Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliye umba mbingu na ardhi, na akafanya giza na mwangaza. Tena baada ya haya walio kufuru wanawafanya wengine sawa na Mola wao Mlezi
Jee, hawaoni vizazi vingapi tulivyo viangamiza kabla yao? Tuliwaweka katika nchi tusivyo kuwekeni nyinyi; tukawapelekea mvua nyingi na tukaifanya mito inapita chini yao. Mwishoe tukawaangamiza kwa madhambi yao; na tukaanzisha baada yao kizazi kingine
Na wao husema: Mbona hakuteremshiwa Malaika? Na kama tungeli teremsha Malaika, basi bila ya shaka ingesha hukumiwa amri, tena hapo wasingeli pewa muhula
Sema: Ni vya nani viliomo katika mbingu na katika ardhi? Sema: Ni vya Mwenyezi Mungu. Yeye amejilazimisha nafsi yake kurehemu. Hakika atakukusanyeni Siku ya Kiyama isiyo kuwa na shaka. Walio jikhasiri wenyewe hawaamini
Sema: Je, nimchukue rafiki mlinzi asiye kuwa Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye Muumba mbingu na ardhi, naye ndiye anaye lisha wala halishwi? Sema: Mimi nimeamrishwa niwe wa kwanza wa wenye kusilimu. Na wala kabisa usiwe miongoni wa washirikina
Na ikiwa Mwenyezi Mungu akikugusisha madhara, basi hapana wa kukuondolea hayo ila Yeye. Na ikiwa akikugusisha kheri, basi Yeye ndiye Mwenye uweza wa kila kitu
Sema: Kitu gani ushahidi wake mkubwa kabisa? Sema: Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye shahidi baina yangu na nyinyi. Na nimefunuliwa Qur'ani hii ili kwayo nikuonyeni nyinyi na kila inayo mfikia. Ati kweli nyinyi mnashuhudia kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu wapo miungu wengine? Sema: Mimi sishuhudii hayo. Sema: Hakika Yeye ni Mungu mmoja tu, nami ni mbali na mnao washirikisha
Na wapo miongoni mwao wanao kusikiliza; na tumezitia pazia nyoyo zao wasije kuyafahamu. Na upo uziwi masikioni mwao, na wakiona kila Ishara hawaiamini. Hata wakikujia kwa kujadiliana nawe, wanasema walio kufuru: Hizi si chochote ila hadithi za watu wa kale
Na unge ona watakapo simamishwa kwenye Moto, wakawa wanasema: Laiti tungeli rudishwa, wala hatutakanusha tena Ishara za Mola wetu Mlezi, na tutakuwa miongoni wa Waumini
Bali yamewadhihirikia waliyo kuwa wakiyaficha zamani. Na kama wangeli rudishwa bila ya shaka wange yarejea yale yale waliyo katazwa. Na hakika hao ni waongo
Na lau ungeli ona watavyo simamishwa mbele ya Mola wao Mlezi, akawaambia: Je, si kweli haya? Na wao watasema: Kwani? Tunaapa kwa Mola Mlezi wetu ni kweli. Yeye atasema: Basi onjeni adhabu kwa sababu ya vile mlivyo kuwa mnakataa
Hakika wamekhasirika walio kanusha kukutana na Mwenyezi Mungu, mpaka ilipo wajia Saa kwa ghafla, wakasema: Ole wetu kwa tuliyo yapuuza! Nao watabeba mizigo yao juu ya migongo yao. Ni maovu hayo wanayo yabeba
Na hakika walikanushwa Mitume wa kabla yako. Nao wakavumilia kule kukanushwa, na kuudhiwa, mpaka ilipo wafikia nusura yetu. Na hapana wa kubadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu. Na bila ya shaka zimekujia baadhi ya khabari za Mitume hao
Na ikiwa ni makubwa kwako huku kukataa kwao, basi kama unaweza kutafuta njia ya chini kwa chini ya ardhi, au ngazi kwendea mbinguni ili uwaletee Ishara -- Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angependa angeli wakusanya kwenye uwongofu. Basi usiwe miongoni mwa wasio jua
Na wamesema: Kwa nini hakuteremshiwa muujiza kutoka kwa Mola wake Mlezi? Sema: Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuteremsha muujiza. Lakini wengi wao hawajui
Na hapana mnyama katika ardhi, wala ndege anaye ruka kwa mbawa zake mbili, ila ni umma kama nyinyi. Hatukupuuza Kitabuni kitu chochote. Kisha kwa Mola wao Mlezi watakusanywa
Na walio kanusha Ishara zetu ni viziwi na mabubu waliomo gizani. Mwenyezi Mungu humwachia kupotea amtakaye, na humweka katika Njia iliyo nyooka amtakaye
Basi walipo sahau walio kumbushwa tuliwafungulia milango ya kila kitu. Mpaka walipo furahia yale waliyo pewa tuliwashika kwa ghafla, na mara wakawa wenye kukata tamaa
Sema: Mwaonaje Mwenyezi Mungu akanyakua kusikia kwenu, na kuona kwenu, na akaziziba nyoyo zenu, ni mungu gani asiye kuwa Mwenyezi Mungu ataye kuleteeni hayo tena? Angalia vipi tunavyo zieleza Ishara, kisha wao wanapuuza
Sema: Mimi sikwambiini kuwa ninazo khazina za Mwenyezi Mungu. Wala sijui mambo yaliyo fichikana. Wala sikwambiini kuwa mimi ni Malaika. Mimi sifuati ila yanayo funuliwa kwangu. Sema: Je, wanakuwa sawa, kipofu na mwenye kuona. Basi hamfikiri
Wala usiwafukuze wanao mwomba Mola Mlezi wao asubuhi na jioni kwa kutaka radhi yake. Si juu yako hisabu yao hata kidogo, wala hisabu yako si juu yao hata kidogo, hata uwafukuze na uwe miongoni mwa wenye kudhulumu
Na hivi ndivyo tunavyo wajaribu wao kwa wao, ili waseme: Ni hao ndio Mwenyezi Mungu amewafadhilisha miongoni mwetu? Kwani Mwenyezi Mungu hawajui wanao shukuru
Na wanapo kujia wanao ziamini Ishara zetu waambie: Assalamu alaikum! Amani iwe juu yenu! Mola wenu Mlezi amejilazimisha rehema, ya kwamba atakaye fanya uovu miongoni mwenu kwa ujinga, kisha akatubu baada yake na akatengenea, basi hakika Yeye ni Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu
Sema: Mimi nipo kwenye sharia iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu Mlezi, nanyi mnaikanusha. Mimi sinacho hicho mnacho kihimiza. Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu. Yeye anasimulia yaliyo kweli; naye ni Mbora wa kuhukumu kuliko wote
Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye tu. Na Yeye anajua kilioko nchi kavu na baharini. Na halidondoki jani ila analijua. Wala punje katika giza la ardhi, wala kinyevu, wala kikavu ila kimo katika Kitabu kinacho bainisha
Naye ndiye anaye kufisheni usiku, na anakijua mlicho fanya mchana. Kisha Yeye hukufufueni humo mchana ili muda ulio wekwa utimizwe. Kisha kwake Yeye ndiyo marejeo yenu, na tena akwambieni mliyo kuwa mkiyafanya
Naye ndiye Mwenye nguvu za kushinda, aliye juu ya waja wake. Na hukupelekeeni waangalizi, mpaka mmoja wenu yakimjia mauti wajumbe wetu humfisha, nao hawafanyi taksiri
Sema: Ni nani anaye kuokoeni katika giza la nchi kavu na baharini? Mnamwomba kwa unyenyekevu na kwa siri, mkisema: Kama akituokoa na haya bila ya shaka tutakuwa miongoni mwa wanao shukuru
Sema: Yeye ndiye Muweza wa kukuleteeni adhabu kutoka juu yenu au kutoka chini ya miguu yenu, au kukuleteeni fujo la mfarakano, na kuwaonjesha baadhi yenu jeuri ya wenzao. Tazama vipi tunavyo zieleza Aya ili wapate kufahamu
Na unapo waona wanao ziingilia Aya zetu, basi jitenge nao mpaka waingilie mazungumzo mengine. Na kama Shet'ani akikusahaulisha, basi baada ya kutanabahi usikae pamoja na watu madhaalimu
Waachilie mbali walio ifanya dini yao ni mchezo na pumbao, na uhai wa dunia ukawaghuri. Nawe kumbusha kwayo, isije nafsi ikaangamizwa kwa sababu ya iliyo yachuma, nayo haina mlinzi wala mwombezi ila Mwenyezi Mungu. Na ingatoa kila fidia haitokubaliwa. Hao ndio walio angamizwa kwa sababu ya yale waliyo yachuma. Wao watapata kinywaji cha maji ya moto kabisa, na adhabu chungu
Sema: Je, tumuombe asiye kuwa Mwenyezi Mungu ambae hatufai wala hatudhuru, na turejee nyuma baada ya Mwenyezi Mungu kwisha tuhidi? Tuwe kama ambao mashet'ani wamempumbaza katika ardhi, amebabaika? Anao marafiki wanao mwita ende kwenye uwongofu, wakimwambia: Njoo kwetu! Sema: Hakika uwongofu wa Mwenyezi Mungu ndio Uwongofu. Nasi tumeamrishwa tusilimu kwa Mola Mlezi wa viumbe vyote
Naye ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi kwa Haki. Na anaposema: Kuwa! Basi huwa. Kauli yake ni Haki. Na ufalme wote ni wake Siku litapo pulizwa barugumu, Mjuzi wa yaliyo fichikana na yanayo onekana. Naye ndiye Mwenye hikima na Mwenye khabari
Na alipo liona jua linachomoza akasema: Huyu ndiye Mola Mlezi wangu. Huyu mkubwa kuliko wote. Lilipo tua, alisema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika hayo mnayo fanyia ushirikina
Na watu wake wakamhoji. Akasema: Je, mnanihoji juu ya Mwenyezi Mungu, na hali Yeye ameniongoa? Wala siogopi hao mnao washirikisha naye, ila Mola wangu Mlezi akipenda kitu. Mola wangu Mlezi amekusanya ilimu ya kila kitu. Basi je, hamkumbuki
Na vipi nivikhofu hivyo mnavyo vishirikisha, hali nyinyi hamkhofu kuwa nyinyi mmemshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu ambacho hakukiteremshia uthibitisho. Basi kundi gani katika mawili haya lina haki zaidi kupata amani, kama nyinyi mnajua
Na hizo ndizo hoja zetu tulizo mpa Ibrahim kuhojiana na watu wake. Tunamnyanyua kwa vyeo tumtakaye. Hakika Mola Mlezi wako ni Mwenye hikima na Mwenye ujuzi
Na tukamtunukia (Ibrahim) Is-haq na Yaakub. Kila mmoja wao tulimwongoa. Na Nuhu tulimwongoa kabla. Na katika kizazi chake tulimwongoa Daud na Suleiman na Ayyub na Yusuf na Musa na Harun. Na hivi ndivyo tunavyo walipa wafanyao wema
Na hawakumkadiria Mwenyezi Mungu kwa haki ya kadri yake, walipo sema: Mwenyezi Mungu hakumteremshia mwanaadamu chochote. Sema: Nani aliyo teremsha Kitabu alicho kuja nacho Musa, chenye nuru na uwongofu kwa watu, mlicho kifanya kurasa kurasa mkizionyesha, na mengi mkiyaficha. Na mkafunzwa mlio kuwa hamyajui nyinyi wala baba zenu? Sema: Mwenyezi Mungu. Kisha waache wacheze katika porojo lao
Na hiki ni Kitabu tulicho kiteremsha, kilicho barikiwa, chenye kuhakikisha yaliyo tangulia, na ili uuwonye Mama wa Miji na walio pembezoni mwake. Na wenye kuamini Akhera wanakiamini hichi, nao wanazihifadhi Sala zao
Nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzuliya uwongo Mwenyezi Mungu, au anaye sema: Mimi nimeletewa wahyi; na hali hakuletewa wahyi wowote. Na yule anaye sema: Nitateremsha kama alivyo teremsha Mwenyezi Mungu. Na lau ungeli waona madhaalimu wanavyo kuwa katika mahangaiko ya mauti, na Malaika wamewanyooshea mikono wakiwambia: Zitoeni roho zenu! Leo mtalipwa adhabu ya fedheha kwa sababu ya mliyo kuwa mkiyasema juu ya Mwenyezi Mungu yasiyo ya haki, na mlivyo kuwa mkizifanyia kiburi Ishara zake
Nanyi mlitujia wapweke kama tulivyo kuumbeni mara ya kwanza. Na mkayaacha nyuma yenu yote tuliyo kupeni, na wala hatuwaoni hao waombezi wenu, ambao mlidai kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu kwenu. Yamekatika makhusiano baina yenu, na yamekupoteeni mliyo kuwa mkidai
Hakika Mwenyezi Mungu ndiye mpasuaji mbegu na kokwa, zikachipua. Humtoa aliye hai kutoka maiti, naye ni mtoaji maiti kutokana na aliye hai. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu. Basi vipi mnageuzwa
Ndiye anaye pambazua mwangaza wa asubuhi; na ameufanya usiku kwa mapumziko na utulivu, na jua na mwezi kwenda kwa hisabu. Hayo ndiyo makadirio ya Aliye tukuka Mwenye nguvu, Mwenye ujuzi
Na Yeye ndiye aliye kuzalisheni kutokana na nafsi moja. Pako pahali pa kutulia na pa kupita njia. Hakika tumezichambua Ishara hizi kwa watu wanao fahamu
Na Yeye ndiye anaye teremsha maji kutoka mbinguni; na kwayo tunatoa mimea ya kila kitu. Kutokana na baadhi yao tukatoa mimea ya majani, tukatoa ndani yake punje zilizo pandana; na kutokana na mitende yakatoka kwenye makole yake mashada yaliyo inama; na bustani za mizabibu na mizaituni, na makomamanga, yaliyo fanana na yasiyo fanana. Angalieni matunda yake yanapo zaa na yakawiva. Hakika katika hayo pana Ishara kwa watu wanao amini
Bado wamemfanyia Mwenyezi Mungu majini kuwa washirika wake, na hali Yeye ndiye aliye waumba. Na wakamzulia, bila ya ujuzi wowote, kuwa ana wana wa kiume na wa kike. Subhanahu, Ametakasika na ametukuka juu ya hayo wanayo mbandikiza nayo
Yeye ndiye Muumbaji wa mbingu na ardhi bila ya ruwaza. Itakuwaje awe na mwana naye hakuwa na mke? Naye ndiye aliye umba kila kitu. Naye ni Mwenye kujua kila kitu
Zimekwisha kukujieni hoja wazi kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Basi anaye ona ni kwa faida yake mwenyewe, na anaye pofuka basi ni khasara yake. Nami si mtunzaji wenu
Wala msiwatukane hao wanao waomba badala ya Mwenyezi Mungu, wasije na wao wakamtukana Mwenyezi Mungu kwa jeuri bila ya kujua. Namna hivyo tumewapambia kila umma vitendo vyao. Kisha marejeo yao yatakuwa kwa Mola wao Mlezi, naye atawaambia waliyo kuwa wakiyatenda
Na waliapa kwa Mwenyezi Mungu kwa ukomo wa viapo vyao, kuwa ikiwafikia Ishara wataiamini. Sema: Ishara ziko kwa Mwenyezi Mungu. Na nyinyi hamjui kuwa zitapo kuja hawato amini
NA LAU kuwa tungeli wateremshia Malaika, na maiti wakazungumza nao, na tukawakusanyia kila kitu mbele yao, bado wasingeli amini, ila Mwenyezi Mungu atake. Lakini wengi wao wamo ujingani
Na kadhaalika tumemfanyia kila Nabii maadui mashet'ani wa kiwatu, na kijini, wakifundishana wao kwa wao maneno ya kupamba-pamba, kwa udanganyifu. Na angeli penda Mola wako Mlezi wasingeli fanya hayo. Basi waache na wanayo yazua
Je, nimtafute hakimu ghairi ya Mwenyezi Mungu, naye ndiye aliye kuteremshieni Kitabu kilicho elezwa waziwazi? Na hao tulio wapa Kitabu wanajua ya kwamba kimeteremshwa na Mola wako Mlezi kwa Haki. Basi usiwe katika wanao tia shaka
Na ukiwat'ii wengi katika hawa waliomo duniani watakupoteza na Njia ya Mwenyezi Mungu. Hawa hawafuati ila dhana tu, na hawakuwa ila ni wenye kusema uwongo tu
Na kwa nini msile katika walio somewa jina la Mwenyezi Mungu, naye amekwisha kubainishieni alivyo kuharimishieni, isipo kuwa vile mnavyo lazimishwa? Na hakika wengi wanapoteza kwa matamanio yao bila ya kuwa na ilimu. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Mjuzi kushinda wote kuwajua wanao pindukia mipaka
Wala msile katika wale wasio somewa jina la Mwenyezi Mungu. Kwani huo ni upotofu. Na kwa yakini mashet'ani wanawafunza marafiki zao kubishana nanyi. Na mkiwafuata basi hapana shaka nyinyi mtakuwa washirikina
Je, aliye kuwa maiti kisha tukamhuisha, na tukamjaalia nuru inakwenda naye mbele za watu, mfano wake ni kama aliyoko gizani akawa hata hawezi kutoka humo? Kama hivyo makafiri wamepambiwa waliyo kuwa wakiyafanya
Kadhaalika katika kila mji tumewajaalia wakubwa wa wakosefu wao wafanye vitimbi ndani yake. Na wala hawafanyii vitimbi isipo kuwa nafsi zao, nao hawatambui
Na inapo wajia Ishara, wao husema: Hatutoamini mpaka tupewe mfano wa walio pewa Mitume wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi kuliko wote kujua wapi anaweka ujumbe wake. Itawafikia hao walio kosa udhalili na adhabu kali kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu ya vitimbi walivyo kuwa wakivifanya
Basi yule ambaye Mwenyezi Mungu anataka kumhidi humfungulia kifua chake kwa Uislamu. Na anaye taka apotee hukifanya kifua chake kina dhiki, kimebana, kama kwamba anapanda mbinguni. Namna hivi Mwenyezi Mungu anajaalia uchafu juu ya wasio amini
Na ile Siku atapo wakusanya wote awaambie: Enyi makundi ya majini! Hakika nyinyi mmechukua wafuasi wengi katika wanaadamu. Na marafiki zao katika wanaadamu waseme: Mola Mlezi wetu! Tulinufaishana sisi na wao. Na tumefikia ukomo wetu ulio tuwekea. Basi Mwenyezi Mungu atasema: Moto ndio makaazi yenu, mtadumu humo, ila apendavyo Mwenyezi Mungu. Hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye hikima, na Mwenye kujua
Enyi makundi ya majini na watu! Je, hawakukujieni Mitume kutokana na nyinyi wenyewe wakikubainishieni Aya zangu, na wakikuonyeni mkutano wa Siku yenu hii. Nao watasema: Tumeshuhudia juu ya nafsi zetu. Na yaliwadanganya maisha ya dunia. Nao watajishuhudia wenyewe ya kwamba walikuwa makafiri
Na Mola wako Mlezi ndiye Mkwasi, Mwenye rehema. Akipenda atakuondoeni na awaweke wengine awapendao badala yenu, kama vile alivyo kutoeni kutokana na uzazi wa watu wengine
Na wamemwekea sehemu Mwenyezi Mungu katika mimea na wanyama alio umba, nao husema: Hii ni sehemu ya Mwenyezi Mungu - kwa madai yao - na hii ni ya miungu tunao washirikisha. Basi vile walivyo wakusudia miungu yao havimfikii Mwenyezi Mungu, na vilivyo kuwa vya Mwenyezi Mungu huwafikia miungu yao. Ni uovu kabisa hayo wanayo yahukumu
Na kadhaalika hao washirika wao wamewapambia wengi katika washirikina kuwauwa watoto wao ili kuwaangamiza na kuwavurugia dini yao. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli penda wasinge fanya hayo. Basi waache na hayo wanayo yazua
Nao husema: Wanyama hawa na mimea hii ni mwiko. Hawatokula ila wale tuwapendao - kwa madai yao tu. Na wanyama hawa imeharimishwa migongo yao kupandwa. Na wanyama wengine hawalitaji jina la Mwenyezi Mungu juu yao. Wanamzulia uwongo tu Mwenyezi Mungu. Atawalipa kwa hayo wanayo mzulia
Na husema: Waliomo matumboni mwa wanyama hawa ni kwa ajili ya wanaume wetu tu, na wameharimishwa kwa wake zetu. Lakini ikiwa nyamafu basi wanashirikiana. Mwenyezi Mungu atawalipa kwa maelezo yao hayo. Hakika Yeye ni Mwenye hikima, Mwenye kujua
Hakika wamekhasirika wale ambao wamewauwa watoto wao kwa upumbavu pasipo kujua, na wakaharimisha alivyo waruzuku Mwenyezi Mungu kwa kumzulia Mwenyezi Mungu. Hakika wamepotea, wala hawakuwa wenye kuongoka
Na Yeye ndiye aliye ziumba bustani zenye kutambaa juu ya chanja, na zisio tambaa, na mitende, na mimea yenye matunda mbali mbali, na mizaituni na mikomamanga inayo fanana na isiyo fanana. Kuleni matunda yake inapo zaa, na toeni haki yake siku ya kuvunwa kwake. Wala msitumie kwa fujo. Hakika Yeye hawapendi watumiayo kwa fujo
Na katika wanyama amekujaalieni wenye kubeba mizigo na kutoa matandiko. Kuleni katika alivyo kuruzukuni Mwenyezi Mungu, wala msifuate nyayo za Shet'ani. Hakika yeye ni adui yenu dhaahiri
Amekuumbieni namna nane za wanyama: Wawili katika kondoo, na wawili katika mbuzi. Sema je, ameharimisha yote madume wawili au majike wawili, au waliomo matumboni mwa majike yote mawili? Niambieni kwa ilimu ikiwa nyinyi mnasema kweli
Na wawili katika ngamia, na wawili katika ng'ombe. Sema: Je, ameharimisha yote madume wawili au majike wawili, au waliomo matumboni mwa yote majike? Au, nyinyi mlikuwapo Mwenyezi Mungu alipo kuusieni haya? Basi ni nani dhaalimu mkubwa kuliko yule aliye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo, kwa ajili ya kuwapoteza watu bila ya ilimu? Hakika Mwenyezi Mungu hawahidi watu madhaalimu
Sema: Sioni katika yale niliyo funuliwa mimi kitu kilicho harimishwa kwa mlaji kukila isipo kuwa kiwe ni nyamafu, au damu inayo mwagika, au nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni uchafu; au kwa upotofu kimechinjwa kwa jina la asiye kuwa Mwenyezi Mungu. Lakini mwenye kushikwa na dharura, bila ya kutamani wala kupita mipaka, basi hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu
Na wale walio fuata dini ya Kiyahudi tumewaharimishia kila mwenye kucha. Na katika ng'ombe na kondoo na mbuzi tumewaharimishia shahamu yao, isipo kuwa ile iliyo beba migongo yao au matumbo yao, au iliyo gandamana na mifupa. Tuliwalipa hivyo kwa sababu ya uasi wao. Na bila ya shaka Sisi ndio wasema kweli
Watasema walio shirikisha: Lau kuwa Mwenyezi Mungu ange taka tusingeli shiriki sisi, wala baba zetu; wala tusingeli harimisha kitu chochote. Vivi hivi walikanusha walio kuwa kabla yao mpaka walipo onja adhabu yetu. Sema: Je, nyinyi mnayo ilimu mtutolee? Nyinyi hamfuati ila dhana. Wala hamsemi ila uwongo tu
Sema: Leteni mashahidi wenu watao shuhudia kuwa Mwenyezi Mungu ameharimisha hawa. Basi wakishuhudia, wewe usishuhudie pamoja nao. Wala usifuate matamanio ya walio zikanusha Ishara zetu, wala hawaiamini Akhera, na ambao wanamlinganisha Mola Mlezi wao na wengine
Sema: Njooni nikusomeeni aliyo kuharimishieni Mola wenu Mlezi. Nayo ni kuwa, msimshirikishe Yeye na chochote. Na wazazi wenu wafanyieni wema. Wala msiwauwe watoto wenu kwa sababu ya umasikini. Sisi tunakuruzukuni nyinyi na wao. Wala msikaribie mambo machafu, yanayo onekana, na yanayo fichikana. Wala msiuwe nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameharimisha kuiuwa, ila ikiwa kwa haki. Hayo amekuusieni ili myatie akilini
Wala msiyakaribie mali ya yatima ila kwa njia ya wema kabisa, mpaka afikilie utu-uzima. Na timizeni vipimo na mizani kwa uadilifu. Sisi hatumkalifishi mtu ila kwa kadiri ya uwezo wake. Na msemapo semeni kwa uadilifu ingawa ni jamaa. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu itekelezeni. Hayo amekuusieni ili mpate kukumbuka
Na kwa hakika hii ndiyo Njia yangu Iliyo Nyooka. Basi ifuateni, wala msifuate njia nyingine, zikakutengeni na Njia yake. Haya amekuusieni ili mpate kuchamngu
Tena tulimpa Musa Kitabu kwa kumtimizia (neema) aliye fanya wema, na kuwa ni maelezo ya kila kitu, na uwongofu na rehema, ili wapate kuamini mkutano wao na Mola wao Mlezi
Au mkasema: Lau kuwa tumeteremshiwa sisi Kitabu tungeli kuwa waongofu zaidi kuliko wao. Basi imekufikieni bayana kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na uwongofu, na rehema. Basi nani aliye dhaalimu mkubwa zaidi kuliko yule anaye kanusha Ishara za Mwenyezi Mungu, na akajitenga nazo? Tutawalipa wanao jitenga na Ishara zetu adhabu kali kabisa kwa sababu ya kujitenga kwao
Wanangoja jengine ila wawafikie Malaika, au awafikie Mola wako Mlezi, au zifike baadhi ya Ishara za Mola wako Mlezi? Siku zitakapo fika baadhi ya Ishara za Mola wako Mlezi, kuamini hapo hakutomfaa mtu kitu, ikiwa hakuwa ameamini kabla yake, au amefanya kheri katika Imani yake. Sema: Ngojeni, nasi pia tunangoja
Hakika walio igawa Dini yao na wakawa makundi makundi, huna ukhusiano nao wowote. Bila ya shaka shauri yao iko kwa Mwenyezi Mungu; kisha atawaambia yale waliyo kuwa wakiyatenda
Sema: Kwa hakika mimi Mola wangu Mlezi ameniongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka, Dini iliyo sawa kabisa, ambayo ndiyo mila ya Ibrahim aliye kuwa mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina
Sema: Je nitafute Mola Mlezi asiye kuwa Mwenyezi Mungu, na hali Yeye ndiye Mola Mlezi wa kila kitu? Na kila nafsi haichumii ila nafsi yake. Na habebi mwenye kubeba mzigo wa mwenziwe. Kisha marejeo yenu ni kwa Mola wenu Mlezi, naye atakuambieni mliyo kuwa mkikhitalifiana
Naye ndiye aliye kufanyeni makhalifa wa duniani, na amewanyanyua baadhi yenu juu ya wengine daraja kubwa kubwa, ili akujaribuni kwa hayo aliyo kupeni. Hakika Mola Mlezi wako ni Mwepesi wa kuadhibu, na hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu