Back to Languages

Swahili - Chapter 40 - Ghafir

Translation by Ali Muhsin Al Barwani — Permalink

Verse 1 — Surah Ghafir 40:1

Verse 2 — Surah Ghafir 40:2

Uteremsho wa Kitabu umetoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mwenye kujua

Verse 3 — Surah Ghafir 40:3

Anaye samehe dhambi na anaye pokea toba, Mkali wa kuadhibu, Mwenye ukarimu, hakuna mungu ila Yeye; marejeo ni kwake

Verse 4 — Surah Ghafir 40:4

Hawazibishi Ishara za Mwenyezi Mungu ila walio kufuru; basi kusikughuri wewe kutanga tanga kwao katika nchi

Verse 5 — Surah Ghafir 40:5

Kabla yao walikadhibisha kaumu ya Nuhu na makundi mengine baada yao. Na kila taifa lilikuwa na hamu juu ya Mtume wao wamkamate. Na walibishana kwa upotovu ili kuipindua haki. Kwa hivyo niliwakamata. Basi ilikuwaje adhabu yangu

Verse 6 — Surah Ghafir 40:6

Namna hivi limewathibitikia makafiri neno la Mola wako Mlezi ya kwamba wao ni watu wa Motoni

Verse 7 — Surah Ghafir 40:7

Wale wanao beba A'rshi, na wanao izunguka, wanamsabihi na kumhimidi Mola wao Mlezi, na wanamuamini, na wanawaombea msamaha walio amini kwa kusema: Mola wetu Mlezi! Umekienea kila kitu kwa rehema na ujuzi. Basi wasamehe walio tubu na wakaifuata Njia yako, na waepushe na adhabu ya Jahannamu

Verse 8 — Surah Ghafir 40:8

Mola wetu Mlezi! Na waingize katika Bustani za Milele ulizo waahidi. Na uwape haya pia wale walio fanya mema miongoni mwa wazee wao na wake zao na dhuriya zao. Hakika Wewe ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima

Verse 9 — Surah Ghafir 40:9

Na waepushe na maovu; kwani umwepushaye maovu siku hiyo, hakika umemrehemu; na huko ndiko kufuzu kukubwa

Verse 10 — Surah Ghafir 40:10

Kwa hakika wale walio kufuru watanadiwa: Bila ya shaka kukuchukieni Mwenyezi Mungu ni kukubwa kuliko kujichukia nyinyi nafsi zenu, mlipo kuwa mnaitwa kwenye Imani nanyi mkakataa

Verse 11 — Surah Ghafir 40:11

Watasema: Mola wetu Mlezi! Umetufisha mara mbili, na umetuhuisha mara mbili! Basi tunakiri madhambi yetu. Basi je, ipo njia ya kutoka

Verse 12 — Surah Ghafir 40:12

Hayo ni hivyo kwa sababu mlikuwa akiombwa Mwenyezi Mungu peke yake mnakataa. Na akishirikishwa mnaamini. Basi hukumu ni ya Mwenyezi Mungu Mtukufu Mkuu

Verse 13 — Surah Ghafir 40:13

Yeye ndiye anaye kuonyesheni Ishara zake, na anakuteremshieni kutoka mbinguni riziki. Na hapana anaye kumbuka ila anaye rejea

Verse 14 — Surah Ghafir 40:14

Basi mwombeni Mwenyezi Mungu mkimsafia Dini Yeye tu, na wangachukia makafiri

Verse 15 — Surah Ghafir 40:15

Yeye ndiye Mwenye vyeo vya juu, Mwenye A'rshi. Hupeleka Roho kwa amri yake juu ya amtakaye katika waja wake, ili kuonya kwa Siku ya Mkutano

Verse 16 — Surah Ghafir 40:16

Siku watakayo dhihiri wao. Hapana kitacho fichikana chochote chao kwa Mwenyezi Mungu. Ufalme ni wa nani leo? Ni wa Mwenyezi Mungu Mmoja Mtenda nguvu

Verse 17 — Surah Ghafir 40:17

Leo kila nafsi italipwa kwa iliyo chuma. Hapana dhulma leo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu

Verse 18 — Surah Ghafir 40:18

Na waonye siku inayo kurubia, wakati nyoyo zitakapo fika kooni, nao wamejaa huzuni. Madhaalimu hawatakuwa na rafiki, wala mwombezi wa kuitikiwa

Verse 19 — Surah Ghafir 40:19

(Mwenyezi Mungu) anajua khiyana ya macho na yanayo ficha vifua

Verse 20 — Surah Ghafir 40:20

Na Mwenyezi Mungu huhukumu kwa haki; lakini hao wanao waomba badala yake hawahukumu chochote. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia Mwenye kuona

Verse 21 — Surah Ghafir 40:21

Kwani hawatembei katika ardhi wakaona jinsi ulivyo kuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao? Hao walikuwa wamewazidi hawa kwa nguvu na athari katika nchi. Na Mwenyezi Mungu aliwatia mkononi kwa sababu ya madhambi yao. Na wala hapakuwa wa kuwalinda na Mwenyezi Mungu

Verse 22 — Surah Ghafir 40:22

Hayo ni kwa sababu walikuwa wanawajia Mitume wao kwa hoja zilizo wazi, lakini wakawakataa, ndipo Mwenyezi Mungu akawakamata. Bila ya shaka Yeye ni Mwenye nguvu, Mkali wa kuadhibu

Verse 23 — Surah Ghafir 40:23

Na kwa yakini tulimtuma Musa pamoja na Ishara zetu na uthibitisho ulio wazi

Verse 24 — Surah Ghafir 40:24

Kumwendea Firauni na Hamana na Qaruni, wakasema: Huyu ni mchawi, mwongo mkubwa

Verse 25 — Surah Ghafir 40:25

Basi alipo waletea Haki inayo toka kwetu, walisema: Waueni watoto wanaume wa wale walio muamini na wawacheni hai wanawake wao. Na haviwi vitimbi vya makafiri ila katika upotovu

Verse 26 — Surah Ghafir 40:26

Na Firauni akasema: Niachieni nimuuwe Musa, naye amwite Mola wake Mlezi! Mimi nachelea asije kubadilishieni dini yenu, au akatangaza uharibifu katika nchi

Verse 27 — Surah Ghafir 40:27

Na Musa akasema: Mimi najikinga kwa Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi anilinde na kila mwenye jeuri asiye iamini Siku ya Hisabu

Verse 28 — Surah Ghafir 40:28

Na akasema mtu mmoja Muumini, aliye kuwa mmoja katika watu wa Firauni aliye ficha Imani yake: Mtamuuwa mtu kwa sababu anasema Mola wangu Mlezi ni Mwenyezi Mungu? Na hali naye amekujieni na hoja zilizo wazi? Na akiwa yeye mwongo basi uwongo wake ni juu yake mwenyewe, na akiwa mkweli yatakufikieni baadhi ya hayo anayo kuahidini. Hakika Mwenyezi Mungu hamwongoi apindukiaye mipaka, mwongo mkubwa

Verse 29 — Surah Ghafir 40:29

Enyi watu wangu! Leo mna ufalme, mmeshinda katika nchi; basi ni nani atakaye nisaidia kutuokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu kama ikitufikia? Firauni akasema: Sikupeni shauri ila ile niliyo iona, wala sikuongozeni ila kwenye njia ya uwongofu

Verse 30 — Surah Ghafir 40:30

Na akasema yule aliye amini: Enyi watu wangu! Hakika mimi nakukhofieni mfano wa siku za makundi

Verse 31 — Surah Ghafir 40:31

Mfano wa hali ya watu wa Nuhu na A'di na Thamudi na wale wa baada yao. Na Mwenyezi Mungu hataki kuwadhulumu waja

Verse 32 — Surah Ghafir 40:32

Na enyi watu wangu! Hakika mimi nakukhofieni Siku ya mayowe

Verse 33 — Surah Ghafir 40:33

Siku mtakapo geuka kurudi nyuma. Hamtakuwa na wa kukulindeni kwa Mwenyezi Mungu. Na mwenye kuhukumiwa na Mwenyezi Mungu kupotea, basi huyo hana wa kumwongoa

Verse 34 — Surah Ghafir 40:34

Na alikwisha wajieni Yusuf zamani kwa dalili zilizo wazi, lakini nyinyi mliendelea katika shaka kwa yale aliyo kuleteeni; mpaka alipo kufa mkasema: Mwenyezi Mungu hataleta kabisa Mtume baada yake. Kama hivyo Mwenyezi Mungu humwacha kupotea anaye pindukia mipaka katika maasi anaye jitia shaka

Verse 35 — Surah Ghafir 40:35

Hao ambao wanajadiliana katika Ishara za Mwenyezi Mungu pasipo ushahidi wowote ulio wafikia, ni chukizo kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya walio amini. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu apigavyo muhuri juu ya kila moyo wa jeuri anaye jivuna

Verse 36 — Surah Ghafir 40:36

Na Firauni akasema: Ewe Hamana! Nijengee mnara ili nipate kuzifikia njia

Verse 37 — Surah Ghafir 40:37

Njia za mbinguni ili nikamwone Mungu wa Musa. Na kwa hakika mimi bila ya shaka namjua kuwa ni mwongo tu. Na hivi ndivyo Firauni alivyo pambiwa ubaya wa vitendo vyake, na akazuiliwa Njia. Na vitimbi vya Firauni havikuwa ila katika kuangamia tu

Verse 38 — Surah Ghafir 40:38

Na yule aliye amini alisema: Enyi watu wangu! Nifuateni mimi, nitakuongozeni njia ya uwongozi mwema

Verse 39 — Surah Ghafir 40:39

Enyi watu wangu! Hakika haya maisha ya dunia ni starehe ipitayo tu, na hakika Akhera ndiyo nyumba ya daima

Verse 40 — Surah Ghafir 40:40

Mwenye kutenda uovu hatalipwa ila sawa na huo uwovu wake, na anaye tenda wema, akiwa mwanamume au mwanamke, naye ni Muumini, basi hao wataingia Peponi, waruzukiwe humo bila ya hisabu

Verse 41 — Surah Ghafir 40:41

Na enyi watu wangu! Kwa nini mimi nakuiteni kwenye uwokofu, nanyi mnaniita kwenye Moto

Verse 42 — Surah Ghafir 40:42

Mnaniita nimkufuru Mwenyezi Mungu na nimshirikishe na yule ambaye simjui, nami nakuiteni kwa Mwenye nguvu Mwenye kusamehe

Verse 43 — Surah Ghafir 40:43

Bila ya shaka mnaye niitia kumuabudu hastahiki wito duniani wala Akhera. Na hakika marejeo yetu ni kwa Mwenyezi Mungu. Na wanao pindukia mipaka ndio watu wa Motoni

Verse 44 — Surah Ghafir 40:44

Basi mtayakumbuka ninayo kuambieni. Nami namkabidhi Mwenyezi Mungu mambo yangu. Hakika Mwenyezi Mungu anawaona waja wake

Verse 45 — Surah Ghafir 40:45

Basi Mwenyezi Mungu akamlinda na ubaya wa hila walizo zifanya. Na adhabu mbaya itawazunguka watu wa Firauni

Verse 46 — Surah Ghafir 40:46

Wanaonyeshwa Moto asubuhi na jioni. Na itapo fika Saa ya Kiyama patasemwa: Waingizeni watu wa Firauni katika adhabu kali kabisa

Verse 47 — Surah Ghafir 40:47

Na watapo hojiana huko Motoni, wanyonge watawaambia walio jitukuza: Hakika sisi tulikuwa wafuasi wenu, basi je, hamtuondolei sehemu ya huu Moto

Verse 48 — Surah Ghafir 40:48

Watasema walio jitukuza: Hakika sote sisi tumo humo humo! Kwani Mwenyezi Mungu kesha hukumu baina ya waja

Verse 49 — Surah Ghafir 40:49

Na walio Motoni watawaambia walinzi wa Jahannamu: Mwombeni Mola wenu Mlezi atupunguzie walau siku moja ya adhabu

Verse 50 — Surah Ghafir 40:50

Nao watasema: Je! Hawakuwa wakikufikieni Mitume wenu kwa hoja zilio wazi? Watasema: Kwani? Watasema: Basi ombeni! Na maombi ya makafiri hayawi ila ni kupotea bure

Verse 51 — Surah Ghafir 40:51

Hakika bila ya shaka Sisi tunawanusuru Mitume wetu na walio amini katika uhai wa duniani na siku watapo simama Mashahidi

Verse 52 — Surah Ghafir 40:52

Siku ambayo hautawafaa madhaalimu udhuru wao, nao watapata laana, na watapata makaazi mabaya kabisa

Verse 53 — Surah Ghafir 40:53

Na kwa hakika tulimpa Musa uwongofu, na tukawarithisha Wana wa Israili Kitabu

Verse 54 — Surah Ghafir 40:54

Ambacho ni Uwongofu na Ukumbusho kwa wenye akili

Verse 55 — Surah Ghafir 40:55

Basi subiri. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli. Na omba msamaha kwa dhambi zako, na umtakase Mola wako Mlezi kwa kumhimidi jioni na asubuhi

Verse 56 — Surah Ghafir 40:56

Hakika hao wanao bishana katika Ishara za Mwenyezi Mungu bila ya uthibitisho wowote uliyo wajia, hawana vifuani mwao ila kutaka ukubwa tu, na wala huo hawaufikilii. Basi jikinge kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona

Verse 57 — Surah Ghafir 40:57

Bila ya shaka kuumba mbingu na ardhi ni kukubwa zaidi kuliko kuwaumba watu. Lakini watu wengi hawajui

Verse 58 — Surah Ghafir 40:58

Na kipofu na mwenye kuona hawalingani; na walio amini na watendao mema hawalingani na muovu. Ni machache mnayo yakumbuka

Verse 59 — Surah Ghafir 40:59

Hakika Saa (ya Kiyama) itafika, nayo haina shaka. Lakini watu wengi hawaamini

Verse 60 — Surah Ghafir 40:60

Na Mola wenu Mlezi anasema: Niombeni nitakuitikieni. Kwa hakika wale ambao wanajivuna na kuniabudu Mimi wataingia Jahannamu wadhalilike

Verse 61 — Surah Ghafir 40:61

Mwenyezi Mungu aliye kufanyieni usiku ili mpate kutulia humo, na mchana wa kuonea. Hakika Mwenyezi Mungu bila ya shaka ni Mwenye fadhila juu ya watu, lakini watu wengi hawashukuru

Verse 62 — Surah Ghafir 40:62

Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi, Muumba wa kila kitu. Hapana mungu ila Yeye; basi mnageuzwa wapi

Verse 63 — Surah Ghafir 40:63

Namna hivi ndivyo walivyo geuzwa walio kuwa wakizikataa Ishara za Mwenyezi Mungu

Verse 64 — Surah Ghafir 40:64

Ni Mwenyezi Mungu aliye kufanyieni ardhi kuwa ni pahala pa kukaa, na mbingu kuwa dari. Na akakutieni sura, na akazifanya nzuri sura zenu, na akakuruzukuni vitu vizuri. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote

Verse 65 — Surah Ghafir 40:65

Yeye ndiye aliye Hai - hapana mungu isipo kuwa Yeye. Basi muabuduni Yeye mkimsafishia Dini Yeye. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote

Verse 66 — Surah Ghafir 40:66

Sema: Mimi nimekatazwa kuwaabudu hao mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu, zilipo nijia hoja zilizo dhaahiri kutokana na Mola wangu Mlezi. Na nimeamrishwa nisilimu kwa Mola wa walimwengu wote

Verse 67 — Surah Ghafir 40:67

Yeye ndiye aliye kuumbeni kwa udongo, kisha kwa tone la manii, kisha kwa pande la damu, kisha akakutoeni katika hali ya mtoto mchanga, kisha mpate kufikilia utu uzima, kisha mpate kuwa wazee. Na kati yenu wapo wanao kufa kabla, na ili mfikie muda ulio kwisha wekwa, na ili mpate kufahamu

Verse 68 — Surah Ghafir 40:68

Yeye ndiye anaye huisha na anaye fisha. Akihukumu jambo liwe, basi huliambia: Kuwa! Likawa

Verse 69 — Surah Ghafir 40:69

Je! Huwaoni wale wanao bishana katika Ishara za Mwenyezi Mungu? Wanageuziwa wapi

Verse 70 — Surah Ghafir 40:70

Ambao wamekanusha Kitabu na yale tuliyo watuma Mitume wetu. Basi watakuja jua

Verse 71 — Surah Ghafir 40:71

Zitakapo kuwa pingu shingoni mwao na minyororo, huku wanabururwa

Verse 72 — Surah Ghafir 40:72

Katika maji ya moto, kisha wanaunguzwa Motoni

Verse 73 — Surah Ghafir 40:73

Tena wataambiwa: Wako wapi mlio kuwa mkiwashirikisha

Verse 74 — Surah Ghafir 40:74

Badala ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Wametupotea, bali tangu zamani hatukuwa tukiomba kitu! Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anawaachia makafiri wapotelee mbali

Verse 75 — Surah Ghafir 40:75

Haya ni kwa sababu mlikuwa mkijitapa katika ardhi pasipo haki, na kwa sababu mlikuwa mkijishaua

Verse 76 — Surah Ghafir 40:76

Ingieni kwenye milango ya Jahannamu, mdumu humo milele. Basi ni maovu yaliyoje makaazi ya wanao takabari

Verse 77 — Surah Ghafir 40:77

Basi subiri, hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. Na ama tukikuonyesha baadhi ya yale tuliyo waahidi au tukikufisha, lakini wao watarudishwa kwetu tu

Verse 78 — Surah Ghafir 40:78

Na bila ya shaka tuliwatuma Mitume kabla yako. Wengine katika hao tumekusimulia khabari zao, na wengine hatukukusimulia. Na haiwi Mtume alete Ishara yoyote ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Basi ikija amri ya Mwenyezi Mungu huhukumiwa kwa Haki, na hapo wapotofu watakhasiri

Verse 79 — Surah Ghafir 40:79

Mwenyezi Mungu aliye kujaalieni nyama hoa, mifugo, ili muwapande baadhi yao, na muwale baadhi yao

Verse 80 — Surah Ghafir 40:80

Na katika hao mnayo manufaa kadhaa wa kadhaa, na mnapata kwao haja ziliomo vifuani mwenu; na mnachukuliwa juu yao, na juu ya marikebu

Verse 81 — Surah Ghafir 40:81

Naye anakuonyesheni Ishara zake. Basi Ishara gani za Mwenyezi Mungu mnazo zikataa

Verse 82 — Surah Ghafir 40:82

Kwani hawatembei katika ardhi wakaona ulikuwaje mwisho wa walio kuwa kabla yao? Wao walikuwa wengi kuliko hawa, na wamewashinda kwa nguvu na athari katika nchi. Wala hayakuwafaa hayo waliyo kuwa wakiyachuma

Verse 83 — Surah Ghafir 40:83

Walipo wajia Mitume wao kwa dalili zilizo wazi walijitapa kwa ilimu waliyo kuwa nayo. Basi yakawazunguka waliyo kuwa wakiyafanyia maskhara

Verse 84 — Surah Ghafir 40:84

Walipo iona adhabu yetu walisema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu kuwa ni wa pekee, na tunaikataa miungu tuliyo kuwa tukiishirikisha naye

Verse 85 — Surah Ghafir 40:85

Lakini imani yao haikuwa yenye kuwafaa kitu wakati ambao wamekwisha iona adhabu yetu. Huu ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu ulio kuwa kwa waja wake. Na hapo walio kufuru walikhasiri