Back to Languages

Swahili - Chapter 17 - Al-Isra

Translation by Ali Muhsin Al Barwani — Permalink

Verse 1 — Surah Al-Isra 17:1

SUBHANA, Ametakasika aliye mchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyo uzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya Ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona

Verse 2 — Surah Al-Isra 17:2

Na tukampa Musa Kitabu, na tukakifanya uwongofu kwa Wana wa Israili. (Tukawambia): Msiwe na mtegemewa ila Mimi

Verse 3 — Surah Al-Isra 17:3

Enyi kizazi tuliyo wachukua pamoja na Nuhu! Hakika yeye alikuwa mja mwenye shukrani

Verse 4 — Surah Al-Isra 17:4

Na tukawahukumia Wana wa Israili katika Kitabu kwamba: Hakika nyinyi mtafanya fisadi katika nchi mara mbili, na kwa yakini mtapanda kiburi, kiburi kikubwa

Verse 5 — Surah Al-Isra 17:5

Basi itapo fika ahadi ya kwanza yake tutakupelekeeni waja wetu wa kali kwa vita. Watakuingilieni ndani ya majumba. Na hii ilikuwa ahadi iliyo timizwa

Verse 6 — Surah Al-Isra 17:6

Kisha tukakurudishieni nguvu zenu dhidi yao, na tukakusaidieni kwa mali na wana, na tukakujaalieni mkawa wengi zaidi

Verse 7 — Surah Al-Isra 17:7

Basi mkifanya wema, mnajifanyia wema nafsi zenu. Na mkifanya ubaya, mnajifanyia wenyewe. Na ikifika ahadi ya mwisho ili waziharibu nyuso zenu, na waingie Msikitini kama walivyo ingia mara ya kwanza, na waharibu kila walicho kiteka kwa uharibifu mkubwa

Verse 8 — Surah Al-Isra 17:8

Huenda Mola wenu Mlezi akakurehemuni. Na mkirudia na Sisi tutarudia. Na tumeifanya Jahannamu kuwa ni gereza kwa ajili ya makafiri

Verse 9 — Surah Al-Isra 17:9

Hakika hii Qur'ani inaongoa kwenye ya yaliyo nyooka kabisa, na inawabashiria Waumini ambao wanatenda mema ya kwamba watapata malipo makubwa

Verse 10 — Surah Al-Isra 17:10

Na yakwamba wale wasio iamini Akhera tumewaandalia adhabu chungu

Verse 11 — Surah Al-Isra 17:11

Na mwanaadamu huomba shari kama vile aombavyo kheri, kwani mwanaadamu ni mwenye pupa

Verse 12 — Surah Al-Isra 17:12

Na tumefanya usiku na mchana kuwa ishara mbili. Tena tukaifuta ishara ya usiku, na tukaifanya ishara ya mchana ni yenye mwangaza ili mtafute fadhila itokayo kwa Mola wenu Mlezi, na mpate kujua idadi ya miaka na hisabu. Na kila kitu tumekifafanua waziwazi

Verse 13 — Surah Al-Isra 17:13

Na kila mtu tumemfungia a'mali yake shingoni mwake. Na Siku ya Kiyama tutamtolea kitabu atakacho kikuta kiwazi kimekunjuliwa

Verse 14 — Surah Al-Isra 17:14

Ataambiwa: Soma kitabu chako! Nafsi yako inakutosha leo kukuhisabu

Verse 15 — Surah Al-Isra 17:15

Anaye ongoka basi anaongoka kwa ajili ya nafsi yake. Na anaye potea basi anapotea kwa khasara yake mwenyewe. Wala habebi mbebaji mzigo wa mwengine. Wala Sisi hatuadhibu mpaka tumpeleke Mtume

Verse 16 — Surah Al-Isra 17:16

Na pindi tukitaka kuuteketeza mji huwaamrisha wale wenye starehe na taanusi, lakini wao huendelea kutenda maovu humo. Basi hapo kauli huthibiti juu ya mji huo, nasi tukauangamiza kwa maangamizo makubwa

Verse 17 — Surah Al-Isra 17:17

Na kaumu ngapi tumeziangamiza baada ya Nuhu! Na Mola wako Mlezi anatosha kabisa kuwa ni Mwenye kuzijua na kuziona dhambi za waja wake

Verse 18 — Surah Al-Isra 17:18

Anaye taka yapitayo upesi upesi, tutafanya haraka kumletea hapa hapa tunayo yataka kwa tumtakaye. Kisha tumemwekea Jahannamu; ataingia humo hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa na kufurushwa

Verse 19 — Surah Al-Isra 17:19

Na anaye itaka Akhera, na akazifanyia juhudi a'mali zake, naye ni Muumini, basi hao juhudi yao itakuwa ni ya kushukuriwa

Verse 20 — Surah Al-Isra 17:20

Wote hao tunawakunjulia - hawa na hao - katika neema za Mola wako Mlezi. Wala neema za Mola wako Mlezi hazizuiliki

Verse 21 — Surah Al-Isra 17:21

Angalia vipi tulivyo wafadhili baadhi yao kuliko wenginewe. Na hakika Akhera ni yenye daraja kubwa zaidi na fadhila kubwa zaidi

Verse 22 — Surah Al-Isra 17:22

Usimfanye mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, usije ukawa wa kulaumiwa uliye tupika

Verse 23 — Surah Al-Isra 17:23

Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa hishima

Verse 24 — Surah Al-Isra 17:24

Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma. Na useme: Mola wangu Mlezi! Warehemu kama walivyo nilea utotoni

Verse 25 — Surah Al-Isra 17:25

Mola wenu anajua kabisa yaliyo nyoyoni mwenu. Ikiwa nyinyi mtakuwa wema, basi hakika Yeye ni Mwenye kuwaghufiria wanao tubia kwake

Verse 26 — Surah Al-Isra 17:26

Na mpe aliye jamaa yako haki yake, na masikini, na msafiri; wala usitumie ovyo kwa fujo

Verse 27 — Surah Al-Isra 17:27

Hakika wabadhirifu ni ndugu wa Mashet'ani. Na Shet'ani ni mwenye kumkufuru Mola wake Mlezi

Verse 28 — Surah Al-Isra 17:28

Na ikiwa unajikurupusha nao, nawe unatafuta rehema ya Mola wako Mlezi unayo itaraji, basi sema nao maneno laini

Verse 29 — Surah Al-Isra 17:29

Wala usiufanye mkono wako kama ulio fungwa shingoni mwako, wala usiukunjue wote kabisa, utabaki ukilaumiwa muflisi

Verse 30 — Surah Al-Isra 17:30

Hakika Mola wako Mlezi humkunjulia riziki amtakaye, na humpimia amtakaye. Hakika Yeye kwa waja wake ni Mwenye kuwajua na kuwaona

Verse 31 — Surah Al-Isra 17:31

Wala msiwauwe wana wenu kwa kuogopa umasikini. Sisi tunawaruzuku wao na nyinyi. Hakika kuwaua hao ni khatia kubwa

Verse 32 — Surah Al-Isra 17:32

Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya

Verse 33 — Surah Al-Isra 17:33

Wala msiuwe nafsi ambayo Mwenyezi Mungu amekataza isipo kuwa kwa haki. Na aliye uliwa kwa kudhulumiwa basi tumempa madaraka mrithi wake. Lakini asipite mpaka katika kuuwa. Kwani yeye anasaidiwa

Verse 34 — Surah Al-Isra 17:34

Wala msiyakaribie mali ya yatima, isipo kuwa kwa njia iliyo bora, mpaka afike utuuzimani. Na timizeni ahadi. Kwa hakika ahadi itasailiwa

Verse 35 — Surah Al-Isra 17:35

Na timizeni kipimo mpimapo. Na pimeni kwa mizani zilizo sawa. Hayo ni wema kwenu na khatimaye ndio bora

Verse 36 — Surah Al-Isra 17:36

Wala usiyafuate usiyo na ujuzi nayo. Hakika masikio, na macho, na moyo - hivyo vyote vitasailiwa

Verse 37 — Surah Al-Isra 17:37

Wala usitembee katika ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala kufikia urefu wa milima

Verse 38 — Surah Al-Isra 17:38

Haya yote ubaya wake ni wenye kuchukiza kwa Mola wako Mlezi

Verse 39 — Surah Al-Isra 17:39

Haya ni katika hikima alizo kufunulia Mola wako Mlezi. Wala usimweke pamoja na Mwenyezi Mungu mungu mwengine, usije ukatupwa katika Jahannamu ukilaumiwa na kufurushwa

Verse 40 — Surah Al-Isra 17:40

Je! Mola wenu Mlezi amekuteulieni wavulana, na Yeye akawafanya Malaika ni banati zake? Kwa hakika nyinyi mnasema usemi mkubwa

Verse 41 — Surah Al-Isra 17:41

Na tumekwisha bainisha katika Qur'ani hii ili wapate kukumbuka. Lakini haikuwazidisha ila kuwa mbali nayo

Verse 42 — Surah Al-Isra 17:42

Sema: Lau kuwa wangeli kuwa pamoja naye miungu mingine kama wasemavyo, basi wangeli tafuta njia ya kumfikia Mwenye Kiti cha Enzi

Verse 43 — Surah Al-Isra 17:43

Subhanahu Wa Taa'la, Ametakasika na Ametukuka juu kabisa na hayo wanayo yasema

Verse 44 — Surah Al-Isra 17:44

Zinamtakasa zote mbingu saba na ardhi na vyote viliomo ndani yake. Na hapana kitu ila kinamtakasa kwa sifa zake. Lakini nyinyi hamfahamu kutakasa kwake. Hakika Yeye ni Mpole na Mwenye maghfira

Verse 45 — Surah Al-Isra 17:45

Na unapo soma Qur'ani tunaweka baina yako na wale wasio iamini Akhera pazia linalo wafunika

Verse 46 — Surah Al-Isra 17:46

Na tunaweka vifuniko juu ya nyoyo zao wasije wakaifahamu, na tunaweka kwenye masikio yao uziwi. Na unapo mtaja katika Qur'ani Mola wako Mlezi peke yake, basi wao hugeuka nyuma wakenda zao

Verse 47 — Surah Al-Isra 17:47

Sisi tunajua vyema kabisa sababu wanayo sikilizia wanapo kusikiliza, na wanapo nong'ona. Wanapo sema hao madhaalimu: Nyinyi hamumfuati isipo kuwa mtu aliye rogwa

Verse 48 — Surah Al-Isra 17:48

Tazama vipi wanavyo kupigia mifano. Basi wamepotea. Kwa hivyo hawawezi kuipata njia

Verse 49 — Surah Al-Isra 17:49

Na walisema: Je! Tutapo kuwa mifupa na mapande yaliyo vurugika, tutafufuliwa kwa umbo jipya

Verse 50 — Surah Al-Isra 17:50

Sema: Kuweni hata mawe na chuma

Verse 51 — Surah Al-Isra 17:51

Au umbo lolote mnalo liona kubwa katika vifua vyenu. Watasema: Nani atakaye turudisha tena? Sema: Yule yule aliye kuumbeni mara ya kwanza! Watakutikisia vichwa vyao, na watasema: Lini hayo? Sema: A'saa yakawa karibu

Verse 52 — Surah Al-Isra 17:52

Siku atakapo kuiteni, na nyinyi mkamuitikia kwa kumshukuru, na mkadhani kuwa hamkukaa ila muda mdogo tu

Verse 53 — Surah Al-Isra 17:53

Waambie waja wangu waseme maneno mazuri, maana Shet'ani huchochea ugomvi baina yao. Hakika Shet'ani ni adui aliye dhaahiri kwa mwanaadamu

Verse 54 — Surah Al-Isra 17:54

Mola wenu Mlezi anakujueni vilivyo. Akipenda atakurehemuni, na akipenda atakuadhibuni. Na hatukukutuma ili uwe mlinzi juu yao

Verse 55 — Surah Al-Isra 17:55

Na Mola wako Mlezi anawajua vilivyo waliomo mbinguni na katika ardhi. Na hakika tumewafadhilisha baadhi ya Manabii kuliko wengine; na Daudi tulimpa Zaburi

Verse 56 — Surah Al-Isra 17:56

Sema: Waombeni hao mnao wadaia badala yake Yeye. Hawawezi kukuondoleeni madhara, wala kuyaweka pengine

Verse 57 — Surah Al-Isra 17:57

Hao wanao waomba, wao wenyewe wanatafuta njia ya kwendea kwa Mola wao Mlezi - hata miongoni mwao walio karibu mno - na wanataraji rehema zake na wanaikhofu adhabu yake. Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi yafaa kutahadhari nayo

Verse 58 — Surah Al-Isra 17:58

Na hapana mji wowote ila Sisi tutauteketeza kabla ya Siku ya Kiyama, au tutaupa adhabu kali. Haya yamekwisha andikwa katika Kitabu

Verse 59 — Surah Al-Isra 17:59

Na hapana kinacho tuzuia kupeleka miujiza ila ni kuwa watu wa zamani waliikanusha. Na tuliwapa Wathamudi ngamia jike kuwa ni Ishara iliyo dhaahiri, lakini walidhulumu kwaye. Nasi hatupeleki Ishara ila kwa ajili ya kuhadharisha

Verse 60 — Surah Al-Isra 17:60

Na tulipo kwambia: Hakika Mola wako Mlezi amekwisha wazunguka hao watu. Na hatukuifanya ndoto tulio kuonyesha ila ni kuwajaribu watu, na mti ulio laaniwa katika Qur'ani. Na tunawahadharisha, lakini haiwazidishii ila uasi mkubwa

Verse 61 — Surah Al-Isra 17:61

Na pale tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam. Wakamsujudia isipo kuwa Iblisi. Akasema: Je! Nimsujudie uliye muumba kwa udongo

Verse 62 — Surah Al-Isra 17:62

Akasema: Hebu nambie khabari ya huyu uliye mtukuza juu yangu. Ukiniakhirisha mpaka Siku ya Kiyama, hapana shaka nitawaangamiza dhuriya zake wasipo kuwa wachache tu

Verse 63 — Surah Al-Isra 17:63

Akasema Mwenyezi Mungu: Ondokelea mbali! Atakaye kufuata katika wao, basi Jahannamu itakuwa ndiyo malipo yenu, malipo ya kutimia

Verse 64 — Surah Al-Isra 17:64

Na wachochee uwawezao katika wao kwa sauti yako, na wakusanyie jeshi lako la wapandao farasi na waendao kwa miguu. Na shirikiana nao katika mali na wana, na waahidi. Na Shet'ani hawapi ahadi ila ya udanganyifu

Verse 65 — Surah Al-Isra 17:65

Hakika wewe huna mamlaka juu ya waja wangu. Na Mola wako Mlezi anatosha kuwa ni wa kutegemewa

Verse 66 — Surah Al-Isra 17:66

Mola wenu Mlezi ndiye anaye kuendesheeni marikebu katika bahari ili mtafute katika fadhila zake. Hakika Yeye ni Mwenye kukurehemuni nyinyi

Verse 67 — Surah Al-Isra 17:67

Na inapo kufikieni taabu katika bahari, hao mnao waomba wanapotea, isipo kuwa Yeye tu. Na anapo kuvueni mkafika nchi kavu, mnageuka. Ama mwanaadamu ni mwingi wa kukanusha

Verse 68 — Surah Al-Isra 17:68

Je! Mmeaminisha ya kuwa hatakudidimizeni upande wowote katika nchi kavu, au kwamba hatakuleteeni tufani la kokoto? Kisha msipate wa kumtegemea

Verse 69 — Surah Al-Isra 17:69

Au mmeaminisha ya kuwa hatakurudisheni humo mara nyengine na kukupelekeeni kimbunga cha upepo akakuzamisheni kwa mlivyo kufuru, na kisha msipate wa kukunusuruni nasi

Verse 70 — Surah Al-Isra 17:70

Na hakika tumewatukuza wanaadamu, na tumewapa vya kupanda nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tulio waumba

Verse 71 — Surah Al-Isra 17:71

Siku tutapo waita kila kikundi cha watu kwa mujibu wa wakifuatacho - basi atakaye pewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, basi hao watasoma kitabu chao wala hawatadhulumiwa hata chembe

Verse 72 — Surah Al-Isra 17:72

Na aliye kuwa hapa kipofu, basi atakuwa kipofu Akhera, na atakuwa aliye ipotea zaidi Njia

Verse 73 — Surah Al-Isra 17:73

Na hakika walikaribia kukushawishi uache tuliyo kufunulia ili utuzulie mengineyo. Na hapo ndio wangeli kufanya rafiki

Verse 74 — Surah Al-Isra 17:74

Na lau kuwa hatukukuweka imara ungeli karibia kuwaelekea kidogo

Verse 75 — Surah Al-Isra 17:75

Hapo basi bila ya shaka tungeli kuonjesha adhabu mardufu ya uhai, na adhabu mardufu ya kifo. Kisha usinge pata mtu wa kukunusuru nasi

Verse 76 — Surah Al-Isra 17:76

Na walitaka kukukera ili uitoke nchi. Na hapo wao wasingeli bakia humo ila kwa muda mchache tu

Verse 77 — Surah Al-Isra 17:77

Huo ndio mwendo kwa Mitume tulio watuma kabla yako. Wala hupati mabadiliko katika mwendo wetu

Verse 78 — Surah Al-Isra 17:78

Shika Sala jua linapo pinduka mpaka giza la usiku, na Qur'ani ya al fajiri. Hakika Qur'ani ya alfajiri inashuhudiwa daima

Verse 79 — Surah Al-Isra 17:79

Na amka usiku kwa ibada; ni ziada ya sunna khasa kwako wewe. Huenda Mola wako Mlezi akakunyanyua cheo kinacho sifika

Verse 80 — Surah Al-Isra 17:80

Na sema: Mola wangu Mlezi! Niingize muingizo mwema, na unitoe kutoka kwema. Na unipe nguvu zinazo toka kwako zinisaidie

Verse 81 — Surah Al-Isra 17:81

Na sema: Kweli imefika, na uwongo umetoweka. Hakika uwongo lazima utoweke

Verse 82 — Surah Al-Isra 17:82

Na tunateremsha katika Qur'ani yaliyo ni matibabu na rehema kwa Waumini. Wala hayawazidishii madhaalimu ila khasara

Verse 83 — Surah Al-Isra 17:83

Na mwanaadamu tunapo mneemesha hugeuka na kujitenga kando. Na inapo mgusa shari hukata tamaa

Verse 84 — Surah Al-Isra 17:84

Sema: Kila mmoja anafanya kwa namna yake. Na Mola wenu Mlezi anajua aliye ongoka katika njia

Verse 85 — Surah Al-Isra 17:85

Na wanakuuliza khabari za Roho. Sema: Roho ni katika mambo ya Mola wangu Mlezi. Nanyi hamkupewa katika ilimu ila kidogo tu

Verse 86 — Surah Al-Isra 17:86

Na tungeli penda tungeli yaondoa tuliyo kufunulia. Kisha usingeli pata mwakilishi wa kukupigania kwetu kwa haya

Verse 87 — Surah Al-Isra 17:87

Isipo kuwa iwe rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Hakika fadhila yake kwako ni kubwa

Verse 88 — Surah Al-Isra 17:88

Sema: Wangeli kusanyika watu na majini ili walete mfano wa hii Qur'ani basi hawaleti mfano wake, hata wakisaidiana wao kwa wao

Verse 89 — Surah Al-Isra 17:89

Na hakika tumewaeleza watu katika hii Qur'ani kwa kila mfano. Lakini watu wengi wanakataa isipo kuwa kukanusha tu

Verse 90 — Surah Al-Isra 17:90

Na walisema: Hatutakuamini mpaka ututimbulie chemchem katika ardhi hii

Verse 91 — Surah Al-Isra 17:91

Au uwe na kitalu cha mitende na mizabibu, na utupitishie mito kati yake ikimiminika

Verse 92 — Surah Al-Isra 17:92

Au utuangushie mbingu vipande vipande kama ulivyo dai; au utuletee Mwenyezi Mungu na Malaika uso kwa uso

Verse 93 — Surah Al-Isra 17:93

Au uwe na nyumba ya dhahabu, au upae mbinguni. Wala hatutaamini kupaa kwako mpaka ututeremshie kitabu tukisome. Sema: Subhana Rabbi, Ametakasika Mola wangu Mlezi! Kwani mimi ni nani isipo kuwa ni mwanaadamu na Mtume

Verse 94 — Surah Al-Isra 17:94

Na nini kilicho wazuilia watu kuamini ulipo wajia uwongofu isipo kuwa walisema: Je! Mwenyezi Mungu humtuma mwanaadamu kuwa ni Mtume

Verse 95 — Surah Al-Isra 17:95

Sema: Ingeli kuwa duniani wapo Malaika wanatembea kwa utulivu wao, basi bila ya shaka tungeli wateremshia Malaika kuwa ni Mtume wao

Verse 96 — Surah Al-Isra 17:96

Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Shahidi baina yangu na nyinyi. Hakika Yeye anawajua vyema waja wake na anawaona

Verse 97 — Surah Al-Isra 17:97

Na anaye mhidi Mwenyezi Mungu basi huyo ndiye aliye hidika. Na anaye wapotoa basi huto wapatia walinzi badala yake. Na tutawakusanya Siku ya Kiyama hali wakikokotwa juu ya nyuso zao, nao ni vipofu na mabubu na viziwi. Na makaazi yao ni Jahannamu. Kila moto ukifanya kusinzia tutazidi kuuchochea uwake kwa nguvu

Verse 98 — Surah Al-Isra 17:98

Hayo ni malipo yao kwa sababu walizikataa ishara zetu, na wakasema: Hivyo tukisha kuwa mifupa na mapande yaliyo vurugika tutafufuliwa kwa umbo jipya

Verse 99 — Surah Al-Isra 17:99

Kwani hawakuona ya kwamba Mwenyezi Mungu aliye umba mbingu na ardhi ni Mwenye kuweza kuumba mfano wao? Na Yeye amewawekea muda usio na shaka yoyote. Lakini madhaalimu hawataki ila ukafiri

Verse 100 — Surah Al-Isra 17:100

Sema: Lau kuwa nyinyi mnazimiliki khazina za rehema za Mola wangu Mlezi, basi hapana shaka mngeli zuia kuzitumia kwa ajili ya kukhofu. Na mwanaadamu tangu hapo tabia yake ni mchoyo

Verse 101 — Surah Al-Isra 17:101

Na kwa yakini tulimpa Musa ishara tisa zilizo wazi. Waulize Wana wa Israili alipo wafikia, na Firauni akawaambia: Hakika mimi nakuona wewe Musa umerogwa

Verse 102 — Surah Al-Isra 17:102

Musa akasema: Wewe unajua bila ya shaka kuwa haya hakuyateremsha ila Mola Mlezi wa mbingu na ardhi ili kuwa ni ushahidi wa kuonekana. Na hakika mimi bila ya shaka nakuona wewe, Firauni, kuwa umekwisha angamia

Verse 103 — Surah Al-Isra 17:103

Basi Firauni akataka kuwafukuza katika nchi. Kwa hivyo tukamzamisha yeye na walio kuwa pamoja naye wote

Verse 104 — Surah Al-Isra 17:104

Na tukawaambia baada yake Wana wa Israili: Kaeni katika nchi. Itapo kuja ahadi ya Akhera tutakuleteni nyote pamoja

Verse 105 — Surah Al-Isra 17:105

Na kwa Haki tumeiteremsha, na kwa Haki imeteremka. Na hatukukutuma ila uwe mbashiri na mwonyaji

Verse 106 — Surah Al-Isra 17:106

Na Qur'ani tumeigawanya sehemu mbali mbali ili uwasomee watu kwa kituo, na tumeiteremsha kidogo kidogo

Verse 107 — Surah Al-Isra 17:107

Sema: Iaminini au msiiamini. Hakika wale walio pewa ilimu kabla yake, wanapo somewa hii, huanguka kifudifudi wanasujudu

Verse 108 — Surah Al-Isra 17:108

Na wanasema: Subhana Rabbina, Ametakasika Mola wetu Mlezi! Hakika ahadi ya Mola wetu Mlezi lazima itimizwe

Verse 109 — Surah Al-Isra 17:109

Na huanguka kifudifudi na huku wanalia, na inawazidisha unyenyekevu

Verse 110 — Surah Al-Isra 17:110

Sema: Mwombeni Allah (Mwenyezi Mungu), au mwombeni Rahman (Mwingi wa Rehema), kwa jina lolote mnalo mwita. Kwani Yeye ana majina mazuri mazuri. Wala usitangaze Sala yako kwa sauti kubwa, wala usiifiche kwa sauti ndogo, bali shika njia ya kati na kati ya hizo

Verse 111 — Surah Al-Isra 17:111

Na sema: Alhamdulillah, Himdi zote ni za Mwenyezi Mungu ambaye hana mwana, wala hana mshirika katika ufalme, wala hana rafiki wa kumsaidia kwa sababu ya udhaifu wake. Na mtukuze kwa utukufu mkubwa