Back to Languages

Swahili - Chapter 3 - Al-Imran

Translation by Ali Muhsin Al Barwani — Permalink

Verse 1 — Surah Al-Imran 3:1

Verse 2 — Surah Al-Imran 3:2

Mwenyezi Mungu, hakuna mungu ila Yeye Aliye Hai, Msimamizi wa yote milele

Verse 3 — Surah Al-Imran 3:3

Amekuteremshia Kitabu kwa haki, kinacho sadikisha yaliyo kuwa kabla yake. Na aliteremsha Taurati na Injili

Verse 4 — Surah Al-Imran 3:4

Kabla yake, ziwe uwongofu kwa watu. Na akateremsha Furqani (Upambanuo). Hakika walio zikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu watakuwa na adhabu kali. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye kulipa

Verse 5 — Surah Al-Imran 3:5

Hakika Mwenyezi Mungu hakifichiki chochote kwake, duniani wala mbinguni

Verse 6 — Surah Al-Imran 3:6

Yeye ndiye anaye kuundeni ndani ya matumbo ya wazazi kwa namna apendayo. Hapana mungu ila Yeye, Mwenye nguvu na Mwenye hikima

Verse 7 — Surah Al-Imran 3:7

Yeye ndiye aliye kuteremshia Kitabu hichi. Ndani yake zimo Aya muhkam, zenye maana wazi. Hizo ndizo msingi wa Kitabu hichi. Na ziko nyengine za mifano. Ama wale ambao nyoyoni mwao umo upotovu wanafuata zile za mifano kwa kutafuta fitna, na kutafuta maana yake; na wala hapana ajuaye maana yake ila Mwenyezi Mungu. Na wale wenye msingi madhubuti katika ilimu husema: Sisi tumeziamini, zote zimetoka kwa Mola wetu Mlezi. Lakini hawakumbuki hayo isipo kuwa wenye akili

Verse 8 — Surah Al-Imran 3:8

(Na hao husema): Mola wetu Mlezi! Usizipotoe nyoyo zetu baada ya kwisha tuongoa, na utupe rehema itokayo kwako. Hakika Wewe ndiye Mpaji

Verse 9 — Surah Al-Imran 3:9

Mola wetu Mlezi! Wewe ndiye Mkusanyaji wa watu kwa Siku isiyo na shaka ndani yake. Hakika Mwenyezi Mungu havunji miadi yake

Verse 10 — Surah Al-Imran 3:10

Kwa hakika wale walio kufuru hazitowafaa kitu kwa Mwenyezi Mungu mali zao, wala watoto wao; nao hao ndio kuni za Motoni

Verse 11 — Surah Al-Imran 3:11

Kama yaliyo wapata watu wa Firauni na wale walio kuwa kabla yao. Walikanusha Ishara zetu, basi Mwenyezi Mungu aliwashika kwa madhambi yao; na Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu

Verse 12 — Surah Al-Imran 3:12

Waambie walio kufuru: Karibuni mtashindwa na mtakusanywa, mtiwe kwenye Jahannam; nako huko ni makao mabaya kabisa

Verse 13 — Surah Al-Imran 3:13

Hakika ilikuwa ni Ishara kwenu katika yale majeshi mawili yalipo pambana. Jeshi moja likipigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na jingine kafiri likiwaona zaidi kuliko wao mara mbili, kwa kuona kwa macho. Na Mwenyezi Mungu humuunga mkono amtakaye kwa nusura yake. Hakika katika hayo yapo mazingatio kwa wenye macho

Verse 14 — Surah Al-Imran 3:14

Watu wamepambiwa kupenda matamanio ya wanawake, na wana, na mirundi ya dhahabu na fedha, na farasi asili, na mifugo, na mashamba. Hayo ni starehe ya maisha ya duniani; na kwa Mwenyezi Mungu ndio kwenye marejeo mema

Verse 15 — Surah Al-Imran 3:15

Sema: Nikwambieni yaliyo bora kuliko hayo? Kwa wachamngu ziko Bustani kwa Mola wao zipitazo mito kati yake. Watadumu humo, na wake walio takaswa, na wanazo radhi za Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona waja wake

Verse 16 — Surah Al-Imran 3:16

Ambao husema: Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tumeamini, basi tufutie madhambi yetu, na tuepushe na adhabu ya Moto

Verse 17 — Surah Al-Imran 3:17

Wanao subiri, wanao sema kweli, na wat'iifu, na wanao toa sadaka, na wanao omba maghafira kabla ya alfajiri

Verse 18 — Surah Al-Imran 3:18

Mwenyezi Mungu, na Malaika, na wenye ilimu, wameshuhudia kuwa hakika hapana mungu ila Yeye, ndiye Mwenye kusimamisha uadilifu; hapana mungu ila Yeye Mwenye nguvu na Mwenye hikima

Verse 19 — Surah Al-Imran 3:19

Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu. Na walio pewa Kitabu hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa sababu ya uhasidi ulio kuwa baina yao. Na anaye zikataa Ishara za Mwenyezi Mungu basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu

Verse 20 — Surah Al-Imran 3:20

Na pindi wakikuhoji, basi sema: Mimi nimeusalimisha uso wangu kumwelekea Mwenyezi Mungu, na kadhaalika walio nifuata. Na waambie walio pewa Kitabu na wasio na kisomo: Je! Mmesilimu? Wakisilimu basi wameongoka. Na wakikengeuka basi juu yako ni kufikisha ujumbe tu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona waja wake

Verse 21 — Surah Al-Imran 3:21

Hakika wanao zikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, na wakawauwa Manabii pasipo haki, na wakawauwa watu waamrishao Haki wabashirie adhabu kali

Verse 22 — Surah Al-Imran 3:22

Hao ndio ambao vitendo vyao vimeharibika duniani na Akhera. Nao hawatapata wa kuwanusuru

Verse 23 — Surah Al-Imran 3:23

Huwaoni wale walio pewa sehemu ya Kitabu? Wanaitwa kukiendea Kitabu cha Mwenyezi Mungu ili kiwahukumu baina yao; kisha baadhi yao wanageuka wanakikataa

Verse 24 — Surah Al-Imran 3:24

Hayo ni kwa sababu walisema: Hautatugusa Moto isipo kuwa kwa siku chache tu. Na yakawadanganya katika dini yao yale ambayo wenyewe waliyo kuwa wakiyazua

Verse 25 — Surah Al-Imran 3:25

Basi itakuwaje tutakapo wakusanya Siku ambayo haina shaka kuja kwake? Na kila nafsi italipwa kama ilivyo chuma, bila ya kudhulumiwa

Verse 26 — Surah Al-Imran 3:26

Sema: Ewe Mwenyezi Mungu uliye miliki ufalme wote! Wewe humpa ufalme umtakaye, na humwondolea ufalme umtakaye, na humtukuza umtakaye, na humuangusha umtakaye. Kheri yote iko mikononi mwako. Hakika Wewe ni Muweza wa kila kitu

Verse 27 — Surah Al-Imran 3:27

Wewe huingiza usiku katika mchana, na huuingiza mchana katika usiku. Na humtoa hai kutokana na maiti, na humtoa maiti kutokana na aliye hai. Na unamruzuku umtakaye bila ya hisabu

Verse 28 — Surah Al-Imran 3:28

Waumini wasiwafanye makafiri kuwa wapenzi wao badala ya Waumini. Na anaye fanya hivyo, basi hatakuwa chochote mbele ya Mwenyezi Mungu. Ila ikiwa kwa ajili ya kujilinda na shari zao. Na Mwenyezi Mungu anakuhadharisheni naye. Na marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu

Verse 29 — Surah Al-Imran 3:29

Sema: Mkificha yaliyomo vifuani mwenu au mkiyafichua Mwenyezi Mungu anayajua; na anayajua yaliyomo mbinguni na yaliyomo duniani. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu

Verse 30 — Surah Al-Imran 3:30

Siku ambayo kila nafsi itakuta mema iliyo yafanya yamehudhurishwa, na pia ubaya ilio ufanya. Itapenda nafsi lau kungekuwako masafa marefu baina ya ubaya huo na yeye. Na Mwenyezi Mungu anakuhadharisheni naye. Na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake

Verse 31 — Surah Al-Imran 3:31

Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu

Verse 32 — Surah Al-Imran 3:32

Sema: Mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume. Na wakigeuka basi Mwenyezi Mungu hawapendi makafiri

Verse 33 — Surah Al-Imran 3:33

Hakika Mwenyezi Mungu alimteuwa Adam na Nuhu na ukoo wa Ibrahim na ukoo wa Imran juu ya walimwengu wote

Verse 34 — Surah Al-Imran 3:34

Ni wazao wao kwa wao; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na Mwenye kujua

Verse 35 — Surah Al-Imran 3:35

Alipo sema mke wa Imran: Mola wangu Mlezi! Nimekuwekea nadhiri kilichomo tumboni mwangu kuwa wakfu; basi nikubalie. Hakika Wewe ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua

Verse 36 — Surah Al-Imran 3:36

Basi alipo mzaa alisema: Mola wangu Mlezi! Nimemzaa mwanamke - na Mwenyezi Mungu anajua sana aliye mzaa - Na mwanamume si sawa na mwanamke. Na mimi nimemwita Maryamu. Nami namkinga kwako, yeye na uzao wake, uwalinde na Shet'ani aliye laaniwa

Verse 37 — Surah Al-Imran 3:37

Tena Mola wake Mlezi akampokea kwa mapokeo mema na akamkuza makuzo mema, na akamfanya Zakariya awe mlezi wake. Kila mara Zakariya alipo ingia chumbani kwake alimkuta na vyakula. Basi alimwambia: Ewe Maryamu! Unavipata wapi hivi? Naye akasema: Hivi vinatoka kwa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu

Verse 38 — Surah Al-Imran 3:38

Pale pale Zakariya akamwomba Mola wake Mlezi, akasema: Mola wangu Mlezi! Nipe kutoka kwako uzao mwema. Wewe ndiye unaye sikia maombi

Verse 39 — Surah Al-Imran 3:39

Alipo kuwa kasimama chumbani akisali, Malaika kamnadia: Hakika Mwenyezi Mungu anakubashiria Yahya, ataye kuwa mwenye kusadikisha neno litokalo kwa Mwenyezi Mungu, na ni bwana na mt'awa na Nabii kwa watu wema

Verse 40 — Surah Al-Imran 3:40

Akasema Zakariya: Mola wangu Mlezi! Vipi nitapata mwana na hali ukongwe umenifikia, na mke wangu ni tasa? Akasema: Ndivyo vivyo hivyo, Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo

Verse 41 — Surah Al-Imran 3:41

Akasema: Mola wangu Mlezi! Niwekee alama. Akasema: Alama yako ni kuwa hutasema na watu kwa siku tatu, isipo kuwa kwa kuashiria tu. Na mdhukuru Mola Mlezi wako kwa wingi na mtakase jioni na asubuhi

Verse 42 — Surah Al-Imran 3:42

Na angalia pale Malaika walipo sema: Ewe Maryamu! Kwa hakika Mwenyezi Mungu amekuteuwa, na akakutakasa, na akakutukuza kuliko wanawake wote

Verse 43 — Surah Al-Imran 3:43

Ewe Maryamu! Mnyenyekee Mola Mlezi wako na usujudu na uiname pamoja na wainamao

Verse 44 — Surah Al-Imran 3:44

Hizi ni khabari za ghaibu tunazo kufunulia; nawe hukuwa nao walipo kuwa wakitupa kalamu zao nani wao atamlea Maryamu, na hukuwa nao walipo kuwa wakishindana

Verse 45 — Surah Al-Imran 3:45

Na pale Malaika walipo sema: Ewe Maryamu! Hakika Mwenyezi Mungu anakubashiria (mwana) kwa neno litokalo kwake. Jina lake ni Masihi Isa mwana wa Maryamu, mwenye hishima katika dunia na Akhera, na miongoni mwa walio karibishwa (kwa Mwenyezi Mungu)

Verse 46 — Surah Al-Imran 3:46

Naye atazungumza na watu katika utoto wake na katika utuuzima wake, na atakuwa katika watu wema

Verse 47 — Surah Al-Imran 3:47

Maryamu akasema: Mola wangu Mlezi! Vipi nitampata mwana na hali hajanigusa mwanaadamu? Mwenyezi Mungu akasema: Ndivyo vivyo hivyo, Mwenyezi Mungu huumba apendacho. Anapo hukumu jambo, huliambia: Kuwa! Likawa

Verse 48 — Surah Al-Imran 3:48

Na atamfunza kuandika na Hikima na Taurati na Injili

Verse 49 — Surah Al-Imran 3:49

Na ni Mtume kwa Wana wa Israili kuwaambia: Mimi nimekujieni na Ishara kutoka kwa Mola Mlezi wenu, ya kwamba nakuundieni kwa udongo kama sura ya ndege. Kisha nampuliza anakuwa ndege kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na ninawaponesha vipofu wa tangu kuzaliwa na wakoma, na ninawafufua maiti kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na ninakwambieni mnacho kila na mnacho weka akiba katika nyumba zenu. Hakika katika haya ipo Ishara kwenu ikiwi nyinyi ni wenye kuamini

Verse 50 — Surah Al-Imran 3:50

Na ninasadikisha yaliyo kuwa kabla yangu katika Taurati, na ili nikuhalalishieni baadhi ya yale mlio harimishiwa, na nimekujieni na Ishara kutokana na Mola Mlezi wenu. Kwa hivyo mcheni Mwenyezi Mungu na nit'iini mimi

Verse 51 — Surah Al-Imran 3:51

Hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi na ni Mola wenu Mlezi. Basi muabudni Yeye. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka

Verse 52 — Surah Al-Imran 3:52

Isa alipo hisi kuwa kati yao pana ukafiri alisema: Nani wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu? Wanafunzi wake wakasema: Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu. Tumemuamini Mwenyezi Mungu, na shuhudia kwamba sisi hakika ni Waislamu

Verse 53 — Surah Al-Imran 3:53

Mola wetu Mlezi! Tumeyaamini uliyo yateremsha, na tumemfuata huyu Mtume, basi tuandike pamoja na wanao shuhudia

Verse 54 — Surah Al-Imran 3:54

Na Makafiri walipanga mipango na Mwenyezi Mungu akapanga mipango, na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa wenye kupanga

Verse 55 — Surah Al-Imran 3:55

Pale Mwenyezi Mungu alipo sema: Ewe Isa! Mimi nitakufisha, na nitakunyanyua kwangu, na nitakutakasa na wale walio kufuru, na nitawaweka wale walio kufuata juu ya wale walio kufuru, mpaka Siku ya Kiyama. Kisha marejeo yenu yatakuwa kwangu, nikuhukumuni katika yale mliyo kuwa mkikhitalifiana

Verse 56 — Surah Al-Imran 3:56

Ama wale walio kufuru, nitawaadhibu adhabu kali katika dunia na Akhera, wala hawatapata wa kuwanusuru

Verse 57 — Surah Al-Imran 3:57

Na ama wale walio amini na wakatenda mema basi Mwenyezi Mungu atawalipa ujira wao kaamili. Na Mwenyezi Mungu hawapendi madhaalimu

Verse 58 — Surah Al-Imran 3:58

Haya tunayo kusomea ni katika Aya na Ukumbusho wenye hikima

Verse 59 — Surah Al-Imran 3:59

Hakika mfano wa Isa kwa Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam; alimuumba kwa udongo kisha akamwambia: Kuwa! Basi akawa

Verse 60 — Surah Al-Imran 3:60

Hii ni kweli itokayo kwa Mola wako Mlezi. Basi usiwe miongoni mwa wanao fanya shaka

Verse 61 — Surah Al-Imran 3:61

Watakao kuhoji katika haya baada ya kukufikilia ilimu hii waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wake zetu na wake zenu, na sisi wenyewe na nyinyi wenyewe, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo

Verse 62 — Surah Al-Imran 3:62

Hakika haya ndiyo maelezo ya kweli. Na hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu tu, na hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu na Mwenye hikima

Verse 63 — Surah Al-Imran 3:63

Na kama wakigeuka basi Mwenyezi Mungu anawajua waharibifu

Verse 64 — Surah Al-Imran 3:64

Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lilio sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa Waola Walezi badala ya Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka basi semeni: Shuhudieni ya kwamba sisi ni Waislamu

Verse 65 — Surah Al-Imran 3:65

Enyi Watu wa Kitabu! Mbona mnabishana juu ya Ibrahim, na hali Taurati na Injili hazikuteremshwa ila baada yake? Basi hamzingatii

Verse 66 — Surah Al-Imran 3:66

Angalieni! Nyinyi mlibishana katika yale mliyo yajua. Mbona sasa mnabishana katika yale msiyo yajua? Na Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye, na nyinyi hamjui

Verse 67 — Surah Al-Imran 3:67

Ibrahim hakuwa Yahudi wala Mkristo, lakini alikuwa mwongofu Muislamu, wala hakuwa katika washirikina

Verse 68 — Surah Al-Imran 3:68

Watu wanao mkaribia zaidi Ibrahim ni wale walio mfuata yeye na Nabii huyu na walio amini. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wa Waumini

Verse 69 — Surah Al-Imran 3:69

Kipo kikundi katika Watu wa Kitabu wanao penda kukupotezeni; lakini hawapotezi ila nafsi zao, nao wenyewe hawatambui

Verse 70 — Surah Al-Imran 3:70

Enyi Watu wa Kitabu! Mbona mnazikataa Ishara za Mwenyezi Mungu ilhali nyinyi mnashuhudia

Verse 71 — Surah Al-Imran 3:71

Enyi Watu wa Kitabu! Mbona kweli mnaivisha uwongo, na kweli mnaificha na hali mnajua

Verse 72 — Surah Al-Imran 3:72

Na kikundi katika Watu wa Kitabu walisema: Yaaminini yale waliyo teremshiwa wenye kuamini mwanzo wa mchana, na yakataeni mwisho wake; huenda wakarejea

Verse 73 — Surah Al-Imran 3:73

Wala msimuamini ila anaye fuata dini yenu. Sema: Hakika uwongofu ni uwongofu wa Mwenyezi Mungu, kuwa apewe mtu mfano wa mlio pewa nyinyi au wakuhojini mbele ya Mola wenu Mlezi. Sema: Hakika fadhila zimo mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mjuzi

Verse 74 — Surah Al-Imran 3:74

Yeye humchagua kumpa rehema zake amtakaye; na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye fadhila kubwa

Verse 75 — Surah Al-Imran 3:75

Na miongoni mwa Watu wa Kitabu yupo ambaye ukimpa amana ya mrundi wa mali atakurudishia, na miongoni mwao yupo ambaye ukimpa amana ya dinari moja hakurudishii isipo kuwa ukimsimamia kumdai. Haya ni kwa kuwa wakisema: Hatuna lawama kwa ajili ya hawa wasio jua kusoma. Na wanamzulia uwongo Mwenyezi Mungu, hali nao wanajua

Verse 76 — Surah Al-Imran 3:76

Sivyo hivyo, bali anaye timiza ahadi yake na akamchamngu basi Mwenyezi Mungu huwapenda wachamngu

Verse 77 — Surah Al-Imran 3:77

Hakika wanao uza ahadi ya Mwenyezi Mungu na viapo vyao thamani ndogo, hao hawatakuwa na sehemu ya kheri yoyote katika Akhera, wala Mwenyezi Mungu hatasema nao wala hatawatazama Siku ya Kiyama, wala hatawatakasa, nao watapata adhabu chungu

Verse 78 — Surah Al-Imran 3:78

Na wapo baadhi yao wanao pindua ndimi zao katika kusoma Kitabu ili mdhanie kuwa hayo yanatoka Kitabuni, na wala hayatoki Kitabuni. Na husema: Haya yametoka kwa Mwenyezi Mungu. Na wala hayatoki kwa Mwenyezi Mungu. Na wanamsingizia Mwenyezi Mungu uwongo na wao wanajua

Verse 79 — Surah Al-Imran 3:79

Haiwezi kuwa mtu aliye pewa na Mwenyezi Mungu Kitabu na hikima na Unabii kisha awaambie watu: Kuweni wa kuniabudu mimi badala ya Mwenyezi Mungu. Bali atawaambia: Kuweni wenye kumuabudu Mola Mlezi wa viumbe vyote, kwa kuwa nyinyi mnafundisha Kitabu na kwa kuwa mnakisoma

Verse 80 — Surah Al-Imran 3:80

Wala hatakuamrisheni kuwafanya Malaika na Manabii kuwa ni miungu. Je, atakuamrisheni ukafiri baada ya kuwa nyinyi Waislamu

Verse 81 — Surah Al-Imran 3:81

Na pale Mwenyezi Mungu alipo chukua ahadi kwa Manabii: Nikisha kupeni Kitabu na hikima, kisha akakujieni Mtume mwenye kusadikisha mliyo nayo, ni juu yenu mumuamini na mumsaidie. Akasema: Je, mmekiri na mmekubali kushika agizo langu juu ya hayo? Wakasema: Tumekubali. Akasema: Basi shuhudieni, na Mimi ni pamoja nanyi katika kushuhudia

Verse 82 — Surah Al-Imran 3:82

Watakao geuka baada ya haya basi hao ndio wapotovu

Verse 83 — Surah Al-Imran 3:83

Je, wanataka dini isiyo kuwa ya Mwenyezi Mungu, na hali kila kilichomo mbinguni na katika ardhi kimesilimu kwa kumt'ii Yeye kikipenda kisipende, na kwake Yeye watarejeshwa

Verse 84 — Surah Al-Imran 3:84

Sema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu, na tuliyo teremshiwa sisi, na aliyo teremshiwa Ibrahim, na Ismail, na Is-haak na Yaakub na wajukuu zao, na aliyo pewa Musa na Isa na Manabii wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi. Hatubagui baina yao hata mmoja, na sisi ni wenye kusilimu kwake

Verse 85 — Surah Al-Imran 3:85

Na anaye tafuta dini isiyo kuwa Uislamu haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye kukhasiri

Verse 86 — Surah Al-Imran 3:86

Mwenyezi Mungu atawaongoaje watu walio kufuru baada ya kuamini kwao, na wakashuhudia ya kuwa Mtume huyu ni wa haki, na zikawafikia hoja zilizo wazi? Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu

Verse 87 — Surah Al-Imran 3:87

Hao malipo yao ni kuwa ipo juu yao laana ya Mwenyezi Mungu na ya Malaika na ya watu wote

Verse 88 — Surah Al-Imran 3:88

Humo watadumu. Hawatapunguziwa adhabu wala hawatapewa nafasi

Verse 89 — Surah Al-Imran 3:89

Isipo kuwa wale walio tubu baada ya hayo na wakatengenea; kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu

Verse 90 — Surah Al-Imran 3:90

Hakika wale walio kufuru baada ya kuamini kwao, kisha wakazidi kukufuru, toba yao haitakubaliwa, na hao ndio walio potea

Verse 91 — Surah Al-Imran 3:91

Hakika wale walio kufuru, na wakafa hali ni makafiri haitakubaliwa kutoka kwa yeyote wao fidia ya dhahabu ya kujaza dunia nzima lau wangeli itoa. Hao watapata adhabu chungu, wala hawatakuwa na wa kuwanusuru

Verse 92 — Surah Al-Imran 3:92

KABISA HAMTAFIKIA wema mpaka mtoe katika vile mnavyo vipenda. Na kitu chochote mnacho kitoa basi hakika Mwenyezi Mungu anakijua

Verse 93 — Surah Al-Imran 3:93

Kila chakula kilikuwa halali kwa Wana wa Israili isipo kuwa alicho jizuilia Israili mwenyewe kabla haijateremshwa Taurati. Sema: Leteni Taurati muisome ikiwa nyinyi ni wasema kweli

Verse 94 — Surah Al-Imran 3:94

Na wanao mzulia uwongo Mwenyezi Mungu baada ya hayo, basi hao ndio madhaalimu

Verse 95 — Surah Al-Imran 3:95

Sema: Mwenyezi Mungu amesema kweli. Basi fuateni mila ya Ibrahim mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina

Verse 96 — Surah Al-Imran 3:96

Hakika Nyumba ya kwanza walio wekewa watu kwa ibada ni ile iliyoko Bakka, iliyo barikiwa na yenye uwongofu kwa walimwengu wote

Verse 97 — Surah Al-Imran 3:97

Ndani yake zipo Ishara zilizo wazi - masimamio ya Ibrahim, na mwenye kuingia humo anakuwa katika amani. Na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae njia ya kwendea. Na atakaye kanusha basi Mwenyezi Mungu si mhitaji kwa walimwengu

Verse 98 — Surah Al-Imran 3:98

Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Kwa nini mnakanusha ishara za Mwenyezi Mungu, na ilhali kuwa Mwenyezi Mungu ni Shahidi kwa yote mnayo yatenda

Verse 99 — Surah Al-Imran 3:99

Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Kwa nini mnamzuilia aliye amini Njia ya Mwenyezi Mungu mkiitafutia kosa, na hali nyinyi mnashuhudia? Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na mnayo yatenda

Verse 100 — Surah Al-Imran 3:100

Enyi mlio amini! Mkiwat'ii baadhi ya walio pewa Kitabu watakurudisheni kuwa makafiri baada ya Imani yenu

Verse 101 — Surah Al-Imran 3:101

Na vipi mkufuru hali nyinyi mnasomewa Aya za Mwenyezi Mungu na Mtume yuko kati yenu? Na mwenye kushikamana na Mwenyezi Mungu basi huyo ameongozwa kwenye Njia Iliyo Nyooka

Verse 102 — Surah Al-Imran 3:102

Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu kama ipasavyo kumcha; wala msife ila nanyi ni Waislamu

Verse 103 — Surah Al-Imran 3:103

Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto, naye akakuokoeni nalo. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Ishara zake ili mpate kuongoka

Verse 104 — Surah Al-Imran 3:104

Na uwe kutokana na nyinyi umma unao lingania kheri na unao amrisha mema na unakataza maovu. Na hao ndio walio fanikiwa

Verse 105 — Surah Al-Imran 3:105

Wala msiwe kama wale walio farikiana na kukhitalifiana baada ya kuwafikia hoja zilizo wazi. Na hao ndio watakao kuwa na adhabu kubwa

Verse 106 — Surah Al-Imran 3:106

Siku ambayo nyuso zitanawiri na nyuso zitasawijika. Ama hao ambao nyuso zao zitasawijika wataambiwa: Je! Mlikufuru baada ya kuamini kwenu? Basi onjeni adhabu kwa vile mlivyo kuwa mnakufuru

Verse 107 — Surah Al-Imran 3:107

Ama wale ambao nyuso zao zitanawiri watakuwa katika rehema ya Mwenyezi Mungu. Wao humo watadumu

Verse 108 — Surah Al-Imran 3:108

Hizi ni Aya za Mwenyezi Mungu tunakusomea kwa haki. Na Mwenyezi Mungu hataki kuwadhulumu walimwengu

Verse 109 — Surah Al-Imran 3:109

Na kila kilichomo mbinguni na kilichomo ardhini ni cha Mwenyezi Mungu; na mambo yote yatarejea kwa Mwenyezi Mungu

Verse 110 — Surah Al-Imran 3:110

Nyinyi mmekuwa bora ya umma walio tolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa Watu wa Kitabu nao wameamini ingeli kuwa bora kwao. Wapo miongoni mwao waumini, lakini wengi wao wapotovu

Verse 111 — Surah Al-Imran 3:111

Maadui hawatakudhuruni ila ni maudhi tu. Na wakipigana nanyi watakupeni mgongo, na tena hawatanusuriwa

Verse 112 — Surah Al-Imran 3:112

Wamepigwa na udhalili popote wanapo kutikana, isipo kuwa wakishika kamba ya Mwenyezi Mungu na kamba ya watu. Na wakastahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, na wamepigwa na unyonge. Hayo ni kwa sababu walikuwa wakizikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, na wakiwauwa Manabii pasina haki; hayo ni kwa sababu waliasi na walikuwa wakiruka mipaka

Verse 113 — Surah Al-Imran 3:113

Wote hao si sawa sawa. Miongoni mwa Watu wa Kitabu wamo watu walio simama baraabara, wanasoma Aya za Mwenyezi Mungu nyakati za usiku, na pia wanasujudu

Verse 114 — Surah Al-Imran 3:114

Wanamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na wanaamrisha mema na wanakataza maovu na wanakimbilia katika mambo ya kheri. Na hao ndio miongoni mwa watenda mema

Verse 115 — Surah Al-Imran 3:115

Na kheri yoyote wanayo ifanya hawatanyimwa malipwa yake. Na Mwenyezi Mungu anawajua wachamngu

Verse 116 — Surah Al-Imran 3:116

Hakika wale walio kufuru hazitawafaa kitu mali zao wala watoto wao mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio watu wa Motoni - humo watadumu

Verse 117 — Surah Al-Imran 3:117

Mfano wa vile wanavyo vitoa katika uhai wao wa duniani ni kama upepo ambao ndani yake ipo baridi ya barafu, ukalisibu shamba la watu walio dhulumu nafsi zao, ukaliteketeza. Na Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu, bali wao wenyewe wanadhulumu nafsi zao

Verse 118 — Surah Al-Imran 3:118

Enyi mlio amini! Msiwafanye wasiri wenu watu wasio kuwa katika nyinyi. Hawataacha kukufanyieni ubaya. Wanayapenda yanayo kudhuruni. Imekwisha fichuka chuki yao katika midomo yao. Na yanayo ficha vifua vyao ni makubwa zaidi. Tumekwisha kubainishieni Ishara ikiwa nyinyi mtayatia akilini

Verse 119 — Surah Al-Imran 3:119

Hivyo basi nyinyi ndio mnawapenda watu hao, wala wao hawakupendeni. Nanyi mnaviamini Vitabu vyote. Na wanapo kutana nanyi husema: Tumeamini. Na wanapo kuwa peke yao wanakuumieni vidole kwa chuki. Sema: Kufeni kwa chuki yenu! Hakika Mwenyezi Mungu anayajua yaliomo vifuani

Verse 120 — Surah Al-Imran 3:120

Ikikupateni kheri huwaudhi. Na ikikupateni shari wanafurahia. Na nyinyi mkisubiri na mkajizuilia, hila zao hazitakudhuruni kitu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyazunguka yote wayatendayo

Verse 121 — Surah Al-Imran 3:121

Na pale ulipo toka asubuhi, ukaacha ahali zako uwapange Waumini kwenye vituo kwa ajili ya vita - na Mwenyezi Mungu anasikia na anajua

Verse 122 — Surah Al-Imran 3:122

Makundi mawili miongoni mwenu yakaingiwa na woga kuwa watashindwa - na hali Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wao; na Waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu tu

Verse 123 — Surah Al-Imran 3:123

Na Mwenyezi Mungu alikwisha kunusuruni katika Badri nanyi mlikuwa wanyonge. Basi mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kushukuru

Verse 124 — Surah Al-Imran 3:124

Ulipo waambia Waumini: Je, haitakutosheni ikiwa Mola wenu atakusaidieni kwa Malaika elfu tatu walio teremshwa

Verse 125 — Surah Al-Imran 3:125

Kwani! Ikiwa mtavumilia na mkamchamngu na hata maadui wakikutokeeni kwa ghafla, basi hapo Mola wenu Mlezi atakusaidieni kwa Malaika elfu tano wanao shambulia kwa nguvu

Verse 126 — Surah Al-Imran 3:126

Na Mwenyezi Mungu hakufanya haya ila kuwa ni bishara kwenu, na ili nyoyo zenu zipate kutua. Na msaada hautoki isipo kuwa kwa Mwenyezi Mungu, Aliye tukuka, Mwenye nguvu na Mwenye hikima

Verse 127 — Surah Al-Imran 3:127

Haya ni kwa ajili awakate sehemu katika walio kufuru, au awahizi wapate kurejea nyuma nao wamepwelewa

Verse 128 — Surah Al-Imran 3:128

Wewe huna lako jambo katika haya - ama atawahurumia au atawaadhibu, kwani wao ni madhaalimu

Verse 129 — Surah Al-Imran 3:129

Na ni vya Mwenyezi Mungu vyote vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi. Yeye humsamehe na humuadhibu amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Msamehevu Mwenye kurehemu

Verse 130 — Surah Al-Imran 3:130

Enyi mlio amini! Msile riba mkizidisha juu kwa juu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufanikiwa

Verse 131 — Surah Al-Imran 3:131

Na uogopeni Moto ambao umeandaliwa kwa ajili ya makafiri

Verse 132 — Surah Al-Imran 3:132

Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume ili mpate kurehemewa

Verse 133 — Surah Al-Imran 3:133

Na yakimbilieni maghfira ya Mola wenu Mlezi, na Pepo ambayo upana wake ni mbingu na ardhi, iliyo wekwa tayari kwa wachamngu

Verse 134 — Surah Al-Imran 3:134

Ambao hutoa wanapo kuwa na wasaa na wanapo kuwa na dhiki, na wanajizuia ghadhabu, na wasamehevu kwa watu; na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema

Verse 135 — Surah Al-Imran 3:135

Na ambao pindi wafanyapo uchafu au wakajidhulumu nafsi zao humkumbuka Mwenyezi Mungu na wakamwomba msamaha kwa dhambi zao - na nani anaye futa dhambi isipo kuwa Mwenyezi Mungu? - na wala hawaendelei na waliyo yafanya na hali wanajua

Verse 136 — Surah Al-Imran 3:136

Hao malipo yao ni msamaha kwa Mola wao Mlezi, na Bustani zipitazo mito kati yake. Humo watadumu, na mwema mno ujira wa watendao

Verse 137 — Surah Al-Imran 3:137

Kabla yenu zimepita nyendo nyingi; basi tembeeni katika ulimwengu muangalie vipi ulikuwa mwisho wa wanao kanusha

Verse 138 — Surah Al-Imran 3:138

Hii ni bayana kwa watu wote, na ni uwongofu, na mawaidha kwa wachamngu

Verse 139 — Surah Al-Imran 3:139

Wala msilegee, wala msihuzunike, kwani nyinyi ndio wa juu mkiwa ni Waumini

Verse 140 — Surah Al-Imran 3:140

Kama yamekupateni majaraha, basi na hao watu wengine yamewapata majaraha mfano wa haya. Na siku za namna hii tunaweletea watu kwa zamu, ili Mwenyezi Mungu awapambanue walio amini na awateuwe miongoni mwenu mashahidi. Na Mwenyezi Mungu hawapendi madhaalimu

Verse 141 — Surah Al-Imran 3:141

Na pia ili Mwenyezi Mungu awasafishe walio amini na awafutilie mbali makafiri

Verse 142 — Surah Al-Imran 3:142

Je! Mnadhani mtaingia Peponi na hali Mwenyezi Mungu hajawapambanua wale miongoni mwenu walio pigana Jihadi, na hajawapambanua walio subiri

Verse 143 — Surah Al-Imran 3:143

Na nyinyi mlikuwa mkitamani mauti kabla hamjakutana nayo. Basi sasa mmekwisha yaona na huku mnayatazama

Verse 144 — Surah Al-Imran 3:144

Na Muhammad hakuwa ila ni Mtume tu. Wamekwisha pita kabla yake Mitume. Je, akifa au akauwawa ndiyo mtageuka mrudi nyuma? Na atakaye geuka akarudi nyuma huyo hatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu atawalipa wanao mshukuru

Verse 145 — Surah Al-Imran 3:145

Na haiwezi nafsi kuwa ife ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu kama ilivyo andikwa ajali yake. Na mwenye kutaka malipo ya duniani tutampa; na mwenye kutaka malipo ya Akhera tutampa. Na tutawalipa wenye kushukuru

Verse 146 — Surah Al-Imran 3:146

Na Manabii wangapi walipigana na pamoja nao Waumini wengi wenye ikhlasi! Hawakufanya woga kwa yaliyo wasibu katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawakudhoofika wala hawakuwa wanyonge. Na Mwenyezi Mungu huwapenda wanao subiri

Verse 147 — Surah Al-Imran 3:147

Wala kauli yao haikuwa ila ni kusema: Mola wetu Mlezi! Tughufirie madhambi yetu na kupita kwetu kiasi katika mambo yetu, na isimamishe imara miguu yetu na utunusuru tuwashinde kaumu ya makafiri

Verse 148 — Surah Al-Imran 3:148

Basi Mwenyezi Mungu akawapa malipo ya duniani na bora ya malipo ya Akhera. Na Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao mema

Verse 149 — Surah Al-Imran 3:149

Enyi mlio amini! Ikiwa mtawat'ii walio kufuru watakurudisheni nyuma, na hapo mtageuka kuwa wenye kukhasiri

Verse 150 — Surah Al-Imran 3:150

Bali Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wenu, naye ndiye bora wa wasaidizi

Verse 151 — Surah Al-Imran 3:151

Tutazitia khofu nyoyo za walio kufuru kwa vile walivyo mshirikisha Mwenyezi Mungu na washirika ambao hakuwateremshia hoja yoyote. Na makaazi yao ni Motoni; na maovu yaliyoje maskani ya wenye kudhulumu

Verse 152 — Surah Al-Imran 3:152

Na Mwenyezi Mungu alikutimilizieni miadi yake, vile mlivyo kuwa mnawauwa kwa idhini yake, mpaka mlipo legea na mkazozana juu ya amri, na mkaasi baada ya Yeye kukuonyesheni mliyo yapenda. Wapo miongoni mwenu wanao taka dunia, na wapo miongoni mwenu wanao taka Akhera. Kisha akakutengeni nao (maadui) ili akujaribuni. Naye sasa amekwisha kusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya Waumini

Verse 153 — Surah Al-Imran 3:153

Pale mlipo kuwa mkikimbia mbio wala hamumsikilizi yeyote, na Mtume anakuiteni, yuko nyuma yenu. Mwenyezi Mungu akakupeni dhiki juu ya dhiki, ili msisikitike kwa yaliyo kukoseeni wala kwa yaliyo kusibuni. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote mnayo yatenda

Verse 154 — Surah Al-Imran 3:154

Kisha baada ya dhiki alikuteremshieni utulivu - usingizi ambao ulifunika kundi moja kati yenu. Na kundi jengine nafsi zao ziliwashughulisha hata wakamdhania Mwenyezi Mungu dhana isiyo kuwa ya haki, dhana ya kijinga. Wakisema: Hivyo tuna lolote sisi katika jambo hili? Sema: Mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu. Wanaficha katika nafsi zao wasiyo kubainishia. Wanasema: Lau ingelikuwa tuna lolote katika jambo hili tusinge uliwa hapa. Sema: Hata mngeli kuwa majumbani mwenu, basi wangeli toka walio andikiwa kufa, wakenda mahali pao pa kuangukia wafe. (Haya ni hivyo) ili Mwenyezi Mungu ayajaribu yaliyomo vifuani mwenu, na asafishe yaliyomo nyoyoni mwenu. Na Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo vifuani

Verse 155 — Surah Al-Imran 3:155

Hakika wale walio rudi nyuma miongoni mwenu siku yalipo pambana majeshi mawili, Shet'ani ndiye aliye watelezesha kwa sababu ya baadhi ya makosa waliyo yafanya; na Mwenyezi Mungu amekwisha wasamehe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mpole

Verse 156 — Surah Al-Imran 3:156

Enyi mlio amini! Msiwe kama wale walio kufuru na wakawasema ndugu zao walipo safiri katika nchi au walipo kuwa vitani: Wangeli kuwa kwetu wasingeli kufa na wasingeli uwawa. Ili Mwenyezi Mungu afanye hayo kuwa ni majuto katika nyoyo zao. Na Mwenyezi Mungu huhuisha na hufisha. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona myatendayo

Verse 157 — Surah Al-Imran 3:157

Na pindi mkiuliwa katika Njia ya Mwenyezi Mungu, au mkifa, hakika maghfira na rehema zitokazo kwa Mwenyezi Mungu ni bora kuliko yote wanayo yakusanya

Verse 158 — Surah Al-Imran 3:158

Na mkifa au mkiuliwa ni kwa Mwenyezi Mungu ndio mtakusanywa

Verse 159 — Surah Al-Imran 3:159

Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungeli kuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangeli kukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriana nao katika mambo. Na ukisha kata shauri basi mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanao mtegemea

Verse 160 — Surah Al-Imran 3:160

Akikunusuruni Mwenyezi Mungu hapana wa kukushindeni, na akikutupeni ni nani, basi, baada yake Yeye ataye kunusuruni? Na Waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu tu

Verse 161 — Surah Al-Imran 3:161

Na haiwezekani kwa Nabii yeyote kufanya khiyana. Na atakaye fanya khiyana, atayaleta Siku ya Kiyama aliyo yafanyia khiyana, kisha kila mtu atalipwa kwa aliyo yachuma, kwa ukamilifu; wala hawatadhulumiwa

Verse 162 — Surah Al-Imran 3:162

Je! Aliye yafuata ya kumridhisha Mwenyezi Mungi ni kama yule aliye stahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, na makaazi yake yakawa Jahannamu? Napo ni mahala pabaya pa kurejea

Verse 163 — Surah Al-Imran 3:163

Hao wana vyeo mbali mbali kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona yote wayatendayo

Verse 164 — Surah Al-Imran 3:164

Hakika Mwenyezi Mungu amewafanyia wema mkubwa Waumini vile alivyo waletea Mtume aliye miongoni mwao wenyewe, anaye wasomea Aya zake, na anawatakasa, na anawafunza Kitabu na hikima, ijapo kuwa kabla ya hapo walikuwa katika upotovu ulio wazi

Verse 165 — Surah Al-Imran 3:165

Nyinyi - ulipo kusibuni msiba ambao nyinyi mmekwisha watia mara mbili mfano wa huo - mnasema: Umetoka wapi huu? Sema: Huo umetoka kwenu wenyewe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu

Verse 166 — Surah Al-Imran 3:166

Na yaliyo kusibuni siku yalipo pambana majeshi mawili yalikuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na ili awajue Waumini

Verse 167 — Surah Al-Imran 3:167

Na ili awapambanue walio kuwa wanaafiki, wakaambiwa: Njooni mpigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu au lindeni. Wakasema: Tungeli jua kuna kupigana bila ya shaka tungeli kufuateni. Wao siku ile walikuwa karibu na ukafiri kuliko Imani. Wanasema kwa midomo yao yasiyo kuwamo nyoyoni mwao. Na Mwenyezi Mungu anajua kabisa wanayo yaficha

Verse 168 — Surah Al-Imran 3:168

Hao ndio walio waambia ndugu zao na wao wenyewe wakakaa kitako: Lau wengeli tut'ii wasingeli uliwa. Sema: Ziondoleeni nafsi zenu mauti kama mnasema kweli

Verse 169 — Surah Al-Imran 3:169

Wala kabisa usiwadhanie walio uliwa katika Njia ya Mwenyezi Mungu kuwa ni maiti. Bali hao ni wahai, wanaruzukiwa kwa Mola wao Mlezi

Verse 170 — Surah Al-Imran 3:170

Wanafurahia aliyo wapa Mwenyezi Mungu kwa fadhila yake, na wanawashangilia wale ambao bado hawajajiunga nao, walio nyuma yao, ya kwamba haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika

Verse 171 — Surah Al-Imran 3:171

Wanashangilia neema na fadhila za Mwenyezi Mungu, na ya kwamba Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa Waumini

Verse 172 — Surah Al-Imran 3:172

Walio mwitikia Mwenyezi Mungu na Mtume baada ya kwisha patwa na majaraha - kwa walio fanya wema miongoni mwao na wakamchamngu utakuwa ujira mkubwa

Verse 173 — Surah Al-Imran 3:173

Walio ambiwa na watu: Kuna watu wamekukusanyikieni, waogopeni! Hayo yakawazidishia Imani, wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosha, naye ni mbora wa kutegemewa

Verse 174 — Surah Al-Imran 3:174

Basi wakarudi na neema na fadhila za Mwenyezi Mungu. Hapana baya lilio wagusa, na wakafuata yanayo mridhi Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kuu

Verse 175 — Surah Al-Imran 3:175

Hakika huyo ni Shet'ani anawatia khofu marafiki zake, basi msiwaogope, bali niogopeni Mimi mkiwa nyinyi ni Waumini

Verse 176 — Surah Al-Imran 3:176

Wala wasikuhuzunishe wale wanao kimbilia ukafirini. Hakika hao hawamdhuru kitu Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anataka asiwawekee sehemu yoyote katika Akhera, na yao wao adhabu kubwa

Verse 177 — Surah Al-Imran 3:177

Hakika wale walio nunua ukafiri kwa Imani hawatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu, na yao wao ni adhabu chungu

Verse 178 — Surah Al-Imran 3:178

Wala wasidhani wale wanao kufuru kwamba huu muhula tunao wapa ni kheri yao. Hakika tunawapa muhula wazidi madhambi. Na yao wao ni adhabu ya kuwadhalilisha

Verse 179 — Surah Al-Imran 3:179

Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwaacha Waumini katika hali mliyo nayo mpaka apambanue wabaya na wema. Wala haiwi kwa Mwenyezi Mungu kukujuulisheni mambo ya ghaibu. Lakini Mwenyezi Mungu humteua katika Mitume wake amtakaye. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume yake. Na mkiamini na mkamchamngu mtakuwa na ujira mkubwa

Verse 180 — Surah Al-Imran 3:180

Wala wasidhani wale ambao wanafanya ubakhili katika aliyo wapa Mwenyezi Mungu katika fadhila zake kuwa ni kheri yao. Bali hiyo ni shari kwao. Watafungwa kongwa za yale waliyo yafanyia ubakhili Siku ya Kiyama. Na urithi wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote myatendayo

Verse 181 — Surah Al-Imran 3:181

Mwenyezi Mungu amekwisha sikia kauli ya walio sema: Mwenyezi Mungu ni masikini, na sisi ni matajiri. Tumeyaandika waliyo yasema, na pia kuwauwa kwao Manabii bila ya haki, na tutawaambia Siku ya Kiyama: Onjeni adhabu ya kuungua

Verse 182 — Surah Al-Imran 3:182

Haya ni kwa sababu ya iliyo tanguliza mikono yenu, na kwamba Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja

Verse 183 — Surah Al-Imran 3:183

Walio sema: Mwenyezi Mungu ametuahidi tusimuamini Mtume yeyote mpaka atuletee kafara inayo teketezwa na moto. Waambie: Walikujieni Mitume kabla yangu kwa hoja zilizo wazi na kwa hayo mnayo sema, basi kwa nini mkawauwa ikiwa mlikuwa wakweli

Verse 184 — Surah Al-Imran 3:184

Na wakikukanusha basi walikanushwa Mitume wengine kabla yako walio kuja na hoja waziwazi na Vitabu vyenye hikima, na Kitabu chenye nuru

Verse 185 — Surah Al-Imran 3:185

Kila nafsi itaonja mauti. Na bila ya shaka mtapewa ujira wenu kaamili Siku ya Kiyama. Na atakaye epushwa na Moto na akatiwa Peponi basi huyo amefuzu. Na maisha ya dunia si kitu ila ni starehe ya udanganyifu

Verse 186 — Surah Al-Imran 3:186

Hapana shaka yoyote mtapata misukosuko katika mali zenu na nafsi zenu, na bila ya shaka yoyote mtasikia udhia mwingi kutokana na walio pewa Kitabu kabla yenu na wale walio shiriki. Na ikiwa mtasubiri na mkamchamngu basi hakika hayo ni katika mambo ya kuazimia

Verse 187 — Surah Al-Imran 3:187

Na pale Mwenyezi Mungu alipo fungamana na walio pewa Kitabu kuwa: Lazima mtawabainishia watu, wala hamtokificha, walikitupa nyuma ya migongo yao, na wakanunua kwacho thamani duni. Basi ni kiovu hicho walicho nunua

Verse 188 — Surah Al-Imran 3:188

Usiwadhanie kabisa wale wanao furahia waliyo yafanya, na wakapenda kusifiwa kwa wasiyo yatenda, usiwadhanie kuwa watasalimika na adhabu. Yao wao ni adhabu chungu

Verse 189 — Surah Al-Imran 3:189

Na Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu

Verse 190 — Surah Al-Imran 3:190

Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kukhitalifiana usiku na mchana ziko Ishara kwa wenye akili

Verse 191 — Surah Al-Imran 3:191

Ambao humkumbuka Mwenyezi Mungu wakiwa wima na wakikaa kitako na wakilala, na hufikiri kuumbwa mbingu na ardhi, wakisema: Mola wetu Mlezi! Hukuviumba hivi bure. Subhanaka, Umetakasika! Basi tukinge na adhabu ya Moto

Verse 192 — Surah Al-Imran 3:192

Mola wetu Mlezi! Hakika unaye mtia Motoni umemhizi; na walio dhulumu hawana wasaidizi

Verse 193 — Surah Al-Imran 3:193

Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tumemsikia mwenye kuita akiitia Imani kwamba: Muaminini Mola wenu Mlezi; nasi tukaamini. Basi tusamehe madhambi yetu, na utufutie makosa yetu, na utufishe pamoja na watu wema

Verse 194 — Surah Al-Imran 3:194

Mola wetu Mlezi! Na utupe uliyo tuahidi kwa Mitume wako, wala usituhizi Siku ya Kiyama. Hakika Wewe huvunji miadi

Verse 195 — Surah Al-Imran 3:195

Mola Mlezi wao, akayakubali maombi yao akajibu: Hakika sipotezi kazi ya mfanya kazi miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke, kwani ni nyinyi kwa nyinyi. Basi walio hama, na walio tolewa makwao, na wakateswa katika Njia yangu, na wakapigana, na wakauliwa, kwa yakini Mimi nitawafutia makosa yao, na kwa yakini nitawaingiza katika Mabustani yanayo pita mito kati yake. Hayo ndiyo malipo yanayo toka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu kwake yapo malipo mema kabisa

Verse 196 — Surah Al-Imran 3:196

Kabisa kusikudanganye kubakia kutangatanga kwa walio kufuru katika nchi

Verse 197 — Surah Al-Imran 3:197

Hiyo ni starehe ndogo. Kisha makaazi yao yatakuwa Jahannamu. Na ni mahali pabaya mno pa kupumzikia

Verse 198 — Surah Al-Imran 3:198

Lakini walio mcha Mola wao Mlezi watapata Mabustani yanayo pita mito kati yake. Watadumu humo. Hayo ni makaribisho yao yatokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na vilioko kwa Mwenyezi Mungu ni bora kwa watu wema

Verse 199 — Surah Al-Imran 3:199

Hakika miongoni mwa Watu wa Kitabu wapo wanao muamini Mwenyezi Mungu na yaliyo teremshwa kwenu na yaliyo teremshwa kwao, wakimnyenyekea Mwenyezi Mungu. Hawabadili Aya za Mwenyezi Mungu kwa thamani duni. Hao wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu

Verse 200 — Surah Al-Imran 3:200

Enyi mlio amini! Subirini, na shindaneni kusubiri, na kuweni macho, na mcheni Mwenyezi Mungu, ili mpate kufanikiwa