Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na lishuhudie adhabu yao kundi la Waumini
Mwanamume mzinifu hamwoi ila mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina. Na mwanamke mzinifu haolewi ila na mwanamume mzinifu au mshirikina. Na hayo yameharimishwa kwa Waumini
Na wanao wasingizia wanawake mahashumu, kisha wasilete mashahidi wane, basi watandikeni bakora thamanini, na msiwakubalie ushahidi wao tena. Na hao ndio wapotovu
Na wale wanao wasingizia wake zao na hawana mashahidi ila nafsi zao, basi ushahidi wa mmoja wao utakuwa kushuhudilia mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu ya kwamba hakika yeye ni katika wasema kweli
Hakika wale walio leta uwongo ni kundi miongoni mwenu. Msifikiri ni shari kwenu, bali hiyo ni kheri kwenu. Kila mtu katika wao atapata aliyo yachuma katika madhambi. Na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao, atapata adhabu kubwa
Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake katika dunia na Akhera, bila ya shaka ingeli kupateni adhabu kubwa kwa sababu ya yale mliyo jiingiza
Enyi mlio amini! Msizifuate nyayo za Shet'ani. Na atakaye fuata nyayo za Shet'ani basi yeye huamrisha machafu na maovu. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake juu yenu, asingeli takasika miongoni mwenu kabisa hata mmoja. Lakini Mwenyezi Mungu humtakasa amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua
Na wale katika nyinyi wenye fadhila na wasaa wasiape kutowapa jamaa zao na masikini na walio hama kwa Njia ya Mwenyezi Mungu. Na wasamehe, na waachilie mbali. Je! Nyinyi hampendi Mwenyezi Mungu akusameheni? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu
Wanawake waovu ni wa wanaume waovu, na wanaume waovu ni wa wanawake waovu. Na wanawake wema ni wa wanaume wema, na wanaume wema ni wa wanawake wema. Hao wameepushwa na hayo wanayo yasema; wao watapata msamaha na riziki ya ukarimu
Na msip o mkuta mtu humo basi msiingie mpaka mruhusiwe. Na mkiambiwa: Rudini! Basi rudini. Hivi ni usafi zaidi kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnayo yatenda
Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipo kuwa unao dhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao, au iliyo wamiliki mikono yao ya kuume, au wafwasi wanaume wasio na matamanio, au watoto ambao hawajajua mambo yaliyo khusu uke. Wala wasipige chini miguu yao ili yajuulikane mapambo waliyo yaficha. Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa
Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu. Wakiwa mafakiri Mwenyezi Mungu atawatajirisha kwa fadhila yake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa Mwenye kujua
Na wajizuilie na machafu wale wasio pata cha kuolea, mpaka Mwenyezi Mungu awatajirishe kwa fadhila yake. Na wanao taka kuandikiwa uhuru katika wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki, basi waandikieni kama mkiona wema kwao. Na wapeni katika mali ya Mwenyezi Mungu aliyo kupeni. Wala msiwashurutishe vijakazi vyenu kufanya zina kwa ajili ya kutafuta pato la maisha ya dunia, ilhali wao wanataka kujihishimu. Na atakaye walazimisha basi Mwenyezi Mungu baada ya kulazimishwa kwao huko, atawasamehe, kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu
Mwenyezi Mungu ni Nuru ya Mbingu na Ardhi. Mfano wa Nuru yake ni kama shubaka lenye kuwekwa ndani yake taa. Taa ile imo katika tungi. Tungi lile ni kama nyota inayo meremeta, inayo washwa kwa mafuta yanayo toka katika mti ulio barikiwa, mzaituni. Si wa mashariki wala magharibi. Yanakaribia mafuta yake kung'aa wenyewe ingawa moto haujayagusa - Nuru juu ya Nuru. Mwenyezi Mungu humwongoa kwenye Nuru yake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu
Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Mwenyezi Mungu, na kushika Sala, na kutoa Zaka. Wanaikhofu Siku ambayo nyoyo na macho yatageuka
Na walio kufuru vitendo vyao ni kama sarabi (mazigazi) uwandani. Mwenye kiu huyadhania ni maji. Hata akiyaendea hapati chochote. Na atamkuta Mwenyezi Mungu hapo naye amlipe hisabu yake sawa sawa. Na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu
Au ni kama giza katika bahari kuu, iliyo funikwa na mawimbi juu ya mawimbi, na juu yake yapo mawingu. Giza juu ya giza. Akiutoa mtu mkono wake anakaribia asiuone. Na ambaye Mwenyezi Mungu hakumjaalia kuwa na nuru hawi na nuru
Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu vinamtakasa vilivyomo katika mbingu na ardhi, na ndege wakikunjua mbawa zao? Kila mmoja amekwisha jua Sala yake na namna ya kumtakasa kwake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua wayatendayo
Je! Huoni ya kwamba Mwenyezi Mungu huyasukuma mawingu, kisha huyaambatisha, kisha huyafanya mirundi? Basi utaona mvua ikitoka kati yake. Na huteremsha kutoka juu kwenye milima ya mawingu mvua ya mawe, akamsibu nayo amtakaye na akamuepusha nayo amtakaye. Hukurubia mmetuko wa umeme wake kupofua macho
Na Mwenyezi Mungu ameumba kila kinyama kutokana na maji. Wengine katika wao huenda kwa matumbo yao, na wengine huenda kwa miguu miwili, na wengine huenda kwa miguu mine. Mwenyezi Mungu huumba ayatakayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu
Haiwi kauli ya Waumini wanapo itwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili ahukumu baina yao, ila ni kusema: Tumesikia, na tumet'ii! Na hao ndio wenye kufanikiwa
Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu ukomo wa kiapo chao ya kwamba ukiwaamrisha kwa yakini watatoka. Sema: Msiape! Ut'iifu unajuulikana. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda
Sema: Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume. Na mkigeuka, basi yaliyo juu yake ni aliyo bebeshwa, na yaliyo juu yenu ni mliyo bebshwa nyinyi. Na mkimt'ii yeye mtaongoka. Na hapana juu ya Mtume ila kufikisha Ujumbe wazi wazi
Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walio amini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyo wafanya makhalifa wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao aliyo wapendelea, na atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wawe wananiabudu Mimi, wala wasinishirikishe na chochote. Na watao kufuru baada ya hayo, basi hao ndio wapotovu
Enyi mlio amini! Nawakutakeni idhini iliyo wamiliki mikono yenu ya kulia na walio bado kubaalighi miongoni mwenu mara tatu - kabla ya Sala ya alfajiri, na wakati mnapo vua nguo zenu adhuhuri, na baada ya Sala ya isha. Hizi ni nyakati tatu za faragha kwenu. Si vibaya kwenu wala kwao baada ya nyakati hizi, kuzungukiana nyinyi kwa nyinyi. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kuelezeni Aya zake, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima
Na watoto wanapo fikilia umri wa kubaalighi basi nawatake ruhusa, kama walivyo taka ruhusa wa kabla yao. Hivyo ndivyo anavyo kubainishieni Mwenyezi Mungu Aya zake, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima
Na wanawake wazee wasio taraji kuolewa, si vibaya kwao kupunguza nguo zao, bila ya kujishaua kwa mapambo. Na wakijihishimu ni bora kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua
Si vibaya kwa kipofu, wala si vibaya kwa kiguru, wala si vibaya kwa mgonjwa, wala kwenu nyinyi, mkila katika nyumba zenu, au nyumba za baba zenu, au nyumba za mama zenu, au nyumba za kaka zenu, au nyumba za dada zenu, au nyumba za ami zenu, au nyumba za shangazi zenu, au nyumba za wajomba zenu, au nyumba za dada wa mama zenu, au za mlio washikia funguo zao, au rafiki yenu. Si vibaya kwenu mkila pamoja au mbali mbali. Na mkiingia katika nyumba, toleaneni salamu, kuwa ni maamkio yanayo toka kwa Mwenyezi Mungu, yenye baraka na mema. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kubainishieni Aya zake mpate kuelewa
Hakika Waumini wa kweli ni walio muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake; na wanapo kuwa pamoja naye kwa jambo la kuwakhusu wote hawaondoki mpaka wamtake ruhusa. Kwa hakika wale wanao kuomba ruhusa, hao ndio wanao muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na wakikuomba ruhusa kwa baadhi ya kazi zao, mruhusu umtakaye miongoni mwao, uwaombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemmu
Msifanye wito wa Mtume baina yenu kama wito wa nyinyi kwa nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu anawajua miongoni mwenu wanao ondoka kwa uficho. Basi nawatahadhari wanao khalifu amri yake, usije ukawapata msiba au ikawapata adhabu chungu
Jueni kuwa hakika ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na ardhini. Hakika Yeye anajua mlio nayo. Na siku mtapo rudishwa kwake atawaeleza waliyo yafanya. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu