Back to Languages

Swahili - Chapter 32 - As-Sajdah

Translation by Ali Muhsin Al Barwani — Permalink

Verse 1 — Surah As-Sajdah 32:1

Alif Lam Mim (A. L. M)

Verse 2 — Surah As-Sajdah 32:2

Huu ni mteremsho wa Kitabu kisicho kuwa na shaka yoyote kinacho toka kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote

Verse 3 — Surah As-Sajdah 32:3

Au wanasema: Amekizua? Bali hichi ni Kweli iliyo toka kwa Mola wako Mlezi ili uwaonye watu wasio fikiwa na mwonyaji kabla yako; huenda wakaongoka

Verse 4 — Surah As-Sajdah 32:4

Mwenyezi Mungu ndiye aliye umba mbingu na ardhi na viliomo baina yao kwa siku sita, na akatawala kwenye Kiti cha Enzi. Nyinyi hamna mlinzi wala mwombezi isipo kuwa Yeye tu. Basi, je, hamkumbuki

Verse 5 — Surah As-Sajdah 32:5

Anapitisha mambo yote yalio baina mbingu na ardhi, kisha yanapanda kwake kwa siku ambayo kipimo chake ni miaka elfu kwa mnavyo hisabu nyinyi

Verse 6 — Surah As-Sajdah 32:6

Huyu ndiye Mwenye kuyajua yasiyo onekana na yanayo onekana. Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu

Verse 7 — Surah As-Sajdah 32:7

Ambaye ametengeneza vizuri umbo la kila kitu; na akaanzisha kumuumba mtu kwa udongo

Verse 8 — Surah As-Sajdah 32:8

Na kisha akajaalia uzao wake utokane na kizazi cha maji madhaifu

Verse 9 — Surah As-Sajdah 32:9

Kisha akamtengeneza, na akampulizia roho yake, na akakujaalieni kusikia na kuona, na nyoyo za kufahamu. Ni uchache mnavyo shukuru

Verse 10 — Surah As-Sajdah 32:10

Nao husema: Tutapo kwisha potea chini ya ardhi, ni kweli tutarudishwa katika umbo jipya? Bali wao wanakanusha kwamba watakutana na Mola wao Mlezi

Verse 11 — Surah As-Sajdah 32:11

Sema: Atakufisheni Malaika wa mauti aliye wakilishwa juu yenu; kisha mtarejeshwa kwa Mola wenu Mlezi

Verse 12 — Surah As-Sajdah 32:12

Na ungeli waona wakosefu wanvyo inamisha vichwa vyao mbele ya Mola wao Mlezi, (wakisema): Mola wetu Mlezi! Tumesha ona, na tumesha sikia. Turejeshe tukatende mema, kwani hakika sisi tumekwisha kuwa na yakini sasa

Verse 13 — Surah As-Sajdah 32:13

Na lau tungeli taka tunge mpa kila mtu uwongofu wake. Lakini imekwisha kuwa kauli iliyo toka kwangu: Kwa yakini nitaijaza Jahannamu kwa wote hawa, majini na watu

Verse 14 — Surah As-Sajdah 32:14

Basi onjeni kwa vile mlivyo usahau mkutano wa Siku yenu hii. Na Sisi hakika tunakusahauni. Basi onjeni adhabu ya milele kwa yale mliyo kuwa mkiyatenda

Verse 15 — Surah As-Sajdah 32:15

Hakika wanao ziamini Aya zetu ni hao tu ambao wakikumbushwa hizo, basi wao huanguka kusujudu, na humsabihi Mola wao Mlezi kwa kumhimidi, nao hawajivuni

Verse 16 — Surah As-Sajdah 32:16

Mbavu zao zinaachana na vitanda kwa kumwomba Mola wao Mlezi kwa khofu na kutumaini, na hutoa kutokana na tulivyo waruzuku

Verse 17 — Surah As-Sajdah 32:17

Nafsi yoyote haijui waliyo fichiwa katika hayo yanayo furahisha macho - ni malipo ya yale waliyo kuwa wakiyatenda

Verse 18 — Surah As-Sajdah 32:18

Ati aliye Muumini atakuwa sawa na aliye mpotovu? Hawawi sawa

Verse 19 — Surah As-Sajdah 32:19

Ama walio amini na wakatenda mema, watakuwa nazo Bustani za makaazi mazuri. Ndio pa kufikia kwa waliyo kuwa wakiyatenda

Verse 20 — Surah As-Sajdah 32:20

Na ama wale walio tenda uovu, basi makaazi yao ni Motoni. Kila wakitaka kutoka humo watarudishwa humo humo. Na wataambiwa: Onjeni adhabu ya Moto ambayo mliyo kuwa mkiikanusha

Verse 21 — Surah As-Sajdah 32:21

Na tutawaonjesha adhabu khafifu kabla ya adhabu kubwa, huenda labda watarejea

Verse 22 — Surah As-Sajdah 32:22

Na ni nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye kumbushwa kwa Ishara za Mola wake Mlezi, kisha akazikataa? Hakika Sisi tutajilipiza kwa wakosefu

Verse 23 — Surah As-Sajdah 32:23

Hakika Sisi tulikwisha mpa Musa Kitabu. Basi usiwe na shaka kuwa kakipokea. Na tukakifanya kuwa ni uwongofu kwa Wana wa Israili

Verse 24 — Surah As-Sajdah 32:24

Na tukawafanya miongoni mwao waongozi wanao ongoa watu kwa amri yetu, walipo subiri na wakawa na yakini na Ishara zetu

Verse 25 — Surah As-Sajdah 32:25

Hakika Mola wako Mlezi ndiye atakaye fafanua baina yao Siku ya Kiyama katika waliyo kuwa wakikhitalifiana

Verse 26 — Surah As-Sajdah 32:26

Je! Haijawabainikia kwamba kaumu ngapi tuliziangamiza kabla yao, nao wanapita katika maskani zao hizo? Hakika katika hayo zipo Ishara. Basi, je, hawasikii

Verse 27 — Surah As-Sajdah 32:27

Je! Hawaoni ya kwamba tunayapeleka maji kwenye ardhi kavu, kisha kwayo tunaitoa mimea wanayo kula wanyama wao na wao wenyewe? Je! Hawaoni

Verse 28 — Surah As-Sajdah 32:28

Wanasema: Ushindi huu ni lini, kama mnasema kweli

Verse 29 — Surah As-Sajdah 32:29

Sema: Siku ya Ushindi, wale walio kufuru imani yao haitawafaa kitu, wala wao hawatapewa muhula

Verse 30 — Surah As-Sajdah 32:30

Basi wapuuze, nawe ngonja; hakika wao wanangoja