaume na wanawake wenye kusubiri katika kujiepusha na matamanio na juu ya kufanya matendo ya utiifu na juu ya shida, na wanaume na wanawake wenye kumcha Mwenyezi Mungu, na wanaume na wanawake wenye kutoa sadaka za lazima na za ziada, na wanaume na wanawake wenye kufunga saumu za lazima na za ziada, na wanaume na wanawake wenye kuzihifadhi tupu zao na uzinifu na vitangulizi vyake na kujihifadhi ufunuaji uchi, na wanaume na wanawake wenye kumtaja Mwenyezi Mungu kwa wingi kwa nyoyo zao na ndimi zao, Hao Mwenyezi Mungu Amewaandalia msamaha wa dhambi zao na malipo mema makubwa, nayo ni Pepo

    [36] Na haipasi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke iwapo Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wametoa uamuzi wawe wataenda kinyume nao, kwa kuchagua lile ambalo silo alilolihukumu kwao. Na anayemuasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, amekuwa mbali na njia ya sawa umbali ulio wazi

    [37] Na pindi unaposema, ewe Nabii, kumwambia yule ambaye Mwenyezi Mungu Amemneemesha kwa Uislamu, naye ni Zayd bin Harithah ambaye Mtume , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na wewe ukamneemesha kwa kumuacha huru, «Baki na mke wako, Zaynab binti Jahsh, na usimuache! na muogope Mwenyezi Mungu , ewe Zayd!» na huku unaficha, ewe Nabii, katika nafsi yako kile Alichokuletea wahyi nacho Mwenyezi Mungu cha Zayd kumuacha Zaynab na kuwa wewe utamuoa. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ni Mwenye kudhihirisha ulichokificha, na unaogopa wasije wanafiki wakasema kwamba Muhammad amemuoa mtalaka wa mwanawe wa kubandika, na Mwenyezi Mungu Anastahiki zaidi umuogope. Basi Zayd alipomaliza haja yake kwa Zaynab na akamuacha kisha eda lake likamalizika, tulikuoza wewe, ili uwe ni kiigizo katika kubatilisha mila ya uharamishaji wa kuoa mke wa mwana wa kubandika baada ya kuachwa, wala haitakuwa kosa na dhambi kwa Wamini kuwaoa wake za wale watoto wao wa kubandika baada kuwaacha iwapo wamemaliza haja yao kwao. Na kwa hakika amri ya Mwenyezi Mungu ni yenye kufanyika, hakuna mwenye kuiwekea pingamizi wala kuizuia. Ada ya kujibandika mtoto ilikuwako zama za kijinga (kabla ya Uislamu) kisha ikabatilishwa kwa neno lake Mwenyezi Mungu, «Waiteni wao kwa kuwanasibisha na baba zao..»

    [38] Haikuwa ni dhambi kwa Nabii Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, katika kile Alichomhalalishia Mwenyezi Mungu cha kumuoa mke wa mwanawe wa kujibandika baada ya kumuacha, kama vile alivyowahalalishia hilo Manabii kabla yake yeye, ni mwenendo uliowekwa na Mwenyezi Mungu kwa wale waliopita kabla. Na kwa kweli, amri ya Mwenyezi Mungu ni mpango uliokadiriwa , hauna budi kutokea

    [39] Kisha Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika, Aliwataja Manabii waliopita na Akawasifu kwamba wao ni wale wanaozifikisha jumbe za Mwenyezi Mungu kwa watu, na wanamuogopa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, na hawamuogopi yoyote asiyekuwa Yeye. Na inatosha kuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwahesabu waja Wake kwa matendo yao yote na ni Mwenye kuyaona

    [40] Hakuwa Muhammad ni baba wa yoyote miongoni mwa wanaume wenu, lakini yeye ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu na mwisho wa Manabii, hakuna unabii baada yake mpaka Siku ya Kiyama. Na Mwenyezi Mungu kwa kila jambo miongoni mwa matendo yenu ni mjuzi, hakuna chenye kufichamana Kwake

    [41] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo, mtajeni Mwenyezi Mungu kwa nyoyo zenu, ndimi zenu na viungo vyenu utajo mwingi sana

    [42] Na zishughulisheni nyakati zenu kwa kumtaja Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, asubuhi na jioni, baada ya Swala za faradhi na nyakati za matukio maalumu na sababu, kwani huko kumtaja Mwenyezi Mungu ni ibada iliowekwa na Sheria, inapelekea kwenye mapenzi ya Mwenyezi Mungu na kujizuia na madhambi, na inasaidia kila kheri

    [43] Yeye Ndiye Anayewarehemu na kuwasifu, na Malaika Wake wanawaombea dua, ili awatoe kutoka kwenye giza la ujinga na upotevu kuwaelekeza kwenye nuru ya Uislamu.Na ni Mwenye kuwarehemu Waumini duniani na Akhera, hawaadhibu wao maadamu wao waendelea kumtii na kumtakasa

    [44] Maamkizi ya hawa Waumini kutoka kwa Mwenyezi Mungu huko Peponi Siku ya wao kukutana na Yeye ni Salām na amani kwao kutokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na Amewaandalia wao malipo Mazuri, nayo ni Pepo

    [45] Ewe Nabii! Sisi tumekutumiza uwe ni shahidi juu ya ummah wako kwa kuwafikishia ujumbe, na kuwabashiria Waumini miongoni mwao rehema na Pepo, na uwe ni mwenye kuwaonya na Moto waasi na wakanushaji

    [46] Na uwe ni mlinganizi kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumuabudu Yeye Peke Yake, na uwe ni taa yenye kung’ara kwa anayetaka kupata mwangaza kwako. Kwani jambo lako la haki ambalo umekuja nalo liko wazi kama vile jua katika kuchomoza na kutoa mwangaza, hakuna mwenye kulikanusha isipokuwa mshindani

    [47] Na uwape bishara njema, ewe Nabii, watu wa Imani kuwa watakuwa na malipo makubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, nayo ni mabustani ya Peponi

    [48] Na usilitii, ewe Nabii, neno la kafiri au mnafiki na uuache udhia wao, na hilo lisikuzuie kufikisha ujumbe, na kuwa na imani na Mwenyezi Mungu katika mambo yako yote, na umtegemee Yeye, kwani Yeye Atakutosheleza yanayokutia hamu miongoni mwa mambo yote ya ulimwengu na Akhera

    [49] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Yake kivitendo, mfungapo ndoa na wanawake na msiwaingilie, kisha mkawaacha kabla hamjawaingilia, basi hawalazimiki wakae eda lenu la nyinyi kuwahesabia, basi wapeni kitu cha kuwastarehesha katika mali yenu kulingana na ukunjufu mlionao ili kuwapa maliwazo, na wafungueni washike njia waende zao pamoja na sitara nzuri, bila ya udhia wala madhara

    [50] Ewe Nabii! Tumekuhalalishia wake uliowapa mahari yao, na tumekuhalalishia wajakazi waliomilikiwa na mkono wako miongoni mwa wale ambao Mwenyezi Mungu Amekuneemesha nao, na tumekuhalalishia kuwaoa wana wa kike wa ami zako na wana wa kike wa shangazi zako na wana wa kike wa khalati zako waliohama (kuja Madina) pamoja na wewe, na tumekuhalalishia mwanamke Muumini aliyekutunukia nafsi yake bila mahari, iwapo unataka kumuoa, hili ni lako wewe peke yako, na haifai kwa asiyekuwa wewe kumuoa mwanamke kwa kutunukiwa. Tushajua kile tulichowalazimisha Waumini kuhusu wake zao na wajakazi wao kuwa wasioe isipokuwa wake wanne, idadi wanayoitaka ya wajakazi na ulazima wa walii, mahari na mashahidi juu yao. Lakini tumekuruhusu wewe na tumekupa nafasi ambayo hatukumpa mtu mwingine asiyekuwa wewe, ili kifua chako kisiingie dhiki juu ya kuwaoa wale uliowaoa kati ya aina hizi. Hii ni miongoni mwa ziada ya utunzi wa Mwenyezi Mungu kwa Mtume Wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na takrima Yake kwake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe dhambi za waja Wake Waumini, ni Mwenye huruma kwa kuwapanulia (milango ya riziki)

    [51] Unamkalisha nyuma unayemtaka miongoni mwa wake zako katika ugawaji wa kulala, na unamleta karibu nawe unayemtaka miongoni mwao. Na yoyote unayemtaka kati ya wale uliochelewesha ugawaji wao, huna dhambi katika hilo. Kwani hiyari hiyo iko karibu zaidi ya kuwafanya wao wafurahike wala wasihuzunike na waridhike wote kwa kile ulichowagawia. Na Mwenyezi Mungu Anavijua vilivyomo ndani ya nyoyo za wanaume, vya kuelemea upande wa baadhi ya wake na kutoelekea upande wa wengine. Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa yaliyomo ndani ya nyoyo, ni Mpole, Hafanyi haraka ya kuwatesa wanaomuasi

    [52] Haifai kwako kuwaoa wanawake baada ya wake zako walio mama wa Waumini, na usiwaache wao ukawaoa wengine badala yao, kwa kuwakirimu na kushukuru mazuri waliyoyatenda ya kumchagua Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na Nyumba ya Akhera, hata kama utavutiwa na uzuri wa hao wanawake wengine, isipokuwa kile ambacho mkono wako wa kulia umemiliki, miongoni mwa wajakazi, kwani hao ni halali kwako. Na Mwenyezi Mungu anakiona kila kitu, hakuna chochote kilicho nje ya ujuzi Wake

    [53] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata Sheria Zake kivitendo, msiingie nyumba za Mtume, isipokuwa kwa ruhusa yake, kwa kula chakula bila ya kungoja kuiva kwake. Lakini mkiitwa ingieni, na mkimaliza kula ondokeni, bila ya kujipumbaza kwa mazungumzo baina yenu. Kwani kule kungoja kwenu na kujipumbaza kwenu kunamkera Nabii, naye anawaonea haya kuwatoa kwenye hizo nyumba pamoja na kuwa hiyo ni haki yake, na Mwenyezi Mungu Haoni haya kuieleza haki na kuifunua. Na mkiwaomba wake za Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wawapatie kitu chochote mnachokihitajia katika vyombo vya nyumbani na mfano wake, basi waombeni mkiwa nyuma ya pazia. Kufanya kwenu hivyo kunatakasa zaidi nyoyo zenu na nyoyo zao na kuziepusha na mawazo ambayo yanawapitia wanaume kuhusu mambo ya wanawake na wanawake kuhusu mambo ya wanaume, kwani kuona ndio sababu ya kufitinika. Na haifai kwenu kumkera Mtume wa Mwenyezi Mungu wala kuwaoa wake zake baada ya kufa kwake kabisa, kwa kuwa wao ni mama zenu, na haifai mtu kumuoa mamake. Hakika kumkera kwenu Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kuwaoa wake zake baada yake ni dhambi kubwa kwa Mwenyezi Mungu. Ummah huu ulitekeleza amri hii na ulijiepusha na kile Mwenyezi Mungu Aliukataza nacho

    [54] Mkidhihirisha chochote kwa ndimi zenu, enyi watu, kati ya vitu vinavyomkera Mtume katika vile alivyowakataza navyo au mkakificha ndani ya nafsi zenu, basi Mwenyezi Mungu, aliyetukuka anavijua vilivyomo ndani ya nyoyo zenu na vile mlivyovidhihirisha, na Atawalipa kwa hayo

    [55] Hakuna dhambi kwa wanawake kutojifinika mbele ya baba zao, wana wao wa kiume,ndugu zao wa kiume, wana wa kiume wa ndugu zao wa kiume, wana wa kiume wa ndugu zao wa kike, wanawake waumini na watumwa waliomilikiwa na wao kwa kuwa wanahitaji utumishi wao sana. Na muogopeni Mwenyezi Mungu , enyi wanawake, msipite mpaka mliowekewa mkaonyesha pambo lenu msiofaa kulionyesha, au mkaacha kujifinika mbele ya yule ambaye ni lazima mjifinike mbele yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushuhudia kila kitu, Anashuhudia matendo ya waja , ya nje na ya ndani, na Atawalipa kwayo

    [56] Hakika Mwenyezi Mungu Anamsifu Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, mbele ya Malaika waliokurubishwa. Na Malaika Wake wanamsifu Nabii na wanamuombea Mwenyezi Mungu, basi enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata sheria Zake kivitendo, mswalieni Mtume wa Mwenyezi Mungu na mtakieni amani, kwa kumwamkia na kumtukuza. Na namna ya kumswalia Nabii, rehema na amani zimshukie, imethibiti kwenye Sunnah kwa aina mabalimbali, miongoni mwazo ni: «Ewe Mola! Mrehemu Muhammad na watu wa Muhammad, kama ulivyowarehemu watu wa Ibrāhīm, hakika wewe ni Mwingi wa kushukuriwa ni Mwingi wa kutukuzwa. Ewe Mola! Mbariki Muhammad na watu wa Muhammad kama ulivyowabariki watu wa Ibrāhīm, hakika wewe ni Mwingi wa kushukuriwa, ni Mwingi wa kutukuzwa.»

    [57] Hakika ya wale wanaomuudhi Mwenyezi Mungu kwa kumshirikisha na kufanya maasia mengine, na wakamuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa maneno na vitendo, Mwenyezi Mungu atawafukuza na Atawaweka mbali na kheri duniani na Akhera, na Amewaandalia, huko Akhera, adhabu kali yenye kuwadhalilisha na kuwafanya wanyonge

    [58] Na wale wenye kuwaudhi Waumini wa kiume na Waumini wa kike kwa maneno au vitendo bila ya kosa walilolifanya, basi watakuwa wametenda tendo la urongo na uzushi mbaya kabisa, na wamefanya kosa chafu waziwazi, ambalo kwalo watastahili kupewa adhabu huko Akhera

    [59] Ewe Nabii! Waambie wake zako, watoto wako wa kike na wanawake Waumini wateremshe juu ya vichwa vyao na nyuso zao mashuka yao na mitandio yao, ili kufinika nyuso zao, vifua vyao na vichwa vyao. Kufanya hivyo kuko karibu zaidi kuwafanya wao watenganishwe kwa kusitirika na kuhifadhika, wasiwe ni wenye kusumbuliwa kwa kukerwa wala kuudhiwa. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe na kurehemu kwa kuwa Amewasamehe yaliyopita na Akawarehemu kwa kuwabainishia halali na haramu

    [60] Wasipokomeka, wale wanaoficha ukafiri na kudhihirisha Imani, wale ambao ndani ya nyoyo zao muna shaka na wasiwasi na wale wanaoeneza habari za urongo katika mji wa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na mabaya yao na shari zao, tutakupa uwezo juu yao, kisha hawatakaa pamoja na wewe humo isipokuwa muda mchache

    [61] Hali ya kuwa wamefukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu; mahali popote watakapopatikana watekwe na wawe ni wenye kuuawa muda wa kuendelea kwao katika unafiki na kueneza habari za urongo baina ya Waislamu kwa lengo la kuleta fitina na uharibifu

    [62] Huu ndio mpango wa Mwenyezi Mungu na njia Yake kuhusu ummah waliopita, ni kuwa watekwe na wawe ni wenye kuuawa popote waliopo. Na hutapata , ewe Nabii, mageuzi wala mabadiliko katika njia ya Mwenyezi Mungu

    [63] Wanakuuliza watu , ewe Mtume, kuhusu kipindi cha Kiyama kwa njia ya kukiona ni kitu ambacho ni mbali kutokea na kwa njia ya kukikanusha. Waambie, «Hakika ya mambo ni kwamba Ujuzi wa kipindi cha Kiyama uko kwa Mwenyezi Mungu.» Na ni lipi linalokujuza wewe, ewe Mtume kwamba huenda Kiyama kikawa karibu

    [64] Mwenyezi Mungu Amewafukuza makafiri kwenye rehema Yake duniani na Akhera na Amewaandalia huko Akhera Moto wenye kuwashwa ulio na joto kali

    [65] hali ya kukaa milele humo. Hawatapata mtegemewa wa kuwasaidia na kuwatetea, wala mwenye himaya wa kuwahami, Akawatoa Motoni

    [66] Siku zitakapogeuzwa nyuso za makafiri Motoni, huku wakisema kwa kujuta na kuduwaa, «Tunatamani lau tungalimtii Mwenyezi Mungu na tungalimtii Mtume Wake duniani tukawa watu wa Peponi.»

    [67] Na watasema makafiri Siku ya Kiyama, «Mola wetu! Kwa kweli sisi tumewatii viongozi wetu katika upotevu na wakubwa wetu katika ushirikina wakatuepusha na njia ya uongofu na Imani

    [68] Mola wetu! Waadhibu Motoni mara mbili zaidi ya adhabu unayotuadhibu kwayo, na uwafukuze kutoka kwenye rehema mafukuzo makali.» Katika hii pana dalili ya kwamba kumtii asiyekuwa Mwenyezi Mungu katika kuenda kinyume na amri Yake na amri ya Mtume Wake, kunapasisha kupata hasira za Mwenyezi Mungu na mateso Yake, na kwamba mfuasi na mfuatwa watashirikiana kwenye adhabu. Basi ajihadhari na hilo Muislamu

    [69] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Zake kivitendo, msimkere Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa maneno wala kwa vitendo, wala msiwe mfano wa wale waliomkera Nabii wa Mwenyezi Mungu Mūsā, Mwenyezi Mungu Akamuepusha na kile walichokisema cha urongo na uzushi, na yeye alikuwa kwa Mwenyezi Mungu ni mwenye cheo kikubwa na utukufu

    [70] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata Sheria Zake kivitendo, fanyeni matendo ya kumtii na mjiepushe na matendo ya kumuasi, ili msistahili kupata mateso hayo. Na semeni, katika hali zenu zote na mambo yenu yote, maneno ya kunyoka na yanayolingana na usawa, yasiyokuwa na urongo na ubatilifu

    [71] Mkimuogopa Mwenyezi Mungu na mkasema maneno ya sawa, Mwenyezi Mungu Atawasamehe dhambi zenu, Na mwenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, katika kile alichokiamrisha na akakikataza, basi huyo amefaulu kupata utukufu mkubwa duniani na Akhera

    [72] Sisi tuliiorodhesha amana- ambayo Mwenyezi Mungu Amewapatia waliokalifishwa na Sheria waitunze, nayo ni kufuata maamrisho na kujiepusha na makatazo- kwa mbingu, ardhi na majabali, vikakataa kuibeba na vikaogopa visiweze kusimama kuitekeleza, na akaibeba binadamu na akashikamana nayo pamoja na udhaifu Wake. Hakika yeye ni mwingi wa udhalimu na ujinga wa nafsi yake

    [73] Ili mwisho wa binadamu kuibeba amana uwe ni Mwenyezi Mungu kuwaadhibu wanafiki wa kiume wanaodhihirisha Uislamu na kuficha ukafiri na wanafiki wa kike, na wanaume wanaomshirikisha katika ibada ya Mwenyezi Mungu asiyekuwa Yeye na wanawake washirikina, na ili Awakubalie toba Waumini wa kiume na Waumini wa kike kwa kuzificha dhambi zao na kuacha kuwaadhibu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa wenye kutubia miongoni mwa waja Wake, ni Mwenye huruma kwao

    Saba

    Surah 34

    [1] Shukrani ni za Mwenyezi Mungu kwa sifa Zake ambazo zote ni sifa za ukamilifu, na kwa neema Zake za nje na za ndani za kidini na za kidunia, Ambaye Ana ufalme wa vilivyoko mbinguni na vilivyoko ardhini, na ni Zake Yeye sifa njema zilizotimia huko Akhera, na Yeye Ndiye Mwenye hekima katika matendo Yake, Aliye Mtambuzi wa mambo ya viumbe Vyake

    [2] Anakijua kila kinachoingia ardhini miongoni mwa matone ya maji na kinachotoka humo miongoni mwa mimea, madini na maji, na kinachoshuka kutoka juu miongoni mwa mvua, Malaika na Vitabu, na vinavyopanda huko miongoni mwa Malaika na matendo ya waja. Na Yeye Ndiye Mwenye kuwarehemu waja Wake, Hawaharakishii mateso wale wenye kuasi kati yao, ni Mwingi wa msamaha wa dhambi za wenye kutubia Kwake, wenye kujitegemeza Kwake

    [3] Na makafiri wenye kukanusha kufufuliwa walisema. «Kiyama hakitatujia.» Sema, ewe Mtume, uwaambie, «Kwani! Ninaapa kwa Mola wangu, kitawajia! Lakini hakuna yoyote anayejua wakati wa kuja kwake isipokuwa Mwenyezi Mungu, Mjuzi wa visivyoonekana, Ambaye haufichamani Kwake uzito wa kadiri ya chungu mdogo uliyo mbinguni au ardhini, hata mdogo zaidi kuliko huo na hata mkubwa, isipokuwa uko kwenye Kitabu kilichotunzwa, nacho ni Ubao Uliohifadhiwa

    [4] Ili Awalipe mema wale waliomuamini Mwenyezi Mungu, wakamfuata Mtume Wake na wakafanya matendo mema, hao watakuwa na msamaha wa dhambi zao na riziki njema, nayo ni Pepo.»

    [5] Na wale wanaotembea katika kuizuia njia ya Mwenyezi Mungu, kuwakanusha Mitume Wake na kuzitangua aya zetu huku wakiteta na Mwenyezi Mungu wakipinga amri Zake, hao watakuwa na adhabu mbaya zaidi na yenye ukali mwingi zaidi

    [6] Na wale waliopatiwa elimu wanajua kwamba Qur’ani uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako ndiyo haki na kwamba inaongoza kwenye njia ya Mwenyezi Mungu, Aliye Mshindi Asiyeshindwa wala kuzuiliwa, bali Amekitendesha nguvu kila kitu na Amekishinda, Ndiye Mwenye kusifiwa katika maneno Yake, matendo Yake na Sheria Zake

    [7] Na makafiri wanasema, wakiambiana wao kwa wao kwa njia ya shere, «Je, tuwaoneshe mtu ( wakimkusudia Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie) atakayewaambia kwamba nyinyi mkifa na miili yenu ikawa mbalimbali kabisa kuwa nyinyi mtahuishwa na mtafufuliwa kutoka makaburini mwenu» wanasema hayo kwa kupita kiasi katika kukanusha kwao

    [8] Kwani mtu huyu amemzulia Mwenyezi Mungu urongo, au ana wazimu na kwa hivyo anasema jambo asilolijua? Mambo si vile kama wanavyosema makafiri, bali Muhammad ni mkweli wa wakweli. Na wale wasioamini kufufuliwa na wasiofanya matendo ya kuwafaa huko, watakuwa kwenye adhabu ya milele huko Akhera, na wako kwenye upotevu wa mbali hapa duniani

    [9] Kwani hawaoni makafiri hawa wasioamini Akhera ukubwa wa uweza wa Mwenyezi Mungu juu ya vilivyoko mbele yao na nyuma yao, miongoni mwa mbingu na ardhi, vinavyoshangaza akili, na kwamba viwili hivyo vimewazunguka? Tutakapo tutawazamisha ndani ya ardhi, kama tulivyomfanyia Qārūn, au tutawateremshia vipande vya adhabu, kama tulivyowafanyia watu wa Shu'ayb, kwa hakika mbingu iliwanyeshea moto ukawaunguza. Hakika katika hilo tulilolitaja la uwezo wetu kuna ushahidi wazi kwa kila mja mwenye kurudi kwa Mola wao kwa kutubia, mwenye kukubali upweke Wake na mwenye kumtakasia ibada

    [10] Hakika tulimpa Dāwūd unabii, Kitabu na ujuzi, na tukayaambia majabali na ndege, «Takaseni pamoja naye!» (Dāwūd anapomtakasa Mwenyezi Mungu kwa kuleta tasbihi, fanyeni hivyo pamoja naye). Na tulimlainishia chuma kikawa ni kama unga uliokandwa, anakisinyanga anavyotaka

    [11] (Na tulikwambia, ewe Dāwūd,) «Tengeneze nguo za chuma zilizotimia na zilizo pana, na ukadirie vipimo vya misumari katika vikuku vya kuunganisha nguo hizo za chuma, na usikifanye kikuku kuwa kidogo kwani kitakuwa dhaifu, na kwa hivyo hizo nguo za chuma hazitaweza kumkinga (mwenye kuzivaa). Na usizifanye kubwa zikawa nzito kwa mwenye kuzivaa. Na ufanye, ewe Dāwūd, wewe na watu wako, vitendo vya kumtii Mwenyezi Mungu, kwani mimi kwa mnayoyafanya ni Mwenye kuyaona, hakifichamani kwangu kitu chochote katika hivyo.»

    [12] Na tulimdhalilishia Sulaymān upepo, ukawa unatembea kutoka mwanzo wa mchana mpaka katikati yake mwendo wa mwezi, na kutoka katikati ya mchana mpaka usiku mwendo wa mwezi kwa mwendo wa kawaida. Na tulimyayushia shaba ikawa inatiririka kama vile maji yanavyotiririka, akawa anafanya kwa shaba hiyo anachotaka. Na tulimdhalilishia miongoni mwa majini wenye kutumika mbele yake, na yoyote kati yao anayesita kufuata amri yetu tuliomuamrisha ya kumtii Sulaymān tutamuonjesha kutokana na adhabu ya Moto unaowaka

    [13] Majini wanamfanyia Sulaymān anachotaka miongoni mwa misikiti ya ibada, picha za shaba na ukoa, madishi makubwa kama mabirika ya kukusanyika maji ndani yake na vyungu vilivyojikita visivyotikisika kutoka mahali pake kwa ukubwa wake, na tukasema, «Enyi jamii ya Dāwūd! Fanyeni kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kile Alichowapa, kwa kumtii na kufuata amri Yake.» Na ni wachache, miongoni mwa waja wangu, wenye kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi. Na Dāwūd, yeye na jamii yake, alikuwa miongoni mwa hao wachache

    [14] Tulipopitisha kuwa Sulaymān afe, hakuna kilichowafahamisha majini juu ya kifo chake isipokuwa mchwa kuila fimbo yake ambayo alikuwa ameitegemea, basi Sulaymam akaanguka chini, na hapo majini wakajua kwamba wao lau walikuwa wanajua ghaibu hawangalikaa kwenye adhabu yenye kudhalilisha na kazi ngumu kumfanyia Sulaymān, kwa wao kudhania kuwa yeye ni katika walio hai. Katika hii aya kuna kubatilisha itikadi ya baadhi ya watu kwamba majini wanayajua yasiyoonekana. Kwani lau wao wangaliyajua yasiyoonekana wangalijua kifo cha Sulaymān, amani imshukie, na hawangalikaa kwenye adhabu yenye kunyongesha

    [15] Kwa hakika, kabila la Saba’ la huko Yaman, kwenye makazi ya watu wake kuna dalili ya uweza wetu: mabustani mawili kuliani na kushotoni, «Kuleni riziki ya Mola wenu na mumshukuruni kwa neema Zake juu yenu, kwani nchi yenu ina mchanga bora na hewa nzuri, na Mola wenu ni Mwingi wa msamaha kwenu.»

    [16] Wakaipa mgongo amri ya Mwenyezi Mungu, wakaacha kumshukuru na wakawakanusha Mitume, tukawatumia mafuriko yenye kubomoa yaliyo na nguvu, yaliyoliharibu bwawa la maji na yakayazamisha mabustani. Na tukawageuzia mabustani yao mawili yenye kutoa matunda yakawa ni mabustani mawili yenye miti michache ya khamṭ, nayo ni miti ya matunda machungu yenye ladha ya kuchukiza, na athl, nayo ni miti inayofanana na ṭarfā ’isiyokuwa na matunda, na mikunazi michache yenye miba mingi

    [17] Mabadiliko hayo, kutoka kwenye mambo mazuri kwenda kwenye mabaya, ni kwa sababu ya kukanusha kwao na kutoshukuru kwao neema za Mwenyezi Mungu. Na hatumtesi mateso haya makali isipokuwa mkanushaji sana aliyeendelea kwenye ukanushaji; atalipwa kulingana na matendo yake, sawa kwa sawa

    [18] Na tulijaalia, baina ya watu wa Saba’ na hali wao wako Yaman, na ile miji tuliobarikia, nayo ni Shām, kuwe na miji iliyoshikana, aliye kwenye mji wowote kati ya hiyo huuona mji mwingine. Na tukafanya mwendo wa kutembea humo ni mwendo uliokadiriwa, kutoka nyumba hadi nyumba, bila mashaka, na tukawaambia, «Endeni kwenye miji hiyo , wakati mnapotaka wa usiku au mchana, mkiwa mko kwenye amani hamuogopi adui, njaa wala kiu

    [19] Kwa sababu ya kuruka mipaka kwao, walichoka na raha na amani na maisha ya neema na wakasema, «Mola wetu! Ifanye miji yetu iwe mbali mbali ili safari zetu zirefuke baina ya miji hiyo, tusipate mji ulioimarika njiani tunapokwenda.» Na wakajidhulumu nafsi zao kwa kukanusha kwao, na kwa hivyo tukawaangamiza na tukawafanya ni mazingatio na mazungumzo kwa wanaokuja baada yao, na tukawatenganisha kila namna ya kuwatenganisha, na miji yao ikawa magofu. Kwa hakika yale yaliyoikumba Saba’ ni mazingatio kwa kila mwingi wa uvimilivu juu ya shida na mambo magumu, mwingi wa kushukuru neema za Mwenyezi Mungu Aliyetukuka

    [20] Na kwa hakika alidhani Iblisi dhana isiyo ya ukweli kuwa atawapoteza wanadamu na kwamba wao watamtii yeye katika kumuasi Mwenyezi Mungu, na dhana yake kwao ikawa ya kweli, kwa kuwa wao walimtii yeye na wakamuasi Mola wao , isipokuwa kundi la wenye kumuamini Mwenyezi Mungu, kwani wao walijikita kwenye utiifu wa Mwenyezi Mungu

    [21] Na wala hakuwa iblisi na uwezo wa kuwalazimisha wakanushaji kukufuru, lakini hekima ya Mwenyezi Mungu imepitisha awapambie wanadamu ili ujitokeze ujuzi Wake wa kale tupate kumpambanua anayeamini kufufuliwa, thawabu na adhabu na kumtenganisha na yule mwenye shaka na hilo. Na Mola wako ni Mtunzi wa kila jambo, Analihifadhi na kutoa malipo yake

    [22] Sema, ewe Mtume, uwaambie washirikina, «Waiteni wale ambao mlidai kuwa wao ni washirika wa Mwenyezi Mungu mkawaabudu badala Yake , miongoni mwa masanamu , malaika na binadamu, na wakusudieni katika haja zenu. Kwani wao hawatawaitika. Wao hawamiliki chochote, mbinguni wala ardhini, hata kadiri ya uzito wa chungu mdogo, na wala hawana ushirika katika hizo mbili. Na hakuna yoyote miongoni mwa hawa washirikina mwenye kumsaidia kuumba chochote. Bali Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, ndiye Aliyepwekeka kwa upatishaji.Yeye Ndiye Anayeabudiwa Peke Yake, na hakuna mwingine yoyote asiyekuwa Yeye anayestahiki kuabudiwa

    [23] Na maombezi ya mwenye kuombea hayafal kitu hayanufaishi mbele Yake, isipokuwa kwa yule Aliyemruhusu. Na miongoni mwa utukufu Wake na utisho Wake, Aliyeshinda na kutukuka, ni kuwa Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Anapotamka wahyi na watu wa mbinguni wakayasikia maneno Yake, wanakuwa katika hali ya kutetemeka kwa utisho, mpaka wanakuwa katika hali kama ile ya kukosa fahamu. Na kibabaiko kinapowaondokea kwenye nyoyo zao wanaulizana wao kwa wao, «Amesema nini Mola wenu?» Malaika watasema, «Amesema kweli! Na Yeye Yuko juu kwa dhati Yake, utendaji nguvu Wake na utukufu wa cheo Chake, Aliye Mkubwa juu ya kila kitu.»

    [24] Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina, «Ni nani anayewaruzuku kwa mvua kutoka mbinguni, na kwa mimea na madini na vinginevyo kutoka ardhini?» Hivyo basi hawana budi kukubali kuwa Yeye ni Mwenyezi Mungu. Na iwapo hawatakubali hilo, waambie, «Mwenyezi Mungu Ndiye Mwingi wa kuruzuku, na kwa hakika mojawapo wa mapote mawili, kati ya sisi na nyinyi, limejikita kwenye uongofu au limevama kwenye upotevu ulio wazi.»

    [25] Sema, «Hamtaulizwa kuhusu dhambi zetu, wala hatutaulizwa kuhusu matendo yenu, sababu sisi tumejitenga na nyinyi na ukanushaji wenu.»

    [26] Sema, «Mola wetu Atatukusanya baina yetu na nyinyi Siku ya Kiyama, kisha Atatoa uamuzi wa uadilifu baina yetu. Na Yeye Ndiye Mfunguzi Mwenye kutoa uamuzi baina ya viumbe Vyake, Mwingi wa ujuzi wa yale yanayotakikana yatolewe uamuzi na hali ya viumbe Vyake. Hakuna kinachofichicana Kwake chochote.»

    [27] Sema, «Nionesheni kwa hoja na dalili wale mliomshikanisha na Mwenyezi Mungu mkawafanya ni washirika Wake katika kuabudiwa, je wao wameumba chochote? Mambo si kama walivyoeleza.Bali Yeye Ndiye Mwenye kuabudiwa kwa haki, ambaye hana mshirika wake, aliye Mshindi katika kuwatesa waliomshirikisha, na mwenye hekima katika maneno Yake, vitendo Vyake na upelekeshaji mambo ya viumbe Vyake

    [28] Na hatukukutumiliza, ewe Mtume, isipokuwa ni kwa watu wote, uwabashirie malipo mema ya Mwenyezi Mungu na uwaonye mateso Yake. Lakini wengi wa watu hawaijui haki, hivyo basi wao wanaipa mgongo

    [29] Na hawa washirikina wanasema kwa njia ya shere, «Ni lini wakati wa Ahadi hii ambayo unatuahidi kuwa Mwenyezi Mungu Atatukusanya ndani yake kisha Ahukumu baina yetu, iwapo nyinyi ni wakweli katika kile mlichotuahidi kwacho?»

    [30] Waamnbie, ewe Mtume, «Nyinyi muna maagano ambayo hapana budi yatawajia, nayo ni maagano ya Siku ya Kiyama, hamtachelewa nayo hata muda mchache wa kupata kutubia, na wala hamtatangulia mbele yake mkaadhibiwa hata kwa muda mchache. Basi jihadharini na Siku hiyo na jitayarisheni kwa vifaa vyake.»

    [31] Na waliokanusha walisema, «Hatutaiamini hii Qur’ani wala vile vilivyoitangulia, kina Taurati, Injili na Zaburi.» Kwa hakika washakanusha vitabu vyote vya Mwenyezi Mungu. Na lau utaona pindi madhalimu wamefungwa mbele ya Mola wao ili wahesabiwe, huku wakirudishiana maneno baina yao, kila mmoja anamtupia lawama mwingine, utaona jambo la kutisha! Watakuwa waliokuwa wakifanywa wanyonge wakisema kuwaambia wale waliokuwa na kiburi, nao ni wale viongozi na wakubwa waliopotea na kupoteza, «Lau si nyinyi kutupoteza njia tungalikuwa ni wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake.»

    [32] Viongozi watasema kuwaambia wale waliofanywa wanyonge, «Kwani ni sisi tuliowazuia uongofu baada ya kuwajia? Bali ni nyinyi wenyewe mlikuwa wahalifu kwa kuwa mliingia kwenye ukafiri kwa matakwa yenu na hiyari yenu.»

    [33] Watasema waliofanywa wanyonge kuwaambia wakubwa wao katika upotevu, «Bali ni kule kutupangia kwenu ubaya usiku na mchana ndiko kulikotutia sisi katika majanga. Kwa kuwa mlikuwa mkitutaka tumkanushe Mwenyezi Mungu na tumfanye kuwa ana washirika katika kuabudiwa.» Na watu wa kila mojawapo ya makundi mawili wataficha majuto watakapoiona adhabu ilioandaliwa wao. Na tutaweka minyororo kwenye shingo za wale waliokanusha. Na wao hawatateswa kwa adhabu hii isipokuwa ni kwa sababu ya kumkanusha kwao Mwenyezi Mungu na kufanya kwao matendo mabaya duniani. Katika hii aya kuna onyo kali dhidi ya kuwafuata walinganizi wa upotevu na viongozi wa ukiukaji Sheria

    [34] Na hatukutumiliza Mtume yoyote katika mji wowote alinganie kwenye kumwahidisha Mwenyezi Mungu na kumpwekesha katika ibada, isipokuwa wale wenye kuvama kwenye starehe na matamanio miongoni mwa watu wake huwa wakisema, «Hakika sisi kwa haya mliokuja nayo, enyi Mitume, ni wenye kukanusha.»

    [35] Na wanasema, «Sisi ni wengi zaidi wa mali na watoto, na Mwenyezi Mungu hakutupa neema hizi isipokuwa ni kuwa anaridhika na sisi, na sisi si wenye kuadhibiwa duniani wala Akhera.»

    [36] Sema uwaambie, ewe Mtume, «Hakika Mola wangu Anawakunjulia riziki hapa duniani anaowataka miongoni mwa waja Wake, na Anawabania Anaowataka, si kwa mapenzi wala chuki, lakini Anafanya hivyo kwa kuwatahini. Lakini wengi wa watu hawajui kwamba huo ni mtihani kwa waja Wake kuwa wao hawataamali.»

    [37] Hayakuwa mali yenu na watoto wenu ni vitu vya kuwafanya nyinyi muwe karibu na sisi, na daraja zenu ziwekwe juu, lakini wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na wakafanya matendo mema, basi hao watapata malipo ya nyongeza: kwa jema moja kwa kumi mfano wake mpaka kiwango cha nyongeza Anachokitaka Mwenyezi Mungu. Na wao watakuwa kwenye Pepo ya juu kwa juu, wakiwa wamesalimika na adhabu, kifo na mambo ya huzuni

    [38] Na wale wanaokimbilia kuzibatilisha hoja zetu na wanaozuia njia ya Mwenyezi Mungu isifuatwe wakiwa wapinzani na washindani, hawa wataingia ndani ya adhabu ya Jahanamu Siku ya Kiyama, watahudhuriwa na Zabāniyah, ambao ni askari wa Motoni, na hawatatoka humo

    [39] Waambie, ewe Mtume, hawa waliodanganyika kwa mali na watoto, «Mola wangu anamkunjulia riziki Anayemtaka miongoni mwa waja Wake na Anambania Anayemtaka, kwa hekima Anayoijua. Na namna mtakavyotoa kitu chochote, Yeye Atawapa badala yake duniani na huko Akhera Atawapa malipo mema. Na Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye bora wa wenye kuruzuku, basi tafuteni riziki Kwake Peke Yake na zungukeni kwa kufuata sababu zake Alizowaamuru

    [40] Kumbuka, ewe Mtume, Siku ambayo Mwenyezi Mungu Atawafufua washirikina na waabudiwa badala Yake miongoni mwa Malaika, kisha Awaambie Malaika kwa njia ya kuwalaumu wale waliowaabudu, «Je ni hawa waliokuwa wakiwaabudu badala yetu sisi?»

    [41] Malaika watasema, «Tunakutakasa, ewe Mwenyezi Mungu, na kuwa na mshirika wa kuabudiwa! wewe Ndiye Msimamizi wetu tunayemtii na kumuabudu Peke Yake. Bali hawa walikuwa wakiwaabudu mashetani, wengi wao wanawaamini na kuwatii.»

    [42] Basi Siku ya Ufufuzi, hao waabudiwa hawatakuwa na mamlaka ya kuwanufaisha au kuwadhuru wenye kuwaabudu. Na tutasema kuwaambia wale waliozidhulumu nafsi zao, «Onjeni adhabu ya Moto ambao mlikuwa mkiukanusha!»

    [43] Na wanaposomewa makafiri wa Makkah aya za Mwenyezi Mungu zikiwa wazi wao wanasema, «Hakuwa Muhammad isipokuwa ni mtu anayependa kuwakataza nyinyi kuwaabudu waungu ambao baba zenu walikuwa wakiwaabudu,» na wanasema, «Haikuwa hii Qur’ani isipokuwa ni urongo uliozuliwa, umeuleta wewe mwenyewe na sio kuwa unatoka kwa Mwenyezi Mungu.» Na makafiri walisema kuhusu Qur’ani ilipowajia, «Haikuwa hii isipokuwa uchawi uliojitokeza wazi.»

    [44] Na hatukuwateremshia wakanushaji vitabu vya wao kuvisoma kabla ya Qur’ani vikawa vitawaonyesha wao yale wanayoyadai kwamba kile alichokuja nacho Muhammad ni uchawi, na hatukumtuma kwao kabla yako wewe, mjumbe yoyote wa kuwaonya wao adhabu yetu

    [45] Na walikanusha wale waliokuwa kabla yao, kama vile 'Ād na Thamūd, Na watu wa Makkah hawakufikia ushuri wa kile tulichowapa ummah waliopita cha nguvu, wingi wa mali, umri mrefu na neema nyiginezo, na tukawaangamiza. Basi angalia, ewe Mtume! Ni namna gani yalivyokuwa makemeo yangu na adhabu yangu kwao

    [46] Sema, ewe Mtume, uwaambie hawa wakanushaji washindani, «Mimi ninawapa ushauri mmoja: msimame kumtii Mwenyezi Mungu wawili-wawili na mmoja-mmoja, kisha mfikirie kuhusu hali ya mwenzenu, Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kile alichonasibishwa nacho. Yeye hana wazimu. Hakuwa Yeye isipokuwa ni mwenye kuwatisha na kuwaonya adhabu ya Jahanamu kabla joto lake halijawasumbua.»

    [47] Sema, ewe Mtume, uwaambie wakanushaji, «Malipo niliyowaomba kwa wema huu niliowaletea ni yenu nyinyi. Malipo yangu mimi ninayoyangojea hayapo isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu Mwenye kuyaona matendo yangu na matendo yenu.Hakuna chochote kinachofichamana Kwake. Yeye Anawalipa wote: kila mmoja kwa anachostahiki.»

    [48] Sema, ewe Mtume, umwambie anayekanusha upwekeshaji wa Mwenyezi Mungu na ujumbe wa Uislamu, «Hakika Mola wangu Anauvurumiza ubatilifu kwa hoja za ukweli, hivyo basi ukaufedhehi na ukauangamiza. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi mno wa vitu visivyoonekana, hakuna kinachofichamana Kwake chochote ardhini na mbinguni.»

    [49] Sema, ewe Mtume, «Ukweli na Sheria tukufu itokayo kwa Mwenyezi Mungu umekuja, na ubatilifu umeondoka na mamlaka yake yamepotea, hivyo basi ubatilifu haukusaliwa na kitu cha kukianzisha wala kukirudisha.»

    [50] Sema, «Nikipotoka nikawa kando na haki, basi dhambi la upotevu wangu liko juu ya nafsi yangu, na nikiwa nitalingana sawa juu ya haki, ni kwa wahyi wa Mwenyezi Mungu Ambao Ananiletea mimi. Hakika Mola wangu ni Msikizi wa ninayowaambia, Yuko karibu na yule anayemlingania na kumuomba.»

    [51] Na lau ungaliona, ewe Mtume, pindi watakapobabaika wakanushaji pale watakapoishuhudia adhabu ya Mwenyezi Mungu, ungaliona jambo kubwa! Hawatakuwa na uokozi wala makimbilio na watachukuliwa hadi Motoni kutoka mahali karibu pa kutwaliwa

    [52] Na wakanushaji watasema watakapoiona adhabu huko Akhera, «Tumemuamini Mwenyezi Mungu, Vitabu Vyake na Mitume Wake. Vipi wao waipate Imani na hali ni kwamba kuifikia kwao hiyo Imani ni kutoka mahali mbali?» kushawekwa kizuizi baina yao na hiyo, kwani mahali pake ni ulimwenguni, na huko walikanusha

    [53] Kwa hakika waliikanusha haki duniani na wakawakanusha Mitume. Na wanajisemea kwa kudhani wakiwa mbali na kuifikia haki, hawana tegemezi la dhana yao ya ubatilifu, kwa hivyo hawana njia ya kuifikia haki kama vile mfumaji asivyo na njia ya kulenga shabaha kutoka mahali mbali

    [54] Na kutawekwa kizuizi baina ya wakanushaji na kile wanachokitamani cha toba na kurudi ulimwenguni wapate kuamini, kama vile Mwenyezi Mungu Alivyowafanya wale wanaofanana na wao miongoni mwa wakanushaji wa watu wa mataifa yaliyopita. Kwa kweli wao walikuwa duniani wako kwenye shaka yenye kutia wasiwasi na babaiko kuhusu jambo la Mitume, kufufuliwa na kuhesabiwa, na kwa hivyo hawakuamini

    Muumba

    Surah 35

    [1] Sifa njema zote asifiwe Mwenyezi Mungu kwa sifa Zake ambazo zote ni za ukamilifu, na kwa neema Zake za nje na za ndani, za Akhera na duniani. Muumba mbingu na ardhi na Muanzilishi wa hizo. Mwenye kuwafanya Malaika ni wajumbe kwa waja kwa Anayemtaka miongoni mwa waja Wake, na kwa amri Yake anayoitaka na makatazo Yake. Na miongoni mwa ukubwa wa uweza wa Mwenyezi Mungu ni kuwafanya Malaika ni wenye mbawa, mbilimibili, tatutatu na nnenne, za kurukia: ili kukifikisha Alichoamrisha Mwenyezi Mungu. Katika uumbaji Wake Anaongeza Anachotaka. Hakika Mwenyezi Mungu kwa kila jambo ni Mjuzi, hakuna kitu kinachomshinda

    [2] Chochote kile Anachowafungulia watu Mwenyezi Mungu miongoni mwa riziki, mvua, afya, ujuzi na neema nyinginezo, hakuna yoyote wa kuzuia rehema hii, na chochote kile anachokizuia hakuna yoyote baada Yake, Kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, anayeweza kukiachilia. Na Yeye Ndie Mshindi Mwenye kukitendesha nguvu kila kitu, Mwingi wa hekima Ambaye Anaiachilia rehema na Anaizuia kulingana na hekima Yake

    [3] Enyi watu! Kumbukeni, kwa nyoyo zenu, ndimi zenu na viungo vyenu, neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu. Hakuna muumba wenu isipokuwa Mwenyezi Mungu, Anayewaruzuku nyinyi kwa mvua kutoka mbinguni, na kwa maji, madini na vinginevyo kutoka ardhini. Hapana Mola isipokuwa Yeye, Peke Yake, Asiye na mshirika. Basi vipi nyinyi mtaepushwa na kumpwekesha

    [4] Na watu wako wakikukanusha, ewe Mtume, kwa hakika wamekanushwa Mitume kabla yako wewe. Na kwa Mwenyezi Mungu mambo yanaishia huko Akhera, basi hapo Atamlipa kila mmoja anachostahili. Katika hii pana kumliwaza Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [5] Enyi watu! Hakika agizo la Mwenyezi Mungu la Ufufuzi, malipo mema na mateso ni kweli iliyothibiti, basi yasiwadanganye maisha ya duniani kwa matamanio yake na matakwa yake, wala asiwadanganye Shetani kuhusu Mwenyezi Mungu

    [6] Hakika Shetani ni adui ya binadamu, basi mchukulieni ni adui na msimtii, hakika ni kwamba yeye anawaita wafuasi wake kwenye upotevu ili wawe ni katika watu wa Moto unaowaka

    [7] Wale waliokataa kwamba Mwenyezi Mungu, Yeye Peke Yake, Ndiye Mola wa kweli, na wakakataa kile walichokuja nacho Mitume Wake, watakuwa na adhabu kali huko Akhera. Na wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafanya matendo mema, watapata msamaha kutoka kwa Mola wao na kufutiwa dhambi zao baada ya kuzifanya zisitirike, na watakuwa na malipo mema makubwa, nayo ni Pepo

    [8] Je, yule ambaye Shetani anampambia matendo yake maovu ya kumuasi Mwenyezi Mungu, kukufuru na kuwaabudu wasiyekuwa Yeye miongoni mwa waungu na masanamu, akayaona ni mazuri yenye kupendeza, (Je, yeye) ni kama yule ambaye Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Amemuongoza akaliona zuri kuwa ni zuri na ovu kuwa ni ovu? Hakika Mwenyezi Mungu Anampoteza Anayemtaka na Anamuongoza Anayemtaka. Basi usijiangamize kwa kuwa na huzuni juu ya ukanushaji wa hawa waliopotea. Hakika Mwenyezi Mungu Anayajua maovu yao na Atawalipa kwa hayo malipo mabaya kabisa

    [9] Na Mwenyezi Mungu Ndiye Ambaye Anapeleka upepo, ukatikisa mawingu, tukayaongoza hadi pale kwenye ardhi kavu, hapo mvua ikateremka, tukahuisha kwa mvua hiyo ardhi baada ya ukavu wake, na hapo mimea ikawa rangi ya kijani. Mfano wa kuhuisha huko, Mwenyezi Mungu Atawahuisha wafu Siku ya Kiyama

    [10] Yoyote yule atakaye enzi ya duniani au Akhera, basi aitake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na hilo halipatikani isipokuwa kwa kumtii Yeye, kwani enzi yote ni ya Mwenyezi Mungu. Na mwenye kujienzi na kiumbe, Mwenyezi Mungu Atamdhalilisha; na Mwenye kujienzi na Muumba, Mwenyezi Mungu Atamtukuza. Kwake Yeye utajo wake utapanda, na tendo lema Analiinua juu. Na wale wenye kutenda mabaya watapewa adhabu kali. Na vitimbi vya hao vitaangamia na vitaharibika na havitawafaidisha kitu chochote

    [11] Na Mwenyezi Mungu Alimuumba baba yenu Ādam kwa mchanga kisha Akajaalia kizazi chake kitokamane na maji matwevu, kisha Akawafanya nyinyi ni wanaume na wanawake. Na hakuna mwanamke yoyote anayeshika mimba wala anayezaa isipokuwa Analijua hilo. Na hakuna mtu anayepewa maisha marefu au umri wake ukapunguzwa isipokuwa hayo yamo ndani ya Kitabu kilichoko Kwake, nacho ni Ubao Uliohifadhiwa, kabla mamake hajashika mimba yake na kabla hajamzaa. Hayo yote Mwenyezi Mungu Ameyadhibiti ameyajua kabla hajamuumba, hayataongezwa yale aliyoandikiwa wala hayatapunguzwa. Hakika kule kuwaumba nyinyi, kuzijua hali zenu na kuziandika kwenye Ubao Uliohifadhiwa ni jambo rahisi na sahali kwa Mwenyezi Mungu

    [12] Na hazilingani bahari mbili: hii ni tamu yenye upeo wa utamu, ni laini kupita kooni, inaondosha kiu, na hii (nyingine) ni ya chumvi yenye uchumvi mkali. Na kutokana na kila mojawapo ya bahari mbili mnakula samaki wazuri wenye ladha ya kupendeza, na mnatoa pambo, ambalo ni lulu na marjani, la nyinyi kulivaa. Na utaviona vyombo ndani ya bahari hizo vinapasua maji, ili mkiwa mnatafuta kheri Zake katika biashara na megineyo. Katika haya kuna dalili ya uweza wa Mwenyezi Mungu na upweke Wake, na huenda nyinyi mkamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema hizi ambazo Amewaneemesha nazo

    [13] Na Mwenyezi Mungu Anazitia nyakati za usiku ndani mchana, hivyo basi mchana ukarefuka kwa kadiri ya usiku uliopungua; na Anazitia nyakati za mchana ndani ya usiku, hivyo basi usiku ukarefuka kwa kadiri ya mchana uliopungua. Na Amedhalilisha jua na mwezi vikawa vinatembea kwa wakati maaalumu. Huyo aliyefanya hili ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu. Ni Wake Yeye ufalme wote. Na wale mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu hawamiliki hata utandu mwembamba unaozunguka koko ya tende

    [14] Mnapowaomba, enyi watu, waabudiwa hawa badala ya Mwenyezi Mungu, hawasikii maombi yenu, na lau wangalisikia, kwa kukisia, hawangaliwaitikia nyinyi. Na Siku ya Kiyama, watajiepusha na nyinyi. Na hakuna yoyote wa kukupasha habari, ewe Mtume, mkweli zaidi kuliko Mwenyezi Mungu, Aliye Mjuzi, Aliye Mtambuzi

    [15] Enyi watu! Nyinyi ndio wahitaji wa Mwenyezi Mungu katika kila kitu, hamjitoshelezi Naye hata kiasi cha kupepesa jicho. Na Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Mwenye kujitosheleza na watu na kila kitu miongoni mwa viumbe Vyake, Mwenye kushukuriwa kwa dhati Yake na majina Yake na sifa Zake, Anaeshukuriwa kwa neema Zake. Kwani kila neema waliyo nayo watu inatoka Kwake. Sifa njema zote ni Zake na shukrani kwa kila namna

    [16] Akitaka Mwenyezi Mungu Atawaangamiza nyinyi, enyi watu, na Awalete watu wengine Ambao watamtii na watamuabudu Peke Yake

    [17] Na halikuwa hili la kuwaangamiza nyinyi na kuwaleta viumbe wasiokuwa nyinyi ni jambo lisiowezekana kwa Mwenyezi Mungu, bali hilo ni jambo jepesi na rahisi

    [18] Na kiumbe yoyote Aliyefanya dhambi hatabeba dhambi za mtu mwingine. Na mtu yoyote aliyelemewa na dhambi, akiomba mwenye kumbebea dhambi zake, hatapata mwenye kumbebea chochote, hata kama yule aliyemuomba ana ujamaa wa karibu na yeye, kama baba au ndugu na mfano wao. Hakika ni kwamba wewe, ewe Mtume, unawaonya wale wanaoogopa adhabu ya Mola wao pamoja na kuwa wao hawaioni na wakatekeleza Swala inavyotakikana itekelezwe. Na mwenye kujisafisha na ushirikina na maasia mengine, basi yeye anajisafisha nafsi yake. Na kwa Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, ndio marejeo ya viumbe wote na mwisho wao, hapo Amlipe kila mmoja kile anachostahiki

    [19] Na kipofu asiyeiona Dini ya Mwenyezi Mungu halingani na yule mwenye kuona ambaye anaiona njia ya haki na anaifuata

    [20] Na giza la ukafiri halilingani na mwangaza wa Imani

    [21] wala kivuli hakilingani na upepo wa joto

    [22] Na wale waliohuika nyoyo kwa kukuamini hawalingani na wale waliokufa nyoyo kwa kukanusha. Hakika Mwenyezi Mungu Anamsikilizisha Anayemtaka asikie kwa kufahamu na kukubali. Na wewe, ewe Mtume, si mwenye kuwasikilizisha walio ndani ya makaburi. Na kama usivyoweza kuwasikilizisha wafu makaburini mwao, pia hutawasikilizisha hawa makafiri kwa kuwa nyoyo zao zimekufa

    [23] Wewe hukuwa isipokuwa ni mwenye kuwaonya ghadhabu za Mwenyezi Mungu na mateso Yake

    [24] Sisi tumekutumiliza kwa haki, nayo ni kumuamini Mwenyezi Mungu na Sheria za Dini, hali ya kuwapa bishara ya Pepo wale wenye kukuamini na wakaufuata uongofu wako kivitendo, na hali ya kuwaonya Moto wale waliokukanusha na wakakuasi. Na hakuna taifa lolote la watu isipokuwa limejiwa na muonyaji wa kuwaonya mwisho mbaya wa ukafiri wao na upotevu wao

    [25] Na wanapokukanusha washirikina hawa , basi wale waliopita kabla yao waliwakanusha Mitume wao ambao waliwajia na miujiza iliyo wazi yenye kutolea ushahidi unabii wao, na waliwajia na Vitabu, ambavyo ndani yake zimekusanywa hukumu nyingi, na (waliwajia na) Kitabu chenye kutoa mwangaza chenye kubainisha njia ya kheri na shari

    [26] Kisha nikawakamata wale waliokanusha na kuwapa aina mbalimbali za adhabu. Basi angalia kulikuwa namna gani kukataa kwangu matendo yao na kule kuwashukia wao mateso yangu

    [27] Kwani huoni kwamba Mwenyezi Mungu Ameteremsha kutoka juu maji, tukainywesha kwayo miti iliyo ardhini, tukatoa kwenye miti hiyo matunda yenye rangi tofauti, miongoni mwazo ni nyekundu na miongoni mwazo nyeusi na manjano na zisizokuwa hizo? Na tumeumba majabalini njia zenye rangi tofauti, nyeupe na nyekundu. Na tumeumba miongoni mwa majabali, majabali meusi sana

    [28] Na miongoni mwa watu na wanyama, ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo tumeumba wakiwa rangi tofauti vilevile. Kati ya hao kuna wekundu, weupe weusi na wenye rangi nyinginezo, kama vile kutofautiana rangi za matunda na majabali. Hakika wanaomcha Mwenyezi Mungu na kujikinga na mateso Yake kwa kumtii na kujiepusha kumuasi ni wale wanaomjua Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake,sifa Zake na Sheria Zake, na uweza Wake juu ya kila kitu ambao miongoni mwavyo ni kutofautiana viumbe hivi pamoja na kuwa sababu yake ni moja, na wanayatia akilini yaliyomo ndani ya mawaidha na mazingatio. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mshindi Mwenye nguvu Asiyeshindwa, Mwingi wa kusamehe Anawapa malipo mema watiifu, na Anawasamehe

    [29] Hakika ya wale wanaosoma Qur’ani na wakaifanyia kazi, wakaendelea daima kuswali kwa nyakati zake na wakatumia kile tulichowaruzuku miongoni mwa aina ya matumizi ya lazima na ya yanayopendekezwa, kwa siri na kwa dhahiri, hao wana matumaini kwa hayo kufanya biashara isiyoenda na isiyoanguka, nayo ni kuridhiwa na Mola wao na kufaulu kupata malipo mema mengi Yake

    [30] Ili Awatimizie Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, malipo mema ya matendo yao yakiwa kamili bila kupunguzwa, na wataongezewa mema kwa fadhila Zake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehefu sana wa makosa yao, ni Mwingi wa shukrani kwa mema yao, Atawalipa kwa mema hayo malipo mazuri mengi

    [31] Na Qur’ni tuliyokuteremshia wewe, ewe Mtume, ndiyo haki inayosadikisha Vitabu Alivyoviteremsha Mwenyezi Mungu kwa Mitume Wake kabla yako. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtambuzi wa mambo ya waja Wake, ni Mwenye kuviona vitendo vyao, na Atawalipa wema kwa hayo

    [32] Kisha tukawapa Qur’ani, baada ya ummah waliopita kuangamia, wale tuliowachagua miongoni mwa umati wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie: kati yao kuna aliyeidhulumu nafsi yake kwa kufanya baadhi ya maasia, na kati yao kuna aliyekuwa wastani, naye ni yule mwenye kutekeleza yaliyo wajibu na kuepuka yaliyoharamishwa, na katika wao kuna mwenye kutangulia kufanya mambo ya kheri kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, yaani mwenye kukimbilia na kujitahidi kufanya amali njema, za faradhi na za ziada. Na kupewa Kitabu huko na kuchaguliwa ummah huu ndio nyongeza kubwa

    [33] Pepo za makazi ya daima kwa wale ambao Mwenyezi Mungu Amewarithisha Kitabu Chake, watapambwa huko kwa vikuku vya dhahabu na kwa lulu. Na mavazi yao ya kawaida huko Peponi ni hariri, yaani: nguo laini

    [34] Na watasema watakapoingia Peponi, «Sifa njema zote na shukrani ni za Mwenyezi Mungu Ambaye ametuondolea kila jambo la huzuni. Hakika Mola wetu ni Mwingi wa msamaha, kwa kuwa Anatusamehe sisi madhambi madogo, ni Mwingi wa shukrani, kwa kuwa Ameyapokea mazuri yetu na Ameyaongeza

    [35] Na Yeye Ndiye Aliyetushukisha Nyumba ya Pepo kwa fadhila Zake, haitatugusa humo usumbufu wala uchovu

    [36] Na wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, watakuwa na Moto wa Jahanamu uliowashwa. Hakutatolewa uamuzi juu yao kuwa wafe wakapata kufa na kupumzika, wala hawatapunguziwa adhabu yake. Mfano wa malipo hayo, Mwenyezi Mungu Anamlipa kila mwenye kuendelea kwenye ukafiri na kuwa na ukakamavu juu yake

    [37] Na hawa makafiri watapiga kelele kwa ukali wa adhabu ndani ya Moto wa Jahanamu wakiomba kuokolewa, «Mola wetu! Tutoe kwenye Moto wa Jahanamu na uturudishe duniani tupate kufanya matendo mema ambayo siyo yale tuliokuwa tukiyafanya katika uhai wetu wa duniani, tupate kuamini badala ya kukanusha.» Hapo Mwenyezi Mungu Awaambie, «Kwani hatukuwapa katika kipindi cha uhai kadiri inayotosha ya umri kwa mwenye kutaka kuwaidhika awaidhike, na akawajia Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na pamoja na hivyo msiwaidhike? Basi onjeni adhabu ya Jahanamu! Kwani wenye kukanusha hawana msaidizi wa kuwaokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu

    [38] Kwa hakika Mwenyezi Mungu Anakiona kila kisichoonekana mbinguni na ardhini, na kwa hakika Yeye ni Mjuzi mno wa vilivyofichamana nyoyoni. Basi muogopeni Asiwaone mkiwa mko katika hali ya kudhamiria shaka au ushirikina katika kumpwekeshaYeye au juu ya unabii wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani ziwashukie, au muende kinyume na amri Yake katika mambo madogo ya hayo

    [39] Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyewafanya nyinyi, enyi watu, baadhi yenu washikilie nafasi ya wengine katika ardhi. Basi Mwenye kukanusha upweke wa Mwenyezi Mungu miongoni mwenu madhara yake yatamrudia mwenyewe na ule ukafiri wake. Na hauwaongezei wakanushaji ule ukanushaji wao mbele ya Mola wao isipokuwa hasira na ghadhabu, na hakuwaongezei kule kumkanusha kwao Mwenyezi Mungu isipokuwa upotevu na maangamivu

    [40] Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina, «Nipasheni habari: Ni kitu gani cha ardhi ambacho washirika wenu wamekiumba? Au hawa washirika wenu mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu wana ushirika na Mwenyezi Mungu katika uumbaji mbingu? Au tumewapa kitabu, hivyo basi wana ushahidi kutoka humo?» Lakini wakanushaji hawapeani ahadi isipokuwa udanganyifu na uhadazi

    [41] Hakika Mwenyezi Mungu Anazizuia mbingu na ardhi siziondoke pale zilipo. Na lau zitaondoka pale zilipo, hakuna yoyote baada Yake Atakayezizuia. Mwenyezi Mungu ni Mpole katika kuahirisha mateso kwa makafiri na waasi, ni Mwingi wa kusamehe kwa anayetubia dhambi zake na akarudi Kwake

    [42] Na wakanushaji wa Kikureshi waliapa kwa Mwenyezi Mungu viapo vikali kwamba wakijiwa na mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu wa kuwaonya mateso ya Mwenyezi Mungu, watakuwa ni wenye kusimama wima zaidi na wenye kufuata haki zaidi kuliko Mayahudi, Wanaswara na wengineo. Na alipowajia Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, hilo halikuwaongezea wao isipokuwa kuwa mbali na haki na kuikimbia

    [43] Kuapa kwao si kwa nia nzuri na kutafuta haki, isipokuwa huko ni kuwafanyia viumbe kiburi katika ardhi, wanakusudia kwa huko kuapa kufanya vitimbi vibaya, udanganyifu na ubatilifu. Na vitimbi vibaya haviwashukii isipokuwa wenyewe. Basi je, wana lolote la kunngojea, hao wenye kiburi na wenye vitimbi, isipokuwa ile adhabu iliyowashukia waliokuwa kama wao ambao waliwatangulia? Hutaupatia mpango wa Mwenyezi Mungu mabadiliko wala mageuko. Hakuna yoyote anayeweza kubadilisha wala kujiepusha na adhabu yeye mwenyewe wala mwingine

    [44] Je, hawatembei makafiri wa Makkah kwenye ardhi, wakaona ulikuwa vipi mwisho wa wale waliokuwa kabla yao, kama vile 'Ād, Thamūd na mfano wao, na yale yaliyowapata ya maangamivu na yaliyowapata majumba yao ya uharibifu walipowakanusha Mitume, na makafiri hao walikuwa ni wakali zaidi na ni wenye nguvu zaidi kuliko makafiri wa Makkah? Na hakuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kuna kitu chochote mbinguni wala ardhini chenye kumlemea na kumpita. Hakika Yeye ni Mjuzi sana wa matendo yao ni Mwenye uweza wa kuwaangamiza

    [45] Na lau Mwenyezi Mungu Angaliwatesa watu kwa madhambi na maasia waliyoyatenda, Hangaliacha juu ya mgongo wa ardhi mnyama yoyote anayetembea juu yake. Lakini Anawapa muhula na Anachelewesha kuwaadhibu mpaka wakati maalumu Aliyoupanga. Na wakati wa kuwaadhibu ukija , basi Mwenyezi Mungu kwa waja Wake ni Mjuzi, hakuna yoyote kati yao atakayefichika Kwake, na hakuna chochote miongoni mwa mambo yao kilicho mbali na ujuzi Wake, na Atawalipa wao kwa walichotenda, chema au kibaya

    Yaa Siin

    Surah 36

    [1] «Yā Sīn» Yametangulia maelezo kuhusu herufi zilizokatwa na kutengwa mwanzo wa sura ya Al-Baqarah

    [2] Anaapa Mwenyezi Mungu kwa Qur’ani yenye hekima, kwa hukumu zilizomo, hekima na hoja

    [3] kwamba wewe, ewe Mtume, ni miongoni mwa waliotumilizwa na wahyi wa Mwenyezi Mungu kwa waja Wake

    [4] juu ya njia iliyonyoka na kulingana sawa, nayo ni Uislamu

    [5] Ameiteremsha Mwenyezi Mungu hii Qur’ani ikiwa ni teremsho kutoka kwa Aliye Mshindi, katika kuwaadhibu watu wa ukafiri na maasia, Mwenye kuwarehemu waja Wake waliotubia na wakatenda mema

    [6] Tumekuteremshia wewe, ewe Mtume, ili uwaonye nayo watu ambao baba zao kabla yako wewe hawakuonya, nao ni Warabu. Watu hawa wameghafilika na wamepitikiwa na Imani na msimamo imara wa kufanya matendo mema. Na kila watu ambao uonyaji kwao umekatika, wanaingia kwenye mghafala na kupitikiwa. Katika haya kuna dalili ya ulazima juu ya wanavyuoni, wanaomjua Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, kulingania na kukumbusha, ili wawaamshe Waislamu kutoka kwenye mghafala wao

    [7] Hakika imeshapasa adhabu juu ya wengi wa hawa makafiri, baada ya kuonyeshwa haki wakaikataa, kwa kuwa hawamuamini Mwenyezi Mungu wala Mtume Wake wala hawafuati Sheria Zake kivitendo

    [8] Hakika sisi tumewafanya hawa makafiri, ambao walionyeshwa haki wakaikataa na wakawa wakakamavu kushikilia ukafiri na kuacha kuamini, ni kama wale waliofungwa pingu shingoni mwao, ikakusanywa pamoja mikono yao pamoja na shingo zao chini ya videvu vyao, wakalazimika kuinua juu vichwa vyao. Basi wao wamefungwa na kuepushwa na kila kheri, hawaioni haki wala hawaongoki kuifuata

    [9] Na tumeweka mbele ya makafiri kizuizi na nyuma yao kizuizi. Basi yeye ni kama wale waliyofungiwa njia mbele yao na nyuma yao, hapo tukayapofusha macho yao kwa sababu ya ukanushaji wao na kiburi chao, hivyo basi wakawa hawaoni usawa wala hawaongoki. Na kila mwenye kuukabili ulinganizi wa Uislamu kwa kuupa mgongo na kuufanyia ushindani, basi yeye ni mstahili wa kupata mateso haya

    [10] Kunalingana sawa, mbele ya makafiri hawa washindani, kuwa utawaonya, ewe Mtume, au hutawaonya, kwani wao hawaamini wala hawafanyi matendo mema

    [11] Hakika ni kwamba uonyaji wako unamfaa mwenye kuiamini Qur’ani, akafuata hukumu za Mwenyezi Mungu zilizo ndani yake na akamuogopa Mwingi wa rehema akiwa mahali ambapo hakuna amuonaye isipokuwa Mwenyezi Mungu. Basi huyo mpe bishara njema ya kuwa atapata msamaha wa dhambi zake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na atapata malipo mema kutoka Kwake huko Akhera kwa matendo yake mema, nayo ni Pepo

    [12] Hakika sisi ndio tunaohuisha wafu wote kwa kuwafufua Siku ya Kiyama, na tunaandika waliyoyafanya ya kheri na shari, na zile athari zao njema ambazo wao walikuwa ndio sababu ya kufanyika katika maisha yao na baada ya kufa kwao, ziwe njema kama vile mtoto mwema, elimu yenye manufaa na sadaka yenye kuendelea, na ziwe mbaya kama vile ushirikina na uasi. Na tumedhibiti kwa hesabu kila kitu katika Kitabu chenye ufafanuzi, ambacho ni Asili ya Kitabu, na humo ndio marejeo ya yote hayo, nacho ni Ubao Uliohifadhiwa. Basi ni juu ya mwenye akili airudie nafsi yake, ili awe ni kiigizo katika wema ndani ya maisha yake na baada ya kufa kwake

    [13] Wapigie, ewe Mtume, washirikna wa watu wako wenye kukataa ulinganizi wako, mfano wa wao kuuzingatia nao ni hadithi ya watu wa kijiji walipoendewa na wajumbe

    [14] Tulipowatumia wajumbe wawili wawalinganie kumuamini Mwenyezi Mungu na kuacha kumuabudu asiyekuwa Yeye. Watu wa kijiji wakawakanusha wajumbe wawili hao tukawatilia nguvu kwa mjumbe wa tatu. Basi hao wajumbe watatu walisema kuwaambia watu wa kijiji, «Hakika sisi kwenu nyinyi,enyi watu, tumetumwa.»

    [15] Watu wa kijiji wakasema kuwaambia wajumbe, «Hamkuwa nyinyi isipokuwa ni watu mfano wetu sisi, na Mwenyezi Mungu Hakuteremsha wahyi wowote. Na hamkuwa nyinyi isipokuwa mnasema urongo.»

    [16] Wajumbe wakasema kwa kutilia mkazo,»Mola wetu Aliyetutuma Anajua kwamba sisi, kwenu nyinyi, tumetumwa

    [17] Na si juu yetu isipokuwa ni kufikisha ujumbe kwa uwazi, na hatuna mamlaka ya kuwafanya muongoke, kwani uongofu uko mikononi mwa Mwenyezi Mungu Peke Yake.»

    [18] Watu wa kijiji wakasema, «Sisi tumeingiliwa na kisirani kutokana na nyinyi, basi msipokomeka kutulingania,tutawaua kwa kuwapiga mawe na mtapata kutoka kwetu adhabu kali iumizayo.»

    [19] Wajumbe wakasema, «Kisirani chenu na matendo yenu ya ushirikina na ya shari yako na nyinyi na yanarudishwa kwenu nyinyi. Je, nyinyi mkiwaidhiwa kwa jambo ambalo lina kheri kwenu mnajihisi mmeingiliwa na kisrani na mnatutisha kuwa mtatupiga mawe na kutuadhibu? Bali nyinyi ni watu ambao desturi yenu ni kupita kiasi katika uasi na ukanushaji

    [20] Na akaja mtu kwa haraka kutoka mahali mbali mjini (Napo ni pale ilipojulikana kwamba watu wa kijiji wameazimia kuwaua wajumbe au kuwaadhibu) akasema, «Enyi watu wangu! Wafuateni wajumbe mlioletewa kutoka kwa Mwenyezi Mungu

    [21] Wafuateni wale wasiotaka mali kutoka kwenu kwa kufikisha Ujumbe na hali wao wako kwenye uongofu katika kile wanachowaitia cha kumuabudu Mwenyezi Mungu Peke Yake.» Katika hii kuna kueleza ubora wa mwenye kukimbilia kuamrisha mema na kukataza maovu

    [22] «Na ni kitu gani kitakachonizuia kumuabudu Mwenyezi Mungu Aliyeniumba na Ambaye Kwake mtarejea nyote

    [23] Je, niwaabudu waungu wengine wasiomiliki jambo lolote badala ya Mwenyezi Mungu? Iwapo Mwingi wa rehema Amenitakia mabaya, basi waungu hawamiliki kulikinga hilo wala kulizuia, wala hawawezi kuniokoa mimi na haya niliyonayo

    [24] Mimi nifanyapo hivyo nitakuwa niko kwenya kosa lililo wazi lililojitokeza

    [25] Mimi nimemuamini Mola wenu, basi nisikilizeni nililowaambia na mnitii mimi kwa kuniamini.» Aliposema hilo, watu wake walimrukia wakamuua, na Mwenyezi Mungu Akamtia Peponi

    [26] Aliambiwa baada ya kufa kwake, «Ingia Peponi,» kwa njia ya kutukuzwa

    [27] Akasema na yeye akiwa kwenye starehe na heshima, «Natamani watu wangu wangalijua vile Mola wangu Alivyonisamehe na kunikirimu kwa sababu ya kumuamini kwangu Mwenyezi Mungu na kusubiri kwangu juu ya kumtii Yeye na kuwafuata Mitume Wake mpaka nikauawa, ili nao wamuamini Mwenyezi Mungu na waingie Peponi kama mimi.»

    [28] Na jambo hilo halikuhitajia kuteremsha askari kutoka mbinguni ili kuwaadhibu wao baada ya wao kumuua yule mwanamume anayewapa ushauri mwema na kuwakanusha wajumbe wao, kwani wao ni wanyonge na watwevu zaidi kuliko kuwa ni wenye kufanyiwa hilo na hatukuwa ni wenye kuwateremsha Malaika tukitaka kuwaangamiza, bali tunawateremshia adhabu ya kuwavunjavunja

    [29] Hakukuwa kule kuangamizwa kwao isipokua ni kwa ukelele mmoja, wakitahamaki wao wamekufa, hakuna chochote kilichosalia katika wao

    [30] Ni hasara iliyoje na majuto yalioje ya waja Siku ya Kiyama watakapoiona adhabu! Hawajiwi na mtume yoyote kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, isipokuwa huwa wakimfanyia shere na maskhara

    [31] Kwani hawaoni hawa wanaofanya shere na wakapata mazingatio kwa watu wa kame zilizotangulia kabla yao tulizoziangamiza, kuwa wao hawatarudi kwenye dunia hii

    [32] Hawakuwa watu wa kame hizi tulizoziangamiza na wengineo, isipokuwa wote watahudhurishwa mbele yetu Siku ya Kiyama wahesabiwe na walipwe

    [33] Na ili kuwaonyesha hawa washirikina ushahidi wa uweza wa Mwenyezi Mungu wa kufufua na kukusanya ni hii ardhi iliyokufa isiyo na mimea, tumeihuisha kwa kuteremsha maji, na tukatoa humo aina mbalimbali za mimea ambayo watu na wanyama wanakula. Na Mwenye kuhuisha ardhi kwa mimea Ndiye Atakayehuisha viumbe baada ya kufa

    [34] Na tumejaalia katika ardhi hii mabustani ya mitende na mizabibu, na tukapasua humo mikondo ya maji yenye kuinywesheza

    [35] Yote hayo ili waja wapate kula matunda yake. Na hayo hayakuwa isipokuwa ni rehema ya Mwenyezi Mungu kwao, na si kwa harakati zao za kutafuta na bidii zao, wala si kwa hila zao na nguvu. Basi si wamshukuru Mwenyezi Mungu Aliyewaneemesha neema hizi ambazo hazihesabiki wala hazidhibitiki

    [36] Ametakasika Mwenyezi Mungu Aliye Mkubwa, Aliyeumba mbea zote miongoni mwa aina za mimea ya ardhini, na kutokana na nafsi zao wakiwa wanaume na wanawake, na kutokana na viumbe vya Mwenyezi Mungu na vinginevyo. Hakika Mwenyezi Mungu Amepwekeka kwa uumbaji, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, hivyo basi haifai Ashirikishwe na mwingine

    [37] Na alama kwao yenye kuonyesha upwekeshaji wa Mwenyezi Mungu na ukamilifu wa uweza Wake ni huu usiku ambao kutoka humo unatolewa mchana, wakitahamaki watu wameingiliwa na giza

    [38] Na alama kwao (ya utendakazi wa Mwenyezi Mungu) ni jua ambalo linatembea hadi kituo chake Alichokikadiria Mwenyezi Mungu, halitakipita kituo hiko wala halitatulia kabla ya kukifikia. Huo ni mpango wa Mshindi Asiyeshindwa, Mjuzi Ambaye hakuna kitu chochote kinachofichamana na ujuzi Wake

    [39] Na mwezi ni alama katika viumbe vyake. Tumeukadiria uwe na njia za kupitia kila usiku. Unaanza ukiwa mwezi mwandamo mdogo sana na unaendelea kuwa mkubwa mpaka ukawa mwezi mkamilifu mviringo, kisha unarudi kuwa mdogo kama karara la mtende lililobeteka kwa wembamba, kuinama na umanjano, kwa sababu ya ukale wake na ukavu

    [40] Kila mojawapo kati ya jua, mwezi, usiku na mchana, kina wakati ambao Mwenyezi Mungu Ameukadiria, na hakitangulii kikapita huo wakati. Haiwezekani kwa jua kuufikia mwezi likaufuta mwangaza wake au ukageuza njia yake ya kupitia. Na haiwezekani kwa usiku kuutangulia mchana ukauingilia kabla ya wakati wake kumalizika. Na kila mojawapo kati ya jua, mwezi na nyota ziko katika anga zinatembea

    [41] Na ushahidi na hoja kwao kwamba Mwenyezi Mungu Peke Yake Ndiye Mstahiki wa kuabudiwa, Ndiye mneemeshaji neema nyingi, ni kwamba sisi tuliwabeba wale waliookoka miongoni mwa wanadamu katika jahazi la Nūḥ lililojazwa jinsi mbalimbali ya viumbe, ili maisha yaendelee baada ya mafuriko

    [42] Na tukawaumbia hawa washirikina na wasiokuwa wao kama vile jahazi la Nūḥ, miongoni mwa majahazi na vipando vingine wanavyovipanda vikawapeleka kwenye nchi zao

    [43] Na tukitaka tutawazamisha , w'asipate mwenye kuwasaidia wasizame, na wala wao si wenye kuokolewa na kuzama

    [44] Isipokuwa tuwahurumie, tuwaokoe na tuwastareheshe mpaka muda ukome, huenda wao wakarejea na wakayarakebisha yale waliyoyafanyia kasoro

    [45] Na washirikina wanapoambiwa, «Jihadharini na jambo la Akhera na vituko vyake, hali za dunia na mateso yake, kwa kutarajia rehema ya Mwenyezi Mungu kwenu,» wanapuuza na hawalikubali hilo

    [46] Na huwajii, hawa washirikina, na alama yoyote iliyo wazi kutoka kwa Mola wao, ili uwaongoze kwenye haki na uwabainishie ukweli wa Mtume, isipokuwa wanaipa mgongo na wasinufaike nayo

    [47] Na waambiwapo makafiri, «Toeni ile riziki ambayo Mwenyezi Mungu Amewaneemesha nayo,» wanasema kuwaambia Waumini, wakijenga hoja, «Je, tumpe chakula yule ambaye lau Mwenyezi Mungu Alitaka Angalimpa chakula? Hamkuwa nyinyi, Waumini, isipokuwa mko mbali waziwazi na haki, kwa kutuamrisha sisi hilo.»

    [48] Na wanasema hawa makafiri kwa njia ya kukanusha na kuwa na haraka, «HukuKufufuliwa kutakuwa lini, iwapo nyinyi ni wakweli katika hilo mnalolisema?»

    [49] Hawangojei hawa washirikina wanaolifanyia haraka agizo la Mwenyezi Mungu kwao, isipokuwa mvuvio wa fazaa wakati Kiyama kitakaposimama, kitawachukua ghafla, na hali wao wanagombana katika mambo ya maisha yao

    [50] Hawataweza hawa washirikina wakati wa kuvuviwa barugumu kumuusia yoyote kitu chochote, wala hawataweza kurejea kwa watu wao, bali watakufa wakiwa kwenye masoko yao na pale walipo

    [51] Na kutavuviwa kwenye barugumu mvuvio wa pili, hapo roho zao zirudishwe kwenye miili yao, wakitahamaki wanatoka makaburini mwao wakielekea kwa Mola wao kwa haraka

    [52] Hapo watasema wenye kukanusha Ufufuzi hali ya kujua, «Ewe maangamivu yetu! Ni nani aliyetutoa makaburini mwetu?» Hapo wajibiwe na waambiwe, «Hili ndilo lile Aliloahidi Mwingi wa rehema na wakalitolea habari Mitume walio wakweli.»

    [53] Hakutakuwa kufufuliwa huku isipokuwa ni matokeo ya mvuvio mmoja katika barugumu, punde si punde viumbe wote watasimama watakuwa wamesimama mbele yetu wapate kuhesabiwa na kulipwa

    [54] Katika Siku hiyo hesabu itakamilishwa kwa uadilifu. Hakuna nafsi itakayodhulumiwa kitu chochote, kwa kupunguzwa mema yake au kuongezwa maovu yake. Na hamtalipwa isipokuwa kwa yale mliokuwa mkiyafanya ulimwenguni

    [55] Hakika watu wa Peponi Siku hiyo watakuwa wameshughulishwa kwa aina mbalimbali za neema za wao kustarehe nazo, hawawafikirii watu wengine

    [56] Wao na wake zao watakuwa wanajistarehesha juu ya vitanda vilivyopambwa , na chini ya vivuli vilivyoenea

    [57] Wao Peponi watakuwa na starehe ya matunda yenye ladha ya kila aina, na watakuwa na kila wanalolitaka

    [58] Watakuwa na starehe nyingine kubwa kabisa nayo ni Atakaposema nao Mola wao, Mwenye kuwarehemu kwa kuwasalimia, na hapo watapata amani iliyotimia kwa kila namna

    [59] Na wataambiwa makafiri Siku hiyo, «Jitengeni na Waumini na mjiepushe nao.»

    [60] Na Mwenyezi Mungu Atawaambia kwa kuwalaumu na kuwakumbusha, «Kwani sikuwausia, kupitia ndimi za Mitume wetu kwamba msiabudu Shetani wala msimtii? Hakika yeye ni adui ambaye uadui wake umejitokeza wazi

    [61] «Na nikawaamrisha mniabudu mimi peke yangu, kwani kuniabudu mimi na kunitii na kumuasi Shetani ndiyo Dini iliyonyoka yenye kupelekea kupata radhi zangu na mabustani ya Pepo yangu

    [62] «Hakika Shetani amewapoteza na kuwatoa kwenye haki viumbe wengi kabla yenu. Basi kwani hamkuwa na akili, enyi washirikina, ya kuwakataza nyinyi kumfuata

    [63] «Huu ni moto wa Jahanamu ambao mlikuwa mkiahidiwa duniani kwa kumkufuru kwenu Mwenyezi Mungu na kukanusha kwenu Mitume Wake

    [64] «Basi uingieni leo na mteseke kwa joto lake, kwa sababu ya ukafiri wenu

    [65] Siku hiyo tutaipiga muhuri midomo ya washirikina hawatakuwa ni wenye kusema, na itasema na sisi mikono yao kwa yale iliyoyafanya ya maonevu, na itatoa ushahidi miguu yao kwa yale iliyoyaendea duniani na dhambi ilizozichuma

    [66] Na lau tutataka tutayafuta macho yao na kuondoa maangalizi yao, kama tulivyoifunga midomo yao, hapo waikimbilie njia ya Ṣirāṭ ili waivuke. Basi vipi hilo litakuwa kwao na hali macho yao yamefutwa hayaoni

    [67] Na lau tunataka tutaligeuza umbo lao na kuwakalisha mahali pao, wasiweze kuenda mbele wala kurudi nyuma

    [68] Na yoyote tutakayeurefusha umri wake mpaka awe mkongwe tunamrudisha kwenye hali ya udhaifu wa akili na udhaifu wa mwili. Basi hawatii akilini kwamba yule Aliyefanya hili ni mwenye uweza wa kuwafufua

    [69] Na hatukumfundisha mjumbe wetu Muhammad mashairi, na haipasi kwake kuwa mshairi. Haikuwa hii aliokuja nayo isipokuwa ni Ukumbusho kwa wale wenye busara kujikumbusha nao na ni Qur’ani yenye kufafanua haki na batili, hukumu zake ziko wazi, na pia hekima zake na mawaidha yake

    [70] ili imuonye ambaye moyo wake uko hai na akili yake ina nuru, na ili ithibiti adhabu kwa wenye kumkanusha Mwenyezi Mungu, kwa kuwa wao, kwa hii Qur’ani, hoja ya Mwenyezi Mungu ya mkato imewasimamia

    [71] Kwani viumbe hawaoni kwamba sisi tumeumba kwa ajili yao wanyama tuliowadhalilishia wakawa wanawamiliki na kusimamia mambo yao

    [72] Na tukawadhalilishia (hao wanyama kwao). Katika hao kuna wanaowapanda katika safari, na katika hao kuna wanaowabebesha mizigo, na katika hao kuna wanaowala

    [73] Na katika hao wanyama, wana manufaa mengine ya kunufaika nayo, kama vile kunufaika kwa sufi zao, mabele yao na nywele zao kwa matumizi ya nyumbani, mavazi na mengineyo, na wanakunywa maziwa yao. Basi hawamshukuru Mwenyezi Mungu, Ambaye Amewapa neema hizi, na kumtakasia ibada

    [74] Na washirikina waliwafanya wasiokuwa Mwenyezi Mungu kuwa ni waungu wakawa wanawaabudu, wakitarajia kuwa watawasaidia na kuwaokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu

    [75] Waungu hao hawawezi kuwasaidia wenye kuwaabudu wala kujisaidia wao wenyewe. Na washirikina pamoja na waungu wao wote watahudhurishwa kwenye adhabu, wakiwa baadhi yao wanajitenga na wengine

    [76] Basi kusikutie huzuni, ewe Mtume, kule kumkufuru kwao Mwenyezi Mungu na kukukanusha wewe na kukufanyia shere. Hakika sisi tunayajua wanayoyaficha na wanayoyadhihirisha, na tutawalipa kwa hayo

    [77] Kwani haoni mwanadamu anayekanusha kufufuliwa vile umbo lake lilivyoanza akapata kuchukua dalili ya kuwa atarudishwa uhai, kwamba sisi tumemuumba kwa tone la manii lililopitia miongo tofauti mpaka akawa mkubwa, na ghafla anageuka kuwa ni mwingi wa utesi aliyejitolea wazi kwa kujadiliana

    [78] Na mkanushaji Kufufuliwa alitupigia mfano usiofaa kupigwa, nao ni kulinganisha uweza wa Muumba na ule wa muumbwa, na akasahau kulianzaje kule kuumbwa kwake. Alisema, «Ni nani mwenye kuhuisha mifupa iliyochakaa na kumumunyuka

    [79] Mwambie, «Atakaye kuihuisha ni Yule Aliyeiumba mara ya kwanza, na Yeye kwa viumbe vyake vyote ni Mjuzi, hakifichamani Kwake yeye kitu chochote

    [80] «Ambaye Amewatolea, kwenye mti wa kijani ulio mbichi, moto unaochoma, ambao kwa mti huo mnawasha moto.» Yeye Ndiye Anayeweza kutoa, kwenye kitu, kinyume chake. Katika hayo pana dalili ya upweke wa Mwenyezi Mungu na ukamilifu wa uweza Wake, na miongoni mwa uweza huo ni kuwatoa wafu kutoka makaburini mwao wakiwa hai

    [81] Je, kwani hakuwa yule aliyeumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ni Mwenye uweza wa kuumba mfano wao, Akawarudisha kama Alivyowaanzisha? Ndio , kwa kweli Yeye Analiweza hilo. Na Yeye ni Mwenye sifa kamilifu zauumbaji viumbe vyote , Aliye Mjuzi wa kila Alichokiumba na Atakachokiumba, hakuna kinachofichamana na Yeye

    [82] Hakika amri Yake Anapotaka kitu kiwe ni kukiambia, «Kuwa!» Na kikawa. Na kati ya hizo ni kufisha, kuhuisha, kufufua na kukusanya

    [83] Ameepukana Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kutakasika, na ulemevu na kuwa na mshirika. Yeye Ndiye Mwenye kumiliki kila kitu, Mwenye kuendesha mambo ya viumbe Vyake bila ya kuwa na mshindani au mpinzani. Na zimejitokeza dalili za uwezaWake na ukamilifu wa neema Zake. Na Kwake Yeye mtarejea ili mhesabiwe na mlipwe

    Wanaopanga safu

    Surah 37

    [1] Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anaapa kwa Malaika wanaojipanga, katika kuabudu kwao, mistari iliyofuatana na kushikana

    [2] na kwa Malaika wanaofukuza mawingu na kuyaongoza kwa amri ya MwenyeziMungu

    [3] na kwa Malaika wanaosoma utajo wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na maneno Yake

    [4] kwamba muabudiwa wenu, enyi watu, ni Mmoja, Asiye na mshirika. Hivyo basi mtakasieni ibada na utiifu. Na Anaapa Mwenyezi Mungu kwa Anachotaka miongoni mwa viumbe Vyake. Ama kiumbe, hafai kuapa isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu, kwani kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu ni ushirikina

    [5] Yeye Ndiye Muumba mbingu na ardhi na vilivyoko baina ya hivyo viwili, na Ndiye Mpelekeshaji jua katika sehemu zake za kuchomozea na zile za kuchwea

    [6] Sisi tumeupamba uwingu wa karibu kwa pambo la nyota

    [7] Na tumeuhifadhi huo uwingu, kwa nyota, na kila shetani mwenye kuasi, mjeuri, aliyefukuzwa (kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu)

    [8] Hawawezi hao Mashetani kufika kwenye viumbe vya juu, navyo ni mbingu na Malaika waliyomo ndani yake, wakapata kuwasikiliza wanapoutamka wahyi ambao Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anauleta, unaokusanya sheria Yake na makadirio Yake, na wanavurumizwa vimondo katika kila upande

    [9] kwa kuwafukuza ili wasipate kusikiliza. Na huko kwenye Nyumba ya Akhera watakuwa na adhabu ya daima yenye kuumiza

    [10] Isipokuwa yule aliyenyakuwa, miongoni mwa Mashetani, mnyakuo wa haraka, nao ni lile neno analolisikia mbinguni kwa haraka, akamtupia aliyekuwa chini yake, na yule mwingine akamtupia aliyekuwa chini yake. Basi pengine huenda akafikiwa na kimondo chenye kutoa mwangaza kabla hajalitupa, na pengine huwa amelitupa kwa makadirio ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kabla ya kujiwa na kimondo kikamchoma, na yule mwingine akaenda nalo hadi kwa makuhani wakaongeza juu ya neno hilo maneno mia moja ya urongo

    [11] Basi waulize, ewe Mtume, wenye kukanusha Kufufuliwa: Je kuumbwa kwao ni kugumu zaidi au ni hivyi viumbe tulivyoviumba? Kwa hakika, tulimuumba baba yao Ādam kwa udongo ulioshikana na kuambatana

    [12] Bali ulistaajabu, ewe Mtume, kwa ukanushaji wao na kukataa kwao Kufufuliwa. Na la kustaajabiwa zaidi na lililo kubwa zaidi kuliko lile la kukataa kwao ni kwamba wao wanakucheza shere na kulidharau neno lako

    [13] Na wanapokumbushwa walichokisahau au walichoghafilika nacho, hawanufaiki kwa huo ukumbusho wala hawazingatii

    [14] Na wanapoiona miujiza yenye kutolea dalili unabii wako, wanakufanyia shere na wanastaajabu

    [15] Na wanasema, «Halikuwa hili ulilotuletea isipokuwa ni uchawi uliojitokeza waziwazi

    [16] Je, tunapokufa na tukawa ni mchanga na mifupa iliyochakaa, je sisi ni wenye kufufuliwa kutoka makaburini mwetu tukiwa hai

    [17] au pia watafufuliwa baba zetu waliopita kabla yetu?»

    [18] Waambie, ewe Mtume, «Ndio mtafufuliwa hali mkiwa wanyonge, watwevu.»

    [19] Hakika ni kwamba huo utakuwa ni Mvuvio mmoja, wakitahamaki wao wamesimama kutoka makaburini mwao, wanatazama vituko vya Kiyama

    [20] Na watasema, «Ewe maangamivu yetu! Hii ni siku ya kuhesabiwa na kulipwa!»

    [21] Hapo wataambiwa, «Hii ndiyo Siku ya Uamuzi wa haki baina ya viumbe, ambayo mlikuwa mkiikanusha duniani na mkiikataa.»

    [22] Na Malaika wataambiwa, «Wakusanyeni wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu na wafananao na wao na waungu wao waliokuwa wakiwaabudu

    [23] badala ya Mwenyezi Mungu, na muwasukume kwa nguvu hadi kwenye moto wa Jahanamu

    [24] «Na muwafunge kabla hawajafika kwenye moto wa Jahanamu, kwa kuwa wao ni wenye kuulizwa kuhusu matendo yao na maneno yao yaliyotokana na wao duniani, kwa namna ya kumshtukia kuwakaripia.»

    [25] Na wataambiwa kwa kulaumiwa, «Kwa nini hamsaidiani nyinyi kwa nyinyi?»

    [26] Bali wao Leo ni wenye kufuata amri ya Mwenyezi Mungu, hawataenda kinyume nayo wala hawataepukana nayo, hawajisaidii wao wenyewe

    [27] Na hapo makafiri watakabiliana wao kwa wao wakilaumiana na wakigombana

    [28] Wafuasi watasema kuwaambia wafuatwa, «Nyinyi mlikuwa mkitujia kwa upande wa dini na haki, mkiifanya Sheria ni twevu kwetu, mkitutia chuki nayo na mkitupambia upotevu.»

    [29] Hapo watasema wafuatwa kuwaabia wafuasi, «Mambo si kama vile mnavyodai, bali ni nyoyo zenu zilikuwa zimekataa kuamini, zimeuelekea ukafiri na uasi

    [30] «Na sisi hatukuwa na hoja juu yenu wala nguvu, tukaweza kwa hizo kuwazuilia kuamini. Bali nyinyi wenyewe, enyi washirikina, mlikuwa waasi wenye kupita mipaka ya haki

    [31] «Hivyo basi ndio sisi sote ikalazimu tupate onyo la Mola wetu kuwa ni wenye kuonja adhabu, sisi na nyinyi, kwa yale tuliyoyatanguliza ya madhambi na maasia duniani

    [32] « Ndipo tukawapoteza na njia ya Mwenyezi Mungu na ya kumuamini, kwa kuwa sisi wenyewe tulikuwa ni wapotevu kabla yenu. Na kwa hivyo tukapotea kwa sababu ya ukafiri wetu na tukawaangamiza nyinyi pamoja na sisi.»

    [33] Basi wafuasi na wafuatwa watashirikiana katika adhabu Siku ya Kiyama, kama walivyoshirikiana ulimwenguni katika kumuasi Mwenyezi Mungu

    [34] Hivi ndivyo sisi tunavyowafanyia waliochagua mambo ya kumuasi Mwenyezi Mungu ulimwenguni na wakaacha kumtii, basi tutawaonjesha adhabu kali

    [35] Hakika wale washirikina walikuwa duniani wakiambiwa, «Hapana mola anayepasa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu,» na wakaitwa kwenye mwito huo na wakaamrishwa kuyaacha yanayopingana nao, wanaufanyia kiburi na kumfanyia kiburi aliyekuja nao

    [36] Na wanasema, «Je, tuache kuwaabudu waungu wetu kwa maneno ya mshairi mwenye wazimu?» wakimkusudia Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [37] Wamesema urongo! Muhammad sivyo vile walivyomueleza. Bali amekuja na Qur’ani na upwekeshaji Mwenyezi Mungu, na akathibitisha ukweli wa Mitume katika kile walichokitolea habari kuhusu sheria ya Mwenyezi Mungu na kumpwekesha Yeye

    [38] Hakika yenu nyinyi, enyi washirikina, kwa neno lenu, ukafiri wenu na kukanusha kwenu, ni wenye kuonja adhabu iliyo kali yenye uchungu

    [39] Na hamtalipwa huko Akhera isipokuwa kwa lile la maasia mliokuwa mkilifanya duniani

    [40] Isipokuwa waja wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, waliomtakasia Ibada Yake, Akawatakasa na Akawahusu wao kwa rehema Yake, basi hao kwa hakika ni wenye kuokoka na adhabu yenye uchungu

    [41] Hao waliotakaswa watapata riziki ijulikanayo isiyokatika ndani ya Pepo

    [42] Riziki hiyo ni matunda aina mbalimbali. Na wao ni wenye kukirimiwa kwa takrima ya Mwenyezi Mungu

    [43] kuwafanyia wao ndani ya mabustani ya Pepo ya starehe ya milele

    [44] Na miongoni mwa takrima yao watakayoipata kwa Mola wao, na kukirimiana wao kwa wao, ni kuwa wao watakuwa kwenye vitanda wameelekeana

    [45] Zinazungushwa kwao gilasi za Pombe inayotoka kwenye mito inayotembea, hawachelei kuwa itamalizika

    [46] ni nyeupe rangi yake, ni tamu katika kuinywa

    [47] haina madhara yoyote ya akili wala ya mwili

    [48] Na hapo kwao kwenye makao yao watakuwako wanawake waliojihifadhi, hawawatazami isipokuwa waume zao, wazuri wa macho

    [49] kama kwamba wao ni mayai yaliyotunzwa ambayo hayajaguswa na mikono

    [50] Hapo wataelekeana wakiulizana kuhusu hali zao za duniani na mambo ya usumbufu waliokuwa wakikutana nayo huko, na yale ambayo Mwenyezi Mungu Aliwaneemesha nayo Peponi. Na huku ndiko kuliwazika kuliotimia

    [51] Atasema msemaji miongoni mwa watu wa Peponi, «Kwa kweli, nilikuwa na rafiki duniani aliyeshikana na mimi

    [52] «Aliyekuwa akisema, ‘Ni vipi wewe unaamini Ufufuzi ambao ni upeo wa kustaajabisha

    [53] Je, tunapokufa, tukakatika vipande- vipande na tukawa mchanga na mifupa, kwani ni wenye kufufuliwa, kuhesabiwa na kulipwa kwa matendo yetu?’»

    [54] Atasema huyu Muumini aliyetiwa Peponi akiwaambia wenzake, «Je, nyinyi ni wenye kuchungulia mpate kuona mwisho wa yule rafiki?»

    [55] Hapo akachungulia na akamuona rafiki yake katikati ya Moto

    [56] Muumini atasema kumwambia rafiki yake mwenye kukanusha kufufuliwa, «Ulikaribia kuniangamiza kwa kunizuia nisiamini lau nilikutii

    [57] Na lau si wema wa Mola wangu kwa kuniongoza mimi kwenye Imani na kunithibitisha juu yake, ningalikuwa ni mwenye kuhudhurishwa kwenye adhabu pamoja na wewe

    [58] «Je, ni kweli sisi ni wenye kukalishwa milele na kuneemeshwa, si wenye kufa

    [59] isipokuwa kifo chetu cha mwanzo huko ulimwenguni, na sisi si wenye kuadhibiwa baada ya kuingia kwetu Peponi

    [60] Hakika starehe hii tuliyo nayo ndiyo kufaulu kukubwa

    [61] «Basi kwa kupata mfano wa starehe hizi kamilifu, makazi ya daima na kufaulu kukubwa, na watende wenye kutenda duniani ili wazifikie huko Akhera.»

    [62] Je, hayo yaliyotangulia kuelezwa ya starehe za Pepo ni makaribisho bora na vipewa vya Mwenyezi Mungu, au ni mti mbaya uliolaaniwa wa zaqqūm, ambao ni chakula cha watu wa Motoni

    [63] Sisi tumeufanya ni mtihani waliotahiniwa nao madhalimu kwa ukanushaji na kufanya mambo ya uasi na wakasema kwa njia ya kiburi, «Mtu wenu anawapa habari kwamba motoni kuna mti, na moto unakula miti.»

    [64] Hakika huo ni mti ambao unaota kwenye uketo wa moto wa Jahanamu, matunda yake yana sura mbaya

    [65] kama vichwa vya Mashetani

    [66] Basi yanapokuwa hivyo, usiulize baada ya haya kuhusu utamu wake. Kwani washirikina ni wenye kula kutoka mti huo na ni wenye kujaza matumbo yao kwa matunda hayo

    [67] Kisha wao, baada ya kuyala ni wenye kunywa kinywaji mchanganyiko kilicho kibaya na kilicho moto

    [68] Kisha marejeo yao baada ya adhabu hii ni kuishia (hukohuko) kwenye adhabu ya Moto

    [69] Hakika wao waliwakuta baba zao kwenye ushirikina na upotevu

    [70] na wakakimbilia kuwafuata katika hilo

    [71] na kwa hakika, kabla ya watu wako, ewe Mtume, walipotea na kuwa kando na haki ummah wengi waliotangulia

    [72] Na kwa hakika, tuliwatumiliza kwa ummah hao Mitume waliowaonya adhabu, lakini wakakanusha

    [73] Basi fikiria: ulikuwa vipi mwisho wa ummah hao walioonywa na wakakanusha? Waliadhibiwa na wakawa ni mazingatio kwa watu

    [74] Isipokuwa waja wa Mwenyezi Mungu Aliyowasafisha na Akawachagua kwa kuwapa rehema Yake kwa kule kumtakasa kwao Yeye

    [75] Na kwa hakika Alituita kwa kutuomba Nabii wetu Nūḥ tumlinde na watu wake, basi bora wa wenye kumuitikia tulikuwa ni sisi

    [76] Na tukamuokoa yeye na watu wa nyumbani kwake na Waumini pamoja naye kutokana na maudhi ya washirikina na kutokana na kuzamishwa kwa mafuriko makubwa

    [77] Na tukawafanya watoto wa Nūḥ ndio wenye kusalia baada ya kuzamishwa watu wake

    [78] Na tukamuwekea utajo mwema na sifa nzuri kwa watu waliokuja baada yake wakawa wanamtaja nazo

    [79] Amani imfikie Nūḥ na asalimike na kutajwa kwa ubaya katika kipindi cha watu wa mwisho, bali asifiwe na watu wa vizazi vinavyokuja baada yake

    [80] Mfano wa malipo mema tuliomlipa Nūḥ, tutamlipa kila aliyefanya vizuri, miongoni mwa waja, katika kumtii Mwenyezi Mungu

    [81] Hakika Nūḥ ni miongoni mwa waja wetu wenye kuamini, wenye kumtakasia Mwenyezi Mungu na wenye kufuata amri za Mwenyezi Mungu kivitendo

    [82] Kisha tukawazamisha wengine, wenye kukanusha kati ya watu wake, kwa mafuriko, kisisalie chochote, miongoni mwao, hata jicho lenye kupepesa

    [83] Na miongoni mwa waliokuwa katika nyendo za Nūḥ, njia yake na mila yake ni Nabii wa Mwenyezi Mungu Ibrāhīm

    [84] alipomjia Mola wake kwa moyo uliyojitenga na kila itikadi ya ubatilifu na tabia ya kujitukanisha

    [85] alipomwambia babake na watu wake kwa njia ya kuwakanya, «Ni kitu gani hiko mnachokiabudu badala ya Mwenyezi Mungu

    [86] Je, mnataka kuabudu waungu wa kuzuliwa na mnaacha kumuabudu Mwenyezi Mungu Anayestahiki kuabudiwa Peke Yake

    [87] Mnamdhani Mola wa viumbe vyote Atawafanya nini mkimshirikisha Yeye na mkamuabudu asiyekuwa Yeye

    [88] Akatazama mtazamo mmoja kwenye nyota kulingana na mila ya watu wake kuhusu hilo, huku akifikiria udhuru wa kuutoa ili asipate kutoka na wao kwenda kwenye sherehe zao

    [89] akawaambia, «Mimi ni mgonjwa.» Hii ilikuwa ni ishara ya mbali kutoka kwake

    [90] Basi wakamuacha nyuma yao

    [91] Akabeta kwa haraka kuelekea kwenye masanamu wa watu wake, akasema kwa njia ya kuwakejeli, «Si mkile chakula hiki ambacho washika mlango wenu wanawapatia

    [92] Muna nini nyinyi mbona hamsemi wala hamumjibu mwenye kuwaomba

    [93] Akawaelekea waungu wao kuwapiga na kuwavunja-vunja kwa mkono wake wa kulia, ili kuwathibitishia makosa ya kuwaabudu

    [94] Wakaja kumkabili kwa haraka na mbio huku wana hasira

    [95] Ibrāhīm akakutana na wao akiwa imara kwa kusema, «Vipi mtaabudu masanamu mnaowachonga nyinyi wenyewe na mnaowatengeneza kwa mikono yenu

    [96] na mnaacha kumuabudu Mola wenu Aliyewaumba nyinyi na Akayaumba matendo yenu?»

    [97] Hoja ilipowasimamia, waliamua kutumia nguvu na wakasema, «Jengeni jengo kwa ajili yake, mlijaze kuni kisha mumtupe ndani yake»

    [98] Watu wa Ibrāhīm wakataka kumfanyia vitimbi ili wamuangamize, tukawafanya wao kuwa ndio wenye kutendeshwa nguvu na kushindwa. Mwenyezi Mungu Akavirudisha vitimbi vyao kwenye shingo zao na akaufanya ule moto uwe baridi na salama kwa Ibrāhīm

    [99] Akasema Ibrāhīm, «Mimi nahamia kwa Mola wangu kutoka kwenye mji wa watu wangu kuelekea pale ambapo nitamakinika kumuabudu Mola wangu, kwani Yeye Atanielekeza kwenye kheri ya Dini yangu na dunia yangu

    [100] Mola wangu! Nipe mtoto mwema.»

    [101] Tukamkubalia ombi lake na tukambashiria kuwa atapata mtoto wa kiume atakayekuwa mpole ukubwani mwake, naye ni Ismā'īl

    [102] Alipokuwa mkubwa Ismā'īl, akawa anatembea na babake, babake alimwambia, «Mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchinja, je, una maoni gani?» (na ndoto za Manabii ni za kweli). Ismā'īl akasema, kwa kumridhisha Mola wake, kumtii mzazi wake na kumsaidia juu ya utiifu wa Mwenyezi Mungu, «Endelea katika jambo Alilokuamrisha Mwenyezi Mungu la kunichinja mimi. Utanikuta, Mwenyezi Mungu Akitaka, ni mvumilivu, mtiifu na ni mwenye kutarajia malipo mema (kutoka kwa Mwenyezi Mungu)»

    [103] Walipojisalimisha wao wawili kwa kuifuata amri ya Mwenyezi Mungu na kuiandama, na Ibrāhīm akambwaga Ismā'īl chini, kwa upande wa paji la uso, ili kumchinja

    [104] Na tukamuita Ibrāhīm katika hali hiyo ngumu kwamba: Ewe Ibrāhīm! Umeshalifanya uliloamrishwa na, kwa hivyo

    [105] umeisadikisha ndoto yako. Hakika yetu sisi kama vile tulivyokulipa mema kwa kuamini kwako , ndivyo tunavyowalipa wale waliofanya wema mfano wako, tuwaepushie shida duniani na Akhera

    [106] Hakika amri ya kuwa wewe umuue mwano ndio mtihani mgumu uliodhihirisha ukweli wa Imani yako

    [107] Na tukamuokoa Ismā'īl, na tukamuekea kondoo mkubwa kuwa ni badala yake

    [108] Na tukambakishia Ibrāhīm baada yake sifa njema kwa watu

    [109] Maamkizi kwa Ibrāhīm kutoka kwa Mola wake na kumuombea asalimike na kila dhara

    [110] Kama tulivyomlipa malipo mema Ibrāhīm kwa utiifu wake kwetu na kufuata kwake amri yetu, ndivyo tutakavyowalipa wenye kufanya wema miongoni mwa waja wetu

    [111] Hakika yeye ni miongoni mwa waja wetu Waumini waliyoipa hiyo sifa ya uja haki yake

    [112] Na tukampa bishara Ibrāhīm ya mtoto wake, Isḥāq, kuwa atakuwa Nabii, miongoni mwa watu wema. Hayo yakiwa ni malipo ya uvumilivu wake na kuridhika kwake na amri ya Mola wake na utiifu wake Kwake

    [113] Na tukawateremshia baraka. Na miongoni mwa wale wanaotokana na kizazi chao kuna anayemtii Mola wake, anayeifanyia wema nafsi yake, na kuna anayeidhulumu (nafsi yake) dhulma iliyo wazi kwa ukafiri wake na utendaji wake maasia

    [114] Na kwa hakika tuliwafanyia wema Mūsā na Hārūn kwa kuwapa unabii na utume

    [115] Na tukawaokoa wao wawili na watu wao kutokana na gharika, utumwa na unyonge waliokuwa nao

    [116] Na tukawanusuru, wakawa na enzi, usaidizi na ushindi juu ya Fir'awn na jamaa zake

    [117] Na tukawapa wao wawili Taurati yenye ufafanuzi

    [118] na tukawaongoza njia iliyonyoka isiyokuwa na upotovu, nayo ni Uislamu, Dini ya Mwenyezi Mungu ambayo Amewatumiliza Manabii Wake kwayo

    [119] na tukazifanya sifa zao nzuri na utajo wao mwema ni vyenye kusalia baada yao

    [120] Maamkizi kwa Mūsā na Hārūn kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na sifa njema na kuwaombea wao wasalimike na kila dhara

    [121] Kama tulivyowalipa wao malipo mema , ndivyo tutakavyowalipa wenye kufanya wema miongoni mwa waja wetu wenye kututakasia kwa ukweli, kuamini na kutenda

    [122] Hakika ya wao wawili ni miongoni mwa waja wetu waliojikita katika Imani

    [123] Na hakika mja wetu Ilyas ni miongoni mwa wale ambao tuliwakirimu kwa unabii na utume

    [124] Kumbuka na utaja pindi aliposema kuwaambia watu wake, kati ya Wana wa Isrāīl, «Mcheni Mwenyezi Mungu, Peke Yake, na mumuogope, na msimshirikishe mwengine pamoja na Yeye

    [125] Vipi nyinyi mtaliabudu sanamu ambalo ni kiumbe dhaifu na mtamuacha Mzuri wa kuumba, Mwenye sifa nzuri na kamilifu kabisa

    [126] mkawa hamtamuabudu Mwenyezi Mungu Ambaye ni Mola wenu Aliyewaumba nyinyi na Akawaumba baba zenu waliopita kabla yenu?»

    [127] Watu wa Ilyas walimkanusha Nabii wao. Basi Mwenyezi Mungu , kwa hakika, Atawakusanya Siku ya Kiyama ili wahesabiwe na wateswe

    [128] Isipokuwa wale waja wa Mwenyezi Mungu waliomtakasia Mwenyezi Mungu Dini yao, basi hao ni wenye kuokoka na adhabu Yake

    [129] Tulimfanya Ilyas awe na sifa nzuri kwa ummah waliokuja baada yake

    [130] Maamkizi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na sifa njema kwa Ilyas

    [131] Na kama tulivyomlipa Ilyas malipo mema kwa utiifu wake, ndivyo tutakavyowalipa walio wema miongoni mwa waja wetu Waumini

    [132] Hakika yake yeye ni miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu waliomtakasia wenye kufuata amri zake kivitendo

    [133] Na hakika mja wetu Lūṭ tulimchagua na tukamfanya ni miongoni mwa Mitume

    [134] Tulipomuokoa yeye na watu wa nyumbani kwake wote

    [135] isipokuwa mkongwe aliyezeeka, naye ni mke wake, ambaye aliangamia pamoja na wale walioangamia miongoni mwa watu wake kwa ukafiri wake

    [136] Kisha tukawaangamiza wakanushaji waliosalia miongoni mwa watu wake

    [137] Na hakika yenu nyinyi, enyi watu wa Makkah mnazipitia katika safari zenu nyumba za watu wa Lūṭ na athari zao katika kipindi cha asubuhi

    [138] na pia mnazipitia katika kipindi cha usiku. Basi hamtii akilini, mkaogopa kisije kikawafika nyinyi kile kilichowafika wao

    [139] Hakika mja wetu Yūnus, tulimchagua na tukamfanya ni miongoni mwa Mitume

    [140] Alipokimbia kutoka mji wake, akiwa na hasira juu ya watu wake, akapanda jahazi iliyojaa abiria na vyombo

    [141] Mawimbi makubwa yakaizunguka jahazi hiyo kila upande. Na watu waliokuwa wamepanda jahazi wakapiga kura ili kupunguza shehena ili wasizame. Yūnus akawa ni miongoni mwa wale walioshindwa kwa kura

    [142] Hivyo basi akatupwa baharini na chewa akammeza, na hali ni kwamba Yūnus, amani imshukie, ameleta jambo la kumfanya alaumiwe

    [143] Lau si yale yaliyotangulia kwake, ya wingi wa Ibada na matendo mema kabla ya kuingia ndani ya tumbo la chewa kwa kusema, «Hapana Mola anayepasa kuabudiwa kwa haki isipokuwa wewe, kutakasika na sifa za upungufu ni kwako, mimi nimekuwa miongoni mwa wenye kudhulumu,»

    [144] angalikaa ndani ya tumbo la chewa, na lingalikuwa ni kaburi lake mpaka Siku ya Kiyama

    [145] Tukamtoa kwenye tumbo la chewa na tukamtupa kwenye ardhi tupu, isiyokuwa na miti wala majengo, akiwa dhaifu wa mwili

    [146] Na tukamuoteshea mmea wa matango ili umfinike na anufaike nao

    [147] Tukamtumiliza aende kwa watu wake wanaofikia elfu mia moja, bali wanazidi idadi hiyo

    [148] Wakamuamini na wakafuata aliyokuja nayo kivitendo, na kwa hivyo tukawastarehesha maishani mwao mpaka wakati wa kufika ajali zao

    [149] Basi waulize watu wako, ewe Mtume, «Ni vipi wamemfanya Mwenyezi Mungu ana watoto wa kike ambao wao wenyewe wanawachukia, na wao wana watoto wa kiume wanaowataka?»

    [150] Na waulize wao, «Je, tuliwaumba Malaika wakiwa wanawake, na hali wao wapo (wakishuhudia uumbaji huo)?»

    [151] Na miongoni mwa urongo wao ni kule kusema kwao, «Mwenyezi Mungu Amezaa

    [152] Na kwa hakika, wao ni warongo, kwa kuwa wanakisema wasichokijua.»

    [153] Ni kwa kitu gani Mwenyezi Mungu Achague watoto wa kike na sio wa kiume

    [154] Ni uamuzi mbaya sana mnaoutoa, enyi watu, wa kuwa Mwenyezi Mungu Ana watoto wa kike na nyinyi mna watoto wa kiume, na hali nyinyi hamridhiki nafsi zenu kuwa na watoto wa kike

    [155] Je, hamkumbuki kwamba haifai wala haitakikani Awe na mtoto? Ametukuka Mwenyezi Mungu na kuwa mbali na hilo, umbali ulio juu sana

    [156] Lakini je, mna hoja ya wazi juu ya hilo neno lenu na uzushi wenu

    [157] Iwapo mna hoja ndani ya kitabu kitokacho kwa Mwenyezi Mungu, basi kileteni, mkiwa ni wa kweli katika hilo neno lenu

    [158] Na washirikina walifanya kuwa kuna uhusiano wa kizazi baina ya Mwenyezi Mungu na Malaika, na hakika ni kwamba Malaika washajua kuwa washirikina ni wenye kuletwa Siku ya Kiyama ili kuadhibiwa

    [159] Ametakasika Mwenyezi Mungu na kila lisilofaa asifike nalo miongoni mwa yale wanaomsifu nayo washirikina

    [160] Lakini wale waja wa Mwenyezi Mungu wanaomtakasia katika kumuabudu hawamsifu isipokuwa kwa sifa zinazolingana na utukufu Wake, kutakasika ni Kwake

    [161] Hakika yenu nyinyi, enyi wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, na kile mnachokiabudu badala ya Mwenyezi Mungu miongoni mwa waungu

    [162] hamkuwa ni wenye kumpoteza yoyote

    [163] isipokuwa yule Aliyemkadiria Mwenyezi Mungu aingie kwenye Moto wa Jaḥīm kwa sababu ya ukafiri wake na udhalimu wake

    [164] Malaika wanasema, «Hakuna yoyote miongoni mwetu isipokuwa ana makao maalumu mbinguni

    [165] Na sisi ndio tunaosimama kwa kujipanga kwa safu katika kumuabudu Mwenyezi Mungu na kumtii

    [166] Na sisi ndio tunaomtakasa Mwenyezi Mungu na kila kisichofaa kunasibishwa nacho.»

    [167] Na hakika makafiri wa Makkah walikuwa wakisema kabla hujatumilizwa

    [168] «Ewe Mtume! Lau vingalitujia vitabu na Manabii vile vilivyowajia wa mwanzo kabla yetu

    [169] tungalikuwa waja wa Mwenyezi Mungu wakweli katika Imani, waliotakaswa kwa kufanya Ibada.»

    [170] Ulipowajia wao utajo wa watu wa mwanzo na utajo wa watu wa mwisho na kitabu kikamilifu kabisa na bora wa Mitume, naye ni Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, walimkanusha. Basi wataijua adhabu watakayopatiwa Siku ya Mwisho

    [171] Kwa hakika lishatangulia neno letu, ambalo halina namna ya kurudi, la kuwaahidi waja wetu waliopewa utume

    [172] kwamba watapata usaidizi juu ya maadui zao, kwa hoja na nguvu

    [173] na kwamba askari wetu wanaopigana jihadi katika njia yetu ndio wenye kuwashinda maadui zao kila mahali, kuzingatia mwishoni na marejeo

    [174] Basi wape mgongo, ewe Mtume, wale walioshindana na wasiikubali haki mpaka ukamalizika muda waliopatiwa muhula na ikaja amri ya Mwenyezi Mungu ya wao kuadhibiwa

    [175] wangojee na subiri uone: ni adhabu gani itakayowashukia wao kwa kuenda kinyume nawe? Basi wataiona adhabu ya Mwenyezi Mungu itakayowashukia

    [176] Je kuteremkiwa kwao na adhabu yetu ndilo jambo wanalokuharakishia, ewe Mtume

    [177] Basi adhabu yetu itakapowashukia, asubuhi mbaya zaidi ni asubuhi yao

    [178] Na uwape mgongo mpaka Mwenyezi Mungu Atoe idhini ya wao kuadhibiwa

    [179] Na uwangojee, kwani wataiona adhabu itakayowashukia na mateso

    [180] Mola wa enzi na utukufu Ameepukana na kuwa juu ya kila kile ambacho wanaomzulia urongo wanamsifu nacho

    [181] Na maamkizi ya Mwenyezi Mungu ya daima,sifa Zake na amani Yake ziwafikie Mitume wote

    [182] Na shukrani na sifa njema ni za Mola wa viumbe wote ulimwenguni na Akhera. Yeye Ndiye Mstahiki wa hilo Peke Yake, Hana mshirika Wake

    Swad

    Surah 38

    [1] «Ṣād» Yametangulia maelezo kuhusu herufi zilizotengwa na kukatwa mwanzoni mwa sura ya Al-Baqarah

    [2] Anaapa Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika, kwa Qur’ani inayokusanya ukumbushaji kwa watu kwa yale ambayo wao wameghafilika nayo. Lakini makafiri wanaifanyia kiburi haki na wanaenda kinyume nayo

    [3] Kuna ummah wengi tuliowaangamiza kabla ya hawa washirikina, wakaomba waokolewe na wakaita kutaka toba, na wakati si wakati wa kukubaliwa toba wala wakati wa kukimbia na kuokolewa na yaliyowapata

    [4] Na wameona ajabu washirikina hawa kuwa Mwenyezi Mungu Amewatumia binadamu miongoni mwao awalinganie kwa Mwenyezi Mungu na awaogopeshe adhabu Yake na wakasema, «Hakika yeye si Mtume bali yeye ni mrongo katika maneno yake, anawafanyia uchawi watu wake

    [5] Ni vipi atawafanya waungu wengi kuwa ni mungu mmoja? Hili alilolileta na akalingania kwalo ni jambo la ajabu

    [6] Wakatoka viongozi wa watu na wakubwa wao wakiwahimiza watu wao kuendelea kwenye ushirikina na kuvumilia juu ya waungu wengi, «Hili alilokuja nalo huyu Mtume ni jambo la kupangwa, lengo lake ni uongozi na ukubwa

    [7] Hatujasikia hili analolingania katika dini ya baba zetu wa Kikureshi wala katika Unaswara; halikuwa hili isipokuwa ni urongo na uzushi

    [8] «Je, amehusishwa Muhammad peke yake kwa kuteremshiwa Qur’ani bila ya sisi?» Bali wao wako kwenye shaka ya kuwa mimi nimekuletea wahyi wewe, ewe Mtume, na kukupa utume. Bali wao walisema hilo kwa kuwa hawajaonja adhabu ya Mwenyezi Mungu, na lau wangaliionja adhabu hawangalithubutu kusema waliyosema

    [9] Au kwani wao wanamiliki mahazina ya fadhila za Mola wako, Aliye Mshindi katika ufalme Wake, Aliye Mpaji wa Anachokitaka miongoni mwa riziki Yake na fadhila Zake kwa Anayemtaka miongoni mwa viumbe Vyake

    [10] Au kwani washirikina hawa wana mamlaka ya mbinguni na ardhini na vilivyoko baina ya viwili hivyo, hivyo basi wakatoa na kuzuia? Basi wazishikilie kamba zenye kuwafikisha mbinguni wapate kutoa uamuzi wanaoutaka wa kutoa na kuzuia

    [11] Askari hawa wanaokanusha ni askari wenye kushindwa, kama walivyoshindwa wengineo miongoni mwa mapote ya watu waliokuwa kabla yao

    [12] Walikanusha kabla yao watu wa Nūḥ, 'Ād, Fir'awn mwenye nguvu kubwa

    [13] Thamūd, watu wa Lūṭ, watu wa miti na mabustani nao ni watu wa Shu'ayb. Hao ndio ummah walioshirikiana wakawa pote moja juu ya ukafiri na ukanushaji na wakajikusanya juu yake

    [14] Hakuna watu wa pote lolote kati ya hawa isipokuwa walikanusha Mitume na kwa hivyo wakastahiki kupata adhabu ya Mwenyezi Mungu na yakawashukia wao mateso Yake

    [15] Na hawangojei washirikina hawa, ili adhabu iwashukie wakisalia kwenye ushirikina wao, isipokuwa Mvuvio mmoja ambao hauna kurudi

    [16] Na wanasema, «Mola wetu! Tuharakishie sehemu yetu ya adhabu duniani kabla ya Siku ya Kiyama.» Kusema huku kulikuwa ni uchezaji shere kutoka kwao

    [17] Vumilia, ewe Mtume, kwa unayoyachukia katika hayo wanayoyasema, na umtaje mja wetu Dāwūd, mwenye nguvu juu ya maadui wa Mwenyezi Mungu na uvumilivu juu ya kumtii Yeye. Hakika yeye ni mwingi wa kutubia, ni mwingi wa kurejea kufanya yale yanayomridhisha Mwenyezi Mungu. Katika haya pana kumliwaza Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [18] Hakika sisi tuliyadhalilisha majabali pamoja na Dāwūd, yakawa yanamtakasa Mwenyezi Mungu kwa kumsabihi wakati anapomtakasa kwa kumsabihi mwanzo wa mchana na mwisho wake

    [19] Na tukawadhalilisha ndege pamoja naye, kwa mkusanyiko wao, wakawa wanatakasa kwa kusabihi na kuwa watiifu kwake

    [20] Tukamtilia nguvu ufalme wake kwa haiba, uwezo na ushindi, na tukampa unabii na upambanuzi wa maneno na utoaji hukumu

    [21] Na je, ilikujia, ewe Mtume, habari ya watesi wawili walioparaga ukuta wakamuingilia Dāwūd mahali pake pa kuabudu

    [22] Na Dāwūd akashutuka kwa wao kumuingilia? Walimwambia, «Usiogope! Sisi ni watesi, mmoja wetu amemdhulumu mwenzake. Basi hukumu baina yetu kwa uadilifu, wala usitoe hukumu ya maonevu juu yetu, na utuongoze kwenye njia ya sawa.»

    [23] Mmoja wa wale wawili alisema, «Huyu ni ndugu yangu; ana kondoo tisini na tisa na mimi sina isipokuwa kondoo mmoja, akafanya tamaa kumtaka na akasema, ‘Nipe mimi!’ Na akanishinda kwa hoja.»

    [24] Dāwūd akasema, «Kwa hakika ndugu yako amekudhulumu kwa kutaka kwake kumchukua kondoo wako awe pamoja na kondoo wake. Na kwa hakika, wengi wa washirika, baadhi yao wanadhulumu wengine: wanawadhulumu kwa kuchukua haki zao na kukosa kuwa waadilifu wa nafsi zao. Isipokuwa watu wema walioamini, kwani wao hawadhulumiani, nao ni wachache.» Na Dāwūd akajua kwa yakini kuwa sisi tumemtahini kwa utesi huu, hivyo basi akamuomba msamaha Mola wake, akasujudu kwa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na akarejea Kwake na akatubia

    [25] Tukamsamehe hilo na tukamfanya ni miongoni mwa watu waliosogezwa karibu na sisi, na tumemuandalia mwisho mwema huko Akhera

    [26] Ewe Dāwūd! Sisi tumekufanya ni msimamizi ardhini na tumekupa mamlaka huko, basi hukumu baina ya watu kwa uadilifu na uchungaji haki, na usifuate matamanio katika kuhukumu, kwani hilo litakupotosha na Dini ya Mwenyezi Mungu na Sheria Yake, hakika wale wanaopotea njia ya Mwenyezi Mungu watapata adhabu ya uchungu humo Motoni, kwa kughafilika kwao na Siku ya kulipwa na kuhesabiwa. Katika haya pana ushauri kwa viongozi wahukumu kwa haki iliyoteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, wala wasipotoke nayo wakapotea njia Yake

    [27] Hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake kwa upuuzi na mchezo. Hiyo ndiyo dhana ya waliokufuru. Basi ole wao na Moto wa Siku ya Kiyama, kwa dhana yao ya ubatilifu na ukanushaji wao Mwenyezi Mungu

    [28] Je, tuwafanye walioamini wakafanya matendo mema ni kama waharibifu kwenye ardhi? Au je, tuwafanye wachamungu wenye kuamini ni kama waharibifu waliokufuru? Kusawazisha huku hakulingani na hekima ya Mwenyezi Mungu na hukumu yak, kwani hao hawalingani kwa Mwenyezi Mungu. Bali Mwenyezi Mungu Atawalipa wachamungu malipo mema na Atawatesa waharibifu walio waovu

    [29] Hiki ulicholetewa kwa njia ya wahyi, ewe Mtume, ni Kitabu tulichokuteremshia kilichobarikiwa, ili wafikirie juu ya aya zake na wazitumie njia zake za uongofu na ishara zake njema, na ili wapate kukumbuka watu wenye akili timamu yale Aliyowalazimisha Mwenyezi Mungu

    [30] Na tulimtunukia Dāwūd mwanawe Sulaymān, tukamneemesha yeye (Dāwūd) kwa kumpa Sulyman, na tukamtuliza jicho lake kwake. Neema ya mja ni Sulaymān. Yeye alikuwa mwingi wa kurejea kwa Mwenyezi Mungu na kutubia Kwake

    [31] Kumbuka pindi walipoorodheshwa mbele yake kipindi cha alasiri farasi wa asili wenye kasi za kukimbia, waliosimama kwa miguu mitatu na kuinua mguu wa nne kwa kuwa ni farasi bora na wapesi. Waliendelea kuorodheshwa mbele yake mpaka jua likachwa

    [32] Akasema, «Mimi nimehiari kupenda farasi kuliko kumtaja Mola wangu mpaka jua likachwa na macho yangu yakawa hayalioni

    [33] Warudisheni hao farasi walioorodheshwa hivi punde.» Wakarudishwa, na akaingia kuipiga miguu yao na shingo zao kwa upanga kwa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuwa wao walikuwa ni sababu ya Swala yake kumpita, Na ilikuwa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kwa kuchinja farasi yakubaliwa katika Sheria yake

    [34] Hakika tulimpa mtihani Sulaymān na tukamrushia kwenye kiti chake kipande cha mtoto aliyezaliwa katika kipindi alichoapa kuwa atawapitia wake zake na kila mmoja katika wao atamzalia shujaa atakayepigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, na hakuseme «in shāa Allāh» (Mungu Akitaka). Akawapitia wake zake wote, na hakuna hata mmoja katika wao aliyeshika mimba isipokuwa mmoja aliyezaa mtoto nusu. Kisha Sulaymān alirudi kwa Mola Wake, akatubia

    [35] na akasema, «Mola wangu! Nisamehe dhambi zangu na unipe ufalme mkubwa unaohusika na mimi ambao mfano wake hautakuwa kwa binadamu yoyote baada yangu. Hakika yako wewe, uliotakasika na kutukuka, ni Mwingi wa upaji na utoaji

    [36] Tukamkubalia maombi yake na tukamdhalilishia upepo ukawa unapita kwa amri yake ukiwa mtiifu kwake, hali ya kuwa na nguvu na kasi, ukielekea pale anapotaka

    [37] Na tukamdhalilishia Mashetani, akawa anawatumia katika kazi zake. Katika wao kulikuwa na wajenzi na wazamiaji baharini

    [38] Na wengine, nao ni waasi wa kijini, walikuwa wamefungwa pingu

    [39] Ufalme huu mkubwa na udhalilishiaji huu wa kipekee ni upaji wetu kwako, ewe Sulaymān, basi mpe unayemtaka na umnyime unayemtaka, hapana hesabu juu yako

    [40] Na hakika Sulaymān kwetu sisi, huko Akhera, atakuwa na ukaribu na marejeo mazuri

    [41] Mkumbuke, ewe Mtume, mja wetu Ayyūb alipomlingania Mola wake kwa kusema, «Shetani amenisababishia tabu, mashaka na maumivu katika mwili wangu, mali yangu na watu wangu!»

    [42] Tukamwambia, «Ipige ardhi kwa mguu wako! Yatabubujika kutoka humo maji baridi. Basi kunywa katika maji hayo na uoge, na madhara na maudhiko yatakuondokea.»

    [43] Tukamuondolea shida yake na tukamtukuza, na tukamtunukia watu wake : mke na watoto, na tukamuongezea wana na wajukuu mfano wao. Yote hayo yalikuwa ni huruma kutoka kwetu na takrima kwake kwa uvumilivu wake, na pia ni mazingatio kwa wenye akili timamu, wapate kujua kwamba mwisho wa subira ni faraja na kuondokewa na shida

    [44] Na tukamwambia yeye, «chukua kwa mkono wako mrundiko wa nyasi au mfano wake umpige nao mke wako, ili utekeleze yamini lako na usilivunje. Kwani yeye alikuwa ameapa kuwa atampiga mbati mia moja Mwenyezi Mungu Akimponyesha, alipomkasirikia mkewe kwa jambo dogo alipokuwa mgonjwa. Na alikuwa ni mwanamke mwema na Mwenyezi Mungu Akamhurumia yeye na Akamhurumia mumewe kwa uamuzi huu. Hakika sisi tumemkuta Ayyūb ni mvumilivu katika mitihani. Mja bora ni yeye, kwani yeye ni mwingi wa kurudi kwenye utiifu wa Mola wake

    [45] Wakumbuke, ewe Mtume, waja wetu na Manabii wetu: Ibrāhīm, Is’ḥāq na Ya’qūb. Hakika wao ni watu wenye nguvu katika kumtii Mwenyezi Mungu na ujuzi katika Dini Yake

    [46] Sisi tumewahusisha wao kwa jambo kubwa ambalo ni mahsusi kwao, kwa kuwa tumejaalia ukumbusho wa Nyumba ya Akhera uko ndani ya nyoyo zao, na kwa hivyo wakaifanyia kazi kwa kututii sisi na wakawalingania watu kwenye jambo hilo na kuwakumbusha

    [47] Na kwa hakika, wao kwetu sisi ni miongoni mwa wale tuliowachagua ili watutii na tuliowateua kubeba ujumbe wetu

    [48] Wakumbuke, ewe Mtume, waja wetu: Ismā'īl, Ilyasa' na Dhulkifl kwa utajo mzuri sana. Na kila mmoja miongoni mwao ni katika watu wema ambao Mwenyezi Mungu Aliwachagua miongoni mwa viumbe na Akawachagulia hali na sifa kamilifu kabisa

    [49] Hii Qur’ani ni utajo na utukufu kwako, ewe Mtume, na kwa watu wako. Na wale watu wa uchaji Mwenyezi Mungu na utiifu Kwake watakuwa na mwisho mwema kwetu sisi

    [50] kwenye Pepo za kukaa daima, milango yake ikiwa tayari imefunguliwa kwa ajili yao

    [51] watakuwa ni wenye kutegemea kwenye Pepo hizo juu ya viti vya fahari vilivyopambwa, watataka na kupatiwa kila wanachokitamani miongoni mwa aina nyingi za matunda na vinywaji, kutokana na kila ambacho nafsi zao zitakitamani na macho yao yatapendezwa nacho

    [52] Na huko watakuwa nao wanawake ambao macho yao yanawatazama waume zao tu hali wakiwa marika na wao kimiaka

    [53] Starehe hii ndiyo ile mliokuwa mkiahidiwa, enyi wachamungu, Siku ya Kiyama

    [54] Hiyo ndiyo riziki yetu tuliyowaandalia nyinyi, haina kumalizika wala kukatika

    [55] Hayo, yaliyotangulia kutajwa sifa zake, ni ya wachamungu. Ama wale wenye kuruka mpaka na kuingia ukafirini na maasi, wao watakuwa na marejeo maovu kabisa na mwisho mbaya sana

    [56] nao ni Moto ambao ndani yake wataadhibiwa, utawafinika pande zao zote, basi tandiko baya mno ni tandiko lao

    [57] Adhabu hii ni maji yaliyo moto sana, na usaha unaotiririka kutoka kwenye miili ya watu wa Motoni, basi na wanywe

    [58] Na wao watakuwa na adhabu nyingine ya namna hii, aina na sampuli mbalimbali

    [59] Na watakapoufikia Moto, hao wenye kupita vipimo katika uasi, watatukanana wao kwa wao na watasema baadhi yao kuwaambia wengine, «Hili ni kundi kubwa la watu wa Motoni ni wenye kuingia pamoja na nyinyi.» Na wao wajibu, «Hawana makaribisho mema wala nyumba zao haziwaenei ndani ya Moto. Wao ni wenye kuungulika kwa joto lake kama tunavyoungulika sisi.»

    [60] Hapo kundi la wafuasi litasema kuwaambia wale waliopita vipimo katika uasi, «Bali ni nyinyi msiokaribishwa vyema, kwa kuwa nyinyi ndio mliotusababishia makao ya Motoni kwa kule kutupoteza kwenu duniani, basi ubaya wa nyumba ya mtu kutulia ni Moto wa Jahanamu!»

    [61] Na kundi la wafuasi liendelee kusema, «Mola wetu! Yoyote yule aliyetupoteza duniani akatuepusha na uongofu, muongezee adhabu yake Motoni maradufu.»

    [62] Na watasema wale waliopita vipimo katika uasi, «Mbona hatuwaoni pamoja na sisi Motoni wale watoto ambao tulikuwa tukiwahesabu duniani kuwa ni miongoni mwa watu waovu wakorofi

    [63] Je, kwani kule kuwadharau kwetu na kuwachezea kulikuwa ni makosa Au wao wako pamoja na sisi Motoni lakini macho yetu bado hayajawaona?»

    [64] Kwa hakika, hili la kujadiliana watu wa Motoni na kuteta kwao ni jambo litakalotokea bila shaka

    [65] Sema, ewe Mtume, kuwaambia watu wako, «Hakika mimi ninawaonya nyinyi na adhabu ya Mwenyezi Mungu isiwashukie kwa sababu ya kumkanusha kwenu Mwenyezi Mungu, hakuna mola anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Yeye Peke Yake, Yeye Ndiye Aliyepwekeka kwa ukubwa Wake, majina Yake, sifa Zake na matendo Yake, Mwenye kutendesha nguvu Anayekilazimisha kila kitu na kukishinda

    [66] Mwenye kumiliki mbingu na ardhi na vilivyoko baina yake, Aliye Mshindi katika kutesa Kwake, Mwingi wa kusamehe dhambi za aliyetubia na kurudi kutafuta radhi Zake.»

    [67] Sema, ewe Mtume kuwaambia watu wako, «Kwa hakika hii Qur’ani ni habari yenye manufaa makubwa

    [68] Nyinyi mmeghafilika nayo, mmejiepusha nayo na hamuitumii

    [69] «Mimi sikuwa na ujuzi wa utesi wa Malaika wa mbinguni kuhusu kuumbwa kwa Ādam, lau si Mwenyezi Mungu kunijulisha na kuniletea wahyi kwa hilo

    [70] «Mwenyezi Mungu haniletei wahyi unaokusanya ujuzi wa kitu ambacho sina ujuzi nacho isipokuwa ni kwa kuwa mimi ni muonyaji wenu kutokana na adhabu Yake, ni mwenye kuwabainishia sheria Yake.»

    [71] Kumbuka pindi Aliposema Mola wako kuwaambia Malaika, «Hakika mimi nitamuumba kiumbe kutokana na mchanga

    [72] Basi nitakapousawazisha mwili wake na umbo lake na nikapuliza roho ndani yake na uhai ukatambaa humo, msujudieni» sijida ya heshima na kukirimu, na siyo sijida ya ibada na kutukuza. Kwani ibada haiwi isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu, Peke Yake. Na Mwenyezi Mungu Ameharamisha, katika Sheria ya Kiislamu, kusujudu kwa njia ya maamkizi

    [73] Hapo Malaika wote wakasujudu kwa kutii na kufuata amri ya Mwenyezi Mungu

    [74] isipokuwa Iblisi Yeye hakusujudu kwa ujeuri na kiburi, na alikuwa, katika ujuzi wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, ni miongoni mwa makafiri

    [75] Mwenyezi Mungu Akamwambia Iblisi, «Ni lipi lililokukataza kumsujudia yule niliyemkirimu nikamuumba kwa mikono yangu miwili? Je, umemfanyia kiburi Ādam au umekuwa ni miongoni mwa wale waliomfanyia kiburi Mola wako?» Katika aya hii pana kumthibitishia Mwenyezi Mungu, Mwenye kheri nyingi na kutukuka, sifa ya mikono miwili, kwa namna inayolingana na Yeye, kutakasika ni Kwake

    [76] Iblisi akasema akimpinga Mola wake, «Mimi sikumsujudia kwa kuwa mimi ni bora kuliko Yeye, kwa kuwa umeniumba kwa moto na umemuumba yeye kwa udongo (na moto ni bora kuliko udongo)

    [77] Mwenyezi Mungu Akamwambia, «Basi toka peponi! Wewe, kwa neno lako hilo, umefukuzwa, umeepushwa na kulaaniwa

    [78] Na huko kukufukuza kwangu na kukuepusha na mimi kutaendelea mpaka Siku ya Malipo na Hesabu.»

    [79] Iblisi akasema, «Mola wangu! ucheleweshe ukomo wa maisha yangu wala usiniangamize mpaka wakati ambapo viumbe watafufuliwa kutoka makaburini mwao»

    [80] Mwenyezi Mungu Akasema kumwambia, «Wewe ni miongoni mwa watakaocheleweshwa mpaka Siku ya kipindi maalumu

    [81] nayo ni Siku ya Mvuvio wa Kwanza ambapo viumbe watakufa.»

    [82] Iblisi akasema, «Naapa kwa enzi yako, ewe Mola wangu, na utukufu wako! Nitawapoteza binadamu wote

    [83] isipokuwa wale uliowatakasa miongoni mwa waja wako na ukawalinda nisiwapoteze, na usinipatie njia yoyote ya kuwaathiri.»

    [84] Mwenyezi Mungu Akasema, «Ukweli watoka kwangu , na sisemi isipokuwa ukweli

    [85] Nitaujaza moto wa Jahanamu ukukusanye wewe na kizazi chako na wale wote wenye kukufuata miongoni mwa wanadamu.»

    [86] Sema, ewe Mtume, uwaambie hawa washirikina miongoni mwa watu wako. «Sitaki kwenu ujira au malipo kwa kuwalingania nyinyi na kuwaongoza, na sidai jambo ambalo si langu, bali mimi nafuata yale ninayoletewa kwa njia ya wahyi, wala sijikalifishi kuleta mambo ya dhana na uzushi.»

    [87] Haikuwa hii Qur’ani isipokuwa ni ukumbusho kwa viumbe vyote: majini na binadamu, wapate kujikumbusha kwayo mambo yanayowanufaisha wao ya maslahi ya Dini yao na dunia yao

    [88] Na mtajua, tena mtajua, enyi washirikina, habari ya hii Qur’ani na ukweli wake, pindi utakaposhinda Uislamu na watu kuingia kwenye dini ya Mwenyezi Mungu mapote kwa mapote, na pia pindi mtakaposhukiwa na adhabu na kamba zote kuwakatikia

    Vikosi

    Surah 39

    [1] Kuteremshwa Qur’ani, Hakika ni kwamba, ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu Aliye Mshindi katika uweza Wake na utesaji Wake, Mwingi wa hekima katika uendeshaji mambo Wake na hukumu Zake

    [2] Kwa hakika sisi tumekuteremshia, ewe Mtume, Qur’ani inayoamuru haki na uadilifu. Basi muabudu Mwenyezi Mungu, Peke Yake, na umtakasie mambo yote ya Dini yako

    [3] Jua utanabahi kwamba ni haki ya Mwenyezi Mungu, Peke Yake, kutiiwa utiifu uliyotimia uliosalimika na ushirikina. Na wale wanaomshirikisha mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu wakawafanya wasiokuwa Yeye kuwa ni wategemewa, wanasema, «Hatuwaabudu waungu hawa pamoja na Mwenyezi Mungu isipokuwa wapate kutuombea kwa Mwenyezi Mungu na ili watukurubishe daraja Kwake.» Hivyo basi wakakufuru, kwani ibada na uombezi ni wa Mwenyezi Mungu, Peke Yake. Hakika Mwenyezi Mungu Atawapambanua, Siku ya Kiyama, baina ya Waumini wenye ikhlasi na wale wenye kumshirikisha mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu, katika yale waliokuwa wanatafautiana juu yake kuhusu vile walivyoabudu. Hapo amlipe kila mmoja kwa anachostahiki. Hakika Mwenyezi Mungu hawaelekezi kuongoka kwenye njia iliyonyoka wale wenye kumzulia urongo Mwenyezi Mungu, wenye kuzikanusha aya Zake na hoja Zake

    [4] Lau Angalitaka Mwenyezi Mungu kuwa na mtoto, Angalichagua, miongoni mwa viumbe Vyake, Anachotaka. Ameepukana Mwenyezi Mungu na kutakasika na kuwa na mtoto! Hakika Yeye ni Mmoja Aliye Pekee na kupwekeka, Mwenye kutegemewa kwa kila haja, Mwenye kutendesha nguvu ambaye Amewalazimisha viumbe kwa uweza Wake, basi kila kitu kinamdhalilikia Yeye na kumnyenyekea

    [5] Ameumba Mwenyezi Mungu mbingu na ardhi na viliyomo ndani yake, Anauleta usiku na kuuondoa mchana, na Anauleta mchana na kuuondoa usiku. Na Amelidhalilisha jua na mwezi ili manufaa ya waja yapangike. Kila mojawapo ya hivi viwili vinatembea kwenye sehemu yake ya kuzunguka mpaka kipindi cha kusimama Kiyama. Jua utanabahi, hakika Mwenyezi Mungu Aliyefanya matendo haya na Akawapa waja Wake neema hizi, Ndiye Mshindi juu ya viumbe Vyake, ni Mwingi wa kusamehe dhambi zao

    [6] Amewaumba nyinyi Mola wenu, enyi watu, kutokana na Ādam, na Akamuumba kutokana naye mke wake, na Akawaumbia, katika wanyama-hoa, aina nane za kiume na kike, miongoni mwa ngamia, ng’ombe, kondoo na mbuzi. Anawaumba nyinyi matumboni mwa mama zenu, muongo baada ya muongo wa uumbaji ndani ya magiza ya tumbo, kizazi na kifuko. Huyo Ndiye Mwenyezi Mungu Aliyeumba vitu hivi, Mola wenu Aliyepwekeka kwa ufalme na Aliye Mmoja katika uungu, Anayestahiki kuabudiwa PekeYake. Basi ni vipi mnaacha kumuabudu Yeye na mnaelekea kumuabudu asiyekuwa Yeye miongoni mwa viumbe Vyake

    [7] Mkimkanusha Mola wenu, enyi watu, mkaacha kumuamini na msiwafuate Mitume Wake, basi Mwenyezi Mungu ni Mkwasi na nyinyi, Hana haja kwenu, na nyinyi ndio mnaomuhitajia, na Haridhiki na ukanushaji wa waja Wake, wala Hawaamrishi hilo. Hakika ni kwamba Analoridhika nalo kwao ni wazishukuru neema Zake juu yao. Na hakuna nafsi yoyote itakayobeba dhambi za nafsi nyingine. Kisha kurudi kwa Mola wenu ndio mwisho wenu, na hapo Awapashe habari ya matendo yenu na Awahesabu kwayo. Hakika Yeye ni Mjuzi sana wa siri za nafsi na yanayofichwa na vifua

    [8] Na binadamu akipatwa na balaa, shida na maradhi humkumbuka Mola wake akataka nusura Yake na akamuomba, kisha Akimjibu na Akamuondolea shida yake na akampa neema Zake, huwa yuwasahau yale maombi yake aliyoyafanya kwa Mola wake alipomhitajia, na akawa atamshirikisha mwingine pamoja na Yeye, ili ampotoe mwingine amuepushe na kumuamini Mwenyezi Mungu na kumtii. Mwambie, ewe Mtume, kwa kumuonya, «Starehe na ukafiri wako muda mchache mpaka kufa kwako na kumalizika kipindi chako cha kuishi, hakika wewe ni miongoni mwa watu wa Motoni wenye kukaa milele humo.»

    [9] Je, kafiri huyu anayejistarehesha na ukafiri wake ni bora au ni yule anayemuabudu Mola wake na kumnyenyekea, anatumia nyakati za usiku kusimama kwenye Ibada na kumsujudia, anaogopa adhabu ya Akhera na kutarajia rehema ya Mola wake? Sema, ewe Nabii, «Je, wanalingana wale wanaomjua Mola wao na dini yao ya haki na wale wasiojua chochote katika hayo?» Hawalingani. Kwa hakika wanaokumbuka na kujua tafauti ni wale wenye akili timamu

    [10] Sema, ewe Nabii, kuwaambia waja wangu wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, «Mcheni Mwenyezi Mungu kwa kumtii na kujiepusha na matendo ya kumuasi.» Na wale waliofanya wema katika dunia hii kwa kumuabudu Mola wao na kumtii watapata wema huko Akhera, nao ni pepo, na wema huko duniani, ambao ni afya, riziki, ushindi na vinginevyo. Na ardhi ya Mwenyezi Mungu ni kunjufu, basi hamieni humo muende pale ambapo mtamuabudu Mola wenu na mtamakinika kusimamisha Dini yenu. Hakika Mwenyezi Mungu Atawapa wenye kuvumilia malipo yao mema huko Akhera bila mpaka wala hesabu wala kipimo. Huku ni kuyafanya makubwa malipo ya wenye kusubiri na thawabu zao

    [11] Sema, ewe Mtume, uwaambie watu, «Mwenyezi Mungu Ameniamrisha mimi na anayenifuata kumtakasia Yeye ibada, Peke Yake, bila mwingine

    [12] na Ameniamrisha niwe wa kwanza kujisalimisha miongoni mwa ummah wangu, akasalimu amri Kwake kwa kumpwekesha na kumtakasia Ibada na akajiepusha na kila kisichokuwa Yeye miongoni mwa waungu

    [13] Sema, ewe Mtume, uwaambie watu, «Mimi ninachelea nikimuasi Mola wangu, katika kile alichoniamuru cha kumuabudu na kumtakasia katika kumtii, adhabu ya Siku hiyo ambayo kituko chake ni kikubwa

    [14] Sema, ewe Mtume, «Kwa hakika Mimi ninamuabudu Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Asiye na mshirika, nikimtakasia ibada yangu na utiifu wangu

    [15] Basi nyinyi, enyi washirikina, abuduni mnachotaka badala ya Mwenyezi Mungu miongoni mwa mizimu na masanamu na visiokuwa hivyo katika viumbe Vyake, kwani hilo halinidhuru mimi chochote.» Na hili ni onyo na tahadharisho kwa anayemuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu na akamshirikisha mwingine pamoja na Yeye. Sema, ewe Mtume, «Hakika wale wenye hasara kikweli ni wale watakaohasirika nafsi zao na watu wao Siku ya Kiyama.» Na hiyo ni kwa sababu ya kuwapoteza duniani na kuwapotosha na njia ya Imani. Jua utanabahi kwamba hawa washirikina kupata hasara ya nafsi zao na watu wao Siku ya Kiyama ndiko kupata hasara kuliofunuka waziwazi

    [16] Hao wenye kupata hasara watawekewa juu yau Siku ya Kiyama, wakiwa ndani ya Jahanamu, vipande vya adhabu juu yao vinavyotokana na Moto, kama kwamba ni sakafu zilizojengewa na pia chini yao. Adhabu hiyo yenye sifa hizo ndio ile ambayo Mweyezi Mungu anawaogopesha nayo waja Wake ili wajihadhari nayo. Hivyo basi, enyi waja wangu, nicheni kwa kuzifuata amri zangu na kujiepusha na matendo ya kuniasi

    [17] Na wale waliojiepusha kumtii Shetani na kuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu na wakatubia kwa Mwenyezi Mungu kwa kumuabudu na kumtakasia Dini, basi hao wana bishara njema duniani ya kutajwa vyema na kuafikiwa na Mwenyezi Mungu, na bishara njema huko Akhera ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu na starehe za daima Peponi. Basi wape habari njema, ewe Nabii, waja wangu

    [18] ambao wanasikiliza maneno na kufuata yaliyo sawa zaidi. Na maneno mazuri zaidi na yaliyo sawa zaidi ni maneno ya Mwenyezi Mungu kisha ni maneno ya Mtume Wake. Hao ndio wale ambao Mwenyezi Mungu Amewaafikia kwenye usawa na haki na akawaongoza kwenye tabia na matendo bora zaidi; hao ndio watu wenye akili zilizotimia

    [19] Je, yule ambaye lilipasa juu yake neno la adhabu, kwa kuendelea kwenye upotevu na upotovu wake, kwani huna, ewe Mtume, njia yoyote ya kumuongoa. Je, unaweza kumuokoa aliye Motoni? Wewe si mwenye kuweza hilo

    [20] Lakini wale waliomcha Mola wao, kwa kumtii na kwa kumtakasia ibada, watakuwa na vyumba, huko Peponi, vilivyojengewa baadhi yake juu ya vingine, ambavyo chini ya miti yake mito inapita. Mwenyezi Mungu amewaahidi (vyumba hivyo) waja Wake wachamungu, ahadi ambayo ni yenye kutimia kwa uhakika, na Mwenyezi Mungu Haendi kinyume na ahadi

    [21] Je, huoni, ewe Mtume, kuwa Mwenyezi Mungu Anateremsha mvua kutoka mawinguni, akaitia ardhini, akaifanya ni mikondo yenye kuchimbuka na maji yenye kutiririka, kisha anatoa kwa maji hayo mimea yenye rangi tafauti na aina mbalimbali, kisha inakauka baada ya ubichi wake na mng’aro wake, hapo utaiona imebadilika kuwa rangi ya manjano, kisha Anaifanya kuwa ni mapepe yaliyovunjikavunjika na kumumunyuka? Kwa hakika, katika kitendo hiko cha Mwenyezi Mungu pana ukumbusho na mawaidha kwa wenye akili timamu

    [22] Je, yule ambaye Mwenyezi Mungu Amemkunjua kifua chake, akabahatika kuukubali Uislamu, kuufuata na kuuamini, akawa yuko kwenye uwazi wa jambo lake na uongofu kutoka kwa Mola wake, je ni kama yule ambaye hayuko hivyo? Hao wawili hawalingani. Basi ole wao na maangamivu wale ambao nyoyo zao zilikuwa ngumu na zikajiepusha na utajo wa Mwenyezi Mungu. Hao wako kwenye upotevu ulio kando na haki waziwazi

    [23] Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Aliteremsha Mazungumzo mazuri zaidi kuliko yote, nayo ni Qur’ani tukufu, inayofanana katika uzuri wake, upangikaji wake na kutotafautiana kwake, ndani yake mna hadithi, hukumu, hoja na dalili zilizo wazi. Kusomwa kwake kunarudiwa na ule wingi wa kuikariri hauifanyi ichokeshe. Isomwapo huifanya miili ya wenye kuisikia itetemeke na zitikisike ngozi za wale wanaomuogopa Mola wao, kwa kuathirika na yale yaliyomo ndani yake ya kutisha na kuonya, kisha zikalainika ngozi zao na nyoyo zao kwa kufurahia bishara iliyomo ya ahadi njema na mahimizo ya kufanya kheri. Kuathirika huko na Qur’ani ni uongofu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa waja Wake. Na yoyote yule ambaye Mwenyezi Mungu Anayempoteza asiiamini hii Qur’ani kwa sababu ya ukafiri wake na ushindani wake, basi hana muongozi mwenye kumuongoa na kumuafikia

    [24] Je, Yule atakayetupwa Motoni akiwa amefungwa, akawa hawezi kujikinga na Moto isipokuwa kwa uso wake, kwa ukafiri wake na upotevu wake, ni bora au ni yule anayestarehe Peponi, kwa kuwa Mwenyezi Mungu Amemuongoa? Na madhalimu Siku hiyo wataambiwa, «Onjeni madhara ya yale mliokuwa mkiyachuma duniani ya kumuasi Mwenyezi Mungu

    [25] Wale waliokuwa kabla ya watu wako, ewe Mtume, waliwakanusha Mitume wao, hivyo basi adhabu ikawajia kwa namna ambayo hawakuhisi kuja kwake

    [26] Basi Mwenyezi Mungu Akawaonjesha ummah waliokanusha adhabu na unyonge duniani, na Akawaandalia adhabu kali zaidi na ngumu zaidi huko Akhera. Lau hawa washirikina wangalijua, kuwa kile kilichowashukia ni kwa sababu ya ukafiri wao na ukanushaji wao, wangaliwaidhika

    [27] Na kwa hakika tumewapigia hawa wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu kila mfano katika mifano ya watu wa kame zilizopita, kwa kuwatisha na kuwaonya, ili wakumbuke na wakomeke na lile ambalo wako nalo la kumkufuru Mwenyezi Mungu

    [28] Na tumeijaalia hii Qur’ani ni kwa lugha ya Kiarabu, yenye matamshi yaliyofunuka wazi na yenye maana mepesi yasiyo na uchanganyifu wala upotofu, huenda wao wakamcha Mwenyezi Mungu kwa kufuata amri Zake na kuepuka makatazo yake

    [29] Mwenyezi Mungu Anapiga mfano wa mtumwa aliyemilikiwa na washirika wenye kuteta, na mtumwa mwingine aliyekuwa ni wa mmiliki mmoja tu, akawa yuwajua matakwa yake na yanayomridhisha. Je, mfano wa wawili hao unalingana? Basi Hivyo ndivo alivyo mshirikina. Yeye yuko katika hali ya mshangao na shaka, na Muumini yuko katika raha na utulivu. Sifa njema kamilifu zilizotimia ni za Mwenyezi Mungu, Peke Yake, lakini washirikina hawaijui haki wakaifuata

    [30] Wewe ni mwenye kufa, ewe Mtume, na wao ni wenye kufa

    [31] kisha nyote, Siku ya Kiyama. Kwa Mola wenu mtagombana, hapo Ahukumu baina yenu kwa uadilifu na usawa

    [32] Hakuna yoyote dhalimu zaidi kuliko yule aliyemzulia Mwenyezi Mungu urongo, kwa kumnasibishia sifa isiyofaa kusifika nayo, kama vile kuwa na mshirika na mtoto, au akasema, «Mimi nimeletewa wahyi,» na hali yeye hakuletewa wahyi wa kitu chochote. Na hakuna dhalimu zaidi kuliko yule aliyeikanusha haki iliyoteremka kwa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie. Kwani si yako huko Motoni mashukio na makazi kwa waliomkufuru Mwenyezi Mungu na wasimuamini Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie? Ndio, yako

    [33] Na yule aliyekuja na ukweli wa maneno na vitendo, miongoni mwa Manabii na wafuasi wao, na akaukubali kiimani na kivitendo, hao ndio waliokusanya sifa za uchamungu, akiwa mbele yao yule aliye mwisho wa Manabii na Mitume, Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na wale wenye kumuamini, wanaoifuata Sheria yake kivitendo miongoni mwa Maswahaba, radhi za Mwenyezi Mungu ziwashukie, kisha wale wenye kuja baada yao mpaka Siku ya Malipo

    [34] Wao watayapata wanayoyataka kwa Mola wao miongoni mwa aina ya vitu vya ladha na matamanio. Hayo ndiyo malipo ya anayemtii Mola wake vile inavyopasa kutiiwa na akamuabudu vile inavyopasa kuabudiwa

    [35] Ili Mwenyezi Mungu Awafutie yale maovu zaidi ya matendo waliyoyafanya ulimwenguni kwa sababu ya kile walichokifanya cha kurudi kwa Mwenyezi Mungu kwa kutubia makosa waliyoyatenda huko, na ili Mwenyezi Mungu Awalipe mema, kwa utiifu wao ulimwenguni, malipo mazuri zaidi ya matendo ambayo walikuwa wakiyafanya, nayo ni Pepo

    [36] Je, kwani Mwenyezi Mungu si Mwenye kumtosheleza mja Wake Muhammad vile vitisho vya washirikina na vitimbi vyao kuwa wao hawatamfikia kwa ubaya wowote? Ndio, Yeye Atamtosheleza katika jambo la Dini yake na dunia yake, na Atamtetea dhidi ya yoyote anayemtaka kwa ubaya. Na wao wanakutisha, ewe Mtume, na waungu wao wanaodai kuwa watakudhuru. Na yoyote yule ambaye Mwenyezi Mungu Ameondoa msaada Wake kwake na Akamfanya apotee njia ya haki, basi huyo hana muongozi wa kumuongoza Kwake

    [37] Na yoyote yule ambaye Mwenyezi Mungu Amemuafikia kumuamini Yeye na kufanya matendo yanayoambatana na Kitabu Chake na kumfuata Mtume Wake, basi huyo hana mwenye kumpoteza na kumpotosha na haki ambayo amesimama nayo. Kwani Mwenyezi Mungu si Mshindi katika kuwatesa viumbe Wake waliomkufuru na wale waliomuasi

    [38] Na unapowauliza, ewe Mtume, hawa washirikina wanaomuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu, «Ni nani aliyeziumba hizi mbingu na ardhi?» watasema, «Aliyeziumba ni Mwenyezi Mungu.» Kwa hivyo wao wanamkubali Muumba. Basi waambie, «Je, waungu hawa mnaowashirikisha na Mwenyezi Mungu wanaweza kuniepushia makero ambayo Mwenyezi Mungu Amenikadiria au kuniondolea mambo ninayoyachukia yaliyonifika? Na je, wanaweza wao kuzuia manufaa aliyonisahilishia Mwenyezi Mungu nisiyapate au kunizuilia rehema ya Mwenyezi Mungu isinifikie?» Wao watasema, «Hawawezi hilo.» Waambie, «Mwenye kunitosheleza na kuniridhisha mimi ni Mwenyezi Mungu. Kwake yeye wanategemea wenye kutegemea katika kuleta yanayowafaa na kuzuia yanayowadhuru. Yule ambaye kwenye mkono wake peke yake kuna toshelezo, Yeye Ndiye Mwenye kunitosha na Atanikifia kila linalonitia hamu

    [39] Sema, ewe Mtume, uwaambie watu wako wenye ukaidi, «Fanyeni matendo kwa namna inayoridhisha nafsi zenu, kwa kuwa mmemuabudu asiyestahiki kuabudiwa na asiye na amri ya jambo lolote. Mimi ni mwenye kufanya yale niliyoamrishwa ya kuelekea kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake katika maneno yangu na vitendo vyangu

    [40] Na mtajua ni yupi atakayejiwa na adhabu yenye kumfanya mnyonge katika maisha ya ulimwenguni na atakayeshukiwa na adhabu ya daima kesho Akhera, haitamuepuka wala haitamuondokea

    [41] Hakika sisi tumekuteremshia wewe, ewe Mtume, Qur’ani kwa haki ikiwa ni yenye kuwaongoza viumbe wote kwenye njia ya uongofu. Basi mwenye kuongoka kwa mwangaza wake na akayatumia yaliyomo ndani yake na akasimama imara kufuata njia yake, basi manufaa ya kufanya hilo yatamrudia mwenyewe. Na mwenye kupotea baada ya kubainikiwa na uongofu, basi madhara yake yatamrudia mwenyewe, na hilo halitamdhuru Mwenyezi Mungu kitu chochote. Na hukuwa wewe, ewe Mtume, ni mwakilishwa wa kuyatunza matendo yao, kuwahesabu kwa hayo na kuwalazimisha unayoyataka, jukumu lako wewe si lingine isipokuwa ni kufikisha ujumbe

    [42] Mwenyezi Mungu Ndiye Anayezikamata nafsi wakati zinapokufa. Kufa huku ni kufa kukubwa, kufa kwa kushukiwa na mauti kwa ajali kukoma. Na zile nafsi ambazo hazikufa Anazikamata katika hali ya kulala kwake, nako ndiko kufa kudogo. Hivyo basi Akazizuia, kati ya hizi nafsi mbili, ile Aliyoitolea uamuzi ife , nayo ni ya yule aliyekufa, na anaiachilia nafsi nyingine mpaka ikamilishe muda wake wa kuishi na riziki yake, nako ni kuirudisha kwenye mwili wa mwenye nafsi hiyo. Kwa kweli, katika kule kukamata kwa Mwenyezi Mungu nafsi ya aliyekufa na aliyelala na kuiachilia nafsi ya aliyelala na kuizuia nafsi ya aliyekufa kuna dalili waziwazi za uweza wa Mwenyezi Mungu kwa anayefikiria na kuzingatia

    [43] Au kwani hawa wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu wamewachukua badala Yake Yeye waungu wao wanaowaabudu wakawafanya ni waombezi wakuwaombea kwa Mwenyezi Mungu katika haja zao? Waambie, «Je mnawafanya ni waombezi kama mnavyodai, ingawa waungu hao hawamiliki chochote na hawafahamu kamwe kuwa nyinyi mnawaabudu

    [44] Waambie, ewe Mtume, hao washirikina, «Ni wa Mwenyezi Mungu uombezi wote. Ni Yake Yeye mamalaka ya mbinguni na ardhini na vilivyoko baina yake. Amri yote ni ya Mwenyezi Mungu Peke Yake. Na hakuna yoyote atakayeombea mbele Yake isipokuwa kwa idhini Yake. Yeye Ndiye Anayemiliki mbingu na ardhi na anayeendesha mambo yake. Lilo wajibu ni kutakwa uombezi kutoka kwa anayeumiliki na atakasiwe Yeye kwa ibada, na usitakwe kutoka kwa waungu wasiodhuru wala kunufaisha, kisha Kwake Yeye mtarudishwa baada ya kufa kwenu ili mhesabiwe na mlipwe

    [45] Na Anapotajwa Mwenyezi Mungu Peke Yake zinachukia nyoyo za wasioamini Marejeo na Ufufuzi baada ya kufa, na wanapotajwa wale wasiokuwa Yeye miongoni masanamu, mizimu na wategemewa huwa wakifurahika kwa kuwa ushirikina unaafikiana na matamanio yao

    [46] Sema, «Ewe Mwenyezi Mungu! Ewe Muumba mbingu na ardhi, Mwenye kuanzisha kuzitengeneza bila kuwa na mfano uliotangulia! Mjuzi wa siri na dhahiri! Wewe unatoa uamuzi baina ya waja wako Siku ya Kiyama katika yale ambayo walikuwa wakitafautiana juu yake ya maneno kuhusu wewe, ukubwa wako, utawala wako na kuhusu kukuamini wewe na kumuamini Mtume wako. Niongoze mimi kwenye haki ambayo kumetafautiana juu yake kwa amri yako. Hakika wewe unamuongoza unayemtaka kwenye njia iliyolingana sawa.» Hii ilikuwa ni miongoni mwa dua za Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, nayo ina mafundisho kwa waja watake himaya kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na wamuombe kwa mjina Yake mazuri na sifa Zake tukufu

    [47] Na lau hao wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu wangalikuwa nacho kila kilichoko kwenye ardhi miongoni mwa mali, vitu vya thamani na vingine mfano wake pamoja navyo kuongezea, wangalikitoa Siku ya Kiyama ili wajikomboe kwacho na adhabu mbaya. Na lau wangalikitoa na wakataka kujikomboa kwacho hakingalikubaliwa kutoka kwao na hakingaliwafalia kitu chochote kuwaepushia adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na itawadhihirikia wao Siku hiyo amri ya Mwenyezi Mungu na adhabu Yake wasizokuwa wakizidhania duniani kuwa zitawashukia

    [48] Na yatawadhihirikia hao wakanushaji, Siku ya kuhesabiwa, malipo ya maovu yao waliyoyatenda, kwa kuwa walimnasibishia Mwenyezi Mungu sifa isiyolingana na Yeye, na wakafanya maasia katika maisha yao, na itawazunguka adhabu kali kila upande ikiwa ni mateso kwao kwa kulifanyia shere onyo la adhabu ambayo Mtume alikuwa akiwaahidi kuwa itawapata wakawa hawaitii maanani

    [49] Na ikimpata mwanadamu shida na madhara humuomba Mola wake amuondolee, na tunapomuondolea yaliyompata na tukampa neema kutoka kwetu hurudi kumkanusha Mola wake na kukataa wema Wake na huwa akisema, «Haya niliyopewa yatokamana na ujuzi wa Mwenyezi Mungu kuwa mimi ninafaa na ninastahiki kuyapata. Bali huo ni mtihani wa Mwenyezi Mungu kuwatahini waja Wake, ili Atazame ni yupi anayemshukuru kwa kumtenga na anayemkanusha. Lakini wengi wao, kwa ujinga wao na dhana zao mbaya, hawajui kuwa hayo ni mavuto kideogo-kidogo kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ni mtihani kwao kuhusu kushukuru neema

    [50] Kauli kama hii ilisemwa na ummah waliopita wenye kukanusha, na yasiwafalie kitu, ilipowajia adhabu, yale mali ambayo walikuwa wakiyachuma na watoto

    [51] Yakawapata wale waliyosema kauli hii, miongoni mwa ummah waliopita, mateso ya matendo mabaya waliyoyachuma, hivyo basi wakaharakishiwa laana katika maisha ya duniani. Na wale waliojidhulumu nafsi zao katika watu wako, ewe Mtume, na wakasema kauli hii, yatawapata mateso ya yale mabaya waliyoyachuma kama yaliyowapata waliokuwa kabla yao, na hawakuwa wao ni wenye kumponyoka Mwenyezi Mungu wala kumshinda

    [52] Kwani hao hawajui kwamba riziki ya Mwenyezi Mungu kwa binadamu haimaanishi kuwa aliyeruzukiwa ana hali njema na kwamba Mwenyezi Mungu Ana hekima nyingi, Anamkunjulia riziki Anayemtaka katika waja Wake, awe mwema au muovu, na Anambania Anayemtaka katika wao? Hakika katika kukunjua na kubana riziki kuna dalili zilizo wazi kwa watu wanaoamini amri ya Mwenyezi Mungu na kuifanyia kazi

    [53] Sema, ewe Mtume, kuwaambia waja wangu waliojidhulumu nafsi zao kwa kuyajia madhambi ambayo nafsi zao zinawaitia, «Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu, kwa wingi wa madhambi yenu, kwani Mwenyezi mungu Anasamehe dhambi zote kwa mwenye kutubia kutokana nayo na akayaacha namna yatakavyokuwa. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe madhambi ya wenye kutubia miongoni mwa waja Wake, ni Mwenye kuwarehemu

    [54] «Na rudini kwa Mola wenu, enyi watu, kwa kutii na kutubia, na mnyenyekeeni kabla hayajawashukia mateso Yake, kisha hakuna yoyote Atakayewanusuru badala ya Mwenyezi Mungu

    [55] «Na fuateni bora zaidi wa kile kilichoteremshwa kwenu kutoka kwa Mola wenu, nacho ni Qur’ani tukufu, na yote ni njema, basi jilazimisheni kufuata amri zake na jiepusheni na makatazo yake kabla haijawajia nyinyi adhabu kwa ghafla na nyinyi hamuijui.»

    [56] «Na mtiini Mola wenu na tubieni Kwake ili isije nafsi ikajuta na ikasema, ‘Ee hasara yangu kwa matendo mema niliyoyapoteza ulimwenguni katika yale Aliyoamrisha Mwenyezi Mungu na nikafanya kasoro katika kumtii na kutekeleza haki Yake,! Na ingawa ulimwenguni nilikuwa ni miongoni mwa waliokuwa wakiifanyia shere amri ya Mwenyezi Mungu, Kitabu Chake, Mtume Wake na waliomuamini.’

    [57] «Au ikasema, ‘Lau Mwenyezi Mungu Angaliniongoza kwenye Dini Yake ningalikuwa ni miongoni mwa wenye kujikinga na ushirikina na maasia.’»

    [58] «Au ikasema, itakapo kuiona adhabu ya Mwenyezi Mungu imeizunguka Siku ya Kiyama, ‘Natamani nipatiwe nafasi ya kurudi kwenye maisha ya kilimwengu nikawa huko ni miongoni mwa wenye kufanya wema kwa kumtii Mola wao na kufanya matendo yaliyoamrishwa na Mitume.’»

    [59] Maneno siyo kama unavyosema, Kwa hakika aya zangu zilizo wazi zenye kuitolea ushahidi haki zilikujia ukazikanusha, ukazifanyia kiburi usizikubali na usizifuate na ukawa ni miongoni mwa wenye kumkanusha Mwenyezi Mungu na Mitume Wake

    [60] Na Siku ya Kiyama utawaona hao wakanushaji, waliomsifu Mola wao kwa sifa zisizolingana na Yeye na wakamnasibisha Yeye na mshirika na mwana, nyuso zao zimekuwa nyeusi. Si ndani ya Jahanamu kuna mashukio na makao kwa aliyemfanyia Mwenyezi Mungu kiburi akakataa kumpwekesha na kumtii? Ndio

    [61] Na Mwenyezi Mungu Atawaokoa na Moto wa Jahanamu na adhabu yake wale waliomcha Mola wao kwa kutekeleza faradhi Alizoziamrisha na kujiepusha na yale Aliyoyakataza kwa kufuzu kwao na kutimia matakwa yao, nako ni kufaulu kupata Pepo. Hawataguswa na kitu chochote cha adhabu wala hawatazisikitikia hadhi za duniani walizozikosa

    [62] Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Ndiye Muumba wa vitu vyote, Ndiye Mola wa hivyo vitu na Ndiye Mwenye kuviendesha. Na Yeye ni Mtunzi wa kila kitu. Anayaendesha mambo yote ya viumbe Vyake

    [63] Ni za Mwenyezi Mungu funguo za hazina za mbinguni na ardhini, Anatoa kutoka kwenye hazina hizo kuwapa viumbe Vyake namna Anavyotaka. Na wale waliozikanusha aya za Qur’ani na dalili wazi zilizomo, hao ndio wenye kupata hasara ulimwenguni kwa kutoafikiwa kuamini, na kesho Akhera kwa kukaa milele Motoni

    [64] Sema, ewe Mtume, uwaambie washirikina wa watu wako, «Je, yule asiyekuwa Mwenyezi Mungu, enyi wajinga, mnanishauri nimuabudu na hali ibada haifai kufanyiwa kitu chochote isipokuwa Yeye?»

    [65] Kwa hakika uliletewa wahyi wewe, ewe Mtume, na Mitume waliokuwa kabla yako kwamba lau ulimshirikisha Mwenyezi Mungu na asiyekuwa Yeye amali zako zingalibatilika na ungalikuwa ni miongoni mwa walioangamia waliopata hasara, hivyo basi ukapata hasara ya dini yako na Akhera Yako, kwani pamoja na ushirikina haikubaliwi amali njema

    [66] Bali Mwenyezi Mungu muabudu, ewe Mtume, kwa kumtakasia ibada Peke Yake Asiye na mshirika, na uwe ni miongoni mwa wenye kuzishukuru neema za Mwenyezi Mungu

    [67] Na hawa washirikina hawakumuadhimisha Mwenyezi Mungu vile Anavyostahiki kuadhimishwa, kwa kuwa wamemuabudu asiyekuwa Yeye pamoja na Yeye miongoni mwa wale wasionufaisha wala kudhuru, wakamfanya muumbwa, pamoja na uelemevu wake, kuwa ni sawa na Muumba Mtukufu, Ambaye kotokana na uweza Wake mkubwa ni kwamba ardhi yote itakuwa iko mkononi Mwake Siku ya Kiyama, na mbingu zitakuwa zimekunjwa kwa mkono Wake wa kulia. Ametakasika Mwenyezi Mungu na kutukuka kwa kuepukana na kile wanaomshirikisha nacho hao washirikina. Katika aya hii pana dalili ya kuthibitisha kushika kwa mkono, mkono wa kulia na kukunja kwa Mwenyezi Mungu kama vile inavyolingana na haiba Yake na utukufu Wake bila kueleza Yuko vipi wala kufananisha

    [68] Na kutapulizwa kwenye baragumu na hapo atakufa kila aliye kwenye mbingu na ardhi, isipokuwa anayemtaka Mwenyezi Mungu asife. Kisha Malaika Atapuliza mara ya pili kwenye baragumu akitangaza kufufuliwa viumbe wapate kuhesabiwa mbele ya Mola wao, na wakitahamaki wao wamesimama kutoka makaburini mwao wanangojea yale Atakayowafanyia Mwenyezi Mungu

    [69] Na ardhi itatoa mwangaza Siku ya Kiyama, Atakapo kujitokeza Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, ili kutoa hukumu, na hapo Malaika wautandaze ukurasa wa kila mtu, na Mitume waletwe na mashahidi wa kila ummah, ili Mwenyezi Mungu Awaulize manabii kuhusu ufikishaji ujumbe kwa ummah wao na majibu waliopata kutoka kwao. Kadhalika waje ummah wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu, ili kuutolea ushahidi ufikishaji wa Mitume waliotangulia kwa ummah wao iwapo watakataa kuwa walifikishiwa. Na hapo ushahidi uthibiti juu ya ummah wote, na Mwenyezi Mungu Atoe hukumu baina ya waja kwa uadilifu uliotimia. Na wao hawatadhulumiwa kitu chochote kwa kupunguziwa thawabu au kwa kuongezewa mateso

    [70] Na hapo Mwenyezi Mungu Aipe kila nafsi malipo ya matendo yake, mazuri na mabaya. Na Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake na kutuka ni Kwake, Ndiye Anayejua zaidi yale waliyoyafanya duniani ya utiifu au ya uasi

    [71] Na waongozwe wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu na Mitume Wake kuelekezwa upande wa Jahanamu makundi kwa makundi, na watakapoifikia itafunguliwa milango yake saba na wale washika hazina wake waliowakilishwa kuisimamia hiyo Jahanamu. Na hao washika hazina watawakaripia kwa kusema, «Vipi nyinyi mlimuasi Mwenyezi Mungu na mkakataa kuwa Yeye ni Mola wa haki Peke Yake.? Kwani hamkutumiwa Mitume miongoni mwenu wanaowasomea aya za Mola wenu na kuwaonya na vituko vya Siku ya Leo?» Watasema wakikubali makosa yao, «Ndio, walitujia na ukweli Mitume wa Mola wetu na wakatuonya na Siku ya Leo, lakini lishathibiti neno la Mwenyezi Mungu kwamba adhabu Yake itawafikia wenye kumkanusha Yeye.»

    [72] Na wataambiwa wale wenye kukataa kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Mola wa haki, kwa kuwatweza na kuwadhalilisha, «Ingieni kwenye milango ya Jahanamu, hali ya kukaa humo milele.» Ni mbaya mno mwisho wa wale wanaolifanyia kiburi jambo la kumuamini Mwenyezi Mungu na kufuata kivitendo sheria Yake

    [73] Na wataongozwa wale waliomcha Mola wao, kwa kumpwekwsha na kufanya vitendo vya utiifu Kwake, wapelekwe Peponi, makundi kwa makundi. Na watakapoifikia na waombewe kuingia, milango yake itafunguliwa, na Malaika waliowakilishwa kuisimamia Pepo watawakongowea na watawaamkia kwa ucheshi na furaha kwa kuwa wamesafishika na athari za maasia na watawaambia, «Amani iwe juu yenu! Mmesalimika na kila baya. Hali zenu ni nzuri. Basi ingieni Peponi mkae milele humo.»

    [74] Na hapo Waumini watasema, «Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu Aliyetuhakikishia ukweli wa ahadi Yake Aliyotuahidi kupitia kwa ndimi za Mitume Wake, na Akaturithisha ardhi ya Pepo tukawa tunashukia kwenye ardhi hiyo popote pale tunapotaka. Ni mazuri yaliyoje malipo ya watu wema waliojitahidi kumtii Mola wao.»

    [75] Na utawaona Malaika, ewe Nabii, wameizunguka 'Arshi ya Mwingi wa rehema, wanamtakasa Mola wao na kumuepusha na kila kisichofaa kunasibishwa nacho, (na utaona kuwa) Mwenyezi Mungu Aliyetakasika na kutukuka Amehukumu baina ya viumbe kwa uhaki na uadilifu, Akawakalisha wenye kuamini Peponi na wenye kukufuru Motoni. Na hapo kutasemwa, «Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe wote kwa uamuzi Aliyoutoa baina ya watu wa Peponi na Motoni, shukrani ya kutambua wema na hisani na shukrani ya kutambua uadilifu na hekima.»

    Mghafiri

    Surah 40

    [1] «Ḥā, Mīm» Yametangulia maelezo kuhusu herufi zilizokatwa na kutengwa mwanzo wa sura ya Al-Baqarah

    [2] Kuteremshiwa Qur’ani Nabii Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kunatokana na Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, Mwenye ushindi Ambaye kwa enzi Yake amekilazimisha kila kiumbe, Mwenye ujuzi wa kila kitu

    [3] Mwenye kusamehe dhambi za wafanya dhambi, Mwenye kukubali toba ya wenye kutubia, Mkali wa kutesa juu ya aliyejasiri kufanya dhambi na kutotubia kutokana nayo. Na Yeye. Kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Ndiye Mwenye kuwaneemesha na kuwafadhili waja Wake watiifu. Hakuna muabudiwa yoyote anayefaa kuabudiwa isipokuwa Yeye. Kwake Yeye ndio mwisho wa viumbe wote Siku hiyo ya Hesabu, ili Amlipe kila mmoja kile anachostahiki

    [4] Hakuna anayeteta kuhusu aya za Mwenyezi Mungu na dalili Zake za kutolea ushahidi umoja wa Mwenyezi Mungu, akawa anazikabili kwa ubatilifu isipokuwa wapinzani wenye kukataa kuwa Yeye Ndiye Mola wa kweli Anayestahiki kuabudiwa Peke Yake. Basi kusikudanganye wewe kule kutanga kwao mijini kwa aina mbalimbali za biashara, shughuli za kuchuma, starehe za ulimwenguni na uzuri wake

    [5] Walikanusha, kabla ya makafiri hawa, watu wa Nūḥ na waliowafuata wao miongoni mwa ummah waliotangaza vita vyao dhidi ya Mitume, kama vile 'Ād na Thamūd, kwa kuwa waliazimia kuwaudhi na wakaamua kwa umoja wao wawaadhibu au wawaue. Na kila watu, miongoni mwa ummah hawa wenye kuwakanusha Mitume wao, walitaka kumuua Mtume wao na wakajadiliana na yeye kwa njia ya ubatilifu ili waitangue haki kwa kujadili kwao, na kwa hivyo nikawatesa. Basi ni namna gani kule kuwatesa kwangu kulikuwa ni mazingatio kwa viumbe na mawaidha kwa watakaokuja baada yao

    [6] Na kama yalivyothibiti mateso kwa ummah waliopita waliowakanusha Mitume wao, pia yalithibiti kwa wale waliokufuru kuwa wao ni watu wa Motoni

    [7] Wale wanaoibeba ‘Arshi ya Mwenyezi Mungu miongoni mwa Malaika na wale walioko pambizoni mwake kati ya wale wanaoizunguka miongoni mwao, wanamtakasa Mwenyezi Mungu na kila kasoro, wanamshukuru kwa yale Anayostahiki, wanamuamini Yeye haki ya kumuamini na wanamuomba Awasamehe Waumini kwa kusema, «Mola wetu! Umekienea kile kitu kwa rehema na ujuzi. Kwa hivyo wasamehe wale waliotubia kutokana na ushirikina na maasia na wakafuata njia uliyowaamrisha waifuate, nayo ni Uislamu, na uwaepushie adhabu ya Moto na vituko vyake

    [8] «Mola wetu! Na uwatie Waumini kwenye mabustani ya Pepo ya 'Adn uliyowaahidi wao na baba zao, wake zao na watoto wao waliokuwa wema kwa Imani na matendo mazuri. Hakika wewe Ndiye Mshindi Mwenye kukilazimisha kila kitu, Ndiye Mwingi wa hekima katika uendeshaji Wake na utengenezaji Wake

    [9] «Na uwaepushie mwisho mbaya wa dhambi zao, usiwaadhibu kwa dhambi hizo. Na yoyote yule utakayemuepushia maovu Siku ya kuhesabiwa, huyo umeshamrehemu na umempa neema ya kuokolewa na adhabu yako. Na huko ndiko kufaulu kukubwa ambako hakuna kufaulu kupita huko.»

    [10] Hakika ya wale waliokanusha kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Mola wa haki na wakaielekeza ibada kwa asiyekuwa Yeye, watakapovishuhudia wenyewe vituko vya Moto watajichukia machukivu makubwa, na hapo walinzi wa Moto wa Jahanamu watawaita na kuwaambia, «Machukivu ya Mwenyezi Mungu kwenu huko ulimwenguni, Alipowataka nyinyi mumuamini Yeye na muwafuate Mitume Wake na mkakataa, yalikuwa makubwa zaidi kuliko vile mnavyojichukia nyinyi wenyewe hivi sasa, baada ya kujua kwenu kuwa mnastahili hasira za mwenyezi Mungu na adhabu Yake.»

    [11] Makafiri watasema, «Mola wetu! Umetufisha mara mbili: tulipokuwa matone ya manii ndani ya matumbo ya mama zetu kabla ya kupulizwa roho na ulipokoma muda wetu wa kuishi katika uhai wa duniani, na umetuhuisha mara mbili:katika nyumba ya duniani siku tuliyozaliwa na siku tuliyofufuliwa kutoka makaburini mwetu. Kwa hivyo sisi sasa tunakubali makosa yetu yaliyotangulia, basi je kuna njia yoyote ya sisi kutoka Motoni na uturudishe kupitia njia hiyo duniani tukapate kufanya matendo ya utiifu kwako?» Lakini haliwi hilo kabisa la wao kunufaika kwa kukubali kwao huku

    [12] Adhabu hiyo ambayo itakayowapata, enyi makafiri, ni kwa sababu ya kuwa nyinyi mlikuwa mkiitwa kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtakasia matendo mema Kwake mnalikanusha hilo, na ashirikishwapo Mwenyezi Mungu mnaliamini hilo na mnalifuata. Basi Mwenyezi Mungu Ndiye Muamuzi kwa viumbe wake, Ndiye Muadilifu Asiyedhulumu, Anamuongoza Ananayemtaka na Anampoteza Anayemtaka, Anamrehemu Anayemtaka na Anamuadhibu Anayemtaka. Hapana Mola isipokuwa Yeye, Aliye juu kidhati, kicheo na kinguvu (kupitisha Analolitaka)

    [13] Yeye Ndiye Anayewaonyesha, enyi watu, uweza Wake kwa zile alama kubwa zenye kutolea ushahidi ukamilifu wa Mwenye kuziumba na kuzianzisha, na Anawateremshia mvua kutoka mawinguni ambayo kwayo mnaruzukiwa. Na hajikumbushi kwa alama hizi isipokuwa yule anayerudi kwenye utiifu wa Mwenyezi Mungu na kumtakasia ibada

    [14] Basi, enyi waumini, mtakasieni Mwenyezi Mungu Peke Yake ibada na dua, na endeni kinyume na washirikina katika nyendo zao, na hata kama hilo litawakasirisha wao msiwajali

    [15] Mwenyezi Mungu Ndiye Mtukufu Aliye juu kabisa Ambaye daraja Zake zimepaa juu sana kwa namna ya kuwa Yeye, kwa daraja hizo, Ameepukana na viumbe Vyake na kimekuwa juu cheo Chake. Yeye Ndiye Mwenye 'Arsh iliyo kubwa. Na miongoni mwa rehema Zake kwa waja Wake ni kuwatumia Wajumbe kuwapelekea wahyi ambao kwa wahyi huo wanapata uhai na kuwa kwenye mwangaza wa kuwapa muelekeo katika mambo yao, ili hao Mitume (walioletewa wahyi) wawaogopeshe waja wa Mwenyezi Mungu na wawaonye Siku ya Kiyama ambayo watakutana Siku hiyo wa mwanzo na wa mwisho

    [16] Siku ya Kiyama watajitokeza viumbe mbele ya Mola wao, hakuna chochote kuhusu wao au kuhusu matendo yao waliyoyafanya ulimwenguni kitakachofichamana kwa Mwenyezi Mungu. Hapo Atasema Mwenyezi Mungu Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu, «Ni wa nani ufalme na mamlaka Siku ya Leo?» Na Ajijibu Mwenyewe, «Ni vya Mwenyezi Mungu Aliyepwekeka kwa majina Yake, sifa Zake na vitendo Vyake, Mwenye kutendesha nguvu Aliyevilazimisha viumbe vyote kwa uweza Wake na enzi Yake.»

    [17] Leo italipwa kila nafsi kwa kile ilichokitenda duniani, chema au kiovu; hakuna maonevu leo kufanyiwa yoyote, ya kuongezewa dhambi zake au kupunguziwa thawabu zake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwpesi wa kuhesabu, basi msiione Siku hiyo ni yenye kuchelewa kufika, kwani iko karibu

    [18] Na uwaonye watu, ewe Mtume, na Siku ya Kiyama iliyo karibu, ingawa wao waiona kuwa iko mbali, pindi nyoyo za waja, kwa kuogopa mateso ya Mwenyezi Mungu, zitakapopanda juu vifuani mwao na kushikana na koo zao, na hali wao wamejawa na hamu na huzuni. Madhalimu hawatakuwa na jamaa wa karibu wala rafiki wala muombezi wa kuwaombea kwa Mola wao akawa ni mwenye kukubaliwa

    [19] Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu, Anakijua kile kinachopitishwa na maangalizi ya macho kwa njia ya siri na kuiba na kile ambacho mtu anakidhamiria katika nafsi yake kizuri au kibaya

    [20] Na Mwenyezi Mungu Anahukumu baina ya watu kwa uadilifu kwa kumpa kila mtu haki yake. Na wale waungu wanaoabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu, hawahukumu chochote kwa kutoweza kwao kufanya hivyo. Hakika Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye kuyasikia maneno ya waja Wake, Ndiye Mwenye kuyaona matendo wanayoyafanya, na Atawalipa kwayo

    [21] Kwani hawakutembea katika ardhi hawa wanaoukanusha utume wako, ewe Mtume, wakaangalia ulikuwa vipi mwisho wa ummah waliopita kabla yao? Walikuwa na nguvu zaidi kuliko wao na wenye athari zilizosalia muda mrefu zaidi, na hazikuwafaa wao nguvu zao nyingi wala miili yao mikubwa yenye nguvu, kwani Mwenyezi Mungu Aliwapatiliza kwa kuwatesa, kwa sababu ya ukafiri wao na kutenda kwao madhambi, na hawakuwa na mwokoaji wa kuwaokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu na kuizuia isiwafike

    [22] Adhabu hiyo iliyowafikia wakanushaji waliopita ilikuwa ni kwa sababu ya msimamo wao juu ya Mitume ya Mwenyezi Mungu waliokuja na dalili za yakini za kuonesha ukweli wa madai yao, basi wakawakanusha na wakawafanya warongo na Mwenyezi Mungu Akawapatiliza kwa mateso Yake, hakika Yeye ni Mwenye nguvu hashindwi na yoyote, ni Mkali wa kutesa kwa aliyemkanusha na kumuasi

    [23] Hakika tulimpelekea Mūsā alama zetu kubwa zenye kutolea ushahidi uhakika wa utume aliopewa na hoja zilizofunuka waziwazi juu ya ukweli wake katika ulinganizi wake, na kutanguka yale ambayo walikuwa nayo wale waliopelekewa hao Mitume

    [24] Apate kuenda kwa Fir'awn, mfalme wa Misri, na Hāmān waziri wake, na Qārūn mwenye mali mengi na mahazina ya vitu vya thamani, wakaukanusha utume wake na wakafanya kiburi na wakamwambia, «Yeye ni mchawi mrongo sana, basi ni vipi anadai kuwa yeye ametumilizwa kwa watu kuwa ni Mtume?»

    [25] Basi Mūsā alipomjia Fir'awn, Hāmān na Qārūn kwa miujiza iliyo waziwazi kutoka kwetu, hawakutosheka kwa kuipinga na kuikanusha , bali walisema, «waueni wana wa kiume wa wale walioamini pamoja naye na waacheni wanawake wao watumike na wafanywe watumwa. Na haikuwa mipango ya makafiri isipokuwa ni yenye kupita na kuangamia

    [26] Na Fir'awn alisema kuwaambia watukufu wa watu wake, «Niacheni nimuue Mūsā, na amuombe Mola wake, anayedai kuwa Yeye Amemtumiliza kwetu, Amhifadhi na sisi. Mimi ninachelea asije akaigeuza dini yenu mliyonayo au asije akaeneza uharibifu kwenye ardhi ya Misri.»

    [27] Na Mūsā akasema kumwambia Fir'awn na viongozi wa mamlaka yake, «Mimi nimeomba hifadhi kwa Mola wangu na Mola wenu, enyi watu, Anihami na kila mwenye kiburi cha kukataa kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtii, asiyeiamini Siku ambayo Mwenyezi Mungu Atawahesabu viumbe Wake.»

    [28] Na akasema mtu mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu miongoni mwa jamaa za Fir’awn anayeificha Imani yake akiwakemea watu wake, «Vipi nyinyi mtahalalisha kuuawa kwa mtu asiyekuwa na kosa kwenu isipokuwa anasema, ‘Mola wangu ni Mwenyezi Mungu’ na hali yeye amewajia na hoja za yakini kutoka kwa Mola wenu juu ya ukweli wa anayoyasema? Na iwapo Mūsā ni mrongo basi urongo wake utamdhuru mwenyewe, na iwapo ni mkweli basi baadhi ya yale anayowaonya kwayo yatawapata. Hakika Mwenyezi Mungu Hamuelekezi kwenye haki yoyote mwenye kupitisha mpaka kwa kuiacha haki na kuielekea batili, aliye mwingi wa urongo kwa kumnasibishia Mwenyezi Mungu ukiukaji wake

    [29] «Enyi watu wangu! Utawala ni wenu leo hali ya kuwa mna ushindi katika ardhi ya Misri juu raia wenu miongoni mwa Wana wa Isrāīl na wengineo. Ni nani atakayeizuia adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwa itatushukia?» Fir’awn akasema kuwajibu watu wake, «Siwapatii ushauri, enyi watu, wala mawazo isipokuwa ule ninaouona kuwa ni mzuri na wa sawa kwangu na kwenu. Na siwaiti isipokuwa kwenye njia ya haki na usawa.»

    [30] Na akasema yule Aliyeamini katika jamaa za Fir’awn kumwambia Fir’awn na viongozi wa mamlaka yake kwa kuwapa ushauri na kuwaonya, «Mimi ninawaogopea mkimuua Mūsā mfano wa siku ya makundi yaliyojikusanya dhidi ya manabii wao

    [31] «Mfano wa mwenendo wa watu wa Nūḥ, 'Ād, Thamūd na waliokuja baada yao katika ukafiri na ukanushaji, ambao Mwenyezi Mungu Aliwaangamiza kwa sababu ya hilo. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika, Hataki kuwafanyia maonevu waja, Akawa Atawaadhibu bila dhambi walilolitenda. Mwenyezi Mungu Yuko juu sana mno kwa kujiepusha na maonevu na upungufu

    [32] «Na enyi watu wangu! Mimi ninawachelea nyinyi adhabu ya Siku ya Kiyama. Siku ambyo wataitana watu wao kwa wao kwa kituko cha Kisimamo Siku hiyo

    [33] «Siku ambayo mtazunguka muende hali ya kukimbia, hamtakuwa na mwenye kuwahami wala kuwanusuru. Na yoyote yule ambaye Mwenyezi Mungu Atamuachilia Asimuafikie kuufikia uongofu Wake, basi yeye hatakuwa na mtu mwenye kumuongoza kwenye haki na usawa

    [34] «Na Mwenyezi Mungu Aliwatumilizia kwenu Nabii mtukufu, Yūsuf mwana wa Ya’qūb, amani ziwashukie, kabla ya Mtume Mūsā, Akampatia dalili zilizo wazi juu ya ukweli wake, na Akawaamuru nyinyi kumuabudu Mwenyezi Mungu Peke Yake Asiye na mshirika, mkaendelea kuwa na shaka juu ya yale aliyokuja nayo katika kipindi cha uhai wake mpaka alipokufa. Na alipokufa shaka yenu iliongezeka na pia ushirikina wenu na mkasema, ‘Mwenyezi Mungu Hatatuma mjumbe baada yake.’ Mfano wa upotevu huu ndivyo Mwenyezi Mungu Anavyompoteza kila anayeikiuka haki, mwenye shaka juu ya upweke wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Asimuafikie kwenye uongofu na unyofu

    [35] «Wale wanaobishana na aya za Mwenyezi Mungu na hoja Zake kwa kuzipinga bila kuwa na hoja zenye kukubalika, upinzani wao huo unawaletea machukivu makubwa kwa Mwenyezi Mungu na kwa wale walioamini, kama Alivyopiga muhuri kwenye nyoyo za hawa wapinzani na Akazifinika zisiongoke, ndivyo Anavyoupiga muhuri moyo wa kila mwenye kiburi cha kumfanya akatae kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtii, aliye mjeuri sana kwa wingi wa udhalimu wake na uadui wake.»

    [36] Na Fir’awn akasema akimkanusha Mūsā katika ule mwito wake wa kumkubali Mola wa viumbe wote na kujisalimisha Kwake, «Ewe Hāmān! Nijengee jengo kubwa. Huenda mimi nikafikia milango ya mbingu au nikakifikia kile chenye kunifikisha hapo

    [37] nipate kumtazama Mungu wa Mūsā mimi mwenyewe. Na mimi ninadhani kuwa Mūsā ni mrongo katika madai yake kwamba sisi tuna Mola na kwamba Yeye Yuko juu ya mbingu.» Hivyo ndivyo alivyopambiwa Fir'awn matendo yake mabaya akayadhania ni mazuri, na ndivyo alivyozuiliwa njia ya haki kwa sababu ya ubatilifu aliopambiwa nao. Na hazikuwa hila za Fir’awn na mipango yake ya kuwalaghai watu kuwa yeye yuko katika usawa na Mūsā yuko kwenye ubatilifu isipokuwa kwenye hasara na maangamivu, hakukuwa na kitu chenye kumfidisha isipokuwa ni kupata usumbufu wa duniani na Akhera

    [38] Na akasema yule aliyeamini, akirudia ushauri wake, «Enyi watu wangu! Nifuateni niwaongoze njia ya uongofu na usawa

    [39] «Enyi watu wangu! Hakika ya uhai huu wa kilimwengu ni uhai wa watu kustarehe kidogo, kisha unakatika na kuondoka, basi inatakikana msiutegemee na kwamba Nyumba ya Akhera na starehe za daima zilizomo ndani ndiyo mahali pa makazi ya nyinyi kutulia humo, basi inatakikana muipe kipaumbele na mtende kwa ajili yake matendo mema ambayo yatawapatia furaha huko

    [40] «Mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu katika uhai wake na akapotoka kwenye njia ya uongofu, hatalipwa huko Akhera isipokuwa mateso yanayolingana na maasia yake. Na mwenye kumtii Mwenyezi Mungu na akafanya matendo mema, kwa kufuata maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake, awe mwanamume au mwanamke, na hali yeye ni mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu na kumpwekesha, basi hao wataingia Peponi na humo Mwenyezi Mungu Atawaruzuku kutokana na matunda yake na starehe zake pasi na hesabu

    [41] «Na enyi watu wangu! Vipi mimi ninawalingania kumuamini Mwenyezi Mungu na kumfuata Mtume Wake Mūsā, nao ni ulinganizi utakaowafanya nyinyi muishie Peponi na muwe mbali na vituko vya Moto, na nyinyi mnanilingania kufany matendo yenye kupelekea kwenye adhabu ya Mwenyezi Mungu na mateso Yake Motoni

    [42] «Mnanilingania mimi nimkanushe Mwenyezi Mungu na nimshirikishe Yeye na kitu amabacho sina ujuzi nacho kuwa kinastahiki kuabudiwa badala Yake- na hili ni miongoni madhambi makubwa zaidi na maovu zaidi- Na mimi ninawalingania kwenye njia yenye kupelekea kwa Mwenyezi Mungu Aliye Mshindi katika kutesa Kwake, Mwingi wa msamaha kwa aliyerudia Kwake kwa kutubia baada ya kumuasi

    [43] «Ukweli ni kwamba kile mnachoniitia kukiamini hakistahiki kuitiwa wala kutegemewa kwa kupata himaya duniani wala Akhera kwa kuwa chenyewe kina udhaifu na upungufu. Na mjuwe kwamba mwisho wa viumbe vyote ni kwa Mwenyezi Mungu Aliyetakasika, na Yeye Atamlipa kila mtendaji kwa matendo yake, na wale waliokiuka mipaka Yake kwa kufanya vitendo vya uasi, kumwaga damu na kukanusha, wao ndio watu wa Motoni.»

    [44] Alipowasihi na wasimkubalie aliwaambia, «Basi mtakumbuka kuwa mimi niliwasihi na nikawakumbusha, na mtajuta wakati ambao majuto hayatanufaisha. Na mimi ninahamia kwa Mola wangu nataka hifadhi Yake na ninamtegemea Yeye, hakika Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, ni Mtambuzi wa hali za waja na malipo wanayostahiki malipo, hakuna kinachofichamana Kwake chochote katika hayo.»

    [45] Basi Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika, Akamuokoa mtu huyo aliyeamini na mateso ya vitimbi vya Fir’awn na jamaa zake, na ikawashukia wao adhabu mbaya, kwa kuwa Mwenyezi Mungu Aliwazamisha wote mpaka wa mwisho wao

    [46] Kwanza walipatikana na gharika wakaangamia, kisha wakawa wanaadhibiwa ndani ya makaburi yao ambapo Moto unaorodheshwa kwao, asubuhi na jioni, mpaka wakati wa kuhesabiwa. Na Siku ambayo Kiyama kitasimama kutasemwa, «Watieni Motoni jamaa wa Fir’awn ukiwa ni malipo ya matendo mabaya waliyoyatenda.» Aya hii ndio msingi wa kuthibitisha adhabu ya kaburini

    [47] Na pindi watakapogombana watu wa Motoni na kulaumiana wao kwa wao, hapo wajenge hoja wafuasi wenye kuandama dhidi ya viongozi wao wenye kiburi ambao waliwapoteza na wakawapambia njia ya uovu, kwa kuwaambia, «Je, nyinyi mtatuondolea sehemu ya Moto kwa kujibebesha fungu la adhabu yetu?»

    [48] Viongozi waliokuwa na kiburi watasema, wakieleza ulemevu wao, «Hatutawabebea kitu chochote cha adhabu ya Moto, na hali sisi sote tumo ndani yake, hatuna namna ya kuokoka nao, Mwenyezi Mungu Amegawanya adhabu baina yetu kwa uamuzi Wake wa haki, kila mmoja wetu kwa kadiri anayostahiki.»

    [49] Na watasema wale waliyomo Motoni miongoni mwa watu wakubwa wenye kiburi na wanyonge wakiwaambia walinzi wa Jahanamu, «Muombeni Mola wenu atusahilishie adhabu kwa siku moja ili tupate kiasi fulani cha mapumziko.»

    [50] Washika hazina wa Jahanamu waseme kuwaambia kwa njia ya kuwakaripia na kuwalaumu, «Maombi haya hayatafalia kitu. Kwani hawakuwajia nyinyi Mitume wenu na hoja waziwazi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na mkawakanusha?» Hapo wale wakanushaji walikubali hilo na wasema, «Ndio, wametujia.» Na washika hazina wa Jahanamu wajiepushe na wao na waseme, «Sisi hatutawaombea wala kuingilia kati kuhusu nyinyi. Ombeni nyinyi wenyewe, lakini dua hiyo haitafalia kitu, kwa kuwa nyinyi ni makafiri, na hayawi maombi ya makafiri isipokuwa ni yenye kupotea, hayakubaliwi wala hayaitikiwi.»

    [51] Sisi tutawapa ushindi mitume wetu na wale waliowafuata, na tutawapa nguvu juu ya wale waliowaudhi katika uhai wa kilimwengu na Siku ya Kiyama, Siku ambayo watatoa ushahdi Malaika, Manabii na Waumini juu ya watu waliopita waliowakanusha Mitume wao; watatoa ushahidi kwamba Mitume walifikisha jumbe za Mola wao na kwamba watu hao waliwakanusha

    [52] Siku ya kuhesabiwa, hawatanufaika makafiri waliokiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu kwa zile nyudhuru wanazozitoa za kuwakanusha Mitume wa Mwenyezi Mungu. Watakalolipata ni kufukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu, na watakuwa na Nyumba mbaya huko Akhera, nayo ni Moto

    [53] Kwa hakika tulimpa Mūsā Taurati na miujiza miongoni mwa vitu vinavyoongoza kwenye haki, na tukawafanya Wana wa Isrāīl warithiane Taurati: wanyuma kutoka kwa waliopita

    [54] hali ya kuwa ni yenye kuongoza kwenye njia ya usawa na ni waadhi kwa wenye akili kamilifu

    [55] Basi subiri, ewe Mtume, juu ya udhia wa washirikina, kwani tumekuahidi kulitukuza neno lako, na ahadi yetu ni kweli haiendi kinyume, na utake msamaha wa dhambi zako, na uendelee daima kumtakasa Mola wako na kila sifa isiyonasibiana na Yeye katika kipindi cha mwisho wa mchana na mwanzo wake

    [56] Hakika ya wale wanaoipinga haki kwa ubatilifu, na wanaozirudisha hoja sahihi kwa udanganyifu wa uharibifu bila ya kuwa na dalili wala ushahidi wala hoja kutoka kwa Mwenyezi Mungu, basi hamna ndani ya nyoyo za hao isipokuwa kuifanyia kiburi haki, kwa uhasidi wao juu ya fadhila ambazo Mwenyezi Mungu Amempa mtume Wake na utukufu wa utume ambao Amemkirimu nao, nayo ni mambo wao si wenye kuyafikia wala kuyapata. Basi shikamana na Mwenyezi Mungu akuhifadhi na shari lao, kwani Yeye ni Mwenye kuyasikia maneno yao , ni Mwenye kuyaona matendo yao, na Atawalipa kwayo

    [57] Hakika ni kwamba uumbaji wa Mwenyezi Mungu wa mbingu na ardhi ni mkubwa zaidi kuliko kuwaumba watu na kuwarudisha uhai baada ya kufa, lakini wengi wa watu hawajui kwamba uumbaji wa vyote hivyo ni jambo sahali kwa Mwenyezi Mungu

    [58] Na halingani kipofu na anayeona, pia hawalingani Waumini wanaokubali kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Mungu wa haki Asiye na mshirika, wanaowaitikia Mitume Wake na wanaozifuata kivitendo Sheria Zake (hawalingani) na wenye kukataa ambao wanapinga kuwa Mwenyezi Mungu ni Mungu wa haki, na wakawakanusha Mitume Wake na wasizifuate Sheria Zake kivitendo. Ni uchache sana kwa nyinyi, enyi watu, kuzikumbuka hoja za Mwenyezi Mungu, mkazingatia na mkawaidhika nazo

    [59] Hakika Kiyama ni chenye kuja, hakina shaka. Basi kuweni na yakini ya kuja kwake, kama walivyolitolea habari hilo Mitume. Lakini wengi wa watu hawaamini kuwa kitakuja wala hawafanyi vitendo vya kuwafaa hapo

    [60] Na Anasema Mola wenu, «Enyi waja! Niombeni Peke Yangu na niabuduni mimi tu, nitawakubalia maombi yenu. Hakika ya wale wenye kufanya kiburi kwa kukataa kunipwekesha katika ibada na ustahiki wa kuabudiwa wataingia Moto wa Jahanamu wakiwa watwevu na wanyonge

    [61] Mwenyezi Mungu peke Yake Ndiye Aliyewawekea usiku ili mtulie ndani yake na mpate mapumziko yenu, na Ameufanya mchana kuwa na mwangaza ili muendeshe mambo ya maisha yenu. Hakika Mwenyezi Mungu Ana wema mwingi kwa watu. lakini wengi wao hawamshukuru kwa kumtii na kumtakasia ibada

    [62] Yule Aliyewaneemesha neema hizi si mwingine bali ni Mwenyezi Mungu Mola wenu, Muumba vitu vyote. Hapana Mola Anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Yeye. Basi ni vipi nyinyi mnajiepusha na kumuamini Yeye na mnamuabudu asiyekuwa Yeye miongoni mwa masanamu, baada ya kuwafunukia dalili Zake

    [63] Kama mlivyoikanusha haki, enyi makafiri wa Kikureshi, na mkaipa mgongo na mkaenda kwenye ubatilifu, hivyo ndivyo wanavyopotoshwa na haki na kuiamini wale waliokuwa wakizikanusha hoja za Mwenyezi Mungu na dalili Zake

    [64] Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyewafanyia hii ardhi ili mtulie hapo, Akawasahilishia kukaa juu yake, Akawafanyia mbingu kuwa ni sakafu ya ardhi, Akaeneza huko alama zenye kuongoza, Akawaumba kwa namna kamilifu zaidi na maumbile mazuri zaidi, Akawaneemesha kwa riziki ya halali na vilaji na vinywaji vyenye ladha. Huyo Aliyewaneemesha nyinyi neema hizi ndiye Mola wenu, Mwingi wa kheri, fadhila na baraka, na Ameepukana na kila kisichonasibiana na Yeye. Na Yeye Ndiye Mola wa viumbe wote

    [65] Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika, Aliye hai Ambaye Ana uhai mkamilifu uliotimia, Hapana Mola isipokuwa Yeye. Basi muombeni na ielekezeni ibada Kwake Yeye, Peke Yake, hali ya kumtakasia Yeye Dini yenu na utiifu wenu. Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu na sifa kamilifu ni Zake, Mola wa viumbe wote

    [66] Sema, ewe Mtume, uwaambie washirikina wa watu wako, «Hakika mimi nimekatazwa kuwaabudu wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu baada ya kunijia mimi alama zilizo wazi kutoka kwa Mola wangu na kuniamrisha mimi nimnyenyekee Yeye na nimfuate kwa utiifu mkamilifu Kwake, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Mola wa viumbe wote,»

    [67] Yeye Ndiye Aliyemuumba baba yenu Ādam kwa mchanga, kisha Akawafanya mpatikane kutokana na manii kwa uweza Wake, na baada yake mnahamia kwenye mwongo wa damu nzito iliyo nyekundu, kisha mnapitiwa na miongo kadha ndani ya vizazi, mpaka mnapozaliwa mkiwa watoto wadogo, kisha umbile lenu linapata nguvu (na mnaendelea hivyo) mpaka mnapokuwa wazee, na miongoni mwenu kuna wanaokufa kabla ya hapo. Na ili mfikie kwa miongo hii kipindi kiliotajwa ambacho hapo umri wenu ukome. Huenda nyinyi mkazitia akilini hoja za Mwenyezi Mungu katika hilo na mkazizingatia aya zake mkajua kuwa hakuna Mola isipokuwa Yeye Anayefanya hilo, na kwamba Yeye Ndiye Ambaye haitakiwi kuabudiwa isipokuwa Yeye

    [68] Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Aliyepwekeka kwa kuhuisha na kufisha. Na Akiamua jambo Analiambia, «Kuwa!» na likawa, hakuna mwenye kurudisha uamuzi Wake

    [69] Je, huwaonei ajabu, ewe Mtume, hawa wakanushaji wa aya za Mwenyezi Mungu vile wanavyoshindana nazo, na hali hizo ziko wazi katika kutolea ushahidi upweke wa Mwenyezi Mungu na uweza Wake, ni vipi wao wanaziepuka pamoja na usahihi wake? Na wataenda kwenye kitu gani baada ya huu ufafanuzi kamili

    [70] Washirikina hawa waliokanusha Qur’ani na Vitabu vya mbinguni Alivyoviteremsha Mwenyezi Mungu kwa Mitume Wake ili kuongoza watu, watajua wakanushaji hawa mwisho wa ukanushaji wao

    [71] Pindi watakapotiwa pingu kwenye shingo zao na minyonyoro kwenye miguu yao, na huku Malaika wa adhabu wakiwaburuta

    [72] Wakiwatia kwenye maji moto yaliyochemka sana na yenye uharara mwingi, kisha wachomwe ndani ya Moto wa Jahanamu

    [73] Kisha waambiwe kwa kuwasimanga, na wao wako kwenye hali hii ya unguliko , «Wako wapi waungu mliokuwa mkiwaabudu

    [74] badala ya Mwenyezi Mungu? Je watawatetea nyinyi leo? Basi waiteni ili wawaokoe na balaa hii iliyowashukia iwapo wataweza.» Hapo wakanushaji waseme, «Wametupotea machoni hatuwaoni, na hawakutunufaisha kitu chochote.» Hapo wakubali kuwa wao walikuwa ujingani katika mambo yao, na kuwa kule kuabudu kwao wale waungu kulikuwa ni ubatilifu usio na faida yoyote. Na kama vile Mwenyezi Mungu Alivyowapoteza hawa waliowapotea katika moto wa Jahanamu waliokuwa wakiwaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, ndivyo Mwenyezi Mungu Anavyowapoteza wale wenye kumkanusha

    [75] Adhabu hiyo itakayowapata ni kwa sababu ya kughafilika mliokuwa nako katika uhai wenu wa kilimwengu, kwa kuwa mlikuwa mkifurahika na yale mnayoyatenda ya maasia na madhambi na tabia mliokuwa nazo za gogi, kiburi na kuwafanyia udhalimu waja wa Mwenyezi Mungu

    [76] Ingieni kwenye milango ya Jahanamu ikiwa ni mateso yenu kwa kumkanusha kwenu Mwenyezi Mungu na kumuasi, hali ya kukaa milele humo. Ni mbaya sana Jahanamu kuwa ni mashukio ya wenye kumfanyia kuburi Mwenyezi Mungu duniani

    [77] Basi vumilia, ewe Mtume, na uendelee katika njia ya ulinganizi, hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli na Atakutekelezea kile Alichokuahidi. Basi, ima tukuoneshe katika uhai wako sehemu ya adhabu tunayowaahidi hawa washirikina au tukufishe kabla ya hiyo adhabu kuwashukia, kwani ni kwetu sisi mwisho wao Siku ya Kiyama, na tutawaonjesha adhabu kali kwa yale waliokuwa wakiyakanusha

    [78] Hakika tuliwatumiliza kabla yako, ewe Mtume, Mitume wengi kwa watu wao wawalinganie na wavumilie udhia wao. Miongoni mwao kuna wale tuliokuhadithia habari zao, na miongoni mwao kuna wale ambao hatukukuhadithia. Na wote hao wameaminiwa kufikisha wahyi wa Mwenyezi Mungu kwa watu wao. Na haikuwa ni yenye kuwezekana kwa yoyote miongoni mwao kuleta alama yoyote miongoni mwa alama zinazoonekana au zinazofahamika isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na matakwa Yake. Basi itakapokuja amri ya Mwenyezi Mungu ya kuadhibiwa wakanushaji, itatolewa hukumu ya uadilifu baina ya Mitume na wale waliowakanusha, na hapo watapata hasara waliokuwa wabatilifu kwa kule kumzulia kwao Mwenyezi Mungu urongo na kuabudu kwao asiyekuwa Yeye

    [79] Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika, Ndiye Aliyewapa nyinyi wanyama , ili mnufaike nao kwa kupanda na kula

    [80] na manufaa mengineyo, na ili mfikie, kwa kuwabebesha wengineo, haja ya nafsi zenu ya kufika miji ya mbali. Na juu ya wanyama hao mnabebwa barani, na juu ya majahazi mkiwa baharini mnabebwa pia

    [81] Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anawaonyesha dalili zake nyinygi zilizo wazi zenye kutolea ushahidi uweza Wake na uendeshaji mambo Wake. Basi ni dalili gani miongoni mwa dalili za Mwenyezi Mungu mnazikanusha na hamzikubali

    [82] Kwani hawakutembea kwenye ardhi wakanushaji hawa wakafikiria juu ya maangamivu ya ummah waliokanusha waliokuwa kabla yao ulikuwa vipi mwisho wao? Ummah hao waliopita walikuwa ni wengi kuliko wao kwa idadi, zana na athari ya majengo, viwanda, ukulima na yasiyokuwa hayo. Na yote hayo waliyoyatenda hayakuwafalia kitu ilipowateremkia wao adhabu ya Mwenyezi Mungu

    [83] Walipowajia, hao ummah waliowakanusha, Mitume wao kwa dalili zilizo wazi, walifurahia, kwa ujinga wao, ujuzi walionao unaogongana na yale waliyokuja nayo Mitume, na ikawashukia wao ile adhabu waliokuwa wakiiharakisha kwa njia ya shere na dhihaka. Katika aya hii kuna dalili kuwa kila ujuzi unaogongana na Uislamu au kuutia kombo au kutilia shaka usahihi wake, basi ujuzi huo ni mwenye kutukanika na kuchukiza, na mwenye kuuamini si miongoni mwa wafuasi wa Muhammad, reheme ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [84] Walipoiona adhabu yetu, walikubali wakati ambapo kukubali hakunufaishi, na wakasema, «Tumemuamini Mwenyezi Mungu, Peke Yake, na tumekikanusha kile ambacho tulikuwa tukikishirikisha katika ibada ya Mwenyezi Mungu.»

    [85] Imani yao hiyo haikuwa ni yenye kuwanufaisha walipoiona adhabu yetu, kwa kuwa ni imani ambayo hawakuwa na budi nayo, na si Imani ya hiyari na kutaka. Huo ndio mpango na njia Aliyoiweka kwa ummah wote, kwamba Imani isiwanufaishe wanapoiona adhabu. Na itakapokuja adhabu ya Mwenyezi Mungu, wataangamia wenye kumkanusha Mola wao, wenye kukataa kumpwekesha na kumtii

    Zimefafanuliwa

    Surah 41

    [1] «Hā, Mīm» Yameshatangulia maelezo kuhusu herufi zilizokatwa na kutengwa mwanzo wa sura ya Al-Baqarah

    [2] Hii Qur’ani ni Teremsho linalotoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye kueneza rehema Zake kwa wema na waovu ulimwenguni, Mwenye kuhusisha rehema Zake kwa wema watupu kesho Akhera. Amemteremshia Nabii Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [3] Ni Kitabu kilichobainishwa aya zake ubainifu uliotimia, na yakafafanuliwa maana yake na hukumu zake, ikiwa ni Qur’ani ya Kiarabu iliyofanywa nyepesi kuielewa kwa watu wanaoijua lugha ya Kiarabu

    [4] Hali ya kuwa ni yenye kubashiri malipo ya haraka na ya baadaye kwa anayeiamini na akafanya matendo yanayolingana nayo, na ni yenye kuonya adhabu ya haraka na ya badaye kwa anayeikanusha. Hivyo basi wengi wa watu waliipa mgongo wakawa hawaisikii kusikia kwa kukubali na kuitikia

    [5] Na wanasema hawa wenye kukataa na kumkanusha Nabii Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, «Nyoyo zetu zina vifiniko venye kutuzuilia tusielewe unayotuambia, na masikizi yetu yana uziwi hatusikii, na baina yetu sisi na wewe, ewe Muhammad, pana pazia inayotuzuia kuitika mwito wako. Basi fanya kulingana na dini yako , kama ambavyo sisi tunavyofanya kulingana na dini yetu.»

    [6] Waambie, ewe Mtume, «Hakika yangu mimi ni binadamu kama nyinyi, Mwenyezi Mungu Ananiletea wahyi kwamba Mola wenu Anayestahiki kuabudiwa ni Mola Mmoja Asiyekuwa na mshirika. Basi fuateni njia yenye kufikisha Kwake na mtake msamaha Wake.» Maangamivu na mateso yatawapata washirikina walioabudu masanamu, yasiyonufaisha wala kudhuru, badala ya kumuabudu Mwenyezi Mungu

    [7] Wale wasiojisafisha nafsi zao kwa kumpwekesha Mola wao na kumtakasa, na wasiotoa Zaka kuwapa wanaostahiki, basi hao hawamtakasii Muumba wala hawanufaishi viumbe; na wao hawaamini Ufufuzi wala Pepo na Moto

    [8] Hakika ya wale wanaomuamini Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na Kitabu Chake na wakafanya matendo mema, hali ya kumtakasia Mwenyezi Mungu katika matendo hayo, watapata malipo makubwa yasiyokatika wala kuzuiliwa

    [9] Sema, ewe Mtume, uwaambie washirikina kwa kuwakaripia na kulionea ajabu tendo lao, «Je nyinyi mnamkanusha Mwenyezi Mungu Aliyeumba ardhi kwa siku mbili, mnanmfanya kuwa Ana washirika na wanaofanana Naye mkawa mnawaabudu pamoja Naye? Muumbaji Huyo Ndiye Mola wa viumbe wote

    [10] «Na Akajaalia Mwenye kutakasika katika ardhi majabali yaliyojikita juu yake, Akaibarikia kwa kuifanya iwe na kheri nyingi kwa watu wake, Akakadiria humo riziki za chakula kwa watu wake na yale yanayowafaa maishani kwa kipindi cha Siku nne: Siku mbili Aliumba ndani yake ardhi na Siku mbili Aliweka katika ardhi majabali yaliyojikita na Akakadiria katika Siku mbili hizo riziki zake zikiwa sawa kwa wenye kuuliza, yaani kwa mwenye kutaka kuliuliza hilo apate kulijua

    [11] Kisha Akalingana, kutakasika na kutukuka ni Kwake, yaani Akaikusudia mbingu, na ilikuwa moshi hapo kabla, Akasema kuiambia mbingu na ardhi, «Fuateni amri yangu kwa hiari au kwa nguvu!» Nazo zikasema, «Tumekuja tukiwa watiifu kwako. Hatuna matakwa kinyume cha matakwa yako.»

    [12] Mwenyezi Mungu Akapitisha kuziumba mbingu saba na kuzisawazisha kwa Siku mbili. Na kwa hilo ukatimia uumbaji wa mbingu na ardhi kwa Siku sita kwa hekima Anayoijua Mwenyezi Mungu, pamoja na uweza Wake, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, wa kuziumba kwa mara moja. Na Akapeleka wahyi katika kila uwingu kwa Analolitaka na kuliamuru. Na tumeupamba uwingu wa karibu kwa nyota zinazong’ara na kwa ajili ya kuuhifadhi na Mashetani wanaosikiliza kwa kuiba. Uumbaji huo mzuri ni makadirio ya Aliye Mshindi katika ufalme Wake, Aliye Mjuzi Ambaye ujuzi Wake umekizunguka kila kitu

    [13] Basi wakipuuza wakanushaji hawa baada ya kubainishiwa sifa za Qur’ani zinazotajika vyema, na sifa za Mungu Mkubwa, waambie, «Kwa kweli, ninawaonya nyinyi adhabu yenye kuwamaliza mfano wa adhabu (iliyowashukia watu wa kabila la) 'Ād na Thmud walipomkanusha Mola wao na kuwaasi Mitume wao.»

    [14] Walipowajia Mitume hao kina 'Ād na Thamūd, hawa baada ya wengine wakifuatana, wakiwaamrisha kumuabudu Mwenyezi Mungu Peke Yake Asiyekuwa na mshirika, waliwaambia Mitume wao, «Lau Mwenyezi Mungu Angalitaka tumpwekeshe na tusiabudu chochote kisichokuwa Yeye, Angaliteremsha Malaika kutoka mbinguni wakiwa wajumbe wa hilo unalotuitia kwalo, na Hangaliwatuma nyinyi na hali nyinyui ni binadamu kama sisi, basi sisi kwa lile ambalo Mwenyezi Mungu Amewatuma kwetu la kumuamini Mwenyezi Mungu Peke Yake ni wenye kulikanusha.»

    [15] Ama hao 'Ād, watu wa Hūd, waliwafanyia waja ujeuri bila haki na wakasema kwa kujiona, «Ni nani mwenye nguvu kali zaidi kushinda sisi?» Kwani hawaoni kuwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Aliyewaumba ni Mkali zaidi wa nguvu na kipigo? Na walikuwa ni wenye kuzikanusha hoja zeyu na dalili zetu

    [16] Tukawatumia wao upepo wenye ubaridi mkali, wenye sauti kubwa, katika siku zilizokuwa korofi, ili tuwaonjeshe adhabu ya unyonge na utwevu katika maisha ya kilimwengu. Na adhabu ya Akhera ina unyonge na utwevu mwingi zaidi, na wao hawatasaidiwa kwa kuzuia adhabu isiwapate

    [17] Na ama hao Thamūd, watu wa Ṣāliḥ, kwa hakika tuliwabainishia njia ya uongofu na usawa, wakafadhilisha upofu juu ya uongofu, kikawaangamiza wao kimondo cha adhabu yenye kutweza kwa sababu ya dhambi waliokuwa wakizitenda kwa kumkufuru kwao Mwenyezi Mungu na kuwakanusha Mitume Wake

    [18] Na tukawaokoa wale walioamini kutokana na adhabu iliyowapata kina 'Ād na Thamūd. Na hawa waliookoka walikuwa wanamuogopa Mwenyezi Mungu na kumcha

    [19] Na Siku ambayo maadui wa Mwenyezi Mungu watakusanywa wapelekwe kwenye Moto wa Jahanamu, Malaika wa adhabu watawarudisha wa mwanzo wao wawakusanye na wa mwisho wao

    [20] hata watakapoufikia Moto na wakakanusha makosa yao, yatatoa ushahidi dhidi yao masikio yao, macho yao na ngozi zao kwa yale ambayo walikuwa wakiyafanya duniani ya madhambi na makosa

    [21] Na watasema hao watakaokusanywa kupelekwa Motoni miongoni mwa maadui wa Mwenyezi Mungu kuziambia ngozi zao wakizilaumu, «Kwa nini mmetoa ushahidi dhidi yetu?» Na hapo ngozi zao ziwajibu, «Ametutamsha Mwenyezi Mungu Ambaye Amekitamsha kila kitu, na Yeye Ndiye Aliyewaumba nyinyi mara ya kwanza na hamkuwa ni chochote, na kwake Yeye Ndio mwisho wenu baada ya kufa ili mhesabiwe na mlipwe.»

    [22] Na hamkuwa mkijificha mlipokuwa mkitenda maasia kwa kuogopa yasije masikio yenu wala macho yenu wala ngozi zenu yakatoa ushahidi dhidi yenu Siku ya Kiyama, lakini mlidhani , kwa kufanya maasia kwenu, kuwa Mwenyezi Mungu hajui mengi kuhusu matendo yenu ambayo kwayo mnamuasi Mwenyezi Mungu

    [23] Hiyo ndiyo dhana yenu mbovu ambayo mliidhania kwa Mola wenu; imewaangamiza na kuwatia Motoni, ndipo mkawa Leo ni miongoni mwa wale waliopata hasara nafsi zao na ya watu wao

    [24] Wakivumilia adhabu, basi Moto ndio makazi yao, na wakiomba kurejea duniani waanze kufanya amali njema huko, hawatajibiwa ombi hilo wala hazitakubaliwa nyudhuru zao

    [25] Na tuliwawekea hawa madhalimu wenye kukanusha marafiki wabaya miongoni mwa Mashetani wa kibinadamu na wa kijini, wakawapambia matendo yao machafu duniani, wakawaita kwenye ladha zake na matamanio yake ya haramu, na wakawapambia wao yaliyo nyuma yao katika mambo ya Akhera wakawasahaulisha wasiikumbuke, na wakawalingania wakatae Marejeo (ya Kiyama). Na kwa hjvyo walistahili kuingia Motoni wawe miongoni mwa wale makafiri wa ummah waliopita wa kijini na wa kibinadamu. Wao walikuwa wamepata hasara ya matendo yao duniani na hasara ya nafsi zao na watu wao Siku ya Kiyama

    [26] Na makafiri walisema wakiambiana wao kwa wao wakiusiana baina yao, «Msiisikilize hii Qur’ani wala msiiandame wala msizifuate amri zake. Na ziinueni juu sauti zenu kwa kelele, kupiga mbinja na kumfanya Muhammad achanganyikiwe anaposoma Qur’ani, huenda mkamshinda akaacha kusoma na kwa hivyo tukapata ushindi juu yake.»

    [27] Basi Tutawaonjesha, tena tutawaonjesha, wale waliosema neno hili adhabu kali, duniani na Akhera, na tutawalipa, tena tutawalipa, mabaya zaidi ya makosa waliokuwa wakiyafanya

    [28] Malipo haya ambayo watalipwa waliokufuru ni malipo ya maadui wa Mwenyezi Mungu, nayo ni Moto utakaokuwa ni nyumba yao ya kukaa daima milele, ukiwa ni malipo ya wale waliokuwa wakizikanusha hoja zetu na dalili zetu. Na aya hii inatolea ushahidi ukubwa wa kosa la mwenye kuwapotosha watu na Qur’ani tukufu na kuwazuia wasiizingatie wala wasijiongoze nayo kwa njia yoyote iwayo

    [29] Na watasema wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wao wako Motoni, «Mola wetu! Tuonyeshe mapote mawili yaliyotupoteza miongoni mwa majini na binadamu ili tuyaweke chini ya nyayo zetu yapate kuwa sehemu ya chini kabisa ya Moto.»

    [30] Hakika ya wale waliosema, «Mola wetu ni Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Peke Yake kisha wakasimama imara kufuata Sheria Yake, Malaika watawateremkia wakati wa kufa waseme kuwaambia, «Msiogopeni kufa na yatakayokuwa baada yake, wala msiwe na masikitiko juu ya yale mtakayoyaacha nyuma yenu katika mambo ya kilimwengu, na furahikeni kwa Pepo ambyo mlikuwa mkiahidiwa.»

    [31] Na Malaika watasema kuwaambia wao, «Sisi ndio wasaidizi wenu katika uhai wa ulimwenguni, tunawaelekeza sawa na tunawatunza kwa amri ya Mwenyezi Mungu, na pia tutakuwa na nyinyi huko Akhera. Na mtapata huko Peponi kila kile ambacho nafsi zenu zinakitamani katika vitu mnavyovichagua na ambavyo macho yenu yanatulia kwa kuvipata. Na chochote kile mtakachokitaka kitakuwa mbele yenu

    [32] mkiandaliwa na kuneemeshwa kutoka kwa Mwingi wa kusamehe dhambi zenu, Mwingi wa huruma kwenu.»

    [33] Hakuna yoyote aliye na kauli nzuri zaidi kuliko yule anayelingania kupwekeshwa Mwenyezi Mungu na kuuabudiwa Yeye Peke Yake, na anayesema, «Mimi ni katika Waislamu wanaofuata amri Ya Mwenyezi Mungu na Sheria Yake.» Katika aya hii kuna kusisitiza kulingania kwa Mwenyezi Mungu Aliyetakasika na kueleza utukufu wa wanavyuoni wenye kulingania Kwake kwa ujuzi, kulingana na yale yaliyokuja kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani zimshukie

    [34] Na halilingani jema la waliomuamini Mwenyezi Mungu, wakasimama imara kwenye Sheria Yake, wakawafanyia wema viumbe Vyake (hilo halilingani) na baya la waliomkanusha Yeye, wakaenda kinyume na amri Yake na wakawafanyia ubaya viumbe Vyake. Msukume, ewe Mtume, kwa msamaha wako, upole wako na hisani yako yule anayekufanyia ubaya, na upambane na ubaya wake kwako kwa kumfanyia wema. Hivyo basi yule aliyekutendea ubaya ambaye baina yako wewe na yeye kuna uadui atakuwa kama kwamba yeye ni mtu aliye jamaa yako wa karibu na mwenye huruma na wewe

    [35] Na hawaafikiwi kwenye mambo haya yanayosifika vyema isipokuwa wale wanaojisubirisha juu ya mambo ambayo nafsi zao zinayachukia na wakajilazimisha kwa yale Anayoyapenda Mwenyezi Mungu. Na haafikiwi hayo isipokuwa mwenye fungu kubwa la hali njema ya duniani na Akhera

    [36] Na Shetani anapotia ndani ya nafsi yako ushawishi wa mawazo ya kukufanya umlipe mbaya kwa ubaya, basi omba himaya ya Mwenyezi Mungu na ushikamane na Yeye. Kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia sana maombi yako ya kujilinda Kwake, ni Mwenye kuyajua sana mambo ya viumbe Vyake vyote

    [37] Na miongoni mwa hoja za Mwenyezi Mungu kwa viumbe Vyake, dalili za upweke Wake na ukamilifu wa uweza Wake, ni kutafautiana mchana na usiku na kufuatana (kila mojawapo kuufuata mwingine) na kutafautiana jua na mwezi na kufuatana, vyote hivyo viko chini ya uendeshaji Wake na utendeshaji nguvu Wake. Msilisujudie jua wala mwezi, kwani hivyo viwili vinaendeshwa na vimeumbwa; na msujudieni Mwenyezi Mungu Aliyeviumba, iwapo nyinyi kwa kweli mnafuata amri Yake, mnasikia na mnamtii Yeye, basi muabuduni Yeye Peke Yake Asiye na mshirika

    [38] Na wakifanya kiburi wshirikina hawa kwa kukataa kumsujudia Mwenyezi Mungu, basi Malaika waliyoko kwa Mola wako hawafanyi kiburi cha kukataa hilo, bali wanamsujudia Yeye na wanamtakasa na kila upungufu, usiku na mchana, na wao hawapumziki na hilo wala hawachoki

    [39] Na miongoni mwa alama za upweke wa Mwenyezi Mungu na uweza Wake ni kuwa wewe unaiona ardhi ikiwa kavu haina mimea, na tunapoiteremshia mvua, uhai unatambaa ndani yake na inasukikasukika kwa mimea, na ikafura na kunyanyuka. Hakika Yule Anayeihuisha ardhi hii baada ya ukavu wake ni Muweza wa kuwahuisha viumbe baada ya kufa kwao. Hakika Yeye juu ya kila jambo ni Muweza. Na kama usivyoelemewa uweza Wake kuhuisha ardhi baada ya kufa kwake, hivyo hivyo uweza Wake hauelemewi kuwahuisha waliokufa

    [40] Hakika ya wale wanaopotoka na haki wakaikanusha Qur’ani na wakaipotoa, hawafichamani kwetu sisi, bali sisi tunawaona wao. Je, huyu mwenye kuzipotosha aya za Mwenyezi Mungu atakayetiwa Motoni ni bora au ni yule atakayekuja Siku ya Kiyama hali ya kuwa amesalimika na adhabu ya Mwenyezi Mungu na kustahiki malipo mema Yake kwa kumuamini na kuzisadiki aya Zake? Fanyeni, enyi wapotofu, mnalolitaka, kwani Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anayaona matendo yenu, hakuna kinachofichika Kwake, na Atawalipa kwa hayo. Hapa pana onyo na hadharisho kwao

    [41] Hakika ya wale walioikataa hii Qur’ani na wakaikanusha ilipowajia ni wenye kuangamia na kuadhibiwa. Na hii Qur’ani ni Kitabu kitukufu kwa kuwa Mwenyezi Mungu Amekitukuza na kukitunza na kila ugeuzaji au ubadilishaji

    [42] Ubatilifu haukifikii kutoka upande wowote katika pande Zake, na hakuna kitu chenye kukibatilisha, kwani hiko kimetunzwa kisipunguzwe wala kisizidishwe. Ni teremsho kutoka kwa Mwingi wa hekima katika kuendesha mambo ya waja Wake, Mwenye kushukuriwa kwa sifa za ukamilifu Alizonazo

    [43] Hawakwambii hao washirikina, ewe Mtume, isipokuwa kile ambacho washakisema kabla yao ummah waliopita kuwaambia Mitume wao. Basi vumilia juu ya kinachokupata katika njia ya ulinganizi kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mola wako ni Mwenye msamaha mwingi wa dhambi za wenye kutubia, ni mwenye mateso kwa mwenye kuendelea kumkufuru na kumkanusha

    [44] Na lau tungaliifanya hii Qur’ani tuliyokuteremshia, ewe Mtume, ni kwa lugha isiyokuwa ya Kiarabu, washirikina wangalisema, «Je, si zifafanuliwe aya zake tupate kuzifahamu na kuzijua? Ni vipi hii Qur’ani ni kwa lugha isiyokuwa ya Kiarabu na hali lugha ya huyu aliyeteremshiwa ni ya Kiarabu? Hili haliwi!» Waambie, ewe Mtume, «Hii Qur’ani, kwa wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, ni uongofu kutoka kwenye upotevu na ni ponyesho la yaliyomo vifuani ya shaka na magonjwa. Na wale wasioiamini Qur’ani kuna uziwi ndani ya mashikio yao unaowafanya wasiisikie na wasiizingatie; nayo (hiyo Qur’ani) ni upofu kwao wa nyoyo zao, hawaongoki kwayo.» Basi washirikina hao ni kama yule anayeitwa naye yuko mahali mbali, hamsikii mwenye kulingania wala hamuitiki mwenye kuita

    [45] Hakika tulimpelekea Mūsā Taurati kama tulivyokuletea wewe, ewe Mtume, Qur’ani, wakatafautiana watu wake kuhusu hiyo: katika wao kuna aliyeamini na katika wao kuna aliyekanusha. Na lau si neno (la ahadi) lililotangulia kutoka kwa Mola wako la kuwacheleweshea watu wako adhabu, uamuzi baina yao ungalitolewa wa kuwaangamiza makafiri papo hapo. Na kwa hakika washirikina wana shaka nayo sana Qur’ani

    [46] Mwenye kufanya mema, akamtii mwenyezi Mungu na Mtume Wake, atajipatia mwenyewe thawabu za matendo yake. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, atajionea mwenyewe dhambi za matendo yake. Na Mola wako si Mwenye kuwadhulumu waja kwa kuwapunguzia japo thawabu ya jema moja au kuwaongezea japo dhambi la ovu moja

    [47] Kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Peke Yake, Asiye na mshirika, Ndiko kunakorudishwa ujuzi wa kipindi cha kusimama Kiyama, kwani hakuna yoyote anayejua kipindi hiko isipokuwa Yeye. Na hayatoki matunda kwenye vifuko vyake (mitini), na hakuna kiumbe chochote cha kike kinachoshika mimba wala kinachojifungua mimba yake isipokuwa kinajulikana na Mwenyezi Mungu. Hakuna chochote kinachofichamana kwake kuhusu hilo. Na siku ambayo Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Atawaita washirikina Siku ya Kiyama kwa kuwakaripia na kuonyesha urongo wao, Awaambie,»Wako wapi washirika wangu ambao mlikuwa mkiwashirikisha katika ibada yangu?» Hapo waseme, «Tunakujulisha sasa kuwa hatuna yoyote atakayeshuhudia Leo kuwa wewe una mshirika.»

    [48] Wakawapotea hao washirikina wale washirika wao ambao walikuwa wakiwaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, wasiwanufaishe na wakajuwa kwa yakini kuwa hakuna makimbilio yoyote ya kuwaepusha wao na adhabu ya Mwenyezi Mungu

    [49] Binadamu hachoki kumuomba Mola wake Ampatie mema ya duniani, na akipatikana na umasikini na shida, huwa anakata tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu na anakufa moyo kwa kuwa na dhana mbaya kwa Mola wake

    [50] Na tunapomuonjesha binadamu neema kutoka kwetu baada ya shida na mitihani, hamshukuru Mwenyezi Mungu Aliyetukuka bali anaruka mpaka na kusema, «Haya niliyoyapata yamenijia kwa kuwa mimi ninastahiki kuyapata, na sidhani kuwa Kiyama ni chenye kuja.» Anasema hayo kwa njia ya kukanusha kufufuliwa «Na kwa kukadiria kuwa Kiyama kitakuja na kuwa mimi nitarudi kwa Mola wangu, basi mimi nitapata Pepo Kwake Yeye.» Basi tutawapasha habari wale walioikanusha Siku ya Kiyama kwa yale maovu waliyoyafanya, na tutawaonjesha adhabu kali

    [51] Na tunapomneemesha binadamu kwa afya na riziki au vingineyo, hugeuka na kufanya kiburi kwa kukataa kuifuata haki. Na akipatikana na shida huwa akileta dua ndefu akimuomba Mwenyezi Mungu Amuondolee shida yake; huwa akimjua Mola wake wakati wa shida na hamjui wakati wa neema

    [52] Sema, ewe Mtume, uwaambie hawa wakanushaji, «Hebu nipeni habari, iwapo hii Qur’ani inatoka kwa Mwenyezi Mungu kisha nyinyi mkaikataa na mkaikanusha, basi hakuna mpotevu zaidi kuliko nyinyi, kwa kuwa nyinyi mko kinyume kabisa na haki kwa kuikataa kwenu Qur’ani na kuikanusha.»

    [53] Tutawaonyesha, hawa wakanushaji, aya zetu za kuteka miji na kupata nguvu Uislamu katika majimbo mbalimbali na juu ya dini nyingine na maeneo ya mbingu na ardhi, na katika matukio makubwa Anayoyaleta Mwenyezi Mungu humo na ndani ya nafsi zao, na vile vilivyomo humo miongoni mwa alama za kuvutia za utendakazi wa Mwenyezi Mungu na maajabu ya utengenezaji Wake, (tutawaaonyesha hayo yote) mpaka iwafunukie nyinyi, ufunuzi usiyokubali shaka yoyote, kwamba Qur’ani ndiyo haki iliyoletwa kwa njia ya wahyi kutoka kwa Mola wa viumbe wote. Je hauwatoshi wao ushahidi wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kuwa ni dalili ya kuwa Qur’ani ni haki na kuwa aliyekuja nayo ni mkweli? Kwani Mwenyezi Mungu Ameishuhudilia kwa kuisadikisha, na Yeye ni shahidi wa kila kitu, na hakuna kitu chochote chenye kutolea ushahidi kuliko ushahidi wa Mwenyezi Mungu, aliyetakasika na kutukuka

    [54] Jueni na mtanabahi kuwa hawa makafiri wako kwenye shaka kubwa kuhusu kufufuliwa baada ya kufa. Jueni na mtanabahi kuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, Amekizunguka kila kitu kwa ujuzi, uweza na ushindi, hakuna chochote kinachofichamana Kwake ardhini wala mbinguni

    Shura

    Surah 42

    [1] «Ḥā, Mīm

    [2] Ayn, Sīn, Qāf» Yametangulia maelezo juu ya herufi zilizokatwa na kutengwa mwanzo wa sura ya Al-Baqarah

    [3] Kama Alivyokuteremshia Mwenyezi Mungu, ewe Nabii, hii Qur’ani, Aliteremsha Vitabu na Kurasa kwa Manabii kabla yako. Na Yeye Ndiye Mshindi katika kutesa Kwake, Ndiye Mwenye hekima katika maneno Yake na vitendo Vyake

    [4] Ni vya Mwenyezi Mungu Peke Yake vilivyoko mbinguni na ardhini, na Yeye Ndiye wa juu kwa cheo Chake na utendeshaji nguvu Wake, Aliye Mkuu Ambaye Ana ukubwa na enzi

    [5] Zinakaribia mbingu kupasuka- pasuka, kila moja juu ya ile inayoifuata, kutokana na ukubwa wa Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema na haiba Yake, Mwingi wa fadhila na utukufu, na hali Malaika wanamtakasia Shukurani Mola wao na kumwepusha na kila sifa ambayo hanasibiani nayo, na wanamuomba Mola wao msamaha wa dhambi za waliyoko ardhini miongoni mwa wale wanaomuamini. Jueni mtanabahi kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye kusamehe sana dhambi za waja Wake Waumini na Ndiye Mwenye kuwarehemu

    [6] Na wale waliowafanya wasiokuwa Mwenyezi Mungu kuwa ni waungu badala Yake wakawategemea na kuwaabudu, basi Mwenyezi Mungu Anavidhibiti vitendo vyao, ili Awalipe kwavyo Siku ya Kiyama. Na wewe hukuwakilishwa kuvidhibiti vitendo vyao. Hakika yako wewe ni muonyaji tu, hivyo basi ni juu yako kufikisha na ni juu yetu kuhesabu

    [7] Na kama tulivyowapelekea wahyi Manabii kabla yako wewe, tulikuletea wahyi wa Qur’ani iliyo kwa lugha ya Kiarabu, ili uwaonye watu wa Makkah na watu wote wengine pambizoni mwake, na uwaonye Siku ya Mkusanyiko, nayo ni Siku ya Kiyama, ambayo kuja kwake hakuna shaka, ambapo watu Siku hiyo watakuwa mapote mawili: pote moja litakuwa Peponi, nalo ni lile la waliomuamini Mwenyezi Mungu na wakayafuata yale aliyokuja nayo Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na pote lingine litakuwa Motoni, nalo ni lile la waliomkanusha Mwenyezi Mungu na wakaenda kinyume na yale aliyokuja nayo Mtume Wake, Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [8] Na lau Angalitaka Mwenyezi Mungu Kuwakusanya viumbe Wake kwenye uongofu na kuwafanya wawe kwenye mila moja iliyoongoka angalifanya hivyo, lakini Yeye Anataka kuwatia kwenye rehema Yake Anaowataka miongoni mwa waja Wake. Na wale wenye kuzidhulumu nafsi zao kwa kufanya ushirikina, basi hao hawatakuwa na yoyote wa kumtegemea atakayesimamia mambo yao Siku ya Kiyama, wala msaidizi atakayewanusuru kutokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka

    [9] Bali hawa washirikina waliwachukuwa wasiokuwa Mwenyezi Mungu kuwa ni wategemewa wakawa wanawategemea. Mwenyezi Mungu Peke Yake Ndiye Mwenye kutegemewa, mja anamtegemea kwa kumuabudu na kumtii, na Yeye Anawasimamia waja Wake Waumini kwa kuwatoa kwenye giza kuwatia kwenye mwangaza na kwa kuwasaidia katika mambo yao yote. Na Yeye Anahuisha waliokufa wakati wa kufufuliwa, na Yeye kwa kila jambo ni Mweza, hakuna chochote kinachomshinda

    [10] Na kitu chochote kile mnachotafautiana kwacho , enyi watu, miongoni mwa mambo ya dini yenu, basi hukumu irudishwe kwa Mwenyezi Mungu katika Kitabu Chake na Sunnah ya Mtume Wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie. Huyo Ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wangu na Mola wenu, Kwake Yeye nimetegemea katika mambo yangu, na Kwake Yeye ninarejea katika hali zangu zote

    [11] Mwenyezi Mungu, kutakasika ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Ndiye Muumba mbingu na ardhi na Muanzilishi wa kuzitengeneza kwa uweza Wake na matakwa Yake na hekima Yake. Amewapatia nyinyi wake wanaotokana na nyinyi ili mjitulize kwao, na Amewapatia nyinyi wanyama-howa wa kila aina, wa kiume na wa kike. Anawafanya nyinyi muwe wengi kwa kuzaana kwa njia hii ya kutangamana. Hakuna kinachofanana na Yeye, Aliyetukuka, na kuwa kama Yeye chochote kile miongoni mwa viumbe vyake, si katika dhati Yake wala majina Yake wala sifa Zake wala vitendo Vyake. Kwani majina Yake yote ni mazuri na sifa Zake ni sifa za ukamilifu na utukufu; na kwa vitendo Vyake, Aliyetukuka, Amefanya vipatikane viumbe vikubwa bila ya kuwa na mshirika. Na Yeye Ndiye Mwenye kusikia na Ndiye Mwenye kuona. Hakuna chochote kinachofichamana Kwake cha matendo ya waja Wake na maneno yao, na Atawalipa kwa hayo

    [12] Ni Wake Yeye, kutakasika ni Kwake, ufalme wa mbinguni na ardhini, na mkononi Mwake kuna funguo za rehema na riziki, Anamkunjulia riziki Yake Anayemtaka miongoni mwa waja Wake na Anambania Anayemtaka. Hakika Yeye , Aliyetukuka na kuwa juu, ni Mjuzi wa kila kitu, Hakifichamani Kwake Yeye chochote katika mambo ya viumbe Vyake

    [13] Amewawekea nyinyi, enyi watu, Sheria ya Dini tuliyokuletea kwa njia ya wahyi, ewe Mtume, nayo ni Uislamu, na ile Aliyomuusia Nūḥ aifuate kivitendo na aifikishe kwa watu, na ile aliyowausia Ibrāhīm, Mūsā na Īsā (Watano hawa ndio Ulū al- 'azm [wenye hima] miongoni mwa Mitume kulingana na kauli iliyo mashuhuri) kwamba msimamishe Dini kwa kumpwekesha Mwenyezi Mungu, kumtii na kumuabudu Yeye na sio mwingine, na msitafautiane katika Dini ambayo nimewaamrisha muifuate. Ni kubwa mno juu ya washirikina lile mnalowalingania la kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtakasia ibada. Mwenyezi Mungu Anamchagua Anayemtaka miongoni mwa viumbe Vyake awe ni mwenye kumpwekesha na Anamuongoza yule anayerejea Kwake afanye matendo ya utiifu Kwake

    [14] Na hawakutengana wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu katika dini zao wakawa mapote na makundi mbalimbali isipokuwa baada ya ujuzi kuwajia na hoja kuwasimamia. Na hakuna lililowafanya wao wafanye hivyo isipokuwa ni udhalimu na ushindani. Na lao si neno lililotangulia linalotoka kwa Mola wako, ewe Mtume, la kucheleweshwa adhabu mpaka kipindi kilichotajwa. nacho ni Siku ya Kiyama, hukumu ingalitolewa ya kuharakishiwa adhabu wakanushaji miongoni mwao. Na hakika wale waliorithishwa Taurati na Injili, baada ya hawa wenye kutafautiana juu ya haki, wako kwenye shaka yenye kutia kwenye wasiwasi na kutafautiana juu ya Dini na Imani

    [15] Basi, kwenye dini hiyo iliyolingana sawa ambayo Mwenyezi Mungu Aliwawekea Manabii na Akawausia waifuate, lingania, ewe Mtume, waja wa Mwenyezi Mungu, na uwe na msimamo wa kisawa kama Anavyokuamrisha Mwenyezi Mungu. Na usifuate matamanio ya wale walioifanyia haki shaka na wakapotoka kwa kuwa kando na Dini, na useme, «Nimeviamini Vitabu vyote vilivyoteremshwa kutoka mbinguni kwa Manabiii, Na Mola wangu Ameniamrisha nifanye uadilifu baina yenu katika kuhukumu. Mwenyezi Mungu ni Mola wetu na Mola wenu. Sisi tutapata thawabu ya matendo yetu mema, na nyinyi mtapata malipo ya matendo yenu maovu. Hakuna utesi wala mjadala baina yetu sisi na nyinyi baada ya haki kufafanuka. Mwenyezi Mungu Atatukusanya sisi na nyinyi Siku ya Kiyama Ahukumu baina yetu kwa haki katika yale tuliyotafautiana, na kwake Yeye ndio marejeo na marudio, na huko Amlipe kila mmoja kwa anachostahiki.»

    [16] Na wale wanaojadili kuhusu Dini ya Mwenyezi Mungu niliyomtumiliza kwayo Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, baada ya watu kuikubali na kusilimu, hoja yao na mjadala wao, mbele ya Mola wao, ni zenye kutenguka na kuondoka. Na watashukiwa na adhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu hapa duniani, na huko Akhera watakuwa na adhabu kali, nayo ni Moto

    [17] Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyeteremsha Qur’ani na Vitabu vilivyoteremshwa vinginevyo kwa ukweli. Na Ameteremsha mizani, nayo ni uadilifu, ili Ahukumu baina ya watu kwa usawa. Na ni lipi linalokujulisha na kukufahamisha kuwa huenda wakati ambao Kiyama kitasimama uko karibu

    [18] Wana haraka nako, huko kuja kwa Kiyama, wale wasiokiamini, kwa njia ya shere na mzaha, na wale wanaokiamini wanaogopa kusimama kwake, na hali wao wanajua kuwa ni kweli isiyo na shaka. Basi jua utanabahi kuwa wale wanaojadili kuhusu Kiyama wako kwenye upotevu wa mbali

    [19] Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja Wake, Anamkunjulia riziki Anayemtaka na Anambania hiyo riziki Anayemtaka, Na Yeye Ndiye Mwenye nguvu ambaye nguvu zote Anazo, Aliye Mshindi katika kuwatesa wenye kumuasi

    [20] Yoyote Anayetaka kwa matendo yake malipo mema ya Akhera, Akatekeleza haki za Mwenyezi Mungu na Akatoa katika kulingania Dini, tutamuongezea wema katika matendo yake, tumzidishie thawabu za jema moja mara kumi mpaka kipimo anachokitaka Mwenyezi Mungu cha nyongeza. Na yoyote yule Anayetaka kwa matendo yake ulimwengu peke yake, tutampa tulichomgawia cha huo ulimwengu , na hatakuwa na thawabu zozote huko Akhera

    [21] Je, kwani hawa wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu wana washirika katika ushirikina wao na upotevu wao ambao waliwazulia katika dini na ushirikina kitu Asichoamuru Mwenyezi Mungu? Na lau si hukumu ya Mwenyezi Mungu makadirio Yake ya kuwapa muhula na kutowaharakishia adhabu duniani, wangalihukumiwa kuharakishiwa adhabu. Na kwa hakika wale wenye kumkanusha Mwenyezi Mungu watakuwa na adhabu yenye uchungu na kuumiza Siku ya Kiyama

    [22] Utawaona, ewe Mtume, makafiri Siku ya Kiyama wako katika hali ya kuogopa mateso ya Mwenyezi Mungu kwa yale matendo mabaya waliyoyatenda duniani, na adhabu itawashukia, na wao wataionja hapana budi. Na wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na wakamtii, wataingia kwenye mabustani ya Pepo na majumba yake na starehe za Akhera, na watakuwa na kila kinachotamaniwa na nafsi zao kwa Mola wao. Hayo Aliyowapa Mwenyezi Mungu ya fadhila na utukufu ndiyo nyongeza isiyosifika na isiyofikiwa na akili

    [23] Hayo ambayo niliwapa habari kwayo, enyi watu, miongoni mwa starehe na matukufu ya Akhera ndio yale ambayo Mwenyezi Mungu Anawapa bishara kwayo waja Wake wema waliomuamini na kumtii duniani. Sema, ewe Mtume, uwaambie wale wanaofanya shaka kuhusu Kiyama miongoni mwa washirikina wa watu wako, «Siwaombi kwa huu ulinganizi wangu wa haki niliokuja nao mnipe malipo kwenye mali yenu, isipokuwa mnitekelezee haki yangu ya ujamaa kwenu na muunge kizazi kilichoko baina yangu mimi na nyinyi.» Na yoyote mwenye kutenda jema tutamuongezea mara kumi na zaidi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe kwa wingi dhambi za waja Wake, ni Mwingi wa shukrani kwa mema yao na utiifu wao Kwake

    [24] Au je, wanasema hawa washirikina, kwamba Muhammad amemzulia Mwenyezi Mungu urongo ndipo akaja na hiki anachokisoma kwa kukizua mwenyewe? Basi Mwenyezi Mungu Ataupiga muhuri moyo wako, ewe Mtume, uwapo utafanya hivyo. Na Mwenyezi Mungu Anaiondoa batili na kuifuta, na Anaithibitisha haki kwa maneno Yake, ambayo hayabadiliki wala hayageuki, na kwa ahadi Yake ya kweli isiyoenda kinyume. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi sana wa yaliyomo ndani ya nyoyo za waja, hakuna chochote kinachofichamana kwake

    [25] Na Mwenyezi Mungu, aliyetakasika na kutukuka, Ndiye Anayekubali toba kutoka kwa waja Wake wanaporudi kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtii, Ndiye Anayesamehe makosa na Ndiye Anayejua mnayoyafanya ya kheri na shari, hakuna chochote kinachofichamana Kwake, na Yeye ni Mwenye kuwalipa kwa hayo

    [26] Na wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, wanamuitika Mola wao kwa kile Alichowaitia na wanajisalimisha Kwake, na Yeye Anawaongezea fadhila Zake kwa kuwaongoza na kuwazidishia malipo na thawabu. Na wale wenye kumkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake watapata adhabu kali yenye kuumiza na yenye uchungu Siku ya Kiyama

    [27] Na lau Mwenyezi Mungu Angaliwakunjulia riziki waja Wake Akawapa kwa wingi, wangalipita mipaka katika ardhi kwa kiburi na ujeuri na wangalitoka baadhi yao kuwadhulumu wengine. Lakini Mwenyezi Mungu anawateremshia riziki zao kwa kadiri atakayo ya kuwatosha. Hakika Yeye kwa waja Wake ni mtambuzi kwa yale yanayowafaa, Anaiona mipango yao na mabadiliko ya hali zao

    [28] Na Mwenyezi Mungu Peke Yake Ndiye Anayeteremsha mvua kutoka mbinguni, Akawanyeshea kwayo baada ya kukata tamaa kunyesha kwake, Akaeneza rehema Yake kwa viumbe Vyake, Akawapa mvua ya kuwaenea, na Yeye Ndiye Mtegemewa, Anawasaidia waja Wake kwa hisani Yake na wema Wake, Msifiwa kwa uongozi wake na uendeshaji mambo Wake

    [29] Na miongoni mwa alama za kuonyesha ukubwa Wake, uweza Wake na mamlaka Yake ni uumbaji mbingu na ardhi kwa namna ambayo hakukuwa na mfano uliotangulia na aina mbalimbali za wanyama Alizozieneza humo. Na Yeye, kuwakusanya viumbe baada ya kufa kwao kwa kisimamo cha Kiyama, Anapotaka ni Muweza, hakuna kinachomshinda

    [30] Na msiba wowote uliowakumba, enyi watu, katika Dini yenu na dunia yenu, ni kwa sababu ya dhambi mlizozitenda na makosa. Na Mola wenu Anawasamehe nyinyi makosa mengi Asiwaadhibu kwa kuyafanya

    [31] Na hamkuwa, enyi watu, ni wenye kushindana na uweza wa Mwenyezi Mungu juu yenu wala kuuhepa. Na hamna nyinyi asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mtegemewa wa kusimamia mambo yenu na kuwapa manufaa wala msaidizi wa kuwatetea msipatikane na madhara

    [32] Na miongoni mwa alama Zake zenye kuonyesha uweza Wake mkubwa na mamlaka Yake yenye kushinda ni majahazi makubwa kama majabali yanayotembea baharini

    [33] Anapotaka Mwenyezi Mungu Anautuliza upepo, na majahazi yakawa ni yenye kutulia juu ya mgongo wa bahari na kutotembea. Hakika katika kutembea majahazi haya na kusimama kwake baharini kwa uweza wa Mwenyezi Mungu pana mawaidha na hoja waziwazi za uweza wa Mwenyezi Mungu, kwa kila mwingi wa uvumilivu juu ya kumtii Mwenyezi Mungu, kujiepusha na vitendo vya kumuasi na kukubali makadirio Yake, mwingi wa shukrani wa neema Zake na mema Yake

    [34] Au (Anapotaka) Anayaangamiza hayo majahazi kwa kuyazamisha kwa sababu ya dhambi za wenyewe, na Anasamehe dhambi nyingi Asiwatese wenye kuzifanya

    [35] Na wajue wale wanaojadili kuhusu aya zetu zenye kutolea dalili upweke wetu kwa njia ya ubatilifu, hawatakuwa na mahali pa kupita wala pa kuhamia kujiepusha na mateso ya Mwenyezi Mungu Atakapowatesa kwa dhambi zao na ukanushaji wao

    [36] Na chochote kile mnachopewa, enyi watu, cha mali na watoto na vinginevyo, ni pumbao lenu la uhai wa ulimwenguni, kwa haraka sana litaondoka, na kilichoko kwa Mwenyezi Mungu cha starehe ya Pepo ya daima ni bora zaidi na ni chenye kusalia zaidi kwa wale wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake na wakawa kwa Mola wao wanategemea

    [37] Na wale ambao wanajiepusha na madhambi makubwa yaliyokatazwa na Mwenyezi Mungu, na kila kilichokuwa kichafu na kibaya miongoni mwa maasia, na wanapowakasirikia wale waliowakosea wanaufinika huo ubaya na kuusamehe kwa kuacha kumlipiza mkosa, kwa kutaka malipo mema ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na msamaha Wake. Na hii ni miongoni mwa tabia njema

    [38] Na wale walioitika mwito wa Mola wao wa kumpwekesha Yeye na kumtii, wakasimamisha Swala za faradhi kwa namna zake katika nyakati zake, na wakitaka jambo wanashauriana juu yake , na katika mali tuliyowapa wanatoa sadaka kwenye njia ya Mwenyezi Mungu, na wanatekeleza haki wanazofaradhiwa kuwapatia wanaostahiki kama vile Zaka na matumizi na katika njia nyinginezo za matumizi

    [39] Na wale ambao yakiwapata maonevu wanawalipiza wale waliowaonea bila kupita kiasi. Na wanaposubiri basi mwisho wa subira yao kuna kheri nyingi

    [40] Na malipo ya ubaya wa mtu mbaya ni kumtesa kwa ubaya mfano wake bila kuzidisha. Na mwenye kumsamehe aliyemfanyia ubaya asimtese, na akatengeneza mapenzi baina yake yeye na yule aliyemsamehe kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu, basi malipo mema ya kusamehe kwake yako kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu Hawapendi wenye kudhulumu wanaowaanza watu kwa uadui na kuwafanyia ubaya

    [41] Na yoyote aliyemlipiza yule aliyemdhulumu baada ya kudhulumiwa naye, basi hao hawana makosa ya kuadhibiwa kwayo

    [42] Hakika ni kwamba mapatilizo ni ya wale wanaowaonea watu kwa udhalimu na uadui, wakapita mpaka waliowekewa wa vitu walivyohalalishiwa na Mola wao na wakaingia kwenye eneo la vitu visivyoruhusiwa kwao, wakafanya uharibifu katika ardhi pasi na haki, basi hao Siku ya Kiyama watakuwa na adhabu yenye uchungu na kuumiza

    [43] Na yoyote mwenye kuvumilia juu ya makero na akalipa, kwa ovu alilofanyiwa, kwa kusamehe, kufuta na kufinika, basi hayo ni miongoni mwa mambo makubwa yenye kushukuriwa na vitendo vyenye kusifiwa ambavyo Mwenyezi Mungu Ameviamrisha na Ameviwekea thawabu nyingi na sifa nzuri

    [44] Na yule ambaye Mwenyezi Mungu Anampoteza na kumweka kando na uongofu kwa sababu ya udhalimu wake, hatakuwa na mtu wa kumsaidia na kumuelekeza njia ya uongofu. Na utawaona, ewe Mtume, wenye kumkanusha Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama, watakapo kuiona adhabu, wakisema, kumwambia Mola wao, «Je, tuna njia yoyote ya kurejea duniani ili tufanye matendo ya utiifu kwako?» Na ombi hilo halitakubaliwa kwao

    [45] Na utawaona, ewe Mtume, hawa madhalimu wakiorodheshwa Motoni wakiwa wadhalilifu na wanyonge, wanakutazama kwa jicho la unyonge lililo dhaifu kwa hofu waliokuwa nayo na utwevu. Na watasema waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Peponi, watakapoyaona yaliyowashukia makafiri ya hasara, «Hakika wenye hasara kikweli ni wale waliopata hasara ya nafsi zao na watu wao Siku ya Kiyama kwa kuingia Motoni.» Jua utanabahi kuwa madhalimu, siku ya Kiyama, watakuwa kwenye adhabu ya daima isiyokatika wala kuondoka

    [46] Na hawa wenye kukanusha, Atakapowaadhibu Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama, hawatakuwa na wasaidizi na waokozi wenye kuwanusuru kutokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na yoyote yule ambaye Mwenyezi Mungu Amempoteza kwa sababu ya ukanushaji wake na udhalimu, hatakuwa na njia yenye kumfikisha kwenye haki hapa duniani, na kwenye Pepo kesho Akhera, kwa kuwa yeye atakuwa amezibiwa njia za kuokoka, kwani kuongoza na kupoteza viko mkononi mwa Mwenyezi Mungu, kutakasika na kutukuka ni Kwake, na haviko kwa mwingine

    [47] Itikieni mwito wa Mola wenu, enyi wenye kukanusha, kwa kuamini na kutii kabla haijaja Siku ya Kiyama ambayo haimkiniki kuirudisha. Siku hiyo hamtakuwa na mahali pa kukimbilia penye kuwaokoa na adhabu wala mahali pa kuwasitiri mkawa hamtambulikani hapo. Katika aya hii pana dalili ya ubaya wa kuchelewesha, na pana maamrisho ya kuharakisha kufanya kila tendo zuri linalomtokea mja, kwani kuchelewesha kuna athari mbaya na vizuizi

    [48] Watakapokataa hawa washirikina, ewe Mtume, kumuamini Mwenyezi Mungu, basi hatukukutumiliza kuwa ni mtunzi wa matendo yao mapaka ukawa ni mwenye kuwahesabu kwa hayo. Lazima yako haikuwa isipokuwa ni kufikisha ujumbe. Na sisi tunapompa binadamu rehema kutoka kwetu rehema ya utajiri, ukunjufu wa mali na mengineyo, hufurahika na akapendezwa, na unapowakumba msiba wa umasikini, ugonjwa na mengineyo kwa sababu ya kile kilichotangulizwa na mikono yao cha kufanya matendo ya kumuasi Mwenyezi Mungu, hapo binadamu huwa ni mwenye kukataa sana, huwa akihesabu misiba na akisahau neema

    [49] Ni ya Mwenyezi Mungu mamlaka ya mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake. Anaumba viumbe anavyovitaka. Anamtunuku Anayemtaka miongoni mwa waja Wake wanawake bila kuwa na wanaume pamoja nao, na Anamtunuku Anayemtaka wanaume bila kuwa na wanawake pamoja nao

    [50] Na Anampa, Anayetakasika na kutukuka, Anayemtaka miongoni mwa watu wanaume na wanawake. Na Anamfanya Anayemtaka kuwa tasa asiyezaa. Hakika Yeye ni Mjuzi sana wa Anachoumba, ni Muweza sana kuumba Anachotaka, hakuna chochote kinachomshinda Akitaka kukiumba

    [51] Na haipasi kwa kiumbe yoyote, kati ya binadamu, Mwenyezi Mungu Aseme naye isipokuwa kwa njia ya wahyi ambao Mwenyezi Mungu Anamtumia au Aseme naye nyuma ya pazia, kama vile Alivyosema Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika, na Mūsā, amani imshukie, Au Atume mjumbe, kama Anavoyomtuma Jibrili, amani imshukie, kwa yule anayetumwa kwake ampelekee wahyi wa kile Mwenyezi Mungu Anataka apelekewe, kwa idhini ya Mola wake, na sio kwa mapendeleo yake. Hakika Yake Yeye, Aliyetukuka, Yuko juu kwa dhati Yake, majina Yake, sifa Zake na vitendo Vyake. Amekilazimisha kila kitu, na viumbe vyote vimemdhalilikia, ni Mwingi wa hekima katika uedeshaji Wake mambo ya viumbe Vyake. Katika aya hii pana kuthibitisha sifa ya kusema kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kwa namna inayonasibiana na haiba Yake na ukubwa wa mamlaka Yake

    [52] Na kama vile tulivyowapelekea wahyi Manabii kabla yako wewe, ewe Nabii, tulikuletea wewe wahyi wa Qur’ani itokayo kwetu, hukuwa unajua kabla yake ni vitabu vipi vilivyotangulia wala nini Imani wala zipi Sheria zinazotokana na Mwenyezi Mungu? Lakini tumeifanya Qur’ani ni mwangaza kwa watu ambao kwa huo tunawaongoza waja wetu tunaowataka kwenye njia iliyolingana sawa. Na hakika wewe, ewe Mtume, unamuelekeza na kumuongoza kwa amri ya Mwenyezi Mungu kwenye njia iliyolingana sawa, nayo ni Uislamu

    [53] njia ya Mwenyezi Mungu Aliye na mamlaka ya vyote vilivyoko mbinguni na vilivyoko ardhini, hana mshirika katika hayo. Jua utanabahi kwamba kwa mwenyezi Mungu , enyi watu, yatarudi mambo yote yenu ya kheri na shari, na huko Amlipe kila mtu kwa matendo yake, yakiwa mema alipwe wema na yakiwa mabaya alipwe ubaya

    Mapambo

    Surah 43

    [1] “Hā, Mīm” maelezo yametangulia mwanzoni mwa sura ya Al-Baqarah juu ya herufi zilizokatwa na kutengwa

    [2] Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Ameapa kwa Qur’ani ambayo matamshi yake na maana yake yako waziwazi

    [3] Hakika sisi tumeiteremsha Qur’ani kwa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa lugha ya Kiarabu , huenda nyinyi mkaelewa na mkazingatia maana yake na hoja zake

    [4] Nayo , kwa hakika, katika Ubao Uliohifadhiwa kwetu sisi ina cheo na heshima za juu, iko thabiti, haina tafauti ndani yake wala kugongana

    [5] Je tuwape nyinyi mgongo na tuache kuwateremshia Qur’ani kwa ajili ya kupuuza kwenu, kutofuata na kupita mipaka kwenu katika kukataa kuiamini

    [6] Tumewatumiliza Manabii wengi katika kame za mwanzo zilizopita kabla ya watu wako, ewe Nabii

    [7] Hawajiwi na Nabii yoyote isipokuwa huwa wakimcheza shere kama vile watu wako walivyokucheza shere, basi tukawaangamiza wale waliowakanusha Mitume wetu, nao walikuwa ni wenye nguvu kali na ushujaa wa kivita kuliko watu wako, ewe Mtume

    [8] Na yashapita mateso ya wa mwanzo kwa kuangamizwa kwa sababu ya ukanushaji wao, ujeuri wao na kuwacheza shere Mitume wao. Katika haya pana maliwazo kwa Nabii, rehema na amani zimshukie

    [9] Na unapowauliza, ewe Mtume, hawa washirikina miongoni mwa watu wako, «Ni nani aliyeumba mbingu na ardhi? Wanasema , «Aliyeziumba ni Yule Aliye Mshindi katika mamlaka Yake, Aliye Mjuzi wa hizo na vitu vilivyomo ndani yake, hakuna chochote kinachofichamana Kwake

    [10] Aliyewafanyia ardhi kuwa ni (kama) tandiko na mkeka, Akawasahilishia humo njia za maisha yenu na biashara zenu, ili mjiongoze kwa njia hizo kwenye maslahi yenu ya kidini na ya kidunia

    [11] Na Aliyeteremsha kutoka mawinguni mvua kwa kipimo, Asiifanye mafuriko yenye kuzamisha wala pungufu isiyotosheleza haja, ipate kuendesha maisha yenu na yale ya wanyama wenu, tukahuisha kwa maji hayo sehemu kubwa ya ardhi kavu isiyokuwa na mimea. Na kama tulivyotoa kwa maji hayo tuliyoyateremsha kutoka juu, kwenye ardhi hiyo iliyokufa, mimea na mazao, hivo ndivyo mtakavyotolewa, enyi watu, makaburini mwenu baada ya kutoweka kwenu

    [12] Na Aliyeumba aina zote za wanyama na mimea, na Akawawekea majahazi mnayoyapanda baharini, na Akawaumbia wale mnaowapanda barani miongoni mwa wanyama, kama vile ngamia, farasi, nyumbu na punda

    [13] Mpate kujituliza juu ya migongo ya hivyo mnavyovipanda, kisha mkumbuke neema ya Mola wenu kwenu hapo mnapopanda na mseme, «Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu Aliyetudhalilishia (kipando) hiki, na hatukuwa ni wenye uwezo juu yake.»

    [14] Na ili mseme pia, «Na sisi baada ya kufa kwetu ni wenye kuelekea Kwake na kurejea. Hapa pana dalili ya kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye kuwaneemesha waja Wake kwa neema mbalimbali, Ndiye Mwenye kustahiki kuabudiwa kwa kila hali

    [15] Na hawa washirikina wamemfanya Mwenyezi Mungu kuwa na fungu miongoni mwa waja Wake. Nako ni kule kusema kwao kuhusu Malaika kuwa ni watoto wa kike wa mwenyezi Mungu. Kwa hakika, binadamu ni mwingi wa kukanusha neema za Mola Wake Alizowaneemesha kwazo, ni mwenye kudhihirisha kukataa kwake na kukanusha kwake, anahesabu misiba na anasahau neema

    [16] Je, kwani nyinyi mnadai, enyi wajinga, kuwa Mola wenu Amejichagulia, katika vile Anavyoviumba, watoto wa kike, na hali nyinyi hamliridhii hilo kwenu, na Akawahusu nyinyi kwa kuwapatia watoto wa kiume? Haya ni makaripio kwao

    [17] Na anapopewa bishara mmoja wao ya mtoto wa kike ambaye amemnasibishia Mwingi wa rehema, alipodai kwamba Malaika ni watoto wa kike wa Mwenyezi Mungu, uso wake unageuka ukawa mweusi kwa bishara mbaya aliyopewa ya mtoto wa kike, na huwa na huzuni na kujawa na hamu na unguliko.(Basi vipi wataridhika kwa Mwenyezi Mungu kitu ambacho wao wenyewe hawaridhiki nacho? Ametukuka Mwenyezi Mungu kutukuka kukubwa na Ametakasika na kile wanachosema hao makafiri)

    [18] Je, mnajasiri na kumnasibishia Mwenyezi Mungu mtu anayelelewa katika pambo asiyeweza kutasua hoja kwenye mjadala kwa sababu ya kukulia kwake kwenye pambo na starehe

    [19] Na hawa washirikina waliwafanya Malaika ambao ni waja wa Mwenyezi Mungu kuwa ni wanawake. Je, wao walihudhuria wakati Mwenyezi Mungu Alipowaumba mpaka waamue kuwa wao ni wanawake? Ushahidi wao utasajiliwa, na wataulizwa kuhusu hilo kesho Akhera

    [20] Na hawa washirikina wa Kikureshi wanasema, «Lau Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Angalitaka, hatungalimuabudu yoyote asiyekuwa Yeye.” Na hii ni hoja iliyotanguka, kwani Mwenyezi Mungu Ashasimamisha hoja juu ya waja kwa kuwatumiliza Mitume na kuteremsha Vitabu, basi kujisimamishia hoja ya Mapitisho na Makadirio ni ubatilifu mkubwa zaidi baada ya Mitume kuwaonya. Wao hawana ujuzi wa hakika ya yale wanayoyasema. Hakika ni kwamba wao wanayasema kwa kudhania na kuzua urongo, kwa kuwa hawana habari wala dalili kuhusu hilo kutoka kwa Mwenyezi Mungu

    [21] Je, walishuhudia uumbaji wa Malaika au tuliwapatia kitabu kabla ya hii Qur’ani tuliyoiteremsha, wakawa wameshikamana nacho, wakifanyia kazi na wanajijengea kwa hicho hoja za kukupinga, ewe Mtume

    [22] Bali walisema, «Sisi tuliwakuta baba zetu kwenye njia, madhehebu na dini, na sisi tunafuata na kuandama nyayo za baba zetu katika yale waliyokuwa nayo.”

    [23] Hivyo ndivyo ilivyo, hatukutumiliza kabla yako wewe, ewe Mtume, muonyaji yoyote kwenye kijiji chochote, mwenye kuwaonya adhabu yetu kwa kutukanusha, na akawaonya na kuwahadharisha adhabu yetu, isipokuwa wale ambao ziliwatia kiburi neema miongoni mwa viongozi na wakubwa huwa wakisema, ”Sisi tuliwakuta baba zetu kwenye mila na dini, na sisi ni wenye kufuata mwenendo wao na njia yao.”

    [24] Huyo Muonyaji, akiwa ni Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na wale Mitume waliomtangulia, huwa akisema kuwaambia waliompinga wakitumia udanganyifu huu uliyotanguka, «Je, mtawafuata baba zenu , hata kama mimi nimewajia kutoka kwa Mola wenu na kitu chenye kuongoza zaidi kwenye njia ya haki na chenye kuonyesha zaidi njia ya uongofu kuliko kile mlichowakuta baba zenu wakikifuata cha dini na mila?” Na wao huwa wakisema kwa ushindani, ”Sisi ni wenye kuyapinga na kuyakanusha hayo mliyotumilizwa kwayo.”

    [25] Basi tukawalipiza hao ummah waliowakanusha Mitume wao kwa kuwateremshia mateso ya kuwadidimiza, kuwazamisha na mengineyo. Basi angalia, ulikuwa vipi mwisho wa mambo yao walipozikanusha hoja za Mwenyezi Mungu na Mtume wake? Basi na wajihadhari watu wako wasiendelee kwenye ukanushaji wao ili yasiwapate wao yale yaliyowapata wale

    [26] Kumbuka, ewe Mtume, pindi aliposema Ibrāhīm alipomwambia baba yake na watu wake waliokuwa wakiabudu vitu ambavyo watu wako , ewe mtume, wanaviabudu, ”Hakika mimi nimejiepusha na vile mnavyoviabudu badala ya Mwenyezi Mungu

    [27] «Isipokuwa Yule Aliyeniumba , kwani Yeye Ataniafikia kufuata njia ya uongofu.”

    [28] Na Ibrāhīm, amani imshukie, alilifanya neno la kumpwekesha Mwenyezi Mungu (Lā ilāha illā Allāh) ni lenye kusalia baada yake, kwa kutarajiwa warudi kumtii Mola wao na kumpwekesha. Na kutubia kutokana na ukanushaji wao na dhambi zao

    [29] Bali niliwastarehesha hawa washirikina wa watu wako, ewe mtume, na wazazi wao kabla yao kwa uhai, sikuwaharakishia adhabu kwa ukanushaji wao mpaka ikawajia Qur’ani na Mtume wa kuwabainishia wanachokihitajia katika mambo ya Dini yao

    [30] Na ilipowajia Qur’ani kutoka kwa Mwenyezi Mungu walisema, «Hii uliyotuletea ni uchawi wa kuturogea nao, na si wahyi unaotoka kwa Mwenyezi Mungu, na sisi tunaukanusha.”

    [31] Na hawa washirikina wa Kikureshi walisema, «Iwapo hii Qur’ani inatoka kwa Mwenyezi Mungu kikweli, basi si ateremshiwe mtu mkuu kutoka miji hii miwili: Makkah au Ṭāif

    [32] Je, wao ndio wanaougawa huu utume wakauweka wanapotaka? Sisi tumewagawia wao maisha yao katika uhai wao wa kilimwengu ya riziki na vyakula, na tumewainua daraja baadhi yao juu ya wengine : huyu ni tajiri na huyu ni masikini, huyu ana nguvu na huyu ni mnyonge, ili baadhi yao wawe ni wenye kutumiwa na wengine katika maisha. Na rehema ya Mola wako, ewe Mtume, ya kuwatia wao Peponi ni bora kuliko takataka za dunia zenye kutoweka

    [33] Na lau si kuwa watu watajumuika pamoja kwenye ukafiri, tungalizifanya nyumba za wale wenye kumkanusha Mwingi wa Rehema ziwe na ghorofa za fedha na ngazi za wao kupandia

    [34] Na tukazifanya nyumba zao ziwe na milango ya fedha, tukawafanyia vitanda ambavyo juu yake wanakaa na kutegemea

    [35] na tukawafanya wawe na dhahabu. Na vyote hivyo havikuwa isipokuwa ni sterehe za maisha ya kilimwengu, nazo ni starehe chache zenye kuondoka. Na starehe za Akhera zimehifadhiwa kwa Mola wako kwa wale wachamungu na si kwa wengine

    [36] Na mwenye kuupa mgongo utajo wa Mwingi wa Rehema, nao ni Qur’ani, asiogope mateso yaliyotajwa ndani yake na asijiongoze kwa uongofu wake, tutamwekea Shetani hapa duniani wa kumpoteza, ikiwa ni malipo yake ya kuupa mgongo kwake utajo wa Mwenyezi Mungu. Shetani huyo atakuwa na yeye wakati wote na kufuatana naye, akimkataza ya halali na kumsukuma afanye ya haramu

    [37] Na kwa hakika, Mashetani wanawazuia hawa wanaoupa mgongo utajo wa Mwenyezi Mungu wasifuate njia ya haki, wanawapambia upotevu na wanawafanya wachukie Kumuamini Mwenyezi Mungu na kufanya matendo ya utiifu Kwake. Na wanadhani hawa wenye kupa mgongo, kutokana na vile Mashetani wanavyowapambia upotevu walionao, wanadhani kuwa wao wako kwenye haki na uongofu

    [38] Mpaka pale atakapotujia yule aliyeupa mgongo utajo wa Mwenyezi Mungu pamoja na yule mwenzake Shetani, ili kuhesabiwa na kulipwa, atasema yule mwenye kupa mgongo kumwambia mwenzake, «Natamani lau baina yangu mimi na wewe pana umbali wa baina ya Mashariki na Magharibi, kwani mwenza mbaya zaidi kwangu ni wewe kwa kuwa umenipoteza.”

    [39] Haitawafalia kitu leo, enyi mlioupa mgongo utajo wa Mwenyezi Mungu, kwa kushirikisha kwenu duniani, kuwa mmeshirikiana na wenzenu (wa Kishetani) katika adhabu. Basi kila mmoja ana fungu lake kamili la adhabu kama mlivyoshirikiana katika ukanushaji

    [40] Je, kwani wewe, ewe mtume, unamsikilizisha yule ambaye Mwenyezi Mungu Amemfanya kiziwi akawa haisikii haki, au unamuongoza kwenye njia ya uongofu yule ambaye Mwenyezi Mungu Ameupofusha moyo wake akawa haioni haki, au unamuongoza yule aliyepotoka waziwazi akawa kando ya haki? Hayo si yako. Lako wewe ni kufikisha ujumbe, na si juu yako kuwafanya waongoke, lakini Mwenyezi Mungu Anamuongoza Anayemtaka na Anampoteza Anayemtaka

    [41] Na iwapo tutakufisha, ewe Mtume, kabla hujanusuriwa juu ya wakanushaji wa watu wako, basi sisi ni wenye kuwalipiza wao kwa kuwaadhibu huko Akhera

    [42] Au tutakuonyesha lile tulilowaahidi la adhabu yenye kuwashukia, kama ilivyokuwa siku ya Badr, kwani sisi tuna uweza juu yao tutakupa ushindi juu yao na tutawafedhehi kwa mkono wako na kwa mikono ya wenye kukuamini

    [43] Basi shikamana, ewe Mtume, na kile alichokuamrisha Mwenyezi Mungu katika hii Qur’ani ambayo Mwenyezi Mungu amekuletea, kwa njia ya wahyi. Hakika wewe uko kwenye njia iliyonyoka, nayo ni Dini ya Mwenyezi Mungu aliyoamrisha ifuatwe ambayo ni Uislamu. Hapa pana kumpa moyo Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kumsifu

    [44] Na hii Qur’ani ni utukufu kwako na kwa watu wako miongoni mwa washirikina wa Kikureshi, kwa kuwa imeteremshwa kwa lugha yao, kwa kuwa wao wanaifahamu zaidi kuliko watu wengine na kwa hivyo inatakiwa wawe ni watu wenye kusimama nayo zaidi na ni wenye kufanya matendo yanayoambatana nayo zaidi. Na mtaulizwa , wewe na walio pamoja na wewe, kuhusu vile mlivyomshukuru kuletewa hiyo Qur’ani na mlivyoifanyia kazi

    [45] Na uwaulize, ewe Mtume, wafuasi wa wale tuliowatumiliza kabla yako miongoni mwa Mitume wetu na wabebaji sheria zao, «Je walikuja Mitume wao na ujumbe wa kuabudiwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu?” Wao watakupasha habari kuwa hilo halikutukia, kwani Mitume wote walilingania kile ulichowaitia watu cha kumuabudu Mwenyezi Mungu, Peke Yake Asiye na mshirika, na wakakataza kuabudiwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu

    [46] Kwa hakika tulimtumiliza Mūsā kwa hoja zetu aende kwa Fir’awn na watukufu wa watu wake kama tulivyokutumiliza wewe, ewe mtume, kwa hawa washirikina wa watu wako, na Mūsā akawaambia, «Mimi ni Mtume kutoka kwa Mola wa viumbe wote.”

    [47] Na alipowajia na dalili zilizo wazi zenye kuonyesha ukweli wake katika ulinganizi wake, hapo Fir’awn na viongozi wa utawala wake wakawa wanazicheka zile hoja na mazingatio alivyokuja navyo Mūsā

    [48] Na hatukuwa tukimuonyesha Fir’awn hoja yoyote isipokuwa huwa ni kubwa zaidi kuliko ile iliyokuwa kabla yake na inautolea dalili zaidi usahihi wa kile ambacho Mūsā alikuwa akiwalingania kwacho. Na tuliwapatiliza kwa aina mbalimbali za adhabu , kama vile Nzige, chawa, vyura, mafuriko na nyinginezo ili wapate kurudi kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtii na kuacha kumkanusha

    [49] Na Fir’awn na viongozi wa utawala wake wakasema kumwambia Mūsā, ”Ewe mjuzi! (Na mchawi alikuwa kwao ni mtu mkubwa wanayemheshimu, na haukuwa uchawi ni sifa ya mtu kutukanika), ’Tuombee Mola wako, kwa ile ahadi Aliyokuahidi na yale matukufu Aliyokutunukia wewe mahsusi, Atuepushie adhabu, kwani tukiepushiwa adhabu, kwa hakika sisi ni wenye kuongoka na kuayaamini yale uliotujia nayo

    [50] Basi Mūsā alipoomba adhabu iondolewe kwao na tukawaondolea hiyo adhabu, ghafla wanavunja ahadi na wanaendelea kwenye upotevu wao

    [51] Na Fir’awn aliita mbele ya wakubwa wa watu wake kwa kujigamba na kujisifu kwa ufalme wa Misri, «Je, kwani mimi sina ufalme wa Misri na mito hii inayopita chini yangu? Kwani hamuoni utukufu wangu na nguvu zangu na unyonge wa Mūsā na umasikini wake

    [52] «Bali mimi ni bora kuliko huyu asiye na utukufu. Kwani yeye anajidhalilisha katika kuataka haja zake kwa udhaifu wake na unyonge wake, na hafafanui maneno kwa ajili ya uzito wa ulimi wake.» Na lililomfanya Fir’awn atoe kauli hii ni ukafiri, ushindani na uzuiaji njia ya Mwenyezi Mungu

    [53] «Basi si apewe huyo Mūsā, iwapo ni mkweli kuwa yeye ni Mjumbe wa Mola wa viumbe wote, vikuku vya dhahabu, au waje Malaika pamoja na yeye wameshikana na kukutana na wakafuatana wakimtolea ushahidi kuwa yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwetu sisi.»

    [54] Fir’awn akazichezea akili za watu wake, akawaita kwenye upotevu na wao wakamtii na wakamkanusha Mūsā. Kwa hakika, wao walikuwa ni watu waliotoka kwenye utiifu wa Mwenyezi Mugu na njia yake ya sawa

    [55] Walipotukasirisha, kwa kutuasi na kumkanusha Mūsā na miujiza aliyokuja nayo, tuliwatesa kwa adhabu ya duniani tuliyowaharakishia na tukawazamisha wote baharini

    [56] Tukawafanya hao tuliowazamisha baharini kuwa ni mfano uliotangulia kwa anayefanya matendo kama yao katika wale watakaokuja baada yao kwa kustahiki adhabu, na ni mazingatio na mawaidha kwa watu wa nyuma

    [57] Na washirikina walipopiga mfano wa Īsā mwana wa Maryam walipomjadili Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kumhoji kuwa Wanaswara wanamuabudu, unawakuta watu wako wanainua sauti zao na kupiga kelele kwa furaha na kuterema. Napo ni pale neno la Mwenyezi Mungu Aliyetukuka lilipoteremka (Nyinyi na vile mnavyoviabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Moto, nyinyi nyote ndani ya Moto huo mtaingia). Na washirikina wakasema, «Tumeridhika kwa waungu wetu wawe na cheo cha Īsā, Mwenyezi Mungu Akateremsha neno lake (Hakika wale ambao ilitangulia kutoka kwetu kuwa wao ni wema, hao ni wenye kuepushwa nao huo Moto). Yule anayetupwa Motoni, miongoni mwa waungu wa makafiri, ni yule aliyeridhika kuabudiwa na wao

    [58] Na walisema washirikina wa watu wako, ewe Mtume, ” Je waungu wetu tunaowaabudu ni bora au ni Īsā ambaye watu wake wanamuabudu? Akiwa Īsā atakuwa Motoni, basi nasi natuwe na waungu wetu pamoja na yeye. Hawakukupigia mfano huu isipokuwa kwa kujadili, bali wao ni wabishi kwa njia ya ubatilifu

    [59] Hakuwa Īsā mwana wa Maryam isipokuwa ni mja, tulimneemesha kwa utume na tukamfanya ni alama ya kutolea ushahidi uweza wetu

    [60] Na lau tungakiataka tungaliwajaalia badala yenu Malaika , hawa baada ya wengine, badala ya wanadamu

    [61] Kwa hakika kuteremka kwa Īsā, amani imshukie, kabla ya Siku ya Kiyama, ni dalili ya kukaribia Wakati huo, basi msitie shaka kuwa hilo ni lenye kuwa hapana budi. Na nifuateni mimi katika yale ninayowatolea habari kutoka kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. Hii ni njia imara inayoelekea Peponi, isiyo na mpeto

    [62] Na asiwazuie Shetani, kwa kutia kwake wasiwasi kwa watu, kunitii mimi katika yale ninayowaamrisha na ninayowakataza, kwani yeye ni adui kwenu ambaye uadui wake uko waziwazi

    [63] Na Īsā alipowajia Wana wa lsrāīl kwa dalili zilizofunuka wazi alisema, «Nimewajia na unabii, na ili niwaeleze baadhi ya mambo ya yale mnayotafautiana kwayo katika mambo ya Dini. Basi mcheni Mwenyezi Mungu kwa kufuata amri Zake na kuepuka makatazo Yake, na mnitii mimi katika yale ninayowaamrisha ya kumcha Mwenyezi Mungu na kumtii

    [64] «Hakika Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Ndiye Mola wangu na Mola wenu nyote, basi muabuduni Yeye Peke Yake na msimshirikishe na Yeye kitu chochote. Hili nililowaamrisha la kumcha Mwenyezi Mungu na kumpwekesha kwa ustahiki wa kuabudiwa ndio njia iliolingana sawa, nayo ni Dini ya Mwenyezi Mungu ya kweli Ambaye Hakubali kutoka kwa yoyote dini isiyokuwa hiyo.”

    [65] Hapo makundi ya watu yakatafautiana kuhusu jambo la Īsā, amani imshukie, na wakawa mapote: kati yao kuna waliokubali kuwa yeye ni mja wa Mwenyezi Mungu na ni Mtume Wake, na hiyo ndio kauli ya kweli, na kati yao kuna wanaodai kuwa yeye ni mwana wa Mwenyezi Mungu , na kati yao kuna wanaosema kwamba yeye ni Mwenyezi Mungu, Ametukuka Mwenyezi Mungu kutukuka kukubwa na kutakasika na neno lao hilo. Basi maangamivu na adhabu kali Siku ya Kiyama ni yenye kuwapata wale waliomsifu Īsā kwa sifa ambazo sizo zile Mwenyezi Mungu Alizomsifu nazo

    [66] Je, kwani wana kutu chochote wanachokingojea watu wa makundi hayo waliotafautiana kuhusu Īsā isipokuwa ni kujiwa na Kiyama kwa ghafla na hali wao hawahisi wala hawatambui

    [67] Marafiki katika kumuasi Mwenyezi Mungu duniani watatengana wao kwa wao Siku ya Kiyama. Lakini wale waliofanya urafiki juu ya uchaji Mwenyezi Mungu, urafiki wao utadumu duniani na Akhera

    [68] Wataambiwa hawa wachamungu, «Enyi waja wangu! Hamna khofu yoyote Leo ya kupata mateso yangu, wala nyinyi hamtahuzunika juu ya hadhi za kilimwengu mlizozikosa.”

    [69] Wale walioziamini aya zetu na wakayafuata kivitendo yale walioletewa na Mitume wao, wakawa ni wenye kumtii Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe vyote, kwa nyoyo zao na viungo vyao

    [70] wataambiwa, «Ingieni Peponi , nyinyi na wendani wenu Waumini, mkistareheshwa humo na mkifurahishwa.”

    [71] Watazungushiwa, hawa waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake, chakula ndani ya vyombo vya dhahabu na vinywaji ndani ya gilasi za dhahabu. Na humo watakuwa na kila ambacho nafsi zao zinakitamani na macho yao yanapendezwa nacho, na wao humo watakaa milele

    [72] Na hii Pepo ambayo Mwenyezi Mungu Amewarithisha, ni kwa sababu ya kile mlichokuwa mkikifanya ulimwenguni cha mambo ya kheri na matendo mema, na akaifanya, kwa wema Wake na rehema Yake, ni malipo yenu

    [73] Mtakuwa nayo, humo Peponi, matunda mengi ya kila aina ya nyinyi kuyala

    [74] Hakika ya wale waliochuma dhambi kwa ukanushaji wao, ni wenye kukaa ndani ya adhabu ya Jahanamu

    [75] Hawatasahilishiwa, na wao wakiwa ndani yake watakuwa ni wenye kukata tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu

    [76] Na hatukuwadhulumu wahalifu hawa kwa kuwaadhibu , isipokuwa ni wao wenyewe ndio waliojidhulumu nafsi zao kwa kushirikisha kwao na kukataa kuwa Mwenyezi Mungu Ndie Mola wa haki, Aliye Peke Yake, Asiye na Mshirika na kuacha kuwafuata Mitume wa Mola wao

    [77] Na hao wahalifu waliomkanusha Mwenyezi Mungu, baada ya Mwenyezi Mungu kuwatia kwenye moto wa jahanamu, watamwita Malik, mshika hazina za Moto kwa kusema, «Ewe Malik! Basi na Atufishe Mola wako, tupate kupumzika na haya tuliyonayo,” Hapo Malik awajibu, «Nyinyi ni wenye kukaa, hamna kutoka Motoni na hamna makimbilio ya kujiepusha nao.”

    [78] Kwa hakika, tumewaletea haki na kuibainisha kwenu, lakina wengi wenu mliichukia walipokuja nayo Mitume

    [79] Je, kwani hawa washirikina wamepanga mambo madhubuti ya kuichimba haki tuliyowaletea? Sisi tunawapangia adhabu na mateso

    [80] Au kwani wanadhani, hawa wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, kuwa sisi hatusikii yale wanayoyaficha ndani ya nafsi zao na kunong’onezana baina yao? Basi sivyo hivyo, sisi tunasikia na tunajua, na wajumbe wetu ambao ni Malaika watukufu na watunzi wanawaandikia yote waliyoyafanya

    [81] Sema, ewe mtume, uwaambie washirikina wa watu wako wanaodai kuwa Malaika ni watoto wa kike wa Mwenyezi Mungu, «Iwapo Mwingi wa rehema Alikuwa na mtoto, kama vile mnavyodai, lakini hili halikuwa wala halitakuwa, basi mimi ni wa mwanzo kumuabudu mtoto huyo mnaodai, Ametakasika Mwenyezi Mungu na kuwa na mke na mtoto.”

    [82] Kuepukana na kila sifa ya upungufu na kutakasika ni kwa Mola wa mbingu na ardhi, Mola wa ’Arsh kubwa, na kuwa mbali na urongo na uzushi wanaomzulia washirikina ya kuwa Mwenyezi Mungu Ana mwana na mengineyo ya ubatilifu wanayodai

    [83] Basi waache, ewe Mtume, hao wenye kumzulia Mwenyezi Mungu urongo wavame kwenye ubatilifu wao na wacheze katika dunia yao mpaka wapambane na hiyo Siku yao ambayo wanaahidiwa kuwa wataadhibiwa: ima hapa duniani au kesho akhera au kote kuwili

    [84] Na Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Anayeabudiwa kwa haki, mbinguni na ardhini, na Yeye Ndiye Mwingi wa hekima Aliyeimarisha kuumba Kwake na kuitengeneza Sheria Yake, Mwenye ujuzi wa kila kitu kuhusu hali ya viumbe Vyake. Hakuna chochote kinachofichamana katika hivyo

    [85] Ni nyingi mno baraka za Mwenyezi Mungu na kheri Zake na ni mkubwa mno ufalme Wake, Ambaye ni Yake, Peke Yake, mamlaka ya mbingu saba na ardhi saba na vitu vilivyoko baina yake, na Kwake Yeye Ndiko uliyoko ujuzi wa Wakati ambapo Kiyama kitasimama na viumbe wafufuliwe kutoka makaburini mwao wapelekwe kwenye Kisimamo cha Hesabu, na Kwake Yeye mtarudishwa, enyi watu, baada ya kufa kwenu, na hapo alipwe kila mmoja kwa anayostahiki

    [86] Na hawamiliki, wale ambao washirikina wanawaabudu, uwezo wa kumuombea yoyote mbele ya Mwenyezi Mungu isipokuwa wale waliyoishuhudia haki na wakakubali upweke wa Mwenyezi Mungu na unabii wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na wakawa na yakini ya uhakika wa kile walichokikubali na kukitolea ushahidi

    [87] Na ukiwauliza, ewe Mtume, hao washirikina wa watu wako, ”Ni nani aliyewaumba?” watasema, «Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyetuumba.” Basi vipi wao wanageuka na wanapotoka kwa kuacha kumuabudu Mwenyezi Mungu, Peke Yake, na kumshirikisha na asiyekuwa Yeye

    [88] Na Atasema Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu amani zimshukie, huku akimshtakia watu wake waliomkanusha kwa Mola Wake kwa kusema, «Hawa ni watu hawakuamini wewe wala kile ulichonituma kwao

    [89] Basi wasamehe, ewe Mtume, na uyapuuze makero yao, na lisitokee lolote kutoka kwako isipokuwa amani ambalo ni neno linalosemwa na wenye akili na busara kuambiwa wajinga, kwani wao hawatukanani na wao wala hawawalipizi kwa vitendo vyao vibaya waliowafanyia. Basi watajua watakachokikuta cha balaa na adhabu. Hapa pana onyo na kitisho kikubwa kwa makafiri hawa wenye kushindana na mfano wao

    Dukhan

    Surah 44

    [1] «Ḥā, Mīm” Yametangulia maelezo kuhusu herufu zilizokatwa na kutengwa mwazo wa sura ya Al-Baqarah

    [2] Ameapa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa Qur’ani iliyo wazi kimatamshi na kimaana

    [3] Sisi tuliiteremsha katika Usiku wa Cheo uliobarikiwa wenye kheri nyingi, nao unapatikana katika mwezi wa Ramadhani. Sisi ni wenye kuonya watu kwa kile kinachowanufaisha na kuwadhuru, nako ni kule kupeleka Mitume na kuteremsha Vitabu, ili hoja ya Mwenyezi Mungu iwasimamie waja Wake

    [4] Katika usiku huo linaamuliwa na kupambanuliwa, kutoka kwenye Ubao Uliohifadhiwa na kuletewa waandishi kati ya Malaika, kila jambo lililokadiriwa la muda wa kuishi na riziki katika mwaka huo na mambo mengine yatakayokuwa na kukadiriwa na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, mpaka mwisho wa mwaka, hayabadilishwi wala hayageuzwi

    [5] Mambo haya yaliyopangwa kimadhubuti ni amri inayotoka kwetu, kwani yote yanayokuwa na Anayokadiria Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na wahyi Anaouleta, vyote hivyo vinatokana na amri Yake na idhini Yake na ujuzi Wake. Hakika sisi tumetumiliza Mitume, Muhammad na waliokuwa kabla yake, kwa watu

    [6] Hilo likiwa ni rehema kutoka kwa Mola wako, ewe Mtume, kuwafikia wale wenye kutumilizwa. Hakika Yeye ni Msikizi, Anasikia sauti zote, ni Mjuzi wa mambo yote ya waja Wake yaliyojitokeza nje na yanayofichika

    [7] Muumba mbingu na ardhi na vitu vyote vilivyoko baina ya hivyo viwili. Iwapo nyinyi mna yakini na hilo, basi jueni kuwa Mola wa viumbe Ndiye Mola wa kweli

    [8] hakuna Mola anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Yeye, Peke Yake, Asiye na mshirika, Anayehuisha na kufisha, Mola wenu na Mola wa baba zenu wa mwanzo, basi muabuduni Yeye, na sio waungu wenu ambao hawawezi kudhuru wala kunufaisha

    [9] Bali hawa washirikina wanaifanyia shaka haki; wao wanapumbaa na kucheza na hawaiamini

    [10] Basi ngojea, ewe Mtume, uwaone hawa washirikina siku ambayo mbingu itakuja na moshi uliofunuka waziwazi

    [11] utakaowaenea watu, na hapo waambiwe, «Hii ni adhabu yenye uchungu na yenye kuumiza.”

    [12] Kisha waseme wakiomba iondolewe na iepushwe na wao, «Mola wetu! Tuepushie adhabu, kwani ukituepushia sisi ni wenye kukuamini.” (Na hilo lilifanyika na wasiamini kama walivyoahidi)

    [13] Vipi watakuwa ni wenye kukumbuka na kuwaidhika baada ya kuteremkiwa na adhabu, na hali wamejiwa na Mtume mwenye kufafanua, naye ni Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [14] kisha wakaenda kinyume na yeye na wakasema kwamba alifundishwa na binadamu au makuhani au mashetani na kwamba yeye ni mwendawazimu na si Mtume

    [15] Tutawaondolea nyinyi adhabu kidogo na mtaona kuwa nyinyi mtarudia yale ambayo mlikuwa mkiyafanya ya ukafiri, upotevu na ukanushaji, na kwa hakika sisi tutawaadhibu kwa hayo

    [16] Siku tutakayowaadhibu makafiri wote adhabu kubwa kabisa Siku ya Kiyama, nayo ni Siku ya kuwatesa kwa kuwalipiza

    [17] Hakika sisi tushawafanyia mtihani na kuwajaribu watu wa Fir’awn kabla ya hawa washirikina, na aliwajia wao Mtume mtukufu, naye ni Mūsā, amani imshukie, wakamkanusha na wakaangamia. Basi hivi ndivyo tutakavyowafanya maadui zako, ewe Mtume, wasipoamini

    [18] Na Mūsā aliwaambia, «Nisalimishieni waja wa Mwenyezi Mungu kati ya Wana wa Isrāīl, na muwaachilie pamoja na mimi, wapate kumuabudu Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Asiye na mshirika. Mimi, kwenu nyinyi, ni mjumbe muaminifu juu ya wahyi Wake na ujumbe Wake

    [19] Na msimfanyie kiburi Mwenyezi Mungu kwa kuwakanusha Mitume Wake, kwani mimi ni mwenye kuwajia na hoja waziwazi ya ukweli wa utume wangu

    [20] Na mimi nimejihami kwa Mwenyezi Mungu msipate kuniua kwa kunipiga mawe

    [21] Na iwapo hamniamini kwa haya niliokuja nayo, basi niacheni nifuate njia yangu na muache kuniudhi

    [22] Hapo Mūsā akamuomba Mola wake, Fir’awn na watu wake walipomkanusha, akisema, «Hakika hawa ni watu wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kumkanusha.”

    [23] Basi enda na waja wangu waliokuamini, wakakusadiki na wakakufuata, ewe Mūsā, katika kipindi cha usiku, kwani nyinyi mtafuatwa na Fir’awn na askari wake. Na nyinyi mtaokolewa, na Fir’awn askari wake watazama

    [24] Na iache bahari hali ilivyo utakapopita, ikiwa imetulia haina mchafuko. Hakika Fir’awn na askari wake ni wenye kuzamishwa humo baharini

    [25] Ni vingapi alivyoviacha Fir’awn na watu wake, baada ya kuangamia kwao na kuzamishwa baharini na Mwenyezi Mungu, miongoni mwa mabustani na mashamba yaliyostawi, chemchemi za maji yenye kupita

    [26] Namazao na majumba mazuri na maisha

    [27] waliokuwa nayo ya neema na anasa

    [28] Mfano wa mateso hayo ndivyo Mwenyezi Mungu Anavyowatesa wenye kukanusha na kubadilisha neema za Mwenyezi Mungu kwa kuzikanusha. Na tuliwarithisha neema hizo, baada ya Fir’awn na watu wake, watu wengine waliokuja baada yao wakashika nafasi yao miongoni mwa Wana wa Isrāīl

    [29] Mbingu na ardhi hazikulia kwa kumsikitikia Fir’awn na watu wake, na hawakuwa ni wenye kucheleshewa adhabu iliyowashukia

    [30] Kwa hakika, tuliwaokoa Wana wa Isrāīl kutokana na adhabu yenye kuwafanya wanyonge kwa kuuawa watoto wao wa kiume na kutumishwa wanawake wao

    [31] Kutokana na Fir’awn. Hakika yeye alikuwa mjeuri, miongoni mwa washirikina, aliyepita mpaka katika kujigamba na kuwafanyia kiburi waja wa Mwenyezi Mungu

    [32] Na kwa hakika, tuliwachagua Wana wa Isrāīl, kwa kuwajua kwetu, juu ya walimwengu wa zama zao

    [33] Tukawapatia miujiza, kupitia kwa Mūsā, ambayo ilikuwa ni mtihani na maonjo kwao ya raha na shida

    [34] Hakika hawa washirikina wa watu wako, ewe Mtume, wanasema

    [35] ”Hakuna kifo chochote ila kile kifo chetu tutakachokufia , nacho ndicho kifo cha mwanzo na cha mwisho, na sisi baada ya kufa kwetu hatutakuwa ni wenye kufufuliwa tuhesabiwe na tulipwe mema au tuteswe.”

    [36] Na wanasema pia, «Basi tuletee, ewe Muhammad: wewe na walio pamoja na wewe, wazazi wetu waliokufa, iwapo nyinyi ni wakweli kwamba Mwenyezi Mungu Atawafufua walio makaburini wakiwa hai.”

    [37] Je, hawa washirikina ni bora au watu wa Tubba’ wa Himyar na wale waliokuwa kabla yao miongoni mwa ummah waliomkanusha Mola wao? Tuliwaangamiza kwa uhalifu wao na kukanusha kwao. Hawa washirikina si bora kuliko hao ili tuwasamehe na tusiwaangamize, na hali wao wanamkanusha Mwenyezi Mungu

    [38] Na hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyoko baina yake kwa mchezo

    [39] Hatukuviumba hivyo viwili isipokuwa kwa haki ambayo ndiyo mpango wa Mwenyezi Mungu katika kuumba Kwake na kupelekesha mambo Kwake. Lakini wengi wa hawa washirikina hawalijui hilo, na kwa hivyo hawavitii akilini vitu viwili hivyo, kwa kuwa wao hawatarajii kupata malipo mema wala hawaogopi mateso

    [40] Hakika Siku ya Uamuzi baina ya viumbe kwa waliyoyatanguliza katika dunia yao, ya kheri na ya shari, ndio wakati wa mkusanyiko wao wote

    [41] Siku ambayo hakuna rafiki atayeweza kumuondolea rafiki yake shida yoyote, wala hawatasaidiana wao kwa wao

    [42] isipokuwa yule ambaye Mwenyezi Mungu Amemrehemu miongoni mwa Waumini, kwani yeye huenda akamuombea kwa Mola wake baada ya kuruhusiwa na Mwenyezi Mungu. Kwa hakika Mwenyezi Mungu Ndiye Mshindi katika kuwatesa maadui zake, Ndiye Mwenye kuwarehemu kwa wingi wale wenye kumtegemea na kumtii

    [43] Hakika mti wa zaqqūm unatoka kwenye shina la moto wa Jaḥīm

    [44] Matunda yake ni chakula cha mwenye dhambi nyingi, na dhambi kubwa zaidi kuliko dhambi zote ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu

    [45] Matunda ya mti wa zaqqūm ni kama madini yaliyoyeyushwa

    [46] Yanachoma ndani ya matumbo ya washirikina kama vile maji yaliyofikia upeo wa joto

    [47] Mchukueni huyu mwenye dhambi aliyeasi mumsukume na mumuongoze kwa nguvu hadi katikati ya moto wa Jaḥīm Siku ya Kiyama

    [48] Kisha mmimine juu ya kichwa cha huyu mfanya dhambi maji yaliyo moto sana hadi ya mwisho, na adhabu isimuepuke

    [49] Ataambiwa mfanya dhambi huyo mbaya, «Onja adhabu hii unayoadhibiwa kwayo Leo! Hakika wewe ni mheshimiwa katika watu wako, ulio mtukufu kwao.» Katika haya kuna kumfanyia maskhara na kumlaumu

    [50] Hakika adhabu hii mnayoadhibiwa kwayo Leo, ndiyo ile adhabu mliokuwa mna shaka nayo duniani na mkawa hamuiamini

    [51] Hakika ya wale wanaomcha Mwenyezi Mungu, kwa kufuata amri Zake na kujiepusha na makatazo yake duniani, watakuwa na mahali pa kukaa, hali ya kuwa wameaminika na magonjwa, masikitiko na mengineyo

    [52] Kwenye mabustani ya Pepo.na maji yenye kupita

    [53] Watakuwa wamevaa dibaji nyororo, hali ya kuwa wameelekeana kwa nyuso. Na hawatakuwa wakiangaliana visogo. Makao yao yatakuwa yakizunguka nao pale wanapozunguka

    [54] Kama tutakavyowapa huko Akhera takrima ya kuwaingiza Peponi na kuwavisha hariri nzito na hariri yenye mng’aro, vilevile tutawakirimu kwa kuwaoza wanawake wazuri wenye macho makubwa ya kupendeza

    [55] Wataka wachamungu hao huko Peponi waletewe kila aina ya matunda ya Peponi wanayoyatamani, wakiwa wamejiaminisha kuwa neema hizo hazitakatika wala hazitamalizika

    [56] Hawataonja kifo, wachamungu hao, huko Peponi, baada ya kifo cha kwanza walichokionja duniani. Na Mwenyezi Mungu Atawakinga , hao wachamungu,na adhabu ya moto wa Jaḥīm, kwa wema Wake na hisani itokayo Kwake, Aliyetakasika na kuwa juu

    [57] Takrima hii tutakayowapa wachamungu, huko Akhera, ndiyo kufuzu kukubwa ambako hakuna kufuzu kungine baada ya kufuzu huko

    [58] Hakika sisi tumeyarahisisha matamshi ya Qur’ani na maana yake kwa lugha yao, ewe Mtume, kwani huenda wakawaidhika na wakakemeeka

    [59] Basi ngojea, ewe Mtume, ushindi niliokuahidi juu ya hawa wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu na adhabu itakayowashukia. Wao ni wenye kungojea kufa kwako, kukushinda na kukulazimisha. Basi watajua utakuwa ni wa nani ushindi, kufaulu na sauti ya juu duniani na Akhera. Hivyo ni vyako wewe, ewe Mtume, na vya wale Waumini waliokufuata

    Aliye Piga Magoti

    Surah 45

    [1] «Ḥā, Mīm» Yametangulia maelezo kuhusu herufi zilizokatwa na kutengwa katika mwanzo wa sura ya Al-Baqarah

    [2] Hii Qur’ani imeteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Aliye Mshindi katika kuwatesa maadui Zake, Mwingi wa hekima katika uendeshaji wa mambo ya viumbe Vyake

    [3] Hakika kwenye mbingu saba na ardhi ambapo humo viumbe vinatoka, na vilivyomo baina ya hivyo viwili miongoni mwa viumbe wa jinsi tofauti na aina mbalimbali, kuna dalili na hoja kwa wenye kuziamini

    [4] Na katika kuwaumba nyinyi, enyi watu, na uumbaji wa vilivyotapakaa ardhini miongoni mwa vinavyotambaa juu yake, kuna hoja na dalili kwa watu wenye imani ya yakini juu ya Mwenyezi Mungu na Sheria Yake

    [5] Na katika kupishana usiku na mchana na kufuatana katika kuwajilia na mvua Aliyoiteremsha Mwenyezi Mungu kutoka mawinguni, Akaihuisha kwayo ardhi baada ukavu wake, ikajitikisa kwa mimea na mazao, na katika kuupeleka upepo kwenu kutoka sehemu zote na kuusarifu kwa maslahi yenu, kuna dalili na hoja kwa watu wanaoelewa kuhusu Mwenyezi Mungu hoja Zake na dalili Zake

    [6] Aya hizi na hoja tunakusomea wewe, ewe Mtume, kwa haki. Basi ni mazungumzo gani baada ya Mwenyezi Mungu na dalili Zake kuwa Yeye Ndiye Mola wa kweli Peke Yake, Hana mshirika Wake, wao watayaamini na kuyasadiki na kuyatumia

    [7] Maangamivu makubwa yatampata kila mrongo sana mwenye dhambi nyingi

    [8] Anayezisikia aya za kitabu cha Mwenyezi Mungu akisomewa kisha akaendelea kwenye ukanushaji wake kwa kujiona ni mkubwa zaidi wa kutoweza kumfuata Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kama kwamba yeye hakusikia alichosomewa miongoni mwa aya za Mwenyezi Mungu. Basi mbashirie, ewe Mtume, huyo mrongo sana mwenye dhambi nyingi adhabu yenye uchungu inayoumiza ndani ya Moto wa Jahanamu Siku ya Kiyama

    [9] Na huyu mrongo sana mwingi wa dhambi anapojua kitu katika aya zetu anazifanyia shere na mzaha. Hao watakuwa na adhabu itakayowadhakikisha na kuwatia kwenye hizaya Siku ya Kiyama, ikiwa ni malipo ya kuicheza shere kwao Qur’ani

    [10] Basi mbele ya hao wenye kuzifanyia shere aya za Mwenyezi Mungu patakuwa na moto wa Jahanamu. Na hakitawafalia wao kitu chochote kile walichokichuma cha mali na wana wala waungu wao waliowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Na watakuwa na adhabu kubwa yenye uchungu

    [11] Hii Qur’ani tuliyoiteremsha kwako, ewe Mtume, ni uongofu wenye kuondoa upotevu, ni dalili ya haki na inamuongoza kwenye njia iliyolingana sawa atakayeifuata na akaifanyia kazi. Na wale waliozikataa aya zilizomo ndani ya Qur’ani zenye kutolea dalili Ukweli na wasiziamini, watakuwa na adhabu miongoni mwa adhabu kali zaidi Siku ya Kiyama, yenye uchungu na kuumiza

    [12] Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Ndiye Aliyewadhalilishia bahari, ili majahazi yatembee juu yake kwa amri Yake, na ili mtafute kheri Zake kwa biashara mbalimbali na shughuli za kuchuma, na kwamba nyinyi mpate kumshukuru Mola wenu kuwadhalilishia hayo, na hivyo basi mumuabudu Yeye Peke Yake na mumtii Yeye katika yale Anayowaamrisha na kuwakataza

    [13] Na Akawadhalilishia kila kilichoko mbinguni miongoni mwa jua , mwezi na nyota, na kila kilicho ardhini miongoni mwa wanyama, miti, majahazi na visiokuwa hivyo kwa ajili ya maslahi yenu. Neema zote hizi ni vipaji Alizowaneemesha nazo Mwenyezi Mungu Peke Yake na fadhila inayotoka Kwake Aliyowafadhili nayo. Basi Yeye Peke Yake muabuduni, na msimfanye yoyote kuwa ni mshirika Wake. Hakika katika vitu vile Alivyowadhalilishia Mwenyezi Mungu kuna alama na dalili juu ya upweke wa Mwenyezi Mungu kwa watu wenye kuzitia akilini aya za Mwenyezi Mungu, hoja Zake na dalili Zake, wakazizingatia

    [14] Sema, ewe Mtume, uwaambie wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na wakamfuata Mtume Wake, wawasamehe na kuwaachilia wale ambao hawana matarajio ya malipo mema ya Mwenyezi Mungu na hawaogopi adhabu Yake wanapowakusudia Waumini kuwaudhi na kuwakera, ili Mwenyezi Mungu Awalipe washirikina hawa kwa yale waliyoyachuma duniani ya madhambi na kuwaudhi Waumini

    [15] Yoyote yule, miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu, Anayefanya matendo ya utiifu Kwake, basi malipo mema ya utiifu wake atayapata mwenyewe, na mwenye kufanya matendo mabaya duniani kwa kumuasi Mwenyezi Mungu, basi atakuwa amejikosea mwenyewe. Kisha nyinyi, enyi watu, mtaishia kwa Mola wenu baada ya kufa kwenu, Amlipe mwema kwa wema wake na mbaya kwa ubaya wake

    [16] Hakika tuliwapatia Wana wa Isrāīl Taurati na Injili na tukawaamuru kuhukumu kulingana na yaliyomo kwenye vitabu viwili hivyo, na tukawafanya wengi wa Manabii watokanao na kizazi cha Ibrāhīm, amani imshukie, ni katika wao, na tukawaruzuku vitu vizuri miongoni mwa vitu vya kukimu maisha, matunda na vyakula, na tukawafadhilisha juu ya walimwengu wa zama zao

    [17] Na tukawapatia Wana wa Isrāīl Sheria zilizo wazi juu ya halali na haramu, na dalili zenye kutenganisha haki na batili. Hawakutafautiana isipokuwa baada ya kujiwa na elimu na hoja ikasimama juu yao. Na lililowapelekea wafanye hivyo ni lile jambo la kudhulumiana wao kwa wao kwa kutaka ukubwa na uongozi. Hakika Mola wako Atahukumu baina ya wanaotafautiana miongoni mwa Wana wa Isrāīl Siku ya Kiyama katika yale waliokuwa wakitafautiana juu yake duniani. Kwenye maelezo haya pana onyo kwa ummah huu wasifuate mwenendo wao

    [18] Kisha tukakufanya, ewe Mtume, uwe kwenye njia iliyofunuka wazi kuhusu jambo la Dini. Basi fuata Sheria ambayo Mwenyezi Mungu Amekupatia, na usifuate matamanio ya wajinga wa Sheria ya Mwenyezi Mungu, wasiojua haki. Katika hii aya kuna ushahidi mkubwa juu ya ukamilifu wa Dini hii na utukufu wake na ulazima wa kufuata hukumu zake na kutopotoka kuelemea kwenye matamanio ya makafiri na wapotofu

    [19] Hawa waliomshirikisha Mola wao wanaokuita ufuate matamanio yao, hawatakufalia kitu, ewe Mtume, kwa kukuepushia adhabu ya Mwenyezi Mungu iwapo umefuata matamanio yao. Na hakika madhalimu wenye kukiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu miongoni mwa wanafiki, Mayahudi na wasiokuwa hao wanasaidiana wao kwa wao dhidi ya wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na walio watiifu Kwake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwapa ushindi wenye kumcha Mola wao kwa kutekeleza faradhi Zake na kujiepusha na makatazo Yake

    [20] Hii Qur’ani tuliyokuteremshia, ewe Mtume, ni miangaza ya watu kuiona haki na kuipambanua na batili, na kuijua kwayo njia ya usawa, na ni uongofu na rehema kwa watu wenye kuwa na Imani ya yakini juu ya uhakika wa usahihi wake, na kwamba hiyo ni teremsho kutoka kwa Mshindi Mwenye hekima

    [21] Bali je, wanadhani wale wanaotenda maovu na wanaowakanusha Mitume wa Mwenyezi Mungu na kuenda kinyume na amri ya Mola wao na wakamuabudu asiyekuwa Yeye, kuwa tutawafanya wao ni kama wale wanaomuamini Mwenyezi Mungu na wakawasadiki Mitume Wake na wakafanya matendo mema na wakamtakasia Yeye ibada na sio wengine, na tuwasawazishe na wao ulimwenguni na Akhera? Ni uamuzi mbaya huo wao wa kuwsawazisha baina ya waovu na wema kesho Akhera

    [22] Na Mwenyezi Mungu Ameumba mbingu na ardhi kwa haki, uadilifu na hekima , na ili kila nafsi ilipwe huko Akhera kwa ilichokitenda cha kheri au cha shari, na wao hawatadhulumiwa malipo ya matendo yao

    [23] Unamuona vipi, ewe Mtume, yule aliyoyachukuwa matamanio yake akayafanya ndiye Mola wake, akawa hatamani kitu isipokuwa anakifanya, na Mwenyezi Mungu Akampoteza baada ya ujuzi kumfikia na kusimamiwa na hoja, akawa hasikii mawaidha ya Mwenyezi Mungu wala hazingatii kwa mawaidha hayo, na Mwenyezi Mungu akapiga muhuri juu ya moyo wake akawa hafahamu kitu, na Akaweka finiko kwenye macho yake akawa hazioni hoja za Mwenyezi Mungu? Basi ni nani atakayemuongoza kuifikia haki na uongofu baada ya Mwenyezi Mungu kumpoteza? Kwani hamkumbuki, enyi watu mkajua kwamba mwenye kufanywa hivyo na Mwenyezi Mungu hataongoka kabisa na hatapata wa kumsaidia na kumuongoza? Aya hii ndio msingi wa kuonya kwamba matamanio hayafai kuwa ndio msukumo wa Waumini katika matendo yao

    [24] Na wanasema hawa washirikina, “Hakuna maisha isipokuwa haya maisha yetu ya duniani tuliyonayo; hakuna maisha mengineyo,” kwa njia ya kukanusha kufufuliwa baada ya kufa. “Na hakuna kinachotuangamiza isipokuwa kupitiwa na masiku na michana na umri mrefu,“ wakikanusha kuwa wana Mola Anaowatowesha na kuwaangamiza.” Na hawa washirikina hawana ujuzi wowote juu ya hilo, hawana lolote isipokuwa ni kusema kwa kudhania, kufikiria na kuwaza

    [25] Na wanaposomewa, hawa washirikina wakanushaji, aya zetu zilizo waziwazi, huwa hawana hoja isipokuwa ni kutoa maneno yao kumwambia Mtume Muhammad, “Wahuishe, wewe na Waumini, baba zetu waliokufa iwapo nyinyi ni wakweli kwa mnayoyasema.”

    [26] Sema, ewe Mtume, uwaambie hawa washirikina wenye kukanusha kufufuliwa, “Mwenyezi Mungu Aliyetakasika na kutukuka, Atawahuisha duniani kipindi Anachotaka muishi, kisha Atawafisha humo, kisha Atawakusanya mkiwa hai kwenye Siku ya Kiyama isiyokuwa na shaka.» Lakini wengi wa watu hawajui kwamba Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwafisha, kisha kuwafufua Siku ya Kiyama

    [27] Ni ya Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika, mamlaka ya mbingu saba na ardhi kwa kuziumba, kuzimiliki na kuwa ziko chini ya amri Yake. Na siku Kiyama kitakapokuja ambapo wafu watafufuliwa kutoka kwenye makaburi yao na watahesabiwa, hapo watapata hasara wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu na kukataa kile Alichomteremshia Mtume Wake miongoni mwa aya zilizbainika na dalili zilizofunuka wazi

    [28] Utaona, ewe Mtume, Siku ya Kiyama, watu wa kila mila na dini wamepiga magoti, kila ummah wanaitwa kushuhudia kitabu matendo yao, na wataambiwa, «Leo mtalipwa kwa yale mliokuwa mkiyafanya ya kheri au ya shari

    [29] «Hiki ni Kitabu chetu kinatamka kuhusu matendo yenu yote, bila kuongeza wala kupunguza. Sisi tulikuwa tukiwaamrisha Watunzi wenye kudhibiti wayaandike matendo yenu.»

    [30] Ama wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake duniani, wakafuata amri Zake na wakajiepusha makatazo Yake, hao Atawatia Mola wao kwenye Pepo Yake kwa rehema Zake. Kuingia huko ndiko kufaulu kuliko wazi ambako hakuna kufaulu kupita huko

    [31] Na ama wale waliokataa kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Mola wa haki, wakawakanusha Mitume Wake, na wasifuate Sheria Yake kivitendo, basi wataambiwa kwa kukaripiwa na kulaumiwa, «Kwani aya zangu hazikuwa zikisomwa kwenu huko duniani, mkazifanyia kiburi kwa kutozisikiliza na kutoziamini, na mkawa ni watu wenye kushirikisha, mnachuma maasia na hamuamini thawabu wala mateso?»

    [32] Na mnapoambiwa, «Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kuwafufua watu kutoka kwenye makaburi yao ni kweli, na kwamba kipindi cha kusimama Kiyama ni jambo lisilo na shaka, mnasema, ‘Hatujui ni nini Kiyama? Na hatudhani kuwa kitatokea isipokuwa ni kudhania tu, na sisi si wenye uhakika kuwa kipindi hicho cha Kiyama ni chenye kuja.’»

    [33] Na yakawafunukia hawa waliokuwa wakizikanusha aya za Mwenyezi Mungu yale matendo mabaya waliyoyafanya ulimwenguni, na ikawateremkia adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwa ni malipo ya yale waliokuwa wakiyafanyia shere

    [34] Na wakaambiwa hao makafiri, «Leo tutawaacha ndani ya adhabu ya Moto wa Jahanamu, kama vile mlivyoacha kumuamini Mola wenu na kufanya matendo ya kuwafaa katika makutano ya Siku yenu hii, na makao yenu ni Moto wa Jahanamu, na hamtakuwa na wasaidizi wenye kuwaokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu

    [35] «Haya yaliyowafika ya adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kwa sababu ya kuwa nyinyi mlizifanya aya za Mwenyezi Mungu na hoja Zake kuwa shere na mchezo, na likawadanganya nyinyi pambo la uhai wa kilimwengu.» Basi Leo hawatatolewa Motoni wala hawatarudishwa ulimwenguni ili watubie na wafanye mema

    [36] Basi ni za Mwenyezi Mungu, kutakasika ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Peke Yake, shukrani zote kwa neema Zake zisizohesabika kwa viumbe Vyake, Mola wa mbingu na ardhi na Mwenye kuziumba na kuziendesha, Mola wa viumbe Wote

    [37] Na ni wake Peke Yake utukufu, haiba, enzi, utawala, uweza na ukamilifu, mbinguni na ardhini. Na Yeye Ndiye Mshindi Asiyekuwa na mshindani mwenye kushindana na Yeye, Mwingi wa hekima katika maneno Yake, vitendo Vyake, upangaji Wake na Sheria Zake, Ametukuka na kutakasika, hapana Mola isipokuwa Yeye

    Ahqafu

    Surah 46

    [1] “Ḥā, Mīm” Maelezo kuhusu herufi zilizokatwa na kutengwa yametangulia mwanzo wa sura ya Al-Baqarah

    [2] Hii Qur’ani ni teremsho kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mshindi Asiyeshindwa, Mwenye hekima katika uendeshaji mambo Wake na utengezaji Wake

    [3] Hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyo baina ya viwili hivyo isipokuwa kwa haki, si kwa mchezo na upuuzi, bali tumeziumba ili waja wapate kujua ukubwa wa Muumba wa hizo na wamuabudu Peke Yake na wajue kuwa Yeye ni Muweza wa kuwarudishia waja uhai baada ya kufa kwao, na ili wasimamishe haki na uadilifu baina yao, mpaka wakati huo uaojulikana Kwake. Na wale waliokanusha kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Mungu wa Kweli, wanayapa mgongo yale ambayo Qur’ani inawaonya kwayo; wao hawawaidhiki wala hawafikirii

    [4] Sema, ewe Mtume, uwaambie hawa makafiri, “Je, mnawaona waungu na masanamu mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu? Hebu nionesheni, ni sehemu gani waliyoiumba katika ardhi? Au kwani wao wana fungu katika uumbaji mbingu? Nileteeni kitabu kinachotoka kwa Mwenyezi Mungu kabla ya hii Qur’ani au athari iliyosalia ya elimu, iwapo nyinyi ni wakweli katika madai yenu.»

    [5] Hakuna aliyepotea zaidi wala aliye mjinga zaidi kuliko yule anayewaomba waungu wengine badala ya Mwenyezi Mungu, wasioitikia maombi yake kabisa mpaka Siku ya Kiyama, kwa kuwa waungu hao ni wafu au mawe au miti na mfano wa hivyo, na hali hivyo havina habari ya maombi ya huyo mwenye kuviabudu, havina uwezo wa kumnufaisha au kumdhuru

    [6] Na pindi watu watakapokusanywa Siku ya Kiyama ili wahesabiwe na walipwe, wale waungu waliokuwa wakiwaomba duniani watakuwa ni maadui zao, wakiwalaani na kujiepusha nao na kukanusha kuwa wao walikuwa wanajua kuwa wale wanawaabudu wao

    [7] Na washirikina wanaposomewa aya zetu zilizobainishwa waziwazi, wanasema hao makafiri wakati ule Qur’ani inapowajia, “Huu ni uchawi waziwazi.”

    [8] Au je wanasema hawa washirikina kwamba Muhammad ameizua Qur’ani? Waambie, ewe mtume, “Iwapo mimi nimemzulia Mwenyezi Mungu hii Qur’ani, basi nyinyi hamuwezi kunikinga mimi na adhabu ya Mwenyezi Mungu kitu chochote Akiwa atanitesa kwa hilo. Yeye, kutakasika ni Kwake, ni Mjuzi zaidi wa kile mnachokisema juu ya hii Qur’ani kuliko kitu chochote kingine. Inatosha kuwa Mwenyezi Mungu ni Shahidi juu yangu mimi na nyinyi, na Yeye Ndiye Mwingi wa msamaha kwa waja Wake, ni Mwingi wa rehema kwa waja Wake Waumini.”

    [9] Sema, ewe Mtume, uwambie washirikina wa watu wako, “Sikuwa ni wa mwnzo wa wajumbe wa Mwenyezi Mungu kwa viumbe Wake. Na sijui Atakalofanya Mwenyezi Mngu kwangu wala kwenu hapa duniani. Sifuati katika yale ninayowaamrisha nyinyi na katika yale ninayoyafanya isipokuwa wahyi wa Mwenyezi Mungu Anaoniletea mimi. Na sikuwa mimi isipokuwa ni mwenye kuonya ambaye uonyaji wake uko wazi.»

    [10] Sema , ewe Mtume, uwaambie washirikina wa watu wako, “Nipasheni habari: ikiwa hii Qur’ani inatoka kwa Mwenyezi Mungu na mkaikanusha, na hali ameshuhudia shahidi kati ya Wana wa Isrāīl, kama ‘Abdullāh bin Salām, kwa mfano wa hii Qur’ani, nayo ni yaliyomo ndani ya Taurati ya kusadikisha unabii wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, akaiamini na akayafuata kivitendo yaliyokuja ndani ya Qur’ani, na nyinyi mkakanusha hilo kwa njia ya kiburi. Basi ni upi huu isipokuwa ni udhalimu mkubwa na ukafiri mwingi?” Hakika Mwenyezi Mungu Hawaongozi kwenye Uislamu na kuifikia haki wale watu waliojidhulumu kwa kumkanusha Mwenyezi Mungu

    [11] Na wale walioukanusha unabii wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, walisema wakiwaambia wale waliomuamini, “Lau huko kumuamini Muhammad kwa aliyokuja nayo ni kheri hamngalitutangulia kuamini.” Na kwa kuwa hawakujiongoza na hii Qur’ani wala hawakunufaika na ukweli uliyomo ndani yake, watasema, “Huu ni urongo uliopokewa kwa watu wa kale.”

    [12] Na kabla ya hii Qur’ani, tuliiteremsha Taurati ikiwa ni muongozo kwa Wana wa Isrāīl waiandame na ni rehema kwa wenye kuiamini na kuifuata kivitendo. Na hii Qur’ani inasadikisha Vitabu vilivyokuwa kabla yake. Tumeiteremsha kwa lugha ya Kiarabu ili iwaonye wale waliozidhulumu nafsi zao kwa kukanusha na kuasi. Na bishara njema ni ya wale waliomtii Mwenyezi Mungu na wakafanya wema katika Imani yao na utiifu wao duniani

    [13] Hakika wale waliosema, “Mola wetu ni Mwenyezi Mungu” kisha wakalingana sawa katika kumuamini, basi hao hawatakuwa na khofu ya babaiko la Siku ya Kiyama na vituko vyake, wala hawatasikitka juu ya hadhi za duniani walizoziacha nyuma yao

    [14] Hao ni wa watu wa Peponi, watakaa humo milele kwa rehema za Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, juu yao , na kwa yale waliyoyatanguliza ya matendo mema katika dunia yao

    [15] Na tumemuusia binadamu asuhubiane na wazazi wake wawili kwa vizuri, kwa kuwatenda wema wanapokuwa hai na baada ya kufa kwao. Kwa kuwa mamake alimbeba akiwa mwana wa matumboni kwa mashaka na tabu, na akamzaa kwa mashaka na tabu pia. Na muda wa kubeba mimba yake na mpaka kumaliza kumnyonyesha ni miezi thelathini. Katika kutaja mashaka haya anayoyabeba mama, na siyo baba, pana dalili kuwa haki yake juu ya mtoto wake ni kubwa zaidi kuliko haki ya baba. Mpaka alipofikia binadamu upeo wa nguvu zake za kimwili na kiakili na akafikia miaka arubaini, huwa akimuomba Mola wake kwa kusema, “Mola wangu! Niafikie nishukuru neema zako ulizonineemesha mimi na wazazi wangu wawili, na nijaalie nifanye matendo mema unayoridhika nayo, na unisuluhishie wanangu. Hakika mimi nimetubia dhambi zangu kwako, na hakika mimi ni miongoni mwa wanyenyekevu kwako kwa utiifu na ni miongoni mwa wenye kujisalimisha kufuata amri zako na kuepuka makatazo yako, wenye kuandama hukumu yako.”

    [16] Hao ndio ambao tutayapokea kutoka kwao mazuri zaidi ya matendo mema waliyoyafanya, na tutasamehe dhambi zao, wakiwa ni miongoni mwa watu wa Peponi. Ahadi hii tuliyowaahidi ni ahadi ya ukweli na haki isiyokuwa na shaka

    [17] Na yule aliyesema kuwaambia wazazi wake wawili walipomlingania kwenye kumuamini Mwenyezi Mungu na kuamini kuwa kuna kufufuliwa, “ Ubaya wenu! Je mnaniahidi kuwa nitatolewa kaburini mwangu nikiwa hai na hali kwamba makame ya ummah kabla yangu yashapita, na hakuna hata mmoja miongoni mwao aliyefufuliwa?” Na hali wazazi wake wanamuomba Mwenyezi Mungu Amuongoze na huku wakimwambia, “Ole wako! Amini na usadiki na ufanye matendo mema, hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli isiyokuwa na shaka.” Hapo awaambie, “Hayakuwa haya mnayoyasema isipokuwa ni mambo ya urongo waliyoyaandika watu wa mwanzo, yamenukuliwa kwenye vitabu vyao.”

    [18] Hao ambao sifa zao ni hizi imepasa juu yao adhabu ya Mwenyezi Mungu, na yamewashukia mateso Yake na hasira Zake, wakiwa ni katika jumla ya ummah waliopita kabla yao, miongoni mwa majini na binadamu, waliokuwa kwenye ukafiri na ukanushaji. Kwa kweli wao ni wenye hasara kwa kuchagua upotevu na kuacha uongofu, na kuchagua adhabu na kuacha starehe

    [19] Na kila kundi la watu wema na watu waovu watakuwa tabaka mbalimbali mbele ya Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama, kwa matendo yao waliyoyatenda duniani, kila mmoja kulingana na daraja yake, ili Mwenyezi Mungu Awatekelezee malipo ya matendo yao. Na wao hawatadhulumiwa kwa kuongezewa maovu yao wala kupunguziwa mema yao

    [20] Na Siku ambayo wataorodheshwa Motoni wale waliokufuru ili kuadhibiwa na waambiwe kwa kulaumiwa, “Mmeyapoteza mazuri yenu katika uhai wenu wa duniani na mmestarehe nayo. Basi leo, enyi makafiri, mtalipwa adhabu ya hizaya na unyonge ndani ya Moto, kwa kuwa mlikuwa na kiburi kwenye ardhi bila ya haki na kwa kuwa mlitoka kwenye utiifu wa Mwenyezi Mungu.”

    [21] Na kumbuka, ewe Mtume, Nabii wa Mwenyezi Mungu Hūd, ndugu yao kina 'Ād kinasaba na siyo kidini, alipowaonya watu wake kuwa watashukiwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu wakiwa kwenye nyumba zao hapo Aḥqāf (mahali kwenye mchanga mwingi) kusini mwa Arabuni. Na kwa hakika wamepita Mitume wakawaonya watu wao kabla ya Hūd na baada yake wakiwaambia, «Msimshirikishe Mwenyezi Mungu na kitu chochote mnapomuabudu. Mimi nawachelea nyinyi adhabu ya Mwenyezi Mungu katika Siku yenye kituko kikubwa , nayo ni Siku ya Kiyama.»

    [22] Wakasema, «Je, umetujia kwa ulinganizi wako ili kutuepusha na ibada ya Mola wetu? Basi tuletee hiko unachotuahidi cha adhabu, iwapo wewe ni katika watu wa ukweli wa kauli yako na ahadi yako.»

    [23] Hūd, amani imshukie, akasema, “Hakika ujuzi wa adhabu mliyoahidiwa uko kwa Mwenyezi Mwenyezi Mungu, na kwa kweli mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, ninawafikishia ujumbe Alionituma nao, na lakini mimi ninawaona kuwa ni watu mlio wajinga kwa kuifanyia haraka adhabu na kuwa na ujasiri juu ya Mwenyezi Mungu

    [24] Walipoiona adhabu walioifanyia haraka imejitokeza juu ikielekea kwenye mabonde yao, walisema, “Hiki ni kiwingu chenye kutunyesheza mvua.” Hūd, amani imshukie, aliwaambia, «Hiki si kiwingu cha mvua na rehema kama mlivyodhania, bali hiki ni kiwingu cha adhabu mliyoitaka kwa haraka, huo ni upepo ambao ndani yake muna adhabu yenye uchungu na yenye kuumiza

    [25] «Unaangamiza kila kitu unachokipitia katika vitu ambavyo ulitumwa uviangamize kwa amri ya Mola wake na matakwa Yake.» Wakawa hakuna kinachoonekana chochote katika miji yao isipokuwa nyumba zao walizokuwa wakizikaa. Mfano wa malipo haya ndiyo tunayowalipa makafiri kwa sababu ya uhalifu wao na kupita kiasi kwao

    [26] Na tuliwarahisishia hao 'Ād sababu za kumakinika duniani kwa namna ambayo hatukuwamakinisha nyinyi, enyi Makureshi, na tukawafanya wawe na masikio ya wao kusikia na macho ya wao kuonea na nyoyo za wao kufahamia, wakavitumia katika mambo yanayomfanya Mwenyezi Mungu Awe na hasira nao. Na hilo halikuwafalia kitu chochote kwa kuwa walikuwa wakikanusha hoja za Mwenyezi Mungu, na hiyo adhabu ambayo walikuwa wakiifanyia shere na kuiharakisha. Hili ni onyo kutoka kwa Mwenyezi Mungu, imetukuka shani Yake, na ni tahadharisho kwa wenye kukufuru

    [27] Hakika tuliiangamiza miji iliyokuwa pambizoni mwenu, enyi watu wa Makkah, kama ile ya kina 'Ād na Thamūd, tukazifanya kuta za nyumba za miji hiyo zimeanguka na kulalia sakafu zake zilizovunjika, na tuliwabainishia watu wa miji hiyo aina za hoja na dalili wapate kurudi nyuma na kuyaacha yale waliokuwa nayo ya ukanushaji Mwenyezi Mungu na aya Zake

    [28] Basi si wangaliwasaidia wao, hao tuliowaangamiza miongoni mwa ummah waliopita, waungu wao ambao walichukua kule kuwaabudu ni ibada ya wao kujikurubisha kwa Mola wao, ili wawaombee mbele Yake. Lakini waungu wao waliwapotea, hawakuwaitikia wala hawakuwatetea. Huo ni urongo wao tu na uzushi walioupanga wa kuwafanya wao ni waungu

    [29] Na kumbuka, ewe Mtume, pindi tulipokutumia kundi la majini kusikiliza Qur’ani kutoka kwako. Walipohudhuria, na Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, yuwasoma, waliambiana wao kwa wao, «Nyamazeni tusikilize Qur’ani! Na Mtume Alipomaliza kusoma Qur’ani, na wao wakawa wameielewa na ikawa imewaathiri, walirudi kwa majini wenzao wakawaonya na kuwahadharisha adhabu ya Mwenyezi Mungu wasipoamini

    [30] walisema, «Enyi jamaa zetu! Sisi tumesikia Kitabu kilichoteremshwa baada ya Mūsā, chenye kusadikisha Vitabu vya Mwenyezi Mungu vlivyokuwa kabla yake, ambavyo Mwenyezi Mungu Ameviteremsha kwa Mitume Wake, (Kitabu) ambacho kinaongoza kwenye haki na usawa na kwenye njia sahihi iliyonyoka

    [31] «Enyi jamaa zetu! Muitikieni Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad kwa kile anachowaitia, na muaminini yeye na myafuate kivitendo yale aliyoyaleta, Mwenyezi Mungu Atawasamehe dhambi zenu na Atawaokoa na adhabu yenye uchungu inayoumiza

    [32] «Na asiyemuitikia Mtume wa Mwenyezi Mungu katika yale aliyoyalingania, basi yeye hatamshinda Mwenyezi Mungu katika ardhi Akitaka kumuadhibu, wala hatakuwa na wasaidizi badala ya Mwenyezi Mungu, wenye kumkinga na adhabu Yake. Hao watakuwa wametoka nje ya haki waziwazi

    [33] Je, wameghafilika na wasijue kwamba Mwenyezi Mungu, Aliyeumba mbingu na ardhi pasi na mfano uliotangulia na bila kuelemewa na kuziumba, ni Muweza wa kuhuisha wafu ambao Aliwaumba hapo mwanzo? Ndio, hilo ni jambo jepesi kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Ambaye hakuna chochote kinachomshinda. Hakika Yeye kwa kila jambo ni Muweza

    [34] Na Siku ya Kiyama, wataorodheshwa waliokufuru juu ya Moto wa Jahanamu ili waadhibiwe na waambiwe, «Je, hii adhabu si kweli?». watajibu kwa kusema, «Ndio. Tunaapa kwa Mola wetu kuwa hii ndiyo kweli.» Hapo waambiwe, «Basi onjeni adhabu kwa kuwa mlikuwa mkiikataa adhabu ya Moto na kuikanusha duniani.»

    [35] Basi vumilia, ewe Mtume, kwa yanayokupata ya makero ya watu wako wenye kukukanusha kama vile walivyovumilia Mitume wenye nia thabiti kabla yako wewe, nao, kwa kauli mashuhuri, ni Nūḥ, Ibrāhīm, Mūsā na Īsā, na wewe ni miongoni mwao, wala usiwafanyie haraka watu wako ya kuadhibiwa. Kwani itapotokea na wakaiona, watajihisi kama kwamba hawakukaa duniani isipokuwa muda mchache wa mchana. Haya ni mafikisho kwao na kwa wasiokuwa wao. Na haangamizwi kwa adhabu ya Mwenyezi Mungu isipokuwa watu waliotoka nie ya amri Yake na twaa Yake

    Muhammad

    Surah 47

    [1] Wale waliokataa kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye Peke Yake Mungu wa kweli Asiye na mshirika, na wakawazuia watu na Dini Yake, Mwenyezi Mungu Atazifuta amali zao na kuzipomosha na Atawapa usumbufu kwa sababu ya amali zao hizo

    [2] Na wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na wakafuata Sheria Zake na wakaamini Kitabu Alichomteremshia Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, nacho ndio ukweli usiokuwa na shaka kutoka kwa Mola wao, Mwenyezi Mungu Atawasamehe na Atawafinikia maovu waliyoyafanya na hatawatesa kwa maovu hayo na Atawatengezea mambo yao duniani na Akhera

    [3] Kupoteza huko na kuongoza, sababu yake ni kwamba wale waliokufuru wamemfuata Shetani wakamtii, na kwamba wale walioamini walimfuata Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na yale aliyokuja nayo ya mwangaza na uongofu. Kama Alivyobainisha Mwenyezi Mungu vile Anavyoyafanya mapote mawili ya watu wa ukafiri na watu wa Imani kwa wanavyostahili, vilevile Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika, Anawapigia watu mifano yao, ili kila watu wanaofanana wa aina moja wakutamane na wale wanaonasibiana nao

    [4] Basi mkipambana, enyi Waumini, na wale waliokufuru katika viwanja vya vita, piganeni nao kidhati na mzipige shingo zao. Hata mtakapowadhoofisha kwa kuwaua kwa wingi na mkazivunja nguvu zao, wafungeni kisawasawa wale mnaowateka. Kisha basi ima muwasamehe kwa kuwafungua na kuwaacha bila kutoa fidia badala yake, au wajikomboe kwa kutoa fidia, au watiwe utumwani au wauawe. Na endeleeni kufanya hivyo mpaka vita vimalizike. Hiyo ndiyo hukumu iliyotajwa ya kuwatahini Waumini kwa makafiri na ushindi kuzunguka baina yao. Na lau Mwenyezi Mungu Angalitaka wangalipata ushindi Waumini bila ya vita, lakini Mwenyezi Mungu Amejaalia mateso yao yawe mikononi mwenu ndipo Akaweka sheria ya jihadi ili Awajaribu nyinyi kwa wao na Ainusuru kwa sababu yenu Dini Yake. Na wale Waumini waliouawa katika njia ya Mwenyezi Mungu, Hatayapomosha Mwenyezi Mungu malipo mema ya matendo yao

    [5] Atawaafikia siku za uhai wao duniani wawe watiifu Kwake na wafanye matendo ya kumridhi, Awatengeze hali zao, mambo yao na malipo mema yao duniani na Akhera

    [6] na Awatie Peponi ambayo Aliwajulisha na Akawasifia, na Akawaafikia kusimama kuyafanya yale Ailyowaamrisha, na miongoni mwayo ni kufa shahidi katika njia Yake, kisha atawajulisha wao mashukio yao huko Peponi watakapoingia humo

    [7] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo, mkiinusuru Dini ya Mwenyezi Mungu kwa kupigana jihadi katika njia Yake na kuhukumu kwa Kitabu Chake na kufuata amri Zake na kujiepusha na makatazo Yake, Mwenyezi Mungu Atawapa ushindi juu ya maadui zenu na Atazithibitisha nyayo zenu wakati wa kupigana

    [8] Na wale waliokanusha, basi maangamivu ni yao, na Mwenyezi Mungu Atazifuta thawabu za matendo yao mema

    [9] Hayo ni kwa sababu wao walikichukia Kitabu cha Mwenyezi Mungu kilichoteremshwa kwa Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wakakikanusha, na Mwenyezi Mungu akayatangua matendo yao kwa kuwa yalikuwa katika kumtii Shetani

    [10] Kwani hawakwenda makafiri hawa kwenye ardhi ya Mwenyezi Mungu wakayazingatia yale yaliyowapata ummah waliopita ya mateso? Mwenyezi Mungu Aliyavunjavunja majumba yao. Na makafiri hawa watakuwa na mwisho kama huo uliowafikia ummah hao

    [11] Hilo tulilowafanyia watu wa mapote mawili: pote la Imani na pote la ukafiri, ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Msimamizi wa Waumini na mwenye kuwanusuru, na kuwa makafiri hawana mwenye kuwasimamia wala kuwanusuru

    [12] Hakika Mwenyezi Mungu Atawatia, wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafanya matendo mema, kwenye mabustani ya Pepo ambayo inapita mito chini ya miti yake ikiwa ni takrima kwao. Na mfano wa wale waliokanusha katika kula kwao na kujistarehesha kwao na ulimwengu, ni kama mfano wa mifugo miongoni mwa wanyama ambao hawana hamu isipokuwa kula nyasi, hawafikirii lingine. Na Moto wa Jahanamu ndio makao yao na maskani

    [13] Na wengi miongoni mwa watu wa mijini walikuwa wana nguvu zaidi kuliko watu wa mji wako, ewe Mtume, ambao ni Makkah, waliokutoa watu wake humo. Watu wa miji hiyo tuliwaangamiza kwa adhabu za aina mbalimbali. Hawakuwa na msaidizi wa kuwanusuru kutokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu

    [14] Je yule aliyekuwa na ushahidi ulio wazi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ujuzi kuwa Yeye ni Mmoja, ni kama yule ambaye Shetani amempambia matendo yake maovu na akafuata yale ambayo nafsi yake ilimuita iyafuate ya kumuasi Mwenyezi Mungu na kumuabudu asiyekuwa Yeye bila ya hoja wala ushahidi? Hawalingani

    [15] Sifa ya Pepo ambayo Mwenyezi Mungu Amewaahidi wachamungu: ndani yake kuna mito mikubwa ya maji yasiyobadilika, na mito ya maziwa yasyogeuka tamu yake, na mito ya shizi ambayo wanaionea ladha wenye kuinywa, na mito ya asali iliyosafishwa isiyo na taka. Na wachamungu hawa watapata ndani ya hiyo pepo matunda yote ya aina tafauti na mengineyo. Na kubwa kuliko hayo ni kule kusitiriwa na kusamehewa dhambi zao. Basi je, wale watakaokuwa ndani ya Pepo hiyo ni kama wale watakaokaa Motoni bila kutoka humo na wakanyweshwa maji yaliyo moto sana hadi ya mwisho yakawakata tumbo zao

    [16] Miongoni mwa hawa wanafiki kuna wanaokusikiliza bila ya kuelewa, kwa madharau na kupuuza, mpaka wanapoondoka kutoka kwenye kikao chako, huwa wakisema wakiwaambia wale waliohudhuria kikao chako kati ya wale wenye ujuzi wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa njia ya shere, «Amesema nini Muhammad hivi sasa?» Hao ndio wale ambao Mwenyezi Mungu Amezipiga muhuri nyoyo zao, zikawa haziielewi haki wala hawaongokei kuifikia, na wakayafuata matamanio yao katika ukafiri na upotevu

    [17] Na wale walioongoka kuifuata haki, Mwenyezi Mungu Aliwaongezea uongofu , na kwa hivyo uongofu wao ukapata nguvu na Akawaafikia kwenye uchamungu na akaufanya sahali kwao

    [18] Wakanushaji hawa hawangojei isipokuwa wakati wa Kiyama ambao wameahidiwa kuwa utawajia kwa ghafla. Kwani alama zake zishajitokeza na wao hawakunufaika nazo. Basi watapata wapi kukumbuka wakati wa Kiyama utakapowajia

    [19] Basi jua, ewe Nabii, kwamba hakuna mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, na utake msamaha wa dhambi zako, na uwaombee msamaha Waumini wa kiume na Waumini wa kike. Na Mwenyezi Mungu anazijua harakati zenu mnapoangaza mchana na mahali pa kutulia kwenu mnapolala usiku

    [20] Na wale wanamuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wanasema, «Basi si iteremshwe sura kutoka kwa Mwenyezi Mungu ituamrishe kupigana jihadi na wakanushaji.» Na inapoteremshwa sura iliyoimarika kwa maelezo na mambo ya lazima na ikatajwa jihadi ndani yake, utawaona wale ambao mna shaka ndani ya nyoyo zao juu ya Dini ya Mwenyezi Mungu na unafiki wanakuangalia, ewe Nabii, maangalizi ya mtu ambaye amefinikwa na kicho cha kufa

    [21] Basi lililo bora kwa hawa ambao ndani ya nyoyo zao mna maradhi wamtii Mwenyezi Mungu na wasema neno linaoafikiana na Sheria. Vita vinapopasa na ikaja amri ya Mwenyezi Mungu kuilazimisha, hawa wanafiki wanachukia hilo. Na lau wao wangalikuwa wakweli kwa Mwenyezi Mungu katika kuamini na kutenda mema, hilo lingalikuwa bora kwao kuliko kufanya maasia na kuenda kinyume

    [22] Huenda nyinyi mkikipa mgongo Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Mwenendo wa Nabii wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, mkaja kumuasi Mwenyezi Mungu katika ardhi, mkamkanusha Yeye, mkamwaga damu na mkakata vizazi vyenu

    [23] Hao ndio wale ambao Mwenyezi Mungu Amewaepusha na rehema Yake Akawafanya wasiyasikie yanayowanufaisha wala wasiyaone na zisiwafunukie hoja za Mwenyezi Mungu pamoja na kuwa ni nyingi

    [24] Je, si wayazingatie mawaidha ya Qur’ani wanafiki hawa na wazifikirie hoja zake? Lakini nyoyo hizi zimefungwa, hakuna kitu cha hii Qur’ani kinachozifikia, hivyo basi haziyatii akilini mawaidha ya Mwenyezi Mungu na mazingatio yake

    [25] Hakika ya wale waliyorudi nyuma wakaacha uongofu na Imani na wakageuka kwa visigino vyao wakimkanusha Mwenyezi Mungu baada ya haki kuwafunukia, (hao) Shetani amewapambia makosa yao na akawanyoshea matumaini ya kuishi duniani

    [26] Kule kuwanyoshea wao mpaka wakolee kwenye ukafiri, ni kwa kuwa wao walisema kuwaambia Mayahudi waliokanusha Aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, «Tutawatii katika baadhi ya mambo ambayo yako kinyume na amri ya Mwenyezi Mungu na amri ya Mtume Wake.» Na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Anayajua wanayoyaficha na wanayoydhihirisha. Basi Muislamu ajihadhari na kumtii asiyekuwa Mwenyezi Mungu katika mambo yaliyo kinyume na amri ya Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika, na amri ya Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [27] Basi itakuwa vipi hali yao watakapozikamata Malaika roho zao na huku wanawapiga nyuso zao na migongo yao

    [28] Adhabu hiyo waliyostahili na wakaipata ni kwa kuwa wao waliyafuata mambo yanayomfanya Mwenyezi Mungu Awakasirikie ya kumtii Shetani na wakayachukia yale yanayomfanya Awe radhi nao ya matendo mema, na miongoni mwayo ni kupigana na wakanushaji, baada ya kulifanya hilo ni lazima juu yao, ndipo Mwenyezi Mungu Akazibatilisha thawabu za matendo yao, miongoni mwa sadaka, kuunga kizazi na yasiyokuwa hayo

    [29] Au kwani wanadhani hao wanafiki kuwa Mwenyezi Mungu Hatovitoa vile vilivyomo ndani ya nyoyo zao vya uhasidi na kuuchukia Uislamu na wafuasi wake? Ndio, Mwenyezi Mungu Atamtenganisha mkweli kutokana na mrongo

    [30] Na lau tungalitaka, ewe Nabii, tungalikuonesha hao watu wenyewe, ukawatambua kwa alama zilizo wazi kwao. Na kwa hakika utawajua kutokana na maneno yao yaliyodhihirika yenye kuonyesha malengo yao. Na kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, hakuna chochote kinachofichamana cha matendo ya wanaomtii wala matendo ya wanaomuasi, na Atamlipa kila mmoja kwa anachostahili

    [31] Na tutawatahini nyinyi, tena tutawatahini, enyi Waumini, kwa kupambana na maadui wa Mwenyezi Mungu na kupigana nao jihadi mpaka yajitokeze yale Aliyoyajua Mwenyezi Mungu tangu kale, ili tuwatenge watu wa jihadi kati yenu na uvumilivu wa kupigana na maadui wa Mwenyezi Mungu na tuyatahini maneno yenu na matendo yenu, na hapo adhihirike mkweli miongoni mwenu kutokana na mrongo

    [32] Hakika ya wale waliokataa kuwa Menyezi Mungu Ndiye Mola wa haki Peke Yake Asiye na mshirika, wakawazuia watu na Dini Yake, wakaenda kinyume na Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na wakampiga vita baada ya wao kujiwa na hoja na alama za kuwa yeye ni Nabii kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hawataidhuru Dini ya Mwenyezi Mungu kitu chochote na Atayatangua malipo ya matendo yao waliyoyafanya duniani, kwa kuwa wao hawakutaka kwa matendo hayo radhi za Mwenyezi Mungu Aliyetukuka

    [33] Enyi wale mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafuata Sheria Zake kivitendo! Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume katika maamrisho yao na makatazo yao, na msiyatangue malipo ya matendo yenu kwa kukanusha na kufanya maasia

    [34] Hakika ya wale waliokataa kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Mola wa haki Peke Yake Asiye na mshirika na wakawazuia watu na Dini Yake, kisha wakafa wakiwa katika hali hiyo, Mwenyezi Mungu Hatawasamehe, na Atawapa adhabu ikiwa ndio mateso yao kwa ukanushaji wao, na Atawafedhehesha mbele ya halaiki ya watu

    [35] Basi msiwe wanyonge, enyi wenye kumuamini Mwenyezi Mugu na Mtume Wake, wa kujiepusha na kupambana na washirikina, mkaogopa kupigana nao na mkawaita kwenye suluhu na masikilizano na hali ya kuwa nyinyi ndio wenye ushindi na nguvu juu yao, na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Yuko pamoja na nyinyi kwa kuwanusuru na kuwapa nguvu. Hapa kuna bishara kubwa ya kupatiwa ushindi na kusaidiwa juu ya maadui. Na Mwenyezi Mungu Hatawapunguzia nyinyi malipo mema ya matendo yenu

    [36] Hakika uhai wa duniani ni mchezo na udanganyifu. Na mtakapomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkamuogopa Mwenyezi Mungu kwa kutekeleza mambo Aliyoyafanya ni ya lazima na kujiepusha na mambo ya kumuasi, Atawapa malipo mema ya matendo yenu, na Hatawataka myatoe mali yenu yote katika Zaka, Anachowataka mfanye ni mtoe sehemo ya hayo mali

    [37] Akiwa Atawataka myatoe mali yenu na Akawa Atawakariria na kuwasumbua, mtayafanyia uchoyo na mtakataa kuyatoa, na hapo Atakapowataka myatoe mali yenu Atayatoa nje machukivu yaliyo ndani ya nyoyo zenu

    [38] Haya nyini, enyi Waumini, mnaitwa kutoa kwenye kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na kuinusuru Dini Yake. Basi miongoni mwenu kuna anayefanya uchoyo kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu. Na mwenye kufanya uchoyo huwa anajifanyia uchoyo nafsi yake. Na Mwenyezi Munmgu, Aliyetukuka, Ndiye Mkwasi wa kutowahitajia nyinyi, na nyinyi ndio mnaomhitajia Yeye. Na mkipa mgongo mkaacha kumuamini Mwenyezi Mungu na kufuata amri Zake, Atawaangamiza na Atawaleta watu wengine, na kisha wasiwe ni kama nyinyi katika kuzipa mgongo amri za Mwenyzi Mungu, bali wao watamtii Yeye na kumtii Mtume Wake na watapigana jihadi katika njia Yake kwa mali yao na nafsi zao

    Ushindi

    Surah 48

    [1] Sisi tumekufungulia wewe, ewe Mtume, ufunguzi ulio waziwazi, ambao ndani yake Mwenyezi Mungu Ataipa nguvu Dini Yako na Atakupa ushindi juu ya maadui wako, nao ni mapatano ya Ḥudaybiyah ambayo kwayo watu walikuwa katika hali ya amani, na likapanuka duara la ulinganizi wa Dini ya Mwenyezi Mungu, na watu wakaingia kwenye Dini ya Mwenyezi Mungu mapote kwa mapote. Kwa hivyo, Mwenyezi Mung Aliyaita mapatano hayo “Ufunguzi uliofunuka” yaani uliokuwa wazi wenye kujitokeza

    [2] Tumekufungulia ufunguzi huo na tukakufanyia sahali, ili Mwenyezi Mungu Akusamehe dhambi zako zilizotangulia na zitakazofanyika baadaye, kwa sababu ya utiifu mwingi ulioufanya unaotokana na ufunguzi huu na kwa usumbufu ulioubeba, na ili Akutimizie neema Zake kwako kwa kuipa ushindi Dini yako

    [3] Akunusuru juu ya maadui wako na Akuongoze njia ya Dini iliyolingana sawa isiyopotoka , na Mwenyezi Mugu Akunusuru kwa nguvu kwa namna ambayo Uislamu hautakuwa mnyonge

    [4] Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu Aliyeteremsha utulivu ndani ya nyoyo za wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake katika siku ya Ḥudaybiyah zikatulia na yakini ikajidhatititi ndani ya hizo nyoyo, ili wazidi kumuamini Mwenyezi Mungu na kumfuata Mtume Wake pamoja na kuamini kwao na kufuata kwao. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Ana askari wa mbinguni na ardhini, Anawanusuru kwa askari hao waja Wake Waumini. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi sana wa maslahi ya viumbe Vyake, ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji mambo Wake na utengezaji Wake

    [5] Apate kuwaingiza Waumini wa kiume na Waumini wa kike kwenye mabustani ya Peponi ambayo mito inapita chini ya miti yake na majumba yake ya fahari, hali ya kukaa humo milele, na Awafutie baya walilolifanya asiwaadhibu kwalo. Malipo hayo kwa Mwenyezi Mungu ndio kuokoka na kila kero na ndio kupata kila linalotafutwa

    [6] Na Apate kuwaadhibu wanafiki wa kiume na wanafiki wa kike na washirikina wa kiume na washirikina wa kike wanaomdhania Mwenyezi Mungu dhana mbaya ya kuwa yeye Hatamnusuru Mtume na waliokuwa pamoja na yeye dhidi ya maadui wao na kuwa Yeye Hataipa ushindi Dini Yake. Basi juu ya hao utazunguka mzunguko wa adhabu na kila kilicho kibaya kwao, na Amewaandalia moto wa Jahanamu; na mashukio mabaya ya mtu kuishia ni hayo

    [7] Na Mwenyezi Mungu, Alyetakasika na kutukuka, Ana askari wa mbinguni na ardhini. Anawanusuru kwa askari hao waja Wake Waumini. Na Mwenyezi Mungu ni Mshindi Mwenye uweza juu viumbe Vyake, ni Mwingi wa hekima katika kuendesha mambo yao

    [8] Hakika yetu sisi tumekutumiliza, ewe Mtume, uwe shahidi kwa umati wako juu ya ufikishaji ujumbe, uwabainishie kile ulichotumilizwa kwao, uwabashirie Pepo wanaokutii na uwaonye mateso ya sasa na ya baadaye

    [9] mpate kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, mumnusuru Mwenyezi Mungu kwa kuinusuru Dini Yake, mumtukuze na mumtakase mwanzo wa mchana na mwisho wake

    [10] Hakika ya hao wanaokupa mkono , ewe Mtume, wa ahadi ya kupigana hapo Ḥudaybiyah, wao kwa kweli wanampa mkono wa ahadi Mwenyezi Mungu na wanafanya mapatano na Yeye kwa kutaka Pepo Yake na radhi Zake. Mkono wa Mwenyezi Mungu uko juu ya mikono yao. Hivyo basi Yupo na wao anayasikia maneno yao, Anawaona mahali walipo na Anayajua mambo yao ya ndani na ya nje. Basi mwenye kuivunja ahadi yake aliyoitolea mkono, maangamivu ya jambo hilo yatamrudia mwenyewe; na atakayetekeleza ahadi aliyomuahidi Mwenyezi Mungu ya kuvumilia wakati wa mapambano na adui katika njia ya Mwenyezi Mungu na kumnusuru Nabii wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, Mwenyezi Mungu Atampa malipo mema mengi, nayo ni Pepo. Katika aya pana kuthibitisha sifa ya mkono kwa Mwenyezi Mungu kwa namna inayonasibiana na Yeye, Aliyetakasika, bila kufananisha wala kueleza vile ulivyo

    [11] Watakwambia, ewe Nabii, wale mabedui waliojikalisha nyuma wasitoke na wewe kwenda Makkah utakapowalaumu, «Tulishughulishwa na mali yetu na watu wa nyumbani kwetu, basi tuombee Mola Wako Atusamehe kosa letu la kujikalisha nyuma.» Wanasema hayo kwa ndimi zoa na hayana ukweli wowote maneno yao ndani ya nyoyo zao. Waambie, «Ni nani atakayemiliki kuwafanyia chochote kwa Mwenyezi Mungu iwapo Amewatakia nyinyi kheri au shari?» mambo sivyo kama vile hawa wanafiki wanavyodhania kuwa Mwenyezi Mungu hayajui yale ya unafiki yaliyomo ndani yao. Bali kwa hakika, Yeye Mwenyezi Mungu ni Mtambuzi wa mnayoyafanya, hakuna chochote kinachofichamana Kwake katika matendo ya viumbe Vyake

    [12] Pia mambo sivyo kama mlivyodai kuwa mlishughulishwa na mali na watu wa nyumbani, bali kwa kweli nyinyi mlidhani kuwa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na wale Maswahaba waliokuwa na yeye wataangamia na hawatarudi kwenu kabisa, na Shetani aliwapambia hilo ndani ya nyoyo zenu. Na pia mlidhani dhana mbaya kuwa Mwenyezi Mungu Hatampa ushindi Nabii Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na Maswahaba wake juu ya maadui wao, na mlikuwa ni watu wenye kuangamia msiokuwa na kheri yoyote

    [13] Na asiyemuamini Mwenyezi Mungu na yale aliyokuja nayo Mtume Wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na akazifuata Sheria Zake kivitendo, basi huyo ni kafiri anayestahili kuteswa, kwani hakika sisi tumewaandalia makafiri adhabu yenye kuunguza ndani ya Moto

    [14] Ni ya Mwenyezi Mungu mamlaka ya mbingu na ardhi na vilivyoko baina ya hivyo viwili, Anamsamehe, kwa rehema Zake, Anayemtaka Akamfinikia dhambi zake, na Anamuadhibu, kwa uadilifu Wake, Anayemtaka. Na Mwenyezi Mungu, kutakasika na kutukuka ni Kwake, ni Mwingi wa kusamehe kwa anayetubia Kwake, ni Mwingi huruma kwake

    [15] Watasema wale walioachwa nyuma utakapoondoka, ewe Nabii, wewe na Maswahaba wako kuelekea kwenye ngawira za Khaybar ambazo Mwenyezi Mungu Aliwaahidi nyinyi kuwa mtazipata, «Tuacheni tuende na nyinyi huko Khaybar» wakiwa wanataka kwa hilo kubadilisha ahadi ya Mwenyezi Mungu kwenu. Waambie, «Hamtatoka pamoja na sisi kwenda Khaybar, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Alitwambia kabla hatujarudi Madina kwamba ngawira za Khaybar ni za wale waliohudhuria Ḥudaybiyah pamoja na sisi.» Watasema, «Mambo sivyo kama mnavyosema. Mwenyezi Mungu Hakuwaamrisha nyinyi hili. Nyinyi mnatukataza kutoka na nyinyi kwa uhasidi wenu tusije tukapata ngawira pamoja na nyinyi.» Mambo sivyo kama walivyodai, bali wao walikuwa hawaelewi amri za Mwenyezi Mungu kuhusu haki zao na wajibu wao wa kidini isipokuwa kidogo

    [16] Waambie wale waliojikalisha nyuma miongoni mwa al-a'rāb (nao ni mabedui) ili kujiepusha na kupigana, «Mtaitwa mwende mpigane na watu wenye nguvu nyingi za kupigana, mpigane nao au wasalimu amri bila ya kupigana. Basi mkimtii Mwenyezi Mungu katika hilo Alilowaitia la kupigana na watu hao Atawapa Pepo, na mkimuasi kama mlivofanya mlipojikalisha nyuma msiende Makkah pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu , rehema ya Mwenyezi Mungu na Amani zimshukie, Atawaadhibu adhabu yenye kuumiza.»

    [17] Yule aliye kipofu kati yenu, enyi watu, hana dhambi, wala aliye kiguru hana dhambi, wala aliye mgonjwa hana dhambi, wanapojikalisha nyuma wasishiriki katika kupigana jihadi pamoja na Waumini, kwa kuwa wao hawawezi. Na Mwenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, Atamtia kwenye mabustani ya Pepo ambayo chini ya miti yake na majumba yake ya fahari itakuwa ikipita mito. Na Mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake akajikalisha nyuma ili kuhepa kupigana jihadi pamoja na Waumini, Atamuadhibu adhabu yenye uchungu na kuumiza

    [18] Mwenyezi Mungu Ameridhika na Waumini pale walipokupa mkono wa ahadi, ewe Mtume, chini ya mti (Hii ndio hiyo Bay 'ah al-Ridwān ya hapo Ḥudaybiyah). Mwenyezi Mungu Alijua yaliyomo ndani ya nyoyo za Waumini hawa ya Imani, ukweli na utekelezaji ahadi, basi Mwenyezi Mungu Akawateremshia utulivu, Akaziimarisha nyoyo zao na Akawapa, badala ya kile kilichowapita katika mapatano ya Ḥudaybiyah, ufunguzi wa karibu, nao ni ufunguzi wa kuiteka Khaybar

    [19] na ngawira nyingi za mali za Mayahudi wa Khaybar walizozichukua. Na Mwenyezi Mungu ni Mshindi katika kuwatesa maadui Zake, ni Mwingi wa hekimakatika kuendesha mambo ya viumbe Vyake

    [20] Mwenyezi Mungu Amewaahidi nyinyi ngawira nyingi mtakazozichukua katika nyakati zake alizowakadiria, Akawaharakishia ngawira za Khaybar na Akaizuia mikono ya watu isiwafikie nyinyi, lisiwapate ovu lolote kati ya yale maovu ambayo maadui wenu waliwadhamiria ya vita na mapigano, na lisiwapate wale mliowaacha Madina, na ili kule kushindwa kwao, kusalimika kwenu na kughanimu kwenu kuwe ni alama ya nyinyi kuizingatia na kuchukua dalili kwayo kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye kuwahifadhi nyinyi na kuwanusuru, na yeye Ndiye Anayewaongoza kwenye njia iliyolingana sawa isiyokuwa na mpotoko

    [21] Na hakika Mwenyezi Mungu Amewaahidi nyinyi ngawira nyingine ambayo hamna uwezo nayo, Mwenyezi Mungu, kutakasika na kutukuka ni Kwake, Ndiye Mwenye uweza nayo, nayo iko chini ya mpango Wake na mamlaka Yake, na Ashawaahidi nyinyi kuwapatia, na hapana budi kwamba kile Alichoahidi kitakuwa. Na Mwenyezi Mungu juu ya kila kitu ni Muweza, hakuna chochote kinachomshinda

    [22] Na lau makafiri wa Makkah wangalipigana vita na nyinyi, wangalishindwa na nyinyi na wangaliwapa migongo yao kama vile anavyofanya anayeshindwa vitani, kisha hawatapata, asiyekuwa Mwenyezi Mungu, rafiki wa kushikana na wao kuwapiga vita nyinyi wala msaidizi wa kuwasaidia wao wapigane na nyinyi

    [23] Huo ndio mpango wa Mwenyezi Mungu Alioupanga kwa viumbe Vyake hapo tangu kuwa Atawanusuru askari Wake na Atawashindisha maadui Wake, na hutapata, ewe Nabii, katika mipango ya Mwenyezi Mungu mabadiliko

    [24] Na Yeye Ndiye Aliyeizuia mikono ya washirikina isiwafikie nyinyi, na mikono yenu isiwafikie wao katika bonde la Makkah baada nyinyi kuwaweza wao wakawa chini ya mamlaka yanu. (washirikina hawa ndio wale waliotoka kuishambulia kambi ya askari wa Mtume wa Mwenyezi Mungu , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, hapo Ḥudaybiyah, Waislamu wakawakamata kisha wakawaachilia wasiwaue, na walikuwa ni kiasi cha wanaume themanini.) Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona matendo yenu, hakuna chochote kinafichamana Kwake

    [25] Makafiri wa Kikureshi ndio waliokataa kumpwekesha Mwenyezi Mungu, wakawazuia nyinyi, Siku ya Ḥudaybiyah, kuingia Msikiti wa al-Ḥarām, wakakataza wanyama na wakawafunga wasifike mahali pa wao kuchinjwa, napo ni Ḥarām. Na lau si wanaume Waumini walio wanyonge na wanawake Waumini msiowajua, walio kati ya hawa makafiri wa Makkah, wanaoificha Imani yao kwa kuzichelea nafsi zao, msije mkawakanyaga kwa jeshi lenu mkawaua, mkapata dhambi, aibu na gharama kwa mauaji hayo bila kujua, tungaliwapa nyinyi uwezo juu yao, ili Mwenyezi Mungu Apate kumtia kwenye rehema Zake Anayemtaka kwa kumpa neema ya kuamini baada ya kukanusha. Lau hawa Waumini wa kiume na Waumini wa kike wangalitenganika na washirikina wa Makkah na wakajitoa kati yao, tungaliwaadhibu wale waliokufuru na kukanusha miongoni mwao adhabu yenye uchungu na kuumiza

    [26] Pindi wale waliokanusha walipoingiza ndani ya nyoyo zao ghera, ghera za watu wa zama za ujinga, ili wasikubali utume wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na miongoni mwa hayo ni kule kukataa kwao kwandika «Bi ism Allāh al-Raḥmān al-Raḥīm» katika mapatano ya Ḥudaybiyah, na wakakataa kuandika, «Haya ndiyo yale aliyoyapitisha Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu.» Na Mwenyezi Mungu Akamteremshia utulivu Mtume Wake na Waumini pamoja na yeye, Akawathibitishia neno «Lā ilāha illā Allāh» ambalo ndio kichwa cha ya kila uchamungu. Na Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na Waumini pamoja na yeye ndio wanaostahiki zaidi neno la uchamungu kuliko washirikina. Na hivyo ndivyo walivyokuwa, walistahiki neno hili na sio washirikina. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa ujuzi wa kila kitu, hakuna kitu chochote kinachofichamana Kwake

    [27] Kwa hakika Mwenyezi Mungu Alimsadikishia Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ndoto yake aliyomuotesha kwa haki kwamba utaingia, wewe na Maswahaba wako, Nyumba takatifu ya Mwenyezi Mungu hali ya kuwa mko katika amani, hamuwaogopi watu wa ushirikina, hali ya kuwa mnanyoa vichwa vyenu na mnapunguza. Mwenyezi Mungu Alijua kheri na maslahi ya kuwaepusha nyinyi na Makkah mwaka wenu huo na kuingia huko baadae, msiyoyajua nyinyi, na Akajaalia, kabla ya kuingia kwenu Makkah mliyoahidiwa, ufunguzi wa karibu, nao ni mapatano ya amani ya Ḥudaybiyah na ufunguzi wa Khaybar

    [28] Yeye Ndiye Aliyemtumiliza Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa ubainufu ulio wazi na Dini ya Uislamu, ili aifanye kuwa juu ya mila zote. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni shahidi kwamba Yeye ni Mwenye kukupa ushindi na kuidhihirisha Dini yako juu ya kila dini

    [29] Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na wale walio pamoja na yeye katika dini yake, ni wakali juu ya makafiri, wanahurumiana wao kwa wao, utawaona wakirukuu na kumsujudia Mwenyezi Mungu katika Swala yao, wakimtarajia Mola wao Awatunuku fadhila Zake, Awatie Peponi na Awe radhi nao. Alama ya utiifu wao kwa Mwenyezi Mungu iko wazi kwenye nyuso zao kwa alama ya kusujudu na kuabudu. Hiii ndiyo sifa yao kwenye Taurati. Na sifa yao katika Injili ni kama sifa ya mmea wa nafaka uliotoa kijiti chake na tawi lake, kisha matawi yakawa mengi baada ya hapo, na mmea ukashikana, ukapata nguvu na ukasimama juu ya kigogo chake ukiwa na mandhari mazuri yanayowapendeza wakulima, ili kuwatia hasira kwa Waumini hawa, kwa wingi wao na uzuri wa mandhari yao, makafiri. Katika haya pana dalili ya ukafiri wa wenye kuwachukia Maswahaba, radhi za Mwenyezi Mungu ziwashukie, kwa kuwa yule ambaye Mwenyezi Mungu Anamtia hasira kwa Maswahaba basi ishapatikana kwake sababu ya hasira nayo ni ukafiri. Mwenyezi Mungu Amewaahidi waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake kati yao kusamehewa dhambi zao na kupewa malipo mema mengi yasiyokatika, nayo ni Pepo. (Na ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya ukweli unaoaminiwa usioenda kinyume. Na kila mwenye kufuata nyayo za Maswahaba, radhi za Mwenyezi Mungu ziwashukie, basi yeye anaingia kwenye hukumu yao ya kustahiki msamaha na malipo makubwa, na wao wana ubora, kutangulia mbele na ukamilifu ambao hakuna yoyote katika ummah huu atakayewafikia, radhi za Mwenyezi Mungu ziwashukie na Awaridhishe)

    Vyumba

    Surah 49

    [1] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake msiamue jambo la Sheria za Dini yenu kinyume cha maamuzi ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, mkaingia kwenye uzushi. Na muogopeni Mwenyezi Mungu katika maneno yenu na vitendo vyenu, isije amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake ikaendewa kinyume. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msikizi wa maneno yenu , ni Mjuzi wa nia zenu na vitendo vyenu. Hapa pana onyo kwa Waumini wasifanye uzushi katika Dini au kuleta sheria ambazo Mwenyezi Mungu Hakuziruhusu

    [2] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata Sheria Zake kivitendo, msiinue sauti zenu juu ya sauti ya Nabii mnaposema naye, wala msipige kelele mnapomuita kama mnavyopigiana kelele nyinyi kwa nyinyi, na semeni na yeye kwa namna tafauti ya vile mnavyosema na wengine, kama alivyokuwa tafauti na wengine kwa kuteuliwa kuubeba ujumbe wa Mola Wake, ulazima wa kumuamini, kumpenda, kumtii na kumfuata kwa kuogopa yasitanguke matendo yenu mema na nyinyi hamfahamu wala hamlihisi hilo

    [3] Hakika wale wanaoziteremsha sauti zao chini mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu , hao ni wale ambao Mwenyezi Mungu Amewatahini nyoyo zao na Akazitakasa kwa uchamungu wake, watapata msamaha wa dhambi zao kutoka kwa Mola wao na malipo mema mengi, nayo ni Pepo

    [4] Hakika ya wale wanaokuita, ewe Nabii, nyuma ya vyumba vyako kwa sauti ya juu, wengi wao hawana akili ya kuwapelekea kuwa na adabu nzuri pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kumheshimu

    [5] Na lau wangalisubiri mpaka ukawatokea ingalikuwa bora zaidi kwao mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu Amewaamrisha wao kukuheshimu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa yale yaliyotokea kwao ya madhambi na utovu wa adabu kwa kutojua kwao, ni Mwingi wa rehema kwao kwa kutowaharakishia mateso

    [6] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Zake kivitendo, Akiwajia nyinyi mtu aliyetoka nje ya maadili ya Dini na habari yoyote, ihakikisheni habari yake kabla ya kuiamini na kuisambaza mpaka mjue usahihi wake, kwa kuchelea msiwatuhumu watu wasio na hatia kwa kosa litokalo na nyinyi mkaja kujuta kwa hilo

    [7] Na mjue kuwa baina yenu yupo Mtume wa Mwenyezi Mungu, kuweni na adabu na yeye, kwani yeye anayajua zaidi mambo yanayowafaa kuliko nyinyi, anawatakia nyinyi kheri, na nyinyi huenda mkajitakia shari na madhara ambayo Mtume hawakubalii, na lau yeye angaliwafuata nyinyi katika mengi mnayoyachagua, hilo lingalipelekea muingie kwenye usumbufu. Lakini Mwenyezi Mungu Amewafanya nyinyi muipende Imani na Akaifanya ipambike ndani ya nyoyo zenu ndipo mkaamini, na Amewafanya nyinyi mchukie kumkanusha Mwenyezi Mungu, kutoka nje ya twaa Yake na kumuasi. Hao waliosifika kwa sifa hizi ndio waongofu wenye kufuata njia ya haki

    [8] Kheri hii walioipata ni nyongeza njema kutoka kwa Mwenyezi Mungu juu yao na ni neema. Na Mwenyezi Mungu Anamjua sana anayezishukuru neema Zake, ni Mwingi wa hekima katika kuendesha mambo ya viumbe Vyake

    [9] Na mapote mawili ya Waumini yakipigana, fanyeni upatanishi, enyi Waumini, baina yao kwa kuyaita yakubali kuamuliwa na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunnah ya Mtume Wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kuridhika na uamuzi wa hivyo viwili. Iwapo pote mojawapo ya yale mawili litalifanyia uadui pote lingine na litakataa kukubali mwito huo wa upatanishi, basi lipigeni vita mpaka lirudi kwenye uamuzi wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na likirudi fanyani upatanishi baina ya hayo mawili kwa haki, na mfanyeni uadilifu katika uamuzi wenu kwa kutotoka nje ya hukumu ya wenyezi Mungu na hukumu ya Mtume Wake katika uamuzi wenu. Hakika Mwenyezi Mungu Anawapenda waadilifu katika uamuzi wao, wanaohukumu baina ya viumbe Vyake kwa haki. Katika aya hii pana kuthibitisha sifa ya mapenzi kwa Mwenyezi Mungu kihakika, kama inavyonasibiana na utukufu Wake Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu

    [10] Hakika Waumini ni ndugu katika Dini, basi fanyeni upatanishi baina ya ndugu zenu wawili wakipigana. Na mwogopeni Mwenyezi Mungu katika mambo yenu yote , kwa kutarajia mrehemewe

    [11] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Zake kivitendo, wasitoke wanaume Waumini wakawacheza shere wanaume Waumini wengine, huenda akawa yule anayechezwa shere katika wao ni bora kuliko wale wenye kucheza shere, na wasitoke wanawake Waumini wakawacheza shere wanawake Waumini wengine, kwani huenda yule anayechezwa shere miongoni mwao ni bora kuliko wale wenye kucheza shere. Wala msitiane ila nyinyi kwa nyinyi, wala msiitane majina ambayo yanachukiwa na wenye kuitwa nayo, kwani ubaya wa sifa na jina ni utokaji nje wa maadili ya Dini, nao ni kucheza shere kwa njia ya dharau, kuaibisha kwa maneno au ishara na kupanana majina mabaya, baada ya kuwa mmeingia kwenye Uislamu na mmeufahamu. Na Asiyetubia na huku kuchezeana shere, kutiana ila, na kuitana majina mabaya na utokaji nje wa maadili ya Dini, basi hao ndio watu waliozidhulumu nafsi zao kwa kuyatenda mambo haya yaliyokatazwa

    [12] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Zake kivitendo, Jiepusheni na dhana mbaya nyingi kwa Waumini, kwani dhana nyingine ni dhambi. Wala msipekue aibu za Waislamu, wala msisemane nyinyi kwa nyinyi maneno yenye kuchukiwa na wenye kusemwa na hali wao hawapo. Je, anapenda mmoja wenu kula nyama ya ndugu yake akiwa amekufa? Nyinyi mnalichukia hilo, basi lichukieni lile la kumsengenya. Na muogopeni Mwenyezi Mungu katika yale Aliyowaamrisha nyinyi na kuwakataza. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kukubali toba za waja Wake Waumini, ni Mwingi wa rehema kwao

    [13] Enyi watu! Sisi tumewaumba nyinyi kutokana na baba mmoja, naye ni Ādam, na mama mmoja, naye ni Ḥawwā’, hivyo basi hakuna kufadhilishana baina yenu kinasaba, na tumewafanya nyinyi kwa kuzaana kuwa mataifa na makabila mbalimbali ili mjuane nyinyi kwa nyinyi, hakika mtukufu wenu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule anayemcha Yeye zaidi. Hakika Mwenyezi Mungu Anawajua sana wachamungu na Anawatambua

    [14] Waarabu wa majangwani, nao ni Mabedui, walisema, «Tumemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Imani iliyokamilika.» Waambie, ewe Nabii, «Msijidai kuwa mna Imani kamilifu, lakini semeni, ‘Tumesilimu.’ na bado Imani haijaingia ndani ya nyoyo zenu. Na mkimtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Hatawapunguzia chochote katika thawabu za matendo yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa anayetubia dhambi zake, ni Mwingi wa rehema kwake.» Katika hii aya kuna makemeo kwa mtu anayedhihirisha kuamini na kufuata Sunnah, na hali matendo yake yanashuhudilia kinyume cha hayo

    [15] Hakika ni kwamba Waumini ni wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafuata sheria Zake kivitendo, kisha wasiwe na shaka katika Imani yao, na wakatoa raali yao mazuri na roho zao kwa kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, kumtii Yeye na kutafuta radhi Zake, basi hao ndio wakweli katika Imani Yao

    [16] Waambie, ewe Mtume, hawa Mabedui, «Je mnampasha habari Mwenyezi Mungu kuhusu dini yenu na yaliyomo kwenye dhamiri zenu, na hali Mwenyezi Mungu Anavijua vilivyoko mbinguni na ardhini? Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu, havifichamani Kwake vilivyomo ndani ya nyoyo zenu vya Imani au vya ukafiri na vya wema au vya ubaya.»

    [17] Hawa Mabedui wanakusimulia wewe, ewe Nabii, kusilimu kwao, kukufuata wewe na kukunusuru. Waambie, «Msinisimulie mimi kuingia kwenu kwenye Uislamu, kwani manufaa yake yanawarudia nyinyi wenyewe. Na Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyewafadhili nyinyi kwa kuwaafikia kumuamini Yeye na Mtume Wake, iwapo nyinyi ni wakweli katika kuamini kwenu.»

    [18] Hakika Mwenyezi Mungu Anayajua yasioonekana ya mbinguni na ardhini, hakuna chochote kinachofichamana kwake katika hayo. Na Mwenyezi Mungu Anayaona matendo yenu na Atawalipa kwayo, yakiwa mema Atawalipa wema, na yakiwa maovu Atawalipa uovu

    Qaaf

    Surah 50

    [1] «Qāf» Yametangulia maelezo kuhusu herufi zilizokatwa na kutengwa mwanzoni mwa sura ya Al-Baqarah. Anaapa Mwenyezi Mungu kwa Qur’ani tukufu, yenye ubora na heshima

    [2] Bali wale wenye kumkanusha Mtume waliona ajabu kuwa walijiwa na muonyaji miongoni mwao anayewaonya mateso ya Mwenyezi Mungu, basi wale waliomkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume Wake walisema, «Hili ni jambo geni la kuonewa ajabu

    [3] «Je, tunapokufa na tukawa mchanga, itawezekana vipi kurejea baada ya hapo tukawa kama tulivyokuwa? Hayo ni marajeo ambayo kutukia kwake kuko mbali.»

    [4] Hakika tunakijua kile ambacho ardhi kinakipunguza na kukimaliza katika miili yao, na tuna Kitabu kilichohifadhiwa kutokana na mageuzo na mabadiliko, kilichosajiliwa kila kitu kitakachowapitia katika maisha yao na baada ya kufa kwao

    [5] Bali hawa washirikina waliikanusha Qur’ani ilipowajia. Wao wako kwenye hali ya babaiko na kuchanganyikiwa, hawasimami imara kwenye jambo lolote, na hawana kituo cha kutulia

    [6] Kwani walighafilika walipokanusha Ufufuzi, wasianagalie mbingu juu yao: vipi tulizijenga zikiwa zimelingana sawa pande zote, limeimarika jengo lake, na tukazipamba kwa nyota, na hazina pasuko na nyufa, zimesalimika na hitilafu na kasoro

    [7] Na ardhi tumeipanua na kuitandika, na tukaweka humo majabali yaliyojikita, ili ardhi isiende mrama na watu wake, na tukaotesha humo kila aina ya mimea yenye mandhari ya kupendeza na yenye kunufaisha, inayomfurahisha mwenye kuiangalia

    [8] Mwenyezi Mungu Ameumba mbingu, ardhi na vilivyomo baina ya hivyo viwili miongoni mwa alama kubwa, ili viwe ni mazingatio ya kumfanya mtu aone na atoke kwenye giza la ujinga, na ni ukumbusho kwa kila mja mnyenyekevu, mwenye kucha na kuogopa, mwenye kurejea sana kwa Mwenyezi Mungu Aliyeshinda na kutukuka

    [9] Na tumeteremsha kutoka juu mvua yenye manufaa mengi, tukaotesha kwayo mabustani yenye miti mingi na nafaka za mimea ya nafaka zinazovunwa

    [10] Na tukaotesha mitende mirefu yenye makarara yaliyojaza na kupandana

    [11] Tumeviotesha hivyo viwe ni riziki za waja za wao kuzila kulingana na mahitaji yao, na tukahuisha, kwa maji haya tuliyoyateremsha, ardhi iliyokuwa kavu na kame, haina nafaka wala mimea mingine. Na kama tunavyohuisha, kwa maji hayo, ardhi iliyokufa, tutawatoa nyinyi Siku ya Kiyama mkiwa hai baada ya kufa

    [12] Walikanusha, kabla ya hawa washirikina miongoni mwa Makureshi, watu wa Nūḥ, watu wa Kisima na Thamūd

    [13] Na 'Ād na Fir'awn na watu wa Lūṭ

    [14] Na watu waliokuwa kwenye tuka la miti nao ni watu wa Shu'ayb, na watu wa Tubba' wa Himyar. Watu wote hao waliwakanusha Mitume wao, ikapasa juu yao adhabu ambayo Mwenyezi Mungu Aliwaonya nayo kwa ukafiri wao

    [15] Kwani tulishindwa kuanzisha uumbaji wa kwanza tuliyouanzisha na hakukuwa na kitu chochote, mpaka tushindwe kuwarudisha wao wakiwa viumbe wapya baada ya kutoweka kwao? Hilo halitushindi. Bali sisi ni waweza wa hilo, lakini wao wako kwenye mshangao na shaka juu ya jambo la kufufuliwa na kukusanywa

    [16] Hakika tumemuumba binadamu na tunakijua kile ambacho nafsi yake inamhadithia kwacho. Na sisi tuko karibu na yeye zaidi kuliko ukambaa wa roho (nao ni mshipa ulioko shingoni unaoshikana na moyo)

    [17] Pindi Malaika wawili wanaotunza, kuliani kwake na kushotoni kwake, wanapoyaandika matendo Yake: aliye kuliani anaandika mema na aliye kushotoni anaandika maovu

    [18] Hatamki neno kulisema isipokuwa mbele yake pana Malaika anayetunza maneno yake na kuyaandika, naye ni Malaika ambaye yupo wakati wote aliyeandaliwa kwa hilo

    [19] Na hapo ikaja shida ya mauti na kizaazaa chake na ukweli usiozuilika wala kukimbilika! Hali hiyo ndiyo ambayo ulikuwa, ewe binadamu, ukiikimbia na kuihepa

    [20] Hapo baragumu likavuviwa mvuvio wa pili wa Ufufuzi. Mvuvio huo utakuwa kwenye Siku ya matekelezo ya adhabu ambayo Mwenyezi Mungu Aliwaahidi wakanushaji

    [21] Na ije kila nafsi, wakiwa pamoja nayo Malaika wawili: mmoja anaiongoza kwenye Mkusanyiko, na mwingine Anaitolea ushahidi wa ililolifanya duniani, la kheri na shari

    [22] Kwa hakika wewe ulikuwa katika mghafala kuhusu tukio hili unaloliona leo, ewe binadamu, ndipo tukakifunua kifiniko chako kilichoziba moyo wako, kughafilika kukakuondokea, basi leo macho yako, katika kile unachokitolea ushahidi, ni makali

    [23] Na Malaika mwandishi mwenye kumtolea ushahidi atasema, «Haya ndiyo niliyonayo kutoka kwenye rikodi ya matendo yake. Nayo imetayarishwa, imehifadhiwa na ipo hapa kwangu.»

    [24] Na Mwenyezi Mungu Aseme kuwaambia Malaika wawili: mwenye kuongoza na yule shahidi, baada ya kutolewa uamuzi baina ya viumbe, «Mtupeni ndani ya Jahanamu kila mwenye kukataa kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Mola wa haki, aliye mwingi wa ukafiri na ukanushaji, mwenye kuipinga haki

    [25] mwenye kuzuia kutekeleza haki zilizo juu yake katika mali yake, anaye wadhulumu waja wa Mwenyezi Mungu na kukiuka mipaka Yake, anayelifanyia shaka agizo la Mwenyezi Mungu na onyo Lake

    [26] aliyemshirikisha Mwenyezi Mungu kwa kukiabudu kiabudiwa kingine miongoni mwa viumbe Vyake pamoja na Yeye. Mtupeni ndani ya adhabu ya moto wa Jahanamu ulio mkali.»

    [27] Shetani wake aliyekuwa na yeye ulimwenguni atasema, «Mola wetu! Mimi sikumpoteza, lakini alikuwa kwenye njia iliyokuwa mbali na njia ya uongofu.»

    [28] Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Aseme, «Msitete mbele yangu leo kwenye Kisimamo cha Malipo na Hesabu. Kwani hilo halina faida, na mimi niliwaletea duniani onyo la adhabu kwa aliyenikufuru na kuniasi

    [29] «Halibadilishwi neno kwangu, na simuadhibu yoyote kwa dhambi za mtu mwingine, simuadhibu yoyote isipokuwa kwa dhambi zake baada ya kusimamiwa na hoja.»

    [30] Watajie watu wako, ewe Mtume, Siku tutakayoiambia Jahanamu, «Je umeshajaa?» Na Jahanamu iseme, «Je kuna nyongeza yoyote ya majini na binadamu?» Hapo Mola, uliotukuka utukufu wake, Aweke unyayo Wake ndani yake, na hapo ijikusanye na ijikunjekunje na iseme, «Basi! Basi!»

    [31] Na hapo wachamungu wakaribishiwe Pepo, iwepo mahali ambapo si mbali na wao, wawe waiona, kwa kuwaongezea furaha zao

    [32] Na waambiwe hao Waumini, «Hii ndiyo ile mliokuwa mkiahidiwa, enyi wachamungu, kwa kila mtubiaji dhambi zake, mwenye kukitunza kila kinachomkurubisha kwa Mola Wake miongoni mwa mambo ya lazima na ya utiifu

    [33] mwenye kumcha Mwenyezi Mungu duniani na akakutana na Yeye Siku ya Kiyama kwa moyo wa mwenye kutubia dhambi zake.»

    [34] Na hapo waambiwe hao Waumini, «Ingieni Peponi kuingia kunakoshikamana na kusalimika na maafa na shari, hali ya kuhifadhiwa na mambo yote mnayoyachukia. Hiyo ndiyo Siku ya starehe za milele zisizokatika.»

    [35] Watapewa hawa Waumini ndani ya Pepo wanavyovitaka. Na tuna nyogeza za neema juu ya zile tulizowapa; kubwa zaidi la neema hizo ni kutazama uso wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka

    [36] Na tuliwaangamiza, kabla ya hao washirikina wa Kikureshi, ummah wengi. Walikuwa wana nguvu na ujebari kuliko wao. Walizunguka mijini wakafuata kila njia kutaka kuyakimbia maangamivu. Basi je, kuna makimbilizi yoyote ya kujiepusha na adhabu ya Mwenyezi Mungu itakapowajia

    [37] Hakika katika kuziangamiza kame zilizopita kuna mazingatio kwa aliyekuwa na moyo wa kufahamia na mashikio ya kusikilizia, na akawa yupo kwa moyo wake, hakusahau wala hakughafilika

    [38] Na kwa hakika tuliumba mbingu na ardhi na vilivyoko baina ya hivyo viwili miongoni mwa viumbe kwa muda wa Siku sita, na hatukupata tabu yoyote wala shida. Katika uweza huu mkubwa kuna dalili ya nguvu zaidi ya kuwa Yeye, Aliyetakasika, Ana uweza wa kuhuisha wafu

    [39] Basi vumilia, ewe Mtume, kwa yale wanayoyasema wakanushaji, kwani Mwenyezi Mungu Yuko chonjo nao. Na swali, kwa ajili ya Mola wako kwa kumshukuru, Swala ya Alfajiri, kabla ya jua kuchomoza, na Swala ya Alasiri kabla ya jua kuchwa

    [40] na uswali kipindi cha usiku na umtakase Mola Wako kwa kumshukuru baada ya Swala

    [41] Na usikilize, ewe Mtume, siku Malaika atakapoita kwa kupuliza kwenye Baragumu kutoka sehemu iliyo karibu

    [42] Siku watakapousikia ukulele wa Ufufuzi wa ukweli usio na shaka, hiyo ndiyo Siku ya waliyo makaburini kutoka makaburini mwao

    [43] Ni sisi tunaohuisha viumbe na kuwafisha duniani, na ni kwetu sisi ndipo mwisho wao wote watakapofikia Siku ya Kiyama ili wahesabiwe na walipwe

    [44] Siku ambayo ardhi itapasukapasuka itoe wafu waliozikwa humo, watoke mbio kuelekea upande wa yule anayeita. Kuwakusanya watu hivyo kwenye Kisimamo cha Hesabu ni jambo sahali kwetu na rahisi

    [45] Sisi ni wajuzi zaidi kwa wanayoyasema hawa washirikina, ya kumzulia Mwenyezi Mungu urongo na kukanusha aya Zake. Na hukuwa wewe, ewe Mtume, umepewa nguvu juu yao ya kuwalazimisha waingie katika Uislamu, hakika ni kwamba wewe umetumilizwa uwe mfikishaji. Basi mkumbushe kwa Qur’ani anayeogopa onyo langu, kwa kuwa asiyeogopa onyo (la Mwenyezi Mungu) hafaidiki kwa kukumbushwa

    Zipeperushazo

    Surah 51

    [1] Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anaapa kwa upepo wenye kurusha mchanga

    [2] na mawingu yenye kubeba uzito mkubwa wa maji

    [3] na jahazi zinazopita baharini na kutembea kwa upesi na usahali

    [4] na Malaika wenye kugawanya amri za Mwenyezi Mungu kwa viumbe Vyake

    [5] kwamba mnayoahidiwa, enyi watu, ya kufufuliwa na kuhesabiwa ni tukio lenye kuwa kwa kweli na yakini

    [6] na kwamba kuhesabiwa na kulipwa mema kwa amali njema ni jambo lisilo na budi

    [7] Na Anaapa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa mbingu zenye umbo zuri, kwamba nyinyi, enyi wakanushaji

    [8] mko kwenye neno linalogongana kuhusu Qur’ani na kuhusu Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [9] Anaepushwa na Qur’ani na Mtume yule aliyeepushwa na lile la kuviamini hivyo viwili kwa kuzipa mgongo dalili za Mwenyezi Mungu na hoja Zake za yakini, na kwa hivyo haafikiwi kwenye kheri

    [10] Wamelaaniwa warongo wenye dhana zisizo za kweli

    [11] waliomo ndani ya dimbwi la ukafiri na upotevu hali ya kuwa wameghafilika na kujikita kwenye ubatilifu wao

    [12] Wanauliza hawa wenye kukanusha suali la kuonyesha kuwa ni jambo lisilowezekana na la kuonyesha ukanushaji, «Ni lini Siku ya kuhesabiwa na kulipwa?»

    [13] Siku ya Malipo ni Siku ya wao kuadhibiwa kwa kuchomwa kwa Moto na waambiwe

    [14] «Onjeni adhabu yenu ambayo mlikuwa mkiifanyia haraka duniani.»

    [15] Hakika ya wale wanaomcha Mwenyezi Mungu watakuwa kwenye mabustani ya Pepo makubwa na chemchemi za maji yenye kutembea. Mwenyezi Mungu Atawapa yote wanayoyatamani ya aina mbalimbali za starehe

    [16] Watazipokea neema hizo wakiwa wameridhika nazo na nafsi zao zina furaha. Hakika wao, kabla ya kupata sterehe hizo, walikuwa wema duniani kwa matendo yao mema

    [17] Wema hawa walikuwa wakilala kipindi kichache usiku, wakiswali kwa Mola wao wakimnyenyekea

    [18] na katika nyakati za mwisho wa usiku, kabla ya alfajiri kwa muda mchache, walikuwa wakimuomba Mwenyezi Mungu msamaha wa dhambi zao

    [19] Na katika mali yao kulikuwa na haki ya lazima na ya kupendekezwa kupewa wahitaji wanaowaomba watu na wasiowaomba kwa kuona haya

    [20] Na katika ardhi kuna mazingatio na dalili waziwazi za uweza wa Mwenyezi Mungu kwa watu wenye yakini kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Mola wa haki, Aliye Peke Yake na asiye na mshirika, na wenye kumuamini Mtume Wake. rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [21] Na katika kuwaumba nyinyi kuna dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, na kuna mazingatio ya kuwaonyesha nyinyi upweke wa Muumba wenu na kwamba Yeye hakuna Mola Anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Yeye. Je, mumeghafilika na hilo mkawa hamlioni mkazingatia kwalo

    [22] Na mbinguni kuna riziki yenu na yale mnayoahidiwa ya kheri na shari, na thawabu na mateso na yasiyokuwa hayo. Yote yameandikwa na kukadiriwa

    [23] Anaapa Mwenyezi Mungu kwa dhati Yake tukufu kwamba kile Alichowaahidi ni kweli, msikifanyie shaka kama ambavyo hamshuku kuwa nyinyi mnasema

    [24] Je imekujia wewe, ewe Mtume, habari ya wageni wa Ibrāhīm aliyewakirimu

    [25] na walikuwa ni miongoni mwa Malaika watukufu- wakati walipomjia nyumbani kwake, wakamwamkia kwa kumwambia, «Salama!»Akawarudishia maamkizi kwa kusema, «Salama ni kwenu! Nyinyi ni watu wageni hatuwajui.»

    [26] Akaondoka kwa siri na akaelekea kwa watu wa nyumbani kwake akamlenga ndama mnono akamchinja, akamchoma

    [27] kisha akamuweka mbele yao na akawakaribisha kwa upole kwa kusema, «Si mle»

    [28] Alipowaona hawali aliingiwa na kicho cha kuwaogopa, na hapo wakamwambia, «Usiogope! Sisi ni wajumbe wa Mwenyezi Mungu. Na wakampa bishara kwamba mkewe Sarah atamzalia mtoto atakayekuwa ni miongoni mwa watu wanaomjua Mwenyezi Mungu na kuijua Dini Yake, naye ni Isḥāq, amani imshukie

    [29] Aliposikia mke wa Ibrāhīm maneno ya bishara ya hao Malaika, alielekea upande wao na ukelele, akajipiga uso wake kwa kulionea ajabu jambo hili na akasema, «Vipi nitazaa na mimi ni tasa sizai?»

    [30] Malaika wa Mwenyezi Mungu wakamwambia, «Hivyo ndivyo Alivyosema Mola wako kama tulivyokwambia. Na Yeye Muweza wa hilo, hapana la ajabu kutokana na uweza Wake. Hakika Yeye, Aliyetakasika na kutukuka, Ndiye Mwenyew hekima Anayeviweka vitu mahali pake, Ndiye Mwenye kuyajua maslahi ya waja Wake

    [31] Akasema Ibrāhīm, amani imshukie, kuwaambia Malaika wa Mwenyezi Mungu «Mna jambo gani na mmetumwa na ujumbe gani

    [32] Wakasema, «Mwenyezi Mungu Ametutuma tuende kwa watu waliofanya uhalifu kwa kumkanusha Mwenyezi Mungu

    [33] ili tuwaangamize kwa mawe ya udongo uliokuwa mkavu kama mawe

    [34] uliotiwa alama kutoka kwa Mola wako ya hawa waliokiuka mpaka katika uchafu na uasi

    [35] Tukamtoa kila aliyekuwa kwenye mji wa watu wa Lūṭ katika watu walioamini

    [36] Hatukupata kwenye mji huo isipokuwa nyumba moja ya Waislamu, nayo ni nyumba ya Lūṭ, amani imshukie

    [37] Na tukaacha kwenye mji huo uiliotajwa athari iliyosalia ya adhabu iwe ni alama ya uweza wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na vile alivyowatesa makafiri. Ili hilo liwe ni zingatio kwa wale wanaoiogopa adhabu ya Mwenyezi Mungu iliyo kali na yenye kuumiza

    [38] Na katika kumtumiliza kwetu Mūsā, aende kwa Fir'awn na wakuu wa utawala wake, kwa aya na miujiza yenye kushinda, kuna alama kwa wanaoogopa adhabu kali

    [39] Fir'awn akayapa mgongo akighurika nguvu zake na wasaidizi wake na akasema kuhusu Mūsā, «Yeye ni mchawi au ni mwendawazimu,»

    [40] Tukamchukua Fir'awn na askari wake tukawatupa baharini, na hali ameleta jambo la kulaumiwa kwa sababu ya ukafiri wake, kukanusha kwake na ubaya wake

    [41] Na kuhusu mambo ya watu wa kabila la 'Ād na kuwaangamiza wao kuna dalili na mazingatio kwa mwenye kutia mambo akilini, tulipowapelekea wao upepo usiokuwa na baraka na usioleta kheri yoyote

    [42] hauachi kitu chochote unachokipitia isipokuwa hukifanya ni kama kitu kilichochakaa

    [43] Na kuhusu watu wa kabila la Thamūd na kuangamizwa kwao kuna dalili na mazingatio, walipoambiwa-na msemaji hapa ni Nabii wao Ṣāliḥ, amani imshukie-, «Jistarehesheni mjini kwenu siku tatu mpaka muda wenu wa kuishi ukome

    [44] Wakaasi amri ya Mola wao, wakapatikana na ukelele wa adhabu, na huku wanayaangalia mateso yao kwa macho yao

    [45] Haikumkinika wao kukimbia wala kusimama kwa adhabu waliokuwa nayo, na hawakuwa ni wenye kujitetea nafsi zao

    [46] Na tuliwaangamiza watu wa Nūḥ kabla ya hawa, hakika wao walikuwa ni watu wenye kuenda kinyume na amri ya Mwenyezi Mungu, wenye kutoka nje ya utiifu Kwake

    [47] Na mbingu tuliziumba na tukazitengeneza vizuri, na tukazifanya ni sakafu ya ardhi kwa nguvu na uweza mkubwa, na sisi tutayapanua maeneo yake na pande zake

    [48] Na ardhi tuliifanya ni tandiko la viumbe wapate kutulia juu yake, Basi bora wa wenye kutandika ni sisi

    [49] Na kutokana na kila kitu katika jinsi ya vitu vilivyoko tumeumba aina mbili tafauti, ili mjikumbushe uweza wa Mwenyezi Mungu na mzingatie

    [50] Basi kimbieni, enyi watu , kutoka kwenye mateso ya Mwenyezi Mungu na muelekee kwenye rehema Yake kwa kumuamini Yeye na Mtume Wake, kufuata amri Yake na kufanya mambo ya utiifu Kwake. Hakika mimi, kwenu nyinyi, ni muonyaji ambaye maonyo yake yako waziwazi. Na Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, alikuwa akizungukwa na mambo hukimbilia Swala, na huku ndiko kumkimbilia Mwenyezi Mungu

    [51] Na msimfanye pamoja na Mwenyezi Mungu muabudiwa mwingine, Hakika mimi kwenu nyinyi ni muonyaji amabaye uonyaji wake uko waziwazi

    [52] Kama walivyomkanusha Makureshi Mtume wao Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wakasema, «Yeye ni mshairi, au mchawi, au mwendawazimu.», ndivyo walivyofanya ummah waliowakanusha Mitume wao kabla ya Makureshi, na Mwenyezi Mungu Akawashushia mateso Yake

    [53] Je, waliusiana wa mwanzo na wa mwisho kumkanusha Mtume waliposema hivyo kwa umoja wao? Bali wao ni watu wenye kukiuka mipaka kwa uhalifu, nyoyo zao zimefanana na vitendo vyao kwa ukafiri na ukiukaji mipaka, ndipo waliokuja nyuma wakasema hayo kama walivyosema waliotangulia

    [54] Wapuuze hao washirikina, ewe Mtume, mpaka itakapokujia wewe amri ya Mwenyezi Mungu kuhusu wao, hapatakuwa na yoyote mwenye kukulaumu, kwani ushafikisha yale uliyotumilizwa kwayo

    [55] Pamoja na kuwapuuza wao, ewe Mtume, na kutoshughulika na ufidhuli wao, endelea kuwaidhia wale uliotumilizwa kwao, kwani kukumbusha na kuwaidhia watanufaika nako wale wenye nyoyo zenye kuamini, na katika kufanya mawili hayo kuna kusimamisha hoja kwa wenye kupa mgongo

    [56] Na sikuumba majini na binadamu na kutumiliza Mitume wote isipokuwa kwa lengo tukufu, nalo niabudiwe mimi Peke Yangu, na sio asiyekuwa mimi

    [57] Sitaki kutoka kwao riziki wala sitaki wanilishe, kwani mimi Ndiye Mpaji Mwenye kuruzuku. Kwani Yeye, Aliyetakasika na kila sifa za upungufu, hawahitaji viumbe Vyake, bali wao ndio wahitaji Kwake katika hali zao zote, Yeye Ndiye Mwenye kuwaumba na kuwaruzuku na Aliyejikwasisha nao kwa kutowahitajia

    [58] Hakika Mwenyezi Mungu , Peke Yake, Ndiye Mwenye kuviruzuku viumbe Vyake, Ndiye Anayedhamini chakula chao, Mwenye nguvu Aliye Thabiti, Hatendeshwi nguvu wala hakuna Mwenye kushindana Naye. Ni Wake Yeye uweza wote na nguvu

    [59] Hakika wale waliodhulumu kwa kumkanusha kwao Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wana fungu la adhabu ya Mwenyezi Mungu mfano wa fungu la wenzi wao waliopita kabla yao. Basi wasiifanyie haraka adhabu , kwani hapana budi ni yenye kuwajia

    [60] maangamivu na usumbufu ni wa wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, kutokana na Siku yao wanayoahidiwa kuteremkiwa na adhabu, nayo ni Siku ya Kiyama

    Mlima

    Surah 52

    [1] Anaapa Mwenyezi Mungu kwa Ṭūr, nalo ni jabali ambalo juu yake Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Alizungumza na Mūsā

    [2] Na kwa Kitabu kilichoandikwa, nacho ni Qur’ani

    [3] kwenye nyaraka zilizokunjuliwa

    [4] Na kwa Nyumba Iliyoamirishwa kwa Malaika watukufu wenye kuizunguka daima

    [5] Na kwa sakafu iliyoinuliwa juu, nayo ni uwingu wa duniani

    [6] Na kwa bahari iliyowashwa moto, iliyojaa maji

    [7] Hakika adhabu ya Mola Wako, ewe Mtume, ni yenye kuwashukia makafiri

    [8] Hakuna kizuizi cha kuizuia itakaposhuka

    [9] Siku ya mbingu kutetemeka mpango wake kuharibika na pande zake kusukikasukika, na hapo ni wakati wa mwisho wa dunia

    [10] na majabali yaondoke mahali pake na yatembee kama vile mawingu yanavyotembea

    [11] Maangamivu katika Siku hii ni yenye kuwashukia wakanushaji

    [12] Ambao wao wamevama ndani ya ubatilifu wanapumbaa nao na wanaifanya dini yao kuwa ni shere na mchezo

    [13] Siku ya kusukumwa hawa wakanushaji msukumo wa nguvu wenye kuwadhalilisha hadi kwenye Moto wa Jahanamu

    [14] Na waambiwe kwa njia ya kuwalaumu na kuwakaripia, «Huu ndio huo Moto ambao mlikuwa mkiukanusha

    [15] «Je, ni uchawi adhabu hii mnayoishuhudia au nyinyi hamtazami

    [16] Onjeni ukali wa Moto huu. Vumilieni uchungu wake na ukali wake au msiyavumilie hayo, hamtahafifishiwa adhabu na hamtatoka humo. Ni sawasawa kwenu nyinyi mkivumilia au mkitovumilia. Hakika nyinyi mnalipwa tu yale mliokuwa mkiyafanya duniani

    [17] Hakika wachamungu watakuwa kwenye mabustani ya Pepo na neema kubwa

    [18] Watajistarehesha kwa vile Alivyowapa Mwenyezi Mungu vya neema miongoni mwa aina mbalimbali za ladha na starehe, na Atawaokoa mwenyezi Mungu kutokana na adhabu ya Moto

    [19] Kuleni chakula kwa furaha, na mnywe kinywaji chenye ladha, yakiwa ni malipo ya matendo mema mliyoyafanya duniani

    [20] Na wao watakuwa wametegemea, wako juu ya vitanda vinavyoelekeana, na tutawaoza wanawake weupe wenye macho mapana yaliyo mazuri

    [21] Na wale walioamini na wakafuatwa na watoto wao katika hiyo Imani, Tutawakutanisha watoto wao nao katika daraja yao Peponi, hata kama hawakufikia matendo ya wazazi wao, ili wazazi wafurahike na watoto wao pamoja na wao katika daraja zao. Watakusanywa baina yao kwenye hali nzuri zaidi, na hatutawapunguzia chochote katika matendo yao mema. Kila mtu anafungwa na matendo yake aliyoyachuma, hatobeba dhambi za watu wengine

    [22] Na tutawaongezea, juu ya starehe hizo zilizotajwa, matunda na nyama miongoni mwa vitu vinavyopendwa na kutamaniwa

    [23] Na miongoni mwa starehe hizo ni kuwa wao watapeana gilasi ya pombe, mmoja wao atampa mwenzake, ili furaha yao ikamilike. Kinywaji hiki kinatafautiana na pombe ya duniani, hakimleweshi akili mwenye kukinywa, wala hakisababishi kubobokwa, wala maneno ya makosa na maasia

    [24] Na watawazunguka watumishi waliotayarishwa kuwatumikia kama kwamba wao katika usafi na weupe na utungaji nidhamu ni lulu iliyohifadhiwa kwenye mashaza yake

    [25] Watageukiana watu wa Peponi kuulizana wao kwa wao juu ya ukubwa wa yale waliyonayo na sababu ya kuyapata

    [26] Watasema, «Sisi tulikuwa kabla, huko duniani, na sisi tuko baina ya watu wetu, tunamuogopa Mola wetu, tuna hadhari na adhabu Yake na mateso yake Siku ya Kiyama

    [27] Mwenyezi Mungu Akatuneemesha kwa uongofu na taufiki na Akatuokoa na adhabu ya vuke la Jahanamu, nalo ni moto wake na joto lake. Sisi tulikuwa, hapo kabla, tukimnyenyekea Yeye Peke Yake, hatumshirikishi na Yeye yoyote asiyekuwa Yeye, Atulinde na adhabu ya vuke la Motoni na Atupeleke kwenye starehe ya Peponi

    [28] Mwenyezi Mungu Akatukubalia maombi yetu, na Akatupa tulichokiomba. Hakika Yeye Ndiye Mwingi wa kheri, Mwenye kurehemu. Na miongoni mwa wingi wa kheri Zake na rehema Zake kwetu ni kule kutupa radhi zake na Pepo, na kutuepusha na hasira Zake na Moto.»

    [29] Basi wawaidhie, ewe Mtume, wale uliotumilizwa kwao kwa Qur’ani, kwani hukuwa wewe, kwa neema ya Mwenyezi Mungu Aliokuneemesha kwayo ya unabii na busara ya akili, ni kuhani anayetoa habari za ghaibu bila ujuzi wala mwendawazimu asiyejua analolisema, kama wanavyodai

    [30] Au wanakwambia hao washirikina, ewe Mtume, «Yeye ni mshairi, tunangojea ashukiwe na mauti»

    [31] Waambie, «Yangojeeni mauti yangu, kwani mimi pamoja na nyinyi ni katika wenye kuingojea adhabu yenu, na mtaona ni nani atakayekuwa na mwisho mwema

    [32] Au zinawaamuru akili zao, hao wakanushaji, ziseme neno hili linalogongana (kuwa sifa ya ukuhani, utungaji mashairi, na wendawazimu haiwezekani kukutana wakati mmoja)? Bali wao ni watu waliruka mipaka katika uasi

    [33] Au wanasema hawa washirikina, «Muhammad Ameibuni Qur’ani yeye mwenyewe?» bali wao hawaamini. Na lau wangaliamini, hawangalilisema walilolisema

    [34] Basi na walete maneno mfano wa Qur’ani iwapo wao ni wakweli katika madai yao kuwa Muhammad Ameibuni

    [35] Je, wameumbwa hawa washirikina bila kuwako mwenye kuwaumba na kuwapatisha au wao wamejiumba wenyewe? Na yote mambo mawili haya yametanguka na hayawezekani. Na kwa hivyo, inalazimika kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyewaumba, na Yeye Peke Yake Ndiye Ambaye hakuna anayepasa kuabudiwa, wala kufaa kuabudiwa, isispokuwa Yeye

    [36] Au wao wameumba mbingu na ardhi kwa utengezaji huu wa kipekee? Bali wao hawaamini adhabu ya Mwenyezi Mungu, kwa kuwa wao ni washirikina

    [37] Au wanazo wao hazina za Mola wako wanazitumia? Au wao ni majebari wanaowagandamiza viumbe vya Mwenyezi Mungu kwa kuwatendesha nguvu na kuwanyanyasa? Mambo si hivyo, bali wao ndio walemevu walio madhaifu

    [38] Au wao wana ngazi ya kupandia mbinguni wanasikiliza huko wahyi kwamba yale waliyonayo ndio haki? Basi na aje, yule anayedai kuwa amesikia hilo, na hoja ya waziwazi yenye kusadikisha madai yake

    [39] Je, mwenyezi Mungu , aliyetakasika, Ana watoto wa kike na nyinyi mna watoto wa kiume kama mnavyodai kwa uzushi na urongo

    [40] Au je unawataka, ewe Mtume, hawa washirikina wakupatie malipo ya kuwafikishia Ujumbe, wakawa wao wana tabu na dhiki ya kujilazimisha malipo unayoyataka kutoka kwao

    [41] Au je wao wana ujuzi wa ghaibu wakawa wanawaandikia watu na kuwapa habari yake? Mambo si hivyo, kwani hakika ya mambo ni kwamba hakuna anayejua ghaibu iliyo mbinguni na ardhini isipokuwa Mwenyezi Mungu

    [42] Bali wao wanataka kumfanyia vitimbi Mtume wa Mwenyezi Mungu na Waumini. Basi hao makafiri, vitimbi vyao na njama zao vitawarudia wao wenyewe

    [43] Au wao wana muabudiwa anayestahiki kuabudiwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu? Ametakasika Mwenyezi Mungu na kutukuka na yale wanayoshirikisha. Kwani Yeye Hana mshirika katika mamlaka, na Hana mshirika katika Upweke na ustahiki wa kuabudiwa

    [44] Na wakikiona hawa washirikina kipande cha mbingu kinawaangukia, kikiwa ni adhabu kwao, hawataacha yale waliyo nayo ya ukanushaji, na watasema, «Haya ni mawingu yamekusanyika na kupandana.»

    [45] Basi waache, ewe Mtume, hawa washirikina mpaka wakutane na Siku yao hiyo ya wao kuangamizwa, nayo ni Siku ya Kiyama

    [46] Katika Siku hiyo havitawazuilia wao vitimbi vyao kotokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu kitu chochote, na hatawanusuru yoyote kuwaokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu

    [47] Hakika madhalimu hawa watakuta adhabu duniani, kabla ya adhabu ya Siku ya Kiyama, ya kuuawa, kukamatwa mateka, adhabu ya kaburini na nyinginezo. Lakini wengi wa watu hawajui hilo

    [48] Na uivumilie, ewe Mtume, hukumu ya Mola wako na amri Yake juu ujumbe Aliyokubebesha na juu ya makero yanayokupata kutoka kwa watu wako, hakika wewe uko kwenye maangalizi yetu, hifadhi na utunzi. Na umtakase Mola Wako kwa kumsifu unaposimama kuswali na unapoinuka kutoka usingizini

    [49] Na kwenye kipindi cha usiku mtakase Mola wako kwa kumsifu, umtukuze na umswalie. Na ufanye hayo kwenye kipindi cha Swala ya Asubuhi wakati wa nyota kuondoka. Katika aya hizi pana kuthibitisha sifa ya macho mawili kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa inavyonasibiana na Yeye, bila kufananisha na viumbe Vyake au kuieleza dhati Yake vile ilivyo, kutakasika na kila sifa ya upungufu ni Kwake na sifa njema zote ni Zake, kama lilivyothibiti hilo katika Sunnah na kukubaliana juu yake wanavyuoni waliopita wa Ummah huu

    Nyota

    Surah 53

    [1] Anaapa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kwa nyota zinapozama zikawa hazionekani

    [2] kwamba Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, hakupotoka kwenye njia ya uongofu na haki, na hakutoka nje ya njia ya usawa. Bali yeye yuko kwenye upeo wa unyofu, usawa na uthabiti

    [3] Kutamka kwake hakutokani na matamanio ya nafsi yake. Haikuwa

    [4] Qur’ani na haikuwa Sunnah isipokuwa ni wahyi unaotoka kwa Mwenyezi Mungu kwa Nabii Wake Muahammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [5] Alimfundisha Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, Malaika mwenye nguvu nyingi

    [6] mwenye mandhari mazuri, naye ni Jibrili, amani imshukie, aliyejitokeza kwa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [7] na akalingana kwa umbo lake la kihakika, kwenye pembe za sehemu za juu, nao ni pembe za jua linapochomoza

    [8] Kisha Jibrili akakaribia kwa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [9] na akazidi kukaribia mpaka ikawa kukaribia kwake ni kiasi cha nyuta mbili au karibu zaidi

    [10] Hapo Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, alimpelekea wahyi mja Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kile alichokituma kwa wahyi kupitia Jibrili, amani imshukie

    [11] Haukukanusha moyo wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kile alichokiona kwa macho yake

    [12] Je mnamkanusha Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amni zimshukie, mkajadiliana naye juu ya kile alichokiona na kukishuhudia miongoni mwa alama za Mola wake

    [13] Na Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, alimuona Jibrili, kwa sura zake za uhakika Alizomuumba nazo Mwenyezi Mungu

    [14] mara nyingine hapo penye Sidrah al-Muntahā- mti wa mkunazi ulio kwenye uwingu wa saba ambapo hapo kinakomea kinachopanda juu kutoka ardhini na kinakomea kinachoshuka chini kutoka juu yake

    [15] Mbele ya mti huo kuna Pepo ya al- Ma’wā (Makazi ya Daima) ambayo waliahidiwa wachamungu

    [16] Pindi huo Mkunazi ulipofinikwa kutokana na amri ya Mwenyezi Mungu na kitu kikubwa hakuna ajuaye sifa zake isipokuwa Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka

    [17] Na Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, alikuwa na sifa kubwa ya uthabiti na utiifu, hayakupotoka macho yake kuliani wala kushotoni, wala hakupitisha zaidi ya kile alichoamrishwa kukiona

    [18] Hakika Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, aliona, usiku wa Mi'rāj (kwenda mbinguni) alama kubwa zinazojulisha uweza wa Mwenyezi Mungu na ukubwa Wake miongoni mwa Pepo, Moto na vinginevyo

    [19] Mnawaonaje, enyi washirikina, waungu hawa mnaowaabudu: Lāta, 'Uzzā

    [20] na mwingine wa tatu ni Manātu, je hao wamenufaisha au kudhuru mpaka wawe ni washirika wa Mwenyezi Mungu

    [21] Je huyu mwanamume mnamfanya ni wenu kwa kuwa mnaridhika naye, na mwanamke ambaye hamridhiki naye nyinyi wenyewe mnamfanya ni wa Mwenyezi Mungu

    [22] Hiko ni kigawanyo cha kidhalimu. Hawakuwa hawa masanamu isipokuwa majina yasiyokuwa na sifa zozote za ukamilifu

    [23] Hayo si chochote isipokuwa ni majina mliyoyaita nyinyi na baba zenu kulingana na matamanio yenu yaliyo batili, Mwenyezi Mungu hakuteremsha ushahidi wowote wa kusadikisha madai yenu juu ya hayo. Hawafuati hawa washirikina isipokuwa dhana na matamanio ya nafsi zao zilizopotoka zikawa kando na maumbile ya sawa. Na hakika yaliwajia wao kutoka kwa Mola wao, kwa ulimi wa Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, yale ambayo ndani yake pana uongofu wao, na wao hawakunufaika nao

    [24] Binadamu hatapata kile anachokitamani cha kuwa waabudiwa hawa au wasiokuwa hawa, katika vitu vinavyotamaniwa na nafsi yake, watamuombea

    [25] Basi ni ya Mwenyezi Mungu amri ya duniani na Akhera

    [26] Na kuna Malaika wengi huko mbinguni, pamoja na vyeo vyao vya juu, kuombea kwao hakunufaishi chochote isipokuwa baada ya Mwenyezi Mungu kuwapa idhini wao waombee na Aridhike na yule mwenye kuombewa

    [27] Hakika wale ambao hawaamini kuwa kuna maisha ya Akhera miongoni mwa makafiri wa Kiarabu wala hawafanyi matendo ya kuwafaa huko, wanawaita Malaika vile wanavyowaita wanawake, kwa kuitakidi kwao kuwa Malaika ni wanawake na kuwa wao ni watoto wa kike wa Mwenyezi Mungu

    [28] Na wao hawana ujuzi wowote ulio sahihi, kuhusu jambo hilo, wenye kusadikisha hayo waliyoyasema. Hawafuati isipokuwa dhana ambayo haifalii kitu na haisimami kabisa mahali pa haki

    [29] Basi mpuuze yule anaoupa mgongo utajo wetu, nao ni Qur’ani, na asitake chochote isipokuwa uhai wa kilimwengu

    [30] Hali hiyo waliyonayo ndio upeo wa ujuzi wao na lengo lao. Hakika Mola wako Ndiye Anayemjua zaidi aliyepotoka kutoka kwenye njia ya uongofu, na Yeye ndiye Anayemjua zaidi aliyeongoka na akafuata njia ya Uislamu.. Hapa pana onyo kali kwa wenye kuasi na kukataa kukitumia Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kufuata mwenendo wa Mtume Wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wenye kufadhilisha matamanio ya nafsi na hadhi za ulimwenguni juu ya Akhera

    [31] Ni ya Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, mamlaka ya vilivyoko mbinguni na vilivyoko ardhini, ili Awalipe wale waliokosa kwa kuwatesa kwa maovu waliyoyafanya na Awalipe Pepo wale waliofanya wema

    [32] nao ni wale wanaojiepusha na madhambi makubwa na machafu isipokuwa dhambi ndogondogo nazo ni dhambi ndogo ambazo haendelei nazo mwenye kuzifanya, au zile ambazo mja amezifanya kwa nadra. Kwani hizo pamoja na kufanya mambo ya wajibu na kujiepusha na mambo ya haramu, Atayasamehe nayo Mwenyezi Mungu na Atawasitiria. Hakika Mola wako ni Mkunjufu wa msamaha. Yeye Anazijua zaidi hali zenu Alipomuumba baba yenu Ādam kwa mchanga, na mlipokuwa bado hamjazaliwa, mko ndani ya matumbo ya mama zenu. Basi msizitakase nafsi zenu, mkazipamba na mkazipa sifa za uchamungu. Yeye Anamjua zaidi anayeogopa mateso Yake miongoni mwa waja Wake na akajiepusha na kufanya mambo ya kumuasi

    [33] Unamuonaje, ewe Mtume, yule anayekataa kumtii Mwenyezi Mungu

    [34] na akatoa kidogo katika mali yake kisha akaacha kutoa na akakata hisani yake

    [35] Je huyu anayekata kheri yake ya kutoa ana ujuzi wa ghaibu kuwa yeye atamalizikiwa na mali yaliyoko mkononi mwake ndipo akaizuia kheri yake asiitoe, na akawa aliona hilo waziwazi? Mambo si hivyo! Hakika ni kwamba yeye aliacha kutoa sadaka na kufanya kheri, kutenda wema na kuunga kizazi kwa ubahili na uchoyo

    [36] Kwani hakupewa habari ya yaliyomo ndani ya kurasa za Taurati

    [37] na nyaraka za Ibrāhīm aliyetekeleza kile alichoamrishwa na akakifikisha

    [38] Kwamba haipatilizwi nafsi yoyote kwa kosa la nafsi nyingine, na mzigo wake hakuna yoyote atakayembebea

    [39] Na kwamba binadamu hapewi malipo isipokuwa kwa kile alichokichuma yeye mwenyewe kwa juhudi zake

    [40] Na kwamba juhudi zake zitaonekana Akhera, yapambanuliwe mazuri yake na mabaya yake, ili kumkirimu mtenda wema na kumlaumu mfanya mabaya

    [41] kisha binadamu atalipwa kwa juhudi zake malipo yenye kuenea kikamilifu matendo yake yote

    [42] Na kwamba kwa Mola wako, ewe Mtume, ndipo watakapokomea viumbe Vyake vyote Siku ya Kiyama

    [43] Na kwamba Yeye, Aliyetukuka na kutakasika, Ndiye Anayemfanya Anayemtaka acheke duniani kwa kumfurahisha, na ndiye Anayemfanya Anayemtaka alie kwa kumpa makero

    [44] Na kwamba Yeye Ndiye Anayemfisha Anayetaka afe miongoni mwa vuimbe Vyake na Ndiye Anayemuhuisha Anayetaka ahuike miongoni mwao. Basi Yeye Ndiye Aliyepwekeka, kutakasika ni Kwake, kwa kuhuisha na kufisha

    [45] Na kwamba Yeye Ameumba jinsi mbili: ya kiume na ya kike, kati ya wanadamu na wanyama

    [46] kutokana na tone la manii linalomiminwa kwenye kizazi

    [47] Na kwamba ni juu ya Mola wako, ewe Mtume, kurejesha uumbaji wao baada ya kufa kwao, na huo ndio uumbaji mwingine Siku ya Kiyama

    [48] Na Yeye Ndiye Anayewatajirisha Anaowataka miongoni mwa viumbe Wake kwa mali, na Ndiye Anayewamilikisha na kuwaridhisha nayo

    [49] Na kwamba Yeye Ndiye Mola wa al-Shi'rā, nayo ni nyota inayong’ara ambayo baadhi ya watu wa zama za Ujinga walikuwa wakiiabudu badala ya Mwenyezi Mungu

    [50] Na kwamba Yeye, Aliyetakasika na kutukuka, Aliwaangamiza 'Ād wa mwanzo, nao ni watu wa Hūd

    [51] Na Akawaangamiza Thamūd, nao ni watu wa Ṣāliḥ, Asimbakishe yoyote katika wao

    [52] Na Akawaangamiza watu wa Nūḥ hapo kabla. Hao walikuwa ni wakali zaidi wa uasi na wakubwa zaidi wa ukafiri kuliko wale waliokuja baada yao

    [53] Na miji ya watu wa Lūṭ, Mwenyezi Mungu Aliipindua juu yao Akazifanya sehemu za juu yake kuwa chini yake

    [54] na Akaifinika mawe yaliyowateremkia kwa mfululiza kutoka juu kama mvua

    [55] Basi ni neema zipi za Mola wako, ewe binadamu mkanushaji, unazifanyia shaka

    [56] Huyu Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ni mwonyaji wa haki ambayo kwayo walionya Manabii kabla yake, si kitu kipya katika Mitume

    [57] Kiyama kimekaribia na wakati wake umekaribia

    [58] Hivyo basi hakuna yoyote mwenye kukizuia isipokuwa Mwenyezi Mungu, na hakuna mwenye kujua wakati wa kufika kwake isipokuwa Mwenyezi Mungu

    [59] Je hii Qur’ani mnaionea ajabu, enyi washirikina, kuwa ni sahihi

    [60] Na mnaicheka kwa shere nastihzai na hamlii kwa kuogopa maonyo yake

    [61] na hali nyinyi mnapumbaa na mmeipa mgongo

    [62] Basi msujudieni Mwenyezi Mungu na mtakasieni Ibada Yeye Peke Yake, Na mumuachie Yeye mambo yenu

    Mwezi

    Surah 54

    [1] Kimekaribia Kiyama na mwezi umepasuka pande mbili, pale makafiri wa Makkah walipomtaka Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshikie, awaoneshe alama, na yeye akamuomba Mwenyezi Mungu na akawaonesha hiyo alama

    [2] Na washirikina wakiiona dalili na ushahidi juu ya ukweli wa Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wanakataa kuziamini na kuzisadiki hali ya kukanusha na kupinga, na wanasema baada ya dalili kujitokeza, «Huu ni uchawi wenye ubatilifu na wenye kuondoka na kupotea usiokuwa na sifa ya kudumu

    [3] Na walimkanusha Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wakafuata upotevu wao na kile cha ukanushaji ambacho matamanio yao yaliwavuta kwacho. Na kila jambo, la kheri au la shari, litawashukia wanaostahili Siku ya Kiyama yatakapodhihiri malipo na mateso

    [4] Na hakika ziliwajia makafiri wa Kikureshi habari za ummah waliokanusha mitume wao na adhabu iliyowashukia zinazotosha kuwakemea na kuwafanya warudi nyuma waache ukafiri wao na upotevu wao

    [5] Hii Qur’ani iliowajia ni hekima kubwa iliyofikia upeo. Basi yatawafalia nini maonyo wale watu waliyoipa mgongo na kuikanusha

    [6] Kwa hivyo, wapuuze, ewe Mtume, na uingojee Siku kubwa, Siku Malaika Atakapoita, kwa kuvuvia kwenye baragumu, kwenye jambo linalotisha linalochukiza, nalo ni Kisimamo cha Hesabu

    [7] Hali yakuwa macho yao yamedhalilika, wanatoka makaburini kama kwamba wao kwa kuenea kwao na upesi wa kuenda kwenye kuhesabiwa, ni nzige walioenea pambizoni mwa anga

    [8] hali ya kukimbilia kile walichoitiwa. Hapo waseme makafiri, «Hii ni siku nzito yenye vituko vikubwa.»

    [9] Walikanusha kabla ya watu wako, ewe Mtume, watu wa Nūḥ wakamkanusha mja wetu Nūḥ na wakasema, «Yeye ni Mwendawazimu.» Wakamkaripia huku wakimtisha kwa aina nyingi za mateso iwapo hatakomeka na ulinganizi wake

    [10] Nūḥ akamuomba Mola wake kwamba «mimi ni dhaifu wa kupambana na hawa, basi nisaidie mimi kwa kuwapa mateso yanayotoka kwako kwa kukukanusha wewe.»

    [11] Basi tukayakubali maombi yake, na tukafungua milango ya mbingu kwa maji mengi yenye kuteremka kwa nguvu

    [12] na tukapasua ardhi tukatoa chemchemi za maji yanayotoka kwa kasi, yakakutana maji ya mbinguni na maji ya ardhini kuwaangamiza wao kwa vile Alivyowakadiria mwenyezi Mungu, yakiwa ni malipo ya ushirikina wao

    [13] Tukambeba Nūḥ na waliokuwa pamoja naye juu ya jahazi ya mbao zilizopigwa misumari

    [14] ikawa inatembea kwa uangalizi wetu na utunzi, na tukawazamisha waliokanusha, ikiwa ni malipo yao kwa ukafiri wao na kwa kumnusuru Nūḥ, amani imshukie. Hapa pana dalili ya kuthibitisha sifa ya macho mawili kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, kama inavyonasibiana na Yeye

    [15] Na kwa hakika tulikibakisha kisa cha Nūḥ pamoja na watu wake kiwe ni mazingatio na dalili ya uweza wetu kwa walio baada ya Nūḥ, ili wazingatie na wawaidhike kwa lililowapata ummah huu uliokanusha Mtume wao

    [16] basi je kuna wakuwaidhika awaidhike? Na ilikuwa vipi adhabu yangu na maonyo yangu kwa aliyenikufuru mimi, akawakanusha Mitume wangu na asiwaidhike kwa walichokuja nacho? Hakika hiyo ilikuwa kubwa yenye uchungu

    [17] Kwa hakika tumeyasahilisha matamko ya Qur’ani ili isomwe na ihifadhiwe, na pia maana yake ili ieleweke na izingatiwe. Je kuna mwenye kuwaidhika nayo? Katika aya hii na mfano wake katika hii Sura kuna kuhimiza kusoma Qur’ani kwa wingi, kujifunza na kuifundisha

    [18] Watu wa kabila la 'Ād walimkanusha Hūd tukawatesa, basi ilikuwa vipi vile nilivyowaadhibu wao kwa ukafiri wao na vile nilivyowaonya wao kwa kumkanusha Mtume wao na kutomuamini? Ilikuwa kubwa yenye uchungu

    [19] Hakika sisi tuliwapelekea upepo wenye baridi kali katika siku korofi yenye kuendelea kwao kwa adhabu na maangamivu

    [20] yenye kung’oa watu kutoka mahali walipo kwenye ardhi na kuwatupa kwa vichwa vyao, kuzivunja shingo zao na kuvipambanua vichwa vyao na miili yao na kuwaacha kama mitende iliyong’olewa kutoka mashinani

    [21] Basi ilikuwa vipi adhabu yangu na onyo langu kwa aliyenikufuru na akawakanusha Mitume wangu na Asiwaamini? Hakika ilikuwa kubwa yenye uchungu

    [22] Na kwa hakika tumeyasahilisha matamko ya Qur’ani, ili isomwe na ihifadhiwe, na tumeyasahilisha maana yake, ili ieleweke na izingatiwe kwa anayetaka kuwaaidhika na kuzingatia. Je kuna yoyote mwenye kuwaidhika nayo? Hapa pana kuhimiza kusoma Qur’ani kwa wingi, kujifunza na kufundisha

    [23] Walizikanusha watu wa kabila la Thamūd, nao ni watu wa Ṣāliḥ, alama ambazo walionywa nazo

    [24] wakasema, «Je tumfuate binadamu mmoja miongoni mwetu na hali sisi ni wengi na yeye ni mmoja? Tukifanya hivyo tutakuwa mbali na usawa na tutakuwa ni wenye wazimu

    [25] «Je Ameteremshiwa wahyi na kuhusishwa yeye pekee kwa utume miongoni mwetu, na hali yeye ni mmoja katika sisi? Bali yeye ana urongo mwingi na kiburi.»

    [26] Basi wataona wakati wa adhabu kuwateremkia hapa duniani na huko Akhera, ni nani mrongo mwenye kiburi

    [27] Sisi tutamtoa ngamia waliomtaka kutoka kwenye jiwe, huo ukiwa ni mtihani kwao. Basi ingojee, ewe Ṣāliḥ, adhabu itakaowashukia, na usubiri katika kuwalingania na juu ya makero wanayokufanyia

    [28] Na uwape habari kwamba maji yamegawanywa baina ya watu wako na ngamia: ngamia ana siku yake na nyinyi mna siku yenu, kila siku ya kunywa atakuja yule ambaye ni siku yake aliyogawanyiwa, na atakatazwa yule ambaye si siku yake aliyogawanyiwa

    [29] Wakamuita mwenzao wakimshawishi amchinje, basi akamshika yule ngamia kwa mkono wake na akamchinja, na mimi nikawatesa

    [30] basi ilikuwa vipi nilivyowaadhibu kwa ukafiri wao na nilivyowaonya waliowaasi Mitume wangu? Hakika hiyo ilikuwa adhabu kubwa yenye uchungu

    [31] Sisi tuliwateremshia Jibrili, akawapigia ukulele mmoja, wakatoeka hadi wa mwisho wao, wakawa ni kama nyasi zilizokauka zilizo nyepesi kuvunjika, zinazofanyiwa boma la ngamia na mifugo

    [32] Na kwa hakika tumeyasahilisha matamko ya Qur’ani, ili isomwe na ihifadhiwe, na tumeyasahilisha maana yake, ili ifahamike na izingatiwe kwa anayetaka kuwaidhika na kuzingatia. Basi je kuna yoyote mwenye kuwaidhika nayo

    [33] Walizikanusha watu wa Lūṭ aya za Mwenyezi Mungu walioonywa nazo

    [34] Sisi tuliwateremshia upepo mkali unaowarushia mawe, isipokuwa watu wa Lūṭ wa nyumbani, kwani wao tuliwaokoa na adhabu kipindi cha mwisho wa usiku

    [35] ikiwa ni neema itokayo kwetu juu yao. Kama tulivyompa malipo mema Lūṭ na watu wake wa nyumbani, tukawapa neema na tukawaokoa na adhabu yetu ndivyo tunavyowalipa mema waliotuamini na kutushukuru

    [36] Kwa hakika Lūṭ aliwaonya watu wake mateso ya Mwenyezi Mungu na adhabu Yake, wasimsikilize, bali walilifanyia shaka hilo na wakamkanusha

    [37] Na kwa hakika walitaka kwake kufanya uchafu na wageni wake ambao ni Malaika, tukayafuta macho yao wasione chochote na wakaambiwa, «Onjeni adhabu yangu na onyo langu alilowaonya nalo Lūṭ, amani imshukie.»

    [38] Na iliwajia kipindi cha asubuhi adhabu ya kuendelea, imejikita kwao mpaka iwafikishe kwenye adhabu ya Akhera. Adhabu yenyewe ni kuvurumizwa mawe na kuipindua miji yao kwa namna ambayo kulikokuwa juu kukawa chini

    [39] na wakaambiwa, «Onjeni adhabu yangu niliyowateremshia nyinyi kwa sababu ya ukafiri wenu na ukanushaji wenu onyo langu alilowaonya nalo Lūṭ, amani imshukie

    [40] Na kwa hakika tumeyasahilisha matamko ya Qur’ani, ili isomwe na ihifadhiwe, na tumeyasahilisha maana yake, ili ifahamike na izingatiwe kwa anayetaka kuwaidhika na kuzingatia. Basi je kuna mwenye kuwaidhika nayo

    [41] Kwa hakika lilimjia Fir'awn na watu wake onyo letu la kuwatesa kwa ukafiri wao

    [42] Walizikanusha dalili zetu zote zenye kutolea ushahidi upweke wetu na unabii wa Manabii wetu, tukawatesa kwa adhabu mateso ya Mshindi Asiyeshindwa, Mweza wa Analolitaka

    [43] Je makafiri wenu, enyi mkusanyiko wa Makureshi, ni bora kuliko wale waliotangulia kutajwa miongoni mwa wale walioangamia kwa sababu ya kukanusha kwao? Au nyinyi mmeepushwa na mateso ya Mwenyezi Mungu kwa yaliyomo kwenye Vitabu vilivyoteremshwa kwa Mitume kwa kuwa mtasalimika na mateso

    [44] Au kwani wanasema makafiri wa Makkah, «Sisi ndio wenye ushupavu na busara, na jambo letu ni la pamoja. Sisi ni watu wa ushindi, na hatatushinda anayetutaka kwa ubaya.?»

    [45] Utashindwa mkusanyiko wa makafiri wa Makkah mbele ya Waislamu na watakimbia. Na hili lilitokea siku ya vita vya Badr

    [46] Na wakati wa Kiyama ambao ndio agizo la wao kulipwa wanachostahiki, na Wakati wa Kiyama ni mkubwa na mgumu zaidi kuliko adhabu iliyowafika siku ya Badr

    [47] Hakika wahalifu wa ukafiri wako katika hali ya kuduwaa kutoijua haki na wako kwenye usumbufu na adhabu

    [48] Siku watakapokokotwa ndani ya Moto kwa nyuso zao na waambiwe, «Onjeni ukali wa adhabu ya moto wa Jahanamu.»

    [49] Hakika sisi kila kitu tumekiumba kwa kipimo tulichokikadiri na kukipitisha, na ilitangulia elimu yetu ya kukijua kitu hiko na kukiandika kwenye Ubao Uliohifadhiwa

    [50] Na haikuwa amri yetu ya kuamuru jambo tukitaka liwe isipokuwa ni kuliambia neno moja nalo ni «kuwa» nalo likawa palepale kama vile kupeleka jicho kuangalia kitu, haichelewi hata kiasi cha jicho kupepesa

    [51] Na kwa hakika tuliwaangamiza wale waliofanana na nyinyi katika ukafiri miongoni mwa ummah waliopita. Basi je, kuna mwenye kuwaidhika kwa mateso na adhabu

    [52] Na kila kitu walichokifanya wale wanaofanana na nyinyi waliopita, cha kheri au cha shari, kimeandikwa kwenye Vitabu ambavyo Malaika watunzi wenye kudhibiti waliviandika

    [53] Na kila dogo au kubwa katika matendo yao limesajiliwa ndani ya madaftari yao, na watalipwa kwayo

    [54] Hakika wachamungu watakuwa kwenye mabustani ya Pepo makubwa na mito mipana Siku ya Kiyama

    [55] Kwenye kikao cha haki, kisochokuwa na maneno ya upuuzi wala ya kuwatia madhambini, mbele ya Mwenyezi Mungu, Aliye Mfalme Mkubwa, Muumba vitu vyote, Mwenye uweza wa kila kitu, Aliyetukuka na kuwa juu

    Arrahmani

    Surah 55

    [1] mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema

    [2] Amemfundisha binadamu Qur’ani kwa kurahisisha kuisoma, kuihifadhi na kuelewa maana yake

    [3] Amemuumba binadamu

    [4] Amemfundisha ufasaha wa kujieleza ili kumtenganisha na wengine

    [5] Jua na mwezi zinatembea kwa kufuatana, moja baada ya nyingine, kwa hesabu madhubuti isiyotafautiana wala kugongana

    [6] Na nyota iliyo mbinguni na miti ya ardhini, vinamjua Mola wao, vinamsujudia na vinanyosha shingo zao kufuata vile ambavyo vimepangiwa vifuate vya maslahi ya waja Wake na manufaa yao

    [7] Na mbingu Ameiinua na kuifanya iwe juu ya ardhi, Na Ameweka kwenye ardhi uadilifu Aliouamrisha na kuulazimisha kwa waja Wake

    [8] Ili msipite mipaka na msimfanyie hiyana mnayempimia

    [9] Na simamisheni upimaji kwa usawa na msipunguze mizani mnapowapimia watu

    [10] Na ardhi Ameiweka na Ameitayarisha, ili viumbe vitulie juu yake

    [11] Humo mna matunda na mitende yenye makarara ya matunda. Na humo kuna nafaka zenye maganda, vikiwa ni chakula chenu na wanyama wenu

    [12] Na humo mna kila mmea wenye harufu nzuri

    [13] Bas ni neema gani za Mola wenu, za kidini na za kidunia, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha? Na ni jawabu nzuri ilioje ya majini alipowasomea wao Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, sura hii, kila akipita kwenye aya hii walikuwa wakisema, «Hakuna chochote miongoni mwa neema zako, ewe Mola wetu, tunachokanusha. Sifa njema zote ni zako.» Na hivi ndivyo inavyotakiwa kwa mja anapoelezewa neema za Mwenyezi Mungu na mema Yake akubali na amshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema hizo

    [14] Amemuumba baba wa wanadamu, naye ni Ādam, kwa udongo mkavu kama vyungu

    [15] Na Amemuumba Iblisi, naye ni katika majini, kwa mroromo wa moto uliochanganyika

    [16] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [17] Mola wa pande mbili za Mashariki ya jua, katika kusi na kaskazi, na Mola wa pande mbili za Magharibi ya jua, katika kusi na kaskazi, kwani vyote viko chini ya uendeshaji Wake na ulezi Wake

    [18] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [19] Mwenyezi Mungu Ameyachanganya maji ya bahari mbili, tamu na chumvi, yanakutana, baina yake kuna kizuizi

    [20] mojawapo haiingii sehemu ya nyingine na kuiondoa sifa yake, bali ya tamu inasalia kuwa tamu na ya chumvi inasalia kuwa chumvi pamoja na kukutana kwake

    [21] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [22] Inatoka kwenye bahari mbili hizo, kwa uweza wa Mwenyezi Mungu, lulu na marjani

    [23] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [24] Ni Yake Yeye, Aliyetakasika na kutukuka, mamlaka ya kuyaendesha majahazi makubwa yanayotembea baharini kwa manufaa ya watu, yenye kusimamisha juu milongoti yake na matanga yake kama vile majabali

    [25] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu mnazikanusha

    [26] Kila aliye juu ya uso wa ardhi miongoni mwa viumbe ni mwenye kuangamia

    [27] na utasalia uso wa Mola wako Mwenye utukufu, ubora, kheri nyingi na upaji. Katika aya hii pana kuthibitisha sifa ya uso kwa Mwenyezi Mungu kwa namna inavyonasibiana na Yeye, kutakasika ni Kwake, bila kufananisha wala kueleza namna ulivyo

    [28] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [29] Wanamuomba Yeye walioko mbinguni na ardhini haja zao. Hakuna yoyote anayejitosheleza kutomhitajia Yeye, kutakasika ni Kwake. Kila siku Yeye Yuko kwenye jambo: Anatukuza na Anatweza, Anatoa na Anazuia

    [30] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [31] Nitawatengea kipindi cha kuwahesabu na kuwalipa kwa matendo yenu mliyoyafanya, enyi vizito viwili:-majini na binadamu-, tuwatese watu wa maasia na tuwape malipo mema watu wa utiifu

    [32] Ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [33] Enyi mkusanyiko wa majini na binadamu! Mkiweza kuihepa amri ya Mwenyezi Mungu na uamuzi Wake kwa kukimbia kwenye pambe za mbingu na ardhi basi fanyeni, na hamuwezi kufanya hivyo isipokuwa kwa nguvu na hoja na amri inayotoka kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. (Na vipi mtaweza kufanya hivyo na hali nyinyi hamzimilikii nafsi zenu manufaa yoyote wala madhara)

    [34] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [35] Mtatumiwa mroromo wa moto na shaba iliyoyayushwa, mmiminiwe juu ya vichwa vyenu msiweze kusaidiana

    [36] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazukanusha

    [37] Na pindi mbingu itakapopasuka na kuachana Siku ya Kiyama, ikawa nyekundu kama rangi ya waridi na kama mafuta yaliyochemshwa na risasi iliyoyayushwa, kutokana na mambo magumu na vituko vya Siku ya Kiyama

    [38] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [39] Katika Siku hiyo Malaika hawatawauliza wale wahalifu, miongoni mwa binadamu na majini, kuhusu dhambi zao

    [40] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [41] Malaika watawajua wahalifu kwa alama zao, hapo wawashike kwenye paa za vichwa vyao na nyayo zao wawarushe Motoni

    [42] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [43] Wataambiwa hao wahalifu kwa njia ya kulaumiwa na kudhalilishwa, «Huu ndio moto wa Jahanamu ambao wahalifu duniani walikuwa wakiukanusha

    [44] mara wanaadhibiwa kwenye Jaḥīm, na mara nyingine wananyweshwa Hāmīm, nacho ni kinywaji kilichofikia upeo wa ukali wa moto, kinakata tumbo na sehemu za ndani ya mbavu

    [45] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu mnazikanusha

    [46] Na anayemcha Mwenyezi Mungu, miongoni mwa waja Wake binadamu na majini, akaogopa kusimama kwake mbele Yake, akamtii na akaacha kumuasi atakuwa na mabustani mawili ya Pepo

    [47] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [48] Mabustani mawili hayo ya Pepo yana matawi yaliyostawi kwa matunda ya kila aina

    [49] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [50] Katika Pepo mbili hizo kuna chemchemi mbili za maji zinazopita katikati yake

    [51] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [52] Katika mabustani hayo mawili ya Pepo kuna sampuli mbili za kila aina ya matunda

    [53] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [54] Na wale wanaoogopa kusimama mbele ya Mola Wao watakuwa na mabustani mawili ya Pepo, ambayo ndani yake watastarehe, hali ya kutegemea juu ya matandiko yaliyojazwa dibaji nzito. Na matunda ya mabustani mawili hayo ya pepo yako karibu nao

    [55] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mtazikanusha

    [56] Katika matandiko hayo wapo wake macho yao yanawatazama waume zao tu, hawawatazami wengineo, wamefungamana na wao. Hakuna aliyewaingilia, kabla ya hao waume zao, binadamu yoyote wala jini

    [57] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadanu, mnazikanusha

    [58] Kama kwamba hawa wake wa kihurulaini ni yakuti na marijani katika sifa zao na uzuri wao

    [59] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa najini na binadamu , mnazikanusha

    [60] Je atakuwa na malipo yoyote, huyu aliyekuwa mwema wa matendo duniani, isipokuwa ni afanyiwe wema kwa kupewa Pepo huko Akhera

    [61] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [62] Na chini ya mabustani ya Pepo mawili yaliyotangulia kuna mabustani ya Pepo mawili mengine

    [63] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [64] Mabustani haya mawili ni rangi ya kijani. Ujani wake umeiva sana mapaka umeingia kwenye weusi

    [65] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [66] Ndani ya mabustani mawili hayo ya Peponi kuna chemchemi mbili zenye kububujika maji daima bila kukatika

    [67] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [68] Kwenye mabustani hayo mawili kuna aina za matunda, mitende na mikomamanga

    [69] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [70] Ndani ya mabustani haya manne ya Pepo kuna wake walio wema wa tabia na wazuri wa nyuso

    [71] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [72] Mahurulaini wakunjufu wa macho, waliositiriwa na kuhifadhiwa mahemani

    [73] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [74] Hawajaingiliwa Mahurulaini hawa na binadamu yoyote wala jini kabla ya waume zao

    [75] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [76] Hali ya kuwa wametegemea kwenye mito yenye mifuko rangi ya kijani na matandiko mazuri

    [77] Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha

    [78] Zimekithiri mno baraka za Jina la Mola wako, na kheri Zake zimekuwa nyingi, Mwenye haiba kubwa, utukufu wenye kukamilika na takrima kwa wenye kumtegemea Yeye

    Al Waaqia

    Surah 56

    [1] Kitakaposimama Kiyama

    [2] Hakutakuwa na yoyote mwenye kukanusha kusimama kwake

    [3] Ni chenye kuwainamisha chini maadui wa Mwenyezi Mungu ndani ya Moto na ni chenye kuwainua juu Peponi wale wenye kumtegemea

    [4] Itakapotikiswa ardhi mtikiso wa nguvu

    [5] Na yakamumunyuliwa majabali mmumunyuo wa kina

    [6] Yakawa vumbi lenye kuruka angani lililosukumwa na upepo

    [7] Na mkawa, enyi viumbe, makundi matatu

    [8] Kundi la watu wa upande wa kulia, wenye daraja kubwa. Ni kikubwa kilioje cheo chao

    [9] Kuna na kundi la watu wa upande wa kushoto, wenye daraja duni. Ni mbaya iliyoje hali yao

    [10] Na wale waliotangulia mbele kwenye kheri duniani ndio wenye kutangulia mbele kwenye daraja za juu huko Akhera

    [11] Wao ndio walioletwa karibu kwa Mwenyezi Mungu

    [12] Mola wao Atawatia kwenye mabustani ya Pepo ya starehe

    [13] Watayaingia watu wengi watu wa mwanzo wa ummah huu, na ummah wengineo wasiokuwa wao

    [14] na wachache miongoni mwa watu mwisho wa ummah huu

    [15] wakiwa juu ya vitanda vilivyofumwa kwa dhahabu

    [16] na wakiwa katika hali ya kuvitegemea na huku wanaelekeana na kukutana

    [17] Wanawazunguka wao kuwatumikia watumishi vijana wasiozeeka wala kufa

    [18] wakiwa na vikombe, mabirika na gilasi kutoka kwenye chemchemi ya pombe yenye kupita ndani ya Pepo

    [19] na hawaumwi na vichwa kutokana nayo wala hawarukwi na akili

    [20] Na watawazunguka wao watumishi vijana na kila kitu wanachokichagua miongoni mwa matunda

    [21] nyama ya ndege ambayo nafsi zao inavutika nayo

    [22] Na watakuwa na wanawake wenye macho makubwa kama kwamba wao

    [23] kwa usafi wao na uzuri wao, ni lulu iliyohifadhiwa ndani ya mashaza yake

    [24] hali hayo yakiwa ni malipo yao kwa yale waliokuwa wakiyafanya duniani

    [25] Hawatasikia humo Peponi ubatilifu wala yale ya kuwatia madhambini kuyasikia

    [26] isipokuwa maneno yasiyokuwa na kasoro hizi na kusalimiana wao kwa wao

    [27] Na watu wa upande wa kulia

    [28] ni kikubwa kilioje cheo chao na malipo yao

    [29] Watakuwa kwenye mikunazi isiyo na miba, na ndizi zilizopandana na kupangika

    [30] kila ndizi juu ya nyingine, na vivuli vya daima visivyoondoka

    [31] na maji yanayotembea yasiyokatika

    [32] na matunda mengi

    [33] yasiyomalizika wala kuwaishia wala hakuna kizuizi chochote kinachowazuia wao kuyafikia

    [34] na matandiko yaliyoinuliwa juu ya vitanda

    [35] Sisi tumewaumba wanawake wa watu wa Peponi umbile ambalo silo lile umbile lililokuwa duniani, umbile lililokamilika lisilokubali kutoweka

    [36] na tumewafanya ni wanawali wenye kujipendekeza kwa waume zao

    [37] hali ya kuwa ni marika na wao kimiaka

    [38] Tumewaumbia wanawake hao watu wa upande wa kulia

    [39] Nao ni kundi la watu wengi wa mwanzo

    [40] na kundi la watu wengi wa mwisho

    [41] Na watu wa upande wa kushoto, ni mbaya iliyoje hali yao na malipo yao

    [42] Watakuwa kwenye upepo ulio moto utokanao na joto la Moto wa Jahanamu utakaozuia pumzi zao, na maji moto yanayochemka

    [43] na kivuli cha moshi mweusi sana

    [44] usio na mashukio baridi wala mandhari mazuri

    [45] Kwani wao walikuwa duniani wakijistarehesha kwa vitu vya haramu wakijiepusha na yale ambayo Mitume walikuja nayo

    [46] Na walikuwa wamesimama wima katika kumkanusha Mwenyezi Mungu na kumshirikisha na kumuasi, na hawakuwa na nia ya kutubia kwa hayo

    [47] Na walikuwa wakisema hali ya kukanusha Ufufuzi, «Je hivi sisi tutafufuliwa tutakapokufa na tukawa mchanga na mifupa iliyochakaa?» Maneno yao hayo yanaonesha kuwa wao walikuwa wakiliona jambo hili la kufufuliwa kuwa liko mbali na ukweli na wakilikanusha

    [48] «Je tutafufuliwa sisi na hali baba zetu waliotangulia wamekuwa mchanga uliotapakaa kwenye ardhi?»

    [49] Sema uwaambie, «Hakika wa mwanzo na wa mwisho miongoni mwa binadamu

    [50] watakusanywa katika Siku iliyowekewa wakati maalumu, nayo ni Siku ya Kiyama

    [51] «Kisha nyinyi, enyi mliopotea njia ya uongofu mnaokanusha onyo la Mwenyezi Mungu na agizo Lake

    [52] ni wenye kula kutokana na mti wa zaqqūm

    [53] nao ni katika miti mibaya zaidi, na ni wenye kujaza matumbo yenu kutokana nao kwa sababu ya ukali wa njaa

    [54] na ni wenye kunywa juu yake maji yaliyo moto hadi ya mwisho, yasiyomaliza kiu

    [55] Mtayanywa maji hayo kwa wingi kama vile ngamia wenye kiu wasioshiba maji kwa ugonjwa uliowapata.»

    [56] Adhabu hii watakayoipata ndiyo zawadi Aliyowaandalia Siku ya Kiyama. Katika haya kuna kuwalaumu na kuwacheza shere

    [57] Sisi tumewaumba, enyi watu, na hamkuwa kitu chochote. Basi si msadiki kuwa kuna kufufuliwa

    [58] Mnayaonaje maji ya manii mnayoyatupa ndani ya vizazi vya wake zenu

    [59] je nyinyi ndio mnaomuumba mwanadamu kutokana na hayo au ni sisi ndio wenye kuumba

    [60] Sisi tumekadiria kifo kwenu

    [61] na sisi si wenye kushindwa kubadilisha umbo lenu Siku ya Kiyama na kuwaumba kwa sifa na namna msizozijua

    [62] Na hakika mlijua kuwa Mwenyezi Mungu Aliwaumba uumbaji wa kwanza na hamkuwa kitu chochote. Basi si mkumbuke uweza wa Mwenyezi Mungu wa kuwaumba mara nyingine

    [63] Mnazionaje mbegu mnazozipanda

    [64] Je ni nyinyi mnaoziotesha kutoka ardhini? Sisi ndio tuaozituliza na kuziotesha ardhini

    [65] Lau tungalitaka tungaliifanya mimea inayotokana na mbegu hizo kuwa mapepe, haimkiniki kunufaika nayo kwa kula

    [66] mkawa mnaona ajabu kwa kilichoshukia mimea yenu na mnasema, «Sisi tumepata hasara na ni wenye kuungulika

    [67] Bali sisi tumekoseshwa riziki.»

    [68] Mnayaonaje maji mnayokunywa ili mhuike kwayo

    [69] Je ni nyinyi mliyoyateremsha kutoka kwenye mawingu hadi kwenye kituo cha ardhi au ni sisi tuliyoyateremsha ili kuwarehemu nyinyi

    [70] Lau tungalitaka tungaliyafanya maji haya yawe na chumvi sana, ikiwa haiwezekani kunufaika nayo kwa kunywa wala kwa mimea. Basi si mumshukuru Mola wenu kwa kuteremsha maji tamu kwa kuwanufaisha nyinyi

    [71] Mnaouonaje moto mnaouwasha

    [72] Je ni nyinyi mlioufanya mti wake, unaozalisha moto kwa kukwaruzwa, upatikane au ni sisi tulioufanya upatikane

    [73] Sisi tumeufanya moto wenu mnaouwasha ni ukumbusho kwenu wa Moto wa Jahanamu na pia ni manufaa kwa wasafiri

    [74] Basi mtakase Mola wako, ewe Nabii, Aliye mtukufu Mwenye ukamilifu wa majina na sifa, Mwingi wa wema na kheri

    [75] Mwenyezi Mungu Anaapa kwa mapomoko ya nyota nyakati za kuzama kwake mbinguni

    [76] Nacho ni kiapo kikubwa lau mnajua kadiri yake

    [77] Hakika hii Qur’ani iliyoteremshiwa Muhammad ni Qur’ani yenye manufaa makubwa, yenye kheri nyingi na yenye elimu tele

    [78] iliyo ndani ya Kitabu kilichohifadhiwa, kilichofichwa na macho ya viumbe, nacho ni Kitabu ambacho kiko mikononi mwa Malaika

    [79] Hawaigusi Qur’ani isipokuwa malaika watukufu ambao Mwenyezi Mungu Amewasafisha na aibu na madhambi. Na pia hawaigusi isipokuwa watu waliojitohirisha na ushirikina na janaba na ukosefu wa udhu

    [80] Na hii Qur’ani tukufu imeteremshwa kutoka kwa Mola wa viumbe vyote, kwani hiyo ndiyo haki isiyo na shaka ndani yake

    [81] je hii Qur’ani, enyi washirikina, mnaikanusha

    [82] Na je mnaifanya shukrani yenu kwa neema za Mola wenu ni kuwa nyinyi mnazikanusha na kukufuru? Hapa pana makaripio kwa anayedharau amri za Qur’ani na kutojali mwito wake

    [83] Basi je mnaweza pindi roho ya mmoja wenu inapofika kwenye koo katika uchungu wa kifo

    [84] na hali nyinyi mmehudhuria mnamtazama, kuizuia roho yake ndani ya mwili wake? Hamtaweza hilo

    [85] Na sisi tuko karibu na yeye zaidi, kupitia Malaika wetu, kuliko nyinyi, lakini nyinyi hamuwaoni

    [86] Na je mnaweza, iwapo nyinyi si wenye kuhesabiwa wala kulipwa kwa matendo yenu

    [87] kuirudisha roho kwenye mwili, iwapo nyinyi ni wakweli? Hamtaweza kuirudisha

    [88] Basi iwapo yule anayekufa ni kati ya watu wa upande wa kulia, atapata rehema kunjufu na furaha

    [89] wakati wa kufa kwake, na kila kinachoifurahisha nafsi yake, Na atapata Pepo ya starehe huko Akhera

    [90] Na iwapo yule anayekufa ni kati ya watu wa upande wa kulia

    [91] ataambiwa, «Umesalimika na kuwa kwenye amani, kwa kuwa wewe ni miongoni mwa watu wa upande wa kulia.»

    [92] Na iwapo yule anayekufa ni miongoni mwa wenye kukanusha kufufuliwa, waliopotoka na njia ya uongofu

    [93] basi atapata makaribisho ya kinywaji cha moto wa Jahanamu kilichochemshwa, kilicho na joto hadi ya mwisho

    [94] na atachomwa na Moto na aungulike na adhabu yake kali

    [95] Hakika habari hii tumezokuelezea, ewe Mtume, ni ukweli wa yakini usio na shaka

    [96] Basi litakase jina la Mola wako Aliyetukuka na umtakase na yale ambayo madhalimu na wenye kukanusha wanayasema. Mwenyezi Mungu Yuko juu ya yale wanayoyasema ujuu mkubwa sana

    Chuma

    Surah 57

    [1] Vinamtakasa Mwenyezi Mungu viumbe Vyake vyote vilivyoko mbinguni na ardhini. Na Yeye ni Mshindi juu ya viumbe Vyake, Mwingi wa hekima katika uendeshaji mambo yao

    [2] Ni Yake mamlaka ya mbinguni na ardhini na vilivyomo ndani yake. Yeye Ndiye Mmiliki Mwenye kuendesha mambo ya viumbe Vyake, Anahuisha na kufisha, na Yeye juu ya kila kitu ni Muweza, hakuna kinachomshinda Akikitaka kifanyike, Anachokitaka kinakuwa, na Asichokitaka hakiwi

    [3] Yeye Ndiye wa Mwanzo Ambaye hakukuwa na chochote kabla Yake, na Ndiye wa Mwisho Ambaye hakuna kitu chochote baada Yake, na Ndiye Aliyejitokeza Ambaye hakuna kitu chochote juu Yake, na Ndiye wa ndani Ambaye hakuna kitu chochote kilicho karibu kuliko Yeye, na hakuna chochote kinachofichamana Kwake ardhini wala mbinguni, na Yeye ni Mjuzi wa kila kitu

    [4] Yeye Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi kisha Akawa juu ya 'Arsh Yake iliyo juu ya viumbe Vyake vyote kuwa Juu kunakonasibiana na utukufu Wake. Anavijua vinavyoingia ardhini, miongoni mwa mbegu, mvua na visivyokuwa hivyo, na vinavyotoka humo miongoni mwa mimea, nafaka na matunda, na vinavyoshuka kutoka mbinguni, miongoni mwa mvua na vinginevyo, na vinvyopanda huko, miongoni mwa Malaika na matendo ( ya awaja), na Yeye , kutakasika ni Kwake, Yuko pamoja na nyinyi kwa ujuzi Wake popote mnapokuwa. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona matendo yenu mnayoyafanya na Atawalipa kwayo

    [5] Ni Yake mamlaka ya mbinguni na ardhini, na Kwake Mwenyezi Mungu ndiko mwisho wa mambo ya viumbe huko Akhera na Atawalipa wao kwa matendo yao

    [6] Anazitia saa za usiku zilizopungua ndani ya mchana na hivyo basi mchana ukaongezeka, na Anazitia saa za mchana ndani ya usiku, na hivyo basi usiku ukaongezeka. Na Yeye , kutakasika ni Kwake, ni Mjuzi wa yaliyomo ndani ya vifua vya viumbe Vyake

    [7] Muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na mtoe katika mali amabayo Mwenyezi Mungu Amewaruzuku na Akawafanya nyinyi ni wasimamizi wa mali hayo. Basi wale walioamini miongoni mwenu, enyi watu, na wakatoa mali yao watapata malipo makubwa

    [8] Na mna udhuru gani ya nyinyi kutokaubali upweke wa Mwenyezi Mungu na kutofuata sheria Zake kivitendo na hali Mtume anawalingania juu ya hilo na Mwenyezi Mungu Ashachukua ahadi zenu juu ya hilo, iwapo nyinyi ni wenye kumuamini Mwenyezi Mungu Muumba wenu

    [9] Yeye Ndiye Anayemteremshia mja Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, aya za Qur’ani zilizopambanuliwa zilizo wazi, ili Awatoe nyinyi kwa hizo kwenye giza la ukafiri na kuwatia kwenye mwangaza wa Imani. Na hakika Mwenyezi Mungu, kwa kule kuwatoa nyinyi kwenye giza na kuwatia kwenye mwangaza, Anawarehemu rehema kunjufu katika maisha yenu ya sasa ya ulimwenguni na maisha yenu ya baadaye, na awalipe malipo mazuri kabisa

    [10] Na ni kitu gani kinachowazuia nyinyi kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu? Hakika ni kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye urithi wa mbingu na ardhi, Anavirithi vyote vilivyomo humo, na hatasalia yoyote kuwa ni mwenye kumiliki chochote humo. Hawalingani kimalipo na thawabu wale waliotoa kabla ya ufunguzi wa Makkah na wakapigana na wakanushaji na wasiokuwa wao, kwani wao wana daraja kubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko wale waliotoa katika njia ya Mwenyezi Mungu baada ya ufunguzi na wakapigana na wakanushaji, na kila mojawapo ya makundi mawili haya Mwenyezi Mungu Ameliahidi Pepo. Na Mwenyezi Mungu ni Mtambuzi wa matendo yenu, hakuna chchote katika hayo kinachofichamana Kwake, na Atawalipa nyinyi kwa hayo

    [11] Ni yupi yule anayetoa katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa kutaka thawabu kutoka ndani ya moyo wake bila kusimanga wala kuudhi, ili Amuengezee Mola wake malipo na thawabu na apate malipo mema nayo ni Pepo

    [12] Siku utakapowaona Waumini wa kiume na Waumini wa kike ikitembea nuru yao juu ya njia ya Ṣirāṭ mbele yao na upande wao wa kulia kwa kadiri ya matendo yao mema na waambiwe, «Bishara yenu leo ni kuingia kwenye mabustani ya Peponi yaliyo makunjufu ambayo chini ya miti yake inapita mito, hamtatolewa humo milele.» Malipo hayo ndiyo kufuzu kwenu kukubwa huko Akhera

    [13] Siku watakaposema wanafiki wa kiume na wanafiki wa kike wakiwaambia Waumini, «Tungojeeni tupate mwangaza wa nuru yenu!» Hapo Malaika wawaambie, «Rudini nyuma yenu mtafute nuru (kwa njia ya kuwafanyia shere). Hapo watenganishwe baina yao kwa kuwekwa kizuizi cha ukuta wenye mlango ambao ndani yake , upande wa Waumini, mna rehema, na nje yake, upande wa wanafiki kuna adhabu

    [14] Hapo wale wanafiki wawaite Waumini kwa kusema, «Kwani hatukuwa na nyinyi duniani tukitekeleza ibada za Dini kama nyinyi?» Na Waumini wawaambie, «Ndio, mlikuwa na sisi kidhahiri, lakini nyinyi mlijiangamiza wenyewe kwa unafiki na kufanya maasia, na mkingojea kwa hamu Nabii afe na Waumini wapatikane na mikasa, mkakufanyia shaka kule kufufuliwa baada ya kufa, na yakawadanganya nyinyi matumaini yenu ya urongo na mkasalia katika hali hiyo mpaka mauti yakawajia. Na Shetani aliwadanganya nyinyi kuhusu Mwenyezi Mungu

    [15] Leo haitakubaliwa badala kutoka kwa yoyote miongoni mwenu, enyi wanafiki, ili ajifidie kwayo na adhabu ya Mwenyezi Mungu wala kutoka kwa wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. mwisho wenu nyote ni Moto, huo ni makao mnayostahili zaidi kuliko makao yoyote, na mwisho mbaya kabisa ni huo

    [16] Je haujafika wakati kwa wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakafuata uongofu Wake kulainika nyoyo zao anapotajwa Mwenyezi Mungu na kuisikia Qur’ani, na wasiwe ni wenye ugumu wa nyoyo kama walivyokuwa wale waliopewa Vitabu kabla yao, kati ya Mayahudi na Wanaswara, ambao walipitiwa na muda mrefu wakayageuza maneno ya Mwenyezi Mungu na nyoyo zao zikawa ngumu, na wengi miongoni mwao wakatoka nje ya utiifu wa Mwenyezi Mungu? Katika aya hii pana kuhimiza ulainifu na unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika, wakati wa kuyasikia yale Aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu ya Kitabu na Hekima, na kujihadhari na kujifananisha na Mayahudi na Wanaswara katika ususuwavu wa nyoyo zao na kutoka nje ya utiifu wa Mwenyezi Mungu

    [17] Jueni kwamba Mwenyezi mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Anaihuisha ardhi kwa mvua baada ya kufa kwake ikatoa mimea. Basi vilevile Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuhuisha wafu Siku ya Kiyama, na Ndiye Muweza wa kuzilainisha nyoyo baada ya kususuwaa kwake. Kwa hakika tumewafunulia wazi dalili za uweza wetu, huenda nyinyi mkazielewa na kwa hivyo mkawaidhika

    [18] Hakika ya wale wanaume na wanawake wanaotoa sadaka kutokana na mali yao na wakatumia katika njia ya Mwenyezi Mungu matumizi zikiwa radhi nyoyo zao, kwa kutafuata radhi za Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, wataongezewa malipo mema ya hayo, na juu ya hayo watapata malipo mengi, nayo ni Pepo

    [19] Na wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake na wasimbague yoyote miongoni mwao, hao ndio wakweli iliyokamilika imani yao kwa kile walichokuja nacho Mitume, kiitikadi, kimaneno na kivitendo, na ndio mashahidi mbele ya Mola wao; watapata malipo yao mengi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na nuru yao kubwa Siku ya Kiyama. Na wale waliokufuru na kukanusha dalili zetu na hoja zetu, wao ndio watu wa Motoni, hawatakuwa na malipo mema wala nuru

    [20] Jueni, enyi watu, kwamba uhai wa kilimwengu ni mchezo na pumbao ya miili kuchezea na nyoyo kupumbaa, na pambo la nyinyi kujipamba nalo, na kuoneshana baina yenu kwa vitu vyake vya starehe, na kushindana kwa wingi wa mali na watoto. Mfano wake ni kama ule wa mvua ambayo mimea yake iliwafurahisha wakulima, kisha ikasinyaa na kukauka, ukaiona imekuwa rangi ya manjano baada ya kuwa rangi ya kijani, kisha ikawa ni yenye kukatikakatika na kuwa mikavu na kusagikasagika. Na huko Akhera kuna adhabu kali kwa makafiri na msamaha wa Mwenyezi Mungu na radhi Zake kwa watu wenye kuamini. Na haukuwa uhai wa kilimwengu, kwa mwenye kuushughulikia hali ya kusahau Akhera yake, isipokuwa ni starehe yenye udanganyifu

    [21] Shindaneni, enyi watu, katika kukimbilia sababu za kusamehewa kwa kutubia kidhati na kujiepusha na maasia, ili mlipwe msamaha kutoka kwa Mola wenu na Pepo ambayo upana wake ni kama upana wa mbingu na ardhi, nayo imetayarishiwa wale waliompwekesha Mwenyezi mungu na wakawafuata Mitume Wake. Hizo ni nyongeza za Mwenyezi Mungun Anazompa Anayemtaka miongoni mwa viumbe Vyake. Pepo haipatikani isipokuwa kwa rehema ya mwenyezi Mungu na nyongeza Zake na matendo mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nyongeza kubwa kwa waja Wake Waumini

    [22] Hampatikani na msiba wowote, enyi watu, kwenye ardhi wala ndani ya nafsi zenu, utokanao na magonjwa, njaa na ndwele, isipokuwa umeandikwa kwenye Ubao Uliyohifadhiwa kabla ya kuumbwa viumbe. Hakika hilo, kwa Mwenyezi Mungu, ni jambo sahali

    [23] Ili msisikitike kwa mlichokikosa cha ulimwengu na msifurahike furaha ya kiburi na majivuno. Na mwenyezi mungu Hampendi kila mwenye kujiona kwa alichopewa cha ulimwengu, mwenye kujifahiri nacho juu ya wengine

    [24] Hawa wenye kujiona ndio wale wanaoyafanyia ubahili mali yao, wasiyatoe katika njia ya Mwenyezi Mungu, na wakawaamuru watu wawe mabahili kwa kuwapambia huo ubahili. Na yoyote anayezunguka nyuma kwa kuacha kumtii Mwenyezi mungu hamdhuru yoyote isipokuwa nafsi yake, na hatamdhuru Mwenyezi Mungu chochote, kwani Mwenyezi Mungu Ndiye Mkwasi Asiyehitajia viumbe vyake, Mwenye kuhimidiwa Ambaye Ana kila sifa njema iliyokamilika na kila tendo zuri ambalo Anastahiki kushukuriwa kwalo

    [25] Hakika tumetumiliza Mitume wetu kwa hoja zilizo wazi na kuwateremshia Vitabu vyenye hukumu na sheria, na tukateremsha mizani ili watu waamiliane baina yao kwa uadilifu, na tukateremsha chuma chenye nguvu nyingi na manufaa mengi kwa watu, na ili Mwenyezi Mungu Amjue, ujuzi wenye kujitokeza kwa watu, yule anayetetea Dini Yake na Mitume Wake kwa ghaibu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Asiyetendeshwa nguvu, ni Mshindi hakuna anayeweza kushindana na Yeye

    [26] Na hakika tuliwatumiliza Nūḥ na Ibrāhīm kwa watu wao, na tukajaalia kwenye kizazi chao unabii na vitabu vilivyoteremshwa. Basi miongoni mwa watu wa kizazi chao kuna walioongoka kwenye haki, na wengi kati yao wametoka nje ya utiifu wa Mwenyezi Mungu

    [27] Kisha tukafuatisha, kwenye athari za Nūḥ na Ibrāhīm, Mitume wetu tiliowatumiliza kwa hoja zilizo wazi, na tukamfuatisha 'Īsā mwana wa Maryam na tukampa Injili, na tukajaalia ndani ya nyoyo za wale waliomfuata na kuwa kwenye dini yake ulaini na huruma, wakawa wanapendana wao kwa wao, na walizusha taratibu za kuabudu, kwa kupitisha kiasi katika ibada, ambazo hatukuwalazimisha nazo isipokuwa ni wao wenyewe waliojilazimisha nazo kwa lengo la kupata radhi za Mwenyezi Mungu, lakini hawakusimama nazo vile inavyotakiwa kusimama. Basi tukawapa wale walioamini miongoni mwao malipo yao kulingana na Imani yao, na wengi miongoni mwao ni wenye kutoka nje ya utiifu wa Mwenyezi Mungu na ni wenye kumkanusha Nabii Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [28] Enyi mlioamini! Fuateni amri za Mwenyezi Mungu na mjiepushe na makatazo Yake na muaminini Mtume Wake, Atawapa rehema Zake mara mbili zaidi, na Atawafanya muwe na nuru ambayo kwayo mnajiongoza na Atawasamehe dhambi zenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa waja Wake, ni Mwenye kuwarehemu

    [29] Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Amewapa haya yote ili wapate kujua watu waliopewa Vitabu ambao hawakumuamini Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwamba wao hawawezi chochote kujipa wao wenyewe nyongeza za kheri za Mwenyezi Mungu wala kuwapatia wengine, na kwamba nyongeza zote ziko kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wema mkubwa na vipewa vingi kwa viumbe Vyake

    Mwanamke Anayeomba

    Surah 58

    [1] Ashasikia Mwenyezi Mungu neno la Khawalah binti ya Tha’labah anayekurudiarudia kuhusu mumewe Aws mwana wa al-Ṣāmit na kuhusu kile kilichotokea upande wake cha kufanya ẓihār nako ni kule kutamka mumewe kumwambia yeye, «wewe kwangu mimi ni kama mgongo wa mamangu», yaani katika uharamu wa kumuingilia, na huku anamnyenyekea Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Amtatulie shida yake, na Mwenyezi Mungu Anayasikia maneno yenu na marudiano yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msikizi wa kila neno, ni Muoni wa kila kitu, hakifichiki Kwake chochote chenye kufichika

    [2] wale wanaowafananisha wake zao na mama zao, kwa kutoka mwanamume miongoni mwao kumwambia mkewe, «Wewe kwangu ni kama mgongo ya mamangu» yaani kuwa kumuingilia ni haramu, wamemuasi Mwenyezi Mungu na wameenda kinyume na Sheria. Na wake zao si mama zao kihakika, bali wao ni wake zao; mama zao ni wale tu waliowazaa wao. Na hawa wanaowafananisha wake zao na mama zao, kwa hakika, wanasema neno la urongo lililo baya lisilo sahihi. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamahe na kusitiri kwa wale ambao yametokea kwao baadhi ya mambo ya uvunjaji Sheria kisha wakayarakebisha kwa kutubia kidhati

    [3] Na wale wanaojiharamishia wake zao kwa kuwafananisha na migongo ya mama zao kisha wakarudi nyuma na hilo neno na wakataka kuwaingilia, basi ni juu ya yule mume aliyetoa tamshi la ẓihār, katika hali hii, atoe kafara ya kule kujiharamishia, nayo ni kuacha shingo huru yenye Imani: mtumwa au kijakazi, kabla hajamuingilia yule mkewe aliyemfananisha na mgongo wa mamake. Hiyo ndiyo hukumu ya Mwenyezi Mungu kwa anayemfananisha mkewe na mgongo wa mamake, mnakumbushwa mwaidhike nayo, enyi Waumini, ili msiingie kwenye kosa la kuwafananisha wake zenu na mama zenu na kusema neno la uzushi, na mtoe kafara mnapoingia kwenye kosa hilo, na ili msirudie tena kufanya hilo. Na Mwenyezi Mungu hakifichamani chochote Kwake Yeye katika matendo yenu, na Yeye ni Mwenye kuwalipa kwayo

    [4] Na Asiyepata shingo ya kuiacha huru, basi lililo wajibu kwake ni kufunga miezi miwili iliyofuatana kabla hajamuundama mkewe. Na asiyeweza kufunga miezi miwili kwa udhuru wa kisheria, basi na awalishe masikini sitini chakula kinachowashibisha. Hayo tuliyoyaelezea nyinyi ya hukumu ya kujiharamishia mke wake kwa kumfananisha na mgongo wa mamake ni kwa sababu mmuamini Mwenyezi Mungu na mumfuate Mtume Wake na mfanye matendo yanayoambatana na Sheria ya Mwenyezi Mungu na muache yale ambayo mlikuwa mkiyafanya wakati mlipokuwa kwenye ujinga. Hukumu hizo zilizotajwa ndizo amri za Mwenyezi Mungu na mipaka Yake, basi msiikiuke. Na wenye kuzikataa watapata adhabu yenye uchungu

    [5] Hakika ya wale wanaomfanyia uadui na Mwenyezi mungu na Mtume Wake na wakaenda kinyume na amri zao, watadhalilishwa na watatwezwa kama walivyodhalilishwa ummah waliokuwa kabla yao waliopingana na Mwenyezi Mungu na Mitume Wake. Na tumeteremsha aya zenye hoja zilizo wazi zinazoonyesha kuwa Sheria ya Mwenyezi Mungu na mipaka Yake ni kweli. Na wenye kuzikanusha aya hizo watapata adhabu yenye kudhalilisha ndani ya moto wa Jahanamu

    [6] Na kumbuka, ewe Mtume, Siku ya Kiyama, Siku ambayo Mwenyezi Mungu Atawahuisha wafu wote na Atawakusanya wa mwanzo na wa mwisho katika uwanja mmoja, Awape habari ya yale waliyoyafanya ya kheri na shari. Mwenyezi Mungu Ameyadhibiti hayo na Ameyaandika katika Ubao Uliohifadhiwa, na Amewatunzia wao katika kurasa za matendo yao na hali wao wameyasahau. Na Mwenyezi Mungu ni Shahidi wa kila jambo, hakuna chochote kinachofichamana Kwake

    [7] Kwani hujui kwamba Mwenyezi Mungu Yuwajua kila kitu kilicho mbinguni na ardhini? Hawanong’oni watu watatu, kati ya viumbe Vyake, maneno ya siri isipokuwa Mwenyezi Mungu ni wanne wao , wala watano isipokuwa Yeye ni wa sita wao, wala wachache kuliko idadi hiyo iliyotajwa wala wengi kuliko idadi hiyo isipokuwa Yeye Huwa Yuko pamoja nao kwa ujuzi wake, mahali popote waliopo. Hakuna chochote kinachofichamana Kwake kuhusu mambo yao. Kisha Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Siku ya Kiyama, Atawapa habari ya kile walichokifanya chema au kibaya na Atawalipa kwa walichokifanya. Hakika Mwenyezi Mungu kwa kila kitu ni Mjuzi

    [8] Je, huwaoni, ewe Mtume, Mayahudi waliokatazwa wasizungumze kwa siri maneno yanayowatia shaka Waumini, kisha wanarudi kufanya yale waliyokatazwa, na wanazungumza kwa siri maneno ya dhambi, uadui na kuenda kinyume na amri ya Mtume? Na wanapokujia hawa Mayahudi kwa jambo lolote miongoni mwa mambo, wanakuamkia kwa maamkizi ambayo siyo yale Mwenyezi Mungu Aliyoyafanya ni maamkizi yako, na wanasema, «As-sām ‘alayka» yaani, Mauti yakushukie! Na wanasema wakiambiana wao kwa wao, «Si Atuangamize Mwenyezi Mungu kwa yale tunayomuambia Muhammad, iwapo ni Mtume kikweli.» Moto wa Jahanamu utawatosha: wataungia na watalihisi joto lake, na ubaya wa marejeo ni huo

    [9] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Zake kivitendo! Mnapozungumza baina yenu kwa siri, msizungumze maneno ya dhambi au yenye uadui kwa wengine msiokuwa nyinyi au yanayoenda kinyume na amri ya Mtume. Na zungumzeni yale yenye kheri, utiifu na wema, na muogopeni Mwenyezi Mungu kwa kufuata amri Zake na kujiepusha na makatazo Yake, Kwani Kwake Yeye Peke Yake ndipo mtakaporudi na matendo yenu yote na maneno yenu Aliyowadhibitia, na Atawalipa kwayo

    [10] Hakika kuzungumza kwa siri maneno ya dhambi na uadui ni katika ushawishi wa Shetani. Yeye ndiye anayeyapamba na kuyahimiza ili atie masikitiko kwenye nyoyo za Waumini. Na hilo halikuwa ni lenye kuwaudhi Waumini kitu chochote isipokuwa kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na mapendeleo Yake. Na kwa Mwenyezi Mungu na wajitegemeze wenye kumuamini katika mambo yao yote

    [11] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Zake kivitendo! Mkitakiwa mpanane nafasi kwenye mabaraza basi peaneni nafasi, na mkifanya hivyo Mwenyezi Mungu Atawakunjulia nafasi duniani na Akhera. Na mkitakiwa kwenu, enyi Waumini, muinuke katika mabaraza yenu kwa jambo lolote lenye kheri kwenu, basi inukeni. Mwenyezi Mungu Anavipandisha vyeo vya Waumini miongoni mwenu, na Anavipandisha vyeo vya wenye elimu daraja nyingi kwa kuwapatia malipo mema na daraja za kupata radhi. Na Mwenyezi Mungu Anayatambua matendo yenu, hakuna chochote kinachofichamana Kwake katika hayo, na Yeye ni mwenye kuwalipa nyinyi kwayo. Katika aya pana kutukuza cheo cha wanavyuoni na utukufu wao na kutukuzwa daraja zao

    [12] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Zake kivitendo! Mkitaka kusema na Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa siri baina yenu na yeye, basi tangulizeni kabla ya hilo kutoa sadaka kwa wahitaji. Hilo ni bora kwenu, kwa kuwa lina thawabu, na lenye kusafisha zaidi nyoyo zenu na madhambi. Basi mkitopata cha kutoa sadaka hamna makosa juu yenu. Kwani Mwenyezi Mungu, kwa hakika, ni Mwingi wa msamaha kwa waja Wake Waumini, ni Mwenye huruma kwao

    [13] Je, mmeogopa kuwa mtafukarika mkitanguliza sadaka kabla ya kunong’ona na Mtume wa Mwenyezi Mungu? Basi msipofanya hilo mliloamrishwa, na Mwenyezi Mungu Amewasamehe na Amewaruhusu msilifanye hilo, basi simameni imara na muendelee kusimamisha Swala, kutoa Zaka na kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake katika kila lile mliloamrishwa. Na Mwenyezi Mungu ni Mtambuzi wa Matendo yenu na ni Mwenye kuwalipa kwayo

    [14] Je, huwaoni wanafiki waliowafanya Mayahudi ni marafiki na wakawategemea? Na wanafiki kihakika si miongoni mwa Waislamu wala mayahudi, na wanaapa urongo kuwa wao ni Waislamu na kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na hali wanajua kuwa wao ni warongo kwa kile walichokiapia

    [15] Mwenyezi Mungu Amewatayarishia hawa wanafiki adhabu iliyofikia upeo wa ukali na uchungu. Hakika wao ni mabaya sana yale waliokuwa wakiyafanya ya unafiki na uapaji mayamini ya urongo

    [16] Wanafiki wameyafanya yale mayamini yao ya urongo ni kinga yao wasipate kuuawa kwa ukafiri wao na kuwazuia Waislamu wasiwapige vita na kuchukua mali yao. Na kwa ajili hiyo wanajizuia wao na kuwazuia wengine njia ya Mwenyezi Mungu, nayo ni Uislamu. Basi watapata adhabu yenye kudhalilisha Motoni kwa kufanya kiburi kwao kwa kujiepusha na kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na kwa kuzuia kwao njia Yake isifuatwe

    [17] Hayatawakinga wanafiki hawa mali yao wala watoto wao kitu chochote na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Hao ni watu wa Motoni, watauingia na wasalie humo milele, hawatatoka humo kabisa. Malipo haya yanamkusanya kila anayeiwekea kizuizi Dini ya Mwenyezi Mungu kwa maneno yake au vitendo vyake

    [18] Siku ya Kiyama, Mwenyezi Mungu Atawafufua wanafiki wote kutoka makaburini mwao wakiwa hai, na hapo wamuapie Yeye kuwa wao walikuwa Waumini kama walivyokuwa wakiwaapia nyinyi, enyi Waumini, duniani. Na watadhani kuwa hilo litawanufaisha kwa Mwenyezi Mungu kama lilivyokuwa linawanufaisha ulimwenguni kwa Waislamu. Basi jua na utanabahi kuwa wao ndio waliofikia upeo katika urongo ambao hawakuufikia wasiokuwa wao

    [19] Hao Shetani aliwaghilibu na akawatawala mpaka wakaacha amri za Mwenyezi Mungu na kufanya matendo ya utiifu Kwake. Hao ni kundi la Shetani na wafuasi wake. Jua utanabahi kwamba watu wa kundi la Shetani ndio wenye kupata hasara duniani na Akhera

    [20] Hakika wale wanaoenda kinyume na amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, hao ni miongoni mwa wadhalilifu walioshindwa na kufanywa wanyonge duniani na Akhera

    [21] Ameandika Mwenyezi Mungu kwenye Ubao Uliohifadhiwa na Amepitisha kuwa ushindi ni Wake Yeye, Kitabu Chake, Mitume Wake na waja Wake Waumini. Hakika mwenyezi Mungu, kutakasika ni Kwake, ni Mwenye nguvu, hakuna kitu kinachomuelemea, ni Mwenye ushindi juu ya viumbe Vyake

    [22] Hutakuta, ewe Mtume, watu wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na wanaofanya matendo waliyoamrishwa na Mwenyezi Mungu, wakiwapenda na kuwategemea wale wanaomsimamishia uadui Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wanaoenda kinyume na amri zao, ingawa ni baba zao au wana wao au ndugu zo au jamaa zao wa karibu. Hao wanaofunga urafiki kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na wanaosimamisha uadui kwa ajili Yake ndio wale ambao Mwenyezi Mungu Ameithibitisha Imani ndani ya nyoyo zao na Akawatia nguvu kwa kuwapa ushindi utokao Kwake na msaada dhidi ya adui yao duniani, na Atawaingiza huko Akhera kwenye mabustani ya Peponi ambayo chini ya miti yake inapita mito, hali ya kukaa humo muda mrefu usiomalizika, Amewapa radhi Zake na hatawakasirikia na wao wameridhika na Mola wao kwa yale Aliyowapatia ya utukufu na daraja kubwa. Hao ndio kundi la Mwenyezi Mungu na walioshikana na Yeye, na hao ndio wenye kufaulu kwa kupata furaha ya duniani na Akhera

    Uhamisho

    Surah 59

    [1] Vimemtakasa Mwenyezi Mungu na kumuepusha na kila kisichonasibiana na Yeye, vilivyoko mbinguni na vilivyoko ardhini, na Yeye Ndiye Mshindi Asiyekuwa na mwenye kushindana na Yeye, Mwingi wa hekima katika makadirio Yake, uendeshaji Wake na utengezaji Wake na Sheria Zake, Anaweka kila jambo mahali pake panapostahiki

    [2] Yeye, kutakasika ni Kwake, Ndiye Aliyewatoa wale walioukanusha unabii wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, miongoni mwa watu waliopewa Kitabu, nao ni Mayahudi wa ukoo wa Banū al Nadīr, kutoka majumbani mwao ambayo wakiwa humo walikuwa ni majirani na Waislamu pambizoni mwa Madina. Huko kulikuwa ndio mwanzo wa kutolewa nje ya Bara Arabu hadi Shām. Hamkudhani, enyi Waislamu, kuwa watatoka majumbani mwao kwa unyonge huu na utwevu, kwa silaha kali waliokuwa nazo na hifadhi ya nguvu waliokuwa nayo. Na walidhani Mayahudi kuwa ngome zao zitawakinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu na kuwa hakuna anayeziweza. Basi amri ya Mwenyezi Mungu ilizijilia kwa namna ambayo haikupita kwenye akili zao, na Mwenyezi Mungu Akawatia hofu na kicho kikubwa, wakawa wanazivunja nyumba zao kwa mikono yao na mikono ya Waumini, basi zingatieni, enyi wenye busara timamu na akili nyingi kwa hayo yaliyowafika wao

    [3] Na lau si Mwenyezi Mungu kupitisha na kuamua kuwa wao watoke majumbani mwao, Angaliwaadhibu duniani kwa kuuawa na kutekwa, na huko Akhera watakuwa na adhabu ya Motoni

    [4] Hilo- lililowapata Mayahudi duniani na linalowangojea huko Akhera- ni kuwa wao walienda kinyume sana na amri ya Mwenyezi Mungu na amri ya Mtume Wake, wakawapiga vita na wakafanya harakati za kuwaasi. Basi yoyote mwenye kuenda kinyume na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, hakika Mwenmyezi Mungu Atamtesa vikali

    [5] Mitende mnayoikata au mnayoiacha imesimama juu ya mashina yake bila ya kuigusa , ni kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na amri Yake, na ili Awadhalilishe kwa hilo wale waliotoka nje ya utiifu Kwake wenye kuenda kinyume na amri Yake na makatazo Yake, kwa kuwapa nguvu nyinyi kuikata mitende yao na kuichoma

    [6] Na yale mali ya Mayahudi wa Banū al- Nadīr ambayo Mwenyezi Mungu Amewaletea, hamkupanda farasi wala ngamia ili myapate, lakini Mwenyezi Mungu Anawapa nguvu wajumbe Wake juu ya anayemtaka miongoni mwa maadui Wake, wakajisalimsha bila ya vita. (Mali hayo yanaitwa fay’), na fay’ ni mali yaliyochukuliwa kwa makafiri kwa haki bila ya vita. Na Mwenyezi Mungu kwa kila jambo ni Muweza, hakuna kitu chochote kinachomshinda

    [7] Hayo mali ya washirikina wa watu wa miji ambayo Mwenyezi Mungu Amewaletea bila kupanda farasi wala ngamia, basi hayo ni ya Mwenyezi Mungu na ya Mtume Wake, yatatumiwa kwa maslahi ya Waislamu kwa jumla, jamaa wa karibu wa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na mayatima: nao ni watoto maskini waliofiliwa na baba zao, maskini: nao ni wenye uhitaji na ufukara, na ibn al-sabīl: naye ni mgeni msafiri ambaye matumizi yake yameisha na mali yake yamemalizika. Hiyo ni kwa sababu mali yasiwe ni milki inayozunguka kwa matajiri peke yao, na mafukara na maskini wakanyimwa nayo. Na mali yoyote ambayo Mtume Amewapatia au sheria yoyote aliyowawekea, basi chukueni, na chochote kile alichowakataza basi komekeni nacho. Na muogopeni Mwenyezi Mungu kwa kufuata amri Zake na kuepuka makatazo Yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye mateso makali kwa anayemuasi na kuenda kinyume na amri Yake na makatazo Yake. Na aya hii ni msingi wa ulazima wa kufuata Sunnah iwe ni ya maneno, ya vitendo au ya kukubali jambo lifanyike kwa kutolikataza

    [8] Pia wanapewa mali hayo, ambayo Mwenyezi Mungu Amemletea Mtume Wake, mafukara waliohama, wale waliolazimishwa na makafiri wa Makkah watoke kwenye majumba yao na waache mali yao na huku wanaomba kwa mwenyezi Mungu Awafanyie hisani ya kuwapa riziki duniani na radhi kesho Akhera, na wanaitetea Dini ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake kwa kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Hao ndio wakweli ambao walikuwa wakweli wa maneno yao na vitendo vyao

    [9] Na wale wakazi wa Madina na walioamini kabla ya Waumini wa Makkah hawajahamia Madina, nao ni Anṣār (Waumini wenyeji wa Madina) wanawapenda Muhājirūn (Waumini waliohamia Madina) na wanawaliwaza kwa mali yao wala hawaoni wivu juu yao kwa mali ya fay’ waliyopewa, na wanawatanguliza waliohama na wenye uhitaji na ufukara juu ya nafsi zao, japokuwa wao wana uhitaji na ufukara. Na yoyote aliyesalimika na ubahili na uzuiaji mali yaliyomzidi, basi hao ndio wenye kufuzu waliofaulu kupata matakwa yao

    [10] Na waliokuja miongoni mwa Waumini baada ya Anṣār na Muhājirūn wanasema, «Mola wetu! Tusamehe dhambi zetu, na uwasamehe ndugu zetu katika Dini waliotutangulia katika kuamini, Na usitie ndani ya nyoyo zetu uhasidi na chuki kwa yoyote miongoni mwa wenye kuamini. Mola wetu! Wewe ni Mpole kwa waja wako. Unawarehemu waja wako rehema rehema kunjufu katika maisha yao ya hapa ulimwenguni ya kesho Akhera.» Katika hii aya pana dalili kwamba inapasa kwa Muislamu awataje kwa wema wale waliomtangulia na awaombee dua, na awapende maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na awataje kwa wema na awaombee radhi ya Mwenyezi Mungu

    [11] Je huwatazami hao wanafiki wanawaambia ndugu zao katika ukafiri miongoni mwa Mayahudi wa Banū al Naḍī, «Tunaapa kwamba Muhammad na walio pamoja na yeye wakiwatoa kutoka majumbani mwenu tutatoka na nyinyi! Na hatutamfuata yoyote kuhusu nyinyi anayetutaka tusiwasaidie au tuache kutoka pamoja na nyinyi, na wakipigana na nyinyi tutawasaidia juu yao?» na Mwenyezi Mungu Anashuhudia kwamba wanafiki ni warongo katika yale waliyowaahidi Banū al Naḍī

    [12] Lau Mayahudi watatolewa Madina, wanafiki hawatatoka pamoja na wao, na lau watapigwa vita hawatapigana pamoja na wao kama walivyoahidi. Na lau watapigana pamoja na wao wangalipa mgongo hali ya kukimbia kwa kushindwa, kisha Mwenyezi Mungu Hatawanusuru, bali Atawaacha bila kuwasaidia na Atawadhalilisha

    [13] Kwa hakika, hofu ya wanafiki na Mayahudi kuwaogopa nyinyi, enyi Waumini, ni kubwa mno ndani ya nyoyo zao kuliko vile wanavyomuogopa na kumcha Mwenyezi Mungu. Hii ni kwa sababu ya kuwa wao ni watu wasiouelewa utukufu wa Mwenyezi Mungu na kuwa na Imani Kwake, na hawaogopi mateso Yake

    [14] Hawatakabiliana na nyinyi Mayahudi wakiwa wamejikusanya isipokuwa wakiwa kwenye miji iliyohifadhiwa kwa ngome na mahandaki, au nyuma ya kuta ambazo wanazitumia kwa kujificha kwa uoga wao na kicho kilichojikita ndani ya nyoyo zao. Uadui wao baina yao ni mkubwa, utadhani kuwa wao wamekusanyika kwenye neno moja, lakini nyoyo zao ziko mbalimbali, na hiyo ni kwa sababu wao ni watu wasioitia akilini amri ya Mwenyezi Mungu wala kuzizingatia aya Zake

    [15] Mfano wa hawa Mayahudi kwa mateso yaliyowashukia ni kama mfano wa makafiri wa Kikureshi siku ya Badr na Mayahudi wa Banū Qaynuqā'kwa kuwa walionja mwisho mbaya wa ukafiri wao na uadui wao kwa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, duniani, na huko Akhera watapata adhabu kali yenye uchungu

    [16] Na mfano wa hawa wanafiki katika kule kuwashawishi Mayahudi wapigane na kuwaahidi kuwa watawatetea dhidi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ni kama mfano wa Shetani alipompambia binadamu na kumlingania kwenye ukafiri, na alipokufuru alisema, «Mimi nimejiepusha na wewe; mimi namuogopa Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe wote.»

    [17] Basi mwisho wa Shetani na yule binadamu aliyemtii na akakufuru ni kwamba wote wawili wataingia Motoni hali ya kukaa humo milele. Na hayo ndiyo malipo ya wenye kudhulumu na kukiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu

    [18] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Zake kivitendo! Muogopeni Mwenyezi Mungu na jihadharini na mateso Yake kwa kuyafanya Aliyowaamrisha na kuyaacha Aliyowakataza, na kila mtu ayazingatie matendo aliyoyatanguliza kwa Siku ya Kiyama. Na muogopeni Mwenyezi Mungu katika kila mnachokitenda na mnachokiacha, hakika Mwenyezi Mungu , Aliyetakasika, ni Mtambuzi wa mnayoyafanya, hakuna chochote kinachofichamana Kwake miongoni mwa matendo yenu, na Yeye ni Mwenye kuwalipa nyinyi kwa hayo

    [19] Na msiwe, enyi Waumini, kama wale walioacha kutekeleza haki ya Mwenyezi Mungu Aliyoipasisha juu yao, na kwa sababu hiyo Akawasahaulisha wao kujifanyia wema nafsi zao kwa kufanya matendo mema yenye kuwaokoa wao na adhabu ya Siku ya Kiyama. Hao ndio wenye kusifika kwa uasi, wenye kutoka nje ya utiifu kwa Mwenyezi Mungu na utiifu kwa Mtume Wake

    [20] Hawalingani sawa, watu wa Motoni wanaoadhibiwa na watu wa Peponi wanaostareheshwa. Watu wa Peponi ndio wenye kupata kila kinachotakiwa, ndio wenye kuokoka na kila kinachochukiwa

    [21] Lau tungaliiteremsha hii Qur’ani juu ya jabali moja miongoni mwa majabali, na likaelewa yaliyo ndani yake ya ahadi ya malipo mema kwa watu wema na malipo mabaya kwa watu wabaya, ungaliliona, pamoja na nguvu zake, ugumu wake na ukuu wake, limenyenyekea, limejidhalilisha na limepasukapasuka kwa kumuogopa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. Na hiyo ni mifano tunawapigia watu na kuwabainishia, huenda wao wakafikiria juu ya uweza wa Mwenyezi Mungu na ukubwa Wake. Katika aya hii pana kuhimiza kuizingatia Qur’ani na kujifahamisha maana yake na kuitumia

    [22] Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Anayeabudiwa kwa haki, Ambaye hakuna muabudiwa isipokuwa Yeye, Mjuzi wa yaliyofichika na yaliyojitokeza, Anayajua yaliyoghibu na yaliyoko. Yeye Ndiye Mwingi wa rehema Ambaye rehema Yake imeenea kila kitu, Anayewarehemu wenye kumuamini

    [23] Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu Mwenye kuabudiwa kwa haki, Ambaye hakuna Mola isipokuwa Yeye, Mmiliki wa vitu vyote, Anayeviendesha bila kizuizi chochote wala upinzani, Aliyetakasika na kila upungufu, Aliyeepukana na kila aibu, Anayewasadikisha Mitume Wake na Manabii kwa dalili zilizo wazi Alizowatuma nazo, Anayewatunza viumbe Wake katika matendo yao, Aliye Mshindi Ambaye hakuna wa kushindana na Yeye, Aliye Jebari Ambaye Amewatendesha nguvu waja wote, na Ambaye viumbe vyote vimemdhalilikia, Aliye Mkubwa Mwenye kiburi na utukufu. Ametakasika Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na kila kile ambacho wanamshirikisha nacho katika kumuabudu

    [24] Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu, kutakasika ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Aliye Muumba, Muanzilishi wa uumbaji kulingana na hekima Yake, Aliyewapa sura viumbe Wake kwa namna Atakavyo. Ni Yake Yeye, kutakasika ni Kwake, Majina Mema na sifa tukufu. Vinamatakasa Yeye vyote vilivyoko mbinguni na ardhini, na Yeye ni Mshindi, Mkali wa mateso kwa maadui Wake, Mwingi wa hekima katika uendeshaji Wake mambo ya viumbe Vyake

    Apimwaye

    Surah 60

    [1] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Zake kivitendo! Msiwachukue maadui wangu na maadui wenu mkawafanya ni marafiki halisi na vipenzi, mkawa mnaamiliana na wao kwa upendo na mkawapasha habari za Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na Waislamu wengine, na hali wao wameikanusha haki iliyowajia ya kumuamini Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na Qur’ani iliyoteremshwa kwake. Wanamtoa Mtume na wanawatoa nyinyi, enyi Waumini, kutoka Makkah kwa kuwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu Mola wenu na mnampwekesha. Mkiwa nyinyi, enyi Waumini, mmehama kwa kupigana jihadi katika njia yangu kwa kutafuta radhi yangu kwenu, basi msifanye urafiki na maadui wangu na maadui wenu. Mnawaambia wao kwa siri kuwa mnawapenda, na mimi ninayajua mnayoyaficha na mnayoyadhihirisha. Na yoyote anayefanya hivyo miongoni mwenu, ashakosea njia ya haki na sawa na amepotea njia ya wastani

    [2] Wakiwapatia nafasi nyinyi hao mnaowapenda kwa siri watawapiga vita na watanyosha mikono yao kwenu, wawaue nyinyi na wawateke, na pia ndimi zao, wawatukane nyinyi na wawatusi, na wao walitamani, kwa hali yoyote, lau nyinyi mlikanusha kama wao

    [3] Hawatawanufaisha nyinyi jamaa zenu wa karibu wala watoto wenu kitu chochote mnapofanya urafiki na wakanushaji kwa ajili yao. Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu Atawatenganisha nyinyi na wao, Awatie Peponi wanaomtii na Awatie Motoni wanaomuasi. Na Mwenyezi Mungu Anayaona mnayoyafanya, hakuna chochote kinachofichamana Kwake cha maneno yenu na matendo yenu

    [4] Kwa hakika mlikuwa na kiigizo kizuri, enyi Waumini, kwa Ibrāhīm na wale waliokuwa pamoja na yeye waliposema kuwaambia wakanushaji Mwenyezi Mungu, «Sisi tumejiepusha na nyinyi na vile mnavyoviabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Tumewakanusha nyinyi na tumeukataa ukafiri mlionao, na umejitokeza nje uadui na machukivu ya milele baina yetu sisi na nyinyi madamu bado mko kwenye ukanushaji wenu, mpaka mmuamini Mwenyezi Mungu Peke Yake.» Lakini haliingii kwenye kuigiza tendo la Ibrāhīm la kumuombea msamaha babake, kwa kuwa hilo lilitokea kabla ya Ibrāhīm kufunukiwa kuwa babake ni adui wa Mwenyezi Mungu, na alipofunukiwa kuwa yeye ni adui wa Mwenyezi Mungu alijiepusha na yeye. Mola wetu! Kwako wewe tumetegemea, na kwako wewe tumerejea kwa kutubia, na kwako wewe ndiko marejeo Siku ya Kiyama

    [5] Mola wetu! Usitufanye ni mtihani wa wale waliokukanusha wewe, kwa kutuadhibu au kuwapa nguvu makafiri juu yetu wakatufitini kwa kutuepusha na Dini yetu au wakawa na nguvu juu yetu wakafitinika kwa hilo na hapo waseme, «Lau hawa wangalikuwa kwenye haki haingaliwapata adhabu hii,» na wazidi ukafiri. Na utufinikie dhambi zetu kwa kutusamehe, ewe Mola wetu! Hakika wewe ni Mshindi Asiyekuwa na mwenye kushindana Naye, Mwingi wa hekima katika maneno Yake na matendo Yake

    [6] Kwa hakika mlikuwa, enyi Waumini, na kiigizo chema kwa Ibrāhīm, amani imshukie, na wale waliokuwa na yeye, kwa anayetumai kupata kheri kutoka kwa Mwenyezi Mungu duniani na Akhera. Na yoyote anayeyapuuza yale ambayo Mwenyezi Mungu Anamuitia nayo ya kuwaiga Manabii Wake na akafanya urafiki na maadui Wake, basi Mwenyezi Mungu Ndiye Mkwasi wa kutowahitajia waja Wake, Ndiye Mwenye kuhimidiwa kwa dhati Yake na sifa Zake, Ndiye Mwenye kushukuriwa kwa namna zote

    [7] Huenda Mwenyezi Mungu Akaweka baina yenu nyinyi, enyi Waumini, na wale jamaa zenu washirikina, ambao mlikuwa na uadui nao, mapenzi baada ya machukivu na maelewano baada ya ugomvi kwa kuvifanya vifua vyao viukunjukie Uislamu. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu, na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa waja Wake ni Mwingi wa huruma Kwao

    [8] Mwenyezi Mungu Hawakatazi nyinyi, enyi Waumini, kuwakirimu kwa wema makafiri ambao hawakuwapiga nyinyi vita kwa ajili ya dini wala hawakuwatoa kutoka majumbani mwenu, na kuwafanyia usawa kwa hisani yenu na wema wenu kwao, kwani Mwenyezi Mungu Anawapenda wale wanaofanya uadilifu katika maneno yao na matendo yao

    [9] Hakika Mwenyezi Mungu Anawakataza, kuhusu wale waliowapiga vita kwa ajili ya dini na wakawatoa majumbani mwenu na wakawasaidia makafiri kuwatoa nyinyi, kufanya urafiki nao kwa kusaidiana na kupendana. Na yoyote anayewachukua wao kuwa ni wasaidizi dhidi ya Waumini na ni vipenzi, basi wao ndio madhalimu wa nafsi zao, wenye kutoka nje ya mipaka ya Mwenyezi Mungu.»

    [10] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Zake kivitendo! Wakiwajia nyinyi wanawake Waumini wakiwa wamehama kutoka nchi ya ukafiri kuja kwenye nchi ya Uislamu, wafanyieni mtihani, ili mjue ukweli wa Imani yao, Mwenyezi Mungu Ndiye Mjuzi zaidi wa Imani yao. Mkiwajua kuwa ni Waumini kulingana na alama na ushahidi uliowafunukia, basi msiwarudishe kwa waume wao makafiri. Kwani wanawake Waumini si halali waolewe na makafiri, na makafiri si halali wawaoe wanawake Waumini. Nawapeni waume wa wale wanawake waliosilimu mahari waliotoa kuwapa hao wanawake. Na si dhambi kwenu kuwaoa mkiwapa mahari yao. Na msishikilie kuendelea na ndoa za wake wenu waliokufuru. Na takeni kwa washirikina mrudishiwe mahari mliotoa kuwapa wanawake wenu walioritadi na wakaungana na hao washirikina. Na wao watake kurudishiwa mahari waliotoa kwa wanawake wao waliosilimu na wakaungana na nyinyi. Hukumu hii iliyotajwa katika aya ni hukumu ya Mwenyezi Mungu Anahukumu baina yenu, basi msiende kinyume nayo. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, hakuna kitu chochote kinachofichamana Kwake, ni Mwingi wa hekima katika maneno Yake na vitendo Vyake

    [11] Na pindi baadhi ya wake zenu wanaporitadi na kujiunga na makafiri, na makafiri wasiwape mahari yao miliyotoa kuwapatia, kisha mkapambana na hao makafiri na kupata ushindi juu yao, basi wapeni wale Waislamu, ambao wake zao waliondoka, kitu katika ngawira au kinginecho kama kile cha mahari walichowapa kabla ya hapo. Na muogopeni Mwenyezi Mungu mnayemuamini

    [12] Ewe Nabii! Wakiwajia nyinyi wanawake wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na kuwaahidi kuwa hawatamshirikisha Mwenyezi Mungu katika kumuabudu, wala hawataiba chochote, wala hawatazini, wala hawataua watoto wao baada ya kuzaliwa au kabla yake, wala hawatawanasibishia waume zao watoto wasiotokana na wao, wala hawataenda kinyume na wewe katika jema unalowaamrisha kwalo, basi waahidi kwa hayo na uwaombee msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe sana dhambi za waja Wake wenye kutubia na ni Mwenye kuwarehemu

    [13] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake! Msiwafanye wale ambao Mwenyezi Mungu Amewakasirikia kwa ukafiri wao kuwa ni marafiki na vipenzi, kwani hao washakata tamaa kupata thawabu za Mwenyezi Mungu kesho Akhera kama makafiri walio makaburini walivyokata tamaa ya kupata rehema ya Mwenyezi Mungu huko Akhera, watakaposhuhudia ukweli wa mambo na wakajua ujuzi wa yakini kuwa hawatakuwa na fungu lolote huko au kama walivyokata tamaa makafiri kufufuliwa wafu wao- walio makaburini- kwa kuitakidi kwao kuwa hakuna kufufuliwa

    Safu

    Surah 61

    [1] Vimemtakasa Mwenyezi Mungu na kumwepusha na kila kisichonasibiana na Yeye vyote vilivyoko mbinguni na vilivyoko ardhini, na Yeye ni Mshindi Ambaye hakuna mwenye kushindana na Yeye, Mwingi wa hekima katika maneno Yake na vitendo Vyake

    [2] Enyi miliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Zake kivitendo! Kwa nini mnatoa ahadi au mnasema maneno bila kuyatekeleza? Haya ni makaripio kwa ambaye matendo yake yanaenda kinyume na maneno yake

    [3] Ni machukivu makubwa sana kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwenu nyinyi mnaposema kwa ndimi zenu maneno msiyoyafanya

    [4] Hakika Mwenyezi Mungu Anawapenda wale wanaopigana katika njia Yake wakiwa wamejipanga kama kwamba wao ni jengo lililopangika na kuimarika kwa namna ya kutoweza adui kupenyeza kupitia jengo hilo. Katika aya hii pana maelezo ya ubora wa jihadi na wenye kupigana jihadi, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kila upungufu, Anawapenda waja Wake Waumini wanapojipanga kupambana na maadui wa Mwenyezi Mungu

    [5] Wakumbushe watu wako, ewe Mtume, pindi aliposema Nabii wa Mwenyezi Mungu. Mūsā, amani imshukie, akiwaambia watu wake, «Kwa nini mnaniudhi kwa maneno na vitendo, na hali nyinyi mnajua kuwa mimi ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu kwenu?» Basi walipopotoka na kuwa kando na haki pamoja na kuwa wanaijua na wakaendelea juu ya hilo, Mwenyezi Mungu Aliziepusha nyoyo zao wasiukubali uongofu, ikiwa ni mateso kwao kwa sababu ya upotevu wao waliojichagulia wenyewe. Na Mwenyezi Mungu Hawaongozi watu wenye kutoka nje ya utiifu na njia ya haki

    [6] Wakumbushe ewe Mtume, watu wako pindi Īsā, mwana wa Maryam, alipowaambia watu wake, «Mimi ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu kwenu, ni mwenye kusadikisha Taurati iliyokuja kabla yangu na ni mwenye kushuhudilia ukweli wa Mtume atakayekuja baada yangu, jina lake ni Ahmad, naye ni Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na ni mwenye kulingania watu wamuamini, basi alipowajia Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa aya zilizo wazi walisema, «Huu ni uchawi waziwazi.»

    [7] Na hakuna yoyote aliye dhalimu zaidi na adui zaidi kuliko yule aliyemzulia Mwenyezi Mungu urongo na akamfanya kuwa ana washirika wa kuabudiwa, na hali yeye anaitwa aingie kwenye Uislamu na kumpwekesha Mwenyezi Mungu Peke Yake kwa ibada. Na Mwenyezi Mungu Hawaafikii, wale waliozidhulumu nafsi zao kwa kukufuru na kukanusha, kwenye njia ambayo ndani yake kuna kufaulu kwao

    [8] Hawa madhalimu wanataka kuitangua haki aliyotumilizwa kwayo Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, nayo ni Qur’ani, kwa maneno yao ya urongo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuipa nguvu haki kwa kuitimiza Dini Yake japokuwa wale wapingaji wenye kukanusha watachukia

    [9] Yeye Ndiye Aliyemtumiliza Mtume Wake Muhammad kwa Qur’ani na Dini ya haki ili Aifanye kuwa juu ya dini zilizo kinyume nayo japokuwa washirikina watachukia hilo

    [10] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo! Je niwaonyeshe njia ya biashara yenye mapato makubwa ambayo itawaokoa na adhabu yenye kuumiza

    [11] Ni mwendelee daima kumuamini kwenu Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na mpigane jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kuinusuru Dini Yake kwa mali mnayoyamiliki na nafsi zenu, hilo ni bora kwenu kuliko biashara ya duniani. Basi mkiwa mnajua vitu venye madhara na manufaa, fuateni amri hiyo

    [12] Mkifanya yale ambayo Mwenyezi Mungu Amewaamrisha nyinyi, enyi Waumini, Atayasitiri madhambi yenu na Atawatia kwenye mabustani ya Pepo ambayo chini ya miti yake inapita mito, na makazi yaliyotakasika na kusafishika ndani ya Mabustani ya kukaa daima bila ya kukatika. Huko ndiko kufaulu ambako hakuna kufaulu zaidi yake

    [13] Na kuna neema nyingine kwenu, enyi Waumini, mtaipenda, nayo ni msaada kutoka kwa mwenyezi Mungu utakaowajia na ushindi wa haraka utakaopatikana mikononi mwenu. Na wape bishara Waumini, ewe Mtume, ya kunusuriwa na kupata ushindi duniani na kupata Pepo kesho Akhera

    [14] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo! Kuweni watetezi wa dini ya Mwenyezi Mungu kama walivyokuwa marafiki wa kidhati wa ‘Īsā watetezi wa Dini ya Mwenyezi Mungu alipowaambia wao Īsā, «Ni nani atakayesimama kunihami na kunisaidia katika mambo ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu?» Wakasema, «Sisi ndio watetezi wa Dini ya Mwenyezi Mungu.» Hapo kundi moja la Wana wa Isrāīl likaongoka na kundi lingine likapotea, tukawapa nguvu wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na tukawapa ushindi juu ya wale waliowafanyia uadui miongoni mwa vipote vya Wanaswara, wakawa na nguvu juu yao kwa kutumilizwa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    Ijumaa

    Surah 62

    [1] Vinamtakasa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka vyote vilivyo mbinguni na vyote vilivyo Ardhini, na Yeye Peke Yake Ndiye mfalme wa kila kitu, Aliye Mshindi kwenye utawala Wake bila ya mpinzani, Mwingi wa hekima katika kuyapelekesha mambo Yake na utengenezaji Wake

    [2] Mwenyezi Munu, kutakasika na kila upungufu ni Kwake, Ndiye Aliyetuma kwa Waarabu, wasiojua kusoma wala kuwa na kitabu wala kumbukumbu zozote za utume, Mtume anayetokamana na wao aliyetumwa kwa watu wote, awasomee Qur’ani na awatakase wao na itikadi mbovu na tabia mbaya, na awafundishe wao Qur’ani na Sunnah. Na wao, kwa kweli, tangu alipokuwa hajatumilizwa, walikuwa kwenye ukengeukaji ulio waziwazi kwa kuwa kando na haki. Na Mwenyezi Mungu, kutakasika na kila upungufu ni Kwake

    [3] Amemtuma yeye kwa watu wengine watakaokuja ambao bado hawajakuja miongoni mwa Waarabu na wengineo. Na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Peke Yake, Ndiye Mshindi mwenye kushinda juu ya kila kitu, Mwingi wa hekima katika maneno Yake na matendo Yake

    [4] Kutumilizwa huko kwa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa ummah wa Kiarabu na wasiokuwa wao, ni wema kutoka kwa Mwenyezi Mungu humpa Anayemtaka miongoni mwa waja Wake. Na Yeye, Peke Yake, Ndiye Mwenye wema na upaji mwingi

    [5] Mfano wa Mayahudi ambao walitakiwa kuifuata Taurati kivitendo kisha wakakosa kuifuata ni kama mfano wa punda ambaye yuwabeba vitabu na hajui yaliyo ndani yake. Ni mfano muovu mno wa watu ambao wamezikataa aya za Mwenyezi Mungu na wasifaidike nazo. Na Mwenyezi mungu Hawaelekezi kwenye wema watu madhalimu ambao wanaikiuka mipaka Yake na wanaotoka nje ya utiifu Kwake

    [6] Sema, ewe Mtume, uwaambie wale ambao wameshikamana na desturi za kiyahudi zilizopotoka, «Mkidai kiurongo kwamba nyinyi tu ndio vipenzi vya Mwenyezi Mungu na sio watu wengine, basi tamanini kufa iwapo nyinyi ni wakweli katika madai yenu kuwa Mwenyezi Mungu Anawapenda nyinyi.»

    [7] Na wala hawa Mayahudi hawatatamani kifo kabisa kwa vile wanavyoyapenda maisha ya duniani kuliko Akhera na kwa kuogopa kuteswa na Mwenyezi Mungu kwa sababu ya yale waliyoyatanguliza ya ukafiri na matendo maovu. Na Mwenyezi Mungu Anawajua mno madhalimu, hakifichamani Kwake chochote cha udhalimu wao

    [8] Sema, «Kwa kweli mauti mnayoyakimbia hayakimbiliki, kwani ni yenye kuwajia wakati wenu wa kufa utakapofika, kisha Siku ya kufufuliwa mtarudishwa kwa Mwenyezi Mungu mjuzi wa yale yaliyofichamana na yanayoonekana, na hapo Atawapasha habari ya matendo yenu na Atawalipa nyinyi kwa hayo.»

    [9] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata Sheria Zake kivitendo! Pindi mwadhini atakapoita kwa ajili ya Swala Siku ya Ijumaa, endeni upesi msikilize hutuba na mtekeleze Swala, na muache uuzaji na pia ununuaji na kila kinachowashughulisha nyinyi na hiyo Swala. Hilo mliloamrishwa ni bora kwenu nyinyi kutokana na yaliyo humo ya kusamehewa dhambi zenu na kupatiwa malipo mema kutoka kwa Mwenyezi Mungu.Basi iwapo nyinyi mnayajua manufaa ya nafsi zenu, fanyeni hilo. Kwenye aya hii kuna dalili kwamba kwenda kuhudhuria Swala ya Ijumaa na kusikiliza hutuba ni lazima

    [10] Basi mkisha kuisikia hutuba na mkaitekeleza Swala, tawanyikeni kwenye ardhi na mtafute riziki ya Mwenyezi Mungu kwa kwenda mbio kwenu, na mtajeni Mwenyezi Mungu kwa wingi katika hali zenu zote, ili mfaulu kuzipata kheri mbili: za duniani na za Akhera

    [11] Na pindi wanapoona baadhi ya Waislamu biashara au chochote miongoni mwa viliwazo vya duniani na pambo lake, hutawanyika kwenda huko na wakakuacha wewe umesimama juu ya mimbari unatoa hutuba. Waambie, ewe Nabii, «Yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ya thawabu na neema yana manufaa zaidi kwenu kuliko pumbao na biashara. Na Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Ndiye Bora wa wanaoruzuku na kutoa, basi muombeni na mjisaidie kwa kumtii, ili myapate yaliyoko Kwake ya kheri mbili: ya duniani na ya Akhera

    Wanafiki

    Surah 63

    [1] Wanapohudhuria wanafiki kwenye kikao chako, ewe Mtume, husema kwa ndimi zao, «Tunakubali kuwa wewe kwa kweli ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu Anajua kuwa wewe ni mtume wa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu Anashuhudia kwamba wanafiki ni warongo katika ushahidi wao kwako walioudhihirisha na wakauapia kwa ndimi zao na huku wameuficha ukanushaji wao kwake

    [2] Ukweli ni kwamba wanafiki wamevifanya viapo vyao wanavyoviapa ni kinga na ngao ya kuwakinga wasihukumiwe na kuadhibiwa, na wamejizuia wenyewe na kuwazuia watu njia ya mwenyezi Mungu iliyonyoka. Kwa kweli wao, ni maovu mno yale ambayo walikuwa wakiyafanya

    [3] kwa kuwa wao wameamini kijuujuu kisha kindanindani wamekufuru. Ndipo Mwenyezi Mungu Akapiga muhuri juu ya nyoyo zao kwa ukafiri wao, Hivyo basi wao hawayaelewi yale yenye maslahi kwao

    [4] Na unapowatazama wanafiki hawa, yanakufurahisha maumbile yao na mandhari yao, na wanapozungumza unayasikiliza mazungumzo yao kwa ufasaha wa ndimi zao, na hali wao kutokamana na utupu wa nyoyo zao kuwa hazina Imani na akili zao kuwa hazina fahamu wala elimu yenye manufaa, ni kama vigogo vilivyotegemezwa kwenye ukuta, visivyokuwa na uhai.wanadhania kila sauti ya ukelele inawashukia wao na ina madhara kwao kwa kujua kwao uhakika wa hali yao na uoga wao mwingi na hofu iliyojikita nyoyoni mwao. Wao ndio maadui wa kikwelikweli wenye uadui mwingi kwako wewe na kwa Waumini. Basi jichunge na wao, Mwenyezi Mungu Amewadhalilisha wao na Amewatoa kwenye rehema Yake. Basi ni vipi wao wanaiepuka haki na wanaelekea kwenye yale ambayo wao wamo ndani yake ya unafiki na upotevu

    [5] Na wanapoambiwa hawa wanafiki, «Njooni huku hali ya kutubia mtake udhuru wa hayo yaliyotokea kwenu ya maneno maovu na mazungumzo ya ufidhuli, ili Mtume wa Mwenyezi Mungu awaombee Mwenyezi Mungu msamaha wa dhambi zenu , huvigeuza vichwa vyao na wakavitikisa kwa njia ya shere na kiburi. Na utawaona, ewe Mtume, wanakupa mgongo na huku wao wanalifanyia kiburi jambo la kufuata yale ambayo walitakiwa wayafuate

    [6] Yanalingana kwa wanafiki hawa, uwaombee msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ewe Mtume, au usiwaombee, kwani Mwenyezi Mungu Hatazisamehe dhambi zao kabisa kwa sababu ya kuendelea kwao na uasi na kujikita kwao kwenye ukafiri. Hakika Mwenyezi Mungu Hawaelekezi kwenye Imani watu wanaomkanusha waliotoka nje ya utiifu Kwake

    [7] Wanafiki hawa ndio wao wanaosema kuwaambia watu wa Madina, «Msitoe kuwasaidia Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu waliohama mpaka wajiepushe naye.» Ni za Mwenyezi Mungu, Peke Yake, hazina za mbinguni na ardhini na vilivyomo humo miongoni mwa riziki, Humpa Anayemtaka na Humnyima Anayemtaka, lakini wanafiki hawaelewi kwamba riziki inatoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ujinga wao wa kutomjua Yeye, kutakasika na kila upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake

    [8] Wanasema hawa wanafiki, «Tutakaporudi Madina, kundi letu lenye nguvu zaidi litalitoa kundi la Waumini lililo twevu zaidi.» Kwa hakika, nguvu na ushindi ni vya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ni vya Mtume Wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na ni vya wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, si vya wale wasiokuwa wao, lakini wanafiki hawalijui hilo kwa ujinga wao uliokita mizizi

    [9] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata Sheria Zake kivitendo! Yasiwashughulishe nyinyi mali yenu wala wana wenu na kumuabudu Mwenyezi Mungu na kumtii. Na yoyote atakayeshughulishwa na mali Yake na watoto Wake na hilo la kumuabudu Mwenyezi Mungu, basi hao ndio waliopunjwa hisa zao za makaribisho ya Mwenyezi Mungu na rehema Yake

    [10] Na toeni, enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, sehemu ya kile tulichowapa katika njia za kheri, mkilikimbilia hilo kabla ya kifo hakijamjia mmoja wenu na kuziona dalili zake na alama zake, na hapo aseme kwa kujuta, «Mola wangu! Si unipe muda na uahirishe kifo changu kipindi kifupi! Nipate kutoa sadaka sehemu ya mali yangu na niwe miongoni mwa watu wema wachamungu.»

    [11] Na wala Mwenyezi Mungu hatoichelewesha nafsi yoyote utakapokuja wakati wa kifo chake na umri wake ukakoma. Na Mwenyezi Mungu, kutakasika na kila sifa ya upungufu ni Kwake, ni mtambuzi wa yale mnayoyatenda: mema na mabaya, na Awetawalipa nyinyi kwa hayo

    Kufunuliwa

    Surah 64

    [1] Vinamtakasa Mwenyezi Mungu na sifa zisizonasibiana na Yeye vyote vilivyoko mbinguni na vilivyoko ardhini. Ni Wake Yeye Mwenyezi Mungu, kutakasika na kila upungufu ni Kwake, uendeshaji mambo usio na kizuizi katika kila kitu. Na Yeye Ndiye Mwenye sifa njema zilizo nzuri. Na Yeye juu ya kila kitu ni Muweza

    [2] Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyewafanya nyinyi mpatikane kutoka kwenye hali ya kutokuwako, kati yenu kuna wenye kuukanusha uungu Wake na baadhi yenu kuna wenye kuuamini na kufuata Sheria Zake kivitendo. Na Yeye, kutakasika na kila sifa za upungufu ni Kwake, ni Mwenye kuviona vitendo vyenu, hakuna chochote chenye kufichamana Kwake, na Atawalipa kwavyo

    [3] Ameumba mbingu na ardhi kwa hekima kubwa, na Akawaumba nyinyi katika sura nzuri, na Kwake Yeye ndio marejeo Siku ya Kiyama, Amlipe kila mtu kwa matendo yake

    [4] Anajua, kutakasika na kutukuka ni Kwake, kila kilichoko mbinguni na ardhini, na Anakijua mnachokificha, enyi watu, na mnachokidhihirisha. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yale yanayodhamiriawa na vifua na kufichwa na nafsi

    [5] Je haikuwajia nyinyi, enyi washirikina, habari ya wale waliokufuru miongoni mwa watu waliopita kabla yenu, ulipowafikia wao mwisho mbaya wa ukafiri wao na uovu wa vitendo vyao hapa ulimwenguni na kuwa wao kesho Akhera watakuwa na adhabu kali iumizayo

    [6] Hayo yaliyowapata duniani na yatakayowapata kesho Akhera ni kwamba wao walikuwa wakijiliwa na Mitume wa Mwenyezi Mungu na alama waziwazi na miujiza iliyofunuka wazi, huwa wakisema, «Je binadamu kama sisi wanatuongoza? Hapo wakamkufuru Mwenyezi Mungu, wakaukanusha ujumbe wa Mitume Wake na wakaipa mgongo haki wasiikubali. Na Mwenyezi Mungu Hana haja na kuamini kwao wala kuabudu kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Ana utajiri uliotimia usio na mpaka, ni Mwenye kusifiwa kwa maneno Yake, matendo Yake, na sifa Zake, Hawajali wao wala haumdhuru Yeye upotevu wao chochote

    [7] Walidai wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu kwa ubatilifu kwamba wao hawatatolewa kwenye makaburi yao baada ya kufa. Waambie, ewe Mtume, «Ndio. Naapa kwa Mola wangu! Mtatolewa makaburini mwenu mkiwa hai, kisha mtapewa habari ya yale mliyoyafanya duniani. Na hilo kwa Mwenyezi Mungu ni sahali na rahisi

    [8] Basi mwaminini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, enyi washirikina, na mjiongoze kwa Qur’ani Aliyomteremshia Mtume Wake. Na Mwenyezi Mungu kwa mnayoyafanya ni Mtambuzi, hakuna kinachofichamana na Yeye cha matendo yenu na maneno yenu, na Yeye ni Mwenye kuwalipa kwa hayo Siku ya Kiyama

    [9] Ikumbukeni Siku ya Mkusanyo ambayo Mwenyezi Mungu Atawakusanya wa mwanzo na wa mwisho. Siku hiyo ambayo ina mpunjano na mtengano kati ya viumbe: Waumini wawapunje makafiri na wenye kuasi, na wao hao( hao makafiri na waasi) iwadhihirikie wazi kuwa wao ndio waliopata hasara. Basi wenye Imani wataingia Peponi kwa rehema za Mwenyezi Mungu, na wenye ukafiri wataingia Motoni kwa uadilifu Wake. Na mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu na akafanya matendo ya utiifu Kwake, Atamfutia dhambi zake na Amtie kwenye mabustani ya Pepo ambayo chini ya majumba yake ya fahari inapita mito ya maji, hali ya kukaa milele humo. Kukaa milele huko Peponi ndiko kufaulu kukubwa ambako hakuna kufaulu kushinda huko

    [10] Na wale ambao wanapinga kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye Mola wa haki na wakazikanusha dalili za kuwa Yeye Ndiye Mola na hoja za uungu Wake Alizowatuma nazo Mitume Wake, hao ni watu wa Motoni, ni wenye kukaa humo milele. Moto huo wa Jahanamu ni marejeo maovu mno watakayofikia

    [11] Halimpati yoyote jambo lolote la shida isipokuwa kwa ruhusa ya Mwenyezi Mungu na mapitisho Yake na makadirio Yake. Na yoyote anayemuamini Mwenyezi Mungu, Atauongoza moyo Wake ufuate amri Zake na uridhike na mapitisho Yake. Atauongoza kwenye njia nzuri ya maneno, vitendo na hali. Kwani uongofu hasa ni wa moyo, na viungo vinafuata. Na Mwenyezi Mungu kwa kila kitu ni Mjuzi, hakifichamani Kwake chochote miongoni mwa hivyo

    [12] Na mtiini Mwenyezi Mungu, enyi watu, na muongokee Kwake katika yale Aliyoyaamrisha na Aliyoyakataza, na mfuateni Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, katika yale aliyowafikishia kutoka kwa Mola wake. Na iwapo mtaupa mgongo utiifu wenu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, basi Mjumbe wetu hana madhara yoyote kutokana na kupa mgongo kwenu. Jukumu lake yeye ni kuwafikishia nyinyi yale Aliyotumilizwa kwayo ufikishaji wenye maelezo ya waziwazi

    [13] Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Ndiye Ambaye hukuna muabudiwa wa kweli isipokiuwa Yeye. Na kwa Mwenyezi Mungu tu na wategemee Waumini, kwa upweke Wake, katika mambo yao yote

    [14] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake! Kwa kweli miongoni mwa wake zenu na wana wenu ni maadui wenu, wanawazuia nyinyi na njia ya Mwenyezi Mungu na wanawavunja moyo ya kumtii Mwenyezi Mungu, basi jihadharini nao wala msiwasikilize. Na iwapo mtayasamehe makosa yao, mkayapa mgongo na mkayaficha msiyatangaze, basi Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe ni Mwingi wa rehema, Atawasamehe nyinyi madhambi yenu, kwani Yeye, Aliyetakasika na kila upungufu, ni Mkubwa wa kusamehe ni Mkunjufu wa rehema

    [15] Hayakuwa mali yenu na watoto wenu isipokuwa ni majaribio na mtihani kwenu. Na Mwenyezi Mungu, Kwake Yeye kuna thawabu kubwa kwa aliyechagua kumtii Yeye kuliko kumtii asiyekuwa Yeye na akatekeleza haki ya Mwenyezi Mungu katika mali yake

    [16] Fanyeni juhudi zenu, enyi Waumini, na tumieni nguvu zenu katika kumcha Mwenyezi Mungu, na msikilizeni Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, usikilizaji wa kuzingatia na kufikiri, zifuateni amri Zake na myaepuke makatazo Yake na mtoe katika kile Alichowaruzuku Mwenyezi Mungu, hilo litakuwa bora kwenu. Na atakayeepukana na uchoyo na kubania kilichozidi katika mali, basi hao ndio watakaozipata kheri zote, watakaofaulu kupata kila wanalolitaka

    [17] Iwapo mtatoa mali yenu katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Yeye na kwa moyo mzuri, Atawaongezea Mwenyezi Mungu thawabu za ambacho mmekitoa na Atawasamehe madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kurudisha shukrani kwa watoaji kwa kuwapa malipo mema ya kile walichokitoa, ni Mpole kwa kutoharakisha mateso kwa wanaomuasi

    [18] Na Yeye, kutakasika na kila upungufu ni Kwake, ni Mjuzi wa kila lililofichika lisionekane na lile lililojitokeza likaonekana, ni Mshindi Asiye na mshindani, ni Mwingi wa hekima katika maneno Yake na matendo Yake

    Talaka

    Surah 65

    [1] Ewe Mtume! Pindi mnapotaka, wewe na Waumini, kuwapa talaka wake zenu, basi wapeni talaka wakiwa kwenye hali ya kukabili kipindi cha wao kukaa eda- yaani kwenye hali ya usafi ambao hakukupatikana kuingiliwa, au katika hali ya mimba iliyo wazi- na mshike hesabu ya eda, mpate kujua muda wa kuwarejea iwapo mtataka kuwarejea, na muogopeni Mwenyezi Mungu, Mola wenu. Wala msiwatoe wanawake waliopewa talaka kwenye majumba wanayokaa mpaka eda lao limalizike, nalo ni hedhi tatu kwa asiyekuwa mdogo (asiyeingia damuni) na si kwa aliyekata tamaa ya kuingia damuni (kwa uzee) wala mwenye mimba. Na haifai kwa wanawake hao kutoka majumbani mwao wao wenyewe isipokuwa watakapofanya kitendo kiovu cha waziwazi kama vile uzinifu. Na hizo ndizo hukumu za Mwenyezi Mungu alizozipitisha kwa waja Wake. Na Mwenye kuzikiuka hukumu za Mwenyezi Mungu, basi huyo amejidhulimu nafsi yake na ameipeleka mahali pa maangamivu. Hujui, ewe mtoaji talaka, kwamba Mwenyezi Mungu huenda, baada ya talaka hiyo, Akaleta jambo usilolitazamia ukaja ukamrudia

    [2] Na pindi kipindi cha eda la wanawake waliopewa talaka kinapokaribia kumalizika, basi warudieni na mtangamane nao kwa wema pamoja na kuwapatia matumizi, au waacheni pamoja na kuwatekelezea haki zao bila kuwafanyia mambo ya kuwadhuru. Na wekeni mashahidi mnaporejeana na mnapoachana, wanaume wawili waadilifu miongoni mwenu. Na tekelezeni, enyi mashahidi, ushahidi wenu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu na sio kwa kitu kingine. Hilo ambalo Mwenyezi Mungu Amewaamrisha kwalo yuwawaidhiwa nalo yule anayemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na yoyote atakayemuogopa Mwenyezi Mungu akayafuata kivitendo yale ambayo Amemuamrisha nayo na akayaepuka yale ambayo Amemkataza nayo, Atamtolea njia ya kutoka kwenye kila dhiki

    [3] na Atamfanyia nyepesi njia za kupata riziki kwa namna ambayo haikupita akilini mwake wala haikuwa kwenye hesabu zake. Na yoyote atakayemtegemea Mwenyezi Mungu basi Yeye Atamtosheleza yale yanayomkera katika mambo yake yote. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kulifikilia jambo Lake, Hapitwi na kitu chochote wala haelemewi na kitu chochote kinachotakikana na Yeye, hakika Mwenyezi Mungu Amekiwekea kila kitu muda wake wa kukomea na kipimo ambacho kitu hiko hakiwezi kukipita

    [4] Na wanawake walioachwa ambao damu zao za hedhi zimekatika kwa utu uzima wao, mkitatizika mkawa hamjui: ni nini hukumu yao? Basi, eda lao ni miezi mitatu. Na wanawake wadogo ambao hawajaingia damuni, basi eda lao ni miezi mitatu vilevile. Na wanawake wajawazito, eda lao ni linamalizikia pale wanapozaa. Na yoyote atakayemuogopa mwenyezi Mungu na akatekeleza hukumu Zake, Atamfanyia mambo Yake yawe mepesi duniani na Akhera

    [5] Hayo yailotajwa kuhusiana na mambo ya talaka na eda ni amri ya Mwenyezi Mungu Aliyoiteremsha kwenu, enyi watu, ili muitumie. Na yoyote mwenye kumuogopa Mwenyezi Mungu akawa anamcha kwa kuyaepuka yale ya kumuasi na kuzitekeleza faradhi Zake, basi Atamfutia madhambi yake, Atamuongezea kwa wingi malipo yake huko Akhera na amuingize Peponi

    [6] Wakalisheni, wale walioachwa miongoni mwa wake zenu kwenye kipindi chao eda, mahali mfano wa pale mnapokaa nyinyi kwa kadiri ya ukunjufu wenu na uwezo wenu. Wala msiwafanyie mambo ya kuwadhuru mkawatilia mkazo katika makazi. Na iwapo wake zenu waliopewa talaka ni waja wazito, basi wapeni matumizi pindi wakiwa kwenye eda lao mpaka watakapozaa. Na iwapo watawanyonyeshea nyinyi watoto wao ambao ni wenu kwa malipo, basi wapeni malipo yao, na amrishaneni nyinyi kwa nyinyi wema na roho nzuri. Na iwapo hamkukubaliana juu ya unyonyeshaji wa mama mzazi, basi baba atanyonyeshewa na mnyonyeshaji mwingine asiyekuwa mama aliyepewa talaka

    [7] Na atoe matumizi mume kulingana na kile alichokunjuliwa nacho na Mwenyezi Mungu kumpa mkewe aliyeachana naye na amlipie mwanawe, iwapo mume ana ukunjufu wa mapato. Na yule ambaye amebanika kimatumizi naye ni fukara, basi na atoe kulingana na kile alichopewa na Mwenyezi Mungu katika matumizi. Masikini halazimishwi kutoa kama kile anacholazimishwa tajiri. Mwenyezi Mungu Ataleta, baada ya dhiki na shida, ukunjufu wa maisha na kutosheka

    [8] Na kuna vitongoji vingi ambavyo watu wake waliasi amri ya Mwenyezi Mungu na amri ya Mitume Wake na wakaendelea kwenye ukiukaji wao na ukafiri wao

    [9] tukawahesabu juu ya matendo yao duniani hesabu kali mno na tukawaadhibu adhabu kubwa na mbaya, wakauonja mwisho mbaya wa ujeuri wao na ukafiri wao, na mwisho wa ukafiri wao ulikuwa ni maangamivu na hasara, hapana hasara nyingine baada ya hiyo

    [10] Mwenyezi Mungu Amewaandalia watu hawa, waliokiuka mipaka na wakaenda kinyume na amri za Mwenyezi Mungu na amri za Mitume Wake, adhabu kali sana. Basi muogopeni Mwenyezi Mungu na mjihadhari na mambo Anayoyachukia, enyi watu wenye akili zilizokomaa, mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake na mkazifuata Sheria Zake kivitendo! Kwa hakika Mwenyezi Mungu Ameteremsha kwenu, enyi Waumini, Ukumbusho wa kuwakumbusha nao na kuwazindusha juu ya fungu lenu la kumuamini Mwenyezi Mungu na kuwa watiifu Kwake kivitendo

    [11] Na ukumbusho huu ni Mtume anayewasomea nyinyi aya za Mwenyezi Mungu zinazowafafanulia haki kwa kuitenga na ubatilifu, ili Apate kuwatoa, wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakazifuata Sheria Zake kivitendo na wakamatii, kutoka kwenye giza la ukafiri kuwapeleka kwenye mwangaza wa Imani. Na yoyote atakayemuamini Mwenyezi Mungu na akafanya matendo mema Atamuingiza kwenye mabustani ya Peponi ambayo chini ya miti yake inapita mito ya maji, wasalie humo milele. Kwa hakika Mwenyezi Mungu Ameifanya riziki ya Muumini mwema iwe nzuri huko Peponi

    [12] Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Ndiye Aliyeziumba mbingu saba na Akaumba ardhi saba, na Akateremsha amri kupitia wahyi Aliyowateremshia Mitume Wake na kwa yale Anayowapangia viumbe Vyake kwayo kati ya mbingu na ardhi, ili mpate kujua , enyi watu, kwamba Mwenyezi Mungu juu ya kila kitu ni Muweza, hakuna kinachomshinda na kwamba Mwenyezi Mungu Amekizunguka kila kitu kiujuzi, basi hakuna kitu chochote kilichoko nje ya ujuzi Wake na uweza Wake

    Kuzuia

    Surah 66

    [1] Ewe Mtume! Mbona unajizuia nafsi yako na halali Aliyokuhalalishia Mwenyezi Mungu kwa kuwa unataka kuwaridhisha wake zako? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kukusamehe, ni Mwenye huruma kwako

    [2] Kwa hakika Amepasisha Mwenyezi Mungu kwenu, enyi Waumini, kuvihalalisha viapo vyenu kwa kuvitolea kafara. Kafara yenyewe ni kuwalisha masikini kumi au kuwavisha au kuacha shingo huru. Na asiyepata cha kutoa, basi afunge siku tatu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwanusuru nyinyi na kuyasimamia mambo yenu. Na Yeye Ndiye Mjuzi wa mambo yanayowafaa Akayapitisha kwenu, Ndiye Mwingi wa hekima kwenye maneno Yake na matendo Yake

    [3] Na pindi Mtume alipompa siri mke wake Hafsah, radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie, ya mazungumzo fulani, na yeye alipomwambia maneno hayo mke mwenzake 'Aishah, radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie, na Mwenyezi Mungu Akamjulisha Mtume Wake kuwa mkewe ameitoa siri yake, alimjulisha Hafsah sehemu ya maneno aliyoyatoa na akayanyamazia mengine asimwambie kwa kuchunga heshima. Basi Mtume alipomwambia Hafsah yale mazungumzo aliyoyatangaza, alisema huyo mke, «Ni nani aliyekwambia maneno hayo?» Akasema Mtume, «Aliyenambia hayo ni Mwenyezi Mungu, Aliye Mwingi wa ujuzi na utambuzi, Ambaye hakifichamani Kwake chenye kujificha chochote

    [4] Iwapo mtarudi kwa Mwenyezi Mungu (ewe Hafsah na 'Aishah) basi yatakuwa yamepatikana kwenu yanayopelekea kukubaliwa toba yenu, kwa kuwa nyoyo zenu zilielekea kwenye kuyapenda yale aliyoyachukia Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ya kutoa siri yake. Na mtakaposaidiana juu yake kwa kufanya yanayomuudhi, basi Mwenyezi Mungu Ndiye Msimamizi wake na Mtetezi wake na Jibrili na Waumini wema. Na Malaika, baada ya usaidizi wa Mwenyezi Mungu, ni wasaidizi wake na watetezi juu ya yoyote anayemuudhi na kumfanyia uadui

    [5] Linalotarajiwa kwa Mola wake iwapo atawaacha nyinyi, enyi wake zake, ni amuoze yeye, badala yenu nyinyi, wake wanyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu kwa kumtii, wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, wenye kumtii Mwenyezi mungu, wenye kurudi kwenye yale anayoyapenda Mwenyezi Mungu ya kumtii Yeye, wenye kumuabudu kwa wingi, wenye kufunga sana, wakiwa wake wakuu miongoni mwao na wanawali

    [6] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata Sheria Zake kivitendo! Zilindeni nafsi zenu kwa kuyatenda yale ambayo Amewaamrisha kwayo Mwenyezi Mungu na kuyaepuka yale ambayo Amewakataza nayo, na walindeni watu wenu kwa kile mnachotumia kujilinda nyinyi wenyewe na Moto ambao kuni zake ni watu na majiwe. Watasimamia kuadhibiwa watu wa Motoni Malaika wenye nguvu walio thabiti katika usimamizi wao, wasioenda kinyume na Mwenyezi Mungu katika maamrisho Yake na wanaotekeleza yale wanayoamrishwa

    [7] Na wataambiwa wale waliokanusha kwamba Mwenyezi mungu Ndiye Mola wa haki na wakamkufuru, watakapoingizwa Motoni, «Msitafute nyudhuru Siku ya Leo, ukweli ni kwamba nyinyi mnapewa malipo ya yale ambayo mlikuwa mkiyafanya duniani

    [8] Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na mtume Wake na mkafuata Sheria Zake kivitendo! Acheni madhambi yenu na mrudi kwenye kumtii Mwenyezi Mungu, kurudi kwa mwisho kusikokuwa na ufanyaji maasia tena kwa kutarajia Mola wenu Awafutie maovu ya matendo yenu na Awaingize kwenye mabustani ya Peponi ambayo chini ya majumba yake ya fahari inapita mito ya maji, Siku ambayo Mwenyezi Mungu Hatamfedhehi Nabii na walioamini pamoja naye wala hatawatesa, bali Atavipandisha juu vyeo vyao. Nuru ya watu hawa itakuwa inatembea mbele yao na kuliani mwao huku wakisema, «Mola wetu! Tukamilishie sisi nuru yetu mpaka tuvuke Ṣirāṭ na tuongoke njia ya kwenda Peponi, na utusamehe na uyatupilie mbali madhambi yetu na uyasitiri, kwani wewe Kwa hakika ni Muweza juu ya kila kitu.»

    [9] Ewe Nabii! Pigana jihadi na wale waliouonyesha ukafiri waziwazi na wakautangaza, na pigana nao kwa upanga, na pigana jihadi na wale waliouficha ukafiri na kuufinika kwa hoja na kwa kusimamisha hukumu za Sheria na vitambulisho vyaa Dini. Na utumie ukali na ugumu katika kupigana jihadi na makundi mawili hayo. Na makazi yao ambayo watakwenda kukaa huko Akhera ni moto wa Jahanamu. Na ni marejeo maovu mno hayo watakayoyarejea

    [10] Mwenyezi Mungu Anapiga mfano wa hali ya makafiri- katika kutangamana kwao na Waislamu, kuwa karibu na wao na kutangamana nao na kwamba hilo halitawanufaisha kwa kuwa wamemkufuru Mwenyezi Mungu- kuwa ni kama hali ya mke wa Nabii wa Mwenyezi Mungu, Nūḥ, na mke wa Nabii wa Mwenyezi mungu, Lūṭ, kwa kuwa wote wawili walikuwa chini ya hifadhi ya ndoa ya waja wawili wema miongoni mwa waja wetu, ukapatikana kutoka kwao kuwafanyia uhaini wa kidini, kwani wote wawili walikuwa makafiri. Mitume wawili hawa hawakuweza kuwatetea wake zao na adhabu ya Mwenyezi Mungu, na wakaambiwa wake wawili hao, «Ingieni Motoni pamoja na wenye kuingia huko.» Katika kupiga mfano huu pana dalili ya kwamba kuwa karibu na Manabii na watu wema hakufai kitu iwapo mtu mwenyewe ana matendo mabaya

    [11] Na Mwenyezi Mungu Anapiga mfano wa hali ya Waumini- waliomuamini Mwenyezi Munmgu, wakamuabudu Peke Yake na wakazifuata Sheria Zake kivitendo na kwamba wao hakuwadhuru wao kule kutangamana kwao na makfiri katika maingilaiano yao- kuwa ni kama hali ya mke wa Fir'awn aliyekuwa kwenye hifadhi ya ndoa ya aliyekuwa muovu mno miongoni mwa wale waliomkufuru Mwenyezi Mungu, na hali yeye alikuwa anamuamini Mwenyezi Mungu, pindi aliposema, «Mola wangu! Nijengee Nyumba huko kwako Peponi na uniokoe na utawala wa Fir'awn na ukafiri wake na yale matendo maovu yanayotokana na yeye, Na uniokoe na watu wenye kumfuata katika udhalimu na upotevu, na uniokoe na mateso yao

    [12] Na Mwenyezi Mungu Anapiga mfano kwa walioamini. Mfano wenyewe ni Maryam binti 'Imran aliyeihifadhi tupu yake na akailinda na uzinifu, basi mwenyezi Mungu Akamuamrisha Jibrili, amani imshukie, apulize kwenye mfuko wa nguo yake. Na ule mpulizo ukafika kwenye uzao wake. Hapo akabeba mimba ya ‘Īsā, amani imshukie, akayaamini maneno ya Mola wake, akafuata kivitendo Sheria Zake Alizozipasisha kwa waja Wake na vitabu Vyake Alivyoviteremsha kwa Mitume Wake, na akawa ni miongoni mwa wale wenye kumtii Yeye

    Ufalme

    Surah 67

    [1] Zimekithiri kheri za Mwenyezi Mungu na wema Wake kwa viumbe Vyake, Ambaye mkononi Mwake upo ufalme wa duniani na Akhera na mamlaka ya viwili hivyo, Anapitisha amri Yake na uamuzi Wake kwenye mamlaka Yake hayo, na Yeye kwa kila jambo ni Muweza. Faida inayopatikana katika aya hii ni kuwa inathibitisha sifa ya mkono kwa Mwenyezi Mungu Aliyetakasika na kutukuka, kwa namna inavyonasibiana na utukufu Wake

    [2] Aliyeumba mauti na uhai ili awatahini nyinyi, enyi watu, ni yupi miongoni mwenu aliye mwema wa matendo na utakasaji wa nia? Na Yeye Ndiye Mshindi Ambaye hakuna chochote kinachomshinda, Ndiye Mwingi wa msamaha kwa anayetubia miongonu mwa waja Wake. Katika aya hii pana kuhimiza kufanya utiifu na makaemeo ya kutenda maasia

    [3] Aliyeumba mbingu saba zilizopangika, baadahi yake juu ya nyingine, huoni katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema, ewe mwenye kuangalia, tofauti yoyote wala mpambanuko, basi rudia tena kuangalia mbinguni: je unaona pasuko zozote au nyufa

    [4] Kisha rudia kuangalia tena, mara baada ya mara, yatakurudia hayo macho yakiwa manyonge na matwevu hayakuona upungufu wowote na hali yakiwa ni yenye usumbufu na uchovu

    [5] Na hakika tumeupamba uwingu wa karibu unaoonekana na macho kwa nyota kubwa zenye kung’ara, na tumezifanya nyota hizo ni vimondo zenye kuwachoma wenye kusikiliza kwa kuiba miongoni mwa mashetani, na tumewaandalia wao huko Akhera adhabu ya Moto wenye kuwaka wakawa ni wenye kuadhibika kwa joto lake

    [6] Na wenye kumkanusha Mola wao watapata adhabu ya moto wa Jahanamu, na ubaya zaidi wa mahali pa mtu kurejea ni ni huo moto wa Jahanamu

    [7] Waingizwapo hao wakanushaji ndani ya moto wa Jahanamu, watausikia ukitoa sauti kali yenye kutisha , huku ukichemka machemko makali sana

    [8] unakaribia huo moto wa Jahanamu kurarukararuka kwa ukali wa hasira ulizonazo juu ya wakanushaji. Kila linapotiwa humo kundi la watu, wale wawakilishi wa kusimamia mambo ya huo moto wa Jahanamu watawauliza kwa njia ya kuwalaumu na kuwakaripia: Je kwani hakuwajia nyinyi, huko duniani, mjumbe wa kuwatahadharisha na adhabu hii ambayo nyinyi mmo ndani yake

    [9] Watawajibu kwa kusema, «Ndio! Tumejiwa na Mjumbe anayetoka kwa Mwenyezi mungu akatuonya na tukamkanusha na tukasema kuhusu miujiza aliyokuja nayo: Mwenyezi Mungu hakumteremshia binadamu kitu chochote. Hamkuwa nyinyi, enyi Mitume, isipokuwa mmeenda mbali na haki

    [10] Na watasema kwa kukubali makosa, «Lau tungalikuwa tunasikia usikivu wa mwenye kutafuta haki, au tunafikiria juu ya yale tunayoitiwa kwayo, hatungekuwa ni kati ya watu wa Motoni.»

    [11] Hivyo basi wakakubali kukanusha kwao na kukufuru kwao kulikowafanya wastahili adhabu ya Moto. Basi kuwa mbali na rehema ya Mwenyezi Mungu ni kwa watu wa Motoni

    [12] Hakika wale wanaomuogopa Mola wao, wakamuabudu na wasimuasim na hali wako mbali na macho ya watu na wanaiogopa adhabu ya Akhera kabla hawajaiona, watapata msamaha wa dambi zao katoka kwa Mwenyezi Mungu na malipo mema makubwa ambayo ni Pepo

    [13] Na yaficheni maneno yenu, enyi watu, katika jambo lolote miongoni mwa mambo yenu , au yadhihirisheni, kwani yote mawili mbele ya Mwenyezi Mungu ni sawa. Hakika Yeye , kutakasika ni Kwake, ni Mjuzi wa yaliyomo ndani ya vifua, basi yatafichamana vipi maneno yenu na matendo yenu Kwake Yeye

    [14] Je, kwani hajui, Mola wa viumbe, viumbe Vyake na mambo yao na hali ni kuwa Yeye Ndiye Aliyewaumba, Akalitengeneza umbo lao na Akalifanya zuri? Na Yeye Ndiye Mpole kwa waja Wake, Ndiye Mwenye kuwatambua wao na matendo yao

    [15] Mwenyezi Mungu Peke Yake Ndiye Aliyewafanyia ardhi iwe nyepesi iliyotayarishwa mpate kutulia juu yake. Basi tembeeni sehemu zake na pande zake na mle riziki ya Mwenyezi Mungu Anayowatolea humo. Na Kwake Yeye Peke Yake ndio Ufufuzi kutoka makaburini mwenu ili mhesabiwe na mlipwe. Katika hii aya pana ishara ya kuhimiza utafutaji riziki na uchumaji. Pia pana dalili kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Muabudiwa wa haki Peke Yake Asiye na mshirika, na pana dalili ya uweza Wake, kukumbusha neema Zake na kuonya kuelemea duniani

    [16] Je mmesalimika, enyi makafiri wa Makkah, na Mwenyezi Mungu Aliye mbinguni kuwa Hatawadidimiza ardhini ikawa inatetemeka na nyinyi mpaka mkaangamia

    [17] Au mmesalimika kuwa Mwenyezi Mungu Aliye juu ya mbingu kuwa Hatawatumia upepo wenye kuwapiga mawe madogomadogo na hapo mkajua, enyi makafiri, ni vipi onyo langu kwenu mnapoiona adhabu? Na huko kujua wakati huo hakutawanufaisha. Katika hii aya pana kuthibitisha kuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Yuko juu kwa namna inayonasibiana na utukufu Wake, kutakasika ni Kwake

    [18] Kwa hakika walikanusha wale waliokuwa kabla ya makafiri wa Makkah kama vile watu wa Nuchouh, 'Ād na Thamūd walivyowakanusha Mitume wao. Basi kulikuwa namna gani kule kuwakasirikia kwangu na kuwageuzia kwangu neema waliyokuwa nayo kwa kuwateremshia adhabu na kuwaangamiza

    [19] Je kwani walighafilika hawa makafiri wasiwatazame ndege juu yao wakiwa wanazikunjua mbawa zao angani na wakati mwingine wanazikunja na kuzitia mbavuni mwao? Hakuna mwenye kuwatunza wasianguke wakiwa katika hali hiyo isipokuwa Mwingi wa rehema

    [20] Hakika Yeye Anaona kila kitu, hakuna upungufu wala tofauti.Bali ni nani huyu ambaye, kulingana na madai yenu, enyi makafiri, kuwa ni kundi lenu, anayewanusuru asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema, iwapo Yeye Atawatakia baya? Makafiri hawakuwa, katika madai yao isipokuwa wako katika kudanganywa na kupotezwa na Shetani

    [21] Bali ni nani huyo mpaji anayedaiwa atakayewapa nyinyi riziki iwapo Yeye Atazuia riziki Yake na Atawakatalia kuwapa? Bali makafiri wanaendelea kwenye ukiukaji wao na upotevu wao wakiwa katika hali ya ushindani, kujiona na kuikimbia haki, hawaisikii wala hawaifuati

    [22] Je huyu anayetembea akiwa kichwa chake kimeinama hajui pa kuelekea wala namna ya kwenda yuko katika kulingana zaidi kwenye njia na ameongoka zaidi au ni yule anayetembea sawasawa, akiwa na kimo kilicholingana, aliye mzima, afuataye njia iliyofunuka wazi isiyokuwa na mpeteko? Na huu ni mfano Mwenyezi Mungu Amempigia kafiri na na Muumini

    [23] Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyewapatisha nyinyi kutoka kwenye hali ya kutokuwako, na akawafanya nyinyi muwe na mashikio ili msikie kwayo, macho ili muonee na nyoyo ili muelewe kwazo. Basi ni uchache, enyi makafiri, mnavyomtekelezea shukrani Mola wenu kwa neema hizi alizowaneemesha

    [24] Waambie, «Mwenyezi Mungu ndiye Aliyewaumba na Akawaeneza ardhini. Na Kwake Yeye, PekeYake, mtakusanywa baada ya huku kutengana, ili mhesabiwe na mlipwe.»

    [25] Na wanasema hao makafiri, «Ni lini itakapohakikika ahadi hii, ewe Muhammad? Tupeni habari ya kipindi chake, enyi Waumini, iwapo nyinyi ni wakweli katika yale mnayoyadai.»

    [26] Waambie hao, ewe Mtume, «Hakika ujuzi wa kipindi cha kusimama Kiyama uko kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake Ndiye Anayehusika nacho. Na hakika si lingine ni kwamba mimi ni muonyaji kwenu, ninawaogopesha mwisho mbaya wa ukafiri wenu na ninawaeleza kile Alichoniamrisha Mwenyezi Mungu nikibainishe upeo wa kubainisha

    [27] Watakapoiona makafiri adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwa iko karibu nao na wakaishuhudia, utajitokeza unyonge na unguliko kwenye nyuso zao na waambiwe, kwa njia ya kuwalaumu na kuwakaripia, «Hii ndiyo ile mliokuwa mkitaka iharakishwe ulimwenguni.»

    [28] Sema, ewe Mtume, uwaambie hawa makafiri, «Nipasheni habari, iwapo Mwenyezi Mungu Atanifisha pamoja na Waumini walio pamoja na mimi, kama mnavyotamani, au Ataturehemu avicheleweshe vipindi vyetu vya kufa na Atuepushie adhabu yake, basi ni nani huyo ambaye atawahami aizuie adhabu kali yenye kuumiza isiwafikie?»

    [29] Sema, «Ni Mwenyezi Mungu! Yeye Ndiye Mwingi wa rehema. Tumemuamini na tumeifuata Sheria Yake kivitendo na tumemtii. Na Kwake yeye, Peke Yake, tumetegemea katika mambo yetu yote. Basi mtajua, enyi makafiri, itakapoteremka adhabu, ni yupi kati ya makundi mawili miongoni mwetu: sisi na nyinyi, yuko mbali waziwazi na njia ya Mwenyezi Mungu iliyonyoka.»

    [30] Sema, ewe Mtume, Uwaambie hawa washirikina, «Nipasheni habari iwapo maji yenu mnayokunywa ni yenye kupotea ndani ya ardhi, mkawa hmyafikii kwa namna yoyote, basi ni nani asiyekuwa Mwenyezi Mungu Atakayewaletea maji yenye kutembea ardhini na yenye kuonekana na macho»

    Kalamu

    Surah 68

    [1] «Nūn» Yametangulia maelezo kuhusu herufi zilizokatwakatwa na kutengwa mwanzo wa sura ya Al-Baqarah

    [2] Anaapa Mwenyezi Mungu kwa Kalamu ambayo kwayo Malaika na watu wanaandikia, na kwa kile wanachokiandika cha kheri, manufaa na aina za elimu

    [3] Hukuwa wewe, ewe Mtume, kwa sababu ya neema ya Mwenyezi Mungu kwako, ya unabii na utume, ni mchache wa akili wala mwenye uduni wa maoni. Na wewe una malipo makubwa yasiyopunguzwa wala kukatwa kwa yale matatizo unayopambana nayo ya ufikishaji ujumbe

    [4] Na hakika wewe, ewe Mtume, uko juu ya tabia kubwa, nazo ni zile tabia njema zilizomo kwenye Qur’ani. Kwani kule kuifuata Qur’ani kulikuwa ni sifa yake, akitekeleza amri zake na kukomeka na yale yanayokatazwa nayo

    [5] Kwa kipindi cha karibu kijacho, utaona ewe Mtume, na wataona

    [6] makafiri ugonjwa wa akili na wazimu viko kwa nani miongoni mwenu

    [7] Hakika Mola wako , kutakasika ni Kwake, Ndiye Mjuzi zaidi wa kumjua mpotofu aliyeenda kombo na Dini ya Mwenyezi Mungu na njia ya uongofu, na Yeye Ndiye Mjuzi zaidi wa kumjua mchamungu aliyeongoka kwenye njia ya haki

    [8] Basi jikite kwenye msimamo ulionao, ewe Mtume, wa kuenda kinyume na wakanushaji, na wala usiwatii

    [9] Wanatamani na wanapenda lau wewe unakuwa laini kwao na kuwakubalia baadhi ya misimamo waliyonayo, na wao wakawa laini kwako

    [10] Usimkubalie, ewe Mtume, kila mtu mweye kuapa mayamini sana

    [11] mrongo sana, mtwevu, msengenyaji watu, anayetembea baina yao kwa kuchochea ugomvi na kuchukua maneno ya baadhi yao kuwapelekea wengine kwa lengo la kuharibu baina yao, bahili wa mali mwenye uchoyo wa kuyatumia katika njia ya haki

    [12] mwenye kuzuia sana ufanyaji wema, anayevuka mpaka wake katika kuwafanyia watu uadui na kutumia yaliyohartamishwa, mwingi wa madhambi

    [13] mshupavu katika ukafiri wake, mchafu na muovu na anayenasibishwa na baba asiye wake

    [14] Na kwa kuwa yeye ni mwenye mali na wana ndipo akakiuka mipaka na akaifanyia kiburi haki

    [15] Ikawa akisomewa aya za Qur’ani na mtu yoyote huzikanusha na kusema kuwa hizo ni maneno ya urongo na itikadi za watu waliopita. Aya hizi, ingawa zimeteremka kwa baadhi ya washirikina, kama vile al-Walīd bin \al-Mughīrah, zina onyo ndani yake kwa Muislamu asikubaliane na anayesifika kwa sifa hizi zenye kutukanika

    [16] Tutaweka alama ya kudumu juu ya pua yake isiyomuepuka, ili afedheheke mbele za watu

    [17] Sisi tumewatahini watu wa Makkah kwa njaa na ukame kama tulivyowatahini wenye shamba walipoapa wakiwa pamoja kwamba watakwenda kuvuna matunda ya shamba lao asubuhi mapema, ili wasiokuwa wao, kati ya masikini na mfano wao, wasipate kula katika mavuno hayo

    [18] Na wasiseme walipopanga hayo, «Mwenyezi Mungu Akitaka»

    [19] Mwenyezi Mungu akaliteremshia shamba hilo moto ukaliteketeza kipindi cha usiku na hali wao wakiwa wamelala

    [20] Na likapambaukiwa nalo lishachomeka limekuwa leusi kama usiku wa giza

    [21] Hapo wakaitana kipindi cha asubuhi

    [22] «Haya tokeni mapema mwende kwenye shamba lenu iwapo bado mnataka kuvuna matunda!»

    [23] Wakatoka kwa haraka, huku wakinong’ onezana

    [24] «Leo msimpe nafasi masikini yoyote kuingia shamba lenu.»

    [25] Wakaenda kipindi cha mwanzo wa mchana kuelekea kwenye shamba lao wakiwa na lengo baya la kuwanyima masikini matunda ya shamba, wakiwa wana uwezo kamili wa kulitekeleza hilo kulingana na madai yao

    [26] Walipolishuhudia shamba lao limechomeka walilikataa na wakasema, ‘Kwa hakika tumepotea njia ya kulifikia!» na walipojua kuwa hilo ndilo shamba lao walisema

    [27] «Bali sisi tumekoseshwa mazao yake kwa sababu ya nia yetu ya uchoyo na kuwanyima masikini.»

    [28] Akasema muadilifu zaidi miongoni mwao, «Kwani sikuwaambia myafunge maneno yenu na matakwa ya mwenyezi Mungu kwa kusema ‘Mwenyezi Mungu Akitaka’?»

    [29] Hapo wakasema, baada ya kurudi kwenye fahamu za uongofu, «Mwenyezi Mungu Mola wetu Ametakasika na udhalimu katika haya yaliyotupata, lakini ni sisi ndio tuliojidhulumu nafsi zetu kwa kuacha kuyafunga maneno yetu na matakwa ya Mwenyezi Mungu na kwa lengo letu baya.»

    [30] Wakazungukiana wao kwa wao wakilaumiana kwa kuacha kuyafunga maneno yao na matakwa ya Mwenyezi Mungu na kwa lengo lao baya

    [31] wakasema, «Ewe ole wetu! Sisi tulikuwa tumekiuka mpaka kwa kuwanyima masikini na kuenda kinyume na amri ya Mwenyezi Mungu

    [32] Tunatarajia kwa Mola wetu kuwa Atatupa kilicho bora zaidi kuliko shamba letu, kwa kuwa tumetubia na tumekubali makosa yetu. Sisi tuna matumaini mema kwa Mola wetu, tunatarajia msamaha na tunaomba kheri. Mfano wa mateso hayo tuliyowatesa nayo wenye shamba ndivyo yanavyokuwa mateso yetu duniani kwa kila anayeenda kinyume na amri ya Mwenyezi Mungu na akazifanyia uchoyo neema za Mwenyezi Mungu Alizompa kwa kutotekeleza haki ya Mwenyezi Mungu katika neema hizo

    [33] Na kwa hakika adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kubwa zaidi na ni kali zaidi kuliko adhabu ya duniani. Lau wao wangalijua wangalijiepusha na kila jambo lenye kusababisha kupata mateso hayo

    [34] Hakika wale waliojikinga na mateso ya Mwenyezi Mungu kwa kufanya yale Aliyowaamrisha na kuacha yale Aliyoyakataza, watapata kwa Mola wao huko Akhera, mabustani ya Peponi ambayo ndani yake kuna starehe za daima

    [35] Je tuwafanye wale wanaomnyenyekea Mwenyezi Mungu kwa kumtii ni kama wale waliokufuru

    [36] Mna nini nyinyi? Vipi mnatoa uamuzi huu wa kudhalimu, mkalinganisha baina yao katika malipo

    [37] Au nyinyi mna kitabu kilichoteremshwa kutoka mbinguni ambacho mnakuta ndani yake kuwa mtiifu ni kama muasi, mkawa mnayasoma hayo mnayoyasema

    [38] Hivyo basi nyinyi ndani ya kitabu hiki mna kila mnachokitamani. Basi hilo nyinyi hamnalo

    [39] Au nyinyi mna ahadi na mapatano ya lazima juu yetu kuwa mtapata mnayoyataka na kuyatamani

    [40] Waulize washirikina, ewe Mtume, «Ni yupi katika wao anayeichukulia hukumu hiyo dhamana na ahadi kwamba atayapata hayo?»

    [41] Au wau wana waungu wanaowachukulia dhamana kwa wanayoyasema na kuwasaidia kuyafikia hayo wanayoyataka? Basi na wawalete iwapo wao ni wakweli katika madai yao

    [42] Siku ya Kiyama, mambo yatakuwa magumu na kituko chake kitakuwa kikubwa, na hapo Mwenyezi Mungu Aje ili kutoa uamuzi baina ya viumbe, Afunue muundi Wake usiofanana na kitu chochote. Amesema, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, «Atafunua Mola wetu muundi Wake, hapo amsujudie kila mwanamume aliyeamini na mwanamke aliyeamini, na atasalia yule aliyekuwa akisujudu duniani kwa kujionesha na kusikika, aende kusujudu na mgongo wake ugeuke kuwa mfupa mmoja.» Imepokewa na Bukhari na Muslim

    [43] Yatakuwa yameinama macho yao, hawayainui, wamefinikwa na unyonge mkubwa kutokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu, na hali wao walikuwa ulimwenguni wakiitwa kuswali na kumumuabudu Mwenyezi Mungu wakiwa na nguvu zao na uwezo wa kufanya hivyo, wakawa hawasujudu kwa kiburi na kujiona wakubwa

    [44] Basi, niache, ewe Mtume, na wale wanaoikanusha hii Qur’ani! Ni juu yangu kuwalipa na kuwatesa. Tutawanyoshea mambo yao kwa kuwapa mali, watoto na neema nyiginezo kwa njia ya kuwavutavuta kwa namna ya wao kutofahamu kuwa hiyo ndiyo njia ya kuwaangamiza

    [45] Na ninawapa muhula na kuurefusha umri wao, wapate kuendelea kufanya dhambi. Hakika vitimbi vyangu kwa watu makafiri ni vya nguvu na vikali

    [46] Au unaomba, ewe Mtume, hawa washirikina ujira wa kidunia kwa kuufikisha ujumbe, hivyo basi wao wakawa wamelazimishwa kubeba mzigo mzito wa gharama

    [47] Au wao wana ujuzi wa ghaibu, wakawa wanaandika kutokana nao kile wanachokiamulia nafsi zao kwamba wao wana cheo bora zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko wale wenye kumuamini

    [48] Basi vumilia, ewe Mtume, kwa kile Alichokiamua Mola wako na kukipitisha. Na miongoni mwa hivyo ni kuwapa muhula na kuchelewesha ushindi wako kwao. Na usiwe ni kama yule mtu wa chewa, naye ni Yūnus, amani imshukie, alipokasirika na kutokuwa na uvumilivu na watu wake, pindi alipomuita Mola Wake, na huku amejawa na makero, akimuomba Awaharakishie adhabu

    [49] lau si yeye kufikiwa na neema ya Mola Wake kwa kumwafikia kutubia, angalitupwa chini, kutoka tumboni mwa chewa, kwenye ardhi kavu yenye kuangamiza, na hali amefanya jambo la kulaumiwa

    [50] Mola Wake Akamchagua kwa ujumbe Wake, Akamjaalia ni miongoni mwa watu wema waliokuwa wazuri wa nia, matendo na maneno

    [51] Kwa hakika wanakaribia makafiri wanapoisikia Qur’ani kukudhuru kwa jicho la uhasidi kwa kukuchukia, lau si Mwenyezi Mungu kukuokoa na kukuhami, na wanasema kwa matamanio yao kwamba yeye ni Mwendawazimu

    [52] Na haikuwa Qur’ani isipokuwa ni mawaidha na ukumbusho kwa viumbe wote miongoni mwa binadamu na majini

    Haqqa

    Surah 69

    [1] Kiyama chenye kutukia kikweli ambacho ndani yake inahakikika ahadi ya Mwenyezi Mungu na onyo Lake

    [2] Kiyama chenye kutukia kikweli ni zipi sifa zake na hali zake

    [3] Na kitu gani kilichokujulisha wewe, ewe Mtume, na kukueleza uhakika wa Kiyama na kikakupa wewe picha ya janga lake na shida zake

    [4] Thamūd, nao ni watu wa Ṣāliḥ, na ‘Ād, nao ni watu wa Hūd, walikikanusha Kiyama ambacho kinagonga nyoyo kwa vituko janga lake

    [5] Ama hao Thamūd waliangamizwa kwa ukelele mkubwa uliopita kiasi ukali wake

    [6] na ama‘Ād waliangamizwa kwa upepo baridi unaovuma kwa nguvu

    [7] Mwenyezi Mungu Aliwasaliti nao masiku saba na michana minane yenye kufuatana, isiyokatika wala kusimama. Utawaona watu katika masiku hayo na michana wamekufa, kama kwamba wao ni vigogo mitende iliyo mibovu iliyolika ndani

    [8] Basi je utamuona mtu yoyote miongoni mwao mwenye kusalia bila kuangamia

    [9] Na akaja mpita kiasi katika uasi Fir’awn na ummah waliomtangulia waliokanusha Mitume wao, na watu wakazi wa vijiji vya watu wa Lūṭ ambao majumba yao yaliwapindukia kwa sababu ya kitendo kibaya walichokifanya, cha ukafiri, ushirikina na mambo machafu

    [10] Kila ummah kati yao walimuasi mjumbe wa Mola wao ambaye alitumwa kwao, basi Mwenyezi Mungu Akawashika mshiko mkali mno

    [11] Sisi, maji yalipopita kipimo chake, mpaka yakawa juu na kuangatika juu ya kila kitu, tuliwabeba watu wa asili zenu pamoja na Nūḥ ndani ya jahazi ambayo ilikuwa ndio sababu ya kuokoka Waumini na kuzamishwa makafiri

    [12] hili likiwa ni mazingatio na mawaidha, na lipate kulihifadhi tukio hilo kila shikio ambalo kazi yake ni kuhifadhi, na lielewe kile ambacho limekisikia

    [13] Pindi Malaika atakapopuliza kwenye barugumu mpulizo mmoja, nao ni mpulizo wa kwanza ambao hapo patapatikana maangamivu ya ulimwengu

    [14] Na pindi ardhi na milima itakapoinuliwa kutoka mahali ilipo ikavunjwavunjwa na kugongwagongwa mara moja

    [15] Wakati huo Kiyama kitasimama

    [16] Na mbingu zitafanya ufa na ziwe dhaifu na kulegea Siku hiyo, hazitakuwa na mshikamano wala ugumu

    [17] Na Malaika watakuwa kwenye pambizo na pande zake, na wataibeba «Arshi ya Mola wako juu yao Siku ya Kiyama Malaika wanane miongoni mwa Malaika wakubwa

    [18] Katika Siku hiyo, mtaorodheshwa kwa Mwenyezi Mungu, enyi wat, ili mhesabiwe na mlipwe, hakuna chochote kitakachofichamana kwa Mwenyewzi Mungu miongoni mwa siri zenu

    [19] Ama yule Atakayepewa kitabu cha matendo yake kwa mkono wake wa kulia, atasema akiwa katika hali ya ubashasha na furaha, ‘Chukueni kitabu changu mkisome

    [20] Mimi nilikuwa na yakini duniani kuwa nitapata malipo yangu Siku ya Kiyama, nikajiandalia nayo kwa matayarisho ya Imani na matendo mema.»

    [21] Basi yeye atakuwa kwenye maisha ya furaha ya kumridhisha

    [22] kwenye Pepo ya juu kimahali na daraja

    [23] matunda yake yako karibu, anayachuma anayesimama, anayeketi na anayelala

    [24] Wataambiwa, «Kuleni na mnyweni kila aina ya vyakula na vinywaji, mkiwa mbali na kila kero, mkiwa mmesalimika na kila mnalolichukia, kwa sababu ya matendo mema mliyoyatanguliza siku za ulimwenguni.»

    [25] Na ama yule atakayepewa kitabu cha matendo yake kwa mkono wake wa kushoto

    [26] atasema akiwa katika hali ya kujuta na kupata hasara

    [27] «Natamani lau mimi sikupewa kitabu changu na sikujua malipo yangu! Natamani lau kile kifo nilichokufa duniani kilikuwa ndicho chenye kukata kabisa mambo yangu na nisifufuliwe baada yake

    [28] Mali yangu niliyoyakusanya hayakuninufaisha duniani

    [29] Hoja zangu zote zimenionokea, na sina hoja tena ya kuitumia kama hoja.»

    [30] Hapo waambiwe walinzi wa Moto wa Jahanamu, «Mchukueni mhalifu huyu mfanya dhambi, ikusanyeni mikono yake shingoni mwake muitie pingu

    [31] kisha mtieni kwenye Moto unaowaka sana, apate kulihisi joto lake

    [32] Kisha mfungeni mnyororo wa chuma ambao urefu wake ni dhiraa sabini mumkokote nao na mumtie humo

    [33] Kwani yeye hakuwa akiamini kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Mola wa Haki, Peke Yake, Asiye na mshirika

    [34] Wala hakuwa akitenda matendo yanayoambatana na uongofu Wake, wala hakuwa akiwahimiza watu duniani kuwalisha wenye uhitaji miongoni mwa masikini na wengineo

    [35] basi kafiri huyu Siku ya Kiyama hatakuwa na jamaa wa karibu wa kumuepushia adhabu

    [36] wala hatakuwa na chakula isipokuwa kile kinachotokana na usaa wa watu wa motoni

    [37] hakuna mwenye kukila isipokuwa wale wenye dhambi, wanaoshikilia kumkanusha Mwenyezi mungu

    [38] Naapa kwa mnavyoviona miongoni mwa vitu vinavyooonekana

    [39] na vile msivyoviona miongoni mwa vile vilivyoghibu kwenu., hakika Qur’ani ni maneno ya Mwenyezi Mungu

    [40] Inasomwa na mjumbe mkubwa wa cheo na utukufu

    [41] Na si maneno ya mshairi kama mnavyodai, ni uchache mno mnavyoamini

    [42] Wala si tungo kama zile tungo za makuhani, ni kuchache mno kule kukumbuka kwenu na kutia akilini kuwa kuna tafauti baina ya mawili hayo

    [43] Lakini hiyo Qur’ani ni maneno ya Mola wa viumbe wote Aliyoyateremshia Mtume Wake Muhaammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [44] Na lau Muhammad angalitusingizia maneno tusiyoyanena

    [45] tungalimtesa na tungalimkamata kwa nguvu na uweza, kwani nguvu ya kila kitu iko kwenye upande wake wa kulia

    [46] kisha tungalimkata mshipa wa moyo wake

    [47] hataweza yoyote kuyazuia mateso yetu yasimpate

    [48] Na hii Qur’ani ni mawaidha kwa wachamungu wanaofuata amri za Mwenyezi Mungu na kuyaepuka makatazo yake

    [49] Na sisi kwa hakika tunajua kwamba miongoni mwenu kuna wanaoikanusha hii Qur’ani pamoja na kuwa dalili zake ziko wazi

    [50] Na kwa hakika kuikanusha Qur’ani ni majuto makubwa kwa wenye kuikanusha pindi watakapoiona adhabu yao na kuona starehe za wenye kuiamini

    [51] Na kwa hakika hii Qur’ani ni haki iliyothibiti na yakini isiyo na shaka

    [52] Basi Mwepushie Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, kila sifa isiyonasibiana na haiba Yake, na umtaje kwa jina Lake tukufu

    Daraja

    Surah 70

    [1] Ameapiza mwenye kuapiza miongoni mwa washirikina, kujiapiza mwenyewe na kuwaapiza watu wake kuteremkiwa na adhabu

    [2] nayo ni yenye kuwashukia bila shaka Siku ya Kiyama

    [3] Hakuna mzuiaji yoyote wa kuizuia isipokuwa Mwenyezi Mungu, Mwenye utukufu na haiba

    [4] Malaika na Jibrili wanapanda kuenda Kwake, Aliyetukuka, kwa siku moja ambayo kadiri yake ni myaka elfu hamsini katika myaka ya duniani, nayo kwa aliyeamini ni kama muda wa Swala moja ya faradhi

    [5] Basi vumilia, ewe Mtume, kule kufanya kwao shere na kutaka kwao wafikiwe na adhabu kwa haraka, uvumilivu usiokuwa na babaiko wala kumshtakia asiyekuwa Mwenyezi Mungu

    [6] Kwa kweli makafiri wanaiona adhabu kuwa iko mbali na wanaona kuwa si yenye kutukia

    [7] Na sisi tunaiona ni yenye kutukia kwa kipindi cha karibu bila shaka

    [8] Siku ambayo mbingu itayayuka iwe ni kama rojo la mafuta

    [9] na majabali yawe ni kama sufi iliyochanganywa na iliyoshanuliwa na kupeperushwa na upepo

    [10] Wala mtu hatamuuliza jamaa yake wa karibu kuhusu jambo lake, kwani kila mmoja ameshughulishwa na nafsi yake

    [11] Watawaona na watawajua, na hakuna yoyote atakayeweza kumnufaisha yoyote. Kafiri atatamani lau ajikomboa nafsi yake na adhabu ya Siku ya Kiyama kwa watoto wake

    [12] mkewe, nduguye

    [13] jamaa zake wanaomuhami na ambao anajinasibisha nao kwa ujamaa

    [14] na kwa wote walio kwenye ardhi miongoni mwa binadamu na wengineo ili aokoke na adhabu ya Mwenyezi Mungu

    [15] Mambo siyo kama vile unavyotamani yawe, ewe kafiri, ya kujikomboa

    [16] Huo ni moto wa Jahanamu, moto wake unawaka na kuroroma, joto lake linatoa kwa nguvu ngozi ya kichwa na sehemu nyingine za mwili

    [17] unamwita aliyeipa mgongo haki duniani na akaacha kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake

    [18] na akakusanya mali na kuyaweka kwenye mahazina yake na asitekeleze amri ya Mwenyezi Mungu kwenye mali hayo

    [19] Hakika binadamu ameumbwa akiwa na tabia ya babaiko na pupa

    [20] Yakimpata makero na shida, anababaika sana na kufa moyo

    [21] Na yakimpata mambo mazuri na ukunjufu wa maisha, huwa ni mwingi wa kuzuia na

    [22] Isipokuwa wenye kusimamisha Swala

    [23] wanaochunga kuitekeleza katika nyakati zake zote, hakuna shughuli yoyote inayowashughulisha nayo

    [24] Na wale ambao katika mali yao kuna fungu maalumu alililowafaradhia Mwenyezi Mungu, nalo ni Zaka

    [25] wanaozitoa kwa anayeomba msaada na kwa na kwa asiyeomba

    [26] Na wale ambao wanaiamini Siku ya kuhesabiwa na kulipwa wakajiandaa nayo kwa matendo mema

    [27] Na wale ambao wao wanaiogopa adhabu ya Mwenyezi Mungu

    [28] kwani adhabu ya Mola wao haipaswi kwa yoyote kujiaminisha nayo

    [29] Na wale ambao wao ni wenye kutunza tupu zao na kila alichokiharamishia Mwenyezi Mungu

    [30] isipokuwa wake zao na vijakazi vyao, hakika wao kwa hao hawapatilizwi

    [31] Basi mwenye kutaka kumaliza matamanio yake ya kimwili kwa wasiokuwa wake zake au vijakazi vyake, basi hao ndio wenye kukiuka mipaka ya halali kuingia kwenye haramu

    [32] Na wale ambao wanazitunza amana za Mwenyezi Mungu na amana za waja, na wanatunza ahadi zao pamoja na Mwenyezi Munmgu, Aliyetukuka, na pamoja na waja

    [33] Na wale ambao wanatekeleza ushahidi wao kwa ukweli bila kubadilisha au kuficha

    [34] Na wale ambao wanatunza utekelezaji Swala wala hawaharibu chochote cha wajibu katika hiyo Swala

    [35] Hao waliosifika kwa sifa hizo njema, ni wenye kutulia kwenye mabustani ya Pepo ya starehe, ni wenye kukirimiwa humo kwa kila aina ya takrima

    [36] Ni msukumo gani unaowasukuma makafiri watembee kwa haraka kuelekea upande wako, ewe Mtume, na huku wamenyosha shingo zao kwako, wamekukabili kwa macho yao

    [37] wanajikusanya kuliani kwako na kushotoni kwako, wakiwa wamekaa kwa kupiga maduara na wamejigawa vikundi mbalimbali, wanazungumza na kuona ajabu

    [38] Je ana tamaa kila mmoja miongoni mwa makafiri kuwa Mwenyezi Mungui Atamuingiza kwenye Pepo ya starehe ya daima? Mambo siyo kama vile wanavyotazamia. Wao hawataiingia hiyo Pepo kabisa

    [39] Hakika sisi tumewaumba kwa kile wanachokijua cha maji matwevu kama wengineo, na vilevile hawakuamini. Basi vipi watapata heshima ya kuingia Pepo ya sterehe

    [40] Sivyo hivyo. Najiapia Mimi Mwenyewe niliye Mola wa pande za kuchomoza na kutua jua, mwezi na sayari nyinginezo, kwa yanayopatikana humo miongoni mwa dalili waziwazi za kujulisha kufufuliwa

    [41] kuwa Sisi tunaweza kuwaleta watu badala yao walio bora zaidi kuliko wao na watiifu zaidi wa Mwenyezi Mungu. Na hakuna yoyote atakayetushinda na kutuponyoka na kutuelemea iwapo tunataka kumrudisha uhai baada ya kufa

    [42] Basi waache wavame kwenye ubatilifu wao na wacheze kwenye ulimwengu wao mpaka wakutane na Siku ya Kiyama ambayo wanaahidiwa kuwa wataadhibiwa

    [43] Siku watakapotoka makaburini wakienda kwa haraka, kama wlivyokuwa duniani wakienda mbio na haraka kwa waungu wao wakiwaabudu badala ya Mwenyezi Mungu

    [44] hali ya kuwa macho yao ni madhalilifu yanatazama chini, wamefinikwa na unyonge na utwevu. Hiyo ndiyo Siku waliyoahidiwa duniani na walikuwa wakiifanyia shere na kuikanusha

    Nuhu

    Surah 71

    [1] Kwa hakika sisi tulimpeleka Nūḥ kwa watu wake na tukamwambia, «Waonye watu wako kabla ya kufikiwa na adhabu yenye kuumiza.»

    [2] Nūḥ akasema, «Enyi watu wangu! Mimi kwenu nyinyi ni mwonyaji waziwazi, anayewaonya nyinyi adhabu ya Mwenyezi Mungu iwapo mtamuasi

    [3] Na mimi ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu kwenu. Muabuduni Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Peke Yake na muogopeni Yeye na nitiini mimi katika kile ninachowaamrisha nyinyi na kuwakataza. Basi mkinitii mimi na mkanikubalia

    [4] Mwenyezi Mungu Atawasamehe dhambi zenu na kuwafinikia, atawarefushia umri wenu mpaka kipindi kilichokadiriwa katika ujuzi wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka. Kwani kifo kikija hakicheleweshwi kabisa. Lau mngalijua hilo mngalifanya haraka kuamini na kutii.»

    [5] Nūḥ akasema, «Mola wangu! Kwa hakika mimi nimewalingania watu wangu usiku na mchana ili wakuamini wewe na wakutii

    [6] Ulinganizi wangu kwao ili waamini, haukuwaongezea kitu isipokuwa ni kukimbia na kuipa mgongo haki

    [7] Na mimi kila nikiwalingania wao ili wakuamini wewe, ipate kuwa hiyo ni njia ya wewe kuwasamehe dhambi zao, hutia vidole vyao masikioni mwao, ili wasisikie ulinganizi wa haki, na hujifinika nguo zao wasipate kuniona, na hujikita kwenye ukafiri wao na hufanya kiburi sana cha kutoikubali haki

    [8] Kisha mimi ni kawalingania wao kwenye Imani waziwazi na sio kwa kujificha

    [9] Kisha nikawatangazia wao ulinganizi kwa sauti kubwa wakati mwingine, na nikausirisha huo ulinganizi kwa sauti ya chini wakati mwingine

    [10] Ni kawaambia watu wangu, ‘Muombeni Mola wenu msamaha wa dhambi zenu na tubieni Kwake kutokana na ukafiri wenu, hakika Yeye ni Mwingi wa kusamehe kwa anayetubia miongoni mwa waja Wake na akurudia Kwake.’»

    [11] Mtakapotubia na mkaomba msamaha, Mwenyezi Mungu Atawateremshia mvua nyingi ya mfululizo

    [12] Atayaongeza mali yenu na pia watototo wenu, Atawafanya muwe na mabustani ya nyinyi kuneemeka kwa matunda yake na uzuri wake, na Atawajaalia nyinyi muwe na mito ambayo mtaitumia kwa kuipatia maji mimea yenu na pia wanyama wenu

    [13] Mnani nyinyi, enyi watu, hamuogopi ukuu wa Mwenyezi Mungu na uweza Wake

    [14] na hali yeye Amewaumba nyinyi katika miongo yenye kufuatana : tone la manii, kisha pande la damu, kisha nofu la nyama, kisha mifupa na nyama

    [15] Kwani hamtazami namna alivyoumba Mwenyezi Mungu mbingu saba zilizopandana, kila uwingu juu ya mwingine

    [16] Akajaalia mwezi, katika mbigu hizi, ni wenye mwangaza,, na Akajaalia jua ni taa yenye kung’ara ili kuwapatia mwangaza watu walioko ardhini

    [17] Mwenyezi Mungu aliumba asili yenu kutokana na ardhi

    [18] kisha Atawarudisha humo ardhini baada ya kufa, na Awatoe Siku ya kufufuliwa kuwatoa kihakika

    [19] Na Mwenyezi Mungu Amewafanyia hii ardhi ni tandiko kama mkeka

    [20] Ili mfuate humo njia zilizo kunjufu

    [21] Nūḥ alisema, «Mola wangu! Kwa hakika watu wangu wameendelea sana kuniasi na kunikanusha, na wanyonge miongoni mwao wakawafuata viongozi wapotevu ambao mali yao na watoto wao havikuwaongezea isipokuwa upotevu wa duniani na mateso ya Akhera

    [22] Na hao viongozi wa upotevu wakawafanyia wafuasi wao wanyonge vitimbi vikubwa

    [23] na wakawaambia, ‘Msiache kuwaabudu waungu wenu mkaelekea kwenye kumubadu Mwenyezi Mungu Peke Yake, ambaye Nūḥ anawalingania nyinyi mumuabudu, na msimuache Wadd, Suwā‘, Yghūth, Ya’ūq wala Nasr.» Na haya ni majina ya masanamu wao ambao walikuwa wakiyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, na yalikuwa ni majina ya watu wema. Walipokufa, Shetani alitia kwenye mawazo ya watu wao wawasimamishie masanamu na picha ili wapate moyo, kama wanavyodai, wa kuwa watiifu wanapoyaona. Walipoondoka hao waliosimamisha masanamu na muda mrefu ukapita, wakaja watu wasiokuwa wao, Shetani aliwatia tashwishi kwamba wakale wao waliopita walikuwa wakiyaabudu haya masanamu na picha na kutawasali nayo. Hii ndio hekima ya kuharamishwa masanamu na kuharamishwa ujengaji wa makuba juu ya makaburi. Kwa kuwa hayo kwa kupitiwa na muda yanakuwa ni yenye kuabudiwa na wajinga

    [24] Na hawa wafuatwa wamewapoteza watu wengi kwa vile walivyowapambia njia za upotofu upotevu. Kisha Nūḥ akaendelea kusema, «Na usiwaongezee, ewe Mola wetu, hawa waliozidhulumu nafsi zao kwa ukanushaji na ushindani isipokuwa kuwaepusha na haki.»

    [25] Kwa sababu ya dhambi zao na ukakamavu wao juu ya ukafiri na uasi, walizamishwa kwa mafuriko na wakaingizwa baada ya kuzamishwa kwenye Moto unaowakia sana na kuchoma, na wasimpate, badala ya Mwenyezi Mungu, mwenye kuwaokoa au kuwaepushia adhabu ya Mwenyezi Mungu

    [26] Na akasema Nūḥ, amani imshukie, baada ya kukata tama na watu wake, «Mola wangu! Usimuache yoyote miongoni mwa wale wanaokukanusha kuwa ni mwenye kuishi juu ardhi akizunguka na kutembea

    [27] Hao ukiwaacha, bila kuwaangamiza, watawapoteza waja wako waliokuamini na kuwapotosha njia ya haki, na haji yoyote kutokana na migongo yao na vizazi vyao isipokuwa yule aliyepotoka na njia ya haki na kukukanusha wewe sana na kukuasi

    [28] Mola wangu! Nisamehe mimi, wazazi wangu wawili, mwenye kuingia nyumbani kwangu na hali yeye ameamini, wanaume na wanawake waliokuamini wewe, na usiwaongezee makafiri isipokuwa maangamivu na hasara, duniani na Akhera.»

    Majini

    Surah 72

    [1] Sema, ewe Mtume, «Mwenyezi Mungu Ameniletea wahyi kwamba kundi la majini walisikiliza kisomo changu cha Qur’ani, na baada ya kusikia walisema kuwaambia watu wao, «Sisi tumeisikia Qur’ani iliyopambika katika uzuri wa maneno yake, ufasaha wake, hekima zake, hukumuzake na habari inazozielezea

    [2] inalingania watu kwenye ukweli na uongofu, na sisi tukaiamini na kuifuata kivitendo, na hatutomshirikisha Mola wetu Aliyetuumba na yoyote katika kumuabudu

    [3] «Na kwamba Yeye Ambaye utukufu Wake uko juu na haiba Yake, Hakumfanya yoyote kuwa mke au mtoto

    [4] «Na kwamba fidhuli wet, Iblisi, alikuwa akisema kumsingizia Mwenyezi Mungu aliyetukuka neno lililo mbali na ukweli na usawa, la kudai kuwa Yeye ana mke au mtoto

    [5] «Na kwamba sisi tulidhani kuwa hakuna yoyote atakayemzulia Mwenyezi Mungu Aliyetukuka urongo, si katika binadamu na si katika majini, wa kumnasibishia Yeye mke na mtoto

    [6] «Na kwamba wanaume miongoni mwa binadamu walikuwa wakijilinda na wanaume miongoni mwa majini, na hawa wanaume wa kijini wakawazidi binadamu kwa kuwa binadamu wanajilinda nao kwa hofu, kicho na kutishika.» Kujilinda huku na asiyekuwa Mwenyezi Mungu, ambako Mwenyezi Munghu Aliwatangazia watu wa zama za watu wa ujinga, ni katika ushirikina mkubwa ambao Mwenyezi Mungu hausamehe isipokuwa kwa kutubia kidhati kutokana nao. Katika aya hii pana onyo kali juu ya kitendo cha kuwaewndea wachawi, makuhani na mfano wao

    [7] «Na kwamba makafiri wa kibinadamu walidhania kama mlivyodhania, enyi majini, kuwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka hatamfufua yoyote baada ya kufa

    [8] «Na kwamba sisi, mkusanyiko wa majini, tulitaka kufika mbinguni,kusikiliza maneno ya watu wake, tukaipata imejazwa Malaika wengi wenye kuilinda na vimondo vya moto ambavyo wanarushiwa wenye kuikaribia

    [9] «Na sisi tulikuwa kabla ya hapo tunakalia sehemu fulani za mbingu ili kusikiliza habari zake. Basi mwenye kujaribu sasa kusikiliza kwa kuiba atapata kimondo cha moto chenye kumngojea kimchome na kimuangamize.» Na katika aya mbili hizi pana kubatilisha madai ya wachawi na makuhani wanaodai kuwa wanajua ghaibu na kuwadanganya wachache wa akili kwa urongo wao na uzushi wao

    [10] «Na kwamba sisi, mkusanyiko wa majini, hatujui: ni mabaya ambayo Mwenyezi Mungu Anataka kuwateremshia watu wa ardhini au Anawatakia mazuri na uongofu

    [11] «Na kwamba sisi, miongoni mwetu kuna wema wachamungu na miongoni mwetu kuna watu ambao wako chini ya hapo: wao ni makafiri na wenye kuasi. Sisi tuko mapote na mila tofauti

    [12] «Na kwamba sisi tuna yakini kuwa mwenyezi Mungu Ana uweza juu yetu, na sisi tuko kwenye mkamato Wake na mamlaka Yake; hatuwezi kumponyoka Anapotaka kutufanya jambo popote pale tulipo. Na hatutaweza kuyahepa mateso Yake kwa kukimbila kwenda mbinguni iwapo Anatutakia mabaya

    [13] «Na sisi tulipoisikia Qur’ani tuliiamini na tukakubali kuwa ni ukweli unaotoka kwa Mwenyezi Mungu. Basi mwenye kumuamini Mola wake, kwa hakika yeye hataogopa kupunguziwa mema yake wala kudhulumiwa kwa kuongezewa makosa yake

    [14] «Na kwamba miongoni mwetu kuna wenye kumnyenyekea Mwenyezi Mungu kwa kumtii, na miongoni mwetu kuna waliopotoka walio madhalimu ambao walienda kombo na njia ya haki. Basi mwenye kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu na kumnyenyekea kwa utiifu, hao ndio walioelekea njia ya haki na usawa, wakajibidiisha kuichagua na Mwenyezi Mungu Akawaongoza kuifikia

    [15] Ama wale waliopotoka na njia ya Uislamu, watakuwa ni kuni za Moto wa Jahanamu.»

    [16] Na lau makafiri wa kibinadamu na kijini wangalifuata njia ya Uislamu na wasijiepushe nayo, tungaliwateremshia maji mengi na tungaliwakunjulia riziki duniani

    [17] ili tuwafanyie mtihani: vipi watazishukuru neema za Mwenyezi Mungu juu yao? Na yoyote mwenye kupa mgongo utiifu wa Mwenyezi Mungu na kusikiliza Qur’ani na kuizingatia na kuifuata kivitendo, Mwenyezi Mungu Atamuingiza kwenye adhabu kali iliyo ngumu

    [18] Na kwa hakika misikiti ni ya kuabudiwa Mwenyezi Mungu Peke Yake, basi msiabudu humo asiyekuwa Yeye. Na mtakasieni maombi na ibada humo, kwani misikiti haikujengwa isipokuwa kwa ajili Mwenyezi Mungu Aabudiwe humo Peke Yake, na sio mwingine asiyekuwa Yeye. Katika haya kuna ulazima wa kuiepusha misikiti na kila kinachokoroga utakasaji wa Mwenyezi Mungu na ufuataji Mtume Wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [19] Na kwa hakika Aliposimama Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kumuabudu Mola wake, walikaribia majini kumwangukia wakiwa makundi yaliyojikusanya na kupandana kwa kusongamana sana ili wapate kuisikia Qur’ani kutoka kwake

    [20] Waambie, ewe Mtume, hawa makafiri, «Kwa hakika mimi ninamuabudu Mola wangu Peke Yake, wala simshirikishi na Yeye kitu chochote katika kuabudu

    [21] Sema, ewe Mtume, uwaambie hawa makafiri, «Mimi siwezi kuwaondolea shida yoyote wala kuwaletea manufaa yoyote.»

    [22] Sema, «Hakika mimi sina yoyote wa kuniokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu iwapo nitamuasi, na sitapata asiyekuwa Yeye mahali pa kukimbilia niepukane na adhabu Yake

    [23] Ninachokiweza mimi na kukimiliki ni kuwafikishia kutoka kwa Mwenyezi Mungu kile Alichoniamrisha niwafikishie na ujumbe Wake ambao Alinituma niwaletee. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na akaipa mgongo Dini ya Mwenyezi Mungu, basi malipo yake ni moto wa Jahanamu ambao hatatoka humo milele

    [24] Mpaka watakapoishuhudia washirikina adhabu anayoahidiwa, hapo watajua itakapowashukia wao: ni nani ambaye mtetezi wake na msaidizi ni mnyonge zaidi na ambaye askari wake ni wachache zaid

    [25] Waambie hawa washirikina, ewe Mtume, Mimi sijui: Je adhabu hii mliyoahidiwa zishakaribia zama zake au Mola wangu ataufanya muda wake wa kuja uwe mrefu

    [26] Na Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, ni mjuzi wa kisichoonekana na macho. Hatakitoa wazi hiko kisichoonekana kwa yoyote miongoni mwa viumbe Wake

    [27] Isipokuwa kwa yule Aliyemchagua Mwenyezi Mungu na kumpendelea kwa kumpa utume, kwani Yeye huwajuza baadhi ya yale yaliyofichika yasionekane. Na Anatuma, mbele ya huyo Mtume na nyuma yake, Malaika wenye kumhifadhi na majini, ili wasiisikilize kwa kuiba jambo hilo la ghaibu, kisha wakaambiana kwa siri kisha wakawadokeza makuhani

    [28] Ili Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ajue kwamba Mitume kabla yake walikuwa kwenye hali kama yake ya ufikishaji haki na ukweli, na kwamba yeye atalindwa kutokana na majini kama walivyolindwa wao, na kwamba Mwenyezi Mungu, ujuzi Wake umeyazunguka mambo yao waliyonayo ya nje na ya ndani, miongoni mwa sheria na hukumu na mengineyo, hakuna chochote kinachompita katika hayo, na kwamba Yeye Amekidhibiti kila kitu kwa hesabu, hakuna chochote kinachofichamana Kwake

    Aliyejifunika

    Surah 73

    [1] Ewe ulijifinika nguo zako

    [2] Inuka uswali kipindi cha usiku isipokuwa sehemu chache yake

    [3] Inuka kwa muda wa nusu ya usiku au kupungua nusu kidogo mpaka ufikie theluthi

    [4] Au ongeza zaidi ya nusu mpaka ufikie theluthi mbili. Na usome Qur’ani kwa utaratibu na utulivu, uzifafanue herufi na vikomo

    [5] Hakika sisi tutakuteremshia, ewe Nabii, Qur’ani tukufu inayokusanya maamrisho na makatazo na hukumu za kisheria

    [6] Hakika ibada inayo inayofanya ndani ya usiku ina athari kubwa zaid moyoni, na maneno yanabainika zaidi, kwa kuwa moyo uko mtupu hauna mashughuli ya kilimwengu

    [7] Hakika wewe katika kipindi cha mchana una wakati wa kuzunguka na kushughulika katika mambo yenye maslahi nawe na kufanya harakati nyingi kwa majukumu ya utume, basi wakati wa usiku ipe nafasi nafsi yako kumuabudu Mola wako

    [8] Na ulitaje, ewe Nabii, jina la Mola wako, umuombe kwalo na utindikie Kwake kikamilifu katika ibada yako na ujitegemeze Kwake

    [9] Yeye Ndiye Mmiliki wa Mashariki na Magharibi. Hakuna muabudiwa ka haki isipokuwa Yeye. Basi mtegemee Yeye na umuachie Yeye mambo yako

    [10] Na uvumilie kwa yale ambayo washirikina wanayasema kuhusu wewe na kuhusu Dini yako. Na uende kinyume na wao katika maneno yao ya ubatilifu pamoja na kuwapuuza na kuacha kuwalipiza

    [11] Na uniache mimi, ewe Mtume, na hawa wakanushaji wa aya zangu, wenye starehe na gogi la ulimwengu, na uwape muhula wa muda mchache kwa kucheleweshewa adhabu mpaka muda wa wao kuadhibiwa ufikie ukomo wake

    [12] Kwa hakika wao watapata kwetu sisi huko Akhera pingu nzito na Moto wenye kuwaka ambao watachomwa nao

    [13] na chakula cha kuchukiza chenye kusakama kooni kisicho na ladha, na adhabu inayoumiza

    [14] Siku itakapotikisika na kusukikasukika ardhi na majabali mpaka majabali yawe mlima wa mchanga wenye kutiririka na kupeperuka, baada ya kuwa kwenye hali ya ugumu na ukavu

    [15] Hakika sisi tumemtumiliza kwenu nyinyi, watu wa Makkah, Muhammad kuwa ni Mtume, mwenye kutoa ushahidi wa ukafiri na uasi unaotokana na nyinyi, kama vile tulivyomtumiliza Mūsā kuwa ni Mtume kwenda kwa Fir’awn aliyepita kiasi katika uasi

    [16] Basi Fir’awn akamkanusha Mūsā na asiukubali utume wake, na akakataa amri yake, tukamuangamiza maangamivu makali. Hapa pana onyo la kumuasi Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa kuogopea isije ikamfika yule aliyeasi mfano wa kile kilichomfika Fir‘awn na watu wake

    [17] Vipi mtajikinga nafsi zenu, mkikufuru, na adhabu ya Siku ya Kiyama ambayo huwafanya watoto wadogo watokwe na mvi kwa ukubwa wa janga lake na unguliko lake

    [18] Mbingu zitakuwa na pasuko Siku hiyo, kwa ukubwa wa janga lake, hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ya kuwa Siku hiyo itakuja ni yenye kutukia bila shaka

    [19] Hakika aya hizi zenye kutisha ambazo ndani yake kuna vigongaji na vikemeaji ni mawaidha na mazingatio kwa watu. Basi mwenye kutaka kuwaidhika na kunufaika nazo, na achukue utiifu na uchamungu kuwa ni njia ya kumfikisha kwenye radhi za Mola wake Aliyemuumba na kumlea

    [20] Hakika Mola wako, ewe Mtume, Anajua kuwa wewe unasimama kwa swala ya Tahajudi kipindi cha usiku, wakati mwingine chini ya theluthi mbili za usiku, na wakati mwingine unasimama nusu yake, na wakati mwingine theluthi yake. Na wanasimama pamoja na wewe kundi la Maswahaba wako. Na Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Ndiye Anayekadiria usiku na mchana na Anajua vipimo vyake na kipindi kinachopita na kusalia cha mchana na usiku. Mwenyezi Mungu Anajua kwamba haiwezekani kwenu nyinyi kusimama usiku wote, hivyo basi akawafanyia mambo kuwa mepesi kwenu. Na msome kwenye Swala ya usiku kile kilichokuwa chepesi kwenu kukisoma katika Qur’ani. Mwenyezi Mungu anajua kuwa miongoni mwenu kuna wanaoelemewa na ugonjwa wasiweze kusimama usiku. Na kuna watu wengine wanatembea ardhini kwa biashara na kazi wakitafuata riziki ya Mwenyezi Mungu ya halali. Na kuna watu wengine wanapigana jihadi katika njia ya Mwenye kuliinua neno Lake na kutangaza dini Yake. Basi someni kutoka kwenye Qur’ani kile kilicho chepesi kwenu, na endeleeni kutekeleza faradhi za Swala, na toeni Zaka za lazima kwenu, na toeni sadaka za mali yenu katika njia za wema na hisani kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu. Na chochote kile mnachokifanya miongoni mwa njia za wema na kheri na matendo ya utiifu, mtapata malipo yake na thawabu zake kwa Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama, hali ya kuwa ni bora zaidi kuliko kile mlichokitanguliza duniani na ni chenye thawabu kubwa zaidi. Na mtake msamaha wa Mwenyezi Mungu katika hali zenu zote. Hakika Mwenyezi Mumngu ni Msamehefu sana kwenu ni Mwenye huruma na nyinyi

    Aliyejivika Nguo

    Surah 74

    [1] Ewe uliojifinika nguo zako

    [2] Inuka kutoka kwenye malazi yako owaonye watu adhabu ya Menyezi Mungu

    [3] Na umkusudie Mola wako, Peke Yake, kwa kumtukuza, kumpwekesha na kumuabudu

    [4] Na usafishe nguo zako kutokana na najisi, kwani usafi wa nje ni katika kutimia usafi wa ndani

    [5] Na uendelee daima kuyaepuka masanamu na mizimu, na matendo ya ushirikina yote usiyakaribie

    [6] Na usitoe kitu kumpa mtu kwa lengo la kupata zaidi ya hiko. Na kwa ajili ya kupata radhi ya Mwenyezi Mungu

    [7] vumilia juu ya maamrisho na makatazo

    [8] Pindi patakapopulizwa kwenye barugumu mpulizo wa Ufufuzi na Uenezaji

    [9] wakati huo ni wakati ambao ni mgumu kwa makafiri

    [10] si rahisi kwao kusalimika na yale walionayo ya kujadiliwa hesabu zao na vituko vingine vikubwa

    [11] Niache mimi, ewe Mtume, na huyu niliyemuumba ndani ya tumbo la mamake akiwa peke yake, hana mali wala watoto

    [12] Nikamfanya awe na mali mengi yenye kuenea na watoto waliyoko na yeye hapo Makkah hawamuondokei. Na

    [13] nikamsahilishia kwa kumrahisishia njia za maisha. Kisha yeye anatarajia, baada ya vitu hivi alivyopewa

    [14] nimuongezee kwenye mali yake na watoto wake na huku yeye amenikanusha. Mambo sivyo kama anavyodai huyu mwenye kuasi, mtenda dhambi

    [15] Simuongezei zaidi ya hiko nilichompa

    [16] kwa kuwa yeye alikuwa mshindani mkanushaji wa Qur’ani na hoja za Mwenyezi Mungu kwa viumbe Wake

    [17] Nitambebesha mateso magumu na usumbufu usio na mapumziko. Anayekusudiwa hapa ni Al-Walid mwana wa Al-Mughi rah aliyekuwa akishindana na haki na akijitokeza kupigana vita na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Haya ndiyo malipo ya kila mwenye kushindana na haki na kuipiga vita

    [18] Kwa kweli yeye aliwaza ndani ya nafsi yake akatayarisha la kusema kumtukana Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na Qur’ani

    [19] Hivyo basi akalaaniwa na akastahili, kwa hilo, maangamivu: alijiandaa vipi ndani ya nafsi yake kwa hayo matukano

    [20] Kisha pia akalaaniwa

    [21] Kisha yeye alifikiria kuhusu kile alichokipanga na kukitayarisha cha kuitia dosari Qur’ani

    [22] Kisha akafinya uso wake na akazidi katika hali ile ya ukunjaji uso kwa kukosa hila za kufanya na kutopata ila yoyote ya kuitia dosari Qur’ani

    [23] Kisha akarudi kuipa mgongo haki na akajiona ni mkubwa wa kutofaa kuikubali

    [24] hapo akasema kuhusu Qur’ani, «Haya anayoyasema Muhammad si chochote isipokuwa ni uchawi uliopokewa kutoka kwa watu wa mwanzo waliopita

    [25] Haikuwa hi Qur’ani isipokuwa ni maneno ya viumbe ambayo Muhammad amejifunza kutoka kwao kisha akadai kuwa yanatoka kwa Mwenyezi Mungu.»

    [26] Basi nitamuingiza kwenye moto wa Jahanamu ili alionje joto lake na achomeke kwa moto wake

    [27] Na ni lipi lililokujulisha wewe ni kitu gani hiyo Jahanamu

    [28] Haibakishi nyama wala haiachi mfupa isipokuwa huvichoma

    [29] Unageuza ngozi ya mwili, unazifanya ngozi kuwa nyeusi na unazichoma

    [30] Wanasimamia mambo yake na kushikilia kazi ya kuwatesa watu wake Malaika kumi na tisa katika washika zamu wa Motoni wenye nguvu

    [31] Na hatukuwafanya washika hazina wa Motoni isipokuwa miongoni mwa Malaika washupavu. Na hatukuiweka idadi hiyo isipokuwa kuwatahini wale waliomkufuru Mwenyezi Mungu, na ili imani ya yakini ipatikane kwa wale Mayahudi na Wanaswara waliopewa Vitabu kwamba yaliyokuja ndani ya Qur’ani juu ya washika hazina wa Motoni ni ukweli utokao kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, kwani hayo yanaafikiana na vitabu vyao, na ili Waumini wazidi kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na waifuate Sheria Yake kivitendo, na ili wasilifanyie shaka hilo wale Mayahudi na Wanaswara waliopewa Vitabu wala wale wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na ili wapate kusema wale wenye unafiki ndani ya nyoyo zao na makafiri, «Ni lipi alilolikusudia Mwenyezi Mungu kwa idadi hii ya ajabu?» Kwa mfano wa hayo yaliyotajwa, Mwenyezi Mungu Anampoteza Anayetaka kumpoteza na Anamuongoza Anayetaka kumuongoza. Na hakuna ajuwaye idadi ya askari wa Mola wako, na miongoni mwao ni Malaika, isipokuwa Mwenyezi Mungu Peke Yake. Na haukuwa huu Moto isipokuwa ni ukumbusho na mazingatio kwa watu

    [32] Mambo sivyo kama walivyotaja ya ukanushaji Mtume katika yale aliyokuja nayo! Anaapa Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu, kwa mwezi

    [33] na kwa usiku unapogeuka kwenda zake

    [34] na kwa asubuhi inapotoa mwangaza na kufunuka

    [35] hakika Moto ni mojawapo ya mambo makubwa

    [36] kwa ajili ya kuwaonya na kuwatisha watu

    [37] kwa anayetaka miongoni mwenu kujiweka karibu na Mola wake kwa kufanya matendo ya utiifu, au kujikalisha nyuma kwa kufanya matendo ya uasi

    [38] Kila nafsi imefungwa na kuwekwa rahani kwa ilichokitenda, miongoni mwa matendo mema au mabaya, kwa kukichuma. Haifunguliwi mpaka itekeleze haki zilizo juu ya lazima yake na ipatiwe mateso yanayostahili kupatiwa

    [39] Isipokuwa Waislamu waliotakaswa, watu wa upande wa kulia waliojikomboa shingo zao kwa utiifu

    [40] Wao watakuwa kwenye mabustani ya Peponi ambayo sifa zake hazifikiwi ukomo. Watakuwa wakiulizana wao kwa wao

    [41] kuhusu makafiri waliojikosea nafsi zao

    [42] «Ni lipi lililowaingiza kwenye moto wa Jahanamu na likawafanya

    [43] mlionje joto lake lililo kali sana?» Wahalifu waseme , «Hatukuwa ni miongoni mwa wanaoswali duniani

    [44] na hatukuwa tukitoa sadaka na kuwafanyia wema wahitaji na maskini

    [45] na tulikuwa tukizungumza maneno ya ubatilifu na watu wa upotofu na upotevu

    [46] na tulikuwa tukiikanusha Siku ya kuhesabiwa na kulipwa

    [47] mpaka kifo kikatujia na hali sisi tuko kwenye mambo hayo mabaya ya upotevu

    [48] Basi hayatawafalia neno maombezi ya wenye kuombea wote, miongoni mwa Malaika, Manabii na wengineo, kwa kuwa aombewaye ni yule aliyechaguliwa na Mwenyezi Mungu na akamuidhinisha mwenye kumuombea

    [49] Basi wana nini hawa washirikina wamejiepusha na Qur’ani na

    [50] mawaidha yaliyomo ndani yake? Kama kwamba wao ni pundamilia wanaobabaika

    [51] wanaomkimbia simba mshambulizi

    [52] Lakini kila mmoja, miongoni mwa hawa washirikina, ana matumaini ateremshiwe kitabu kutoka mbinguni kilichokunjuliwa kama kile kilichoteremshiwa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [53] Mambo si hivyo kama wanavyodai. Ukweli ni kwamba wao hawaiogopi Akhera wala hawaamini kuwa kuna kufufuliwa na kulipwa

    [54] Ni kweli kwamba Qur’ani ni mawaidha yenye ufasaha, yanayotosha kuwafanya wao wawaidhike

    [55] Anayetaka kuwaidhika, basi na awaidhike kwa yaliyomo ndani yake na anufaike na uongofu wake

    [56] Na hawawaidhiki kwayo isipokuwa iwapo Mwenyezi Mungu Amewatakia kuongoka. Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Anayestahiki kuogopewa na kutiiwa, na Ndiye Anayestahiki kumsamehe anayemuamini Yeye na kumtii

    Kiyama

    Surah 75

    [1] Anaapa Mwenyezi Mungu kwa Siku ya Hesabu na Malipo

    [2] na Anaapa kwa nafsi yenye kuamini na kuchamungu, inayomlaumu mwenyewe kwa kuacha matendo ya utiifu na kufanya matendo yenye kuangamiza, kwamba watu watafufuliwa

    [3] Je anadhanihuyu binadamu kafiri kuwa sisi hatutaweza kuikusanya mifupa yake baada ya kuwa mbalimbali

    [4] Ndio! Tutaikusanya na tunaweza kufanya vidole vyake au ncha za vidole vyake- baada ya kuvikusanya na kuzioanisha- viwe kwenye umbo la sawasawa, kama vilivyokuwa kabla ya kufa

    [5] Bali binadamu anakanusha kufufuliwa, anataka asalie kwenye kufanya ubaya kwa siku za mbeleni za maisha yake

    [6] Kafiri huyu huwa akiuliza, akiliona jambo la kusimama Kiyama kuwa liko mbali, «Ni lini Siku ya Kiyama?’

    [7] Basi macho yatakapoduwaa na yakashituka kwa kutishika na kile yalichokiona cha vituko vya Siku ya Kiyama

    [8] na ukafutika mwangaza wa mwezi

    [9] na vikakusanywa jua na mwezi katika kukosa mwangaza, kikawa kila mojawapo ya hivyo viwili hakina mwangaza

    [10] wakati huo binadamu atasema, «Pa kukimbilia ni wapi kuiepuka adhabu?»

    [11] Mambo sivyo kama unavyotamani yawe, ewe binadamu, ya kutaka kukimbia. Huna mahali pa kukimbilia wala pa kupata uokozinfsi yake

    [12] Kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake ndio mwisho wa viumbe Siku ya Kiyama na ndipo mahali pao pa kutulia, na hapo Amlipe kila mtu kwa kile alichostahiki

    [13] Atapashwa habari binadamu Siku hiyo kwa matendo yake yote, mema na mabaya, aliyoyatanguliza miongoni mwa hayo katika maisha yake na aliyoyachelewesha

    [14] Bali binadamu ni hoja iliyo wazi juu ya nafsi yake, yenye kumfuata kwa alichokitenda na alichokiacha

    [15] hata kama atakuja na kila udhuru wa kuelezea sababu ya uhalifu wake, hilo halitamfaa

    [16] Usitikise, ewe Nabii, ulimi wako kwa Qur’ani wakati wahyi unapoteremka ili ufanye haraka kuihifadhi kwa kuogopa isikuponyoke

    [17] Kwani ni juu yetu sisi kuikusanya kwenye kifua chako kisha uisome kwa ulimi wako wakati utakapo. Mjumbe wetu Jibrili akikusomea

    [18] basi kisikilize kisomo chake na umpulikize. Kisha isome kama alivyokusomea

    [19] kisha ni juu yetu kukuelezea kilichokutatiza kukifahamu katika maana yake na hukumu zake

    [20] Mambo sivyo kama mlivyodai, enyi mkusanyiko wa washirikina, kuwa hakuna kufufuliwa wala kulipwa

    [21] Bali nyinyi ni watu mnaopenda dunia na pambo lake na mnaacha Akhera na starehe zake

    [22] Nyuso za watu wema Siku ya Kiyama zitakuwa ni zenye kung’ara, nzuri na zenye furaha

    [23] zitamuona Mola Aliyeziumba na Anayezimiliki, na zitastarehe kwa hilo

    [24] Nyuso za watu wabaya Silku ya Kiyama zitakuwa ni zenye kukunjana na kusinyaa

    [25] zinatazamia kushukiwa na msiba mkubwa wenye kuvunja

    [26] Ni kweli! Pindi roho itakapofika sehemu za juu za kifua

    [27] na wakasema baadhi ya waliohudhuria kuwaambia wengine, «Je kuna mtu wa kumzungua na kumpoza kutokana na hali hii aliyonayo?»

    [28] Na yule ambaye yuko katika hali ya kufa akajua kwamba lile lililomshukia ni kuaga dunia, kwa kuwa anawaona Malaika wa mauti

    [29] Na ikashikana shida ya mwisho wa duniani na shida ya mwanzo wa Akhera. Kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka

    [30] Watu watapelekwa Siku ya Kiyama: ima Peponi au Motoni

    [31] Hakuwa kafiri ni mwenye kumuamini Mtume na Qur’ani, wala hakuwa ni mwenye kumtekelezea Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Swala za faradhi

    [32] Lakini aliikanusha Qur’ani na akaipa mgongo Imani

    [33] kisha akaenda kwa watu wake akijiona hali ya kujigamba katika kutembea kwake. Basi maangamivu

    [34] ni yako baada ya maangamivu

    [35] Kisha maangamivu ni yako baada ya maangamivu

    [36] Je anadhani huyu binadamu anayekanusha kufufuliwa kuwa ataachwa bure: haamrishwi wala hakatazwi, hahesabiwi wala hateswi

    [37] Kwani hakuwa binadamu huyu ni tone la manii dhaifu linalotokana na maji matwevu yanayomwagwa na kumiminwa kwenye kizazi

    [38] kisha yakawa ni kipande cha damu iliyo kavu. Mwenyezi Mungu Akaliumba kwa uweza Wake na Akazilinganisha sura zake katika umbo la mwili lililo zuri kabisa

    [39] Akafanya kutokana na binadamu huyu jinsi mbili: ya kiume na ya kike. Je kwani hakuwa Mola huyo Muumba wa vitu hivyo ni Muweza wa kuwarudisha viumbe wakiwa hai baada ya kutoweka kwao

    [40] Ndio! Anaweza. Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, kwa hakika ni Muweza wa hilo

    Dahri

    Surah 76

    [1] Kishampitia binadamu kipindi kirefa cha wakati kabla hajapulizwa roho ambapo hakuwa ni kita kinachotajika wala haijulikani athari yake

    [2] Sisi tumemuumba binadamu kutokana na tone la manii la mchanganyiko wa maji ya mwanamume na maji ya mwanamke, ili tumtahini kwa lazima za kisheria baadaye, hivyo basi tumfanya ni mwenye masikio ya kusikia na macho ya kuonea, apate kuzisikia aya na kuziona dalili

    [3] Sisi tumembainishia na kumfahamisha njia ya uongofu na upotevu na wema na ubaya ili awe ima ni mwenye kuamini na kushukuru. Au awe ni mwenye kukanusha na kukataa

    [4] Sisi Tumewaandalia wakanushaji pingu za chuma za kuifunga miguu yao na minyororo ya kufungiwa mikono yao hadi shingo zao na moto ambao watachomwa nao

    [5] Hakika watu wa utiifu na ukweli wa Imani wanaotekeleza haki za Mwenyezi Mungu, watakunywa, Siku ya Kiyama, kutoka kwenye kikombe ambacho ndani yake mna Pombe lililochanganywa na aina bora kabisa ya harufu nzuri, nayo ni maji ya kafuri

    [6] Kinywaji hiki kilichochanganywa na kafuri, ni chemchemi wanayokunywa waja wa Mwenyezi Mungu, wanaitumia na kuipitisha wanavyotaka mapitisho mazuri

    [7] Hao walikuwa huko duniani wanatekeleza kile walichojilazimisha nafsi zao cha utiifu kwa Mwenyezi Mungu, na wakiogopa mateso ya Mwenyezi Mungu, Siku ya Kiyama, ambayo madhara yake ni hatari na ubaya ni wenye kusambaa na kuenea kwa watu isipokuwa wale ambao Mwenyezi Mungu Amewarehemu

    [8] Na wanalisha chakula, pamoja na kuwa wanakipenda na kukihitajia, kumpa fukara asiyeweza kuchuma, asiyemiliki chochote katika vitu vya kilimwengu, na kumpa mtoto aliyefiliwa na babake kabla ya kubaleghe na asiye na mali, na kumpa mtu aliyetekwa vitani miongoni mwa washirikina na wengineo

    [9] na huku wanasema katika nafsi zao, «Hakika sisi tunawafanyia wema kwa kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu na kutaka malipo yake. Hatutaki badala wala hatukusudii kushukuriwa wala kusifiwa na nyinyi

    [10] Kwa kweli, sisi tunaiogopa, kutoka kwa Mola wetu, Siku ngumu ambayo ndani yake nyuso zitakunjana na mapaji yatasinyaa kutokana na mambo yake mazito na vituko vyake vikubwa

    [11] Basi hao Mwenyezi Mungu Atawaokoa na shida za Siku hiyo na Atawapa uzuri na mwangaza katika nyuso zao na furaha ndani ya nyoyo zao

    [12] na Atawalipa, kwa kuvumilia kwao duniani juu ya utiifu, Pepo iliyo kubwa ambayo kutoka humo watakula wanachokitaka na watavaa humo hariri nyororo

    [13] hali ya kuwa wametegemea juu ya vitanda vilivyopambwa kwa nguo na pazia za fahari. Hawataona humo joto la jua wala ukali wa baridi

    [14] Na karibu nao, kutakuwa na miti ya Pepo yenye kuwafinika ambayo wamerahisishiwa kuyachuma matunda yake

    [15] Watawazunguka wao watumishi wakiwa na vyombo vya vyakula vya fedha, na vikombe vya vinywaji vya ukoa

    [16] ukowa wa fedha, ambavyo wanyweshaji wamevima kadiri ya watakavyotamani wenye kunywa, haviongezeki wala havipungui

    [17] Na watu wema hawa watanyweshwa Peponi kikombe kilichijazwa Pombe iliyochanganywa na tangawizi

    [18] watakunwa kutoka kwenye chemchemi iliyoko Peponi inayoitwa Salsabīl, kwa kuwa kinywaji chake kina usalama na kuwa kina ulaini na ladha ya kupendeza

    [19] Na watawazunguka wema hawa wakiwatumikia wavulana wenye hali moja ya kudumu, ukiwaona utawadhania, kwa uzuri wao na usafi wa rangi zao na mng’aro wa nyuso zao, kuwa ni lulu iliyotenganishwa inayong’ara

    [20] Na utazamapo mahali popote katika Pepo utaona starehe isiyosifika na ufalme mkubwa uliop mkunjufu usiosiokuwa na mwisho

    [21] Juu ya miili yao pana nguo zilizoipamba, ambazo sehemu zake za ndani kuna hariri nyembamba ya rangi ya kijani, na nje yake kuna hariri nene. Na miongoni mwa mapambo watakayovishwa ni makuku ya fedha. Na Mola wao Atawanywesha, juu ya sterehe hizo, kinywaji kisicho na uchafu wala rojo

    [22] Na wataambiwa, «Hakika nyinyi mmetayarishiwa haya yakiwa ni badala ya matendo yenu mema, na matendo yenu duniani yalikuwa ni yenye kukubaliwa na kuridhiwa na Mwenyezi Mungu.»

    [23] Hakika sisi tumekuteremshia Qur’ani, ewe Mtume, materemsho yanayotoka kwetu, ili uwakumbushe watu yale yaliyomo ndani ya maagizo mema, matahadharisho ya ubaya, malipo mazuri na mateso

    [24] Basi yavumilie maamuzi ya Mola Wako Aliyokupangia na uyakubali, na usonge mbele kufuata maamrisho yake ya Kidini, na usiwatii washirikina waliovama kwenye matamanio au waliokolea kwenye ukafiri na upotevu

    [25] na uendelee kutaja jina la Mola wako na kumuomba mwanzo wa mchana na mwisho wake

    [26] Na wakati wa usiku, mnyenyekee Mola wako na umswalie na umuabudu kipindi kirefu cha usiku

    [27] Kwa hakika hawa washirikina wanaupenda ulimwengu na wanaushughulikia, na wanakuacha nyuma ya migongo yao kule kufanya matendo ya kuwafaa Akhera na kuwaokoa katika Siku yenye shida kubwa

    [28] Sisi Ndio tuliowaumba na tukalipa uthabiti umbo lao. Na tunapotaka tunawaangamiza na kuwaleta watu walio watiifu zaidi wa Mwenyezi Mungu kuliko wao

    [29] Hakika ndani ya sura hii, kwa yaliyomo ya kuvutia na kuogopesha, ya kuahidi mema na kuonya mabaya, kuna mawaidha kwa viumbe wote. Basi mwenye kujitakia wema nafsi yake ya duniani na Akhera, na ashike njia ya Imani na uchamungu itakayomfikisha kwenye msamaha wa Mwenyezi Mungu na radhi Zake

    [30] Na hamtataka jambo lolote miongoni mwa mambo isipokuwa kwa makadirio ya Mwenyezi Mungu na matakwa Yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa hali za viumbe Vyake, ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji na utengezaji Wake

    [31] Anamuingiza Anayemtaka miongoni mwa waja Wake katika rehema Yake na radhi Yake, na wao ni wale walioamini. Na Amewaandalia madhalimu waliokiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu adhabu yenye kuumiza

    Wanaotumwa

    Surah 77

    [1] Anaapa Mwenyezi Mungu kwa upepo unapovuma kwa mfululizo, huu baada ya huu

    [2] Na kwa upepo wenye kuvuma kwa ukali wenye kuangamiza

    [3] Na kwa Malaika waliopewa jukumu la mawingu, wakawa wayapeleka pale anapotaka Mwenyezi Mungu

    [4] Na kwa Malaika wanaoshuka, kutoka kwa Mwenyezi Mungu

    [5] na amri zinazopambanua baina ya haki na batili na halali na haramu

    [6] Na kwa Malaika wanaoupokea wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kuuteremsha kwa Manabii Wake, unaowapa viumbe wake udhuru kutoka kwa Mwenyezi Mungu na pia onyo kutoka Kwake, ili watu wasiwe na hoja

    [7] Hakika jambo la Kiyama mnaloahidiwa pamoja na lile la kuhesabiwa na kulipwa ni lenye kuwa hapana shaka

    [8] Basi nyota zitakapofutwa na mwangaza wake ukaondoka

    [9] na mbingu zitakapopasuka

    [10] na majabali yatakapopeperuka na kukueanea huku na kule na yakawa ni mapepe yanayorushwa na upepo

    [11] Na Mitume watapowekewa wakati na muda wa baina yao na ummah wao na kusemwe

    [12] «Ni Siku kubwa gani Mitume wameahirishiwa?»

    [13] Wameahirishiwa Siku ya hukumu na uamuzi baina ya viumbe

    [14] Na nilipi lililokujulisha wewe, ewe binadamu, ni siku gani hiyo ya kutolewa uamuzi na ni zipi shida zake na vituko vyake

    [15] Maangamivu makubwa Siku hiyo ni ya wale waliyoikanusha Siku hii iliyoahidiwa

    [16] Kwani hatukuawaangamiza walitangulia kati ya umma waliopita kwa kuwakanusha kwao Mitume, kama vile watu wa Nūḥ, ‘Ād na Thamūd

    [17] Kisha tutawakutanisha na wao wale waliokuja nyuma kati ya wale waliokuwa ni kama wao katika ukanushaji na uasi

    [18] Mfano wa uangamizaji huo mkali ndivyo tutakavyowafanya wahalifu kati ya makafiri wa Makkah, kwa kumkanusha kwao Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [19] Maangamivu na adhabu kali Siku ya Kiyama kwa kila mwenye kuukanusha upweke wa Mwenyezi Mungu, unabii, kufufuliwa na kuhesabiwa

    [20] Je kwani sisi hatukuwaumba nyinyi, enyi mkusanyiko wa makafiri, kutokana na maji dhaifu yaliyo matwevu nayo ni tone la manii

    [21] tukayaweka maji haya kwenye mahali palipohifadhika, napo ni kizazi cha mwanamke

    [22] mpaka kipindi maalumu kinachojulikana na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka

    [23] Tukaweza kumuumba, kumtia sura na kumtoa. Basi bora wa wenye kuweza ni s isi

    [24] Maangamivu na adhabu kali Siku ya Kiyama kwa wenye kukanusha uweza wetu

    [25] Je kwani hatukuifanya hii ardhi mnayoishi juu yake

    [26] ikusanye juu ya mgongo wake walio hai wasiohesabika, na ndani ya matumbo yake wafu wasiodhibitika, na

    [27] tukajaalia iwe na majabali yaliyojikita yaliyo marefu ili isitikisike na nyinyi, na tukawanywesha maji tamu yaliyo mazuri

    [28] Maangamivu na adhabu kali Siku ya Kiyama kwa waliozikanusha neema hizi

    [29] Wataambiwa makafiri Siku ya Kiyama, «Endeni kwenye adhabu ya moto wa Jahanamu mliokuwa mkiukanusha duniani

    [30] Endeni mjifinike kwenye kivuli cha moshi wa moto wa Jahanamu ambacho hapo panachembuka vipande vitatu

    [31] Kivuli hiko hakimfanyi mtu ahifadhike na joto la Siku hiyo wala hakizuii muwako wa Moto chochote

    [32] Hakika moto wa Jahanamu unarusha macheche makubwa ya moto, kila cheche moja katika hayo ni kama jengo lililoimarishwa katika ukubwa na urefu wa kuenda juu

    [33] Kama kwamba hizo cheche za moto wa Jahanamu zinazopaa juu ni ngamia weusi ambao rangi yao imeingia kwenye umanjano.»

    [34] Maangamivu na adhabu kali kwa wenye kukanusha mateso yaliyoahidiwa na Mwenyezi Mungu

    [35] Hii ndiyo Siku ya Kiyama ambayo wakanushaji hawatatamka maneno ya kuwanufaisha

    [36] wala hawatapewa idhini ya kusema wakatoa nyudhuru, kwa kuwa hawatakuwa na udhuru wowote

    [37] Maangamivu na adhabu kali kwa wenye kuikanusha siku hii na yaliyomo ndani yake

    [38] Hii ni Siku ambayo Mwenyezi Mungu Atatoa uamuzi baina ya viumbe, na ukweli na ubatilifu utapambanuka. Tutawakusanya nyinyi Siku hiyo, enyi makafiri wa ummah huu, pamoja na makafiri wa mwanzo miongoni mwa ummah waliopita

    [39] Basi mkiwa na hila za kujitoa na adhabu, tumieni hila zenu na mziokoe nafsi zenu na msukosuko wa Mwenyezi Mungu na mateso Yake

    [40] Maangamivu na adhabu kali Siku ya Kiyama kwa wenye kuikanusha Siku ya Kiyama

    [41] Hakika ya wale waliomuogopa Mola wao duniani na wakaiogopa adhabu Yake kwa kufuata amri Zake na kujiepusha na makatazo Yake. Wao Siku ya Kiyama watakuwa kwenye vivuli vya miti vilivyonyoka, na chemchemi za maji zinazotembea

    [42] na matunda mengi yanayopendwa na nafsi zao ambayo wao wanastarehe nayo. Hapo waambiwe

    [43] «Kuleni chakula chenye ladha na mnyweni kinywaji chenye kufurahisha kwa sababu ya matendo mema mliyoyatanguliza duniani.»

    [44] Sisi, kwa mfano wa malipo hayo makubwa, tutawalipa watu wema katika matendo yao na utiifu wao kwetu

    [45] Maangamivu na adhabu kali Siku ya Kiyama kwa wenye kuikanusha Siku ya Malipo na Hesabu, na kuzikanusha sterehe na mateso yaliyomo Siku hiyo

    [46] Kisha Mwenyezi Mungu Akawaonya makafiri kwa kusema, «Kuleni aina ya vyakula vya ladha duniani na stareheni kwa matamanio yake yenye kumalizika kwa muda mchache, hakika nyinyi ni wahalifu kwa kumshirikisha kwenu Mwenyezi Mungu.»

    [47] Maangamivu na adhabu kali Siku ya Kiyama kwa wenye kuikanusha Siku ya kuhesabiwa na kulipwa

    [48] Na wanapoambiwa hawa washirikina, «Mswalieni Mwenyezi Mungu na mnyenyekeeni,» hawanyenyekei wala hawaswali, bali wanaendelea kuonyesha kiburi chao

    [49] Maangamivu na adhabu kali Siku ya Kiyama kwa wenye kuzikanusha aya za Mwenyezi Mungu

    [50] Iwapo wao hawataiamini hii Qur’ani, basi wataamini kitabu gani na maneno gani baada yake? Na Qur’ani yenyewe ni Kitabu kilichobainisha kila kitu, kilicho wazi katika hekima zake, hukumu zake na habari zake, chenye kushinda katika matamko yake na maana yake

    Khabari

    Surah 78

    [1] Kuhusu kitu gani baadhi ya makafiri wa Kikureshi wanaulizana

    [2] Wanaulizana kuhusu habari iliyo na uzito mkubwa kabisa

    [3] nayo ni Qur’ani tukufu inayotoa habari za kufufuliwa ambako makafiri wa Kikureshi wana shaka nako na wanakukanusha

    [4] Mambo sivyo kama wanavyodhania hawa washirikina. Hapo watajua hawa washirikina upeo wa kukanusha kwao na kitawadhihirikia waziwazi kile Atakachowatenda Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama

    [5] Kisha litahakikishika kwao jambo hilo na utahakikishika kwao ukweli wa yale aliyokuja nayo Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kuhusu Qur’ani na kufufuliwa. Huu ni utisho na makemeo kwao

    [6] Kwani hatukuwatandazia ardhi kama tandiko

    [7] Na Tukawafanyia majabali kuwa ni vigingi, ili isitisike nanyi

    [8] Na Tukawaumba aina mbali-mbali, mume na mke

    [9] Na Tukafanya usingizi wenu ni mapumziko kwa viwiliwili vyenu: ndani yake mnatulia na kupumzika

    [10] Na Tukaufanya usiku kuwa ni vazi, unawavisha giza lake na kuwafinika, kama nguo inavyomsitiri mwenye kuivaa

    [11] Na Tukaufanya mchana ni kipindi cha kutafuta maisha, mnaenea humo kwa ajili ya maisha yenu na mnatembea humo kwa ajili ya maslahi yenu

    [12] Na Tukajenga juu yenu mbingu saba, madhubuti jengo lake, lilioumbwa kwa uzuri, halina mapasuko wala nyufa

    [13] Na Tukalifanya jua kuwa ni taa iwakayo na kung’ara

    [14] Na Tukateremsha kutoka kwenye mawingu yanyeshayo maji yamiminikayo kwa wingi

    [15] ili Tutoe kwa maji hayo nafaka inayoliwa na watu

    [16] nyasi zinazoliwa na wanyama na miti iliyosongamana kwa kutawanyika tagaa zake

    [17] Hakika Siku ya Uamuzi kati ya viumbe

    [18] nayo ni Siku ya Kiyama, imekuwa ni wakati na ahadi iliyowekewa muda maalimu kwa watu wa mwanzo na wa mwisho

    [19] Na zikafunguliwa mbingu zikawa ni zenye milango mingi kwa ajili ya kuteremka Malaika

    [20] Na yakalipuliwa majabali baada ya kuwa yamekita, yakawa ni kama mangati

    [21] Hakika Jahanamu, Siku Hiyo, itawalindiza wenye ukafiri ambao Moto huo umeandaliwa wao

    [22] Kwa makafiri ndio marejeo

    [23] Watabakia humo muda mrefu ufuatanao, usiokoma

    [24] Hawatakula humo chochote kitakachozizimisha joto la moto kwao

    [25] Wala kinywaji kitakachowaondolea kiu yao. Isipokuwa maji moto na usaha wa watu wa motoni

    [26] Watakuwa wanalipwa kwa hilo malipo ya sawa yanayolingana na vitendo vyao walivyovitenda duniani

    [27] Hakika wao walikuwa hawaiyogopi Siku ya Hesabu, na kwa hivyo hawakujitayarisha nayo kwa kufanya matendo ya kuwafaa

    [28] Na waliyakanusha waziwazi yaliyoletwa na Mitume

    [29] Na kila kitu Tulikijua na Tukakiandika katika Ubao uliohifadhiwa (Al-Lawḥ Al-Maḥfūd)

    [30] Basi Onjeni, enyi makafiri, hayo yakiwa ni malipo ya vitendo vyenu, Hatutawazidishia isipokuwa adhabu juu ya adhabu yenu

    [31] Hakika kwa wale ambao wanamuogopa Mola wao na huku wanatenda mema kuna kufaulu kwa kuingia Peponi

    [32] Hakika watapata Mabustani makubwa na zabibu

    [33] Na watapata wanawake wenye umri mdogo, wenye vifua vilivyojaza, marika na waume zao

    [34] Na watapata glasi zlizojaa pombe

    [35] Hawatasikia katika Pepo hiyo maneno ya upotofu wala kudanganyana

    [36] Watayapata yote hayo yakiwa ni malipo na zawadi na kipewa kingi cha kuwatosha kutoka kwa Mwenyezi Mungu

    [37] Mola wa mbingu na ardhi na vilivyomo kati ya hizo, Mwenye kuwarehemu duniani na Akhera. Hawataweza kumuomba isipokuwa kile walichopewa ruhusa kumuomba

    [38] Siku atakaposimama Jibrili na Malaika wengine hali ya kujipanga mlolongo. Hawatamuombea isipokuwa yule aliyetolewa ruhusa na Mwingi wa Rehema ya kuombewa na akasema maneno ya haki na ya sawa

    [39] Hiyo ndiyo siku ya haki isiyokuwa na shaka kuja kwake. Kwa hivyo, yule atakaye kuokoka na vituko vya Siku hiyo, na ajifanyie njia ya marejeo kwa Mola wake kutenda vitendo vyema

    [40] Sisi Tunawaonya nyinyi adhabu ya Siku ya mwisho iliyo karibu. Siku ambayo atayaona kila mtu aliyoyatenda katika kheri au aliyoyachuma miongoni mwa madhambi. Na kafiri atasema, kwa kitisho cha Hesabu, «Laiti mimi nilikuwa mchanga na sikufufuliwa.»

    Wanang'oao

    Surah 79

    [1] Anaapa Mwenyezi Mungu kwa Malaika ambao huzing’oa roho za makafiri mng’oo mkali

    [2] Na kwa Malaika ambao huzitukua roho za Waumini kwa uchangamfu na upole

    [3] Na kwa Malaika wanaoogelea katika kushuka kwao kutoka mbinguni na kupaa kwao kwenda mbinguni

    [4] Na kwa Mlaika ambao wanakimbilia kutekeleza amri za Mwenyezi Mungu

    [5] Na kwa Malaika wanaopitisha amri za Mola wao katika mambo ya ulimwengu waliowakilishwa kuyafanya na kuyasimamia, - Wala haifai kwa kiumbe kukiapia chochote kile, bali yapasa kiapo chake kiwe ni kwa jina la Mola wake Muumba au sifa Zake. Na lau ataapa kwa asiye Muumba wake, basi huyo amekuwa mshirikina - Watafufuliwa viumbe bila shaka na watahesabiwa

    [6] Siku ambayo ardhi itatetemeka kwa mvuvuo wa kwanza

    [7] mvuvio wa kufisha, ukifuatiwa na mvuvio mwingine wa kuhuisha

    [8] Nyoyo za makafiri, Siku hiyo, zitakuwa na papatiko kwa kicho kikubwa

    [9] Macho ya makafiri hao yatakuwa madhalilifu kwa kitisho watakachokiona

    [10] Wanasema hawa wakanushao kufufuliwa

    [11] «Je, tutarudishwa baada ya kufa kwetu kwenye yale tuliyokuwa nayo katika ardhi? Je, tutarudishwa na hali tushakuwa mifupa iliochakaa?»

    [12] Wakasema: «Kurejea kwetu huko kutakuwa kutupu kusikokuwa kweli.’

    [13] Hakika tukio hilo litakuwa kwa mvivio mmoja tu

    [14] Wakitahamaki wao wako hai juu ya ardhi baada ya kuwa walikuwa ndani yake

    [15] Je imekujilia, ewe Mtume, habari ya Mūsā

    [16] Pindi Mola wake Alipomwita katika bonde lililotakaswa na kubarikiwa, la Ṭuwā. Akamwambia

    [17] «Enda kwa Firauni. Hakika yeye amekiuka mno katika kuasi

    [18] Ukamwambie, ‘Je, unapendelea kuitakasa nafsi yako na upungufu na kuipamba na imani

    [19] Na nikuelekeze njia ya kumtii Mola wako, upate kumcha na kumuogopa?’»

    [20] Mūsā alimuonyesha Firauni alama kubwa: fimbo na mkono

    [21] Hapo Firauni alimkanusha Nabii wa Mwenyezi Mungu , naye ni Mtume Mūsā, amani imshukie, na alimuasi Mola wake Aliyetukuka

    [22] Kisha alikengeuka hali ya kuipa mgongo Imani na kufanya bidii katika kumpinga Mūsā

    [23] Hapo aliwakusanya raia wa utawala wake na akawaita kwa

    [24] kuwaambia,»Mimi ndiye mola wenu ambaye hakuna mola mwengine aliye juu yake.»

    [25] Hapo Mwenyezi Mungu Alimtesa kwa adhabu ya duniani na ya Akhera

    [26] Na Akaifanya adhabu hiyo iwe ni mazingatio na ni onyo kwa watu mfano wake kati ya wale waasi. Hakika Firauni na kile kilichompata cha adhabu ni mawaidha kwa mwenye kuwaidhika na kutishika

    [27] Je, kufufuliwa kwenu, enyi watu, baada ya kufa ni kugumu zaidi, katika vipimo vyenu, au ni kuumbwa kwa mbingu

    [28] Amezipanga juu yenu kama jengo. Na Ameinua sakafu yake angani, haina tofauti wala nyufa

    [29] Na Ameutia giza usiku wake kwa kutwa kwa jua lake. Na Ameweka wazi mchana wake kwa kuchomoza kwake

    [30] Na ardhi baada ya kuumba mbingu Ameitandaza. Na Ameweka humo manufaa yake

    [31] Na Ametumbua humo chemchemu za maji. Na Ameotesha humo mimea inayolishwa

    [32] Na Ameyakita humo majabali yakiwa ni vigingi vyake. Ameumba, Aliyetakasika na kila upungufu

    [33] neema zote hizi zikiwa ni manufaa kwenu na kwa wanyama wenu. (Hakika kurudisha kuumbwa kwenu, Siku ya Kiyama, ni sahali kwa Mwenyezi Mungu kushinda kuumba viumbe hivyo vyingine. Na vyote hivyo, kwa Mwenyezi Mungu, ni rahisi na ni vipesi)

    [34] Pindi kitakapokuja Kiyama Kikubwa na balaa nzito, nao ni Mvuvio wa pili. Kipindi hicho zitaoneshwa kwa binadamu vitendo vyake vyote, za kheri na za shari

    [35] Hapo atazikumbuka na kuzitambua

    [36] Na utaoneshwa Moto wa Jahanamu kwa kila aonaye, uwe waonekana waziwazi

    [37] Ama yule atakayekiuka amri ya Mwenyezi Mungu

    [38] na akapendelea maisha ya ulimwenguni kuliko ya Akhera

    [39] basi kwa kweli marejeo yake ni Motoni

    [40] Na ama yule atakayeogopa kusimama mbele ya Mwenyezi Mungu kuhesabiwa na akaikanya nafsi yake na matamanio mapotofu

    [41] basi Peponi ndiko makazi yake

    [42] Wanakuuliza washirikina, ewe Mtume, kwa madharau, kuhusu wakati wa kuanzia Kiyama unachowaonya

    [43] Wewe huna kamwe ujuzi nacho

    [44] Bali mambo ya ujuzi huo yarejeshwe kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye Sifa Tukufu

    [45] Wewe linalokuhusu katika habari zake ni kumuonya nacho yule anayekiogopa

    [46] Kama kwamba wao siku watakapouona Kiyama kimesimama, watakuwa hawakukaa katika maisha yao ya duniani, kwa vituko vya hiko Kiyama, isipokuwa ni kama kwamba wamkaa kati ya adhuhuri mpaka kutwa juwa, au ni kama kati ya kuchomoza jua mpaka nusu ya mchana

    Alikunja Nuso

    Surah 80

    [1] Yalidhihiri mabadiliko na mkunjiko katika uso wa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [2] na akapa nyongo kwa sababu ya kwamba Abdallah bin Ummi Maktum alimjilia akitaka aelekezwe. Na alikuwa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ameshughulika kuwalingania miamba wa Kikureshi katika Uislamu

    [3] Ni kitu gani kinakufanya wewe ujue uhakika wa jambo lake? Kwani huenda ikawa, kwa kuuliza kwake, nafsi yake itatakasika na kusafika

    [4] Au pengine apate mazingatio zaidi na kutishika

    [5] Basi yule alijyejitosheleza na kutouhitajia uongozi wako

    [6] wewe ndiye unayemjali na wapulikiza maneno yake

    [7] Na ni kitu gani kinachokupa jukumu kwako iwapo hakusafika na ukafiri wake

    [8] Ama yule ambaye amekuwa na pupa la kukutana na wewe

    [9] na huku anamuogopa Mwenyezi Mungu asiwe na kasoro katika kupata uongofu

    [10] wewe unampuuza. Ilivyotakikana ufanye si kama ulivyofanya, ewe Mtume

    [11] Hakika Sura hii ni mawaidha kwako na kwa kila anayetaka kuwaidhika

    [12] Basi atakaye atamkumbuka Mwenyezi Mungu na kumtaja na atafuata Wahyi Wake

    [13] Wahyi huu, nao ni Qur’ani, uko katika kurasa zilizotukuzwa

    [14] zenye kuheshimiwa, zenye cheo cha juu

    [15] zilizosafishwa na uchafu, uongezaji na upunguzaji

    [16] Zilizoko mikononi mwa Malaika waandishi, mabalozi kati ya Mwenyezi Mungu na viumbe Wake, wenye maumbile mema, tabia zao ni nzuri na njema na pia matendo yao

    [17] Amelaaniwa mtu kafiri na ataadhibiwa. Ni uovu ulioje wa ukafiri wake kwa Mola wake

    [18] Kwani hajui ni kwa kitu gani Mwenyezi Mungu Alimuumba kwacho mwanzo wake

    [19] Mwenyezi Mungu Alimuumba kwa maji machache, nayo ni manii. Akayakadiria miongo yake

    [20] Kisha Akambainishia njia ya kheri na ya shari

    [21] Kisha humkosesha uhai, na Amemuekea mahali pa kuzikiwa

    [22] Kisha Akitaka Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na sifa mbaya, Atamhuisha na kumfufua baada ya kifo chake, kwa ajili ya kuhesabiwa na kulipwa

    [23] Mambo siyo kama yale anayoyasema kafiri na anayoyafanya. Bado hajatakeleza Aliyomuamrisha kwayo Mwenyezi Mungu katika kuamini na kutenda wema kwa kumtii

    [24] Na azingatie binadamu, vipi Mwenyezi Mungu Amekiumba chakula chake ambacho ndicho kinachoendeleza maisha yake

    [25] Aone kwamba Sisi Tumeyamimina maji ya mvua juu ya ardhi kwa wingi

    [26] Kisha Tumeipasua ardhi kwa Tulivyo vitoa kutoka humo miongoni mwa mimea tofauti

    [27] Tukaotesha humo nafaka

    [28] na zabibu, na nyasi za wanyama.Na mizaituni na mitende

    [29] Na mabustani yenye miti mikubwa

    [30] Na matunda

    [31] na ndisha

    [32] Mnajistareheshea kwazo, nyinyi na wanyama wenu

    [33] Utakapokuja Ukelele wa Siku ya Kiyama, ambao utayatia uziwi, kwa kitisho chake, masikizi

    [34] Siku mtu atakapomkimbia, kwa kitisho cha Siku Hiyo, nduguye

    [35] na babake na mamake na

    [36] mkewe na wanawe

    [37] Kila mmoja Siku Hiyo, atakuwa na jambo litakalomzuia asishughulike na mwingine

    [38] Nyuso za wenye neema, Siku Hiyo, zitakuwa ni zenye kung’ara

    [39] zenye furaha na nderemo

    [40] Na nyuso za watu wa Motoni zitakuwa na giza

    [41] nyeusi, zafinikwa na unyonge

    [42] Hao wenye kusifika na sifa hiyo ndiwo wale waliozikufuru neema za Mwenyezi Mungu na wakazikanusha aya zake na wakayakeuka Aliyoyaharamisha kwa kutenda maovu na kukiuka mipaka

    Kukunja

    Surah 81

    [1] Pindi jua litakapokunjwa, na mwangaza wake ukaondoka

    [2] Na pindi nyota zitakapopuputika na nuru yake ikafutika

    [3] Na pindi majabali yatakapoondoshawa kwenye uso wa ardhi yakawa ni vumbi linaloenea

    [4] Na pindi ngamia wenye mimba watakapoachwa na kupuuzwa

    [5] Na pindi wanyama mwitu watakapokusanywa na kutangamanishwa, ili Mwenyezi Mungu Awape nafasi ya kulipizana wao kwa wao

    [6] Na pindi bahari zitakapowashwa moto zikawa ni moto unaowaka

    [7] Na pindi nafsi zitakapokutanishwa na mfano wake na sampuli yake

    [8] Na pindi mtoto wa kike aliyezikwa akiwa hai atakapoulizwa, Siku ya Kiyama, suala la kumbembeleza na kumkejeli aliyemzika

    [9] ni kwa dhambi gani ilikuwa kuzikwa kwake

    [10] Na pindi kurasa za matendo zitakapoonyeshwa

    [11] Na pindi mbingu zitakapong’olewa na kuondoshwa zilipokuwa

    [12] Na pindi Moto utakapowashwa na ukawaka

    [13] Na pindi Pepo , Nyumba ya Neema, itakaposongezewa watu wake wachamungu

    [14] Litakapotokea hilo, itayakinisha kila nafsi na kujua kile ilichokitanguliza cha kheri au shari

    [15] Anaapa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa nyota zinazofichika nuru yake mchana

    [16] zinazotembea na zinazoghibu katika anga zake

    [17] Na Anaapa kwa usiku unapojitokeza na giza lake

    [18] Na kwa asubuhi unapojitokeza mwangaza wake

    [19] Hakika Qur’ani ni ujumbe wa mjumbe mtukufu , naye ni Jibrili, amani imshukike

    [20] Mwenye nguvu katika kuyapitisha yale anayoamrishwa. Mwenye cheo cha juu kwa Mwenyezi Mungu. Anayesikilizwa na Malaika

    [21] Anayeaminiwa juu ya Wahyi anaoteremka nao

    [22] Hakuwa Muhammad mnayemjua ni mwendawazimu

    [23] Na kwa hakika Muhammad alimuona Jibrili anayemjia na utume katika pambizo kubwa

    [24] Wala yeye hafanyi ubakhili katika kufikisha Wahyi

    [25] Wala haikuwa hii Qur’ani ni neno la Shetani aliyefukuzwa na kutolewa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu. Lakini Qur’ani hii ni maneno ya Mwenyezi Mungu na ni Wahyi wake

    [26] Akili zenu zawapeleka wapi katika kukanusha baada ya hoja hizi zilizo wazi na zenye nguvu

    [27] Hayakuwa haya isipokuwa ni mawaidha kutoka kwa Mwenyezi Mungu yanapewa watu wote

    [28] Kwa atakaye, kati yenu, kulingana juu ya haki na Imani

    [29] Wala nyinyi hamtotaka isipokuwa kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe wote

    Kupasuka

    Surah 82

    [1] Pindi mbingu zitakapopasuka na ukaharibika mpango wake

    [2] Na pindi nyota zitakapoangukiana

    [3] Na pindi Mwenyezi Mungu Atakapozifanya bahari kulipuka na maji yake kutoweka

    [4] Na pindi makaburi yatakapogeuzwa kwa kufufuliwa waliokuwamo ndani yake

    [5] Wakati huo itajua kila nafsi vitendo vyake vyote ilivyovifanya, vilivyotangulia na vilivyoahirika na italipwa kwa vitendo hivyo

    [6] Ewe binadamu unayekanusha kufufuliwa! Ni kipi kilichokufanya uhadaike na ughurike kuhusu Mola wako Mpaji Mwenye kheri nyingi, Anayestahiki kushukuriwa na kutiiwa

    [7] Kwani si Yeye Aliyekuumba, Akalisawazisha umbo lako, Akakuweka katika hali ya sawa na Akakurekibisha ili uweze kutekeleza nyadhifa zako

    [8] katika sura yoyote ile Aliyoitaka Akakuumba

    [9] Mambo hayako kama vile mnavyosema kwamba nyinyi mna haki ya kumuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Bali nyinyi mnaikanusha Siku ya Hesabu na Malipo

    [10] Na mjue kuwa wako na nyinyi Malaika wachunguzi

    [11] watukufu kwa Mwenyezi Mungu, waandishi wa yale waliyowakilishwa kuyadhibiti. Hakiwapiti, katika vitendo vyenu na siri zenu, chochote

    [12] Wanayajua mnayoyafanya, ya kheri au ya shari

    [13] Hakika wachamungu wanaotekeleza haki za Mwenyezi Mungu na haki za waja wake watakuwa kwenye neema

    [14] Hakika watu waovu waliopuuza haki za Mwenyezi Mungu na haki za waja wake watakuwa katika Moto mkali

    [15] Ukali wake, Moto huo, utawapata Siku ya Malipo.Na wala wao hawatakuwa ni wenye kughibu

    [16] wakawa hawamo ndani ya Moto wa Jahanamu, si kwa kutoka wala kwa kufa

    [17] Ni kipi kinachokujuza ni upi utukufu wa Siku ya Hesabu

    [18] Kisha ni kipi kinachokujuza ni upi utukufu wa Siku ya Hesabu

    [19] Siku ya Hesabu, hataweza yoyote kumnufaisha yoyote. Na amri zote Siku Hiyo ni za Mwenyezi Mungu Peke yake Ambaye hakuna mwenye kumshinda, wala hakuna mwenye kumtendesha nguvu, wala hakuna mwenye kushindana na Yeye

    Wanao punguza

    Surah 83

    [1] Adhabu kali ni ya wale wanaopunja vipimo vya vibaba na mezani

    [2] Ambao wakinunua kwa watu cha kupimwa kwa vibaba au kwa mizani hujikamilishia wao wenyewe

    [3] Na wakiwauzia watu kinachouzwa kwa vibaba au mizani wanapunguza vipimo

    [4] Basi itakuwaje hali ya yule anayeiba na kupunja katika vipimo vyote hivyo, au yule anayeiba katika vipimo hivyo na huku awapunja watu vitu vyao? Hakika huyo yuwastahiki mateso zaidi kuliko wapunguzaji wa vipimo vya vibaba na mizani. Kwani hawaamini wale wapunjaji ya kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mwenye kuwafufua na kuwahesabu juu ya vitendo vyao

    [5] katika Siku itakapokuwa na kitisho

    [6] Siku watakaposimama watu mbele ya Mweyezi Mungu ili Awahesabu kwa machache na mengi walioyatenda, hali ya kuwa wao Siku Hiyo ni wenye kumnyenyekea Mwenyezi Mungu, Mlezi wa viumbe vyote

    [7] Hakika marejeo ya watu waovu na makazi yao yatakuwa katika hali ya dhiki

    [8] Na ni kipi kinachokujulidha dhiki hii ni ipi

    [9] Hakika hiyo itakuwa ni jela ya kudumu na adhabu iliyo na uchungu. Penye jela hiyo ni pale walipoandikiwa kuwa watakwenda. Wameandikiwa na imepitishwa. Hapana kitakachozidishwa wala kupunguzwa

    [10] Adhabu kali Siku Hiyo ni ya wale wenye kukanusha

    [11] Wale ambao wanakanusha kuwako tukio la Siku ya Malipo

    [12] Na wala haikanushi Siku Hiyo isipokuwa kila dhalimu mwenye madhambi mengi

    [13] Anaposomewa aya za Qur’ani, husema, «Hizi ni hadithi za urongo za watu wa kale.» Mambo yalivyo si kama wanavyodai

    [14] Bali hayo ni maneno ya Mwenyezi Mungu na Wahyi Wake kwa Mtume Wake

    [15] Na hakika zimezibwa nyoyo zao zikawa hazimkubali Mwenyezi Mungu. Na kile kilichoziziba nyoyo hizo ni kufinikwa na wingi wa madhambi wanayoyafanya. Mambo hayako kama vile wanavyodai makafiri! Bali hakika wao, Siku ya Kiyama watazibwa wasimuone Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kushinda. Aya hii ni ushahidi kwamba Waumini watamuona Mola Wao Peponi

    [16] Kisha hakika hao makafiri ni wenye kuingia Motoni, na wataziona na kuzihisi dharubu zake

    [17] Kisha wataambiwa,»Haya ndiyo malipo ya yale ambayo mlikuwa mnayakanusha.»

    [18] Ni kweli kabisa kwamba kitabu cha watu wema, nao ni wachamungu, kiko katika ngazi za juu Peponi

    [19] Na ni kipi kinachokujulisha ni zipi hizi ngazi za juu

    [20] Ni kitabu cha watu wema kilichopitishwa mambo yake, hakizidishwi kitu humo wala hakipunguzwi

    [21] Wanayatazama yaliyomo ndani yake Malaika waliokurubishwa, wa kila mbingu

    [22] Hakika wale wenye ukweli na kufuata amri za Mwenyezi Mungu watakuwa Peponi wnaneemeka

    [23] juu ya viti vya fahari wanamwangalia Mola wao na wanaangalia yale waliyoandaliwa miongoni mwa kheri nyingi

    [24] Unaonekana katika nyuso zao mng’aro wa neema

    [25] Watanyweshwa tembo safi, lililotengezewa vyombo kwa ustadi na mwishowe kuna harufu ya miski

    [26] Katika kuzipata neema hizo, nawashindane wenye kushindana

    [27] Na kinywaji hiki, mchanganyo wake watokana na chemchemi iliyoko Peponi linalojulikana, kwa ubora wake, kwa jina la Tasnīm

    [28] Hiyo ni chemchemi iliyoandaliwa wale waliokurubishwa kwa Mwenyezi Mungu na watajiburudisha nayo

    [29] Hakika wale waliotenda maovu walikuwa duniani wakiwacheza shere Waumini

    [30] Na wanapowapitia wanakonyezana kwa kuwakejeli

    [31] Na wnaporudi, hawa waovu, kwa watu wao na jamaa zao, huwa na vihunzi na wao kwa kuwafanyia maskhara Waumini

    [32] Na hawa makafiri wanapowaona Maswahaba wa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wamefuata uongofu, huwa wakisema, «Hakika hawa wamepotea kwa kumfuata Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [33] Na wala waovu hawa hawakutumwa wawe ni wachunguzi kwa Maswahaba na Mtume , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [34] Basi Siku ya Kiyama wale waliomkubali Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakafanya vitendo vinavyolingana na sheria Zake, watawafanyia maskhara makafiri kama makafiri walivyokuwa wakiwafanyia mashara duniani

    [35] Juu ya viti vya fahari, watakuwa Waumini wanaangalia yale Aliyowapa Mwenyezi Mungu miongoni mwa mambo matukufu na neema, wakiwa Peponi. Na neema kubwa ya zote ni kuangalia Uso wa Mwenyezi Mungu Mtukufu

    [36] Je, wamelipwa makafiri, pindi watakapo kufanyiwa hayo, malipo muwafaka na yale waliyoyafanya duniani ya shari na madhambi

    Kupasuka

    Surah 84

    [1] Pindi mbingu itakapopasuka na kudhihiri mawingu katika pasuko zake Siku ya Kiyama

    [2] Na ikatii amri ya Mola wake ya kuwa ipasuke, na inastahili kufuata amri hiyo

    [3] Na pindi ardhi itakapotandikwa na kukunjuliwa

    [4] Na milima yake kuvunjwa-vunjwa Siku hiyo

    [5] Na ikatii amri ya Mola wake ya kuwa ifanye hivyo, na inastahili kufuata amri hiyo

    [6] Ewe binadamu, wewe unaenda kwa Mwenyezi Mungu na unafanya amali nzuri na mbaya, kisha utakutana na Yeye Siku ya Kiyama. Na huna budi kupata kutoka Kwake malipo mazuri zaidi ya amali yako njema au yanayolingana na amali yako mbaya

    [7] Yule mwenye kupewa waraka wa amali zake kwa mkono wake wa kulia

    [8] naye ni yule aliyemuamini Mola wake, atahesabiwa hesabu pesi

    [9] Na atarudi kwa watu wake Peponi akiwa ni mwenye furaha

    [10] Na yule mwenye kupewa waraka wa amali zake kwa nyuma ya mgongo wake

    [11] naye ni yule aliyemkanusha Mwenyezi Mungu, ataita maangamvu na hasara

    [12] na ataingia Motoni

    [13] Hakika yeye alikuwa kwa watu wake ulimwenguni ni mwenye furaha na majivuno, hafikirii mwisho wake utakuwa namna gani

    [14] Alidhani hatarudi kwa Muumba wake, akiwa hai, kwa kuhesabiwa

    [15] Sivyo hivyo! Mwenyezi Mungu Atamrudisha kama alivomuumba na kumlipa kwa amali zake. Kwani Yeye kwake ni Mtambuzi na kwa hali yake ni Mjuzi kuanzia Alipomuumba mpaka kumfufua

    [16] Mwenyezi Mungu Ameapa kwa wekundu wa pambizo za mbingu wakati wa kutwa jua

    [17] Na kwa usiku na viunbe tofauti - tofauti vya kutambaa, kuruka na kutembea kwa miguu, uliokusanya

    [18] Na kwa mwezi ukamilikapo mwangaza wake

    [19] Mtapitia, enyi watu, miongo mbalimbali na hali tofauti : kutoka kwenye tone la manii, kuptia pande la damu, nofu la nyama hadi kutiwa roho, mpaka kufa na mpaka kufufuliwa. Haifai kwa kiumbe kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, afanyapo hilo atakuwa ameingia kwenye ushirikina

    [20] Ni kitu gani kinachowazuia kumwamini baada ya aya zake kufafanuliwa kwao

    [21] Na wana nini wao wanaposomewa Qur’ani hawamsujudii Mwenyezi Mungu wala hawajisalimishi kufuata yaliyokuja ndani yake

    [22] Hakika tabia ya waliokufuru ni kuikanusha na kuikataa haki

    [23] Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi wa ukaidi wao wanaouficha kwenye nyoyo zao hali wao wanajua kuwa yale yaliyoletwa na Qur’ani ni kweli

    [24] Basi wape bishara, ewe Mtume, kuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, Amewaandalia adhabu yenye uchungu

    [25] Lakini wale wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakatekeleza amri waliyofaradhiwa na Mwenyezi Mungu watakuwa na malipo, Siku ya Akhera, yasiyokatika wala kupungua

    Buruji

    Surah 85

    [1] Mwenyezi Mungu Anaapa kwa mbingu zenye njia za kupitia jua na mwezi

    [2] Na kwa Siku ya Kiyama ambayo Amewaahidi viumbe kuwa Atawakusanya

    [3] Na kwa shahidi, mwenye kutoa ushahidi, na mwenye kutolewa ushahidi juu yake. Mwenyezi Mungu Huapa kwa Anachokitaka. Lakini kiumbe hafai kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu ni ushirikina

    [4] Wamelaaniwa waliofukua chini ya ardhi shimo kubwa ili kuwatesa Waumini

    [5] Wakawasha moto mkubwa wenye kuni nyingi

    [6] Wakawa wamekaa kwenye kingo za shimo hilo

    [7] Wakishuhudia vitendo vya mateso na adhabu wanavyowafanyia Waumini

    [8] Na hawakuwatesa mateso hayo isipokuwa wenye kuteswa walikuwa wanamuamini Mwenyezi Mungu Mshindi Asiyeshindwa, Mhimidiwa wa maneno Yake vitendo Vyake na sifa Zake

    [9] Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi Ambaye, kutakasika na sifa za upungufu ni kwake, Anashuhudia kila kitu, hakuna kinachofichika kwake

    [10] Hakika, wale waliowachoma kwa moto Waumini, wa kike na wa kiume, ili kuwazuia watu na dini ya Mwenyezi Mungu, kisha wasitubie, watapata, Siku ya Akhera, adhabu ya Jahanamu na watapata adhabu kali yenye kuchoma

    [11] Wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafanya amali njema, watapata Pepo ambayo chini ya majumba yake ya kifahari yapita mito. Huko ni kufaulu kukubwa

    [12] Hakika malipizo ya Mola wako kwa maadui Zake na mateso Yake juu yao ni mazito

    [13] Ndiye Yeye Mwenye kuanzisha kuumba na kisha kurudisha

    [14] Ndiye Yeye Mwingi wa kusamehe kwa wenye kutubia, Mwingi wa mapenzi kwa wanaoikurubisha kwake

    [15] Mwenye Arshi tukufu

    [16] Mfanya Alitakalo: hakuna kitu Anachotaka kiwe kisiwe

    [17] Je, ewe Mtume, imekufikia habari ya makundi yaliyokufuru na kukanusha Mitume walioletwa, ya

    [18] Firauni na Thamūd, misiba na adhabu iliyowashukia? Hawakuzingatia kwa habari hiyo

    [19] Bali waliokufuru waendelea kukanusha kwao, kama walivyokuwa waliokuja kabla yao

    [20] Na Mwenyezi Mungu Amewazunguka kwa Ujuzi na Uweza Wake, hakuna chenye kufichika Kwake kuhusu wao na vitendo vyao. Hii Qu’ani siyo kama wanavyodai wenye kukanusha katika washirikina kuwa ni mashairi na uchawi ndipo wakaikanusha

    [21] Bali hii ni Qur’ani kubwa iliyo tukufu

    [22] iliyomo kwenye Ubao Uliohifadhiwa, haufikiwi na kubadilishwa wala kupotoshwa

    Anayekuja Usiku

    Surah 86

    [1] Mwenyezi Mungu Anaapa kwa mbingu na nyota yenye kuchomoza usiku

    [2] Na ni lipi lilokujulisha ni ukubwa gani wa nyota hiyo

    [3] Hiyo ni nyota ing’arao na kuzagaa

    [4] Hakuna nafsi yoyote isipokuwa amewakilishwa kwayo Malaika mwenye kuchunguza na kusjili amali zake ili ihesabiwe Siku ya Kiyama

    [5] Basi aangalie binadamu mwenye kukanusha kufufuliwa ameumbwa kwa kitu gani? Ili ajue kuwa kurudisha umbo lake mara ya pili si vigumu kama kuumbwa mara ya kwanza

    [6] Aliumbwa kwa manii yenye kupenyeza ndani ya uzao kwa haraka

    [7] Yatokayo kwenye mgongo wa mwnamume na kifua cha mwanamke

    [8] Hakika yule Aliyemuumba binadamu kwa maji haya ni muweza wa kumrudisha kwenye uhai baada ya kufa

    [9] Siku zitakapofunuliwa wazi siri ziliofichwa na nafsi na kupambanuliwa njema na mbovu

    [10] Binadamu hatakuwa na nguvu ya kuitetea nafsi yake wala hatakuwa na mtetezi wa kumwepushia adhabu ya Mwenyezi Mungu

    [11] Na Anaapa kwa mbingu yenye mvua ya kukaririka

    [12] Na ardhi yenye pasuko za kufanya mimea ichipuke

    [13] Hakika Qur’ani ni neno lenye kupambanua baina ya haki na batili

    [14] Na si upuuzi. Haifai kiumbe kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Akifanya hivyo atakuwa amemshirikisha Mwenyezi Mungu

    [15] Hakika wenye kumkanusha Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na Qur’ani wanafanya vitimbi na mipango ili kuipinga haki na kuitilia nguvu batili

    [16] Na Mimi nafanya vitimbi kuidhihirisha haki ingawa makafiri wanatukia.Usiwe na haraka nao, ewe Mtume, kutaka wateremshiwe adhabu

    [17] Wape muhula uwangojee muda mchache wala usiwafanyie haraka, utaona adhabu itakayowafikia, mateso na maangamivu

    Aliye Juu

    Surah 87

    [1] Takasa Jina la Mola wako Aliyetukuka na kuepukana na mshirika na kila sifa pungufu kwa namna inayonasibiana na utukufu Wake na utakatifu Wake

    [2] Aliyeumba viumbe Akalitengeneza umbo lao na kulifanya zuri

    [3] Na Aliyekadiria kila kitu na kukipeleka njia inayonasibiana nacho

    [4] Na Aliyeotesha nyasi mbiti zenye rangi ya kijani

    [5] Akazifanya baadaye kuwa kavu zilizobadilika rangi

    [6] Tutakusomea, ewe Mtume, hii Qur’ani kisomo ambacho hutakisahau

    [7] Isipokuwa iwapo Mwenyezi Mungu Ataka usahau kwa hekima na maslahi anayoyajua Yeye. Kwani Yeye ni Mjuzi wa yaliyo wazi na yaliyofichika, ya maneno na ya vitendo

    [8] Tutakufanyia mapesi mambo yako yote; miongoni mwayo ni kukusahilishia kubeba majukumu ya utume na kuifanya nyepesi Dini uliyokuja nayo

    [9] Basi wawaidhie kaumu zako, ewe Mtume, kwa namna tulivyokutayarishia ufanye kwenye wahyi ulioletewa, uwaongoze njia yenye kheri na wao na uwahusu kwa mawaidha yako wale wanaotarajiwa kuwaidhika nayo. Wala usijisumbue kuwashauri wale ambao mawidha hayawaathiri isipokuwa kuwatia ujeuri na kuwafanya wayakimbie

    [10] Atanufaika kwa mawaidha anayemcha Mola wke

    [11] na atajiepusha na mawaidha aliye mbaya asiyemuogopa Mola wake

    [12] atakayeingia kwenye Moto wa Jahanamu akiadhibika kwa ukali wake

    [13] Kisha hatakuwa ni mwenye kufa akapumzika wala ni mwenye kuishi akanufaika

    [14] Hakika amefuzu mwenye kuisafisha nafsi yake na tabia mbovu

    [15] na akamtaja Mwenyezi Mungu, akampwekesha, akamuomba, akafanya vitendo vya kumridhisha na akasimamisha Swala kwa nyakati zake kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu na kufuata sheria Aliyoiweka

    [16] Hakika yenu, nyinyi watu, mnafadhilisha pambo la maisha ya kilimwengu juu ya starehe za Akhera

    [17] Na hakika ya mambo ni kuwa nyumba ya Akhera na starehe zake ni bora zaidi kuliko ulimwngu na ni yenye kusalia zaidi

    [18] Haya mlioosimuliwa ndani ya Sura hii ni miongoni mwa yaliyotajwa kimaana katika Kurasa zilizotangulia kuteremshwa kabla ya Qur’ani

    [19] Nazo ni Kurasa za Ibrāhīm na Mūsā, amani ziwashukie

    Ghashia

    Surah 88

    [1] Je, ilikujia,ewe Mtume, habari ya Kiyama chenye vituko venye kuwaenea watu

    [2] Nyuso za Makafiri, Siku hiyo, zitakuwa zimenyongeka kwa adhabu

    [3] Zishughulishie, zimechoka na kutaabika

    [4] Zinachomwa kwa Moto wenye kuwaka kwa ukali

    [5] Zitanyweshwa maji ya chemchemi yenye moto sana

    [6] Watu wa Motoni hawatakuwa na chakula isipokuwa kinachotoka kwenye mti wa miba ilioshikana na chini. Ni kibaya sana chakula hiko na ni kichafu mno

    [7] Hakimnoneshi mwenye kukila, awapo amekonda, wala hakimuondolei njaa, awapo na njaa

    [8] Nyuso za Waumini, siku ya Kiyama, zitakuwa kwenye neema

    [9] Kwa kuwa zilijishughulisha ulimwenguni kumtii Mwenyezi Mungu na kuridhika na Akhera

    [10] Zitakuwa kwenye Pepo ya daraja ya juu

    [11] Hutasikia humo hata neno moja la upuuzi

    [12] Ndani yake kuna chemchemi yenye kuteremka maji yake

    [13] Ndani yake mna vitanda vilioangatika

    [14] na vikombe vilivyotayarishwa kwa wenye kunywa

    [15] na mito iliyopangwa, mmoja baada ya mwingine

    [16] na mazulia mengi yaliyotandikwa

    [17] Kwani, hawa makafiri wenye kukanusha, hawaangalii ngamia namna walivyoumbwa kiajabu

    [18] Na mbingu namna zlizoinuliwa juu kwa namna ya kupendeza

    [19] Na milima namna iliyoimarishwa ukapatikana uthabiti na utulivu wa ardhi

    [20] Na ardhi namna ilivyotandikwa na kutayarishwa

    [21] Basi wawaidhie, ewe Mtume, wale wenye kupa nyongo yale uliyotumilizwa kwayo wala usihuzunike kwa kupa mgongo kwao

    [22] Kwani wewe ni muwaidhiaji kwao, na si juu yako kuwalazimisha kuamini

    [23] Lakini yule mwenye kuyapa mgongo makumbusho na mawaidha na akawa mkakamavu kwenye ukafiri wake

    [24] Mwenyezi Mungu Atamuadhibu adhabu kali Motoni

    [25] Hakika wao watarudi kwetu baada ya kufa

    [26] Kisha ni juu yetu kuwalipa kwa waliyoyafanya

    Alfajiri

    Surah 89

    [1] Mwenyezi Mungu Anaapa kwa wakati wa alfajiri

    [2] na masiku kumi ya kwanza ya Mfungotatu na kwa kile kilichoyafanya yawe matukufu

    [3] kwa kila idadi igawanyikayo na isiyogawanyika

    [4] kwa usiku upitapo na giza lake

    [5] Kwani hakuna katika kiapo kiliyotajwa chenye kukinaisha kwa mwenye akili

    [6] Huoni, ewe Mtume, vipi Mola wako

    [7] Alivyoiangamiza kaumu ya Ād'. kabila la Irama lenye nguvu na majengo yaliyoinuliwa juu ya vipia

    [8] ambalo hakukuumbwa mfano wake katika miji, kwa ukubwa wa miili na wingi wa nguvu

    [9] Na vipi Alivyowafanya Thamūd, kaumu ya Ṣāliḥ, ambao waliweza kuchonga jabali na kufanya nyumba ndani yake

    [10] Na vipi Alivyomfanya Firauni, mfalme wa Misri, aliyekuwa na askari waliouhami ufalme wake na kuutilia nguvu

    [11] Hawa ndio waliokitumia nguvu na kudhulumu mijini

    [12] Wakaeneza humo, kwa dhuluma zao, uharibifu

    [13] Mwenyezi Mungu Akawamiminia adhabu kali

    [14] Hakika Mola wako,ewe Mtume, Anamwangalia mwenye kumuasi kwa kumpa muhula kidogo, kisha Humpatiliza kwa uwezo na ushindi

    [15] Huyu binadamu, Mola wake Anapompa mtihani wa neema, Anapomkunjulia riziki yake na kumpa maisha mazuri, huwa akidhani kuwa hayo ni kwa kuwa yeye ana cheo kwa Mola wake na huwa akisema :»Mola wangu Amenitukuza.»

    [16] Na Anapomuonja na Akambania riziki yake, huwa akidhani kuwa hayo ni kwa kuwa yeye amefanywa mnyonge na Mwenyezi Mungu na huwa akisema: «Mola wangu Amenifanya mnyonge.»

    [17] Hali ya mambo si kama anavyodhania binadamu huyu, kwani mtu hutukuzwa kwa kumtii Mwenyzi Mungu na hufanywa mnyonge kwa kumuasi Mwenyezi Mungu. Na nyinyi hamwakirimu mayatima na kuwatendea wema

    [18] Wala hamhimizani kulisha maskini

    [19] Na mnakula haki za watu, katika kurithi, kwa pupa

    [20] Na mnapenda mali kupita kiasi

    [21] Basi hali zenu zisiwe namna hiyo. Kumbukeni pindi ardhi itakapotikiswa na kuvunjwavunjwa

    [22] Na Akaja Mola wako kutoa uamuzi kwa waja Wake hali Malaika wamepiga safu

    [23] Na ukaletwa, Siku Hiyo kubwa, moto wa Jahanamu. Hiyo ndiyo Siku kafiri atakumbuka na kutubia. Kutamfalia nini sasa kukumbuka kwake na kutubia, na yeye katika ulimwengu alikuwa ameyapuuza hayo, na wakati wake umekwisha kupita

    [24] Atakuwa akisema: ‘Laiti mimi nilitanguliza ulimwenguni amali zenye kunifaa katika maisha yangu ya Akhera’

    [25] Katika Siku Hiyo ngumu yenye vituko, hakuna atakaye kuweza kuadhibu kama adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa anayemuasi

    [26] Na hakuna atakaye kuweza kufunga kama kifungo Chake wala kufikia hadi yake

    [27] Ewe nafsi iliyotulia kwa kumtaja Mwenyezi Mungu, kumwamini Yeye na kuamini starehe ya Pepo Aliyowaandalia waumini

    [28] Rudi kwa Mola wako hali ya kuridhika na takrima ya Mwenyezi Mungu kwako na hali ya kuwa Mwenyezi Mungu Ameridhika na wewe

    [29] Ingia miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu walio wema

    [30] na ingia kwenye Pepo yangu

    Mji

    Surah 90

    [1] Mwenyezi Mungu Anaapa kwa mji huu mtakatifu wa Makkah

    [2] Na wewe, ewe Nabii, ni mkazi wa mji huu mtakatifu

    [3] Na Anaapa kwa mzazi wa wanaadamu, ambaye ni Ādam, amani imshukie, na kilichozalikana na yeye

    [4] Hakika Tumemuumba binadamu katika usumbufu na shida za kilimwengu

    [5] Kwani anadhani kwa mali aliyoyakusanya kuwa Mwenyezi Mungu Hatakuwa na uwezo juu yake

    [6] Huwa akisema kwa kujigamba: «Nimetumia mali mengi.»

    [7] Kwani anadhani, kwa kitendo chake hiko, kuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kushinda, Hamuoni wala hatamhesabu juu ya kubwa na dogo

    [8] Kwani hatukumpa macho mawili ya kuonea

    [9] ulimi na midomo miwili ya kusemea

    [10] na kumfafanulia njia mbili: ya kheri na ya shari

    [11] Basi ajiepushe na janga la Akhera kwa kutoa mali yake ili aokoke

    [12] Ni kitu gani kilichojulisha ni lipi hilo janga la Akhera na ni mambo gani yenye kusaidia kujiepusha nalo

    [13] Ni kuacha huru shingo iliyoamini kuikomboa na utumwa

    [14] Au kulisha, wakati wa shida ya njaa

    [15] yatima mwenye ujamaa, ili ipatikane fadhila ya sadaka na ya kuunga kizazi

    [16] au masikini asiyekuwa na kitu

    [17] Kisha akawa, baada ya kufanya amali njema zilizotajwa, ni miongoni mwa waliotakasa Imani yao kwa Mwenyezi Mungu, wakausiana kusubiri juu ya kumtii Mwenyezi Mungu kwa kufuata maamrisho Yake na kujiepusha na vitendo vya kumuasi na wakausiana kuwahurumia viumbe

    [18] Wenye kufanya hayo ndiwo watu wa kulia ambao watapelekwa Siku ya Kiyama upande wa kulia kuelekea Peponi

    [19] Na wale waliokanusha Qur’ani ndio ambao watapelekwa, Siku ya Kiyama, upande wa kushoto kuelekea Motoni

    [20] Malipo yao ni Moto wa Jahanamu wenye kuwafinika na kuwaziba

    Jua

    Surah 91

    [1] Mwenyezi Mungu Anaapa kwa jua na mchana wake na mwangaza wake wa asubuhi

    [2] Na kwa mwezi unapolifuata wakati wa kucha na kutwa

    [3] Na kwa mchana unapoliondoa giza na kulifunua

    [4] Na kwa usiku unapoifinika ardhi ikawa giza

    [5] Na kwa mbingu na kujengeka kwake kiimara

    [6] Na kwa ardhi na kutandikika kwake

    [7] Na kwa kila nafsi na namna Mwenyezi Mungu alivyoikamilisha umbo lake ili itekeleze kazi iliyoumbiwa nayo

    [8] Akaibainishia njia ya shari na njia ya kheri

    [9] Amefaulu mwenye kuisafisha na kuikuza kwa kheri

    [10] Na ameingia kwenye hasara mwenye kuitia nafsi yake kwenye maasia

    [11] Kabila la Thamūd lilimkanusha Nabii wake kwa kuvama kwenye uasi

    [12] Pindi walipotoka wabaya zaidi wa kabila hilo kumchinja Ngamia. Mtume wa Mwenyezi Mungu’ Ṣāliḥ, amani imshukie

    [13] akawaambia: «Tahadharini kumgusa kwa ubaya ngamia ambaye ni miujiza ilioletwa na Mwenyezi Mungu kwenu inayoonyesha ukweli wa Nabii wenu, na msizuie kinywaji chake. Yeye ana siku yake ya kunywa na nyinyi mna siku yenu maalumu ya kunywa.» Hilo likawa zito kwao

    [14] Wakamkanusha na kulipuza onyo lake wakamchinja.Mola wao Akawafinika kwa adhabu, akaisawazisha juu yao na hakuna aliyeweza kuponyoka

    [15] Wala Haogopi, Mwenye uwezo uliotukuka, athari ya adhabu kali Aliywateremshia

    Usiku

    Surah 92

    [1] Mwenyezi Mungu Anaapa kwa usiku unapoifinika ardhi na vilivyoko juu yake kwa giza lake

    [2] Na kwa mchana unapofunuka mwangaza wake kutoka kwenye giza la usiku

    [3] Na kwa kuumba mbea mbili: ya kiume na ya kike

    [4] Kuwa vitendo vyenu vinatofautiana: kuna wenye kufanyia dunia na wenye kufanyia Akhera

    [5] Ama mwenye kutoa kwenye mali yake, akamcha Mwenyezi Mungu katika huko kutoa

    [6] akaamini «Lā Ilāha Illā Allāh» na yanayotakiwa na Imani hiyo na akaamini malipo yanayofungamana nayo

    [7] Tutamuongoza na kumuafikia njia za kheri na wema na kumsahilishia mambo yake

    [8] Na ama mwenye kuyafanyia ubakhili mali yake, asiwe na haja ya malipo ya Mola wake

    [9] akakanusha neno la «Lā Ilāha Illā Allāh» na yanayotakiwa na neno hilo na akakanusha malipo yanayofungamana nalo

    [10] Tutamnyoshea njia za mateso

    [11] Wala hayatamfaa yeye mali yake aliyoyafanyia ubakhili atakapotumbukia Motoni

    [12] Ni juu Yetu, kwa fadhila Zetu na busara Yetu, kueleza njia ya uongofu yenye kufikisha kwa Mwenyezi Mungu na ya upotevu

    [13] Na Sisi Tuna mamlaka ya maisha ya Akhera na maisha ya ulimwenguni

    [14] Ndipo nikawaonya , enyi watu, na kuwatisha moto wenye kuwaka, nao ni moto wa Jahanamu

    [15] Hataingia Moto huo isipokuwa aliyekuwa mbaya sana. Mwenye kumkanusha Nabii Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

    [16] na akakataa kumwamini na kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake

    [17] Na ataepushwa nao mchaji Mwenyezi Mungu sana

    [18] Ambaye hutoa mali yake kwa kutaka nyongeza za kheri

    [19] kutoa Kwake si kwa kulipa zema alizofanyiwa na mtu

    [20] Lakini anatoa kwa kutaka uso wa Mola wake na radhi zake. Basi Mwenyezi Mungu atampa

    [21] huko Peponi, malipo ya kumridhisha

    Asubuhi

    Surah 93

    [1] Mwenyezi Mungu Anaapa kwa wakati wa dhuha, na uliokusudiwa ni wakati wa mchana mzima

    [2] Na kwa usiku utuliapo na viumbe na likashadidi giza lake. Mwenyezi Mungu Huapa kwa Atakacho katika viumbe vyake. Ama kiumbe, hafai kuapa kwa asiyekuwa Muumba wake. Kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu ni ushirikina

    [3] Hakukuwacha Mola wako, ewe Mtume, wala Hakukuchukia kwa kuchelewesha kukuteremshiaWahyi

    [4] Na Nyumba ya Akhera ni bora kwako kuliko nyumba ya ulimwengu

    [5] Na Atakupa Mola wako, ewe Mtume, neema ya kila sampuli uridhike

    [6] Kwani Hakukupata, kabla ya hapo, kuwa ni yatima Akakukusanya na kukutunza

    [7] Na Akakupata hujui Kitabu wala Imani, Akakufundisha yale amabayo ulikuwa huyajui na akakuafikia kufanya amali bora

    [8] Na Akakupata masikini, Akakuletea riziki yako na Akakutajirisha kwa kutosheka na kusubiri

    [9] Basi yatima usimtende ubaya

    [10] Na muombaji usimkaripie, bali mlishe na umtimizie haja yake

    [11] Na ama neema ya Mola wako Aliyokuneemesha nayo izungumze

    Kufurahisha

    Surah 94

    [1] Kwani Hatukukunjulia, ewe Mtume, kifua chako kwa sheria za Dini, kulingania watu kwa Mwenyezi Mungu na kujipamba kwa tabia nzuri

    [2] Tukakuondolea mazito yako yaliyoemea mgongo wako

    [3] na Tukakuweka, kwa matukufu Tuliyokuneemesha

    [4] kwenye cheo cha juu

    [5] Usirudi nyuma katika kueneza ujumbe uliotumwa nao kwa makero ya maadui zako. Kwani kwenye dhiki kuna faraji

    [6] Hakika kwenye dhiki kuna faraji

    [7] Basi utakapomaliza mambo ya kidunia na shughuli zake jipinde kwa kufanya ibada

    [8] Na kwa Mola wako Peke Yake weka matumaini yako

    Tini

    Surah 95

    [1] Mwenyezi Mungu Anaapa kwa tini na zaituni, nayo ni miongoni mwa matunda yanayojulikana

    [2] Na Anaapa kwa jabali la Ṭūr Sīnā’ ambalo Mwenyezi Mungu Alisema na Mūsā juu yake

    [3] Na Anaapa kwa Mji huu wa amani, usiokuwa na mambo ya kutisha. Nao ni mji wa Makkah, chimbuko la Uislamu

    [4] Hakika Tumemuumba binadamu katika sura nzuri

    [5] Kisha Tutampeleka Motoni akiwa hakumtii Mweyezi Mungu na hakuwafuata Mitume

    [6] Isipokuwa wale walioamini na wakafanya amali njema; wao watakuwa na malipo makubwa yasiyokatika wala kupungua

    [7] Ni lipi linalokupelekea wewe, ewe binadamu, kukanusha kufufuliwa na kulipwa, hali ya kuwa kuna dalili wazi kwamba Mwenyezi Mungu Ana uweza wa kufanya hayo

    [8] Je, Hakuwa Mwenyezi Mungu , Ambaye Ameiweka Siku hii kutoa uamuzi baina ya watu, ni muadilifu zaidi ya wanaosifika kuwa ni waadilifu katika kila Alichokiumba? Kwani? Alikuwa. Basi wataachwa viumbe rebe: hawaamrishwi wala hawakatazwi wala hawalipwi kwa mema wala hawateswi kwa mabaya? Hilo si sahihi wala haliwi

    Alaki

    Surah 96

    [1] Soma, ewe Nabii, Qur’ani uliyoteremshiwa ukianza kwa Jina la Mola wako Aliyepwekeka kwa kuumba

    [2] Aliyemuumba kila binadamu kwa pande la damu nzito nyekundu

    [3] Soma, ewe Nabii, kile ulichoteremshiwa, na Mola wako ni Mwingi wa wema, Mwingi wa ukarimu

    [4] Aliyewafundisha viumbe vyake kuandika kwa kalamu

    [5] Alimfundisha binadamu vitu ambavyo hakuwa akivijua. Akamtoa kwenye giza la ujinga, Akampeleka kwenye nuru ya elimu

    [6] Kweli, binadamu hukiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu

    [7] akijiona ametosheka kwa utajiri wake

    [8] Basi, ajue kila mwenye kutupa mipaka kuwa mwisho atarudi kwa Mwenyezi Mungu Ambaye Atamlipa kila binadamu kwa alilolitenda

    [9] Je, umeona ujeuri wa ajabu zaidi kuliko wa mtu huyu, Abu jahl

    [10] Anayemkataza mja wetu, Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, anapomsalia Mola wake

    [11] Waonaje iwapo mwenye kukatazwa kusali yuko uongofuni, vipi anamkataza

    [12] Au iwapo anaamrisha mwigine kumcha Mungu, vipi anamkataza hilo

    [13] Waonaje iwapo huyu mwenye kukataza anakanusha lile alinganiwalo kwalo na kulipa mgongo

    [14] hajui kuwa Mwenyezi Mungu anaona kila analolifanya

    [15] Basi mambo si kama anvyodai Abu Jahl. Na asipokomeka na ushindani alionao na udhia wake, Tutamshika upaa wake kwa nguvu na kumtia Motoni

    [16] Upaa wake ni upaa wenye maneno ya urongo na vitendo vya makosa

    [17] Basi na awalete, mtupaji mipaka huyu, watu wa baraza ili wamsaidiye

    [18] Sisi Tutawaita Malaika wa adhabu

    [19] Mambo si kama Abu Jahl anavyoyadhania. Yeye, ewe Mtume, hawezi kukufanya lolote la kukudhuru Usimfuate kwa lile alilokuitia la kuwa uache Swala, bali msujudie Mola wako na uwe karibu na Yeye kwa kujipendekeza Kwake kwa kumtii

    Kadar

    Surah 97

    [1] Sisi Tumeiteremsha Qur’ani katika usiku wa cheo na utukufu , nao ni moja wa masiku ya mwezi wa Ramdhani

    [2] Na nilipi liliokujulisha, ewe Mtume, ni upi usiku wa cheo na utukufu

    [3] Usiku wa cheo na utukufu ni bora fadhila zake kuliko fadhila za miezi elfu moja isiyokuwa usiku huo

    [4] Usiku huo hushuka Malaika na Jibrili, amani iwashukie, kwa ruhusa ya Mola wao kwa kila jambo Alilolikadiria liwe mwaka huo

    [5] Usiku huo wote ni amani, hakuna shari, mpaka kutokea alfajiri

    Bayyina

    Surah 98

    [1] Hawakuwa wenye kukufuru miongoni mwa Mayhudi na Wanaswara na washirikina ni wenye kuacha ukafiri wao mpaka uwajilie wao ushahidi walioahidiwa katika vitabu vilivyopita

    [2] Nao ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, atakayewasomea Qur’ani iliyomo kwenye kurasa safi

    [3] Ndani ya kurasa hizo mna habari za kweli na amri za uadilifu zenye kuongoza kwenye haki na kwenye njia ilionyoka

    [4] Na hawakutofautiana wale waliopewa Kitabu, miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara, juu ya kuwa Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ni Mtume wa kweli, kwa sifa zake waliokuwa wakiziona katika vtabu vyao isipokuwa baada ya kuwathibitikia kuwa yeye ndiye Nabii waliyoahidiwa katika Taurati na Injili. Walikuwa wanakubali , kwa umoja wao, kuwa unabii wake ni wa kweli. Lakini alipotumilizwa waliukanusha na wakatofautiana

    [5] Na hawakuamrishwa katika sheria zote zilizopita isipokuwa ni wamuabudu Mwenyezi Mungu Peke Yake, wakikusudia kwa ibada yao kupata Radhi Zake, hali ya kuepuka upande wa ushirikina na kuelekea kwenye Imani, wasimamishe Swala na watoe Zaka. Kufanya hayo ndio Dini iliyolingana , nayo ni Uislamu

    [6] Hakika wale waliokufuru miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara na Washirikina, mateso yao ni Moto wa Jahanamu. Watakuwa ni wenye kukaa milele humo. Wao ndio viumbe waovu kabisa

    [7] Hakika wale waliomuamini Mwenyezi Mungu, wakamfuata Mtume wake na wakafanya amali njema, wao ndio bora wa viumbe

    [8] Malipo yao , mbele ya Mola wao Siku ya Kiyama, ni Pepo ya makazi na utulivu yenye upeo wa uzuri, ambayo chini ya majumba yake ya fahari inapita mito; watakaa milele humo. Mwenyezi Mungu Ameridhika nao Akakubali amali zao njema. Na wao wameridhika na Yeye kwa maandalio Aliyowafanyia ya aina mbalimbali za takrima. Malipo mazuri hayo ni ya aliyemuogopa Mweyezi Mungu na akajiepusha na maasia

    Tetemeko

    Surah 99

    [1] Itakapotikiswa ardhi mtikiso wa nguvu

    [2] Na ikatoa vilivyomo ndani yake: wafu na makandi

    [3] Na akauliza binadamu, kwa babaiko, «Imezukiwa na nini?»

    [4] Siku ya Kiyama ardhi itatoa habari ya mambo iliyofanyiwa ya uzuri na ubaya

    [5] kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Ameiamuru itoe habari ya mambo iliyofanyiwa

    [6] Siku hiyo wataondoka kutoka kwenye kisimamo cha Hesabu wakiwa makundi, ili Mwenyezi Mungu Awaoneshe waliyoyatenda, mazuri na mabaya, na Awalipe kwayo

    [7] Yoyote mwenye kufanya jema wezani wa chungu mdogo atayaona malipo yake Akhera

    [8] Na yoyote mwenye kufanya baya wezani wa chungu mdogo atayaona malipo yake Akhera

    Wanaokimbilia Vita

    Surah 100

    [1] Mwenyezi Mungu Anaapa kwa farasi wenye kwenda shoti katika njia Yake kumkabili adui, wakitoa sauti kwa kasi ya kukimbia. Haifai kwa kiumbe kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu ni ushirikina

    [2] Na wenye kutoa cheche za moto kwa kwato zao ngumu wanapokimbia kwa kasi

    [3] Wenye kushambulia maadui kipindi cha asubuhi

    [4] Wakarusha vumbi kwa mbio zao

    [5] Wakautia kati, kwa kuuzunguka kwa vipando vyao, mkusanyiko wa maadui

    [6] Hakika binadamu ni mkanushaji sana neema za Mola wake

    [7] Na yeye anakubali ukanushaji wake

    [8] Na yeye ana pupa sana la mali

    [9] Kwani binadamu hajui linalomngojea mbele yake, pindi Mwenyezi Mungu Atakapowatoa wafu makaburini waende kuhesabiwa na kulipwa

    [10] Na (kwani yeye hajui) yakatolewa yaliyo ndani ya vifua: mema au maovu

    [11] Hakika Mola wao kwao na kwa amali zao, Siku Hiyo, ni Mtambuzi; hakuna chenye kufichamana Kwake

    Msiba

    Surah 101

    [1] Kiyama chenye kugonga nyoyo za watu kwa vituko vyake

    [2] Ni kitu gani hiko chenye kugonga

    [3] Na ni lipi lililokujulisha ni kipi hiko chenye kugonga

    [4] Siku hiyo watu watakuwa , kwa wingi wao, kugawanyika kwao na kuzunguka kwao, ni kama pandzi walioenea. Nao ni wale wanaojitupa motoni

    [5] Na majabali yatakuwa ni kama pamba yenye rangi tofauti inayochambuliwa kwa mkono ikawa ni mapepe na ikamalizika

    [6] Basi mwenye kuwa mizani za mema yake ni nzito

    [7] atakuwa kwenye maisha ya kuridhika Peponi

    [8] Ama mwenye kuwa mizani za mema yake ni nyepesi na mizani za maovu yake ni nzito

    [9] makazi yake yatakuwa ni Moto wa Jahanamu

    [10] Ni lipi lililokujulisha, ewe Mtume, ni ipi hii Jahanamu inayoitwa «Hāwiyah»

    [11] Ni Moto unaowaka sana kwa kuni ziliomo ndani yake

    Kujifaharisha

    Surah 102

    [1] Kumewashughulisha kujifahiri kwa mali na watoto mkawacha kumtii Mwenyezi Mungu

    [2] Kujishughulisha kwenu na hilo kumeendelea mpaka mkawa makaburini na mkazikwa humo

    [3] Siyo namna hii inatakiwa iwapumbaze kushindana kwa wingi wa mali. Itawadhihirikia kuwa Nyumba ya Akhera ni bora kwenu

    [4] Kisha tahadharini mtajua mwisho mbaya wa kutojishughulisha na Akhera

    [5] Siyo namna hii inatakiwa iwashughulishe kushindana kwa wingi wa mali.Lau mnajua kikweli, mngalirudi nyuma na mngaliangusiliza kuokoa nafsi zenu kutoka kwenye maangamivu

    [6] Mtauona Moto

    [7] Kisha mtauona bila shaka

    [8] Kisha mtaulizwa kuhusu kila aina ya starehe mliyokuwa nayo

    Al Asri

    Surah 103

    [1] Mwenyezi Mungu Anaapa kwa zama

    [2] kwamba wanadamu wako kwenye maangamivu na upungufu. Haifai kwa mja kuapa isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu, kwani kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu ni ushirikina

    [3] Isipokuwa wale waliomuamini Mwenyezi Mungu, wakafanya amali njema, wakausiana wao kwa wao kushikamana na haki, kufanya matendo ya kumtii Mwenyezi Mungu na kusubiri juu yake

    Msengenyaji

    Surah 104

    [1] Shari na maangamivu yatampata kila mwenye kusengenya watu na kuwatukana

    [2] Ambaye hamu yake ni kukusanya mali na kuyahesabu

    [3] Akidhani kuwa mali yake ambayo ameyakusanya yatampa dhamana ya kuishi milele duniani na kuhepa kuhesabiwa

    [4] Anavyodhania sivyo. Atatiwa ndani ya Moto ambao huvunjavunja kila kinachotiwa

    [5] Lipi lililokujulisha, ewe Mtume, ni upi huo Moto unaovunjavunja

    [6] Huo ni Moto wa Mwenyezi Mungu uliowashwa

    [7] Ambao kwa ukali wake hupenyeza miilini ukafikia kwenye nyoyo

    [8] Moto huo umefungiwa juu yao wakiwa wametiwa minyororo

    [9] na pingu ndefu ili wasitoke

    Tembo

    Surah 105

    [1] Je hujui, ewe Mtume, namna Alivyowafanya Mola wako watu wa ndovu: Abraha Mhebeshi na jeshi lake ambalo alikuja nalo ili kuivunja Alkaba tukufu

    [2] Kwani Hakuijaalia mipango yao mibaya waliyoifanya ni yenye kuvunjika na kupita patupu

    [3] Na Aliwapelekea makundi yaliyofuatana

    [4] ya ndege waliokuwa wakiwatupia wao vijiwe vya udongo mkavu mgumu

    [5] Akawapondaponda, wakawa ni kama majani makavu yaliyoliwa na wanyama na halafu kutupwa

    Quraishi

    Surah 106

    [1] Oneni ajabu ya mazowea ya Makureshi, amani walionayo, kuwaendea uzuri mambo yao

    [2] kupangika na kusahilika misafara yao ya kwenda Yamani kipindi cha kusi na kwenda Shamu kipindi cha kaskazi, ili kuleta vitu wanavyohitajia

    [3] Basi, wamshukuru na kumuabudu Bwana wa Nyumba hii ya Alkaba, Ambaye kwa ajili Yake wametukuzwa, na wampwekeshe na kumtakasia ibada

    [4] Ambaye Amewapa wao chakula wakati wa njaa kali na akawapa amani na utulivu kutokana na kicho kikubwa na babaiko

    Msaada

    Surah 107

    [1] Je, waiona hali ya yule ambaye akanusha kufufuliwa na kulipwa

    [2] Huyo ndiye yule anayemkaripia yatima kwa nguvu akimnyima haki yake kwa sababu ya ususuavu wa moyo wake

    [3] Na wala hawahimizi wengine kulisha masikini. Vipi yeye mwenyewe atamlisha

    [4] Basi adhabu kali itawafikia wenye kusali

    [5] ambao wameghafilika na Swala zao: hawazisimamishi kama ipasavyo wala hawazisali kwa nyakati zake

    [6] Ambao huonyesha watu amali zao za kheri kwa njia ya ria

    [7] Na wanakataa kuwaazima watu vitu ambavyo hawadhuriki kwa kuviazima, kama vyombo vya kutumia na vinginevyo. Wao hawakujifanyia wema nafsi zao kumuabudu Mola wao wala hawakuwafanyia wema viumbe Vyake

    Al Kauthar

    Surah 108

    [1] Sisi tumekupa, ewe Nabii, kheri nyingi za dunia na Akhera, miongoni mwazo ni mto wa Kauthar ulioko Peponi ambao pambizo zake ni mahema ya lulu na mchanga wake ni miski

    [2] Basi, mtakasie Mola wako ibada yako yote na uchinje mnyama wako kwa ajili Yake, Peke Yake, pamoja na kutaja jina Lake

    [3] Mwenye kukutukia wewe na kuyatukia uliyokuja nayo ya uongofu na nuru ndiye itakayokatika athari yake na yeye mwenyewe kukatiwa kila kheri

    Makafiri

    Surah 109

    [1] Sema, ewe Mtume, kuwaambia waliokufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake: «Enyi wenye kumkanusha Mwenyezi Mungu

    [2] «Mimi siabudu mnavyoviabudu miongoni mwa masanamu na waungu wa urongo

    [3] «Wala nyinyi si wenye kuabudu Mola Mmoja ninayemuabudu Ambaye ndiye Anayestahiki kuabudiwa

    [4] «Wala mimi si mwenye kuabudu mnavyoviabudu miongoni mwa masanamu na waungu wa urongo

    [5] «Wala nyinyi si wenye kuabudu mbeleni ninayemuabudu.» Aya hii imeteremka juu ya watu makhsusi miongoni mwa washirikina ambao Mwenyezi Mungu Alijua kuwa hawataamini kabisa

    [6] «Nyinyi mna dini yenu mnayoiamini na mimi nina Dini yangu ambayo sitaki nyingine.»

    Nusra

    Surah 110

    [1] Utakapotimia kwako , ewe Mtume, ushindi juu ya makafiri wa Kikureshi na ukafutahi Makkah

    [2] Na ukaona watu wengi wanaingia kwenye Dini ya Mwenyezi Mungu makundi kwa makundi

    [3] Yatakapotokea hayo, jitayarishe kukutana na Mola Wako kwa kumtakasa na kumhimidi na kumuomba msamaha kwa wingi. Kwani Yeye ni Mwingi wa kuwakubalia toba wenye kumsabihi na kumuomba msamaha, kwa kuwasamehe na kuwarehemu

    Moto

    Surah 111

    [1] Imehasirika mikono miwili ya Abu Lahab, na yeye mwenyewe ameangamia, kwa kumuudhi Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie. Hasara ya Abu Lahab ilithubutu

    [2] Hayakumfalia kitu mali yake na watoto wake. Kwani hivyo havitamkinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu pindi ikimshukia

    [3] Ataingia kwenye Moto wenye kuroroma

    [4] yeye na mke wake ambaye alikuwa akibeba miba na kuiweka kwenye njia anayopita Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ili kumuudhi

    [5] Kwenye shingo yake patakuwa na kamba imara ya lifu gumu lilio kavu; atabebewa nayo kwenye Moto wa Jahanamu, kisha atarushwa nayo mpaka chini

    Ikhlasi

    Surah 112

    [1] Sema, ewe Mtume, «Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu Aliyepwekeka kwa ustahiki wa kuabudiwa, uumbaji na utakatifu wa Majina na Sifa, Asiye na mshirika katika hayo

    [2] «Mwenyezi Mungu Ambaye Peke Yake Ndiye Mwenye kukusudiwa kwa kukidhi haja na matakwa

    [3] «Hana mwana wala mzazi wala mke

    [4] «Wala hakuna yoyote katika viumbe Vyake mwenye kufanana wala kushabihiyana na Yeye katika Majina Yake, Sifa Zake wala vitendo Vyake.»

    Al Falaqi

    Surah 113

    [1] Sema, ewe Mtume, «Najilinda na kutaka hifadhi kwa Bwana wa asubuhi

    [2] «Kutokana na shari la viumbe na udhia wao

    [3] «Na shari la usiku wenye giza lingi ungiapo na ujikitapo na mashari na maudhi mbalimbali yaliyomo ndani yake

    [4] «Na shari la wchawi wenye kupuliza kwenye mafundo wanayoyafunga kwa lengo la kuroga

    [5] «Na shari la hasidi mwenye kutukia watu, anapowahusudu na kuwadhuru, kwa kutaka neema za Mwenyezi Mungu Aliyewaneemesha ziwaondokee.»

    An-Naas

    Surah 114

    [1] Sema, ewe Mtume, «Ninajilinda na kutaka hifadhi kwa Bwana wa watu, Mwenye uweza, Peke Yake, wa kulirudisha shari lao

    [2] «Mfalme wa watu, Mwenye kupeleka mambo yao yote Anavyotaka, Aliye Mkwasi kutowahitajia

    [3] «Mola wa watu, Ambaye hapana mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye

    [4] «Kutokana na udhia wa shetani ambaye hutia watu wasiwasi wanapoghafilika na hujificha atajwapo Mwenyezi Mungu

    [5] «Mwenye kupenyeza shari na shaka kwenye vifua vya watu

    [6] «Miongoni mwa mashetani wa kijini na kibinadamu.»